Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amina Nassoro Makilagi (10 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu jioni ya leo. Vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu, muweza wa yote aliyeniwezesha kusimama kuweza kuzungumza jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana sana wananchi wa Tanzania kwa kujua mchele ni upi na pumba ni zipi na kuchagua Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa upande wa Wabunge 73% na kwa upande wa Madiwani 74% na kwa upande wa Viti Maalum 80%, kwa kweli wananchi Mwenyezi Mungu awajalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoweza kusema hapa, tunawaahidi kwamba imani huzaa imani, tutaendelea kuwatumikia kwa moyo wetu wote na hata pale ambako Chama cha Mapinduzi hakikupata kura tutawahudumia bila ubaguzi likiwemo Jimbo la Arusha na Majimbo mengine ambako CCM haikushinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana, mpendwa wetu Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi alivyoanza kutekeleza kazi. Ameanza vizuri, anafanya kazi nzuri na kama kura zingepigwa leo ushindi wa CCM ungekuwa ni 69.999%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya utangulizi huo, napenda sasa kujielekeza kwa mambo machache ambayo nimeyapanga kuyatilia mkazo katika hoja iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa, naomba kuunga mkono hoja iliyo mbele yetu kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu yangu ya kwanza ni kwamba, Waziri wa Fedha na timu yake yote wameandaa vizuri Mwelekeo wa Mpango wa mwaka 2016/2017. Ni Mpango unaoeleweka, wenye matumaini na ambao umelenga kuwakomboa Watanzania katika suala zima la kuwakomboa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa sababu endapo Mpango huu utapangwa na ukatekelezwa, nina imani yale ambayo tumeyaandika kwenye Ilani ya CCM yataweza kufikiwa. Naomba sasa nitoe ushauri kwa mambo machache yafuatayo na nitaanza suala zima la ukusanyaji wa kodi. Ili mpango utakaotengenezwa usiendelee kubaki kwenye makaratasi, nilikuwa naishauri Serikali yetu hii ya CCM ijielekeze katika kuhakikisha inakusanya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupongeza kazi nzuri ambayo imeanza kufanywa ya kukusanya mapato, lakini bado kuna baadhi ya mapato yanaishia mifukoni mwa watu, pia bado kuna mashine za kukusanyia mapato ni feki na bado kuna taasisi ambazo zinatumia vitabu ambavyo havieleweki katika mfumo wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niishauri Serikali ili Mpango wa Maendeleo uweze kutekelezwa katika mwaka 2016/2017, lazima pia tuweke mkakati namna ambavyo Serikali itakusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nishauri Serikali yetu na Mawaziri wetu kwamba, katika kutekeleza Mpango huu, hauwezi kutekelezeka kama hawajadhibiti upotevu wa mapato na matumizi yasiyokuwa ya lazima. Naiomba sana Serikali yetu, ijielekeze katika kuhakikisha Mpango unaokuja 2016/2017 unalenga kwenda kuwakomboa Watanzania na hasa wanawake. Naomba Mpango unaokuja 2016, tujielekeze katika kuhakikisha suala zima la maji na hasa vijijini linapatiwa ufumbuzi ili wanawake wetu wanaotembea umbali mrefu waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, mwaka jana tulipanga mpango mzuri, lakini kwa bahati mbaya sana, hivi ninavyozungumza, sekta ya maji imepata asilimia nane tu ya bajeti. Sasa kama tutatengeneza mpango mzuri kama utakavyokuja na kama fedha hazikutafutwa na zikatengwa, Mpango wetu utabaki kwenye makaratasi na matokeo yake lengo ambalo limekusudiwa halitafikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika kuhakikisha Mpango unatekelezwa ni lazima tujielekeze sasa kuweka vipaumbele katika sekta ambazo zitaongeza mapato na napongeza mpango wa Serikali wa kuhakikisha tunafufua viwanda, tunaanzisha viwanda vipya na kukaribisha wawekezaji waje kuwekeza, lakini hapa naomba nitoe ushauri.
Naomba niishauri Serikali kwamba isijitoe katika suala zima la uwekezaji wa viwanda na naomba Serikali isitegemee wawekezaji kutoka nje peke yao. Ni lazima Serikali ijipange kuhakikisha tunawawezesha Watanzania wa kati, wafanyabishara wadogo na wafanyabiashara wakubwa ili wawe na uwezo wa kujenga viwanda hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo viwanda peke yake, ni pamoja na kilimo na hasa Mwenyekiti hapa ninaposisitiza, uchumi wetu hauwezi kukua kama kilimo chetu bado ni cha kutegemea mvua. Nahimiza twende na kilimo cha umwagiliaji na tuongeze wigo, badala ya kutegemea mikoa ya Nyanda za Kaskazini ndiyo zilishe nchi nzima, hebu tuangalie na Kanda ya Ziwa iliyozungukwa na mito na maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie mikoa ya Kanda ya Kati ambayo bahati mbaya ni mikoa kame, kuna Mkoa wa Tabora, Singida, Dodoma ambapo sasa hivi mvua zinanyesha mpaka tunakosa pa kupita, lakini Mkoa wa Dodoma kila siku wanalia njaa na tunategemea Mkoa wa Ruvuma na Rukwa. Naiomba Serikali iipe sekta ya kilimo fursa ya pekee na katika bajeti inayokuja tuipe nafasi inayostahili, tuipe fedha ya kutosha ili sekta ya kilimo iweze kuleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri ili tuweze kufikia malengo tunayokusudia, ni lazima tujielekeze katika suala la uvuvi na tujielekeze katika kuvua katika kina cha bahari kuu. Tujenge Bandari na hasa hiyo ya Bagamoyo na Bandari zingine. Kama hatutaweza kwenda kuvua kwenye kina cha maji marefu, tukaifanya sekta ya uvuvi kama ni sekta ya uzalishaji ya kiuchumi, Mpango wetu utabaki kuwa kwenye makaratasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia, hebu watumie ushauri aliotoa Mwenyekiti Chenge na timu yake wakati ule wa bajeti, Waziri wa Fedha, achukue ushauri ule, ni ushauri mzuri sana, kuna mambo mengi sana yapo mle, hebu angalieni vyanzo vipya ili uchumi wa nchi yetu uweze kukua na tuweze kupiga hatua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali yetu, pamoja na mipango mizuri iliyowekwa hapa, lakini tujielekeze katika kuwawezesha wanawake kiuchumi. Nimefurahishwa na Mpango uliopo wa kupeleka milioni 50 katika kila kijiji na mtaa, naomba katika mpango unaokuja, lazima tuweke mfumo, hizi milioni 50 zitafikaje katika kila kijiji…
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama na kutoa mchango wangu katika hoja iliyo mbele yetu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizi, naomba nijielekeze kuchangia. Kwanza, pongezi na shukrani kwa Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Naomba nianze kwa kumshukuru sana na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo yafuatayo:-
(i) Kwa jinsi alivyounda Wizara hizi nyeti mbili na kuzifanya ziwe chini ya usimamizi wa Ofisi yake na jinsi alivyowateua Mawaziri na Naibu Waziri wenye weledi wa hali ya juu na wenye uchapakazi pia, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Suleiman Jafo.
(ii) Kwa jinsi alivyoanza kazi na kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na nidhamu ya kazi, wanakuwa waadilifu na wenye uwajibikaji wa hali ya juu ndani ya Serikali aliyoiunda. Lengo likiwa ni kuleta tija kwa Watanzania wote bila kuleta itikadi za dini, vyama, kabila wala jinsia zao na kuleta maendeleo ya hali ya juu ndani ya muda mfupi na mabadiliko yanaonekana.
(iii) Kwa kubana matumizi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na kutoa zaidi vipaumbele katika miradi ya kuinua uchumi wa nchi.
(iv) Kwa jinsi alivyolipa kipaumbele suala zima la watumishi hewa kwani ameweza kuokoa fedha nyingi ambazo zilikuwa zinapotea bure na kwenda kwa watu wasiohusika wala kuzifanyia kazi. Badala yake fedha hizi hivi sasa zinakwenda kuendeleza miradi mbalimbali hasa kwa wananchi waishio katika kaya maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi anayoifanya Mheshimiwa Rais na timu yake ndani ya Serikali imeleta matunda mazuri ndani ya nchi yetu katika muda mfupi kiasi kwamba wale Watanzania ambao hawakumpigia kura wanasikitika sana. Watanzania sasa wanasema itakapofika 2020 hawatafanya makosa tena na CCM kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani watashinda kwa 100%.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nitoe ushauri katika maeneo machache niliyoyachagua, kwanza, ni uchangiaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake na Vijana (10%). Pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuzielekeza Mamlaka ya Serikali za Mtaa kutenga 10% kwa ajili ya kusaidia vikundi vya maendeleo ya wanawake na vijana lipo tatizo kubwa la fedha za Mfuko huu kutopelekwa kwa vikundi vya wanawake na vijana kama ilivyokusudiwa kwa sababu halmashauri zilizo nyingi hazitengi kabisa fedha hizi na zinazotenga zinatenga kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili linaonekana kama jambo la hiari katika mamlaka husika, napenda kujua, je, utaratibu huu wa kutenga 10% kwa vijana na wanawake upo kwa mujibu wa sheria? Kama ni kwa mujibu wa sheria, je, ni kwa nini halmashauri hazitengi fedha hizi? Je, ni hatua gani zinazochukuliwa dhidi ya watu wasiotenga fedha hizi? Kama utaratibu wa kutenga 10% ya Mfuko wa Vijana na Wanawake hauko kwa mujibu wa sheria, je, ni lini Serikali italeta Muswada huu hapa Bungeni ili tuweze kutunga sheria hiyo itakayowabana wale wote wasiotenga na kufikisha fedha hizo katika vikundi husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ucheleweshaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Utaratibu wa fedha za miradi ya maendeleo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimekuwa ni changamoto kubwa kwani hazitolewi kwa wakati, zinazotolewa ni kidogo na hazitoshelezi kukamilisha miradi na uwiano wa kutoa fedha hizi hauzingatiwi kwani halmashauri zingine zinapata nyingi na zingine kidogo au hakuna kabisa. Napenda Waziri atuambie hapa tatizo ni nini na Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati gani wa kukabiliana na changamoto hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, upungufu wa wafanyakazi katika mamlaka mbalimbali za Serikali. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kupeleka watumishi wa kada mbalimbali katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, bado lipo tatizo kubwa sana la watumishi katika Halmashauri za Mitaa na hasa Walimu wa sayansi katika shule za sekondari; Madaktari na Wauguzi katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati; Maafisa Ugani wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; na Wakuu wa Idara katika halmashauri nyingi ni wale wanaokaimu. Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akihitimisha hoja yake naomba atoe maelezo Serikali imejipangaje kuhakikisha inapeleka wafanyakazi hao katika mamlaka mbalimbali za Serikali ili utendaji wao uweze kuleta tija kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, maslahi ya wafanyakazi. Pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali za kuboresha maslahi ya wafanyakazi bado kuna wafanyakazi wa umma na sekta binafsi wana matatizo ya mikataba; kupata mishahara midogo ya kima cha chini sana; kukosa posho zao za kujikimu au kutopatiwa kwa wakati na makazi yao ni duni sana hasa wale waishio vijijini. Naiomba sana Serikali pamoja na vipaumbele ilivyojiwekea waangalie maslahi ya wafanyakazi hasa Walimu, Wauguzi, Maaskari na wafanyakazi wa halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, uimarishaji wa Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa ndiyo sekta pekee inayotoa huduma kwa wananchi siku hadi siku kwa ukaribu zaidi. Ili kuboresha sekta hii nashauri:-
(a) Serikali ithubutu na kufanya uwekezaji ili Mamlaka ya Serikali za Mtaa ziwe na vyanzo vyake vya mapato vya kutosha na kutoa mchango wake katika pato la Taifa;
(b) Mamlaka za Serikali za Mitaa zielekezwe kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea, wawe wabunifu ili waongeze wigo wa ukusanyaji wa mapato; na
