Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Leonard Haule (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti na muhimu kwa Taifa letu, Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia, ningeomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na uwezo huu lakini niwashukuru sana wananchi wa Mikumi kwa kuweza kuniamini na kunikopesha kura zao, nawaahidi nitawalipa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzo kabisa naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole sana ndugu zangu wa Kilosa ambao siku mbili zilizopita tumepata maafa makubwa ya mafuriko. Wenzetu wawili wamefariki dunia, Mungu awalaze mahali pema peponi lakini pia familia nyingi zimetaabika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapo hapo ni kwamba katika Wilaya ya Kilosa imekuwa kama ni kawaida sasa hivi ikifika kipindi cha mvua basi mafuriko yanakuwa ni lazima. Hii imesababisha kuleta matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza mpaka sasa Watanzania wenzetu 4,765 wameathirika na mafuriko hayo, kaya zilizoathirika ni 1,238, nyumba 144 zimebomoka kabisa na heka za mashamba 3,707 zimeharibika kabisa na wenzetu wapo kwenye hali mbaya sana. Pia visima 18 vimeharibika kabisa, kwa hiyo, wenzetu wanapata taabu ya maji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, imekuwa kama kawaida kwa kule Kilosa ambapo inaonekana tatizo kubwa ni miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na kingo za mito ambazo zinazidiwa na maji. Sasa hivi tunapozungumza ile barabara ya Mikumi - Kilosa ya kilometa 78 haipitiki kabisa. Ukitaka kutoka Mikumi kwenda Kilosa inabidi uzunguke mpaka Morogoro, ufike Dumila halafu ndiyo uelekee Kilosa kitu ambacho kinaleta taabu sana kwa wananchi wengi wa Jimbo la Mikumi. Taarifa hii tumeileta Ofisi ya Waziri Mkuu na imeahidi kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ombi kubwa katika Kata ya Masanze tatizo kubwa ya mafuriko haya yaliyoleta maafa makubwa yamesababishwa na tuta la Mto Miyombo ambalo kila siku mvua zikinyesha zimekuwa zikileta taabu sana katika maeneo yale. Kwa Kilosa kwa ujumla wake Bwawa la Kidete ambalo limekuwa likimwaga maji kwenda pale Kilosa limekuwa likileta matatizo sana na ndiyo maana unaona kila mwaka tunakuwa na kazi ya kukarabati reli maeneo ya Godegode na Fulwe ambapo kila siku imekuwa ikisombwa na haya maji. Kwa Kata ya Tindiga kingo za Mto Mkondoa ndiyo zimebomoka na kuleta athari kubwa sana kwa wananchi wetu wa Kata ya Tindiga.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Serikali tujaribu sana kuboresha miundombinu hii ili tuache kupiga zile kelele za kuomba misaada kila siku. Mwezi wa kwanza tu hapa nilimuomba Mheshimiwa Waziri, Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama akatusaidia tani 200 na sasa hivi tena tumeleta maombi tusaidiwe tani 100, tutakuwa tukiomba hivi mpaka lini? Tunaomba tutafute solution, tuangalie jinsi ya kukarabati mito au miundombinu hiyo. Nawaomba sana mngeiwezesha Wizara ya Mazingira kwa kuuboresha Mfuko wa Mazingira ili uweze kutumika katika kuboresha vitu kama hivyo. Vinginevyo kila siku tutakuwa tukilia ndugu zetu wanakufa na tunapeana pole.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kata ya Ruhembe tumekuwa tukipiga kelele kuhusu kuvuka Daraja la Ruhembe ambapo ndugu zetu wamekuwa wakitaabika. Ndilo hilo daraja ambalo kuna mwalimu mmoja ambaye ni Afisa Elimu amefariki dunia kwa sababu alikuwa anataka kumuokoa kijana aliyekuwa anabebwa na maji. Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu wa daraja lile, ni daraja muhimu na la msingi, naomba itengeneze daraja hili ili kuokoa Watanzania wa Kata ya Ruhembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nataka niongelee kuhusu utawala bora. Utawala bora ni pamoja na ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji. Tumekuwa kila siku tukisema na kupiga kelele tukiwaomba Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji watusaidie kwenye kampeni mbalimbali kwa sababu wenyewe ndiyo wanahusika na wananchi moja kwa moja. Mfano suala la elimu bure wahusika wa kwanza ni Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji. Tumekuwa tukiomba walipwe posho lakini imekuwa ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi sasa hivi imefika kipindi viongozi wetu wa Serikali katika Wilaya zetu, mfano sisi Kilosa kuna Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amekuwa akiingilia sana madaraka ya Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji kiasi kwamba amewafanya wakae na woga na kuwa na hofu kubwa. Hapa napozungumza Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuyuni amesimamishwa na ofisi imefungwa na hili suala nililipeleka kwa Waziri wa TAMISEMI. Pia Mkuu wa Wilaya amefungia shimo la mchanga la Ruaha na kutisha kijiji cha Ruaha na kusema kwamba atauondoa uongozi wa Ruaha ni kwa sababu tu za kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ruaha ina vijiji vinne na vyote vimechukuliwa na CHADEMA, huo ndio ukweli. Ina vitongoji 21 na vitongoji 20 vimechukuliwa na CHADEMA, huo ndio ukweli na Diwani ni wa CHADEMA. Sasa msitake kuzuia haya maendeleo ya watu wa Ruaha kwa sababu tu za kiitikadi. Siku zote mmekuwa mkituomba tuonyeshe ushirikiano na tuwe pamoja lakini mnapokuwa mnanyanyasa viongozi wa vitongoji na vijiji inatuwia vigumu kuweza kupata yale maendeleo ambayo tumekusudia kuyapata. Ili kuboresha suala la utawala bora tuendelee kushirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ameenda mbali zaidi, nilimuomba ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kuja kutusaidia kule kwa wakulima wa miwa ambapo aliingilia uozo uliokuwa unaendelea katika chama cha RCGA. Kwa sababu alisoma ripoti ya Tume iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya ilikuwa ikisema kwamba ule uongozi haufai, Mheshimiwa Mwigulu kwa ujasiri na kuwapenda Watanzania aliuondoa ule uongozi na kuweka uongozi mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotustaajabisha ni kwamba yule Mkuu wa Wilaya anapinga maamuzi ya bosi wake yaani anasema Waziri alikurupuka…
MHE. JOSEPH L. HAULE: Anasema Waziri alifanya haya mambo bila kumshirikisha. Mkuu wa Wilaya ni nani mbele ya Waziri wake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri ripoti hiyo ndiyo ipo vile, wakulima wale wa miwa wanakushukuru sana kwa sababu hata bei ya miwa imepanda kutoka 72,000 mpaka 79,000. Sasa hivi inavyoonekana hata percentage ya kuingiza miwa imepanda kutoka asilimia 45 kwenda asilimia 60 yaani wakulima wa nje wanaingiza asilimia 60 na wenye kiwanda wamekubali asilimia 40. Haya yote ni matunda ya wewe kutembelea kule lakini Mkuu wa Wilaya anataka kukukwamisha anasema wewe ni jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende mbali zaidi, Mheshimiwa Mwigulu umeonyesha ushirikiano mzuri na kweli umeonyesha kwamba sio mzalendo wa tai bali ni mzalendo kutoka moyoni, nakupongeza sana ndugu yangu.
