Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Kangi Alphaxard Lugola (7 total)

MHE. PETER J. SERUKAMBA (K.n.y. MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Athari za mazingira ni kubwa na vyanzo vingi vya mito (water sources) vimeathirika sana (mfano Mto Makere):-
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na mrefu wa kukabili hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, napenda nichukue fursa hii ya mwanzo kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kwenye Baraza lake. Nishukuru pia Wabunge wenzangu ambao wamenipa ushirikiano na wewe mwenyewe Mwenyekiti ulikuwa mjumbe mwenzangu wa Tume kwenye Utumishi wa Bunge, nakushukuru sana kwa ushirikiano ulionipa. Niwashukuru wananchi wa Mwibara pia kwa kunifanya Mbunge wao na Rais akaniona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwako, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji, Serikali ilipitisha Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006. Mkakati huu umeainisha hatua za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji. Aidha, mwaka 2008, Serikali iliandaa Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Maziwa, Mabwawa na Mito ili kuhifadhi maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012, Serikali ilipitisha kwa ajili utekelezaji Mkakati wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, mwaka 2016, Serikali ilielekeza utekelezaji wa Programu ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na pia Serikali inakusudia kuzuia matumizi ya kuni kwenye taasisi za umma ili zianze kutumia nishati mbadala. Mikakati yote hii inalenga kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi zilizoainishwa na mkakati wa mwaka 2006 ni pamoja na kuwaondoa wafugaji waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji; kusimamisha shughuli zote za kilimo na kuwaondoa wavamizi kwenye maeneo yaliyoharibika sana; kuzitaka taasisi na watumiaji wengine wakubwa wa miti, kuni na mkaa kuwa na mshamba yao ya miti; kudhibiti shughuli za umwagiliaji usio endelevu na kuzitaka wilaya zote kubainisha vyanzo vya maji na kufanya tathmini ya hali ya mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zingine ni kudhibiti matukio ya uchomaji moto wa misitu; kupiga marufuku upandaji wa miti isiyofaa katika maeneo ya vyanzo vya maji; kuendeleza Kampeni ya Taifa na Kupanda na Kutunza Miti; Kuendeleza Program ya Kitaifa ya Elimu ya Mazingira kwa Umma; kuwa na programu za hifadhi ya mazingira na mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi kwa kila wilaya na kutekeleza na kupiga marufuku uchimbaji holela wa madini kwenye vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda wa kati ni pamoja na kujenga na kuendeleza malambo, visima na mabwawa katika maeneo ya wafugaji na wakulima; kuhuisha na kusambaza kwa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi ili uanze kutumika mara moja na kuianisha na kuondoa miti isiyofaa kwenye vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mrefu ni pamoja na kuendeleza teknolojia sahihi za kuvuna, kuhifadhi na kusambaza maji ya mvua na ya ardhini, kuharakisha matumizi ya njia mbadala za kuzalisha umeme ili kupunguza gharama za umeme kwa watumiaji na hatimaye kupunguza mahitaji ya kuni na mkaa. Aidha, Serikali imeanzisha Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza Miti. Lengo la tuzo hii ni kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji. Tuzo hii hutolewa kila baada ya miaka miwili.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI Aliuliza:-
