Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haroon Mulla Pirmohamed (2 total)

MHE. HAROON M. PIRMOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri amesema Serikali iliunda timu ya wataalam kupitia upya mipaka iliyotangazwa ili kutoa mapendekezo kuhusu mipaka hiyo ya GN. Na. 28. Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba zoezi hili litamalizika lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa mgombea Urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana aliwaahidi wananchi wa Mbarali wanaoishi katika vijiji hivyo 21 kumaliza kero hiyo na kwa kuwa mgombea huyo sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, Mheshimiwa Waziri kuendelea kuchelea kutoa jibu hili haoni kama anapinga ahadi aliyotoa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni lini au ni baada ya muda gani zoezi hilo ambalo linakamilishwa na Kamati iliyoundwa litakamilika? Nimepitia taarifa ya awali ya Kamati hiyo ambayo tumesema inakamilisha kazi iliyopewa, napenda kukufahamisha kwamba kazi hiyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja itakuwa imekamilika ikiwa ni pamoja na kwenda kufanya ukaguzi wa maeneo yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, pengine jambo muhimu si kuzungumzia zaidi kwamba kuna ukiukwaji au kuna utaratibu ambao unaonekana kupingana na ahadi aliyoitoa Mheshimiwa Rais, jambo la msingi hapa ni kwamba kazi hii ni muhimu na suala la kushughulikia changamoto za wananchi pia ni ahadi ya Serikali hii ya Awamu ya Tano na katika kipindi hicho ambacho nimekisema suala hilo litakuwa limekamilika na kupatiwa uvumbuzi.
MHE. HAROON M. PIRMOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu lake Mheshimiwa Waziri amesema kazi ya usanifu pamoja na utayarishaji wa tender documents umefanyika tangu mwezi Agosti, 2012 sasa ni zaidi ya miaka mitano. Sasa nimuombe kwamba airuhusu Wizara yake itenge fedha kwa mwaka 2018/2019 kwa ajili ya kukamilisha barabara ya Rujewa – Madibira ili ujenzi wa lami ukamilike? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia, anafuatilia sana barabara hii. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja tumetenga fedha za kutosha na kwamba ujenzi wa barabara hii utaanza.
Pia nikufahamishe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbarali, pamoja na barabara hii pia iko barabara hii ya Igawa – Mbarali ambayo umekuwa ukiifuatilia; sehemu ya Mbarali – Ubaruku kilometa 8.9 nayo iko kwenye mpango katika mwaka unaofuata tutaijenga barabara hii. Ahsante sana.