Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Saul Henry Amon (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Vilevile niwashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Rungwe kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, sina mengi lakini vilevile siko mbali na Profesa Norman alichokizungumza, kwamba, utalii na hata mzungumzaji aliyepita ameongea hicho hicho, utalii umeangaliwa sehemu moja, hilo ndilo langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu misitu. Pamoja na kwamba kuna historia na jiografia ya misitu iliyopo na inayovunwa lakini naona ni Mufindi, Mufindi, Mufindi wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msitu pale Mbeya ulikuwepo siku zote, siku hizi naona ni jangwa. Msitu wa Kawetele, toka ulivyovunwa sijui mwaka gani lakini mpaka leo hii Kawetele hakuna miti, Kawetele ni jangwa, hatujui kwa nini wanafanya hivi na kwa nini Maliasili na Utalii wameamua kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sababu ya kujiuliza, tunashangaa hata Mbeya, Iringa tuna matatizo ya madawati, lakini hiyo miti ingeweza kusaidia madawati kwa ajili ya thamani ya ofisi zetu na shule zetu. Mimi kwa Mheshimiwa Waziri nina ombi kwamba, ningependa kuona mapema iwezekanavyo Kawetele inarudishwa kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna watu wanaoshambulia misitu ambayo imewekwa kama hifadhi. Rungwe na misitu mingine ya asili bado haihifadhiwi inavyotakiwa, sijajua ni wapi ambako mnaangalia, ni nchi nzima au kuna kipande ambacho mmeamua kukiangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utalii, tunapozungumza maliasili, ni lazima tuzungumzie nchi yote kwa ujumla; kwa sababu pamoja na kwamba, ina faida kwa ajili ya kupata fedha, lakini vilevile kuna faida kwa ajili ya mazingira yanayoharibika na kupotea bure kwa sababu tu wahusika hawafuatilii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haiwezi itupe wananchi wa Mbeya tupande ile miti tuweze kuitumia ile ardhi; kwa sababu Mbeya kuna watu wengi. Ukiangalia Mbeya misitu mingi imepandwa na wananchi na bado inavunwa vizuri na wananarudishia iweje Serikali ambayo inapata faida, kwa sababu ile ni kama biashara ya Serikali. Chukueni faida yenu lakini rudisheni mtaji pale pale, kwamba wakati wa kuvuna vilevile irudishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye Sekta ya Utalii. Mchangiaji hoja aliyepita ameongea habari ya kwamba, kuna service mbovu, lakini hiyo yote ni kwa sababu ya kutokuwa na utamaduni. Hatuna chuo ambacho ni thabiti kwa ajili ya kufundisha watu watakaohudumia hoteli zetu ili kuwe na kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunacho chuo lakini hakitoi na tumebakia kugombana na kusema hawa hawafai. Angalia wenzetu wanaotoka nje standard zao wanavyofanya, ni kwa sababu wamewekeza kwenye vyuo vya utalii. Huko wanapata ma-manager wazuri, wapishi wazuri, wahudumu wazuri. Sisi hivyo vyuo viko wapi? Kweli mtu atoke Mwanza, aje ajifunze Dar es Salaam peke yake ni kweli? Mtu atoke Mbeya aende Dar es Salaam kujifunza habari ya chuo. Vyuo vilivyopo havikidhi haja ambayo inaweza ikatoa international services.