Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John Wegesa Heche (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa sababu ni mara yangu ya kwanza, kuchangia, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, ambaye ametupigania mpaka leo tupo hapa. Jambo la pili niwashukuru sana wananchi wa Tarime ambao kwa miaka mingi na miaka yote wameonesha imani kwangu walinichagua, kuwa Diwani wa Kata ya Tarime Mjini nikiwa Mwanafuzi wa Chuo Kikuu, lakini vilevile pamoja na mapambano makali yaliyokuwepo kwenye uchaguzi huu mpaka mauaji yaliyofanyika tarehe kumi mwezi wa Tisa, wananchi walisimama imara na wamenileta hapa na nataka niwahakikishie nitawawakilisha na nitasimamia kero zao kwa nguvu zangu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana usiku nilijitahidi sana kusoma na ku-google nchi mbalimbali kuhusiana na Uongozi, nikajaribu kuangalia mambo yaliyofanyika siku za hivi karibuni hapa Bungeni, ya Polisi kuingia ndani ya Bunge wakiwa wamevaa Head gear, bunduki, sijui mipini kujaribu kupiga Wabunge waliokuwa hawana silaha. Nikagundua kwamba hata Idd Amini, hata Adolf Hitler, hakuwahi kuingiza Polisi kwenye Bunge kujaribu kupiga watu wanaopinga. Kwa hiyo, hapo mtajaza wenyewe kwamba mna uongozi wa aina gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuongoza nchi hii kwa takwimu za uongo. Hapa Dkt. Mpango naomba unisikilize vizuri, nimesoma vitabu vya Mpango hivi, takwimu zilizoko hapa, ni takwimu feki, na kwa takwimu hizi hamuwezi kufanya kitu chochote hata muwe na nia njema. Kwa nini nasema hivyo, kwa mfano, maji vijijini kitabu hiki kinaonesha cha Mpango kwamba kuna maji Vijijini kwa asilimia 68.
MHE. JOHN W. HECHE: Nimejaribu kuangalia kwenye Jimbo langu peke yake…
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri!....
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu, naamua kuwapuuza wote niendelee tu. Nilikuwa nazungumzia kuhusu takwimu. Takwimu za maji kwa mfano vijijini wamesema maji yapo kwa aslilimia 68, lakini nimeangalia Jimbo langu ni Jimbo la Vijijini tuna Kata 26, katika Kata 26 hizo asilimia 68 ya 26 ni Kata 17 ina maana kwa mujibu wenu kwenye Kata 17 kuna maji hivi sasa tunavyozungumza, kitu ambacho ni uwongo na hakipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mijini mmesema kuna maji asilimia 95, hii ni aibu ina maana kila watu 10 watu tisa wanapata maji, au kila watu 100, watu 95 wanapata maji, lakini pale Dar es Salaam ni kielelezo, kipindupindu kinawaumbua kila siku, kwamba hakuna maji na takwimu mnazoleta humu ni za uongo. Kwa hiyo, kama mnataka kulitoa Taifa hili hapa ni lazima tuwe na takwimu ambazo zinaeleza ukweli, na takwimu ambazo zitawasaidia kujenga kwenda mbele, lakini mkija na takwimu za uongo hapa mnajidanganya wenyewe na wananchi wanawaona.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara, zetu ni mbovu
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!
MWENYEKITI: Taarifa...
MHE. JOHN W. HECHE: Nawashauri Mawaziri tulieni msikilize, kwa mujibu wa sera ya maji ya Taifa hili, maji ambayo mnahesabu kwamba watu wanapata wapate ndani ya mita 400 kutoka wanapokaa, sasa kwenye hivi vijiji mimi ninavyosema watu wanafuata maji mpaka kilometa moja, mbili, sasa unatoa taarifa gani hapa. Tulia usikilize tukueleze wananchi watapima kule anasema nani uongo kama maji yapo au kama hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, barabara zetu ni mbovu, kwa mfano barabara za Tarime. Kutoka Tarime kwenda Serengeti ambako kuna Mbuga kubwa ya wanyama. Inapita Nyamongo kwenye eneo la Mgodi wa Nyamongo, barabara ni mbovu, na mimi ninamwomba sana Waziri achukue hii hoja ya barabara hii iwemo kwenye Mipango ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nishati; leo mnakuja hapa kuzungumza kuendeleza Taifa, wakati watu wanapikia kuni. Dar es Salaam peke yake, ambayo mkaa unakwenda pale magunia tani na tani, mngeweza kama kweli mnataka kuendeleza Taifa hili, kuliko kurukaruka hapa, mngechukua Dar es Salaam ile peke yake, mkazuia utumiaji wa mkaa na magogo na kila kitu mkapeleka gesi pale kwa bei rahisi watu wote watumie gesi pale Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, tayari mngekuwa mmesaidia misitu ya Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnakuja humu mnaimba tu misitu tuta-conserve misitu, mazuia watu. Kama kule Jimboni kwangu naona eti Afisa Misitu anazuia watu wasitumie mkaa, nimemwambia wananchi watakuchapa wewe! Wapelekee kwanza gesi ndiyo uwazuie kutumia mkaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makusanyo ya Serikali; nataka mtuambie hapa, hicho mnachojisifia kwamba mmekusanya mwezi wa 12 ni arrears au ni vyanzo vipya mmeleta na mmekusanya. Kwa sababu msije mkajisifu hapa tumekusanya tirioni 1.4 kumbe ni arrears za huko nyuma ambazo ni za watu ambao ni majipu na majipu wengine wako humu mnawajua wanatakiwa walipe na ni madeni. Sasa huko mbele mmetengeneza vyanzo gani, mmvionesha wapi kwenye Mpango huu, vyanzo vipya. Leo mnataka mchukue pesa kwenye Halmashauri na hili msithubutu Mheshimiwa Waziri, Halmashauri watu wakusanye pesa wao wenyewe, wakupelekee Benki Kuu, halafu wewe ndiyo urudishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, tunaidai Serikali pesa za ardhi ambazo ni asilimia 30 miaka karibia sita zaidi ya milioni 500, tunapeleka pesa zetu wakati wa kurudi hazirudi. Leo ndiyo wamerudisha milioni 27, leo tena tuchukue pesa zetu za mapato ya ndani tuwapelekee na nyie mnajua, kama mnataka kuendeleza uchumi wa watu kule vijijini mabenki yaliyoko kule Wilayani ndiyo yanakopesha watu wanaofanya biashara ndogondogo na benki hizi zinategemea pesa kutoka kwenye Halmashauri, leo mnataka mchukue pesa zitoke Halmashauri mabenki yakose pesa, yashindwe kukopesha watu wetu kule chini, biashara zife kule chini, halafu mnasema mnataka kuendeleza Watanzania au mnataka kuwa-suffocate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekuja hapa mnasema viwanda, kila mtu anasimama hapa viwanda. Viwanda gani, viwanda vinategemea foreign direct investment, Wazungu hawa mnaoenda kukinga mabakuli wamesema wako concerned na mambo yaliyofanyika Zanzibar, hakuna amani, Zanzibar kule kuna Nkurunziza. (Makofi)
Mmechukua hamtaki kutoa nchi kwa mtu aliyeshinda, kwa maana hiyo Wazungu wanakwenda kuzuia hiyo misaada sijui mtapata wapi pesa za kuanzisha hivyo viwanda.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika naomba ukae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
