Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwanne Ismail Mchemba (17 total)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye kutia matumaini makubwa, naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara hizi zimeathirika kiasi kikubwa wakati huu wa mvua ambazo zimenyesha kwa wingi na kwa kuwa mpaka hivi sasa barabara hizo hazipitiki, je, Serikali iko tayari kutengeneza sehemu korofi ili usafiri uendelee kama ilivyokuwa zamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza kwamba vijana wetu wa TANROADS pamoja na Mameneja wa TANROADS Mkoa hivi sasa waelekeze nguvu katika kufungua mawasiliano kwa sehemu zote zilizoathiriwa na mvua. Hii ikiwa ni pamoja na barabara hii ya Nyahua - Chaya ambayo imekatika kwa kipindi kirefu kidogo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, humu ndani maswali yote huwa yanaelekeza nyumba za Polisi. Je, Waziri anasema nini kuhusu nyumba za Askari Magereza hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia tuna tatizo la upungufu wa nyumba katika Jeshi la Magereza. Kama ambavyo ipo katika Jeshi la Polisi, pia iko programu ya ujenzi wa nyumba ambazo zinakwenda sambamba na hizi za Polisi, kwenye Polisi tuna nyumba 4,136 na Magereza tuna nyumba takribani 9,500 kama nitakuwa sijakosewa sawasawa takwimu zake. Kwa hiyo, tunatambua hiyo changamoto na zipo katika hatua nzuri tu za utekelezaji naamini kabisa katika kipindi cha miaka mitano hii, tutaanza kuona miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba hizi pindi mipango ya upatikanaji wa fedha na taratibu za kifedha kupitia Hazina itakapokamilika basi nyumba za Polisi na Magereza kwa pamoja zitakwenda sambamba.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa nchi ya Tanzania ilikuwa koloni la Mwingereza na hivyo kuwa na mahusiano mazuri mpaka hivi sasa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuishawishi sasa Serikali ya Uingereza ili waweze kurejesha huduma hiyo hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huu mpya wa Serikali ya Uingereza ni wa duniani kote, siyo kwa Tanzania tu. Kwa hiyo, siyo kwamba ni sisi pekee ndio tumebanwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimweleze tu kwamba kuhamishwa kwa Kituo cha Kuchakata Visa za Uingereza kwenda Pretoria nchini Afrika Kusini hakujaathiri utoaji wa visa. Sana sana kinachotakiwa kwa sasa ni kwamba ujipange mapema, ufanye maombi mapema, lakini kimsingi muda umebaki vilevile, gharama ni zile zile. Kwa hiyo, wao walichofanya ni kupunguza gharama zao za kuchakata visa kwa kuhakikisha kwamba wanaipa Kandarasi Kampuni ya Tele-Performance, badala ya wao wenye kufanya hiyo kazi. Kwa hiyo, namhakikishia tu kwamba hakuna madhara makubwa ambayo yametokea kwa sababu hiyo.
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naitwa Mwanne Ismail Nchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tatizo la Wakimbizi wa Katumba linafanana na tatizo la Wakimbizi wa Ulyankulu na kwa kuwa hawakufanya uchaguzi wa Madiwani. Je, Serikali inasema nini, ni lini utafanyika uchaguzi wa Madiwani katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hao ni wananchi wake, akiwa Mbunge wa Viti Maalum ana kila sababu ya kuona maeneo hayo yanafanyika uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka swali hili nilijibu katika Mkutano wetu wa Bunge uliopita, nilisema pale kuna takribani Kata tatu uchaguzi haujafanyika kwa sababu za msingi, bado suala zima la utengamano linaendelea na pale sasa hivi bado Jeshi na Wizara ya Mambo ya Ndani wanaendelea kumiliki eneo lile. Utararibu utakapokamilika jukumu letu kubwa watu wa TAMISEMI baada ya ule mtangamano kuwa vizuri zaidi na eneo lile sasa rasmi likishakuwa chini ya TAMISEMI, mchakato wa uchaguzi sasa utaendelea ili watu wa pale wajikute nao wana Serikali yao halali iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Namba 292
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Naibu Waziri amesema kwamba watumishi ambao wameajiriwa na ushirika huo wanapewa semina mbalimbali za kitaalamu na kwa kuwa kama tunavyofahamu suala la hesabu kwa nchi yetu ni tatizo, hawajui hesabu, je, Serikali inajua kwamba mpaka hivi sasa wanunuzi wa tumbaku ambao wamejitawala wanadaiwa na wakulima shilingi bilioni 14 za mwaka 2014/2015 ambazo hawajalipwa mpaka sasa? Je, Serikali inasemaje kufuatilia suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mpaka hivi sasa soko la mwaka huu halijaanza, linasuasua na unapochelewa kupima tumbaku maana yake unapunguza kilo za tumbaku. Je, Serikali inasema nini kufuatilia suala la soko la tumbaku kwa sasa hivi ili liweze kukamilika kwa muda muafaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama anavyosema kwamba wakulima