Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John Wegesa Heche (25 total)

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka niseme nimesikitika sana kwa majibu yaliyotolewa na Serikali na nataka niwahakikishie Bunge lako kwamba wananchi wa Tarime hawatakubaliana na hali hii. Nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mhesimiwa Spika, katika sehemu ya kwanza ya majibu yaliyotolewa na Serikali, maeneo yote yaliyotajwa hapo, yalifanyiwa tathmini na mgodi wa North Mara na wakati fulani hivi baada ya tathmini, mgodi ulikwenda mbele zaidi kufyeka mazao ya wananchi na Mheshimiwa Spika kwa mujibu wa sheria ya madini, wananchi wanatakiwa wakae umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo uchimbaji unafanyika.

Mheshimiwa Spika, wakati wote wananchi walipofanyiwa tathmini wamezuiliwa kuendeleza maeneo yao, mashamba yao yameharibika, nyumba zimebomoka na nyingi zimebomoka kutokana na blasting inayofanywa na mgodi lakini naambiwa hapa kwamba hawatalipwa wakati walifanyiwa tathmini.
Sasa swali langu ni hili, ni kwa nini mgodi ulifanyia tathmini nyumba, maeneo na mazao ya watu na kuzuia kuyaendeleza na sasa inasema kwamba haiwezi kulipa wakati ilifanyia tathmini yaani evaluation?

Swali la pili, haya majibu ya kukurupuka yasiyo na research, Serikali imesema kwamba wanalipa kwa mujibu wa viwango na North Mara inalipa fidia kubwa kweli kuliko ya Serikali, sasa mimi nina cheque hapa mbili za wananchi wa Tarime waliolipwa na haya ni matusi!

Mheshimiwa Spika, Nyamakaya Mbusiro amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 3,871/= kama fidia ya shamba lake na nitawasilisha mezani kwako, cheque ya pili Chacha Muhabe Mwita amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 7,273/= na ni nyingi mno, mashamba ya wananchi masikini. Nauli ya kutoka eneo la Nyamongo, Nyamwaga mpaka kufika Tarime Mjini ni shilingi 15,000/=.

Je, hii fidia ndiyo Serikali ya CCM inawaambia wananchi kwamba ni kubwa kuliko viwango ambavyo vinatakiwa kulipwa?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mambo ya fidia ya Nyamongo historia yake imeanza toka miaka ya 1980 na Mheshimiwa Mbunge atastaafu bado madeni yale yakiwepo. (Makofi)

Mimi mwenyewe nimekaa na wenyeji pale, kuna kitu kinaitwa ‘mtegesho’ na mtegesho umefanywa hata na wafanyakazi wa Serikali.

Kuna mtu anakuwa na nyumba, anamkaribisha mtu, watu wamejenga nyumba za thamani hata ya milioni 200 wakitegea mgodi uwalipe. Nimefanya vikao wakati ule na wenyeji wa Tarime, wenyewe baadaye wakasema hawa wenye mitegesho ndiyo wanakuja kuharibu taratibu za hayo malipo.

Kwa hiyo, hayo mashamba na hiyo ni kwamba tathmini ilifanyika na niliitisha kikao nikiwa na DC na wenyeji wananchi wa pale, nikaleta na wazee nikajaribu hata kuweka viongozi wa madhebu ya dini, Mheshimiwa Heche tumeongea naye nikasema baada ya Bunge suala la Nyamongo itabidi tuende tukae pale kama siku tano na itakuwa ya ukweli.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Heche asiondoke tutaenda, hayo mashamba saa zingine ni mtu anatafuta kaeneo, anaweka mimea usiku, asubuhi anataka tathmini ndiyo maana inakuja shilingi 3,000/=.

Kwa hiyo, kutatua tatizo la Nyamongo, itabidi mimi, Mheshimiwa Heche, DC, wale wananchi na viongozi wenyewe twende eneo moja baada ya lingine.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitambue jitihada ambazo zimefanywa na Waziri, Mheshimiwa Muhongo katika kujaribu ku-ssetle down issue hii na wananchi wa Tarime wanasubiria kwa hamu sana majibu yake kuhusu malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, niulize maswali mawili ya nyongeza. Nataka Waziri atambue kwanza kwamba neno „mongo’ siyo neno la siku moja, ni neno la Kikurya lenye maana ya sehemu ya kutunza mali. Kwa hiyo, mgodi ule upo enzi na enzi na watu wa pale wametegemea maisha hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo Waziri anakuja na jibu hapa, siku moja nilimwambia awe anafanya research, anasema hakuna mkataba wowote ambao kijiji kinaingia na mgodi. Mimi nina mikataba ya Serikali ya Vijiji hivi, hii hapa ya mwaka 1995 ambayo mgodi uliingia na Serikali za Vijiji alivyovitaja hapo kwamba kwenye kila uchimbaji watakuwa wanatoa asilimia moja kama royalty kwenye Serikali za Vijiji. Hizi fedha zimesomesha watoto wetu pale, zimejenga shule na maisha ya vijiji vile wamekuwa wakifaidika na pesa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tangu waanze kwenda underground wameacha kulipa royalty kwenye Serikali za Vijiji. Nataka Waziri atuambie ni lini mnauamuru mgodi huu uanze kulipa royalty, kwa sababu mnasema hauchimbi kwenye eneo la kijiji lakini pamoja na underground wako eneo la kijiji, hawako Singida wala hawako Mwanza, wako Tarime. Kwa hiyo, nataka majibu hayo atuambie ni lini wanaanza kulipa hiyo royality? Mkataba husika nitawapa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Naibu Waziri wa Mazingira tangu mwezi wa Pili amekuja akachukua pale sample za maji na kwa wiki nzima hii pit ya Gokona imekuwa ikimwaga maji kwenye Mto Tigite ambapo watu wanalalamikia kwamba yana sumu na yanaathiri mali zao. Sasa nataka Waziri atoe kauli kuhusiana na hili kwamba pit ya Gokona sasa inamwaga maji kwenye Mto ule na yanaathiri maisha ya watu pale, mifugo na jamii nzima. Nataka atoe kauli kuhusiana na suala hilo ambalo linafanyika kwa wiki nzima sasa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Mheshimwa Heche, kwamba neno mongo ni utajiri kule kwao na kuhila ni utajiri kule kwetu Usukumani, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu sasa kwa weledi sana swali lake la kwanza. Nimsahihishe kidogo Mheshimiwa Heche, mikataba iliyoingiwa kati ya vijiji saba pamoja na mgodi wa Acacia ni mkataba wa malipo ya royalty siyo mikataba ya uchimbaji. Hilo ni suala la msingi sana Mheshimiwa Heche na Waheshimiwa Wabunge kulielewa. Pamoja na hayo, nikubali tu kwamba ule mkataba ulioingiwa kati ya vijiji na mgodi ambapo kila kijiji kinalipwa royalty asilimia moja bado unaendelea na wataendelea kulipwa kwa mujibu wa mikataba ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye swali lake la pili, inaonekana kwamba mtaalam wa NEMC ameenda kuangalia kwenye Mto Gokona na kuona kwamba kuna athari za mazingira. Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Waziri wangu tarehe 22/2/2016 aliunda Kamati Maalum ya kufanya uchunguzi wa matatizo yote katika Mgodi wa North Mara. Katika Kamati ya watu 27 iliyoundwa Mheshimiwa Heche ametoa wawakilishi wake wanne. Kwanza, Mheshimiwa Heche tunakupongeza sana kwa kutuma wawakilishi wako wanne kwenye Kamati ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza masuala yote ya Mgodi wa North Mara ikiwa ni pamoja na matatizo ya kimazingira ina ToR (Hadidu za Rejea) 27. Kati ya hizo, tano zinahusiana na matatizo ya athari ya mazingira kwenye Mto Gokona. Kwa hiyo, naamini kwamba taarifa itakapokuja na imeshakuja tunaifanyia kazi, utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati hiyo yatatolewa na Mheshimiwa Heche atapewa maelekezo ya hatua za Serikali zilizochukuliwa.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima, wafugaji, mafundi na kila mmoja katika Taifa hili ambaye amefikia umri wa miaka 60 amelitumikia Taifa hili kwa njia mbalimbali. Wakulima ndio waliolima chakula ambacho kinaliwa na watumishi wa Serikali, kwa maana ya kwamba utumishi wao unakuwa pensionable baadaye. Wafugaji ndiyo waliofuga mifugo ambayo tunatumia maziwa, nyama na kila kitu. Wajenzi ndiyo waliojenga nyumba ambazo watumishi wa Serikali wanaishi, lakini Taifa hili limekuwa likilipa watumishi wa Serikali tu pensheni lakini watu wengine waliolitumikia Taifa hili kwa njia moja au nyingine hawalipwi pensheni na mpaka sasa Serikali imekuwa ni mchakato na nyimbo mbalimbali.
