Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (6 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niliuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Obama mimi mwenyewe naitwa Dkt. Hadji Mponda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa mkataba kati ya Halmashauri ya Buhigwe na ile Hospitali ya Mission umesitishwa kwa sababu ya fedha, sasa ni nini Serikali wana njia mbadala ya kutoa huduma za afya bure kwa makundi haya ya wazee na watoto?
Swali la pili, mkataba kama huo huo uliofanyika Buhigwe na mwaka 2011 - 2013 ulifanyika katika Wilaya ya Ulanga ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga waliingia mkataba na Hospitali ya Lugala, ni Hospitali ya Mission, lakini mkataba ule ulidumu kwa muda wa miezi sita mpaka leo umesitishwa. Sasa swali langu ni lini Halmashauri hiyo ya Malinyi pamoja na TAMISEMI wataufufua mkataba ule kwa kurudisha huduma hizi bure kwa makundi haya mawili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza katika sehemu ya (a) ni kwamba nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, mkataba huu haujasitishwa, kilichotokea ni kwamba kuna fedha za quarter ya kwanza ambayo imekuja mpaka mwezi Disemba ambapo tunarajia sasa kuna pesa zingine zitakuja mpaka hivi sasa na nimesema pale mwanzo kwamba matarajio zile pesa zikishafika Halmashauri, basi lazima zielekezwe katika sehemu hizi tatu ilimradi wananchi waendelee kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, kwa sababu hili ni suala la Hospitali ya Lugala Mission sijakuwa na taarifa nayo za kutosha, lakini nina imani kwamba mikataba yote kilichozingatiwa ni kwamba, inakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwezekano ni kwamba naomba nishauri hasa Baraza la Madiwani hasa katika vikao vyao vya Kamati ya Fedha. Lazima fedha zinapokuja, wasimamie fedha hizi maelekezo yake ni wapi, kwa sababu sehemu zingine inawezekana fedha zikapita lakini watu katika kufanya maamuzi wakaelekeza pesa sehemu ambazo siyo muafaka mwisho wake wakati mwingine mikataba inavunjika wakati kumbe kuna watu hawajatimiza majukumu yao. Imani yangu ni kwamba, kila mtu atatimiza wajibu wake ilimradi wananchi wetu waweze kupata huduma bora kwa ajili ya kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika katika nchi yetu.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vile vile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri kuhusu daraja hilo na mwendelezo wa ujenzi wake lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Daraja hili la Kilombero unahusisha pia ujenzi wa barabara zinazoingia kwenye daraja hilo. Barabara hizo za maingilio ya daraja zinaunganishwa na barabara itokayo kwenye mto huo kwenda Lupilo – Malinyi - Kilosa - Mpepo - Londo - Lumecha hadi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Namtumbo. Barabara hii niliyoitaja hadi sasa haipitiki kabisa kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na mvua na mkandarasi yupo site hawezi akamaliza ukarabati wa uharibifu ambao umefanyika. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura kusaidia kunusuru hali mbaya ya usafiri katika barabara hiyo ambayo nimeizungumzia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kivuko cha Mto Kilombero baada ya kukamilika daraja lile, tumekubaliana kupitia Mfuko wa…
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Baada ya kukamilika kivuko kile tulikubaliana kiende kwenye Kivuko cha Kikove, je, ni lini Serikali wataanza ujenzi wa gati hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni jirani yangu lazima akiri kwamba, katika mipango ya kunusuru maeneo ya dharura hatuwezi tukaanza sisi majirani kwa sababu maeneo yenye matatizo ni mengi sana. Hata hivyo, simaanishi nawakatisha tamaa wananchi wa Namtumbo ambao ndiyo wamenileta hapa pamoja na majirani zao wa Malinyi, sina maana hiyo, maana yangu kubwa ni kwamba tatizo hili la kukatika mawasiliano ni la Tanzania nzima. Maadam mvua imeanza kupungua, tunaamini sasa kazi ya kurejesha mawasiliano itafanyika kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba nichukue nafasi hii kuwaelekeza TANROADS Mikoa yote sasa tuanze kuelekeza nguvu ya kurudisha mawasiliano katika maeneo yaliyokatika kwa sababu mvua sasa zimepungua. Fedha tutakazotumia hazitapotea bure kwa sababu mvua imepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, naomba Mheshimiwa Dkt. Mponda turudi kule tulipokubaliana ambapo ilikuwa katika kikao cha Mkoa na sisi tuliwakilishwa na watu wa TEMESA tuangalie kama mahitaji ya TEMESA Mkoa hayatoshi, wao watatuletea Kitaifa halafu tutaangalia utekelezaji wa hilo suala.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali nayo pia imeahidi ujenzi wa barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo - Lumecha - Namtumbo Songea katika kiwango cha lami. Sasa ni muda barabara hiyo bado haijaanza kujengwa.
Swali langu, ni lini sasa hii kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakamilika na barabara hii kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dokta Hadji Mponda, Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Wabunge wote wanaohusika na barabara hii ya kutoka Ifakara - Malinyi - Namtumbo - Songea kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Labda nimhakikishie tu kwamba kazi iliyofanyika hadi sasa ni kubwa. Unafahamu kwamba kipande kile cha kutoka Lumecha - Londo kimeshakamilika kwa maana kufunguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tumebakabiza kilometa 4 tu kukamilisha kuifungua hii barabara, wakati kazi ya feasibility study na detail design ikiendelea kufanyika. Nikuhakikishie kazi hii ya feasibility study na detail design pamoja na kipande hiki cha kilometa 4 kilichobaki cha kufunguliwa barabara hii itakamilika katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 unaoanza Ijumaa.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza kati ya hifadhi na wananchi nayo yanajitokeza katika Pori Tengefu la Bonde la Kilombero. Tumeiomba Serikali, naomba niwaulize hapa Serikali, ni lini sasa mtarudisha ardhi ile ya Buffer Zone katika Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza niseme kwamba Buffer Zone tafsiri yake ya moja kwa moja isiyohitaji utaalam mwingi sana ni eneo ambalo linapaswa kuwa siyo la yeyote kati ya pande mbili zinazopakana. Eneo hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu, linapaswa kuwa ni eneo ambalo shughuli za uhifadhi zinakuwa mild, lakini pia shughuli za matumizi ya kibinadamu na zenyewe zinakuwa mild kwa maana ya kwamba siyo eneo ambalo linatumika moja kwa moja kwa asilimia mia moja na pande zote mbili zinazopakana. Kwa hiyo, kusema kwamba lirudishwe kwa wananchi, pengine inaweza kuwa siyo sahihi sana kwa sababu halijawahi kuwa kwa asilimia mia moja upande wa hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema na ninarudia tena, mazoezi haya yote ya kupitia hifadhi baada ya hifadhi; iwe hifadhi ya misitu, iwe hifadhi ya wanyamapori au hifadhi nyingine yoyote ile chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii; maeneo yote hayo yameorodheshwa kama sehemu ya migogoro ya ardhi na yameorodheshwa hivyo na Wizara ya Ardhi. Pia tunakwenda kufanya team work miongoni mwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi yenyewe, TAMISEMI, eneo ambalo sasa Mheshimiwa Mbunge atashirikiana na Serikali ya Wilaya pale, lakini pia Wizara ya Nishati na Madini, pale patakapokuwa panahusika na mambo ya madini; lakini pia masuala ya maji kwa sababu tunahusika pia. Kwa kutunza misitu tunatunza pia vyanzo vya maji, basi pale itakapobidi kwamba kuna chanzo cha maji tunataka kukifanya kiwe endelevu, kukilinda, basi na Wizara ya Maji itahusika. Kwa kuanzia ni Wizara hizo tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wananchi wote na kupitia swali hili la Mheshimiwa Mbunge, wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho ni kipindi cha mpito ambapo Serikali sasa inakwenda kutafuta majibu ya kudumu kwenye migogoro hii ya mipaka na hifadhi na migogoro ya ardhi kwa ujumla.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi, Wilaya ya Ulanga na Kilombero, tunaishukuru Serikali na tunawapa pongezi kutekeleza ahadi ambayo wametuahidi ya ujenzi wa daraja la Kilombero ambayo imekuwa jawabu kubwa la kero ya miundombinu katika Wilaya hizo tatu. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ujenzi huo wa daraja la Kilombero unahusisha pia na barabara za maingilio na barabara hiyo ya maingilio inaunganisha barabara inayotoka Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo, Lumecha, Namtumbo mpaka Songea. Barabara hii kipindi cha masika inachafuka sana kutegemea na mazingira ya mvua maeneo yale na inakuwa inapitika kwa tabu sana. Sasa, je, Serikali inajipangaje na ukarabati wa kudumu wa maeneo korofi katika barabara hiyo niliyotaja?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; barabara hii niliyotaja inajulikana kwa T16, barabara hiyo iko katika upembuzi yakinifu unaosanifu kwa kina ambao umekamilika. Barabara inatakiwa ijengwe kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo inayotoka Ifakara, inatobokea mpaka Songea ambayo itakuwa sio kwa ajili ya mkaazi wa Morogoro itasaidia pia na ndugu zetu majirani wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwa niaba ya Serikali pongezi alizotupa na kwa kweli ni wajibu wetu kutekeleza ahadi zote ambazo tumezitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoongelea nayo iko katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015 hadi 2020 ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi na usanifu wa kina haujakamilika – physically umekamilika lakini taarifa bado haijakamilika na tunatarajia hiyo kazi itakamilika mwezi Mei, 2017. Kwa sasa taarifa ya rasimu imeshawasilishwa TANROADS wanaipitia kwa kina ili hatimaye wamrudishie maoni yule Mhandisi Mshauri ambaye ni kampuni ya Kyong Dong na baada ya hapo ndio atakuja kukamilisha kuandika taarifa ya mwisho. Kwa ratiba ilivyo ataiwasilisha taarifa ya mwisho mwezi Mei, 2017. Baada ya hapo Serikali itaanza kujipanga kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la ukarabati wa maeneo korofi kwa sasa ili iweze kupitika muda wote; nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Hadji Mponda Mbunge wa Malinyi na wananchi wote wa Malinyi hadi Kilosa kwa Mpepo kwamba Serikali ina mkakati kabambe na kila mwaka tunatenga fedha na nafahamu mwaka huu kuna wakandarasi wawili wako site katika maeneo korofi wanafanyia ukarabati wa hali ya juu ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika mwaka mzima bila matatizo.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yanayowakumba wakazi wa Lulindi, Masasi, yanafanana kabisa na wakazi wa Wilaya ya Malinyi katika kata za Sufi, Kilosa Mpepo; swali langu, kata hizo ninazozitaja ni kwamba kama alivyosema jibu la msingi Mheshimiwa Waziri, kwamba, kupitia Mfuko wa Fursa ya Mawasiliano kwa Wote (UCAF), wamejenga minara miwili katika Kata ya Ngoeranga na kata ya Sufi, lakini minara hiyo ambayo imejengwa chini ya Tigo haifanyi kazi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali nangu. Je, ni lini Serikali watarekebisha minara hiyo na vilevile kumalizia Kata zile mbili ambazo hazina mawasiliano kabisa, kata ya Sufi na kata nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwakikishie kwamba kata hizo mbili alizozieleza ambazo hazina mawasiliano kabisa ikiwa ni pamoja na kata ya Kilosa Mpepo, tutahakikisha kwamba tunazifikishia mawasiliano kwa kadri tutakapopata fedha na maadamu ulishawasilisha hilo mapema Mheshimiwa Mponda nadhani utakumbuka Mheshimiwa Waziri wangu alivyokujibu na nikuthibitishie lie jibu alilokupa Waziri wangu na mimi nitalifuatilia utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mponda kuhusiana na kata mbili ambazo…
Alitaja kata nne na nimeongelea kata mbili, kata hizo mbili ambazo Tigo wamejenga minara nitazifuatilia kuhakikisha kwamba minara hiyo inafanya kazi.