Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa (16 total)

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mwaka 2013 Bunge lilirekebisha Sheria ya Ushirika wa Tumbaku ili iendane na hali ya sasa ya ushirika huo nchini:-
Je, ni marekebisho gani yaliyowanufaisha wakulima moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 ambayo ni kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa shughuli za Vyama vya Ushirika vya aina zote Tanzania Bara na siyo kwa ajili ya Vyama vya Ushirika wa Tumbaku pekee. Sheria hiyo ilianza kufanya kazi mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, marekebisho yaliyowanufaisha wakulima moja kwa moja ni pamoja na:-
Moja, sheria imeruhusu ushindani baina ya Vyama vya Ushirika ili kuongeza ufanisi kwa kuruhusu kuanzishwa Vyama vya Ushirika zaidi ya kimoja vinavyofanya shughuli ya aina moja katika eneo moja, jambo ambalo halikuwepo katika Sheria ya 2003. Hii pia imeondoa migogoro kama ule wa Vyama vya Ushirika vya Mishamo Mkoani Katavi ambapo wakulima wa tumbaku walikuwa na mgogoro mkubwa kiasi cha kutishia amani.
Pili, sheria hii imeweka mazingira ya wanachama wa Vyama vya Ushirika kujiunga na kunufaika na huduma mbalimbali kama zile zinazotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambazo ni Mafao ya Uzeeni, Fidia, Bima ya Afya na Mikopo. Hadi mwezi Septemba, 2015 zaidi ya wanachama 50,000 wamejiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kunufaika kwa kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 50 kupitia mpango unaojulikana kama Wakulima Scheme.
Tatu, Sheria imepunguza idadi ya chini kabisa ya watu wanaoweza kuunda Chama cha Ushirika cha Mazao kutoka 50 hadi 20 ili kuwawezesha wakulima kuunda vyama wanavyohitaji kwa wepesi zaidi ilimradi viwe na uhai wa kiuchumi. Vyama vya Ushirika 60 vimeandikishwa kufikia mwezi Disemba, 2015.
Mheshimiwa Spika, nne, Vyama vya Ushirika vimetumia sheria hiyo katika kujihusisha na zaidi ya zao moja na hivyo kuepuka kupata hasara pale ambapo bei ya zao inapokumbwa na misukosuko kama vile kushuka kwa bei. Vyama vya Ushirika wa Tumbaku vya Mkoa wa Tabora vimeanza kuweka mipango ya kuzalisha mazao mengine kaka vile alizeti, karanga na nyonyo ambayo yana soko na bei nzuri.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya moja kwa moja ya Sheria mpya ya Ushirika kwa wakulima yataongezeka zaidi mara baada ya kukamilika mfumo wa usimamizi ambao unaainishwa katika sheria hiyo ambao unaanza ngazi ya Wilaya hadi Taifa, utakaotekelezwa kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo muundo wake tayari umeshapitishwa na Serikali.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kujenga Vyuo vya VETA kwa Wilaya zote nchini na Chunya ni kati ya Wilaya 10 za mwanzo kupata chuo hicho:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia majengo yaliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya lami pale Chalangwa kwa ajili ya Chuo cha VETA, ili kuokoa gharama kubwa za ujenzi wa majengo mapya.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ufundi, imebaini kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara husika kampuni ya ujenzi iliacha majengo yaliyokuwa yanatumika kama ofisi na makazi.
