Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Kangi Alphaxard Lugola (11 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: MheshimiwaMwenyekiti, nashukuru. Nimepata masikitiko makubwa sana kutika kwenye Wizara husika ambayo inasimamia shughuli za mazingira nchini. Kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia au inaongoza Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2014; na kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo inasimamia Mfuko wa Mazingira Nchini; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo ina fedha kutoka mashirika mbalimbali nchini na duniani kote inayosimamia shughuli zote za mazingira nchini, inanijibu kwamba haitoi, haihangaiki, haina chochote, hamna jibu linalohusu shughuli za kusimamia fedha za ku- address issues za climate change nchini na tunaona dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yameleta madhara makubwa, majira ya mvua hayajulikani, kuna ukame, na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kujua, hii Wizara ipo au haipo? Na kama ipo, mbona imenyamazia kimya issue ya mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninamheshimu sana Dkt. Sware ambaye Ph.D yake ameisoma kule Stockholm, Sweden, Masters yake ameichukulia Norway, namheshimu sana, lakini kwa sababu anashindwa kutofautisha kati ya maneno mawili ambayo ni rahisi sana, yeye ameuliza swali la ruzuku na ruzuku kwa kiingereza kwa faida yako Dokta tunaita subsidies, lakini kuna kitu kingine tunaita misaada, misaada ni grants.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yeye ameuliza ruzuku, ndio nimemjibu sisi hatuna ruzuku. Lakini haya aliyoyasema leo kama angejiongeza akauliza hayo, kwa faida ya Watanzania, kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na nchi yetu mpaka leo kuanzia tarehe 6 mpaka 17 wako Bonn, Ujerumani wanashiriki mkutano mkubwa wa kimataifa kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Na sisi Tanzania ni nchi wanachama ambao tulisaini Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kule Mjini Paris na tunayo mifuko ifuatayo ambayo sisi tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa kwanza unaitwa Adaptation Fund, yani kwa maana kwamba ni mfuko wa kuhimuli mabadiliko ya tabianchi. Mfuko wa pili, unaitwa ni Least Developed Countries Fund, yaani kwa maana Mfuko wa Nchi Maskini Duniani. Na mfuko mwingine ni GEFT ambao ni Global Environmental Facility. Mfuko mwingine ni Mfuko wa Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumepata grants hizi ambazo sasa tunapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi maeneo mbalimbali hapa nchini. Tuna mradi mkubwa sana ambao Ocean Road pale kwa sababu kina cha bahari kimeongezeka tunajenga ukuta mkubwa wa kilometa moja, ili kingo za bahari zisije zikasombwa na kuharibu makazi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni tunajenga ukuta mkubwa ili kudhibiti kingo zisiendelee kubomoka. Vilevile kupitia grants hizo kule Rufiji tunarudishia mikoko ambayo ilikuwa imekatwa na mradi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Zanzibar Kisiwapanza, kule Zanzibar Kisakasaka pamoja na Kilimani mifuko hiyo inaendelea. Kule Pangani tunajenga ukuta pamoja na kurudishia mikoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bagamoyo tunajenga visiwa 28 kwa wananchi wa Bagamoyo, zikiwepo na sekondari mbili mojawapo inaitwa Kinganya ambayo ni ya Mheshimiwa Dkt. Kawambwa. Mifuko hiyo, tunaitumia kwa ajili ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania hivi sasa tunaelekea katika uchumi wa viwanda. Na moja ya ajenda/ suala muhimu ambalo linazingatiwa hivi sasa ni ujenzi wa viwanda. Na kwa kuwa viwanda ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira, kwa mfano nchi ya China pamoja na Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo hazikukubali kusaini Mkataba wa Kyoto kutokana na viwanda. Sasa ninachotaka kujua tu ni kwamba, Tanzania kwa sababu tunahitaji viwanda.
