Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kangi Alphaxard Lugola (19 total)

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa majibu yake na hasa swali langu la (a) amelijibu kikamilifu na kuonyesha ni kwa kiwango gani mradi huu wa MACEMP umeweza kuwasaidia wavuvi hasa hawa wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la (b) bado nina wasiwasi kidogo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa swali langu la msingi lililenga Ziwa Victoria na hususani Mwibara wavuvi na wao wapate mradi huu wa kuwapa nyavu zinazoruhusiwa halafu wanachukua zile nyavu zisizoruhusiwa ili kuwasaidia wavuvi wadogo badala ya kuendelea kuchoma nyavu zao na wakashindwa kupata nyavu zingine ili waweze kujikimu katika maisha yao. Sasa kwa kuwa amesema Serikali itaanzisha miradi kama hii, naomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie Wanamwibara kwamba mradi huu utakapoanza Wanamwibara ndiyo watakao kuwa wa kwanza kunufaika na mradi huu wa kuwapatia wavuvi nyavu badala ya kuwachomea nyavu zao?
Swali la pili, kwa kuwa katika majibu yake ameelezea kwamba manufaa mojwapo ya mradi huu ni kuanzisha kwa BMU hao walinzi wa rasilimali, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, BMU hizi katika Ziwa Victoria kimekuwa ni kichaka cha kuwasumbua na kuwanyanyasa wavuvi, kimekuwa ni kichaka cha kuwa-harass na kuwasumbua akina Mama kuwanyang‟anya samaki, kumwaga samaki katika mwavuli wa BMU. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na sasa hivi pale Kibara pale kwenye Kijiji cha Mwibara kinamama juzi wamenyang‟anywa samaki na matokeo yake…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lugola naomba uulize swali tafadhali.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Ndiyo nauliza. Serikali itatoa kauli gani kwa BMU nchi nzima ambao sasa BMU wa Kibara pale wanaitwa Boko Haram ambao wamewanyang‟anya akina mama samaki na kuwatoza faini ya cement mifuko nane na shilingi 5,000/= wakiongozwa na VEO Ndugu Moshi, Azimio Lufunjo, Nyafuru Mgoli, Fredy Moma, Kabezi Chitalo, Mrungu….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lugola unavunja Kanuni sasa.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataja watu ambao wanawanyanyasa akina Mama Serikali inatoa kauli gani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mafanikio ya mradi huu katika maeneo mbalimbali na nia ama azma ya Serikali ya kutekeleza miradi ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mwibara, kwa kuwa Mbunge amesema anahitaji niwahakikishie wananchi wake, na mimi niseme kwamba tutakapokuwa tumeshapata uwezo huo nilioutaja na tukaanza kutekeleza kwa kuwa Mbunge ni mdau mkubwa wa kukomesha uvuvi haramu ambao amesema wananchi wake wakipewa zana wataachana na uvuvi haramu, na mimi nimhakikishie kwamba na yeye Jimbo lake na Wilaya yake itakuwa katika maeneo ya vipaumbele vya kuweza kupata mradi huo ili waachane na uvuvi haramu.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la kuanzisha shule za kidato cha tano katika nchi yetu linafanana kabisa na tatizo ambalo liko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ambayo ni kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna hata high school moja kwenye hiyo Halmashauri yetu ya Wilaya ya Bunda. Wananchi katika miaka mitano tumewahamasisha, tumejenga mabweni na mabwalo lakini tumeshindwa kukamilisha kwa sababu ya fedha na Serikali tumekuwa tukiitaka itusaidie.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kuambatana na mimi na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere ili twende kwenye Halmashauri yetu ukajionee juhudi za wananchi ili muweze kutusaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kiufupi Mheshimiwa Kangi Lugola ndugu yangu nikuambie kwamba, mimi niko tayari kuambatana na wewe na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere ambaye ni jirani nyuma yangu hapa. Tutajitahidi tuende pamoja siyo kwa suala hilo la shule tu inawezekana tukabaini mambo mengi sana kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ucheleweshaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo limejitokeza kwenye Jimbo la Mwibara ambako Miradi ya Maji ya Bulamba, Kibara pamoja na maji ya Mji wa Bunda kutoka Nyabehu, zaidi sasa ya miaka saba, fedha bado zinacheleweshwa kwenda. Hili ambalo analisema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, lazima certificate zile ziandaliwe na zihakikiwe, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na Engineer ya Maji wa Wilaya, tulishasukuma sana hizi certificate na kuna mabarua mengi Wizara ya maji. Sasa je, Mheshimiwa Naibu Waziri ataliambia vipi Bunge hili kwamba hata zile certificate ambazo zilishahakikiwa bado fedha haziendi, ni uzembe wa Wizara au ni uzembe wa mtu gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane moja kwa moja, aje ofisini kwa sababu sina taarifa kwamba kuna certificate ambayo haijalipwa. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa bilioni 15 na certificate zote zimelipwa, sina pending certificate ambayo imebaki kwenye ofisi ambayo haijalipwa. Kwa hiyo, kurahisisha kazi Mheshimiwa Mbunge, naomba awasiliane na mimi ili tuweze kuangalia ni nini kimetokea.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa, Jimbo la Mwibara ambalo kwa muda mrefu kulingana na jiografia yake matukio kwenye visiwa ya ujambazi tulishaomba kuwa na Wilaya ya kipolisi. Je, Serikali mpaka sasa ina mpango gani wa kujenga kituo cha Polisi na kutupa hadhi ya Wilaya ya kipolisi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, upo mpango wa kujenga vituo vya Polisi nchi nzima, ambapo kimsingi tuna upungufu mkubwa wa vituo vya Polisi vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 4,500 nchi nzima ikiwemo eneo ambalo Mbunge amelizungumza. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua changamoto ya upungufu wa vituo vya Polisi ikiwemo katika Jimbo lake na tupo katika harakati za kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo hilo katika Jimbo hilo na maeneo mengine ya nchi nzima.
MHE. KANGI. A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila raia wa nchi hii anayo haki ya kuishi na katika Ibara hiyo haikuainisha haki ya kuishi kwa kutumia vigezo vya itikadi za vyama, wala kigezo cha ukabila, wala kigezo cha udini, wala kigezo cha umri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa kauli gani kwa Watanzania na hata Wabunge ambao wamekuwa na tabia ya kuhusisha kila vifo vinavyotokea na masuala ya itikadi za kisiasa ili liwe fundisho kwa wananchi wenye tabia hiyo kwa sababu maswali kama hayo yanaleta uchochezi na yanaweza yakasababisha maafa na hata uhasama wa kudumu kati ya koo ambazo yule mwananchi amekufa? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na niseme kitu hiki na Watanzania wasikie na wapokee.
Moja, Mtanzania hawi na madaraja kutokana na chama chake, dini yake ama kabila lake. Hakuna nusu Mtanzania kwa sababu ya chama alichonacho na hakuna Mtanzania daraja la pili kutokana na chama alichonacho. Watanzania wote ni Watanzania daraja la juu na wana haki sawa za kuishi na viongozi wanaowagawa Watanzania na kuwatengenezea chuki hata wakadhuriana kwa misingi ya kisiasa wanapaswa kupuuzwa na ndio maana sisi tukiona kiongozi anayefanya vitu vya aina hiyo tunachukua hatua.
