Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Issa Ali Abbas Mangungu (11 total)

MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Jimbo la Mbagala lina wakazi zaidi ya 800,000 kutokana na sensa ya watu na makazi lakini ina Mahakama ya Mwanzo Kizuiani tu.
(a) Je, kwa nini Serikali imeshindwa kujenga mahakama katika Jimbo la Mbagala kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakazi?
(b) Kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma za mahakama Jimbo la Mbagala katika Kata za Chamazi, Mbande, Kijichi, Kibungwa, Kibondemaji na Tuangoma; je, Serikali ipo tayari kujenga mahakama katika kata hizo hata kwa mpango wa dharura?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kukuona na afya njema.
Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Mahakimu Namba 2 ya mwaka 1984, Mahakama ya Wilaya huanzishwa kwa kuzingatia kuwepo kwa Mamlaka ya Wilaya ya Kiserikali. Uanzishwaji wa Makahama ya Wilaya hutegemeana na hali ya upatikanaji wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miundombinu mingine kama majengo, viwanja na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, aidha, uanzishwaji wa Mahakama za Mwanzo (Primary Courts) huhitaji walau kila kata za Wilaya husika iwe na Mahakama ya Mwanzo moja ingawa hakuna kizuizi kwa mamlaka kuanzisha Mahakama za Mwanzo zaidi ya moja kwenye kata moja kutegemeana na mahitaji ya eneo husika na vipaumbele vya mahakama na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa una Wilaya tano kiutawala (Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na Ubungo) na kata zaidi ya 102 zenye idadi ya wakazi zaidi ya 5,000,000 wanaohitaji huduma hii muhimu, ni dhahiri kwa takwimu tajwa hapo juu Mkoa wetu wa Dar es Salaam unahitaji Mahakama za kisasa za Wilaya tano na Mahakama za Mwanzo 102 angalau kukidhi kila kata ukilinganisha na mahakama 12 zilizopo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mahitaji hayo, tayari Wizara kwa kushirikiana na mahakama tumepeleka maombi maalum kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya na Halmashauri zake waweze kutupatia viwanja vya umma (public plots) vyenye kutosheleza mahitaji ya Mahakama za Mwanzo na Wilaya kwenye maeneo ya makazi ya mjini na yenye shughuli nyingi kama Jimbo la Mbagala. Tunashukuru uongozi wa baadhi ya Wilaya kwa kuanza kutupatia viwanja ambavyo tumeanza kufanya maandalizi ya ujenzi wa mahakama hizo.
(b) Mheshimiwa Spika, tunamuhimiza Mheshimiwa Mbunge na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Wilaya zake kutoa viwanja vyenye nyaraka rasmi ili tuweke kwenye mpango wa dharura wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwenye maeneo yenye kuhitaji kama vile Chamazi, Mbande, Kijichi, Kiburugwa na Kibondemaji.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Riba kubwa katika benki zetu nchini imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake na vijana kupata mikopo.
