Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John John Mnyika (12 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Katiba na Sheria ina wajibu wa kuiwezesha nchi kuwa na mfumo mbalimbali wa Kikatiba na Kisheria katika kufanikisha Mipango ya Maendeleo ya Taifa. Pamoja na wajibu huu muhimu hotuba nzima ya Waziri haijazungumzia kabisa kuhusu mchakato wa Katiba mpya. Aidha, katika vitabu vya bajeti hakujatengwa fedha zozote/kiasi chochote kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Katiba mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali inadhihirisha kwamba Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli lazima dhamira ya kuendeleza kwa wakati mchakato wa mabadiliko ya katiba. Hivyo ni vyema Serikali ikatoa kauli hii Bungeni ni kwa nini haijatenga fedha kwa ajili ya mchakato huu muhimu kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika aya ya 20, 21, 22, Waziri wa Katiba na Sheria amezungumzia kuhusu utekelezaji wa mkakati wa kuboresha huduma za Mahakama ikiwa ni pamoja na kufanya ujenzi na ukarabati wa Mahakama mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika orodha hiyo imetajwa Wilaya mpya ya Kigamboni, hata hivyo Wilaya mpya ya Ubungo haijatajwa hivyo, Serikali itoe kauli ni kwa nini Wilaya mpya ya Ubungo haijajumuishwa na lini Mahakama ya Wilaya ya Ubungo itajengwa. Aidha, Mahakama hiyo ni vyema ikajengwa katika Jimbo la Kibamba yalipo Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Ubungo kama ilivyopendekezwa kwa nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya kurekebisha Sheria ina wajibu na mpango muhimu ya maboresho ambayo yamependekezwa muda mrefu ni pamoja na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mfumo mzima wa Mahakama na utungaji sheria nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeeleza kuwa imefanya uchaguzi kuhusu mabadiliko yaliyowasilishwa katika THUB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa Mbunge wa Ubungo niliwasilisha malalamiko na madai ya kutaka, uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi yake ya utawala bora juu ya mgogoro wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matatizo ya maji katika Kata ya Goba naomba kupatiwa majibu juu ya hatua ambazo Tume imechukua na kupatiwa nakala ya ripoti ya Tume kuhusu uchunguzi huo. Aidha pamoja na uwekezaji mkubwa wa Serikali juu ya miradi ya Ruvu juu na Ruvu chini tume ielewe kwamba Goba bado imeachwa kama kisiwa kwa kuwa haina mtaro wa mabomba.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kugawanywa kwa Manispaa ya Kinondoni na kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Ubungo, Hospitali ya Mwananyamala kwa sasa inahudumia zaidi Manispaa ya Kinondoni. Hospitali ya Sinza Palestina iliyobaki katika Wilaya ya Ubungo haina hadhi na uwezo wa kutoa huduma kwa Manispaa nzima. Hivyo, Wizara ichukue hatua za haraka za kuboresha huduma katika hospitali hiyo ya Palestina ilingane na wajibu wa kutoa huduma kwa Manispaa mpya ya Ubungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, hospitali hiyo iko mbali na Jimbo la Kibamba lenye Kata za Goba, Saranga, Msigani, Mbezi, Kwembe na Kibamba; na pia kimuundo Wilaya ya Ubungo inapanuka kuelekea Kata hizo za pembezoni makao makuu ya muda ya wilaya yakiwa kwenye Kata ya Kibamba na ya kudumu yakitarajiwa kujengwa kwenye Kata ya Kwembe. Kadhalika kuna ujenzi wa Mji Mpya wa Viungani (Satelite town) katika eneo la Luguruni hivyo, ni muhimu kukawa na mkakati wa kupandishwa hadhi kituo cha afya kuwa hospitali ya wilaya na zahanati kuwa, kituo cha afya katika kila mojawapo ya kata hizo za pembezoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba, kuna hospitali kubwa katika Chuo Kikuu cha Afya (MUHAS), Campus ya Mloganzila. Hata hivyo, hospitali hii hadhi yake itakuwa sawa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo, haitakuwa rahisi kwa wananchi wa Jimbo la Kibamba kupata huduma za kawaida zinazotolewa na vituo vya afya na hospitali za wilaya. Hivyo, ni vyema Wizara ikafanyia kazi mchango huu na kunipatia majibu yanayostahili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOHN J. MNYIKA: Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ina wajibu mkubwa wa kujenga Taifa linalohabarishwa, lililoshamiri kiutamaduni, lenye kazi bora za sanaa na lenye umahiri wa michezo. Hata hivyo, wajibu huu haujaweza kutekelezwa mpaka sasa na bajeti ya mwaka 2017/2018 haielekei kujenga msingi mzuri wa kuwezesha azma hiyo kutekelezwa ifikapo 2025.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maendeleo ya Sekta ya Habari, Taifa linarudi nyuma kwenye kuwezesha uhuru na haki kwa mujibu wa ibara ya 18 na 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966 ambao Serikali imeridhia. Hivyo, Serikali ifanye marekebisho ya Sheria zote zilizotungwa katika Bunge la Kumi na Bunge la Kumi na Moja zenye kukwaza uhuru na haki wa/ya habari. Aidha, Waziri katika majumuisho aeleze hatua ambazo Serikali imechukua kwa viongozi na watendaji wa Serikali walioingilia uhuru wa habari ikiwemo juu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuvamia Clouds Media akiwa na watu wenye silaha.

Maendeleo ya utamaduni wa nchi yetu yanategemea sana ukuaji wa lugha ya Kiswahili na matumizi yake. Katika majumuisho Wizara ieleze Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika ngazi zote za mahakama nchini. Aidha, Serikali inapoleta Miswada ya Sheria Bungeni inaleta Miswada hiyo kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili ambayo inafanya kisheria lugha rasmi ya sheria hizo kuwa Kiingereza, Wizara ishawishi katika Baraza la Mawaziri na ngazi zote za Serikali ili Miswada yote iletwe ikiwa katika lugha ya Kiswahili pekee.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika aya ya 45 ya Hotuba ya Waziri ukurasa wa 25 imetajwa Kamusi kuu mpya ya Kiswahili. Ni vyema Wabunge tukapatiwa nakala ya kamusi husika.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa TFF kuandaa vituo vya ufundi vitakavyokuwa na vifaa stahiki kila mkoa kwa madhumuni ya kulea vipaji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya michezo. Hata hivyo, kwa Mkoa wa kiserikali wa Dar es Salaam idadi ya vijana wenye vipaji ni kubwa kwa mkakati kuweza kutekelezwa kwenye ngazi ya mkoa. Hivyo ni vyema mkakati huo ukatekelezwa kwenye ngazi ya Wilaya na nawasilisha rasmi ombi kwa TFF kwa kituo kuwekwa katika wilaya mpya ya Ubungo katika Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa upande wa maendeleo ya soka la wanawake, TFF itoe majibu kwa Wizara ni kwa kiwango gani imeifaidia timu ya Mburahati Queens ambayo inatoa wachezaji wengi kwenye timu ya Taifa ya wanawake kama ilivyoahidi kwa nyakati mbalimbali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze na hili suala la nyongeza ya fedha kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji. Tunaweza tukakimbilia kufanya maamuzi, maamuzi ambayo yakawa na athari ya ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi, kwa hiyo, badala ya kupunguza tatizo tukaongeza tatizo. Tatizo letu la msingi ambalo naliona katika Serikali hii inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi ni vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kama Serikali inaamua kununua ndege (Dreamliner) kwa quotation ya watu wa Boeing wanasema dola milioni 224 ambayo ni takribani shilingi bilioni 400 Serikali haitaki kusema walichokubaliana hasa ni kiasi gani wanasema ni pungufu ya shilingi bilioni 400. Kama tunaweza tukatoa pesa kununua ndege shilingi bilioni 400 hivi ni nini kinatushinda kutoa shilingi bilioni 400 kuongeza kwenye bajeti ya Wizara ya Maji? Kwa hiyo, ndiyo maana nimeanza kwa kusema kwamba, tatizo letu kubwa ni kipaumbele. Serikali ya CCM kwa awamu zote pamoja na kuwa inatamka kuwa maji ni kupaumbele number one katika nchi hii, lakini kwenye bajeti kwa nyakati mbalimbali maji hayajawahi kufanywa kipaumbele number one katika nchi hii.

