Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amina Nassoro Makilagi (8 total)

MHE. AMINA NASSORO MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa khanga hii ni vazi ambalo mwanamke wa Kitanzania analivaa akiwa nyumbani, ni vazi ambalo analivaa akiwa shambani analima, ni vazi ambalo analivaa anapokuwa kwenye shughuli za kijamii kwenye misiba na kwenye shughuli za harusi, ni vazi ambalo mama anakuwa nalo hata anapokwenda leba. Ni vazi ambalo linampokea mtoto hata anapotoka leba. Ni vazi rasmi la Mwanamke wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kanga ambazo zinatengenezwa katika viwanda vyetu vya Tanzania kwa kiwango kikubwa hazikidhi mahitaji ya wanawake wa Tanzania na hasa kwa kuzingatia kwamba vipimo vinavyotumika na ukilinganisha upana na viwango walivyonavyo wanawake wa Tanzania. Wanawake wa Tanzania wanaishi kwa amani na utulivu wako sawa katika afya zao, kanga wanazozivaa haziwatoshi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna baadhi ya viwanda hata hizi sentimita zilizozungumzwa hawafikii; unakuta urefu ni wa mita 100, sentimita 120 kwa kweli ukiangalia hata wewe mwenyewe haikutoshi hata kwa urefu peke yake. (Kicheko/Makofi)
Sasa swali langu la kwanza, kwa kuwa vazi hili kwa kweli ni vazi la mwanamke wa Kitanzania. Matokeo yake wanawake wameanza kuvaa kanga zinazotoka India na China, wanawake sasa wamehamia kwenye madera, jambo ambalo kwa kweli hawakuzoea, ningependa kujua sasa Serikali inamkakati gani wa kuhakikisha inaielekeza TBS (Shirika la Viwango Tanzania) ili kufuatilia vazi hili, liendane na ubora halisi wa maumbo ya wanawake wa Kitanzania na hasa kwa kuzingatia kwamba kanga hii hata ukiivaa inateleza haifungiki sasa hivi; kwa hiyo hata malighafi wanayoitumia siyo pamba. (Makofi)
Swali la pili, ningependa kujua sasa kwa sababu hili vazi la kanga limekuwa ni dogo, na wanawake wameamua kuachana nalo kwa kuwa na India. Ningependa sasa kujua Serikali ina mkakati gani kwa sababu sasa vazi la dera limekuwa likiwapendeza wakina mama na ni vazi la heshima, ina mkakati gani sasa la kuhamasisha viwanda vya hapa nchini vitengeneze dera badala ya kuwanufaisha mataifa ya mbali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amina Makilagi, Mbunge maalum na machachari kwa akina mama kama ifuatavyo:- (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kama Serikali ni kweli, kwanza nitambue viwanda tulivyonavyo hapa nchini vingi kabisa tulivirithi toka ukoloni na vichache tulivijenga miaka ya 1970 na vingine miaka ya 1980. Viwanda ambavyo tunavyovitambua kama Mwatex, Murutex, Urafiki, ni vya Nida ndiyo vimeongezeka hivi karibuni. Kwa hiyo ni kweli kabisa viwango vyake ni vya chini na hiyo ninakubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua ambazo Serikali imechukua sasa kwa kutambua mabadiliko ya maendeleo siyo mabadiliko ya uchumi tu hata makuzi ya binadamu. Kwa hiyo ninatambua size za kina mama na hata akina baba, akina baba na nyie mko wapi? Na zenyewe zinakuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kwanza ambayo Serikali imechukua viwango vilivyowekwa na TBS vinavyotumika sasa kwa upande wa nguo za kanga kama nilivyosema ni urefu wa sentimita 165 na upana sentimita 116. Lakini kwa upande wa vitenge urefu wa sentimita 200 na upana wa sentimita 116; lakini ni viwango vya mwaka 2009. Kwa hiyo sasa TBS mkakati wa kwanza kabisa inafanyia maboresho viwango hivyo, akina mama sasa mkae tayari kuvaa viwango vikubwa vya nguo. Viwango vinapitiwa na vitaanza kutumika mwezi Juni, mwakani.
