Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susan Limbweni Kiwanga (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mara ya kwanza kuongea katika Bunge hili la Kumi na Moja, nilikuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa miaka mitano. Kwa kutambua kwamba wanawake tunaweza bila kuwezeshwa, nikaenda kugombea Jimbo la Mlimba, na wananchi wa Mlimba bila kujali itikadi zao walinipa kura za kutosha na sasa ni Mbunge wa Jimbo jipya la Mlimba ndani ya Wilaya Kilombero Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nawashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Mlimba Mabibi na Mabwana na Wachungaji na Mashekhe waliokuwa wananiombea bila kujali itikadi yangu, bila kujali dini yangu, na jinsia yangu, nasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mara ya kwanza nachangia nikiwa Mbunge wa Jimbo kwenye haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Naomba nijikite kwenye mambo kadhaa, ambayo nikijikita nayo, nikizungumza hapa nitakuwa nawasemea na wananchi wa Jimbo la Mlimba na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango kwa sasa umekuja kama mapendekezo na natarajia haya ninayoongea hapa na Wabunge wengine wanayoyaongea, basi katika mpango kamili unaokuja basi kutakuwa na vionjo ambavyo sisi kama Wabunge tumetoa mapendekezo yetu na mpango wakauchukua ili kwenda kupatikana kwenye hiyo bajeti inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Utawala Bora; Hivi ninavyokuambia Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijaapisha Madiwani wake, hivi ninavyokuambia Halmashauri zingine zote zimeshaanza kukaa na kuangalia bajeti ili waingize kwenye Bajeti Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijawahi kufanya kikao chochote, Madiwani hawajaapishwa, uchaguzi haujafanyika, eti kwa sababu tu kwa kazi tuliyofanya ndani ya Wilaya Kilombero CHADEMA, UKAWA tumepata Madiwani wengi na Wabunge wote tumebeba, sasa ni kigugumizi Serikali ya Chama cha Mapinduzi, inashindwa kupitia Waziri wa TAMISEMI anashindwa kuruhusu wananchi wa Kilombero wapate Wawakilishi wao. Ni kilio, ni kizungumkuti, hapa hamna utawala bora bali kuna wizi, utapeli, uliokithiri kipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maendeleo ya Wilaya ya Kilombero yatarudi chini, Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo mawili, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero, leo Mbunge Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, Waziri wa TAMISEMI ameandika barua, eti asiwe mpigakura ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, shame! Hiyo haikubaliki. Sasa, katika utawala bora nataka mtuambie, Wilaya ya Kilombero mnatuweka wapi, tuko Tanzania au tuko nje ya Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti inayokuja ya Wilaya ya Kilombero itaidhinishwa na nani ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero? Naomba majibu ya Serikali maana hapa hamna utawala bora. Hili ni jambo kubwa sana kama ulikuwa hulijui ni aibu kwa Taifa hili, ni aibu Serikali kujisifu kwamba ina utawala bora lakini kuna ukandamizaji uliopitiliza, wanatutolea Wabunge wa Viti Maalum kutoka Dodoma eti waende wakaape Kilombero, wanaijua wao Kilombero? Matatizo ya Kilombero tunayajua sisi hawezi kujua mtu mwingine. Kilombero hatuna barabara, Kilombero kuna migogoro ya ardhi, Kilombero hakuna maji, Kilombero pamoja tunazalisha umeme kwenye vituo viwili, Kihansi na Kidatu, lakini vijiji vingi havina umeme. Mnatutaka nini wananchi wa Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo halikubaliki, katika utawala bora naishia hapa ingawaje kuna mambo mengi, kwa sababu katika utawala bora na haki za binadamu, tulitakiwa tuwe na kituo cha Polisi Kilombero, lakini hakuna Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero tangu uhuru. Wilaya ya Kilombero Askari wamejibana kwenye kituo cha Maliasili, hivi wakati wa mafuriko Askari wanaogelea kama bata pale, kwenye mpango nataka tujue ni namna gani Wilaya ya Kilombero, tutapata kituo cha Polisi, cha uhakika kilichojengwa na Serikali hii ili wananchi wapate huduma zao na haki zao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba ni kubwa lenye Kata 16, hakuna kituo cha Polisi, Askari wamejibana kwenye kituo kidogo kwenye ofisi za TAZARA. Mnatutaka nini wananachi sisi, mnatutaka ubaya kwa sababu gani, tumewakosea nini, lakini ukiachilia hiyo, pale pale hakuna Mahakama ya Mwanzo. Leo mahabusu wakipatikana ndani ya Jimbo la Mlimba wanawekwa Idete, haki za binadamu zinavunjwa hata miaka miwili, kwa sababu hawana usafiri wa kuwapeleka Mahakamani, hawana Mahakama ya Mwanzo, huu utawala bora na haki za binadamu ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango u-reflect ni namna gani mtatuboreshea katika utawala bora ndani ya Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi oevu, utawala bora uko wapi? Leo ninavyoongea kuna