Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Devotha Methew Minja (15 total)

MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:-
Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ikilinganishwa na kazi zao wanazofanya kwa jamii:-
Je, Serikali ina mpango gani kuwaboreshea makazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu askari kuboreshewa makazi, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi. Namwona rafiki yangu hapa anashusha kichwa ananyanyua. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na mpango wake wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na kwenye baadhi ya magereza kujenga nyumba na vilevile kuendelea kuona mahitaji ya nyumba na hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 4,221 hivyo kuwepo upungufu wa nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya askari kuishi nje ya Kambi za Jeshi la Magereza. Hata hivyo, kasi ya utekelezaji wa mpango huu umekuwa ni mdogo kutokana na kuathiriwa na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar kama nilivyozungumza kwenye bajeti yetu. Aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbadala ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadiri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika. Mkakati huu utakwenda sambamba na mipango. Nirudie tena, mkakati huu utakwenda sambamba na mipango ya maendeleo ya Serikali ikilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaoajiriwa baadaye.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:-
Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ukilinganisha na kazi zao wanazofanya kwa jamii.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaboreshea makazi.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kama haya ndani ya Bunge lako Tukufu mara kadhaa kuhusu Askari kuboreshewa makazi yao, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya Askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea na mpango wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba kwenye baadhi ya magereza na kujenga nyumba mpya. Mahitaji ya nyumba hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 4,221 hivyo kuwepo kwa upungufu wa takribani nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya Askari wa Magereza kuishi nje ya kambi za jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limesaini mkataba na kampuni ya Poly Technologies ya China kwa kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya magereza nchini. Mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo ni Makao Makuu Magereza nyumba 472, Mkoa wa Arusha nyumba 377, Dar es salaam 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo cha KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani 84.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika Mikoa 17; hii Mikoa 17 tunayozungumzia, tafsiri yake ni kwamba Mikoa 15 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar, wameichukulia Unguja na Pemba kama Mkoa kitu ambacho siyo sahihi. Kwa hiyo usahihi wake ni kwamba Mikoa 15 ya Tanzania Bara na Mikoa 5 ya Zanzibar inafanya kuwa Mikoa 19 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimeona nifanye marekebisho kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukizungumza hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, miradi shirikishi na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakapokuwa ikiimarika. Mkakati huu unakwenda sambamba na mipango ya maendeleo ya Serikali ikilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaoajiriwa baadaye.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kupunguza gharama za upimaji viwanja ambazo ni kubwa sana ili kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma hiyo na kuondoa migogoro ya ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe kwanza maelezo ya awali kwa sababu swali hili juzi limejibiwa, liliulizwa pia na Mbunge wa Mbozi. Kwa hiyo, majibu nitakayoyatoa pengine yanaweza yakafanana na yale yale kwa sababu swali linafanana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi hapa nchini unafanywa na wapima ardhi wa Serikali walioajiriwa na Serikali na wapima binafsi waliosajiliwa na Bodi ya Wapima Ardhi na kupewa leseni za biashara ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali, gharama za upimaji rasmi kwa sasa ni Sh. 300,000/= kwa hekta moja ya shamba na pia kwa kiwanja kimoja. Gharama hizi zilipunguzwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu mwaka 2015/2016 ambapo kabla ya hapo zilikuwa Sh. 800,000/= kwa hekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji zinatokana na sababu zifuatazo:-
(i) Halmashauri nyingi nchini hazijajengewa uwezo wa wataalam na vifaa. Jukumu la kuajiri wataalam na kununua vifaa ni la Halmashauri zenyewe ila upungufu wa vifaa na wataalam ni mkubwa kwa nchi nzima.
(ii) Gharama za vifaa vya upimaji ni kubwa. Ili kupata seti moja ya kawaida ya upimaji kwa kutumia total station ni shilingi milioni 18 na seti moja ya GPS ni shilingi milioni 48. Ukubwa huu wa gharama za vifaa husababisha wapimaji wengi kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa na hivyo kutegemea kukodi kwa gharama kubwa na hivyo kufanya pia upimaji kuwa ghali ili kuwezesha kurejesha gharama za vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la gharama za upimaji nchini, Serikali ina mpango wa kusogeza huduma zote zinazotolewa Wizarani kwenda kwenye kanda. Hatua hii itawezesha kanda hizo kujenga uwezo na hivyo kuchangia kupunguza gharama. Katika kuzijengea uwezo, Serikali inategemea kununua vifaa vya upimaji kupitia mradi wa Benki ya Dunia na kuvigawa vifaa hivyo kwenye kanda ambavyo vitasaidia Halmashauri katika kanda husika na hivyo kuwafikia Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja na kuajiri wataalam wa kutosha katika kada hii ya upimaji na wengine wa sekta ya ardhi ili kuondokana na gharama kubwa za kukodisha vifaa hivyo toka kwenye taasisi binafsi.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Waandishi wa Habari wanafanya kazi nzuri katika kuelimisha jamii.
Je, ni lini Serikali itaanzisha mfumo utakaotambua kazi zinazofanywa na tasnia ya habari?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu swali hili, naomba uniruhusu nianze kwa kuipongeza timu yetu ya vijana ya Serengeti kwa ushindi wa mabao mbili kwa moja dhidi ya Angola jana nchini Gabon. (Makofi)
Vilevile nichukue nafasi hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kushikamana na kushirikiana pamoja kuichangia na kuishangilia pamoja na kuitakia kheri timu yetu hii ya vijana ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huu mfupi, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini kazi zinazofanywa na vyombo vya habari nchini. Mchango wa tasnia ya habari ni mkubwa katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua mchango huo, Serikali imeruhusu uwepo wa vyombo vya habari vya umma na sekta binafsi, yakiwemo makampuni binafsi, mashirika ya kidini na kijamii. Aidha, mchango wa vyombo vya habari unatokana na sera, sheria, mipango na taratibu zilizowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotambua kazi za tasnia ya habari nchini upo tayari. Katika kudhihirisha hilo, Serikali ilitunga Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na sasa ina Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha wanahabari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ili kulinda amani na utulivu katika nchi yetu. Wizara yangu kwa sasa inaainisha mahitaji ya wataalamu katika tasnia ya habari ili kushirikiana na wadau wa ndani na nje tuweze kuwapatia mafunzo kwa lengo la kuboresha kazi zao.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Idadi ya wanafunzi wanajiunga na Vyuo Vikuu vya Mkoa wa Morogoro imepungua kutokana na wanafunzi wengi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika elimu ya juu nchini, ambapo mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 427.54 kugharamia mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Kiasi hiki ni kwa ajili ya wanafunzi 112,623, ambapo wanafunzi 30,000 ni mwaka wa kwanza na wanafunzi 92,623, ni wale wanaoendelea na masomo. Katika robo ya kwanza kiasi cha shilingi bilioni 147.06 tayari kimeshatolewa kwa wakati, hivyo Serikali haitarajii kuwepo kwa ucheweleshwaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, aidha, wanafunzi 3,307 kutoka katika vyuo vitano vya mkoani Morogoro walipata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 11.49 katika mwaka 2016/2017. Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, na Chuo Kikuu cha Sokoine.