Mheshimiwa Spika, aidha, ukubwa wa ardhi iliyokuwa imetolewa na kijiji kwa kampuni hiyo ni hekari 25, taarifa ya kitaalamuimebainisha kwamba eneo ilipo kambi hiyo ni zuri kwa maana ya kufikika na kuwa na huduma za umeme na maji. Hata hivyo, majengo yaliyoachwa na kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara hayakidhi viwango vya kutolea mafunzo ya ufundi stadi kutokana na ukweli kwamba majengo hayo siyo ya kudumu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Chuo cha VETA katika Wilaya ya Chunya tayari ilikwishafanya maandalizi ya awali ya ujenzi wa chuo cha VETA. Maandalizi hayo ni pamoja na kufanya utambuzi wa stadi zinazohitajika kutolewa katika chuo hicho. Aidha, Wilaya ya Chunya imekwishatenga eneo la ujenzi wa Chuo hicho katika Kijiji cha Mkwajuni na tayari Halmashauri ya Wilaya imekwisha pima eneo hilo, lenye ukubwa wa hekari 10.1 Kiwanja nambari 1 kitalu (B) na hati ya kiwanja ilikwishapatikana. Katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi imeshateua wataalam elekezi watakaoshindanishwa kutayarisha andiko la jinsi ya kufanya kazi ya kubuni majengo na gharama ya kazi hiyo. Mtaalam elekezi wa kubuni majengo ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Chunya anatarajiwa kupatikana mwezi Februari, 2016.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Barabara ya Mbeya – Chunya - Makongorosi imejengwa kwa kiwango cha lami kwa asilimia 80. Je, ni lini Serikali itaweka mizani katika barabara hiyo ya lami ili kuilinda iweze kudumu muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Barabara ya Mbeya – Chunya – hadi Makongorosi yenye urefu wa kilometa 117 ni barabara kuu inayohudumiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya. Barabara hii imejengwa kwa kiwango cha lami, sehemu ya barabara kati ya Mbeya hadi Chunya ambayo ni kilometa 72 na imekamilika hivi karibuni. Aidha, Serikali inafanya maandalizi ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Chunya hadi Makongorosi ambayo ni kilometa 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inatambua kuwa katika Wilaya ya Chunya kuna shughuli nyingi za kiuchumi kama vile uchimbaji wa madini, kilimo na mazao ya misitu ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa upitishaji wa magari yenye mizigo mizito na hivyo kuna umuhimu wa kuweka mizani kwenye barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itajenga mizani katika barabara ya Mbeya - Chunya hadi Makongorosi wakati wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Chunya - Makongorosi. Aidha, katika kipindi hiki ambacho ujenzi wa mizani ya kudumu haujafanyika, Serikali kupitia TANROADS itaendelea kudhibiti uzito wa magari katika barabara hiyo kwa kutumia mizani ya kuhamishika (mobile weighbridge).
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Kituo cha Afya Chunya kilipandishwa hadhi kuwa hospitali ya Wilaya mwaka 2008 lakini kuna tatizo la ukosefu wa chumba cha kuhifadhia maiti:-
Je, ni lini Serikali italitatua tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Chunya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeanza mchakato wa ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya ya Chunya ambacho kinatarajiwa kugharimu shilingi milioni 230 hadi kukamilika. Ujenzi wa jengo utagharimu shilingi milioni 60 na majokofu yatagharimu shilingi milioni 160. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti yaani mortuary.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa sasa kipo chumba maalumu ambacho kimetengwa kikiwa na uwezo wa kuhifadhia maiti mbili tu. Chumba hicho hakitoshelezi huduma hiyo hali ambayo inawalazimu wananchi kufuata huduma ya aina hiyo katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mwaka 2013 Bunge lilirekebisha Sheria ya Ushirika wa Tumbaku ili iendane na hali ya sasa ya ushirika huo nchini:-
Je, ni marekebisho gani yanayowanufaisha wakulima moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ushirika wa tumbaku kwa ujumla unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ubadhirifu katika vyama hivyo, madeni makubwa, tozo na makato mengi na usimamizi hafifu wa Vyama vya Ushirika. Changamoto hizi ni miongoni mwa vitu vilivyochochea kuwepo kwa sheria mpya ya ushirika, Sheria Na. 6 ya mwaka 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya marekebisho yanayowanufaisha wanachama wa Vyama Ushirika wakiwemo wakulima wa tumbaku ni pamoja na:-
(i) Kwa kutumia sheria mpya viongozi wabadhirifu katika Vyama vya Ushirika wamechukuliwa hatua. Kwa mfano, katika maeneo yanayolima tumbaku, viongozi wabadhirifu wa Vyama vya Ushirika 26 katika Mkoa wa Ruvuma wakiwemo na Maafisa Ushirika wawili wamesimamishwa kazi na kufikishwa Mahakamani. Viongozi wa Chama Kikuu cha WETCU waliohusika na ubadhirifu Mkoani Tabora, waliondolewa madarakani ili kupisha uchunguzi. Hatua zaidi zimechukuliwa katika Vyama vya Ushirika vya Korosho kwa viongozi watendaji na watendaji 822 kupewa hati za madai katika maana ya surcharge.