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo bado kwenye utalii. Utalii hautangazwi Nyanda za Juu Kusini na kusini mwa Tanzania na maeneo mengine, watu mmejikita maeneo ya kaskazini peke yake. Mheshimiwa Waziri aende Malawi, akaone utalii unavyofanya kazi kwenye Ziwa Nyasa. Sisi hapa tuna Ziwa Nyasa na tuna fukwe ambazo ni nzuri, ambazo hazichafuki, hazina takataka, lakini hatuzitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono asilimia mia moja mchangiaji aliyepita kwa uchangiaji wake, ametoa mchango wa kizalendo. Naomba Wizara na vitengo vyake, viweze kutangaza utalii uliopo. Kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini wameongea habari ya barabara kwenda kwenye mbuga za wanyama, vilevile tunaongea habari ya barabara kwenda Mlima Rungwe, hakuna barabara watu waende wakatembelee Mlima Rungwe. Hatuna barabara kwenda kwenye fukwe nzuri za Nyasa, kuna Ziwa Ngozi ambalo haliingizi maji wala halitoi maji, hamna anayetangaza. Tuna Ziwa Kisiba, kuna ziwa zuri sana ambalo halichafuki, halitoi maji na wala haliingizi maji lakini hatulitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo wangu ninavyojua ni kwamba, hii Wizara inafanya biashara, tunaweza kufikiria kwamba, inafanya biashara kwa kulipa Serikali mapato ya bilioni 10 au15, lakini si biashara ambayo watu tungejiwekeza zaidi kwenye hayo maeneo kama ingekuwa zaidi ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingi sana ambazo ningeweza kuchangia, lakini kufikia hapo haya yalikuwa ni mawazo yangu na kwamba, tuchukulie umuhimu wa hali ya juu kutangaza vitega uchumi vyote, vivutio vyote ambavyo vipo maeneo yote ya Tanzania bila kujali ni wapi, watu waende kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempa Mheshimiwa Waziri mfano wa kwenda Malawi akaangalie, wanatoka watu sehemu mbalimbali lakini fukwe tulizonazo sisi ni nzuri zaidi kuliko zilizoko Malawi. Haya ni yangu machache kwa leo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hii Wizara ya Miundombinu, vilevile namshukuru Mungu kwa kunipa huu muda wa kuchangia Wizara hii ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niaze kushukuru na kumpongeza Rais kwa uamuzi wa kuanzisha hii standard gauge. Nimpongeze Rais vilevile kwa ununuzi wa ndege bila kujali watu watasema nini, kuna watu wanakebehi kwamba ndege hazina maana, lakini tunavyojua kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi zile ndege zilizonunuliwa ni manufaa ya Taifa zima pamoja na utalii wa ndani kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri wa Miundombinu ambaye nimemwona kwenye tv akizunguka kila kona ya Tanzania kuangalia ujenzi wa miundombinu ya nchi hii, nakupongeza sana. Vilevile nimpongeze Naibu wake na Katibu wake ambao wote huwa nawaona kwenye vyombo vya habari wakizunguka na kuzungukia kuangalia miundombinu ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipongeze pia ujenzi wa flyover zilipo Dar es Salaam kwani zitapunguza msongamano mkubwa uliopo Dar es Salaam ambao umesababisha shughuli nyingi za kimaendeleo zisiende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa standard gauge ambao utaharakisha maendeleo ya nchi yetu kwa kubeba mizigo, abira na sasa Mwanza tutakuwa tunaenda kwa saa nane badala ya siku mbili. Kigoma tutakuwa tutakwenda kwa saa nane mpaka tisa badala ya siku mbili. Hivyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake na watendaji wake wakuu wakiwemo Mawaziri pamoja na Manaibu wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, nia yangu ambayo nimeijia hapa hasa kwa Mkoa wangu wa Mbeya. Mkoa wa Mbeya kama mnavyoujua na wote Mawaziri mmeshafika pale, barabara