Je, Serikali inataka kutuambia kwamba hawa watu hawakuwa muhimu katika utumishi wao kwa Taifa hili ndio maana mpaka sasa hawajaanza kulipwa pensheni? (Makofi)
Swali la pili, wimbo wa mipango, michakato, maandalizi umekuwa ni wimbo wa kawaida katika nchi hii, nataka Waziri atuambie, ni lini sasa Serikali itaanza kulipa wazee hawa ili waache kuteseka, wengine mnaona wanauawa kule vijijini Usukumani huko kwamba ni wachawi kwa sababu tu hawana pesa za matumizi na wana...
MHE. ANTONY P. MAVUNDE - NAIBU WAZIRI (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inathamini mchango wa kila mmoja. Serikali inafahamu na inathamini mchango wa wazee wetu walioutoa katika ujenzi wa Taifa hili katika nyanja tofauti za kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kutekeleza mpango huu kwa wazee wote ambao wametumikia Taifa hili. Nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais na Ilani ya uchaguzi ya CCM inavyosema mpango huu utatekelezwa kwa ajili ya wale wote ambao walitoa mchango wao kwa Taifa hili bila ubaguzi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amezungumza ya kwamba imekuwa ikisemwa kila mara mipango, michakato na ni lini Serikali itatekeleza mpango huu. Suala hili la mpango wa pensheni kwa wazee ni suala ambalo lilikuwa linahitaji maandalizi ya kutosha na zipo taratibu ambazo zilikuwa zimekwishatekelezwa na imebaki hatua chache za kuweza kwenda kutekeleza mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mchakato huu zipo prerequisites ambazo lazima kwanza zitekelezwe na zifanyiwe kazi, huwezi kwenda tu moja kwa moja mpaka upitie katika utaratibu kwamba ni namna gani kuona mpango huu utatekelezeka. Nimtoe hofu kwamba ni dhamira ya Serikali lakini vilevile ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na hili litatekelezeka. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa majibu yaliyotolewa hapa na kwa niaba ya watu wa Ukerewe ambao Mbunge wao anaumwa ameniomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, barabara hii imeanza kujengwa mwaka 2013 mpaka leo ni zaidi ya miaka minne barabara iko asilimia 14 na Serikali inakiri hapa kwamba ujenzi unasuasua. Hii ni barabara inayounganisha Mkoa kwa Mkoa wala hata siyo Wilaya kwa Wilaya. Sasa ni lini au ni miaka mingapi, kwa sababu tukigawa hapa asilimia 85 iliyobaki ni miaka zaidi ya sita, ina maana mtoto azaliwe leo afikishe miaka sita aanze shule hamjamaliza barabara ambayo mmeanza kujenga miaka 13. Ni lini mnamaliza ujenzi wa barabara hii ambayo inaunganisha Mkoa kwa Mkoa msaidie watu wa Ukerewe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, mara nyingi tumeuliza hapa hilo swali Waziri, barabara ya kutoka Tarime Mjini - Nyamwaga - Nyamongo - Serengeti ambayo inapita kwenye Mgodi wa Nyamongo ambapo kila siku pale Serikali inapata pesa nyingi za wananchi wa Tarime. Ni lini mtaijenga barabara hii ili wale watu na wao wafurahie maisha kwamba ndiyo wanaotoa dhahabu inayochangia kwenye ujenzi wa miundombinu hii?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, lini tunamaliza kujenga hiyo barabara siyo rahisi kumwambia lini, lakini anafahamu kwamba barabara hii ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 - 2020. Ni ahadi yetu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu Serikali hii ya Awamu ya Tano ikiahidi inatekeleza.Kwa hiyo, mimi namhakikishia barabara hii itakamilika katika kipindi hiki cha miaka mitatu na anafahamu fedha hizi zinatokana na kodi ambazo tunakusanya. Mheshimiwa Mbunge ajitahidi tukusanye kodi nyingi barabara hii tuikamilishe kwa muda ambao yeye na mimi tutakubaliana.