Kwa hiyo, wao kwa watanzania maeneo popote pale walipo wasije wakagawanywa kwenye misingi hiyo na niliwahi kuisema eneo moja na ninarudia tena wasije wakaenda kwenye kuuana kwa misingi ya vyama ile hali sisi ambao tunakuwa viongozi huku na wakati mwingine tunawasukuma kufanya hivyo tukija huku wakishatuchagua tunagongesha glass za juice marazote tunapoonana hapa ili hali wao kule wameshasababisha yatima, wajane na kusababisha matatizo katika familia. Kwa maana hiyo nitoe rai kwa Watanzania na nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba tunalinda Utanzania wetu na undugu wetu ambao tumeachiwa na hawa waasisi wetu na ili Taifa letu liweze kupata heshma inayolinda utu.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa suala hili linahusu masuala ya Balozi; na kwa kuwa katika nchi yetu tuna Mabalozi wa CCM ambao wanafanya kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo, na pia kusuluhisha migogoro ambayo inajitokeza maeneo ya vijijini; je, Serikali iko tayari kuwasaidia Mabalozi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu nitoe maelezo ya kushauri tu kwamba Mabalozi ninaowazungumzia mimi ni Mabalozi wa Mambo ya Nje. Lakini labda Mheshimiwa Kangi Lugola amewahusianisha hawa Mabalozi wa Mambo ya Nje kwa sababu ya mchanganyiko uliotolewa na Kambi ya Upinzani, kuwafananisha Mabalozi wa Mambo ya Nje na Mabalozi wa Nyumba Kumi Kumi. Lakini nimhakikishie tu kwamba sisi tunazungumzia Mabalozi wa Tanzania wanaotuwakilisha nje ya nchi na wanafanya kazi yao vizuri. Lakini vilevile najua kabisa kwamba, Mabalozi wa Nyumba Kumi Kumi walioko ndani ya Tanzania wanafanya kazi yao vizuri kuhakikisha kwamba masuala yanakaa salama.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mwaka 2015 niliuliza hapa Serikali imejipanga vipi kupambana na magugu maji kwenye lambo la Kabainja ambalo liko Wilaya ya Bunda Jimbo la Mwibala na Serikali hii ikaahidi Bunge hili kwamba malambo yote ambayo yana magugu maji na malambo yote ambayo yalichakachuliwa kwa maana kwamba hayakukamilika itatenga fedha na kuanzisha mpango maalum ambao nadhani Mheshimiwa Chenge alikuwa anashauri. Je, kwa nini Serikali sasa haizungumzii mpango huu ambao waliuzungumzia mwaka 2015 sasa wanaanza kutupa majibu mengine mapya kana kwamba ndiyo wanataka wajipange upya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya siyo majibu mapya ni mpango ule ule wa Serikali unaendelea. Nimjulishe Mheshimiwa Kangi Lugola lengo letu ni nini. Maana suala la magugu maji ni jambo moja lakini malambo mengine tukiyafanyia utafiti kuna mengine yanakufa kutokana na shughuli za kijamii ambazo zinazunguka malambo hayo. Kwa hiyo, mpango wa Serikali katika kuhakikisha tunapambana na magugu maji uko pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaenda kwenye detail ya kila Halmashauri kuonyesha imejipanga vipi katika kushughulikia suala hilo lakini tunaendelea vilevile na suala la kutoa elimu maana kuna maeneo ambapo malambo yanakufa siyo kwa sababu ya magugu maji bali ni kutokakana na kazi za kijamii hasa kilimo. Watu wanapofanya shughuli za kilimo na mifugo kuzunguka haya malambo mwisho mvua inaponyesha udongo unasombwa unajaza malambo na kusababisha yafe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna mpango mpana, licha ya suala la magugu maji lakini elimu katika maeneo mbalimbali inaendelea kutolewa kwa wananchi. Lengo kubwa ni kuhifadhi vyanzo vya maji ili visije vikafa kabla ya muda uliokadiriwa. Hili limekuwa ni tatizo kubwa hasa malambo mengi kujaa matope na mchanga ukiachia magugu maji ambapo ndani ya muda mfupi yanakufa lakini inasababishwa na wakazi wenyewe wa maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Serikali tumeendelea kutoa elimu na tunaomba sana ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge wote. Agenda hii ni yetu sote, lazima tupambane nayo. Mwisho wa siku ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maji katika maeneo yake.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Majibu ya Serikali kwa kweli yanawakatisha tamaa walemavu na hasa ambao wako vijijini. Kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hii Sheria Namba 9 ni tangu mwaka 2010, lakini leo katika majibu yake ya msingi ndiyo anatamka mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali sasa inawaagiza watendaji waharakishe kuunda Kamati za Walemavu Vijijini.
