Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Elly Marko Macha (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia Mpango ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa suala zima la upunguzaji wa umaskini. Katika jamii watu ambao ni maskini kuliko wote ni watu wenye ulemavu kwa sababu ulemavu unasababisha umaskini na umaskini unasababisha ulemavu. Pia niseme kwamba hapa Tanzania statistics tunazotumia katika kuelezea idadi ya watu wenye ulemavu katika nchi hii zina upungufu mkubwa. Tanzania Bureau of Standard wanasema asilimia nne, tano au milioni mbili ndiyo watu wanaoishi na ulemavu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa sensa hakuna ushirikishi katika kuhakikisha kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanajumuishwa katika sensa. Kuna ulemavu wa aina nyingi mwingine unaonekana kama mimi nilivyo sioni, naonekana kama sioni, lakini kuna ulemavu ambao hauonekani (hidden disability) kama viziwi au watu wa pyschosocial, watu wa down syndrome, dyslexia, huwezi kuona. Kwa hiyo, wanapofanya zile sensa wanasahau kujumlisha aina nyingi sana za ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mipango yetu katika Wizara zote tufuate ile statistic iliyotolewa na WHO pamoja na World Bank kwenye Disability World Report ya 2011 inayosema kwamba katika kila nchi asilimia 15 ni watu wenye ulemavu. Sasa basi sisi Tanzania ambao tuko milioni 46 mpaka 50 tukitumia hiyo statistic ya World Report ina maana kwamba watu wenye ulemavu nchi hii ni kati ya milioni 6.2 mpaka milioni 7.0, hii si idadi ndogo. Naomba Mipango inapopangwa itumie hiyo ripoti mpaka hapo itakapofanyika sensa nyingine ya kuonyesha jinsi data ya watu wenye ulemavu itakavyokuwa captured katika sensa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ulemavu unasababisha umaskini na umaskini unasababisha ulemavu, unakuta watu wenye ulemavu wako katika hali mbaya. Nataka kusema kwamba hii bajeti inayokuja izingatie kuweka bajeti kwa ajili ya maendeleo ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, mtu asiyeona akitaka kwenda hospitali inabidi aende na msindikizaji au kiziwi inabidi aende na mkalimani na unapokwenda na msindikizaji ina maana kwamba unalipa nauli yako na ya msindikizaji wako na kiziwi inabidi alipe nauli yake na ya mkalimani wake. Ina maana kwamba spending ya mtu mwenye ulemavu ni mara mbili kuliko ya mtu asiyekuwa na ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo basi naomba familia zile zenye watu wenye ulemavu ambao ni severely disability, kuna familia ambazo zina watoto wenye ulemavu ambao hawawezi kutembea, hawawezi kuongea, hawawezi chochote na anahitaji uangalizi masaa 24 siku saba. Hizi familia ni nyingi, nimeshaanza kufanya data collection, wafikiriwe kupewa cash ya kuwawezesha kuishi. Kwa mfano, hawa akinamama ambao wanatunza watoto ambao ni severely disabled hawana nafasi kabisa ya kufanya kitu chochote kile cha kuwasaidia kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaposema itafikiria pension kwa wazee, ifikirie pia pension kwa wale members of family ambao hawana nafasi hata kidogo ya kutafuta kibarua ili aweze kuishi. Mtu anakuwa na mtoto mwenye ulemavu kuanzia asubuhi mpaka jioni na siku zote hana nafasi ya kutafuta chakula. Kwa hiyo, nao wapewe hiyo pension angalau hata Sh.30,000 kwa mwezi kwa maana ya Sh.1000 kwa siku ili waweze kununua chakula cha kuishi kwa sababu hawana nafasi kabisa ya kushughulika na shughuli za kujiongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo cash transfer wenzetu wengine wameshaanza ku-effect, nchi kama Malawi na Kenya. Nafikiri sisi siyo maskini kuliko Malawi lakini wanafikiria pamoja na wazee na wale severely disabled people wapewe hiyo cash transfer ili waweze kuishi. Utakuta wengi ambao wanaachwa na hawa watoto ambao ni severely disabled ni akinamama kwa sababu baada ya mama kupata mtoto mlemavu au mtoto aliyelemaa, waume zao huwakimbia na kuwaacha akinamama wakihangaika na hao watoto. Naomba Serikali ifikirie kuwapa jinsi kuishi hizi familia ambazo zina walemavu ambao ni severely. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nilioutoa, kuna wafanyakazi ambao wana ulemavu matumizi yao yako juu, Serikali inaonaje kuanza kuwapunguzia ile tax ya Pay As You Earn (PAYE) kwa sababu hizo nilizozieleza. Mtu mwenye ulemavu anatumia zaidi kuliko mtu asiye mlemavu. Kwa hiyo, Serikali imsaidie yule anayefanya kazi kwa kumpunguzia kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, wenzetu wa Kenya Serikali yao ilishaona hili miaka mitano iliyopita, sasa hivi mwenye ulemavu yeyote pale Kenya anayelipwa mshahara wa kuanzia Sh.1-150,0000 ya Kenya ina maana Sh.3,000,000 ya Tanzania, inapozidi Sh.151,000 ile Sh.1 ndiyo wanaanza kuitoza kodi lakini ile Sh.150,000 wanamuachia kwa sababu wanajua matumizi ya mtu mwenye ulemavu ni makubwa. Naomba Serikali hii ifikirie katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika suala la elimu, kweli elimu imetolewa bure mpaka kidato cha Nne. Nategemea watoto wenye ulemavu pamoja na kwamba watasoma bure lakini vifaa vyao ambavyo vingi havipatikani hapa Tanzania vinaagizwa, vitabu vyao vinachapishwa katika maandishi ambayo wanaweza kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ina mtambo wa kuchapisha vitabu vya wasioona lakini huu mtambo kwa miaka mingi umefanya kazi chini ya kiwango chake. Hauna vifaa, hauna fedha za kununua makaratasi, matokeo yake ni kwamba watoto wasioona ambao wanahitaji braille na wale wa uoni hafifu ambao wanahitaji large print hawana vitabu vya kiada katika shule mbalimbali hapa nchini. Serikali kupitia Wizara ya Elimu ifikirie kukiboresha kile kiwanda cha kuchapisha vitabu vya wasioona na wale wenye uoni hafifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala lingine la uchukuzi. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi mnavyojua usafiri wa bodaboda unasababisha vifo na ajali nyingi na vina-create ulemavu kwa watu wengi sana hapa nchini. Baada ya miaka mingi mtakuta Watanzania wamelemaa kwa ajili ya hizi bodaboda. Nashauri Serikali iweke measures za kusimamia hawa waendesha bodaboda, aidha wawapatie training au watafute njia nyingine ili kupunguza watu wanaolemaa migongo, wamekatika miguu kutokana na hizi ajali nyingi zinazosababishwa na bodaboda.
kwamba kuna mkakati wa kufufua viwanda. Naomba Serikali ikumbuke kwamba watu wenye ulemavu pia wanahitaji ajira, hivyo viwanda viwe accessible ili waweze kuajiriwa kama wanavyoajiriwa Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nilisikitika kwa vile nilinyoosha mkono niulize swali la nyongeza sikupata nafasi. Waziri alipokuwa anazungumzia Morogoro akasema kuna asilimia tano ya fedha za TASAF kwa ajili ya wanawake, asilimia tano kwa ajili ya vijana, kwa nini hakuna asilimia tano kwa ajili ya watu wenye ulemavu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kusema kwamba Tanzania iliridhia ule Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa 2006 na pia ikaja na Sheria Na.9 ya 2010 kuhusu Watu Wenye Ulemavu. Naomba sasa implementation ya hizi sheria ifanyike kwa sababu hakuna maana ya kusaini na ku-ratify and then hakuna implementation.