kunipatia nafasi ili niweze kuchangia kwa niaba ya watu wa Tarime. Kwanza nimesoma hiki kitabu cha bajeti na hotuba ya Waziri na niseme tu kwa niaba ya watu wa Mkoa wa Mara, nina masikitiko makubwa sana, na watu wa Mkoa wa Mara, hawataunga mkono bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Rais alichoahidi wakati wa kampeni akiwa Mkoa wa Mara mzima, aliahidi uwongo, kwa sababu nimesoma kitabu hiki, Mkoa wa Mara mzima umepewa 0.8 kilometa za lami, haikubaliki; watu wa Mkoa wa Mara ndiyo wenye mbuga kubwa kuliko zote, Mbuga ya Serengeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mkoa wa Mara ndiyo waliokuwa na mgodi wa Buhemba, ambao umechimbwa umekwisha madini pale, wana mpaka wa Sirari, wana Ziwa Victoria wanatoa samaki pale, wana Mgodi wa Nyamongo ambao unaendeea kuua watu. Halafu inapofika kwenye maendeleo, hamuwapelekei pesa haikubaliki, haitakubalika kwa viwango vyovyote vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nitamtaka Waziri aje atujibu hapa na nimesoma kitabu cha Mpango hiki hapa, Mheshimiwa Waziri amepeleka kiwanja cha ndege Geita Wilaya ya Chato; kutoka Geita Mjini kwenda Chato kwanza ni kilometa zaidi ya 100 na kitu, sijui amepeleka kwa kujipendekeza kwa Rais au ni Rais mwenyewe amemwagiza akipeleke nyumbani kwake sijui hilo atatujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu hapa ni kwamba, Mkoa wa Mara ambao una mbuga ya wanyama ya Serengeti, ina ziwa pale Musoma tunashindwa kujenga uwanja wa Mkoa wa Mara, uwanja wa ndege na kuuboresha uwe wa Kimataifa, wazungu washuke pale walete uchumi kwa watu wa Mkoa wa Mara. Tunachukua mikoa mipya ambayo imeanza juzi, tunaitengea mabilioni ya pesa kwenda kujenga viwanja ambavyo havina muunganiko wowote wa kiuchumi, ni viwanja vya watu kusafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja huu wa Mkoa wa Mara tunauhitaji kwa kweli; naomba sana Waziri anapokuja kuzungumza hapa azungumze hili, kwa sababu ni aibu kwa watu wa Mkoa wa Mara ambapo Mwalimu Nyerere anatoka kule na kila siku mnamsifia, lakini kutendea watu hawa haki hamfanyi hivyo. Hivi kweli watu ambao tunachangia madini yetu mnachukua, samaki wetu mnachukua, kila kitu mnachukua pale, wanyama mnachukua. Jana Mheshimiwa Maghembe alikuwa anasema hata kuchunga hataki tuchunge, anasema ng‟ombe wetu ni tatizo, kwenye ardhi ya kwetu wenyewe, ng‟ombe anasema ni shida; tunachoambulia na mbuga ile ni ng‟ombe wetu kupigwa risasi, ni watu wetu kubaki vilema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukubali hali hii, unapofika wakati wa kutuletea pesa, hospitali ya Kwangwa pale imekuwa wimbo. Haya ni matusi na nitaomba Waziri aje atuambie ni lini mnakwenda kujenga uwanja wa ndege wa Mkoa wa Mara ili kuunganisha watalii waje Serengeti na sisi tuna ziwa pale, watalii wanapenda beach, sisi tuna beach pale, watakuja kuogelea pale, mtuunganishie mtuletee uchumi, hilo ni la muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu barabara. Barabara ya kutoka Tarime kwenda Serengeti ni barabara muhimu. Wote mnajua watu wa Serengeti chakula wanachokula kinatoka Tarime na hii barabara bahati nzuri inapita kutoka Tarime Mjini inakwenda inapita Nyamongo, mnakochukua mawe ya pesa, lakini mnataka wale watu waendelee kufa na vumbi, wakati dhahabu yao mnachukua, na kila siku wanapigwa risasi na jana walipigwa risasi pale, hata kuwapelekea barabara, hamuoni aibu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarime nzima hakuna hata mita moja ya lami ambayo mmetujengea pale, wakati madini yanatoka pale. Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri aje atujibu, hii barabara ndiyo inalisha watu wa Musoma, ndiyo inalisha Bunda, ndiyo inaleta ndizi Mwanza, tofauti na zile zinazotoka Kagera. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu atuambie na hili siyo la kwangu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati akihutubia Nyamwaga na wakati akihutubia Nyamongo, aliwaahidi watu hawa barabara hii ya lami ya kutoka Tarime mpaka Serengeti. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine vinafanyika unashangaa, nimeona hapo mnafumua barabara ya lami hapa Dodoma, yaani watu wengine wanalala porini siku hata 10 hawana hata barabara mbovu, hiyo mnafumua eti imetoboka, mnaweka lami mpya. Hivi haya maamuzi mnayafanya mkiwa wapi? Kwa nini mnafanya maamuzi ya aina hii? Tunahitaji mje mtuambie majibu hapa, ni kwa vipi watu hawa wanapata barabara nzuri ya kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Ndege; nchi hii ni miongoni mwa nchi zinazotia aibu kweli kweli, karibu kwenye kila kitu, leo Rwanda nchi ambayo hailingani hata na Mkoa wa Mara, ina ndege zinaruka dunia nzima. Sisi ndege yetu ni Fast Jet ambayo hata Waziri anajua ukienda hata na begi unalipishwa. Nimelipishwa begi shilingi 200,000 kwenye ndege, Taifa halina hata ndege ya kuruka ndani kwa ndani hapa, acha kwenda Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 55 ya uhuru hatuna ndege, sasa Waziri anakuja kutuambia hapa kwamba watanunua ndege, mtazitunza vipi, wakati watu wanahujumu, wanauza ndege ambazo zingefanya kazi wanauzia trip ma-fast jet, sijui wanahongwa. Kuna watu wako pale Air Tanzania wanakaa kwenye ofisi asubuhi mpaka jioni wanasubiri mshahara, halafu hawafanyi kazi, aibu, yaani hawarushi ndege hata moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mhasibu, kuna Engineer sijui kuna pilot sijui wanarushwa popo mle ndani? Labda kuna popo wanaendesha mle, wanaruka mle ndani, ndiyo ma-pilot wa hao popo.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, anapokuja hapa utoe majibu kwa Watanzania, ni kwa vipi au wana mpango gani wa kwenda kufufua Shirika lao la Ndege na lirushe ndege kwa nchi nzima. Kwa nchi ambayo tuna Maziwa tuna kila kitu, ndege haiwezi kuwa anasa kwa Watanzania kusafiria. Haya ni majibu ambayo Watanzania wanahitaji na tunahitaji kuyasikia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana bajeti ya nchi yetu imekuwa ni formality tu; watu wanakuja hapa wanapiga kelele, mwaka baada ya mwaka, kuwa Serikalini, liwe jipu ni la CCM, uwe usaha ni wa CCM, viwe vyombo vya kutumbulia ni vya CCM, hatuna sababu yoyote ya kutetea majipu, yaani haipo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema, ni kwa nini mpaka sasa watu wa TANROADS ambapo hata mtoto anajua wamejenga barabara ambazo ni sawasawa na zile sahani tunazotumia kwenye hoteli zile disposable yaani barabara ukipiga teke hivi lami inaruka juu. Wamejenga barabara za kiwango kibovu cha aina hiyo, lakini mpaka sasa hatujasikia hata mtu mmoja ametumbuliwa kutoka TANROADS au ni kwa sababu mkubwa ambaye mmesema asiguswe humu alikuwa hapo? Hivi anashindwa vipi kuungamanishwa na hilo? Leo mmetumbua mpaka watu wa nyuki lakini watu wa TANROADS hatujaona wakitumbuliwa. Hatuwachochei mtumbue, tunataka mtumbue waliokosea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Na mimi pia nimshukuru Profesa Muhongo kwasababu kwenye Bunge la mwanzo mwezi wa pili aliunda kamati ya kwenda kuchunguza suala la Nyamongo na ndugu yangu Agness pale anasema aliniteua, mimi sikuteuliwa na Profesa ni vyema nikaweka wazi haya mambo yakajulikana.
Kwa hiyo, nampongeza Profesa kwa ile kazi na wananchi wa Nyamongo wanasubiria majibu yao kwa matatizo yale makubwa ambayo yamekuwa pale kwa miaka yote. Leo nilitaka tu niseme kidogo kuhusiana na historia ya mgodi ule wa Nyamongo na utofauti wake na migodi mingine ili Profesa uelewe unapokwenda kutoa majibu ya wale wananchi, utoe majibu ukijua hilo kichwani kwako.
Kwanza ule mgodi ni tofauti na migodi mingine ambayo wazungu wanakwenda wanapata eneo porini huko, wanaanzisha uchimbaji, wanafanya exploration na wanaanza kuchimba. Ule mgodi ni mgodi wa wananchi tangu mwaka 1911, watu wa pale walianza kuchimba madini pale kabla hata ya ukoloni na kabla ya Uhuru. Watu wa eneo lile hawana hata eneo la kulima, kwa hiyo waalikuwa maisha yao yote yanategemea uchimbaji wa madini ya Nyamongo, ndivyo maisha yao yalivyokuwa kwa miaka yote. Mwaka 1994, Serikali haya maamuzi ya kuamuliwa Dar es Salaam; Serikali ikachukua leseni ikawapa wazungu. Ina maana ikabadilisha economic activity ya watu, kama mimi nafanya biashara ya duka, leo unakuja unafunga duka langu, hunioneshi kazi nyingine mbadala ya kufanya. Kwa hiyo, Serikali ikachukua leseni ikawapa wazungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu wakaja wakatwaa eneo na ule mgodi uko katikati ya makazi ya watu. Wakatwaa eneo, migogoro ikaanza tangia mwaka 1994. Mauaji kila mwaka, tena siyo kila mwaka, karibia kila siku na juzi tarehe 7 mwezi huu umesikia ndiyo mauaji ya mwisho yametokea. Wananchi wale tumebadilisha uchumi wao, hatutaki kuwaandalia njia mbadala, hatujawapa hata mita moja. Nimesoma hapa Profesa uje ufafanue, umesema kwenye ukurasa wa 50 kwamba mmewatengea eneo, liko wapi? Hilo eneo mmewapa wachimbaji wapi? Kwa sababu mimi na wewe tulikuwa pale na demand yao ni hii na mimi najua hujatoa taarifa, hujapeleka taarifa ile kwa wananchi lakini umesema ukurasa wa 50 kuna eneo limetengwa kwa wachimbaji wale, akina nani? Hilo eneo halipo na hii ndiyo imekuwa mgogoro siku zote Profesa, pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka kuingia pale wachukue kwa sababu hawawezi kufa kwa njaa, wakati mali yao wanachukua wazungu wanaondoka nayo, haiwezekani, ni lazima kutafuta suluhu. Tangia mwaka 1994 Watanzania wenzetu zaidi ya 400 wameuawa pale mgodini. Watu wamebaki na vilema vya maisha, wengi tu ambao hawana idadi. Na hili suala ni suala ambalo kama hatutatatua kwa kuwapa wananchi eneo la kuchimba, hakuna suluhu pale. Wale wazungu wametumia shilingi bilioni 21 kujenga ukuta, yaani badala ya kutengeneza mahusiano na wananchi kwa kupeleka hizo pesa kwenye maendeleo wamejenga ukuta zaidi ya kilometa 10 na kitu, shilingi bilioni 21 ukuta mrefu na bado haiwi suluhu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mkuu wa Wilaya anasema kwamba mtu aliyepigwa risasi alikuwa ameenda rompad kuiba madini. Eti anasema rompad kuna madini. Mimi nimefanya kazi pale mgodini Nyamongo, rompad hawaweki madini, wanaweka mawe na mawe yanakuwa pale zaidi ya tani 2,000, 3,000. Mtu anaenda na kamkoba kuchukua jiwe pale ambalo halifiki hata kilo moja unampiga risasi una-justify kifo chake eti alikuwa ameenda rompad kuchukua madini, hata hajui amekurupuka tu. Mkuu wa Mkoa anakuja bila heshima anasema waliopigwa risasi ni wahuni kwamba wananchi wa Tarime wanauawa halafu mnawaita wahuni? na nilitamani Waziri Mkuu awe hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutakubali kauli za aina hiyo kwa wananchi wa Tarime ambao mali yao imechukuliwa, inasafirishwa kila siku na Profesa hapa leo mimi nimekuwa mpole sana kwa sababu nategemea utatoa majibu ambayo ni positive, lakini kauli kama zile za Magesa Mulongo kwa watu wa Tarime na watu wa Mkoa wa Mara; Profesa wewe unajua sisi sio wanafiki – nyeupe ni nyeupe. Nilikuwa naona wengine wanakupongeza huko ambao tu walitumika mwaka jana kuku-crucify. Bora sisi ambao tumesema na msimamo wetu umebaki pale pale. Sisi si wanafiki. Wengine ooh Profesa tunashukuru Mungu amekuleta tena, hawa hawa! (Makofi/Vicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Profesa, ninakuomba tatua mgogoro wa watu wa Nyamongo. Nilipokuwa form two nasoma historia wanasema sababu zilizosababisha kukua kwa miji kama Johannesburg, ni kuwepo kwa madini pale. Lakini wewe umeenda Nyamongo pale hata mita moja ya lami tangu mwaka 1994 hakuna. Halafu mnataka Wakurya waendelee kupigia makofi mambo yale, madini yanaondoka. Tunabaki na mashimo, milima, unakuta vijana zaidi ya 2,000 wako kule juu ya mawe. Siku mgodi ukifungwa sijui watakwenda wapi? Mkoa wa Mara hautakalika. Serikali haioni, sisi tunaolia kila siku saidieni hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, Waziri Mkuu angekuwa hapa asikie, Waziri wa Mambo ya Ndani na Mawaziri wengine msikie. Mgodi unalipa mpaka askari, mimi naamini askari analipwa kulinda mwekezaji na analipwa na Serikali. Lakini mgodi sasa hivi unalipa askari kila siku shilingi 50,000, askari wanaokwenda kulinda ule mgodi na ndiyo maana wamekuwa loyal kwa mgodi. Mtu wa mgodi akiwaamrisha kupiga Mtanzania risasi wanapiga tu, hawajali. Askari wamekuwa wanyama pale. Juzi wanakwenda kwenye Kituo cha Afya, wanapiga risasi Kituo cha Afya? Kuna watu wanafanyiwa upasuaji pale, kuna watu wana pressure pale, wanapiga mpaka mama ambaye anachukua dawa pale, na Tanzania mambo haya mnaona ni sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema na hii ni kauli yangu na ni kweli tupu, lazima yale mauaji yakome pale. Yasipoisha askari wenu wale wataniua mimi, nawaambia ukweli. Wataniua mimi kabla sijamaliza Ubunge wangu. Siwezi kukubali tena waendelee kuua wananchi pale. Nitawapelekea wananchi laki moja pale, watatupiga risasi hawatatumaliza, watajiua wenyewe baadaye. Tangu mwaka 1994 Wakurya wanauawa kama wanyama hata Profesa Maghembe hapa ukigusa swala pale porini hawezi kukubali. Huyu hapa na TANAPA yake gusa swala mle ndani uone kama atakubali, sembuse mtu? Watu wanauawa kama wanyama halafu sisi tukae hapa tunapiga makofi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba Profesa tunaomba suala la wachimbaji wadogo lile lipatiwe ufumbuzi. Watu wapate eneo kwa sababu mzungu amekuja akawakuta wanachimba Nyabirama, amewakuta wanachimba pale Nyarugusu, amechukua lile eneo hamjatengea wananchi maeneo. Bila kufanya hivyo mgogoro ule hautaisha, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, tutaunda kamati na kamati. Achilia mbali DC amekwenda pale amehamisha mto, tulikuwa na wewe unaona pale, umemuhoji bila aibu DC anafanya maamuzi ya kuhamisha mto sasa ule mto mvua ikinyesha una flood kwenye mazao ya watu kwa sababu ya maslahi ya wazungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, DC anakuja pale siku mbili anajifanya mkali, wazungu wanamchukua wanamweka mfukoni tayari anaanza kuimba nyimbo za wazungu kama yule wa pale. Sasa hivi ukigusa mgodi anasema ua, ndiyo suluhu anayoona. Kwa hiyo ninakuomba Profesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili yale magari ya mgodi yanayosomba mafuta, tuko karibu kuyawekea magogo kuyazuia yasitembee kwenye barabara zetu, kwa sababu yale magari wazungu wale hawarekebishi barabara, Halmashauri tunahangaika na barabara kwa vifedha vyetu vidogo wao wanatembeza mzigo mkubwa. Kama wanataka warekebishe ile barabara yao ya chini ya mgodi, ile ya kule chini watembeze magari yao. Wakipita huku juu ntawahamasisha wananchi wataweka magogo watayapiga mawe. Hatuwezi kukubali watembeze pale, hawaleti hela pale wanataka watembeze, wanatembezaje magari kwenye barabara yetu pale? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, Profesa kuna uamuzi unaweza ukafanya ambao hautakusababisha upigiwe makofi sana…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Heche, muda wako umemalizika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili ni chombo cha wananchi na nataka niseme Bunge hili lingefanya kazi yake kama chombo cha wananchi na siyo vikao vya vyama, hii bajeti ya Mheshimiwa Maghembe ilikuwa haipiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri alikwenda kwenye tv anasema wafugaji wanatembea nyuma ya mikia ya ng‟ombe. Waziri anasema ng‟ombe hawana faida, kwanza faida yao Pato la Taifa wanachangia asilimia nne tu! Kwamba utalii sijui unachangia asilimia 22. Sasa unajiuliza hivi leo tungekuwa tumeondoa ng‟ombe wote katika nchi hii, kama sukari tu imetushinda kuagiza, nyama ninyi mngeweza kuagiza watu wakala nyama? Sukari peke yake imetushinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu kwenye ng‟ombe ni pesa, maziwa, kwato, kila kitu! unachotupa pale labda ni sauti tu peke yake. Kila kitu kwenye ng‟ombe ni pesa. Tumeshindwa wenyewe kusimamia ng‟ombe hawa, leo watu wanasimama kwenye Bunge la Watanzania wanasema ng‟ombe wanaharibu mazingira, kwamba mifugo inaharibu mazingira. Ni utafiti wa wapi huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Dar es Salaam watu wanatumia mkaa, nchi nzima ni mikaa. Watu wanakata miti kwa ajili ya mikaa, watu wanatumia nishati, tumeshindwa kupelekea watu nishati tunasema mifugo inaharibu mazingira. Hata mkiua ng‟ombe wote nchi hii halafu mkaacha watu wakaendela kutumia mkaa, nchi hii itakuwa jangwa. Pelekeeni watu nishati Dar es Salaam, pelekeeni watu nishati rahisi Arusha na Mwanza, Majiji matatu peke yake mki-control watu wasitumie mkaa kesho yake nchi hii itakuwa kijani tupu. Leo mnakuja kusema ng‟ombe anaharibu mazingira, ng‟ombe anakata mti? Hiyo haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Maghembe ukumbuke kwenye Bunge la Katiba aliwaita wafugaji nyumbani kwake akawanunulia chakula anawashawishi wapigie Katiba kura, leo unawaita kwamba wanaharibu, unasema ng‟ombe anaambukiza magonjwa, hauli nyama ya ng‟ombe wewe? Utakula pundamilia kila siku kweli? Hilo ni vyema likaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vimeingia kwenye migogoro na TANAPA na mbuga kwa sababu watu wa mbuga wana extend mipaka yao. Vijiji vya Nyanungu, Kegonga, vijiji vya Masanga, hivi vijiji mpaka mwaka 1963 vilikuwepo na vina GN! Baada ya mwaka 1963 mipaka ya mbuga imekuwa extended, ni migogoro kila siku watu wanauawa.
Mheshimiwa Waziri ninaomba Kata tatu hizo nilizozitaja, Kata ya Kwihancha, Kata ya Nyanungu, Kata ya Masanga - Gorong, I mean uende pale ukatatue ile mipaka, vile vijiji vilikuwa nje ya mbuga na mipaka ya TANAPA ndiyo imekuwa extended kufuata mwananchi na mnawahamisha hamna sehemu wanayochungia ndiyo maana inaleta migogoro. Kwa hiyo, hilo nilitaka niliseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo leo tungekuwa tuna Bunge la Wananchi tusingepitisha bajeti hii ni Operesheni Tokomeza. Nina picha hapa, naomba karatasi moja ije mezani kwako na nyingine iende kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 watu waliuawa, watu walichomewa nyumba zao, mifugo ilipigwa risasi, ng‟ombe anauawa, ng‟ombe anaua tembo. Mbuzi waliuawa, watu wakabaki wanalala nje, Bunge likaja likajadili hapa, mkasema watu walipwe fidia. Kuna watu waliuawa kinyama, panga linachomwa moto mtu anaambiwa akanyage kwenye panga, akikanyaga akitoa mguu nyama inabaki pale, watu walipigwa misumari. Bunge likaja likajadili hapa, hakuna kitu chochote mpaka sasa kilichozungumzwa kwenye bajeti hii ya Serikali kwamba hawa watu wanakwenda kulipwa vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali wanapokuja ku-wind up hapa watuambie hoja ya operesheni tokomeza, ambayo ilitokomeza watu wetu, watu maskini! Madiwani, Wenyeviti wa vijiji na mpaka leo majangili wakubwa hawajaguswa na operesheni hii. Hawakuguswa na hawajaguswa. Ninyi wote ni mashahidi mnakumbuka hapa, Al Jazeera walitangaza na BBC kwamba Rais wa China alipokuja Tanzania aliondoka na meno ya tembo. Hamkuwahi kukanusha. Wachina kila siku ndiyo wanakamatwa kwa sababu Serikali yetu inakwenda kupiga magoti kwa Wachina kila siku hamtaki kushughulika na Wachina. mnakuja kushughulika na watu wanyonge! watu maskini. Leo mnasema utalii, utalii huu, mimi sikatai kwamba utalii uwepo na unachangia kwenye Pato la Taifa lakini utalii unagusa mwananchi wa kawaida kule chini kweli kwa maisha yake? Mpaka pesa hizi zije kwenu, mje mzishushe ziende kwa wananchi, mzunguko wenu, mnaweza kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akiwa na matatizo atauza ng‟ombe wake, atatibu mke wake, atasomesha mtoto wake, atafanya maendeleo yake binafsi kwa pesa zake. Lakini pesa ambazo zinaingia Serikalini hatukatai, tunahitaji pesa hizi zije Serikalini, lakini ni lini mtazishusha ziende kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja kule kijijini? Ng‟ombe ana mfungamano au mifugo ina mfungamano na maisha ya watu moja kwa moja ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba anapokuja ku-wind up hapa Waziri atuambie, hatukatai wafugaji watengewe maeneo, wapate maeneo yao ya kulisha, lakini leo tusije hapa tunawapaka rangi kana kwamba wafugaji hawafuati sheria, wafugaji siyo watu wazuri, wafugaji wanahonga Mahakama, yaani kila anayesimama hapa, kuna watu wanafikiri ng‟ombe ni mdudu lakini nyama ya ng‟ombe wanataka kula. Wamesimama huku wanazungumza mpaka wanatetemeka, wanasema tupigwe risasi. Tupigwe risasi kwenye nchi yetu? Tuna kosa gani sisi? Sisi ndiyo tunawaletea nyama mnakula kila siku hapa kantini nawaona pale mnabugia nyama, supu, makongoro sijui nini, yanatoka kwenye ng‟ombe hayo na maziwa, usipoletewa chai ya maziwa unalalamika, unafikiri maziwa ya mbwa hayo? Hayo ni maziwa ya ng‟ombe ni lazima yatoke kwenye ng‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba watu wasizungumze hapa kudhalilisha watu wengine na wakazungumza kana kwamba hii nchi ni ya kwao peke yao. Hatukatai tunahitaji wakulima walime, tunahitaji na wafugaji tupewe nafasi ya kufuga katika nchi yetu.
Ninaomba sana Mheshimiwa Maghembe unapokuja hapa utuambie hawa watu waliouawa kwa mfano kule kwangu waliuawa Peter Maseya alipigwa vibaya sana na akauawa na familia yake mpaka sasa iko traumatized. Aliuawa Nicholas Wegesa Moserega, Mheshimiwa Waziri uje hapa utuambie nyumba zilizochomwa moto, ng‟ombe waliouawa kwenye Kata zile tatu zaidi ya ng‟ombe 184, uje utuambie majibu yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Majaji kwenda kuchunguza na mnachukua vitu hivi kwasababu mmeshawaona Watanzania ni wasahaulifu, mnachukua mnavitunza, mnaunda Tume, hamtoi majibu mnakalia yale majibu. Tunataka hayo majibu tuambiwe ni nini findings za hayo majibu na ni kwa vipi tunakwenda kuondoa matatizo yaliyojitokeza.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri isingekuwa sahihi sana kama Wabunge wengine ambavyo wamezungumza kuanza kuchangia kwenye mpango huu au mipango mingine yoyote ya Serikali kabla ya kufanya tathmini ya mpango uliokuwepo ambao tunaendelea nao sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye quarter ya pili ya bajeti, Halmashauri hazijapelekewa pesa, hazijapelekewa OC, watu wanalia, mnataka wakusanye mapato lakini hamjawawezesha kuweza kukusanya hayo mapato, kwa sababu bila OC sijui mnataka watu watembee kwa miguu kwenda kwenye minada kukusanya pesa, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema hivi, mimi sio mtabiri, lakini nataka nikuambie Waziri Mpango baada ya Waziri aliyetumbuliwa hapa unamkumbuka, anayefuata ni wewe, wewe ndio utakuwa wa pili kutumbuliwa na Mheshimiwa Rais Magufuli. Na kwa nini utakuwa wa pili ni kwa sababu mambo yanapokwama, mipango mliyopanga yote inapokwama wewe ndio utabebeshwa zigo hilo ili aonekane yeye yupo sawa wakati mnakosea wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira; mnaleta hapa kuzungumza mipango hii, mlisema hamuajiri kwa sababu mnafanya tathmini ya watumishi sijui kutafuta watumishi hewa, haya mmetafuta hewa mwaka mzima, vijana wamesomeshwa na baba zao watu maskini wako mitaani, dada zetu wanajiuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo nayo sijui mnatafuta wanafunzi hewa. Kilimo hakuna pembejeo mnatafuta majembe hewa, mnatafuta wakulima hewa? Jambo la msingi ni kwamba mseme Serikali yenu imefilisika na haiweze kutekeleza chochote msaidiwe kuliko mnakuja hapa mnasema watumishi hewa, watumishi hewa mnatafuta mwaka mzima, wakulima hewa mnatafuta mwaka mzima, kilimo kimesimama. Wanafunzi mkawapa mikopo mwaka jana, mambo ya aibu kweli kweli! mwaka jana tumewapa mkopo leo mtu anaingia mwaka wa pili hamtaki kumpa mkopo, wengine wanaingia mwaka wa tatu hamtaki kuwapa mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yenu hii mlitoa matumaini mnasema hapa kazi tu, hapa kazi nini sasa watu hawana mikopo wanafunzi wanalia, mnatoa mtoto kijijini anakwenda chuo anafika pale hana pa kuishi, hakuna mkopo, ni matatizo kwenye familia. Sasa mimi nakutabiria Mpango unakaribia sana kutumbuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu; elimu yetu wakati anazungumza pale Mheshimiwa Mapunda, amesema vitu vinne ambavyo vinahitajika kuwepo kwa viwanda amezungumzia personnel au man power, ni man power ya aina gani ambayo imeelimika ili iweze kuajiriwa kwenye hivyo viwanda?
Leo elimu ni majanga; mama yangu Profesa Ndalichako mimi nilikuwa nakuheshimu sana ukiwa Katibu wa Baraza; umewahi kutoka pale unaonesha watu wamechora ma-zombie kwenye mitihani, wewe umepewa Wizara hii umechora zombie kubwa kuliko wale wanafunzi. Na sijui hata wizi wa mitihani utazuiaje kama wewe Profesa ulitoka hapa kwenda kuiba kura Kinondoni, sijui. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu hivi baada ya wewe kutoka hapo na Uprofesa wako na ni kwa nia njema tu, kwa sababu hili Bunge mmelifanya kama idara fulani ya pale Ikulu labda hata ya umwagiliaji maji pale, kumwagilia maua ndio maana leo Wabunge wanasimama hapa wanasema ukweli hali halisi ya uchumi ni mbaya, wengine wanasimama wanatetea. Jana tu walikuwa wanazungumza hapa wanapiga makofi, sasa hivi wamegeukana na mimi nilijua hamtafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya uchumi ni mbaya hata kwenye kununua vocha tu, ukinunua vocha ulikuwa unapewa GB sita leo ni GB 2.5 kwa shilingi 10,000; yaani hata mtu ambaye hajaenda shule anajua. Kwahiyo, hali ya mazingira ya mtaani elimu inazidi kuporomoka.
Tumetengeneza madawati tumepeleka, maeneo mengine madawati yapo nje yananyeshewa hapa kwenye mpango hamjaonesha mkakati wowote wa kujenga vyumba vya madarasa ili yale madawati tuliyopeleka yaingizwe ndani, yataoza kwenye miti, mwakani tena tuanze kukamatana kupambana na watu wanunue madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwenye elimu hapa Profesa Ndalichako ungekuja na mpango ambao utaondoa elimu yetu hii kwenye mkwamo, ambao tutajua kutakuwepo na maandishi yanayoeleweka kwamba elimu tunayoenda nayo ni ya aina hii, tutoke kwenye elimu ile ya akina Mungai ambayo tulikuwa tunaunganisha hesabu sijui na historia na wewe unaendelea huko huko. Leo mnafanya hivi kesho mnafanya hivi, keshokutwa mnatoa vigezo hivi, siku nyingine mnatoa vigezo hivi. Mimi nawaasa vijana Watanzania wote ambao Serikali hii imewatosa haitaki kuwapa mikopo wajue wana nguvu nyingi sana za kuunganisha kura yao ili mwaka 2020 waondoe Serikali hii kwa sababu hakuna matumaini katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda; amezungumza vizuri sana Mheshimiwa Chegeni hilo ndio jina la yule bwana sio sisi tunaosema ni wananchi. Ukikutana naye hapo nje ukamsimamisha Waziri vipi, nikupe kiwanda? Anaingiza mkono mfukoni, anataka kuchomoa kiwanda mfukoni akukabidhi. (Makofi/Kicheko)
Mpango wenu hamjajenga kiwanda hata kimoja mpaka sasa, mmebaki mkisikia Bakhresa anataka kufungua kiwanda mnakimbia pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda Mheshimiwa Waziri Mpango wewe unajua, ni msomi na uwe unasikiliza watu hapo unaelewa. Kiwanda ndiyo kinaajiri kuanzia mama lishe mpaka engineer kiwandani peke yake. Kwa sababu mama lishe atakuwa pale atawauzia wabeba mizigo wa viwandani, atawauzia madereva wanaobeba mizigo kwenye kiwanda. Kiwanda kitaajiri engineer wa kuendesha mitambo, kiwanda kitaajiri mhasibu, kiwanda kitaajiri kila mtu.
Leo umekuja hapa, kwanza ninyi wenyewe Serikali hii ambayo sasa inataka kufuta eti siyo yenyewe, Serikali hii ya CCM ikaua viwanda, ikauza viwanda. Mmerudi mmeimba Serikali ya viwanda, leo tunaelekea mwaka mmoja na siku kadhaa hata kiwanda cha pini hamna mpango nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkisikia Bakhresa anazindua kiwanda chake mnakimbia pale mnasema sukari tuliyokunyang‟anya tunakurudishia na shamba tunakupa zawadi. Halafu mnatoka pale kwamba tumefungua kiwanda. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa mnakataa hapa kwamba Serikali haijaishiwa kuna taarifa mnatisha wafanyabiashara, mtu amelipa ushuru ana risiti mnamwambia hizo ni risiti fake, Serikali iliyokuwepo ilikuwa inatoa risiti fake. Mnawalipisha watu kodi mara mbili.
Leo Benki zinatangaza hasara, wewe ni msomi utuambie nini implication ya benki kutangaza hasara, CRDB wamesema, nini implication yake kiuchumi? Maana msituambie tu kwamba uchumi unakuwa vizuri, uchumi unakuwa vizuri watu wanalia mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmewaruhusu traffic, Wabunge walikuwa wanalia hapa kila traffic ameambiwa kwamba kwa siku ni lazima apeleke makosa matatu. Leo makosa ya barabarani ni chanzo cha uchumi kwa Serikali ya CCM, aibu. Makosa ambayo yanatakiwa kuzuiwa watu wasifanye makosa ninyi mna-encourage ili mpate uchumi….
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Kuhusu Utaratibu!..
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba unilinde kidogo muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Leo wakuu wa traffic nchi nzima wanatangaza mapato yaliyopatikana kutokana na makosa kwamba mwezi wa tisa tumepata bilioni kadhaa kutokana na makosa, nini maana yake? Kama hamu-cherish yale makosa kwamba ni chanzo cha mapato cha Serikali hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa yale nafikiri yamewekwa ku-discourage watu kuendelea kufanya makosa, lakini unapotangaza unajisifu kwamba ma-traffic wamekamata makosa kadhaa ina maana ni chanzo mmeweka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema siyo kwa nia mbaya ni kwa ajili ya kuwaambia hawa watu wasikie waelewe kwamba waliambiwa hapa tukikosa mapato yanayotokana na bandari mtaanza kufukuzana na bodaboda, watu walisema humu mkatuzomea. Sasa leo tunaposema haya hamtaki tena, mnataka tukae wapi? Tukisema hili ninyi kwenu baya, tukija hapa ninyi kwenu baya mnataka nini sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaambia mkipoteza mizigo nchi hii haitawezekana. Leo eti TRA wanataka wawe TRA ya Congo pia wamesema Wabunge wengine hapa, yaani mnataka kujipa majukumu ya kukusanyia Congo kodi. Kwani kama Congo kule wanakwepa kodi ninyi inawahusu nini? Wamepitisha hapa, wamewalipa mapato yenu, mnachukua mnafanyiakazi, mnataka kuwakusanyia Congo ili wawape nini? Mmekuja hapa mnaongea na Rais wa Congo anawahakikishia mizigo itaongezeka, imeongezeka? Kwa sababu hana mandate ya kuwaambia wafanyabiashara lazima wapitie hapa na wao wamehamia Beira, wamehamia Mombasa sasa wote tunapiga miayo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunadanganyana tumepandisha bajeti kutoka shilingi trilioni 22 desperately kabisa kwenda shilingi trilioni 29 eti mnataka hadi Mama Lishe alipe kodi, Mheshimiwa Mpango, mama lishe alipe kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana mnawaambia hawana ajira eti wajiajiri, wewe mwenyewe umeshindwa kujiajiri umeomba Ubunge hapa unataka kijana wa mtaani ajiajiri. Wabunge wote hawa tumeshindwa kujiajiri tukaenda kuomba ajira kwa wananchi, wengine Profesa sijui na nini. Kijana aliyemaliza mwaka wa kwanza mnamwambia nenda ujiajiri kule! Vijana hawawezi kutengeneza ajira!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la Serikali yoyote duniani kulinda watu wake na ni aibu kwamba leo nchi hii wakati wa hapa kazi tu hakuna madawa kwenye mahospitali; miradi yote mliyoweka ya kielelezo haiendi, barabara hamtengenezi tena na wengine hapa walikuwa wanaitukana Serikali ya…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nashukuru kupata nafasi hii na namshukuru sana Mheshimiwa Paresso kwa kunipa muda wake nitumie kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niseme mambo machache na niseme pale Wabunge wenzangu walipoishia. Tatizo kubwa ninaloliona mimi hasa kwenye uendeshaji wa Serikali za Mitaa ambazo kimsingi ni Serikali kamili, zimepewa mamlaka yake Kikatiba. Leo kila mtu aliyesimama hapa analalamika, aidha, kwa Wakuu wa Wilaya au Wakuu wa Mikoa kuingilia mamlaka za Halmashauri. Hii inafanyika kwa sababu kila mtu anafukuzia kumfurahisha bosi, Mtukufu Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani watu wanafanya madudu pale na imekuwa utaratibu kwamba watu waliofanya madudu wanapandishwa cheo. Sasa na wengine kule Wilayani anatafuta na yeye nitoke vipi. Mkuu wa Wilaya anatembea nyuma kuna kamera utafikiri anaenda sijui kufanya shooting? Mkuu wa Mkoa naye akitembea nyuma kuna kamera, nionekane huko, Mtukufu anione jioni kwenye taarifa, matokeo yake ni kwamba tunaua Serikali za Mitaa. Tunaendesha nchi hii kama duka. Unajua ukiwa na duka asubuhi unasema ile paketi ya sigara iliyokuwa hapa iko wapi, inatafutwa. Ndiyo hayo yanayotuletea matatizo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa Diwani, leo Madiwani wote wazuri wanakataa kugombea na hili Mheshimiwa Simbachawene unalijua, watu wazuri wanakataa kugombea kwa sababu hawalipwi mshahara, wanalipwa posho. Leo hata ile posho ambayo wanalipwa, Mkuu wa Mkoa anaona ni shida anaenda kuwaondolea posho Madiwani wakati yeye mwisho wa mwezi analipwa mshahara. Kama yeye ni mzalendo kiasi hicho kwa nini asiache mshahara wake? Sasa hii ndiyo level ya unafiki ambayo tunaiwea hapa kwamba Mkuu wa Mkoa anataka kuondoa posho ya Madiwani wakati yeye analipwa mshahara, wao hawana mshahara na mnataka wasimamie fedha ambazo mnapeleka Halmashauri, haitawezekana. Ni lazima tuweke heshima kwa Madiwani, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili fedha zote zinazopelekwa Halmashauri zinakwenda kwenye vijiji, vitongoji, kule ndiyo kuna watu. Serikali hii ya CCM tumeimba miaka yote kwa nini hamtaki kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji fedha kama malipo? Hakuna anayetoa majibu. Wenyeviti hawa wa Vijiji ambao wanafanya kazi kwa hisani kila siku utasikia Mkuu wa Mkoa nimekufukuza kazi, nimewaweka ndani, unawekaje mtu ndani kwa vitisho ambaye humlipi hata senti tano? Kwa hiyo, mimi nafikiri tuliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za CAG kufanya ukaguzi. Nyie wenyewe mnasema mnataka kutumbua majipu, kumbe ni unafiki mnataka kujificha madudu yenu myafichie ndani humo. Kheri Mheshimiwa Kikwete aliyeweka wazi watu wakajua, ninyi mnaficha hamtaki kujulikana maovu yanayofanywa, mnamnyima CAG fedha. Wananchi wa nchi hii wajue kwamba Serikali hii ni Serikali isiyotaka kukosolewa ndiyo maana haimpi hata CAG fedha ili aende akakague aone hawa Wakuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya mliyopeleka, walioshindwa kura za maoni za CCM madudu watakayofanya kwa miaka hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wote mliopeleka ni wale walioshindwa kura za maoni za CCM yaani bora wangewachukua ninyi mlioshinda wakawapeleka kuwa Wakurugenzi kuliko kuchukua mtu aliyeshindwa, amekataliwa na wanachama wenzake kwamba wewe huwezi kuongoza, halafu unamchukua unampeleka eti kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri matokeo yake hajui chochote anayochotakiwa kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitatumia muda wangu kuharibu kwa kumjibu yule najua anachofukuzia nitaharibu sana. Naomba niendelee. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Hifadhi za Jamii watu wameweka fedha zao, wewe unakatwa mshahara wako unaenda pale. Leo inasemekana fedha hizi zilipopelekwa Benki Kuu mmechukua mmeenda kununulia Bombardier, mnawakataza watu kuchukua fedha zao ambazo wamehifadhi. Yaani kijana amefanya kazi mgodini, ameteseka maisha yake amehifadhi kule, anataka kujitoa au amefukuzwa kazi achukue fedha ajengee watoto wake, mnamwambia mpaka miaka 60. Mnamkataba na maisha? Akifia hapa katikati huko mtampa nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa matokeo haya ya kuchukua fedha ambapo tunaendesha nchi kama duka, kila kitu mnataka kiwe centralized, Halmashauri mnaua, Mifuko ya Hifadhi za Jamii mnaingilia, kila kitu na fedha mpaka za wananchi wa kawaida mnataka muwe mnachukua kwenye mifuko yao, ni lazima ikome.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakusukuru kwa sababu hata nikianza hii hoja hautanivulimia, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa nami niweze kuchangia kwenye muswada huu wa upatikanaji wa taarifa. Sasa kumekuwa na contradiction kubwa sana hapa, wengine wanasema Muswada wa Upatikanaji wa Habari, wengine Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa. Ni kwa sababu mambo haya yalivyokuja yalikuja kinyumenyume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baadaye tutamhitaji Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe atuambie ni nini hasa ambacho walikusudia kuleta kwa sababu mwanzoni hata kwenye Order Paper ilivyoonekana ni tofauti na tunavyoijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ni yetu sote. Wakati fulani kuna mambo ya msingi yanaletwa hapa, lakini watu wakitaka kuyajadili wanakwekwa na watu wengine baadaye wa kujibu vijembe, wanatoa vijembe upande wa pili bila kusikiliza kile watu wengine tunachokisema. Hata hapa tunajua kwamba kuna watu wameandaliwa, baadaye watachomekwa tu ili waje kushambulia yale tunayozungumza. Mimi sijali, nataka nizungumze na nishauri. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ikitolewa ndiyo inasababisha upatikanaji wa habari. Sasa taarifa ikiwa imetolewa, ikienda kwa public inakuwa habari.
Sasa huu Muswada wa upatikanaji wa taarifa ambao mwisho itakuwa habari umekuja wakati ambapo Taifa letu lipo kwenye majaribu makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye wakati ambao tunajadili Muswada huu ambao kuna mtu mmoja, tunapokuja hapa tunapitisha bajeti yeye anakwenda anapitisha yake huko mtaani. Kama jana mliangalia vyombo vya habari vingi vilionesha, Mheshimiwa Rais alikuwa pale Magomeni, anasema atatoa shilingi bilioni kumi kujenga nyumba pale ambazo hatukupitisha kwenye bajeti. Kwa hiyo, hii ni test kubwa sana kwa sheria zetu. Unakuja wakati ambao sheria inaonekana siyo muhimu kwa Taifa hili. Muswada huu unakuja wakati ambao tunajadili mambo hapa, tunayapitisha yanaenda yanapindishwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tupo katika wakati ambao nafikiri na wananchi wenzangu wafuatilie haya. Je, kuna sababu zozote za Bunge hili kuwa linakaa hapa katika kipindi kama hiki au vipindi hata vya bajeti likatumia mabilioni ya pesa za Watanzania tukajadili jambo ambalo tunajua hatutalifanyia kazi? At least kwenye hii kwa sababu ina vipengele vingi vya kukandamiza, najua hii mnaweza kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo yupo Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, mwanasheria nguli, yupo Mwanasheria wa Serikali hapa, sheria zinapindishwa; watu wamezuiliwa kufanya mikutano kinyume cha sheria; Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo, kaka yangu Masaju tena anatoka Mkoa wa Mara. Sasa watu wa Mkoa wa Mara sisi huwa hatuogopi kusema ukweli na kushauri pale panapostahili. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe yupo, mwanasheria nguli, lakini wote hao wanapiga makofi tu; wanampigia mtu mmoja makofi ambaye anavunja sheria hizi. Sasa ndiyo najiuliza, hivi kuna sababu gani ya kukaa hapa, tukatumia pesa nyingi kujadili mambo ambayo tunajua mwisho wa siku hatutayafanyia kazi kama hii sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye huu muswada. Ukija kwenye kipengele cha 6(6) wamezungumza wenzangu; “mtu yeyote atakayetoa taarifa iliyozuiliwa kinyume cha mamlaka ya umma kisheria hii, atatenda kosa na endapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo cha miaka 15 au 20.” Yaani mtu ametoa taarifa ambayo inakwenda kuwa habari kwa wananchi na Katiba hii Ibara ya 18(c) imetamka kabisa kwamba wananchi wana haki ya kupata habari, mnamfunga miaka 20 Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, huyu mtu ameua mpaka mumfunge miaka yote hiyo? Yaani kwa kutoa taarifa tu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkisema taarifa za Usalama wa Taifa, taarifa za Majeshi; hizo sisi hatuna tatizo nazo; lakini taarifa, leo hata Mtendaji wa Kijiji akizuia taarifa sisi tukaitoa, kwa hiyo tufungwe miaka 20. Sasa nafikiri hii siyo sahihi.Ni lazima unapokuja Dkt. Mwakyembe uoneshe Udaktari wako hapa.
Usiunde tu watu nyumanyuma kuja kujibu hapa vijembe. Rekodi hizi zitabaki kwenye vitabu vya Bunge hili na watu wengine watakuja wasome wakati sisi hatupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha 19(3) unasema mtu yeyote ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa Mkuu wa Taasisi uliofanywa, yaani ya kunyimwa taarifa, hajaridhishwa. Mimi nimekwenda nimenyimwa taarifa na Katibu Mkuu wako, sijaridhika, nikate rufaa kwako, yaani hii ni sawa na ile waswahili wanasema kesi ya ngedere unampelekea nyani. Hakuna kitakachopatikana hapa. Kwa hiyo, hivi vitu ni lazima kama kunatakiwa kuwepo na checks and balances muweke vyombo vingine ambavyo ni huru viweze kuwahoji au kuwalazimisha ninyi mtoe taarifa hizi ambazo zina manufaa ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unataka wewe mtu wa chini yako amekunyima taarifa na katika kipindi hiki ambacho nyie ni waoga vibaya sana, akishasema kule hata kama mnajua imevunjwa Katiba mpo kimya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwona pale kaka yangu Mheshimiwa Masaju na amekuja hapa alivyokuwa anahangaika Mwanasheria mzima kutetea uovu anashindwa; wanahabari wanambana hivi anasema hivi; aibu tupu, kwa sababu tu sheria zipo lakini hamtaki kuzifuata sheria hizi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona siyo sawa kwamba mtu wa chini ameshindwa, tukate rufaa kwako sijui na kwa mtu wa juu yake, hii naona siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 21 kinasema eti mmiliki wa taarifa ambaye maombi ya kupata taarifa yatatumwa kwake anaweza kutozwa ada iliyowekwa kwa ajili ya kutoa hiyo taarifa. Yaani kweli Katiba inasema ni haki ya mwananchi kupata habari na taarifa kwa mambo muhimu yanayohusu nchi yake, leo mnatuambia mtuuzie taarifa, yaani mnataka kweli kabisa Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe umeweka hapa kwamba taarifa inunuliwe, yaani vyombo vya habari vinataka taarifa za Serikali wawatangazie ninyi wananchi wajue mnachofanya, mnataka eti wanunue kutoka kwenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa nini tunatengeneza vitu vya aina hii? Mimi huwa nakaa najiuliza na wakati mwingine mnatunga haya mambo kama mnatukomoa sisi; lakini waangalieni wenzenu akina Basil Pesambili Mramba na wenzake, walikuwa Wabunge humu na Mawaziri tena waliokuwa wanaheshimika. Sasa hivi wananyea ndoo. Akina Harry Kitilya walikuwa watu wakubwa kwenye nchi hii, lakini wako mle ndani sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mnapotunga hivi vitu kama mnafikiria kukomoa watu, muwe mnawaza pia kwamba ipo siku kama historia haitawahukumu nyie wenyewe, watoto wenu hawatakuwa na nafasi hizo mlizonazo au wajukuu zenu hawatapata nafasi hizo mlizonazo, watakutana na mambo haya ya ajabu mliyoyaweka kwa ajili ya kubana watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nipo hapa kushauri na tunashauri kwa nia njema. Mmwambie hata Mheshimiwa Rais na ninyi wote humu mnajua na mnalalamika. Hatuwezi kuwa na Rais ambaye akienda huku, watu tunashika vichwa, leo atasema nini? Yaani hatuelewi! Anakuwa Zanzibar anasema watu watafia kwenye madimbwi ya maji.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaona maturity yako, nakushukuru sana, kwa sababu watu wengine wako humu wanafikiri tukimtaja Mheshimiwa Rais tunamchukia. Hatumchukii, sasa namtaja kwa Utukufu wake, Mheshimiwa Mtukufu Rais. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema, akienda sehemu hatujui ataongea nini; juzi, Mheshimiwa Ummy alikuwa hapa anakanusha taarifa, amesema watu wazae tu. Mheshimiwa Ummy amekanusha; sasa hilo lilikuwa linajulikana ataongea nini? Mtukufu Rais amesema, machinga waingie popote, Mheshimiwa Simbachawene yule pale, akakanusha juzi tu. Labda watu hawa hawana kumbukumbu na hawafuatilii. Ndiyo maana tunasema wala siyo kwa nia ya kurushiana vijembe wala kudhihaki mtu. Tunasema Taifa hili ni lazima tuliweke kwenye utaratibu wa kisheria na mambo yote yawe kwenye chain ya sheria na Katiba ili kila mtu ajue kwamba nikivuka mipaka hii, awe Mheshimiwa Rais, awe Mtukufu Rais kwa sababu nikisema Rais napigiwa kelele; awe nani, ajue nikivuka mipaka hii, sheria za nchi yetu hazitakubali, Katiba ya nchi yangu haitakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yake, kuacha mambo yanajiendea, ndiyo maana unaona hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Makonda anatoa amri eti Mikoa yote tarehe moja ipande miti, yaani Makonda naye ni Rais kwenye nchi hii! Uropokaji wa ajabu! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sheria zinaeleza tuendesheje nchi; mtu anakaa Dar es Salaam kwa sababu amesifiwa mara mbili, amejiona na yeye ni kila kitu, anatoa amri; tarehe 1 mwezi Oktoba watu wote wapande miti nchi nzima. Na yeye anatembea na Wanajeshi, ana Polisi. Sasa tukisema haya hatusemi kwa nia mbaya, tunasema kwamba tunakaa hapa tunatunga sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mnaaibisha professional zenu, yaani mnatia aibu! Hii nchi inatia aibu kweli kweli! Wasomi wa Vyuo Vikuu hawazungumzi, wako kimya…
MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako.