Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zaynab Matitu Vulu (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kwa ruksa yako, niwashukuru wapiga kura wote wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Mheshimiwa Rais wewe endelea na kuchapa kazi kama kaulimbiu yako ulioitoa ya “Hapa Kazi Tu” haya maneno ya humu ndani ni sawa na wimbi la baharini, Waswahili sisi kule baharini tunasema wimbi la nyuma halimsumbui wala halimkeri mvuvi, kwa hiyo ya nyuma yamepita sisi tusonge mbele, tuchape kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye mpango ambao tunao mbele yetu. Mpango huu unauzungumzia ujenzi wa uchumi. Nianze kwa kuipongeza Serikali kuwa na uamuzi wa kufanya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na chekechea yake lakini nitoe msisitizo tunaposema elimu bure tusaidie kutengeneza mazingira bora. Kwenye Mpango haikugusa maeneo ambayo yatamfanya Mwalimu, yatamsaidia Mwalimu kuweza kufanya kazi zake kwa amani zaidi ya hivi sasa anavyofanya. Majengo, Nyumba za Walimu, miundombinu na mambo mengine yale muhimu kwa ajili ya kuendeleza elimu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo itakayotusaidia kuinua uchumi wetu na hasa huo uchumi wa viwanda tunaouzungumzia. Kuna masomo ya sanaa na masomo ya sayansi, tunapozungumzia masomo ya sayansi ndipo tutakapopata wataalam wa viwanda, sasa hivi tujikite katika kujenga vyuo vya VETA, kupeleka wanafunzi wengi, ili waweze kuajiriwa maeneo mbalimbali katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ni vipi Mpango umemuangalia mwanamke katika kuinua uchumi wa viwanda, ni vipi mwanamke atashirikishwa, ni vipi umeme utaweza kusaidia kwenda kijijini ili mwanamke au gesi itakavyoweza kusaidia inayotoka Mtwara ifike mpaka kijijini ili mwanamke yule apungukiwe na mzigo wa kutafuta kuni, apungukiwe na mzigo wa kuhangaika na mambo mengine, aweze kwenda kushiriki katika kazi za kuinua uchumi katika, katika kuajiriwa kwenye viwanda, hata kuweza kuwa na viwanda vyao wenyewe wanawake kama Serikali ilivyotuwezesha kuwa na Benki yetu ya Wanawake kuwa na Benki ya Kilimo. Hayo ndiyo mambo ninayoomba mimi, huu Mpango uangalie na uende ukarekebishe tuone hayo yatafanywaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kumkomboa mwanamke aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi, tuangalie na mazingira ya mtoto wa kike toka anasoma chekechea. Watu wamegusia suala la maji humu ndani, maji ni msingi unaoweza kuleta maendeleo katika nyanja zote, lakini maji hayo kama hayatofika kila mahali na kwa wakati, kuna udumazi wa maendeleo utakaotokea na kuwanyima wengine haki ya kuweza kwenda kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa maana kwamba tunahitaji uvunaji wa maji mashuleni, uwezo wa kuchimba visima kama water table iko chini sana basi itengenezwe miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Mahitaji ya maji ya mtoto wa kike au ya mwanamke ni makubwa zaidi ya wanaume, tunahitaji watoto wa kike wawekewe utaratibu, wanapewa pesa za kuwasaidia lakini wawekewe na utaratibu wa kupewa mataulo ya kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa wa Jimbo la Ludewa Mjini aliyeguswa na maendeleo na mahitaji makubwa ya mtoto wa kike. Nakushukuru sana na nakupongeza, wanawake wote tunasema tuko pamoja na wewe na tumekutaja leo kwenye vikao vyetu tutakushirikisha ili uone tutasaidiaje watoto wa kike katika kuleta maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kutoa misaada. Mtoto wa kike anaweza asiende siku saba shule, yuko nyumbani, mama anahitaji maji zaidi ya baba, anahitaji ndoo tatu, nne kwa siku. Leo hii kama mama hapati maji ya kutosha hawezi kwenda kushiriki kwenye uchumi, kwa hiyo suala la maji ni suala la kuwekea msisitizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la gesi. Naipongeza Serikali kwa juhudi iliyofanya, gesi inatoka Mtwara imefika Dar es Salaam mpango haukueleza, katika Mkoa wetu wa Pwani inapoanzia Rufiji watu watanufaika vipi! Tunahitaji gesi ile ipate manufaa Wilaya ya Rufiji, Wilaya ya