Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi (4 total)

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante ka kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa zipo tafiti nyingi muhimu zilizokwishafanyika, ikiwemo tafiti ya uyoga pori kwa matumizi ya chakula, je, Wizara imejipanga vipi kufikisha matokeo ya tafiti hizo kwa wananchi walio wengi, hasa ambao wako vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri anaweza kuahidi nini kwa vyuo vikuu vilivyoko mkoani Iringa kuhusiana na ongezeko la bajeti yao ya tafiti katika mwaka ujao wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Mwamwindi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo haya ya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tafiti inapofikia katika nafasi ya uendelezaji (commercialization) inakutana na changamoto kubwa ya kuendeleza kutokana na kutokuwa na fedha zinazoweza kuondoa utafiti huo katika awamu ya awali na kufikisha katika hatua ambayo sasa inaenda kwenye matumizi. Vilevile Wizara imeliona hilo, lakini pia, hata wanasayansi wengine wa nchi za SADC wameliona hilo na hivi jitihada iliyopo ni kuona kwamba katika kila nchi, fedha za utafiti angalau ziwe ni asilimia moja ya bajeti ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Chuo cha Iringa kwanza niwapongeze kwa hatua mbalimbali wanazozifanya, lakini niwasisitize kuwa wanachotakiwa ni kuandika hayo maandiko mazuri, ili sasa Wizara iweze kutoa kipaumbele katika ku-support bajeti za utafiti za chuo hicho.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Issue siyo kujenga ukuta kuzuia mwingiliano kati ya wananchi wanaokwenda hospitali na magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vikao vya RCC Mkoa wa Iringa, makubaliano na Wizara ya Mambo ya Ndani ilikuwa kupatiwa eneo mbadala ili Hospitali ya Mkoa wa Iringa ambayo sasa ni Hospitali ya Rufaa iweze kupanuliwa. Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilitekeleza agizo la vikao vya RCC, Magereza walipewa eneo mbadala ambalo liko katika eneo la Mlolo na Serikali kuanzia mwaka 1998 na 2000 imelipa fidia kwa wananchi wote waliokuwa wanamiliki eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali, kama Serikali imeshawalipa wananchi fidia na eneo liko pale kubwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhamishia matumizi ya Gereza pale, eneo lile ni dogo, Hospitali ya Rufaa inatakiwa iendelezwe na TANROADS waliokuwepo pale wameshaondoka, wamepisha eneo hilo kwa ajili ya eneo la Hospitali. Ni lini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaondoa Jeshi la Mageraza pale ambapo ni eneo linalowatunza wafungwa pale?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akubaliane na mimi kwamba Mheshimiwa Mwigulu amekuja Iringa ameona hali halisiā€¦
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua, ni lini sasa magereza wataondoa matumizi yao pale na kuachia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokisema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, na sisi kama Wizara tunakubaliana naye kwa asilimia 100 ya mapendekezo yake aliyoyasema. Niweke sawa sawa hivyo, maana yake nilikuwa naona Mheshimiwa Ritta Kabati hapa anajiandaa kusimama; sasa ili alielewe ni kwamba Wizara inaelewa kwamba kati ya hospitali na gereza kinachotakiwa kuondoka pale mjini ni gereza na siyo hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hospitali ile inahitaji upanuzi, Wizara inakubaliana na gereza kuhama pale na kwenda kwenye eneo lingine ambalo na lenyewe liko ndani ya mji lakini pembeni kidogo kilometa kama saba kutoka pale mjini ili kuweza kuwa na nafasi ambayo hata kiusalama itaruhusu mazingira yale kuwa salama zaidi ya kutunza wafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alichojibu Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba wakati jambo hilo halijafanyika, kuna hatua za mpito ambazo tunazifanya zikiwemo hizo za barabara ile kupitika kwa dharura pamoja na masuala ya ukuta aliyoyasemea. Kadri bajeti inavyoruhusu na taratibu nyingine za ndani ya Wizara ya kutumia nguvu kazi inayoendelea, mpango ni huo huo kuhamisha gereza na kuacha fursa kwa Hospitali ya Mkoa kuweza kuwa na nafasi ya kutosha.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Zahanati ya Mangalali imefunguliwa Februari. Zahanati hii ipo katika Kata ya Ulanda na katika vijiji ambavyo bado vinaendelea kupata huduma kutoka kwenye Zahanati ya Kalenga ni Kijiji cha Makongati ambacho kutoka pale Zahanati ya Kalenga pana kilometa karibu 15, lakini pia Zahanati ya Kalenga ipo jirani kabisa na Makumbusho ya Chifu Mkwawa, lakini pia iko karibu kabisa na Barabara Kuu iendayo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, kwa kuwa mpango wa Serikali ni kila Kata kuwa na Kituo cha Afya, je, Serikali iko tayari kuunga mkono jitihada za wananchi wa Kalenga walio tayari kutoa eneo lao na sehemu ya nguvu kazi kwa ajili ya kupatiwa Kituo cha Afya? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeelezea jinsi ambavyo hakuna uwezekano wa kuongeza majengo katika Zahanati ya Kalenga kutokana na eneo lile kwamba lina makazi na tayari yameshapimwa kiasi kwamba uwezekano wa kutoa compensation Halmashauri haina uwezo huo.
Mhesimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza niungane na Mbunge kwa kumpongeza kwa jinsi ambavyo anapigania suala la kuhakikisha wananchi wanapata afya iliyo bora, lakini pia na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Mgimwa kwa jitihada zake. Kwa taarifa nilizopata ni kwamba mpaka sasa hivi ameshachangia mabati 100 na mifuko 80 ya saruji ili kuhakikisha kwamba Kituo cha Afya kinajengwa Kalenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba Vituo vya Afya vingi vinajengwa ili kupunguza msongamano ambao unajitokeza katika
Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwani kutoka Kalenga kwenda Iringa ni kilometa 15 na pale kuna lami kiasi kwamba wananchi wana option ya kwenda hata kule, lakini lengo ni kuhakikisha kwamba wanapata huduma kwa urahisi zaidi.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mahitaji ni walimu 17, kwa sasa wapo walimu 7, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha ikama ya walimu inakamilika katika Shule ya Msingi Kipela? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, watumishi wasio walimu wapo 7, mahitaji ya shule ile ni watumishi 13. Je, Serikali haioni wakati sasa umefika wa kuhakikisha idadi ya watumishi wasio walimu inakamilika kutokana na uhitaji wa shule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainabu Mwamwindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mwamwindi kwa jinsi ambavyo amekuwa akiwapigania wananchi wake wa Mkoa wa Iringa katika kuhakikisha kwamba wanapata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kutaka kujua Serikali ina mkakati gani, kwanza naomba nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wote kwa sababu umeshatoka Waraka kutoka Ofisi ya Rai, TAMISEMI ukiwataka Wakurugenzi wahakikishe kwamba wale walimu ambao wamejifunza elimu maalum wanapelekwa kufundisha katika shule maalum kwa sababu wana ujuzi nao. Kwa hiyo, ndani ya Mkoa wa Iringa na maeneo jirani ni vizuri Wakurugenzi wakahakikisha stock inachukuliwa ili wale walimu wote ambao wana ujuzi maalum waweze kupelekwa kabla huo mkakati wa pili wa ajira haujatekelezwa kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na upungufu wa watumishi ambao siyo wa taaluma ya elimu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatikana kwa mujibu wa ikama lakini pia itategemea bajeti itakavyoruhusu.