Je, kama Mheshimiwa Amina Mollel asingeuliza swali hili leo ina maana Serikali haikuwa na mpango wa kuwaagiza watendaji kwa ajili ya uharakishaji wa uundaji wa hizi Kamati za Walemavu kule Vijijini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kabisa naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa katika swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Serikali haijaanza kutekeleza Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia huduma kwa watu wenye ulemavu. Naomba nikuhakikishie wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwamba haya yote ambayo mnaona yamekuwa yakiendelea, yanayowagusa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania ikiwemo upunguzaji wa gharama ya vifaa vyao; ikiwemo namna tofauti ya kuhakikisha kwamba elimu inakuwa inclusive kwa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania, ikiwemo namna ya kuunda Mabaraza hayo kwenye maeneo yetu ya Halmashauri zetu ndani ya Serikali za Mitaa. Ni utekelezaji wa sheria hiyo, ninaomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mipango yote ipo na imeshaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha msingi hapa wote kwa pamoja sasa na hasa tunapokaa katika vikao vyetu vya Mabaraza ni kuendelea kuona kwamba yale maagizo ambayo tumeshayaweka na kuyateremsha kwenye Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kwamba yanatekelezeka na kama mnaona kuna tatizo mtupe taarifa ili tuweze kusimamia zaidi. Lakini naomba niwathibitishie kwamba sheria hiyo hiyo imeanza kufanya kazi na sisi kama Serikali tumekuwa tukiisimamia na siyo tu tumesubiri swali hili la Mheshimiwa Amina Mollel. Nakushukuru.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona kwa kuwa kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Doto inaonyesha Wizara ina nguvu za kutosha za kupambana na wananchi ambao wanavamia maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Wizara ya Maliasili itatmia nguvu hizo hizo kuzielekeza kwenye Ziwa Victoria kupambana na mamba ambao pia wamevamia wananchi wangu kuwala na wengine kuwajeuri ili kuhakikisha kwamba wanawavuna wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi wa Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza si sahihi sana kusema kwamba Serikali inatumia nguvu nyingi sana kwa maana ya matumizi ya mabavu wakati wa kusimamia sheria zake. Inawezekana hapa na pale watekelezaji wa sheria pengine huweza kufanya yale ambayo si sahihi sana. Lakini jambo la msingi sana kwa upande wa Serikali ni kusimamia sheria kwanza kwa kutoa elimu kuwaelimisha wananchi ili wasiweze kukiuka sheria na kuweza kutii sheria kwa hiyari huo ndiyo mwelekeo.
Lakini kuhusu suala la mamba wanaosumbua pengine wanaleta madhara ya wananchi kuuawa au kujeruhiwa hili ni suala ambalo limo pia kwa mujibu wa kanuni na taratibu upo utaratibu wa kufanya uvunaji kwa utaratibu ambao unatambulika kisheria na kisayansi na pale ambapo inaonekana kuna haja ya kuchukua hatua ambazo ni za dharura zaidi kuliko ule utaratibu wa uvunaji, basi utaratibu huo unaweza ukafuatwa. Sasa kwa kuwa ametaja eneo mahususi kule Ukerewe nalichukua na naliorodhesha na tutaenda kuangalia ni kwa kiwango tatizo hili la mamba linaleta matatizo kwenye eneo alilolitaja ili tuweze kuona kama tunatumia kanuni za kawaida za uvunaji ama tunaweza kulichukua kama suala la dharura na kuweza kwenda kuchukua hatua zinazostahili.