Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Marwa Ryoba Chacha (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kwanza kabisa niwashukuru wananchi wa Jimbo la Serengeti kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mbunge wa kwanza wa CHADEMA tangu Serengeti iwe Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache nahitaji kuchangia kwenye Mpango. Jambo la kwanza ni kuhusu mapato ya Serikali. Nimekuwa Diwani tangu mwaka 2010 katika vipindi vilivyopita ambapo Mpango wa kwanza ulianza, kwa kweli hali ya makusanyo ya mapato ilikuwa ni hafifu sana. Tangu niwe Diwani nimewahi kuona fedha za maendeleo kwa miaka miwili tu na hata hiyo miaka miwili fedha za maendeleo zinazokuja ni 20% au 22%. Sasa kwa namna hii haya malengo ambayo tumejiwekea hayawezi kufikiwa hata siku moja. Kama hatuwezi kukusanya kiasi cha fedha zinazotosha kwa ajili ya maendeleo yetu ni ngumu sana, tutaendelea kudanganyana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu elimu. Kwanza niwashukuru sana wazazi wa nchi hii kwa moyo wao mkubwa wa kujitoa kujenga shule na madarasa mbalimbali. Natambua Serikali ya CCM inajinasibu kwamba wao wamejenga shule kila kona lakini ukweli wajenzi wa madarasa, wanunuzi wa madawati ni wazazi. Kwa hiyo, nawashukuru sana wazazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya mambo yafuatayo bado hatuta-improve chochote kwenye elimu, mimi kitaaluma ni Mwalimu. Ukiangalia shule za binafsi zinafanya vizuri sana kuliko shule za Serikali, tatizo ni nini? Walimu walewale wanaotoka Serikalini wakienda kule private wanafanya vizuri kwa nini wakiwa Serikalini wanafanya vibaya? Nilichogundua ni kwamba hakuna motivation kwa Walimu wa Serikali. Mwalimu mshahara uleule anaoupokea ndio huohuo afanyie mambo yote, haiwezekani! Lazima ifikie sehemu Serikali iwatazame Walimu, iwa-motivate Walimu mkiwaacha hivi wanakuwa demoralized hawawezi kufanya kazi kwa moyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Serikali imesahau elimu ya chekechea. Huwezi uka-base kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba bila kuangalia elimu ya awali. Elimu ya awali tumeiacha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni issue ya maabara, wazazi wetu wamejitahidi wamejenga maabara kila shule lakini sasa vifaa vya maabara hamna. Siamini kama Serikali hii miaka mitano itaisha ikiwa imepeleka vifaa kwenye shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Serengeti ni Jimbo ambalo sehemu kubwa ya Hifadhi ya Serengeti ipo. Serengeti ni mbuga ambayo inaongoza kwa kuwa na watalii wengi kuliko mbuga zote za wanyama zilizopo katika nchi hii. Hata hivyo, ukija katika Wilaya ya Serengeti, siongelei Serengeti National Park, naongelea wanapoishi binadamu, Mheshimiwa Maghembe nakumbuka mwaka jana umekuja pale, maji ya kutumia ni shida. Kilichosababisha nikawapiga CCM kwa muda mrefu maji hakuna. Tangu 2009 limejengwa Bwawa la Manchila mpaka leo hakuna chujio, hakuna usambazaji wa maji. Kwa hiyo, maji yale yako kwenye Bwawa la Manchila lakini namna ya kuyachukua yale maji kutoka pale kuyasambaza hakuna. Ingawa feasibility study ilishafanyika tangu mwaka 2009 mpaka leo implementation hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango huu kwenye ukurasa wa 14, nilitegemea kuona Bwawa la Manchila lakini sijaona. Sijui huu Mpango ume-base kwenye nini. Ukiangalia kwenye huu Mpango ukurasa ule wa 14 kuhusu maji naona wame-base Dar es Salaam sijafahamu miji mingine itakuwaje. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango unapokuja ku-wind up tuambie kwamba mji mingine kwenye Mpango kwa nini haikuingizwa? Nimeona mme-base zaidi Dar es Salaam, je, miji mingine ambayo iko nje ya Dar es Salaam mnafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni barabara, kwenye ukurasa wa 10 - 12 wa Mpango, nilikuwa najaribu kuangalia barabara za mikoa, karibia mikoa yote nchi nzima imeunganishwa kwa miundombinu ya barabara isipokuwa Mkoa wa Mara. Sasa nikasema ngoja niangalie Mkoa wangu wa Mara kama umeunganishwa na Mkoa wa Arusha. Mwalimu Nyerere kabla hajaondoka madarakani ali-propose ujenzi wa barabara ya Musoma – Butiama – Isenye - Nata - Mugumu - Tabora B na kadhalika lakini mpaka leo zimepita awamu nne barabara ile haijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mimi sijawa Mbunge nilikuwa natazama Bunge nasikia kwamba zimetengwa billions of money kwa ajili ya ujenzi wa barabara ile, lakini hata mita moja ya lami haijawahi kujengwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango unapokuja ku-wind up kwenye huu Mpango, hebu tuambie watu wa Mkoa wa Mara barabara ya kutuunganisha na Mkoa wa Arusha itaanza kujengwa lini na itakamilika lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni vizuri tufahamu kwamba Mkoa wa Mara na hususan Wilaya ya Serengeti kitega uchumi kikubwa tulichonacho ni Serengeti National Park na Game Reserve zilizopo lakini watalii ili waje Serengeti ni lazima tuwe na miundombinu mizuri ya barabara. Kwa mfano, barabara ya kuanzia Tarime - Mugumu, barabara ya Musoma - Sirori Simba - Magange - Ring‟wani - Mugumu, ni vizuri zikawekwa lami ili watalii wanapokuja basi waweze ku-enjoy sasa hivi ni za vumbi hata hazieleweki. Haiwezekani mji wa Mugumu ukakua kwa haraka. Ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais wakati anafanya kampeni mwaka jana Serengeti hakuja kwa sababu ya tatizo la barabara. Barabara za Serengeti ni mbovu kuliko zote nchi nzima. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Mipango unapokuja ku-wind up hebu tuambie watu wa Serengeti ni lini barabara ya Musoma – Makutano –Butiama - Nata, Isenye - Tabora B - Clains na Loliondo itakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kilimo. Serengeti kwa sasa chochote tunacholima tunatengenezea tembo. Ukilima mahindi, mihogo, jua unasaidia tembo kushiba. Tukakubaliana wananchi wa Serengeti tulime tumbaku lakini tumbaku tunayoilima haina soko. Sasa tukimbilie wapi watu wa Serengeti? Nyie CCM mmepewa nafasi na wananchi wa nchi hii kwamba muiongoze nchi hii, lakini nawaambia kama msiposimamia rasilimali za nchi hii fursa zikaenda kila eneo mwaka 2020 mtapigwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa Profesa Maghembe jana umetupokea na kwa kweli wananchi wangu wa Serengeti wamekushukuru sana. Naomba utusaidie wananchi wa Serengeti, tumesaidia tembo kutoka 3000 – 7000, sasa hivi tembo wanatutesa, hebu tusaidie basi hata gari moja. Serengeti nzima unapokuja hatuna gari hata moja ambalo mmetupa ninyi Wizara, gari moja tulilonalo alitupa mwekezaji, Grumeti Game Reserve ambalo kwa sasa limechakaa haliwezi kufukuza tembo hebu tusaidieni magari kwa ajili ya kufukuzia tembo. Namshukuru Mungu kwamba tumepata zile ndege (drones) najua zitasaidia lakini haziwezi kusaidia kama hawana magari. Tusaidiane magari ili tuweze kufukuzana na hawa tembo. Sisi watu wa Serengeti tumeamua ku-conserve mazingira ya SENAPA na tumeamua tushirikiane na watu wa Serengeti National Park hebu basi na nyie tuoneni majirani wenu kwamba tunaumia na tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni kuhusu madeni ya Walimu. Nimekuwa Mwalimu Serikalini, nimekuwa Mwalimu private, Walimu wana shida kubwa sana. Sijaona kwenye Mpango kama kuna sehemu yoyote ambayo mmekusudia kuwalipa Walimu. Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up utuambie ni lini mtalipa madeni ya Walimu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano na Mpango huu wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na elimu; ukiangalia Mpango huu umejikita zaidi kwenye mambo ya viwanda ili kubadilisha uchumi wa Taifa letu na maisha ya wananchi wa Tanzania. Nilikuwa najaribu kupitia mpango wote kwenye suala la elimu sijaona kama tumewekeza vya kutosha kwenye suala la elimu. Ninapoongelea suala la elimu, elimu inayoendana na viwanda tumewekeza kwa kiasi gani, Mpango huu umetaja kiwango gani, kiasi gani cha pesa ambazo tumeziwekeza kwenye vocational training.