Swali la pili kuhusu barabara ya Tarime - Nyamwaga - Nyamongo - Serengeti nayo anafahamu ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020. Vilevile anafahamu kwamba tumeshaanza kazi, naomba aiamini Serikali hii, kazi hii tutaifanya. Sisi tuliopata dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara hii tunamhakikishia tutaijenga kwa kadri fedha tutakavyozipata.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Mji wa Sirari, Mji wa Nyamwaga na Mji wa Nyamongo, kwanza Mji wa Sirari una wakazi zaidi ya 40,000, Mji wa Nyamongo una wakazi zaidi ya 32,000, Mji wa Nyamwaga una wakazi zaidi ya 25,000 na hii ni miji ambayo imekua, ni mikubwa sasa kuna nyumba mpaka za milioni 600 pale, lakini kwa sababu tu haijakuwa surveyed wananchi hawawezi kutumia zile nyumba kukopa kama collateral ili waweze kuendesha biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Mji wa Sirari ulitamkwa kwamba ni Mamlaka ya Mji, hakuna Mkurugenzi, bado ni vijiji kwa kifupi tu na miji yote hii, sasa ni lini Serikali itaifanya ile miji iwe Mamlaka za Miji ili iweze kupanga hii miji na kuipima ili wananchi watumie nyumba zao kukopa benki waweze kukwamua maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sisi tunaishi mpakani mwa Kenya na Tanzania, upande wa pili tu pale mtu ana kiwanja square meters 2,000 anakwenda benki anakopa pesa anaendesha maisha, upande wa Tanzania mtu ana eka 20, 30, hawezi kukopa kwa sababu vijiji vyote havijapimwa. Ni lini Serikali itapima vijiji vyote vya Jimbo la Tarime wapatiwe hati za kimila ili waweze kutumia kwenye mabenki kuendesha maisha yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza kwamba ni lini sasa tutafanya mamlaka ya mji. Nakumbuka katika wiki hii nilijibu swali kwamba mchakato ule wa maeneo mbalimbali ambao vikao vya Madiwani na vikao vingine vya kisheria vimekaa na kufika katika RCC na kuja katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tulituma timu ya uhakiki katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu, kwa sababu Mji wa Sirari kama mapendekezo yake yalishafika maana yake ni sehemu mojawapo tunayokwenda kufanyia uhakiki. Kwa hiyo, nithibitishe kwamba ni mchakato unakwenda kwa sababu sija-specify katika eneo lako, lakini tumefanya zoezi hili kwa Tanzania nzima, lengo letu ni nini? Yale maeneo ambayo yanatakiwa kupandishwa hadhi sasa yatapandishwa hadhi kwa kufikia vile vigezo vyao vilivyofikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la upimaji. Ni kweli unaposema kwamba huku Sirari ni changamoto lakini upande wa pili imepimwa vizuri, ndiyo maana katika hili tumetoa maelekezo mbalimbali katika halmashauri zetu, waweke mipango mikakati mipana ya kuhakikisha kwamba wanapima maeneo yao. Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, hatukuishia hapo, tulichokifanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunatafuta funds kutoka maeneo mbalimbali, kupitia DFID sasa hivi katika maeneo yote ya mipakani, lengo letu ni kuweza kuyaboresha yawe mazingira rafiki yakiwemo maeneo ya Sirari. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili litakapokamilika kupitia mradi huu mpana tutayaboresha na kuyapandisha hadhi maeneo yetu, maana yake ni nini, hata thamani ya ardhi katika maeneo yetu itakua na wananchi wetu wataweza kuhakikisha mazingira yao yanakuwa mazingira rafiki hata zile hati zitapatikana, maana yake hata investment ya huku Tanzania itafanana kuwa na investment shindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ndugu yangu Mheshimiwa Heche, naomba niseme kwamba tunaomba ushirikiano wa kutosha, pindi zoezi hili litakapokuja basi niombe halmashauri zote tutoe ushirikiano wa kutosha lengo kubwa ni kwamba tuki-invest pesa hizi pesa ziweze kuleta matunda mazuri. Kwa hiyo tufanye subira tu katika mchakato huu unaokuja kupitia DFID.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri tulikuwa naye Tarime na alifika kwenye Gereza la Tarime. Gereza hili linatumika kama gereza linalotumiwa na wilaya mbili, Wilaya ya Rorya na Wilaya ya Tarime na bahati mbaya hata makazi ya askari Waziri mwenyewe aliona. Gereza limejengwa mwaka 1941 likiwa na uwezo wa kubeba watu 245. Sasa hivi gereza lina wafungwa 600 na mahabusu, watu hawana hata pa kulala, Serikali inasema nini kuhusu kurekebisha hali ile ili isije ikaleta matatizo makubwa pale?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafika kwenye gereza analolisema Mheshimiwa Mbunge, nimejionea hali yake na kumbukumbu zangu zinanionesha kesho nina swali la Gereza la Tarime na nitalifafanua kwa urefu zaidi. Hata hivyo, niseme nimeshapokea jambo hilo na kesho nitalifafanua na sisi kama Wizara tunayafanyia kazi mambo haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyaleta.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na swali langu ni hivi, wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne, darasa la saba kwenye nchi hii na hata wanaomaliza kidato cha sita na wakashindwa kuendelea ni wengi mno na Serikali yenu hii imesema inataka kujenga viwanda, japo ni viwanda vya akina Bhakresa na tunajua tunahitaji ma-technician wengi sana kwenda kufanya kazi kwenye viwanda, makampuni na hata migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu atuambie ni lini kwa mipango yenu nchi nzima hii kutakuwepo na vyuo kwenye Wilaya, kwa sababu siyo kila siku tunasimama hapa tunauliza kwamba swali hili linafanana na la kwangu, lini mnataka muwe mmefikisha vyuo angalau kwenye Wilaya au tuvipeleke kwenye Kata kama shule za sekondari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amezungumzia katika suala lake, maudhui yake ya msingi kwamba kuna tatizo kubwa la mahitaji ya vijana kubakisha ujuzi. Ujuzi unapatikana katika staili za aina mbalimbali, mojawapo ni hiyo ya kuwa na vyuo maalum ikiwemo Vyuo vya Ufundi pamoja na Vyuo hivi vya Maendeleo ya Wananchi, pia tunavyo Vyuo Vikuu, ambavyo vyote vinatoa mafunzo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kutambua mahitaji haya yalivyo mengi, kuna vijana wengine pamoja na watu wazima ambao siku zote wamekuwa wakifanya shughuli za ufundi, lakini wamekuwa hawatambuliwi. Tayari kwa kutambua hilo tunao mpango wa kutambua wale ambao wana ujuzi ambao hawakupitia katika maeneo rasmi na hiyo tukishawatambua wanapewa mafunzo ya ziada ya ujasiriamali na kuwawezesha kutambulika.
Vilevile kupitia mpango ambao ni wa kuwezesha vijana katika mafunzo mbalimbali ya ufundi, hivi juzi tarehe 28 nimezindua tena mpango wa pili wa kuwezesha vijana mbalimbali ambao wataweza kupata mafunzo, yakawezesha kujiajiri na kuwezesha kuhudumia hivi viwanda vidogovidogo kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda jana alivyoeleza ili waweze kufanya shughuli zao. Mpango huo utanufaisha vijana zaidi ya 22,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa staili mbalimbali ambazo tunatumia tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi na kwa muda mfupi zaidi.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya watu wa Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna utofauti wa uelewa wa wachimbaji wadogo kati ya uelewa walionao Serikali na uelewa tulionao sisi wananchi na tunaokaa maeneo ya migodi. Tunapozungumzia wachimbaji wadogo, hatuzungumzii watu wajanja wajanja wanaoweza kwenda mjini wakapata leseni, wakarudi wakajiita wachimbaji wadogo. Tunazungumzia watu waliopo kule kijijini ambao ndio wanachimba kwa kutumia majembe, sururu na nyenzo nyingine ambazo ni duni.
