Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Silafu Jumbe Maufi (12 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii. Kwa kuwa siku ya leo ni siku yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuipata nafasi hii ya kuwawakilisha akina mama wanawake wa Mkoa wa Rukwa. Mwenyezi Mungu, nakushukuru sana.
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, awali ya yote, napenda kuwakumbusha kuhusu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli. Kwa kweli hotuba ile ilikuwa ni hotuba ambayo imesheheni kila upande wa Tanzania hii na kila Jimbo la Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba niwakumbushe ndugu zangu wa Chama cha Mapinduzi kwamba, daima mtoto huwa anapiga madongo ya kila aina kwenye mti wenye matunda au mti wenye neema kwao. Mtoto hawezi kutupa madongo yoyote kwenye mti ambao hauna kitu. Kwa hiyo, haya madongo tunayoyapata kutoka upande wa pili, ni ashirio tosha kwamba mti wa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake imefanya kazi. Hivyo sasa tunahitajika tukaze buti ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, katika hotuba ya Rais iliweza kugusa kila eneo ambalo kwa namna moja au nyingine limegusia hatua ambazo zinahitajika kufikiwa kwa wananchi wetu wa Tanzania. Sasa basi, kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshabainisha nini ambacho anachotakiwa kufanya kwa wananchi wa Tanzania ili waweze kupata uchumi wa kati; kwa hiyo, hatuna budi kumuunga mkono na kuifanya kazi hii ili iwe na maendeleo kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Ndugu zangu, leo tuna shughuli ya kuzungumzia juu ya Mpango wetu wa kazi ambayo tunahitajika kuifanya ndani ya mwaka 2016/2017. Mpango huu ni mzuri, ni Mpango ambao umeainisha nini ambacho Chama cha Mapinduzi imesema itafanya ndani ya miaka yake mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, Mpango huu umeona tatizo ni nini? Mbona maendeleo yetu hayakamiliki? Imebainika kwamba tatizo ni mapato. Sasa Serikali imeelekeza kukusanya mapato na hatimaye kuyarejesha mapato hayo kwa wananchi kwa maendeleo yao. Hilo ni jambo zuri na tunaomba tuliunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulizungumzia suala la afya. Tuliamua ndani ya Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010/2015 kuweka zahanati katika vijiji vyote na kazi hiyo wananchi wameweza kuunga mkono na kujenga hizo zahanati. Tatizo, zahanati hizi haziko katika ramani inayofahamika, kila kijiji wamejaribu kutengeneza zahanati kufuatana na nguvu ya mapato waliyokuwanayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake tumepata tatizo kubwa katika zahanati hizi kwa sababu eneo la kujifungulia limewekwa karibu na eneo la OPD, limewekwa karibu na eneo ambalo watu wa kawaida wanasubiri madaktari, ndipo palipo na chumba cha kuweka akina mama waende kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri wa Wizara inayohusika, kazi ile ya kujifungua akina mama wana kazi pevu na bora iwe usiku kuliko ikiwa mchana. Mifano tunayo, zahanati ya Kisumba, kwa kweli ile ramani siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba katika Mpango wetu uainishe dhahiri nini watafanya katika suala zima la kuhakikisha wanatembelea ama wanaweka mpango mkakati wa kuhakikisha ramani zilizotengenezwa hivi sasa ziboreshwe ili akina mama tupate eneo la kuifadhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, zahanati nyingi hazina vitanda vya kuzalia, hakuna vyumba vya kupumzikia, kwa maana ya kwamba hakuna vitanda vya kupumzikia. Tunaomba tupate vitanda hivyo. Siyo hilo tu ndani ya afya, zahanati zetu nyingi hazina umeme. Pamoja na kwamba kuna umeme wa REA, lakini bado hawajaunganisha kwenye zahanati zetu. Solar zilizopo zimeharibika na hakuna mtu tena wa kutengeneza zile solar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuunganishwe na umeme wa REA, katika zahanati zetu zote. Siyo hilo tu, maji hakuna kwenye zahanati zetu. Tunaomba Mpango Mkakati wa kuhakikisha kwamba zahanati zetu zinapata huduma ili akina mama waweze kujihifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu suala la elimu. Tumeamua kuboresha elimu yetu na iwe elimu bora, lakini kuna maeneo ambayo tumeanza kuweka utaratibu wa watoto wetu waweze kujifunza teknolojia ya kisasa, kwa maana ya kwamba wamepeleka computers katika shule zetu za sekondari. Naomba mipango iwekwe ya kutosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza, mfano Sekondari, darasa lina watoto 40, lakini kuna mikondo miwili; na mikondo hiyo miwili ni watoto 80, zinapelekwa computer 10 ambazo hazitoshelezi. Naomba tuliangalie hilo katika utaratibu. Mifano tunayo, pale Sumbawanga kuna shule za sekondari za Kizito na Mazu wana computer 10 na watoto wako 80, watafanya nini wakati wa mitihani yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni barabara. Maendeleo ya huduma za jamii katika Mikoa ya pembezoni tumekuwa nyuma. Mimi nasikitishwa sana ninaposikia wenzetu wenye barabara, wanaongezewa barabara za juu, wanaongezewa barabara ziwe sita, wapite barabara watu sita. Kwa kweli mimi nasikitishwa sana kwa suala hilo. Maadamu tumeamua kwanza tuunganishe Wilaya, tuunganishe Mikoa, zoezi hili ndugu zangu bado halijakamilika. Sasa kama halijakamilika, huyu aliyekamilika kuongezwa na katika Wilaya zake zimeunganika, Mikoa ya jirani ameunganika; nchi za jirani