Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asha Mshimba Jecha (1 total)

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu yenye kutia moyo ya Mheshimiwa Waziri, hivi anafahamu kituo hiki sasa hivi kimefunga huduma zake na wanatoa huduma kwenye jengo la kuazima? Je, ni lini tathmini hii itafanyika ili gharama ijulikane na umuhimu wa kukijenga pia uonekane? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia anawahakikishia vipi wananchi wanaotumia kituo hiki umuhimu wa kujengwa na kuweza kukitumia kama walivyozoea? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Asha, kwa kweli kwa kufuatilia sana suala la kituo hiki. Mbali na swali la hapa amekuwa pia akiulizia mara zote anapopata fursa ya kutembelea ofisini ama kwenye shughuli za Kamati.
Mheshimiwa Spika, niseme tu, kwa umuhimu huo na kwa ufuatiliaji wake, jambo hili tumesema lifanyiwe tathmini kwa upekee kwa maana ya Kituo cha Dunga kama kituo peke yake mbali ya vituo vingine kwenye maeneo mengine ambavyo vinafanana kama kituo hicho.
Mheshimiwa Spika, mara tathmini hiyo itakapokuwa imekamilika ambapo tunaamini ni katika kipindi hikihiki, basi utaratibu wa upatikanaji wa fedha utaanza na hapo ndipo tunaposema tunatoa rai hata kwa wadau mbalimbali ili tuweze kufanya kama ni jambo mahsusi kufuatana na mazingira ya pale.
Mheshimiwa Spika, mara ukarabati wake utakapokamilika basi niwahakikishie wananchi kwamba matumizi yake yatarejea katika hali ya kawaida na wataendelea kumpongeza na kumpigia kura Mheshimiwa Mbunge ambaye amelitetea sana jambo hili. (Makofi)