Je, tunajiandaaje ili kuhakikisha kwamba viwanda vitakavyojengwa hapa nchini haviwi sababu ya uharibifu wa mazingira? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na baadhi ya nchi matajiri ambao walikuwa hawataki kusaini Mkataba wa Kyoto lakini mkutano niliouzungumzia ambao mpaka sasa wanaendelea kule Bonn, Ujerumani. Mkutano huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa sababu makubaliano yaliyofanyika Mjini Paris kila nchi wanatakiwa sasa wasaini mkataba ule wa mabadiliko ya tabianchi. Ka hiyo, hakutakuwa na nchi hasa hizi tajiri ambazo ndizo zinazalisha hewa ya ukaa ambayo inakuja kuathiri nchi zetu maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tanzania ya viwanda ambayo sasa tunakwenda nayo, sheria yetu ya mazingira ambayo niko nayo hapa, Sheria Namba 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Sheria hii inavitaka viwanda vyote kuhakikisha kwamba kabla hawajaanza uzalishaji wawe katika ile Environmental Impact Assessment pamoja na Environmental Management Plan zao, namna ambavyo watakwenda ku-manage emissions zote ambazo zinaharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kupitia Baraza la Hifadhi la Taifa la Mazingira (NEMC) tumekuwa tukikagua mara kwa mara kuhakikisha viwanda hivi vina-comply masharti yale ambayo hayaharibu mazingira. Ndio maana viwanda ambavyo vinakaidi tunavipiga fine na vingine tunavifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwahakikishia Watanzania, katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli hakuna wazalishaji wa viwanda wanaoharibu mazingira watakaotumia nguvu za fedha kuhakikisha kwamba wanaendelea kuharibu mazingira halafu na sisi tunawatazama, lazima sheria hii itawashughulikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na athari kubwa ambazo zimetokana na mabadiliko ya tabianchi, wakazi wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakihamasishwa sana namna ya kupanda miti na wamejitahidi sana kupanda miti ili kuokoa hii hali ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, kuna wakati wakazi hawa walikuwa wameambiwa kwamba jinsi wanavyoendelea kupanda miti watapata fidia kutokana na jinsi wanavyopata miti kutoka kwenye mashirika mbalimbali duniani. Je, hili limeishia wapi? Ningeomba nipate majibu kutoka Serikalini.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba nchi yetu imeanza kuwa na dalili za kuwa na jangwa, nchi yetu inakuwa na ukame na hatuna option, lazima Watanzania kote nchini tuweze kuwa na tabia ya kupanda miti. Na kama nilivyosema juzi, ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika Ilani hii ya CCM, ukurasa wa 212 mpaka 213 unazitaka Halmashauri zote nchini wapande miti kila mwaka isiyopungua 1,500,000.
Kwa hiyo, kwa kuwa, Wananchi wa Iringa wameanza juhudi hii sisi tuko tayari kuhakikisha kwamba, hewa ya ukaa ambayo inaharibu ozone layer yaani tabaka la ozone na kusababisha miale mikubwa ya jua ule mnururisho uweze kuleta joto jingi duniani, ni kweli mashirika ya kimataifa yananunua kitu tunaita karadha, kwa jinsi ambavyo miti ile ndio inayosaidia kufyonza hewa ya ukaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa wananchi wa Iringa wameanza na wananchi wengine wameanza, Ofisi ya Makamu wa Rais itaanzisha utaratibu wa kuona ni kiwango gani wananchi wameweza kupanda miti ili watalaam sasa waweze kuona kiwango cha karadha ya ufyonzaji wa hewa ya ukaa, ili waweze kupata fidia kwenye mashirika ya kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Wizara imekuwa mara nyingi ikihamasisha tutunze mazingira na sisi kama wawakilishi wa wananchi tumekuwa tukifanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi tumsikilize Rais au tumsikilize Waziri? Mara nyingi tumeambiwa Rais akisema ni sheria. Rais jana amewatangazia wananchi kwamba walime, waingie kwenye mabonde mpaka mvua itakapowatoa na hii sheria ya Rais anayoisema Mheshimiwa Waziri inahusu tu Kanda ya Ziwa na ni sheria namba ngapi kwa sababu anazungumza kila siku kwenye Kanda ya Ziwa, analeta upendeleo wa wazi. Je, tumsikilize Rais au tumsikilize Waziri? Kwa nini kila wakati Rais akienda Kanda ya Ziwa…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msigwa ambaye alikuwa commissioner mwenzangu sasa nime-retire, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu haiongozwi kwa kupendelea wananchi wa eneo moja. Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na Katiba. Nimhakikishie na nirudie tena, alichokisema Rais wetu kule Kagera hajavunja sheria nimekwambia kifungu cha 57 kasome ambacho kinatoa mamlaka ya kuruhusu na hata wewe Mheshimiwa Msigwa kama una shughuli zako unataka kuzifanya kando kando ya ziwa au mto lete Ofisini kwetu utapata kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Mheshimiwa Msigwa mimi nimeenda Kihansi nimekuta wananchi kule Kihansi pamoja Mufindi na Ifakara wanalima kwenye bonde la Mto Kihansi na tumewasaidia kabisa wananchi wale kwenye mradi wetu ili waendeleze lile bonde kwa kilimo. Hii inaonyesha dhahiri kwamba hatubagui, wananchi wote wako sawasawa.
heshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, wananchi ambao wamezoea kuchezea sheria, Serikali ya Awamu ya Tano haitamfumbia macho yeyote ama kwa kuchochea wananchi wavunje sheria ama yeye mwenyewe kuvunja sheria watapambana na mkono wa sheria na sheria hii inatoa adhabu kwa wanaochochea. Ahsante sana. (Makofi/ Vigelegele)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yamedhihirisha kwamba katika kipindi kifupi ambacho ameshika nafasi hii kwa kweli amejua mambo kwa haraka na kwa uzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee mambo mawili, kwanza, Serikali kupitia Ofisi yetu iliziagiza lakini napenda nirudie kutoa agizo tena upya kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Halmashauri zetu kuorodhesha vyanzo vyote vya maji katika maeneo yao na kuvileta kwetu na kuelezea hatua ambazo zinachukuliwa katika kuvilinda, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kifungu cha 57 cha Sheria ya Mazingira, Na.20 ya mwaka 2004, kipengele cha (1) kinaweka zuio la kufanya shughuli mita 60 kwenye kingo za mito, fukwe na maziwa lakini kifungu kinachofuatia cha (2) kinasema, Waziri anaweza kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo yaliyoelezwa kwa mujibu wa kifungu hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya maelekezo mahsusi ya eneo mahsusi alilokuwepo Mheshimiwa Rais, kazi yetu sisi sasa ni kutengeneza mwongozo wa namna ya kufanya shughuli ile katika eneo lile lakini hapo hapo kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niliweke sawa kwa namna hiyo kwamba kutokana na maelekezo yaliyotolewa, sisi sasa sheria inatuelekeza kuweka mwongozo wa pale mahali ambapo wale watu waliomba kufanya ile shughuli namna ya kufanya ile shughuli bila kuathiri mazingira. Kwa hiyo, hakuna blanket permission ya kuvamia vyanzo vya maji na kingo za mito kote nchini. Tutaendelea kufuata sheria kwa sababu sheria bado ipo. Ahsante.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuweka kumbukumbu sawa kwenye jambo moja huku nikipongeza majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri pamoja na Waziri mwenye dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili lililosemwa kwamba Rais anapendelea Kanda ya Ziwa, nataka niweke kumbukumbu sawa kwamba Mheshimiwa Rais siyo kwamba anapendelea Kanda ya Ziwa, isipokuwa Rais amekuwa akisikiliza vilio vya wananchi pale anapokuwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo ambalo nataka nitumie kumbukumbu, Mheshimiwa Rais alipokuwa Bagamoyo, wananchi walipolilia eneo la Magereza alilitoa hapo hapo huku sheria ikiwa inataka eneo lile litumike kwa ajili ya Magereza, lakini kwa kuwa kilio cha wananchi kilikuwa kikubwa na huko siyo Kanda ya Ziwa ni Pwani, hapo hapo wala hata hakusubiri maelekezo ya Wizara kukaa kama alivyosema Kanda ya Ziwa, pale aliamua hapo hapo akasema wananchi hawa wapewe eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndivyo ambavyo nasemea ni kwamba anakuwa anatolea utatuzi changamoto za wananchi na hicho ndicho kilichomfanya achaguliwe na yuko kwa ajili hiyo. Siku atakapokuwa Ruvuma atatoa majibu hayo hayo kwenye kilio cha wananchi, siku akiwa Arusha atatoa majibu hivyo hivyo na maeneo mengine mengi ameshafanya shughuli za aina hiyo, hivyo tusije tukapotosha utekelezaji wa kazi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Uharibifu wa vyanzo vya maji katika Taifa letu la Tanzania ni mkubwa mno. Namshukuru Mheshimiwa Waziri amesema vizuri kwamba sheria tunazo lakini namna ya kusimamia hizo sheria ili vyanzo visiharibike ndiyo hafifu. Je, Wizara sasa inajipambanua vipi kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa kwa nguvu zote hapa nchini Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna wakati ambao Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kulinda vyanzo vya maji kwa nguvu zote ni Serikali ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie wewe na Watanzania wote wanaotusikiliza, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliunda Task Force ikaenda kwenye Great Ruaha ambako walikuwa wanaharibu vyanzo vya maji kuhakikisha kwamba wanafanya usimamizi, kutoa mafunzo na kuwaelekeza wananchi. Pia tumeenda Bonde la Usangu na Ihefu, tumeondoa wafugaji wote kwa maana ya kutumia nguvu kubwa kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinaimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Januari Makamba, ule Mto wa pale Katavi ambao ulikuwa umeziba kabisa, Mto Kachima, alienda pale akakuta mkulima mmoja ameweka banio amezuia maji viboko wanataka kufa njaa na watumiaji wengine hawana maji, akazibua na sasa maji yanaendelea kutoka. Kwa hiyo, tutaendelea kutumia nguvu na sheria kuhakikisha kwamba hakuna atakayevunja sheria. Yeyote atakayevunja sheria hatasalimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenu ninyi nitoe darasa la MEMKWA kwa wale walioikosa yaani Mpango Maalum kwa Walioikosa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria niliyoisema Na.20 ya mwaka 2004, kifungu cha 57, Waziri anaweza akatoa kibali kwenye maeneo ya mita 60 kutokana na changamoto aliyoiona. Ndiyo maana wakati mwingine mnaona hoteli zinajengwa ndani ya mita 60 ni kutokana na vibali. Kwa hiyo, Rais wetu hajavunja sheria na ninyi mtakapowachochea wananchi kuvunja sheria, sheria ya Rais Magufuli itapambana na ninyi. Ahsante sana. (Kicheko/Makofi)
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majawabu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Mto Makere hali yake ni mbaya sana pamoja na Mto Malagarasi, lakini sababu kubwa kuna mifugo mingi sana imeingia huko na hakuna anayeitoa. Nataka kujua ni lini sasa Serikali tutakwenda kutoa mifugo iliyovamia kwenye vyanzo vya Mto Makere pamoja na Mto Malagarasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijajibu swali la nyongeza, nitoe maelezo ya utangulizi. Wananchi wote nchi nzima kwa mujibu wa Sheria yetu ya Na.20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Uhifadhi wa Mazingira kila Mtanzania ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira. Sheria yetu pia inatoa haki kwa kila Mtanzania aishi katika mazingira safi, salama na ya kiafya. Kwa hiyo, sheria inazuia watu wengine wasiwakere watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Makere ni kweli kabisa kwamba mto ule kwenye vyanzo vyake ulivamiwa lakini uvamizi ule ulikuwa unafanywa na wale wahamiaji haramu ambao wanakuja kule Kasulu, wanawakodi wananchi wa Kasulu halafu wengine wanaenda wanakata miti usiku wengine wanalima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Wilaya ya Kasulu tumeweza kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yamevamiwa na kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi mifugo yote tumeiondoa na hata hivyo kuhusu miti; Nyarugusu, Makere yenyewe, Kwamba, Mwadivano na Kalimungoma, katika maeneo yote yale wamepanda miti zaidi ya 50,500,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Watanzania pamoja na vyombo vya habari wameanza kupotosha kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa jana kule Kagera kwamba sasa wananchi ni ruksa kwenda kuvamia maeneo oevu, maeneo ya vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kauli ya Rais isije ikapotoshwa wananchi wakaenda kuvamia maeneo ya mito na kuanza kulima. Kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais Watanzania waelewe vyanzo vya maji ndivyo uhai wetu, mito yote itakauka, hakuna anayeruhusiwa kwenda kwenye chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Rais ametumia kifungu cha 57 cha sheria hiyo kwamba pale ambapo kunakuwa na changamoto, wananchi wale ambao wako Karagwe wamekuwepo pale hawana ardhi, Rais ametuomba tushirikiane na uongozi wa mkoa kuhakikisha wale wananchi wanapatiwa maeneo mengine lakini siyo kuwaondoa.