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukulia kwa mfano Mkoa wa Mara, ndiyo Mkoa ambao umetoa Kiongozi mkubwa katika Taifa hili, ambaye ndiye amesababisha na ninyi mmekaa kwenye hivyo viti vya mbele hapo, Mwalimu Nyerere. Mkoa wa Mara hauna Chuo cha VETA hata kimoja, hauna Chuo Kikuu hata kimoja, Mkoa wa Mara watu wake ni maskini kweli, hakuna kiwanda cha kueleweka, Mkoa wa Mara hauna hospitali ya Wilaya, iko shida kweli kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kuelewa vizuri kwamba nilivyokuwa nasikia Tanzania ya Magufuli itakuwa ni nchi ya viwanda nilitegemea nitaona humu fedha za kujenga viwanda, sijaona! Sasa sijui ni viwanda vya namna gani maana nilitegemea Mkoa wa Mara tutapata pale kiwanda, vijana wetu watapata ajira, kumbe hamna ni blah, blah tupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hivi mmesema elimu bure 20,000/= sekondari, lakini wanaojenga madarasa ni wazazi, hawa wananchi wetu maskini ndiyo wanajenga madarasa, ndiyo wanajenga shule, asilimia 90 ya shule zinaendeshwa na wazazi, wewe umesema umeondoa 20,000/=. Iko hivi, wewe chukua asilimia 90 jenga madarasa, peleka madawati, acha wazazi walipe hiyo 20,000/=, hapo tutakuelewa lakini kama wazazi ndiyo wajenge madarasa wapeleke madawati, msiwadanganye Watanzania Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Serengeti, ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Jimbo ambalo kwa miaka mingi limeongozwa na CCM lakini hakuna hata kipisi kimoja cha lami, hata mita moja ya lami hakuna, hospitali ya Wilaya hakuna, Wilaya ya Serengeti kuna wengine hawajui iko Mkoa gani, iko Mkoa wa Mara! Nimeangalia hapa hata kwenye miundombinu ya barabara wanasema mikoa yote imeunganishwa na barabara ya lami, nikajiuliza hivi Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha umeunganishwa na barabara ya lami, barabara aliyoiasisi Mwalimu Nyerere ya kupita Butiama kwenda Arusha mpaka leo, Mheshimiwa Magufuli alikuwa Waziri wa mambo ya barabara, hata mwaka jana hakuja kuomba kura Serengeti maana barabara haijapita pale, lakini walimpa kura nyingi kuliko Lowassa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimpa kura nyingi eeh! walimpa kura nyingi wanataka kumpima waone kwamba uaminifu walioufanya kwake je, yeye atakuwa mwaminifu kwao, asipokuwa mwaminifu 2020 hawampi, habari ndiyo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema ukienda kiuhalisia kwenye vijiji vyetu, kuna upungufu wa madarasa na baada ya kusema elimu bure watoto wamefurika mashuleni, madarasa hakuna, madawati hakuna, sasa nawauliza CCM fedha za kujenga madarasa ziko wapi humu, kwenye Mpango wenu mbona hausemi, ziko wapi? Mheshimiwa Waziri unisaidie utakapokuja hapa uniambie hela za madarasa na madawati ziko wapi humu au ndiyo zile za Bunge bilioni sita zitatosha? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vijijini kwenye shule za msingi, ninakotoka Serengeti nimeenda Shule ya Msingi Gwikongo haina dawati hata moja, mimi nimeamua kama Mbunge niwe mfano nisaidie angalau tupate madawati machache kwenye shule ile, lakini wamekuweko Wabunge miaka na miaka, dawati hata moja hakuna, ni shule hiyo! Wilaya ambayo imeongozwa na CCM muda mrefu, dawati shule ya msingi hakuna, halafu mnasemaje mipango, mipango gani hii! Upungufu wa Walimu ukienda shule za msingi, kuna shule moja ina walimu wawili tu, tangu uhuru mpaka leo wapo wawili, halafu mnasema wanafunzi wanafaulu wanakwenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM mnamsaidia shetani kazi nawaambia ninyi, maana mnatengeneza majambazi wengi, vibaka wengi, ambao baadaye watakuja kuwatesa ninyi wenyewe, maana ninyi ndiyo mtakuwa matajiri, watawaibia ninyi wenyewe. Unafikiri kama akimaliza darasa la saba, kamaliza form four hana ajira unafikiri atafanya kazi gani, atalala na njaa na wewe unashiba hapa, atakushughulikia!
