Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John John Mnyika (21 total)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika jibu la nyongeza imeelezwa kwamba ulipaji wa pensheni kwa wazee hawa utaanza kwa wazee ambao wana miaka kuanzia 70 wakati ambapo watu wanastaafu wengine wakiwa na miaka 55, wengine miaka 60 na umri wa kuishi Tanzania unajulikana. Je, Serikali hii ya CCM haioni kwamba inasubiri mpaka wazee wengi wafe ndiyo waweke mpango wa kuwalipa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuanzia ulipaji wa pensheni kwa wazee ukienda nchi zote duniani huwa wanakwenda kwa categories na huwa wanaangalia hali ya uchumi wa nchi katika wakati husika. Sisi kwetu tumeona tuanzie katika umri wa miaka 70 kwa kutambua kwamba bado wazee ambao wanastaafu katika kazi wanaanzia umri wa miaka 60. Ukienda kwa mfano Uganda wana kitu wanakiita Senior Citizens’ Grants ambayo wenyewe wanalipa kuanzia miaka 70. Ukienda Nepal ambayo ndiyo nchi ya kwanza duniani ambayo imeboresha pensheni kwa wazee na wenyewe walianza kulipa kwa watu wenye umri wa miaka 70 kwanza baadaye walipoona hali inaruhusu wakashuka kwenye 65 na sasa hivi akina mama ambao ni wajane na wenyewe wameanza kulipwa pensheni hii katika umri wa miaka 55.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mnyika ondoa hofu kwamba hatua hii ya kwanza ni ya kuona kwa namna gani tunaweza tukafanya zoezi hili kwa watu hawa wenye umri wa miaka 70 na baadaye kwa kadri uwezo utakavyoruhusu tutaendelea kushuka ili kuwa-cover wazee wote, nikuondoe hofu tu Mheshimiwa.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri katika sehemu (a) ya swali hajajibu swali. Niliuliza ni lini hii fidia ya hisani italipwa lakini hajajibu ni lini na Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi anafahamu kwamba jambo hili ni la muda mrefu. Mwaka 2009 aliyekuwa Waziri wa Ardhi wakati huo Chiligati aliahidi wangelipwa milioni tisa, hawakulipwa mpaka mwaka 2015 wananchi wakaandamana kwenda Wizarani, Serikali ikaahidi kulipa milioni mbili badala ya ile milioni tisa. Sasa sehemu (a) ni vyema Waziri akajibu ni lini hasa Serikali italipa hii fidia. Au inataka sasa kwa kuwa wakati ule tuliandamana kwenda Wizara ya Ardhi sasa tuandamane kwenda kwa Mheshimiwa Magufuli ajibu ni lini hasa hii fidia italipwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu (b) ya swali. Serikali imesema kwamba haidaiwi mapunjo ya fidia ya maendelezo. Hili jibu la Serikali ni jibu la uongo. Mwezi Aprili mwaka 2014 tulikuwa pamoja na Rais Dkt. Jakaya Kikwete pale Mloganzila, jambo hili likajitokeza na Rais akataka vielelezo tukamkabidhi na sio Rais tu, Wizarani kuna nakala za fomu za watu ambao kimsingi walipunjwa fidia za maendelezo kinyume kabisa na thamani halisi ya mali zilizokuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu Serikali imejibu uongo hapa Bungeni; je, Serikali iko tayari kurudi kwenda kuchunguza malalamiko ambayo yako tayari Wizarani? Vielelezo vyote viko Wizarani na ikalipa fidia ya maendelezo pamoja na kujibu maswali kwa ukweli?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nilijibu swali lake (a) analosema kwamba sikulijibu. Nadhani katika majibu ya awali nilipojibu sehemu (a) na (b) nimesema kwamba watalipwa baada ya kupatikana fedha na hii haijalipwa kutokana na ufinyu wa pesa sasa siwezi kuweka commitment ya Serikali hapa wakati natambua wazi kwamba haya mambo yanakwenda kwa bajeti kama halipo katika bajeti siwezi kukwambia ni kesho tutalipa au kesho kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nilitaka kutoa ufafanuzi huo. Kwa sababu ukisema unaweka commitment leo na pesa haijapatikana, atakuja kusema baadaye kwamba tumedanganya Bunge na sisi hatutaki kulidanganya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu pia hakuna mahali ambapo tumedanganya Bunge. Kwanza kwa sababu hata hao unaowasema wamekuwa wakija sana ofisini wakidai madai yao na tunawaambia nini kilikwisha fanyika na mpaka sasa kitu gani ambacho wanadai. Lakini ukiangalia pale hakuna mapunjo ambayo wanatakiwa walipwe isipokuwa ile iliyosemwa ya hisani ambayo tunasema watakuja kulipwa baada ya kupatikana ndiyo hiyo ambayo Serikali inaifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba kuna watu walipunjwa na ukizingatia kwamba eneo lile ambalo watu wanalipigia kelele bado ilikuwa ni sehemu ya Serikali. Ilikuwa ni viwanja vya Serikali isipokuwa kulikuwa na vijiji vilivyokuwa vinatambulika mle na ndiyo maana Serikali ikawa tayari kulipa fidia ya maendelezo katika yale maeneo waliyokuwa nayo.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wakati
likijibiwa swali juu ya Msitu wa Nyuki, Serikali imeeleza kwamba inakusudia
kuendeleza msitu huu kuwa sehemu ya vivutio vya utalii Dar es Salaam. Kwa
miaka mingi Serikali imekuwa ikitoa ahadi juu ya kuugeuza msitu wa akiba wa
Pande (Pande Forest Reserve) kuwa kivutio cha utalii, ikafikia hatua mpaka
Serikali ikatangaza tenda.
Sasa kama msitu huu mpaka leo haujakamilika kuwa kivutio cha utalii ni
miujiza gani ambayo Serikali inayo ili kuharakisha kwamba haya mapori ya Dar es
Salaam yageuzwe kuwa sehemu za utalii na kuingiza kipato kwa Dar es Salaam
badala ya kuyaacha kama yalivyo na hatimaye kugeuka kuwa misitu ya mauaji
kama ilivyokuwa pori la akiba la Mabwepande.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza
nimpongeze kwa mtazamo ambao ni chanya wa kwamba, kwanza
anakubaliana na dhana nzima ya matumizi bora ya maeneo ya misitu;
hapingani na dhana nzima ya Serikali kuhusiana na kuifanya misitu iwe ni
rasilimali ambayo inaweza kutumika kwa ajili ya maslahi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kwamba kuna ucheleweshaji
kama ambavyo amesema; nataka nimtoe wasiwasi kwamba historia ni nzuri,
inatukumbusha tulipotoka, mahali tulipo na inatuwezesha kuona kule ambako
tunakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Mnyika akubaliane tu na
rai yangu kwamba tumetoka huko tulikotoka, mipango imekuwepo lakini sasa
awamu hii mipango hii ninayoizungumza ni uhakika na kwamba nataka anipe
muda wa mwaka mmoja tu, halafu aweze kuona katika eneo hili tunafanya nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JOHN J. MNYIKA. Mheshimiwa Spika, nashukuru. Inasikitisha majibu yanatoka ya namna hii, hili suala ni la tangu mwaka 2012 kilipovunjwa kituo cha mabasi cha Ubungo; na mwezi Oktoba, mwaka 2014 aliyekuwa Rais, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitamka kwamba kituo kitaanza kujengwa na akatoa mpaka muda mfupi wa kukamilika kwa kituo, lakini majibu mpaka sasa mwaka 2017 yanakuja namna hii.
Sasa swali, ni lini hasa hiki kituo kitakamilika ili kuondoa msongamano ulioko Kituo cha Ubungo ambacho kimeshavunjwa na kiko kwenye hali mbaya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kituo hiki kinajengwa pembeni ya barabara ya Morogoro, na siku chache zilizopita TANROADS wametoa notice kwa wananchi wote wanaoishi pembezoni ya barabara ya Morogoro mita 121 kutoka katikati ya barabara kila upande. Kuweza ndani ya siku 28 kubomoa majengo yao. Ndani ya siku 28 mita 121 pande zote mbili za barabara kutoka katikati ya barabara. Sasa kwa kuangalia umbali ambao TANROADS umeutaja ni wazi ubomoaji huu utahusu kituo cha sasa cha mabasi ya kawaida ya Mbezi kilichopo. Vilevile kama umbali ni huu wa mita 121 kutoka katikati ya barabara hata hiki kituo kipya kitaguswa.
Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali ama Waziri mwenyewe ama Wizara hii ya TAMISEMI ama Wizara ya Ujenzi ijibu; kwa sababu huu umbali utaingilia hiki kituo ni kwa nini Serikali isitengue hili Tangazo lilitolewa na TANROADS la siku 28 ili majadiliano kwanza yafanyike kuhusu huu upana wa barabara sababu ni upana mkubwa sana ambao hauko kwenye barabara yoyote Tanzania? Mita 121 pande zote mbili za barabara kutoka katikati, naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: MheshimiwaMwenyekiti, Mheshimiwa Mnyika kwanza umesema kwamba muda umepita sana, ni kweli. Tuelewe kwamba hata suala zima la kituo hiki ni kituo mkakati sana nadhani na wewe liko katika jimbo lako pale. Ni kituo mkakati ambacho ukiangalia sasa hivi hata hizi barabara za kwenda kasi zinaishia pale Mbezi Mwisho. Nashukuru sana tumepata ushauri wa kamati ya TAMISEMI, walipofika kukagua kile kituo wametoa mapendekezo mengi sana.
Mheshimiwa Spika, hata suala hili la la reserve ya barabara waliliona na wakasema ikiwezekana sasa Jiji la Dar es Salaam na kushirikiana na LAPF lifanye mkakati ili kuhakikisha kwamba wenye zile nyumba za jirani wanalipwa fidia ili ni kuongeza kituo. Vilevile wameenda mbali zaidi kwa kusema kwamba kwa uzoefu uliokuwepo maeneo mbalimbali yanapojengwa vituo ili watu watu wakatishe inabidi kutengeneza madaraja ya juu.
Mheshimiwa Spika, Wajumbe wakapendekeza hata ikiwezekana kujengwe tunnel kupitia katika kituo Mbezi cha zamani, kwa hiyo ilikuwa ni ushauri mbalimbali. Hata hivyo jambo hili linaitaji fedha nyingi sana, na kuhusu suala la fedha tunafahamu, wasitani wa shilingi bilioni 28 si jambo dogo; ndiyo maana kuna kitu negotiation kilifanyika kati ya Jiji na wenzetu wa LAPF na jambo hili bahati nzuri tulivyokwenda site siku ile watu wote walikuwepo pale site ili kukubaliana nini kifanyike. Yote hii ni kwa sababu LAPF wameonekeana kwamba wameshafanya mambo mazuri ya mfano. Kwa mfano pale Msamvu wamejenga stand ya kisasa. LAPF wamekuwa commited, wamesema kwamba tunataka tutengeneze stand ambayo hapa Dar es Salaam itakuwa ni stand kubwa ambayo ita-accommodate magari mengi zaidi kwa ajili ya eneo lile.
Kwa hiyo suala la lini mradi utaanza naomba nikuhakikishe, kwa sababu LAPF walishakuwa committed katika utoaji wa fedha, kwa sababu Jiji halitoi fedha; isipokuwa wataingia katika ile joint venture business ambayo itafanyika vizuri na kwa bahati nzuri na wewe Mheshimiwa Mnyika utakuwa miongoni mwa wafaidika kwa sababu stand ile nawe itanufaisha kwenye mapato katika Jiji lako la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu uvunjaji, kwamba ikiwezekana tutoe tamko hapa ili suala hili lisitishwe. Mimi niseme kwamba Serikali imesikia hiyo concern yako basi kama Serikali itaangalia nini kifanyike kwa ajili ya maslahi mapana kwa ajili ya Dar es Salaam lakini pia kwa wakazi wa Tanzania. Hata hivyo tumependekeza kwamba wataalam wetu wa detailed design waangalie vya kutosha ili ikiwezekana zile barabara ziweze kusogea mpaka hapa Mbezi Luis Mwisho; kwa sababu hata tukijenga ile stand kubwa pale bila kuitanua ile barabara vya kutosha bado tutakuwa na changamoto kubwa sana kwa sababu magari yatazidi kufungana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mambo haya yote kama Serikali inayachukua kwa maslahi mapana kwa mustakabali wa nchini yetu ili kukuza uchumi wetu na wananchi waweze kusafiri vizuri.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, haijui mipaka ya Jimbo la Kibamba, kwa sababu kati ya kata alizozitaja kwamba ni za Jimbo Kibamba, kata zifuatazo ni za Jimbo la Ubungo. Kata ya Ubungo, kata ya Mburahati, kata ya Kimara na kata ya Makuburi. Kwa hiyo, maana yake Kata tano alizozitaja kwenye jibu siyo za Jimbo la Kibamba na siyo sehemu ya swali nililouliza. Ni aibu zaidi kwamba kasi ya upimaji ni viwanja 186 tu, kwa upande wa kata ya Kibamba. Sasa nina maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali la msingi halijajibiwa, je, Serikali iko tayari sasa kuainisha kata kwa kata, mtaa kwa mtaa, kwa upande wa Jimbo la Kibamba, ratiba ya kuharakisha upimaji ili kuepusha sehemu hii ambayo ni Jimbo jipya kabisa nalo kuwa na makazi holela na maeneo mengi yasiyopimwa? (Makofi)
Swali la pili, matatizo haya ya kuchelewa upimaji, na udhaifu katika upimaji yamekwisha leta madhara sasa hivi tunavyozungumza ambapo Serikali imetoa notice na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu kwa wananchi kutoka Stop Over mpaka maeneo ya Kiluvya mita 121 kutoka katikati ya barabara kwa maana ya mita 240 ukijumlisha pande zote mbili za barabara, wananchi wote hawa wanatakiwa kubomoa nyumba zao hivi sasa tunavyozungumza, lakini ninayo hukumu ya Mahakama ya mwaka 2013 yenye kuonesha kwamba wananchi hao walihalalishwa na hati za vijiji kwenye Kijiji cha Kimara, kijiji cha Mbezi na Kijiji cha Kibamba.