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la fidia ambalo linawakabili wananchi wa Mbinga Vijijini katika kupisha ujenzi wa barabara ya lami, ndilo pia linalowakabili wananchi wa Jimbo la Mwibara ambako kuna barabara ya lami ya Nyamuswa – Bunda - Kisolia - Nansio inajengwa kilomita 50 kutoka Bulamba kwenda Kisolia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alitembelea ujenzi wa barabara ile akaahidi kwamba wananchi wale watalipwa fidia. Sasa nataka kupata majibu ya Serikali, wananchi wa Mwibara wategemee lini wataweza kulipwa fidia zao kwa nyumba zilizobomolewa na mashamba yaliyopitiwa na barabara ya lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri, kaka yangu Mheshimiwa Lugola amechomekea hapa vizuri sana. Kwa sababu barabara hizi zina sura tofauti. Hii barabara anayosema Mheshimiwa Kangi Lugola iko chini ya Wizara ya Miundombinu na huku tunazungumzia barabara ya Halmashauri ambayo ilipata ufadhili maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikifanya rejea, siku ya Wizara ya Miundombinu, swali hili liliulizwa vizuri sana na Waheshimiwa Wabunge huko. Nadhani lilitolewa ufafanuzi kwamba Serikali itahangaika kutafuta fedha, pale itakapokuwa mambo yamekamilika, wananchi watalipwa fidia; kwa mujibu wa rejea ninayoifanya ya siku hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nina imani kwamba maswali yale au majibu yale yaliyokuwa yanafanyiwa rejea siku ya Wizara ya Miundombinu, yatabaki vilevile. Naomba nikiri wazi, Kangi Lugola kwa sababu ni mpiganaji mzuri sana, kilio chake kitakuwa kimesikika vizuri na Serikali.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Suala la fidia katika kupisha ujenzi wa barabara kule Mwandiga linafanana kabisa na barabara ya lami inayojengwa kutoka Nyamswa - Bunda - Kisolya - Nansio ambayo na yenyewe wananchi kule wanastahili kufidiwa. Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka nimemsumbua sana juu ya jambo hili, nimemsumbua sana Mheshimiwa Waziri, lakini wananchi kule wanadhani mimi sifanyi kazi wanadhani siwasilishi matatizo yao.
Naomba kupitia kinywa chake ndani ya Bunge hili, Wanamwibara wanamsikia, atuambie ni lini fidia ya Wanamwibara hawa watafidiwa kwa sababu wamepisha ujenzi wa barabara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Kangi Lugola kwa namna anavyofuatilia haki za wananchi wake. Namuomba sana kwamba wale ambao wanastahili kulipwa fidia tulimuahidi kwamba Serikali itahakikisha watu hawa wanalipwa fidia mara tutakapopata fedha. Hapa hatuongelei watu ambao hawastahili kulipwa fidia kwa maana ya wale ambao majengo yao yalikuwa ndani ya eneo la hifadhi.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa fursa niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa
Naibu Waziri katika majibu yake ya msingi ametamka neno fidia, kuhusiana na kuwafidia wale watakaoathirika na ujenzi wa kiwanja cha ndege Singida. Kwa kuwa neno hilo fidia
amewatonesha na kuwakumbusha wananchi wa Mwibara ambao barabara ya Bunda, Kisoria na Nasio kwa miaka mingi hawajafidiwa. Je, wananchi hao wanataka kumsikia Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini watafidiwa au kwenye mwelekeo wa bajeti fidia ya Mwibara ipo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lugola amekuwa akifatilia sana suala la fidia katika eneo lake, na naomba nitumie fursa hii kumdhihirishia yale ambayo tumekuwa tukimwambia ofisini na maeneo mengine ambako amekuwa akituuliza swali hili ni sahihi, kwamba tunatafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia na kwa kweli nimhakikishie mara tutakapopata hizo fedha suala la fidia hilo tutalishughulikia kwa kazi sana.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yenye majimbo ya Mwibara na Bunda ni majimbo mawili ambayo hayapakani. Jimbo la Bunda liko kwingine na Jimbo la Mwibara liko kwingine, lakini ndiyo yanaunda Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili
tulishampelekea Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, na kwa kuwa Mwibara iliwahi kuwa Jimbo tangu mwaka 1974, lakini tulishapeleka TAMISEMI iwe Wilaya mpaka leo vigezo ilishatimiza lakini hatupatiwi.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wana - Mwibara juu ya jambo hili ambalo ni changamoto ya miaka mingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, wasiofahamu hili Jimbo la Mheshimiwa Kangi Lugola ni sawasawa kama unazungumza kama lile bakuli halafu katikati kuna kile kisahani. Katikati ya kisahani pale unapata Jimbo la Dada yangu Mheshimiwa Ester Bulaya, Jimbo la Bunda Mjini. Ukienda huku utakuta Jimbo la ndugu yangu Mheshimiwa Boniphace Getere na huku unakuta Jimbo la Mwibara, kwa