Suala la mabadiliko ya tabianchi ni mtambuka na linagusa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Je, ni mashirika ya umma mangapi yamepokea ruzuku kutoka Wizara/Idara au kwa wafadhili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita? Je, nini madhumuni ya ruzuku hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mashirika ya umma yanayopata ruzuku kutoka kwenye Wizara, Idara au wafadhili.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye kipengele (a), haiwezekani kuelezea madhumuni ya ruzuku ambayo haitolewi.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Mto Songwe umekuwa ukihama hama kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi huku ukiharibu rasilimali za wakazi wanaoishi karibu na mto huo na kingo zake kutokana na mafuriko.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudumu kudhibiti uharibifu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira na maumbile ya Bonde la Mto Songwe pamoja na mgawanyiko wa unyeshaji wa mvua katika bonde hilo ndio sababu kubwa inayofanya kuwepo kwa mafuriko ya mara kwa mara kila mwaka. Inakadiriwa kuwa takribani hekta 9,000 za ardhi huathiriwa na mafuriko katika kila msimu wa mvua na kufanya Mto Songwe kubadili mkondo wake mara kwa mara, hivyo kuathiri pia mpaka kati ya nchi za Malawi na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hali hii, tatizo hili linakuwa kubwa zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu katika bonde. Aidha, matumizi mabaya yasiyo endelevu ya rasilimali zilizoko katika bonde husababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, vyanzo vya maji, mifumo ikolojia na kutokewa kwa bioanuai zilizo katika bonde hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Malawi imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo katika Bonde la Mto Songwe. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha Kamisheni ya Pamoja (Songwe River Basin Commission), ambayo itashughulikia masuala yote ya bonde hilo. Mpaka sasa kuna sekretarieti ya mpito iliyoanzishwa ambayo inaratibu shughuli ya bonge hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tayari programu ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Program) imeshaandaliwa kwa ajili ya utekelezaji. Masuala yaliyoainishwa kwenye programu kwa ajili ya utekelezaji ni kama ifuatavyo; kuendeleza kilimo endelevu, uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya maji, kudhibiti mafuriko ya mto pamoja na kudhibiti kuhamahama kwa mto, uboreshaji wa upatikanaji na usambazaji wa maji, maendeleo ya uvuvi, kukuza utalii na uboreshaji wa mazingira na kuiwezesha kamisheni usimamizi wa pamoja wa rasilimali za Bonde la Mto Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za mafuriko Sekretarieti ya Mpito ya Bonde kupitia programu hii (Songwe River Development Program) itajenga mabwawa matatu ambayo ni Songwe Chini, Songwe Kati na Songwe Juu. Pamoja na mabwawa hayo kutumika kudhibiti mafuriko pia yatatumika katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, usambazaji wa maji na shughuli za uvuvi. Vilevile, kutakuwa na mradi wa mazingira ambao utadhibiti kingo za mto (River Banks Stabilization) ili kuufanya mto usihame hame.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo. Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2007 na mkakati wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua, kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu, ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika suala zima la kuleta maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo kwa kuandaa mpango mahususi wa sekta ya kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mpango wa Taifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo. Katika utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo limezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo, kuongeza tija kupitia kilimo cha umwagiliaji na teknolojia bora za uzalishaji kupitia kilimo shadidi, kuboresha mfumo wa upatikanaji wa mbegu bora, kuwekeza katika utafiti wa mazao ya kilimo, kutumia sayansi na teknolojia za kisasa katika kilimo kulingana na misimu na hali ya ukame na msingi mingine inayolenga kuweka mbinu mbadala za kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Serikali zetu zote mbili zimekuwa kwenye jitihada za kukabiliana na kero za Muungano:-
(a) Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Zanzibar kuhusu ushiriki wa Wizara zisizo za Muungano na Zanzibar kwenye Taasisi za Kimataifa zinazotambua utaifa wa wananchi katika uwakilishi wake?