wa tumbaku wa Tabora na wa mikoa mingine wanadai fedha nyingi, wanawadai vyama vya ushirika pamoja na wanunuzi wa tumbaku. Serikali imekuwa ikiendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba fedha hizi zinalipwa. Tayari mafaili ya watu waliohusika na ubadhirifu mkubwa katika Mkoa wa Tabora yameshawasilishwa Polisi taratibu nyingine ziendelee ili wahusika waweze kupelekwa mbele ya sheria ikiwezekana wakulima waweze kupata fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu soko la tumbaku, ni kweli kama Mheshimiwa alivyosema kwamba suala la soko la tumbaku bado linasuasua na Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya njia mbalimbali ili kuhakikishia wananchi kwamba soko halitapata shida. Jitihada hizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanapatikana wanunuzi wengine wa tumbaku ili kuondoa ukiritimba wa wanunuzi wachache ambao mara nyingi wao ndiyo wanaoamua bei lakini vilevile wao pekee ndiyo wanaendesha soko la tumbaku. Tunaamini kwamba wanunuzi wengine wakipatikana itaondoa tatizo hili na italeta ushindani na hivyo kuondoa tatizo katika bei na soko la tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishaahidi kwamba tukitoka kwenye Bunge hili tutaenda Tabora na maeneo mengine kwa wadau wa tumbaku tujadiliane namna bora ya kuboresha zao la tumbaku. Nimhakikishie tu kwamba pamoja na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kuhama, ambaye ndiye aliyetoa ahadi, ahadi ile ilikuwa ni ya Wizara na iko pale pale. Niwahakikishie tu kwamba tukimaliza bajeti Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ataelekea Tabora kwa ajili ya kwenda kuongea na wadau kuhusu masuala ya tumbaku.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa ongezeko la ajira kwa watoto wadogo ni kubwa sana hapa nchini; na kwa kuwa tatizo hilo kuchangiwa na kuvunjika kwa ndoa kwa kutokuwa na msingi na kuachiwa akina mama kulea hao watoto. Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka kuleta mabadiliko ya sheria ya mwaka 1971 ili wanawake na watoto hawa waweze kupata haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa TASAF III imeonesha mpango mzuri sana na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwenye mashamba makubwa watoto hao wapo wengi na wanaonekana kama vile kwenye mashamba ya tumbaku, kahawa, chai, pamba na kadhalika, je, Waziri yuko tayari kuwakusanya hawa watoto na kuwapa elimu ya kutosha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa swali lake la kwanza kuhusiana na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, bahati nzuri suala hili limekuwa likizungumzwa katika nyakati mbalimbali na hata katika Bunge hili na Mkutano huu wa Tatu, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria amelisemea sana, lakini vilevile Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto pia ameweza kulizungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kwa mara nyingine tena, ni kweli sheria hii ilionekana kuna upungufu. Ukiangalia viko baadhi ya vifungu vinavyoruhusu masuala mazima ya ndoa za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kutambua kwamba katika masuala haya ya ndoa kuna mkanganyiko wa masuala ya kimila na kidini, ikaonekana kwamba ni vema suala hili likapatiwa suluhu kwa kupata maoni ya wananchi wengi zaidi kupitia mchakato wa White Paper. Mwanzo wakati zoezi hili Wizara ya Katiba na Sheria ilipotaka kulianza, taratibu zote karibia zilikuwa zimeshakamilika, lakini ikawa imeingiliana na mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Ikaonekana itakuwa si wakati mzuri kuwachanganya wananchi, huku wanatakiwa watoe maoni kuhusiana na Katiba Mpya lakini wakati huo huo unawapelekea zoezi lingine kuhusiana na marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Vilevile ilionekana kwamba huenda wakati ule kwenye kukusanya maoni ya Mabadiliko ya Katiba wananchi wangeweza kulisemea jambo hili lakini kwa kiasi kikubwa halikusemewa sana. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria bado wanasubiria wakati mzuri zaidi wa kuweza kulipeleka lakini ni lazima liende kupitia Waraka wa Maoni kupitia White Paper.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwa watoto ambao wamekuwa wakifanya ajira mbalimbali za utotoni, niseme tu kwamba kupitia Wizara ya Kazi kwa Mheshimiwa Jenista, wamekuwa wakifanya kazi hii na wanaendelea kufanya kazi hii kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wako katika ajira za utotoni wanaelimishwa, lakini zaidi kuhakikisha kwamba wazazi wao wanapewa elimu hii. Ndiyo maana kupitia TASAF kama nilivyoeleza, nichukulie tu kwa upande wa Zanzibar, zaidi ya watoto laki moja na mbili wamekuwa wakinufaika na ruzuku hii ili kuwawezesha kwenda shule.