Je, Serikali iko tayari maana hili jambo tumeishauriana muda mrefu, kwa sababu sasa hivi ni dharura hili jambo, kutoa kauli ya kusitisha notice hii ya TANROADS kwanza ili majadiliano yafanyike kuhusu utata huu wa upana wa barabara, maana maeneo mengine yote ni mita 60 lakini hapa peke yake ni mita 121.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mnyika, siyo aibu kwa sababu tunajua nini tunachokifanya. Hapa tulikuwa tunazungumzia matatizo ya Watanzania kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI na unafahamu Jimbo lako limegawanywa juzi tu.
Mheshimiwa Mnyika, ukisema aibu na wakati wewe ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani na taarifa tunazipata mwaka mzima toka Baraza halijaanza, ndiyo maana mambo mengine ya msingi unashindwa kuyasimamia kwa wananchi wako, hilo ndio jambo la msingi lazima tukubaliane nalo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo hoja ya msingi kwanza, mipango ya Serikali tumesema nimezungumza maeneo mbalimbali na jinsi Serikali inavyochukua hatua mbalimbali na ndiyo nimekuambia Mheshimiwa Mnyika hii ni politics, haya ni mambo rahisi hata hayataki nguvu haya. Kikubwa zaidi naomba niwasihi Waheshimiwa Wabunge, katika mipango hii ya upimaji katika maeneo yetu tunapaswa wenyewe tuwe karibu jinsi gani tutafanya ili maeneo yetu yapimwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema katika jibu letu la msingi, leo hii ukiaangalia maeneo mengine wamefanya vizuri kwa kutumia wataalam wao mipango shirikishi zaidi na kutumia makampuni mbalimbali, kufanya mipango shirikishi ambayo mwisho wa siku inaweza kujibu jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Serikali imesikia kilio chako Mheshimiwa Mbunge, wala usiwe na hofu, itajitahidi kufanya kila liwezekanalo eneo la Jimbo la Kibamba kama nilivyosema, nashukuru sana, kwa sababu timu sasa iko site na Wizara ya Ardhi siku moja ilikuwa inajibu kijumla yake swali la ardhi katika Wilaya ya Ubungo kwa ujumla wake. Naomba nikutoe hofu kwamba, Serikali itashirikiana vema na Baraza la Madiwani kwa kuangalia jinsi tutakavyofanya ili tuweze kupima, ambayo itakuwa ni manufaa makubwa kwa wananchi wako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la upana wa barabara. Upana wa barabara upo kwa mujibu wa sheria, bahati nzuri wenzetu wa Wizara ya Ujenzi hapa ndiyo wanajua sheria ukianzia ile sanamu pale Posta mpaka unafika Ubungo kuna upana maalum ambao umezungumzwa kisheria, na ukitoka pale mpaka ukija pale Kimara Temboni kuna sheria inaelekeza. Ukitoka pale mpaka unafika maeneo ya karibu na Mto Ruvu sheria inazungumza hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile kuna notice nadhani wenzetu wa Wizara ya Ujenzi wanajua nini wanachokifanya katika eneo lao hilo watatoa maelekezo kwa kadri wanavyoona kwamba inafaa, kutokana na notice iliyotolewa na utaratibu wa kisheria jinsi ulivyo katika eneo lao la kazi. (Makofi)
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika majibu yake imesema kwamba upana huo wa mita 120 ni kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 1932; sheria ambayo kwa sasa haipo, kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007, kifungu cha 62.41 sheria hiyo ya mwaka 1932 ilifutwa. Kwa hiyo, tafsiri yake nini? Serikali ilifanya bomoa bomoa haramu, ambayo ni kinyume cha sheria. Sasa kwa kuwa Rais Magufuli akiwa Mwanza alitoa kauli ya kibaguzi yenye kueleza kwamba…
…nauliza swali sasa.
Nauliza swali, kwa kuwa Rais magufuli alitoa kauli ya kibaguzi yenye kuonesha kwamba wananchi wale wa Mwanza hawatabomolewa…
Swali ninalotaka kuuliza Serikali; kama Mheshimiwa Rais Magufuli si mbaguzi, Serikali itoe kauli hapa ya kuwalipa fidia wananchi wa Jimbo la Kibamba waliobomolewa kwenye barabara ya Morogoro.
Swali la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu serikali imesingizia Sheria, mimi nilichukua hatua kama Mbunge Rais alipopiga Mbezi akasema kwamba kama Wabunge wanataka upana wa barabara urekebishwe wapeleke Muswada wa Sheria Bungeni nilileta muswada wa sheria wa marekebisho ili barabara yote iwe mita 60 lakini Serikali ikaa njama na Katibu wa Bunge aliyekuwepo Dkt. Kashililah kuzuia muswada huu. Ni lini sasa Serikali itaachana na hizi njama na itakubaliana na kauli ya Mheshimiwa Rais na muswada utaletwa hapa Bungeni ili barabara hii iwe na upana wa mita 60 kama zile barabara nyingine nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara limeainishwa vizuri katika sheria kuanzia sheria niliyoitaja katika jibu la msingi, sheria ya mwaka 1932. Vilevile nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba iko pia Sheria Namba 27 ya mwaka 1959, ipo Sheria Namba 40 ya mwaka 1969, pia iko Sheria Namba 13 ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi zilivyokuwa zikitungwa zilikuwa zinatazama maendeleo ya barabara siku za usoni na wala siyo siku za nyuma na ukizisoma sheria hizi zilikuwa zinaainisha barabara. Kwa mfano hii sheria ya mwaka 1932 ilitaja kabisa barabara kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Ruvu na maeneo gani yawe na ukubwa gani, eneo lipi liwe na ukubwa upi kwa ajili ya kuzingatia maendeleo na ukuaji wa shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimshauri Mheshimiwa Mnyika, ziko taratibu za kuhakikisha kwamba kama kuna barabara inatakiwa itajwe na kufanyiwa maboresho ziko taratibu zinaanzia katika Halmashauri na Mamlaka ambazo zinasimamia barabara. Atumie fursa hiyo kuwasiliana na mamlaka yake upande wa Serikali ya Manispaa ya Kibamba ili kweza kuleta maombi. Na kwa hii Sheria Namba 13 inampa nafasi Mheshimiwa Waziri kupitia maombi kutoka kwenye mamlaka zinazosimamia barabara kuona kama kuna eneo linaweza likafanyiwa jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hakuna njama yoyote na suala la fidia itakwenda kwa mujibu wa sheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ambayo ameyatoa hivi punde. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninayo majibu machache tu ya nyongeza. Kwa mujibu wa kanuni zinazoendesha Bunge sehemu ya Nne ya kanuni zetu zinaonesha mpangilio wa shughuli katika Bunge letu. Sehemu ya Tano ya kanuni zetu inaonesha mpangilio wa namna majadiliano yatakavyofanywa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa faida ya Watanzania, si kweli, si kweli, si kweli kwamba Serikali ilikula njama na Ofisi ya Bunge ili kuzuia muswada wowote ambao uliletwa katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, ili kuweka majibu ya Serikali vizuri katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnyika tunaomba tulieleze Bunge lako Tukufu kwamba swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mnyika si swali ambalo lina tafsiri ya ukweli wa hali halisi iliyojitokeza katika muswada wake, na Bunge hili linaongozwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu na sisi Serikali hatuna utaratibu wowote wa kula njama na Bunge hili.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mradi wa Ruvu Juu umekamilika na kwamba maeneo ya ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu yanapata maji hivi sasa na ameyataja maeneo ya Kibamba, Mbezi, Msigani na kwingineko ambayo yako ndani ya Jimbo la Kibamba. Ukweli ni kwamba ule mradi haujakamilika, yapo maeneo ambayo yana mabomba ya Mchina ambayo maji bado hayatoki.