Katika mazingira ya namna hii ya Serikali ya CCM kupuuza kero ya msingi ya wananchi, mimi kwa maoni yangu kwa muda ambao nimekaa Bungeni nianze na hili la kwanza, ufumbuzi hauwezi kupatikana katika huu mjadala tulioanza jana unaohitimishwa kesho. Ufumbuzi kwa maoni yangu unapatikana kwa Watanzania kutambua kwamba kwa miaka mingi wamedanganywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ufumbuzi ni kuindoa Serikali ya CCM madarakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya bila kusubiri Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hotuba kesho. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishazungumza leo na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo Kiongozi wa Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipojibu maswali, swali mojawapo liliulizwa asubuhi leo kuhusu maji, nilitarajia Mheshimiwa Waziri Mkuu kuelezwa namna ambavyo hii bajeti ya maji imepungua, yaani mwaka jana bajeti ya maendeleo ilikuwa bilioni 915, leo bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 623 yaani tumepunguza bajeti kwa shilingi bilioni 292; nilitarajia Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Kiongozi wa shughuli za Serikali aliposimama hapa kujibu swali Bungeni angesema; kwa kweli nimesikia kilio cha Wabunge kuanzia jana na nimesikia vilevile swali nililoulizwa leo na naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutakaa tena katika Serikali, tutaongeza bajeti ya Wizara ya maji badala yake Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa kauli hapa Bungeni leo kwamba Wabunge tuipitishe bajeti kama ilivyo. Kwa maneno mengine mheshimiwa Waziri huyu wa Maji hatarajiwi kuja na jipya lolote kama Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa mwelekeo wa Serikali tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya namna hii Serikali hii ni vyema ikakiri tu kwamba imekwishashindwa kwenye suala la maji. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 aya ya 67 iliahidi kwamba ikifika mwaka 2010 asilimia 65 ya wananchi vijijini watakuwa na maji na asilimia 90 ya wananchi watakuwa na maji mijini.

Mheshimiwa Nasibu Spika, kwa maneno mengine, wale wananchi wenzangu walionituma Bungeni wa Kata ya Kibamba, iwe ni Kiluvya na maeneo mengine ya pembezoni Kibwegere na kadhalika kule Kwembe kule iwe ni Kisopwa, iwe ni Kwembe Kati katiza mpaka Kata ya Msigani, Malambamawili, nenda Mbezi kule maeneo ya pembeni, Mpiji Magohe, Goba sijui Kinzudi, Matosa maeneo yote haya ya Saranga, King’ong’o, Mavurunza yaani kwa ahadi hii ya Serikali; Serikali ya CCM iliahidi mwaka 2010 asilimia 90 wangepata maji, mwaka 2010 ikafika hawakupata maji, Serikali ikaahidi tena kwenye ilani nyingine ya CCM ya mwaka 2010/2015 kwamba ikifika mwaka 2015 asilimia 90 watapata maji, asilimia 65 watapata maji, ahadi nyingine ya uongo miaka 10 ikapita ikafika 2015, Serikali ikarudia tena ahadi ile ile ya kuahidi tena mwaka 2020 ndiyo matatizo haya yatatauliwa na Mheshimiwa Waziri ulijibu uongo Bungeni naomba tu utakapohitimisha ujibu ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipouliza swali Bunge hili, ukasema kwamba kwa sasa na hata katika kitabu chako umeonyesha tena kwamba kiwango cha maji kimeongezeka kutoka mita 300 mpaka 504 milioni na kwamba sasa kero kwa maneno yako mwenyewe umetumia maneno; “huduma ya maji imeimarika.” Wakati unanijibu swali Bungeni ulisema kuanzia sasa kilomita 12 huku, kilomita 12 huku kwenye barabara ya Morogoro, maeneo yote haya sasa yenye mabomba ya Mchina maji yatakuwa yanatoka. Ukaniahidi hapa Bungeni Mkutano huu huu ukasema maji yameshasukumwa tatizo ilikuwa ni umeme tu, maji yamesukumwa mpaka tanki pale Kibamba na sasa maji yatatoka, lakini Mheshimiwa Waziri ulisema maelezo ya uongo Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema, kwa haya majibu ya Serikali ambayo kimsingi Waheshimiwa Wabunge na hapa nitaomba nafasi kwa mujibu wa Kanuni ya 69(1) kabla ya kuingia kwenye hatua ya Kamati, kama Mheshimiwa Waziri hatatumia Kanuni ya 58(5) kuindoa hii hoja ili Serikali ilete commitment ya kurudisha zile shilingi bilioni 300 zilizoondolewa, kama Mheshimiwa Waziri hatatoa commitment hapa, Wizara ya Fedha haitasema ni kwa nini mpaka sasa imetoa asilimia 19.8 na wakati mpaka sasa ilipaswa pesa zitoke asilimia 75, kama hakutakuwa na commitment ni afadhali mjadala huu tuuahirishe kimsingi ili Serikali ikajipange upya ili bajeti hii ya maji iweze kuletwa ikiwa ina marekebisho ya msingi pesa za maji ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa Serikali hii ni muendelezo tu wa kusema uongo Bungeni, ni muendelezo wa kutotekeleza ahadi, kama hamtayafanya haya ni wakati wa Watanzania kote nchini wenye kero kubwa ya maji, kero number one kujipanga kuindoa CCM madarakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kwamba mnaogopa haya yasiende kusemwa kwenye majimbo yenu ndiyo maana mnazuia mikutano ya vyama vya siasa. Lakini nawaambia mtatuzuia humu Bungeni, mtatuzuia majimboni, mtatuzuia maeneo mbalimbali lakini Watanzania wanauelewa ukweli wa kudanganywa na Ilani za CCM za toka miaka niliyoitaja. Bila kero ya msingi ya maji kuondolewa watachukua hatua mwaka 2019/2020.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika majumuisho Wizara ya Maliasili na Utalii itoe maelezo ni kwa nini mpaka sasa haijawezesha Pori la Akiba la Pande kugeuzwa kuwa bustani ya wanyama na kivutio cha utalii? Suala hili Serikali imekuwa ikinipa ahadi toka mwaka 2011. Mwaka 2015 Serikali ilijibu Bungeni na kuomba ipewe mwaka mmoja tu, huu ni mwaka 2017, miaka miwili imepita.
Aidha, baada ya Mkutano huu wa Bunge Wizara iandae ziara ya kikazi pamoja na Mbunge kutembelea pori husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 mpaka 2015, nilihoji kuhusu Kiwanda cha Tembo Chipboard kilichopo Mkumbara ambacho kiko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Wizara ilijibu kuwa kulikuwa na matatizo katika ubinafsishaji, hali iliyosababisha kiwanda kuacha kufanya kazi. Wizara iliahidi kwamba itaingilia kati kuwezesha kiwanda kuweza kufanya kazi ipasavyo. Hata hivyo, mpaka sasa kiwanda hakijarejea katika hali ya kawaida.