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kuomba Serikali isaini ule Mkataba wa Kimataifa kuhusu copyright kwamba watu wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida wakiwepo wasioona, wenye uoni hafifu, wenye dyslexia, wenye down syndrome, wale publishers wa-publish kazi zao kwa maandishi ambayo ni accessible ili watu wenye ulemavu waweze kusoma vitabu. Naomba Serikali isaini na kuridhia ule Mkataba ili na sisi watu wenye ulemavu wa kutoweza kusoma maandishi ya kawaida tufaidike na treaty hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii ya kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote napenda kumpongeza Waziri wa Elimu na Naibu Waziri pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Elimu kwa kutayarisha Hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa pole Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye amefiwa na mama yake mpenzi, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Kabla sijachangia kwenye hotuba hii kwanza kabisa ninalo ombi, ombi langu ni kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Waheshimiwa Mawaziri. Wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanatumia dehumanizing terminologies kwa mfano vilema, siyo wote nimesema baadhi na pia kuna baadhi ya Mawaziri wanatumia neno kama vilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotumia neno vilema, maana yake vi ni non-living object yaani ni kitu ambacho hakina uhai tunasema viti, vikombe, vijiko lakini watu wenye ulemavu ni watu. Kwa hiyo, naomba tutumie lugha ya kuwathamini na kuwapa utu watu wenye ulemavu, kwamba ni watu wenye ulemavu na sio vilema. Ahsante naona hilo limeshakuwa noted. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kuchangia hotuba, kwanza napenda kumshukuru Waziri alipokuwa akitoa Hotuba yake alisema kwamba, elimu maalum ameipa kipaumbele katika Wizara yake, hiyo nashukuru. Katika kuipa elimu maalum kipaumbele, napenda kuchangia kwa kuanzia ule mtambo wa kuchapisha vitabu vya nukta nundu ambapo upo chini ya Wizara ya Elimu, upo pale Uhuru Mchanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mtambo ulianzishwa katika miaka ya 70 kwa msaada wa Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la CIDA kwa ajili ya kuisadia Wizara ya Elimu iweze kutoa maandishi ya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona pamoja na maandishi makubwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu, pamoja na kutengeneza zile hearing aids kwa wale wanafunzi ambao wana upungufu wa kusikia. Hata hivyo, baada ya Shirika la Sweden kusitisha msaada wake kwenye miaka ya 80, ufanisi wa ule mtambo wa kuchapisha vitabu vya maandishi ya braille ambao ni mtambo pekee hapa Tanzania, Tanzania nzima, mashule yote ya msingi pamoja na sekondari yanategemea mtambo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi wa mtambo huu umekuwa ni duni, jengo limechakaa, mashine ni mbovu, Mheshimiwa Waziri mwenyewe alishafika pale anajua. Wafanyakazi wanaopelekwa pale ni wafanyakazi wasiokuwa na uwezo na mara nyingi Wizara ya Elimu imekuwa ikipeleka wafanyakazi ambao wana matatizo, wale wanaohitaji light duty ndiyo wanapelekwa kufanya kazi pale. Matokeo yake hivi tunavyoongea katika shule zote za watoto wasioona na wale wenye uoni hafifu, msingi pamoja na sekondari hawana vitabu vya text book na hawana vitabu vya kiada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria mwanafunzi anaingia darasani, wenzake wanapata vitabu vya masomo yote jiografia, historia, lakini mwanafunzi asiyeona hana kitabu chochote anachosoma, anaingia pale kusikiliza na kuondoka bila kupata vitabu, ni kwa sababu uzalishaji wa vitabu vya namna hiyo umekuwa ni duni na umekuwa na matatizo, mashine hakuna zilizopo ni mbovu, rasilimali hakuna wenye uwezo. Kwa hiyo, production ya ile Braille Press imekuwa chini kiasi kwamba shule zetu sasa hivi wanafunzi wetu wasioona na wale wenye uoni hafifu hawana vitabu vyovyote vya kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ambaye hili suala analijua afanye jitihada kuona kwamba ule mtambo umekuwa equipped, jengo limetengeneza, wanapelekwa pale wataalam wenye uwezo wa ku-produce hiyo braille press ili supply ya vitabu vya nukta nundu mashuleni liweze kutosheleza, ambapo sasa hivi hakuna kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo la kile chuo kimoja tu Tanzania nzima, Chuo cha Patandi ambacho kinatoa