kesi Namba 161 ya mwaka 2012, wananchi, wakulima na wafugaji wameipeleka Serikali Mahakamani, hasa Wizara ya Maliasili na Mahakama Kuu ikatoa order kwamba wale wananchi wasibughudhiwe kwenye lile eneo la oevu kwa sababu, walivyoweka mipaka kule hawakuwashirikisha wadau na Wizara ilikubali inakwenda kurekebisha mipaka, tangu mwaka 2012 mpaka leo! Leo wananchi wanashindwa kulima kule! Hii njaa itaingia mwaka huu! Watu wanapigwa, wafugaji wanachukuliwa pesa zao! Hawapewi risiti, nimelalamika, nimekwenda kwa Waziri Mkuu, nimekwenda kwa Waziri wa Maliasili, Mkurugenzi wa Wanyamapori, hivi ninyi mnatutaka nini sisi? Kwa nini mnatuonea namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wasukuma wako kule wafugaji na makabila yote ukienda ndani ya Wilaya ya Kilombero Jimbo la Mlimba wapo kule, kuna uchakataji, utafutaji wa gesi, wananchi hawajui! Wanakuja tu na magari yao wanaondoka kwa nini msitoe taarifa kwa wananchi kwamba mnakwenda kuchakata kule kutafuta gesi na mafuta?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Mpango utuambie ni namna gani tunaboresha masuala mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilombero, hususan Jimbo la Mlimba. Najua kuna mradi mkubwa wa upimaji ardhi, kama nilivyoongea na Mheshimiwa Lukuvi, lakini mradi huo pamoja unavyokuja sawa, Wilaya ya Kilombero na Ulanga, lakini hivi sasa wakulima wameshindwa kulima! Mnataka mwaka huu tukale wapi? Mnataka mtuletee chakula cha msaada sisi Mlimba, hatukubali! Aisee muda hautoshi! Mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, balaa! Mnasema eti katika Mpango, Mheshimiwa Mpango naomba unisikie, mnasema tu reli ya kati, mmeisahau TAZARA? TAZARA mnaiboreshaje? TAZARA mnaifanyaje? Wafanyakazi hawalipwi! Reli shida! TAZARA mliijenga kwa gharama kubwa wakati wa Nyerere, leo mnaiua kwa sababu gani? Nataka Mpango u-reflect ni namna gani mtaboresha barabara, reli ya TAZARA, Mpango uzungumzie barabara ya kutoka Ifakara mpaka Mlimba, Mlimba mpaka Madeke-Njombe mtaiboreshaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ghala la chakula liko Jimbo la Mlimba. SAGCOT, kuna kilimo kikubwa cha mpunga pale KPL (Kilombero Planting Limited), malori yanapita pale yanye tani 30 kila siku yamebeba mchele, barabara hamna! Leo kwenye Mpango hakuna hata ile barabara hamuizungumzii! Naomba mzungumzie hiyo barabara.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Susan Kiwanga, Taarifa hiyo unaikubali au vipi?
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siikubali.
MWENYEKITI: Haya, malizia dakika yako moja!
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimpe tafsiri kwamba, shame, maana yake aibuuu! Kwa Taifaaa! Hiyo ndiyo habari ya sasa. Halafu wewe tuna wasiwasi na uraia wako!
Mheshimiwa Mwenyekiti, linda dakika zangu. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Ulikuwa na dakika moja tu.
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mpango uzungumzie kuhusu barabara ya kutoka Ifakara – Mlimba, Mlimba mpaka Madege, Njombe, hili ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mpango uzungumzie masuala ya elimu; leo ninavyozungumza kuna shule moja ya Tanganyika mwaka uliopita hakufaulu hata mwanafunzi mmoja wa darasa la nne! Elimu kule siyo nzuri sana, nitawapa takwimu baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; pamoja na kuwa Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba lina mito 38, ilikuwa mpaka 49 lakini maji hakuna! Naomba Wizara ya Maji ifanye mkakati, sisi hatuhitaji visima, mkaboreshe ile mito, ili tupate maji. Kama inatoa umeme kwa nini maji ya kunywa safi na salama tusipate?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwape vyanzo vya mapato, kimoja tu! Naomba mfanye pilot area Dar-es-Salaam kuna umeme, hebu hamasisheni mtu ukienda dukani leo mtu anakuhamasisha, nikupe risiti ya TRA au nikupe ya mkono? Hii hapa ina kodi, hii hapa haina kodi! Hivi ni nani Mtanzania leo atakubali yenye kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wekeni mfano mzuri kwa pilot area ambayo ina umeme kwamba, wale wote Watanzania na mtu yeyote atakayenunua kwa risiti ya umeme ile ya TRA, baada ya muda fulani, mwaka mmoja, mnampigia hesabu amelipa kodi kiasi gani halafu mnamrudishia kitu kidogo! Mtaona kama watu hawatadai hizo risiti madukani; hicho kitakuwa chanzo kikubwa cha kukusanya kodi ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia Mpango huu kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa Mpango huu uliowasilishwa Bungeni kuhakikisha unaendana na hali halisi ya ukusanyaji kodi na udhibiti wa mapato hayo. Mpango huu ujikite kuwezesha Mashirika ya Umma kama STAMICO, TPDC, TANAPA, TAZARA, ATC, TRL na kadhalika yajiendeshe kibiashara ili kuchangia katika bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu unapozungumzia miundombinu napenda kuona ni namna gani Serikali:-
(i) Itaboresha TAZARA.