Hivyo, ni vema Wizara ikafanya utaratibu mkataba uliokuwepo uvunjwe na kiwanda kirejee katika hali yake ya awali ya kufanya kazi. Wizara izingatie kuwa Serikali ilishatoa ahadi Bungeni kwamba viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa lakini waliopatiwa wameshindwa kutimiza masharti ya kimkataba, vitarejeshwa Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka imepita toka Bunge lipitishe maazimio kuhusu Operesheni Tokomeza. Nilitarajia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri angeeleza hatua ambazo zimechukuliwa katika kutekeleza maazimio husika ya Bunge.

Hivyo basi, katika majumuisho Mheshimiwa Waziri aelezwe hatua ambazo Wizara imechukua kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu Operesheni Tokomeza.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mkataba mmoja pamoja na Itifaki mbili na nimepata wasaa wa kuzisoma soma hapa, lakini kwa kuwa kuna dakika tano nitajielekeza kwenye mambo machache tu.

Mheshimiwa Msigwa aliposema Bunge dhaifu husababisha Serikali dhaifu amenikumbusha kauli ambayo niliisema Bungeni hapa tarehe 19 mwaka 2012. Na kinyume chake, Serikali dhaifu vilevile husababisha Bunge kuwa dhaifu na ndiyo hali ambayo tunayo hivi sasa. Bunge letu limefanywa dhaifu sana na limefanywa dhaifu na Serikali na Serikali hii ingekuwa na nguvu ingejiamini sana, isingefanya Bunge kuwa dhaifu, lakini kwa sababu Serikali ni dhaifu ni lazima na Bunge nalo liwe dhaifu.

T A A R I F A . . . . .

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwombea Mwenyenzi Mungu Mheshimiwa Mlinga aweze kubadilika hiyo tabia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limekuwa dhaifu kwa kiwango ambacho miswada, mkataba mmoja na Itifaki mbili zinaletwa zote kwa siku moja wakati ambapo Bunge lenye nguvu lingesema kwamba siku hii tunajadili mkataba huu, tunaujadili vizuri vinatafakari hoja umetolewa. Siku hii tunajadili mkataba huu, siku hii tunajadili mkataba huu. Kwa udhaifu huu wa Bunge unaoendelea anasema sikuwepo siku nyingi. Hii siku nyingine sikuwepo si Mwenyekiti unajua mlinitoa ndiyo maana sikuwepo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya udhaifu huu Wabunge Mheshimiwa Halima Mdee hatakuwepo kwa muda wote ambao hatakuwepo, akija kurudi mtamwambia maneno haya haya. Mheshimiwa Ester Bulaya hatakuwepo hakirudi mtamwambia maneno haya haya. Sasa hii hoja ya uchafunzi wa mazingira upande wa bahari nizungumzie kwa niaba ya Mheshimiwa Mdee wa Jimbo la Kawe ambaye bahari inazunguka eneo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba hii Serikali iliisaini muda mrefu, lakini hakuna kinachofanyika kuzuia uchafuzi, hakuna kinachofanyika cha kutosha kunufaisha wavuvi. Nataka kusema nini hapa, kuridhia mikataba hii peke yake na Kambi ya Upinzani hapa inairidhia inaunga mkono kuridhiwa kwa hii mikataba haitoshi kama mwisho wa siku masharti ya msingi yaliyoko kwenye Itifaki, masharti ya msingi yaliyoko kwenye mikataba hayatekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaruhusu Serikali kuendelea kuwa dhaifu na Bunge kuendelea kuwa dhaifu ni wazi siku zote tutapitisha mikataba na sheria lakini utekelezaji hakuna. Tuna Mkataba muhimu sana hapa, huu mkataba unahusu rasilimali za kijenetiki ambao nchi iliuingia mwaka 2010 tumeletewa leo kuridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matajiri unaowakuta duniani iwe ni akina Bill Gates, iwe ni tajiri wa Apple aliyefariki matajiri mnawakuta duniani walipata utajiri kwa sababu ya ubunifu. Wenzetu wana ubunifu wa kiteknolojia sisi tunawabunifu wengi sana ambao wangeweza kunufaika na rasilimali za kijenetiki kwenye ugunduzi wa dawa, tiba, vitu na mbalimbali lakini kwa sababu mambo haya hatuyafanyi vile inavyostahili ndiyo maana hatufiki pale ambazo tunafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeingia katika sekta ambayo wengine ndiyo tunadhani ina manufaa zaidi ya madini. Kumbe huku kuna madini kwenye jenetiki, lakini hatufanyi ipasavyo. Hata kwenye madini tumewaambia muda mrefu leteni mikataba hapa Bungeni tumewaambia muda mrefu leteni mikataba leteni mikataba, tumeimba kwa miaka mingi leteni mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnatuletea hoja mnasema kwamba tunaleta sheria ya kulipa Bunge mamlaka juu ya mikataba halafu mnataka propaganda kama vile sisi ambao ndiyo tulikuwa tunasema mikataba iletwe tunakataa, sisi tunachokataa ni kwamba ninyi wa kuzileta sheria kwa Hati ya Dharura mnatunga sheria mbovu ambazo mwisho wa siku hazileti tija ambayo inasukudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli ninyi mnataka kuisaidia nchi kwenye masuala ya madini, hata kama tukianzia na hapo ambapo nilisema Rais angekuwa makini asingeanzia na makinikia angeanzia na madini. Hata kama tukiamua kuanzia na makinikia cha kwanza ambacho Bunge ingetaka kwenye Bunge hili kabla hata kuletewa miswada kusoma kwa mara ya kwanza zile ripoti mbili zile, zile ripoti alizokabidhiwa Mheshimiwa Rais, ipaswa ziwasilishwe hapa Bungeni Mawaziri wazisome tuzijadili Wabunge halafu tuseme sasa Serikali kaandae mapendekezo ya muswada ya kuhusu hiki, kuhusu hiki, kuhusu hiki, iletwe hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nachotaka kusema hapa ni kuwa, badala ya kuanza kujadili Miswada ya Sheria kwa Hati ya Dharura, Bunge hili liletewe kwa udharura huo huo ripoti mbili za Rais kuhusu makinikia, zisomwe hapa Bungeni, zijadiliwe hapa Bunge msipofanya hivyo ile kauli niliyosema kwamba Rais makini alipaswa kuanza na madini kabla ya makinikia kuna siku itakuja kuwatafuna.