ameunganika; kwa nini aongezewe tena mradi wa barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuelekeze Mkoa wa Rukwa. Hatujaungana na Katavi, hatujaungana na Kigoma wala na Tabora. Nawaomba ndugu zangu, huo Mpango uje ukionyesha mikakati, tunajitengeneza vipi kuhusu hizi barabara kuweza kuunganika? Vilevile Mkoa wa Rukwa, tumeungana na nchi ya Zambia barabara haijakamilika, nchi ya Zaire bado barabara haijakamilika. Tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji, tuna mradi mkubwa sana pale Mkoa wa Rukwa karibia shilingi bilioni 30, lakini mradi ule bado haujakamilika, bado pale mjini watu wanahangaika na maji; bado vijijini vya jirani vinahangaika na maji, tuanomba Mpango unaokuja, huo mwezi wa tatu, uwe umekamilika ili na sisi tuweze kupata maji katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ardhi, tunaomba wataalam wa upimaji wa vijiji, hawapo wa kutosheleza na hata vifaa vyake havipo vya kutosheleza. Tunaomba tuhesabu ili tuweze kukamilisha.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kiasi katika suala zima la bajeti hii iliyowasilishwa asubuhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa shukurani za dhati na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Vile vile nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nisipompongeza Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi wanayoifanya, nasema big up. Pia napenda kutoa shukrani za dhati kwa akinamama wa Mkoa wa Rukwa walioniwezesha kuingia katika jengo hili na kuweza kuwazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati za Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika kutambua na kujipanga na kuona kwamba wanahitaji kufanya nini katika kukinga na kuyaboresha mazingira ya nchi yetu ili iweze kuwa katika maendeleo ya wananchi kwa ujumla, nawapongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyeketi, napenda kuzungumzia suala la mazingira na hasa katika Mkoa wetu wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa kwa maana ya jina la Mkoa wa Rukwa imetokana na Ziwa Rukwa tulilonalo. Ziwa hili linaanza kupoteza kina cha Ziwa lile kutokana na maporomoko ya mito inayotoka milimani kuanzia Mlima Liambaliamfipa mpaka milima inayozunguka ziwa lile; kuna mito mingi mno ambayo inatiririka kiasi cha kuchukua udongo na kujaza katika lile ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu Wizara imejipanga vipi katika kulinusuru ziwa hili lisiweze kupotea na Mkoa wetu wa Rukwa ukakosa kupata jina. Naomba Serikali ifikirie namna ya kuweza kuyakinga haya maji kwa namna moja au nyingine yakaweza kutusaidia katika suala zima la umwagiliaji au Serikali iweze kukinga maji haya wakayaweka mahali ambapo wanaweza wakafanya utaratibu wa kuyasambaza na kuya-treat, hatimaye kuyasambaza kwa wananchi wetu na kupata maji safi na salama. Kwa kufanya hivyo, itakuwa imewasaidia akinamama wangu wa sehemu ya Bonde la Rukwa kupata maji kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linapelekea hili Ziwa letu kuwa na kina kifupi ni mifugo mingi iliyoko katika Bonde la Rukwa. Bonde la Rukwa lina mifugo mingi na mifugo mingine ni kwamba wakati wa mnada wa Namanyere kupeleka ng‟ombe Mbeya ni lazima watapita barabara ya bondeni na barabara ile ni barabara ya vumbi inayotoka Nyamanyere hadi Kibaoni, Kibaoni mpaka Mtowisa, Mtowisa –Ilemba, Ilemba - Kilyamatundu hadi kufikia Kipeta na hatimaye kuondoka kuingia Chunya - Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ng‟ombe wale wanaweka tifutifu, wakati wa mvua, lile tifutifu ambalo ni udongo unachukuliwa na maji na kupelekwa katika Ziwa Rukwa. Sasa Wizara ina mpango gani wa kushauriana na Wizara husika kuhakikisha barabara ile ya kutoka kibaoni hadi Kilyamatundu kuelekea Kamsamba iwe ni ya lami badala ya kuwa ya vumbi ili isiendelee kujaza udongo katika ziwa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu mzima wa mazingira sehemu yetu ile ya Rukwa ni kutokana na akinamama kuingia mle na kukata miti na kuitumia kama nishati. Sasa tunaomba nishati mbadala kwa lile Bonde la Rukwa kwa kuhakikisha kwamba umeme unapatikana. Umeme ukipatikana mama zangu watapata nishati mbadala na hatimaye ile miti itaweza kukua na kuhifadhi mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naweza kuzungumza katika suala zima la mazingira ni suala zima la utafiti. Karibu Wizara zote ambazo nimewahi kuzisikia na ninazoendelea kuzisikia, daima huwa wanaweka utafiti, tathmini, katika sehemu ambazo kwamba zimekwisha piga hatua. Kwa nini wasifanye utafiti na wakafanya tathmini ya maendeleo ya jambo katika Nyanda za Juu Kusini ambapo tuko pembezoni tumechelewa kwa kila kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa utafiti uelekee upande wa Nyanda za Juu Kusini ili na sisi tuwe makini, tuweze kuelewa nini elimu ya mazingira, tunatakiwa kufanya nini kuhusiana na mazingira yetu na sisi tusije tukawa jangwa kama mikoa mingine ambayo imetajwa ndani ya taarifa hii ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio yaliyokuwa yamekadiriwa katika Wizara hii hayatoshelezi mahitaji. Hayatoshelezi mahitaji kwa nini? Kwa sababu suala la mazingira ni suala pevu na ni suala pana ambalo kila Wizara ikitamkwa humu ndani, maendeleo yake huhitaji mazingira yake yawe ni bora zaidi. Sasa suala la mazingira ni suala pana ambalo linahitaji kuwa na bajeti kubwa ya kutosha. Mheshimiwa