(c) Serikali za Mitaa kuna upotevu wa fedha kwa matumizi yasiyo na tija na kutozingatia matumizi ya fedha. Kwa hiyo, Serikali lazima ihakikishe kuwa kanuni za fedha zinafuatwa na fedha zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa hasa katika kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niunge mkono hoja na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru wewe na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu kwa ustawi wa Taifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Joyce Lazaro Ndalichako na timu yake yote kwa kuandaa na kuwasilisha vizuri sana hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2016/2017. Pia natoa pole kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kuondokewa na mzazi wake mpendwa. Naomba Mwenyezi Mungu ampe moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na roho ya marehemu iwekwe mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa mchango wangu kwenye makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa vitabu vinavyotumika kufundisha mashuleni, wakati soko huria la utengenezaji na usambazaji wa vitabu likilenga kupunguza uhaba wa vitabu Serikali idhibiti ubora wa vitabu ili kuhakikisha vitabu vinavyotumika shuleni vinakuwa na ubora ili kuzalisha wasomi wazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa nini kifanyike kwenye mtaala wa elimu, Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu itengeneze mfumo ambao vijana wengi watakwenda kwenye Vyuo vya Ufundi na hivyo kuwa na wazalishaji wengi ambao wataweza kuunda vitu mbalimbali na sio kuwa na kundi kubwa la wasomi wa vyuo vikuu ambao watakuwa wanatafuta kazi baada ya kutunukiwa shahada zao. Ni muhimu sana Serikali ipitie upya mfumo wetu wa elimu ambao kwa kiasi kikubwa unawaandaa wasomi wetu kuwa waajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/2015, idadi ya vyuo iliongezeka kutoka 26 hadi 50 kati ya mwaka 2005 hadi 2014 na hivyo idadi imeongezeka kutoka wanafunzi 40,719 kwa mwaka 2005 hadi wanafunzi 200,986 kwa mwaka 2014. Wasomi wote hawa wanaandaliwa kuwa watawala ambao wataanza kutafuta ajira na hivyo kusababisha nchi kuwa na wasomi wengi ambao watahitaji kuajiriwa na siyo kuwa wazalishaji kutokana na mfumo wetu wa elimu kuwa na nadharia nyingi na siyo vitendo. Katika karne ya sasa ni muhimu Serikali kufanya marekebisho katika mfumo wetu wa elimu ili uwezeshe vijana wetu kuwa wazalishaji pindi tu wanapohitimu elimu ya vyuo vikuu na hivyo kuweza kujiajiri wenyewe badala ya kusubiria ajira za Serikali na mashirika binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Wizara zake ielekeze pesa nyingi kwenye miradi ya maendeleo na sio kwenye matumizi ya kawaida. Mfano, kwa mujibu wa hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyosomwa Bungeni na Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, kwa mwaka 2015 sekta ya utalii peke yake ilitoa ajira rasmi kwa vijana 500 na ajira 1000 zisizo rasmi.
Aidha, kwa mwaka 2016/2017, Serikali iendelee kuboresha mazingira ya utalii kama vile kununua ndege, kujenga barabara na kujenga viwanja vya ndege ili sekta ya utalii ifanye vizuri ziaidi na hivyo kusaidia kupunguza tatizo la ajira ambalo kwa kiasi kikubwa linatokana na mfumo wetu wa elimu, kuzalisha wasomi wengi wenye shahada ambao wanategemea kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya sasa Serikali lazima itambue kuwa tatizo la ajira kwa wasomi wetu wa vyuo vikuu linazidi kuongezeka kila siku kutokana na mfumo wetu wa elimu kuwaandaa vijana wetu kuwa waajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwandishi wa kitabu cha Rich Dad Poor Dad Robert Kiyosaki anasema mifumo ya elimu yenye mtazamo wa go to school, study hard, get good grades and find a safe and secure job umepitwa na wakati.
Aidha, mwandishi huyu anashauri mifumo ya elimu ya sasa iwe na mtazamo wa go to school, study hard, get good grades, build your business and become a successful investor. Serikali itazame namna ya kuhakikisha vijana wengi wanapata elimu ya ufundi ambayo itawasaidia vijana wengi kuwa wazalishaji wa moja kwa moja na siyo kutegemea ajira. Katika nchi zilizoendelea kiteknolojia kama China na Japan vifaa vingi vidogo vidogo vinatengenezwa na vijana ambao kwa kiasi kikubwa wana elimu ya ufundi tu. Ingawa tuna vyuo vya ufundi stadi, bado idadi ya wanafunzi wanaojiunga katika vyuo hivi ni ndogo kama ilivyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, ukurasa wa 95.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa vyuo vya ufundi kila mkoa; umefika wakati sasa Serikali ianzishe vyuo vya ufundi kila mkoa ambavyo vitawasaidia vijana wetu kupata elimu ya kuwawezesha kujitegemea na siyo kutegemea kuajiriwa na Serikali. Aidha, vyuo hivi vitoe elimu kutokana na mazingira ya eneo husika. Mfano, vyuo vitakavyojengwa Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya vitoe elimu ya ufundi juu ya matumizi ya mazao ya mbao na vile vitakavyojengwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa vijengwe vyuo vya kutoa elimu ya ufundi na ujuzi na kusindika samaki. Kama Serikali itaweka mfumo ambao vijana wengi watakwenda kwenye vyuo vya ufundi wataweza kuzalisha samani nyingi ambazo Serikali pia inaweza kununua samani ambazo zitakuwa zinazalishwa na vijana wetu hapa hapa nchini kwa matumizi mbalimbali na hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kutokana na kununua samani nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais za kujenga Tanzania ya viwanda, ni muhimu vijana wengi wawe na elimu ya ufundi ambao wataanzisha viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vitazalisha samani mbalimbali. Aidha, wasomi wetu wenye elimu ya ufundi wanaweza kuunda viwanda vikubwa ambavyo vitasaidia katika kuleta mapinduzi ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi 2016/2017, je, Serikali imejipangaje kwa mwaka 2016/2017 kutatua changamoto za upungufu wa madawati, upungufu wa nyumba za Walimu na madai ya Walimu ambayo ni muhimu hasa katika kuimarisha sekta ya elimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike kwa mwaka 2016/2017, katika Wizara hii, baada ya Serikali ya Awamu ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli imeanza kutoa elimu bure na hivyo watoto wengi wamejitokeza shuleni na hivyo kusababisha shule kufurika watoto wengi. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili, Wizara ya Elimu na wadau mbalimbali wa maendeleo waweke mpango mkakati wa kutatua changamoto hizi kama vile kushawishi wananchi, taasisi binafsi na Serikali katika kuchangia ununuzi wa madawati na ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwezesha watoto wengi kupata elimu.
Aidha, kwa mwaka 2016/2017, Serikali iendelee kuboresha mazingira ya kazi na makazi ya Walimu hasa wale walioko vijijini. Walimu wapandishwe madaraja na kulipwa stahili zao bila kucheleweshewa, pia kwa mwaka 2016/2017, Serikali ianze kuwapa motisha ili kuwapa moyo na kuwahamasisha wengine kufanya kazi kwa bidii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kuunga mkono makadirio ya mapato na matumizi Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi 2016/2017 yapitishwe, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Wizara imeomba kupitishiwa jumla ya shilingi trilioni 1.396 huku matumizi ya kawaida yakiwa ni shilingi bilioni 499 sawa na 35.7% ya bajeti yote huku miradi ya maendeleo ikitengewa shilingi bilioni 897 sawa na 69.1%. Ili kuunga mkono jitihada za kuinua kiwango cha elimu kwa mwaka 2016/2017, Serikali imedhamiria kuinua kiwango cha elimu kwani kati ya shilingi bilioni 897, Serikali imetoa shilingi bilioni 620 sawa na 69.1%, ni fedha za ndani huku 30.9% ikiwa ni fedha za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017, Serikali ihakikishe kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Elimu zinapelekwa kwa wakati ili kuimarisha kiwango cha elimu nchini. Mfano wa mwaka 2015/2016 hadi tarehe 30 Aprili, 2016 Serikali ilipeleka shilingi bilioni 789 sawa na 72.12% ya bajeti yote. Kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano imejiimarisha katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi ni vizuri kwa mwaka 2016/2017 Serikali ipeleke fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuinua kiwango cha elimu, Serikali imeongeza kiwango cha bajeti kutoka shilingi trilioni 1.094 hadi shilingi trilioni 1.396 sawa na ongezeko la 21.6% kutoka mwaka 2015/2016 hadi 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja hizi mbili ambazo zipo mbele yetu za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utumishi wa Umma.
Awali ya yote napenda nichukue nafasi hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu muweza wa yote, aliyenipa nafasi kuweza kusimama na kutoa mchango wangu katika Bunge lako hili Tukufu. Naomba nianze kabisa kwanza kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kiwango cha hali ya juu sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Rais kwa masuala machache yafuatayo:-
Nitaanza kusema kwamba, nianze kumpongeza Rais kwa jinsi alivyounda hizi Wizara mbili, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utumishi na jinsi alivyozipanga na kuhakikisha Wizara hizi zinakuwa chini yake, nimpongeze kwa kuwachagua Mawaziri mahiri, Mheshimiwa Angellah Kairuki, na mwenzake Mheshimiwa Simbachawene. Hakika Mawaziri hawa wana weledi mkubwa, wanafanya kazi kwa uaminifu mkubwa, ni watendaji ambao ni wachapakazi na kwa kweli tuna imani nao. Ukweli umedhihirisha jinsi walivyoandaa hotuba zao, na jinsi ambavyo wameziwasilisha kwa kwelie napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza.
Vilevile nimpongeze Rais kwa jinsi alivyoanza, kuhakikisha anapunguza na kumaliza tatizo kubwa sana sugu la mishahara hewa katika nchi yetu ya Tanzania. Ni ukweli usiopingika mara tu baada ya Rais kuchagua Wakuu wa Mikoa aliwapa siku 19 wahakikishe wanabaini watumishi hewa, lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zilizokwenda kwenye mishahara hewa ziweze kwenda kwa wananchi.
Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais, kipekee niwapongeze sana Wakuu wa Mikoa kwa kazi njema wanayoendelea kuifanya kuhakikisha wanabaini wafanyakazi wote hewa ili fedha itakayokuwepo iweze kwenda kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais jinsi anavyobana matumizi, katika uendeshaji wa Serikali, ni ukweli usiopingika kwanza amechagua Baraza dogo, vilevile hata yale matumizi yasiyokuwa na tija Mheshimiwa Rais ameyabana, ninaomba aendelee kufanya hivyo ili kuhakikisha fedha zile ambazo zilikuwa zinatumika katika matumizi ya kawaida ziweze kuelekezwa kwa wananchi na hasa katika masuala mazima ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa utendaji wake bora, amesimamia nidhamu ya watumishi na uwajibikaji katika Serikali yake aliyoiunda. Ni ukweli usiopingika tangu ameingia madarakani wafanyakazi wote nchini wameonesha uwezo mkubwa kufanya kazi kwa kuwajibika, wanawahi kazini, wameendelea kuwa waaminifu, wanafanya kazi kufa na kupona ili kuhakikisha dhamira ya Mheshimiwa Rais inakutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema wale wote wanaobeza juhudi za Rais naomba Watanzania tuwapuuze kwa sababu ndiyo kawaida yao, maana kila siku wanaamka na jipya, tulipokuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne walisema Serikali hii siyo sikivu, Serikali imechoka, Serikali ina watu wapole sana; amekuja Dkt. John Magufuli, ameanza kazi leo wameanza kulalamika. Naomba wananchi muwapuuze na Dkt. John Pombe Magufuli endelea kuchapa kazi, akina mama na Watanzania tuko nyuma yako na ninapenda kuwathibitishia Watanzania na Wabunge wenzangu kwamba kabla ya kuja hapa nimetembea zaidi ya Mikoa tisa wananchi wanasema kama kura zingepigwa leo ushindi wa CCM kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani ungekuwa zaidi ya asilimia 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanasema, hata wale ambao hawakumchagua Mheshimiwa Magufuli, wanatamani uchaguzi ungerudiwa leo na hata wale ambao hawakumchagua wanajuta, wanasema turudie uchaguzi leo ili wampigie kura zote Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Dkt. Rweikiza alisema ukiona kule watu wanaanza, ukiona wanafanya jambo halafu wapinzani wanapiga kelele umewabana pabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Magufuli endelea tuko nyuma yako na nakuomba endelea kutumbua majipu na hata yale yaliyosababisha mishahara hewa na mengine yako humu ndani na ndiyo maana mengine yalikimbia ili nchi yetu ipate tija, kwa maendeleo yetu...
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mara baada ya kusema hayo napenda niendelee kumwomba Mheshimiwa Rais asisikilize porojo na propaganda zozote kwa sababu suala zima la mihemko huwa lina wakati wake na mihemko ina mwisho wake.
TAARIFA...
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nimeipokea na huo ndiyo ukweli, wataisoma namba, mara baada ya uchaguzi huo sasa...