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida, ukienda sekondari Walimu wa sayansi ni kilio, hivi viwanda mnavyosema mnaanzisha siyo maana yake sayansi, Physics, Chemistry, Biology, Mathematics Walimu wako wapi? Walimu wa Sayansi wamekimbia Ualimu maana Ualimu haulipi, hata mimi ni mwalimu wa sayansi nimekimbia kwa sababu hali ni ngumu. (Makofi)
Walimu wanalia, walimu wa sayansi unakuta Mwalimu ni mmoja ana vipindi 50 kwa wiki, Mwalimu wa art ana vipindi vinne kwa wiki lakini mshahara unajua ni ule ule, hiyo biashara ngumu mzee! Kwa hiyo, walipeni walimu wa sayansi vizuri. Vijana wanapomaliza wamefaulu vizuri sayansi form four na form six wanaenda kwenye udaktari, wanaenda kwenye mambo mazuri na hata ninyi ambao mko hapa, wengi ambao mmesoma sayansi mmekimbia huko, wengi siyo walimu! Naomba Waziri unapokuja tuambie mmefanya nini kuhusu elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu mapato. Serikali ya CCM ni ya ajabu sana, wakiona Halmashauri za Wilaya zimetengeneza vyanzo vizuri vya mapato wanabeba, kule Serengeti tulikuwa na bed fee wakabeba, nimesikia sasa hivi wanataka wachukue property tax.
MHE. MARWA R. CHACHA: Sasa ninyi kwa nini msitengeneze vyanzo vya kwenu huko Serikali Kuu, Halmashauri itengeneze vyanzo vya mapato, ninyi mbebe, halafu madawati sisi tutatoa wapi tuwapelekee wale watoto, yaani ninyi mnachukua fedha zote mnakula, eeh mnatumia zote, kwa mfano, mimi nimekuwa Diwani tangu 2010, miaka yote Capital Development Grant (CDG) 26 percent ndiyo inakuja, mnafanya nini? Hamuwezi kufanya chochote.
Nawaambia CCM pumzikeni tupeni CHADEMA hapa tuongoze nchi tuwaoneshe mambo, maana mmeshindwa! nenda kwenye pembejeo ni kilio, kila kitu ni kilio, ukija nimepewa mahindi ambayo mkulima wangu ameenda amepanda hayakuota, sasa hivi wanapaka rangi wanasambazia wananchi kule hiyo ndiyo Serikali ya CCM. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya wananchi wa Serengeti naomba nichukue nafasi hii kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nianze na Mawasiliano. Katika Wilaya ya Serengeti tuna maeneo mengi sana ambayo mitandao ya simu hakuna na tunavyoongelea Serengeti, ndiko kwenye mbuga ambayo inaingiza fedha nyingi katika nchi hii, yaani ndiyo mbuga ambayo inasaidia ku-finance watumishi wa TANAPA kwenye mbuga nyingine kama Mikumi na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mbuga hii kuna maeneo mengi ambayo hayana mawasiliano. Kwa mfano Robo ambako kuna Hoteli ya Robo hakuna mawasiliano kabisa, Bilila iko shida. Mheshimiwa Waziri nikuombe wakati wa ku-wind up hebu njoo na jibu la kueleweka kwamba sasa hoteli ambazo ziko ndani ya hifadhi watapata minara kwa ajili ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni barabara. Sasa naomba niseme kuhusu barabara ya Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo – Mto wa Mbu. Aliyeanza kuwa na maono ya kujenga barabara hii ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati huo ikiitwa Makutano – Nata – Ikoma Gate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye alipokuja Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ndipo wakaanza kuiweka kwenye Ilani ya CCM. Mkapa akaondoka, katika miaka yake kumi hakujenga barabara hii. Akaja Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ikawekwa