Mheshimiwa Spika, suala la mikopo pekee si sababu ya ongezeko au kupungua kwa wanafunzi. Mambo mengine ni pamoja na viwango vya ufaulu alama za ukomo katika udahili, ubora wa vyuo na programu zinazotolewa kulingana na uhitaji wa soko.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Mchango wa kazi za wasanii umeonekana katika kutoa ajira lakini bado wasanii wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kuhujumiwa kazi zao ambapo Mheshimiwa Rais ametoa maagizo mbalimbali ya kushughulikia watu wanaohujumu kazi za wasanii.
Je, mpaka sasa ni hatua gani zimechukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Devotha naomba kwa ruhusa yako nichukue nafasi hii kutoa taarifa fupi ya mafanikio ya mrembo Aisha Mabula ambaye tulimuona hapa hivi karibuni Bungeni, aliewezeshwa na Waheshimiwa Wabunge kushiriki mashindano ya ulimbwende ya Miss World Super Model nchini China.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya washiriki walikuwa 52 kutoka nchi mbalimbali duniani lakini kutoka Afrika ni wawili ambapo mmoja wao ni huyo Bi. Aisha Mabula na Aisha Mabula alifanikiwa kuingia 14 bora kama fainali na katika fainali hiyo alishika nafasi ya tisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Bi. Aisha kwa kuiwakilisha vizuri nchi yetu ya Tanzania pamoja na Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kabisa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa moyo wenu wa ukarimu ambapo mlimchangia na kumuwezesha kushiriki katika mashindano hayo ya kidunia ambayo naamini kabisa mafanikio haya yatamuwezesha kupata ajira na kuendelea kuitangaza nchi yetu Kimataifa na hasa katika sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huu mfupi naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Kamati ya Urasimishaji wa Kazi za Filamu na Muziki nchini inayojumuisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) hutoa miongozo mbalimbali kuhusiana na masuala ya ulinzi na kazi za sanaa.
Aidha, kwa kushirikiana na COSOTA Wizara kupitia BASATA na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) hutoa copyright clearance certificate kwa mmiliki wa kazi yoyote ya sanaa kabla ya kupewa stempu ya kodi ya TRA. Lengo la stempu hizo ni kurasimisha sekta ya filamu na muziki katika uuzaji wa CD, DVD, kanda na kadhalika na hivyo kukabiliana na hujuma katika kazi za wasanii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo sheria na taratibu za forodha na za kulinda hakimiliki zinakiukwa na hivyo kuathiri maslahi ya wasanii, Serikali huendesha operesheni za kukamata kazi hizo za sanaa zenye utata. Hadi kufikia Machi 2017, Wizara ilifanya operesheni kubwa mbili na za kawaida sita dhidi ya filamu zinazoingia sokoni bila kufuata utaratibu ambapo jumla ya kazi 2,394,059 zilikamatwa zikiwemo kazi za nje ya nchi 2,393,529 zenye thamani ya zaidi ya shilingi 3,590,293,500 na za ndani 530 zenye thamani ya shilingi 1,590,000.
Aidha, mitambo ya kufyatua kazi za filamu (duplicators) 19, printers za CD/DVD nane, DVD writers 31, kompyuta tatu na UPS saba zilikamatwa katika operesheni hizo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Wamiliki wa majengo wameanza kupangisha majengo kwa kutumia fedha za kigeni kama vile dola ya Kimarekani badala ya fedha ya Kitanzania hali inayosababisha kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Je, Serikali ina mpango gani kuchukua hatua kulinda thamani ya shilingi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO aliijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania hapa nchini yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 na tamko la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.
Aidha, mwezi Desemba, 2017 Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alitoa tamko lingine kwa Umma kwamba kuanzia tarehe 1 Januari, 2018, matumizi ya fedha za kigeni hapa nchini yazingatie mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
Pili, bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi, zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na visa kwa wageni na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
Tatu, viwango vya kubadilishana fedha vitavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni benki ina maduka ya fedha za kigeni ndiyo pekee yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
Nne, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni. (Makofi)
Tano, vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matamko ya Serikali ya kupiga marufuku matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni ili kulinda thamani ya shilingi, hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei ya huduma na bidhaa, kuhamasisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kupitia programu ya Export Credit Guarantee Scheme na kudhibiti biashara ya maote katika soko la fedha za kigeni hapa nchini.
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y MHE. DEVOTHA M.
MINJA) aliuliza:-
Viwanja vingi vya michezo vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi vimechakaa kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu. Mfano, Kiwanja cha SabaSaba Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kuna haja ya kubinafsisha viwanja hivyo ili viendelee kutumika katika michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inaelekeza kuwa utunzaji wa viwanja utafanywa na taasisi zinazomiki viwanja hivyo. Kwa hiyo, viwanja vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi mfano kiwanja cha SabaSaba katika Manispaa ya Morogoro ni sawa na viwanja vingine vya michezo vya taasisi binafsi, mashirika ya umma, vilabu na vyama vya michezo. Hivyo, suala la utunzaji na ukarabati vinabakia kuwa jukumu la mmiliki.
Mheshimiwa Spika, viwanja vyote bila kujali mmiliki wake vinatakiwa kutunzwa vizuri ili vitumike kulingana na makusudio yake. Pale ambapo uwezo haupo inashauriwa kutafuta wabia na wafadhili ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali hiyo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Serikali iliahidi kutaifisha mashamba makubwa ya uwekezaji yasiyoendelezwa:-
Je, mpaka sasa mashamba mangapi yametaifishwa?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wote wa ardhi nchini ambao wameendelea kukiuka masharti ya umiliki yaliyomo katika Hati Miliki walizopewa. Kwa upande wa mashamba, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015, Disemba mpaka sasa imebatilisha miliki za mashamba 32 yenye ukubwa wa jumla ya ekari 67,393.6, Mashamba haya yapo katika Halmashauri za Kinondoni, Temeke, Kilosa, Mvomero, Morogoro, Iringa, Kibaha, Busega, Muheza, Lushoto, Bukoba na Arumeru.
Mheshimiwa Spika, mbali na mashamba hayo Wizara yangu imeendelea kupokea mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba yasiyoendelezwa kutoka kwenye Halmashauri mbalimbali nchini, zikiwemo Halmashauri za Wilaya ya Tarime, Serengeti na Mkinga ambapo taratibu za ubatilishaji wa mashamba hayo zinaendelea kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini ambazo zimebaini kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa au mashambapori katika maeneo yao kuendelea kuwahimiza Maafisa Ardhi wa Wilaya zao kutuma ilani za ubatilisho au ilani za utelekezaji ardhi kwa wamiliki wa mashamba hayo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura 113 na kuwasilisha mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba hayo katika Wizara yangu ili taratibu za kuyabatilisha zikamilishwe kwa mujibu wa sheria.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya za Mvomero na Kilosa Mkoani Morogoro inaendelea kugharimu maisha ya watu, mifugo pamoja na uharibifu wa mazao.