(a) Je, Serikali ipo tayari kuandaa utaratibu maalum wa riba elekezi itakayowawezesha wanawake na vijana kupata mikopo benki kwa riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuziagiza benki za biashara kulegeza masharti ya dhamana kwa vijana na wanawake ambayo yanarefusha mchakato wa upatikanaji wa mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye kipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha nchini ya mwaka 1991, Serikali iliruhusu benki binafsi kutoa huduma za kibenki hapa nchini kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma hizo zilikuwa zinatolewa na vyombo vya fedha vya Serikali tu. Hatua hii ilikusudia kuongeza ushindani katika sekta ya fedha na kuhakikisha kwamba huduma za kibenki zinatolewa kwa ufanisi na kwa kutegemea nguvu na mfumo wa soko huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maombi mbalimbali juu ya kupunguza viwango vya riba ikiwa ni pamoja na Benki Kuu kuweka ukomo wa riba au riba elekezi ya mikopo. Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Benki Kuu imepewa dhamana ya kusimamia sekta ya fedha na usimamizi wa mabenki hapa nchini. Kama msimamizi wa mabenki, Benki Kuu kuweka ukomo wa riba sio tu inapingana na jukumu lake la msingi la kusimamia mabenki hayo, bali pia inapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria. Kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, Benki Kuu haina mamlaka kisheria ya kuweka ukomo au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya riba katika mabenki na taasisi nyingine za kifedha hupangwa kwa kutegemea nguvu ya soko, sifa za mkopaji, ushindani katika soko, gharama za upatikanaji wa fedha, mwenendo wa riba za dhamana za Serikali, gharama za uendeshaji na matarajio ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Benki Kuu imeendelea na jukumu lake la msingi la kuhakikisha kuwa mfumo huu unaendeshwa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ili kulinda maslahi ya Taifa na uchumi kwa kusimamia na kudhibiti mambo yafuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa ingezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko kuhakikisha kuwa ongezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei;
(ii) Ongezeko la mikopo ya mabenki haliathiri uzalishaji mali na linalingana na malengo ya ujazi wa fedha;
(iii) Soko la dhamana za Serikali linaendeshwa kwa ufanisi ili liweze kutoa riba elekezi kulingana na hali ya soko na uchumi kwa ujumla; na
(iv) Mwisho kuhimiza mabenki na taasisi zote za fedha kutumia takwimu za Credit Reference Bureau.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Wazee wa Mabaraza katika Mahakama Kuu hasa Dar es Salaam husikiliza kesi zinazohusu mauaji na kulipwa sh. 5,000:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuwaongezea posho wazee hao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa Wazee wa Baraza katika Mahakama zetu na umuhimu wa kutoa posho kama motisha. Kutokana na umuhimu huo, Serikali ingetamani sana posho za wazee hao ziongezeke ili kuendana na hali ya uchumi, lakini kwa bahati mbaya posho hizo hutokana na bajeti ya matumizi mengineyo (other charges) ambazo hutengwa na Serikali kwa kila fungu.
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017, Mahakama ya Tanzania ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.27 na mwaka 2017/2018, Mahakama imetenga shilingi bilioni 1.85 kwa ajili ya malipo ya posho ya wazee wa Baraza. Fedha kwa ajili ya Wazee wa Baraza ni fedha zinazotengwa katika eneo la matumizi ya kawaida, hivyo Serikali kupitia Mahakama itaendelea kutenga au kuongeza posho kwa malipo mbalimbali zikiwemo posho kwa ajili ya Wazee wa Baraza.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala kwamba Wazee wa Mahakama wataongezewa posho zao kwa kadri bajeti itakavyokuwa inapatikana.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
Je, ni lini miradi ya umeme yenye zabuni Na. PA/001/2015/DZN/W/12 maeneo ya Chamazi Dovya, Kwa Mzala 1 – 3, Mbande kwa Masista na Chamazi Vigoa itakamilika ili wananchi wa maeneo hayo wapate umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi tajwa hapo juu katika maeneo yaliyotaja Mheshimiwa Mbunge ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Chamazi Dovya kulikuwa na miradi mitatu na yote imekamilika. Kazi ya kupeleka umeme ilijumuisha ujenzi wa kilometa 3.297 za ujenzi ya njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 11, kilometa 1.4 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 na ufungaji wa transfoma nne za KVA 100 na transfoma mbili za ukubwa wa KVA 200 kila moja. Miradi hiyo mitatu iligharimu jumla ya shilingi 585,271,539 na ilikamilika kati ya Juni, 2016 na Januari, 2017 na kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanapata umeme.
Mheshimiwa Spika, Mbande kwa Masista kuna miradi mitatu; Masista Magogo Na. 1, Masista Magogo Na. 2 na Masista Magogo Na. 3 na kazi ya kupeleka umeme ilijumuisha ujenzi wa kilometa 3.5 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 11, kilometa 15.8 za njia umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 na ufungaji wa transfoma tatu zenye ukubwa wa KVA 100 na transfoma tatu za ukubwa wa KVA 200 kila moja.
