Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. James Kinyasi Millya (2 total)

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yasiyoridhisha, ni dhahiri kwamba Serikali haijajipanga kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo. Kinachonisikitisha zaidi, eti Serikali imejipanga kwenye kituo cha madini, kitakachoanzishwa na AICC na Wizara, kijengwe Arusha. Mjini Sri-Lanka, geuda sapphire...

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Sri-Lanka. Kwa kuwa Sri-Lanka imejipanga kwenye geuda sapphire red stone, kwenye Mji wa Ratnapura; Madagascar Afrika, kwa nini Serikali ya Tanzania isijipange kati ya Mererani na Naisinyai, ianzishe kituo hiki ili heshima hii ipewe Simanjiro? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kati ya Disemba na Januari, Wizara ikishirikiana na Jeshi la Polisi, wamewakamata vijana wasio na ajira wa Simanjiro kati ya Mererani na Arusha, wamenyanganywa madini yao, vijana hawa hawajasoma, wanajitafutia maisha. Ni lini Serikali inayojitapa inatafutia vijana ajira, itawasaidia vijana hawa kupata ajira na kutowanyanyasa kwenye nchi yao? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Serikali haijawasaidia wachimbaji wadogo. Kama ingekuwa hivyo, kama kweli wachimbaji wadogo wasingefaidika, kwenye Kikao chao cha Geita, wasingenichagua mimi niwe mlezi wao Kitaifa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ruzuku ya kwanza tuliyoitoa, sisi Wizara ndiyo tuliitafuta, tuliitoa kwa vikundi zaidi ya 10 na kila Kikundi kilipewa ruzuku ya dola 50,000. Awamu ya Pili, tumetoa ruzuku ambayo kiwango cha juu kabisa ni dola 100,000 ambavyo ndiyo Naibu Waziri alikuwa anasema, tumetoa kwenye vikundi 111.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) limefungua desk, wameweka Idara kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Sasa hivi tunavyofanya ni kwamba eneo la wachimbaji wadogo likitengwa (geological survey). Wakala wa jiolojia hapa anaenda kwa gharama ya Serikali, wanafanya utafiti kabla hatujawapatia wachimbaji wadogo maeneo. Kwa hiyo, kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye Tanzanite. Ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge, tumejadili naye na kwa heshima kabisa, nimekusanya watu kesho ofisini na mwenyewe anajua. Namleta Kamishna, naleta watu kutoka Arusha, waje wakae naye kwanza wampe somo la mambo ya biashara ya Tanzanite. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga naye anafahamu hivyo. Mbali na hapo Mheshimiwa Mbunge atakubali kwamba wakati sisi tunatengeneza mambo ya Tanzanite, watu walilalamika wakasema wamejitokeza Watanzania wapewe huo mgodi. Nawe unajua kuanzia jana wananchi wamegoma, hawawataki hawa wawekezaji mliokuwa mnawashabikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kutatua suala la Tanzanite kwa jinsi linavyotatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifano aliyoitoa Mheshimiwa Mbunge ya Sri-Lanka na Madagascar, kwa heshima zote siyo kweli. Kwa sababu mimi nimeenda Madagascar mara nyingi sana; na nilikuwa nashughulikia gem stones za Madagascar na Sri-Lanka. Ukienda Madagascar utakuta badala ya vijana kuuza karanga na njugu, wao wanauza gemstones wamezichonga, wameweka kwenye kama viberiti. Huko labda ndiko tutakapokwenda. (Kicheko/Makofi)
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Ni masikitiko makubwa kwamba kwa miaka takribani miwili, shilingi milioni 15 imezuia kuanzishwa kwa EPZ iliyotarajiwa na Serikali. Mwanzoni mwa mwaka huu mwezi wa Pili, kilo mbili za Tanzanite, kilo mbili Waheshimiwa Wabunge ni takribani bilioni mbili, siyo kama gold, zilikuwa zinaibiwa kutoroshwa nje ya nchi…
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mafupi mawili ya nyongeza. Wahindi hawa wanaoshirikiana na baadhi ya Watanzania waliolelewa na Wahindi walikuwa wanatorosha madini ya Tanzanite nje ya nchi, je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwamba EPZ hii itaanza kujengwa Simanjiro ili madini yetu yasije yakatoroshwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza, Mheshimiwa Rais wakati akifungua Bunge hili alisisitiza kuhusu madini haya, Mheshimiwa Waziri juzi wakati akihitimisha hoja yake alisema kuna matatizo makubwa ya Tanzanite. Naomba nitoe takwimu, mwaka 2014…
MWENYEKITI: Tafadhali, swali tu, hakuna takwimu. Naomba kama umemaliza Mheshimiwa Waziri ajibu.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali; mwaka 2014, dola za Kimarekani milioni 300 za Tanzanite zilitoroshwa India, Kenya milioni 100, lakini Tanzania ikauza milioni 38, je, ni lini Serikali ya Tanzania itakuwa makini ili kuwasaidia Watanzania kunufaika na madini yao, na wachimbaji wadogo kama akina Chusa, wachimbaji wadogo kama akina Onee watanufaika na rasilimali hii kubwa waliyopewa na Mungu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuligeuza eneo la Mererani Special Economic Zone na mojawapo ya kuweka eneo lile huru la kiuchumi ni kudhibiti ile malighafi au maliasili inayozalishwa pale. Sasa ninachofanya kwa mamlaka niliyopewa, natafuta wawekezaji kama nilivyosema, ili waje pale watengeneze eneo ambako madini yale na madini mengine yatakuwa yanauzwa pale. Tayari ninao wawekezaji watakaobadilisha Mji ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, wamenipa hekta 500, nataka hekta 1000 nyingine zaidi zifike hekta 1,500. Nitatengeneza Special Economic Zone, namwagiza Katibu Mkuu anayeshughulikia uwekezaji wale wawekezaji ambao wanataka kuwekeza Arusha waje Bungeni wafanye demonstration yao ili watu wa Kanda ya Kaskazini muweze kuona wenyewe, niwaachie mzigo ninyi mshindwe kutoa ardhi inayotakiwa.