Mheshimiwa Spika, napenda Mheshimiwa Naibu Waziri ajibu ukweli, kwa maeneo ambayo yana mabomba ya maji lakini maji hayatoki mpaka sasa, ni lini maji yatatoka kama anavyosema mradi umekamilika? Je, yuko tayari baada ya hapa twende tukakague huo mradi anaosema umekamilika lakini maji hayatoki?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, tunaposema kwamba mradi umekamilika ni kwamba sasa maji yameanza kutoka na tumeanza kusambaza. Kwenye jibu la msingi tumeelezea kwamba tutakwenda kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Awamu ya kwanza tumeeleza maeneo ambayo tayari yameanza kupata maji.
Mheshimiwa Spika, maeneo hayo anayosema ya mabomba ya Mchina ni sehemu ambayo maji yale yatakwenda. Yamechelewa kufika kwa wakati kwa sababu kulikuwa kuna tatizo la umeme pale Ruvu Juu. Sasa hivi tayari mitambo imeshawashwa na imeshajaribiwa tayari maji yameanza ku-flow mpaka tanki la Kibamba, kwa hiyo, tunaendelea kuunganisha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuangalia hayo maeneo unayosema yana mabomba ya Mchina kwamba yameanza kupata maji au vipi lakini lengo letu ni maji yale yafike kule.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi kwa mitambo hii miwili, ya Ruvu Chini na Ruvu Juu tunazalisha lita milioni 466 kwa siku, ni maji mengi sana. Kwa hiyo, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha kwamba mitandao ile ambayo ina mabomba inapata maji lakini maeneo mengine yale ambayo hayana mitandao, Serikali inaweka bajeti yake. Hata bajeti ambayo nitaisoma baada ya wiki moja nitaelezea mipango ambayo tumeiweka kwa ajili ya fedha za ndani kuweza kusambaza maji zaidi maeneo ambayo hayana mtandao.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la umeme wa Gridi ya Taifa kutokufika kwa wananchi haliko tu Mkoa wa Katavi, bali pia liko katika Jimbo la Kibamba, Jijini Dar es Salaam ambapo kwenye Kata ya Mbezi maeneo kama ya Msumi kwa Londa hayana kabisa miundombinu ya umeme. Kata ya Goba kuna mitaa ambayo haina umeme, Kata ya Msigani kuna mitaa ambayo haina umeme, Kata ya Kwembe kuna mitaa haina umeme, Kata ya Saranga kuna mitaa haina umeme na Kata ya Kibamba kuna mitaa haina umeme.
Sasa kwa kuwa TANESCO iko jirani kabisa na Jimbo la Kibamba, je, Serikali iko tayari baada ya Mkutano huu wa Bunge kufanya ziara maalum kwenye kata hizi zote sita kwenda kuwaeleza wananchi ni lini hasa maeneo haya yatapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Spika, niseme kwanza Serikali iko tayari ndiyo maana imeanzisha REA III, na tayari maeneo mengi miradi imezinduliwa kuhakikisha kwamba vijiji vyote tulivyonavyo katika Tanzania vinapata umeme. Kwa hiyo, tayari imeshaanza, lakini niseme Mheshimiwa Mbunge mimi na wewe ni Madiwani tuna uwakilishi ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, ni kazi yetu sasa kwamba wewe kwasababu ni Mbunge uko ndani ya Bunge na matamshi haya ya Serikali umeyasikia, urudi kwenye Jimbo lako ukawaambie kuwa “jamani sasa Awamu ya Tatu ya REA inafika na kwetu tunapatiwa vijiji moja, mbili, tatu” na vijiji vyako vimeainishwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwa hiyo uende ukatoe taarifa.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali jambo hili Mheshimiwa Tundu Lisu Mbunge wa Singida Mashariki amekuwa akilifuatia kwa muda mrefu sana, Serikali imeeleza kwamba leseni ya Shanta ni ya toka mwaka 2004...
lakini mpaka mwaka 2012 miaka nane Shanta walikuwa hawajajenga mgodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ubaguzi nilishakuandikia muda kwamba nauliza hili swali kwa niaba…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali; la kwanza toka 2004 mpaka sasa kampuni ya Shanta haijajenga mgodi wala haijaanza kuchimba. Ni kwa nini leseni yote wasinyang’anywe wakapewa wachimbaji wadogo wakaenda kuchimba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia Mheshimiwa Rais…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Kishoa nina haki ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba niendelee…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia mwaka jana 2017 ilielezwa kwamba kampuni ya Acacia haipo kisheria…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza ni kwa nini Serikali ilipofuta leseni siku chache zilipopita haikuifutia leseni kampuni ya Acacia, kampuni ya Pangea, kampuni ya Barrick na kampuni ya Bulyanhulu kwa sababu zinadaiwa mabilioni hazijalipa na zinavunja sheria na pesa hatujapewa toka, Serikali itoe ripoti ya makinikia?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Shanta umepewa leseni siku za nyuma toka mwaka 2002 walipewa leseni ambayo ni prospect license yaani leseni ya utafiti. Baada ya pale miaka minne iyopita kampuni ya Shata ilipewa leseni ya uchimbaji yaani mining license. Walipewa mining license namba 455, 456 na 457. Leseni hizo wamepewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na leseni hizo zinadumu kwa muda wa miaka kumi; mwekezaji anatakiwa ndani ya miaka kumi aweze kujenga mgodi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi Shanta walikuwa wamekwama kutokana na kwamba kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi yaani wenye surface areas walikuwa wamegoma kutoka, mmojawapo alikuwa ni Diwani Emili wa eneo lile. Hata hivyo, mpaka sasa hivi diwani yule na bwana mwingine ambaye alikuwa lile eneo wamekwishakubali kupewa fidia na sasa wako tayari kuondoka na wengine wako tayari kuachiwa maeneo kwa ajili ya kuwajengea wale wakazi wa maeneo yale kuwajengea nyumba za kudumu, kwa maana ya kuwaondoa lile eneo la uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwezi Novemba Shanta wataanza kujenga processing plant na vilevile wataanza kujenga TSF na vilevile wataanza kufungua lile eneo la kufanyia uchimbaji wa mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Acacia na makinikia na kuhusu kutoa zile leseni au leseni zilizofutwa. Leseni za juzi zimefutwa na Tume ya Madini na leseni zilizofutwa siyo mining license wala siyo leseni za utafiti, zilifutwa leseni ambazo ni za kusubiria land detention license, mwekezaji anaweza akaomba leseni ya kusubiri uzalishaji kwa muda fulani. Sasa Serikali imegundua kwamba kuna watu wengine wanakaa muda mrefu na zile leseni bila kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake mwaka 2017 zile sheria baada ya kufanya marekebisho leseni za retention license zimeamua kuondolewa na zinarudishwa Serikalini na Serikali itaangalia namna bora ya kuwapa tena wawekezaji wengine ambao wako serious ili waweze kuwekeza na waweze kuzalisha ili Serikali ipate kipato na wananchi waweze kupata ajira na faida zingine Serikali, nashukuru sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nipende tu kuongezea maana yake kumekuwa na mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na wengine wanaofuatilia, wafuatilie kifungu cha (16) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake mwaka 2017 na wasome pia na kanuni ya 21(1) na (2) ya kanuni zetu za madini ya mwaka 2018 kuhusiana na mineral rights ataweza kuona ndiyo maana detention license zile 11 zimeweza kufutwa kutokana na sababu hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwamba sheria imetungwa tangu mwaka 2007 lakini mpaka sasa Serikali haijaanza kutoa msaada wa kisheria.