Mheshimiwa Lema amesema kwamba kama hamtasikia maoni yetu basi ni afadhali mfike hatua mfute Kambi ya Upinzani. Mheshimiwa Lema kabla hawajafuta Kambi ya Upinzani kama wataendelea kutosikiliza maoni yetu imefikia hatua Watanzania waiondoe hii Serikali madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnadhani tumechelewa, kama mnashindwa tu kuwadhibiti wale watu wa Kibiti, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kama mnashindwa kuwadhibiti watu wa Kibiti wanaotumia silaha, ndugu zangu hamuwezi kuwadhibiti Watanzania hawa wakiamua kutumia silaha yao, kadi yao kupigia kura kwenye sanduku la kura. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Toka jana nimekuwa nikisikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na leo na nimepitia taarifa ya Kamati na nimetafakari katika miaka niliyokaa Bungeni, nimekuja kugundua kwamba kwa miaka nane kwa kweli Bunge hili linajadili mambo yale yale, yaani ukiwa umeingia Bungeni leo tu au jana ukawa hujasikiliza Bunge huko nyuma, unaweza kufikiri sasa kuna Chama na Serikali mpya katika Bunge hili inajaribu kurekebisha mambo ya zamani. Kumbe ni chama kile kile na Serikali ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sentensi moja ambayo iko bayana katika haya ni kwamba ninyi mmeshindwa kutekeleza na kutimiza matakwa ya wananchi kwenye masuala ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kabla sijaendelea mbele nisisitize ninachoendelea kusisitiza kwamba tiba ya kudumu ya haya matatizo tuliyonayo ni wananchi wa Tanzania kuwaondoa Serikali ya CCM madarakani na kuweka Serikali nyingine katika utawala wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa unakumbuka vizuri kwa sababu ulikuwa kwenye kiti hicho hicho wakati ukiwa Naibu Spika. Tarehe 4 Februari, 2013 nilipoleta hoja Bungeni hapa juu ya maji Dar es Saalam na maji vijijini na namna ambavyo Wabunge wa CCM wakati huo Mheshimiwa Rais akiwa ndani ya Bunge, akiwa Waziri wa Ujenzi naye akisikiliza mlivyoshabikia kwa pamoja kwamba mambo yapo kwenye mkondo sahihi, kila kitu kipo sawasawa, hoja hii iondolewe isijadiliwe, hatimaye maji yakasababisha vurugu kubwa sana hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miaka mitatu au miwili na ushee, toka mwaka 2016 hadi 2017 na mpaka sasa mlinyamaza kimya kusema kuhusu maji, nikifikiri kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa sababu alikuwa Mbunge anayajua vizuri matatizo haya ya maji na kwa sababu alikuja hapa Bungeni akaahidi kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 95 ya wananchi mijini ikiwemo Dar es Salaam watakuwa na maji na asilimia 85 wa vijijini watakuwa na maji, nikafikiri kwamba kutakuwa na tofauti. Nimekuja kugundua kwamba Mheshimiwa Magufuli ni yule yule na CCM ni ile ile, mambo ni yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huwa tunajengewa matumaini sana. Mwaka 2006, mwaka 2007 katika Bunge la Bajeti Waheshimwia Wabunge walisema mambo haya haya ambayo wanasema sasa tukajengewa matumaini wakati wa majumuisho ya Serikali kwamba kutakuwa na mabadiliko. Safari hii mmekuja na mkakati huo huo; na sasa kuna debate ya tozo ya mafuta ya shilingi 50 ili ikishafika hatua ya majumuisho Serikali iki-coincide kutoa tozo ya shilingi 50 watu walainike wote, bajeti ipite, halafu mambo yaendelee kuwa yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati inasema mpaka mwezi Machi Serikali imetoa asilimia 22 tu ya pesa za maendeleo. Hizi asilimia 22 za pesa maendeleo ni katika bajeti ya maji ambayo imepunguzwa badala ya kuingezwa kutoka bajeti iliyotangulia. Halafu kwenye umwagiliaji haIi ni mbaya zaidi asiliamia 12 na kati ya hiyo 12 pesa za ndani ni 0.8. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala la sukari ulisimama ukataka kuonesha ukali. Maji katika maisha ya wananchi ni zaidi ya sukari kwa sababu ukikosa sukari unaweza ukanywa chai bila sukari. Katika suala la mafuta umeonesha ukali, maji ni zaidi ya mafuta, kwa sababu ukikosa mafuta unaweza ukapika bila ya mafuta. Ila ukikosa maji huwezi kunywa bia, ukikosa maji huwezi..., ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, onesha ukali wako katika hili. Na mimi nakuomba ukubali, kwa sababu tumeishauri Serikali vya kutosha sana, lakini haisikii. Sasa nani wakati Bunge kutumia mamlaka yake ya Kikatiba kuisimamia Serikali. Mamlaka hayo yanaanza kwa kukubaliana kwamba hii bajeti ya Wizara ya Maji tusiipitishe sasa. Tukubaliane kwamba hii bajeti ya Wizara ya Maji tusiipitishe sasa. Sasa najua kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu wana shauku sana ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, ingekuwa siyo shauku ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ningesema nasimama sasa hivi kwa mujibu wa Kanuni ya 69(1) ambayo inaruhusu Mbunge kusimama wakati wowote kutoa hoja ya kwamba mjadala uahirishwe. Ningeweza kabisa kusema kwamba mjadala uahirishwe, sasa ni mwezi Mei na kuna bajeti zinajadiliwa mpaka mwanzoni mwa mwezi Juni, tungesema mjadala uahirishwe mpaka mwishoni mwa Mei ili Serikali katika makusanyo yake ya mwezi huu wa Serikali iingize pesa katika Wizara ya Maji, tuvuke kutoka hii asilimia 22, tufike juu ya asilimia 22.

Mheshimiwa Spika, tuna uwezo kabisa wa kufanya hivyo kwa kanuni za Bunge na tuna haki hiyo. Kwa sababu Waheshimwia Wabunge wenzangu wana shauku ya kuendelea kuchangia, bado tunayo nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, ruhusu Wabunge wengine waendelee kuchangia lakini wakishamaliza kuchangia kesho, Serikali isiruhusiwe kuhitimisha, mjadala uahirishwe na nipewe nafasi ya kutoa hoja hiyo kesho, mjadala uahirishwe mpaka tarehe ngapi kwa mujibu wa kanuni.

T A A R I F A . . .

MHE. JOHN J. MNYIKA. Mheshimiwa Spika, nilisema awali kwamba ni mbinu tu ya kukwepesha hii bajeti ipite.