kwenye Ilani ya CCM, wakati huo Mheshimiwa John Pombe Magufuli akiwa ndiye Waziri wa Wizara ya Ujenzi. Ikapita miaka kumi wala hakuna chochote kilichofanyika. Sasa amekuja ambaye alikuwa Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha. Wakati mwingine watu wa Mkoa wa Mara wanalalamika hawanufaiki na utalii, hawanufaiki na fursa zilizopo za utali, ni kwa sababu barabara hii haijafunguka kuunganisha mkoa wa Mara na mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu sana, barabara hii mwaka 2013 ilitengewa fedha kwenye bajeti ili ianze kujengwa na mwezi wa tatu mwaka 2013 ujenzi wa barabara ukaanza, ambapo wakandarasi wa ndani ndio waliokuwa awarded tender ya kujenga barabara hii. Na bahati nzuri mmoja wa wakandarasi anaitwa Steven Makigo, rafiki yake sana Magufuli, akapewa kazi ya kujenga barabara hii. Yeye na wenzake contractors kumi, tangu mwaka 2013 mwezi wa tatu mpaka leo ninavyoongea wamepewa shilingi bilioni 14 hawajajenga hata mita moja ya lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia; waliopewa kujenga barabara hii ya lami, Makutano – Nata – Mto wa Mbu ni contractors wa ndani wakiongozwa na Kampuni ya Mayanga ambayo Mkurugenzi wake ni huyu Steven Makigo, wako contractors kumi. Wakaisajili kwa jina moja wanasema Mbutu Bridge Contractors; ni wa kwetu ni wazawa. Tangu 2013 wamepewa shilingi bilioni 14 hata mita moja ya lami hakuna halafu mnasema hapa kazi tu, hapa kazi kwa issue gani? Kama mmewapa bilioni 14 wameshindwa wanyang‟anyeni, watumbueni majipu wale, anzeni na huyu mkandarasi, yaani hakuna chochote anachofanya lakini munampa mahela tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nimeuliza swali hapa Mheshimiwa Waziri hakulijibu na hiyo wamepewa kujenga 50 kilometers kuanzia Makutano mpaka Sanzate. Sasa hivi ninavyoongea mkataba wa kujenga barabara ile uliisha mwaka 2015 mwezi wa tano, baadaye wakaomba extension wakaongezewa mpaka Machi 2016, hivi huu ni mwezi gani? Mpaka leo bado hawajajenga hata mita moja, bado tunaendelea ku-entertain watu wa namna hii, si afadhali mtuwekee pale Mchina ajenge ile barabara ikamilike haraka.
KUHUSU UTARATIBU...
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, kwa kanuni aliyoisoma; inasema hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa maudhui ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani kwani mimi nimewashawishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombo niendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi simuongelei Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, namuongelea yule aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu, kama watu wamepewa shilingi bilioni 14 hata mita moja ya lami hawajajenga halafu unaniambia nisiongee, I have to talk. Nimeletwa hapa kama Mbunge wa Jimbo la Serengeti niongee kwa niaba ya wananchi wa Serengeti. Tunachokiongea hapa si mambo ya chama, hata kama ingelikuwa kwako wewe wametumia shilingi bilioni 14 hawajajenga kilometa moja ya lami utasikia vizuri, au huyo malaika akiguswa mnasikiaje? Tulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni yenyewe sasa hivi wanajenga daraja la Mto Kiarano, hata structural engineer hawana, material engineer hayupo! Hivi hii Wizara ikoje hii?