Je, Serikali imejipanga vipi katika kutafuta suluhu ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika Wilaya za Mvomero na Kilosa, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri husika imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji na Wilaya kwa ajili ya kuainisha matumizi mbalimbali ikiwemo suala la kilimo na ufugaji; kupima mipaka ya vijiji na kuiwekea alama za kudumu; kupima vipande vya ardhi za wananchi na kuwapatia hati za hakimiliki za kimila, lakini pia kubatilisha miliki za mashamba yasiyoendelezwa na kuyapangia matumizi mengine na kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yenye migogoro ili kuyapatia ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo Wizara inaelekeza mradi wa majaribio ya kuwezesha umilikishaji wa ardhi ya vijiji (Land Tenure Support Program) katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi. Mradi huu unatarajiwa kusambaa (ku-scale up), katika Wilaya zingine za Mkoa wa Morogoro zikiwemo Wilaya za Mvomero na Kilosa. Lengo la kukamilika kwa kazi hii ya uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, upimaji wa mipaka na vijiji na upimaji wa vipande vya ardhi na kukamilisha kumilikisha wananchi na hivyo kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wananchi katika Wilaya ya Kilosa na Kilombero kuendelea kuheshimu Sheria za Ardhi, hususan kufuata mipango ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa na hivyo kuondoa uwezekano wa kuibuka kwa migogoro isiyokuwa ya lazima.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Wakati wa kampeni Mkoani Morogoro Mheshimiwa Rais aliahidi kumaliza tatizo la ajira kwa vijana kwa kuhakikisha anarudisha viwanda, vilivyokufa na kuwachukulia hatua walioviua ili kurudisha ajira kwa vijana na wanawake:-

