Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kangi Alphaxard Lugola (1 total)

MHE. KANGI A. N. LUGOLA aliuliza:-
Mapambano dhidi ya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi yamekuwa yakihusisha njia ya kuwanyang‟anya zana haramu wavuvi wadogo kupitia mradi wa MACEP na kuwapatia zana za uvuvi zinazoruhusiwa:-
(a) Je, mradi huo umefanikiwa kwa kiwango gani?
(b) Kama umefanikiwa; je, ni lini mradi huo utaanzishwa kwa wavuvi wadogo wa Jimbo la Mwibara katika Ziwa Victoria?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa usimamizi wa mazingira ya Ukanda wa Pwani na Bahari Marine and Coastal Environment Management Project (MACEMP) ulitekelezwa mwaka 2005/2006 hadi 2012/2013 katika Halmashauri 16 za Ukanda wa Pwani upande wa Tanzania Bara na Halmashauri kumi kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Lengo la mradi huu lilikuwa kuimarisha usimamizi na matumizi ya rasilimali za uvuvi katika Bahari Kuu na kuinua hali ya maisha za jamii hizi za Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa MACEMP umekuwa na mafanikio kadhaa ikiwemo kuimarisha usimamizi wa rasilimali na uvuvi katika Ukanda wa Pwani kwa kuanzisha mamlaka ya usimamizi na uvuvi katika Bahari Kuu yaani (Deep Fishing Authority) kuwepo kwa mtambo wa kufuatilia mwenendo wa meli pamoja na kuwezesha kununuliwa kwa boti 16 za doria. Lakini pia kumekuwepo na kuwezesha uendeshaji wa doria katika nchi kavu na anga na kuwezesha kuanzishwa kwa vikundi 182 vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi, yaani Beach Management Units (BMUs). Pia vikundi 47 vyenye wavuvi 193 na wavuvi 436 kutoka katika Hifadhi ya Bahari za Mafia na Mtwara walipatiwa zana za uvuvi na kuondokana na matumizi ya zana haramu.
Vilevile mradi umewezesha jamii za Pwani kuibua miradi midogo 470 ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.6 ambayo ililenga kuboresha maisha ya Jamii hizo na kunufaisha wananchi wapatao 8000. Aidha, mradi uliwezesha ujenzi wa mialo mitatu ya kisasa ambayo ni pamoja na mwalo wa samaki Kilindoni ulioko Mafia, Masoko ulioko Kilwa na Nyamisati ulioko Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba muda wa kutekeleza mradi wa MACEMP umemalizika na Serikali itatekeleza miradi yenye malengo kama hayo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mwibara kutokana na uwezo wa Serikali. Miradi yenye malengo sawa na MACEMP imekuwa ikitekelezwa katika Ukanda wa Ziwa Victoria ambayo ni pamoja na Mradi wa Utekelezaji wa Mpango wa Usimamizi wa Uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria uliotekelezwa mwaka 2003 hadi Agosti, 2010 ambao umesaidia ukuaji na uendelezaji wa uchumi katika Ukanda huo na rasilimali za uvuvi zilizoko katika Ziwa Victoria.
Pili, Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Ziwa Victoria wa Awamu ya Kwanza na ya Pili na Tatu kumekuwepo na utekelezaji wa pili ambao ulitekelezwa hadi mwaka 2005 na kwenda hadi mwaka 2013 ambao ulikuwa na malengo hayo hayo. Mradi huu umewezesha kuimarika kwa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi na kuongeza ajira na kuboresha huduma za uvuvi katika jamii hizo zinazozunguka Ukanda wa Ziwa Victoria.