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya utangulizi huo naomba nijielekeze kutoa mchango wangu katika maeneo machache ambayo nimeyachagua na kuyatilia mkazo kama ifuatavyo; pamoja na kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kupeleka fedha kwa ajili ya mifuko ya wanawake na vijana asilimia kumi kwa ajili ya vijana na wanawake, na mkakati uliopo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi, wa kupeleka shilingi milioni 50 katika kila mtaa na kila kijiji, naomba kutoa ushauri ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kupeleka asilimi kumi ya vijana na wanawake, kwenye baadhi ya Halmashauri imekuwa ni kitendawili, bado kuna baadhi ya Halmashauri hapa nchini na Manispaa na Miji na Majiji agizo hili hawalitekelezi kikamilifu, ombi langu nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa mbele yetu, atuambie hivi suala la kupeleka asilimia kumi kwa ajili ya vijana na wanawake ni la hiari, ni la kisheria, ni la utaratibu gani, na kama ni la kisheria ni kwa nini Halmashauri, Manispaa na Majiji hawatengi fedha kama ilivyokusudiwa na Serikali yetu? Nitapenda Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akihitimisha hotuba yake, atuambie kama jambo hili siyo la kisheria, je, yeye kama Waziri ambaye ameaminiwa na Mheshimiwa Rais ana mkakati gani kuhakikisha, anaileta hii sheria hapa Bungeni ili tuweze kutunga hiyo sheria itakazozibana Halmashauri, Majiji na Miji ambayo hawatengi asilimia kumi ya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu wanawake wa vijijini, wanawake wa mijini, wanavikundi vya VICOBA, wanavikundi vya ujasiriamali, wana SACCOS lakini Halmashauri zetu na Miji yetu bado wanafanya mzaha katika kupeleka fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali, katika ule mkakati wa kutekeleza Ilani ya CCM ya kupeleka shilingi milioni 50 kila kijiji na shilingi milioni 50 kila mtaa, naomba kabla ya Bunge hili halijaisha tunataka kuona fedha hizo, nataka tuone fedha hizo hata kama zinapitia kwenye Serikali za Mitaa, hata kama zitapitia Benki ya Wanawake, hata kama zitapitia Benki ya NMB, hata kama zitapitia kwa Wizara yenyewe ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, hata kama zitapitia kwenye Mfuko wa Vijana, tunaomba fedha hizi, kabla ya Bunge hili halijafungwa, Waziri wa Fedha aje hapa mbele yetu atuambie fedha hizi ziko wapi, tuziangalie katika kitabu hiki ziko wapi, na zianze kupelekwa vijijini kama ambavyo zimekusudiwa ili wanawake na vijana wa Tanzania waweze kunufaika na mpango huu wa Chama cha Mapinduzi kwa sababu Chama cha Mapinduzi kimedhamiria kuwaondoa katika umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika masuala mazima ya maslahi ya wafanyakazi. Wafanyakazi wa Tanzania, wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya utendaji kazi katika nchi yetu, hata haya matunda tunayoyaona mazuri ya utekelezaji wa ilani ya CCM, wafanyakazi wa Tanzania wana mchango mkubwa. Ombi langu katika kupeleka mishahara ya wafanyakazi, ile Bodi ya Tume ya Mishahara iangalie uwiano, tusipishane sana, unakuta Mbunge anapata mara mbili, unakuta kiongozi wa shirika anapata mara tatu, lakini huyu karani, huyu dereva, huyu askari polisi, huyu nesi, huyu daktari, tufanye uwiano ili mishahara na hao wafanyakazi wa kawaida wanaofanya kazi zilizo sawa, waweze kutendewa haki maana kwa kweli ndiyo tegemeo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la wafanyakazi, kuna nyumba za wafanyakazi, kuna maslahi yao na hasa wanaoishi vijijini walimu wetu, manesi, madaktari, askari…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, mengine nitayaleta kwa maandishi, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyo mbele yetu, hoja ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana wewe na kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote aliyenipa nafasi ya kuweza kusimama na kuweza kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu iliyo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nianze kuungana na Wabunge wenzangu wote kukupongeza sana wewe Naibu Spika kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuendesha Bunge letu Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi na uwezo mkubwa sana wa kiwango cha kupigiwa mfano. Hakika Dkt. Tulia ni kijana mdogo, ni mara yako ya kwanza kuwa Naibu Spika na ni mama ambaye kwa muda mfupi umetushangaza wanawake, umewashangaza Watanzania na umeshangaza hata ulimwengu kwa jinsi ulivyo mwaminifu, mvumilivu na siyo hivyo tu na jinsi unavyojua Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umetukumbusha mpaka enzi za Mzee Mkwawa na Maspika waliopita. Una muda mfupi ndani ya Bunge, umepitia Hansard kwa muda mfupi na kila unaporejea Kanuni pia unarejea Hansard na unatoa mifano ya Maspika wenzako. Kwa kweli, wale wanaokubeza nakuambia lala usingizi, wanawake tupo nyuma yako na tumejiandaa kikamilifu, wameanza wao tutamalizia sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema hatuna muda wa kupoteza, mara baada ya Bunge Tukufu kukamilisha kazi zake utatusikia na huko tutakwenda kuongea na wananchi kwa sababu uwezo tunao. Dkt. Tulia tutakutetea, chapa kazi na tupo nyuma yako maana kama ingekuwa ni adhabu wangempa Mzee Chenge ambaye yeye ndiye aliyewatoa leo iweje wanakususia wewe ambaye umesimamia Kanuni na taratibu za Bunge! Hongera sana Dkt. Tulia, songa mbele, tupo nyuma yako, Watanzania na wananchi wenye weledi wanakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wanasema ukiona baadhi ya wanaume anapokalia mwanamke kiti wanakimbia, nafikiri hapo jibu lao mnalo, maana mwanaume hakimbii boma. CCM oyee, aah, sorry. (Makofi/Kicheko) [Maneno haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya utangulizi huo, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hii ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa asilimia 100 na sababu ninazo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ya kuunga mkono, Mheshimiwa Waziri na timu yake yote imeandaa bajeti hii kwa weledi wa hali ya juu sana. Bajeti hii kwa kweli imekonga moyo wangu na imekonga mioyo ya Watanzania kwa sababu ni bajeti inayokwenda kujibu matatizo ya wananchi, inakwenda kujibu kero za wananchi, inakwenda kuwapa wananchi fursa mbalimbali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, inakwenda kutekelezwa kwa kuhakikisha inaweka nidhamu ya uwajibikaji ndani ya watumishi wa umma na siyo kwa watumishi wa umma peke yake na hata wananchi na inakwenda pia kutekeleza maandiko ya Vitabu Vitakatifu ambavyo vinasema asiyefanya kazi na asile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na timu yake kwa sababu bajeti hii pia inakwenda kuondoa kodi zote ambazo zilikuwa ni kero kwa wananchi. Mfano, bajeti hii inakwenda sasa kuondoa kodi ya madawa ya maji, mimi kama mama ni jambo ambalo nimelizungumza. Katika miaka mitano nilikuwa kwenye Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Kamati ile ilipiga kelele kwa miaka mitano haikufanikiwa lakini bajeti hii inakuja na pendekezo la sisi Wabunge kwenda kuondoa kodi ya madawa ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inakuja na pendekezo la kuondoa ushuru na kodi katika mazao ya kunde ikiwemo maharage ya soya, karanga na siyo hivyo tu, mboga mboga na hata mazao mengine ambayo yanakwenda sasa kuimarisha lishe ya Watanzania na hasa kwa kuzingatia kwamba kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika inaonesha bado Tanzania na hasa watoto na wanawake wanaojifungua wana utapiamlo. Kwa hiyo, kupitia bajeti hii pia inakwenda kuwakomboa wanawake na watoto kwa sababu imeondoa kero ambazo ni sumbufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya utangulizi huo nijielekeze katika mambo ambayo nimechagua kuyazungumzia ambayo ni machache kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimefurahishwa na kufutwa misamaha ya kodi ambayo haileti tija kwa wananchi na moja ya jambo hili ni kwenda kufuta misamaha ya kodi katika maduka ya majeshi na maduka mengine katika taasisi zetu za kijeshi. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hapa asituambie kwamba atakwenda kushauriana na viongozi wa wakuu wa majeshi, no! Namuomba na kumshauri aje kabisa na mpango mzima utakavyokuwa, kama inawekwa posho kwa ajili ya hawa askari wetu ijulikane, kama ni shilingi laki moja kwa mwezi ijulikane, ni shilingi laki moja na hamsini ijulikane. Maana akisema anakwenda kushauriana nao endapo watasema ni shilingi laki tatu ataipata kupitia bajeti ipi? Ina maana itakuwa ni mwaka mwingine wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hivyo kwa sababu askari wa nchi hii wamenituma, ma-CP, ma-WP ma-Constable huwa naongea nao sana, wanataka Serikali itoe kauli leo kwamba inakwenda kufanyaje sasa kwa sababu ushuru umeondolewa katika maduka yale ambayo yalikuwa ni msaada kwao. Serikali iweke kabisa fedha kama ni shilingi laki moja na hamsini kama ni shilingi laki tatu kwa kila mwezi ijulikane badala ya kwenda kufanya mazungumzo na viongozi wa jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nyingine ni suala zima la kupeleka fedha kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Naomba niungane na wenzangu wote walioiomba Serikali yetu Tukufu ambayo ni sikuvu kuongeza fedha, shilingi bilioni 47 kwa ajili ya CAG haitoshi! Kwa bahati njema katika Bunge hili umenipa fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC kwa muda mfupi tumekagua Halmashauri 30 hazikufanya vizuri, tumejionea madudu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za miradi ya maendeleo zinaliwa sana kwenye baadhi ya Halmashauri zetu lakini Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ndiye anayetuletea taarifa. Wenzangu wameshafanya uchambuzi sitapenda kurudia, ili TAKUKURU aweze kufanya kazi yake vizuri lazima na huyu CAG tumpe fedha ili ziende kutekeleza kazi ambayo tumekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliposikia kwamba CAG hana fedha baadhi ya Wakurugenzi wasio waaminifu wameanza kushangilia maana wanajua kuna baadhi ya madudu yanafanyika huko hawachukuliwi hatua yoyote, CAG peke yake ndiye atakayetukomboa. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu akae na timu yake tena, akaa na timu ya Mama Segasia na wenzake, wajaribu kuona ni wapi wanaweza wakapunguza fedha tukampa huyu CAG ili aweze kufanya kazi yake kikamilifu. Changamoto ya kukosa fedha tumeshaanza kuiona. Mimi niko kwenye Kamati ya LAAC, sasa hivi tunajiandaa kwenda Mikoani, tunajiandaa kuita Halmashauri, unamuona CAG anavyokuja anasuasua maana fedha anazopata hazitoshi. Kama hatumpi fedha za kutosha CAG, tutatenga fedha lakini zitaishia mikononi mwa wajanja kwa sababu watakwenda kufanya sivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie utaratibu wa upelekaji wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika Serikali yetu. Hapa naomba nianze kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imekuwa ikifanya. Tumejionea wenyewe imejenga miradi mikubwa sana ikiwemo jiji la Dar es Salaam na katika miji mingine saba hapa nchini na miradi ya mikakati katika nchi yetu na taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha imeeleza vizuri zaidi na hata taarifa ya Wizara ya Maji. Ombi langu kwa Serikali, kwa sababu zipo shilingi milioni 900 zimetengwa kwa ajili ya maji, tunaomba ule mfuko kwa ajili ya kupeleka maji vijijini uimarishwe, badala ya kutoza Sh.50 kwa kila lita ya mafuta ya diesel na lita 50 ya petrol iwe Sh.100. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu hali ya upatikanaji wa maji na hasa vijijini ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri sijui kama amepata fursa ya kwenda vijijini, mimi ninayezungumza ni mdau wa wanawake na nikienda vijijini sifanyi mikutano ya ndani naitisha mikutano ya hadhara. Hivi navyozungumza nimetoka site siongei mambo ya mezani. Napoitisha mikutano ya hadhara kuongea na wananchi ukiuliza kero ya kwanza kwa wananchi wote, wanawake, wanaume, vijana na watoto ni maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri hebu sasa huu Mfuko wa Maji akubali uongezwe tozo kutoka Sh.50 mpaka Sh.100 kwa kila lita ya diesel na lita ya petrol. Ushauri huu unakuja sasa mara ya pili, Wizara ya Fedha kuna kigugumizi gani cha kufanya uamuzi? Mnahofia kwamba eti mkipandisha hapa wananchi watapata matatizo, siyo sawa. Nawaomba sana mshughulikie suala hili kwani kero ya maji ndiyo changamoto ya kwanza. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama na kuweza kuchangia
katika hoja hii muhimu iliyo mbele yetu katika sekta hizi muhimu za miundombinu na nishati.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kukipongeza Chama cha
Mapinduzi kwa kutimiza miaka 40 kwa kuzaliwa kwake kwa mafanikio makubwa sana katika
kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo miundombinu ya barabara, reli, mawasiliano ya simu
na bandari na kadhalika. Maana ni ukweli usiopingika kwamba kabla ya miaka 40 ya Chama
cha Mapinduzi, hali yetu haikuwa namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukishukuru Chama cha
Mapinduzi na ninaomba kukitakia kila la heri katika miaka mingine 40, kiendelee kutekeleza Ilani
yake na miaka mingine 40 tuwe tumefika mbele zaidi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wote wa
Tanzania walioshiriki katika uchaguzi wa kata 19 katika chaguzi ndogo za Madiwani na uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Dimani ambako Chama cha Mapinduzi kiliibuka mshindi wa kishindo kwa
kupata kata 18 na Jimbo la Dimani Chama cha Mapinduzi kilipata 75%. Kipekee nichukue nafasi
hii kuwashukuru wananchi wa Tanzania na ninaomba niwaambie kwamba imani huzaa imani
na leo tunazungumzia suala la miundombinu ya barabara, tunazungumzia mawasiliano ya simu,
tunazungumzia suala la nishati vijijini, waendelee kuwa na imani na CCM, yote tuliyowaahidi
kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi tutayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya utangulizi huo naomba sasa nijielekeze
kwenye mambo machache niliyoyachagua kuyatilia mkazo. Jambo la kwanza naomba
niwakumbushe Wabunge kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya
miradi ya barabara, reli, nishati na kadhalika. Lakini kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa hali
inaonekana kwamba fedha hazipelekwi kwenye miradi kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kuishauri Serikali, kwa sababu