(ii) Kuhusu madeni, sheria ya sasa inakataza vyama kukopa zaidi ya asilimia 30 ya mali zake ili kuzuia vyama kuingia kwenye madeni makubwa yasiyolipika. Aidha, sheria ya sasa inaweka usimamizi wa karibu ambapo vyama hivi vitakuwa vikikaguliwa mara kwa mara kuzuia ubadhirifu.
(iii) Kuhusu tozo, kuanzia sasa Mkutano Mkuu utakuwa chini ya Uenyekiti huru utakaochaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kinyume na hapo awali ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku ndiye anayekuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu. Lengo ni kulinda maslahi ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tozo zote zinazoidhinishwa na Mkutano Mkuu zinakuwa na maslahi kwa wakulima wa tumbaku.
(iv) Muundo wa sasa wa Tume ya Ushirika unafanya Maafisa Ushirika wote kuwajibika moja kwa moja kwenye Tume. Hii itaongeza ufanisi na watumishi hawa wa Vyama vya Ushirika kwa ujumla.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Katika bajeti ya 2013/2014, Serikali iliahidi kujenga Mahakama ya Wilaya ya Chunya.
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mahakama ya Tanzania ni kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa kujenga miundombinu na kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wote na kwa wakati. Katika kusogeza huduma, Serikali imedhamiria kujenga Mahakama Kuu kila Mkoa, Mahakama ya Wilaya kila Wilaya nchini na Mahakama za Mwanzo kila Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mwaka wa 2014/2015 tuliahidi kujenga Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Chunya. Hata hivyo ahadi hiyo haikuweza kutekelezwa kikamilifu kutokana na upatikanaji hafifu wa fedha za maendeleo. Mahakama katika mwaka 2014/2015 ilipata asilimia nane tu ya fedha za maendeleo zilizotengwa, hivyo haikuweza kutekeleza miradi yote iliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya umezingatiwa katika mpango wetu wa ujenzi kwa mwaka 2016/2017.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Katika mpango wa Serikali wa kuchimba visima katika vijiji 10 vya kila Halmashauri, katika Mji Mdogo wa Makongorosi maji hayakupatikana kwenye kisima kilichochimbwa na kuwa mji huo unakua kwa kasi sana na kero ya maji ni kubwa sana:-
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Makongorosi ni moja ya miradi ya awali iliyopewa kipaumbele kutekelezwa kwenye mpango wa vijiji 10 kwa kila Halmashauri. Baada ya maji kukosekana kwenye kisima kilichochimbwa, mradi huu haukuweza kuendelea kutekelezwa na jitihada za kutafuta chanzo kingine zinaendelea.
Mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Makongorosi umepangwa kutekelezwa upya kwenye Awamu hii ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Chunya imepangiwa bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 561.5 na kazi zilizopangwa kufanyika ni kutafuta chanzo kingine kufanya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya mradi.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Kata za Ifumbo, Lualaje, Mafyeko na Kambikatoto katika Wilaya ya Chunya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu umeanza rasmi nchi nzima tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele-mradi vitatu vya densification, grid extension pamoja na off grid renewable ambapo inalenga kuongeza wingi wa usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo vimefikiwa na umeme lakini kwenye vitongoji havijaunganishwa. Kata za Ifumbo, Kambikatoto, Lualaje na Mafyeko zimejumuishwa katika mradi wa REA Awamu ya Tatu wa grid extension ambao utaanza na kukamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika kata hizo itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 20, ujenzi wa njia ya umeme ya msongo ya kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 76, ufungaji wa transfoma kumi pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,145. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 3.142.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Chunya.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Chunya ni moja ya Wilaya za zamani ambazo mpaka sasa hazina majengo kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya. Kwa sasa Mahakama inendeshwa katika majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na nafasi ndogo sana kukidhi matumizi ya huduma za Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati wa maboresho ya huduma za Mahakama tumepanga kujenga jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chunya katika mwaka huu wa fedha, 2017/2018. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Chunya kuwa na subira, wakati mipango inafanyika ya kujenga Mahakama hiyo.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Wananchi wa Wilaya ya Chunya wameanza kujenga uwanja wa michezo wa kisasa wa Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi huu ili ukamilike haraka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 kifungu cha 5.1.8(b) (vi) inaelekeza wajibu wa mamlaka ya Serikali za Mitaa kushirikiana na wananchi katika kujenga, kulinda na kutunza miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja vya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo wa Chunya unatekelezwa kwa kuzingatia sera ya michezo ikisimamiwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Chunya kwa ushirikiano wa karibu na wananchi pamoja na wadau. Mradi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni nane umetumia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na Hamashauri ya Wilaya ya Chunya katika mwaka huu wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Seriakli kupitia Halmashauri ya Chunya imetenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuendelea na hatua mbalimbali za mradi wa ujenzi wa uwanja huo wa michezo.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni nini Sera ya Magari ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magari ya Serikali, kama ilivyo kwa mali zingine za Serikali samani, ardhi na majengo, madini, misitu, uoto wa asili na kadhalika husimamiwa na sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha menejimenti ya mali za Serikali, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeanza kuandaa Sera ya Menejimenti ya Mali za Serikali (Government Asset Management Policy). Sera hiyo ambayo inaandaliwa chini ya uratibu wa Wizara ya Fedha na Mipango itasimamia menejimenti ya mali zote za Serikali yakiwemo magari. Sera hiyo pamoja na mambo mengine itaelekeza utaratibu mzima wa ununuzi, utunzaji na ufutaji/uondoshaji wa mali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inaendelea kukamilisha Sera hiyo, ununuzi, utumiaji na uondoshaji wa magari ya Serikali utaendelea kusimamiwa na Sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Sura ya 410 na kanuni zake, Sheria ya Fedha na kanuni zake pamoja na miongozo inayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa magari yote ya Serikali hununuliwa kwa pamoja (bulk procurement) ili kuipunguzia Serikali gharama za ununuzi. Kwa mujibu wa sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Sura 410, Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi wa Serikali (GPSA), ndiyo yenye dhamana ya ununuzi baada ya kupata kibali cha ununuzi wa magari hayo toka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuzingatia viwango (specifications) vinavyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma pamoja na kanuni zake, matengenezo na usimamizi wa matengenezo ya magari yote ya Serikali hufanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA). Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, miongozo inayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma uondoshaji (disposal) wa magari ya Serikali katika matumizi ya umma hufanywa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Matwiga Wilayani Chunya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji ilipanga kutekeleza mradi wa bwawa la Matwiga kwa awamu mbili. Katika awamu ya kwanza Serikali imekamilisha ujenzi wa bwawa la Matwiga lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo 248,000 kwa ajili ya kuhudumia vijiji 16 vya Matwiga, Isangawana, Mazimbo, Mtanila, Igagwe, Kalangali, Lupa, Ifumwe, Lyeselo, Nkung’ung’u, Majengo, Magungu, Lualaje, Mwinji, Mamba na Mtande. Ujenzi wa bwawa hilo ulianza tarehe 17 Mei, 2015 kwa kwa kumtumia Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Bwawa (DDCA) ambapo ulikamilika tarehe 23 Desemba, 2017. Hivi sasa mradi huu uko katika kipindi cha mwaka mmoja wa matazamio (Defect Liability Period).
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha katika kipindi hiki ambapo bwawa lipo katika muda wa matazamio, kumetokea uharibifu kwenye baadhi ya miundombinu ya utoro wa maji (spillway) ambapo mkandarasi ameagizwa kufanya marekebisho na kuyakamilisha mara baada ya mvua za masika kusisima.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya utekelezaji wa ujenzi wa Bwawa wa Matwiga inahusu ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji kwenye bwawa hili kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji vilivyokusudiwa. Tathmini ya kumpata mtaalam mshauri wa kusanifu miundombinu ya usambazaji wa maji inaendelea na usanifu wa miundombinu unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2018. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, Idara ya Mahakama iliandika Ripoti za Sheria (Law Reports) ngapi kwa mwaka 2017?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Tanzania inatumia mfumo wa kisheria wa Common Law ambao maamuzi ya Mahakama za juu yana nguvu ya kisheria na yanazibana Mahakama nyingine za chini katika kufanya maamuzi ya kesi. Msingi huo wa kisheria unaofahamika stare decisis unazitaka Mahakama kutumia misingi ya tafsiri ya kisheria yaliyotolewa na Mahakama za juu na wakati mwingine zilizoamuliwa na Mahakama iliyo na mamlaka sawa endapo kesi zinafanana. Hata hivyo, Mahakama ya juu kabisa kama ilivyo Mahakama ya Rufani hapa Tanzania inaweza na ina mamlaka ya kubadilisha msingi au tafsiri ya sheria iliyotajwa huko nyuma inaposikiliza shauri jipya.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha msingi huo unafuatwa, uchapishaji wa mara kwa mara wa maamuzi ya Mahakama katika Law Reports ni muhimu ili wanasheria, Majaji na watu wote waweze kujua ni msingi gani na uamuzi upi wa sheria umewekwa na Mahakama katika kesi fulani iliyofikishwa Mahakamani na kuamuliwa. Kwa kufuata utaratibu huo, tangu mwaka 1921 Law Reports zimekuwa zikichapishwa Tanzania. Hivyo basi, taarifa za sheria ni mfululizo wa vitabu ambavyo vina maoni ya Mahakama kutoka kwenye baadhi ya kesi zilizoamuliwa na Mahakama ambazo zinatakiwa kufuatwa na Mahakama nyingine.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017 Mahakama ya Tanzania kupitia Bodi ya Uhariri ya Taarifa za Sheria za Tanzania (Tanzania Law Reports Editorial Board) imeandaa Law Reports zipatazo nne ambazo ni Law Report ya mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017. Kwa sasa Law Reports hizo zipo katika hatua na taratibu za mwisho ikiwa ni pamoja na kufanyiwa uhakiki wa kina wa kiuhariri na taratibu zingine za ununuzi kwa ajili ya kumpata mzabuni wa kuchapisha Law Reports rasmi.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni muswada wa kurekebisha Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2004 ambayo imepitwa na wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hapa nchini husimamiwa na Sheria ya Tumbaku Na. 24 ya mwaka 2001, Sura ya 202 ya Sheria za Tanzania (Tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 2000) pamoja na Kanuni za Sheria ya Tumbaku za mwaka 2012 (Tangazo la Serikali Na. 392 la mwaka 2012). Kabla ya Sheria ya mwaka 2001 zao la Tumbaku lilikuwa likisimamiwa na Sheria ya Bodi ya Tumbaku ya mwaka 1984 yaani The Tobacco Processing Marketing Board, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997 ambazo zilifutwa kwa Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya urazinishaji wa bodi za mazao, Sheria ya Sekta ya Tumbaku ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2009 kupitia Sheria Na. 20 ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mazao ya mwaka 2009. Pamoja na mambo mengine, Sheria ya Tumbaku iliweka majukumu ya pamoja, majukumu ya usimamizi, ugharamiaji wa majukumu pamoa na mkutano wa wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, sheria na kanuni hizo zinaweka masharti ya msingi kwa ajili ya kuzingatiwa na mkulima, mnunuzi na msindikaji wa tumbaku ili kuhakikisha kuwa tumbaku inayozalishwa na kusindikwa hapa nchini inakidhi ubora unaokubalika kimataifa na hivyo kuwezesha kupata soko la uhakika pamoja na kumlinda mlaji au mtumiaji wa bidhaa ya tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 Wizara inatarajiwa kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali za mazao ikiwemo Sheria ya Tasnia ya Tumbaku. Kwa sasa Wizara inaendelea kupitia sheria zinazosimamia sekta ya kilimo ili kuimarisha na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazao mbalimbali hususani mazao ya biashara.
Kuhusu Sheria ya Tumbaku Wizara kwa kushirikianna wadau inaendelea kupitia na kuainisha changamoto zilizopo katika sheria hiyo na baada ya zoezi hilo kukamilika, marekebisho ya sheria hii yatawasilishwa Bungeni kwa mujibu wa Kanuni na taratibu zilizopo. Aidha, sheria hiyo haijapitwa na wakati, bali marekebisho yanayokusudiwa kufanyika ni kwa ajili ya kuboresha sheria hiyo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa zao la tumbaku.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Shirika la Kilimo Uyole lina Kituo cha Utafiti katika Kitongoji cha Nkena, Kata ya Mtanila, Wilayani Chunya; na kwa kuwa kituo hicho kimehodhi eneo kubwa sana na hakijafanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi na tano (15):-
Je, ni lini Serikali italiacha eneo hilo kwa wananchi kwa shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa kilimo, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, nianze kutoa maelezo ya utangulizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lililokuwa linajulikana kama Shirika la Kilimo Uyole sasa hivi ni Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole ambacho makao yake yapo Uyole Mbeya. Kituo hiki kiko chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI - Tanzania Agricultural Research Institute) chini ya Wizara ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Utafiti Tumbaku Tanzania (TORITA - Tobacco Research Insitute of Tanzania) inatumia maeneo ya ardhi yaliyopo Tumbi, Tabora pamoja na Mtanila, Chunya na Seatondale kule Iringa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa tumbaku kwa lengo la kuwapatia wakulima wa tumbaku teknolojia bora ikiwemo mbegu bora zinazostahili visumbufu vya tumbaku na ujengaji wa mabani bora. Aidha, watafiti kutoka Uyole Mbeya wamekuwa wakitumia kituo hiki kwa nyakati tofauti kufanya utafiti kwa mazao mbalimbali ikijumuisha mahindi na maharage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya utafiti wa Tumbaku Tanzania TORITA bado inahitaji rasilimali ardhi hiyo kwa ajili ya shughuli za utafiti kwa mahitaji ya sasa na ya baadaye. Ikumbukwe rasilimali ardhi kwa ajili ya matumizi ya utafiti huwa inatengwa kwa kuzingatia mahitaji ya miaka mia mbili ijayo. Taasisi hii ina mikakati mikubwa ya kuwezesha wakulima kupata mbegu bora suala ambalo litahitaji eneo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hivi sasa inaendelea kuboresha huduma zake mbalimbali za utafiti kupitia TARI ambayo itakuwa na msukumo mkubwa na kujiendesha yenyewe ikishirikiana na sekta binafsi. Hivyo, kuhitaji eneo hilo kwa ajili ya kupanua shughuli zake zote za utafiti.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Gereza katika Wilaya ya Chunya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi sasa nchini kuna Wilaya 51 ambazo hazina Magereza ya Wilaya ikiwemo ya Chunya. Hata hivyo, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na Gereza ili kuwahifadhi wahalifu wa Wilaya husika, kwani uwepo wa Gereza kwenye kila Wilaya utapunguza gharama za kuwasafirisha wahalifu kutoka Wilaya moja na kuharakisha uendeshwaji kesi sambamba na kupunguza msongamano wa mahabusu.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa magereza kwa awamu kwenye Wilaya zisizokuwa na magereza. Hata hivyo, kasi ya ujenzi huo imekuwa ni ndogo kutokana na kuathiriwa na uhaba wa rasilimali fedha. Hivyo Serikali inadhamiria kujenga na kuendelea na ujenzi huo kwenye Wilaya zisizo na Magereza ikiwemo Wilaya ya Chunya kadri ya hali ya Bajeti itakavyoruhusu.