Sasa swali langu, kuna maeneo ambayo yalikuwepo na watu wanachimba pale na bahati mbaya watu wanatoka kule vijijini wanakwenda Dar es Salaam wanapewa leseni, Serikali haishirikishi hata Serikali za Vijiji, wanarudi wanaondoa wachimbaji wadogo, kama eneo moja linaitwa Tigite, bwana mmoja ameondoa zaidi ya watu 20 pale. Sasa nataka Naibu Waziri anijibu, ni lini Serikali itatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo walioko kule vijijini, sio hawa wenye leseni wanaokwenda Dar es Salaam? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati Mgodi wa North Mara unaanza, ulitwaa eneo kwa maana ya ile leseni waliyopewa, walipewa eneo kubwa sana na kuna maeneo ambayo mpaka sasa hawayatumii na hawayafanyii kazi. Mojawapo ya eneo hilo ni Serengeti Crossing. Kwa nini Serikali isiuombe mgodi utoe lile eneo kwa wananchi kwa sababu mgodi haulitumii kabisa, ili wananchi wafanye kazi pale wajipatie kipato na waendeshe maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Heche jinsi ambavyo ameendelea kutupa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya migogoro ya wananchi wa Nyamongo. Nakupongeza sana Mheshimiwa Heche. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, nijielekeze kwenye maswali yake ya nyongeza, ni lini Serikali itatenga maeneo katika maeneo mengine hasa katika eneo la Tigite ambalo amelitaja? Naomba tu mara baada ya kikao hiki nikutane na Mheshimiwa Heche atupatie maeneo kwa sababu Serikali bado inaendelea kuongea na mgodi ili ipate maeneo mengine kwa wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, nitazungumza na Mheshimiwa Heche kuhusiana na hili ili eneo la Tigite alilotaja pia litengewe wananchi wa Nyamongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwanza tu nieleze kwamba Mheshimiwa Heche anavyosema kwamba North Mara imepewa maeneo makubwa, ni kweli, yapo maeneo ambayo Serikali inazungumza na mwekezaji ambayo ni makubwa na mgodi haujaanza kuyatumia. Tunafanya majadiliano, yakishakamilika, tutaongea na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kabla leseni hazijatoka, utaratibu tulioweka sasa ni pamoja na kushirikisha viongozi wa maeneo yale ili leseni itakapotoka waweze kutupa ushirikiano mkubwa. Kwa hiyo, eneo hili ambalo ni kubwa kwa wachimbaji wakubwa, tutazungumza na Mgodi wa North Mara, maeneo ambayo tutayapata Mheshimiwa Heche tutashirikiana na wewe ili wananchi waendelee kupelekewa maeneo zaidi.
MHE. JOHN H. WEGESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa mara nyingine kwa kuniona na kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza kwa niaba ya watu wa Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, GN hizi zilizotangaza haya maeneo na kuweka mipaka ya mapori ni ya miaka 1984; vijiji vingi ni vya miaka ya 1970, 1975 na kuendelea. Kwa hiyo, GN hizi zimetangazwa vijiji vikiwepo ukichukua Kata kwa mfano ya Kwihancha, Goronga na Nyanungu vimepakana na Pori la Serengeti; vijiji vyote vya maeneo haya ni vya miaka ya 1970 na vimesajiliwa vina usajili. Lakini watu wa Serikali wameanza kuhamisha kwa kutumia GN miaka ya 1990 mpaka sasa hivi wanazidi kurudisha watu nyuma, watu hawana maeneo ya kulima wala ya kuchungia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Waziri watatue hili tatizo kwa haraka ili watu waendelee kuishi maisha yao ya kawaida na wasiendelee kuona wafugaji kwamba ni wahaini katika nchi yao, wawaruhusu ng’ombe wao waendelee kuchunga kwenye maeneo ambayo ni ya vijiji vyao kihalali na kisheria.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ulivyosema kwa kiwango kikubwa yale yalikuwa ni maoni au ushauri lakini ni vyema sauti ya Serikali ikasikika na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kufanya marekebisho madogo tu kwamba sio vyema kujumuisha au kutoa kauli ya jumla kwamba GN zote ni za miaka 1980. Nadhani katika eneo mahususi analolitaja inawezekana ipo hivyo lakini utaratibu ambao utaweza kutufikisha mahali ambapo patakuwa ndio pana usahihi zaidi ni kwa kuchambua kila kesi kwa kesi na kila hoja kwa hoja kwamba eneo fulani linahusishwa na GN namba fulani,
tutakwenda kuiangalia kwamba ni ya mwaka gani ili tuweze kujua eneo lililohifadhiwa na kijiji kilichopo kipi kilitangulia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo kutangulia au kuja baadae pengine inaweza kuwa sio hoja ya msingi sana; hoja ya msingi itakuwa ni uhifadhi kwa maslahi ya Taifa. Na hivyo ndio maana tumesema kwamba tunayo tume
ambayo inaendelea kufanya kazi ambayo itahusisha pia na kufanya mapitio ya hayo yote tunayoyazungumzia. Kamati ambayo nimesema jana wakati najibu swali, lakini narudia tena leo ipo katika hatua ya kupitiwa na Makatibu Wakuu
na baada ya pale itakwenda kwenye hatua ya Mawaziri halafu baadae kwenye ngazi za mamlaka za juu za Serikali.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Suala la kahawa kule kwetu kuna kata zaidi ya tano zinalima kahawa; Kata ya Mriba, Nyanungu, Itirio na maeneo mengine ya Tarime Mjini pia Kitale wanalima kahawa. Watu wa maeneo mengine wamefyeka kahawa zao kwa sababu wanaona ni kilimo kisichokuwa na tija. Mwenzangu amelalamikia kodi na tozo, ni kweli zipo, lakini kule kwetu nalalamikia bei. Ukichukua bei za kahawa zinazonunuliwa kwa mfano upande wa Kaskazini, japo bado zipo chini, ni tofauti na za Tarime na maeneo mengine ya kule Mara. Ukichukua bei zilizoko Kenya, sisi tuko mpakani, Kenya bei iko juu…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kenya mpakani bei inakuwa juu kuliko sisi. Sasa nauliza Serikali ni kwa vipi watu wengine wote bei zao zinakuwa tofauti na sisi? Ni kwa nini wasifanye bei hiyo ipande ili wakulima wale wasifyeke kahawa zao iwe ni kati ya zao ambalo linawapatia faida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anavyosema kwamba nchi za jirani bei ya kahawa ni nzuri kuliko bei tuliyonayo nchini. Moja kati ya sababu zinazofanya bei yetu ya kahawa iwe chini ukilinganisha na nchi za jirani ni kwa sababu ya utitiri wa tozo na kodi ambazo zinafanya ile bei anayopata mkulima kuwa ndogo. Ndiyo maana nimesema mwaka huu tutapunguza tozo na kodi kuzidi mategemeo yenu kwa wakati wowote ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kodi hizi sio kwamba zina athari tu kwa bei ya zao hili kwa wakulima lakini zina athari katika mazingira ya ufanyaji biashara. Wawekezaji na wanunuzi wengi wa kahawa hawaji Tanzania kwa sababu kimsingi mazingira ya kufanya biashara ni magumu, ikisababishwa pamoja na mambo mengine na utitiri wa kodi na nyingine zinawagusa wao moja kwa moja. Kwa hiyo, tunapopunguza zitakuwa na faida sio tu ya kuongeza bei anayopata mkulima lakini vilevile kuwavutia wanunuzi wengi zaidi ili ushindani uwe mkubwa na hivyo bei kuongezeka. Naomba naye asubiri tarehe 22 ataona mapinduzi haya ambayo tunayazungumzia.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Rais alipokuja kufanya kampeni yake katika Mji Mdogo wa Nyamongo ambao una wakazi karibia 45,000 aliahidi kuwapatia maji. Kwenye kitabu cha bajeti ya mwaka jana ilioneshwa kwamba upo mradi kwa ajili ya kutoa maji Mto Mara na kupeleka kwenye Mji wa Nyamongo ambao vyanzo vyake vyote vya maji vimechafuliwa na mgodi na sumu ambazo zimeingia mgodini samaki wanakufa na watu hawana maji ya kutumia. Serikali imefikia wapi kuwapelekea watu wa Nyamongo maji kwa sababu ni ahadi ya Rais na ilikuwa kwenye mpango wa Serikali wa mwaka uliopita? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakamilisha usanifu wa mradi mkubwa utakaotoa maji Ziwa Victoria kupeleka mpaka Tarime kupitia kwenye eneo la Nyamongo. Kwa hiyo, tuko kwenye hatua nzuri, Mheshimiwa asubiri tu tunakamilisha na kutafuta fedha na tutatekeleza mradi huo.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ziko kwenye Mji mdogo wa Sirari na Mji mdogo wa Nyamongo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais akiwa pale na ziko TARURA.