Mkuranga, Wilaya ya Kisarawe, Wilaya za Kibaha, Bagamoyo, ambako pia nako kuna uwezekano pamoja na Mkuranga kupata gesi tuone tutafaidika vipi, viwanda vingapi tumeandaliwa kuletewa, gesi imekuja, tunawaambia watu wasikate mkaa, watu wamezoea kukata mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam yote inalishwa mkaa unaotoka Pwani, sasa Mpango huu unaelezaje, gesi hii imeandaliwa vipi na Serikali ili wale wakataji wa mkaa waweze kunufaika na biashara yao wakaacha, misitu yetu ikarudi pale pale. Sasa hivi misitu imekuwa kama vipara, eeh unakwenda unakuta pembeni kuna miti lakini ukienda katikati miti hakuna. Mama anahangaika kutafuta kuni asubuhi mpaka jioni. Watani zangu kule Usukumani miti yote imekwisha matokeo yake wanatumia mavi ya ng‟ombe. Kwa hiyo, niwaombe, ufanywe utaratibu Serikali ihakikishe gesi na umeme inafika kwa watu wote ili kuleta maendeleo ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wangu mniwie radhi nasema ukweli wa maisha. Niseme kwamba suala la maendeleo katika Wilaya ya Mkoa wa Pwani, naomba tuliangalie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Rufiji. Rufiji watu wameanza ujasiriamali, wanachonga vitanda lakini ushuru wa kitanda ni laki moja na ishirini. Huyo muuzaji atanunua hicho kitanda kiasi gani? Ushuru wa mkaa umepanda asilimia moja na kumi na nne, huyo mwananchi anayekata miti na mbao anafanya biashara ya kujisaidia ataendelea vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Nyamwage mpaka Utete na Utete ndiyo kuna hospitali ya Wilaya, tunatarajia watu watolewe Utete wapelekwe kwenye hospitali ya Wilaya Kibaha, barabara mbaya, Wilaya ile ni miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii, mpaka leo hii hatujaiona lami. Tunaomba suala hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika twende Mafia. Kuna barabara inaanza Kilindoni hadi Bweni haina lami, lakini pia Mafia kuna utalii, naomba Serikali kupitia Wizara ya Utalii, hebu ijaribu kuangalia ni vipi watainua wilaya ile na kuifanya wilaya ya kiutalii. Watalii wengi sana wanakwenda, tunashukuru, gati limejengwa tunangoja tishari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuu uwanja wa ndege umejengwa tunasubiri taa ziwekwe, watalii waingie asubuhi na jioni hali kadhalika na wananchi waingie asubuhi na jioni. Hata hivyo, bado tuna tatizo la hospitali zetu, Wilaya zetu za Mkoa wa Pwani, zimepakana na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwenye vituo vya afya na zahanati na hospitali za Wilaya...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge muda wako umekwisha!
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MH. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliyenijalia kusimama hapa na nichukue pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa kwetu, pia wala sitaki kusema neno baya kwa upande wa pili niwapongeze kwa sababu wametupa nafasi na sisi tuweze kuongea, wananchi wajue Serikali yao chini ya Chama cha Mapinduzi imefanya nini na itaendelea kufanya nini. Niseme kwa niaba yenu, niwaambie wale ahsanteni sana, acheni tujimwage kwa raha zetu ndani ya Ukumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia suala la afya. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake ameligusia vizuri sana suala la afya, ukiangalia bila afya bora hakuna ambaye anaweza akafanya kitu chochote, hata humu ndani kama afya zetu zisingekuwa bora tusingeweza kuja humu ndani, hivyo ninampongeza sana kwa kuliona hilo na kwa kulizungumzia lakini naiomba Serikali tusaidiane, tumeambiwa tuhamasishe suala la mfuko wa afya CHF wananchi wamepokea wito kwa nguvu zao zote, tatizo linakuja kwenye utoaji wa dawa. Wanafika kwenye dirisha hawapati dawa, sasa ni wakati muafaka, MSD (Medical Store Department) iwezeshwe vya kutosha, nimpongeze Waziri wa Afya na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini MSD isimamie suala la upelekaji dawa ili watu wapate dawa afya zao ziweze kuimarika na waweze kufanya kazi vizuri. Mtu hawezi kwenda shambani kama afya yake siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo. Bila