Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. James Kinyasi Millya (3 total)

MHE. JAMES K. MILLYA aliuliza:-
Madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania tu katika Wilaya ya Simanjiro, tofauti na dunia inavyopotosha kuwa madini hayo yanatoka India na Kenya, ambako huenda Serikali hizo huwapa mitaji wafanyabiashara wao:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia Watanzania wanaofanya biashara ya Tanzanite kwa kuwapatia mitaji ili waweze kushindana na wafanyabiashara wa nje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania tu katika Wilaya ya Simanjiro. Maelezo kwamba yanapatikana sehemu nyingine duniani, ni upotoshwaji mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika kwamba Serikali za India na Kenya zinawasaidia wafanyabiashara wa Tanzanite katika nchi zao kwa kuwapa mitaji ili kufanya biashara na ushindani wa nchi za nje. Lakini Serikali ya Tanzania inawasaidia wafanyabiashara wa madini wakiwemo wa Tanzanite kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kibiashara kwa kuhakikisha kwamba wanakuwa na leseni halali za brokers au dealers ili wafanye biashara zao kihalali kwa kutumia mitaji yao ya kifedha na pia kwa kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Arusha International Conference Center ina mpango wa kujenga jengo katika Jiji la Arusha kwa ajili ya biashara ya madini ambalo litakuwa na miundombinu inayotakiwa kwa ajili ya biashara hiyo. Lengo ni kuwahakikishia wafanyabiashara wa madini wanauza madini yao nchini kwa usalama na uhakika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiandaa maonesho ya madini ya vito nchini maarufu kama Arusha Gem Fair yanayofanyika kila mwaka jijini Arusha. Lengo ni kuwaunganisha wafanyabiashara wa madini nchini pamoja na wale wa Kimataifa ili kujitangaza kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kuwa biashara ya madini inaenda sambamba na shughuli zinazofanywa na wachimbaji wa madini wadogo wadogo. Hivyo, Serikali imekuwa ikiwasaidia wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kuwapatia ruzuku, ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara ilitoa ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 7.2 kwa wachimbaji wadogo. Kadhalika ilitoa ruzuku hiyo kwa watoa huduma migodini, wakiwemo wanaofanya biashara ya Tanzanite.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao hawakukidhi vigezo, wamepewa barua kueleza sababu za kutokidhi vigezo hivyo na wanakaribishwa kuomba ruzuku tena mara watakapopata fedha na kutoa tangazo la kibiashara kwa ajili ya ruzuku ya awamu inayofuata.
MHE. JAMES K. MILLYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza wazo la kuanzisha mradi wa EPZ ambao umetengewa eneo kwenye Mji mdogo wa Mererani ili kuwezesha kuwepo kwa soko la Tanzanite Wilayani Simanjiro ambalo linadhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite na kuwapatia vijana wetu ajira?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Millya Kinyasi, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara umetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 530.87 kwa ajili ya matumizi ya EPZ katika Kijiji cha Kandasikra - Mererani, Wilayani Simanjiro. Pamoja na kwamba juhudi za kutenga eneo hilo zilianza mwaka 2007, bado halikuwa tayari kwa uendelezaji kutokana na taratibu za kuhamisha miliki ya ardhi kuchukua muda mrefu. Taratibu hizo zimekamilika mwezi Julai, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji pia ulichangiwa na kuchelewa kulipwa kwa fidia kwa wananchi sita ambao walikuwa hawajafanyiwa uthamini waliokuwa wanadai jumla ya shilingi milioni 15.05. Mamlaka ya EPZ kupitia Halmashauri ya Simanjiro ilifanikiwa kulipa fedha hizo tarehe 31 Machi, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa eneo hilo lipo huru na hivyo taratibu za uendelezaji, ikiwemo kuandaa mpango kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo (Master Plan) na hatimaye kuanza ujenzi wa miundombinu wezeshi kama barabara, umeme, maji, mifumo ya maji machafu, majengo ya huduma zitafanyika. Maandalizi hayo ya ujenzi wa miundombinu yatafanyika sambamba na uhamasishaji wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwekeza katika eneo hilo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. JAMES K. MILLYA) aliuliza:-
Tangu kuanzishwa kwake Wilaya ya Simanjiro haijawahi kupata maji ya uhakika licha ya ahadi mbalimbali ikiwemo ile ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kuwa Simanjiro itatengewa shilingi bilioni 30 ili kuleta maji kutoka Mto Ruvu hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Orkesumet.
Je, Serikali itatekeleza lini ahadi hiyo ili kuwakomboa wananchi wa Simanjiro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, huyo ni Mbunge wa Simanjiro siyo Mbunge wa Viti Maalum. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, naomba nirudie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) na Mfuko wa Nchi Zinazozalisha Mafuta (OFID) inatekeleza mradi wa maji safi utakaohudumia Mji wa Orkesumet ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Simanjiro. Mradi huu utagharimu dola za Marekani milioni 18.4 ambapo BADEA watatoa dola za Marekani milioni nane, OFID watatoa dola za Marekani milioni nane na mchango wa Serikali kwa mradi huo ni dola za Marekani milioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu umepangwa kutekelezwa katika vipande viwili, yaani lots mbili. Kipande cha kwanza kitahusu ujenzi wa chanzo cha maji kutoka Mto Pangani eneo la Ruvu, mtambo wa kusafisha maji pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka. Makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha kwanza yamewasilishwa BADEA kwa ajili ya kupata kibali yaani no objection cha kutangaza zabuni. Kipande cha pili kinahusu ujenzi wa bomba kuu, matanki ya kuhifadhi maji na mabomba ya usambazaji maji. Kibali cha kutangaza zabuni kimepatikana na taratibu za kutafuta mkandarasi zimekamilika na Wizara inasubiri kibali kwa ajili ya kuanza ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo. Mradi huo utakapokamilika, utahudumia wakazi wapatao 52,000.