Sasa kwa kuwa mazingira ya Tarime ni maalum; kuna Mgodi wa North Mara pale Nyamongo na wananchi wengi wanabambikiziwa kesi za unyang’anyi na mauaji kutokana na mgogoro na mgodi; kuna mbuga ya Serengeti pale na wananchi wanabambikiziwa kesi za mauagi na unyang’anyi kutokana na mgogoro na mbuga, je, Serikali iko tayari kuagiza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakati huo mwongozo ukisubiriwa iende Gereza la Tarime ili ufumbuzi wa haraka uweze kupatikana?
Mheshimiwa Mwenyekitil, swali la pili, nilikuwa mahabusu ya Segerea na matatizo haya ya ubambikiziwaji wa kesi yapo Tarime lakini yapo Segerea na mahabusu nyingine. Sasa kwa kuwa hali hii imekithiri magereza mengi sana, ili hali hii ya kubambikiza kesi iweze kukoma Serikali ni lini itaanza kutoa fidia kwa wananchi waliobambikiziwa kesi ili utamaduni huu wa kubabikiwa kesi ukome? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge si kweli kwamba Sheria hii ya Huduma za Kisheria imetungwa mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii ni ya mwaka 2017, imepitishwa mwaka jana ni Sheria Namba Moja ya mwaka 2017, kwa hiyo na hivi sasa ndiyo imeanza utekelezaji wake. Hoja iliyoletwa hapa kwamba kuiomba Tume ya Haki za Binadamu kwenda katika eneo la Tarime kwa ajili ya kwenda kushughulika na hawa ambao wamebambikiziwa kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo ni huu kwamba huduma za msaada wa kisheria hizi zinatolewa na organization mbalimbali ambazo zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria hii. Mpaka sasa ninavyozungumza tayari tunazo 66 ambazo zinafanya kazi hii. Kinachosubiriwa hapa ni muongozo kati ya Polisi na Wizara ya namna bora ya kuweza kutoa huduma ya kisheria kwa mahabusu walipo vituoni kwa mujibu wa kifungu cha 36(1) cha sheria, lakini si kweli kwamba watu hawapati huduma za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika historia ya nchi yetu mpaka ninavyozungumza hivi sasa ni kazi kubwa sana imefanyika katika eneo hili. Kwa sababu huduma hii ya kisheria imeanza mwaka 1969 ikianzia katika Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini baadae ikatungwa sheria Namba 21 ya mwaka 1969, lakini baadae mwaka 1984 kwenye Katiba yetu tukaingiza Bill of Human Rights ikawa enshrined na baadae ikatungwa sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukiangalia Serikali imekuwa ikifanya kazi hii kwa kiwango kikubwa sana, na mpaka hivi sasa ninavyozungumza tayari wananchi wameweza kupata huduma za kisheria kupitia hizo organizations.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameuliza kuhusu watu wanaobambikiziwa kesi na namna ambavyo Serikali inaweza kuwalipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kimahakama uko wazi na unajieleza vizuri kabisa. Inapotokea mtu yeyote ameshitakiwa mahakamani na baadae ikagundulika kwamba amebambikiziwa kesi utaratibu wa kisheria upo wa kumtaka yeye kufungua kesi ya madai, lakini Serikali hailipi suo moto moja kwa moja. Kwa hiyo wale wote wanahisi wamebambikiziwa kesi utaratibu upo na wafuate sheria.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kukatika katika kwa umeme liko vilevile kwenye Jimbo la Kibamba kwenye Kata za Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi, Saranga na Goba ambako kuna tatizo vilevile la kupungua kwa umeme (low voltage). Sasa ni hatua gani ambazo Serikali inachukua kuhakikisha kwamba hili tatizo la kukatika katika na kupungua kwa umeme linamalizika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mnyika juu ya suala la kukatika katika kwa umeme kwa maeneo ya Jimbo lake la Kibamba pamoja na Kata alizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mnyika, Serikali kupitia Shirika la TANESCO lina mpango wa kujenga kituo kikubwa cha kupokea na kupoozea umeme maeneo ya Kibamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo anafahamu katika Mkoa wa Dar es Salaam kulikuwa na ukarabati wa miundombinu ya umeme na ujenzi wa vituo mbalimbali hasa baada ya kuongezeka kwa mahitaji; na ilionekana ile njia ya msongo wa KV132 inayotoka Ubungo kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali imezidiwa, hivyo baada ya kukamilika kwa vituo vya Gongo la Mboto, Kipawa, Mbagala na Kurasini, Serikali sasa kupitia TANESCO imejielekeza katika ujenzi wa kituo hicho cha Kibamba.
