Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amina Nassoro Makilagi (17 total)

MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali watu katika kukuza uchumi wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa rasilimali hiyo ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini, matumizi ya rasilimali watu ni muhimu sana. Ili kuhakikisha kuwa rasilimali watu inawezeshwa na kutumika kukuza uchumi wa Taifa, Serikali imeweka mikakati ifuatayo:-
(i) Serikali imeandaa mkakati wa Kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi (apprenticeship and internship programs). Aidha, ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo, Serikali imeanzisha program maaalum ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti. Utaratibu huu unawapa fursa vijana wetu na kuendelea na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi na hivyo kupata nafasi kuchangia katika kujenga uchumi wa Taifa.
(ii) Kuhamasisha vijana wenye utaalam mbalimbali kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususan kilimo na biashara. Aidha, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvu kazi nchini kuwa katika Sekta ya Viwanda ifikapo mwaka 2020, kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia sekta na taasisi zake mbalimbali inaendelea kuhakikisha rasilimali watu iliyopo nchini inatumika sawasawa ili iweze kuchangia uchumi wa nchi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Fedha za miradi ya maendeleo kutotolewa kwa wananchi kwa wakati jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara na miradi ya maendeleo kuchelewa kukamilika:-
Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Bunge lako Tukufu linavyofahamu, muundo wa bajeti yetu unavyopitishwa na Bunge, una vyanzo viwili vya mapato; mapato ya ndani na mapato kutoka nje. Wakati wa utekelezaji wa bajeti, kiwango cha mgao hutegemea zaidi mapato halisi kutoka vyanzo vyote viwili. Hivyo basi, mapato pungufu au chini ya malengo kutoka kwenye chanzo chochote kati ya hivyo vilivyotajwa, yataathiri mgao wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia pekee na muafaka ya kukabiliana na changamoto hiyo ni Serikali kuongeza mapato yake kutoka vyanzo vya ndani. Hatua kadhaa za kuongeza mapato ya ndani tayari zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na kubana na kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kuwa kila anayestahili kulipa kodi, analipa kodi stahiki na kupanua wigo wa kodi kwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuweka mazingira rafiki au wezeshi kwa mlipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la hatua hizi ni kuongeza mapato ya Serikali na hatimaye kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ambayo inaambatana na masharti kadhaa, baadhi yake yakileta usumbufu na hasara kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wanatambua hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli katika kudhibiti suala la kukwepa kodi na kuongeza mapato ya Serikali. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali yetu.
MHE. AMINA NASSORO MAKILAGI aliuliza:-
(a) Je, Viwanda vinavyozalisha nguo aina ya khanga vipimio vyake na ubora wake vinafaa kwa matumizi ya wanawake wa Kitanzania?
(b) Je, upande wa khanga kwa kila kiwanda ni mita ngapi?
(c) Je, malighafi gani inayotumiwa kuzalisha khanga kati ya pamba, uzi wa katani, uzi wa nailoni, au uzi wa sufi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vipimo vya ubora wa khanga zinazozalishwa na viwanda hapa nchini, vinafaa sana kwa matumizi ya wanawake hapa Tanzania. Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia shirika la viwango Tanzania (TBS) limetoa viwango elekezi vya uzalishaji wa khanga kwa kutumia pamoja na nyombo vingine ni 16165 ya 2009. Viwango hivi vimezingatia mahitaji ya watumiaji na matakwa ya wataalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa khanga kwa kila kipande unatofautiana kutoka kiwanda kimoja hadi kingine.
Aidha, kiwango cha centimeter 165 cha 2009 kinaelekeza upande wa khanga uwe wa kipimo kisichopungua urefu wa centimeter 165 na upana wa centimeter 116. Hata hivyo, kila kiwanda kinachozalisha khanga kinapaswa kuzingatia vipimo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, khanga husokotwa kwa kutumia malighafi za nyuzi pamoja na pamba. Hata hivyo, katika umaliziaji wa kipande hicho hutengenezwa kwa kutumia asilimia 100 lakini polyester kwa asilimia 100 au mchanganyiko wa pamba pamoja na polyester.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Zao la mwani limekuwa ni ukombozi kwa vikundi vya akina mama katika mwambao wa Pwani:-
(a) Ni lini Serikali itavipatia mtaji vikundi vya wanawake wa kilimo cha mwani ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 12,000 hadi 20,000 kwa mwaka?