elimu maalum kwa Walimu wa elimu maalum. Mpaka 2010 Tanzania hii ilikuwa na shortage ya Walimu wa elimu maalum 16,000 na sasa hivi wameongezeka. Chuo cha Patandi ambacho kina miundombinu ambayo ni mibaya, inahitaji matengenezo, hawana vifaa vya kufundishia wala vya kujifunzia, kinahitaji kupewa vipaumbele na Wizara ya Elimu ili kiweze kutoa Walimu wa elimu maalum wa kutosha. Kwa mwaka wanatoa Walimu kati ya 150 mpaka 250 tu, lakini nimesema upungufu hadi sasa ni zaidi ya 16,000 wa elimu maalum wanaohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo shule za msingi ambazo zinakaribia 90 ambazo zinachukua wanafunzi mbalimbali wasioona na walemavu wa aina nyingine. Tunazo shule za sekondari, lakini pamoja na hayo Walimu wa elimu maalum ni wachache na chuo ni kimoja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009, Wizara ya Elimu ilitoa inclusive and special need education frame work ambapo ilisema kati ya 2009 mpaka 2017 vyuo vingine vitakuwa vinatoa dozi ya elimu maalum kwa ajili ya kwamba Walimu wanapohitimu wanakuwa na ufahamu wa jinsi ya kuwashughulikia au jinsi ya kuwapokea na kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpaka sasa hivi ile frame work bado haijatekelezwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri afuatilie hiyo education frame work ya inclusive education ili tuweze kuona inafanya kazi na vyuo vingine vyote vinapata component ya special education ili waweze kuwapokea wanafunzi wenye elimu maalum katika shule zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija suala la elimu bure, Waziri sijaona ni mipango gani ameiainisha kwenye hotuba hii, jinsi wanafunzi wenye ulemavu nao watakavyofaidika na huu mpango wa elimu bure. Wapo wengi ambao wana umri wa kwenda mashuleni wapo majumbani, shule zilizopo hazitoshelezi na sijaona mikakati ambayo ipo kwa ajili ya kuwafaidisha wanafunzi au watoto wenye umri wa kwenda shule wenye ulemavu na wao wafaidike na hii elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wanafunzi viziwi, mpaka sasa hivi wanafunzi hawa wana matatizo ya kupata Walimu wakalimani wa lugha ya alama wa kuwafundisha katika mashule. Kwa hiyo, naomba pia kuwe na mkakati wa kuimarisha mafunzo ya lugha ya alama ili wanafunzi hao nao wapate nafasi ya kupata elimu kama wanavyopata wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Elimu awasiliane na Waziri anayeshughulika na sera kuhusu watu wenye ulemavu. Kuna Treaty ya Kimataifa ambao inaitwa Marrakesh Treaty, hii Treaty inatakiwa iwe ratified na nchi 20 ili iweze kufanya kazi na inasema kwamba inawalazimisha publishers au wachapishaji waweze kutoa maandishi ya vitabu vyao wanavyochapisha katika accessible format.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ikiwa imeshasaini na kuridhia, Serikali ina uwezo wa kuwalazimisha publishers waweke maandishi yao katika maandishi ambayo yanaweza kusomwa na watu wasioona pamoja na watu wengine ambao wana matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida kama watu wenye Dyslexia au kama watu wenye down syndrome ama kama watu wenye uoni hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii sheria kama itaridhiwa itasaidia pia ile wanaita cross border literature, ni kwamba kama kuna nchi moja inatoa vitabu ambavyo vinaweza kutumia katika nchi nyingine, hiyo sheria inawataka wale watu wenye copyright waruhusu kazi zao ziweze kusafirishwa katika nchi nyingine ili wanafunzi wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida waweze kupata nafasi ya kusoma vitabu hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itilie mkazo somo la computer kwa wanafunzi wenye ulemavu waweze kwenda na teknolojia. Wanafunzi wenye ulemavu wakipata nafasi ya kujua teknolojia, ya kujua kompyuta watakuwa na uwezo zaidi wa ku-access information, wataweza kwenda kwenye vyuo vikuu bila matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha tena kuwa na afya njema ya kuchangia hoja ambayo inachangiwa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukupongeza, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ambayo mimi ni Mjumbe na pia kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, napenda kuwapongeza Waziri wa Afya, Naibu Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi njema wanayoifanya na kwa hotuba walioiwasilisha mbele yetu ambayo sasa tunaijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika masuala matatu; suala la kwanza, ni kwamba jana na leo Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamezungumzia suala la watu wenye ulemavu mbalimbali katika Wizara hii. Sipendi kurudia ambayo yameshazungumzwa, nina imani kwamba Mawaziri wanaohusika wame-take note ya hayo yote, lakini napenda kwenda mbele zaidi kuwasilisha ombi kwa Wizara hii kwamba kuna umuhimu sana Waziri anayehusika Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake baada ya Bunge hili kwenda kuanzisha desk ama focal point kwa masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ulemavu ni cross-cutting na japokuwa mambo ya walemavu yako chini ya Waziri Mkuu, lakini Wizara zote na critically ni Wizara ya Afya, inatakiwa kuwa na department au kuwa na desk au focal point kwa ajili ya masuala ya watu wenye ulemavu. Ni kwa nini? Kwanza tukumbuke kwamba ulemavu unasababishwa aidha kwa kuzaliwa nao ama unapatikana kutokana na magonjwa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Waziri na Wizara yake amelipa kipaumbele suala la kinga, kwa sababu kunapokuwa hakuna kinga, ndipo magonjwa mengi yanasababisha ulemavu. Kwa hiyo, ni critical hii Wizara iwe na professional advice kwamba masuala ya walemavu yawe katika muundo wa Wizara. Mambo ya Waziri Mkuu kule yaliko ni mambo ya sera, mambo ya sheria, mambo ya ushauri, lakini mambo ya huduma, mambo ya matibabu, mambo ya kinga, yanatakiwa yashughulikiwe kikamilifu na Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ulemavu nimesema ni profession, kwa hiyo, naomba Wizara inayohusika iwe na kitengo au department ambayo itakuwa inashauri kuhusu mambo ya ulemavu, kwa sababu kuna watoto wenye ulemavu, wanapokuwa na matatizo itakuwa vipi? Kuna wazee wenye ulemavu, kuna masuala ya jinsia; mambo ya wanawake wenye ulemavu. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara hii ikiwa na idara ama kitengo ambacho kitashughulikia masuala ya ulemavu ili kumshauri Waziri pamoja na timu yake jinsi gani ya ku-deal na masuala haya yanayotokana na ulemavu kutokana na jinsi Wabunge walivyochangia hapa tangu jana na leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kupata ufafanuzi kutoka kwa Waziri ni suala la watu wa Ustawi wa Jamii. Sijui watu wa Ustawi wa Jamii wako wapi! Sijui kama wameunganishwa na Maendeleo ya Jamii; lakini nina imani kwamba bado wako katika Wizara hii. Kuna Maafisa Ustawi wa Jamii Mikoani, Wilayani na mpaka kwenye ngazi za Mitaa. Sasa hawa wana-belong katika Wizara gani? Kama wana-belong katika Wizara hii, role yao ni ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kugusia suala la watoto, kuna vituo mbalimbali hapa nchini kwetu ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya kuhudumia watoto yatima na suala la watoto yatima linahudumiwa na Mashirika ya Serikali na pia yasiyokuwa ya Serikali. Kuna NGOs nyingi ambazo zimeanzisha vituo na centre za watoto yatima, lakini katika vituo hivi, pamoja na kwamba kuna wengi wana nia nzuri ya kusaidia watoto yatima, lakini pia kuna mambo mengine ambayo hayastahili, yanaendelea kwenye hivyo vituo vya watoto yatima. Kuna vituo vingine vya watoto yatima ambapo kuna child abuse sana inaendelea na vingi pia viko chini ya wafadhili wengine kutoka nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafadhili wengine wamekuja hapa wakianzisha