Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kangi Alphaxard Lugola (15 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mtemi wa Kabila la Wasukuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ya kushauri. Pengine nianze na hili la retention ambalo limezungumzwa na Mbunge aliyepita Mheshimiwa Rwamlaza. Retention kwa mapendekezo ya Serikali ni jambo zuri kwa sababu uzoefu unaonesha sisi ambao tumekuwa tukishughulika na mahesabu ya Serikali, ziko taasisi ambazo wanatumia fedha hizi vibaya. Kwa hiyo, Mpango huu wa Serikali ni mzuri, waendelee nao, isipokuwa Halmashauri zote nchini pamoja na Mifuko ya Hifadhi za Jamii, hao wasiwekwe kwenye kundi la kupeleka fedha kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, waendelee kubaki na makusanyo. Bahati nzuri Mheshimiwa Rwamlaza tuko Kamati moja nadhani kule tutaendelea kushauriana vizuri ili Halmashauri zetu zisije zika-suffocate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la kilimo. Iko mikoa ambayo kila mwaka inakumbwa na njaa na haipungui mikoa 12 lakini kwenye Mipango yetu hapa sijaona mipango mahsusi na ya makusudi ya kuhakikisha kwamba mikoa hii wanaiwekea miundombinu ya umwagiliaji. Mikoa mingi upande wa Kanda ya Ziwa tuna maji ya uhakika, tunahitaji miundombinu ya umwagiliaji, tumechoka kuletewa chakula kila mwaka. Labda tuambizane hapa kwamba mikoa ile ambayo inakuwa na njaa kila mwaka tumeitelekeza na kwamba tutaendelea na Kamati za Maafa ili tuwe tunaendelea kuwapelekea tani za chakula ilhali wao ndiyo wamebahatika kuwa na maji ya uhakika, wanaweza wakamwagilia na tukapata chakula tukajitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano pale Bunda tayari eneo la EPZ limetengwa zaidi ya hekari 1,350. Naishauri Serikali kwenye Mpango huu, hebu sasa mikoa ile ya Kanda ya Ziwa kwa kuanza na maeneo hayo ya EPZ watuwekee miundombinu ya umwagiliaji ili tusiendelee kuombaomba chakula. Kila mmoja hapa anajua madhara ya njaa, watu wenye njaa hawatawaliki, watu wenye njaa hawatulii na watu wenye njaa hawawezi wakashiriki kwenye maendeleo ya huu Mpango tunaouweka hapa. Utashirikije kwenye maendeleo wakati una njaa? Wakati mwingine hatutulii humu ndani, hakuna amani na utulivu kwa sababu watu wana njaa za aina mbalimbali humu. Wengine wana njaa ya pesa, wengine wana njaa ya kushika madaraka, huwezi kutulia humu ndani, ni mifano ya njaa ukiwa na njaa huwezi kutulia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la reli. Kwenye Mpango huu nishauri jambo moja na hii itakuwa ni hatari kwa Serikali. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukurasa wa 12 ameelekeza kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam - Rwanda na kwa kwenye Mpango Serikali inasema itajenga reli ya kati kwa standard gauge. Sasa kitendo cha kunyamaza au cha kuwa na kigugumizi sijui kimetoka wapi cha kutotaja reli yetu ya kati ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na michepuko yake ya kwenda Kalema kwenda Msongati, michepuko ya kwenda Mwanza na baadaye twende Dutwa kule kwa ajili ya nickel. Serikali inaweza kutumia uchochoro huo na kwa sababu wanamshauri vibaya Mheshimiwa Rais, kama wameweza kutaja michepuko ya kutoka Mtwara kwenda Liganga na Mchuchuma, michepuko ya reli kutoka Tanga kwenda Arusha na Musoma na michepuko ya Minjingu na Engaruka kuna kigugumizi gani cha kutotaja reli ya kati kwamba ndiyo inayoenda kujengwa kwa standard gauge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango huu kuna eneo la kukarabati reli ya kati. Kwa hiyo, tunaweza kukuta ule mtandao wetu wa reli ya kati ukaishiwa kukarabatiwa halafu tusiwe na standard gauge matokeo yake wanampelekea Rais Kagame. Nani asiyejua Kagame anatamani Bandari ya Dar es Salaam? Nani asiyejua Kagame aliwahi kusema akipewa mwezi mmoja atakusanya fedha za Bandari ya Dar es Salaam kuendesha Rwanda kwa mwaka mzima? Nani asiyejua Kagame alianzisha UKAWA ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakamtenga Rais wetu ili waweze kujenga reli ya Mombasa mpaka Rwanda na sasa wanavuka Naivasha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye utalii. Tunahitaji kuinua pato la Taifa na ili tuliinue ni lazima tushughulike na ujangili ambao unatishia wanyamapori na ujangili unaotishia watalii kuja Tanzania.
Naomba Mheshimiwa Maghembe haya mambo ya kuandika humu kwamba tunataka kuboresha miundombinu, kununua zana za kupambana na majangili, mpaka sasa zana za kupambana na majangili unazo, tulikuwa na helkopta juzi majangili wameitungua, hizo ndizo zana za kupambana na majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama majangili wameanza kutungua ndege ambazo ndizo zana za kupambana na majangili maana yake tukiendelea kukupa hizi zana za kupambana na majangili wataendelea kuzitungua. Idara yako ya Wanyamapori na Hifadhi yako ya Ngorongoro ndiko kwenye wafanyakazi wasiowaaminifu kwenye Idara ya Intelejensia ambao wanaazimisha silaha za kivita, wanawapa majangili halafu wanatungua ndege. Waheshimiwa Wabunge, hizi ndege zinaendelea kuanguka kwenye hifadhi hata ile ya Marehemu Filikunjombe ilianguka kwenye Hifadhi ya Selous. Kwa nini nisiamini kwamba inawezekana kwa sababu walikuwa kwenye Hifadhi ya Selous ambako ujangili wa tembo ni mkubwa, ni majangili hawa hawa waliangusha ndege ya Mheshimiwa Filikunjombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje ninyi katika kuajiri askari wa wanyamapori na kwenye Kikosi cha Intelejensia hamuwa-vet? Watu wengine wamefukuzwa polisi ndiyo hao mnawachukua, mnawachukua kwa sababu ya ubinamu, ujomba na mwingine ameshiriki kuangusha ndege ya Rubani Gower, maskini Mungu aiweke roho yake mahali pema. Mtu huyu ameajiriwa wakati alifukuzwa ni mhalifu, ni jambazi matokeo yake ameshiriki kwenye tukio hili.
Mheshimiwa Maghembe unafanya kazi gani na yule Mhifadhi pale ambaye ndiye anashughulika na ajira za watu wa namna hii? Tutaendelea kuwa na majangili hata ukileta zana za kupambana nao kama wafanyakazi wa Idara yako hautawa-vet na kuwasimamia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja. Mpango huu ni mzuri sana na katika uzuri wake ndiyo maana tunaomba kuendelea na mapendekezo haya ili Serikali ije na rasimu ikiwa inaonesha sasa Mpango huu unatekelezeka. Nakuhakikishia Mpango huu ukirudi jinsi ulivyo mkadharau mapendekezo ya Wabunge hautatekelezeka, zitabaki ni hadithi, zitabaki ni porojo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kutaja maeneo ambayo reli yetu inaenda kujengwa kwa standard gauge kwa kisingizio kwamba hamuwezi kutaja kila kitu, kama hamuwezi kutaja kila kitu mbona maeneo mengine mmetaja? Kama mtakuja hapa bila mwelekeo wa reli ya kati, nitakuwa mtu wa kwanza kusema kwamba rasimu hii hatuikubali, nitakuwa mtu wa kwanza kutokubaliana na bajeti ya kupitisha mpango ambao hauna dhamira nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule pembezoni Kanda ya Ziwa mfuko mmoja wa simenti shilingi 20,000 wakati Dar es Salaam ni shilingi 12,000, Watanzania hawa watajenga lini nyumba? Misumari, nondo, gharama za usafirishaji zinakuwa kubwa lakini tunaendelea kupiga chenga zaidi ya miaka 15. Hayo makelele yenu mliyonayo huko kwenye mambo ya tender, sisi hatutaki vurugu zenu huko, endeleeni kukaa vizuri, tunachotaka ni kujenga reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taarifa, reli hii Waheshimiwa Wabunge…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Ahsante sana Mtemi wa Wasukuma. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia kwenye bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza mtumbua majipu Rais wa nchi yetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo ameonesha kwa vitendo na kwa kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake aliyosema kwamba Ikulu ni mahali patakatifu, Ikulu haiwezi kugeuzwa kuwa pango la walanguzi. Ndiyo maana kwa ushupavu kabisa na bila kupepesa macho aliamua kumtumbua Katibu Mkuu Kiongozi ambaye alikuwa Ikulu mahali ambapo ni patakatifu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Kilimo na Naibu wake wanafanya kazi nzuri, ni wachapakazi hodari na ndiyo maana kukiwa na tatizo kwa wakulima Mheshimiwa Mwigulu huyo na Naibu wake, kukiwa na tatizo kwa wavuvi, Mheshimiwa Mwigulu huyo na Naibu wake, kukiwa na tatizo la mifugo Mheshimiwa Mwigulu huyo na Naibu wake. Mheshimiwa Mwigulu tutaendelea kukupa support katika Bunge hili ili uweze kushughulika na Wizara hii nyeti, Wizara ambayo asilimia 80 ya Watanzania wanaitegemea katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbiu yako inasema kwamba kama tunaitaka mali tutaipata shambani. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hatuwezi tukapata mali shambani kama Wizara yako hautatumbua majipu ambayo yameota sehemu nyeti na Wizara yako ni sehemu nyeti. Kama Kanuni zinaruhusu, kuna majipu nje pale uyaruhusu yaingie humu ndani yaulize kila Mbunge ni mahali gani ya wote kwenye mwili wake, hakuna Mbunge atakayekubali jipu limuote sehemu nyeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana gani? Mheshimwia Rais ametumbua jipu la watumishi hewa, Mheshimiwa Mwigulu Wizara ya Kilimo kama Wizara nyeti ina wakulima hewa na wakulima hewa hawa ni jipu ambalo inabidi ulitumbue. Jimboni kwangu na nchi nzima hizi voucher za pembejeo ni jipu la wakulima, wanasajili wakulima hewa, wanasajili wengine wamekufa halafu wanalipa fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimboni kwangu kwenye kata moja ya Namhula, voucher za pembejeo zenye thamani ya shilingi 46,320,000 wamewapa wakulima ambao hawapo. Kuna mmoja anaitwa Belita Mnyabwilo yuko Kayenze Mwanza wamemuandika Mwibara kule Mkoa wa Mara kwamba ni mkulima wakati siyo kweli. Kuna Mangasa Mfungo na mdogo wake Ally Mfungo wako Kata nyingine ya Chitengule wameorodheshwa kwenye Kata ya Namhula. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba tumbua jipu la wakulima hewa vinginevyo hatutapata mali shambani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jipu lingine la kutumbua Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni la mbegu za pamba zisizoota aina ya quton. Ukiangalia jedwali ukurasa wa 23 wa hotuba ya bajeti, zao la pamba limeshuka mwaka hadi mwaka na sababu kubwa ni mbegu ya quton, mbegu ya kampuni ya mwekezaji fake. Wabunge tumepiga kelele kwenye Bodi ya Pamba wanamkumbatia, hili ni jipu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ikiwezekana ukitoka hapa ukatumbue jipu hili la Kampuni hii ya Quton. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jipu lingine ni la viwanda vya samaki. Wavuvi wanaokwenda kuuza samaki kiwandani, wakifika pale wamefoleni msururu wa magari saa nne, ina bei yake, saa tano bei inashuka, saa sita bei inashuka mpaka kuja kufika saa 12 Wahindi wenye viwanda wanaendelea kushusha bei kwa wavuvi hawa.