ya kuingia katikati ya mji ni tatizo kubwa sana. Kama alivyozungumza mchangiaji aliyepita amesema kwamba mahali pa dakika kumi tunatumia saa mbili, ni kweli mtu ukifika Uyole kama ndege itaondoka baada ya saa mbili na nusu itakuacha, mahali ambapo tunaweza kutumia nusu saa tu kutoka Uyole mpaka Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya bypass ya Mbeya ambayo ni Uyole bypass kwenda mpaka Songwe tunaomba wananchi wa Mbeya ifanyiwe upembuzi yakinifu haraka ili iweze kujengwa kwani Mbeya ni lango kuu kabisa ambalo linatumia nchi zaidi ya nane kwa kutumia barabara hiyo. Barabara hiyo ni kwa ajili ya kwenda Zambia, Malawi, Congo, Zimbabwe wote wanapita njia hiyo lakini usumbufu ni mkubwa sana, naomba mtusaidie.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nina ombi kwa Waziri kuhusu uwanja wa ndege tumewahi kurudi zaidi ya mara mbili, kwa sababu tu uwanja hauna taa za kuongozea ndege pale chini. Gharama yake sijajua ni kiasi gani kikubwa, mwaka huu naona ni mwaka wa pili tukizungumzia suala hilo wakati huo huo Serikali ilishaahidi kwamba itatoa hela ingawa nimeona bajeti ya mwaka jana sijaona hata senti tano iliyoenda Songwe, kama ipo nitaomba kuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudi kwenye Jimbo langu la Rungwe. Jimbo la Rungwe ni moja kati ya majimbo ambayo yanatoa chakula, viazi vingi mnavyoviona vinatoka Rungwe pamoja na ndizi zote zinatoka Rungwe, lakini Katika Wilaya ya Rungwe kuna kata tatu hazina barabara kabisa, hivi ninavyozungumza saa hizi zimekatika ukienda kata ya Swaya, kata ya Kinyala hakupitiki. Matokeo yake wakulima wa kule wanapata taabu kweli, tungeomba hizo barabara badala ya kuendelea kushughulikiwa na Halmashauri barabara ya kutoka Igogwe - Lubala - Vibaoni - Malangali mpaka Mbeya Vijijini tungeomba iwe barabara ya mkoa kwani pale pana mazao mengi, nazungumza sasa hivi hata tukiongozana na Waziri ataenda kukuta mazao yanavyoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuyatoa mazao katika eneo hilo inabidi urudi umbali mrefu kilometa 40 halafu ndiyo uanze kupandisha nayo kwenda Mbeya kiasi kwamba wakulima wa eneo hilo pamoja na kwamba wanalima sana viazi, mahindi, maharage yananunuliwa kwa bei rahisi kiasi kwamba hawapati faida na gharama ya kilimo kile inakuwa ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba hiyo barabara uiangalie. Narudia hiyo barabara kama hujaiandika, barabara ya Igogwe kwenda Lubala - Vibaoni - Malangali ambayo inakwenda Swaya kwenda kutoka Mbeya Vijijini.

Hiyo ni barabara muhimu sana na kuna vyakula vingi sana, wakati kuna sehemu zingine watu wanakufa kwa njaa wanaumia kwa njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ambayo imepandishwa daraja, ninawashukuru sana Waziri pamoja, Naibu Waziri na Watendaji wako kwa kuipandisha daraja kuwa ya Mkoa. Barabara ya kutoka Pakati - Njugilo - Masukuru kwenda mpaka mpakani. Ile barabara wenzetu upande wa Kyela wamefika mpaka kwenye mpaka. Ni sehemu ndogo ili uweze kwenda Kyela kutoka eneo la Matwebe inabidi uzunguke utumie saa mbili badala ya kutumia dakika 20, vyakula, matunda, mpunga hapo vinaaribika kwa sababu hakuna mtu ambaye anaweza akazunguka kwa kiasi kikubwa wakati huu wa mvua. Ikifika kipindi cha mvua pale mahali panakuwa ni kisiwa, huwezi tena kuenda, hizo Kata mbili zinakuwa zimebaki na kila tunapokwenda kwa ajili ya kampeni tatizo ni hilo hilo.