Unasemaje kuhusu kutupa angalau kilometa mbili za lami ili kuondoa matatizo kwenye Mji ule ambao una watu wengi Miji miwili hii ambayo ni Sirari na Nyamongo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi za Mheshimiwa Rais zimetolewa maeneno mengi na sisi sote ni mashuhuda kwamba tumeletewa taarifa kwamba uratibu utafanyika kuhusiana na ahadi zote ambzo zilitolewa na Mheshimiwa Rais na kimsingi katika kutekeleza ahadi hizo tunahitaji miaka mitano, ndani ya miaka mitano tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba ahadi za Rais zinatekelezwa naamini katika kipindi hicho na eneo lake litatekelezwa kwa kujengewa hiyo barabara ya lami.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika kwa majibu ya Serikali kwasababu vifaa vya ujenzi hata vikijenga barabara, vikijenga kila kitu mwisho wa siku ina mahusiano ya moja kwa moja na maisha ya wananchi wa kawaida. Barabara hizi zimekuwa zikijengwa kwa gharama kubwa na wananchi ndio wanalipa kodi kwa hiyo Serikali hii haioni bado kuna sababu ya kuwapunguzia wananchi wake mzigo kwenye gharama ya vifaa vya ujenzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pilli katika zile basic human needs kuna nyumba, mavazi na kuna chakula na heshima ya binadamu yoyote ni mahali anapokaa kwa maana ya makazi. Na nchi nyingine zimeenda mbali kuwapatia wananchi wake makazi hata ya bure, Serikali yenu ya CCM inaona ni muhimu zaidi kutoza kodi kuliko maisha ya wananchi ambao wanaishi kwenye maisha duni na makazi duni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi na naomba ifahamike kwamba uhai wa Taifa lolote ni kodi hakuna maendeleo ya Taifa lolote bila kodi na kama nilivyosema wafanyabiashara wapo wengi wanafanya kazi hizi na kusema kwamba hapa tunasamehe kwa sababu wanakwenda kujenga nyumba ni watu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, niulize tu swali na mimi labda hivi kabla ya kodi hii ya VAT mwaka 1998 wananchi walikuwa wakijenga tofauti na wanavyojenga leo baada ya kuwa tunakodi ya VAT? Hiyo si sahihi hata kidogo hali ya ujenzi ipo na sasa hivi tunaona Watanzania wengi wameinuka kimaendeleo na wanajenga nyumba za kudumu kwa asilimia kubwa kuanzia mijini mpaka vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makazi ya bure anayosema Mheshimiwa Heche, makusanyo ya kodi ndio yatakayosababisha tutoe huduma kwa wananchi wetu, na sisi tunapoelekea ndio huko huko inawezekana kabisa tukafika sehemu baada ya kuimarisha makusanyo ya kodi ikiwepo kodi ya VAT tukaweza kutoa huduma nyingi kwa wananchi wetu bure lakini kwa kuzingatia kwmba uhai wa Taifa lolote ni kodi na hakuna maendeleo bila kodi.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tarime tumejitahidi na Mheshimiwa Kandege alikuwepo, tumejenga hospitali kubwa pale ya Wilaya ambayo iko Nyamwaga, tumejenga vituo vya afya karibia vine, kuanzia Nyandugu, Mriba na Sirari ambako ni kituo ambacho Waziri Mkuu alisema kiwe cha mfano nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa shida yetu ni watumishi, ni lini mnatuletea watumishi hasa kwenye Hospitali ya Nyamwaga ambayo tumeshanunua na vifaa ili ile hospitali ianze kuhudumia wananchi wa Tarime ambao wamefanya kazi kubwa pale kuijenga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maneno kwamba wakifanya vizuri upande wa Upinzani hatuwapongezi, lakini kwa dhati kabisa naomba nipongeze kazi nzuri ambayo imefanywa na wananchi wa Tarime akiwepo na Mbunge Mheshimiwa Heche kwa sababu tumeenda tukatizama kwa macho na kuona ni kusadiki, mmefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Heche atakubaliana na mimi kwamba katika ziara aliyofanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, aliahidi kwamba taratibu zikamilike mara moja ili Hospitali ya Nyamwaga ianze kufanya kazi na tena ni matarajio yetu kwamba muda sio mrefu itakuwa ni miongoni mwa Hospitali za Wilaya. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. CSR ipo kwa mujibu wa sheria, lakini hii migodi wamekuwa wakionyesha kama ni hisani fulani wanawapatia wananchi. Kwa nini sasa Serikali isiwaagize hizi pesa zipelekwe moja kwa moja kwenye Halmashauri na zisimamiwe na Madiwani wetu katika kutekeleza miradi hii, kwa sababu unaona gharama zinazoandikwa ni kubwa kweli ukilinganisha na kazi halisi ambazo zinakuwa zinafanyika, yaani ziende kama vile kodi zingine zinavyoenda lakini zikiwa specific kama CSR ili zisimamiwe na Baraza la Madiwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba hesabu zinazoonekana ni hesabu kubwa sana zilizotumika kuliko miradi yenyewe ilivyo, hilo tunakubaliana kabisa. Nimepita baadhi ya maeneo kwa mfano, GGM na North Mara tumewaagiza kwanza watupe taarifa ya utekelezaji wa zile fedha zilizotengwa kwa miaka miwili iliyopita ili tujiridhishe tuone zile fedha zilizotengwa na wamepeleka wapi na nini kimefanyika. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu hizi fedha za corporate social responsibility huwa zinatolewa kutokana na jinsi wao wanavyotengeneza faida na kwa sasa hivi ni sheria lazima watoe zile fedha. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Madiwani husika wakakae na zile Kampuni waamue kwamba watekeleze miradi ile kwa jinsi wao walivyoweka kipaumbele chao.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna fedha ambayo inakwenda moja kwa moja kwenye Halmashauri, fedha hiyo ni service levy ambayo ni asilimia 0.3 ya mauzo ya madini wanayoyapata. Kwa hiyo, nadhani tu kwamba tuendelee kutoa ushirikiano na sisi kama Wizara ambayo tunasimamia Sheria ya Madini tutahakikisha kwamba zile fedha zinazotengwa zinakwenda zinavyostahili na Madiwani wasimamie utekelezaji wa miradi ambayo wamejipangia. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini. Napenda kusema kwamba sheria ya sasa na kanuni kuhusiana na uwajibikaji kwa jamii ziko wazi.