Kwa hiyo akina mama Mheshimiwa Mwakilagi nikupongeze sana; Mheshimiwa Naibu Spika hata wewe nadhani unaendelea kukua utavivaa mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Pili ambao sasa Serikali inafanya, imetenga maeneo maalum kwa ajili ya viwanda vitakavyokuwa vinazalisha sasa nguo aina mbalimbali, vikiwemo vitenge vya kuvaa lakini hata ambavyo vimeshonwa, wametenga hekta 2100 kule TAMCO - Kibaha, pamoja na hekta 431 kule Kigamboni. Kwa hiyo Waheshimiwa akina mama taratibu za kiserikali zinafanyika kuwahakikishia sasa mtavaa nguo bila wasiwasi.
Kuhusiana sasa na madera ni kweli kabisa hata sisi akina baba tunashangaa, unaona akina mama wanavaa madera kila sehemu, kumbe ni kwa sababu hata nguo za kuwabana sasa siyo fashion tena. Sasa hatua za Serikali za makusudi kabisa ambazo imezichukua, sasa hivi vipo viwanda vitatu vinavyozalisha nguo za kuvaa, kiwanda cha kwanza ni cha TUKU ambacho kipo pale Mabibo, lakini viwanda vingine pamoja na Sunflag, pamoja na kile kiwanda cha Mzava karibu na maeneo ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mavazi aina ya madera Serikali imekaribisha wawekezaji wa Kichina na Kihindi ili waje wawashonee nguo sasa aina ya madera akina mama mnayoyataka. Kwa hiyo Serikali imeshachukua hatua asante sana Mheshimiwa.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Tizeba kwa kuchaguliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na pia kumshukuru kwa majibu mazuri sana pamoja na kwamba ameanza kazi leo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa zao la mwani limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo kutofahamika kwa zao lenyewe lakini vilevile kukosa soko, pembejeo na hivyo kufanya wakulima wa mwani na hasa wanawake kuhangaika kutafuta masoko na pembejeo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha zao hili la mwani linaongezewa thamani kwa kujenga viwanda katika maeneo yote yanayozunguka ukanda wa bahari ili zao hili lilete tija kwa wanawake na hasa ikizingatiwa kwamba zao hili limekuwa linachukuliwa tu na Wachina na soko lake liko China, Korea na maeneo mengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vikundi vya ujasiriamali kwa asilimia kubwa vimekuwa vikitegemea mabenki ya kibiashara ambayo kwa kweli riba yao imekuwa kubwa sana na hivyo kufanya vikundi vya wanawake na vijana kushindwa kabisa kumudu kwenda kukopa katika mabenki hayo. Serikali ina mkakati gani kupitia upya mabenki yote na vyombo vyote vya fedha ili kuangalia hizi riba zinazotozwa na kulinganisha na hali halisi ilivyo ili wanawake na vijana waweze kunufaika na mabenki haya? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa sasa hili zao la mwani soko lake siyo zuri sana hapa nchini. Kama alivyosema yeye mwenyewe, wakulima wa mwani wanauza kwa makampuni ya kutoka huko Korea, China na India.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sababu kubwa ya msingi ya kutoongeza thamani ya zao hili hapa hapa nchini ni uzalishaji mdogo ambao uko katika zao hili kwa sasa. Ili uzalishaji uweze kuwa na tija kwa mwekezaji mwenye kiwanda kwa uchache zinahitajika tani 12,000 kwa mwaka au zaidi, ndiyo mtu akiwekeza kwenye kiwanda cha kuchakata mwani anaweza kupata faida. Sasa hivi uzalishaji tulionao ni tani 600 tu kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana sasa Serikali, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kupitia huu mradi wa SWIOFish tunajipanga kupitia vikundi vya uzalishaji wa mwani ili viweze kupatiwa mikopo. Nitoe wito kupitia nafasi hii kwamba Halmashauri zote ambazo ziko katika Ukanda wa Pwani watie jitihada kubwa katika kuviorodhesha hivi vikundi ili hizi fedha ambazo zinatolewa na Benki ya Dunia ziweze kutumika vizuri kwa vikundi hivyo vya akina mama na hata wasio akina mama kwa sababu zao hili siyo kwa ajili ya akina mama na vijana peke yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko fedha ambazo Serikali imeshapata kutoka Benki ya Dunia, Dola za Kimarekani milioni 36. Dola za Marekani milioni 17 zitatumika kwa Tanzania Bara na Dola milioni 11 zitatumika kwa Tanzania Zanzibar na Dola milioni 8 hivi zitatumiwa na taasisi zinazohudumia utafiti katika eneo