Kwa hiyo, ni imani yangu bado kupitia Serikali kwa ujumla wake na mipango mbalimbali na TASAF ikiwemo tutahakikisha tunatoa elimu hii, lakini vilevile kuona ni kwa namna gani watoto wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo. Nakushukuru.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi name niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la Mwanza linafanana na tatizo la Tabora Manispaa, Kata ya Malolo na mpaka sasa hawajalipwa fidia ya aina yoyote na wakati huo huo Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliwahi kufika na kutoa agizo. Je, Serikali inasemaje kuhusu kulipa fidia ya hawa wakazi wa Kata ya Malolo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama nilivyosema katika majibu ya awali ambayo nilikuwa naongezea kwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI), nimesema Wizara imejipanga katika kupitia; kwa sababu tumekusanya madai haya au migororo na fidia anazozisema mengi yako katika ile orodha tuliyoichukua. Kwa hiyo, tutakachofanya sisi ni kukumbusha taasisi zinazohusika na fidia hiyo ili waweze kulipa, kwa sababu ni nyingi kweli zimekaa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna namna nyingine ya kufanya kwa sababu Serikali haiwezi kulipa fidia ambayo inadaiwa taasisi au maeneo mengine tofauti. Kwa hiyo, tutakachofanya sisi ni kupeleka kumbukumbu za kuwakumbusha wahusika na pale ambapo Serikali inahusika yenyewe basi itajipanga namna ya kuweza kuilipa.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Busega linafanana na tatizo la Mkoa wa Tabora, hususan Tabora Manispaa; na kwa kuwa tuna bwawa la Kazima ambalo kina chake ni kifupi: Je, Serikali ipo tayari sasa kukarabati bwawa hilo ili tuweze kupunguza tatizo la maji Mkoa wa Tabora hususan Tabora Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la Kazima lilijengwa mwaka 1946 na bwawa hili lilijengwa na watu wa reli kwa ajili ya kupata maji ya kupoza engine zile ambazo zilikuwa zinatumia mkaa. Mwaka 1990 matumizi yalibadilika baada ya kupata engine ambazo zinatumia diesel, kwa hiyo, ikaamuliwa bwawa hili liwe linatumika kwa ajili ya maji ya kunywa. Sasa hivi linamilikiwa na Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Tabora (TUWASA) na linazalisha lita milioni 1,400 ya maji safi na salama kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka imeomba shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha lile tuta kwa sababu mwaka huu maji yalijaa sana, lakini pia lipo shirika linalohudumia maeneo ya Lake Tanganyika. Mamlaka wameomba ili waweze kulikarabati lile bwawa liendelee kuhimili kuweka maji mengi na kuendelea kuwahudumia wananchi wa Tabora. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwanne nikuhakikishie kwamba suala hili linafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba bwawa hili linakarabitiwa.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo. Kwa kuwa matatizo ya Wilaya ya Nkasi yanafanana na matatizo ya Mkoa wa Tabora na kwa kuwa nyumba za Polisi na Magereza za Mkoa wa Tabora ni mbovu sana ikiwa ni pamoja na miundombinu ya vyoo. Pamoja na kipaumbele katika Mkoa wa Tabora yuko tayari twende naye kwa gharama zangu akaone hali halisi ya vyoo?