hiyo anachozungumza ni kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie
Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine tunapoenda kufanya maamuzi ya mgawanyo wa haya maeneo wakati mwingine hatuweki mipaka sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pale hata
ukiangalia ni kama yai, katikati kiini cha yai ndiyo Jimbo la Mheshimiwa Ester Bulaya hata ninaamini inawezekana ukatokea ugomvi mkubwa wa wapi Halmashauri ya Jimbo hilo itajengwa inawezekana ni kutokana na huko mwanzo maamuzi yetu hayakuwa sahihi. Inawezekana ilikuwa ni mihemko ya kisiasa ya kugawanya, jinsi gani tugawanye, hatukufanya maamuzi sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba hili kweli ni changamoto kubwa. Kama Mheshimiwa Kangi Lugola nafahamu kweli changamoto yako ni kubwa na nimefika mpaka kule ziwani siku ile nilivyofika, nimechanginyikiwa kweli Jimbo lako lilivyo. Basi mtajadiliana kwa pamoja kule katika vikao vyenu kuangalia nini cha
kufanya. Jukumu letu kubwa Serikali ni kuona jinsi gani tutafanya ili wananchi waweze kupata huduma. Hivi sasa ninaamini wewe na Mbunge mwenzako ni lazima mkae vizuri la sivyo inawezekana mkapishana wapi Makao Makuu yenu itaenda kujengwa kwa maslahi mapana ya maeneo yenu. Ahsante sana.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa suala la umbali linalowakabili wagonjwa wa UKIMWI kule Njombe ndilo hilo hilo ambalo linawakabili akina mama wajawazito wa Jimbo la Mwibara. Kutoka katika Kituo cha Afya cha Kasiguti pamoja na Kisorya kwenda Hospitali ya Misheni ni takribani kilometa 40. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la bajeti kuambatana na mimi ili twenda kwenye Kituo cha Afya cha Kisorya na Kasuguti ajionee namna ambavyo wananchi wametumia nguvu zao kujenga wodi ili Serikali iweze kutusaidia kukabiliana na changamoto ya umbali mrefu inayowakumba akina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Waziri wangu Mheshimiwa Boniface Simbachawene tumekuwa na mkakati mkubwa sana wa kuyafikia maeneo mbalimbali. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa tutaangalia tufanye utaratibu gani ili tuweze kufika katika maeneo yake, lakini siyo hapo peke yake tutafika mpaka Rorya pamoja na Tarime kule kwa sababu kuna changamoto mahsusi katika Mkoa wa Mara ambazo lazima twende tukazifanyie kazi.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Wilaya ya Bunda ni Wilaya kubwa na ina majimbo matatu ya uchaguzi, ikiwemo Bunda, Bunda Mjini na Mwibara; na kwa kuwa tayari Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, miaka saba sasa iliyopita tulishaamua Mwibara iwe Halmashauri ya Wilaya lakini mpaka leo Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia mambo ya uchambuzi na vigezo; je, ni lini mambo ya uchambuzi na vigezo vitafikiwa ili Jimbo la Mwibara sasa miaka saba tangu wananchi wameomba iweze kupatiwa Halmashauri yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kangi Lugola amehamisha goli, lakini hakuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Mheshimiwa Kangi alivyosema Jimbo la Mwibara, kwanza anafahamu kwamba zamani kwanza walikuwa na majimbo mawili pale, lakini walikuwa na Halmashauri moja, baadaye wakagawanyika tukapata majimbo matatu na Halmashauri mbili; Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Bunda Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyokuwepo ni kwamba haya majimbo mawili; Jimbo la Mwibara na Jimbo la Bunda Vijijini ukiangalia jiografia yake, haiko sawasawa. Unatoka Jimbo la Mheshimiwa Boniphace Getere, unaenda katika Jimbo la Mheshimiwa Bulaya, halafu unaenda tena Jimbo la Mheshimiwa Kangi Lugola.