(b) Je, Serikali inapata ugumu gani kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kabisa kila kero za Muungano zinazopatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kwamba Wazanzibari kwa muda mrefu wamekuwa na kero ya kutoshirikishwa katika medani za Kimataifa. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake, masuala ya mambo ya nje yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikishirikishwa kwa kiasi kikubwa katika taasisi za Kimataifa zinazotambua utaifa wa Tanzania kwenye Wizara zisizo za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa katika mikutano ya Kimataifa na taasisi za Kimataifa, kama vile Mikutano ya mabadiliko ya Tabianchi, Mikutano ya Shirika la Kazi Duniani, Mikutano ya Kamisheni ya Hali ya Wanawake, Mikutano ya Shirika la Kazi Duniani, Mkutano kuhusu utekelezaji wa lengo Namba 14 la Maendeleo Endelevu linalohusu Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Bahari na Rasilimali zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Viongozi wa Mashirika ya Kimataifa waliofanya ziara hapa nchini kwa mwaka 2017, walitembelea pia Zanzibar na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao ni Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkurugenzi wa FAO, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali haijawahi kupata ugumu wala kugugumizi katika kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kuhusu changamoto zilizopatiwa ufumbuzi na hata zile ambazo ziko katika hatua mbalimbali ya kutafutiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nikiwa Waziri mwenye dhamana ya Muungano, nimefanya jitihada kubwa za kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kabisa kuhusu jitihada za Serikali katika kutatua changamoto za Muungano kupitia vyombo vya habari mfano television, redio na magazeti, makongamano, hotuba za viongozi wakati wa maadhimisho ya Muungano na hata kupitia Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuza:-
Je, ni kwa nini mikakati ya dhati ya Serikali katika kunusuru na kuzuia uchafuzi wa mazingira ya Mto Rubana ambao unaingiza maji yake katika Ziwa Victoria na ni chanzo kikubwa cha maji katika Vijiji vya Tingirima, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Sarakwa, Kihumbu na Hunyari katika Jimbo la Bunda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Rubana ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa vijiji vilivyoko maeneo unakopita mto na pia kwa shughuli za uhifadhi. Maji ya mto huu hutumiwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunyweshea mifugo, kilimo na uvuvi. Aidha, maji ya Mto Rubana hutumiwa na wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la akiba la Grumeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Mto Rubana kama chanzo cha maji na shughuli za uhifadhi, Serikali imechukua hatu zifuatazo ili kunusuru na kuzuia uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika mto huo:-
(i) Kuziagiza Halmashauri za Serengeti, Bunda na Bunda Mjini kuzingatia na kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006 na Mkakati wa Hatua za Haraka za kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa wa mwaka 2008 katika maeneo yao ili kuzuia uharibifu wa Mto Rubana.
(ii) Kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa viongozi wa Halmashauri za vijiji na wananchi wote wa Kata za Hunyari, na Mugeta kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 inayozuia ukataji miti ovyo na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.
(iii) Kufanya doria za mara kwa mara na kukamata wanaokaidi na kukiuka sheria na kusababisha uharibifu wa mazingira ya mto kwa kukata miti ovyo na uchomaji wa mkaa.
(iv) Kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kuzuia wananchi kunyweshea mifugo kwenye mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wadau wote ikiwemo viongozi katika ngazi ya Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa Kata na Vijiji na wananchi wote katika maeneo hayo kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya Serikali ili jitihada za kunusuru Mto Rubana na kuzuia uchafuzi zifanikiwe kikamilifu.
MHE. JEROME D. BWANAUSI (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati mifereji ya maji na matuta ambayo yalijengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita katika Mji wa Mikindani ili kupunguza athari ya maji ya bahari kwenye mitaa na makazi ya watu hasa kipindi cha mvua kali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mipango ya ukarabati wa mifereji ya maji ya mvua na matuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani. Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imekuwa ikifanya ukarabati wa mifereji ya maji ya mvua inayoingia baharini katika mji wa Mikindani kila mara mahitaji yanapojitokeza kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetuma kiasi cha shilingi milioni tatu kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri katika kufanya ukarabati wa mfereji uliopo Kata ya Magengeni. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 37 zilitumika kufanya ukarabati wa mfereji katika Kata ya Mtonya, Magengeni na Mitengo kupitia fedha za Mfuko wa TASAF.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ukarabati wa mifereji na matuta, Halmnashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati huo. Hivyo, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imetenga kiasi cha fedha shilingi milioni 50 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mifereji kata za Mtonya, Magengeni na Kisungule.