NAIBU WAZIRI WA MAMABO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari lakini siyo kwa gharama zake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri nilikuwa na ratiba ya kutembelea Tabora pamoja na Rukwa katika kipindi hiki kwenye ile ziara yetu pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotokea huko kwenye kambi za makazi ya waliokuwa wakimbizi. Basi tutaunganisha ziara hiyo weekend moja kabla hatujaondoka Dodoma, tuwasiliane baadaye kwa ajili hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wengi wamejitolea kujenga maboma ambayo wamejitolea kujenga zahanati, nyumba za Walimu na mpaka sasa halmashauri hazijaweza kukamilisha. Je, ni lini sasa Halmashauri zitakamilisha miradi ambayo ni viporo ambavyo wananchi wameweza kujenga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maboma ni mengi na kumbukumbu yangu kati ya tarehe 12 na 13 nilikuwa kule Tabora katika Mkoa wako na nishukuru sana ushirikiano wako japokuwa ulikuwa na changamoto za kuuguliwa. Katika kupita huko huko katika Mkoa wa Tabora lakini na mikoa mingine tatizo la maboma limekuwa ni kubwa ndiyo maana katika maelekezo yetu tumeagiza kwanza lazima tumalize vile viporo vya mwanzo. Kama maboma ya ujenzi wa zahanati, nyumba za Walimu lazima tumalize hilo kwanza.
Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana mtaona katika maelekeo ya bajeti yetu itakayokuja ya mwaka mwingine wa fedha unaokuja, tutahakikisha suala zima la maboma sio suala katika sekta ya elimu peke yake hali kadhalika katika sekta ya afya tumalize hayo halafu ndiyo tuweze kuanza upya. Haiwezekani wananchi wamefanya nguvu kubwa za kutosha halafu nguvu zikapotea bure; Serikali imeliona hilo na ndio maana tuna mpango mkakati mpana sana kuondoa kero hiyo katika Jamhuri yote ya Tanzania.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali madogo ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa ugonjwa huu ni wa kitaalam zaidi na kwa kuwa elimu yake haijatolewa kikamilifu; je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwenye vituo vya afya, zahanati na Wilaya wanapohudhuria kliniki wakina mama. Kwa sababu waathirika wakubwa ni wakina mama, je, Serikali inasema nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa ugonjwa huu dawa zake zina gharama sana, je, Serikali iko tayari kuzitoa dawa hizo bure ili akina mama na wananchi wote waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu elimu Serikali tayari inatoa elimu kuhusiana na ugonjwa wa sicklecell na magonjwa mengine yote kwa kina mama kwenye kliniki ya uzazi pindi akina mama wanapokwenda kuhudhuria, aidha wao wenyewe kwa mahitaji yao mbalimbali ama watoto wao walio chini ya umri wa miaka mitano, kwa hiyo, elimu inatolewa.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa kwenye kutoa elimu ipo kwenye kutoa elimu kwa vijana ambao wanatarajia kushika mimba siku za usoni. Changamoto hii ni kwamba bado katika nchi yetu hatubajeti sana fedha kwa ajili ya kinga zaidi kwa kweli tunatumia fursa ya kliniki na watu wanaokwenda hospitalini ama fursa ya shule kutoa elimu ya afya kwa umma, kama tungepata fursa ya kibajeti ya kuweza kufanya hivyo tungeweza kufanya.