Nimshauri tu Ndugu yangu Mheshimiwa Nape kwa sababu Mheshimiwa Mwigulu alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Tawala na anafanya haya mambo kwa ajili ya Watanzania basi na wewe kwa sababu ulikuwa Mwenezi hebu achia TBC ionekane wazi na Watanzania waweze kukuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye suala la afya. Suala hili kwenye Wilaya yetu ya Kilosa limekuwa ni zito kwani hospitali yetu ya Wilaya imekuwa na taabu nyingi, dawa zinachelewa kufika, tunapoomba dawa MSD zinachelewa na nyingine hawana kabisa na malipo yanakuwa yameshafanyika hatuwezi kupata dawa nyingine. Kitu ambacho kimetuumiza ni kwamba tumekosa misamaha ya kodi. Hospitali ya Kilosa iliagiza ambulance na kuiomba Serikali isamehe kodi ili waweze kuingiza ambulance ile lakini Serikali ilikataa kutoa kodi hiyo kwa kitu ambacho kingeweza kuwasaidia Watanzania wenzetu kule. Watanzania wanataabika na wanahitaji msaada mkubwa, inapofika sehemu tunaagiza vifaa tiba vya hospitali za Serikali ambazo zinakimbiliwa sana na Watanzania walalahoi basi tuangalie uwezekano wa kuweza kuwasaidia Watanzania kwa kuruhusu na kusamehe kodi zile. Kwa Kilosa haijafanyika hivyo na hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa sababu Hospitali ya Kilosa inahudumia wananchi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika Zahanati ya Mikumi, zahanati ile ni kama haipo. Nilipoongea na Daktari wa zahanati ile ameniambia ile zahanati ipo lakini kama haipo. Tunategemea Hospitali ya St. Kizito ambayo ni ya private, ni ya mission na inapewa milioni sitini kwa mwaka lakini bado walalahoi wanashindwa ku-afford gharama za matibabu pale. Naomba Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aweze kuboresha Hospitali ya Mikumi ili walalahoi wajisikie kwamba ni hospitali yao na waweze kutibiwa kwa bei rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hospitali ya St. Kizito kuna kaya maskini ambazo zinapata msaada lakini imeonekana zikienda pale zinakuwa charged kwa pesa nyingi, maskini mnamsaidia kwa kumpa chakula inakuwaje unamuomba hela za dawa? Mtengenezee hospitali yake ya pale Mikumi ili aweze kwenda akajisikia yupo kwake. Pale kwenye Zahanati ya Mikumi sasa hivi hata kupima malaria ni shida na watu wanalalamika, tumewashawishi sana waingie kwenye mfuko wa afya lakini wakienda pale hata kupima inakuwa ni shida wanaambiwa kapime dirisha lile kachukue dawa dirisha lile as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihamie kwenye suala la elimu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niweke yangu tena ya muhimu katika hoja hii iliyopo mezani ya bajeti ya Wizara muhimu na uti wa mgongo ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze na suala zima la VETA-Mikumi. Kwa kuwa Chuo cha VETA - Mikumi ndiyo chuo pekee kilichopo katika Jimbo la Mikumi na kwa kuwa ukombozi wa vijana wengi wanaohitimu shule za sekondari zilizopo Jimboni kila mwaka hukosa mwelekeo, hivyo ni muhimu kukipa kipaumbele chuo hicho kwa kukiboresha katika maeneo yafuatayo:-
(i) Kupanua wigo katika fani zinazotolewa ili ziendane na mazingira ya Jimboni, kuongeza fani ya ufundi-kilimo (agro-mechanics);
(ii) Kukiongezea uwezo wa udahili kwa kuongeza idadi ya mabweni hasa kwa ajili ya wasichana ili kuendana na sera ya kuleta uwiano katika udahili kati ya wasichana na wavulana;
(iii) Kuongeza idadi ya madarasa na karakana za kujifunzia, pia kupanua wigo wa mafunzo kwa vitendo; na
(iv) Kuongeza na kuboresha vifaa vya kujifunzia ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuwajengea vijana uwezo wa kitaalamu unaoendana na mabadiliko yanayotokea sokoni kila wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye changamoto zinazoikabili VETA-Mikumi kama ifuatavyo:-
(i) Baadhi ya watumishi kukaa muda mrefu sana bila kuhamishwa, wapo waliokaa zaidi ya miaka 20, hii inaathiri sana utendaji wa kazi kwa kuwa wanafanya kazi kwa mazoea na ufanisi kupungua;
(ii) Kuna upendeleo katika udahili hasa katika chaguo la pili hivyo kupelekea aidha ndugu wa viongozi au watu wao wa karibu kujaza nafasi hizo huku wananchi wazawa wa Mikumi wakikosa fursa hiyo. Katika udahili mwaka wa masomo 2016, wananchi wa Mikumi waliopata fursa ni asilimia 10 tu ingawa tunatambua kuwa usaili huwa unajumuisha waombaji kutoka kila kona ya nchi lakini vijana wa Mikumi walipaswa kupewa kipaumbele hasa katika chaguo la pili;
(iii) Kuwepo kwa uongozi usiofuata tararibu, kanuni za utumishi wa umma na utawala bora. Uongozi wenye mfumo kandamizi usiokubali kufanya kazi na watu waadilifu, uongozi unaofanya ubadhirifu na maamuzi yasiyokuwa na tija kwa VETA na Taifa kwa ujumla;
(iv) Chuo kimepeleka mini-bus kwa matengenezo Dar es Salaam zaidi ya wiki moja katika gereji bubu katika kipindi cha mwezi Mei 2016 bila kufuata taratibu za manunuzi. Pia kukiuka maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka magari yote ya umma kwa matengenezo TEMESA;
(v) Uongozi wa chuo (Afisa Rasilimali Watu na Mkuu wa Chuo) kuwa na mtandao mpana kuanzia VETA-Makao Makuu wa kuwakataa, kuwapinga na kuwahamisha watumishi wanaonekana kutokubaliana na mawazo yao ya kibadhirifu.