Mwenyekiti Mwenyekiti, haya majimbo mawili ambayo ni kwa upande mmoja Magharibi na mmoja Mashariki, katikati kuna Jimbo lingine lakini haya majimbo mawili ni Halmashauri moja. Hili sasa tusema kwamba inawezekana kuna mapungufu yaliyofanyika kule mlipokuwa mnafanya maamuzi kwamba Jimbo hili ligawanyike vipi, ndiyo changamoto kubwa iliyokuwepo hapo. Kwa hiyo, kikubwa zaidi tuseme kwamba mchakato ule ulikwenda lakini tulipata majimbo haya mawili ya Mji na Bunda Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaelekeza, pale itakapoonekana kuna mahitaji ya ziada hasa katika maeneo yale inaonekana kuhudumia Halmashauri ile katika Majimbo mawili ambayo yako sehemu mbili tofauti ni changamoto kubwa, basi mtaleta maombi haya ili tujadili kwa pamoja nini kifanyike. Lengo kubwa ni kuwapatia wananchi huduma ya karibu katika maeneo yao.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwa kinywa chake katika majibu yake ya msingi kwamba, kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi yetu hakuna uhusiano na utozaji wa bidhaa au huduma kwa dola.
Je, anataka kuwaaminisha wachumi wote Tanzania na duniani kote na Bunge hili kwamba hata miaka mitano tukiamua kutumia dola tu bila kutumia shilingi na baadaye tukairejea baada ya miaka mitano tutakuta uchumi wetu haujaathirika na wala shilingi yetu haijaathirika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, si kuwaaminisha Wachumi, kama nilivyosema nimeeleza sababu ya kushuka kwa thamani ya currency yoyote ile hata kama sio shilingi ya Tanzania. Kuweka quotation kwa bei ambayo siyo shilingi ya Tanzania si sababu mahsusi, lakini naomba kumwambia Mheshimiwa Kangi Lugola kwamba ni asilimia 0.1 tu ya watu ambao wanaweka quotation kwa bei ambayo sio shilingi ya Tanzania ambao wako tayari kupokea fedha hii kwa kutumia currency ile waliyo-quote. Zaidi ya asilimia 99.9 ya Watanzania na wafanyabiashara wanaoweka quotation kwa pesa ambayo sio T-Shillings wako tayari kupokea bei yao na kuuza bidhaa zao na kupokea shilingi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kangi Lugola kama nilivyosema ziko indicators. Viko viashiria mbalimbali vinavyosababisha kushuka kwa uchumi na hatuna sababu ya kusema kwamba tuweze kuweka miaka mitano tufanye quotation na tusitumie shilingi yetu ya Tanzania. Nimesema kupitia Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, Kifungu cha 26 ni shilingi ya Tanzania ndiyo legal tender document ambayo inaruhusiwa ndani ya Taifa letu. (Makofi)
MHE. ALPHAXARD K. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alishuhudia mgawanyo wa majimbo mawili ya Bunda na Mwibara kutokutana ndani ya Halmashauri moja. Na kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri wa wakati huo, Mheshimiwa Simbachawene alikuja kushuhudia na kuamua kwamba, wabadilishe mipaka Jimbo la Bunda lirudi Bunda Mjini wawe Halmashauri moja na Mwibara ibaki yenyewe iwe halmashauri wakatuahidi watatoa Government Notice muda si mrefu na ilikuwa mwezi wa saba. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo GN imefikia hatua gani, Wana-Mwibara wanataka kusikia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli analozungumza Mheshimiwa Mbunge hapa hazushi na bahati nzuri mimi nimepata fursa ya kutembelea majimbo haya yote matatu, Jimbo la Mwibara, Jimbo la Bunda Vijijini, hali kadhalika Jimbo la Bunda Mjini. Mgawanyiko wake kwa kweli, ulikuwa una changamoto kubwa sana na bahati nzuri harakati hizi zimeshaanza.