Mheshimiwa Spika, miradi hiyo ka ujumla ina thamani ya shilingi 726,075,289.40. Mradi wa Masista Magogo Na. 1 ulikamilika tarehe 17 Juni, 2017 na wateja wanapata umeme. Aidha, miradi ya Masista Magogo Na. 2 na Na. 3 itakamilika mwishoni mwa mwezi Disemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, Chamazi Vigoa kazi ya kupeleka umeme ilihusisha ujenzi wa kilometa 0.99 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 11; kilometa 3.92 za njia ya umeme wa kilovoti 0.4 na ufungaji wa transfoma tatu za ukubwa wa KVA 100 kila moja. Mradi huu wenye thamani ya shilingi 178,584,000 ulikamilika tarehe 9 Juni 2016 na wateja wanapata umeme.
MHE. JAMAL KASSIM ALI (K.n.y MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
Serikali ilitoa mafunzo kwa walimu ambao walihitumu mwaka 2015 lakini walimu hao hawajaweza kuajiriwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaajiri walimu hao walioachwa ingawa kiuhalisi bado kuna uhaba mkubwa wa walimu katika shule za sekondari hasa vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2017 Serikali imeajiri walimu 3,081 wa masomo ya sayansi na hisabati ambao wameshapangwa na kuripoti katika shule walizopangiwa nchi nzima. Ajira hizo zimetolewa kwa walimu waliohitimu mafunzo mwaka 2015 na mwaka 2016. Mpango wa Serikali ulikuwa ni kuajiri walimu 4,129. Hata hivyo, walimu 1,048 wa masomo hayo ya sayansi na hisabati hawakupatikana katika soko wakati wa uhakiki wa vyeti uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepanga kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo walimu katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
(a) Je, Mabaraza ya Wazee katika Mahakama za Mwanzo yapo kwa mujibu wa sheria?
(b) Mahakama ya Mwanzo Kizuiani hulipa posho za Wazee wa Baraza kiasi cha shilingi 5,000 kila wanapomaliza shauri. Je, kwa nini sasa yapata miezi tisa wazee katika Mahakama ya Mwanzo Kizuiani hawajalipwa posho zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya Wazee wa Mahakama nchini yamehalalishwa na sheria. Kifungu cha 9(1), (2) na (3) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 ya sheria za nchi kinaeleza kuwa kutakuwa na matumizi ya Wazee wa Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo na Mahakama za Wilaya na Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mahakama ya Mwanzo ya Mbagala kama ilivyo katika Mahakama nyingine, malipo ya posho za Wazee wa Baraza yamekuwa yakipewa kipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha. Malipo haya yamekuwa yakifanyika kwa mkupuo wa miezi mitatu au minne ili kutoa fursa ya kuweka kumbukumbu za malipo baada ya mchakato wa kukokotoa malipo stahiki kwa kila mlipwaji kulingana na idadi ya mashauri yaliyomalizika ambayo mhusika ameshiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wazee wa Mahakama zote za Mwanzo katika Mkoa wa Dar es salaam ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Mbagala walilipwa posho zao zote. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wazee wa Baraza katika Mahakama ya Mwanzo Mbagala wameshalipwa posho zao kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2017 kiasi cha shilingi 5,760,000. Vilevile kiasi cha shilingi 2,840,000 ambacho ni madai ya wazee hao kwa kipindi cha Desemba, 2017 hadi Februari, 2018, kipo katika mchakato wa malipo na hivyo hakutakuwa na deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa umuhimu wa kipekee katika malipo ya posho ya Wazee wa Baraza ili kutokwamisha mashauri yaliyopo Mahakamani hususan kwa Mahakama za Mwanzo.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
(i) Je, ni lini ujenzi wa kituo kidogo cha kupoza umeme (substation) ya Mbagala utakamilika?