Mheshimiwa Spika, tulishapitisha bajeti hii ambayo Serikali imetoa asilimia 22. Serikali ikishapitisha Bajeti ni wajibu wa Serikali kutoa pesa. Nasema tuahirishe mjadala ili Serikali ilazimishwe kutoa hizo pesa. Sasa masuala ya tozo ni masuala ya kwamba tunakwendaje mbele? Tukifika huko napo hata katika tozo, kuna tozo zinatozwa na bado pesa nyingine haziendi vilevile. Kama ilivyo kwenye maji, kama ilivyo kwenye umeme, kwenye REA, hiyo ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameeleza na kwa miaka kadhaa tumeeleza kuhusu ufisadi katika sekta ya maji na miradi ya ambayo kimsingi ni miradi ambayo imejengwa lakini maji hayatoki na matumizi mabaya ya fedha katika masuala ya miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii imeendelea, ipo katika sura nyingi hata mtu akisoma kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri, ukiangalia tu uchimbaji wa visima vya DCCA kuanzia ukurasa wa 267 utaona jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri anavyojipendelea katika Mkoa wa Katavi na katika Jimbo lake. Mimi nazungumzia kipengele cha matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchini na miradi ya maji kutokufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya kero nyingi za ufisadi wa namna hii unaozungumzwa, nitaomba nafasi na ninaomba nitoe notice kabisa kwa mujibu wa Kanuni ya 120 ya Kanuni za Bunge 2A kwamba baada ya mjadala huu kukamilika, nipewe nafasi ya kutoa hoja ya kuundwa kwa Kamati teule ya kwenda kuchunguza masuala ya ufisadi na miradi mibovu katika masula ya maji maeneo yote nchini na katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe umeonesha kutaka kuunda Kamati za kiuchunguzi, umeunda Kamati ya Gesi, umeunda Kamati ya Tanzanite, umeunda Kamati ya Almasi na umeunda Kamati mbalimbali, lakini hizi Kamati zako ambazo taarifa zake hazijadiliwi humu Bungeni na Wabunge wote, sasa katika hili kwa sababu ya uzito wake iiundwe Kamati Teule ili ikachunguze na taarifa iletwe Bungeni ijadiliwe na hatua zichukuliwe. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 21 ukurasa wa tisa na 10 ya hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, imeelezwa kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam imeimarika baada ya kukamilika kwa maboresho ya mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. Hata hivyo, Wizara izingatie kuwa hali haijaimarika katika maeneo yanayohudumiwa na Ruvu Juu kwa upande wa Jimbo la Kibamba katika kata za Kwembe, Mbezi, Msigani, Saranga na Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema kufanya ziara ya haraka ya kikazi yenye kumhusisha Waziri wa Maji, Mbunge, DAWASA na DAWASCO ili kukagua maeneo yote ya mabomba ya Mchina ambayo nilipowasilisha hoja binafsi tarehe 4 Februari, 2013 Bungeni Serikali iliahidi kwamba baada ya kukamilika kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na ujenzi wa bomba maji yangekuwa yanatoka. Aidha, kwa upande wa maeneo katika kata hizo za Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani na Sarange ambayo hayana mtandao wa usambazaji wa maji, kasi ya kuwaunganishia wananchi ni ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba katika aya ya 135 ukurasa wa 72 na 73, Wizara imetaja maeneo ya Mbezi hadi Kiluvya na maeneo ya Kibamba, Msakuzi, Makabe, Malamba Mawili na Msigani. Upanuzi wa mfumo wa kusambaza maji katika maeneo hayo unasuasua, kadhalika yapo maeneo mengine katika kata hizo hayajatajwa katika orodha hiyo. Hivyo naomba Wizara inipatie orodha ya maeneo yote ambayo hayana mfumo wa kusambaza maji safi katika kata hizo tano na ratiba yenye kuonyesha ni lini maeneo hayo yatasambaziwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ruvu Chini ieleweke kwamba katika Jimbo la Kibamba kata pekee inayopata maji kutoka chanzo hiki ni kata ya Goba, katika aya ya 135 ukurasa wa 73 yanatajwa maeneo ya Kinzudi, Matosa na Mtaa wa Goba. Hata hivyo mtandao wa mabomba ya maji katika maeneo hayo haulingani kabisa na mahitaji. Aidha, ipo mitaa mingine katika kata ya Goba ambayo haipo katika orodha ya kusambaziwa maji katika mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kupewa orodha ya maeneo yote ya kata ya Goba yasiyokuwa na mtandao wa mabomba ya maji yenye kuonyesha ratiba ya lini yatawekewa mabomba ya maji. Naomba Wizara inaposhughulikia miradi ya maji ya Ruvu Chini kwa upande wa DAWASA na DAWASCO itoe kipaumbele maalum kwa kata ya Goba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika aya ya 133 ukurasa 71, Serikali imeeleza kwamba inaendelea kutekeleza mradi wa Bwawa la Kidunda unaogharimu dola za Marekani milioni 215. Hata hivyo, kimsingi hakuna utekelezaji unaoendelea kwa kuwa pamoja na usanifu kukamilika muda mrefu, mpaka sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha. Mradi huu ni wa kutoka wakati wa Mwalimu Nyerere mwaka 1980 na sasa ni wa dharura kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Kumi niliwasilisha Bungeni maelezo binafsi kuhusu tathmini ya ukusanyaji wa kodi ya majengo Jijini Dar es Salaam uliokuwa unafanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kulinganisha na wakati ambapo ukusanyaji huo ulikuwa ukifanywa na Halmashauri. Maelezo hayo yalieleza bayana kwamba kodi ilikusanywa kwa ufanisi zaidi na Halmashauri zaidi ya TRA.

Aidha, maelezo hayo yalipendekeza hatua za kuchukuliwa kuboresha kasoro ndogo katika Halmashauri ili kuongeza ufanisi. Wizara ya Fedha irejee maelezo hayo na kuleta marekebisho wakati wa Muswada wa Sheria ya Fedha ili kurejesha ukusanyaji wa mapato hayo kwa Halmashauri. Kitendo cha TRA kukusanya shilingi bilioni 20.2 tu wakati makadirio yalikuwa shilingi bilioni 47.6 pekee ni ushahidi kuwa yale niliyoyaeleza kwenye maelezo binafsi kwa TRA haiwezi kuwa wakala bora wa ukusanyaji wa kodi hizi.

Mheshimiwa Spika, izingatiwe kuwa hata makadirio ya shilingi bilioni 47.6 kwa nchi nzima ni madogo kwa kuwa hata Halmashauri na Jiji la Dar es Salaam ikiwemo ya kwetu ya Ubungo zingepewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo zingevuka malengo yaliyowekwa na TRA. Hatua hii ya kurejesha kodi ya majengo ichukuliwe pia kwenye ada za mabango na vyanzo vingine vya mapato ambavyo Serikali Kuu imeamua kuvihodhi/kuvitwaa. Kitendo cha kuminya vyanzo vya uhakika vya mapato vinafanya Halmashauri kushindwa kutumia ipasavyo dhamana za Serikali za Mitaa (Municipal bonds) kujipatia fedha za vitega uchumi na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka za kurejesha Tume ya Mipango na kufanya marekebisho ya sheria kuipa mamlaka zaidi kuwa chombo huru. Hatua ya sasa ya masuala ya mipango kuwa kama sehemu ya Wizara ya Fedha kumefanya masuala ya mapato na matumizi kupewa kipaumbele bila mipango thabiti.