Sasa tunashirikiana na wadau mbalimbali kama Chama cha Kitaifa cha Sickle Cell ambacho kinatoa elimu nchi nzima kuhusiana na ugonjwa huu, pia kuna taasisi ya utafiti iko pale Muhimbili nayo inatoa elimu kwa umma nchi nzima kuhusiana na ugonjwa huu. Kwa vijana ambao wanatarajia kwenda kujifungua ama wanapata mwenza ni vema wakapima kama wao ni carriers wa sickle cell ama laa. Kwa sababu carrier wa sickle cell akiona na carrier wa sickle cell wakashika mimba maana yake mtoto ana hatari ya asilimia zaidi ya 25 ya kupatwa na ugonjwa huu kama homozygous yaani kuwa na sickle cell ambayo imekomaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na gharama za matibabu ya sickle cell hapa nchini, ugonjwa wa sickle cell napenda kumpa taarifa yeye, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba ni miongoni mwa magonjwa ambayo kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Taifa ya mwaka 2007 ugonjwa wa sickle cell unatibiwa bure. Tiba ya sickle cell ni bure kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya, sasa hivi kuna taasisi imetufuata inataka kutekeleza huo mradi wa kutoa elimu kwa umma nchi nzima ili kuwa-screen watu wote wajue hali zao kuhusiana na sickle cell kama wao ni carrier ama siyo carriers.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Mlele linafanana sana na tatizo la Tabora Manispaa, Uyui pamoja na Kaliua, je, Serikali inasema nini kuhusu kukamilisha au kuandaa mpango wa kukamilisha hospitali ambazo hazipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, Serikali kama tulivyosema kipaumbele chake ni kuhakikisha huduma ya afya inapatikana na ndiyo maana siwezi ku-disclose
information zote, lakini kuna juhudi kubwa sana inafanyika lakini kiukweli ni kwamba kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kwanza kipaumbele cha kwanza kinawekwa na Halmashauri, japokuwa mnajua kwamba katika suala zima la cealing ya bajeti wakati mwingine ile cealing ikishaondoka vipaumbele vingine vinakwama, lakini tutaangalia jinsi gani tutafanya, lengo letu kubwa ni kwamba wananchi katika kila
maeneo waweze kupata huduma. Na ndiyo maana tunafanya harakati mbalimbali kufanya marekebisho makubwa katika sekta ya afya lakini imani yangu ni kwamba tutafika mahali pazuri tutasimama vizuri. Kwa hiyo wananchi, ndugu zangu wa Tabora ambao wengi ni watani wangu naomba msiwe na hofu kwamba Serikali yenu iko nanyi kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa mazuri.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wananchi wengi
wamekuwa waoga kwenda kwenye kituo cha polisi hususan wanawake na kwa kuwa maeneo mengi hayana vituo vya polisi hususan vijijini. Je, Serikali iko tayari sasa kugatua madaraka kwa Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili waweze kupata matibabu pale wanapopata ajali?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuona uhalisia unaotokea kwenye grass root. Niseme tu tumepokea wazo hilo, itabidi tuongee na wenzetu wa TAMISEMI kwa sababu likiamuliwa kufanyika katika msingi huo kuna vitu ambavyo lazima tujiridhishe navyo na aina ya maumivu ambayo yanaweza yakatumika kwenye ngazi ya viongozi wetu wa Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu ambacho huwa tunakiepusha na kulazimisha ipitie polisi hasa ni kwa wale ambao wanaweza wakafanya makosa makubwa kwa mfano, mtu aliyeenda kuiba akawa amejeruhiwa angetamani sana asipitie polisi aende moja kwa moja hospitalini. Kwa hiyo, huwa tunaona apitie polisi na wale
wengi wanaokwepa kupitia polisi tunakuwa tunajua watakuwa wana vitu wanavyovihofia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa vitu ambavyo
vimefanyika katika ngazi ya familia labda mtu amepata ajali ya kawaida katika ngazi ya familia ama katika eneo na anafahamika, ana kumbukumbu nzuri za kutokuwa na vitendo vya kihalifu ni maeneo ambayo tunaweza tukaongelea tukaenda katika taswira hiyo aliyoisemea Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kituo cha afya cha Manonga jengo lake la upasuaji limekamilika; na kwa kuwa mpaka sasa hakifanyi kazi, je, Serikali ni lini, itapeleka vifaa vya upasuaji katika kituo hicho cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna tatizo katika kituo cha afya cha Manonga, pia tulikuwa na tatizo hili katika vituo vya afya mbalimbali ambapo tulivijenga kupitia mradi wa ADB, bahati nzuri tumepata mafanikio katika Mkoa wako katika kituo cha afya cha Itobo na Bukene vimeshaanza kufanya kazi, Manonga pale vifaa vilikuwa bado havijakamilika. Hivi sasa tunaendelea kuangalia ni jinsi gani tufanye kwa sababu