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haina watu wa kwenda kukagua pale waone kwamba kuna structural engineer, material engineer? wataalamu wa namna hii hawapo? Sasa unajenga barabara ya kuunganisha mkoa na mkoa key personnel are not there, ninyi vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nataka Waziri anapokuja atuambie hii barabara itakamilika lini? Kwa mwendo huu ndiyo mtatuambia hapa kazi tu, hakuna cha kazi hapa tunadanganyana. Na kama kweli Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli anaipenda nchi hii, anawapenda wananchi wa Mkoa wa Mara, anawapenda wananchi wa Serengeti, aanze ku-deal na huyu mkandarasi. Kama mtu anaweza kutumia shilingi bilioni 14 halafu hakuna chochote alichofanya halafu watu wanaona sawa tu eti usimguse nitakugusa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara tumesema ni mkoa ambao ni very potential, una mbuga ya wanyama, una migodi ya Nyamongo, tuna watalii na watalii wengi kama mnavyojua wanatokea uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta – Nairobi, wanapita Sirali, Tarime wanakuja Serengeti. Ninavyoongea kwa sasa barabara zote Serengeti zimekatika na tunaelekea kwenye high season, sijui hata hayo mapato tunayoyategemea kutokana na utalii tutayapata wapi kama barabara zimekatika inakuwa ni chaos kwa watalii?
Mheshimiwa Maghembe uko hapo unafahamu, watalii wengi wanatokea Nairobi, sasa kama hatutaki kujenga hata barabara ya Tarime - Mugumu watalii watakata tamaa. Kuna Barabara ya Musoma – Sirori Simba, Magange Ring‟wani ya kuingia Mugumu, barabara zote hizo hazina hata lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Serengeti ndiyo wilaya pekee ambayo mtoto anaweza akazaliwa akasoma Shule ya Msingi Ring‟wani akaenda sekondari ya Ring‟wani akamaliza akaenda form six pale Nata sekondari, akasoma Chuo cha Kisare hajawahi kuona hata lami. Ni Wilaya pekee ya kitalii ambayo haina hata mita moja ya lami…
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi namuomba Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Muda wako umemalizika Mheshimiwa Marwa!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niseme mambo machache na ninaomba Mheshimiwa Waziri unisikilize kwa makini kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza mwaka jana kuna vijana wamepotea katika Jimbo langu la Serengeti, walikamatwa porini vijana zaidi ya 20, mpaka leo ninavyoongea ndugu zao wamewatafuta hawajulikani waliko. Inasemekana wameuawa na askari wa wanyama pori, unapokuja hapa niambie wako wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri unakumbuka walikuja hapa Wajumbe wa WMA mwaka huu, walikuja Madiwani, walikuja Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, walikuja na baadhi ya watendaji kwa ajili ya tatizo la single entry! Sasa tulikutana na wewe ukasema Kamati imekataa. Inawezekana Kamati imeamua, imechukua maamuzi haya kwa sababu haijafika Serengeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumet Game Reserve pamoja na WMA ya Ikona, jiografia ya kwake ni tofauti kabisa na WMA ambazo ziko maeneo mengine.
Mimi ninakuomba Mheshimiwa Waziri tusaidiane wote na Kamati iende ikakutane na Wajumbe wa Ikona WMA, otherwise you want to kill WMA! Na WMA ikifa pale maana yake mapori ya akiba yale yote yataangamia. Maana kama yataangamia maana yake hakuna ajira. Vijana wataanza kuwinda, no conservation will proceed there. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri fanya juu chini, Kamati yako itembelee Serengeti ili ikajiridhishe nini kilio cha watu wa pale Serengeti, lakini kama mkikaa hapa mezani mkaamua, kule mtaua yale mapori na hakuna kitakachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Serengeti National Park imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na imekuwa Gazzeted kwenye Gazeti la Serikali tangu mwaka 1968 kwenye GN Na. 235; ukisoma ile GN iko clear, inataja mipaka ya Hifadhi ya Serengeti National Park. Kilichotokea Wizara yako imeendelea ku-extend mipaka kila kunapoitwa leo. Tangu GN itangazwe wame-extend mipaka zaidi ya mitano, wamechukua maeneo ya wananchi. Sasa sielewi nini maana ya GN? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama GN imetangaza mipaka, leo Wizara yako ina-violate, inachukua maeneo ya wananchi na bahati nzuri beacon zilipo zote tunazifahamu sisi watu wa Serengeti na Mheshimiwa Waziri ukitaka tutakuonesha. Naomba kitu kimoja, unapokuja naomba uniambie uko tayari wewe na Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Lukuvi, kwenda kuhakiki mipaka ambayo ilitangazwa kwenye GN mwaka 1968? Ninataka hayo majibu wakati unapokuja kujumuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tembo na simba. Nimepiga kelele sana kwenye maswali na imefikia sehemu ninaitwa tembo. Iko hivi, hakuna watu wanaopata shida kama wananchi wa Serengeti dhidi ya tembo na simba. Tembo siku hizi anatembea tu kama binadamu wa kawaida, mnagongana naye kama binadamu wa kawaida, hakuna mtu anayechukua hatua dhidi ya tembo na simba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja simba wamevamia kijiji cha Park Nyigoti, sasa wananchi siku hizi walishaelewa ili askari waje hawasemi simba amekamata mnyama, wanapiga simu wanasema tumeuwa simba hapa, dakika tano haziishi wameshafika. Kwa hiyo maana yake ni nini! Tembo, simba ni wa thamani kuliko binadamu. (Kicheko)
Sasa Mheshimiwa Waziri nataka pia unapokuja hapa utuambie katika Sheria ya Wanyamapori mko tayari ku-review, kuileta hapa Bungeni tuipitie upya vile viwango vya kifuta machozi na kifuta jasho? Maana tunajua hamtoi fidia. Mnatoa kifuta machozi na kifuta jasho ambavyo kimsingi haviendani na wakati tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tembo wamekula mashamba ekari tano unampa mtu shilingi 100,000 for what? Shilingi 100,000 kwa eka tano shilingi 100,000 inatosha hata kwa mbegu? Mtu akiuawa mnampa shilingi 1,000,000 hata hiyo shilingi 1,000,000 ataomba miaka 10 ndiyo mnampa. Wewe ni shahidi unafahamu, hamjawahi kulipa. Pale Serengeti watu wameuawa wengi sana na tembo, sijawahi kuona mtu amelipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimeona wameleta wanalipa laki moja moja kwa baadhi ya watu, wengine wote walioathirika hakuna.
Sasa naomba unapokuja ku-wind up uniambie ni lini utaleta ile sheria tuipitie, kifuta machozi, kifuta jasho ili kiendane na wakati tulionao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu barabara. Mimi sijawahi kuona, ninasikia sijatembea sana, lakini nasikia kuna Mbuga inaitwa Kruger iko Afrika ya Kusini, ukitembea kwenye ile mbuga na wanasema ndiyo mbuga inayoingiza watalii wengi na ndiyo mbuga inaingiza mapato mengi, lakini ukienda kwenye mbuga ile kuna lami. Wale ambao mmefika mtakuwa mashahidi, lakini kwenye Mbuga yetu ya Serengeti, hiyo hakuna! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Serengeti ukianzia Tarime, watalii wengi wanatokea Tarime, Sirari. Barabara ile watalii wanalalamika kila leo ingawa ninyi mnapuuza lakini watalii wanalalamika. Wanahitaji kutembelea Serengeti, lakini kutokana na barabara mbovu zilizopo wanaogopa.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, gharama ambayo mnaitumia kila siku ku-maintain barabara za hifadhini ni afadhali mngeangalia zile barabara za msingi, zile ambazo zinatumiwa na magari mkaziwekea lami, hizo nyingine za kawaida kwa sababu hazina magari mazito, mnaweza kuzi-maintain kwa kutumia kifusi na kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ukija kwenye Mbuga ya Wanyama ya Serengeti National Park kuna hoteli lukuki, zaidi ya hoteli 100 ziko mle. Kuna camp nyingi lakini hayalipi service levy wamekimbilia mahakamani yet Serikali mko hapa, hamzisaidii Halmashauri zetu kupata mapato! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapochukulia Halmashauri kama Wilaya ya Serengeti kwa muda mrefu hatunufaiki na utalii. Inafikia sehemu watu wanakata tamaa. Sasa hakuna wananchi wenye nidhamu kama wananchi wa Serengeti kwenye conservation. Huwa wanakuja pundamilia (zebra), tunawarudisha, tunawapigia simu wanakuja wanawachukua. Wananchi wana nidhamu kweli, lakini itafikia sehemu tutachoka. Hebu tusaidie Mheshimiwa Maghembe tupate service levy! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, mkatunyang‟anya na bed fee, gate fee unajua ya kwamba Serengeti mizigo tunayoipata, vitu vya madukani tunavyovipata tunatoa Arusha, lakini mnawa-charge wafanyabiashara wa Serengeti kwenye mageti ya Ikoma Gate, wapi huko kwenda Ngorongoro wanachajiwa (charge) gharama kubwa! Vitu Serengeti ni bei ya juu kweli kweli. Mfuko wa saruji ninavyoongea sasa hivi ni shilingi 23,000 nadhani ndio inaongoza…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chacha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimshukuru jirani yangu Mwita Gatere, Mbunge wa Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la tembo. Tembo ni tatizo Mkoa wa Mara. Tembo ni tatizo Serengeti ni tatizo Bunda, ni tatizo Tarime. Nichukue nafasi hii kutangaza janga la tembo Serengeti, Tarime na Bunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika sehemu tembo anaenda kutafuta chakula kwenye ghala, anabomoa ghala, juzi hapa, ameenda kwenye Kijiji cha Nyichoka, wakabomoa ghala wakala chakula isitoshe wananchi wakahamishia chakula ndani ya nyumba akaenda akabomoa nyumba akala chakula chote, wananchi wamebaki hawana chakula. Bahati nzuri amekuja Naibu Waziri, tumempeleka mpaka maeneo hayo amekuta nyumba zimebomolewa.(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo anauwa wananchi kwa wingi sana sasa hivi, tembo amekuwa ni hatari sana kwenye ukanda wetu huo. Kama Serikali isipochukua hatua ni hatari kubwa mtasikia huko. Sasa hivi majambazi wanauwa tembo hawaendi kuwatafuta hifadhini wanakuja kuwavizia kwenye vijiji vya Serengeti nje kabisa. Juzi hapa nilimwambia Mheshimiwa Waziri wamekuja wakaua tembo sita katika kijiji cha Merenga, wakawapiga wakaua wakang’oa meno wakaenda. Kwa hiyo, sasa hivi majambazi hawasumbuki kwenda kutafuta tembo hifadhini maana tembo wanakuja huku kusambua wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Wizara ya Maliasili na Utalii chukua hatua ya ku-protect wananchi wa Serengeti, Bunda na Tarime dhidi ya tembo. Kama hamtafanya hivyo tembo wanaenda kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni WMA.WMA ni chombo cha wananchi, wananchi wameji-organize wakatoa maeneo ya wakaunda WMA. Leo Wizara ndiyo inakusanya mapato yanayotokana na WMA kwa nini? Kwa mfano, tumeenda Babati kwenye ile WMA ya Burunge Wizara inakusanya mapato, imekusanya shilingi bilioni sita inawapelekea milioni 800 for what? Unakusanya bilioni sita unarudisha milioni 800 itafanya nini? Kwa hiyo, mimi niiombe Serikali, suala la WMA ukusanyaji wa mapato, uendeshaji wa WMA waachie WMA wenyewe, waendeshe wenyewe, wakusanye mapato yao, wajiletee maendeleo wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalotesa WMA ni single entry. Tunaomba Serikali ifanye utaratibu wa kurekebisha bila kurekebisha issue ya single entry WMA zitakufa. Kule kwangu Serengeti WMA ya Ikona sasa hivi mahoteli yaliyokuwa ndani ya hifadhi wawekezaji wameanza kuondoka, kwa sababu hakuna wageni. Serikali naomba mrekebishe hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mauaji, kwangu Serengeti wameuwawa watu 50 na askari wa wanyamapori, ninayo taarifa ambayo nimeandikiwa na Serikali za Vijiji, Watendaji wa Vijiji ambavyo viko kandokando mwa hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba orodha hii nitakuletea uone askari wa wanyamapori wanauwa Watanzania wenzao kisa amekanyaga ndani ya hifadhi anapigwa risasi anauawa. Mimi binafsi Ryoba nimeshuhudia wameuwa, hivi huu ndiyo utaratibu au ndiyo maana Magufuli ameweka Katibu Mkuu mwanajeshi, Mwenyekiti wa Bodi Waitara mwanajeshi ili kuwaua Watanzania wanaoingia hifadhini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu wameuwawa vijana 50, huu ndiyo utaratibu wa Tanzania kuua vijana wake? Ndiyo utaratibu wa Serikali ya CCM? Hebu ninaomba Serikali chukua hatua, kama hamtachukua hatua nitawashughulikia mwenyewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Ryoba dakika zako zimeisha.