vituo hivyo, wana nia njema, lakini kuna wengine wana agenda zao katika hivyo vituo. Wanakuwa wanapiga picha wale watoto, wanawapeleka kwao kwenda kufanya fundraising na wanapata pesa nyingi; na wanapokuja na pesa hizo utakuta wanawaleta watu wa kwao wengi in the name of volunteers; na wale Watanzania ambao wameajiriwa katika hivi vituo wanalipwa pesa kidogo sana na pesa nyingi walizo-fundraise wanawalipa wale watu wa kwao waliokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Wizara kwamba kuna haja ya kuwa na monitoring mechanism ya kuhakikisha kwamba wale wanaoendesha hivi vituo vya watoto yatima kweli wahakikishe vinaendeshwa katika misingi inayokubalika na wale watoto wasitumike katika ku-fundraise kwa ajili ya faida yao, bali ile fundraising inayofanyika itumike katika kuendeleza watoto hao na katika kuwalipa Watanzania vizuri wanaofanya kazi katika hivyo vituo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine pia katika vituo hivi nilivyosema. Kwa mfano, kule Arusha kuna kituo kimoja kiko chini ya Wamarekani, wale Wamarekani wanaoendesha kile kituo cha watoto yatima, watoto wanapougua pale hawawapeleki hospitali, wanasema tuwaombee. Ilitokea hata mwaka 2015 mtoto mwingine alikufa. Kwa hiyo, kuna hizo imani kwamba watoto tuwaombee na hakuna kuwapeleka hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni child abuse na kama Wizara haita-monitor mambo kama hayo tutakuta watoto wetu wengine ambao ni yatima wanafanyiwa vitu ambavyo havistahili. Kwa hiyo, kuna haja ya kuwa na monitoring system ambayo inaeleweka ku-control hawa ambao wanaendesha hivi vituo, ambao wana nia nzuri waeleweke na wale ambao wana nia mbaya pia waweze kugundulika ili vitendo kama hivyo vikomeshwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la Benki ya Wanawake. Naiomba Wizara na Waziri, Mheshimiwa Ummy, kwamba hii Benki ya Wanawake kuna affirmative action gani ambayo imechukuliwa kuhakikisha kwamba wanawake wenye ulemavu nao wanafaidika na mikopo na huduma za hiyo Benki. Kama hakuna affirmative action tutaendelea labda kusema hapa. Lilionekana hili ni suala la Wabunge wenye ulemavu, lakini hili ni suala la kila mwanamke na Waziri pia na aliweke katika mikakati yake awe na affirmative action ya kuhakikisha kwamba wanawake wenye ulemavu nao wanafaidika na mikopo ya hiyo ya Benki ya Wanawake iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuchangia ni kama nilivyosema, jinsi gani watu wanapata matatizo katika hizi bodaboda. Mheshimiwa Waziri alieleza katika hotuba yake kwamba kuna pesa zimetengwa katika kuimarisha kile kituo cha MOI pale Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuimarisha kituo cha MOI, lakini pia kuna haja kuwepo na mikakati madhubuti kwa ajili ya kuelimisha hawa waendesha bodaboda ambao kwa kweli kwa upande mmoja ni ajira ambayo wamepata vijana wengi lakini kwa vile hakuna mafunzo yanayotolewa, ajali ni nyingi na ulemavu unasababishwa siku hadi siku, watu wengi wanavunjika, watu wengi wanazidi kulemaa kutokana na hizi bodaboda.
Kwa hiyo, nafikiri kuna haja ya kuwa na mkakati wa kutoa elimu kwa hawa wanaofanya hii biashara ya bodaboda ili kupunguza wale watu wanaoathirika katika kulemaa kwa ajili ya ajali mbalimbali zinazosababishwa na hizi bodaboda, ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia hapo. Nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia huu Muswada wa The Access to Information Bill. Kwanza kabisa namwomba Waziri anayehusika pamoja na team yake kuongezea title ya hiyo Bill iwe The Access to Information in Accessible Format. Nasema in accessible format kwa sababu kama tunavyojua nchi yetu asilimia 10 mpaka asilimia 15 ni watu wenye ulemavu. Kuna watu wenye ulemavu mbalimbali ambao hawawezi ku-access katika normal print au katika maandishi ya kawaida yaliyozoeleka. Kwa hiyo hii Bill inatakiwa iwe access to information in accessible format.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano, mimi hapa nilipo, kwanza hiyo Bill yenyewe sijaweza kuipata, kwa hiyo sijai-access, hivyo kuchangia kwangu pia hakutakuwa na impact sana kwa sababu sijaisoma, naona labda kwa vile mimi ni minority in this Bunge, kwa hiyo access to information bado ni problem. Kwa hiyo, naomba kwamba kama hii Bill itawazingatia watu wenye ulemavu ihakikishe kwamba tusiishie kusema access to information bali tuseme access to information in accessible format.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wenye ulemavu ambao ni viziwi ambao wanahitaji sign language interpretation. Kama watu wenye ulemavu wasioona kama mimi hapa vile ambaye nahitaji access to information in accessible format katika braille, kuna watu ambao ni dyslexia, kuna watu ambao ni downs syndrome na kadhalika. Kwa hiyo namwomba Waziri aboreshe hiyo title ya hii Bill iwe access to information in accessible format ili kila Mtanzania mwenye ulemavu awe na haki ya ku-access information katika mfumo ambao anaweza kuupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua access to information ni tatizo hasa kwa watu wenye ulemavu, kwa sababu siyo mambo ya maandishi tu hata ile verbal communication. Kuna watu wengine hawawezi ku-communicate kwa verbal information – wanahitaji accessible format kama sign language interpretation. Kwa vile sijaisoma hiyo Bill ningeomba lizingatiwe kwamba access to information ianzie hapa Bungeni halafu tuboreshe hii Bill iwe access to information in accessible format.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi niliyopata. Kwanza, napenda kuanza kwa kueleza masikitiko yangu kwamba hizi document tunazopitia za miswada mbalimbali hakuna hata moja ambayo mimi nimeweza kui-access. Nashindwa kuelewa ni kwa nini. Najua Mbunge asiyeona niko peke yangu lakini sitaki kufikiri kwamba Bunge halinithamini, lakini najua kwamba kukiwa na ile will, accessibility ya hizi document naweza kuipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuitambua Wizara ya Elimu ambayo inanijali sana kwa sababu wao wanahakikisha kwamba nimepata document zao at least two days in advance, nimezisoma lakini hakuna Wizara nyingine yoyote ambayo inanikumbuka, kwa hiyo nasikitika kwa hilo. Hata Order Paper, tangu tumeanza Bunge hili bado sijaweza kupata Order Paper yoyote katika braille. Kwa hiyo, naomba nisionekana niko peke yangu, nafikiri nina haki sawa na Wabunge wenzangu, ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikichangia hoja iliyo mbele yetu napenda kuchangia kwa kifupi tu kuhusu Mkemia Mkuu wa Serikali na Bodi yake. Wabunge wengine hapa walichangia tangu juzi wakisema kwamba hii Bodi haina wanawake, mimi naenda mbele zaidi nikisema hii Bodi pia inatakiwa iwe na mtu mwenye ulemavu kwa sababu kuna masuala mbalimbali ambayo Bodi ikiwa na mwakilishi ambaye anaelewa masuala ya watu wenye ulemavu atakuwa katika position ya kuishauri ipasavyo. Kwa mfano, kuna watu wenye ulemavu mbalimbali hasa ulemavu wa akili ambao wanabakwa na wengi wanabakwa na family members iwapo katika composition ya hiyo Bodi atakuwepo mtu mwenye ulemavu atakuwa katika position ya kutetea masuala kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunavyojua ulemavu pia unatokana na genetics, kwa hiyo, wale akina mama wanaokuwa wajawazito ambao kwa njia moja au nyingine watoto wao watazaliwa na ulemavu, akiwepo mtu katika hii Bodi ataweza kutoa ushauri na kuandaa hawa akina mama kisaiokolojia ili watakapojifungua wakiwa na watoto wenye ulemavu watakuwa wameshaelewa na itapunguza matatizo ya akina mama au akina baba kuwatelekeza watoto wao kwa ajili ya ulemavu au kuwa-abandoned.
Kwa hiyo, nashauri Waziri anayehusika na huu muswada amuingize katika hii Bodi mtu mwenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.