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba nenda Mwanza pale ukastukize viwanda hivi utaona kilio cha wavuvi wanapunjwa bei, samaki kwa sababu wanaoza wanakosa mahali pa kupeleka. Majipu haya yako sehemu nyeti ya Wizara hii nenda uyatumbue Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mbolea. Kama kweli Serikali imekuwa committed kwamba itakuwa Serikali ya viwanda na katika nchi yetu tayari tuna Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu, kwa nini Serikali isikitazame kiwanda hiki kwa jicho la huruma kuhakikisha kwamba wanajengewa uwezo wa kuzalisha mbolea kwa wingi ambayo ita-stabilize soko la mbolea na tutaweza kuagiza mbolea kidogo sana kutoka nchi za nje na hatutahitaji dola nyingi za kimarekani. Mheshimiwa Waziri, wewe ni mchapakazi, nenda pale Minjingu angalia matatizo yao, viwanda ambavyo tayari vipo tuanze kuvijengea uwezo hivi kabla hatujajenga vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la leseni za uvuvi. Wavuvi hawa wakilipa leseni leo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda samaki wanahama wanakimbilia Wilaya ya Busega wavuvi wanawafuata wakifika Busega wanatozwa fedha za leseni nyingine. Samaki wanakimbia wanaenda Ilemela kwa Mheshimiwa Angeline Mabula wanatozwa fedha za leseni kwamba wako Halmashauri nyingine. Samaki wanaogopa upepo siyo rafiki wanakimbilia Ukerewe wakifika kule wanatozwa fedha za leseni. Ndani ya wiki moja, wavuvi hawa maskini wanatozwa leseni kwenye Halmashauri zaidi ya tano na ushahidi tunao.
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hili ni jipu lingine, leseni hizi zinatozwa kitaifa. Kwa nini magari yetu unatoka Songea unakwenda Kagera, unakwenda Lindi…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa muda wako ndiyo huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Naomba nianze na mambo haya ili kuweka mambo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao tulibahatika kucheza mpira wa soka, kuna wachezaji wa aina mbili, kuna mchezaji ambaye ana uwezo wa kutumia mguu mmoja tu wa kulia na kuna mchezaji mwingine anatumia miguu yote kulia na kushoto. Kwa wale tunaotazama mpira tunajua siku zote mchezaji anayetumia mguu mmoja tu wa kulia maadui wakishamgundua wakambana wakamfanyia tight making kwenye mguu wa kulia hawezi akacheza mpira uwanjani, sana sana atatolewa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Kamati ya Kanuni kukaba mguu wa kulia wa hotuba ya Kambi ya Upinzani wameshindwa sasa kutumia mguu wa kushoto na ndiyo maana wamejiondoa na kutoendelea kusoma hotuba yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina mbili ya wazungumzaji, kuna mzungumzaji mwingine ukishamdhibiti kusema uwongo, ukamdhibiti kutoa lugha ya matusi atajitoa kwenye mazungumzo kwa sababu hana uwezo tena wa kuendelea kuongea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana Mheshimiwa Lema kunizulia mambo ambayo mimi sijawahi kuyasema, hii inatokana na kukabwa mguu wa kulia akashindwa namna ya kuendelea kutumia mguu wa kushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili lipo kwa ajili ya Watanzania, kwa ajili ya kutenda haki na ndiyo maana hakuna kiti wala Kamati ya Kanuni iliyozuia Mheshimiwa Lema kutozungumzia jambo la Lugumi, hakuzuiwa ameambiwa arekebishe maneno fulani yeye anasema amezuiwa, hajazuiwa ni kwa sababu anashindwa kuchangia hoja…
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama suala la Lugumi limeongelewa kwenye ukurasa wa 12 na ukurasa wa 13 na Kamati hiyo Mwenyekiti huyo hakuzuiwa na ndiyo ripoti tuliyonayo mezani na hapo ndipo ninapozungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niheshimu busara za kiti chako, niende moja kwa moja..
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa nne wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia majukumu ya msingi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwangu mimi majukumu hayo hayawezi yakafanyika kwa ufanisi endapo hatutakuwa na jeshi lenye nidhamu, endapo hatutakuwa na jeshi lenye makazi bora ya askari, endapo hatutakuwa na askari wenye afya bora, hatutakuwa na askari wenye moral ya kazi, ufanisi ndani ya majukumu haya hautatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie makazi ya askari, sisi ambao tupo kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tumekuwa tukipata fursa ya kukagua na kutembelea nyumba za askari vyombo vyote hivi vya ulinzi na usalama si Magereza, si Uhamiaji, si Zimamoto, si Jeshi la Polisi, makazi yao ni duni. Alichosema Mheshimiwa Kawambwa kwamba ukiingia kwenye makazi ya Polisi, makazi ya Askari Magereza na vyombo vingine vya ulinzi na usalama amesema unaweza ukatoka ukiwa na masikitiko. Ninayo picha hapa nilikutana nayo kwenye gazeti la uhuru tarehe 17 Novemba, 2015 inahusu ukaguzi wa nyumba za askari uliofanywa na Mheshimiwa Waziri Kitwanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, picha hii ambayo nitaileta kwako, utayaona makazi haya ni makazi duni na picha inamwonesha Mheshimiwa Waziri Kitwanga alipokuwa anatoka kwenye nyumba hiyo alishindwa kupita akainama akapindisha mgongo haikutosha ikabidi akunje na miguu ndipo akatoka kwenye nyumba hii. Nyuma yake kuna AGP Mangu analia ametoa na kitambaa mfukoni anapangusa machozi, picha hii inasikitisha sana. Kwa nini AGP ndani ya dakika chache anaingia kwenye nyumba analia? Je, askari ambaye amekaa kwenye nyumba hiyo miezi nenda rudi, miaka nenda rudi, amelia kwa kiwango gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii picha nitaileta kwako uone jinsi ambavyo AGP analia kwa sababu ya uduni wa makazi ya askari. Mheshimiwa Kitwanga kutuambia kwamba kuna fedha za Wachina kujenga nyumba za askari lazima pia tutumie vyanzo vyetu vya ndani tujenge nyumba badala ya kusubiri Wachina. Katika bajeti yakehakuna mahali popote ambapo ametenga fedha za ndani kwa ajili ya kujenga nyumba bora za askari. Ndiyo maana nikasema askari mwenye nidhamu ambaye anatakiwa apatikane kwa urahisi ikitokea dharura ni yule ambaye yupo kwenye nyumba ambazo ni za askari kwenye kituo anachofanyia kazi. Kwa hiyo, kwa stahili hii Wizara ya Mambo ya Ndani itakuwa katika kipindi kigumu sana kama hawatatenga fedha za ndani kwa ajili ya makazi ya askari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la posho ya chakula kwa vyombo vyote hivi vya ulinzi na usalama. Nilishasema hapa kwamba posho hii inayoitwa ya chakula ni posho ya lishe kwa ajili ya kuwatengeneza askari, wanatakiwa wapate lishe. Hii elfu kumi kwa siku ni lishe gani ambayo askari anaweza akabajeti akapata lishe halafu akaweza kuhimili kufanya doria, kufanya kazi zenye shuruba. (Makofi)
Nimeshangaa sana Kamati ilishasema viwango hivi vya posho ya chakula ya lishe iwe inahuishwa kila mwaka, lakini mwaka huu Mheshimiwa Kitwanga ameshindwa kuhuisha posho hizi. Ndiyo maana juzi hapa Waheshimiwa Wabunge getini kwetu hapa askari ambaye ameshindwa kupata lishe bora amevamiwa na mama mmoja akamchoma kisu yule askari kwa kukosa lishe bora, hana nguvu alishindwa kuhimili kumtoa yule mwanamama aliyekuwa amemchoma kisu. Tunalipeleka wapi jeshi hili, Wizara ya Mambo ya Ndani Mheshimiwa Kitwanga angalia lishe ndiyo inawapa moral askari hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye OC bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani imekatwa bilioni nane kutoka ile ya mwaka wa fedha uliopita. Hapa tunasema jeshi lazima liwe na fedha za kutosha OC kwa ajili ya kufanya doria kwenye maziwa, kwenye bahari wakiwa na marine police watu wa Uhamiaji waweze kudhibiti mipaka yote kwa ajili ya doria, wakimbizi waweze kushughulikiwa, magereza waweze kufanya shughuli yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inakuwaje Wizara ya Mambo ya Ndani, fedha za OC mnadhani na zenyewe ni fedha za maandazi, mnadhani ni fedha za soda, za biskuti. Fedha hizi ni kwa ajili ya shughuli za kutoa huduma kwa ajili ya Watanzania. Sasa mnapunguza fedha mpaka zile za kununulia taarifa za wahalifu ambazo ma-RCO wote wanakuwa nazo zikitoka kwa DCI yaani Criminal Investigation Fund, watafanyaje kazi bila fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani, fedha zake za OC zinafanana na fedha za maendeleo kwenye Wizara zingine kwa sababu huduma hizi zinatakiwa zifanyike kila wakati, magari yanahitajika kwenye vyombo vyote, mafuta yanahitajika. Kwa hiyo, msifikiri kwamba OC ni fedha za kukata kata tu kila wakati, wakati kwenye vyombo vya ulinzi na usalama fedha hizi ni sawa na zile ambazo zipo kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la vituo vya polisi. Kadiri siku zinavyokwenda mahitaji makubwa ya vituo vya polisi kwenye nchi yetu yanaongezeka. Ndio maana Jeshi la Polisi walikuwa wana utaratibu wa kujenga vituo vya polisi vya tarafa ili kila tarafa iwe na vituo vya polisi. Hata hivyo, matokeo yake ni nini? Tumekuwa tukisubiri fedha zingine hizi za maendeleo ndipo zikajenge vituo hivi vya tarafa, hatutaweza kuvijenga mpaka tuhakikishe zile fedha ambazo wanazikusanya kwenye maduhuli, Bunge hili liwaruhusu fedha hizi wanapozikusanya wapate ile asilimia ambayo moja kwa moja itakwenda kujenga vituo vya polisi. Vinginevyo tutaendelea kuwalalamikia kwamba uhalifu unatokea polisi ukiwaita hawafiki kwa wakati na hata vile vituo ambavyo vipo maeneo hayo wako kwenye nyumba za kupanga, hawana magari, wengine hawana hata pikipiki, tutaendelea kuwalaumu kama jambo hili hatutalifanya kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie magereza kwenye suala lao lenye mahitaji maalum na ndiyo maana Mheshimiwa Kitwanga katika hili naomba angalau ufungwe siku moja tu ndani ya magereza yetu ili uweze kuona jinsi wafungwa na mahabusu na hawa mahabusu nadhani kuna wakati itabidi tubadilishe sheria kwa sababu ni mahabusu lakini ukienda kule nao wanakula mlo mmoja, ukienda kule na wao mahali pa kujisaidia ni shida. Nimekwenda kule wanakwenda kujisaidia kila mmoja anawaona, tufike mahali Mheshimiwa Kitwanga tusidhani kila mtu aliye…
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru sana kunipa fursa ya kwanza kabisa kuchangia mjadala huu wa Watanzania kuwa na haki ya kupata taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria mama, ndiyo ambayo msingi wa Mtanzania yeyote bila kujali cheo chake, hadhi yake, bila kujali kazi anayoifanya, anayo haki ya Kikatiba ya kupata taarifa. Pia upo msemo wa Kiingereza unaosema information is power. Ili Mtanzania aweze kuwa powerful katika sekta ya kilimo, katika kuzalisha, katika sekta ya uvuvi, katika sekta ya biashara, katika sekta ya utafiti, sekta ya elimu na sekta nyingine zote, lazima awe informed; lazima awe na taarifa mbalimbali zitakazomsaidia yeye katika shughuli ambazo anazifanya hasa shughuli za kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia uhusiano wa wakulima wangu kule Mwibara na wakulima wote nchini na namna ambavyo taarifa zinazohusu kilimo chao, uvuvi wao, ufugaji wao zinavyoweza kuwanufaisha katika maisha yao. Tunayo Taasisi ya Takwimu ya Taifa (Tanzania Bureau of Statistics), Idara hii kwa muda mrefu wamekuwa hawafanyi tafiti zinazohusiana na masuala ya kilimo, uvuvi, ufugaji ili kuweza kukusanya taarifa ambazo zinaweza zikawasaidia wakulima kule vijijni waweze kunufaika na kilimo, uvuvi na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri kwamba badala ya kusema tu kwamba leo tunatunga sheria inayompa haki mwananchi ya kupata taarifa anayoitaka, pengine inahusu masoko au kilimo au ufugaji, sheria hii pia ingeweka wajibu kwenye hizi taasisi za umma zote ambazo zinapata fedha ili wawe na wajibu ikiwezekana on a monthly or quarterly basis wawe wanatoa taarifa muhimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, magazeti, redio, televisheni, ili wananchi waweze kuwa informed juu ya taarifa mbalimbali ambazo zinaweza zikawasaidia katika kilimo chao kuwa cha tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema tu kwamba mwananchi leo ndio tunamtungia sheria ya yeye kupata habari, lakini taasisi hizi za umma ambazo zinapata fedha lakini hatuziwajibishi kuhakikisha kwamba wanajitokeza kwa wananchi na kuwapa taarifa mbalimbali, sheria hii na yenyewe inaweza isimsaidie mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo lingine ambalo pengine kwenye taarifa ya Kamati walijaribu kuligusia na kwenye sheria yenyewe ya ule muda ambao mhusika wa kutoa taarifa kwa mwananchi anayohitaji, muda wa siku 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi naona ni nyingi, kwa sababu inategemea na taarifa ambayo huyu Mtanzania anaihitaji. Kunaweza kukawa na taarifa ambayo ni very urgent ambayo ingeweza kumsaidia, sasa kama huyu Afisa atajiona kwamba muda alionao ni mwingi anaweza akakaa tu matokeo yake kuja kumpa ile taarifa huyu mwananchi inakuwa imeshapitwa na wakati, anakuwa haihitaji tena. Kwa hiyo, inakuwa ni kama alikuwa anapoteza muda wake.