pembejeo, bila mbegu nzuri hakuna kilimo kitakachoweza kuwa kizuri. Ufunguaji wa milango ya biashara, ukimwezesha Mkulima kuna uhakika wa kutosha, akipata pembejeo, akipata mbegu bora, atalima yeye na atalima kwa ajili ya kuuza nje hata ndani ya nchi, hilo naomba tuliangalie na tulipe kipaumbele chake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka Mkoa wa Pwani. Mkoa wa Pwani tuna mabonde na mito mingi sana, tuna Mto Ruaha, tuna Mto Wami, tuna Mto Rufiji, tuna Mto Ruvu, tuna mambonde mengi sana, tunaomba kilimo cha umwagiliaji kiwekewe mkazo katika mabonde hayo ili wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wakiwezeshwa, wakipewa teknolojia ya umwagiliaji hatutaweza kuwaona tena wanakwenda kucheza pool, tuwawezeshe vijana walime zao ambalo ni jepesi kulima kwenye mabonde, zao la mpunga, zao la nyanya, zao la vitunguu, zao la bamia, mbogamboga hata mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo, naiomba Serikali iweke utaratibu mzuri katika kilimo, pia kutumia maji katika mito yetu na kuweza kufanya zoezi la umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ya mito niliyoitaja mitatu, naiomba Serikali ifikie wakati sasa ule mradi wa Kisemvule uanze kazi mara moja. Mradi ule uko Wilaya ya Mkuranga lakini utakapowezeshwa utawanufaisha hata watu wa Dar es Salaam kama mradi wenyewe unavyosema. Lakini mpaka sasa hivi katika maeneo ya Wilaya ya Kisarawe, Wilaya ya Mkuranga, hata Wilaya ya Kibaha Vijijini na Mjini bado tuna matatizo ya maji, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuwezesha upatinaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha mradi huo wa Kisemvule tuone Serikali imechukua hatua zipi sasa za kuweza kuuwezesha mto Rufiji ufike kwenye maeneo jirani, ufike kwenye Wilaya Mkuranga, ufike Wilaya ya Kisarawe hata Dar es Salaam, maji ya Rufiji yanaweza yakasaidia badala ya kuyaacha maji yale yanakwenda yanaingia baharini hatuoni faida kwa watu wengine. Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutusaidia katika upatikanaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongee Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kauli mbiu yake aliyoitoa ya kwamba Tanzania sasa iwe nchi ya uchumi na viwanda. Kweli huu ndiyo wakati muafaka umefika, Serikali ina wajibu wa kufanya hilo na sisi tunaunga mkono. Kwa kuanzia katika Mkoa wetu wa Pwani pamoja na maeneo mengine viwanda vipo lakini Wilaya ya Mkuranga tayari inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi, ninaiomba Serikali iangalie umuhimu wa kuwasaidia Watanzania kwanza, tuweke mikataba ambayo itakuwa endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwaangalie Watanzania wenye elimu ya kutosha, waweze kupata nafasi kusimamia shughuli za viwanda isiwe vijana wa ajira ndogo ndogo ndiyo waajiriwe katika viwanda vile. Kweli tunasema viwanda ni mkombozi, nimuombe kaka yangu na ndugu Mheshimiwa Mwijage ahakikishe kwamba wale Wawekezaji nazungumzia kwa upande wa Mkuranga sasa hivi ambapo ndiyo tunapokea malalamiko, wanalipwa shilingi 5000 kwa siku, anaingia saa mbili asubuhi, anatoka saa 2 usiku, shilingi 5,000 ukipiga hesabu elfu tano kwa mwezi ni shilingi 150,000, hapa tumemsaidia au tunatumia nguvu zake tu kuwasaidia wale wenye viwanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali iangalie hasa Wizara husika ya ajira ipite kwenye viwanda, ikibidi hata tufuatane naye Waziri husika akaangalie ili aweze kuona hata usalama wa wale wafanyakazi, tunachohitaji viwanda kwa ajili ya ajira, lakini pia vitakavyozalishwa vije kwa Watanzania waweze kununua na pato la nchi liongezeke, lakini tuangalie na maslahi ya Watanzania watakaouwa wameajiriwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mikopo. Suala la mikopo kwa wakulima limeoneka vizuri, lakini naomba kujua je, wavuvi wao wamefikiriwaje? Watajiendelezaje katika uvuvi mdogo mdogo? Tunao wavuvi wa baharini, tuna wavuvi wa kwenye maziwa, pia kuna wavuvi wengine wapo kwenye mito yetu ambayo inatuzunguka katika nchi yetu ya Tanzania.
Ninaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwawezesha wavuvi na kuangalia zile sheria, sheria zinamlindaje mvuvi mdogomdogo pamoja na hata yule mvuvi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kuleta mkopo kuwawezesha wananchi milioni 50 kila kijiji, milioni 50 kila mtaa, ni wazo jema, tulipangie utaratibu mzuri, tuwawezeshe wanawake, tuwawezeshe vijana wetu bila kuwasahau wananume, wako ambao na wao wanahitaji kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nichukue nafsi hii kusema kwamba naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu na tuko tayari Watanzania kufanya kazi kwa kuijenga nchi yetu na kukijenga Chama chetu ahsante sana.(
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku ya leo kujadili hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuunga mkono hoja, naomba nipate maelezo ya kina juu ya juhudi za Serikali kuhusiana na zao la nazi maana ni zaidi ya miaka 10 sasa zao hili limekuwa linapotea kwa kushambuliwa na wadudu mwishowe hufa. Mimi natoka Mkoa wa Pwani ambako sehemu kubwa tunalima zao hili na ndilo linaendesha maisha ya Wanapwani. Zao hilo halihitaji mvua na wala halina matatizo kipindi cha jua. Zao hili huvunwa mara nne kwa mwaka. Kwa taarifa tu, maeneo mengi kwa sasa watu wananunua nazi zinazotoka Mombasa. Kwenye mnazi tunapata samani, mafuta ya kula, kujengea nyumba na maji (madafu) ni kiburudisho na pia hutumika kama tiba mbadala inapobidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na kituo cha utafiti wa zao la nazi pale Mikocheni. Kwa masikitiko sijaona juhudi zozote za kusaidia tiba ya mdudu huyu mharibifu. Pia naomba Serikali iwe na mpango wa kuwasaidia waathirika wa minazi hiyo ama kwa kuwapa zao mbadala au miche mipya ya minazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika Mheshimiwa Waziri na Naibu wake mtalipa Kipaumbele ombi langu na kunipatia majibu stahiki, kwani nimekuwa nauliza jambo hili katika kila bajeti sijapata jibu. Pia naomba mfikirie kuanzisha bodi ya zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la wavuvi hasa wadogo wadogo ambao wanatozwa leseni ambao kipato chao ni kidogo. Naomba Serikali ijiwekeze kwenye viwanda vya samaki ili kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo ambao wanauza samaki kwa wenye viwanda. Wavuvi hawa hupata hasara maana wenye viwanda hushusha bei kila baada ya masaa na mvuvi anapoingia baharini au ziwani hana uhakika wa wingi wa samaki na hao anaowapata huuza kwa bei ndogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za wavuvi wadogo na wakubwa ni vyema zikaagaliwa tena hasa ile ya uvaaji wa vifaa vya kuokolea kwenye kina kirefu cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchomaji wa nyavu za wavuvi nao uangaliwe upya. Ni vema kuzuia uingizaji wa nyavu hizo ili wasiweze kuzipata. Naomba msimamo wa Serikali juu ya suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema, ametujalia na leo tumeiona siku yetu ya Ijumaa, basi azidi kutupa heri na baraka na atuongoze kwa kila jambo lilokuwa na heri na sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbele yetu kuna hoja inayohusu viwanda. Viwanda tunavyovizungumzia tunataka vituletee mabadiliko ambayo tayari Watanzania tulianza kuwanayo katika miaka ya nyuma. Kwenye miaka ya 1970 tulikuwa na viwanda vingi kwenye maeneo mbalimbali. Msimamizi mkuu katika shughuli hizo za viwanda ilikuwa ni NDC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapozungumzia uchumi wa viwanda, nasi Watanzania tuko tayari, tumesema tutaupokea uchumi wa viwanda. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyotuwasilishia; ameyataja maeneo mbalimbali ya Tanzania kwamba tutapata viwanda ikiwemo Mkoa wa Pwani ninakotoka mimi. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kwanza atufufulie viwanda ambavyo vilikuwepo na vimekufa. Viliuzwa kwa watu, iweje mpaka leo hakuna kitu chochote ambacho kimeendelezwa au kimefanyika katika viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hotuba yake ameelezea kwamba kutakuwa na utaratibu wa viwanda ambapo wenye viwanda watashirikiana na wananchi waliokuwepo katika maeneo yale kwa maana ya kuwa wakulima watakaotumia maeneo yale kwa kilimo na vile viwanda vitatumia mazao yale kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai au ushauri kwake, sasa hivi tumeona kuna viwanda vingi nchini, ikiwemo Mkuranga na Bagamoyo, lakini kwa nini jambo hili la kuchukua wakulima wadogo wadogo wanaozalisha mazao yao wasianze sasa hivi tukaona mfano? Hata sisi Wabunge tutakapokuwa tunazungumzia suala la kuhimiza na kushawishi watu kuja kutengeneza viwanda kwa maeneo yetu, tuwe na mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Arusha kuna maeneo wanazalisha maua, lakini pia kuna wakulima wadogo wadogo ambao wanazalisha yale maua, yanauzwa kwenye viwanda, wao wanasaidia zile mbegu na dawa za kuzuia uharibifu wa mazao kwa maana ya maua. Kwa hiyo, naomba na huku kwetu uwezekano wa wakulima wadogo wadogo waweze kununuliwa mazao yao kwa sababu Mkoa wa Pwani, mfano, tuna machungwa mengi, maembe mengi, na matunda ya aina mbalimbali. (Makofi)
Mhshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuthibitisha hilo, msimu wa matunda pita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani uone mazao yanavyoharibika kwa sababu hakuna pa kuyapeleka. Mkulima hasa mwanamke; asilimia 80 ya wanawake ni wakulima wadogo wadogo. Naomba basi uwezekano Serikali kufikiria ni vipi watakwenda kununua mazao hayo kwa wakulima kuwawezesha na wao wainue kipato chao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapozungumzia viwanda, nilizungunguzia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Kwenye viwanda vyetu vilivyokuwepo sasa hivi nchini, vijana wetu wanatumika vibaya sana. Wao wanaajiriwa kwa mshahara mdogo sana, wakati sisi tunatarajia waajiriwe wapate fedha zitakazowaendesha katika maisha yao, lakini kinyume chake wanapewa mshahara wa shilingi 150,000 kwa mwezi. Shilingi 150,000 kwa mwezi anaifanyia nini kijana yule, mama yule, dada yule, kaka yule? Naomba kama tunakwenda kwenye mtindo wa kuwa na viwanda vingi, basi hata mshahara uwekwe kabisa, aambiwe mwekezaji kwamba mshahara wa kima cha chini isiwe shilingi 5,000 kwa siku.
Mhehimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama kutakuwa na uwezekano kwa Serikali yetu ichukue hata vile viwanda ambavyo vilikufa, vikawezeshwa na wakachukuliwa akina mama wakapewa kiwanda kile waendeshe wao. Wako ma-engineer, wako wataalam wa aina mbalimbali, iwe mfano wa kiwanda kile tuone uzalishaji utakotoka pale. Akina mama ni wachapakazi! Sisemi kama wanaume hawafanyi kazi, lakini nasema uchumi wa viwanda umkomboe na mwanamke katika viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema viwanda, tuangalie na mazao tunayoyalima katika maeneo yetu. Mkoa wa Pwani tunalima nyanya nyingi sana, lakini mwisho wa siku tunanunua nyanya za kopo, zinazotoka nje ya nchi, haipendezi! Tuwe na viwanda vyetu, tuwe na nyanya tunazotengeneza wenyewe, tuwe na matunda ya aina mbalimbali ambayo akina mama wanaweza wakatengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie na hotuba ya Wapinzani kwenye ukurasa kama sikukosea ni wa 16, waligusia ahadi ya Mheshimiwa Rais, kwamba aliahidi atajenga kiwanda cha Korosho, Mkuranga na Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie neno moja tu, Waswahili wana msemo wao wanasema hivi, tena hata waimbaji waliimba, “mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waje waone wenyewe.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi toka imetolewa hata miezi sita haijakamilika. Subirini muone kazi itakavyokwenda. Nawaomba himizeni wapiga kura wenu, wananchi wetu, wasimamie uzalishaji wa korosho, wasimamie uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali ili tuweze kuhakikisha viwanda vyetu vitakuwa na malighafi, inayotoka ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nasema ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwa ajenda yake ya uchumi wa viwanda. Watanzania na hasa akina mama, tumesimama imara, tutaifanya kazi katika viwanda vitakavyoletwa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake wa hotuba ya bajeti. Viwanda vidogovidogo vilivyokuwepo kwa tathmini ya mwaka 2012 imeonesha kulitolewa ajira milioni 5.2 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) ambapo ajira hizo zilisaidia kuwezesha familia kujiendesha na kupunguza uzururaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba, kiasi cha shilingi bilioni 81, kilichoombwa kwa mwaka 2016/2017 kinashabihiana na kasi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli cha kutaka kujenga Tanzania ya viwanda kwa sababu asilimia 49.3 ya pesa zote zinaenda kwenye shughuli za maendeleo na asilimia 50.7 iende kwenye matumizi ya kawaida. Ili tuwe na viwanda ambavyo vitazalisha kwa uhakika, suala la miundombinu ya umeme, barabara na reli iwe imeimarika zaidi tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuwepo leo na kuchangia hotuba ya Wizara yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri Mheshimiwa Ramo Makani na watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa na ombi langu kwa Wizara hii ni kwamba naomba Wizara inipe majibu ni lini itaweka utaratibu wa kuzuia wananchi ambao hupata kipato chao kupitia uvuvi kwenye bwawa/mabwawa yaliyopo Selous, lakini Serikali imezuia na hata kufikia kuwaua. Hili ni tatizo naomba ufafanuzi.