Naomba Waziri kwa vile umeipandisha hadhi hiyo barabara naomba uifanyie angalau ukarabati kwa sababu kule hata material ile moram ni nyingi sana maeneo yale ambayo ni kazi ndogo, kwa sababu daraja ni moja na sehemu korofi hazizidi tatu ambazo ukisizimamia zinaweza zikawa zinakapitika moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine haya ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendeleza kujenga barabara ya Tukuyu kwenda mpaka Lwangwa kujenga barabara ya njia panda mpaka Matema hiyo nashukuku na tunaomba kila mwaka tuendelee kuzitafutia hela zile barabara, kwani zitafunguka, utalii ni mkubwa ukizungumza Matema ni utalii mkubwa sana na pale mnajenga bandari kwa ajili ya meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka niishukuru na kuipongeza Wizara hii ni kwa kutengeneza na kutimiza ahadi. Ahadi ya kutengeneza meli katika Ziwa Nyasa. Zile meli tumeziona zimeshaingia majini na meli ya tatu ya abiria inakaribia kuisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwashukuru sana na kuwapongeza sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Fedha. Kwanza nimshukuru Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti yake, mimi nina mambo mawili makubwa. Wakati wa kukusanya kodi, kodi ni sawa na biashara nyingine yoyote lakini hapa kuna vikwazo ambavyo wafanyabiashara wengi tunavipata na kama Waziri hajalisikia hilo atume timu yake kwa wafanyabiashara, hasa wanaoingiza mizigo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna huu mfumo wa TBS na tukiangalia kwamba nchi ya Tanzania sio nchi yenye viwanda kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wa Tanzania sio wakubwa wa kila mmoja kwenda kutafuta kiwanda chake cha kuleta mizigo. TBS kuna tatizo, hasa la ile faini ya asilimia 15 ya invoice value ya mzigo anapoleta hapa Tanzania. Hilo ni tatizo kubwa sana ambalo naomba Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha iliangalie upya ni namna gani wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna Wizara mbili, kuna Wizara ya Afya kupitia TFDA kwa mambo ya vyakula na dawa na TBS ambayo inafanya sehemu zote. Hata hivyo, utaratibu wa TFDA ni mzuri, unaeleweka, pamoja na kwamba ni ghali, unakwenda unasajili bidhaa zako hapa Tanzania na wanakupa certificate. Ukishapewa mara moja huna usumbufu tena baada ya hapo, kwa hiyo TFDA hawana matatizo ukishasajili bidhaa zako, lakini TBS tatizo lake ambalo linawafanya Watanzania wengi wasiweze kuingiza mizigo, Watanzania wengi wapite porini ndiyo maana unasikia, Mheshimiwa Bashe ameongea hapa kwamba watu wanapita Kenya, wanapita Kenya kwa sababu ya kuikimbia TBS, wanaingizaje, haijulikani.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS wangechukua mfumo wa TFDA nina uhakika kwamba ingepunguza usumbufu mkubwa sana, kwamba mimi nilete bidhaa zangu, TBS wazikague kwa sababu viwanda vinavyotengeneza mizigo inayopita TFDA ndiyo hivyohivyo vinavyotengeneza kupita TBS, lakini TBS kila unapoingiza mzigo unakuwa na certificate yake. TFDA wakikusajili utaisajili tena hiyo mizigo yako baada ya miaka miwili, unakuta usumbufu wa TFDA unakuwa haupo lakini TFDA anakwambia chakula ingiza, unaingiza TBS anakwambia hujasajili na kama hujasajili TBS ulipe asilimia 15 ya invoice value. Kwa kweli imewafanya wafanyabiashara wengi sana wawe na manung’uniko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri na timu yake awaulize wafanyabiashara nini kikwazo kikubwa cha biashara. Kama anavyojua tunavyoingiza mizigo ndivyo tunavyoweza kuuzia nchi nyingine za jirani, na ukiuzia nchi nyingine za jirani tutapata faida si moja tu kwa ajili ya kuingiza mizigo, kwanza wanakuja kuchukua mzigo, wanakuja wanalala, wanatumia usafiri wa nchi wa ndani