Kwa hiyo, naomba kwenye sheria hii tungeweka kipengele ambacho pia kinajaribu kuainisha categories za taarifa, ni taarifa gani ambayo inaweza ikachukua muda wa siku 30 au ni taarifa gani ambayo ni very urgent ambayo mwananchi huyu anaihitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna siku moja nilikuwa nahitaji mkopo benki kwa ajili ya kumlipia ada mwanangu na vinginevyo hataweza kusoma, lakini kwa sababu benki wanasema wana siku 15 za ku-process mkopo, na mimi mkopo nilikuwa nauhitaji kwa muda usiozidi siku tano, lakini baada ya wao kuwa wamechukua muda mrefu, nikaenda kukopa kwa mtu binafsi akanipa hela. Baada ya siku 15 ndiyo wakaniambia mkopo wako uko tayari. Nikawaambia mkopo wenu umeshapitwa na wakati. Kipindi ambacho nilikuwa nauhitaji, sasa hivi hauna tija yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri anayehusika ajaribu kuhakikisha kwamba tunaingiza aina za taarifa na tukazitengenezea schedule kwamba taarifa fulani ikiwa kwenye first schedule hii inaweza ikachukua siku fulani, taarifa ambayo ipo kwenye second schedule inaweza ikachukua siku fulani mpaka pengine na kwenye third schedule. Vinginevyo mwananchi atakuwa ametungiwa sheria ya kupata tu haki lakini katika zile siku ambazo mtumishi anajisikia ile taarifa isiweze kumsaidia sana mwananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo lingine ambalo linahusu vyanzo vya taarifa. Ukumbuke hata sisi wanasiasa pia ni vyanzo vya taarifa. Sisi wanasiasa kama Wabunge, ni vyanzo pia vya taarifa. Kama Wabunge pia tunatumia fedha za umma kama taasisi, yaani Mbunge kama taasisi. Wananchi wanaweza kuwa wanahitaji taarifa kutoka kwa Mbunge ama kwenye Ofisi ya Mbunge au kwa Mbunge mwenyewe kupitia mkutano, wanahitaji taarifa ambayo wanaweza wakajua nini kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati sisi Wabunge kama wanasiasa ambao ni vyanzo vya taarifa, utaratibu huu wa sisi Wabunge kuwekewa siku kumi za Jimboni kufanya mikutano, sisi kama wanasiasa ambao ni vyanzo vizuri vya taarifa, siku hizi zinakuwa ni kidogo sana kwa Mbunge kuweza kuzunguka Jimbo zima kwa muda wa siku kumi kwa ajili ya kuwapa taarifa wananchi. Kwa sababu haitakuwa rahisi; wananchi wanamwandikia Mbunge na wenyewe wana-request, Mbunge naye anaambiwa baada ya siku fulani kwa sababu ni taasisi ya umma na anatumia fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri eneo hili pia tuliangalie vizuri. Mbunge kama chanzo cha taarifa; je, anaweza aka-deliver taarifa muhimu kwa wananchi kabla ya kusubiri wananchi wenyewe ndio wa-request kutoka kwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la vyombo vya habari ambavyo ni taasisi binafsi, vingine ni vya Serikali na vyombo vya habari vingine vya Serikali vinapata fedha za umma, magazeti ya Serikali, Daily News, Habari Leo na magazeti mengine ya Uhuru; na sisi kama chama tunapata ruzuku ya Serikali; magazeti mengine ya Tanzania Daima ambayo nayo ni ya chama kingine wanapata ruzuku kuendesha magazeti haya…
MWENYEKITI: Mjadala uelekeze kwa kiti.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Ndiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa anadhani anafukuza mapepo kwa mtu aliyepandwa na mapepo. Hatuko Kanisani hapa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia vyombo vya habari na nikawa najaribu tu kuvitolea mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vyombo vya habari ambavyo vinapata fedha, najaribu kumshauri Mheshimiwa Waziri anayehusika kwamba vyombo hivi pia kuna haja ya kuviwekea wajibu, kwa kuwa ni vyombo vinavyopata fedha zikiwemo na televisheni za Serikali kama TBC ambazo zinapata fedha; kwamba wafike mahali wawajibike kutoa taarifa kwa wananchi, wawe ni wakulima, wawe ni wavuvi, kuhusu vipindi mbalimbali; kwa mfano zamani kulikuwa na kilimo cha kisasa, masuala ya masoko yako wapi, badala ya kuviacha vyombo hivi vikawa vinaweka Mabango ya Chereko, maharusi sijui vitu gani na vinatumia fedha za umma badala ya kurusha taarifa ambazo zinawahusu wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata magazeti pia yasiachwe yakawa yanaandika habari nyingi ambazo zinahusu mambo ambayo hayawasaidii sana wananchi wanaposoma kuwa informed ili waweze kutumia taarifa hizi katika shughuli zao za uzalishaji. Wanakuwa na mambo mengi mno, hasa hasa ya siasa ndiyo wanaweka front page; leo akitokea mwanasiasa tu pale kaenda pale mfano Mheshimiwa Mrema, au kaenda pale sijui Mheshimiwa Mbowe, akisema tu jambo, utakuta magazeti haya ambayo ndiyo yanapata fedha za umma, front page yanaruka na vichwa vya habari juu ya hao watu; badala ya kuruka na taarifa zinazozungumzia kwamba mwananchi fulani kule Mwibara ameibiwa nyavu zake, majambazi wamepora mashine ili wananchi hawa taarifa hizi ziweze kufika kwa wanaohusika ili wazifuatilie na kuzifanyia kazi.
Sasa tukiacha hali hii ikaendelea bila sheria hii kuvibana vyombo hivi, matokeo yake vitakuwa ni vyombo vinavyotoa taarifa kwa wananchi ambazo haziwasaidii sana, ni vyombo vya kifedha zaidi kwamba wakiweka hii kwenye front page ndiyo wanaweza wakauza magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, vyombo vya habari kama redio na magazeti ni vyombo muhimu sana kwa wananchi na kuna redio nyingi siku hizi zinaanzishwa kule vijijini, Wilayani; sasa redio kama hizi inabidi Serikali izisaidie sana kwa sababu unakuta Redio ya Taifa au redio hizi nyingine binafsi ambazo wanarusha matangazo, matangazo haya hayafiki kule kwa wananchi.
Kwa hiyo, redio hizi ambazo wanawekeza kule Wilayani au vijijini, redio hizi wazisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi hapa niliona mlolongo wa orodha ya redio nyingi zimefungwa, zimeondolewa kwa kisingizo kwamba wengine hawalipi kodi, kwa kisingizio kwamba wengine wameenda kinyume na ethics za utangazaji. Sasa kitendo hiki kinawafanya wananchi wetu vijijini wanaotegemea vyombo hivi kutopata habari na matokeo yake watu wa mjini ndio ambao wanaweza waka-access kwenye hizi taarifa ambazo wao huzipata kupitia vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri sana Mheshimiwa Nape. Mimi nilikuwa shabiki sana wa redio hii inaitwa Magic FM ya akina Salum Mkambala sijui na watu gani wale wana sauti nzuri za bass zile. Sasa ghafla juzi juzi hapa nikaona umeweka gate valve pale. Mheshimiwa Waziri hebu vyombo hivi uvitazame vizuri, vyombo hivi vinatusaidia sana na wanapokuwa wanachambua taarifa zao wanasaidia sana Watanzania kuelewa, ni wachambuzi, wanachambua sana. Kwa hiyo, kama kunakuwa na hizi kasoro nyingine ndogo ndogo Mheshimiwa Nape, ni wa kuwapa maonyo. Siamini kama kuna maonyo ambayo Mheshimiwa Waziri ulishawapa hawa Magic FM, lakini ukawawekea tu gate valve.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge hili, badala ya kuwafungia; ni wachambuzi wazuri sana kama kuna mahali waliteleza, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuwafungulia pengine na kuwapa adhabu ya onyo badala ya kuwafungia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kuja na muswada huu ambao ni mzuri sana ambao nafikiri kwamba haya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yetu pamoja na michango ya Wabunge itaweza kuuboresha zaidi na hatimaye tuwe na sheria nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye lile eneo ambalo pengine wanazungumzia taarifa za kiusalama, nitoe mfano kwenye Jeshi la Polisi. Mwananchi anaweza kuwa amekamtwa yuko ndani, lakini ndugu zake wanakwenda kituoni kufuatilia kujua tu angalau huyu mtu kwa nini amewekwa ndani na sababu ni ipi? Hata hiyo yenyewe wanaweza wakasema kwamba ni nani wewe tukupe taarifa ya huyu ndugu yako kuwa humu ndani? Kwa hiyo, tuangalie taarifa hizi mnazosema za kiusalama, msije mkadhani kwa kuwa Jeshi la Polisi ni suala la usalama, basi hata mtu kupata taarifa ya kwa nini ndugu yake yuko ndani na yenyewe…
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi na mimi kuchangia miswada miwili iliyowasilishwa leo asubuhi. Lakini mimi kwa sababu ya muda ntajikita kwenye Muswada wa Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kama ntapata muda nitaingia kwenye professional ya hawa wakemia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niishukuru Wizara, Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kuona umuhimu na haja ya kuharakisha muswada huu muhimu na kuuleta mbele ya Bunge lako Tukufu.
Lakini pia nimshukuru sana in-charge ambaye ni Mkemia Mkuu wa Serikali na watumishi walio chini yake ambao wamesukuma muswada huu, kwa sababu kwa miaka mingi wamefanya kazi katika mazingira magumu, mazingira ya kudakiadakia sheria nyingine zilizopo halafu wanafanya shughuli zao. Na ndiyo maana kwa mazingira magumu hayo hata vyombo vingine vilivyopo kama Jeshi la Polisi waliokuwa wanamtegemea wanapopeleka sampuli wamepata shida sana, na katika kupata shida hiyo magereza yetu yamekumbwa na wimbi kubwa la msongamano wa mahabusu. Wengine wana kesi za mauaji wana miaka kumi, wengine wana kesi za robbery wana miaka kumi; tatizo ni kwa sababu bado uchunguzi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali haujakamilika. Kwa hiyo mimi nipongeze jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na mazuri yote hayo ninayo mambo ambayo ningependa kuboresha muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na changamoto iliyopo kwenye jina la muswada wenyewe, kwamba ni wa Kuanzisha Mamlaka ya Maabara za Serikali. Sasa jina hili linanifanya nikumbuke kwamba majukumu yaliyoainishwa katika kifungu cha tano, majukumu ambayo yatakuwa ya mamlaka hii hayaendani au hayaendi sambamba na jina ambalo liko kwenye muswada huu. Kwa nini nimesema hivyo, kama hivyo ndivyo kwamba ni Mamlaka ya Maabara za Serikali, mamlaka maana yake ni chombo ambacho kinavisimamia vyombo vingine ambavyo ndivyo vinatenda, kwamba Serikali inazo maabara zake mbalimbali lakini lazima kuwe na chombo chenye mamlaka kwa ajili ya kusimamia vyombo hivyo, na ndiyo maana wana-set standards za vyombo hivyo; standards za wataalamu, standards za vifaa ili waweze kuvifikia kwa ajili ya kuleta ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi ambao ni waumini kuna kitu kinaitwa Mungu Baba, Mungu Mwana, Mungu Roho Mtakatifu. Ukiangalia kifungu cha tano kinasema mamlaka itakuwa maabara ya rufaa. Inakuaje mamlaka hiyo hiyo tena ndiyo iwe maabara, kwa maana kwamba mamlaka ni chombo kinachosimamia maabara chenyewe hicho hicho tena ndicho kina-operate? Kwa hiyo, tayari kunakuwa na conflict of interest, jambo ambalo litaleta ugumu sana katika kutekeleza sheria hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima tukubaliane, ama tunatunga Sheria ya Government Chemist au tunatunga Sheria ya Authority (ya mamlaka). Na ndiyo maana hata juzi tulipitisha sheria hapa ma-valuer, ma-valuer hawa wamo mpaka ma-valuer binafsi ambao wanasimamiwa na chombo ambacho tulikipitisha hapa juzi. Sasa mimi nadhani kwamba Wizara ingekuwa na upana zaidi kwa sababu kutakuwa na maabara za watu wengine ambao wangeweza kutaka ku-invest kwenye masuala ya hizi maabara, sasa itakuwa ni shida sana kuwa accommodated chini ya sheria kama hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna chombo kinaitwa TCRA. TCRA hawawezi wakawa na kampuni ya simu; sisi tuna chombo kinaitwa EWURA, EWURA hao hao hawawezi wakawa na kituo cha mafuta; sisi tuna chombo kinaitwa TCAA (usafiri wa anga) haohao hawawezi wakamiliki ndege waka-operate; tuna TIA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege), haohao hawawezi na wao wakasajili, wakaandikisha viwanja vya watu wengine. Kwa hiyo, lazima mamlaka hii iwe ni mamlaka ambayo ni independent. Na inapokuwa independent tunaipa majukumu ya kumsimamia Chief Government Chemist, kulisimamia Jeshi la Polisi ambalo nalo lina maabara zake maana yake Jeshi la Polisi nao wana DNA, wana forensic pale, awasimamie, pamoja na maabara nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana mimi sijawahi kuona rufaa ya maabara, maabara inakuwa na rufaa sijawahi kuiona. Tukiruhusu maabara kuwa na rufaa hatutakuwa na ufanisi kwenye maabara yoyote. Na ndiyo maana mambo haya ni ya kisayansi. Inakuwaje uende kwenye zahanati ya Bunge kupima malaria unaambiwa negative, unaenda Benjamin Mkapa - UDOM unaambiwa una positive malaria, unaenda General Hospital unaambiwa huna, unakimbia Lacent unaambiwa unayo, kwa kutumia kipimo hichohicho cha darubini, jambo ambalo haliwezekani. Kwa hiyo, tunachotafuta hapa ni kwamba kama tuna darubini iliyoko kwenye maabara zote, darubini hiyohiyo lazima iseme una malaria, lazima iseme huna malaria kwenye darubini zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inakuaje wapeleke mtoto kumpima kama si wa Mheshimiwa Shabiby! Ah, samahani Mheshimiwa Shabiby. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama sio mtoto wake wanabishania wanampeleka kwenye DNA ya Polisi halafu baadaye Mheshimiwa huyu analalamika anasema aah, kumbe maana yake kwa sababu tumetunga sheria hii inaonesha kuwepo maabara ya rufaa wanaenda kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kufika pale DNA inasema huyu mtoto sio wa Mheshimiwa Shabiby, tutaleta machafuko makubwa sana katika nchi hii. Tutaleta machafuko kwa sababu kipimo fulani kinasema ni wa kwako, sikuridhika nikakata rufaa kumbe kuna kingine cha kukata rufaa kinasema huyu sio wa kwako hivi kweli hao watu wataishi katika mazingira gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake lile tatizo huo mgogoro hautaisha kwa sababu kila mmoja anaamini mbona mimi mahali fulani niliambiwa ni wa kwako, na huyu anasema mbona mimi mahali fulani nimeambiwa sio wa kwangu. Lazima tuwe na standards. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, maabara hizi zote ambazo ni za Serikali, ni za wadau hawa ni labaoratory operators. Kwa hiyo, kutegemea na pale sampuli itakapopelekwa maana yake matokeo ya uchunguzi yaliyopo pale ndiyo matokeo kwa sababu mamlaka inayosimamia maabara hizi imejihakikishia kwamba pale kuna wataalam kutokana na standards tulizoweka, pale kuna DNA machine ambayo tumeweka standards, kwa hiyo jambo hili litakuwa handled vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi lilikuwa na kitu kinaitwa modernization. Sasa kama Jeshi la Polisi tumesema liwe la kisasa lina maabara zake za DNA, za forensic, lakini leo humu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuna sheria mbalimbali ambazo unazitunga chini ya sheria hii, ambapo katika hotuba yako umesema kwamba sheria hii haitaleta mgongano, lakini kuna mgongano mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria zao wanayo database yao, wanayo masijala ya kumbukumbu ambapo wanatunza kumbukumbu za wahalifu, lakini kwenye sheria hii unasema wale laboratory operators wapeleke taarifa zao kwa Mkemka Mkuu wa Serikali, tayari sheria hizi zinaanza kugongana. Kuna sheria za ushahidi ambazo zinazungumzia expert opinion, huku nako unasema kuna mambo ya conclusive na finality. Mambo kama haya pia yatakwenda kuleta mgongano mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika nimemsikia mchangiaji mmoja, nadhani ni Mheshimiwa Susan Lyimo, anasema kuna polisi hapa kwenye bodi anakwenda kufanya nini. Polisi hawa ndio wanaohusika na upelelezi wa kesi za jinai katika nchi yetu, na mojawapo ya jukumu la msingi kwenye Jeshi la Polisi ni investigation, na ndiyo maana sasa katika investigation hii ya sayansi ya jinai pamoja na kemia lazima polisi hawa; na ndiyo sababu sheria imemuweka polisi ambaye ana cheo cha juu ambaye ni Inspekta anakwenda juu, ndio maana akienda katika ile Bodi ataleta connection nzuri sana kati ya Jeshi la Polisi ambacho ni chombo pia cha kisheria ambacho kinahusika na makosa ya jinai na wao pia wana maabara zao, kwa hiyo ni kiungo muhimu sana ndiyo maana umeona na watumishi wengine wako pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hizi sampuli ambazo wanasema kwamba zitasimamiwa na Mkemia Mkuu wa Serikali. Jambo hili litakuwa ni gumu sana, lazima hizi maabara zote kuanzia hiyo ya Mkemia Mkuu wa Serikali na hizi nyingine ambazo zote zinatakiwa ziwe chini ya mamlaka moja katika kusajiliwa, lazima kila maabara ipewe uwezo wa kufanya managemet ya sampuli zake, management ya records zake ili mradi katika regulations ambazo wataziweka wanakuwa wame-set standards. Vinginevyo huyu ambaye ni Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo kuna maeneo mengine anatoza fedha kwa maana anafanya biashara, yeye huyo huyo; kwanza anajisajili kwa sheria hii yeye huyo huyo, halafu kuna element ya kufuta wengine, sijui kama atajifuta yeye huyo huyo, ni jambo ambalo halitawezekana. Kwa hiyo, lazima tuziache hizi laboratories nyingine za Serikali ziweze ku-manage sampuli zao, waweze ku-manage na records zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kuna element ya mchunguzi kwenye definition. Kama sheria hii itapita jinsi ilivyo Jeshi la Polisi watapata taabu sana kwa sababu na wao ni wachunguzi, wana maabara zao, lakini kwenye sheria hii imejaribu kumuonesha kwamba yule ambaye atakuwa ni mchunguzi kwa mujibu wa sheria hii ni yule ambaye ameteuliwa au ametangazwa na Mheshimiwa Waziri wa sheria inayohusika ambayo ni Wizara ya Afya; lakini yule Police Officer ambaye yuko kwenye maabara ya polisi, yeye sasa atakosa hadhi ile hata mahakamani wanaweza wakam-question kwamba wewe unatoa hii expert opinion kama nani. Kwa hiyo, lazima sheria hii isije ikaenda ikafifisha upande wa Jeshi la Polisi halafu wakapata taabu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la professionals. Nishukuru sana kwamba sasa tunakwenda kutunga sheria ya professionals. Lakini professionals hawa kwa mujibu wa muswada huu uwajibikaji wao utakuwa wa shida sana kutokana na namna ambavyo Mheshimiwa Waziri anayehusika amekuwa na mamlaka makubwa sana juu ya watu hawa. Kwa hiyo, kule kwenye utumishi wao, kwenye utendaji wao itakuwa ni sekeseke, wengi watakuwa wanafukuzwa, wengi watakuwa wanafutwa kwa sababu sheria hii ambayo tumempa mamlaka watakuwa mahali pa kukimbilia inakuwa ni shida, mara baadaye wakakate rufaa mahakamani. Kwa hiyo mwisho wa siku, sheria hii badala ya kuwa rafiki itatuletea shida sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba pamoja na schedule of amendements ambazo nitaleta, Mheshimiwa Waziri ajaribu kulitafakari jambo hili, jambo hili ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii pia tunasema kwamba inatekelezwa Tanzania Bara, lakini sheria hii iko kwenye Wizara ambayo si ya Muungano, Wizara ya Afya. Sasa mimi nilikuwa najiuliza, Jeshi la Polisi ambalo linafanyakazi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania; Pemba, Unguja, Geita, Musoma pale Mwibara pale kote kule inakwenda kwa sababu ni Wizara ya Muungano. Lakini sheria hii ambayo tunaitunga leo msimamizi wake mkubwa ni Wizara isiyokuwa ya Muungano lazima kwa vyovyote vile nilivyosema kutatokea mgongano mkubwa sana kati ya hizi sheria ambazo chombo cha Jeshi la Polisi kinatumia ikiwemo ile nyingine ambayo mwenzetu amezungumzia, road traffic act, sheria ya ushahidi, Sheria ya Jeshi la Polisi; kwahiyo kutakuwa na shida sana.
Kwa hiyo nilikuwa namshauri Mheshimiwa Waziri yale maeneo yale ambayo kwa dhahiri yanahusu au kuonesha kwamba kutakuwa na migongano, maeneo hayo…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa mabadiliko ambayo nimeyapendekeza na nitaleta schedule of amendments, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti, ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda pengine nianzie alipomalizia Mheshimiwa Shonza, amenikumbusha, hii hoja ya kwamba UKAWA wananyanyaswa vyuoni, ni bahati nzuri sana nimkumbushe Mheshimiwa Ally Saleh na Mheshimiwa James Mbatia, nikiwa pamoja na mimi, tulikuwa Chuo Kikuu, tukaonekana tunashiriki mambo ya siasa, tukashughulikiwa na Serikali, hatukuwa UKAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la Serikali kushughulika na wanafunzi kwenye vyuo, ni jambo linguine na suala la kushughulikia wanafunzi kivyama si sahihi kulihusisha na chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana hotuba nzuri ya Mheshimiwa Ndalichako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti imekuja katika wakati ambao ni muafaka, wakati ambao tunataka kuzungumzia suala la elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ukurasa wa 24 wa hotuba. Ukurasa wa 24 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imejaribu kutoa majibu, kwenye hoja ambayo Mheshimiwa Chumi aliiwasilisha Bungeni hapa kama hoja binafsi, juu ya wanafunzi 489 ambao wanaonekana kwamba hawana sifa za kudahiliwa kusoma kozi ya Ualimu wa Sayansi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie ukweli Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize kwa makini, Wizara ya Elimu imekuwa na tatizo la kubomoa na kufumuafumua mifumo ya elimu katika Taifa letu. Mambo haya yanafanywa, kila Waziri anayekuja, anafumua mifumo iliyotengenezwa na Mawaziri wengine. Ni lini tutakuwa na mifumo ambayo inaheshimika? Ina maana kwamba, kwenye Wizara ya Elimu, hawa ambao ni Maprofesa wameshindwa kabisa kuja na mitaala, mifumo ambayo itatupeleka miaka mingi bila kufumuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uingereza tunasema kuna Cambridge, mpaka leo Cambridge haifi, hivi Tanzania tumeshindwa kuwa na Cambridge ya Watanzania; kila anapokuja Waziri anafumua mifumo ya elimu. Kwa nini nasema mifumo ya elimu inafumuliwa? Inaniuma sana baada ya kuwa na matatizo ya Walimu wa sayansi katika nchi yetu, tukaona kwamba kwa sababu wanafunzi wanapomaliza kidato cha nne, wanapokwenda kidato cha tano, wale ambao wanachukuliwa wamefaulu sayansi, wakimaliza forms six, hawataki kwenda kwenye kozi za Ualimu wa sayansi au kozi za Ualimu, wanaenda engineering, wanaenda kuchukua kozi zingine. matokeo yake shule zetu za Kata na shule za Serikali tumeshindwa kuwa na mikakati ya kuzalisha Walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu hawa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne, wale ambao wana credit nzuri kuanzia C, ndio wanaofaulu kwenda kidato cha tano, wale wanaobaki na alama za D, ndiyo wanaonekana wamefeli. Sasa kukawa na utaratibu, kwamba kwa nini kama wanafunzi wanakwepa kusoma Ualimu wa sayansi, kwa nini tusianzishe utaratibu maalum, ambao waliuita five years integrated bachelor degree program, ili mtaala huu, uweze kuwachukua wanafunzi wa kidato cha nne, ambao wana alama za D, waweze kusoma miaka mitano na siyo miaka mitatu. Katika kipindi cha miaka mitano wawalee, wawanoe, wawapike, iwe kama wamesoma certificate, diploma mpaka degree na wanakuwa wamechujwa hapa katikati, wale wanaofeli wanaondoka, kumaliza miaka mitano tunakuwa na Mwalimu tuliyemfundisha sayansi ili wafundishe shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake Mheshimiwa Waziri anakuja hapa anatuambia kwamba hawakustahili, hawana sifa, wakati wamekuwa na sifa ndani ya mtaala maalum ambao umewasilishwa na Chuo cha Mtakatifu Joseph; kuna nini hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulipokuwa na mahitaji ya Walimu, tulianzisha Walimu wa UPE na wenyewe hawakuwa na sifa, lakini tukawa-qualify na ndiyo wametufundisha sisi, nimefundishwa na Mwalimu wa UPE mimi. Vile viel tulipoona kuna mahitaji ya Walimu, tulianzisha programu miezi mitatu, kumfundisha Mwalimu, wakabatizwa jina la yeboyebo, sijui voda fasta, yote hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya mahitaji ya Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulipokuwa na mahitaji ya Walimu tulianzisha combination ambazo unasoma HG Education, PC Education, CB Education, yote hiyo ilikuwa ni kutatua matatizo ya Walimu. Sasa leo kupitia mtaala maalum mnawaita hawa watoto ni vihiyo haiwezekani, hawa siyo vihiyo. Mheshimiwa Ndalichako, kuniambia kwamba wengine walikuwa arts, kwa nini wameenda kusoma, kwenye arts wanasoma biology pamoja na mathematics masomo mawili hayo ni sayansi hata kama wako arts, wakienda kusoma masomo hayo wamesoma sayansi, leo unasema ni vihiyo; matokeo yake umewafukuza wanafunzi 489. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haiwezekani, huu ni ukatili, unyama na kama umesema umemshirikisha Mheshimiwa Rais, umemshirikisha kwa kumpotosha. Umemweleza mambo ambayo si sahihi na ndiyo maana, Mheshimiwa Ndalichako anataka tucheze muziki anaotulazimisha kucheza sisi, haiwezekani!
Niliwahi kusema hapa kwamba, hatuwezi kukubali kuchezeshwa kama Joyce wowowo hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Ndalichako wanafunzi hawa wamedahiliwa na TCU, wamepewa mikopo na Serikali, itakuwaje wawe wahanga, muwafukuze. Hatutakubali, utakapokuja kuhitimisha, tunataka majibu kwa nini wanafunzi hawa umewafukuza, lazima muwarejeshe hatuwezi kukubali, tumepoteza fedha za Serikali kwa sababu ya matatizo yenu huko TCU, matatizo yenu yasije yakatuletea uhanga kwa wanafunzi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye ada elekezi. Hii ada elekezi mnaelekeza kitu gani? Mkitaka shule za binafsi wapunguze ada, mkitaka shule za binafsi zife ni shule za Serikali kuwalipa Walimu vizuri, kuwa na madarasa, kuwa na nyumba za Walimu, kuweka msosi yaani chakula, hakuna mtu binafsi atakayepandisha ada na ninyi kama mtaendelea kuhakikisha mazingira haya hamyajengi kila mtu ana uchaguzi kupeleka mtoto Ulaya, kupeleka mtoto shule binafsi. Shule binafsi mmezirundikia kodi nyingi sana, mara wapake magari rangi, mara sijui wafanya nini, sasa watarudishaje hizo fedha mnazowaambia wapake rangi magari, kodi kede kede, tunakwenda wapi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM ni gari kubwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni gari kubwa tukiacha gari ku….
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kangi Lugola muda wako umemalizika.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache sana ya kuchangia kama ifuatavyo:
Kwanza kabisa ni wavuvi wamekuwa wakichomewa nyavu zao ambazo ni haramu, nyavu hizo zimeendelea kwa kiasi kikubwa kuzalishwa na viwanda na kusambazwa na wanafanya biashara kila kona hapa nchini. Kwa kuwa, hali hii inaendelea kuwafanya wavuvi kuwa maskini, wengi wa wavuvi wanachukua mikopo benki na taasisi zingine za fedha kama PRIDE, FINCA, SACCOS na kadhalika. Kwa muda mrefu sasa Wabunge tumekuwa tukitaka Serikali ya Awamu ya Tano kukomesha uzalishaji na usambazaji wa nyavu hizo ili zisiwafikie wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni mkakati gani uliopo kuhakikisha kwamba, nyavu hizo haramu hazizalishwi na kusambazwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizaji wa nyavu hizo kutoka nje ya nchi? Naomba maelezo ya kina juu ya kuwepo kwa mkakati huo kama upo au la.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kwa kuwa nchi yetu ilianzisha mpango mahsusi wa uwekezaji wa EPZ wa kutenga maeneo ambapo baadhi ya maeneo Serikali ililazimika kuwaondoa wananchi. Je, mpaka sasa kwa nini eneo la EPZ Wilayani Bunda Mkoa wa Mara halijatekelezwa? Ni vema tukajua utaratibu wa uwekezaji katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo machache naunga mkono hoja!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALPHAXARD K. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu ya kumpongeza Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Naibu wake Mheshimiwa Kalemani kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha nchi yetu inapata umeme. Aidha, nawapongeza kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini, nawatakia kila la kheri chapeni kazi bila wasiwasi kwani Wabunge tuko nyuma yenu kuhakikisha mnakuwa katika mazingira rafiki ya kufanya kazi. Pia nawapongeza kwa kuwasilisha bajeti nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali juu ya mpango wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Yapo maeneo hapa nchini ambayo yana changamoto kubwa sana katika usambazaji wa umeme. Maeneo hayo ni yale ya visiwa vingi ambavyo viko katika maziwa na bahari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba ili kupunguza gharama za kutumia marine cable kupeleka umeme katika visiwa, basi REA wasambaze umeme huo kwa njia ya solar (umeme jua) Jimboni kwangu nina visiwa katika Ziwa Victoria vya Nafuba, Sozia, Namuguma, Machwela, Rwiga, Buyanza, Kwigali, Bwenyi na Nyakalango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shughuli kubwa za kiuchumi katika visiwa hivi ni uvuvi, umeme huu utasaidia sana kuhifadhia mazao ya samaki pamoja na viwanda vidogovidogo vya kuchakata samaki na kutengenezea boti na mitumbwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, na kabla sijafika mbali Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango naomba masuala mawili haya ambayo kwenye hotuba yako hujayazingatia nipate ufafanuzi; sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuna ushuru na tozo mbalimbali ambazo toka Bunge lililopita tunapiga kelele kwamba wakulima katika sekta hiyo hawatafika mbali kwa sababu ya ushuru na tozo ambazo hazina tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye hotuba yako hapa umebaki tu kutaja kwamba kuna hizo changamoto, lakini hujatuletea hizo sheria mbalimbali kwa ajili ya kuzifuta ili wakulima waweze kuifanya Tanzania yetu kuwa nchi ya viwanda. Na wewe Mheshimiwa Mwijage hivyo viwanda unavyovihubiri havitakuwepo kama sekta hii ya kilimo tunafanya nayo mzaha wa namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la maji. Maji vijijini tulitenga Shilingi 50 kila lita ya mafuta ya petrol na diesel kuanzia Bunge lililopita kuwekwa kwenye mfuko wa maji, lakini zile fedha zikapelekwa maji mjini matokeo yake mpaka leo vijijini bado kunashida ya maji. Wabunge hapa tulisema na tukashauri tuongeze kutoka shilingi 50 kwenda shilingi 100, lakini kwenye hotuba yako ya bajeti unasema itabaki hivyo hivyo shilingi 50. Tunaomba tuweke shilingi 50 kwenye mafuta ili tuweze kuwa na mfuko mzuri wa maji vijijini; na hakutakuwa na mfumuko wa bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, John Pombe Maghufuli, kwa juhudi zake anazozifanya za kutumbua majipu katika nchi yetu na nimshukuru kwamba analeta Mahakama ya Mafisadi na zile rushwa kubwa za manyangumi. Lakini juhudi hizi za Mheshimiwa Rais, hatazifikisha mwakani endapo atabaki peke yake mtumbua majibu wakati mtambua na mbaini majipu ambaye ni CAG ataendelea kuwa na fedha shilingi bilioni nne katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha kupunguza bajeti ya CAG ambapo mwaka jana alikuwa na shilingi bilioni 74; wakati fedha za miradi ya maendeleo zilikuwa ni kidogo kuliko mwaka huu, tuna trilioni 11 halafu ndipo mnampa shilingi bilioni 44. Hii ni dalili kwamba bajeti hii inataka kukumbatia mafisadi kwa sababu CAG ndiye anayekagua miradi na mikataba ambayo ni ya kifisadi. Kitendo cha kuminya Ofisi ya CAG, nakuambia Mheshimiwa Waziri Mpango, utumbuaji wa majibu utaishia mwaka huu; Rais hatakuwa na majipu ya kutumbua tena kama bajeti ya CAG haitaongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niseme bayana, hata hawa watumishi hewa ambao sasa wanatumbuliwa, juhudi kubwa zilifanywa na CAG Bunge lililopita akawa anabaini watumishi hewa, miradi hii ambayo mingine tunapigwa kwenye barabara na sasa tunapeleka asilimia 40 kwenye miradi ya maendeleo, kama CAG ofisi yake itaminywa haya majipu yakifisadi nani atayabaini na hizi fedha mnazosema mnawezesha TAKUKURU; TAKUKURU atawachunguza mafisadi gani ambao hawajabainiwa na CAG?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwangu mimi bila kumwongeza fedha CAG ambaye ndio jicho, ambaye ndiye ameikomboa nchi hii kwa kubaini mafisadi, nakuhakikishia Mheshimiwa Rais wetu, mwakani hatakuwa hata na kijipu uchungu; hata kipele cha kuweze kutumbua, kwa sababu CAG atakuwa hajafanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hii hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mpango ya kuondoa msamaha kwenye mafao ya Wabunge. Mheshimiwa Mpango naomba nikuulize, hawa Wabunge ambao unaondoa msamaha kwenye mafao yao unajua kwamba hawana pensheni? Unajua kwamba Wabunge hawa sio pensionable?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge sisi hufanya kazi yetu miaka mitano tu hapa, hatuna pension, matokeo yake tunaambulia hicho kidogo; fedha nyingine ni nauli, mizigo, vifedha vingine ndio vile ambavyo tumevidunduliza kwenye mshahara tunawekewa kila mwezi. Sasa wewe unataka kuondoa msamaha. Nataka nikuhakikishie kuanzia utawala Mkapa, Wabunge walikuwa wanaomba hata watumishi wengine mafao yao yasije yakakatwa kodi kwa sababu wamefanya kazi miaka 30, 40 watumishi wanakatwa fedha, wanaenda wengine wanakufa kesho yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tumefika pazuri baada ya kuondoa kundi la Wabunge. Tulitarajia katika Bajeti hii sasa unatuletea sheria ya kwenda hata kufuta hizo kodi za mafao ya watumishi wengine Serikalini, sasa matokeo yake unatuletea tena kufuta za Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi, akiwepo Mheshimiwa Makinda hapa alisema amechoka kusumbuliwa Wabunge ambao walishastaafu wamekuwa wakija ofisini wanamwomba hela, wamekuwa ombaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge leo maslahi yetu tumedunduliziwa na kila mwezi tunakatwa kodi ya mapato halafu tena mafao yetu ambayo yamelimbikizwa na yenyewe yakakatwe kodi mnataka turudi mtaani halafu muanze tena kutucheka. Lazima Wabunge tulinde maslahi yetu, Mheshimiwa Waziri usicheze na maslahi yetu, lazima tulinde maslahi yetu. Hatuwezi kukubali fedha ambazo sisi kila mwezi tunakatwa kodi Pay as You Earn na nyingine ile tunawekewa pale halafu baada ya kutoka hapa uanze tena kututoza kodi. Waheshimiwa Wabunge tusikubali sisi hatuna pensheni lazima kodi hii isiwekwe kwenye fedha za Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mpango, sisi Wabunge mshahara wetu ni mdogo sana kuliko wa kwako, wewe mshahara wako ni mkubwa. Sisi Wabunge kule mtaani ndio ATM hata sasa hivi humu kila simu ya Mbunge sijui kuna msiba wapi, kuna kisima kimeharibika, kuna darasa upepo umeezua, ndipo hapo hapo tunapotoa pesa. Halafu Mheshimiwa Mpango unataka kucheza na maslahi ya Mbunge na wewe hapo ulipo wewe Jimbo lako ni Mheshimiwa Rais, sisi Jimbo letu ni wananchi kule. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiomba fedha hata za kukarabati chuma kidogo tu kwenye pampu ya maji kutoka Halmashauri unaambiwa wewe Mbunge saidia. Tunaomba Halmashauri kuna kadaraja pale kamekatika kidogo pelekeni fedha wanasema kazi ya Mbunge, kazi ya mwenge. Halafu leo hata hicho kidogo na ndiyo maana unanikumbusha lile tangazo kwenye TV walikuwa wameweka kakuku pale linakuja lile kama fisadi mara ya kwanza likakata robo tatu ya kuku haaam! Halafu kakabaki karobo likamalizia tena haamm! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango asitupeleke huko, fedha zetu ni kidogo sana matokeo yake unaanza kuzikwangua tena, je, tutakapofika mwakani utakuja tena na ajenda gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu wa CHADEMA hapa alikuwa anawasilisha bajeti hapa nikaona mhh! Huyu ndiye Silinde kweli? Anashabikia kwamba eti na sisi tunaunga mkono hii kodi wakatwe.
Mheshimiwa Mpango wewe ni mchumi kuna kitu kinaitwa free rider problem, huyu pamoja na kuipiga panga kwamba haitaki wanajua sisi tukiitetea na wao pia watapata free rider problem. Asidanganye wananchi hapa UKAWA wata-enjoy free rider problem baada ya sisi kuitetea na wewe ni mchumi unajua maana ya free rider problem, hatutakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anazungumzia masuala ya sitting allowance, leo, mimi nadhani alikuwa anachomekea tu kwa sababu wana ugomvi na mama yetu pale wanachomekea chomekea vitu na sisi hivi vitu vya kuchomekea hivi mama wala usiwe na wasi wasi wewe ndiye Naibu Spika na wao walikuchagua na sisi tumekuchagua hicho kiti utakikalia mpaka wewe mwenyewe utakaposema sasa basi. (Makofi)
Mheshimiwa Mpango utakapokuja kutoa majumuisho fedha hizi za CAG bila kupanda na bila kutoa kauli hapa kwamba hicho ulichojaribu cha kutu-beep juu ya maslahi yetu hatutaelewana. Na ninashukuru umetu-beep na sisi tumeamua kukupigia. Tunakwenda wapi? Na watumishi wengine wote wale tulishasema fedha zao zile msizikate kodi zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KANGI A.N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru pia kunipa nafasi ya mwisho katika kuchangia hoja ya Mpango wa Maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge wenzangu, sisi ni binadamu husahau, sisi ni binadamu ambao wakati mwingine hatuwezi tukaukubali ukweli hata kama ukweli utabaki kuwa ukweli. Niwakumbushe Wabunge wenzangu kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Bunge hili pamoja na mambo mengine aliliomba Bunge hili, alituomba Wabunge kwamba ameomba kazi ya kutumbua majipu tumsaidie ahakikishe anatumbua majipu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aliliomba Bunge hili limsaidie pale anapoleta mipango yake ya Serikali tumsaidie ili mipango hiyo iweze kutekelezeka, tuweze kuijenga nchi yetu. Hata hivyo, Bunge hili sasa linapoteza mwelekeo, limepoteza kumbukumbu limebaki sasa ni Bunge la kumlaumu Rais, limebaki ni Bunge la kulialia. Bunge hili litakuwa halimtendei haki Mheshimiwa Rais wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Rais ana nia njema na Taifa, najua Mheshimiwa Rais kwa kauli mbiu ya hapa kazi tu inasababisha watu ambao walikuwa wanaishi kwa mazoea waweze kumlaumu na kumlilia kwamba anaharibu nchi yao. Tunamtia moyo, tunamwunga mkono aendelee kushika na kukandamiza mahali ambapo amekandamiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazoea ni ya ajabu sana, tulizoea kwa makundi, wako wafanyabiashara walizoea kukwepa kodi, leo wameshikwa pabaya wanaanza kulia kwamba sasa biashara imekufa. Watumishi tulizoea posho za hapa na pale, tulizoea kusafiri, sasa wameshikwa pabaya wanaanza kulialia. Wabunge tulizoea kwenye Kamati tunapata chai nzuri, tunakula andazi la inchi kumi na nane leo tunakula andazi la sentimita mbili, tumeshikwa pabaya tunaanza kulialia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge sasa tunaanza kulialia kwa sababu tumeshikwa pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge kwamba wao ndiyo wanaonewa kwamba wao ndiyo hawana fedha. Mambo mengine ni ya ajabu sana, mpaka unajiuliza huyu ndiye Mheshimiwa Mbowe? Mbowe naye leo anailaumu Serikali imefilisika! Hivi ni Mbowe huyu kweli ambaye analipiwa gari na Serikali, shangingi, mafuta yamejaa, kiyoyozi kiko masaa 24, anasema Serikali imefilisika? Huku ni kuwatumia wananchi vibaya, ni kutaka kuwachonganisha wananchi na Serikali yao na Rais wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Msigwa kwa bahati mbaya leo hayupo, Mheshimiwa Msigwa yeye kama Mchungaji nilitarajia atatumia taaluma yake kuwashauri wenziwe kwamba hata wakati ule kwenye Biblia wakati Musa anawachukua wana wa Israel kutoka Misri awapeleke kwenye nchi ya ahadi, nchi yenye maisha mazuri jangwani walipata shida, hawana maji, wanang’atwa na nyoka lakini hatimaye kwa kuwa walikuwa na Mungu, Musa aliwafikisha salama na wakaishi maisha mazuri. Mheshimiwa Msigwa awashauri wenzake kwamba katika safari hii kutakuwa na misukosuko ya hapa na pale, lakini Musa wetu Mheshimiwa Rais Magufuli anatupeleka nchi ya Kaanani twende kuishi maisha ya asali. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo pia machache ya kumshauri Rais wetu wa nchi hii. Rais wetu alituahidi kwamba sisi Watanzania ambapo yeye ni dereva na sisi ni abiria wake anatusafirisha kutoka mahali tulipopandia basi atupeleke kwenye nchi ya ahadi. Namshauri Mheshimiwa Rais barabarani yeye kama dereva kuna matuta lazima ajue matuta haya akiendesha vibaya yataleta ajali na Watanzania hatutafika mahali anapotupeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri pia anapoendesha gari kuna zebra cross, wanafunzi wana-cross, ng’ombe wanapita, aendeshe vizuri Watanzania atufikishe salama. Naomba nimshauri pia anapoona wameandika speed 50 na yeye aende speed 50 ili Watanzania atufikishe salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango nimeusoma, Mpango huu ni mzuri, yako maeneo ya kushauri. Tunayo dira yetu ya Taifa ya Maendeleo 2025, tunayo Ilani ya CCM, vitabu hivi viwili ndivyo vinavyomsaidia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika kuja na mapendekezo mazuri ambayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM. Mheshimiwa Waziri yako maeneo humu ambayo inabidi nimshauri, kwenye Ilani yetu kuna mambo ya kilimo, kwenye mambo ya kilimo mpango wake umeacha kabisa mazao ya biashara kama vile pamba, tumbaku, kahawa, katani na pamba pamoja na mazao mengine imeshuka sana. Nimpe mfano, mwaka 2012/2013, tulizalisha pamba tani 356,000 na 2016/2017 imeshuka mpaka tani 120,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Kama leo watoto wetu wa maskini wanakosa mikopo ya elimu ya juu…
Kimbilio lao ni kwa wazazi wao ambao wanalima pamba. Kama wazazi wao wanalima pamba na humu hajaweka mpango wa kusaidia zao la biashara la pamba, watoto wa maskini hawatasoma, watoto hawa watakuwa wa mitaani. Namshauri atakapoleta Februari rasimu yake isheheni masuala ya kilimo cha mazao ya biashara, masuala ya mbolea ili watoto wa maskini waweze kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani Mheshimiwa Waziri ameweka kanda maalum za kiuchumi. Kanda maalum za kiuchumi Mheshimiwa Mpango tuna Ziwa Viktoria katika nchi yetu, zawadi ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, maji ya Ziwa Viktoria yamebaki kunufaisha Sudan na Misri wakati sisi wa Mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Shinyanga, Mara na Mwanza tunatakiwa tuwe na miradi mikubwa ya uzalishaji kwa sababu tuna maji na ardhi nzuri. Kwa hiyo, Ziwa Viktoria liwekwe kwenye kanda maalum za kiuchumi ili tuweze kuzalisha kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la elimu ya juu. Kwenye Ilani tulisema tutajenga Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere, Wilaya ya Butiama. Sasa kama mpaka leo Waziri analeta mpango hauoneshi kwamba tutajenga Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Butiama na ujenzi wa chuo kikuu ni miundombinu mikubwa, chuo hicho kitajengwa lini Mheshimiwa Mpango? Namwomba kwenye rasimu yake aje na mpango wa kujenga Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere pale Butiama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwana CCM ambaye niliapa kabisa nitasema kweli daima. Ninyi Mawaziri wa Serikali yangu ya CCM na ninyi ni abiria kwenye basi analoendesha Rais wetu na ninyi mmekaa siti za mbele, wakati mwingine abiria ndiyo humchochea dereva kwamba mnataka kufika mapema. Baadhi ya Mawaziri msimdanganye Rais, msimpotoshe Rais…
Asije akatuletea matatizo kwa sababu Rais anatakiwa ashauriwe vizuri, Rais wetu siyo mchumi. Hivi kweli mtamshaurije Rais kwamba kupotea kwa pesa ni kwa sababu watu wameficha kwenye magodoro, haiwezekani!
Pesa zimepotea kwa sababu Benki Kuu wamezichukua kutoka kwenye mabenki maana yake hazionekani. Pesa zimepotea, mshaurini ni kwa sababu madeni ya ndani hayalipwi, mumshauri vizuri. Itakuwaje mnamshauri Rais kununua ndege kwa cash wakati…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Spika naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa kuwa mchangiaji wa siku ya leo kuhusu mkataba wa Ubia wa uchumi baina yetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu ambao mimi nimeushika hapa mkononi ni miongoni mwa mikataba ambayo ni mibovu, ni miongoni mwa mikataba ambayo ni mibaya, ni miongoni mwa mikataba ambayo inanikumbusha enzi za miaka ya zamani. Mikataba kama hii ndiyo ambayo tulisoma kwenye historia ya akina Carl Peters na kwamba Wazee wetu wakiwemo wakina Mangungu waliweza kusaini mikataba mibovu na ya ajabu kama huu.
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Jemedari John Pombe Magufuli ambaye kwa kutumia mkono wake alikataa kabisa mkono wake usitumike katika kusaini mkataba mbovu huu katika Ikulu ya Tanzania, mjini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema mkataba huu ni mbovu? Niliwahi kuja Bungeni hapa nikiwa na semi-trailer ambalo nilishindwa kuliingiza humu ndani nikaliacha pale nje lilikuwa limesheheni bidhaa mbalimbali vikiwemo vijiti vya kutolea nyama kwenye meno, chaki, vikiwemo vitambaa, zikiwemo peremende.
Mheshimiwa Spika, kama nchi yetu imekuwa na bidhaa ambazo zimezagaa na kusababisha sisi tusiweze kuimarisha na kujenga viwanda vyetu, tukisaini mkataba wa namna hii nchi yetu itakuwa ni dampo la bidhaa nyingi za ajabu na matokeo yake dhamira njema ya Mheshimiwa Rais ya kutaka nchi hii sasa iwe ni nchi ya viwanda hakika hatutaweza kufanikiwa kama tutasaini mkataba wa namna hii.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu ambapo katika aya zake 146 zaidi ya vifungu 20 ni vifungu ambavyo vina matatizo, na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi kwa sababu ya muda sina sababu ya kuvipitia tena. Vifungu hivi vina matatizo, vifungu hivi vinatufanya tukisaini mkataba nchi yetu ya Tanzania haitakuwa na nafasi ya kujitanua katika ku-negotiate tutakuwa tumefungwa. Tukisaini mkataba huu kwenye vifungu ambavyo vinahusu masuala ya kilimo, masuala ya mifugo, masuala ya miundombinu tutakuwa tunasaini mkataba ambao kwa kweli nchi yetu itaingia kwenye matatizo makubwa.
Mheshimiwa Spika masuala haya ya nchi za Ulaya kuwinda nchi zetu katika umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanajua kabisa kwamba nchi ya Kenya ambayo wamepiga hatua kiviwanda, sote tunajua viwanda vya nchi ya Kenya viwanda vingi ndivyo hawa hawa ambao wanatoka kwenye Jumuiya ya Ulaya. Kwa hiyo, leo hii tukisaini mkataba kama huu ambapo tunashirikiana na nchi ya Kenya kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa vyovyote vile tutaingia katika matatizo makubwa.
Mheshimiwa Spika, kuna mifano ambayo iko hai. Sisi tulipoanzisha General Tyre wakati ule tulijua kabisa kwamba tutakuwa na soko zuri na tutaweza kuwa na viwanda ambavyo vitatusaidia, lakini Kenya hawa hawa ambao walitumiwa na nchi za Jumuiya ya Ulaya waliweza kuanzisha Kiwanda cha Fire Stone, leo hii kiwanda chetu cha General Tyre kimekufa. Kwa hiyo, tukisaini mikataba kama hii kwa kweli tutaendelea kuwa na matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Spika niseme, wenzetu wa Kenya ndiyo hata miaka ya nyuma wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuwa ni chanzo cha kuua Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo tuliianzisha wakati ule. Leo nina wasiwasi tukiendelea na Mkataba huu tukiwa tunashirikiana na Wakenya kwa vyovyote vile Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki ambayo tumeianzisha kwa nguvu kubwa, kwa nia njema lazima Jumuiya hii matokeo yake itaenda kuvunjika tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo viongozi wetu wa Serikali, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara na Uwekezaji, hakikisheni kwamba wataalam wetu waendelee kuuchambua mkataba huu ili maeneo yote yale ambayo yana matatizo yaweze kufanyiwa kazi. Na niseme bayana, lazima katika negotiation nchi yetu itakapofanya uchambuzi waweze kuwa na negotiation framework ambayo imetokana na mawazo ya Wabunge waweze kuboresha mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba mkataba huu kuna maeneo ambayo ni mazuri, lakini kwa sababu maeneo makubwa yana matatizo, hatuwezi tukaingia kwenye risk kwa sababu tu kuna mambo ambayo ni mazuri wakati mambo makubwa ndiyo mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo sisi tuna Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye EALA lazima Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki iweze pia kushirikisha Wabunge kwa Chapter ya Tanzania na wenyewe wajaribu kuchambua katika Bunge lao, waende kupiga marufuku muswada kama huu kuendelea kusainiwa ukiwa mbovu namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuna Mabunge mawili, Bunge letu hili kwa leo mimi kama Mbunge wa CCM, Mbunge ambaye naamini Serikali yetu inahitaji mkataba wa kufanya biashara na nchi za Ulaya, lakini hatuwezi kukubali Serikali ya CCM ikaingia mkataba ambao ni mbovu, ambao ni fake kama huu.
Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, bila kujali itikadi zetu, lazima nchi hii tuitendee mema, lazima mkataba huu tuukatae, Mkataba huu ni mbovu, urudi uchambuliwe halafu lazima Bunge hili baadaye lishiriki tena kuangalia ile negotiation framework ili tuone kwamba sasa tunaweza tukaenda kusaini mkataba ambao ni mzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mikataba mingine kama hii, humu humu ndani mimi nimesoma vifungu vingine vinajaribu kuwa na mwelekeo pia wa kutuletea mambo mengine ya ushoga kama ambavyo mikataba mingine inaleta mambo ya ushoga. Kwa hiyo, lazima Wabunge tuwahurumie Watanzania na hasa Watanzania ambao ni wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusipokuwa macho, sehemu zao nyeti zinaweza zikaingiliwa kwa sababu ya mikataba mibovu kama hii. Hatuwezi sisi tukakubali. Lazima tulinde haki za binadamu sisi kama Wabunge wa Bunge hili. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mimi ninakushukuru sana. Nitawashangaa Wabunge wenzangu ambao tumepata semina hapa nzuri ya maprofesa na madokta waliobobea halafu matokeo yake Mbunge unasimama, unakuja kuupongeza na kusema tupitishe mkataba wa namna hii. Nitakushangaa sana, na ndiyo maana hii mbingu mnayoiona hii yuko Mwenyezi Mungu anatutazama, analitazama Bunge hili namna gani mlivyo na huruma na uchungu na wananchi ambao ni watu wa Mungu. Mkisaini mkataba huu nawaambieni itakuwa ni vigumu sana hata ninyi kuuona ufalme wa Mungu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Siungi mkono kupitisha mkataba huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majeshi yetu ya Polisi, Magereza, Uhamiaji pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni majeshi ambayo yamesahaulika, ni majeshi ambayo yanachukuliwa kama ni ya kawaida, ni majeshi ambayo yanadhaniwa watendaji walioko mle hawana professionalism ya aina yoyote. Ndiyo maana majeshi haya yamefanywa kama majeshi ya miujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Yesu peke yake Mwana wa Mungu aliye hai ambaye ni bingwa wa miujiza, ambaye alikufa akafufuka, ambaye alimfufua Lazaro, ambaye alitembea juu ya maji. Hivi kweli kama majeshi haya hatutawekeza, hatuwezi tukapunguza uhalifu katika nchi yetu, hatuwezi tukajenga nidhamu ya majeshi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe kidogo Waheshimiwa Wabunge, hima himaaa, Tanzania sauti hii ukiona vyaelea vimeundwa, msidhani magwaride haya mnayofurahi jinsi majeshi wanavyopiga mguu chini, jinsi wanavyotoa sauti yao ya kutoa heshima ya utii kwa Amiri Jeshi Mkuu, mkadhani sauti hii imekuja hivi hivi. Sauti hii inatengenezwa na lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje askari wetu tunawapa shilingi 10,000, shilingi 10,000 hii aiache kwa familia, shilingi 10,000hii aende nayo kwenye lindo la benki, shilingi 10,000 hii aende nayo doria, asubuhi mpaka jioni haitawezekana. Ndiyo maana Waziri anapotuambia katika

ukurasa wake wa 21 katika hotuba yake kwamba Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watendaji wa vyombo vya usalama kwa kuwapatia ration allowance za kila mwezi. Mheshimiwa Waziri unasema unaendelea kuboresha ration allowance mbona kwenye kitabu chako humu hujaboresha, umeweka maneno tu yasiyoboresha? Tunahitaji uboreshe maslahi haya ili askari wetu waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari hawa mnaosikia wengine wanatekwa kwenye mabenki, wengine wanavamiwa kwenye doria, wakati mwingine wanakuwa kwenye stress, hajui leo familia yake itakula nini, hajui yeye atakula nini, anabaki askari wa kupiga miayo tu kwenye benki matokeo yake wanamnyang’anya bunduki. Tunahitaji kuboresha maslahi ya Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye mafunzo, Mheshimiwa Mwigulu ulipokuwa Wizara ya Kilimo ulikuwa na kauli mbiu mkitaka mali mtaipata shambani. Sasa leo uko Wizara ya Mambo ya Ndani nataka nikushauri, ukitaka kupunguza msongamano magereza, siyo kujenga mabweni ni kupunguza uhalifu katika nchi yetu. Ukitaka kupunguza uhalifu katika nchi yetu lazima uzingatie mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya miaka kumi sasa hakuna traffic courses kwenye Jeshi la Polisi, imebaki tu wewe askari kesho unapigiwa simu unakuwa traffic na ndiyo maana ghafla mnaona traffic anachoropoka kwenye vichaka kwa sababu hawana mafunzo ya aina yoyote. Mnagombana na askari traffic hawana mafunzo, tunataka mafunzo ya askari wa usalama barabarani wasomee magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya CID. Msongamano utaendelea kwa sababu upelelezi uko kiwango cha chini sana, kesi zinachukua muda mrefu kwa sababu ya kutokuwa na mafunzo katika kupeleleza, kwa sababu ya kutokuwa na fedha ya kutosha kwenye Criminal Investigation Fund, mfuko ambao unatumika kuwapatia watu wanaoleta taarifa, taarifa ni za kununua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la CRO wenzangu ambao hamkupita kwenye Jeshi kama hilo maana yake mimi nimepita huko nina-declare interest. Pale mnapoita kaunta pale, pale ni CRO pale kulikuwa na mafunzo ya CRO, lazima anayekuwa in charge pale awe amefundishwa namna ya kupokea mashitaka, namna ya kujua hili ni kosa la jinai au ni kosa la civil, matokeo yake kunakuwa na malalamiko mengi ndani ya Jeshi la Polisi, kwa sababu hakuna kozi kama hizi za CRO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Mwigulu kozi hizi zirudi na wafundishwe Askari ili wajue kupokea mashtaka, tunaposema watu wanabambikizwa kesi ni pamoja na kutokujua hii ni ya criminal au ni ya civil kwa sababu hawajapata mafunzo ya CRO muda mrefu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye vitendea kazi. Kwenye PGO lazima askari anapopanga ile duty roster pale kituoni, kunakuwa na askari wa standby…

(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Mnyika nataka nikuhakikishie kwamba ni vyepesi sana ngamia kupenya tundu la sindano kuliko upinzani kuiondoa CCM madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya kwa kuwatetea wanyonge wa Tanzania na kutetea maslahi ya nchi hii. Ninampongeza kwa sababu amejitoa mhanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukawa Rais lakini usijitoe mahanga kwa ajili ya kupigania maslahi ya watanzania na kuziacha rasilimali zikiporwa na kutumiwa na watu wachache; ninampongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na ndiyo maana zile pushapu alizopiga, na yale majina ya tingatinga tuliyompa na zile nyimbo tulizokuwa tunaimba za Kisukuma ling’ombe lyamapembe, lyekumakinda mumbazu ndiyo maana sasa matunda tunaanza kuyaona, ndiyo maana amewanyima pumzi mafisadi, wakwepa kodi amewanyima pumzi hawapumui, wenye vyeti fake hao nao na wenyewe sasa ndio wanakandamizwa, ninakuomba Mheshimiwa Rais uendelee kukandamiza hapo hapo na wala usibadilishe gear. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge nianze kwa kuwapa nukuu zifuatazo, nianze na ukurasa wa 30 wa kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anasema; “Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa ndiye msemaji mkuu (champion) wa masuala yanayohusu maji Barani Afrika.” Na kwamba Waziri mwenyewe ni Rais wa Baraza la Mawaziri wa maji Afrika kwa kipindi cha miaka miwili. Waheshimiwa Wabunge, u- champion huu naomba niwakushe, u-champion wa maji wa Mheshimiwa Rais wetu aliuanza wakati ule alipopiga push up kwenye kampeni, na aliponyanyuka kutoka chini kwenye push up aliwaambia Watanzania kwamba najua Watanzania akina mama mna tatizo la maji, ninakwenda kutatua tatizo la maji na ole wake Waziri wa Maji nitakayemteua asipowaleteeni maji nitamgeuza kuwa maji na Watanzania waweze kumnywa. Mheshimiwa Waziri, bajeti hii jiandae sasa unaenda kugeuzwa maji endapo tozo ya shilingi 50 haitakubalika na kuongeza pesa kwenye bajeti hii, kwa ajili ya kutatua kero ya maji kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini champion mkuu wa maji Waheshimiwa Wabunge ni Yesu Kristu Mwana wa Mungu. Ukisoma Yohana 19:26-28 Yesu alipopata maumivu msalabani anateswa wakati mama yake yuko pembeni, alimwambia; “mama tazama mwanao” na baadaye alipoona kwamba lazima haya yakamilike akasema; “naona kiu.” Hakuna kitu kingine ambacho Yesu alikiona ni isipokuwa kiu, kiu ni maji na ndiye champion mkuu wa maji kwa ajili ya akina mama katika Taifa letu. Tatizo la maji kwa akina mama, huu ni mwaka wa saba nilipoingia Bungeni humu niliingia na nyoka ya shaba, nikawaambia akina mama msichague Wabunge ambao watapitisha bajeti isiyotatua kero ya maji. Leo ni mwaka wa saba maji bado ni kero kwa wananchi hasa Watanzania akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie Wabunge wenzangu atakaye kwenda kupitisha bajeti hii kwa ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Wakati Bajeti hii, haijaongezwa pesa ya tozo ya shilingi 50, niko tayali na mimi kuanzisha mwenge, mwenge wa sauti nitachukua kwenye Hansard sauti za Wabunge za ndiyo nitazikimbiza nchi zima kuwaambia akina mama sikilizeni Wabunge wanavyowasaliti na nyinyi hampati maji katika nchi yenu. Lazima tuwe na huruma kwa akina mama. Waheshimiwa Wabunge ni nani ambaye hakunyonya mtindi kwenye ziwa la mama yake katika nchi hii? Waheshimiwa Wabunge ni nani ambaye hakuishi miezi tisa kwenye tumbo la mama yake halafu leo inakuja bajeti ambayo haitatui tatizo la maji tunaendelea kufanya ushabiki katika suala la msingi la bajeti ya maji, hatutakubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule vijijini kule Mwibara kule, miradi ya Buramba, miradi ya Kibara, Bunda Mjini amesema Mheshimiwa Ester Bulaya hapa, zaidi ya miaka kumi akina mama hawapati maji, kwa nini, ni kwa sababu ya Bunge hili lenye uwezo wa kutatua kero ya maji kwa akina mama tunafanya ushabiki na kupitisha bajeti ambazo hazitekelezeki. Naomba Waheshimiwa Wabunge tukatae. Nitashangaa kwa kweli Mbunge atakayepitisha bajeti hii ambayo haijaongezwa pesa za maji. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, ngoja ni waambie, kule vijijini wako wanaume ambao sasa hivi ni vilema ambao akina mama wanawaacha vitandani saa kumi usiku na kurudi saa tano ilhali wanadhani wana wivu kwamba akina mama wanakwenda kufanya mambo mengine wanapanda juu ya miti, matokeo yake wanadondoka wanakuwa ni vilema, leo tunakuja kufanya mzaa hapa. Waheshimiwa Wabunge, kule vijijini wanaoga kwa zamu maji hayatoshi. Aoge baba, aoge mwanafunzi aende shule, lakini hata wale wanaopata maji ya kuoga na wao wanachagua sehemu nyeti tu za kuoga kwa sababu maji hayawatoshi, halafu tunakuja tunafanya mzaa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye umwagiliaji. Nilishasema hapa Bungeni. Kule Mwibara kuna bonde zuri kwenye Ziwa Victoria kuanzia Musoma Vijijini kule Bugwema linakuja linapita kwenye kata ya Butimba maeneo ya Kabainja linaenda Karukekele, Namhula, Bulendabufwe, Igulu matokeo yake linaingia mpaka Genge, Kisolya mpaka Nansimo lakini hatuna umwagiliaji. Tumechoka kuletewa mahindi ya msaada ya kilo nne kwa familia ilhali tuna maji ya Ziwa Victoria. Tunaomba miundombinu ya umwagiliaji. Nimeangalia kwenye kitabu hiki hakuna kabisa, lazima tutende haki kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mgawanyo wa fedha za maji. Nilikuwa nasoma humu unakuta kuna Halmashauri nyingine zina kata sita wana shilingi bilioni nne za maji. Kuna Halmashauri nyingine wanakata 20 mpaka 30; kuna Halmashauri nyingine zina majimbo mawili lakini wanapata shilingi milioni 800 tutakwenda wapi sisi, tutawambia nini wananchi wetu kwenye mgawanyo kamba huu? Tunasema tunagawana sungura mdogo, haiwezekani Halmashauri nyingine; niliona ya Mheshimiwa Kitwanga hapa ana shilingi bilioni nne wengine tuna shilingi 500,000,000 au kwa sababu anatishia kung’oa mitambo ya maji ndiyo sababu mnapatia maji? Haiwezekani, huyu sungura mdogo lazima tugawane hapa pasu kwa pasu; haiwezekani kabisa Halmashauri ipate shilingi milioni 500 wengine wana shilingi bilioni nne; haiwezekani tukamla kuku wengine wakachukua mapaja, wengine wakachukua mnaita chenye mafuta mafuta kile, halafu wengine mafuta mafuta yale, kakiuno kana mafuta na haka kakiuno kenye mafuta ndiko ambako wewe Waziri umechukua, ndiko wewe Naibu Waziri umechukua na sisi tunakataka hako, na sisi tunataka mafuta haiwezekani…(Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ALPHAXARD K. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye huu Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Yanga inacheza TP Mazembe pale Dar es Salaam na haya marekebisho tunayoyafanya leo ya sheria hii nina imani kama Yanga itashinda na marekebisho haya yatakuwa mazuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kulikumbusha Bunge lako tukufu kwamba, katika Bunge la Kumi Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Ununuzi na tukatunga Sheria Namba 7, 2011 kwa kufuta kabisa Sheria Namba 21 ya mwaka 2004. Ilionekana ile sheria tulioifuta ilikuwa na mapungufu makubwa sana na hivyo Wabunge tukajiridhisha kwamba sheria tuliyoitunga kwenye Bunge la Kumi ingeweza kuondoa matatizo katika sekta ya ununuzi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwa bahati mbaya leo Serikali inawasilisha tena Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na marekebisho ambayo tunaenda kuyafanya leo. Nilikuwa naangalia muswada wenyewe, tunakwenda kubadilisha vifungu 40 na vifungu 40 ni vingi sana, ni vifungu ambavyo tunaenda kuvibadilisha katika hati ya dharura, kwa hiyo ninayo mambo ambayo ningependa niitahadhalishe Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwenye ukurasa wa 11 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Tulipotunga Sheria Namba 7 ya 2011 tuliangalia kwamba sekta ya ununuzi wa umma kwenye Halmashauri zetu lazima tuweke sharti ambalo linamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuwasilisha mbele ya Kamati ya Fedha na Mipango maamuzi yaliyofanywa na Bodi ya Zabuni ili Kamati ile iweze kuchambua na kuridhia juu ya utoaji wa tuzo kwa mzabuni aliyeshinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanya vile kwa sababu ndipo sasa dhana ya D by D (ugatuaji wa madaraka) kwenda vijijini ulikuwa unajidhihirisha. Kamati ya Mipango na Fedha ndiyo inayofanya ziara kwenye eneo lao la Halmashauri na kukagua miradi yote ya maendeleo ambako wazabuni hawa wanakuwa wanatekeleza zile zabuni walizoshinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa, leo muswada unaoletwa mbele ya Bunge lako tukufu. Mheshimiwa Waziri anapendekeza kwa lugha ya kusema kuboresha kwa kufuta kabisa na kuondoa sharti la Kamati ya Fedha na Mipango kutopokea tena taarifa ya maamuzi ya utoaji wa zabuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli kamati hii kupitia na kuchambua uamuzi huu ni kasoro na ni upungufu? Mimi nilidhani kuendelea kuwapa lungu zaidi Kamati ya Mipango na Fedha.Ndipo pale ambapo watahakikisha fedha za wananchi katika manunuzi ya umma kwenye miradi inatumika ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana kamati hii inapokuwa inapokea taarifa hii na kuichambua.Wao hawaiambii bodi kwamba mpeni huyu zabuni, hapana! Wao jukumu lao ni kuangalia inawezekana katika kaguzi walizofanya za miradi wakakuta kuna mzabuni. Kampuni ya ukandarasi imechakachua mradi, imejenga mradi chini ya kiwango, wanayo mamlaka ya kuiambia bodi kwamba huyu mkandarasi ana matatizo ili waweze kuiangalia upya zabuni ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninamtahadhalisha sana Waziri wa Fedha na Mipango alitazame hili ili tuhakikishe kwamba sharti hili la kuipa Kamati ya Fedha na Mipango liendelee kama lilivyokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala hili la bei ya soko. Sababu nyingi zinazotolewa na hasa katika muswada huu za kwamba Serikali imekuwa ikiingia hasara kwa sababu zabuni hizi wanaweka bei ya juu tofauti na bei ya soko. Na hivyo leo tufanye marekebisho kwa kutazama kwamba wazabuni hawa wawe wanaleta zabuni zao kwa kuangalia bei ya soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimtahadhalishe Mheshimiwa Waziri amejipanga vipi kuhakikisha kwamba yale mambo yaliyokuwa yanawafanya ghawa wazuni kuweka bei ya juu Serikali inayatazama.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza wazabuni hawa wanapokuwa wanaleta bei zao Serikali hii imekuwa haiwalipi kwa wakati! Na hivyo wamekuwa wakiingia hasara, wanafuatilia madai yao miaka nenda rudi Serikali haiwalipi na matokeo yake hata zile fedha wanazofatilia zinakuwa haziwasaidii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni nyingi zimefilisika, watu wanalisha shule, wanalisha magereza lakini malipo kutoka Serikali inakuwa ni kizungumkuti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo mnaposema kwamba walete bei za soko na wakati ninyi Serikali hamjabeba jukumu katika sheria hii hii kwamba na ninyi muwalipe kwa wakati, nina imani kwamba sheria hii tunayoibadilisha leo haitaleta mafanikio, wazabuni hawa hawa mtaendelea kupata bei za juu na vinginevyo hamtawapata wazabuni mtarudi kule kule kuanza kufanya manunuzi nyinyi wenyewe. Ndiyo maana leo hii Mkurugenzi ambaye ana cash money ukimtuma kwenda kwenye duka ana uwezo wa kununua bei ya soko lakini Mkurugenzi huyo huyo akienda kwa kauli ya kukopa alipe baadaye bei ile lazima haitakuwa hiyo ambayo mnaiita ni bei ya soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine Serikali imejipangaje kwenye suala la rushwa kwenye hizi tenda za zabuni? Kwa sababu rushwa ndiyo husababisha wazabuni hawa wanaleta bei ambazo ziko juu na wamekuwa wakifanya mawasiliano na wazabuni kwamba katika kujenga barabara hii au katika kuleta jenereta, katika kuleta fridge, katika kulisha shule ndizi moja lazima ulete bei fulani kwa ajili ya kushindana na hao wengine. Wanafanya hivyo kwa sababu wazabuni hawa au wakandarasi ili waweze kulipa ile 10 percent ambayo ni ya corruption lazima waweke bei za juu, hawawezi wakatumia hela zao za mfukoni katika kulipa hawa kwa njia ya rushwa. Kwa hiyo, nilitaka kujua Serikali imejipangaje, haya mambo ya kuwaambia wazabuni wanapoleta zabuni zao wawe wameandika kwamba hawatajihusisha na rushwa, yale yamekuwa ni maandishi tu ni makaratasi lakini bado kumekuwa na matatizo kwenye zile zabuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo namtahadharisha ambalo inabidi pia walichukue kwa makini, katika masuala haya ambayo tumesema kwamba tujaribu kupunguza muda wa hizi tenda ambapo mwanzoni walikuwa wanatumia muda mwingi sana, lazima ule muda tungeuoanisha na huu muda ambao tunataka kuboresha wa manunuzi ya dharura. Tusipooanisha muda huu na yale manunuzi ya dharura, nina uhakika lazima Bodi ya Zabuni watakuwa hawatengenezi ule mpango wa manunuzi kwa mwaka, watakuwa wanasubiri wajifanye kila kitu wananunua kwa dharura na watakuwa wanasubiri pia waweze kuzigawa zile tenda. Kwa sababu kwenye Sheria ya Manunuzi kuna kile kiwango ambacho hawaruhusiwi katika tenda moja Mkurugenzi kutoa maamuzi kwa ajili ya manunuzi lazima waende kwenye tenda. Kwa hiyo, ule muda tusipouoanisha vizuri na hizi zabuni za kawaida pamoja na haya manunuzi ya dharura, tunaweza tukarudi kule kule tukasema kwamba sheria tuliyoipitisha lazima tuirekebishe tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Leo tunakwenda kufanya maboresho 40 kwa Sheria ya Manunuzi na tunafanya maboresho haya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kangi, naomba umalizie sekunde 10 muda wako umekwisha.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya, naunga mkono hoja.