Naomba nichukue ombi lako hili Mheshimiwa Kangi, twende tukalifanyie kazi kwa undani kujua kwamba, hili jambo limefikia wapi na hasa taratibu zilizofuatwa pale, baadaye tutaweza kutoa maamuzi sahihi, lakini sitaki kutoa commitment ya moja kwa moja hapa, tunalifahamu hili jambo tutaenda kulifanyia kazi kwa maslahi mapana ya hizi halmashauri zetu ambazo ziko kule.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha kutokukamilika mradi wa maji wa Kibara, mradi wa maji wa Bulamba na mradi wa maji wa Nyabehu na hata Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda alifika maeneo yale na Mheshimiwa Maghembe. Sasa nataka kujua miradi hiyo mitatu kwasababu ni zaidi ya miaka nane itakamilika lini kwa sababu Mbunge wao amepiga kelele sasa mpaka hata mate yamenikauka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema kwamba mradi umechukua miaka nane ni ukweli. Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tumeianza kwenye bajeti ya mwaka 2006/2007; kwa hiyo, umakta ijumlisha mpaka leo unakuta inakwenda kwenye hiyo miaka saba mpaka miaka nane. Ndani ya hiyo programu tulikuwa na miradi 1810, hadi leo tumeshakamilisha miradi 1333, bado 477. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndani ya hiyo ambayo imebaki ni pamoja na miradi yako Mheshimiwa Mbunge na tumeendelea kutenga fedha na mwaka wa fedha huu tulionao 2016/2017 tuliamua sasa kila Halmashauri kuiwekea bajeti, tukaweka maelekezo kwamba wakamilishe kwanza miradi inayoendelea kabla ya kuingia kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mbunge, kama kuna changamoto yoyote ile ambayo kama Wizara tunaweza kuingilia kitaalam basi naomba tuwasiliane ili tuweze kushughulikia hilo kuhakikisha kwamba miradi hiyo imekamilika.
MHE. KANGI A.LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Waheshimiwa Wabunge hapa kila tukigusa maombi ya fedha kwenye miradi ya maji, barabara na afya tunaambiwa pale hali ya uchumi itakapokuwa nzuri. Leo pia tunagusa suala la posho za Madiwani tunaambiwa hali ya fedha itakapokuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye bajeti hii anasema hali ya uchumi ni nzuri na kwenye ukurasa wa tatu wa taarifa ya Benki, hii hapa ninayo, wanasema uchumi umekuwa kwa asilimia saba, ni kiwango kikubwa sana cha kimataifa. Sasa je, hii hali ya uchumi wanayotaka ni asilimia ngapi ndiyo hali ya uchumi itakayokuwa nzuri? Mimi nashindwa kuelewa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza hali ya uchumi itakapokuwa nzuri; ni kweli tunakwenda vizuri, lakini malengo ya Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kwenda mbali zaidi na ndiyo maana najua suala hili la posho si kwa Madiwani peke yake ni hata Walimu pamoja na watumishi wengine, kila mtu anataka angalau mshahara wake uweze kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumesema kwamba acheni Serikali kwanza ijipange vizuri katika hili. Tunajua tuna vipaumbele vyetu vingi sana ambavyo ni lazima vyote tuvitekeleze. Ngoja tujipange vizuri, lakini kila kundi litaweza kufikiwa kwa kadri Mheshimiwa Rais alivyojipanga na Serikali yake ya Awamu ya Tano na hatimaye kila mtu ata-realize kwamba kweli hatukufanya makosa katika kupanga mipango muafaka kwa ajili ya nchi yetu.