(ii) Je, makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa kituo hicho ulikuwa wa muda gani?
(iii) Je, mkandarasi wa mradi huo yupo ndani ya muda au amechelewesha kazi kwa mujibu wa mkataba na je ni hatua gani zimechukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya Mbagala, Shirika la Umeme nchini (TANESCO) mwezi Februari, 2018 kupitia Mradi wa TEDAP (Tanzania Energy Development and Access Expansion Project) lilikamilisha utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa njia za usafirishaji, usambazaji na vituo vya kupoza umeme katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro. Mradi huu ulitekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi huu kumeimarisha upatikanaji wa umeme katika eneo la Mbagala ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Mbagala ulikamilika na kuanza kufanya kazi rasmi kuanzia tarehe 25 Februari, 2018.
• Makubaliano ya awali ya mkataba wa ujenzi wa mradi mzima ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Mbagala ulikuwa wa miezi 18 kutoka siku mkandarasi alipokabidhiwa maeneo ya ujenzi wa mradi.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi amekamilisha kazi hii nje ya mkataba wa awali kutokana na kuzuiwa kufanya kazi katika baadhi ya maeneo kutokana na baadhi ya wananchi kudai kwamba hawakuridhika na fidia na hivyo kumfanya mkandarasi asikamilishe utekelezaji wa mkataba huu kwa wakati. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa hali ya umeme imeimarika katika maeneo ya Mbagala na Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kuhakikisha hali ya umeme Mbagala inaendelea kuwa ya uhakika. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. EDWIN A. NGONYANI (K.n.y. MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo hayamo katika miradi ya umeme vijijini, maeneo kama vile Changanyikeni, Ponde, Malela, Vikindu, Goroka A, B katika Kata ya Tuangoma na Majimatitu A, Vigozi, Machinjioni A, Mponda katika Kata ya Mianzini, Mzala, Kwa Mapunda, Kisewe, Dovya, Sai A, B katika Kata ya Chamazi?
b) Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la low voltage katika Jimbo la Mbagala hasa maeneo ya Kiburugwa, Kilungule, Charambe, Kijichi, Kibondemaji Chemchem na Tuangoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika maeneo ya Changanyikeni, Ponde, Malela, Vikindu, Goroka ‘A’ na Goroka ‘B’, Dovya Kata ya Tuangoma na maeneo ya Mponda, Vigozi, Churuvi Kata ya Mianzini ilianza Oktoba, 2017 na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Spika, kazi za mradi zinahusiana ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 12.95, njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 41.34, pamoja na ufungaji wa transfoma 19 za Kv 100 na Kv 200, gharama ya mradi ni shilingi milioni 523.84 na utekelezaji wake umefikia asilimia 90.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mbagala hususan maeneo ya Kiburugwa, Kitungule, Charambe, Kijichi, Kibondemaji, Chemchem na Tuangoma kulikuwa na tatizo la uwepo wa umeme mdogo, kuanzia mwezi Juni, 2018 Serikali imechukua hatua za makusudi kuondoa tatizo hilo kwa kuboresha nguvu ya umeme kwenye maeneo hayo na hali ya umeme katika maeneo ya Mbagala imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha msongo wa kilovoti 132/33 chenye uwezo wa Mv 50 Mbagala kilichozinduliwa tarehe 22 Februari, 2018 kimeimarisha hali ya umeme katika maeneo hayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Serikali ilikuwa na utaratibu wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) lakini kwa sasa imefutwa:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali iliifuta posho hiyo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuirejesha posho hiyo?
(c) Katika Jimbo la Mbagala, shule nyingi hazina nyumba za walimu; mfano, Shule za Msingi Mbagala, Maji Matitu na Rangi Tatu. Je, ni lini Serikali itatatua kero hii kwa mkakati maalum kama ilivyoweka mkakati wa upatikanaji wa madawati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haikufuta Posho ya Kufundishia bali iliijumuisha katika mshahara wa mwalimu kwa lengo la kuongeza kiwango cha fedha (pensheni na kiinua mgongo) baada ya kustaafu. Awali posho hiyo ilikuwa inatolewa kwa watumishi nje ya mshahara, hivyo, haikuwa sehemu ya kikokotoo cha mafao ya watumishi baada ya kustaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua upungufu wa nyumba za walimu uliopo katika maeneo yote mijini na vijijini. Hata hivyo, kutokana na urahisi wa walimu na watumishi wengine wa Serikali kupata nyumba za kupanga maeneo ya mjini kama ilivyo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam, kipaumbele cha juu cha ujenzi wa nyumba za walimu kimewekwa zaidi katika maeneo ya vijijini kule ambako kuna mazingira magumu ya kupata nyumba za kupanga ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwenye maeneo hayo.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-

(a) Je, barabara ya Kilwa imeshakabidhiwa kwa Serikali kutoka kwa mkandarasi aliyejenga barabara hiyo (KAJIMA)?

(b) Je, barabara hiyo ipo katika kiwango kinachotakiwa?

(c) Je, ni nani anagharamia ukarabati usiokwisha wa barabara hiyo kati ya Serikali na mkandarasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taratibu za mikataba ya ujenzi wa barabara, kabla ya mradi haujapokelewa na Serikali panakuwepo kipindi cha matazamio ambacho mkandarasi hutakiwa kurekebisha kasoro zozote zitakazojitokeza katika kipindi hicho kwa gharama zake mwenyewe. Utaratibu huu ndiyo unaotumika katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Kilwa ambapo mkandarasi alifanya marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha matazamio cha miaka miwili kuanzia tarehe 15 Mei, 2012 hadi tarehe 31 Desemba, 2014 kwa gharama zake mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyeiiti, mara baada ya mkandarasi kufanya marekebisho ya sehemu zilizokuwa na mapungufu, wataalam wa Wizara walifanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa barabara hiyo ina viwango vya ubora vinavyokubalika kulingana na matakwa ya mkataba na kukabidhiwa rasmi Serikalini tarehe 31 Desemba, 2014. Hivyo, majukumu ya mkandarasi (KAJIMA) yamekamilika katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya kawaida ya barabara hii kama ilivyo kwa barabara zingine ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-

Serikali ilianzisha Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam na kufanya Wilaya ya Temeke kuwa Mkoa wa Kipolisi; tangu Temeke iwe Mkoa wa Kipolisi kumekuwa na ongezeko kubwa la uhalifu hasa maeneo ya Jimbo la Mbagala:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbala?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Vituo vya Polisi na kuviongezea askari, vitendea kazi na kujenga nyumba za askari katika maeneo ya Jimbo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbagala ni Wilaya mpya ya Kipolisi iliyopo katika Mkoa wa Kipolisi wa Temeke. Kama ilivyo kwa wilaya nyingine katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Wilaya ya Mbagala inahitaji kujengewa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Kwa sasa wananchi wa Mbagala wanahudumiwa katika Kituo cha Polisi cha Mbagala Kizuiani ambacho miundombinu yake haitoshelezi. Aidha, hali kibajeti itakaporuhusu, Serikali itaweka mpango wa kuwajengea wananchi wa Mbagala Kituo kipya cha Polisi, nyumba za makazi ya askari na ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kukabiliana na uhalifu, Wilaya ya Kipolisi Mbagala imepata mgao wa magari matatu (3) aina ya Leyland Ashock Stile yenye Na. PT 3779; PT 3881 na PT 3891 na kufanya jumla ya magari yote katika Wilaya ya Mbagala kuwa tisa ambayo yanatumika kwa shughuli za doria, upelelezi na operesheni mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha usalama katika Wilaya ya Mbagala.