Kwa mfano Salum Ulimwengu (Mratibu Mafunzo) aliyekaa kwa kipindi cha miaka miwili na kuhamishiwa Arusha baada ya kuvutana na menejimenti baada ya Mkuu wa Chuo kukiuzia chuo gari bovu lililokuwa likimilikiwa na rafiki yake, pamoja na ununuzi wa spea hewa za magari ya mafunzo. Suala hili lilichunguzwa na ofisi ya CAG na hakuna ripoti yoyote iliyotoka. Hata hivyo, uuzwaji wa gari hilo haukuhusisha ofisi ya Afisa Mafunzo ila Kitengo cha Ufundi magari bila kufuata taratibu za mamlaka;
(vi) Kukataa kumpokea na kushindwa kumkabidhi ofisi Mratibu wa Mafunzo kwa kipindi cha mwaka mzima kinyume cha section 3.13 ya VETA Staff Regulations and Conditions of Service ambayo inatamka kuwa mabadiliko yoyote ya kiutumishi lazima yafanyike kwa makabidhiano ya kimaandishi (Rejea Internal Audit Report VETA- Mikumi, March- December 2014);
(vii) Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu kushinikiza uhamisho ili kulinda wizi wa mali za umma na ubadhirifu. Mfano mwingine, Msuya (Stores Officer) aliyekaa kwa kipindi cha mwezi mmoja na kupelekwa Morogoro. Joseph Riganya (Stores Officer) aliyevutana na uongozi wa chuo na kuhamishiwa Ofisi ya Kanda kwa kisingizio cha matibabu. Riganya alipinga ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi na ubadhirifu katika manunuzi unaofanywa na Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu; mfano katika ripoti ya ukaguzi wa ndani (internal Audit report) ya Machi hadi Desemba 2016 inaonyesha kuwa Afisa Rasilimali Watu, Mhasibu na Mwalimu mmoja walipokea vifaa vya thamani ya shilingi milioni 35 kinyume na taratibu kwani Kamati ya Mapokezi ndiyo yenye dhamana ya kupokea vifaa hivyo. Walifanya hivyo ili kulinda maslahi yao binafsi;
(viii) Ukiukwaji wa taratibu za ajira kwa kumpa mkataba Neema Bui ambaye hana sifa na anafanya kazi za manunuzi kwa maslahi ya Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu kwa kuwa kila Afisa Manunuzi anayeletwa anaondolewa kwa hila ili asizibe mianya ya wizi; na
(ix) Afisa Manunuzi Rogate aliyehamishiwa mwezi Februari 2016 kutoka Tabora amepewa vitisho kwenye kikao cha menejimenti na sasa anafanya mpango wa kuhama kuwapisha wanaojiita wenye chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuwasimamisha kazi Afisa Rasilimali Watu na Mkuu wa Chuo ili kupisha uchunguzi;
(ii) Kuwahamisha watumishi waliokaa muda mrefu sana katika chuo hiki ambao ndiyo chanzo cha kulea ubadhirifu;
(iii) Kuangalia kama ilikuwa halali kumhamisha Afisa Mafunzo, Ndugu Salum Ulimwengu aliyekaa kwa kipindi cha miaka miwili na ambaye amehamishwa mwezi mmoja tu tangu amhamishe mke wake katika Sekondari ya Mikumi, hivyo mtu aliyepigania maslahi ya Taifa kuteswa kisaikolojia na kifamilia;
(iv) Kufanya uchunguzi maalumu juu ya masuala ya manunuzi na fedha katika chuo cha VETA-Mikumi; na
(v) Kufuatilia ilipoishia ripoti ya CAG ya Oktoba 2015 juu ya Mkuu wa Chuo kukiuzia chuo gari chakavu kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala zima la elimu bure ambapo kumekuwa na changamoto nyingi kama ifuatayo:-
(i) Ruzuku inayotoka Serikalini ya kila mwezi haikidhi mahitaji ya shule mfano mpaka sasa Walimu Wakuu hawana fungu la mlinzi, umeme na maji;
(ii) Idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na Walimu, madarasa na miundombinu mingine kuna vyoo, madawati na kadhalika;
(iii) Huduma ya chakula shuleni irudishwe ili kuhamasisha watoto waende shule; (iv) Upungufu mkubwa wa Walimu wa sayansi kwenye Jimbo la Mikumi;
(v) Walimu kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu na pia wengi kuchelewa kupandishwa madaraja; na
(vi) Hakuna nyumba za Walimu na pia hawalipwi posho za uhamisho na pesa zao za likizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni baadhi tu ya changamoto nyingi za elimu kwenye Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika hoja hii iliyo mezani inayohusu Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa tumekuwa tukipanga mikakati mingi na kujinasibu kwamba tunataka kuipeleka nchi yetu kwenda kwenye uchumi wa kati ili tuweze kuipata Tanzania ya viwanda, wakati tunasahau kuwa hatuwezi kuwa na nchi ya viwanda nchi nzima kama bado tuna tatizo sugu na kubwa la nishati ya umeme katika sehemu zetu nyingi za vijijini ambako ndiko tunataka na tunapaswa kupeleka viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tutakuwa tunafanya kazi bure kama hatutaweka mkakati wa dhati huku tukisukumwa na dhamira ya mioyo yetu ya kufufua sekta ya kilimo. Yatupasa kuwekeza zaidi kwenye kilimo mfano, pamba, kahawa, korosho, miwa na kadhalika ili tuweze kutimiza dhamira yetu ya kuipata Tanzania ya viwanda ambayo pia itatusaidia kutoa ajira kwa watu wetu na kuongeza kipato kwa wakulima wetu na kujiletea maendelea ya nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumekuwa kila siku tukisema tunataka kufufua viwanda ambavyo vimekufa lakini hatutaki kusema ni nini kimeua viwanda vyetu. Mfano Mkoa wetu wa Morogoro ulikuwa ni moja ya mikoa iliyoshamiri kwa viwanda kadha wa kadha ambavyo sasa vimebinafsishwa, vingine vimeshakufa kabisa na kuwa mabanda ya kufugia mbuzi na kuku na vingine vipo njiani kufa maana kama ni mgonjwa basi yupo ICU anapumulia mipira kupata hewa na ndugu wapo mbioni kuzima mashine yenyewe ya kupumulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa mzima wa Morogoro, Mheshimiwa Waziri kabla ya kusema ni vipi atafufua hivi viwanda, pia atuambie hali halisi ya viwanda vyetu vya Mkoa wa Morogoro ambavyo vilikuwa vinatoa fursa ya ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Morogoro. Mfano, nataka kujua viwanda vyetu vya Mang’ula Mechanical and Machine Tools Limited (MMMT), Morogoro Canvas Mill Limited, Tobacco Processing Factory na MOPROCO vipo kwenye hali gani na vinasaidia nini kwenye ubinafsishaji uliofanyika na kama vina tija kwa Taifa letu. Pia kwenye Jimbo langu la Mikumi kuna kiwanda cha Kilombero Sugar Company Ltd. ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa sukari lakini kilibinafsishwa Aprili mwaka 1998 kwa Kampuni ya ILLOVO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuwasisitiza wakulima wa Wilaya ya Kilosa walime miwa na kuacha kulima mpunga na mahindi lakini wakulima hao wa miwa wamekuwa wakilalamika sana kunyonywa kuhusu idadi ya asilimia ya miwa inayoingizwa kwenye kiwanda hicho cha ILLOVO. Lakini pia wakiwa na malalamiko mengi ya upimaji wa utamu wa miwa hiyo (sucrose) na pia mabaki ya miwa hiyo (buggers) ambayo ni mabaki ya miwa yamekuwa yakitengeneza umeme na pia kuna morales ambayo inatengenezea pombe kali (spirits) lakini wakulima wamekuwa hawalipwi zaidi ya tani za utamu wa sukari tu ambapo sasa ndani ya kiwanda cha ILLOVO pia kuna kiwanda kingine cha kuzalisha pombe na bado wanasema kiwanda kinapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kupata sukari ya kutosha kama hatutaweka mazingira mazuri na salama kwa wakulima wa miwa. Wakulima wa miwa wa nje wanataabika sana na wanayonywa sana na wanahitaji sana msaada wa Serikali kuwasaidia wakulima wao wapate mzani wao wa uhakika ili waweze kupima na kuingiza miwa yao kwa haki badala ya sasa kuwekewa mzani wasiouamini. Wapimaji ndio hao hao wenye kiwanda ambao pia ndio wanaopanga bei ya zao hilo, nasisitiza na naomba sana Serikali ifanye mpango wa kuwaletea wakulima mzani ili wapate haki yao na kufutwa machozi yao ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko makubwa sana ya wafanyakazi wa Kiwanda cha ILLOVO ambapo kumekuwa na mateso na unyanyasaji mkubwa sana wa wafanyakazi wa ngazi ya chini wa kiwanda hicho. Nakushauri siku moja uende pamoja na mimi kwenye Kiwanda cha ILLOVO ili tukasikilize kilio cha wafanyakazi wao na ninakuomba usiende kuonana na uongozi wa kiwanda bali tuonane na viongozi wa vyama vya wafanyakazi au wafanyakazi wenyewe ambao wamekuwa kama watumwa ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, lakini pia kumekuwa na malalamiko makubwa ya ajira za kindugu, ajira za kirafiki na ajira za rushwa ya ngono. Vyeo vinapandishwa kwa upendeleo mkubwa, lakini mbaya zaidi ni mishahara midogo sana ambapo Kampuni ya Sukari Kilombero (ILLOVO) imekuwa ikiwadanganya wafanyakazi kwamba wanapata hasara pindi linapokuja suala la majadiliano ya mishahara ingawa ukweli ni kwamba hakuna mwaka waliopata hasara bali ndiyo kwanza wanaendelea kuongeza kiwanda kingine cha tatu cha pombe, pamoja na ununuzi wa vifaa vyote vya usafiri kama magari, pikipiki ambavyo kila mtu akitumia kwa miaka mitatu tu viongozi hao wanauziwa kwa shilingi 100,000 tu.
Hii ni kama ile kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa John Magufuli, ni kwamba viongozi wa Kampuni ya ILLOVO wanaishi kama malaika na wafanyakazi wa chini ambao kimsingi wamekuwa wakifanya kazi ngumu kwa jasho na damu wanaishi kama mashetani. Sasa kuna wafanyakazi wa kigeni 23 pale ILLOVO, wakati wafanyakazi wa kigeni hawakutakiwa kuzidi wafanyakazi watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo kubwa sana la wafanayakazi zaidi ya 2000 waliokuwa wanafanya kazi kwenye kiwanda cha Kilombero Sugar Company, kwa masikitiko makubwa sana nataka nipate majibu ni lini watatendewa haki zao na kulipwa mafao yao kama wanavyostahili kwa kupitia mkataba wao na mwajiri Na. 4/1995 ambapo walilipwa miezi kumi badala ya miezi 40 kadri ya Kifungu Na. 10.3.7 kinachohusu upunguzwaji kwenye mkataba huo wa hali bora za wafanyakazi, hivyo basi walipunjwa kiasi cha miezi 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri aje na majibu ya hoja hii ya msingi sana ambapo pia wafanyakazi hao walifutiwa malipo ya utumishi ya muda mrefu kama wanavyostahili kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya vipimo vya kazi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi za vipimo. Sera waliyonayo ni kuhakikisha wanawapa vipimo vikubwa ili wasiweze kumudu kumaliza, hivyo kwao inawasaidia kubana matumizi kwani mfanyakazi asipomaliza kipimo kile alichopewa hawezi kulipwa hata kama kazi imebaki robo. Huu ni utumwa wa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inabidi ilifuatilie kwa kina na kuchunguza makampuni haya ya sukari yenye mashamba kwani wananchi hawa wanateseka sana. Serikali inaweza kufurahia kwamba wananchi wanapata ajira kumbe wamo utumwani ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningeiomba Serikali ituambie ni lini itaanza kujenga viwanda vya kusindika viazi ambapo kilimo hicho cha viazi kimeshamiri sana katika Kata ya Kisanga ambapo tumebarikiwa kulima viazi kwa msimu mzima kwa wingi kushinda hata Gairo. Na pia napenda kuishauri Bodi ya Sukari itimize wajibu wake wa kuhakikisha inasimamia haki stahiki za wakulima wa miwa kuanzia kwenye mikataba yao dhidi ya makampuni ya sukari na wamiliki wa viwanda maana kwa sasa unyonyaji umezidi kwa wakulima wa miwa na kilio chao kikubwa ni kuwa na mzani wa kupimia sukari unaomilikiwa na wakulima wenyewe, tofauti na sasa ambapo mwenye kiwanda ndiye anayemiliki mizani hiyo na kuleta malalamiko ya miwa mingi kutupwa kwa kukosa ubora na utamu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Waziri aje na majibu, ni tani ngapi za wakulima maskini zimeshatupwa mpaka sasa na ni hasara gani ambayo wakulima wameipata mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niongeze kidogo kwenye mchango wangu niliowasilisha jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Ujenzi aipe barabara ya Ruaha Mbuyuni - Mlolo (Chabi) - Ibanda - Mlunga - Ileling‟ombe mpaka Mpwapwa ya kilometa 74 ambapo inaunganisha Wilaya mbili za Kilosa na Mpwapwa. Hii inamaanisha kuwa inaunganisha mikoa ya Iringa, Morogoro na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mfuko wa Barabara wa Mkoa wa Morogoro walifanya tathmini na kuipitisha barabara hii kuwa chini ya TANROADS na pia waliwaalika wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi ambao nao waliipitisha na kusema inafaa kufanyiwa kazi haraka sana kadri inavyowezekana. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up aje atupe majibu, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii ili kuunganisha wananchi hawa wa mikoa ya Dodoma na Morogoro na Iringa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Moja kwa moja nianze mchango wangu nikiuelekeza kwenye kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kata ya Malolo ambao wapo kwenye Jimbo la Mikumi wakilalamikia fidia yao ya uharibifu mkubwa sana wa mazao na mashamba yao uliosababishwa na kupasuka kwa bomba kubwa la mafuta ya TAZAMA Pipeline.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2011 bomba la TAZAMA lilipasuka na kusababisha hasara kubwa sana siyo tu kwa mazao bali zaidi kwenye afya za wananchi wa Kata hiyo ya Malolo hasa kwenye Vijiji vya Mgogozi, Chabi, Malolo „A‟, Malolo „B‟ na maeneo mengine yaliyozungukwa na bomba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na wataalam walikuja kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea na walikubaliana na wananchi wa Kata ya Malolo kuwa watalipwa fidia ya sh. 320,000,000/= kwa madhara hayo. Tofauti na walivyokubaliana, wananchi wakaambiwa na Halmashauri ya Kilosa kuwa watalipwa sh. 50,000,000/=. Sasa wananchi wa Malolo wanataka kujua ni lini watalipwa sh. 320,000,000/= zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Malolo kwa masikitiko makubwa sana wanaiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi iwape majibu, ni lini itawafuta machozi yao kwa kuwalipa haki yao hii muhimu ya fidia hii ambayo hawajalipwa tangu mwaka 2011?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, napenda sana kuchangia kuhusu mradi huu wa REA. Inasikitisha sana kuona Jimbo la Mikumi halijaguswa kabisa kwenye mradi wa REA I na REA II na sasa tunaingia kwenye REA III tukiwa na sintofahamu kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mikumi limebatizwa jina na sasa kuitwa Jimbo la giza kwa sababu ya vijiji vingi sana vya Jimboni Mikumi kukosa umeme. Nilishaandika na kuipeleka barua kwa Mkurugenzi wa REA na kumwelezea hali halisi ya Jimbo langu la Mikumi lakini pia baada ya kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambaye naye alinijibu kwamba atahakikisha mradi wa REA III vijiji vyangu vya Jimbo la Mikumi vyote vitaingizwa kwenye mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho yake atuambie ni lini vijiji vifuatavyo vya kwenye Jimbo langu la Mikumi vitapata umeme?
(1) Kata ya Maloo – Vijiji vya Mgogozi, Malolo A & B, Chabi, Itipi;
(2) Kata ya Vidunda – Vijiji vya Vidunda, Udungu na Chonwe, Itembe;
(3) Kata ya Uleling‟ombe – Vijiji vya Uleling‟ombe, Mlunga, Lengewaha;
(4) Vijiji vya Mhenda – Vijiji vya Mhenda, Kitundueta, Ilakala, Maili 30;
5. Kata ya Masanze – Vijiji vya Munisagara, Chabima, Dodoma Isanga;
6. Kata ya Tindiga – Vijiji vya Malui, Tindiga, Kwalukwambe, Malangali;
7. Kata ya Ulaya – Vijiji vya Nyameni, Mbuyuni, Kibaoni, Ng‟ole, Nyalanda;
8. Kata ya Kilangali – Vijiji vya Mbamba, Kiduhi;
9. Kata ya Mikumi – Vijiji vya Ihombwe, Tambuka Reli, Msimba;
10. Kata ya Zombo – Vijiji vya Kigunga, Madudunizi, Nyali, Zombo; na
11. Kata ya Ruhembe – Kijiji cha Kielezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nijielekeze moja kwa moja kwenye migogoro mbalimbali iliyopo katika Jimbo langu la Mikumi ambapo pamoja na mimi mwenyewe kuileta kwenye Ofisi ya Waziri wa Ardhi mkono kwa mkono lakini cha kusikitisha ni kuwa sio tu kwamba haijaorodheshwa kwenye kitabu cha Waziri alicholeta na kukigawa kwa Wabunge, lakini pia migogoro hiyo haijatajwa kabisa mahali popote.
Naomba Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho anipe majibu ni lini na ni nini hatma ya migogoro hii ya ardhi na mashamba pori yafuatayo ambayo yapo kwenye Jimbo la Mikumi na kusababisha Watanzania wenzetu wazalendo kukosa ardhi na nyingi kupewa wanaoitwa wawekezaji ambao wameyafanya mashamba pori na mengine kuyabadilisha matumizi.
(i) Kata ya Mikumi - mgogoro kati ya wananchi wa Kitongoji cha Vikweme na JWTZ na wananchi wa Kikwalaza na Hifadhi.
(ii) Kata ya Ruhembe – mgogoro wa wananchi wa Kitete Msindazi na Hifadhi; wananchi wa Ruhembe na Hifadhi; wananchi wa Kielezo na Hifadhi na wananchi wa kijiji cha Kidogobasi na wavamizi wa ekari 98.
(iii) Kata ya Kilangali - mgogoro wa muda mrefu kati ya Kijiji cha Kilangali na Kijiji cha Tindiga; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Mbamba na Kijiji cha Kiduhi ni wa muda mrefu sana; mgogoro wa kijiji cha Kilangali na Shamba la Mbegu la ASSA, huu nao ni wa muda mrefu sana na mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kata nzima ya Kilangali.
(iv) Kata ya Uleling‟ombe - kuna mgogoro mkubwa sana kati ya wananchi wa Uleling‟ombe na Msitu wa Ukwiva ambapo eneo hili lilihamishwa mpaka mwaka 1972 na wananchi wanaomba warudishiwe mpaka wa zamami (awali) wa mwaka 1957 ili wapate maeneo ya kulima na kujiletea maendeleo.
(v) Kata ya Ulaya - mgogoro wa ardhi kati ya Basso Masumin na Serikali ya Kijiji cha Ng‟ole; mgogoro wa ardhi kati ya wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Mbuyuni; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Mbamba; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Ulaya Kibaoni, mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Mhenda na mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Nyalanda.
(vi) Mgogoro mkubwa wa shimo la mchanga kati ya Kata ya Ruaha na Kata ya Ruhembe (Kijiji cha Kitete).