pale kulikuwa na mapungufu ambayo yalijitokeza huku, katika suala zima mchakato wa ujenzi ule kuna mambo mengine hayakwenda sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inalichukua hili tuangalie nini tufanye ili kituo cha afya cha Manonga kiweze kukamilika vizuri kuwa na vifaa pale na wananchi wa eneo lile wajisikie kwamba wana viongozi wao Mbunge wao Mheshimiwa Mwanne Mchemba na Mheshimiwa Gulamali wanawawakilisha huku. Sasa Serikali tumelichukua hili kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ajali hizi za wanaoendesha vyombo vya moto ni nyingi sana hapa nchini, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kila anayehitaji leseni anakuwa na bima ya afya ili waweze kurahisisha matibabu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mchemba kwa concern hiyo ya vijana wetu, tumelipokea kama Serikali na tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Afya. Lakini kubwa si kwa anayehitaji leseni, tunaongelea kwa wale ambao wanafanya ile shughuli yenyewe. Kwa sababu kwenye leseni kuna kuwepo na vitu vya aina mbili, kuna yule anayemiliki na kuna wale wanaoendesha ambao ndio wamekuwa wakipata zaidi ajali kuliko wale wanaomiliki bodaboda zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na viongozi wa vijiwe hivi tumeendelea kuwaelekeza kwamba wahakikishe katika makundi yale wanatambuana wale wanaohusika na akiongezeka ambaye hayuko kwenye kijiwe chao na hawajui kuhusu leseni zao, nao wachukue wajibu huo kwa sababu kwa kweli ni jambo ambalo linatoa ajira, lakini limekuwa likitugharimu sana maisha ya vijana wetu hawa wanapofanya kazi hizo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Wilaya ya Uyui tayari ina eneo kubwa ambalo wawekezaji wanaweza wakalitumia. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapeleka wataalam kuhakikisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wawekezaji wengi hapa nchini hukiuka maandiko au mikataba wanayoingia na Serikali. Je, Serikali iko tayari sasa kuipitia upya ile mikataba na kuivunja kabisa mikataba ambayo wameingia hapa nchini kwa mfano Kiwanda cha Manonga na Kiwanda cha Nyuzi? Je, Serikali inasema nini? Je, Waziri yuko tayari sasa kwenda kuviona viwanda hivyo jinsi walivyoviharibu? Naomba majibu. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Uyui, kwenye kongamano nililolisema ambalo analisimamia Mkuu wa Mkoa na Meneja wa Tan Trade na mimi nitakuwepo. Kwa hiyo, nitakwenda Uyui na wataalam tutaangalia hali itakavyokuwa na tutaweza kuwashauri namna ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si wawekezaji wote wanakiuka, mmoja anayekiuka umlete tutamshughulikia, ni case by case. Wawekezaji si wabaya, wawekezaji ni wazuri lakini yule anayekiuka tutamshughulikia kulingana na tukio lenyewe.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yamekidhi lakini naomba niongeze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Tabora una historia nyingi sana ukizingatia pia na historia ya Baba wa Taifa, lakini wakati anajibu majibu yake Baba wa Taifa hakuwepo, hawakuongeza, kwa hiyo, niombe Wizara ya utalii iongeze kuitangaza historia ya Baba wa Taifa.
Lakini lingine kuna historia ya miembe ambayo ina umri wa miaka 100 nayo ipo kwenye njia ya watumwa. Kwa hiyo niombe niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa hivi sasa njia ya utmwa inatambulika, je, Serikali iko tayari kuikarabati ile njia kutoka Tabora hadi Kigoma - Ujiji ili iwarahisishie watalii kupita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine, je, Serikali iko tayari kuwatuma wataalam kuhakikisha vivutio vyote ambavyo vipo katika Mkoa wa Tabora vinaorodheshwa? Ukilinganisha na mapato yaliyopatikana tangu 2013 mpaka 2017 ni milioni mbili, milioni mbili kuna nini? Kwa hiyo nasema kwa uchungu kwamba bado tunahitaji utangazaji wa utalii kwa Mkoa wa Tabora ni muhimu sana naomba izingatiwe, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukarabati hii njia ambayo inatoka Tabora hadi Kigoma hili tutalifanyia kazi, tutaangalia kadri upatikanaji wa fedha utakavyokuwepo katika bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuhusu kuorodhesha vituo, ni kweli kabisa Tabora ina historia ndefu sana ikiwa ni pamoja na hiyo aliyoisema ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliweza kusoma katika Mkoa ule na mambo mengine mengi na mimi mwenyewe nimefika katika yale maeneo, nimetembelea na nimeyaona. Kwa hiyo orodha tuliyonayo ni kubwa na tutaendelea kuifanyia kazi, kuiuhisha ili tuweze kuongeza mapato yatokanayo na utalii katika Mkoa huu wa Tabora.