Waziri Januari sitaona ajabu kabla ya mwisho wa mwaka ukaomba tukuongezee bajeti ya utekelezaji wako. Sasa naomba, Serikali ione uwezekano wa kuiboresha hii bajeti ili iongezeke, tuweze kupata uhakika wa kuweza kuiendeleza vizuri Wizara yetu hii ya Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Wizara hii ya Mazingira katika wilaya zetu na mikoa yetu hawa watu hawaonekani kutokana na kazi nzito iliyoko ya Mazingira. Nawaomba tuongezewe idadi ya watumishi ili watumishi hao waweze kujigawa kuweza kutoa elimu kwa wananchi wetu kuhusu suala zima la mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na hawa wataalam, ni vema wakatengewa fungu la kutosha kupata elimu ndani na nje ya nchi ili waweze kwenda na nyakati zinavyoweza kusomeka katika suala zima la mabadiliko ya tabianchi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kupewa taarifa rasmi na Mheshimiwa Waziri mhusika hasa kuhusu kuhakikisha kwamba Ziwa letu la Rukwa linakingwa na linaweza kuboreshwa na hatimaye kuwa ziwa zuri na kuweza kuimarika, kwa sababu Ziwa Rukwa lina mamba wengi mno. Suala la Mamba pia ni suala la Maliasili, kwa hiyo tunawaomba muwalinde mamba hawa wasiweze kupotea ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba Mheshimiwa Waziri mhusika aweze kuniambia ni mikakati ipi ambayo imewekwa au anayotarajia kuifanya kuboresha mazingira yanayoanza kupotea katika Nyanda ya Juu Kusini na hususani Mkoa wetu wa Rukwa ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Elimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nguvu kwa kuniwezesha mimi kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati na kumpongeza ndugu yangu Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri ambayo ameanza nayo katika kipindi hiki kifupi na kuleta matumaini kwa wale wanohitaji elimu bora katika nchi hii, ahsante sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kutoa shukrani kwa dada yangu Stella Manyanya Naibu Waziri. Awali ya yote tunamuomba Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema mama yetu mpenzi na mwanga wa milele umwangazie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika suala zima la msingi wa elimu. Elimu ni kila kitu ndugu Waheshimiwa Wabunge, hakuna kitu ambacho kitakachoanzishwa ama kitakachofanyika katika nchi au mahali popote pale pasipokuwa na elimu, kwa hiyo elimu ndio msingi wa maisha yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninapenda kuzungumzia kwenye suala zima la elimu ya awali. Tumeweza kuanzisha madarasa katika shule za msingi madarasa ya awali lakini bahati mbaya walimu husika na kufundisha madarasa yale ya awali hawapo walimu hao na kama wapo hawatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia kwamba, hawapo ni kwa sababu katika shule zetu walimu wakuu wanachukulia sifa ya kumpatia mwalimu kufundisha darasa la awali ni mwalimu ambaye amefundisha kwa muda mrefu au ni mwalimu ambaye amebakiwa na miaka miwili au mitatu ya kustaafu ndio anayoelekezwa kwenda kufundisha watoto wa somo la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hilo sio sahihi, tunaomba Serikali ijipange na ijitoe kuhakikisha ya kwamba inaandaa walimu wa kwenda kufundisha watoto wetu wa madarasa ya awali kwa sababu ndio msingi wa elimu. Bila kuwa na msingi bora ni dhahiri kusema ya kwamba uinuaji wa elimu bora na mafunzo bora katika nchi yetu hautawezekana kwa sababu watoto hawa watakuwa hawajapata msingi bora wa ufundishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Serikali, ninaomba Wizara iweke utaratibu maalum wa kufuatilia kwanza, kufatilia katika shule zetu za msingi kuona ile elimu inayotolewa kwa watoto wetu kama inaafiki ama inaswii katika kuhakikisha kwamba wanapata elimu bora. Hapo ndipo tutakapoonda kwamba kweli tumedhamilia kuinua elimu bora na mafunzo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu watoto wasichana, wasichana ni kwa maana ya kwamba, hao ndio watakaokuwa wakina mama wa kesho kama sio wakina mama wa leo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia ni ujenzi wa mabweni ya shule za sekondari. Ninawaomba Serikali iliweka msukumo wa kujenga sekondari kila kata na tumejenga sekondari kila kata na katika sekondari zile kuna watoto wasichana na watoto wa kiume, lakini hawa watoto wasichana ambao akina mama wa kesho wanakuwa na mitihani walimu wanawapa mimba, wananfunzi wenzao wanawapa mimba, sisi wenyewe wakubwa tunawapa mimba kwahiyo hawa watoto wanakuwa na mtihani mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ione umuhimu wa kukamilisha mabweni ya watoto wasichana katika mashule yetu kuhakikisha kwamba samani zinakuwemo ndani ya mabweni hayo vitanda, magodoro na kadhalika ili kujenga mabweni yale yawe ni rafiki kwa watoto wetu wasichana ili angalau wapunguze ile taratibu ambayo wanaopata mimba ambazo zisizokuwa na wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la hawa akina dada, wale wanaowapa mimba wanapobainika ninawaomba wapatiwe adhabu kali tena kali sana. Kwa sababu wanapunguza muonekano wa wale akina mama katika mafunzo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba ninaiomba Serikali hawa watoto wanaopata mimba ninawaomba wawaandalie fursa muafaka wa kuwawezesha hawa watoto wanapomaliza kujifungua, watoto wabaki wazazi wao, wao waendelee na masomo jamani, hili limekuwa ni kilio cha kila mara sasa limefikia wakati kwa Mama Ndalichako nafasi kwa Mama Manyanya mmepewa ninyi wanawake kwa sababu mnauchungu na watoto.