(ii) Barabara ya kutoka Ifakara-Mlimba hadi Madeke Njombe ionekane kwenye bajeti hii ili wananchi ambao asilimia 90 ni wakulima na ni eneo linatoa mazao mengi kama mpunga, ufuta, ndizi, cocoa, miti, ng‟ombe na kadhalika. Jimbo hilo ni jipya ndani ya Wilaya ya Kilombero ambapo barabara hiyo ikijengwa itaunganishwa na Mkoa wa Njombe.
(iii) Jimbo la Mlimba halina barabara, halina Kituo cha Polisi, halina hospitali ya uhakika, halina Mahakama isipokuwa moja ndani ya Kata 16. Halina maji safi na salama ingawa lina mito mingi mikubwa ukiwemo na Mto Mpanga. Hali ya shule za msingi, awali ni tete sana, hakuna Chuo cha Ufundi wala Walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi Mpango huu na bajeti hii ione namna bora ya kuingiza hela kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishashauri Bunge lililopita na naendelea kushauri namna bora ya kuhamasisha Watanzania kusaidia Serikali kukusanya kodi. Ni hivi, Dar es Salaam uwe mkoa wa majaribio ili ukifanikiwa uende nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila anayenunua bidhaa ahakikishe anapewa risiti ya TRA (electronic receipt) ambapo ataitunza na Serikali itaweka kiwango maalum cha fedha alizotumia na mwishoni mwa mwaka mtunza risiti huyo atarejeshewa kiasi fulani cha fedha alizotumia kama motisha. Ni muhimu Serikali ikajifunza toka nchi za wenzetu mbinu za ukusanyaji kodi. Haitoshi kusema tu, Watanzania daini risiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliwezeshe Shirika la Umma STAMICO kwa kuwapa maeneo mapya ya kuchimba madini ya dhahabu na kadhalika ili ichangie pato la Taifa. Isiwe kama ilivyo sasa Shirika hilo la STAMICO linarithi migodi iliyoachwa na wawekezaji na kushindwa kuzalisha madini matokeo yake linapoteza pesa. Mfano, Mgodi wa tanzanite, Kiwira, Tulawaka na kadhalika, hata ukiangalia ni kiasi gani cha fedha zinazochangia kwenye bajeti ni sifuri, sana sana Serikali inazidi kulipa watumishi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Mpango huu umedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara hivyo katika maboresho hayo kuwepo na msisitizo wa kujenga Barabara ya Ifakara-Mlimba-Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Napenda kupata majibu ya Serikali, je, unawezaje kuzalisha vyakula kwa wingi na kuingiza fedha kwenye miradi ya kilimo bila hali hiyo kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu kama barabara na kadhalika. Ni lini Wizara hii itashirikiana na Wizara ya Ujenzi ili kuleta matokeo mazuri kwa wananchi hasa wa Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua Serikali inachukua hatua gani kwa Wawekezaji wa KPL wanaolima eneo dogo la shamba na maeneo mengine wanawakodisha wafugaji na wakulima. Pia kuhusu uhamishaji wa ubia na mali zilizopo na hadi sasa mali hizo hazipo, je zimepelekwa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata majibu ya Serikali ni lini itamaliza migogoro iliyopo kwenye maeneo ya uwekezaji mfano Rupia, Ngalimila, ambako yameonyeshwa kwenye hotuba ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itawasikiliza wafugaji waliopo Jimbo la Mlimba na kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jimbo la Mlimba lina mazao mengi ya biashara kama cocoa, ufuta, ndizi, mpunga, mahindi na kadhalika, ni lini Serikali itawapa elimu wakulima hao pia kuanzisha dirisha la mkopo kwa wakulima ili wakope na wasaidiwe utaalam wa kuboresha kilimo cha mazao hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kaya takribani 400 zenye hekari karibuni elfu moja zimeathirika na madawa ya Mwekezaji KPL, (kwa hisia zao) na Mheshimiwa Waziri ulifika na kuwapa matumaini utapeleka majibu ndani ya siku ya 21 tangu tarehe 4/5/2016 na hadi leo tarehe 4/5/2016 na hakuna majibu na wananchi hawatavuna kabisa, msimu wa kilimo umepita. Je, Serikali iko tayari sasa kupata idadi kamili ya watu walioathirika na kupeleka chakula cha msaada kwani hali ya chakula ni mbaya? Ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme elimu kwanza iwe ya darasani au mitaani. Kama Serikali ingekuwa makini katika vipaumbele vya nchi elimu ingewekwa ya kwanza nchini ili kupata matokeo makubwa. Hivi bila elimu hata mimi nisingeweza kuchangia, Daktari, Mbunge, Waziri, Rais, Mwalimu, viongozi na wataalum wote wasingekuwepo. Sasa kwa nini Serikali inafanya mzaha katika suala la elimu? Jamani tusione aibu, tuseme tulikosea sasa tushirikishe wadau tuanze upya ni kweli tumejikwaa na kujikwaa si kuanguka, bado hatujaanguka tujipange.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mengi ya walimu nchini lakini naomba nizungumzie matatizo yanayowapata walimu katika Jimbo la Mlimba, pia miundombinu ya shule, upungufu wa walimu na elimu ya awali pia watoto walemavu wanaoishi katika Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za sekondari kata changamoto ziko tofauti, kuna uwekaji wa umeme wa jua ambako REA haifiki katika shule za sekondari za Kiburubutu, Uchindile, Matundu Hill na Mofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ununuzi wa samani (meza na stuli) za maabara kwa shule zote za Serikali zilizoko katika Jimbo la Mlimba ambazo ni Masagati, Utegule, Mutenga, Kamwene, Mlimba, Tree farms, Chisano, Chita, Mchombe, Kiburubutu, Nakangutu, Mbigu, Mofu na Matundu Hill. Pia ujenzi wa hosteli shule za sekondari za Chisano na Matundu Hill.
Aidha, kuna uhitaji wa madarasa 1,166 yaliyopo 467 hivyo hakuna madarasa 699; nyumba zinahitajika 1,036, zilizopo ni 199, hakuna nyumba 837; vyoo mahitaji ni 897, vilivyopo 290 hakuna vyoo 607
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nitawasilisha hali halisi ya hali ya elimu Jimbo la Mlimba.
Mheshimiewa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba kuna kituo kimoja tu cha ufundi kilichopo Mchombe. Kituo hicho cha ufundi stadi kina changamoto ya uchakavu wa madarasa ya nadharia na vitendo, upungufu wa zana na vifaa vya kufanyia kazi katika fani zote za useremala, uashi, chuma na sayansi kimu pia walimu. Hivyo naomba ukiangalie kwa jicho la pekee kituo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali ya shule za awali na msingi ni duni sana, hali ya walimu ndio kabisa, nyumba za walimu ndio usiseme, ukizingatia ni Jimbo la vijijini na miundombinu ya barabara ni mbaya hivyo wanahitaji kuwezeshwa usafiri angalau wa pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kuwa utalipa kipaumbele Jimbo la Mlimba kwa kuwapelekea walimu wa shule za sekondari na msingi katika ajira zijazo. Mahitaji sahihi nitakupatia, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hotuba hii ya Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kabisa na kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 75 - 76, naomba kunukuu, nitakwenda pale mwishoni kidogo; “Naomba kutoa taarifa kwamba Serikali inatarajia kuwasilisha katika Bunge lako Tukufu Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Bima ya Afya. Muswada huo una mapendekezo mbalimbali ikiwemo sharti la ulazima wa wananchi wote kujiunga na Bima ya Afya na wale wote wenye uwezo kuchangia bima hiyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kipengele kimenitetemesha mwili mzima nikaikumbuka Mlimba, wananchi watakaolazimishwa kuchangia ikishakuwa sheria ya nchi hii. Mlimba yenye kata 16, yenye kituo kimoja cha afya yaani sitaki hata kusema, ndiyo maana nilikuomba Mheshimiwa Waziri ufike uone mwenyewe. Kama alivyosema Mbunge aliyetangulia kwamba unaonekana una haiba na kweli ndivyo ulivyo, lakini mzigo huu wa Wizara uliyopewa ni mkubwa sana, lakini bila pesa utaishia kulia jinsi kina mama, wazee na watoto wanavyoteseka katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri nimekukaribisha uje Mlimba, mnakwenda tu kwenye yale maeneo ambayo mmeyazoea, naomba mje Mlimba, Jimbo lenye kata 16, vijiji 61, vitongoji mia mbili na zaidi. Mimi nitakupeleka kwenye kitongoji, kutoka kwenye kitongoji mpaka kijiji ni kilometa 20 yaani kutoka kitongojini mpaka katika kijiji kilometa 20 halafu hapo kwenye kijiji hakuna zahanati, unatakiwa uende tena kilometa 30, ukiongeza na 20 zinakuwa 50, mtoto anaumwa umembeba, wakati wa mvua barabara hazipitiki, maji mpaka kiunoni unaweza kuogelea, jamani kama kuna watu wanakufa nchi hii basi ni Jimbo la Mlimba, hali ni mbaya kuliko maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuuliza ni lini katika bajeti hii itatambua kwamba Mlimba kuna wananchi? Bahati mbaya sana Mlimba tulikuwa wachache, lakini leo tumewapokea watu wa aina mbalimbali, kila kabila unaloliona humu ndani liko Mlimba, ndugu zenu wako kule. Kwa sababu gani, Mlimba ni eneo la rutuba, ukipanda ndizi twende, mpunga twende, kokoa twende, ufuta twende, miti usiseme, mahindi twende, kwa nini wasikimbilie kule, kila kitu kinakubali. Gesi ndiyo iko kule, umeme wa Kihansi upo, kuna shida tena Mlimba? Kwa hiyo, watu wameingia wengi lakini huduma sifuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimesimama hapa kuchangia hii hotuba, siwezi nikachangia maeneo makubwa sana ya Kitaifa kwa sababu nina wajibu ndani ya Jimbo la Mlimba. Naomba chonde chonde, mje mtembelee Mlimba, mlinganishe na haya ninayoyasema halafu mtaona wenyewe kama hamkulia huku mimi nawaambia. Mimi wakati wa kampeni nilikuwa nalia, hata nilivyokuwa nasikia ooh, waganga wa kienyeji wanafungiwa, fungieni huku huku, kule watu wanatibiwa na waganga wa kienyeji. Hakuna hospitali, hakuna zahanati, hakuna chochote, kwa nini mtu asiende kwa mganga wa kienyeji. Hiyo huduma mnayosema ya wazee labda mjini huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini dada yangu hapa Mheshimiwa Mollel anasema alikuwa huko Muhimbili, ameshuhudia kwa macho yake mzee amekuja Muhimbili aliambiwa aende akapimwe lakini amekwenda kule laboratory akaambiwa baba shilingi 40,000 ni mzee anatembelea mkongojo. Mheshimiwa Mama Mollel akaingilia kati kwa uchungu, kwa nini mnaacha kumtibu huyu baba, wanasema bila shilingi 40,000 hakuna bure, ikabidi atoe amalipie yule mzee apate matibabu. Sasa hii huduma ya wazee iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Dar es Salaam namna hii Mlimba kuna kitu tena kule? Giza totoro, haki ya Mungu kama hatujapata uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde, mfike Mlimba. Kwa sababu kama kuna kata 16 kituo cha afya kimoja na chenyewe kinademadema, hawana wodi ya wazazi yaani ni aibu kwa Jimbo la Mlimba. Kutoka Mlimba mpaka Ifakara ambapo kuna Hospitali ya Wilaya ama St. Francis ni kilometa 150 barabara zote kama zina makaburi ya watoto kutokana na hayo mashimo, tumewakosea nini? Kule ni hatari jamani, naomba mje muone. Halafu unamwambia ananitania tu, jamani pelekeni vitu kule Jimboni vya Bunge, aah sasa hivi hatuwezi kwenda mvua, kwani tunaoishi kule wanyama? Twendeni hata wakati wa mvua mkaone hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TAMISEMI kama mpo hapa mchukue, haiwezekani vijiji 61 kuna zahanati 18, haiwezekani! Wananchi kule wanapata wapi matibabu! Hali ni mbaya kuliko maelezo! Kina mama wanakufa kule, kina baba wazee wanateseka kule, watoto wanakufa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ukurasa wa 75 mlivyoandika kwamba mnakwenda kuleta bima ya afya lazimishi, Mlimba muitoe katika hayo mambo, hiyo sheria iseme kabisa Mlimba aah aah, tutalazimisha maeneo mengine tu. Kwa sababu haiwezekani, kwanza dawa zenyewe hawapati sasa unalazimishaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, muandae kwanza mazingira ya kuandaa vituo vya afya venye Madaktari, Manesi na dawa za kutosha, mkilazimisha hiyo ni sawa. Msilete sheria kabla hamjaandaa mazingira sahihi ya watu kupata huduma, nendeni mkakague mjiridhishe. Kwa hiyo, mimi naomba hii sheria mmeiandika tu hapa lakini ichelewe kabisa, bado tuko miaka 20 nyuma. Ni nzuri sana kwa sababu nchi za wenzetu wanatekeleza sheria hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichukua takwimu kutoka kwenye halmashauri yangu, nina takwimu hapa na nitakuletea lukuki, kama za TAMISEMI ziende TAMISEMI, kwenye Wizara yako, maana hapa tunapiga, uchungu mwingine, mateso mengine wanatuletea TAMISEMI, ninyi TAMISEMI ninyi, ni matatizo makubwa! Haiwezekani sera inasema zahanati kila kijiji lakini vijiji vyote havina zahanati. Wananchi maeneo mengine wamechangia, wamejenga zahanati, haijamaliziwa, hakuna choo, hakuna mtumishi, hakuna chochote. Kwa nini mnawafanyia hivyo Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina maneno mengi, nasema mje Mlimba mjionee wenyewe kama haya maneno ninayosema ni ya uongo ili watu wapate huduma yao kwa mujibu wa kodi wanazolipa, mtushirikishe. Kambi ya Upinzani wamesema vizuri, lakini sasa Serikali hii hata mkishauri mpango mzuri hapa, basi kwa mpango huu CHF na dawa, ili Wizara ya Afya ipate hela ingizeni hata shilingi 50,000 kwenye mafuta ya magari, uongo, kweli? Tukikubaliana hapa kama REA hela sijui mmeipeleka wapi, ninyi vipi? Yaani hapa hata tukipitisha mpango mzuri wa kukusanya shilingi shilingi kwa Watanzania mnapeleka hela sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niishie hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na leo niko hapa nawakilisha Bunge kupitia Jimbo la Mlimba kwa tiketi ya CHADEMA. Ahsante sana wananchi wa Mlimba kwa kunipa heshima hii na ahsante Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kuniteua kuwa Mbunge bila kujali jinsia yangu na nitawakilisha na nitatoa heshima kwa chama na nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitaunga mkono Kitaifa Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara hii. Sasa kwa kuwa chama changu kimeniamini na kunipeleka Jimbo la Mlimba, niwatendee haki wananchi wa Jimbo la Mlimba kwa sababu ni Jimbo jipya na mambo mengine yote yanakwenda kiupya upya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali Bungeni na nikapata jibu zuri kutoka kwa Wizara husika kwamba mwezi Juni kwenye ile barabara ya Ifakara mpaka Madeke-Njombe, inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe inakwenda kumalizika kwa ule utaalam wanasema feasibility study. Sasa, baada ya feasibility study wananchi wengi wakisikia wanadhani ikimalizika hiyo ndipo wanakwenda kujenga barabara, kumbe kuna ile detailed design ambayo itahusika na mambo ya michoro, ujenzi, gharama halisi na mambo kadhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kupata majibu ya Serikali, inifahamishe na iwafahamishe wananchi, baada ya kumalizika mwezi wa Sita hiyo michoro ya ujenzi na gharama halisi ya ujenzi ni lini Serikali itakwenda kufanya na itachukua muda gani? Baada ya hapo je, Mkandarasi Mshauri atapatikana wakati gani na ujenzi wa barabara hii utaanza lini? Pia je, Serikali imejiandaa vipi kutenga fedha katika kujenga barabara hii yenye urefu wa kilometa 124.2. Nikipata majibu haya ya Serikali itanipa furaha na itanipa kujiandaa ni namna gani barabara hii itakwenda kujengwa, siyo kila wakati nilete maswali Bungeni, maana nitajua ni muda gani barabara hii inaweza ikaanza kujengwa. Naomba nipate majibu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia katika kitabu cha randama cha Waziri nimekwenda kwenye ukurasa wa 100 inaonyesha miradi ya maendeleo ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 111, miradi inayotekelezwa kwa miradi ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 116, mchanganuo wa miradi ya barabara za mikoa inayoendelezwa kwa kutumia Mfuko wa Barabara 2016/2017, imo Ifakara – Tawete – Madeke including crossing of Mngeta. Si Mgeta, kwenye kitabu chenu mmeandika Mgeta, mgeta si Mlimba, Mgeta iko Morogoro, iko Mvomero, naomba mrekebishe wekeni Mngeta, siyo Mgeta.(Makofi)
Sasa nimekwenda ukurasa wa 136, nikaona matengenezo ya muda maalum kutumia fedha za Mfuko wa Barabara Mlimba hakuna. Nimekwenda ukurasa wa 139 mpaka 147, barabara za mikoa za changarawe, udongo Ifakara – Taweta – Madeke, kilometa 57.59 makadirio mmetenga milioni 594, hapa kuna shida! Hii barabara naijua, naipita mara nyingi, matengenezo hayo bora mngechanganua, kama ni changarawe weka changarawe kilometa kadhaa, kama udongo weka udongo kilometa kadhaa. Mkiweka jumla hivyo hii barabara inatengenezwa kwa udongo asilimia 100. Kwa hiyo, ni vyema kuchanganua ili tujue kilometa ngapi changarawe, kilometa ngapi udongo ili wananchi wapate kufuatilia na mimi mwenyewe kama Mbunge nipate kufuatilia wakati napita hiyo barabara maana tunadanganywa sana na wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 157 mpaka 163, maeneo korofi; kutumia fedha za Mfuko wa Barabara za Mikoa Mlimba hakuna, eeh! Hapo ndipo nikashangaa. Hii barabara muda wote haipitiki na mpaka mje kujenga itachukua miaka kadhaa. Sasa kama hamtengi pesa katika barabara hii katika maeneo korofi huyu Mkuu wa TANROAD Mkoa wa Morogoro mnayempigia simu kila kukicha wakati matatizo yanapotokea atapata wapi hela za kwenda kutengeneza maeneo korofi katika barabara ya Ifakara – Mlimba mpaka Madeke-Njombe? Naomba mrekebishe vitabu vyenu, iingizeni na hiyo barabara ili tunapopata matatizo tupate kutibu haya maeneo korofi. (Makofi)
Barabara za mikoa na madaraja mmeweka, tuna madaraja saba, yaani ni hivi, katika Mkoa wa Morogoro na nchi hii, kama kuna mkoa wenye madaraja mengi basi ni Morogoro. Hata mkiangalia kwenye ile list ya madaraja utakuta tumekwenda mpaka 291, hakuna mkoa mwingine Tanzania wenye madaraja mengi. Madaraja hayo ukiangalia mengi yako katika Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba, kwa hiyo, ni bora mtuangalie kwa umakini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na mambo hayo, ngoja nieleze hali halisi ya Jimbo la Mlimba, najua Waziri hajafika, Naibu Waziri hajafika, naomba mfike mkaangalie ili mnapopanga mipango yenu muone ni namna gani mtasaidia Jimbo la Mlimba. Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha mpunga, mradi unaitwa KPL, uwekezaji, karibuni hekta elfu tano na kitu! Magari yanayotoka pale kupeleka mchele si chini ya tani 30 na barabara hiyo ni ya udongo. Kwa hiyo, muone hali halisi ya Jimbo la Mlimba na ni namna gani mtaiwekea, kama barabara zitapelekwa kwenye eneo la uwekezaji, basi Mlimba ingepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Mlimba lina mradi mkubwa wa umwagiliaji pale Kijiji cha Njagi, wasilianeni na watu wa Idara ya Umwagiliaji wa Kilimo. Kuna mradi mkubwa, Serikali inaingiza mabilioni ya fedha, sasa kama hatuna barabara ina maana hizo hela mnazowekeza Serikali ni bure. Naomba mlipe kipaumbele Jimbo la Mlimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha ndizi, kokoa, ufuta, kila aina, kuna mradi wa umeme Kihansi, kuna mradi wa RUBADA, unakwenda kulimwa kule katika Kijiji cha Ngalimila, hekari na mahekari. Hebu angalieni miradi inayopelekwa Mlimba na hali halisi ya barabara, barabara ni mbovu, hazipitiki mwaka mzima, sasa utajiri wa Mlimba na kuhusu miundombinu haifanani kabisa, naomba muipe kipaumbele.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika masuala ya usafiri wa treni ya TAZARA, ingekuwa treni ya TAZARA imeimarika angalau wananchi wangepata fursa ya kusafiri, lakini TAZARA bado iko kwenye mgogoro mkubwa, wafanyakazi wa TAZARA wako kwenye shida kubwa. Ni namna gani mafao yao, ni namna gani mishahara yao, kwa kweli, naomba muangalie suala la TAZARA hasa katika Jimbo la Mlimba, imepita karibuni jimbo zima, wapeni mafao yao, imarisheni reli, najua itachukua muda mrefu, basi muwaimarishe, muwape mafao yao ili wananchi wale wapate kuishi maisha yanayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano, nimekwenda nimeangalia katika kitabu cha mawasiliano ukurasa wa 18, ni kweli mmesema, kuna kata mbalimbali ambazo hakuna mawasiliano, lakini mmesema mnara haujawashwa, naona sasa, ni vyema mkawashe, kwa sababu hatuna barabara, simu hatuna, jamani, sisi tuko kwenye dunia gani? Naomba sasa mtuimarishie mawasiliano ya simu, mpeleke minara, muharakishe ili tupate mawasiliano ya barabara, maeneo korofi tupate hela na vilevile mawasiliano ya simu ili yaani ni shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ukiona akinamama na watoto wanakufa, basi wanatokea Jimbo la Mlimba kwa sababu hakuna barabara, hospitali kubwa hamna. Matatizo ni makubwa mno. Naomba mtembee, mje katika Jimbo la Mlimba muone hali halisi ili wakati mwingine mnapokuja na bajeti muiangalie kwa jicho la huruma, jicho la kweli katika Jimbo la Mlimba ili tupate maendeleo na sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi, mambo mengine nitaleta mwa njia ya maandishi katika ofisi yako, maana mnakosea majina ya maeneo yangu na vijiji, ili muone kwamba mwaka ujao nikija angalau nije sasa na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa busara na hekima kwa kunipatia angalau hizi dakika tano na mimi nipate kuzungumzia masuala kadhaa ambayo yananikera katika maisha ya Watanzania, hususan Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kwa makini hiki kitabu cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, muda hautoshi, lakini kuna mambo mengi ambayo yanaizingira nchi yetu. Kwa mfano, ukurasa huu wa 33 wanasema umuhimu wa uzalishaji wa mbegu bora nchini, sasa katika Wilaya ya Kilombero pale Ifakara tangu mimi sijazaliwa kuna kituo cha utafiti Katrin pale Ifakara, lakini mimi sijawahi kuona katika maisha yangu matokeo ya Kituo hiki cha Katrin kwenda angalau katika Wilaya ya Kilombero tu siyo Tanzania, kwenda kuwaelimisha wakulima ni mbegu gani sahihi wanatakiwa watumie na kuna magonjwa yanayokabili mpunga na kile kituo kinasema kinafanya utafiti pamoja na mpunga, lakini wananchi wa Wilaya tu ya Kilombero hawajafaidika. Sasa sielewi, Serikali naomba mtupe maelezo kwa nini kituo hiki hakina matokeo chanya? Ama hamuwapi hela au kuna kitu gani, yaani tunasikia tu lakini hatuoni faida yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi ya mpunga; wakati nakuja Bungeni nikapishana na Waziri tena nikasikia na wananchi Waziri anakuja wapi Mngeta, KPL, anakuja kufanya nini huyu kwa wawekezaji, amekwenda kule usiku kwa usiku, nikampigia simu akasema hata saa moja nitafika. Kaenda usiku wa manane, kaenda kuangalia KPL, kaenda kuangalia ghala la chakula, sijui ndiyo uliambiwa ufanye utafiti wa chakula kiko wapi, watu wanasema mna njaa ninyi hamna, lakini usiku kwa usiku mnaingia pale mnaenda kuangalia ghala la chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, KPLni eneo ambalo linazalisha mpunga na mahindi, sasa nauliza hivi, hivi akiba ya chakula ni kwa mahindi tu, je mpunga sisi tunaolima mpunga hiyo siyo akiba ya chakula, kwa nini Serikali hamuweki katika mpango kununua mazao mbalimbali ya chakula kama mpunga. Mmedharau sana lakini ndiyo kilimo ambacho kipo katika nchi hii. Kwa hiyo hata kwenye upungufu wa chakula mnaweza mkapeleka mpunga watu wapate kula. Sasa nataka majibu ya Serikali, je mpunga lini mtauingiza katika bajeti upate kununuliwa kwa ujumla? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masuala ya maji, maji Kilombero na Jimbo la Mlimba yanatokea wakati wa mafuriko, lakini mafuriko yakiisha na maji yanaondoka, lakini kuna mito ya ajabu. Sasa Wizara ya Maji hebu chukueni angalau kuwe na Wilaya moja ya mfano, maana kila Mbunge hapa akisimama maji, hebu chukueni hata Wilaya moja ya mfano muoneshe kwamba mmefanya kwa asilimia fulani na angalau Mbunge mmoja akifika hapa awapongeze, basi muende kwa awamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali njooni Kilombero ambako ni ghala la chakula, kuna mito karibu 39 lakini wananchi wa Kilombero hawana maji, wananchi wa Mlimba hawana maji, naomba mje. Naibu Waziri wa Maji ameahidi akihamia Dodoma baada ya Bunge hili atakuja kutembelea Jimbo la Mlimba, tumuoneshe miradi mbalimbali ya umwagiliaji na maji ya kunywa, miaka na miaka hela zinaingia lakini miradi haiishi, naomba mje mtagundua ufisadi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, kuhusu wafugaji na wakulima. Wafugaji na wakulima ni kero ndani ya nchi hii, lakini hawa wote wanategemeana, mfugaji anafuga mkulima analima. Hawa watu wanaowagombanisha ni Serikali kwa kutokupanga mipango bora ya ardhi ili kuwatengea maeneo wafugaji wafuge na wakulima walime, hawa wote wanategemeana, lakini katikakati kuna Serikali ndiyo inayoleta uchonganishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Kilombero…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.