Mheshimiwa Spika, niombe tu ushirikiano Waheshimiwa Wabunge pamoja na Halmashauri zetu za Wilaya na Miji waweze kutoa ushirikiano na kutupatia taarifa endapo wanaona kuna miradi imetekelezwa ipo chini ya viwango, lakini kiwango ambacho kimekuwa-declared ni kidogo kuliko fedha halisi ambayo inatamkwa kwamba imetumika.
Mheshimiwa Spika, pili; pamoja na maelezo aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tumewataka GGM waweze kutoa maelezo na taarifa zao za miaka miwili, tutaenda kwa migodi yote ambayo imekuwa ikifanya uwajibikaji kwa jamii na tutapitia na kukagua na yeyote ambaye ataonekana alifanya udanganyifu, hatua kazi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, ninafikiri kwamba ni vema Mawaziri wetu wanapokuja kutoa majibu hapa wajue Watanzania wanawaangalia na Watanzania wanasikitika sana pale wanapokuwa wanatoa taarifa ambazo siyo za kweli. Kwa mfano, juzi amekamatwa Mwenyekiti wa Kijiji anaitwa Tanzania Omutima, Kijiji cha Kewanja kwa tuhuma tu, amekaa siku nne hajafikishwa Mahakamani na wala hajapelekwa polisi. Pia amekamatwa kijana anaitwa Mudude Nyagali, amewekwa ndani zaidi ya siku 30.
Mheshimiwa Spika, ninachoomba Waziri atoe tamko kwamba ni marufuku kuanzia sasa watu wa abide na sheria, kukamata mtu na kukaa naye zaidi ya yale masaa ambayo sheria inaruhusu kama mtu amefanya hivyo afikishwe kwenye utaratibu, ashitakiwe kwa kukiuka sheria ambayo tunayo mpaka sasa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza napingana kabisa na kauli yake kwamba Mawaziri hapa tunatoa majibu ambayo siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu ambayo tunayotoa hapa ni majibu ambayo tumeyafanyia utafiti wa kina na tunajiamini kwamba tunachokizungumza hapa ni kitu ambacho ni sahihi kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka tutoe tamko, matamko tumekuwa tukitoa kila siku na siyo lazima atoe matamko kwa sababu sheria zinajulikana, tunachokifanya ni kusimamia sheria ambazo tumezitunga humu Bungeni na Mheshimiwa Heche anazifahamu. Kwa hiyo, iko wazi kwamba yeyote ambaye hafuati sheria na hakuna ambaye yuko juu ya sheria, ikiwemo Wasimamizi wa Sheria ambao ni Vyombo ya dola.
Mheshimiwa Spika, tunasema kila siku kwamba kama kuna Askari yeyote ambaye anatumia nafasi yake vibaya kinyume na maadili yake ya kazi, tutamchukulia hatua na tumekuwa tukifanya hivyo, tukiwachukulia na tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Heche.
Mheshimiwa Spika, pengine nitoe fursa ya kuelimisha kidogo hii dhana ya saa 24 kukaa mahabusu. Kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, unapomkamata kwa mara ya kwanza mtuhumiwa na kumuweka mahabusu, kwa maana ya matakwa ya saa 24. Saa 24 yale yanaendana na upelelezi wa awali. Kuna mazingira ambapo uliyemweka ndani hata kabla ya saa 24 hayajafika mtamtoa ndani katika upelelezi ama kuna mahala anaenda kuonesha silaha, ama kuna mahala anaenda kuonesha ushahidi fulani kutokana na maelezo yake. Mnapotoa atakaporudi mahabusu huyo mtuhumiwa anaanza kuhesabiwa masaa yake upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya wananchi wanahesabu tangu alipokamatwa, lakini kisheria tunahesabu tofauti. Kwa hiyo, nimuelimishe Mheshimiwa Heche, huyo anayemsema Mwenyekiti wa Kijiji ambaye aliyekamatwa pale Nata, kulikuwa na masuala ya vielelezo vya documents kwa sababu fedha za kijiji zaidi ya shilingi milioni 300, vilevile ilikuwa inahusisha na Kampuni ya Uwekezaji wa Grument. Kwa hiyo, aliyekuwa amekamatwa tulitoa maelekezo. Mheshimiwa Heche dhana hii muifahamu vizuri ya masaa 24.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naona wananchi waelewe dhana ya saa 24 inaanza wakati gani na inaisha wakati gani. Siyo nia ya Serikali kuwatesa wananchi wake, na ndiyo maana majibu niliyoyatoa mwanzo nilisema wale askari ambao watakiuka sheria hiyo ya kuwaweka ndani tunachukua hatua, hakuna yeyote ambaye tunamfumbia macho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Heche uwe na amani huyo mtu unayemsema tumeshatoa maelekezo na tunajua concern yako. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri hizi pesa za REA ni pesa ambazo ziko ring fenced, lakini mpaka sasa ninavyozungumza kwenye Jimbo langu mradi wa densification haujafanyika hata mmoja kwenye maeneo ya Nyamorege, Nyabitocho, Kyoruba, Pemba na Matongo ambayo ni maeneo makubwa yenye watu wengi. Kwa mfano, Nyamorege ina watu zaidi ya 20,000 wenye uwezo wa kutumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza, ni lini mkandarasi atakwenda pale? Kwa sababu mnasema pesa zipo, lakini yeye anasema hajalipwa pesa; lini anakwenda kuwekea watu wa Tarime umeme hasa Kata ya Susuni ambayo haina umeme kabisa kata nzima na ina watu wengi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Heche ameeleza kwamba kuna mradi wa densification, haoni maendeleo yoyote. Nataka niseme hii miradi iko tofauti. Densification kwa kweli hela zake zipo na unafadhiliwa na Serikali ya Norway pamoja na Serikali ya Tanzania na ni shilingi bilioni 62. Sasa labda baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu, namwomba Mheshimiwa Mbunge tukutane ili tuongee na mkandarasi nijue tatizo lake ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa densification hauna matatizo kabisa na kwa kuwa Mkoa wa Mara uko katika mikoa ile nane ya awali na sasa hivi matarajio yetu ni mwezi Mei miradi yote ya densification iwe imekamilika ili tuanze na densification awamu ya pili. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane baada ya hapa ili tuweze kuona tatizo ni nini ili niweze kulishughulikia.