hili la uzalishaji viumbe katika Ukanda wetu wa Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujibu swali lake la pili la nyongeza, hivi vikundi vijiorodheshe. Hizi fedha hasa ndiyo zimelenga kuwakomboa hawa watu wa vikundi kuondokana na mikopo ambayo siyo rafiki sana wakati mwingine kutoka kwenye taasisi za fedha kwa sababu, watapewa msaada wa pembejeo, ruzuku za dawa na vitu vingine ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji wao. Tutakapofika tani 12,000 au zaidi, watu wengi wanayo nia ya kuwekeza katika viwanda hapa nchini vya kuchakata hizi mwani na ndiyo hapo sasa hata thamani ya hili zao itaweza kuongezeka.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo la nyumba na ofisi katika Halmashauri mpya ya Wilaya ya Nyang’hwale ni sambamba na matatizo katika Halmashauri nyingi zilizoanzishwa hapa nchini ambazo ni mpya. Sasa napenda kujua, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga ofisi mpya na nyumba mpya katika Halmashauri zote nchini zilizoanzishwa ikiwemo na Halmashuri ya Butiama ambako ndiko alikotoka Baba wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa mama yangu na wamama wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Amina Makilagi kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili ni lazima nilijibu taratibu sana kwanza. Kweli hoja aliyoitoa Mheshimiwa Mama Makilagi ni ya msingi sana, ndiyo maana siku tulipokuwa tukihitimisha bajeti yetu ya TAMISEMI nilisema kwamba Halmashauri zile mpya lazima tuhakikishe tunaweka miundombinu na ni lazima nyumba zijengwe. Ndiyo maana katika kipaumbele chetu sisi cha TAMISEMI katika bajeti yetu ya mwaka huu, tuliziorodhesha zile Halmashauri ambazo ujenzi unaanza, lakini Halmashauri nyingine mpya hata ujenzi haujaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali hili ni kubwa na zito na limetolewa na Mbunge mzito, niseme yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuliona hili tunaweka kipaumbele; kuna Halmashuri mpya zipatazo 20 tumezitengea kila moja shilingi bilioni 2,140,000,000 kila Halmashuri moja! Halmashauri hizo ni Buchosa, Bunda TC, Chalinze DC, Handeni TC, Ifakara TC, Itigi DC, Kasulu TC, Kibiti DC, Kondoa TC, Madaba DC, Mafinga TC, Malinyi DC, Mbinga TC, Mbulu TC, Mpimwa TC, Nanyamba TC, Newala TC, Nzega TC, Songwe DC na Tunduma TC. Hizi kila moja tumezitengea shilingi bilioni 2,140,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna Halmashauri zipatazo 44 tumezitengea kati ya shilingi milioni 500 na shilingi milioni 850. Hii maana yake ni nini? Wajumbe mbalimbali inawezekana wakasimama hapa kutaka kujua juu ya hoja hiyo.
Nakala hii iko hapa, mtu anaweza akafanya reference katika Halmashauri yoyote ambapo mwaka huu tumeweka kipaumbele, lazima Ofisi ya Rais, TAMISEMI ihakikishe inajenga miundombinu katika maeneo hayo, ili mradi wafanyakazi waweze kupata huduma bora na waweze kupata mazingira rafiki ya kufanyia kazi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada na Bunge lililopita Wabunge tukatunga sheria kali sana ambayo itawabana wale wote waliokuwa na tabia ya kuwaoa watoto. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania iliiagiza Serikali iifanyie marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kama kweli dhamira ni nzuri kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza, ningependa kujua, ni kwa nini Serikali iliamua kukata rufaa badala ya kutekeleza maamuzi ya Mahakama? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa sheria nyingi sana ambazo zinawakandamiza wanawake na watoto, bado zipo katika nchi yetu ya Tanzania, zikiwepo hata sheria za kimila na nyingine na nyingine. Ningependa kujua sasa, Serikali ina mkakati gani na hasa Wizara ya Katiba na Sheria, kuhakikisha inaleta sheria zote kandamizi zinazowabana wanawake na watoto ili sheria hizi tuweze kuzifanyia marekebisho? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amina Makilagi kwa kupigania haki za akinamama bila kuchoka, matunda ya juhudi zenu, wewe mwenyewe Mheshimiwa pamoja na wanawake wenzako yanaonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusu kesi iliyokuwepo Mahakamani na kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali imebidi akate rufani, nimeeleza katika jibu langu la msingi kwamba Serikali inaona tatizo katika Sheria ya Ndoa, si kwamba haioni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotupeleka Mahakama ya Rufani ni vitu viwili. Kwanza, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, tayari iko katika mchakato chini ya Wizara yangu na utaratibu tunaoutumia tulidhani itakuwa vyema kwa mshikamano wa Taifa letu tukaendeleza majadiliano kama tulivyofanya wakati wa kuitunga hii sheria ya mwaka 1971. Sisi tunataka tu kupata busara za Mahakama ya Rufani kuhusu suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, haki ya kukata rufani si tu ya wananchi, lakini vilevile hata Serikali pale ambapo inaona kuna kitu ambacho kinahitaji kupewa msimamo madhubuti zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii anaweza akatokea Jaji mwingine wa Mahakama Kuu akatoa uamuzi tofauti kwa sababu wote wako katika maamuzi. Sasa tunachotafuta na anachotafuta Attorney General ni kupata sasa maamuzi kwenye Mahakama yetu ya juu katika nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni kweli kabisa bado kuna baadhi ya sheria zinamkandamiza mwanamke lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Amina Makilagi na wanawake wenzake kwamba tumepiga hatua kubwa mno toka uhuru katika kuhakikisha kwamba mwanamke anapata haki sawa kama ambavyo Katiba yetu inavyosema chini ya Ibara ya 13.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke, tumefanya mabadiliko ya sheria nyingi, tukumbuke Sheria ya Ardhi namba Nne (4) na namba Tano (5) imeondoa kabisa ubaguzi uliokuwepo kwa mwanamke. Sasa hivi mwanamke ana haki sawa chini ya sheria hizo. Leo si kawaida tena kwa mume akatoka tu asubuhi akauza nyumba, akauza kiwanja bila kupata ridhaa ya mama na mama akienda Mahakamani hiyo sale ama mauzo hayo hayana maana kabisa. Leo hii akinamama talaka haitokei akaondoka hivi hivi lazima kugawana matrimonial property, hizo zote kwa kweli ni faida ambazo tumezipata katika mabadiliko mbalimbali ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nenda Jela; wafungwa wengi wanaotumikia vifungo virefu katika nchi hii ni wale ambao wana makosa ya kunyanyasa akinamama. Namshukuru Mheshimiwa Makilagi ameelezea kuhusu sheria tuliyobadilisha juzi tu hapa Sheria ya Elimu ambapo leo hii mtoto wa kike aliye sekondari, aliye shule ya msingi, akipata mimba ole wako wewe uliyefanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii ni kulinda na baada ya muda si mrefu tutaleta Muswada hapa wa Huduma ya Msaada wa Sheria ambayo nakuhakikishia utakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa akinamama walioko vijijini ambao katika mfumo tulionao usiojali mtu kutokujua sheria; kwamba ignorance of the law is not defence, akinamama wengi watafaidika sana. (Makofi)
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, wanawake wa Tanzania kwa kiwango kikubwa walio wengi ndiyo wakulima; na kwa kuwa wanawake wa Tanzania hawana fursa za kiuchumi zitakazowafanya wafikie Benki hii ya Wakulima kwa sababu ya kukosa dhamana. Napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanawake wengi ambao ni wakulima waishio vijijini wanafikia fursa hii ya kupata mikopo katika Benki ya Wakulima kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wanawake wengi wa Tanzania ndiyo wanaojihusisha katika kilimo hapa nchini. Serikali kwa kutambua hilo imeweka mipango mbalimbali ikiwemo ukopeshaji wa vikundi vya akinamama katika uzalishaji kupitia Halmashauri zao lakini pia tunatoa kipaumbele katika Mfuko wa Pembejeo. Wanawake wanaokwenda kukopa katika Mfuko wa Pembejeo wanapata kipaumbele kwa sababu wao wanafahamika ndiyo wanaoshiriki zaidi katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio Benki ya Kilimo tu inayotoa mikopo katika sekta ya kilimo, benki nne hapa nchini kwa sasa zinatoa fedha katika shughuli za kilimo. Utoaji wa fedha hizi hauko katika shughuli yenyewe ya kilimo tu, isipokuwa benki zinatoa fedha katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Benki ya NMB mwaka huu pekee wa fedha imetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya shughuli za kilimo na akinamama wana kipaumbele. Masharti ya mikopo katika benki ambazo tumezungumza nazo za NMB, Commercial Bank of Africa, CRDB, wote wamepunguza masharti katika mikopo ya kilimo ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa wale wasio na dhamana kuweza kupata mikopo hii kwa urahisi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amethibitisha kwamba kweli ziko sheria ambazo zimeshapitwa na wakati na Tume ya Kurekebisho ya Sheria ya Serikali inaendelea kuzifanyia marekebisho. Ningependa kujua ni sheria gani hizo sasa ambazo ziko katika huo mchakato na pia ningependa kujua hizi sheria zinaletwa hapa lini ili Bunge lako tukufu liweze kuzipitisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na kilio cha muda mrefu na hata leo Mheshimiwa Mwenyekiti imethibitisha kwamba kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha Waheshimiwa Wabunge Wanawake na Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumekuwa na kilio kikubwa sana cha wanawake na vijana juu ya kutungwa sheria ya mfuko wa wanawake na vijana na walemavu. Lakini pia kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wakulima wadogo wadogo kwamba kilimo chao hakiwaletei tija kwa sababu hakuna sheria inayoweka mfumo mzuri wa wakulima wadogo waweze kuletewa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua sasa. Serikali ina mkakati gani wa kuleta hizi sheria Bungeni. Hili suala la kuwa kila siku tunaambiwa Serikali itaweka msukumo kuhakikisha asilimia 10 ya wanawake na vijana inatengwa ili tuweze kufikia mahali panapohitajika. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya akina mama nchini na ni kazi kubwa amekuwa akiifanya kwa ajili ya akina mama wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza ni sheria gani zipo katika mchakato. Kama nilivyosema, kazi kubwa ya Tume ya Kurekebisha Sheria ni kupitia sheria na baadaye kutoa mapendekezo kupitia taarifa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu wa fedha Tume inafanya kazi ya mapitio ya sheria za mambo ya jinai (criminal justice) wanafanya pia mapitio ya sheria ya mambo ya evidence law, utoaji wa ushahidi mahakamani, lakini pia wanafanya mapitio ya sheria ya ufilisi (insolvency law) na vilevile wanafanya mapitio ya sheria ya huduma za ustawi wa jamii. Kwa hiyo, hizo ndiyo kazi ambazo zinafanyika katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika swali lake la pili ameuliza kuhusu lini Serikali italeta sheria mahsusi kwa ajili ya utungwaji wa uundwaji wa mifuko hii maalum kwa ajili ya akinamama na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mifuko ya akina mama na vijana ipo na inaongozwa na miongozo yake tayari na imekuwa ikifanya kazi katika utaratibu huo wa kuchangia asilimia 10 hizo za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwongozi tayari upo. Labda ambacho kinaweza kikafanyika ambapo Serikali imekuwa ikijibu hapa ni kuboresha na kuona namna bora ya kuweza kuwafikishia kwa urahisi zaidi akina mama na vijana huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wakulima wadogo wadogo kutungiwa sheria. Kama Serikali tunaichukua na tutaona umuhimu wake hapo baadaye wa kuweza kulifanyia kazi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na jitihada za Serikali za kuongeza zana za uvuvi katika sekta hii ya uvuvi na pamoja na kupongeza jitihada zinazoendelea. Ningependa kujua, pamoja na mwanzo huu mzuri uliofanywa na Serikali, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuongeza wigo zaidi ili zana hizi zipatikane katika bahari yote ya Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta ambazo zinaweza zikaleta tija katika Taifa letu na kuongeza Pato la Taifa, tumeshuhudia miaka iliyopita wakati Mheshimiwa Rais, Dkt. Joseph Magufuli, akiwa Waziri wa Uvuvi, alikamata meli moja tu na ikaleta tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa kutengeneza meli za kutosha ili ziweze kwenda kuvua katika kina kirefu na kuongeza Pato la Taifa katika Taifa letu? (Makofi). Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kazi nzuri anayoifanya wakati wote ya kuwapambania wavuvi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, anataka kujua juu ya mkakati wa Serikali wa kusambaza teknolojia hii. Katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba Taasisi yetu ya Utafiti ya TAFIRI inafanya utafiti wa kujiridhisha juu ya ufanisi wa teknolojia hii katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Mara tu baada ya kuwa tumefanikiwa na kujiridhisha kwamba teknolojia hii inaweza kutupatia tija, naomba nimhakikishie tutaisambaza kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo katika maeneo mengine ya bahari yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, anataka kujua juu ya mkakati wa Serikali wa kupata meli kubwa kwa ajili ya kuweza kuvua na kupata faida kubwa kwa ajili ya nchi yetu. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tumejipanga vizuri na tupo katika programu ya kuhakikisha tunapata meli hiyo, hivi sasa tupo katika hatua kabla ya kwenda katika ununuzi wa meli hiyo, tuanzishe na kulifufua Shirika letu la TAFICO ambalo hili ndilo litakalokwenda kuwa msimamizi mkuu wa hata hiyo meli ambayo tunatarajia kuinunua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba aendelee kuvuta subira na kutuunga mkono ilimradi tuweze kufikia katika hatua hii tunayoifikiria. (Makofi)
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hapa nitoe ombi kwamba ni vizuri akatuletea takwimu hizi kwa maandishi kwa sababu tatizo la kutelekeza watoto ni kubwa sana katika nchi yetu, na mfano ni pale Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama alipofanya zoezi la kuwatambua watoto waliotelekezwa. Nilikuwa naomba hapa atuletee kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa viwango vilivyowekwa vya kutunza watoto waliotelekezwa ni vidogo, lakini hata nilipopitia hii sheria haioneshi kwamba mzazi anayeacha watoto wake anatakiwa apeleke kiasi gani kwa mwezi au kiasi gani kwa mwaka badala yake ni busara ya Mabibi Maendeleo ya Jamii, badala yake ni mahakama zinatumia busara wanalipisha kiwango cha shilingi 2,000 kwa mwezi kiwango ambacho hakitoshi kabisa kutunza watoto.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu wa kisheria utakaowafanya wazazi wanaotelekeza watoto waweze kubanwa kisheria na waweze kutunza watoto?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu baadhi ya wazazi walio wengi katika jamii yetu wanatekeleza watoto kwa kisingizio kwamba si watoto wao, na kwa sababu katika vituo vyetu vya afya na katika zahanati zetu hapa nchini hakuna vipimo vya kupima DNA.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa Serikali ina mkakati gani ili kupeleka vifaa hivi na kuweza kuwabana wazazi wote wanaokwepa kulea watoto wao kwa visingizio kwamba si watoto wao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, mwitikio wa swali hili unaonesha kwamba suala hili la utelekezaji wa watoto ni changamoto kubwa hata ndani ya nyumba yako. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Amina Makilagi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taratibu tulizonazo ni kwamba, kiwango na gharama za matunzo ambazo zinatolewa yanapatikana baada ya kufanya assessment ya yule mhusika kuona hali yake ya kipato na hali ya maisha na umri wa yule mtoto na pale ndipo mahakama inaweka utaratibu wa kiwango ambacho kinatolewa. Mimi niseme tu kwamba katika suala hili sisi kama Wizara tunaendelea kufanya mapitio ya sera zetu na vilevile kuja na sheria ambayo itajaribu sasa kufanya mapitio ya yote haya kuangalia sasa ni utaratibu gani mzuri tunaweza tukaweka kuhakikisha kwamba wale wote wanaotelekeza watoto basi wanabanwa vizuri zaidi na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Makilagi ameuliza kuhusiana na kupanua huduma za upimaji wa DNA. Niseme tu kwamba upimaji wa DNA unafanywa na ofisi au taasisi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Upimaji huu si upimaji ambao holela mtu anaweza akanyanyuka akaenda na sampuli yake pale anapojisikia kwenda kufanya upimaji. Kuna taratibu ambazo zimewekwa kwamba ni mamlaka ikiwa ni pamoja na Mahakama, Maafisa Ustawi wa Jamii au Polisi ambao wanaweza wakaagiza na si kila mtu ambaye ukiwa na sampuli yako unafikiri kwamba mtoto si wako unaweza ukaenda pale ukafanya, hatufanyi upimaji, request zote zinapatikana kupitia mamlaka husika.