Kwa hiyo, naomba niendelee kuwahimiza watu wa TANESCO wafanye haraka huo mradi uanze ili uweze kutatua matatizo ya kukatika katika kwa umeme na low voltage katika Jimbo la Kibamba na Kata alizozitaja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ujenzi wa magereza katika maeneo mbalimbali vilevile utasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu. Pia amesema kuwa ujenzi huo kwa sasa unakwamishwa na uhaba wa rasilimali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi huu hauwezi kuendelea kwa haraka kwa sasa; na kwa kuwa kuna msongamo mkubwa wa mahabusu katika magereza mbalimbali kutokana na kubambikiziwa kesi ama mashtaka yasiyokuwa na dhamana na hukumu ambazo kimsingi zinajaza tu magereza yetu, je, Serikali ipo tayari sasa kutekeleza operesheni maalum ya kupunguza mahabusu katika magereza mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nirekebishe kauli yake si kwamba msongamano wa mahabusu chanzo chake kikubwa ni ubambikiziwaji wa kesi. Tunajua tuna changamoto ya ubambikiziwaji wa kesi na pale ambapo tunabaini na tumekuwa tukifanya kazi hiyo ya kuhakikisha wale ambao wanahusika na upambikaji kesi wanachukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, lakini msongamano wa mahabusu unatokana na changamoto za uhaba wa magereza. Magereza yetu yamejengwa muda mrefu na idadi ya watu inaongezeka na changamoto ya uhalifu inasababisha msongamano huu pia kuongezeka. Hata hivyo, Serikali tumefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano huu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake kuhusu operesheni, hivi tunavyozungumza tuna utaratibu wa kamati za kuharakisha kesi ambazo zinahusisha wadau mbalimbali ambapo wanahakikisha wale ambao wanatakiwa dhamana kwa haraka wanasikilizwa. Vilevile, tumekuwa tukitumia sheria zetu mbalimbali, kwa mfano, Sheria ya Bodi ya Parole, Sheria ya Huduma za Jamii, Sheria ya EML na msamaha Mheshimiwa Rais ambao amekuwa akitoa kila mwaka, yote haya yanasaidia kupunguza msongamano wakati Serikali ikiendelea na jitihada zake za kujenga mabweni na kuongeza na kupanua idadi ya magereza yetu ili yaweze kuchukua idadi kubwa zaidi ya wafungwa.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, katika majibu yake, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba asilimia 80 ya wananchi wa Kibamba wanapata maji ya bomba, jambo ambalo ni taarifa ya uongo imetolewa Bungeni. Kwa sababu ukiangalia mtandao wa maji ulivyo, kuna maeneo mengi hayana kabisa mabomba ya maji na hata yenye mabomba ya maji, bado kuna maeneo ambayo hayatoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa mfano, kuna kata sita tu Jimbo la Kibamba; Kata ya Goba, Mitaa ya Goba, Matosa, Tegeta A, na kadhalika. Pamoja na Mheshimiwa Waziri kuahidi kwamba Februari maji yatatoka, lakini hayatoki; Kata ya Mbezi, Mitaa ya Mbezi Luisi, Makabe, Msakuzi hakuna kabisa mabomba; Makabe mabomba yapo lakini maji hayatoki; Fijimagohe na Msumi hakuna mambomba; Kata ya Kibamba kule Hondogo, Kibwegere, hakuna mtandao wa maji wa kuwezesha maji kutoka; Kata ya Kwembe, Kinazi B na mitaa mingine kwa ujumla; Kata ya Msigani, maeneo ya Msingwa, maeneo ya Malamba na maeneo mengine yote yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa jibu la Uongo Bungeni, sasa je, yuko tayari kutoa Takwimu ya ukweli ya hali halisi ya upatikanaji wa maji Jimbo la Kibamba na orodha mtaa kwa mtaa ya upatikanaji wa maji na hatua za utekelezaji? Hilo swali la kwanza.

Swali la pili, siku chache zilizopita, Mheshimiwa Rais akiwa ziarani, amesema kwamba Wizara ya Maji ni kati ya Wizara ambayo ina ma-Engineers wana-perform ovyo ovyo. Kuna miradi mingi ya maji kwa assessment ya Wizara ya Maji ambayo ni miradi hewa, badala ya kutoka maji, inatoka hewa. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameshatoa hiyo kauli na naamini kauli ya Rais ni agizo:-

Je, Wizara ya Maji iko tayari kuleta Bungeni taarifa ya assessment ya Wizara ya Fedha aliyoisema Mheshimiwa Rais ili tupitie hatua kwa hatua, tuchukue hatua juu ya miradi hewa katika maeneo mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimhakikishie kaka yangu Mheshimiwa Mnyika, Serikali imefanya kazi kubwa sana, naye anafahamu kabisa. Kipindi cha nyuma kulikuwa kuna mgao mkubwa sana, lakini sasa hivi kuna utekelezaji zaidi ya asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mnyika anasema taarifa tuliyoisema ni ya uongo. Nisome swali lake kipengele cha (b), anataka kujua ni mitaa ipi katika Jimbo la Kibamba maji hayatoki. Sasa kama Mbunge mitaa yako hujui ipi inayopata maji, unawezaje kuniuliza mimi Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa ushauri mdogo tu, nimshauri kaka yangu, afanye ziara katika Jimbo lake, aone kazi kubwa inayofanywa na Serikali. Aende Hodongo aone utekelezaji wa mradi unaofanyika, aende katika katika Kata ya Matosa aone utekelezaji wa miradi unavyofanyika. Nami niko tayari kuongozana naye nikamwonyeshe kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie, anayelala na mgonjwa ndio unayejua mihemo ya mgonjwa. Namshauri aende Jimboni na afanye ziara aone kazi kubwa inayofanyikwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu swali la pili, tunatambua kabisa baadhi ya utekelezaji wa miradi ya maji imekuwa ya kusuasua. Sisi kama Wizara ya Maji tumekuwa tukichukua hatua kwa Wahandisi wababaishaji, lakini pia tumeanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Nataka niwahakikishie, tumejipanga vizuri katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Wahandisi wote wababaishaji hawana nafasi katika Wizara ya Maji, tumejipanga katika kuhakikisha Wakalaa huu unaenda kutatua tatizo la maji vijijini. Ahsante sana.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwamba mipango ya kuendeleza barabara za miji ni pamoja na Mpango wa DMDP. Katika Manispaa ya Ubungo mpango wa DMDP, unatekelezwa kwa upande wa Jimbo la Ubungo peke yake lakini upande wa Jimbo la Kibamba kwenye Kata sita za Kwembe, Msigani, Mbezi, Saranga, Goba mpango huu hautekelezwi kabisa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua utekelezaji wa mpango wa DMDP ili kuzigusa kata sita za Jimbo la Kibamba kwenye masuala ya miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnyika, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mkoa wa Dar es Salaam ikiwepo maeneo ambayo ametaja ya Ukonga na maeneo mengine, tunatekeleza awamu ya kwanza ya mpango ya DMDP. Naomba niwahakikishie kwamba itakapokuja awamu ya pili Wabunge watashirikishwa waweze kuainisha maeneo yao ili tupanue wigo zaidi wa kuendeleza Mji wetu wa Dar es Salaam.