(vii) Mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Kitundueta (Mhenda) na Kijiji cha Ihombwe kilichopo Mikumi.
(viii) Kata ya Kidodi - mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Lumango na hifadhi.
(ix) Kata ya Tindiga - mgogoro mkubwa sana na unaopoteza maisha ya Watanzania wengi sana kati ya wakulima na wafugaji na umedumu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda Mheshimwa Waziri atuambie ni lini mashamba makubwa yaliyotelekezwa na wanaoitwa wawekezaji yatarudishwa kwa wananchi. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilileta orodha ya mashamba pori 38 kwenye ofisi ya Waziri wa Ardhi bila mafanikio. Baadhi ya mashamba hayo ni:-
(i) Kata ya Kilangali - shamba Na.120 la Kivungu.
(ii) Kata ya Kisanga - shamba la SAS (Kisanga).
(iii) Kata ya Masanze - shamba la Miyombo; shamba la Dodoma Isanga na shamba la Changarawe.
(iv) Kata ya Ulaya - shamba la Ulaya.
(v) Kata ya Tindiga - shamba la Sumagro.
(vi) Kata ya Ulaya - shamba la Nyaranda
(vii) Shamba la Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu kilicholetwa na Mheshimiwa Waziri hakina takwimu shahihi ukilinganisha na hali za mashamba pori hayo yaliyopo Jimboni Mikumi. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aje mwenyewe Jimboni Mikumi ili ashuhudie mapori makubwa yasiyoendelezwa wala kulimwa kama ambavyo amepewa taarifa na kusababisha wananchi wengi kukosa sehemu za kujiletea maendeleo na kuleta tija na maendeleo kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza sana naomba Mheshimiwa Waziri anipe ahadi ya kwenda pamoja na mimi Jimboni Mikumi ili akajionee mwenyewe. Ahsante sana, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Maliasili na Utalii maana ukizungumzia Jimbo la Mikumi moja kwa moja unazungumzia masuala haya muhimu ya utalii na maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa niongelee jinsi ambavyo wananchi wa Mikumi wamekuwa wakilia kutokana na jinsi ambavyo wanabanwa na migogoro mbalimbali ambayo inasababishwa na kuongezwa mara kwa mara kwa mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana wananchi wa Jimbo la Mikumi waliokuwa wakiishi katika maeneo ya Kipogoga pamoja na Mgoda walihamishwa mwaka 1963 na kupelekwa kwenye Vijiji vipya vya Vikweme, Rwembe maeneo ya Tindiga na sehemu nyingine. Hiyo ilisaidia kuifanya hifadhi ya Mikumi iweze kuanza mwaka 1963, lakini sasa hivi mipaka hiyo imeonekana kuwa inaongezwa na sasa hivi wananchi wamefuatwa kwenye vijijji, kwa mfano Kijiji cha Vikweme wanaambiwa tena waondoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Vikweme wamekuwa na kilio cha muda mrefu sana ambapo upande mmoja wanakabwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na sasa hivi wameambiwa wahame maeneo yale kwa sababu ni ya Jeshi, lakini upande wa pili Hifadhi ya Mikumi inasema ni eneo lao, mnataka wananchi hao wa Mikumi waende maeneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wazee ninaozungumza wamehamishwa mwaka 63 ni pamoja na akina mzee Leonard Haule ambaye tulimzika mwaka 1981, ambaye ni babu yangu. Wazee mwenzake akina mzee Mbegani mpaka leo wamekuwa wakitaabika na wakiililia Serikali kwamba mnataka waende wapi wakati wenyewe ndiyo watu wa Mikumi wazawa waliokuwa pale?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro mingi kutokana na hifadhi kuongeza mipaka katika maeneo mengine kama ya Uledi, Ng‟ombe ambapo inaonekana kuna heka karibu 200 za wakazi wa Lugawilo ambao hifadhi pia imesema huu mpaka ni mpya. Wananchi wa huku wamekuwa wakilia kwa muda mrefu wakiitaka Serikali iweze kurudisha ule mpaka wa zamani wa mwaka 1957 uliokuwa ukiwawezesha kupata ardhi ya kulima na kujenga nyumba zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi kama wa Vikwema, Kitete Msindazi, maeneo ya Mululu, maeneo ya Msange pamoja na maeneo ya Lumango wameonekana kuwa wanataabika kwa sababu wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara na watu wa hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la buffer zone. Eneo la Buffer Zone limekuwa likiongezeka kila siku. Eneo hili wananchi hawatakiwi kuingia kabisa. Mama zetu wamekuwa wakipigwa kwa sababu ya kuingia kuokota kuni kwenye maeneo haya. Ndugu zetu wamekuwa wanataabika na sasa tumesema kuwa Mikumi mpya ya Profesa J. tunataka haya mambo yakome na tuweze kukaa chini na wananchi ili tuweze kusuluhisha. (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, tunapozungumzia masuala ya hifadhi tunazungumzia ujirani mwema. Hapo zamani sisi tulipokuwa tunakua tulikuwa tunaingia kwenye mbuga ya wanyama ya Mikumi kwenda kuona wanyama, lakini pia tukicheza michezo pamoja na Maaskari wa Wanyamapori na vitu vingine kama hivyo. Pia walikuwa wakitusaidia kujenga zahanati, shule na wanafunzi walikuwa wakibadilishana uwezo. Sasa hivi kumekuwa na uadui mkubwa kati ya watu wanaokaa katika vijiji vinavyopakana na hifadhi na wahifadhi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiongelea suala la ujirani mwema kwa sababu tunasema wananchi kama watathaminiwa watapewa thamani wanaostahili na fidia lakini pia watashirikishwa kwenye mambo mbalimbali, hii itawasaidia sana kulinda rasilimali zetu na wanyama wetu. Kwa hiyo, tunataka tusisitize suala la ujirani mwema ili tuweze kuwatumia wananchi kuweza kulinda wanyama wetu na rasilimali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa style hii mnayosema kila siku kuna ujangili, wananchi wanawachukia tembo, wanawachukia askari wa wanyamapori na ndiyo wamewaweka kama maadui, kwa hiyo hata wakiona majangili wanaingia hawawezi kuwapa ripoti ndugu zangu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnataka tulinde rasilimali zetu, tuwape nafasi hiyo wananchi wa Tanzania tuwaoneshe umoja na ushirikiano, tuwaoneshe jinsi ya kucheza michezo ya pamoja; na kama inahitajika tuwape elimu ili wajue kitu gani cha kufanya na kipi sio cha kufanya, lakini sasa hivi ndugu zetu wanaokaa kwenye vijiji vinavyopakana na mbuga wameonekana kuwa wanateswa. Niwaambie tu Mikumi kuna watu wengine tumezika nguo kwa sababu hata maiti zao hatujaweza kuzipata kwa sababu wamepigwa risasi ndani ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kutokana na hilo tunataka