wa kwetu na mambo mengine, akina mama lishe wanapata vyakula, wanapata hela. Kwa hiyo kupitia TBS kwa kweli hilo ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iliangalie hilo, kwa nini kazi za TFDA zisiwe za kwake. Tumepita nchi nyingi, ukiangalia Nigeria, Marekani na kwingineko, ukiambiwa kwamba hawa wanashughulika na mambo ya vyakula na dawa ni Wizara nyingine na ambao wanashughulika na mambo ya viwango ni Wizara nyingine na viwango vingekwenda kwa viwango na TFDA wangeendelea na kazi yao ya kukagua kwamba hivi vyakula na madawa viko salama kwa mlaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mapato ya nchi yataongezeka, watu watapungua. Kwa sababu ukiangalia TRA hakuna usumbufu kabisa kama ilivyokuwa zamani, ukiangalia bandarini hakuna usumbufu kama ilivyokuwa zamani lakini ukifika unakwama, kwa sababu sisi wafanyabiashara wa Tanzania wengi ni wadogo, ni watu ambao hatuna mitaji mikubwa, tunavyoenda kununua mizigo iwe ni Ulaya, iwe ni Marekani, iwe ni China au Dubai, tunachanganya, hivyo huwezi kupata na usumbufu wake ni mkubwa mno. Wakati unanunua mzigo utachukua zaidi ya wiki sita ili kupata certificate ya TBS. Hilo naomba waliangalie walipe umuhimu wa hali ya juu, watu wanatoroka na mizigo kupita sehemu nyingine kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapo Mheshimiwa Waziri amenielewa na kama nilivyomwambia, sehemu nyingine zake zote ziko sawasawa; TRA ambako watu walikuwa wanaogopa pako sawasawa, vitu vinakwenda sawasawa wala ndani hatuingii. Ukienda TFDA unakwenda na certificates zako nimeleta mzigo huu, hatusumbuliwi, unapewa invoice. Hata hivyo, ikifika sasa, kama ninavyomwambia, ni kweli nikikaguliwa nitakwenda kukaguliwa wiki sita, badala ya kuondoka siku tatu nitakwenda kukaa zaidi ya miezi miwili nikisubiria ukaguzi na mizigo, lakini kibaya zaidi, kwa nini hawa TBS ambao wana jukumu wasichukue kwamba wewe unachukua kiwanda gani, mimi nitasema nauza vipodozi nachukua Procter and Gamble, basi lete hivyo vitu tuvipime kama viko sawasawa, au nimechukua Unilever, tuvipime viko sawasawa, wanipe certificate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kuvipima kama viko salama, lakini na wenyewe watupe certificate ili tusiwe tunasumbuka kila mara tunapoingiza mizigo. Huu usumbufu Mheshimiwa Waziri ataona sasa hivi umetengeneza monopoly, maana ukizungumza atakuwa analeta mtu mmoja, ukimwambia huyu ndio anayeleta chuma basi ataleta huyo huyo kwa sababu ndiye aliye na nafasi na access ya kwenda kwenye kiwanda hicho kinachohusika na kumpimia mizigo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hilo ambalo watu wengi wameliongelea, nadhani ni la kuongezea tu, kuhusu hizo milioni 50. Kwa kweli ni matatizo, Waziri akakae na timu yake, milioni 50 watu tuliwaahidi na zilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kila tukienda kwenye mikutano tunaulizwa kama vile tuliwakopa. Kwa hiyo, wakae wakijua kwamba ahadi ni deni, hilo waliangalie kwa uzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wameliongelea watu na mimi nasisitiza tu, kwamba Serikali iangalie kwamba kuzichukua zile hela waangalie namna ya kuzirudisha na namna ya kuzifuatilia lakini zirudi benki tuendelee kukopa. Mambo yetu yamekwama, benki wanakataa kutupa hela, benki kama CRDB ambayo walikuwa wanaweza kukupa mara moja, hawana hela. Tafuteni utaratibu, zirudisheni kule kama na ninyi mnataka riba basi chukueni riba kutoka benki ili tuendelee kukopeshwa na ndiyo uchumi wenyewe, hakuna uchumi mwingine, kama wananchi hawana hela utapata wapi hiyo kodi, maana hawanunui, utapata wapi hiyo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hayo ndiyo niliyokuwa nayo. Ahsante kwa kunipa nafasi hii kutoa mchango huu.