(b) Ni lini Serikali itawapatia nyenzo na utaalam ili vikundi vya wanawake na vijana viweze kuzalisha chaza, walulu, kaa, kamba na pweza?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijajibu swali, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa imani yao kwangu katika kuniteua kuongoza Wizara hii nyeti ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, sasa basi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba zao la mwani limekuwa chanzo cha mapato kwa akina mama wanaoishi katika Ukanda wa Pwani lakini hata hivyo kuna changamoto za upatikanaji wa mitaji na nyenzo za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imehamasisha wakulima wa mwani zaidi ya 3,000 kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka kwenye taasisi za kifedha, kama vile Benki ya Kilimo. Vikundi vilivyopo hivi sasa ni Msichoke kilichoko Bagamoyo, Maliwazano na Kijiru vilivyoko Mkinga, Jibondo kilichoko Mafia, Mikocheni, Ushongo na Mkwaja vilivyoko Pangani, Naumbu na Mkungu vilivyoko Mtwara Mjini. Vilevile Umoja wa Wakulima wa Mwani umeanzishwa mwaka 2013 ili uweze kuwa kiunganishi kati ya taasisi za kifedha na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na kuvisajili. Aidha, Serikali itawezesha wakulima zaidi ya 1,200 kwa kuwapatia mtaji kwa njia ya VICOBA kupitia mradi wa SWIOFish unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kuongeza uzalishaji.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwapatia elimu, nyenzo na utaalam wazalishaji wa lulu, kaa na kamba mti kupitia mradi wa Marine and Coastal Environment Management Project ulioisha mwaka 2012. Vikundi vifuatavyo vimewezeshwa na mradi huo:-
(i) Vikundi vya ulimaji wa mwani cha Msichoke kilichoko Bagamoyo, Maliwazano na Kijiru vya Mkinga, Mikocheni, Ushonga na Mkwaja vya Pangani, Jibondo kilichoko Mafia;
(ii) Vikundi vya unenepeshaji wa kaa vya Nyamisati - Rufiji, Kipumbwi -Pangani;
(iii) Vikundi vya utengenezaji wa lulu vya Akili Kichwa kilichoko Mtwara Mjini;
(iv) Vikundi vya ufugaji samaki aina ya mwatiko ni Naumbu na Mkungu vilivyoko Mtwara Vijijini na Tangazo - Mtwara Vijijini; na
(v) Vikundi vya ufugaji wa kambamti ni Mpafu - Mkuranga na Machui - Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itaendelea kutoa elimu na ruzuku kwa wakuzaji wa viumbe kwenye maji kwa kupitia bajeti ya Serikali na mradi wa SWIOFish na hivyo kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Masuala ya watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa yanazungumzwa na kushughulikiwa katika maeneo ya mijini na kusahau maeneo ya pembezoni ambapo kuna watu wa jamii hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani kuhusu watu wenye ulemavu waishio vijijini ambapo matatizo yao ni mengi na makubwa kulingana na jamii inayowazunguka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu waishio vijijini. Ili kuwa na mipango mahsusi ya kushughulikia kundi la watu wenye ulemavu vijijini Serikali imefanya ugatuaji wa shughuli zinazohusu watu wenye ulemavu kwenda katika Serikali za Mitaa. Serikali inaendelea kuzijengea uwezo wa Halmashauri na watoa huduma wengine ili kutatua kero zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 mwaka 2010 imeelekeza kuanzisha Kamati za Baraza la Huduma na Ushauri kwa watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa hadi ngazi ya Taifa ambazo zitasaidia utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu. Katika kusimamia utekelezaji wa matakwa ya sheria hii Serikali imewaagiza Makatibu Tawala wote wa Mikoa kusimamia uanzishwaji wa Kamati za Mikoa, Halmashauri Kata na Vijiji, kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu maana ndiko watu wenye ulemavu wengi waliko.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Sheria ya Ndoa imekuwa kandamizi kwa wanawake na watoto:-
Je, ni lini sheria hii italetwa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi kupitia Waraka wa Serikali namba moja wa mwaka 1969. Lengo la mjadala huo lilikuwa kupata muafaka kuhusu maudhui ya sheria hiyo ambayo yaligusa imani, mila na desturi za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya miaka zaidi ya 20 kupita tangu sheria hiyo ya ndoa itungwe, Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria iliifanyia mapitio ya sheria hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Kutokana na maoni hayo ya Tume, Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliandaa mwaka 2008 Waraka wa Baraza la Mawaziri uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Kwa kuzingatia chimbuko la sheria hiyo, Baraza liliiagiza Wizara kuandaa Waraka Maalum wa Serikali (White Paper) ili kupata mjadala mpana na shirikishi kama ilivyokuwa awali. Mapema mwaka 2010 Wizara ilikamilisha maandalizi ya waraka huo ambao pamoja na kubainisha hoja ambazo wananchi wangetakiwa kuzitolea maoni uliainisha utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Desemba, 2010 kabla waraka huo haujajadiliwa na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukaanza na kulilazimu Baraza kusitisha kwa muda mchakato wa marekebisho ya ndoa. Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, wananchi wangetoa maoni kuhusu Sheria ya Ndoa, Mirathi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake, ilibainika kwamba wananchi wengi hawakujielekeza kwenye maudhui ya Sheria ya Ndoa, hivyo Wizara ya Katiba na Sheria ikaamua kuendeleza juhudi za awali kwa kukamilisha taratibu za kupata maoni ya wananchi kwa utaratibu wa White Paper, zoezi hili litakamilika ndani ya muda si mrefu.
MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kupima ardhi yote ya Tanzania na kuipangia matumizi yaliyo bora kufuatia kuwepo kwa tatizo kubwa la migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na Mamlaka ya Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuondoa migogoro ya ardhi kote nchini na ili kufikia azma hiyo, Serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa programu
hii, kila kipande cha ardhi nchini kitapangiwa matumizi na kupimwa, hali ambayo itaondoa mwingiliano baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi na hivyo kupunguza uwezekano wa kuibuka kwa migogoro ya ardhi. Mpango huu utasaidia ardhi yote kutunzwa na watumiaji husika na kuhifadhi maliasili zilizopo katika mazingira kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, pia jamii inayozunguka maeneo
hayo yaliyohifadhiwa itawezeshwa kutambua mipaka yao na kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi na kudhibiti uvamizi wa maeneo ya hifadhi. Aidha, utekelezaji wa programu hii utajenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda ardhi inayomilikiwa dhidi ya uvamizi wowote, kuwezesha kukabliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha makazi ya wananchi na kuleta usalama na ustawi wa maliasili za Taifa.
Mheshimiwa Spika, programu ya kupanga, kupima
na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini itahusisha Halmashauri zote 181 nchini na imepangwa kufanyika katika kipindi cha miaka kumi kwa awamu ya miaka mitano kwa kila awamu kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Aidha, programu hii itakuwa na miradi mikubwa miwili ambayo ni miradi ya upimaji wa kila kipande cha ardhi vijijini na mradi wa upimaji wa kila kipande cha ardhi mijini.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa programu hii kwa awamu ya kwanza, umeanza kupitia Mradi wa Land Tenure Support Program ambao unatekelezwa katika Wilaya tatu za mfano katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo hadi sasa jumla ya mipaka ya vijiji 50 imeshapimwa na kazi ya uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, upimaji wa vipande vya ardhi na utoaji wa hatimiliki za kimila, unaendelea.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) Aliuliza:-
Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika Kata za Etaro, Ifulifu, Nyegina na Nyakatende wanakabiliwa na taizo la maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa kata hizo maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Amina Makilagi naomba kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyoionyesha kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika Kata za Itaro, Ifulifu, Nyegina na Nyakatende wanakabiliwa na tatizo la maji kwa sababu mahitaji halisi ya maji katika kata hizo ni lita 953,550 wakati uzalishaji wa maji katika vyanzo vilivyopo ambavyo ni visima sita katika Vijiji vya Keimba na Kabegi kwenye Kata ya Ifulifu, Kijiji cha Mkikira katika Kata ya Nyegina na Vijiji vya Kigera, Nyegina na Kamguruki katika Kata ya Nyakatende vinazalisha lita 5,100 kwa siku pamoja na mradi wa maji ya bomba katika Kata ya Nyegina unazalisha lita 50,000 kwa siku na hivyo kufanya jumla ya lita zinazozalishwa kwa sasa kuwa 55,100 tu ambazo ni asilimia sita ya mahitaji.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuboresha huduma za maji kwenye eneo hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia wakazi wa Manispaa ya Musoma pamoja na wakati wa Kata za Nyamkanga, Bukabwa na Busimwa katika halmashauri ya Wilaya ya Butiama na wakazi kwenye Kata za Etaro, Nyegina na Nyakatende katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Hadi sasa Serikali imeshapeleka shilingi milioni 900 kwenye Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma, ambayo inasimamia utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, kazi ambazo zimeshatekelezwa hadi sasa ni kupima njia ya bomba, kuchonga barabara kuelekea Mlima Balima kutakakojengwa tenki lenye ujazo wa lita milioni mbili ambalo litasambaza maji kwa mtiririko kupeleka huduma za maji safi na salama katika kata nilizotaja. Aidha, taratibu za ununuzi wa mabomba yenye urefu wa kilometa 35 zimekamilika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, nini mipango ya Serikali ya kumaliza tatizo kubwa la nyumba za askari hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna tatizo kubwa sana la nyumba za Askari za kuishi. Kwa kufahamu hilo Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya ujenzi wa makazi ya Askari kwa awamu kulingana na uwezo uliopo. Aidha pamoja na kutenga fedha hizo Wizara yangu itajielekeza zaidi kutumia rasilimali zilizopo na teknolojia rahisi ya ujenzi wa nyumba ili kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ubia baina ya Serikali na sekta binafsi Jeshi la Polisi limefanikiwa kujenga nyumba 353 Kunduchi na Mikocheni, Dar es Salaam kwa ajili ya askari wa kawaida na maafisa. Aidha, Jeshi la Magereza linaendelea na ujenzi wa nyumba 320 Ukonga, Dar es Salaam kwa fedha za Serikali na lipo katika mazungumzo ya ubia na Shirika la Nyumba la Taifa utakaowawezesha kujenga nyumba 100 Msalato, Dodoma. Kadhalika, Idara ya Uhamiaji inafanya makubaliano na Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya ununuzi wa nyumba 103 Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la kuhamia Dodoma. Utaratibu huu utaendelezwa katika Mikoa mingine ili kupunguza changamoto hii kwa Askari wetu. (Makofi)
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Zipo sheria nyingi ambazo zimepitwa na wakati na sheria nyingine ni kikwazo katika kufanikisha shughuli muhimu za Taifa letu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzitambua sheria zote zilizopitwa na wakati na zile zinazochelewesha ukuaji wa uchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakati wote imekuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinapitiwa na kufanyiwa marekebisho kadri inavyohitajika ili kukidhi mahitaji. Mkakati huo unasimamiwa na Wizara kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171. Tume hii ni chombo mahsusi cha Serikali chenye kazi ya kusimamia mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1983, Tume ya Kurekebisha Sheria imefanikiwa kuandaa ripoti 37 za mapitio na marekebisho ya sheria mbalimbali na kuziwasilisha Serikalini ambapo baadhi yake zilishatungiwa sheria na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya mapitio ya sheria ili kubaini sheria zilizopitwa na wakati na hatimaye kupendekeza marekebisho, kutunga sheria mpya au kufutwa kwa sheria ni endelevu na imekuwa ikifanyika muda wote ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Wavuvi wadogowadogo hawana teknolojia rafiki inayowawezesha kuvua kwenye maeneo yenye samaki wengi:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha maeneo ya uvuvi kwa kutumia teknolojia rafiki kuweka vifaa vya kuvulia samaki (Fish Aggregating Devices) ili kuongeza upatikanaji wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imeandaa programu ya kuweka vifaa maalum vya kuvutia samaki (Fish Aggregating Devices – FADs) kwenye bahari kwa kushirikiana na wavuvi. Kwa kuanzia programu hii inatekelezwa katika Wilaya ya Bagamoyo kwa upande wa Tanzania Bara na Nungwi, Tanzania Visiwani, ambapo vikundi viwili vya wavuvi kila upande vinafundishwa jinsi ya kutengeneza FADs na kuziweka baharini ili kuwasaidia wavuvi kupata samaki wengi na kutumia muda mfupi katika kuvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu inafadhili programu hii ambapo jumla ya FADs 70 zimekwishatengenezwa na kuwekwa baharini katika maeneo ya Bagamoyo, Mafia na Visiwa vya Unguja na Pemba. Vilevile, wavuvi wameweka FADs za asili ambazo hutengenezwa kwa kutumia magogo ya minazi na magari chakavu katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Aidha, Serikali inaandaa mpango wa kufuatilia upatikanaji wa samaki baada ya FADs hizo kuwekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itahakikisha programu hii inafanikiwa na teknolojia hii inasambazwa katika maeneo mengine ili wavuvi waweze kufaidika.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka sheria kali zitakazowabana wazazi ambao wamekuwa wakitelekeza watoto na familia zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto ni haki ya mtoto kwa mujibu wa Sheria Na. 21 ya mwaka 2009. Aidha, kifungu cha 7 mpaka cha 9 kinatoa majukumu kwa mzazi/mlezi na mtu yeyote mwenye jukumu la kumlea mtoto kuhakikisha kwamba anawatunza na kuwalea watoto ikiwemo kuwapatia huduma zote muhimu kama chakula, malazi, mavazi, elimu na kuwalinda na vitendo vya nyanyasaji, ukatili, unyonyaji na utelekezaji. Kifungu cha 14 cha Sheria ya Mtoto kinatoa adhabu kwa mzazi/mlezi yeyote atakayekiuka kifungu hiki atatozwa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya mashauri 6,557 yanayohusu matunzo na malezi ya watoto na wanawake yalishughulikiwa katika ngazi mbalimbali za Halmashauri na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wazazi/ walezi na wote wenye jukumu la kutoa malezi na matunzo kwa watoto wahakikishe wanatimiza wajibu wao kikamilifu. Vilevile familia zote ambazo zimetelekezwa zitoe taarifa katika Ofisi za Ustawi wa Jamii zilizoko katika Halmashauri wanapoishi ili mashauri yao yaweze kusikilizwa na watoto kupata huduma stahiki kwa ajili ya makuzi yao.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote za Serikali kuhakikisha kuwa wanashughulikia kwa haraka mashauri yanayowasilishwa kwenye ofisi zao kwa kutumia sheria na taratibu zilizopo.
MHE. AMINA N. MAKILLAGI aliuliza:-

Tatizo la maji linaendelea kuwa kubwa siku hadi siku katika maeneo mbalimbali:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya majisafi na salama vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha inayokabili ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia programme ya maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili iliyoanza mwezi Julai, 2016, imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kutenga na kutoa fedha za kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo ya maji Vijijini, Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji midogo pamoja na Miji na Vijiji vinavyohudumiwa na miradi ya maji ya Kitaifa. Lengo ni kufikia asilimia 85 ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama katika maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maji mijini ifikapo 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha fedha za ndani zinapatikana za kutosha na kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji ambao umekuwa chanzo cha uhakika wa fedha kwa ajili ya miradi ya maji hususan vijijini. Kutokana na jitihada hizo za kutafuta fedha za miundombinu ya maji, hadi sasa huduma ya maji vijijini imefikia asilimia 64.8 na kwa upande wa mijini imefikia asilimia 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha miundombinu ya maji inajengwa katika maeneo mbalimbali na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI Aliuliza:-

Baadhi ya watu katika jamii bado wanaendeleza vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwadhulumu wanawake:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza kabisa vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua ukatili wa kijinsia ni pamoja na vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwadhulumu wanawake na watoto. Aidha ukatili wa kingono na kisaikolojia ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali za kuzuia na kutokomeza ukatili huo. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kuandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha mwaka 2021/2022. Mpango huo unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000; Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia wa mwaka 2005; na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008. Kutokana na utekelezaji wa mpango huu, hadi kufikia 2018, jumla za Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto 10,988 zimeanzishwa katika ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa. Kamati hizi zina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa mpango kazi katika ngazi husika.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Jeshi la Polisi 420 kwa kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia. Aidha, Serikali imeanzisha huduma za One Stop Center kwenye Mikoa saba ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Shinyanga, Pwani, Iringa Mbeya na Mwanza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imewezesha kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Namba 1 ya mwaka 2017. Sheria hii inatoa fursa kwa wanawake waliofanyiwa unyanyasaji au kudhulumiwa kupata haki zao kupitia vyombo vya usimamizi wa sheria pasipo kujali uwezo wao wa kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa elimu kwa jamii. Mfano katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara imetoa elimu ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kwa Wahariri na Waandishi wa Habari ili waweze kuelimisha jamii kuhusu suala hili pamoja na kufichua matukio ya ukatili wa kijinsia. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali imeratibu midahalo kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na kuwasilisha wasanii katika kampeni za kutokomeza ukatili huo.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya cha Kiagata kwani Wananchi wote wa Wilaya ya Butiama wanategemea Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA Z A MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyeiti, katika mwaka wa fedha 2017/2028 Serikali iliidhinisha na kutoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha miundmbinu ya Kituo cha Afya cha Kiagati. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya mtumishi, wodi ya wazazi, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la kuhifadhia maiti na kichomea taka. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kupitia mapato yake ya ndani imetumia kiasi cha shilingi milioni 37.5 kwaajili ya kukamilisha miundombinu iliyosalia pamnoja na kununua Jokofu la kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, KItuo hicho cha afya kwa sasa kinatoa huduma za upasuaji wa dharura, huduma za ultrasound, huduma za Mama na Mtoto na kulaza wagonjwa.
MHE. AMINA N. MAKILAGI Aliuliza:-

Vyama vya Ushirika ndio mkombozi wa wakulima na wafugaji.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha vyama hivyo vinaimarika na kuleta tija kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 22 kifungu (f), (g) na (h) kuwa ushirika ndiyo suluhu pekee inayoweza kumkwamua mkulima mdogo kupitia kuungana na kutengeneza chombo imara cha kuwatetea.

Aidha, Wizara inatambua mapungufu yaliyomo sasa katika mfumo wa vyama vya ushirika wa mazao mbalimbali ikiwemo pamba, kahawa, miwa, ufuta ambapo baadhi ya viongozi ambao sio waaminifu wamekuwa wakifanya vitendo visivyofaa ikiwemo ubadhirifu wa rasilimali za ushirika, hali iliyopelekea ushirika kutoaminika miongoni mwa wanachama walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Tume imeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji katika Vyama vya Ushirika kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara mara mbili kwa mwaka na kaguzi za mwisho wa mwaka, kusimamia chaguzi za viongozi na mikutano mikuu ya vyama vya ushirika na kufuatilia utekelezaji wa hoja zinazotokana na matokeo ya ukaguzi na uchunguzi. Aidha, Wizara inafanya tathmini kupitia mfumo mzima wa ushirika kwa kuangalia muundo wake, uendeshaji, usimamizi wa rasilimali zake na fedha za wanachama ili kuleta tija na kufanya uwe wa kibiashara zaidi kuliko udalali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine ni pamoja na kuhamasisha wadau mbalimbali hususan vijana, wanawake na vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika kujiunga au kuanzisha vyama vya ushirika ili kuongeza idadi ya wanachama, kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo yaani SACCOS kwenye vyama vya ushirika vya kilimo na masoko yaani AMCOS ili kuwajengea wakulima tabia ya kuweka akiba na kupata mikopo yenye masharti nafuu. Aidha, Wizara kwa sasa inahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, kuandaa mkakati wa utekelezaji pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Sheria ya Ukaguzi ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 1985 ili kuongeza ufanisi katika ushirika. (Makofi)
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-

Wanawake 24 hufariki kila siku wakati wa kujifungua nchini:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru vifo vya Wanawake wakati wa kujifungua?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (k.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Takwimu ya Taifa ya Mwaka 2015 zinaonyesha vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Hii ni sawa na vifo 32 kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kupunguza vifo hivi ikiwa ni pamoja na:-

(i) Kuboresha Vituo vya Afya kwa ajili ya kutoa huduma muhimu sa dharura kwa matatizo yatokanayo na uzazi na watoto wachanga. Pia kuendelea kuvipatia vituo vya kutolea huduma za afya vifaa tiba na vitendeakazi kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya uzazi.

(ii) Kutoa mafunzo mbalimbali ya huduma muhimu za dhahrura kwa matatizo yatokanayo na uzazi na watoto wachanga kwa watoa huduma za afya ili waweze kutoa huduma zenye viwango kwa jamii. Aidha, mafunzo haya pia hutolewa kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kama njia ya kushirikisha jamii ili waweze kusaidia katika kupunguza vifo hivyo.

(iii) Kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa ajili ya uzazi salama ikiwemo dawa ya oxytocin kwa ajili ya kuzuia mama mjamzito kutokwa na damu nyingi wakati na baada ya kujifungua na dawa ya magnesium sulphate kwa ajili ya kuzuia kifafa cha mimba.

(iv) Kuimarisha huduma za rufaa kwa kuzambaza magari ya kubebea wagonjwa. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016 magari 67 yalitolewa kwa Halmashauri mbalimbali ili kusaidia kuimarisha huduma hizi.

(v) Wizara ilitoa mafunzo elekezi nchi nzima kwa watoa huduma wa afya ngazi za Mkoa na Halmashauri kuhusu upitiaji na utoaji wa taarifa za vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga ili kutambua tatizo lililotokea na kuweka mikakati ya kuzuia vifo hivyo visitokee tena.

(vi) Kushirikisha jamii kutambua kuwa inayo wajibu wa kutengeneza mikakati na Kanuni zitakazowawezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga katika jamii husika.