tuisisitize Serikali kama kweli mnataka tulinde rasilimali za Mikumi tupunguze uadui huu kati wa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi na watu wa hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuzungumzie pia masuala ya tembo. Wanyama hawa sasa hivi imekuwa kama fashion kila mtu anayekaa karibu na hifadhi anazungumzia masuala ya tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa juzi, karibu wiki mbili katika kijiji kilicho katikati ya Kilosa na Mvomero kinachoitwa Mangae mtu mmoja ameuawa na tembo. Sasa ndugu zangu Serikali kila anapokufa mtu ndipo mnataka mje? Kila siku tunalia, tunapaza sauti ndugu wanakufa lakini hakuna linalochukuliwa lolote. Tunataka tuwaambie tunawapenda tembo, tunapenda ralisilimali zetu, tunaomba mtusikilize na sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wanalima mashamba makubwa ya mpunga, watu wanatumia hela nyingi, lakini tembo wanakula zile mali. Wananchi wanapata tabu, sasa hivi kuna mafuriko huko Mikumi, watu wana njaa, wanajitahidi kulima lakini tembo wanakula, Serikali imekaa kimya. Kuna Kata inaitwa Kilangali kila siku wimbo ni kuhusu tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, tunaomba watuangalie kwa jicho pevu, itafika kipindi hawa wananchi watachoka na tutaamua kufanya jambo litakalokuwa baya, watatuongeza kwenye magereza yao. (Makofi)
Mheshimimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kinatakiwa kusema ni kwamba, tunaangalia sana utaratibu wa kuwatunza tembo wetu lakini pia kuna suala la mamba, ambapo katika mto Mwega kwenye Kata ya Maloyo, mamba wameonekana kujeruhi sana ndugu zetu na watu wengine wamekufa. Kitu cha kustaajabisha ni kwamba, Halmashauri ya Kilosa imenunua bunduki mbili kwa ajili ya kuongezea nguvu kwenye maliasili, lakini cha ajabu ni kwamba mpaka leo wameshindwa kupata vibali kutoka mkoani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atumie nafasi hii. Halmashauri ya Kilosa imenunua bunduki, lakini vibali vinaonekana kupigwa chenga. Sasa tusije tukawafanya wananchi na sisi tukawaambia watumie mbinu mbadala ili kuweza kukabiliana na wanyama hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pale Mikumi tozo lote limeonekana kuwa linakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, wananchi wa Mikumi wamekuwa lonely, pesa ya pale haiwahusu, ni kama wamekaa kisiwani hata mbuga imekuwa kama sio mali yao tena. Tunataka wananchi wa Mikumi wasikie ownership, waone ile mbuga kama ni ya kwao, tuwashirikishe wakae pale wajione kwamba ile mbuga ni ya kwetu na sisi ni watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi kila kitu kinatolewa kinapelekwa Dar es Salaam, Mikumi hakuna kitu. Waheshimiwa Wabunge mnapita sana Mikumi pale mnaangalia wanyama mnapiga selfie, lakini mnashindwa kujua hata mnawasaidiaje wananchi wa Mikumi ambao mbuga ipo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali iliangalie kwa jicho pevu mnawaachaje watu wa Mikumi? Maana imekuwa kama kisiwa, tunakuwa maskini wakati tumebarikiwa kuwa na mbuga nzuri ya wanyama ndugu zangu. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali tunataka tutengeneze kijiji cha makumbusho. Kama Zanzibar wameweza kuwa na mji mkongwe, watu wakishafanya utalii pale wanakaa tunacheza ngoma tunakula misosi, tunakula vyakula vya asili na kuuza vitu vyetu ambavyo vitakuwa pale Mikumi. Kwa hiyo tunataka tutengeneze kijiji cha makumbusho pale Mikumi wazungu na ninyi mkitoka mbugani kuzunguka mnaweza kuzunguka Mikumi ili ku- boost uchumi wa watu wa mikumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Wizara wanatuacha kama kisiwa, hakuna shughuli yoyote ya utalii inayoendelea Mikumi. Tena nimesikia wametenga bilioni moja ambazo zimeenda kwenye vijiji vinavyohusika na mbuga, kwa Mikumi sijasikia, mimi ndiye Mbunge lakini sijasikia hayo madawati sijui walimpa nani au hiyo michango imekuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipouliza kuhusu giving back kwenye society kuchangia vitu vingine wamesema sasa hivi hawataki kujadili kuhusu majengo, hospitali na vitu vingine bali wanataka sasa hivi kuweka hela inayozunguka zunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine. Kuna ile Mikumi Lodge ambayo ilikuwa pale Mikumi, ndiyo iliyokuwa tegemeo la watu wa Mikumi kwenda kutalii, lakini sasa hivi ile hoteli ilibinafsishwa tukasikia imechomwa moto. Nataka Waziri akirudi hapa aje atuambie nini mustakbali wa ile Mikumi Lodge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye barabara inayopita Mikumi ya kilomita 50, takwimu zinaonesha mnyama mmoja anagongwa kila siku, wanyama 956 wanagongwa kwa miaka mitano, tangu 2011 mpaka 2015 wamegongwa wanyama 956. Nataka Serikali ije na majibu ituambie wanataka kufanya jambo gani kuhusu kukomboa hawa wanyama wa Kitanzania na ina mpango gani na hawa wanyama ambao wanagongwa kila siku na wanawaona na takwimu wanazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza na hayo, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niweze kuchangia kidogo katika hoja hii muhimu iliyokuwa mbele yetu. Kwanza na-declare, ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na nimeshiriki kikamilifu na nipongeze sana hotuba hii ya Kamati kwa asilimia zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya ziara kadhaa katika mashirika kadhaa ya umma lakini pia tuliweza kufanya ziara kadhaa katika makampuni hapa na pale ili kuangalia uwekezaji ambao taifa letu imefanya. Nishukuru sana Mashirika hayo aliyoonesha ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nijikite moja kwa moja katika hoja iliyopo ambapo bado inaonekana kuna tatizo kubwa sana la kusaini mikataba ambayo taasisi zetu za umma zimekuwa zikifanya na wawekezaji mbalimbali. Mfano; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilisaini mkataba na kampuni kutoka Botswana inaitwa Mlimani GH na mkataba huo ni wa miaka 50 ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Serikali itakuwa inapata asilimia 10 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha jinsi gani ambavyo tumekuwa tukisaini mikataba hiyo, lakini pia inaonesha kwamba baada ya matumizi hayo na uwekezaji huo na Serikali kupata hiyo asilimia 10 baada