inabana matumizi katika kuendesha shughuli zake, inakusanya mapato, imebuni vyanzo vipya.
Ninachoiomba Serikali fedha hizo zilizotengwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ninaomba ipelekwe ili miradi iweze kutekelezwa kama ilivyokusudiwa kwa sababu, nimepitia
ripoti za Kamati mbalimbali zilizowasilishwa, Kamati ya Miundombinu kabisa inaonekana hata
30% bado hawajafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kutazama Kamati ya Nishati na Madini kiwango
kilichopelekwa ni zaidi ya 25% tu. Ninaiomba Serikali na kwa kweli na Waziri wa Fedha yuko
hapa, hebu tujipange vizuri kupeleka fedha za maendeleo katika miradi iliyokusudiwa kwa
sababu kama haikupelekwa fedha hata kama Mawaziri ni hodari namna gani, hata kama
watendaji ni hodari namna gani hatutafikia lengo lililokusudiwa.
Naomba Serikali ibuni mipango mipya ya kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo
zinapelekwa ili miradi yote iliyokusudiwa iweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kuna miradi mingi ya maendeleo ya
miundombinu ya barabara, miundombinu ya reli na miundombinu mingine, na hasa hapa
nizungumzie ya barabara. Kuna miradi mingi iliyoanzishwa mwaka 2010 haikukamilika, 2011
haikukamilika na sasa hivi tuko mwaka 2017 miradi ya baadhi ya barabara haijakamilika na
alipomalizia Mheshimiwa Mipata na hapa nitoe mifano ya barabara za Mkoa wa Mara.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafurahi sana Waziri wa Miundombinu juzi amekwenda na
amejionea mwenyewe zile barabara hali yake ilivyo, inasikitisha. Barabara ya kutoka Makutano,
Butiama kwa Baba wa Taifa, barabara ya kutoka Butiama kuelekea Mugumu mpaka Loliondo,
mpaka Mto wa Mbu, kwa kweli ni hatari. Ile barabara tangu imeanza kujengwa hakuna
kinachoendelea, Mheshimiwa Waziri amekwenda amejionea kuna wakandarasi wazalendo
zaidi ya 10 wanajenga ile barabara, mimi nimekata tamaa kwa sababu ninachokiona sasa hivi
ni kuchimba tu udongo wanaleta barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile ni barabara ya kihistoria, ni barabara aliyopita
Baba wa Taifa kudai uhuru wa nchi hii, ni barabara ambayo hatupaswi kupiga kelele namna
hiyo, Mwalimu Nyerere aliangalia Watanzania wote bila kujijali yeye mwenyewe, leo barabara
ya kutoka Butiama kuelekea nyumbani kwake, kwenda Mugumu, kwenda mpaka Loliondo,
kwenda mpaka Arusha ili kufungua barabara wananchi wa Mkoa wa Mara na hasa ukizingatia
kuna mbuga ya wanyama ya Serengeti, kuna ziwa, kuna uchumi uliotukuka, lakini barabara hii
kwa kweli sasa inatuchonganisha kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejaribu kuzungumza, wananchi wa Mkoa wa Mara wana
imani na CCM, wamechagua CCM, lakini barabara hii sasa inawafanya wanaanza kujenga
wasiwasi.
Ninaomba hatua zichukuliwe, kama Serikali imekuwa ikichukua hatua kwa makandarasi
wabovu, makandarasi ambao wako tayari naomba na hatua zinazostahili huyu mkandarasi
anayejenga hii barabara atazamwe upya, je, anao uwezo? Kwa sababu nimefuatilia fedha
ameshalipwa, ni kwa nini hajengi hii barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sio barabara hii peke yake, barabara zote za ule mkoa haziko
sawasawa. Barabara ya Kisorya - Bunda mpaka hapo Mugumu kupita Nyamuswa mpaka
Serengeti haiendelei! Barabara zote ambazo kwa kweli zimetengewa fedha na zilipitishwa
kuanzia mwaka 2010 hakuna kinachoendelea.
Naomba Serikali hebu ichukue hatua za haraka ili Mkoa wa Mara na wenyewe ufunguke
kwa sababu, ni mkoa wa kiuchumi. Na ukifunguka kuanzia kule Ukerewe mpaka Mara uchumi
wa samaki, uchumi wa madini, uchumi wa mbuga za wanyama na kadhalika. Hata Kaburi la
Baba wa Taifa ni uchumi, maana watalii wanakuja kuangalia kaburi, lakini hawana pa kupita
kwa ajili ya uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie suala zima la fedha za Mfuko wa
Barabara (Road Fund). Nimefuatilia kitabu hiki kunaelekea kuna tatizo, hizi fedha pia hazitoki.
Sasa ningependa tutakapokuwa tuna wind up, hebu Waziri atuambie tatizo ni nini? Maana hii
fedha iko kwenye ringfence, hazitakiwi zitoke. Kwa nini haiendi kuhudumia Mifuko ya Barabara
Vijijini, kumetokea kitu gani? Barabara hazipelekewi fedha, barabara zimeharibika tena ni za
vumbi zinazounganisha vijiji na vijiji, kata na kata, lakini hazijengwi kwa Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitoe ushauri, kwa sababu zimekuwa zikitengwa fedha
nyingi na Watanzania wanakatwa kodi kwa ajili ya kuimarisha hizi barabara za vijijini, barabara
zinajengwa na baada ya muda mfupi mvua ikinyesha barabara zinabomoka. Ushauri
ninaoutoa hebu tuangalie sasa mbinu mpya, badala ya kuwa tunajenga barabara za vumbi za
changarawe na kila baada ya mwaka barabara inaondoka na fedha inapotea hebu twende
na mpango mpya sasa wa kujenga hata lami kwa kilometa hata tano, tano. Tunajenga kitu
cha kudumu, kuliko mabilioni ya fedha yanateketea na baada ya muda barabara inaondoka,
halafu sasa tunatenga nyingine kila mwaka. Hebu naomba tubadilike tujaribu kutumia
wataalam wetu wa barabara, hebu watushauri at least tujenge kila kata kilometa tano, tano ili
tuweze kupata matokeo ya haraka na ya mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la upanuzi wa Bandari ya Dar
es Salaam. Nimefurahishwa na maoni ya Kamati yaliyo kwenye ukurasa wa 35 mpaka ukurasa
wa 40. Nayaunga mkono kabisa, na hapa naishauri Serikali na Mamlaka inayohusika, hebu
chukueni ushauri walioutoa Kamati ya Miundombinu muufanyie kazi. Ile gati ya kwanza mpaka
ya saba zipanuliwe, lakini na ile gati ya 13 na yenyewe ijengwe ili Dar es Salaam ipanuke na
meli ziweze kuja za mizigo, zinashusha mzigo kwa haraka na uchumi uweze kukua kwa haraka.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa nishauri, hebu tuangalie na Bandari ya Bagamoyo,
ilikuwa kwenye mpango mzuri na maendeleo yalishafikia hatua nzuri, lakini mimi sioni kama
inazungumzwa na sioni kinachoendelea. Bandari ya Bagamoyo ingejengwa kama ambavyo
tulikusudia na kama ambavyo tuliweka kwenye mpango, nina imani uchumi wa haraka katika
nchi yetu ungeweza kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nishauri tujenge na bandari ya Tanga kwa sababu,
Bandari ya Tanga itatuimarisha zaidi maana itawezesha nchi mbalimbali na ikiwemo na Bandari
ya Musoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote, aliyenipa fursa na mimi kuweza kusimama kutoa mchango wangu katika hoja yetu hii iliyo muhimu ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuunga mkono hoja na sababu ninazo. Sababu ya kwanza ni kwamba, tangu Serikali imeingia madarakani imefanya kazi kubwa sana yenye kutukuka. Kama kura zingepigwa leo, ushindi wa CCM ungekuwa 99.999%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kama tutamaliza miaka 10 na Rais huyu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, makofi tuliyompigia juzi Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Wabunge tutasimama juu ya meza kwa kazi anazozifanya. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana unayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mwaka mmoja Rais umethubutu kutununulia ndege. Ni Bunge hilihili na Wabunge hawahawa walikuwa wanasema na ndiyo maana mimi wakati mwingine huwa nashangaa watu wanakuwa na ndimi mbili; leo wanasema Tanzania haina ndege tunazidiwa na Rwanda, Rais ananunua ndege wanabeza. Waswahili wanasema akutukanaye hakuchagulii tusi na ukiwa kwenye maji unaoga akija mwendawazimu haumkimbizi. Mheshimiwa Rais chapa kazi, tuko pamoja, kazi ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Rais huyuhuyu Mheshimiwa Dkt. John Magufuli amefanya uamuzi wa busara akasema elimu iwe bila malipo kwa watoto wetu. Ni ukweli usiopingika watoto walioandikishwa wamevuka kiwango cha miaka yote iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Rais huyuhuyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, amethubutu. Kwa miaka mingi tangu nchi yetu imeanza, dhamira ya kuhamia Dodoma ilikuwepo, lakini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ndiyo ameweza.
Hongera sana Rais wetu, chapa kazi, panga Mji wetu wa Dodoma, maendeleo yaendelee na Watanzania wanakuthamini, endelea baba na usiwe na wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Rais wetu huyuhuyu aliyesikiliza kilio cha Wabunge cha muda mrefu kwamba, mapato mengi ya Tanzania yanapotea, akaziba mianya yote ya upotevu wa mapato. Si Rais mwingine ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Rais huyuhuyu ambaye Wabunge na wengine nawaona wako humu ndani, tulipaza sauti tukasema Rais apunguze safari za kwenda nje ya nchi. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amepunguza, Wabunge hatuendi nje ya nchi, Rais haendi nje ya nchi,
watumishi tuko humu ndani, gharama za kuendesha Serikali zimepungua. Ni Wabunge ndio tulioshauri ndio maana mimi wakati mwingine nashangaa kuona watu wenye ndimi mbili. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana unayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Rais huyuhuyu ambaye tulimtaka aangalie mishahara hewa. Amedhibiti na leo tunashuhudia jinsi anavyokabiliana na mishahara hewa, wakiwemo watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kueleza mafanikio ya Serikali hii ya Awamu ya Tano tutalala hapa. Kama tungeanza kuandika kitabu, Mheshimiwa Rais kwa mwaka huu mmoja ameshafanya mengi ambayo kwa kweli Watanzania na hasa wanawake ambao mimi nawawakilisha, zaidi ya milioni 50 wanawake walioko hapa wamenituma nije kusema wanamshukuru sana Rais, achape kazi na timu yake akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Mama Samia, kijana Mheshimiwa Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Jenista na Baraza lote la Mawaziri na Watendaji wote wa Serikali msirudi nyuma, songeni mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unabaki palepale ndiyo maana watu sasa wamekosa hoja, tunaanza sasa kuzungumza watu, hatuna cha kusema. Ndiyo maana kila mtu anayesimama anazungumza mtu badala ya kuzungumza maendeleo ya wananchi kwa sababu Mheshimwa Dkt. John Magufuli amefuta na hakuna mtu mwenye swali kwa Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapoona Wabunge sasa wanaacha kujadili matatizo ya wananchi, binafsi nafurahia kwamba Serikali sasa inasonga mbele, kero zimeisha na ndiyo maana tunaanza kuzungumza mtu mmoja mmoja badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu, nizungumze mambo machache ambayo nimejielekeza kuyachangia kama ifuatavyo.
Taarifa...
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa taarifa nzuri, ndege zinahitaji television. Si jambo baya, ndege zijazo tutakazozinunua miaka ijayo tutaweka television ili Wabunge mfurahie matunda yenu. Mheshimiwa Mwenyekiti, zile nyingine zinazokuja tutaweka television mtembee raha mustarehe kwa sababu Mheshimiwa Dkt. John Magufuli amedhamiria. Ahsante sana kwa taarifa nzuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ndio maana mimi nasema watu wenye ndimi mbili. Ni Mheshimiwa Kikwete huyuhuyu walisema alikuwa hafanyi kitu, leo hapa mtu anasema haya yalifanywa na Mheshimiwa Kikwete. Ahsante sana kwa kutambua kwamba na Mheshimiwa Kikwete alitoa hayo mawazo ya elimu bure. Ahsante Mheshimiwa Waitara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika mambo matatu ambayo nimeyapanga kuyatilia mkazo. La kwanza, nimejipanga kuelezea uwezeshaji wa wananchi na la pili, masuala ya maji, sekta ya afya na kama muda utaniruhusu nitazungumzia kidogo elimu na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 15 - 17 Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kwa kina jinsi ambavyo Serikali ya CCM ina dhamira nzuri sana ya kuwawezesha wananchi. Hapa naomba nishauri katika maeneo machache ambayo nimeyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika kuwawezesha uchumi wanawake na vijana. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali, nimejaribu kupekua kwenye hivi vitabu, sijaona ile milioni 50 katika kila kijiji. Ningependa kumwomba Waziri Mkuu, atakapokuja kusimama hapa mbele yetu hebu atuambie hii milioni 50 iko wapi? Maana Bunge lililopita tulipitisha zaidi ya bilioni 50 kwa ajili ya kupeleka kwenye vikundi vya wananchi vya kiuchumi. Napenda Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja hapa atuambie ziko wapi na zinatoka lini na utaratibu wa kutoa mikopo hii utakuwa ni nini na wanawake na vijana na wananchi kwa ujumla waweze kushiriki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimepekua katika vitabu vyote ambavyo tumepewa, sijaona ule Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Ni ukweli usiopingika kwamba wanawake ndiyo wazalishaji wa Taifa hili, ndiyo nguvu kazi, ndiyo wenye vikundi, ndiyo walezi wa familia, ndiyo
wajasiriamali, lakini kwa bahati mbaya sana ule mfuko ambao ulikuwa ndiyo ukombozi kwa wanawake siuoni katika vitabu hivi. Napenda kumwomba Waziri Mkuu atakapokuja atuambie hivi mpango ni nini katika suala zima la kuwakomboa wanawake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama mfuko haujawekwa, hatujachelewa. Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto itakuja. Turejee Mheshimiwa na Kamati ya Bajeti itusaidie fedha hizi ziingie kwa ajili ya wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni 5% ya Vijana na Wanawake inayotokana na Halmashauri zetu. Kwa bahati njema mimi niko kwenye Kamati ya LAAC, nimejionea kwamba Halmashauri nyingi hazitengi fedha. Nimefanya utafiti nimegundua kwamba hawatengi fedha kwa sababu, hakuna sheria. Wanatekeleza Waraka wa Waziri Mkuu tena wakati ule alikuwa Mheshimiwa Sumaye, ni muda mrefu sana. Naishauri Serikali, hebu ilete sheria hapa Bungeni tutunge sheria itakayoweka masharti ya kutenga fedha hizi kwa ajili ya halmashauri ziende kuwakomboa wanawake na vijana kwa sababu wameanzisha vikundi vingi sana, hawana uwezo wa kufikia vyombo vya fedha na huu mfuko peke yake ndiyo ukombozi kwa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masharti ya vyombo vya fedha. Kuna taasisi za FINCA, PRIDE na mabenki mengine wanatoa mikopo, tunawashukuru sana kwa kazi nzuri wanayofanya. Naiomba Serikali iweke riba elekezi kwa sababu baadhi ya taasisi zinatoza riba kuanzia 1% - 35%. Hawa wanawake na vijana wanashindwa kurudisha huo mkopo matokeo yake wananyang’anywa magodoro na vitu vyao vya ndani. Badala ya mkopo kumsaidia yeye unamsaidia yule aliyemkopesha fedha. Hebu Serikali chukueni ushauri wangu, wekeni riba elekezi ili wanawake na vijana waweze kunufaika. (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe na Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kunipa nafasi ya kusimama na kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu ya mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuipongeza Serikali ya CCM kwa kutimiza mwaka mmoja kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na Serikali kuhamia Dodoma. Naungana na mpango wa Serikali kuufanya Mji wa Dodoma kuwa mji
wa kisasa uliopangwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri iliyogusa nyanja zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimejielekeza katika kutoa mchango wangu katika mambo matatu yafuatayo:-
(i) Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi;
(ii) Maji; na
(iii) Afya, elimu na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa15 – 17 wa hotuba ya Waziri Mkuu taarifa inaonyesha jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuwezesha wananchi kupitia mipango na programu mbalimbali kwa kuwekeza nguvu zaidi kwa wanawake na vijana na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupongeza Serikali nina ushauri katika maeneo yafuatayo; wanawake ndio nguvu kazi, wanawake ndio walezi wa familia, unapomkomboa mwanamke kiuchumi unakomboa familia na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shilingi milioni 50 kwa kila kijiji; katika Mkutano wa Bajeti wa mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 Bunge lilipitisha fedha ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kupeleka shilingi milioni 50 kila kijiji katika baadhi ya mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni kiasi gani cha fedha kilitolewa na kilipelekwa katika mikoa ipi, na ni vikundi vingapi vilikopeshwa vikiwemo vya wanawake na Vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kujua ni kiasi gani cha fedha kimetengwa na ni mikoa gani na mingapi itapelekewa fedha hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ningependa kujua ni mamlaka gani imepewa jukumu la kusimamia mpango wa shilingi milioni 50 kila kijiji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kutoka Serikali Kuu umekuwa ni mkombozi. Kwa vipindi vya miaka ya hivi karibuni na hata bajeti ya mwaka 2017/2018 mfuko huu haukutengewa fedha, naishauri Serikali itenge na kutoa fedha kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya vikundi vya wanawake kama ilivyofanyika kwa vijana, kutotenga fedha kwa ajili ya wanawake ni kurudisha nyuma jitihada za wanawake katika kujikomboa kiuchumi kwa sababu mfuko huu unaotolewa na Wizara ulikuwa ni ukombozi kwa vikundi vya wanawake badala ya kutengewa asilimia 10 ya mfuko wa wanawake na Halmashauri tu ambao pia hakuna uhakika kwa sababu Halmashauri nyingi hazitengi na kutoa fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo katika Halmashauri kutotenga asilimia 10 kwa ajili ya mfuko wa vikundi vya maendeleo ya wanawake na vijana katika Halmashauri zetu. Naomba kutoa ushauri kwamba kwa kuwa utaratibu wa kutoa fedha hizo asilimia 10 ya vikundi vya wanawake na vijana ni maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu miaka zaidi ya 20 iliyopita, naishauri Serikali kuleta muswada ili Bunge litunge sheria itakayoweka utaratibu wa kutenga, kutoa na kurudisha fedha hizo kwa vikundi vya maendeleo ya wanawake na vijana kuliko ilivyo sasa, kwani jambo la kutoa fedha hizo limebaki kama ni jambo la hisani na si jambo la lazima kwa sababu hakuna sheria inayotekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila unapofanyika ukaguzi linatokea tatizo la kutotoa fedha vikundi vya wanawake na vijana na katika Halmashauri zilizo nyingi zimeonyesha yapo madeni makubwa. Hapa ningependa kusikia kauli yako Mheshimiwa Waziri Mkuu juu ya ulipaji wa madeni haya ili fedha hizi zielekezwe katika kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, riba katika taasisi zinazotoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wananchi; pamoja na kuzipongeza taasisi za fedha kwa kutoa mikopo midogo na mikubwa kwa vikundi vya wanawake na vijana. Lipo tatizo katika baadhi ya taasisi za fedha viwango vyao vya riba ni vikubwa sana mpaka kufikia asilimia 35 jambo ambalo husababisha wanawake na vijana kushindwa kujikomboa kiuchumi, badala yake wameambulia kufanya kazi za uzalishaji na kuwanufaisha waliowapa mikopo na wao kuambulia kutaifishiwa mali zao kwa mfano vifaa vya nyumbani kama vitanda, magodoro, vyombo na kuuziwa mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba naiomba Serikali itoe riba elekezi kwa taasisi zote zinazotoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana lengo likiwa ni wanawake na vijana wanufaike na mikopo hiyo kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake ilianzishwa kuwakomboa wanawake waishio vijijini na mijini ambao hawana fursa za kufika taasisi nyingine za fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, naomba Serikali itoe fedha kwa Benki hii ili ipate mtaji wa kufungua matawi katika mikoa yote hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake pia yaangaliwe upya kwa sababu masharti hayatofautiani na masharti ya benki zingine, hivyo wanawake walio wengi hasa waliolengwa na kuanzishwa kwa benki ni wanawake wanyonge ambao hawana mali za kuweka kama dhamana wanashindwa kukopa katika benki hii. Hivyo malengo ya kuanzishwa kwa benki hii bado hayajafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali irejee upya masharti ya kutoa na kurudisha mikopo ili benki hii ya wanawake iwe ni mkombozi kwa wanawake na Watanzania kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya maji, katika ukurasa 38 – 39 Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kwa kina jitihada zinazofanywa na Serikali za kujenga miundombinu ya maji. Naipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya kujenga miundombinu ya maji katika miji mbalimbali hapa nchini. Pia katika ukurasa wa 38 – 39 taarifa inaonyesha kuwa kufikia mwezi Julai na Desemba, 2016, miradi 90 ya miundombinu ya maji vijijini ilikamilika na kufanya mradi iliyokamilika kuwa 1,301 na kubakia miradi 509.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, suala la maji bado ni tatizo kubwa sana, wanawake bado wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji, wanawake bado wameshindwa kushiriki shughuli za kiuchumi kwa sababu wanatumia muda mrefu kwenda kutafuta maji, bado dhamira ya CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwatua wanawake ndoo kichwani bado haijafikiwa kiwango kizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yafuatayo:-
(a) Kutafuta fedha za kutosha hata kama ni kwa mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya maji hasa vijijini.
(b) Serikali na Bunge likubali kuongeza tozo ya mafuta ya petroli na dizeli kutoka shilingi 50 kila lita ya mafuta hadi shilingi 100 katika kila lita ya mafuta. Fedha zitakazopatikana zielekezwe katika ujenzi wa miundombinu ya maji hasa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo baadhi ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha za nje mfano, ujenzi wa mradi wa maji Mwanga, Same hadi Korogwe, ujenzi wa mradi wa maji Mgango, Kiabakari, Butiama, ningepeda kujua fedha za kutekeleza
miradi hii zimekwishapatikana na mradi wa Mwanga, Same na Korogwe upo katika hatua gani? Je, mradi wa Mgango, Kiabakari na Butiama unaanza lini? Kwa sababu mpango wa mradi huu ni wa muda mrefu sana. Mradi wa Muyayango, Sokoni Butiama ni miradi ya muda mrefu lakini mpaka sasa miradi hii ya Mgango, Kiabakari Butiama haijaanza na Mwanga, Same na Korogwe ni wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya katika ukurasa wa 39 Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kazi inayofanywa na Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata afya bora kwa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na kuimarisha huduma ya mama na mtoto ili
kupunguza vifo vya wanawake na watoto pamoja na kazi nzuri ya Serikali, naomba kuishauri Serikali kufanya yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuweka mikakati itakayopunguza vifo vya wanawake wanaofariki kwa kujifungua kwa mujibu wa utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa kila saa moja mwanamke mmoja anafariki kwa tatizo la kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi vituo vya afya ambavyo havijakamilika Serikali ijitahidi kukamilisha vituo vya afya vilivyojengwa ambavyo havijakamilika. Serikali ijitahidi kutafuta fedha na kukamilisha miundombinu ya vituo hivyo ili viweze kuanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vipya vya afya kila Kata; naishauri Serikali itafute fedha na kujenga vituo vya afya kila mwaka tuwe na vituo vya afya kila Halmashauri za Wilaya vinavyojengwa ikiwa ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu; naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya kutoa elimu isiyo na malipo pamoja na pongezi, nashauri Serikali kufanya yafuatayo:-
(i) Kuongeza madarasa katika kila shule ya msingi kwa sababu ongezeko la wanafunzi limeleta tatizo la ukosefu wa madarasa ya kutosha.
(ii) Ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari kwa sababu watoto wetu na hasa watoto wa kike wanapata adha kuishi mtaani, kutembea umbali mrefu jambo linasababisha pia mimba za utotoni.
(iii) Kuongeza nyumba za walimu na maslahi ya walimu.
(iv) Upungufu wa walimu wa sayansi, hapa ningependa kujua Serikali kwa sasa ina mkakati gani wa kuongeza walimu hao wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, nashauri Serikali iongeza wigo kwa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yanayozungukwa na maziwa na mito na maeneo yenye ukame ili kuongeza upatikanaji wa chakula kwa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na hizi dakika za Mgimwa najua utanipatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nikushukuru wewe na nimshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote aliyenipa nafasi ya kuweza kusimama na kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu ya Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuunga mkono hoja na sababu zangu ni mbili zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hotuba imeandaliwa vizuri sana, pili, dhamira ya Serikali chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na watendaji wote wa Serikali hasa katika sekta hii ya afya na maendeleo ya jamii kwa kweli wamejipanga. Wanaonesha kabisa dhamira nzuri ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora. Kwa msingi huo naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe ushauri kwamba kwa kuwa Wizara imejipanga vizuri na kwa sababu changamoto za Wizara ya Afya na changamoto za Wizara ya Maendeleo ya Jamii ni kubwa, nimefurahi leo nimemuona Waziri wa Fedha yupo hapa, ninaomba Serikali ipeleke fedha katika Wizara hii kwa sababu bila afya hakuna kilimo, uchumi wala chochote katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Fedha ijitahidi kupeleka fedha kwenye sekta ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, nimejaribu kupitia kitabu hiki kila kitu inaonekana kama taasisi hii hakuna kitu. Taasisi hii ni mtambuka; bila Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kweli hakuna chochote. Ninafurahi Waziri wa Fedha ananisikiliza na katika mwaka wa fedha ujao tunataka kuona sasa percent inaongezeka katika sekta hii ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali iboreshe maslahi ya wafanyakazi katika sekta hii. Wanafanya kazi ngumu sana ma-nurse wetu, madaktari na watumishi wetu katika huduma za maendeleo ya jamii, bibi na bwana maendeleo ya jamii, lakini kwa bahati mbaya ni kundi ambalo wakati mwingine linasahaulika.

Nimefurahishwa na hotuba ya Rais juzi wakati wa Mei Mosi kwamba anakwenda kuboreshwa maslahi ya wafanyakazi. Naomba sekta hii ya afya hebu angalieni ma- nurse wetu wanavyofanya kazi kwa tija, angalieni madaktari wetu wanafanya kazi usiku na mchana, wanafanya kazi saa za ziada, hawana kupumzika wala kuchoka lakini zile stahili na posho zao hawazipati kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali ipeleke vifaa tiba kama ambavyo imeanza kununua dawa, ipeleke vifaa tiba katika vituo vya afya na ipeleke wataalam wa kutosha na hasa kutokana na hili sekeseke lililotokea juzi, watalaam sasa wamepungua katika taasisi zile. Naomba Serikali iwe makini ihakikishe hakuna kituo kinachopungukiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwenye ujenzi wa vituo vya afya. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia wanawake wanafariki kwa kukosa huduma, watoto chini ya miaka mitano wanafariki. Ni ukweli usiopingika kwamba vituo vya ya ni vichache, tunaomba Serikali sasa ije na mkakati maalum na hapa naomba nitoe ushauri kwamba sasa Serikali kila Halmashauri tujenge kila mwaka vituo viwili, ukipiga mahesabu kwa Halmashauri tulizonazo 183, kama tutajenga vituo viwili, viwili kila mwaka na inawezekana, tutaweza kufika mbali; mara baada ya miaka mitatu tunaweza kuwa tumejenga vituo zaidi ya 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna vituo vya afya vipo ni maboma, vimejengwa hakuna mabaara, havijakamilika, nguvu za wananchi zimeishia pale. Ninaomba sana Wizara ya Fedha hebu tafuteni fedha zozote hata kama ni kwa mkopo, pelekeni ili hivi vituo vianze kwa sababu wananchi wamejikusanya wameishia pale kwa kushirikiana na Wabunge kupitia Mifuko ya Majimbo. Sasa Serikali ni jukumu lake kuhakikisha vituo hivi vinakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii pia iweke utaratibu wa kuhakikisha inaongeza fedha katika maeneo mbalimbali na hasa katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Mara. Ameongea Mheshimiwa Bonny Hospitali ya Rufaa ile ya Mkoa Mwalimu Nyerere Memorial Centre ni kituo ambacho kitakuwa ni ukombozi kwa watanzania na hasa wa Kanda ya Ziwa. Bugando sasa imeelemewa, tukipata kituo hiki na Serikali ikipeleka fedha za kutosha kila mwaka badala ya inavyofanya hivi sasa shilingi milioni 200 kila mwaka hakitakwisha leo.

Ninaomba Serikali ikiwezekana ipeleke hela kwa mkupuo shilingi bilioni 10 mwaka mwingine shilingi bilioni 10 ile hospitali ijengwe iwe ni ukombozi kwa hospitali za Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wanaofariki kabla ya kufikisha miaka mitano. Ninashukuru jitihada za Serikali vifo vimepungua. Kuna tatizo la watoto wanaozaliwa njiti. nimejaribu kupitia kwenye hotuba ya Waziri sikuona eneo hili. Katika vifo vya watoto wanaofariki chini ya umri wa miaka mitano miongoni mwao ni watoto wanaofariki wakiwa njiti ni asilimia 40 na ni sehemu ya pili ya watoto wanaofariki. Ukiangalia takwimu kila siku watoto 100 wanafariki na kila mwaka watoto 9,000...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama na kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto. Nianze kwa kuunga mkono hoja na sababu zangu za kuunga mkono hoja ni kama ifuatavyo:-

(i) Randama na hotuba ya Waziri imeandaliwa vizuri na kitaalam; na
(ii) Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara hii wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha wanaboresha huduma za afya hapa nchini. Ni ukweli usiopingika kuwa katika kipindi hiki kifupi, wameendelea kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya CCM ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi, kwanza napenda kushauri Serikali:-

(a) Itoe fedha za kutosha za utekelezaji wa majukumu ya sekta hii muhimu;

(b) Iboreshe maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya afya na maendeleo ya jamii na kuongeza idadi ya wafanyakazi;

(c) Iendelee kununua vifaa tiba katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa;

(d) Ipeleke wataalam kama vile Madaktari na Wauguzi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zote;

(e) Iandae mpango maalum utakaoleta matokeo ya haraka ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na ukamilishaji wa mpango wa hospitali za rufaa za kila mkoa, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za Muhimbili, KCMC na Bugando. Hapa naishauri Serikali kujenga vituo vya afya viwili viwili katika kila halmashauri, kwa halmashauri tulizonazo 183 x 2 x 3 = 1,098;

(f) Ikamilishe vituo vya afya vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi ili visaidie kutoa huduma badala ya kubaki kuwa magofu;

(g) Iongeze fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Mwalimu Nyerere Memory Center);

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kuongelea huduma ya afya ya uzazi na mtoto. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma inayotakiwa kwa wanawake kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na wiki sita baada ya kujifungua, naomba niungane na Serikali katika ukurasa wa 16 kuwa kweli bado ipo changamoto kubwa ya wanawake wanaofariki wakati wa uzazi. Kwa mujibu wa tafiti zilizopo hapa nchini ya mwaka 2015 zinaonesha kwamba vifo vinavyotokana na uzazi havijapungua, idadi ya vifo ni 556 kwa kila vizazi 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza mpango wa Wizara ulioandaliwa na unaotekelezwa kuanzia 2016 hadi 2020. Hapa napenda nipate muhtasari juu ya mpango huo, tangu mpango huo umeanza kutekelezwa tumeweza kuokoa vifo vingapi vya wanawake? Ni kwa nini vifo vimeongezeka badala ya kupungua? Takwimu za 2016/2017 zinaonesha hali ikoje juu ya vifo vya wanawake ikilinganishwa na ya mwaka 2015?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti). Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamaye 2017 kwa kushirikiana DFID, watoto 2,013 wanazaliwa kabla ya wakati na watoto 3,900 waliozaliwa bila kufikisha umri, wanafariki dunia. Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pia ni sababu ya watoto wanaofariki kabla ya kufikisha miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kunusuru maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati naishauri Serikali kufanya yafuatayo:-

(i) Tuwe na wodi/chumba maalum kwa ajili ya watoto hawa kwa sababu hali ilivyo sasa hakuna vyumba maalum katika baadhi ya vituo vya afya na hospitali zetu;

(ii) Kuwe na vitanda vya kutosha kwa ajili ya kuwalaza watoto hao;

(iii) Kuwe na mashine ya kusaidia watoto kupata joto ili kuwafanya waishi;

(iv) Kuwe na mashine za kuondolea ugonjwa wa manjano; na

(v) Elimu kwa jamii itolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ugonjwa wa saratani – shingo ya kizazi, matiti na tezi dume. Pamoja na kuishukuru Serikali kwa jitihada zake za kupambana na ugonjwa wa saratani kwa kuboresha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na hospitali za kanda ili ziweze kutoa huduma kwa wagonjwa wa saratani, bado ugonjwa wa saratani umekuwa ndio ugonjwa tishio kwa wanawake na wananchi wengine kwa ujumla. Kwa kuwa ugonjwa huu ni hatari na dawa za saratani ni ghali sana, naiomba Serikali itenge na kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba vya ugonjwa wa saratani. Pia naomba Serikali itoe msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wa saratani kama ilivyo kwa wagonjwa wa UKIMWI kwa sababu wanawake na wananchi wanaougua ugonjwa huu wa saratani hawana uwezo wa kumudu kununua dawa za ugonjwa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, dirisha la wazee, wanawake na wajawazito na watoto chini ya miaka mitano. Pamoja na kupongeza Serikali kwa kuweka na kuanzisha dirisha la wazee na wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, bado ipo changamoto kubwa ya utoaji huduma hii kwa wazee, wanawake wajawazito na watoto. Changamoto kubwa sana ya kundi hili ni dawa/ fedha zinazopelekwa hazitoshelezi. Nashauri, Serikali iwapatie huduma za bima ya afya wazee, wanawake na watoto. Pia iongeze fedha kwa ajili ya kuhudumia kundi hili na kuondoa adha wanayoipata kwa kukosa huduma ya afya kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Wanawake ndiyo nguvu kazi, wanawake ndiyo walezi wa familia, unapomkomboa mwanamke kiuchumi unakomboa familia kwa ujumla. Taarifa inaonesha jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuwezesha wanawake kupitia mipango na program mbalimbali kwa kuwekeza nguvu zaidi kwa wanawake na watu wenye ulemavu. Pamoja na kupongeza Serikali, nina ushauri katika maeneo yafuatayo:-

(i) Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kutoka Serikali Kuu. Mfuko huu umekuwa ni mkombozi. Kwa vipindi vya miaka ya hivi karibuni na hata bajeti ya mwaka 2017/ 2018, mfuko huu haukutengewa fedha. Naomba Serikali itenge na kutoa fedha kwa aili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kama ilivyofanyika kwa vijana. Kutotenga fedha kwa ajili ya wanawake ni kurudisha nyuma jitihada za wanawake katika kujikomboa kiuchumi kwa sababu mfuko huu unaotolewa na Wizara ulikuwa ni ukombozi kwa vikundi vya wanawake badala ya kutengewa 10% ya Mfuko wa Wanawake na Halmashauri tu ambao pia hakuna uhakika kwa sababu Halmashauri nyingi hazitengi na kutoa fedha hizo.

(ii) Tatizo la kutolipa 10% ya wanawake na vijana. Lipo tatizo katika Halmashauri kutotenga 10% kwa ajili ya mfuko wa vikundi vya maendeleo ya wanawake na vijana katika Halmashauri zetu. Naomba kutoa ushauri kwamba kwa kuwa utaratibu wa kutoa fedha hizo 10% ya vikundi vya wanawake na vijana ni maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu miaka zaidi ya 20 iliyopita, Serikali ilete Muswada ili Bunge litunge sheria itakayoweka utaratibu wa kutenga, kutoa na kurudisha fedha hizo kwa vikundi vya maendeleo ya wanawake na vijana kuliko ilivyo sasa, kwani jambo la kutoa fedha hizo limebaki kama ni jambo la hisani na si jambo la lazima kwa sababu hakuna sheria inayotekelezwa.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila unapofanyika ukaguzi linatokea tatizo la kutotoa fedha kwa vikundi vya wanawake na vijana, Halmashauri zilizo nyingi zimeonesha yapo madeni makubwa. Hapa ningependa kusikia kauli ya Serikali juu ya ulipaji wa madeni haya ili fedha hizi zielekezwe katika kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana.

(iii) Riba katika taasisi zinazotoa mikopo kwa vikundi vya wanawake. Pamoja na kuzipongeza taasisi za fedha kwa kutoa mikopo midogo na mikubwa kwa vikundi vya wanawake na vijana, lipo tatizo kwa baadhi ya taasisi za fedha viwango vyao vya riba ni vikubwa sana mpaka kufikia 35%. Jambo hili husababisha wanawake na vijana kushindwa kujikomboa kiuchumi badala yake wameambulia kufanya kazi za uzalishaji na kuwanufaisha waliowapa mikopo na wao kuambulia kutaifishiwa mali zao kwa mfano vifaa vya nyumbani kama vitanda, magodoro, vyombo na kuuziwa mashamba. Nashauri Serikali itoe riba elekezi kwa taasisi zote zinazotoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana lengo likiwa ni wanawake na vijana wanufaike na mikopo hiyo kuliko ilivyo sasa.

(iv) Benki ya Wanawake ilianzishwa kuwakomboa wanawake waishio vijijini na mijini ambao hawana fursa za kufika taasisi nyingine za fedha. Nashauri Serikali itoe fedha kwa benki hii ili ipate mtaji wa kufungua matawi katika mikoa yote hapa nchini. Vilevile masharti ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake yaangaliwe upya kwa sababu hayatofautiani na masharti ya benki zingine, hivyo wanawake walio wengi hasa waliolengwa na kuanzishwa kwa benki ni wanawake wanyonge ambao hawana mali za kuweka kama dhamana wanashindwa kukopa katika benki hii. Hivyo, malengo ya kuanzishwa kwa benki hii bado hayajafikiwa. Pia Serikali irejee upya masharti ya kutoa na kurudisha mikopo ili Benki hii ya Wanawake iwe mkombozi kwa wanawake na Watanzania kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.