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike, tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike na tunajua ya wazi kwamba, ukimuelimisha mwanamke mmoja umeelimisha jamii nzima. Sasa kwanini tuwapoteze hawa kwa kuweza kuja kuendeleza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweke fursa maalum ya kuhakikisha hawa watoto wa kike wanapomaliza kujifungua watoto wanawaacha nyumbani wao wanaendelea na masomo ili tuweze kupata maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kulizungumzia suala zima la wanasayansi. Tumesema nchi yetu itakuwa ni nchi ya viwanda, tuanze na viwanda vidogo vidogo, lakini hatuwezi kuwa na viwanda endelevu ikiwa hatuna wataalam wa kisayansi, ni lazima tuandae wanasayansi wa kuja kuendesha hivi viwanda vyetu, ili viwanda vyetu visiweze kufa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanyaje basi, tumeanzisha maabara katika shule za sekondari zote, lakini maabara hizi katika mashule yetu yana changamoto, changamoto iliyopo ni walimu wa sayansi hatuna. Vifaa vya sayansi katika maabara yetu havipo na ukiachia Halmashauri uwezo wa kununua vifaa vile ni aghali sana hawawezi Halmashauri kuweza kutekeleza na kuweka katika maabara zote za Sekondari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali natunamuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atuaeleze amejipangaje na uwekaji wa vifaa au samani za maabara katika mashule yetu ili tupate walimu wa kutosha na hatimaye tupate wanasayansi wa kuja kuendeleza viwanda vyetu hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri ni vyema wakaweka utaratibu maalum wa kuweka vivutio kwa walimu hawa wa sayansi, na kuweka vivutio kwa wanafunzi hawa wanaopenda sayansi, vinginevyo tutaweza kupoteza maana ya kuhakikisha kwamba, tunajenga viwanda katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika suala la walimu, walimu wanaokuja katika maeneo yetu kama sisi Mikoa yetu ya pembezoni Mkoa wa Rukwa, kwenda kule vijijini wamekuwa na taratibu za kuja ku-report wakishaingia kwenye payroll wale walimu wana-disappear katika yale maeneo kwa sababu mazingira yale ni mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikuwepo utaratibu na hata na baadhi ya Mikoa walijaribu kuanzisha taratibu hizo za kuwawezesha walimu hawa kwenda kuishi kule mfano Rukwa walianzisa Nyerere Fund ambayo kwamba sasa hivi hai-operate vizuri, lakini vilevile na Serikali wangeweza kuweka package nzuri ya kuhakikisha kwamba huyu mwalimu anapokwenda kule anakwenda katika ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Rukwa walikuwa wanapewa vitanda, magodoro, vyombo na sehemu kidogo ya kwenda kuanzia maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Wizara iweze kuona suala hili ili tuwe na walimu hawa katika shule zetu, katika ukamilifu. Walimu wanafanya kazi moja kubwa mno, sisi sote hapa tusingekuwepo kama kungekuwa hakuna mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi tunachokiomba hii Wizara ya TAMISEMI imepewa mambo mengi mno, kwa sababu changamoto zote za walimu, changamoto za wanafunzi zipo TAMISEMI, lakini wanaolaumiwa ni Wizara ya Elimu, tunaomba hii Wizara ya Elimu ijitegemee kwa sababu ina mambo mengi ya kuweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wameanza Tume ya Walimu lakini bado haitoshelezi mahitaji, tunahitaji elimu iwe na Wizara inayojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenykiti, lingine ni kuhusu na VETA Mkoa wa Rukwa umeanzishwa nadhani ni mwaka 1974 ama ni 75 lakini mpaka hivi leo Mkoa wa Rukwa hatuna VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la saba, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la 12 lakini wanakuwa hawana mahali pa kushika, hawawezi kujiajiri na wala hawawezi kuajiriwa. Kwa hiyo tunaomba katika Bajeti hii ya 2016/2017 katika mipangilio yao wafanye utaratibu wa kuanzisha VETA katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na napenda kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa jitihada na matarajio makubwa ya nchi kuwa na Viwanda na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Watendaji wote walioteuliwa nae, kwa kasi yenye uchungu wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania kwa kuwapatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Madhumuni ya kuanzisha SIDO ni kuwezesha kutoa ushauri na mafunzo kwa vijana wetu wajasiriamali kuboresha uwezo wa kujiajiri kwao. Lakini Mkoa wa Rukwa kuna mapungufu ambayo yamekwamisha utekelezaji wa ufanisi na wenye tija wa SIDO kwa vijana na wajasiriamali wetu.
Majengo yapo, mashine zilizokuwepo hazipo kwa sasa, ambazo zilitoa ajira na mafunzo kutokana na hali hiyo majengo yamepangishwa kwa wafanyabiashara wa mashine za kukoboa mpunga na kusaga unga. Naomba Serikali kufuatilia majengo hayo na kurejesha mashine zilizokuwepo ili kufufua SIDO madhumuni yake kwa vijana na wajasiriamali wengi wao ni kina Mama.
Mapungufu yafanyikayo SIDO-Rukwa, kwa namna watoavyo mafunzo kwa vijana wetu na wajasiriamali kwa kufanya mchango kutoka kwa washiriki hao ndiyo wafanye maandalizi ya mafunzo. Inakatisha tamaa na mafunzo hupatikana kwa wachache. Serikali ipange fungu maalum la kuendesha mafunzo kwani watalamu wapo bila ya kufanya hivyo watakuwa wanapata mishahara bure.