ya miaka 50 ndiyo Serikali itakuja kunufaika na kupewa hayo majengo. Kwa mtaji huo tunarudi kule kule kwenye business as usual kwa sababu hakuna mtu ana guarantee kwamba Mlimani City kwenye miaka 50 ijayo itakuwa kwenye hali gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii inapelekea Taifa letu kukosa magawio, lakini pia imekuwa ikipata hasara kubwa na kushindwa kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali na mwisho wa siku kuleta mzigo mzito sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, moja kati ya Kamati ilipopitia na kuona, imeona kwamba mkataba kama huu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umekuwa ni mkataba ambao ni mzigo mzito sana kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tangu sijawa Mbunge wa Mikumi, nilikuwa nikisikia mkataba uliokuwa ukiendelea kati ya TANESCO na IPTL, tunaweza kuona kwamba mkataba huu pia umeonekana kuwa mzigo mzito na sisi tulikuwa tukisikia katika Bunge la 2014, Novemba. Bunge hili liliamua kwamba ule mkataba usitishwe na zile mali ziweze kutaifishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri atakapokuja hapa tuweze kujua mkataba huo umeishia wapi kwa sababu umeonekana kuwa mzigo mzito sana kwa Watanzania, kwa sababu Tanzania inaonekana kulipa shilingi milioni 300 kwa IPTL. Kwa hiyo, inaonekanaka milioni 300 kwa siku, ni mzigo mkubwa sana kwa Taifa letu ambalo kila siku tunasema bado liko kwenye hali ya checheme checheme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hiyo, mashirika mengi ya umma yamekuwa yakiilalamikia Serikali, imekuwa ikiyapa madeni mazito, inakopa katika masuala haya ya msingi. Mfano, katika taasisi za umma kama TANESCO, inaidai Serikali pesa nyingi, lakini pia suala la maji safi na taka inadai pesa nyingi. Vile vile mifuko ya kijamii imekuwa ikidai pia pesa nyingi sana kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Juni 2016 imeonekana kwamba Serikali inadaiwa trilioni mbili nukta sita na PSPF. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi gani Serikali imekuwa ikipeleka mizigo mizito sana kwa hii mifuko ya kijamii ambayo sasa ili kuweza kututumka imeanza kupeleka hili gao la mafao sasa hivi watu wanaambiwa mpaka wafikishe miaka 55. Mpaka hapa ninavyoongea nimepigiwa simu na watu wangu wa Kilombero Sugar Company wananiambia walikuwa wakitaka kusaini na PPF kwenye fomu zao lakini wameambiwa wasubiri mpaka miaka 55. Huo ni mzigo mzito sana kwa Watanzania ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweze kulipa madeni yake ambayo inadaiwa na taasisi zake. Hiyo nimetaja mfano tu wa PSPF lakini mifuko mingi ya kijamii inaonekana kukopwa na Serikali bila kulipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, tunajaribu kuangalia migongano ya Sera na Sheria. TR ndiyo msimamizi wa mashirika yote ya umma lakini inaonekana mifuko hii ya kijamii inapotaka kwenda kufanya manunuzi au inapotaka kufanya michanganuo ya kujiendesha na kuweka uwekezaji imekuwa ikipata miongozo kutoka sehemu tofauti. Mara huku wanaambiwa na BOT, mara huku wanaitwa na SSRA miluzi mingi inampoteza mbwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko hii ya jamiii inaonekana kwamba inashindwa jinsi ya kwenda kwa sababu TR anakuwa hana taarifa rasmi za kuhusu uwekezaji unaotaka kufanyika kwa sababu viongozi wa sehemu mbalimbali wakiwemo BOT pamoja na SSRA wameonekana kuwa wakitoa miongozo tofauti kitu ambacho kinapelekea mashirika haya kwenda kununua bidhaa au kununua viwanja na ardhi kwa bei kubwa ambayo inapelekea mashirika haya yajenge nyumba kwa pesa nyingi ambazo mwisho wa siku Mtanzania maskini ndiyo anataabika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Shirika la Nyumba kama NHC linataka kujenga nyumba ambazo zitakuwa na uwezo na kumfanya mwananchi wa kawaida aweze kumudu lakini kwa gharama ambazo zipo hadi sisi Wabunge tunaanza ku-beep kwamba jinsi gani tunaweza tukanunua hizo nyumba hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo nyumba zinazosemwa za bei nafuu tumeenda kukagua juzi mradi wa NHC kule Chamazi ni hela nyingi sana ambayo kiukweli kwa maskini wa Kitanzania itakuwa ngumu sana kuweza kuchukua nyumba kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana pamoja na yote, lakini pia kwenye Bodi za Wakurugenzi wameonekana wakichaguliwa watu ambao hawana uwezo kiasi kwamba wanapeleka mashirika mengi kufa na mashirika mengine pia kuweza kuwa na watendaji ambao ni wabovu. Wakurugenzi wengi wanaoteuliwa wanateuliwa kirafikirafiki na wengine wanapewa ahsante ahsante, kitu ambacho kinapelekea mashirika yetu ya muhimu kwa Taifa letu kuweza kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa hiyo tunashauri upatikanaji wa Watendaji hao uweze kufanyika kwa recruitment ili waweze kushindanishwa na wafanyiwe interview ili majina matatu yaweze kupelekwa kwenye mamlaka ambazo zinaweza kuteua mmoja atakayekuwa na tija na kusaidia mashirika yetu ya umma kwa ajili ya kwenda kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mambo mengine yanayosumbua ni pamoja na wanasiasa kuingilia mashirika haya ya umma ambayo mengine yanafanya biashara. Utasikia kuna miongozo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara fulani mara Naibu Waziri anasema hiki na hiki, fungu liende huku, kitu ambacho kinapelekea matatizo makubwa sana kwenye haya mashirika yetu ya umma na kufanya mengi yaweze ku-stuck na kushindwa kuendelea na kazi ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisisitize tunahitaji kuwaachia watendaji wetu wakuu ambao tumewapa madaraka na mamlaka ya kuweza kuongoza ili waweze kutupeleka kwenye sehemu nzuri itakayopeleka uwekezaji wenye tija kwa sababu tumeshuhudia sehemu mbalimbali watendaji hao walikuwa wanafanya kazi chini ya kiwango lakini tumeendelea kucheka na nyani na mwisho wake Tanzania inaendelea kuvuna mabua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu nitakapokuja hapa mtupe majibu jinsi gani ambavyo mtaweza kuwezesha Ofisi ya TR ili aweze kuwa na meno na nguvu ya kuweza kuyasimamia mashirika haya ambayo sasa hivi madaraka yake TR anaonekana kuwa ameporwa na sasa hivi anafanya kazi nusu nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja.