Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Leonard Haule (10 total)

MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niongeze maswali mawili ya ziada. Serikali iliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri waorodheshe mashamba ambayo yametelekezwa na wameshafanya hivyo. Je, ni lini Serikali itakwenda kutupa majibu ya moja kwa moja?
Swali la pili, kwa kuwa kuna wawekezaji wana mashamba makubwa mfano mashamba ya Miombo Estate, Kilosa Estate, SUMAGRO, Isanga Estate ambao wamebadilisha matumizi na kuvunja sheria na utaratibu, Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuyarudisha mashamba hayo kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli maelekezo yalikwishatolewa kwa Wakurugenzi wote na hasa kupitia katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa ili kuweza kuainisha migogoro yote iliyopo katika maeneo hayo ili Wizara iweze kuchukua hatua mpaka sasa mashamba ambayo tayari yamekwishaainishwa na kuletwa pale Wizarani ni jumla ya mashamba 75, lakini pia tunavyo viwanja 694. Haya yameainishwa ni katika mashamba yale kuanzia mwaka 2002 mpaka 2015 na utoaji wake sasa tayari uko katika process za kawaida.
Mheshimiwa Spika, vile vile kwa wale ambao wameshindwa kabisa kuendeleza na tayari mapendekezo yameshaanza kushughulikiwa kwa ajili ya kubatilishwa kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 tunatarajia pia kuwa kazi hiyo itafanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni, kwa sababu haya yako katika utaratibu na maelekezo yamekwishatolewa.
Waheshimiwa Wabunge, ninachowaomba kwa sababu pia kila Mbunge alipata maelekezo hayo ambayo tunawaomba mfanye kazi hiyo kwa kusaidiana na Halmashauri zenu muweze kuleta na kuainisha migogoro yote na siyo migogoro yote inapaswa kuletwa Wizarani kuna mingine ambayo pia inaweza ikamalizwa na ofisi zetu za Kanda kwa sababu tuna ofisi karibu katika Kanda nane nchi nzima. Kwa hiyo, kuna mengine yanaweza yakatatuliwa katika maeneo hayo ilimradi tu taratibu nilizozitaja katika jibu la msingi basi ziweze kufuatwa na Wizara itakuwa tayari kuyashungulikia.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Suala la Arumeru Magharibi linafanana sana na tatizo ambalo lipo Mikumi, je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kero ya maji katika Kata ya Mikumi, Ruaha, Uleling’ombe na maeneo ya Tindiga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake ametoa taarifa kwamba tunaingia katika progamu ya pili kupitia sera ya mwaka 2002 ya kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 ya Watanzania wote watakuwa wanapata maji katika vijiji na asilimia 95 katika miji.
Mheshimiwa Mbunge, kwa upande wa Jimbo lako la Mikumi na Kata zake, tutahakikisha kwamba tunazipa kipaumbele kuhakikisha zinapata maji katika hii progamu ya pili. Na ninakuomba sana baada ya Bunge hili tuwasiliane ili tuweze kupata taarifa iliyo nzuri zaidi tuanze utekelezaji.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala hili la Mbeya Vijijini linafanana sana na tatizo sugu la umeme katika Jimbo letu la Mikumi.
Swali langu ni kwamba, je, ni lini Serikali itapeleka umeme huu wa REA kwenye Kata za Tindiga, Mabwerebwere, Ulaya, Zombo, Muhenda, Uleling’ombe na Vidunda?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hapa tulipofika REA Awamu ya Pili tunatarajia ikamilike mwezi Juni mwaka huu. Vijiji vyote ambavyo vitakuwa vimesalia bila ya kuwa na umeme pamoja na vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge vya kwenye Wilaya pamoja na Jimbo la Mikumi, vyote tunatarajia tuvifikishie umeme kwenye REA Awamu ya Tatu. Kwahiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyake vyote vitapata umeme wa REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, kama tutakavyoleta bajeti yetu, tuna matumaini makubwa kwamba bajeti yetu ya kupeleka umeme vijijini itapitishwa na Waheshimiwa Wabunge na ikishapitishwa, kama tunavyosema siku zote, kwa sababu suala la umeme ni la kufa na kupona, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupeleka umeme kwenye vijiji vyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kwenye Awamu ya Tano ifikapo 2025 vijiji ambavyo vitakuwa havina umeme vitakuwa ni vya kutafuta. Kwahiyo, vijiji vyote vitapata umeme wa REA Awamu ya Tatu. Ahsante.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la Nachingwea linafanana sana na tatizo la Mikumi. Ningependa nipate majibu ya Serikali ni lini itatengeneza barabara ya lami ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi yenye urefu wa kilometa 78, ambayo ni kichocheo kikubwa sana cha uchumi wa Kata za Mikumi, Muhenda, Ulaya, Zombo, Masanze pamoja na Magomeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, natambua juhudi za Mheshimiwa Haule na umekuja ofisini, tumeongelea kuhusu hii barabara na ninawashukuru mlipitisha bajeti yetu, katika bajeti ile unafahamu kwamba kuna bajeti ya kujenga hiyo barabara. Mimi nakuhakikishia, tutahakikisha tunasimamia vile fedha ambazo mmetutengea tutatekeleza ikiwa ni pamoja na kujenga eneo hili la barabara ya kutoka Kilosa hadi Mikumi.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kutenga bajeti ya daraja hili la Ruhembe kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kutokana na kilio na mateso makali pamoja na vifo vya watu wa Ruhembe ambao wamekuwa wakilia kwa muda mrefu, Serikali ipo tayari kuleta pesa hizi kule Mikumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimesema hapa tumetenga shilingi milioni 700 na hii milioni 700 Mheshimiwa Joseph Haule anachosema ni kweli, katika lile daraja tumepoteza watu wengi sana, takribani watu wanane hivi kwa mujibu wa takwimu nilizozipata na mtu mmoja ambaye tumempoteza pale ni mtumishi wa Serikali katika Ofisi yetu ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, jambo hili sisi wengine tunalifuatilia na tunalijua vizuri sana. Ndiyo maana tumeona katika suala zima la bajeti, mwaka jana waliomba shilingi milioni 600, lakini kilichopitishwa Hazina ilikuwa ni shilingi milioni 300 na ilikuja milioni 100 peke yake. Katika msisitizo mwaka huu tukaona ile milioni 700 lazima irudi katika bajeti kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linatugusa sana kwa sababu, wananchi pale wakitaka kuvuka kufika ng‟ambo ya pili ni mpaka watembee au wazunguke karibu kilometa 20. Tatizo ni kubwa, ndiyo maana ofisi yetu sasa imefanya harakati za kutosha kuhakikisha tunawasiliana na wenzetu wa TANROAD na hivi sasa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunapewa daraja la mudam lile la chuma kupitia ofisi ya TANROAD, si muda mrefu sana angalau liweze kufungwa wakati tukisubiri mpango mrefu kuhakikisha daraja lile linajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo sasa angalau tutapunguza kilio cha watu wa eneo lile na imani yangu kubwa ni kwamba, watu wa TANROAD kuanzia wiki hii sasa muda wowote watakwenda kulifunga ili kuondoa tatizo kwa wananchi wa eneo lile.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza ninasikitika sana kwa majibu ya Naibu Waziri anaposema kwamba wafugaji hawapati maji kwa sababu wakulima wamekuwa wakikinga hayo maji, nadhani wana upungufu wa research. Inaonesha kwamba mto Mkondoa na mto Miyombo inafika mpaka sehemu ambazo wafugaji wapo na tatizo lao kubwa siyo maji, tatizo lao kubwa ni malisho. Ndiyo maana wameonekana sehemu za Malangali wakilisha katika sehemu za mashamba ya watu na sehemu ambazo watu wamehifadhi mazao yao.
Mheshimiwa Spika, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Tindiga pamekuwa siyo mahali salama kwa watu kuishi na kwa kilimo kwa sababu wafugaji wameonekana ku-take over maeneo yale na hapa nnavyozungumza na wewe pamekuwa na mauaji kila mwezi; tarehe 8 Juni ameuawa kijana anaitwa Ally Mbarouk Makakala na juzi tarehe 6 Septemba wameuawa watu wawili Elia Emmanuel Mbwane na Ramadhani John Mashimba.
Je, Serikali inawahakikishiaje usalama wa wakulima wa pale Tindiga lakini pia inawahakikishiaje usalama wananchi wa Tanzania ambapo suala la migogoro ya wakulima na wafugaji limeonekana kuwa kero kubwa sana hapa nchini? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilikuja Tindiga na kutoa baadhi ya maagizo ambayo mpaka sasa hayajafanyiwa kazi na kupelekea vifo vya hao watu wawili vilivyotokea juzi.
Je, Naibu Waziri pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wapo tayari kuambatana pamoja na mimi kuelekea Tindiga kuona hali halisi ya mauaji na hali ya kutotulia katika Jimbo la Mikumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge haridhiki na maelezo yangu nafikiri bado tuna fursa ya kuangalia suala hilo ili tuweze kupata maelezo mengine na ninamuahidi kwamba tukitoka hapa nitakaa naye tuone namna gani tunaweza tukapata taarifa ambazo zitatusaidia kuboresha hiyo ambayo tunayo ili tuweze kufanya yale ambayo ni ya muhimu kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu mauaji ambayo yametokea Mheshimiwa Mbunge amewasiliana na sisi. Tunafahamu kwamba ni sehemu ya changamoto kubwa tuliyonayo nchi nzima ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Ndiyo maana kama nilivyoeleza katika swali la awali Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara zingine ikiwepo Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na TAMISEMI tayari kuna timu ya Wizara hizo inafanya ground work kuja na mapendekezo ambayo yatatusaidia kuondoa migogoro tuliyo nayo. Kwa hiyo, naamini Mheshimiwa Mbunge akiwa na subira na katika muda ambao siyo mrefu tutafikia muafaka wa namna ya kusuluhisha matatizo haya.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba maagizo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama hayajatekelezwa. Vilevile nipo tayari nikitoka hapa kuwasiliana na Mheshimiwa DC wa kule kujua ni kwa nini maagizo yale hayajatekelezwa, ikibidi kama anavyopendekeza mimi mwenyewe sitasita kuandamana naye kwenda Jimboni kwake kuangalia hali hii. Pamoja na kwamba tayari nafahamu aliyekuwa wakati huo Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba tayari alishafika kwenye eneo hilo. Serikali hatutaki hii migogoro iendelee na pale panapotakiwa tufanye jambo lolote la kunusuru na kusuluhisha tutafanya hivyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo shida kwenda Jimboni kwake kuangalia hii hali. Nashukuru sana. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu sahihi aliyoyatoa. Niseme tu na mahali pote wasikie kwamba hakuna shamba lolote ambalo linafanana na thamani ya maisha ya mwanadamu, wala hakuna kundi lolote la mifugo ambalo linafanana na maisha ya mwanadamu. Kwa hiyo, hakuna mgogoro wowote ule ambao unaleta uhalali wa kuua mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia kigezo hiki nitoe maelekezo katika Mkoa husika na Wilaya husika kuwasaka wowote wale waliohusika na mauaji hayo na sehemu yoyote ile ambako watatumia vigezo vya mgogoro kuua watu, wakamatwe na wafikishwe kwenye mkono wa sheria. Kama watatumia kigezo cha mob nielekeze katika Kijiji husika ambacho watapoteza maisha ya mwanadamu, wakamate vijana wote wenye nguvu ambao wanaweza wakawa wawefanya hivyo ili kuweza kupekua na kuweza kupata wale waliofanya kazi hiyo. Kama Magereza hayatoshi wawaachie huru vibaka wote walioiba simu na vitu vidogo vidogo, wakamate wale wanaoua watu wawekwe ndani ili tuweze kukomesha utaratibu wa watu kuua wananchi wasiokuwa na hatia na kuwasababishia matatizo. (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa
kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Miundombinu ya mradi
wa umwagiliaji wa Bwawa la Dachi lililopo katika Kata ya Malolo liligharimu
takribani sh. 600,000,000 ambazo zilifadhiliwa na Shirika la JICA la Japan lakini
miundombinu hiyo imeharibika vibaya na imejengwa chini ya kiwango.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwashughulikia wale wote waliofanya
ubadhilifu huu na inachukua hatua gani ya kuokoa mradi huu ambao sasa Mto
Mwega umejaa mchanga na kuharibika na wananchi wakiwa wanategemea
sana bwawa hili kwa ajili ya umwagiliaji pale Malolo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kwanza nashukuru kwa kunipa taarifa kwamba kuna mradi wa umwagiliaji
umejengwa eneo la Malolo na kwamba mradi huo pengine umepata shida
kutokana na mafuriko au pengine kutokana na usanifu haukuwa sawasawa au
ujenzi haukufanyika vile inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kitu tutakachofanya tutakwenda
kuchunguza kuona ni nini kilichopo na tukishachunguza kitu cha kwanza ni
kuhakikisha tunaboresha mradi huo ili uendelee kufanya kazi iliyotarajiwa. Baada
ya kufanya uchunguzi kama kuna tatizo lolote ambalo tutaliona kwamba lipo,
basi litashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jitihada za Serikali za kukamilisha huu mradi wa World Bank, Mji wa Mikumi ni Mji wa kitalii na umekuwa ukipata wageni mbalimbali na idadi ya watu imeongezeka wamekaribia wakazi 30,000, lakini Mikumi kuna vyanzo vingi kama Iyovi, Madibila na pia Mto Muhanzi.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweza kutumia
vyanzo vingine ili viweze kusaidiana na mradi huu ili iweze kusaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi na kadhia hii?
Swali la pili, katika ziara ya Naibu Waiziri ulipokuja uliagiza watalaam waje kuangalia chanzo cha maji cha Sigareti pale Kata ya Ruaha ambapo kingeweza kusaidia Kata ya Ruaha na Rwembe, wameshafanya hivyo na kukuletea taarifa na imeonekana takribani shilingi bilioni mbili zinahitajika ili kuwezesha wananchi wa Ruaha waweze kupata mradi huo.