Serikali kuona umuhimu kwa Mkoa wa Rukwa kufufua SIDO kwa kuhakikisha majengo yake yanarejeshewa mashine zake na vijana, akina mama wajasiriamali waweze kufaidika na uwepo na SIDO Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa wapo vijana wa kutosha wanaomaliza elimu ya msingi na Sekondari wanakosa elimu ya kujiajiri, wanajishirikisha kwenye Ujasiriamali pasipo na uwelewa wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo. Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wametenga eneo la kujenga chuo cha VETA lakini hakuna kinachoendelea. Ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kujenga Chuo hiki kwa maslahi ya Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Waziri napenda kupata utaratibu na mikakati ya kufufua SIDO-Rukwa na ujenzi wa VETA-Rukwa katika kutukwamua huku pembezoni ambako hakuna hata viwanda vya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza jitihada za kuendeleza michezo ingawa haijafika mahali inapotakiwa kwani tunaporomoka Kitaifa na Kimataifa kwa sababu vijana wetu hawana maandalizi ya awali na endelevu kwa fani maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo ya michezo haikidhi mahitaji katika kuimarisha miundombinu na mazingira kwa kuleta ufanisi katika michezo. Kwa ujumla bajeti ya Wizara haitoshi, inahitajika kuangaliwa upya mwaka ujao wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuandaa watalaam wa kuwaandaa vijana wetu shuleni kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari. Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya pekee hakitoshi kuandaa watalaam wa kutosha kuwasambaza kwenye shule hapa nchini, ni vema Serikali kuona umuhimu wa kupandisha daraja vituo vya michezo kuwa vyuo vya maendeleo ya michezo kuongeza hao watalaam ili kuinua michezo na Taifa kufahamika duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamishwa kwa nini Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya na vituo vya michezo Arusha na Songea hawakuwekewa makadirio ya mishahara 2016/2017?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhuru wa vyombo vya habari vilivyokithiri hapa nchini kwa upande wa magazeti ambayo baadhi yana poromosha maadili ya vijana wetu, Serikali ni bora kusitisha usajili wa magazeti na kuyafuta yanapobainika kwenda kinyume na maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, umeme ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na ajira kwa wananchi wetu. Bado naendelea kuzungumza kuhusu Mikoa ya Pembezoni kwa kuchelewa kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa tunao umeme wa jenereta unaosaidiana na umeme kutoka Zambia ambao una changamoto zake, naomba Serikali kuona umuhimu wa kutuunganisha na grid ya Taifa kutokea Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la usambazaji wa umeme vijijini huu wa REA, tukaongeze kasi kwa mikakati maalum kuharakisha vijiji vya mipakani kupata umeme huo, Kata zifuatazo Kabwe, Mirando, Kipili, Wampembe, Kala, Kasanga, Wampambwe, Sopa, Katete, Mambwenkoswe. Vilevile vijiji vya Bonde la Rukwa ukizingatia ni wakulima wazuri wa mpunga na alizeti wanahitaji kuwa na mashine za kukoboa mchele na kusindika alizeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kuwa bajeti ya nishati haikidhi mahitaji kwa Mkoa wa Rukwa, baada ya kukamilika kwa barabara ya Tunduma, Sumbawanga ambayo ni mwanzo wa kufunguka Mkoa wa Rukwa. Naomba Serikali kuangalia Mkoa huu kwani unahitaji kupiga hatua kwa maendeleo ya wananchi wake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uteuzi wa Waziri na Naibu Waziri kwa Wizara hii na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwani ni watendaji wenye weledi mkubwa kwa kujituma kwao na kujitoa kwao katika kupatikana utatuzi wa mambo yanayowakera wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuendelea kujipanga na kuandaliwa sheria maalum ya kuwawezesha wawekezaji kutoa mchango wa maendeleo ya huduma za jamii kwenye vijiji vinavyomzunguka hilo liwe mojawapo ya sharti maalum kwa mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinaongezeka ndani ya Wizara hii kwenye maeneo yetu ya vijiji, miji na majiji ni upungufu wa watumishi ukizingatia hadi sasa ni asilimia 24 tu kati ya mahitaji yanayohitajika kuanzia Halmashauri hadi Wizara. Ushauri kwa Serikali ni uwepo uthibitisho wa kuthubutu kuongeza ajira na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na mtandao wa dunia. Angalau kwa asilimia 50 ya watumishi, wanaohitajika tupate ufanisi katika nyanja zote na tuepukane na migogoro iliyokithiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wamekuwa na migogoro ya wawekezaji na vijiji, panaposhindikana kulipwa kwa fidia ndani ya muda wa uthamini, ni vema Serikali kuona mwelekeo wa kuwapimia wawekezaji nje ya maeneo ya wananchi kwani wao wana uwezo wa kuweka huduma zote za jamii, popote watakapowekwa kuliko kuwachanganya wananchi na kuwazorotesha maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu kuliko yote na kuwezesha yote yaliyopangwa kutekelezwa ni kuhakikisha fedha zilizopangwa kutolewa kwa wakati na katika ukamilifu kama Bajeti iliyopangwa na kuidhinishwa na Bunge hasa shilingi 20,000,000,000 kwa miradi ya maendeleo, kwa nini tumekuwa na viporo vingi vya miradi ndani ya nchi yetu ambayo inawadhoofisha wananchi. Ingawa kiasi hicho hakitoshelezi kwa maendeleo ya jumla kwa Wizara hii. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote chini ya Katibu Mkuu wa Wizara katika kipindi kifupi wameweza kufanya kazi ya kuwapa matumaini makubwa wananchi, ingawa matatizo ni mengi kwenye sekta ndani ya Wizara hii. Pamoja na yote tunapaswa kuwa na subira ya kujipanga na kuweka miundombinu ya mikakati ya kusafisha matatizo yaliyopo kwa kuyaweka katika kipaumbele ndani ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatana na hali halisi ya wananchi kuongezeka na ardhi/nchi ipo vilevile ni dhahiri haya mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42 yawezekana yamepotea au kupungukiwa sifa ya kuwa mapori ya akiba au mapori tengefu. Nashauri Serikali kufanya utafiti wa kukagua maeneo hayo na kupata idadi halisi ya uhalisia uliopo sasa na tupatiwe idadi na orodha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu tunaitumia wananchi katika shughuli mbalimbali na kuendelea kupungua kutokana na ukosefu wa nishati mbadala na kusababisha baadhi ya watumishi wa maliasili kuwa wasumbufu kwa wananchi wetu. Mazao ya misitu yamekuwa yanawanufaisha wachache na kukosesha mapato kwa Serikali. Ni vyema tukaweka mkakati wezeshi wa kupunguza usumbufu wa tozo zinazoingiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA inajitahidi katika kujenga mahusiano mazuri na wananchi wetu, nashauri badala ya makusanyo yote kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu, ni vyema wakabakiwa na hata asilimia 30 ili kuboresha shughuli wazifanyazo kwa wananchi wanaozunguka maeneo yao ya huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii una mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa. Mkoa wa Rukwa una vivutio kadhaa, mfano, Kalambo Falls. Tunahitaji vivutio vipitishwe na kutambuliwa na kufanyiwa matangazo, huku miundombinu ya kufikia kwenye eneo inafanyiwa kazi. Barabara ya kiwango cha lami (Matai – Kisumba – Mpombwe (Kapozwa) – Kalambo Falls) kwani eneo hilo linatumiwa zaidi na utalii wa Zambia kuliko Tanzania wenye eneo kubwa linalovutia katika kuyaona maporomoko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuona umuhimu wa kukuza utalii wa Nyanda za Juu Kusini (Rukwa), kubadilisha mwelekeo wa Mashariki na Kaskazini. Nchi hii pande zote kuna vivutio vya utalii. Naomba Waziri atuthibitishie vivutio vyetu vitatambuliwa lini ili watalii wafike na tuongeze Pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha na kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU JUMBE MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza jitihada ya kazi nzito ifanyikayo katika kuendeleza, kuilinda na kujenga hasa mahusiano nchi za nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki. Waziri na jopo lake kwa kazi yenye matumaini kwa nchi yetu ya uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Serikali kuona upya namna ya kujipanga na kuweka bajeti yenye tija hasa katika kuwezesha ujenzi wa mahusiano wa nchi za nje, kwa kupata wataalam wa kuwajengea uwezo vijana wetu na kusimama wenyewe na hata upatikanaji wa Wawekezaji mahiri ambao wakitumia malighafi zilizopo na wanapoondoka viwanda vyetu kuendelea kuzalisha, yaani tuweze kubakiwa na viwanda mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuona umuhimu wa kuweka msukumo wa kusimamia ongezeko la bajeti kuwezesha nchi yetu kupiga hatua sasa ya kuwajenga vijana wetu, kwa kukiwezesha Chuo cha Kidiplomasia kwa kuongeza idadi ya udahili, tukifahamu kuwa chuo hiki Tanzania ni kimoja tu hivyo kipanuliwe au kuwa na branch kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi za Mabalozi wetu huko nje, kuendelea kupanga na makazi ya Mabalozi, ni suala la kuangaliwa upya, madamu tunazo Taasisi na Mifuko ya Jamii inaonesha uwezo wa ujenzi wa majengo makubwa,
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
222
kwani hawawezi kupewa ukandarasi wa ujenzi wa majengo hayo. Ni lini sasa Serikali itayafanyia kazi na kuondokana na utaratibu wa upangaji huko nje, kwani wao kwetu wanajenga?
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa wananchi katika kusafiri kwenda nchi za nje, kuna urasimu sana, kuliko wanaoingia nchini na sasa idadi yao inatisha na wote wanakuwa ni wafanyabiashara na wawekezaji na baadhi yao kuwa wahalifu nchini. Serikali inalazimika kuongeza nguvu zaidi ya kiusalama katika maeneo yote na kudhibiti hii hali ya mwingiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kutoa shukrani kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipatia afya njema na leo hii kuweza kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kuzungumza haya nitakayozungumza muda si mrefu. Nakutakia kila la kheri, Mwenyezi Mungu akupatie afya njema, akupatie wepesi kutokana na kazi nzito unayoifanya. Ujue ya kwamba tunakuombea na tunaendelea kukuombea upate afya hiyo mpaka mwisho wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu bajeti ya Serikali. Nadhani wataalam tuliokuwa nao waliweza kujifunza katika kipindi kilichopita cha Awamu ya Nne na kufuatana na kasi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuhitaji kuweka asilimia 40 ya fedha kwenye maendeleo ya wananchi wake basi itawekwa msingi madhubuti kuweza kumhakikishia Rais huyu kusimama kwa miguu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya nimeona kila Mbunge anayesimama hapa hayuko rafiki na bajeti hii, sijui hii Wizara haikuwa makini kufikiria na kuona hii kasi ya Mheshimiwa Rais itakwendaje ama itaanzaanza vipi katika kuhakikisha kwamba asilimia 40 inapatikana na maendeleo ya wananchi yanapatikana. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu Wizara hii imekwenda tofauti na Kamati ya Bajeti jinsi ilivyotoa mapendekezo yake, hii inaashiria wazi kwamba Wizara haikuona umuhimu wa Kamati hii kufanya kazi kwa niaba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nastaajabu kwa nini ameileta bajeti hii kwetu na sisi Wabunge wenzetu walikataa mapendekezo yao? Kama kweli aliona thamani ya Wabunge kwamba lazima wapitishe bajeti hii basi angehakikisha mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yanazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala la afya. Tunafahamu wazi kabisa kwamba afya ya mtoto mama ndiye anayesimamia siyo hilo tu mama ndiye anayesimamia hata malezi ya baba. Baba akiugua ndani ya nyumba mama ndiye mwajibikaji wa kuhakikisha afya ya baba inakuwa katika usalama na hali kadhalika ya mtoto. Sasa mama huyu tunamwekea mazingira ambayo siyo mazuri kwake, tunaendelea kumuongezea mzigo juu ya mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia nini? Nazungumzia zahanati. Ukichukulia mfano wa Wilaya ya Sumbawanga Mjini kuna kata saba zinazozunguka mji ule lakini hazina kituo cha afya, zina zahanati lakini baadhi ya zahanati kwenye vijiji ni maboma ambayo bado hayajakamilika. Halafu Waziri wa Fedha anasema hakuna fedha ambazo zimewekwa kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizi, kwa ajili ya kukamilisha vituo hivi ili huyu mwanamama awe na huduma ya afya karibu na yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Wizara hii kwa sababu inafahamu wazi kanuni sijui sheria ya 106 inayosema kwamba sisi kama Bunge hatuwezi kubadilisha kifungu chochote labda ndiyo maana amekuwa na kichwa cha kusema kwamba hata wakisema hayawezi kubadilika kwa wakati huu. Sisi tunasema ni vyema Wizara ikawa na ushauri mzuri ama ikawa na maelekezo mazuri na kutukubali sisi Wabunge kama ndiyo tunaosimamia Serikali katika kuiongoza nchi hii. Waziri akienda kinyume na ukweli huo hatakuwa rafiki wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kama amekosea kipindi hiki tunaomba kipindi kinachokuja aje na fungu maalum la kuhakikisha miundombinu ya zahanati, miundombinu ya vituo vya afya inakamilika kwa maana ya theater ili akina mama waweze kufanyiwa upasuaji wakati wa zoezi la kuongeza idadi ya wananchi wa Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu shilingi milioni 50 kwa vijiji ambapo shilingi bilioni 59 zimetengwa. Imesemwa hapa kwamba hazitasambazwa nchi nzima bali watachukua maeneo maalum kama pilot program. Mimi nasema Mheshimiwa Rais alisema ni kwa nchi nzima leo hii tukisema tunachukua baadhi ya mikoa iwe ndiyo shamba darasa la hizi shilingi milioni 50 ndani ya vijiji vyao tutakuwa hatujawatendea haki wengine. Ushauri wangu kama ni kutafuta mashamba darasa ya kuona hii shilingi milioni 50 itakwendaje basi ni vyema hizi shilingi bilioni 59 zigawanywe ili kila Jimbo waweze kupata vijiji viwili ama vijiji vitatu viwe ni pilot program katika maeneo hayo ili na wale ambao wanawazunguka waweze kujifunza nini makosa ya wenzao kuliko ukisema kwamba pilot program inakuwa Tanga mimi niko Rukwa wapi na wapi? Tunaomba tuweke kwa kila Jimbo ili tuweze kupata pilot area ya kujifunza sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la asilimia 10 halikuweza kutekelezeka kwa sababu ndani ya Kamati ya Bajeti ama Kamati ya Fedha ya Halmashauri hakuna anayelizungumzia wala hakuna anayelifuatilia wala hakuna mwenye uchungu nalo. Kwa nini? Ni kwa sababu Wabunge wa Viti Maalum ama Waheshimiwa Madiwani wa Viti Maalum kwenye ile Kamati hawamo na ndiyo wenye uchungu na vijana na akina mama wenzao. Naomba Wizara inayohusika isiwe na kigugumizi itoe tamko rasmi kwamba hawa Madiwani wa Viti Maalum na Waheshimiwa Wabunge waingie kwenye Kamati ya Fedha za Halmashauri wakazungumzie na kufuatilia asilimia yao 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya bajeti yetu tumesema Wizara ya Utalii ndiyo ambayo inaleta fedha za kutosha takribani asilimia 25 lakini mazingira yanayotengenezwa kwa huu utalii si rafiki. Badala ya kupata zaidi ya asilimia 25 ni dhahiri katika kipindi kifupi tutapata chini ya asilimia 25 na kwa maana hiyo uchumi wetu utaanguka. Nasema hivyo kwa sababu wenzetu wa Kenya katika bajeti ya mwaka 2016/2017 wametenga shilingi bilioni 90 sisi tumeweka shilingi bilioni 135 lakini si kwa utalii peke yake ni pamoja na Maliasili na Utalii. Kama wakigawana pasu hawa kila mmoja anapata shilingi bilioni 67.
Hii saa inasema uongo sasa. Naomba kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naunga mkono Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018, pamoja na kutofahamishwa rasmi mafanikio na upungufu wa utekelezaji wa mwaka 2016/2017 hadi sasa ili kutupa picha kwa mapendekezo ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka asilimia 40 ya bajeti kwa maendeleo lakini hadi sasa fedha hizo hazijafika kwenye Halmashauri zetu na kupelekea kuzorota kwa utekelezaji wa maendeleo kwenye huduma za jamii kama afya, maji na umeme. Nashauri katika kipindi hiki, kabla ya kufika mwaka 2017/2018, kuboresha mwenendo wa usambazaji wa fedha za maendeleo kwa angalau asilimia 75 kwa miradi ya maji, afya na umeme kwani huduma hizi zinawagusa wananchi wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kusonga mbele na kuendelea kuweka mazingira ya malalamiko kwa baadhi ya viongozi na wananchi kwa maendeleo yao kiuchumi, nashauri Serikali kujikita zaidi kujenga mikakati ya kufufua mazingira bora ya kilimo, biashara na fursa za ajira binafsi kwa vijana wetu. Pia kuwepo na uratibu wa malalamiko na kuyapanga kwa utekelezaji ili kuepusha malalamiko kujirejea ndani ya mipango yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mapendekezo haya ya Mpango wa mwaka 2017/2018.