MHE. JOHH J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika kujibu swali la msingi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali iliandaa mkakati maalum wa kudhibiti ajali barabarani na kwamba umetekelezwa kwa kiwango cha ajali kupungua kwa asilimia 43. Sasa Je, Serikali ipo tayari kuleta huo mkakati iliouandaa Bungeni pamoja na taarifa ya utekelezaji Bungeni ili tuweze kupima kama Wabunge ni ukweli ajali zimepungua kwa asilimia 43?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Mnyika Mbunge wa Ubungo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleze kwanza kwa ufupi kabisa kuhusiana na mkakati huu. Mkakati huu upo kwa awamu, tulianza mkakati wa miezi sita ambao ulikuwa na lengo la kupunguza ajali kwa asilimia kumi, tukafanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia kumi na moja. Tukaja mkakati wa awamu ya pili ambao ulikuwa miezi sita, tuka-target asilimia kumi, tukapunguza ajali kwa asilimia 45 nadhani. Tukaona kwamba tuna haja ya kuongeza sasa malengo tukaweka mkakati wa asilimia 25 kupunguza ajali wa miezi sita vilevile, ambao tulifanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 25. Hivi tunazungumza tupo katika mkakati wa awamu ya nne ambao tumelenga kupunguza ajali kwa asilimia 25. Kwa hiyo asilimia 43 tuliyozungumza ni kwa jumla wake kwa maana ya mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niliona nimpe kwanza utangulizi huo aelewe kwamba si mkakati mmoja, ni mkakati ambao tumekuwa tukijipima awamu kwa awamu kupitia Baraza la Usalama Barabarani na mkakati huu upo wazi na Mheshimiwa Mbunge atakapohitaji wakati wowote sisi tutakuwa tayari kumpatia. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa sababu malengo ya mikakati hii tunapomaliza tunakuwa tunashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge, hata yeye mwenyewe Mheshimiwa tulimwalika juzi katika Kongamano letu la Usalama Barabarani ambapo tulizungumzia mkakati huu Dar es Salaam na Wabunge wengine wa Mkoa wa Dar es Salaam wote, lakini bahati mbaya hatukumwona Mheshimiwa Mnyika japokuwa barua niliisaini mimi mwenyewe kwa mkono wangu ili kuonyesha kwamba hili jambo ni jambo shirikishi na tunatambua umuhimu wa kuwashirikisha na tutaendelea kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika swali hili Serikali imeeleza inalipa Dola za Marekani 38,000 kwa mwezi ambazo ukipiga kwa mwaka ni takribani shilingi bilioni 1 na Serikali imeanza kulipa kuanzia 2008, kwa hiyo, ni takribani shilingi bilioni 9 kama all facts are being equal zimelipwa. Wizara hii ina experience kwenye ujenzi wa hosteli za chuo kikuu pale walisema block moja iligharimu shilingi milioni 500, ukigawanya kwa wastani wa hizo shilingi bilioni 9 kwa kipindi hiki kungeweza kujengwa maghorofa kati ya 18 mpaka 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali kama hii, ni kwa nini Serikali imeachia hali ikae muda mrefu na ni lini hasa ujenzi huu utafanyika ili pesa zisiendelee kutumika kwa kiwango kikubwa namna hii kwenye kulipa kodi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba gharama hizo ni kubwa, hata hivyo, ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ni suala la kimkataba na wala haliamuliwi na Serikali peke yake, inabidi kukaa kukubaliana, michoro. Kwa hiyo, ni suala ambalo sio sisi wenyewe, ingekuwa ni kawaida kwamba ni la kwetu tungeshajenga lakini kama nilivyoliarifu Bunge lako Tukufu, tayari hatua za ujenzi zimefika mbali. Tumeshapata eka 20, michoro tayari, kwa hiyo muda wowote jengo hilo litajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba avute subira sanasana ucheleweshwaji umetokea kwa sababu majadiliano yanaendelea kuhusu namna gani jengo hilo lijengwe kwa sababu sio letu peke yetu lazima tuongee na Mahakama ya Afrika pamoja na Umoja wa Afrika.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali imekwepa kujibu msingi wa swali kwa sababu msingi wa swali langu ni kwamba Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba imesema Bunge linaweza kutunga sheria ya kuipa tume jukumu la kusimamia suala lingine lolote na Ibara hiyo ya Katiba pamoja na kuwa kwenye majukumu ya Tume kulikuwa hakuna jukumu la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba, sheria ikatungwa na Bunge ya kura ya maoni…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnyika uliza swali.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Sasa ndio najenga msingi wa swali kwa sababu amejibu tofauti kabisa. ni kwa nini Serikali imeogopa kuleta Bungeni Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ingeondoa mamlaka kwa Waziri wa TAMISEMI ingeweka daftari la kudumu kutumika na ingepeleka majukumu yote kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili uchaguzi usimamiwe na Tume ya Uchaguzi badala ya kusimamiwa na Serikali yenyewe kwa maana ya Waziri wa TAMISEMI ambaye ni interested part ndio alazimike kutunga kanuni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye sehemu ya mwisho ya majibu amesema kwamba kanuni zimeandaliwa kushirikisha wadau, bahati nzuri nilikuwepo kwenye kikao kilichofanyika mwezi Aprili cha kujadili kanuni. Tumekaa kikao kama vyama, anasema vyama vimeshirikishwa; tumekaa kikao Aprili, Aprili hiyohiyo tarehe
25 mwezi wa nne, Waziri akatoa Kanuni kwa siri zilizochapishwa, zimekuja kutolewa hadharani mwezi Agosti na Kanuni zile hazijazingatia maoni ya vyama, wadau na tayari Kanuni hizo zimeanza kutumika vibaya, tunaona Wakuu wa Mikoa ambao ni viongozi wa kisiasa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa sasa ndio wanapewa jukumu la kusimamia uchaguzi wakati ni makada wa Chama cha Mapinduzi, kutakuwa na uchaguzi wa uhuru na haki katika mazingira kama hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, majibu ya Serikali ni sahihi kulingana na swali ambalo ameliuliza. Nikirejea swali la Mheshimiwa Mbunge anasema je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili kusimamia uchaguzi wa Vitongoji na Vijiji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja anayosema swali la kwanza kwamba kwa nini Serikali isilete mabadiliko ya Katiba, Serikali inaweza ikaleta Muswada wa kubadilisha Katiba lakini pia Mheshimiwa Mbunge ana nafasi hiyo na hajafanya hivyo. Kwa hiyo, angeleta mabadiliko hayo tungeyajadili lakini kwa sasa tunazungumza uchaguzi wa Serikali za Mitaa as by now kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zilizopo utasimamiwa na Waziri mwenye dhamana, hakuna mabadiliko ya Katiba ambayo yamekwishafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; Mheshimiwa Mbunge ananiuliza kwamba kanuni hizi hazikuzingatia miongozo, sio kweli na yeye mwenyewe bahati nzuri amethibitisha kwamba alihudhuria, sasa mkiitwa kwenye kikao kujadili na kutoa maoni siyo lazima Serikali ichukue kila kitu mnachokisema, maoni yakitolewa wataalam wanakaa, wanaangalia katiba, sheria, miongozo mbalimbali na practice ya kawaida halafu tunaamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni hizo sasa hivi wala hazikumpa dhamana yoyote Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya kwamba wakasimamie uchaguzi, muongozo huu hapa. Mheshimiwa Mnyika Naibu Katibu Mkuu wa chama chake cha CHADEMA alikuwepo siku hiyo Mheshimiwa Waziri anatangaza kanuni, amepewa kanuni za uchaguzi, mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mwongozo wa Mpiga kura. Na kanuni inasema pia asasi za kiraia na mtu yeyote yule anaweza akapewa hii akasoma na akaomba miongozo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mnyika asiwe ana hofu, Mheshimiwa Mnyika uchaguzi huu utakuwa ni huru na haki na kanuni imeeleza vizuri nani anapaswa kusimamia uchaguzi huu. Tujipange, tukutane kazini, ahsante. (Makofi)