Je, Mheshimiwa Waziri unaweza kuwaahidi vipi wananchi wa Ruaha ambao sasa wanakutazama kwamba je, huu mradi utaingizwa katika Bajeti ya 2017/2018 ili uweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotaja kwamba ni kweli nilishawahi kutembelea Jimbo la Mikumi kwenda kuangalia miundombinu ya maji. Ni kweli tulienda na yeye mpaka Kijiji cha Ruaha na tukaona chanzo cha Segereti na tukaagiza. Kwa sababu kwa sasa hivi tuna utaratibu Wizara kwamba tunaweka fedha kila Halmashauri, basi kwa kutumia nafasi hili niagize ule mradi ambao tuliagiza kamba waufanyie mchakato wa kufanyiwa usanifu ukikamilika basi watumie fedha tutakazozitenga katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia chanzo cha Madibira tayari tumeshamuagiza Mkurugenzi wa Maji wa Mamlaka ya Morogoro (MORUWASA) ambaye Aprili anatanganza tender, ifikapo Juni na Julai tayari atakuwa amempata mkandarasi kwa ajili ya kuboresha kile chanzo cha Madibira ambacho kina umbali wa kilometa 17 kutoka chanzo kuja mjini Mikumi na kazi zitakazofanyika ni pamoja na kwanza kuboresha chanzo chenyewe cha maji cha Madibira ili kiweze kupanuliwa kuongeza kiwango cha maji na kuweka mabomba mapya ambayo yataleta maji katika Mji wa Mikumi.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika ziara yake Naibu Waziri pale Wilayani Kilosa alitembelea bwawa la Kidete na alijionea jinsi ambavyo limekuwa likileta madhara makubwa ya mafuriko na kuharibu mpaka reli kwenye Wilaya yetu ya Kilosa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa hili la Kidete ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa nilitembelea hilo eneo na nikaenda kuona shida iliyoko katika lile bwawa. Palikuwa na mkataba lakini tayari Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba sasa unafanyika usanifu upya na fedha ilishatengwa katika bajeti ya mwaka huu tunaokwenda nao. Kwa hiyo, wakati wowote tutatangaza tenda baada ya kukamilisha usanifu mpya ili tuweze kulijenga lile bwawa katika standard ile inayotakiwa isilete madhara tena kwa wananchi wa Kilosa.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nisikitishwe sana na majibu haya ya Serikali ambayo wamekuwa wakiyajibu mara kwa mara, kiukweli yanakatisha sana tamaa. Kwa sasa huu utaratibu wa Serikali wanaosema ni kifuta jasho kwa wananchi ambao wanakuwa wameuliwa na tembo au mazao yameharibiwa kiukweli haina uhalisia na haileti haki kwa wananchi ambao wamekaa kwenye mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii yote inatokana na sheria ya wanyamapori ambayo imeonekana kuwa na usumbufu na upungufu mkubwa sana. Ni lini Serikali itaileta sheria hii hapa Bungeni ili iweze kubadilishwa ili iweze kwenda na uhalisiana kurudisha fidia na hili neno la kifuta jasho libadilishwe iwe fidia iliyokuwa imetathiminiwa kutokana na matatizo ambayo wamepata wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juzi kuamkia jana katika Kijiji cha Kikwaraza pale Mikumi ambapo Mbunge wa Mikumi anaishi, simba alivamia zizi la mfugaji anaitwa Agrey Raphael na kuua ng’ombe mmoja pamoja na kujeruhi ng’ombe wawili.Sasa hayo matatizo na changamoto kama hizi zimekuwa nyingi sana kule Mikumi kwenye Kata kama Mikumi, Luhembe, Kidodi, Kilangali, pamoja na maeneo ya Mhenda. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuelekea kule mikumi ili akasikilize changamoto nyingi za wananchi ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutokana na matatizo kama haya ya wanyamapori kabla hawajaamua kuchukua sheria zao mikononi kwa kutumia silaha za jadi? Ahsante. (Makofi) [Maneno haya siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba….
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu iko sasa hivi inafanya kuiisha tunapitia upya sera na sheria pamoja na taratibu mbalimbali ambazo zinatumika katika kutoa hiki kifuta jasho na machozi, ni hivi karibuni tu tutaileta hii sheria hapa ndani Bungeni ili Bunge lako Tukufu liweze kushauri na liweze kuipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la kuambatana naye, nataka nimwambie tu niko tayari mara baada ya shughuli za Bunge kukamilika, nitaambatana naye kwenda kuangalia maeneo hayo yote yalioathirika. Ahsante.