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala la uchakavu na wingi wa mahabusu na wafungwa kwenye magereza, yaani kwa maana kwamba magereza kuzidiwa. Kwa mfano Gereza la Tarime lilijengwa mwaka 1947 kwa ajili ya kuchukua wafungwa 140 tu. Hivi tunavyoozungumza kuna watu mpaka 700. Je, Serikali ya CCM haioni kwamba kubeba watu wengi ndani ya magereza ni kukiuka haki za binadamu na kuwaumiza watu ndani ya magereza haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, wingi wa watu magerezani si ukiukwaji wa haki za binadamu kwa sababu wako magerezani kwa mujibu wa sheria. Kitu ambacho nadhani ningemshauri Mheshimiwa Mbunge ni kwamba aendelee kuwa balozi mzuri wa wananchi wa Tarime kuhakikisha kwamba wanafuata sheria na wasifanye uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itajitahidi kupunguza msongamano pale ambapo inawezekana na tunafanya hivyo. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa akifanya kazi nzuri ya kuona kwamba atumie mamlaka yake ya Kikatiba aliyokuwa nayo kusamehe wafungwa wale ambao amekidhi vigezo.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushuru japo swali hili lilikosewa na kwa sababu hakukuwa na muda wa kufanya marekebisho na bahati nzuri Mheshimiwa Kandege anajua mazingira ya pale vizuri. swali langu Mheshimiwa lilihusu Zahanati ya Nyamwaga ambayo Halmashauri ya Wilaya imejenga majengo kumi wodi theatre, mochwari na tukaiomba iwe-upgraded kuwa Hospitali ya kwanza sasa ya halmashauri kwa sababu ina mazingira yote yanayoruhusu. Wewe tulikwenda pale na Waziri Mkuu unapajua, tumepeleka vifaa vya milioni mia tatu, swali langu linauliza ni lini, Zahanati ya Nyamwaga ambayo inazidi hata Hospitali ya Wilaya itafanywa kuwa Hospitali ihudumie wananchi kama hospitali na ipolekewe Wataalamu kwa sababu vifaa vipo? Ndio swali hilo na wewe unapafahamu vizuri pale.
MWENYEKITI: Lakini silo uliloliuliza, wewe umeuliza swali lingine, na Serikali imekujibu swali lako, sasa wewe umekuja na swali jipya, sasa nakubaliana na wewe, maswali ya Afya ni muhimu jimboni mwako na nakushukuru umelitolea, Mheshimiwa Waziri baadaye kaa na Mheshimiwa Mbunge mueleze majibu namna gani mnaweza ku-coucas na kujibu, hongera kwa swali zuri.
MHE. JOHN. W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali hili limekuja wakati mzuri kwa sababu ni swali linalohusu Tarime na ilikuwa Wilaya moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais amekuja Tarime Mwezi Julai, alisimama kwenye Mji wa Nyamongo kwenye Kijiji cha Kewanja na akaahidi kwamba Mwezi wa Tatu mwaka huu, watu wa Nyamongo ambao ni zaidi ya 35,000 wakazi wa pale na wakazi wa Sirari watakuwa wamepata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje kuhusu hilo likiendana sana hasa na swali hili ambalo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mwezi Julai?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimjibu tu kwa ufupi Mheshimiwa Mbunge. Ahadi ni deni; na Mheshimiwa Rais anapoahidi sisi hatuna kikwazo cha kushindwa kutekeleza. Kwa hiyo, tumejipanga katika kuhakikisha tunalitekeleza hilo jambo ili wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami niulize swali dogo la nyongeza. Kuna kata iko pale inaitwa Kata ya Sirari, kata kubwa kabisa, ina wakazi zaidi ya 45,000, watu wana majumba mpaka ya milioni 200 pale; Kitongoji cha Nyamorege, Niroma, kuna maeneo ya Kimusi, tumezungumza na Waziri muda mrefu sana, watu wanahitaji umeme na wana uwezo wa kulipia. Ni lini hao watu watapata umeme kwenye hayo maeneo niliyoyataja kwa sababu watu wanahitaji umeme na wana nguvu za kulipa?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ni kweli nilitembelea eneo hilo na kutoa maelekezo na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anafahamu. Utekelezaji wa kupeleka umeme katika eneo hilo mpakani kabisa na Sirari umeshaanza na Kitongoji anachokisema cha Nyamorege ambacho kiko jirani sana na wilaya moja wapo ya mkoa wa kwanza kutoka Kenya tayari kuna umeme na wakandarasi kupitia kampuni yetu inayopeleka umeme vijijini kule Mara umeshaanza. Tarehe ya kumaliza kazi hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge ni tarehe 12 Juni, mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali imeteua maafisa watano; na tunajua kwa miaka mitano ya uongozi wa awamu hii maafisa wengi wamerejeshwa Tanzania na hivyo Balozi nyingi hazina maafisa kwa sababu ya hofu labda ambazo wanazijua ndani ya chama chenu. Sasa maafisa watano tu katika Balozi nyingi ambazo ziko kwenye nchi mbalimbali hamuoni kwamba mnawapatia Watanzania wanaoishi nje ya nchi matatizo ya kupata huduma ambayo ni ya kimsingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarehe 31 mwezi wa kwanza mwaka huu Serikali ilisitisha matumizi ya passport za zamani; na tunajua Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji passport ambayo ndiyo inawapa uwezo wa kuishi huko wanakoishi na kufanya shughuli zao. Ni lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaoishi huko wanapata huduma hii kwa haraka ili wasionekane kama wamekuwa-condemned kurudishwa huku kwa sababu hawana passport?