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo ya kukosekana kwa madaraja na kusababisha watu kushindwa kuvuka yapo vilevile kwenye Kata ya Goba hasa Mtaa wa Kulangwa na kwenye mitaa kadhaa. Kwa sababu Serikali inalifahamu suala hili na Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali alisema kuna fedha maalum wanazitafuta. Je, watakapotafuta fedha maalum ni pamoja na Kata ya Goba ili kwenda kuondoa matatizo ya madaraja Mtaa wa Kulangwa na mitaa mingine? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunafahamu maeneo yenye changamoto mbalimbali ikiwepo katika Jimbo a Kibamba na tukifahamu wazi kwamba katika eneo la Dar es Salaam kuna maeneo mengi tumeanza kuya-address kupitia mradi wa DMDP lakini hata hivyo kuna maeneo mengine bado hasa katika Wilaya ya Kigamboni na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ubungo. Siwezi kutoa commitment ya moja kwa moja hapo kwa sababu mimi sitaki kuzungumza biashara ya uongo lakini kama Serikali tunaichukua changamoto hii na kuhakikisha wataalam wetu wanapitia maeneo hayo halafu kuangalia kipi kiwekwe kwenye kipaumbele cha kwanza ili kuwasaidia wananchi wetu waweze kusafiri na kutekeleza kufanya huduma zingine za kijamii. Ahsante.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi iliulizwa kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Katika Jimbo la Kibamba, Shirika la Nyumba la Taifa lilikabidhiwa eneo kubwa kidogo kwa ajili ya ujenzi wa Mji wa Viungani wa Luguruni kwa maana ya Luguruni Satellite Town ambayo ingehusisha nyumba za gharama nafuu, nyumba za kupangishwa, nyumba za kibiashara na miundombinu mingine. Hata hivyo, kwa miaka mingi pamoja na National Housing kupewa jukumu la kuwa mwendelezaji mkuu mpaka sasa hakuna chochote kilichoendelea na kimsingi eneo lile limeanza kugeuka kuwa kijipori.

Je, ni lini hasa National Housing itatekeleza huu wajibu wa kwenda kuujenga Mji wa Luguruni ikiwemo ujenzi wa nyumba za gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnyika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli National Housing wana eneo kule Luguruni na walikuwa wamepanga kujenga Satellite City kama ambavyo mkakati ulivyokuwa umepangwa. Eneo hilo halijajengwa mpaka sasa si kwamba limetelekezwa, isipokuwa katika ujenzi, bado kuna utaratibu ambao unaendelea katika kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ilikuwa inasimamiwa na imepangwa kujengwa, inajengwa. Kwa hiyo eneo lile mpaka sasa taratibu ziko vile vile na tungependa kutoa rai watu wasivamie eneo kwa sababu bado matumizi yapo pale pale kama ilivyopangwa. Nami nimhakikishie tu baada ya hii miradi mingine inayoendelea kukamilika, mji ule utajengwa kama ilivyokuwa imepangwa.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze kidogo kwamba maeneo mengi ambayo yamechukuliwa na National Housing nchi hii, mengine tumeweka kama Land Bank ya Serikali kwa sababu National Housing ndiyo mwendelezaji mkuu wa miliki kuliko waendelezaji wengine. Sisi tulijua lile eneo tusingelichukua sisi leo lisingekuwepo na ndiyo maana kwa sababu tumelichukua sisi hakuchukua mtu binafsi, tumeweza kuwapa hawa Ubungo eneo la kujenga wilaya pale Luguruni hivi sasa. Tumeweza kuwapa watu wa MSD kujenga ghala kubwa, walikuwa wanatumia zaidi ya bilioni tatu kupanga kwa ajili ya kuweka dawa lakini tumeweza kuwapa pale. Kwa hiyo wasichukulie tu kwamba maeneo tunayachukua National Housing ni kwa ajili ya uendelezaji wa haraka, lakini tuliya-protect kutokana na manyang’au wanaotaka kulangua ardhi zote za msingi katika maeneo ya miji na kuweka Land Bank.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kwa taarifa yake Mheshimiwa nataka nimhakikishie kama isingekuwa National Housing kuchukua lile eneo wao wasingepata mahali pa kujenga Makao Makuu ya Wilaya.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri aliesema kwamba kwa upande wa wilaya mpya, Serikali inatafuta fedha ili iongeze bajeti kwa ajiliya ujenzi. Sasa Wilaya yetu ya Ubungo ni Wilaya mpya na Serikali kupitia Serikali, nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo, tumejega kituo cha polisi cha wilaya pale Gogoni.

Mheshimiwa Spika, sasa kituo kile cha polisi ni kituo kikubwa, lakini huduma zinakuwa finyu kwa sababu Askari wanatoka maeneo ya mbalimbali sana. Sasa je, Serikali iko tayari, katika kutafuta fedha za ujenzi, itafute vilevile fedha za kujenga nyumba za Askari katika Jimbo la Kibamba karibu na Kituo cha Polisi cha Gogoni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza naye nimpongeze kwa jitihada zake kama alivyozungumza, kwamba kupitia Mfuko wake wa Jimbo na nguvu za wananchi wameweza kujenga hicho kituo. Nikijibu swali lake ni kwamba, tutakuwa tayari, pale ambapo fedha zikipatikana basi tutashirikiana naye katika kumaliza ujenzi wa nyumba iki kituo hicho kiweze kutumika masaa yote.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Majimbo ya Kibamba na Ubungo kabla hayajaondolewa kwenye Manispaa ya Kinondoni yalikuwa yanahudumiwa na Hospitali ya Mwananyamala. Sasa baada ya kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Ubungo, huduma tunazipata kwenye Hospitali ya Sinza Palestina ambayo hailingani na wingi wa watu wa Majimbo haya mawili ya Kibamba na Ubungo na haina eneo kubwa kwa ajili ya kuipanua kuwa hospitali kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa je, Serikali iko tayari sasa kwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Ubungo yako ndani ya Jimbo la Kibamba eneo la Kwembe na kuna ardhi kubwa imepimwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa satellite town Luguruni: Je, Serikali iko tayari sasa kwenda kujenga hospitali ya wilaya kule ili wananchi wa maeneo ya kule wapate huduma ya eneo la karibu zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anazungumza, lakini katika Mkoa wa Dar es Salaam tumepeleka fedha kuimarisha kituo pale Kinondoni, tumepeleka fedha shilingi milioni 200 pale Sinza, tumepeleka fedha Kigamboni shilingi milioni 1.5 kwa awamu ya kwanza na pale Ilala na tumeongeza shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, naomba tupokee ombi hili. Ukweli ni kwamba kila palipo na Makao Makuu ya Wilaya patakuwa na huduma ya wananchi. Awamu hii ikimalizika tutapeleka fedha katika eneo hilo ili wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)