Mheshimiwa Spika, hali hii imeathiri pia bajeti za Wizara kwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa kutokuzingatiwa kwenye vipaumbele. Aidha, ni muhimu Kitabu cha Mapato (Volume 1) kipewe kipaumbele na utengwe muda wa kutosha na Bunge kujadili kuhusu mapato kabla ya kujikita katika matumizi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majumuisho naomba majibu ya Serikali kuhusu masuala yafuatayo mahsusi ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Kata ya Goba kuna shida ya maji mitaa yote. DAWASCO/DAWASA waliahidi kwamba maji yatapatikana baada ya ujenzi wa matenki ya maji Sabasaba na Changanyikeni. Hata hivyo, ukweli ni kuwa maji hayajapatikana kwa wakati kwa kuwa mabomba ya maji hayajaanza kabisa kusambazwa. Wizara ieleze lini mabomba yataanza kusambazwa kwenye Kata nzima ya Goba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Msigani ina mitaa mitano; mitaa ya Msingwa, Malambamawili, Temboni, Msigani na kwa Yusuph yapo mabomba ambayo yalijengwa awamu ya kwanza (maarufu kama mabomba ya Mchina) na ya sasa (maarufu kama mabomba ya Kihindi) ambayo mpaka sasa hayatoi maji. Ni lini yataanza kutoa maji? Aidha, yapo maeneo katika mitaa hiyo ambayo hakuna kabisa mabomba. Ni lini maeneo hayo mabomba yatasambazwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Saranga, mitaa saba ina mabomba ya maji lakini si maeneo yote maji yanatoka. Hivyo, DAWASCO ifuatilie katika maeneo ambayo maji hayatoki. Hata hivyo katika kata hiyo kuna mitaa miwili ya Saranga na Ukombozi ambayo hayana kabisa mabomba ya maji. Wizara ieleze ni hatua gani ya haraka zinachukuliwa kuhakikisha kwamba mabomba ya maji yanasambazwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kibamba miradi ya maji inasuasua, kuna maeneo mabomba yamerundikwa bila kuchimbiwa kwa muda mrefu na mitaro imeachwa wazi. Hivyo, hatua zichukuliwe kuhakikisha mabomba hayo yanachimbwa na pia maeneo ambayo hayana mabomba nayo mabomba yatandazwe kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mbezi mitaa ya Msakwi na Msakwi Kusini hali ya maji ni mbaya. Yapo mabomba ambayo kwa muda mrefu hayatoi maji. Aidha, mitaa ya Mpiji Magohe na Msumi haina kabisa mabomba ya maji hivyo Wizara ieleze ni lini mabomba ya maji yatasambazwa katika maeneo hayo. Wizara ihakikishe fedha zilizopaswa kupelekwa kwa Manispaa ya Ubungo zinafikishwa kwa haraka kupunguza ukubwa wa tatizo. Lakini izingatie kuwa misaada hiyo hailingani na ukubwa wa mahitaji na kasi ya ukuaji wa maenezo ya wakazi katika mitaa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kunajitokeza tatizo katika eneo linalojengwa barabara ya lami kutoka Mbezi kwenda Goba ambapo TANROADS walijenga juu ya mabomba bila tahadhari hivyo mabomba yamepasuka wananchi kukosa maji na miundombinu kuharibika hasa karibu na Mazulu Kanisani na Njiapanda ya Goba na Makabe. Hali hiyo iko pia Mbezi mwisho round about.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kwembe ipo mitaa ambayo mabomba yamewekwa lakini mpaka sasa maji hayatoki, ni lini maeneo hayo yatatoka maji? Aidha, limejitokeza tatizo katika maeneo hayo la mkandarasi kutoshindilia vya kutosha na kuweka kifusi mwaka baada ya kuchimba mitaro na kuwekwa mabomba. Matokeo yake ni kuwa mvua zimenyesha na udongo kuondoka na mabomba kubaki wazi na miundombinu ya barabara kuharibika. Kabla ya wakandarasi kumaliziwa malipo yao watakiwe kwenda kurekebisha miundombinu hiyo. Aidha, kuna mitaa kwenye kata hiyo ambayo haina kabisa mabomba, ni lini yatasambazwa? Kwa ujumla kuchukua hatua kamili DAWASCO ikutane.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dharura na madiwani na wenyeviti wa mitaa na watendaji wa Jimbo la Kibamba mapema mwezi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa maji katika eneo linalohudumiwa na Ruvu Chini si wa uhakika pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye mitambo ya Ruvu Chini. Hali ni tete zaidi wakati wa ukame ikilinganisha na kipindi cha mvua. Hali itakuwa mbaya zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi (climate change). Hivyo, ujenzi wa Bwawa la Kidunda unapaswa kuharakishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri pamoja na taarifa ya Kamati zinajenga matumaini hewa kwamba ujenzi unakwenda kuanza. Hata hivyo, ukweli ni kuwa randama ya Wizara inaonesha kuwa ili mradi ukamilike kinahitajika kiasi cha dola za Marekani milioni 215. Taarifa nilizonazo ni kuwa mpaka sasa Serikali imeshindwa makubaliano na masharti ya kupata mkopo kuhusu mradi huo. Hivyo Wizara ieleze katika majumuisho ni namna gani fedha za mradi huo zitapatikana kwa kiasi cha kutosha katika mwaka huu wa fedha na ni lini mradi huo utakamilika? Wizara izingatie kuwa miaka nane iliyopita tumehoji kuhusu mradi huo na Wizara imekuwa ikitoa majibu ya kutoa matumaini bila utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mchakato unaoendelea wa kuunganisha DAWASA na DAWASCO, naomba Wizara katika majumuisho itoe maelezo ya kina juu ya mchakato huo. Aidha, kama Mbunge wa Jiji la Dar es Salaam naomba kupatiwa nakala ya taarifa zilizoombwa na Kamati kuhusu mchakato huo hasa kwa kuzingatia pia suala hilo linapaswa kuhusisha marekebisho ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya ya kusimamia masuala ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani ya Mkoa wa Pwani yanayohudumiwa na mabomba ya Ruvu Juu na Chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge la Kumi kutokana na ukubwa wa matatizo ya maji nchini na haja ya Wabunge kupata majibu ya kina nilitoa hoja na Serikali ikakubali kwamba kwenye kila Mkutano wa Bunge Serikali ilikuwa ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa hali ilivyo kwa sasa ya wastani wa upatikanaji wa maji vijijini wa asilimia 56 tu kwa vijiji na asilimia 69 kwa mijini pamoja na hoja ya nyongeza ya fedha, upo umuhimu wa Bunge hili la Kumi na Moja Serikali kuweka utaratibu wa Wizara ya Maji kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kila Mkutano wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa ya maswali ya Wabunge pekee haitoshi ndiyo maana kwenye Mkutano wa Bunge, Wabunge husimama kutaka maswali ya nyongeza bila kupata nafasi. Katika kujibu michango ya Wabunge, Serikali ieleze itakavyotekeleza utaratibu huo.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Asubuhi ulianza kutuongoza na Dua; Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumba Mbingu na Dunia, umeweka katika Dunia Serikali za wanadamu na Mabunge ya Mataifa ili haki yako itendeke. Ni kwa bahati mbaya sana tunasali tunataja jina la Mungu kwamba haki itendeke lakini haki haitendeki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunalitaja jina la Mungu, huku haki haitendeki, maana yake tunalitaja bure jina la Mungu na tunatenda dhambi. Siku chache zilizopita tumetoka kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mwezi wa toba, lakini badala ya kutubu, mnarudia makosa yale yale ya kulitaja bure jina la Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu ameiumba nchi hii ikiwa na rasilimali nyingi sana. Ukiitazama ile nembo ya Taifa pale, unaweza kuona rasilimali moja baada ya nyingine zikiwakilishwa na rangi mbalimbali na kauli mbiu ya Taifa letu ikiwa ni Uhuru na Umoja lakini bahati mbaya wenzetu ninyi wa CCM, hamna uhuru kwenye Chama chenu na matokeo yake mmesababisha Bunge halina umoja kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhambi hii ya kulitaja bure jina la Mungu maana yake ni kwamba ni wazi inaambatana na matumizi mabaya ya rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amejalia Taifa letu. Kwa bahati mbaya, badala ya kurekebisha hali hiyo kwa kuleta sheria bora na kufikiria kwa muda mrefu tukae tuzijadili kwa umakini, mmeamua kutenda dhambi ile ile ya kuleta Miswada kwa Hati ya Dharura; miwili ijadiliwe kwa siku moja na matokeo yake hatutafanya kazi ya maana inayotajwa kwenye sala hii. Hii ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, leo ulituambia tukipita hapa, tuwe tunainama, maana mjadala huu umeibuka kutokana na report ya Rais ya masuala ya Makinikia kuhusu dhahabu na pale kuna siwa inayofanana kidogo na dhahabu, lakini siyo dhahabu, kwa maneno mengine inawezekana ni sehemu ya makinikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya mjadala tulionao, ilipaswa kabla hatujajadili Miswada hii, Bunge liletewe report zote mbili za Rais juu ya makinikia tuzijadili kwa kina, tuielekeze Serikali ikafanye nini, Serikali ndiyo ilete Miswada inayofikiri miaka 50 ijayo, inayofikiri miaka 500 ijayo inayofikiri mbele sana juu ya mustakabali wa Taifa letu, lakini ninyi mmeleta Muswada wa kufikiria miaka mitano tu ya kuelekea uchaguzi. Kuna mtu aliwahi kusema, Politicians think about election; Leaders, think about generation. Ni bahati mbaya sana Mheshimiwa Rais ameamua kuwa mwanasiasa badala ya kiongozi, anafikiria uchaguzi.