Kwa hiyo, hamruhusiwi na msije mkasema kwamba Rais amewaruhusu wananchi kinyume na sheria. Ahsante.
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa hapa hivi sasa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza nataka kuuliza. Je, Serikali inasema nini katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji maji kwa kupitia mito mikubwa, maziwa na mabwawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na kilimo cha umwagiliaji maji, je Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo hicho. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumejibu kwenye swali letu la msingi ambapo Serikali imeweka mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji na hasa pale ambapo tunakuwa na matatizo ya ukame; matatizo ambayo yanasababisha mvua zisijulikane sana. Ndio maana mipango ambayo nimeisema katika majibu yangu ya msingi, inabidi izingatiwe.
Mheshimiwa Spika, vilevile wakulima wanashauriwa katika kilimo hiki cha kutumia maji vizuri, kikiwemo na kilimo hiki ambacho tunaita drip irrigation. Kilimo ambacho kinatumia matone ya maji na hivyo kuweza kuwa na maji mengi kwa ajili ya watumiaji wengine.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la pili ambalo ni la elimu kwa wakulima. Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la NEMC tumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwapa wakulima elimu. Vilevile kwenye Sikukuu ya Wakulima ya Nane Nane tumekuwa tukichapisha majarida mbalimbali; majarida mengine ambayo ninayo hapa ambayo baada ya hapa nitampatia Mheshimiwa Mbunge. Wadau mbalimbali na wakulima wamekuwa wakitembelea mabanda yetu na kupata vipeperushi pamoja na majarida mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mikakati ambayo tumeizungumzia hapa, nitampatia Mheshimiwa Mbunge kuna hii ya National Climate Change Strategy ambayo tumeizungumzia ya mwaka 2012 halafu vilevile tunayo miongozo ambayo ni ya kisera kuhusiana na suala la sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, niseme pia kwa faida ya Watanzania wote, masuala ya mazingira ambayo yanaathiri kilimo yameanzia kwenye Biblia ukisoma Mwanzo 10:15 ambapo Mungu alianzisha utaratibu kwenye ile mito minne akamwambia mwanadamu nakuagiza ukalime na kuitunza.