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika suala zima katika suala zima la Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuendelea kumwombea heri na baraka na apate wepesi Mheshimiwa Spika wetu, afya yake iendelee kuwa njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Ardhi, kwa Waziri mwenyewe, Naibu Waziri na Kaimu Kamishna Mkuu ambaye ni Mthamini Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzito waliyoifanya na kukubaliana kwamba sasa ni wakati muafaka wa sheria hii kuweza kuletwa katika Bunge hili ili kuweza kujadiliwa na hatimaye kupitishwa ili iweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 52 cha uhalali wa uthamini wa masuala kwa wananchi wetu ilikuwa ni kazi nzito sana na ikajenga kero miongoni wa wananchi, lakini kwa sasa kutokana na speed aliyonayo Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wakifuata speed ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ni dhahiri kusema kwamba sheria hii itaweza kuwa-push na kuifanya kazi yao katika ukamilifu tunaouhitaji na unaotarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la ulipaji wa fidia. Hili suala la ulipaji wa fidia ndani ya miaka miwili na ulipaji wa ribandani ya miezi sita litaweza kutoa ufafanuzi mzuri kwa wananchi wetu na kuleta muafaka wa kuweza kuona kwamba Serikali yao ni kweli ni Serikali ya wanyonge. Hili suala la thamani; uthamini ulikuwa ukifanyika toka huko awali, ulikuwa upo, lakini walikuwa wamechanganywa pamoja na ma-surveyor. Sasa hivi hii sheria itakuwa ni ma-valuer peke yao ambao watakuwa wanaitumia kwa maana ya kuweka ufanisi na weledi katika kazi yao ya uthamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninachoomba na ninaamini ya kwamba katika taarifa hiyo uliyotuletea ni dhahiri kusema kwamba Wizara imekubaliana na mapendekezo ya Kamati ya kuzungumza kwamba huyu Mthamini Mkuu awe huru. Hapa imethibitisha wazi ya kwamba ni huru kwa sababu atateua wenzie wa kumsaidia kazi kwenye eneo la kanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Sheria hii ni nzuri, ninaiomba Serikali katika kifungu cha 5 kinachuhusu kuteua Wathamini Wasaidizi, ni vyema suala hili likafanyiwa kazi na hizo sifa ni sahihi kwa sababu hao Wathamini wapo tokea awali isipokuwa Bodi ndiyo ilikuwa haipo. Sasa Bodi ya Wathamini imepatikana; na katika mchanganuo na ushirikiano uliowekwa kwa kila sekta inayotakiwa katika suala zima la uthamini, wamo katika Bodi. Kwa maana hiyo ndiyo kusema ya kwamba wale Wathamini walioko wa miaka mitano hawatakuwa wazee peke yao, watakuwa ni pamoja na vijana watakaotimiza hivyo vigezo vinavyohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba katika kipengele hiki cha namba 5 kwa utaratibu chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma wangefanya haraka iwezekanavyo kuwateua hawa Wathamini Wakuu Wasaidizi ili Mthamini Mkuu aweze kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima katika Ibara ya 8(1) mpaka (4) ambacho kinapelekea kwamba Wathamini Wasaidizi wa Kanda watakuwepo katika Kanda. Naomba katika uteuzi wa Wathamini hawa, naomba kila Halmashauri ya nchi hii wapate Wathamini angalau wawili, watatu kwa sababu migogoro mingi ambayo imeorodheshwa na Wizara ya Ardhi, iliyopo katika orodha ya migogoro, migogoro mingi iko kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba Wathamini wawepo katika Halmashauri zetu ili wale Wathamini Wakuu Wasaidizi wa Kanda waweze kusaidiana nao katika ile migogoro inayowahusu kutatuliwa mmoja baada ya mwingine; ili migogoro ile ikianza kutatulika ni dhahiri ya kusema kwamba hii miaka miwili ya uthamini kuanzia sasa itakwenda vizuri na hatimaye tutakuwa tumefuta migogoro yote na hatutakuwa tena na migogoro mingine mipya itakayooana ama kushahibiana na ile ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba ni kwamba Sheria hii ya uthamini ni nzuri na kuweza kumpatia Mthamini Mkuu kuweza kuteua Wathamini Wakuu Wasaidizi na Wathamini ambao wataidhinishwa katika maeneo yetu. Hii inamaanisha ya kwamba katika kifungu cha 11(1), kinampa mamlaka ya kuweza kukasimu mamlaka yake, kinampa mamlaka kuteua. Katika kuteua mamlaka ile, anaweza akafikia kutoa agizo la jukumu lake yeye la kusaini hati. Sasa akimtafuta mtu ambaye sio wa ngazi yake itakuwa ni tofauti na sheria ambayo tumeitunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba ni kwamba wale Wathamini Wasaidizi wabakie vilevile kwa sifa zile zile za kifungu cha 5 ili waende sambamba na Mthamini Mkuu na ili atakapowakasimia madaraka ya kazi zake, ziwe zinakwenda kwa mtu muafaka anayehitajika kuifanya kazi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza mafungu hayo matatu, napenda kusema kwamba hii sheria ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba tukubaliane kwamba itatatua matatizo yaliyopo na itafuta kabisa matatizo haya kujirejea tena kwa wananchi wetu. Hivyo, naomba tuiunge mkono kwani speed ya Mheshimiwa Waziri na speed ya Mheshimiwa Rais na speed ya Naibu Waziri katika kutatua matatizo ya hawa wananchi nina imani kabisa ya kwamba itaweza kwisha na sisi tutakuwa tumepumua na hii sheria itatoa pumzi kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile itamuunga mkono Mthamini Mkuu kwa sababu sasa hivi Wizara hii ina Mthamini Kaimu; yaani Kaimu Mthamini Mkuu. Kutokana na hali hii ya sheria hii ya kumpa uhuru wa kufanya kazi hii, nina imani kabisa ya kwamba katika kifungu 52 atakitimiza kwa kazi ngumu hiyo, ataitimiza kwa weledi mkubwa na uaminifu mkubwa ili aweze kujithibitishia yeye mwenyewe kwa Mheshimiwa Rais aweze kumteua na kuwa Mthamini Mkuu wa Serikali katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kabisa kwamba sheria hii imefika wakati muafaka wa kutatua matatizo ya wananchi wetu na kwa hiyo, tuiunge mkono iweze kupita tuondokane na matatizo kwa wananchi wetu, ahsante sana.