Pia Mkoa wa Pwani kumezungukwa na misitu hivyo kwa wale ambao wanafanya biashara ya mbao (kutengeneza samani) hutozwa ushuru mkubwa wa shilingi 120,000 hata kama kitanda au samani ishatumika zaidi ya miaka 20. Naomba kauli ya Serikali lini itapunguza ushuru huo wa samani na mkaa? Naomba majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu iliyopo Mkoa wa Pwani mingi imebaki vichaka kwa kuwa hakuna usimamizi mzuri na kupelekea ukataji hovyo wa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkuranga eneo la Mwandege kuna msitu ambao kwa neno msitu kwa sasa si sahihi kwani ni kichaka na kuficha wahalifu wengi, naiomba Serikali itoe maelekezo au kubadili matumizi ya eneo hilo ili kupendezesha eneo hilo, laa kama hiyo haiwezekani basi uwepo upandaji upya wa miti na ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maelezo ya Serikali na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Niwe miongoni mwa wale ambao watachangia katika jambo lililo mbele yetu ambalo ni Muswada. Muswada huu ni muhimu sana, kwa waandishi wa habari, lakini pia Muswada huu ni muhimu sana, kwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri ameweka historia. Sote tunajua, waandishi wa habari walikuwa wanalitaka jambo hili kwa muda mrefu sana, kiasi ambacho kulianzishwa taasisi zisizo za kiserikali kwa maana ya NGO’s za wanahabari wanawake, za wanahabari wa michezo, za wanahabari wa mazingira, wote hawa walikuwa na lengo moja la kutaka kupata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Muswada umeletwa, niombe Muswada huu uharakishwe kama Mheshimiwa Rais alivyosema na bahati nzuri tunaumaliza leo Jumamosi, kesho unasafirishwa, Jumatatu anaweka saini kazi mbele kwa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, lakini niombe katika yaliyozungumzwa mle niweke msisitizo kwa mambo machache. La kwanza, bodi iwe na uwiano, wanawake watazamwe, kanuni ziharakishwe, kwa sababu ndiyo zitakazosaidia mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa umuhimu wa Muswada huu, ndugu yangu Kubenea hayupa a.k.a Yuda Iskarioti, amezoea kuajiri watu kuwalipa kwa posho ya stori anauogopa Muswada huu. Uharakishwe, wanaonyanyasika na wanaodhalilika, waandishi wa habari ambao hawajawahi kupata mshahara kwa wakati, basi hii sheria itakwenda kuwasismamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ni suala la bima. Tumeshuhudia waandishi wa habari, wanapita katika maeneo mbalimbali hawana bima wanahitaji kupatiwa bima kwa sababu hayo waajiri walikuwa hawayaangalii. Kwa hiyo, nina hakika hili litawasaidia na litawapeleka kwenda kufanya kazi zao vizuri na kwa uadilifu na kwa uangalifu. Napata kigugumizi wanaposema watu wasipatiwe leseni, hivi dereva gani atakayepita na gari barabarani asiwe na leseni, traffic akamwacha, Daktari gani atakayemtibu mgonjwa hana cheti, tumeshuhudia Madaktari feki wangapi wanaokamatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana kwenye tasnia ya habari, kwamba ilikuwa inaachwa nyuma haiangaliwi. Niombe wenzangu mliokuwa humu ndani tuhakikishe tunaupitisha na nawashukuru wale waliotoa historia ndugu yangu Tundu Lissu ametoa historia nzuri sana, wengine tumejifunza mengi, tulikuwa hatuyajui. Baada ya kuchangia yeye akaona atoe historia mdogo wangu na Devota Minja na yeye hali kadhalika. Kwa hiyo, nasema Muswada huu umekuja kwa wakati tuupitishe uweze kufanya kazi kwa urahisi kwa ajili ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.