Mheshimiwa Spika, hivyo, vyanzo vya maji ni asili yake kwenye Biblia. Hii ndio maana na sisi kwa kutunga Sheria hii namba 20 ya 2004, vilevile tumechukua kipengele hicho tukaweka kifungu cha sita (6) ambacho kinatoa wajibu wa kisheria kwa kila mtanzania kutunza na kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Spika, Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Waziri bado nina swali moja la nyongeza. Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutuletea taarifa zote pale ambapo changamoto za Muungano zinapopatiwa ufumbuzi ndani ya Bunge hili ili sisi Wawakilishi wa Wananchi tuweze kumsaidia Mheshimiwa Waziri kuzifikisha kwa wananchi kwa wepesi zaidi? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga ambaye ni nyara ya CCM na tegemeo kubwa la CCM kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hilo ni zuri kwamba iko haja ya kuleta taarifa zote kwa namna ambavyo Ofisi ya Makamu wa Rais wanavyoweza kupitia Kamati yetu ya pamoja ya kero za Muungano hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu imekuwa ikitoa taarifa hizi kila wakati kama nilivyosema kwenye majibu yetu ya msingi. Zile taarifa ambazo zinatolewa kwenye maeneo hayo ya siku ya Muungano kwenye televisheni Mheshimiwa Waziri wetu tunatekeleza amekuwa akiongelea mambo haya, hata hapa Bungeni ambapo anasema ni vema tukazileta. Naomba nimhakikishie hizi Hansard hizi zimesheheni taarifa mbalimbali kuhusu namna ambavyo Serikali imekuwa ikitatua kero za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa, Mheshimiwa Najma nitakupatia hizi Hansard hizi na tayari nimeonesha maeneo yale ili usipate usumbufu ili uweze kuona namna ambavyo Serikali yeu inavyotoa taarifa hiyo. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya ndugu yangu Kangi Lugola nuru ya wanyonge, Jimbo la Mwibara, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa chanzo kikubwa cha maji ya binadamu, mifugo na wanyamapori katika eneo hili la vijiji tisa ni Mto Rubana, na kwa kuwa hakuna chanzo kingine mbadala kwa wananchi wa maeneo hayo, na kwa kuwa ardhi haiongezeki na watu wanaongezeka na mifugo inaongezeka. Je, ni lini sasa Serikali kwa kupitia Wizara yake ya Mazingira itapeleka mradi mkubwa wa maji katika vijiji hivi viwili ili kuviokoa na tatizo la maji?
Swali la pili, kwa kuwa Mto Rubana, ndiyo mpaka kati ya vijiji tisa vinavyopakana na pori hilo la akiba, la Grumeti. Je, ni lini agizo lako ulilolitoa miezi miwili iliyopita, ulipotembelea maeneo hayo kwamba mita 500 za eneo la wazi kutoka eneo la mpaka kwenda vijijini na mita 500 kutoka eneo la mpaka kwenda porini wataweka beacon?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Getere wapiga kura wako wanakuita Tingatinga la maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba baada ya uteuzi wangu nilitembelea Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na kuweza kufanya mikutano miwili Maliwanda pamoja na Hunyari, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu tayari kwa kuzingatia kwamba wananchi walikuwa wanatumia maji ya Mto Rubana kunyweshea mifugo, uvuvi pamoja na matumizi ya nyumbani, tayari katika Kijiji cha Kyandege, Kijiji cha Mugeta na Kijiji cha Mariwanda Serikali tulishawajengea malambo ya kunyweshea mifugo na mabirika ya kunyweshea mifugo yanafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna taasisi inaitwa Rubana Corridor Invironmental Development Strategy wako mbioni na wamekamilisha mchoro wa kujenga bwawa moja kubwa katika Kijiji cha Kihumbu. Pia Halmashauri ya Wilaya Bunda, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 wametenga jumla ya milioni 30 kukarabati lambo la Kihumbu na pia Foundation for Civil Society kushirikiana na asasi niliyoitaja mwanzo, tayari wanataka kujenga visima viwili vya maji katika Kijiji cha Kihumbu, ikiwa ni pamoja na kuongeza lambo moja kubwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uvuvi uliofanyika Rubana usiendelee na kuchafua mazingira, tayari Foundation for Civil Society wameendesha mafunzo ya vijiji vinne kwa ufugaji wa nyuki na sasa watasambaza mizinga 100 kwa ajili ya kuwafanya wananchi wasiende kuchafua mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu changamoto ya mita 500. Ni kweli kabisa Sheria namba 5 ya mwaka 2009 kifungu cha 74 kinazungumzia kuweka buffer zone ya mita 500 kwenda kwa wananchi. Nimhakikishie Mbunge tayari Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshawasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa TAWA pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwamba wanashughulikia masuala ya beacon. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba beacon zinazohusu wanyama na wanadamu ni beacon ambazo siyo endelevu, leo utaweka beacon ya mita 500 kwa wananchi, na hawa wanyama wao hawajui kama kuna beacon ya mita 500, baadae watasogea tena kwenye mita 500, baadae wananchi watasema wanyama wamesogea tuweke tena beacon za mita 500, mwishowe vijiji vyote vitaisha kwa kuwa beacon ya hifadhi. Hiyo ndiyo changamoto iliyopo. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Tatizo lililopo katika Jimbo la Bunda linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Jimbo la Tabora Manispaa, chanzo cha maji cha Mto Gombe kinasumbuliwa sana na tatizo la mazingira katika eneo hilo.
Je, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ina mpango gani wa kusaidia wananchi wale kunusuru afya zao za maji ambayo wanatumia wakati tukisubiri maji ya Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nchi yetu ina changamoto ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira, kwenye vyanzo vingi vya maji. Ndiyo maana mkakati mmojawapo wa kunusuru vyanzo vya maji nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa January Makamba alishatoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaorodhesha vyanzo vyote vya maji katika maeneo yao, vikiambatana na changamoto ambazo zinakabili vyanzo hivyo ili Serikali ijipange katika kunusuru vyanzo hivyo, hili la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika Ilani hii ya CCM ambayo naamini Mheshimiwa Hawa Mwaifunga anaiamini na kuisimamia itekelezwe katika maeneo yake, katika ukurasa wa 212 mpaka 213 Ilani hii inaagiza Halmashauri zote katika nchi yetu, kuhakikisha kila mwaka wanapanda miti ya kuhifadhi mazingira na kwenye vyanzo vya maji isiyopungua milioni 1.5.
Hivyo kupitia swali hili, naziagiza Halmashauri zote nchini, zitekeleze Ilani hii na baada ya Bunge hili wajue wana deni ambalo dawa ya deni ni kulipa nitaenda kukagua kuona sasa miaka miwili kwamba wana miti si chini ya milioni tatu.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa uchafuzi wa mazingira ni pamoja na uchomaji misitu hovyo unaosababisha uzalishaji hewa ya ukaa, na kwa kuwa tayari Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kupitia Mbunge wao tulishandaa andiko la mradi kwa ajili ya kupambana na uchomaji moto Mradi unaoitwa Participatory Community Based bush Fire Management and Livelihood Improvement na tukawasilisha Wizara ya Muungano na Mazingira kwa ajili ya kuanza na vijiji 15 kati ya vijiji 75.
Je, ni lini Wizara yenye dhamana itawezesha ili Halmashauri tuweze kutekeleza mradi huu ambao unaonekana kuwa na tija, kwa sababu tutapanda miti ni macadamia na ufugaji wa nyuki vitakavyopelekea kutoa ajira lakini na kudhibiti mazingira, ni lini Wizara yenye dhamana itawezesha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Alex Gashaza amekuwa akifuatilia sana juu ya andiko lake katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakikishie Waheshimiwa Wabunge na nitoe wito kwa Watanzania wote na hasa ambao wanamiliki viwanda, suala la hewa ya ukaa ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumzia ambalo ndio msingi na chimbuko la andiko lake, mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatokea sasa yanaanza kuandama nchi yetu, ni kutokana na hewa ya ukaa inayozalishwa kwenye nchi zilizoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika nchi yetu tumeanza kuwa na maendeleo ya viwanda, kwa hiyo viwanda vihakikishe vinadhibiti hewa ya ukaa isije na vyenyewe vikaendelea kuongeza ukubwa wa tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza hewa ya ukaa, pamoja na kwamba upandaji wa miti utasaidia sana kwa sababu mchana miti inavuta hewa ya ukaa, kwa hiyo, ni kweli kwamba tukipanda miti kwa wingi tutaweza kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hewa ya ukaa ni bidhaa ambayo ni adimu sana inauzwa kupitia Mfuko wa Mazingira Duniani. Ukiwa na hewa ya ukaa ukaivuna takwimu zile ukizipeleka kule ni fedha nyingi sana.
Kwa hiyo andiko lako Mheshimiwa Gashaza, Ofisi yetu inaendelea kulifanyia kazi, ili kuhakikisha maandiko ambayo tumeomba fedha kwenye mifuko ya Mazingira Duniani itakapopatikana basi andiko lako ambalo wataalam wetu wameliona ni zuri sana tutakwenda kulitekeza. Ahsante sana.