KUHUSU UTARATIBU...

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Juu ya Muswada wa Sheria ya kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, nitaomba muda wangu ambao umeuchukua, ulindwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sheria hii imetoa mamlaka makubwa sana kwa Rais kuhusiana na masuala ya umiliki wa rasilimali za nchi. Sheria hii imedhihirisha ni kwa nini sisi Wapinzani na wananchi tulioungana pamoja kutaka rasimu ya Warioba ili kupunguza mamlaka ya Rais kwenye masuala mbalimbali.

KUHUSU UTARATIBU...

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ukiangalia ile Nembo ya Taifa kuna rasilimali yetu mojawapo, zile pembe za ndovu zina rangi nyeupe. Ndiyo maana nasema ninyi, samahani sana, kuna miongoni mwenu mnaabudu miungu badala ya Mungu. Mimi nawashauri mtubu, msafishike muwe weupe kama theluji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)

Kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti katika Mikataba ya Maliasili kwa nchi ya mwaka 2017, sisi tumedai mikataba mara nyingi sana, tumedai mikataba muda mrefu sana. Sasa mmeleta sheria ya kuleta mikataba lakini sheria hiyo mmeleta kwanza mmetumia neno “may” kwa maana ni hiari lakini pili mnaileta mikataba siyo kwa majadiliano kwa mapitio ya moja kwa moja kwa sababu mikataba hii hamjaweka kifungu chenye
kuonesha kwamba Bunge linapaswa kuiridhia mikataba hiyo. Kwa maneno mengine kifungu hiki kitafanya mambo yawe yale yale kama ya miaka 50 iliyopita na Taifa litakuwa pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka 2008 kwenye Maazimio ya Bunge kuhusu Richmond kulikuwa na Azimio ambalo lilisema bayana toka mwaka 2008 kwamba kuanzia mwaka 2008 Kamati za Bunge za Kisekta na hili nililikumbushia wakati wa mjadala wa Escrow nilileta mapendekezo ya marekebisho, Kamati za Bunge za Kisekta ziwe zinapewa mikataba na Serikali kabla ya Serikali kwenda kuridhia mikataba husika. Hata hivyo, kwenye marekebisho ya sheria hii hamjaleta kifungu cha namna hiyo na kwa bahati mbaya mmetubana tusilete marekebisho, mmekataa marekebisho yetu asubuhi tulivyoyaleta, kwa hiyo mmeamua kabisa kutunga sheria hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho yameletwa machache, mengi yamekataliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya namna hii, namkumbuka Mzee wangu Dkt. Emmanuel Makaidi, kabla hajafariki tarehe 30 Machi, 2014 tukiwa kwenye Bunge la Katiba alinikabidhi Emma’s Encyclopedia Tanzania of National Records, aliweka records za toka mwaka 1497 mpaka mwaka 1995; za miaka 498 ambazo nyingine zimegusa masuala ya rasilimali nchi yetu inaelekea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Viongozi, kati ya mambo ambayo yalitokea katika Taifa letu ni Vita ya Majimaji ya mwaka 1905 mpaka 1907 wananchi wakikataa kuporwa rasilimali zao. Kama ninyi mnasema mmeanzisha vita ya kiuchumi basi ni wakati sasa wa kuwa na Vita ya Majimaji ya kuwaondoa ninyi madarakani. (Makofi)

Kwa sababu katika hali iliyopo Watanzania hawawezi tena kuitegemea CCM hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na vita ya silaha, hii itakuwa ni vita ya kisiasa na kiuchumi, wananchi wakihamasishwa kutumia silaha yao kuu (sanduku la kura) kuiondoa CCM madarakani mwaka 2019 na mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mmeonesha wazi hamtaki kutuletea Katiba Mpya, mmeikataa Rasimu ya Warioba iliyotaka maadili, iliyotaka uadilifu, iliyotaka wananchi wanufaike na rasilimali, mmekataa na hamtaki kuwa na Katiba Mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa maneno ambayo yameandikwa katika Biblia ya Mfalme Nebukadneza ambaye yeye aliamua kuisifu miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu, shaba, chuma, miti na mawe. Miungu ambayo haioni wala haisikii, haijui lolote lakini Mungu ambaye uhai wako uko mkononi mwake na njia zako zi wazi mbele yako hukumheshimu basi Mungu ametuma mkono uandike maandishi haya, maandishi yenyewe ni haya; “Mene Mene Tekeli Peresi” na hii ndiyo maana yake. Mene maana yake Mungu amehesabu siku za ufalme wako na kuukomesha. Tekeli maana yake wewe umepimwa katika mizani nawe ukaonekana huna uzito wowote. Peresi maana yake ufalme wako umegawanywa kati ya Wamedi na Waajemi.
Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Asubuhi ulianza kutuongoza na Dua; Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumba Mbingu na Dunia, umeweka katika Dunia Serikali za wanadamu na Mabunge ya Mataifa ili haki yako itendeke. Ni kwa bahati mbaya sana tunasali tunataja jina la Mungu kwamba haki itendeke lakini haki haitendeki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunalitaja jina la Mungu, huku haki haitendeki, maana yake tunalitaja bure jina la Mungu na tunatenda dhambi. Siku chache zilizopita tumetoka kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mwezi wa toba, lakini badala ya kutubu, mnarudia makosa yale yale ya kulitaja bure jina la Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu ameiumba nchi hii ikiwa na rasilimali nyingi sana. Ukiitazama ile nembo ya Taifa pale, unaweza kuona rasilimali moja baada ya nyingine zikiwakilishwa na rangi mbalimbali na kauli mbiu ya Taifa letu ikiwa ni Uhuru na Umoja lakini bahati mbaya wenzetu ninyi wa CCM, hamna uhuru kwenye Chama chenu na matokeo yake mmesababisha Bunge halina umoja kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhambi hii ya kulitaja bure jina la Mungu maana yake ni kwamba ni wazi inaambatana na matumizi mabaya ya rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amejalia Taifa letu. Kwa bahati mbaya, badala ya kurekebisha hali hiyo kwa kuleta sheria bora na kufikiria kwa muda mrefu tukae tuzijadili kwa umakini, mmeamua kutenda dhambi ile ile ya kuleta Miswada kwa Hati ya Dharura; miwili ijadiliwe kwa siku moja na matokeo yake hatutafanya kazi ya maana inayotajwa kwenye sala hii. Hii ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, leo ulituambia tukipita hapa, tuwe tunainama, maana mjadala huu umeibuka kutokana na report ya Rais ya masuala ya Makinikia kuhusu dhahabu na pale kuna siwa inayofanana kidogo na dhahabu, lakini siyo dhahabu, kwa maneno mengine inawezekana ni sehemu ya makinikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya mjadala tulionao, ilipaswa kabla hatujajadili Miswada hii, Bunge liletewe report zote mbili za Rais juu ya makinikia tuzijadili kwa kina, tuielekeze Serikali ikafanye nini, Serikali ndiyo ilete Miswada inayofikiri miaka 50 ijayo, inayofikiri miaka 500 ijayo inayofikiri mbele sana juu ya mustakabali wa Taifa letu, lakini ninyi mmeleta Muswada wa kufikiria miaka mitano tu ya kuelekea uchaguzi. Kuna mtu aliwahi kusema, Politicians think about election; Leaders, think about generation. Ni bahati mbaya sana Mheshimiwa Rais ameamua kuwa mwanasiasa badala ya kiongozi, anafikiria uchaguzi.

KUHUSU UTARATIBU...

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Juu ya Muswada wa Sheria ya kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, nitaomba muda wangu ambao umeuchukua, ulindwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sheria hii imetoa mamlaka makubwa sana kwa Rais kuhusiana na masuala ya umiliki wa rasilimali za nchi. Sheria hii imedhihirisha ni kwa nini sisi Wapinzani na wananchi tulioungana pamoja kutaka rasimu ya Warioba ili kupunguza mamlaka ya Rais kwenye masuala mbalimbali.

KUHUSU UTARATIBU...

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ukiangalia ile Nembo ya Taifa kuna rasilimali yetu mojawapo, zile pembe za ndovu zina rangi nyeupe. Ndiyo maana nasema ninyi, samahani sana, kuna miongoni mwenu mnaabudu miungu badala ya Mungu. Mimi nawashauri mtubu, msafishike muwe weupe kama theluji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)

Kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti katika Mikataba ya Maliasili kwa nchi ya mwaka 2017, sisi tumedai mikataba mara nyingi sana, tumedai mikataba muda mrefu sana. Sasa mmeleta sheria ya kuleta mikataba lakini sheria hiyo mmeleta kwanza mmetumia neno “may” kwa maana ni hiari lakini pili mnaileta mikataba siyo kwa majadiliano kwa mapitio ya moja kwa moja kwa sababu mikataba hii hamjaweka kifungu chenye
kuonesha kwamba Bunge linapaswa kuiridhia mikataba hiyo. Kwa maneno mengine kifungu hiki kitafanya mambo yawe yale yale kama ya miaka 50 iliyopita na Taifa litakuwa pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka 2008 kwenye Maazimio ya Bunge kuhusu Richmond kulikuwa na Azimio ambalo lilisema bayana toka mwaka 2008 kwamba kuanzia mwaka 2008 Kamati za Bunge za Kisekta na hili nililikumbushia wakati wa mjadala wa Escrow nilileta mapendekezo ya marekebisho, Kamati za Bunge za Kisekta ziwe zinapewa mikataba na Serikali kabla ya Serikali kwenda kuridhia mikataba husika. Hata hivyo, kwenye marekebisho ya sheria hii hamjaleta kifungu cha namna hiyo na kwa bahati mbaya mmetubana tusilete marekebisho, mmekataa marekebisho yetu asubuhi tulivyoyaleta, kwa hiyo mmeamua kabisa kutunga sheria hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho yameletwa machache, mengi yamekataliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya namna hii, namkumbuka Mzee wangu Dkt. Emmanuel Makaidi, kabla hajafariki tarehe 30 Machi, 2014 tukiwa kwenye Bunge la Katiba alinikabidhi Emma’s Encyclopedia Tanzania of National Records, aliweka records za toka mwaka 1497 mpaka mwaka 1995; za miaka 498 ambazo nyingine zimegusa masuala ya rasilimali nchi yetu inaelekea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Viongozi, kati ya mambo ambayo yalitokea katika Taifa letu ni Vita ya Majimaji ya mwaka 1905 mpaka 1907 wananchi wakikataa kuporwa rasilimali zao. Kama ninyi mnasema mmeanzisha vita ya kiuchumi basi ni wakati sasa wa kuwa na Vita ya Majimaji ya kuwaondoa ninyi madarakani. (Makofi)

Kwa sababu katika hali iliyopo Watanzania hawawezi tena kuitegemea CCM hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na vita ya silaha, hii itakuwa ni vita ya kisiasa na kiuchumi, wananchi wakihamasishwa kutumia silaha yao kuu (sanduku la kura) kuiondoa CCM madarakani mwaka 2019 na mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mmeonesha wazi hamtaki kutuletea Katiba Mpya, mmeikataa Rasimu ya Warioba iliyotaka maadili, iliyotaka uadilifu, iliyotaka wananchi wanufaike na rasilimali, mmekataa na hamtaki kuwa na Katiba Mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa maneno ambayo yameandikwa katika Biblia ya Mfalme Nebukadneza ambaye yeye aliamua kuisifu miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu, shaba, chuma, miti na mawe. Miungu ambayo haioni wala haisikii, haijui lolote lakini Mungu ambaye uhai wako uko mkononi mwake na njia zako zi wazi mbele yako hukumheshimu basi Mungu ametuma mkono uandike maandishi haya, maandishi yenyewe ni haya; “Mene Mene Tekeli Peresi” na hii ndiyo maana yake. Mene maana yake Mungu amehesabu siku za ufalme wako na kuukomesha. Tekeli maana yake wewe umepimwa katika mizani nawe ukaonekana huna uzito wowote. Peresi maana yake ufalme wako umegawanywa kati ya Wamedi na Waajemi.