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Heche kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina hofu, ni suala la utaratibu tu. Kwamba kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi, kwamba kwa kutambua upungufu huo wa Maafisa Uhamiaji ndiyo maana maafisa watano wako mbioni kupelekwa wakati wowote. Hata hivyo nataka nimhakikishie kwamba kutokuwa na Maafisa wa Uhamiaji katika kila Balozi hakumaanishi kwamba wananchi au wageni wanaotaka kupewa huduma hizo wanashindwa kupata; kwa sababu kwanza hivi sasa hivi tuna Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao nitauelezea kwa kifupi ili pamoja na mambo mengine utakuwa umeweza ku-cover lile swali lake la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao unahusisha uhamiaji kwa maana ya e-passport, e-visa, e-permit pamoja na e-gate umerahisisha sana kutoa huduma kwa wananchi kwani sasa haihitaji mwananchi kwenda moja kwa moja kwenye Ofisi zetu na badala yake anaweza kwenda kwenye mtandao tu na kujaza fomu zake na kuweza kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo maafisa ambao wapo katika Balozi zetu wameshapata training juu ya matumizi haya ya uhamiaji mtandao, na pale ambapo wananchi ama wageni wanapohitaji huduma hizo kwa maeneo ambayo hakuna Maafisa Uhamiaji basi Maafisa wa Mambo ya Nje waliopo katika Balozi zetu huwa wanatoa msaada kwa wale ambao wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo kwa ufupi ni dhahiri kwamba uchache huo wa maafisa ambao ameuzungumzia Mheshimiwa Heche hauna madhara yoyote mpaka sasa hivi kwa huduma mbalimbali za raia na wageni ambao wanataka kuzipata katika Balozi zetu duniani.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda nami nimuulize Naibu Waziri swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata zaidi ya sita pale Jimboni kwangu Tarime Vijijini ambapo nguzo zimesimamishwa huu ni mwezi wa nne lakini bado hakuna nyaya wala activity yoyote inayoendelea. Sasa sijui ni nini kinachoendelea na napenda awaambie wananchi ni lini sasa nyaya zitapitishwa pale ili waanze kupata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Heche, Mjumbe wetu wa Kamati ya Nishati na Madini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameulizia kuhusu kata sita kwenye jimbo lake ambapo amesema nguzo zimesimama lakini hakuna kinachoendelea. Nimwombe tu Mheshimiwa Heche baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane ili niweze kufuatilia kwa karibu kwa nini mkandarasi DERM ambaye anaendelea na kazi katika Mkoa wa Mara hafanyi vizuri kwa sababu tunaamini mkandarasi yule ni miongoni mwa wakandarasi sita wanaofanya vizuri. Kwa hiyo, tukutane ili nijue kwa nini katika maeneo hayo bado nyaya hazijasambazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu tu wakazi wa Mkoa wa Mara na nchi nzima, miradi hii tunatarajia mpaka Desemba kazi ya ujenzi wa miundombinu iwe imekamilika, ibaki kazi ya uunganishaji wa wateja ambapo kwa mujibu wa mkataba Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakamilika Juni, 2020. Kwa hiyo, niendelee kuwatoa hofu lakini kweli kuna umuhimu wa kuongeza kasi zaidi, tutalifuatilia kwa pamoja ili kujua ni nini kimekwamisha kazi hiyo. Pia napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi karibuni baada ya Bunge hili nina ziara ya Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge na awaambie Watanzania kwa mujibu wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 kampuni inatakiwa kulipa fidia ifanye relocation na ifanye resettlement kama inahamisha watu. Lakini hawajawahi kuhamisha mtu wala kumfanyia relocation na licha ya hivyo mpaka sasa kwa mfano wananchi wa Tarime waliofanyiwa uthamini maeneo ya Nyamongo kuanzia mwaka 2009 mpaka leo tunavyozungumza hawajawahi kulipwa. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Madini alikuwa pale ametoa kauli lakini mgodi unakiuka hausikilizi, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri ni lini hasa watu hawa wanaoendelea kuteseka kwa zaidi ya miaka 10 au 15 watalipwa sasa ahsante? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Heche Mbunge wa Tarime kwa kifupi tu na kwa sababu leo ni bajeti yetu tutaeleza kwa kina hayo yote.

Mheshimiwa Spika, nieleze kwamba ni kweli kulikuwa na changamoto ya muda mrefu toka mwaka 2012 kwenye fidia za maeneo ya mgodi wa North Mara huko Nyamongo. Lakini kama Serikali tumechukua hatua kubwa sana kwa sababu kuna maeneo mengine ambapo kwa kweli tungekimbilia tu wananchi walipwe fidia walikuwa wamepunjwa sana, kwa mfano awamu ya 47 wananchi 66 ambao walikuwa wanadai fedha walithaminiwa kiasi cha shilingi milioni 224 peke yake, tumekwenda kule tumeangalia tumekuta wale wananchi walikuwa wamepunjwa sana tumeagiza uthamini huo ufanyike upya ili wananchi walipwe stahiki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Heche anafahamu Awamu ya 24 na Awamu ya 34 wananchi hawa walikwenda mahakamani na kwa kuwa wamekwenda mahakamani tuliwashauri kwamba wamalize shauri lao mahakamani wakishakumaliza sisi kama Serikali huku tutasimamia utaratibu wao wa kulipwa. Lakini Awamu ya 30, 32 (a) na (b) ambazo mgodi hauhitaji hayo maeneo Chief Valuer ameelekeza mgodi uwalipe kifuta jasho wananchi hao.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Heche kwamba jambo hili tumelifanya pamoja na kwenye bajeti tutalieleza kwa kina awe na subira tusiharakishe shughuli za Bunge ahsante. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na mimi nilitaka kumuuliza Waziri kuhusu mazao, sisi kule Tarime tuko mpakani, kwa mfano, upande wa Kenya, tumbaku wananunua kwa bei juu na soko lipo, kahawa wananunua bei juu soko lipo, mahindi wananunua bei juu kuliko Tanzania na soko lipo na watu wa Tarime wanalima wenyewe, wanaweka mbolea wenyewe. Kwa nini mnawazuia kupeleka mazao yao kwenye soko na bei ya uhakika na wanapolipwa kwa muda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza ni kwamba kuna mazao ya kimkakati na mazo ya chakula ya kawaida na Serikali kimsingi haijazuia kuuza tunatafuta masoko, kinachohitajika ni kufuata taratibu zinazotakiwa ili pia tuweze kuwa na uratibu mzuri wa kusema kwamba katika mwaka huu, kwa mfano, katika zao fulani tumeuza nini, kwa sababu kama hakuna uratibu maalum itakuwa hata tukiulizwa swali hatuwezi kujibu kwasababu mtu anakuwa ameuza kwa njia za panya na Serikali pia inakuwa imekosa mapato mengine ambayo yanahitajika pale inapotakiwa kutozwa katika mazao hayo.