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa visivyofanya kazi vinafufuliwa na kuanza kazi ili vichangie katika uchumi na kutoa ajira kwa vijana. Aidha, Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vipya kutegemeana na fursa zinazopatikana nchini.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Morogoro una jumla ya viwanda 14 vilivyobinafsishwa, kati ya viwanda hivyo, viwanda nane vinafanya kazi na viwanda sita havifanyi kazi. Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa nchini
vikiwemo vya Mkoa wa Morogoro na kubaini kuwa baadhi ya wawekezaji hawajatekeleza kikamilifu makubaliano ya mikataba ya mauzo ikiwa ni pamoja na kutofanya uwekezaji kulingana na mpango uliokubaliwa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia kutoridhika na baadhi ya wawekezaji ambao hawakutekeleza mikataba ya mauzo kufikia mwezi Februari, 2019, Serikali imetwaa viwanda 14 vilivyobinafsishwa vikiwemo viwanda viwili vya Mkoa wa Morogoro. Viwanda vilivyorejeshwa Serikalini kwa Mkoa wa Morogoro ni Mang’ula Mechanical and Machine Tools na Dakawa Rice Mill Ltd. Kwa sasa viwanda vyote 14 vilivyorejeshwa Serikalini vinaandaliwa utaratibu wa kutafuta wawekezaji wenye uwezo wa kuvifufua. Kiwanda cha Morogoro Canvas Mill Ltd ambacho nacho kimefungwa majadiliano yanaendelea kati ya mwekezaji na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, inaendelea kufuatilia kwa karibu viwanda vilivyobaki ambavyo havifanyi kazi vikiwepo viwanda vya Mkoa wa Morogoro ili kuchukua hatua stahiki.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Barabara ya Meimosi Nanenane katika Manispaa ya Morogoro imegharimu fedha nyingi sana za Serikali lakini barabara hiyo haikujengwa katika viwango vinavyofaa.

Je, kwa nini Wakandarasi waliohusika na ujenzi wa barabara hiyo wasichukuliwe hatua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maluum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Meimosi-Nanenane yenye urefu wa kilometa 5.1 (Meimosi (2.6 km), Meimosi 2 (1km) na Meimosi 3 (1.5 km) ilijengwa kwa kiwango cha lami nzito (asphalt concrete) kwa gharama ya Shilingi bilioni 11.81. Ujenzi ulianza Julai, 2015 na kukamilika mwaka 2017 chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri Ms DOCH Ltd ambaye alikabidhi mradi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro mnamo tarehe 30 Aprili, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zote zilizoainishwa kwenye mradi huu zilifanyika kwa viwango vya ubora vilivyoelekezwa na upimaji wa ubora kwa kila hatua ulifanyika. Tangu barabara hii ilipokabidhiwa, haijaonesha udhaifu wowote na inatumika kama ilivyokusudiwa hivyo, Serikali haina sababu yoyote ya kuchukua hatua kwa Mkandarasi aliyejenga barabara hiyo, ahsante.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Matukio ya watu kupoteza maisha kutokana na ajali za moto yamezidi kuongezeka nchini:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukiwezesha Kikosi cha Zimamoto ili kufanya kazi ipasavyo kwenye Miji na nje ya Miji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Pia, Serikali imekuwa ikitenga na itaendelea kutenga fedha za maendeleo katika bajeti ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kuzima moto pamoja na vifaa mbalimbali vya kuzima moto na uokoaji ili kutoa huduma zake ipasavyo ikiwemo kwenye miji na nje ya miji.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inashirikiana na Shirika la Nyumbu katika utengenezaji wa magari mapya ya kuzima moto na uokoaji. Pia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesaini hati ya makubaliano na Kampuni ya ROM Solution ili kupata mkopo wenye masharti nafuu utakaowezesha kupata vitendea kazi mbalimbali ikiwemo magari ya kuzimia moto na uokoaji pamoja na vifaa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo nje ya Miji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kutoa elimu kwa Umma ya kuzuia na kupambana na majanga mbalimbali ili kuzuia na kupunguza matukio ya moto nchini. Pia, Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kumiliki vizimia moto katika maeneo yao ili kuukabili moto katika hatua za awali.
MHE. GRACE V. TENDEGA (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:-

Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars imefanya vizuri na kuliletea Taifa heshima miaka iliyopita hivi karibuni:-

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhamasisha soka kwa wanawake katika ngazi za wilaya na mikoa kuwa na timu za soka za wanawake kama ilivyo kwa wanaume?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Timu ya Soka ya Taifa ya Mwanawake (Twiga Stras) pamoja na ile ya Kilimanjaro Queens miaka ya hivi karibuni zimefanya vizuri na kuliletea taifa heshima. Kwa kutambua mchango wa wanawake katika kukuza soka la nchi yetu Serikali kwa kushirikiana na wadau hususani Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini Tanzania, imejipanga kutekeleza yafuatayo:-

(i) Serikali inaendelea kusajili vyama na vilabu mbalimbali vya michezo pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kusajili vilabu vyao vikiwemo vya soka la wanawake;

(ii) Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wote kushiriki katika michezo ukiwemo mpira wa miguu kwa wanawake;

(iii) Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeendelea kujenga mazingira mazuri kwa vyama na mashirikisho ya michezo kufaya kazi zao. Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pia wameridhia kuanzishwa kwa ligi ya wanawake ya mpira wa miguu;

(iv) Mafunzo mbalimbali ya ukocha na uamuzi wa mpira wa miguu kwa wanawake yametolewa na kwamba tunao wanawake waamuzi (referees) wanaotambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwahamasisha wanawake kujihusisha katika kucheza mpira wa miguu kwa kuwa ni mchezo maarufu na kwamba utatoa fursa ya ajira kwa mtoto wa kike.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Wazee ni hazina ya Taifa lakini wapo wazee wasiojiweza ambao Serikali imewapa hifadhi katika kambi mbalimbali ikiwemo Kambi ya Fungafunga ya Mjini Morogoro. Hata hivyo, kambi hiyo ni chakavu kwa muda mrefu hali inayosababisha wazee kuendelea kuishi katika mazingira magumu:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati kambi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa waliotoa wazee katika ujenzi wa Taifa hili. Aidha, wazee ni rasilimali muhimu katika ustawi na maendeleo ya nchi. Kwa kutambua hili, Serikali inatoa matunzo kwa wazee wasiojiweza katika kambi 17 nchini ikiwemo makazi ya Fungafunga Mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma katika makazi haya, Serikali imefanya tathmini ya hali ya utoaji wa huduma na miundombinu. Taarifa ya tathmini imebainishwa na kuainisha hali ya majengo na miundombinu katika makazi haya ikiwemo makazi ya Fungafunga na imeweka mkakati wa kuboresha hali ya majengo na miundombinu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inajali haki na ustawi wa wazee kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 na itafanya ukarabati wa kambi hizi kwa awamu kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha.