Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omary Tebweta Mgumba (20 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu. Nichukue nafasi hii kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa dhamana kubwa waliyonipa kuwawakilisha ndani ya Jimbo hili. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uhai wa kufika siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nijielekeze katika suala la miradi mikubwa ile, hasa suala lile la miradi mkubwa wa Village City ambao uko Mkulazi unapatikana katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ndani ya Morogoro Vijijini katika Jimbo ninalotoka mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nijielekeze hapa kwa sababu huu siyo mradi wa kwanza kupewa ndani ya Jimbo hili lakini utekelezaji wake unachukua muda mrefu. Kwa mfano, tuna mradi wa bwawa la Kidunda mpaka sasa hivi unaenda una suasua. Hata hivyo, tunaishukuru sana Serikali kwa kutupa mradi huu, lakini naomba nisisitize katika utekelezaji ufanyike haraka iwezekanavyo; hasa katika kuandaa miundombinu rafiki kwa ajili ya uwekezaji. Kwa mfano, sasa hivi Mkulazi vijiji vyake vyote vinne ambavyo ni Usungura, Chanyumbu, Mkulazi yenyewe na Kidunda vyote havina mawasiliano, vyote barabara haipitiki mwaka mzima, lakini pia hata maji yenyewe ndiyo hayo ya kubahatisha pia havina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeiomba Serikali ingekuja na mpango kabla ya kuwekeza huo mradi mkubwa kuandaa hayo mazingira ili kuwavutia wawekezaji, hata wale watu wenye nia ya kuja kuwekeza ndani ya Morogoro vijijini, ndani ya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki wawe na moyo kwamba mazingira yanaruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu suala la viwanda, Morogoro ambayo ndiyo Mji wa mwanzo kabisa baada ya uhuru Serikali iliamua kabisa kuitenga mahsusi kwa ajili ya viwanda. Tunashukuru kwa hilo na kulikuwa na viwanda vingi tu ambavyo viikuwa vinasaidia ajira ndani ya Morogoro vijijini, Morogoro Mjini na Taifa kwa ujumla, lakini viwanda vile vingi havifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kabla ya kuja na Mpango wa Pili wa viwanda wangekaa na hawa ambao waliobinafsishiwa ili kujua changamoto gani ambazo zimewakabili mpaka sasa haviwezi kuzalisha vile viwanda na kutoa ajira kwa Watanzania. Tulikuwa na viwanda vya Moro Shoes, Viwanda vya Ngozi, Viwanda vya Mafuta, Viwanda vya Nguo vyote hivyo vimekufa vimebaki vya Tumbaku na vile vya Sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwauliza wale wa wawekezaji wanatuambia jambo moja tu, wanasema kwamba viwanda tukizalisha hapa havilipi, kwa hiyo, ndiyo maana rai yangu Serikali ni vizuri mkakaa na hawa mliowabinafsishia mkajua changamoto zao, hata kama mnataka tuvichukue tena lakini itatusaidia kubaini changamoto mapema ambazo zitatusaidia katika Mipango mipya kwa hapo kuanza kwenda mbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu viwanda hivyo hivyo, suala la Viwanda vya Tumbaku kuwa Morogoro. Morogoro kwanza watu tusisahahu kwamba na sisi ni wazalishaji wa tumbaku, lakini pia unapoanzisha kiwanda mahali popote, wote humu Wabunge tungetamani kila Jimbo kuwe na kiwanda. Hata hivyo, kiwanda unaanzisha kwa kutugemea cost benefit, unatazama wapi nikiweke hiki kiwanda ambacho kitanilipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya makampuni Morogoro ilijaliwa kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe katika kuwa pale, kwa sababu ndiyo mikoa michache ambayo ilikuwa na rasilimali nzuri tangu wakati huo, lakini pia ndiyo sehemu iliyokuwa na maji ya uhakika, kulikuwa na umeme wa uhakika, lakini pia Morogoro ndiyo karibu na Dar es Salam ambako ndiyo kuna bandari kuu ya kusafirisha mazao. Kwa ushahidi huu ndiyo maana hata sasa hivi wafanyabiashara binafsi bado wanaitamani kuwekeza Morogoro kwa sababu ya jiografia na hali ya hewa iliyokuwepo Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii Serikali muendelee kutupa nafasi kubwa zaidi Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kwa sababu mazingira ni rafiki ambayo yanavutia na yana gharama nafuu sana ya uendeshaji. Nitoe mfano tu, hiyo tumbaku inazalishwa songea, Morogoro, Iringa na Tabora na mikoa mingine. Siyo rahisi kwa mwekezaji kuweka kila kiwanda katika kila mkoa ni kwa sababu inategemea na wingi wa raw material. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie kuhusu wajasiriamali. Mpango huu umekuja lakini umeweka nje wajasiriamali, kwa sababu tukizingatia hivi maendeleo ya viwanda ambao ndiyo Mpango wa muda wa Pili huu unakuja utategemea sana maendeleo ya kilimo. Hata hivyo, wajasiriamali wa nchi hii, hususani wanaojishughulisha katika mazao ya kilimo wamewekwa kando ya mfumo wa soko letu hapa Tanzania. Leo hii mfanyabiashara au kijana aliyemaliza elimu ya Chuo Kikuu au elimu ya sekondari ambaye anataka kujiajiri mwenyewe hususani katika shughuli za kilimo hana fursa hiyo kwa mfumo wa soko uliokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana aneyesifiwa mfanyabiashara mzuri ni yule anayefanya importation, akienda nje ya nchi akinunua mazao kitu chochote bidhaa amuuzie mkulima huyo anaruhusiwa na atapewa vigelegele, lakini yule ambaye anakwenda kununua mazao kwa mkulima afanye exportation ataambiwa mwizi, kibaraka, mnyonyaji, kibaraka wa Wahindi na majina yote ya ajabu ajabu atapewa huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali waje na Mpango mzuri jinsi ya kuliboresha soko letu ili sekta hii ya sehemu hii wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa waweze kushiriki kikamilifu katika ununuzi wa mazao ya biashara kutoka kwa wakulima moja kwa moja. Kwa sababu sasa hivi mfumo uliopo umewatenganisha kati ya mnunuzi na muuzaji. Leo hii mnunuzi hajui mzalishaji anahitaji nini na mzalishaji hajui mnunuzi anahitaji nini kwa viwango ambavyo wanavitaka. Matokeo yake baadaye biashara zetu zinakosa masoko baada ya uzalishaji na hatimaye wakulima wetu wanakuwa watu wa kuhangaika, leo wanazalisha zao hili, kesho zao lile, hakuna zao moja ambalo ana uhakika nalo la kumuinua kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nizungumzie mgogoro wa wafugaji na wakulima. Sisi Morogoro kiasili ni wakulima lakini sasa hivi tumevamiwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji wasiofuata sheria, taratibu hata na kanuni zile za kufuga. Baada ya kuchunguza muda mrefu nimeona wanahama kwa sababu wanakosa malisho maji huko wanakotoka. Niiombe Serikali ije na mpango mkakati wakuboresha miundombinu ya wafugaji huko wanakotoka na kuwapa elimu ya kufuga kisasa ili waendele kubaki huko ili janga ambalo mnatuletea Morogoro limeshakuwa kubwa linatuzidi uwezo wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kwa mfano jana tu, wakulima wangu kule Kata ya Tununguo na Vijiji vyake wamepigwa na wafugaji. Mfugaji anakuja anaingia ndani ya shamba anamwambia mkulima kwamba, mifugo ni muhimu kuliko chakula wanageuza mazao ya wakulima ndiyo chakula cha mifugo. Wanawatandika bakora hata wakienda sehemu yoyote hawasikilizwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ije na Mpango mkakati wa kumaliza tatizo hili la wafugaji nchini, hasa kujenga miundombinu ya wafugaji sehemu za wafugaji na kupima ardhi yote ili tuweze kujua eneo la wafugaji lipi na wakulima? lakini hasa kuimarisha hiyo miundombinu ya kifugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho haina maana kwa umuhimu, kuhusu suala hapo hapo suala la kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo na najua maendeleo ya viwanda vinakuja baada ya maendeleo ya kilimo kuwa endelevu. Serikali kwenye Mpango wenu mmesema kabisa haijafanya vizuri kwenye kilimo, bila kuimarisha kilimo hata hivi viwanda tunavyotaka kuviweka vitakuja kukosa raw material baadaye italazimika tu-import raw material kwa ajili ya viwanda hivyo. Niishauri Serikali ije na Mpango Mkakati thabiti wa kuimarisha kilimo, kuongeza uzalishaji, kuwavutia masoko ili ku-adress matatizo ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi hasa Awamu ya Tano, kwa mwanzo mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hasa katika utumbuaji majipu na dhamira thabiti ya ukusanyaji mapato ambao unakwenda kujibu changamoto kubwa ambayo ilikuwepo kwa ajili ya ufinyu wa mapato Serikalini ambapo inatuonesha mwanga sasa miradi ya maendeleo itakwenda kwa maana ya fedha kupatikana kwa wakati na maendeleo kufika kwa wananchi.
Pia, nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango kwa Mpango mzuri aliouwakilisha leo wa miaka mitano ambao unaonesha mwanga wa Tanzania mpya ambayo Watanzania walikuwa wanasubiri mabadiliko tuliyowaambia watayapata ndani ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, nchi nyingi zimeendelea kwa kupitia mlango wa viwanda, nchi nyingi zimepiga hatua kwa maendeleo ya viwanda, lakini pamoja na maendeleo ya viwanda pia viwanda vinategemea maendeleo ya miundombinu kwanza, kwa sababu miundombinu ndiyo ufunguo wa maendeleo ya viwanda, pamoja kwamba maendeleo ya viwanda ndiyo ufunguo wa maendeleo ya uchumi, lakini bila miundombinu rafiki, miundombinu mizuri na wezeshi maendeleo ya viwanda yatakuwa yana walakini kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yangu kwa sababu ili kuwe na maendeleo ya viwanda, lazima Serikali ije na mpango mzuri wa kuboresha hii miundombinu ukizingatia Mheshimiwa Waziri anasema miongoni mwa changamoto ambazo awamu ya kwanza haikuweza kutekeleza vema katika maendeleo mazuri ya miundombinu, kwa mfano, katika miradi mitano ile mikubwa ya mpango huu, lipo suala la Mkulazi, Kijiji cha kilimo lakini miundombinu kule siyo mizuri. Matokeo yake kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, mradi ule unatakiwa kutekelezwa pamoja na ushirikishwaji wa private sector, sasa private sector nyingi zikienda kule kufanya ukaguzi zinashindwa kufika kwa wakati. Hivi ninavyosema sasa hivi mawasiliano yamekatika huko Mkulazi kwenyewe, tunakwenda miezi sita kipindi cha miezi mitatu hii ya mvua huwezi kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ili kuwavutia hao private sector waje, katika kuutekeleza mpango huu kwa uhalisia wake ni vizuri kuboresha miundombinu ya Mkulazi ukizingatia barabara, mawasiliano, umeme pamoja na maji ili lile eneo liwe rafiki, na liweze kuwavutia wawekezaji wengi kwa ajili ya mradi huu ambao utakuwa unajibu changamoto nzuri kuhusu maendeleo ya kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nichangie katika suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo kinachangia asilimia 75 ya ajira ya Watanzania, kilimo kinachangia pato la Taifa zaidi ya asilimia 25, lakini pia kinachangia katika fedha za kigeni asilimia 30 na pia kilimo ndiyo source kubwa ya mapato katika Halmashauri zetu nyingi Tanzania...
MHE. KHATIB SAID HAJI: Taarifa....
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza unilindie muda wangu na pia taarifa yake siipokei, kwa sababu nilikuwa sisomi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nachangia katika umuhimu wa kilimo, lengo lilikuwa kwa sababu ya umuhimu wa kilimo kama nilivyosema, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mpango wake anapokuja, ni vizuri akaongeza bajeti ya kilimo kutoka iliyopo sasa angalau ingefikia asilimia 10, kwa umuhimu wa kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la kilimo, kilimo kinategemea ardhi na sasa hivi tumeona changamoto kubwa iliyopo hapa nchini ni migogoro ya ardhi, nilitegemea katika mpango huu, Serikali ingekuja na majibu ya kutatua changamoto hiyo, hasa katika kupima ardhi, kuzingatia matumizi bora ya ardhi, ili kila eneo lipate mmiliki na wale wananchi waweze kumilikishwa ile ardhi waweze kuitumia kwa ajili ya kupatiwa Hati Miliki kama Hati zile za Kimila, zinaweza zikawasaidia katika kujipatia mikopo katika taasisi za fedha na kuanza kulima kilimo cha kibiashara zaidi kama walivyojiajiri katika hicho kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tatizo la kilimo katika nchi yetu hii siyo wakulima tu, tatizo kubwa ni miundombinu ya kilimo imeachwa nyuma. Ningeshauri Serikali iongeze bajeti ya kilimo katika miundombinu ya umwagiliaji, ili kilimo kiweze kuwa na uhakika wa mavuno na kiweze kuzivutia taasisi za fedha ili kuwakopesha wakulima badala ya sasa wanategemea mvua na ndiyo maana wakulima wanashindwa kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hata pale Serikali ilipokuja na mpango wa kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhia mazao, pesa zile zingetumika zaidi kwenye miundombinu ya kilimo, hasa umwagiliaji. Nafikiri tatizo la maghala wangekopeshwa tu, taasisi za fedha wangeweza kutoa kwa sababu, vile ni vifaa wezeshi tu vya kuhifadhia ambavyo vinavutia hata taasisi za fedha kukopesha wakulima, tofauti na sasa hawawezi kuwakopesha wakulima kwa sababu hawana uhakika mkulima huyu kama atavuna au atafanyaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali ingeelekeza zaidi kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo badala ya mambo mengine, nina uhakika kikiwepo kilimo cha uhakika hizi taasisi za fedha zote zitavutika kwenda kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu wana uhakika mkulima atavuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tukiwezesha katika mipango bora hii ya ardhi kupima, tukiwatengea wafugaji eneo lao, kuwatengenezea miundombinu na kuwaweka pamoja nina uhakika hata hawa wafugaji wataweza kukopesheka na wataweza kuendelea na itawavutia wawekezaji wa viwanda vya maziwa waje kuwekeza katika maeneo yale, badala ya sasa wanashindwa kuwasaidia hawa wafugaji kwa sababu wamekuwa wachungaji badala ya wafugaji na mtu anajua kwamba hata akiwekeza katika kiwanda cha maziwa hana uhakika wa kupata raw material ya maziwa kwa sababu hawa wafugaji ni wa kuhamahama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la masoko ya kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda hapa alizungumza neno la busara kabisa na ni ukweli, kwa sababu alizungumza vizuri akasema, ili bidhaa zetu za kilimo za viwanda ziweze kuuzika lazima bei zetu ziwe za chini, kuna watu wamembeza kwa sababu tunataka tulete siasa katika suala la kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli uliopo haya mazao ya kilimo tunayolima, yaliyo mengi sisi siyo watumiaji tunategemea soko la nje. Soko la nje wauzaji siyo peke yetu, lazima lina ushindani wa hali ya juu, kama bidhaa zetu zitakuwa na gharama kubwa wanunuzi wana nafasi kubwa ya kwenda nchi nyingine au kununua sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mchangiaji mmoja alizungumza hapa akasema wakulima hawana uhakika mwaka huu wanalima mbaazi bei imepanda, mwakani imeshuka analima ufuta! sababu kubwa haya ni mazao ya muda mfupi na kama mazao ya muda mfupi, mwaka huu Tanzania mkilima ufuta mkipata bei nzuri mwakani nchi nyingine nazo zinalima, matokeo yake supply inakuwa kubwa kuliko demand, ndiyo maana bei inashuka bei nyingine inapanda, sasa tukitaka tulete siasa katika mambo ya uchumi hatuendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Serikali kwa mipango mizuri inayokuja nayo, Waziri wa Viwanda tuelezane ukweli na ndiyo maana nilishauri siku moja ni vizuri kukaundwa taasisi ya utafiti wa masoko ulimwenguni ili kutoa taarifa kwa wakulima wetu kuwaambia nini kinachohitajika ulimwenguni sasa hivi kilicho na bei nzuri badala ya kilimo cha historia, umezaliwa baba yako analima kahawa, analima mkonge, unataka ulime kitu hicho tu, wakati mwingine zao hilo halihitajiki huko kwa walaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la migogoro ya ardhi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa aliyoifanya na mimi ni mnufaika mmojawapo. Alifika kijijini kwangu katika Kata ya Tununguo katika Kijiji cha Mliringwa na alichukua maamuzi hapo hapo baada ya kuona ubabaishaji. Aliweza kuirudisha kwa wakulima ardhi ya heka zaidi ya 3,500 kutoka kwa wawekezaji wababaishaji ambao waliipata kwa ujanja-ujanja. Nakuomba Mheshimiwa Waziri urudi tena, kama unavyoona Morogoro mkipita yote yale ni mapori, lakini siyo mapori ni mashamba ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la mashamba pori, wenyewe wenyeji hatuna pakulima, kila shamba lina hati, lakini hayaendelezwi. Nakuomba sana urudi myahakiki, ili mturudishie tuweze kuendelea. Morogoro ilikuwa ndiyo hifadhi ya chakula, lakini kila mwaka uzalishaji wa chakula unapungua, sababu kubwa ni ardhi imeshikwa na watu ambao wameenda kukopea hela badala ya kuitumia kwa ajili ya uzalishaji mali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho, naomba katika mpango ule wa Mkulazi, shamba namba 217 lenye hekta 63,000, mpango wa Serikali hekta zote 63,000 mnataka muwape Wawekezaji, heka 3,000 tu ndiyo mmetubakizia watu wa Mkulazi, watu wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla, hizi heka 3,000 hazitoshi kwa Watanzania katika kijiji hiki cha mfano kinachotaka kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu na naishauri Serikali, tusiiuze hii ardhi kwa mgongo wa wawekezaji kwa watu wachache kama mpango unavyosema, heka 20,000 kwa mwekezaji mmoja wa miwa, heka 20,000 kwa mwekezaji wa pili wa miwa na heka elfu tano tano kwa maana ya 20,000 zilizobaki kwa wawekezaji wanne wa mpunga, halafu Watanzania tuliobaki au watu wa Morogoro heka 3,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ni vizuri ardhi hii ikagawanywa mara mbili, nusu ikaenda kwa outgrowers kwa maana ya watu wa Mkulazi, Morogoro na Watanzania kwa ujumla waje wapate elimu ya kilimo cha kisasa pale kwenda kusambaza kwingine badala ya kuiondoa ardhi hii yote kuwapa wawekezaji huko mbele tunakokwenda kutakuwa ni kweusi, tusije kupata madhara kama wanayoyapata nchi nyingine, huko mbele vizazi vyetu vikaja kugombea ardhi na kuuana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza, kabla ya yote naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, maana yake nisije nikatiririka mpaka nikajisahau kama ule upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya bajeti ambayo inagusa, inakidhi na inajibu changamoto nyingi za Watanzania mpaka imewaogopesha upande wa pili kwa sababu watachangia nini wakati Waziri Mkuu amemaliza kila kitu na ukija kuchanganya na utendaji wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewamaliza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa wamekuwa kigeugeu sana. Tuwaambie kabisa CCM imejaa viongozi wa kila aina. Awamu ya Nne hawa hawa walikuwa wanalalamika Serikali haichukui maamuzi, ikichukua maamuzi inachelewa, tukawaambia sasa tunaleta Rais ambaye anachukua maamuzi haraka. Sasa wameanza kulalamika, wanalalamika nini, ni kwa sababu ameshawapiga Dokta John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza bajeti ya Waziri Mkuu kwa hali halisi, kuna Mbunge mmoja huku huwa anasema kwamba maneno yanadanganya lakini hesabu hazidanganyi. Nataka nimpeleke huko huko kwenye hesabu, hii bajeti imemaliza kila kitu, ukurasa wa mwisho kabisa kwenye fedha pale zilizopitishwa kwa sababu Waziri Mkuu ameonesha kwamba anaenda kutokana na maneno wanayozungumza Serikali ya Awamu ya Tano na vitendo vinaelekea vitakuwa hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tu kwenye fedha alizoomba tuzipitishe ni Sh. 236,759,874,706 wakati mwaka 2015/2016 fedha zilizopitishwa zilikuwa ni shilingi milioni 391.966 kwa kukaribisha, ni punguzo zaidi la asilimia 40 maana yake ni jinsi Serikali ilivyojipanga kubana matumizi na kuleta bajeti halisi ambayo inalingana na uwezo wa nchi yetu. Pia data hizo hizo, katika OC, mwaka 2015/2016 ilikuwa shilingi bilioni 349.288 mwaka huu OC imepunguzwa mpaka imekuwa shilingi bilioni 71.564, ni punguzo la asilimia zaidi ya 79.5, kujibana kwenye matumizi ya hovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupunguza pesa hizo katika bajeti halisi ameenda kuziongezea kwenye masuala ya maendeleo. Suala la maendeleo mwaka 2015/2016 ilikuwa ni shilingi bilioni 42.6 lakini bajeti ya Waziri Mkuu hii aliyoileta hapa ni shilingi bilioni 165.196, ni sawa na ongezeko la asilimia 122.5. Ndiyo maana nimesema naunga mkono hoja siyo kishabiki kwa uhalisia na namba halisi alizoleta Waziri Mkuu. Inaonesha ni jinsi gani bajeti hii inavyoenda kuwakomboa Watanzania walio wengi ambao kama anavyosema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba waliteseka muda mrefu sasa nao ni zamu ya kuteseka upande wa pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema upande wa pili unaona wanavyolalamika ni baada ya hii kasi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kutumbua majipu na hasa baada ya jipu kumfikia mkwe wao. Baada ya mkwe kuwekwa ndani ndiyo hawa wapambe wanaanza kulalamika na kujihami wanaona huu moto unakuja. Niwatoe shaka tu kwamba aliyekuwa msafi ataendelea kuwa msafi, wale wachafu mkono wa sheria utaendelea kuwafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya facts hizo, naomba nishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-
Kwanza suala la ajira, naiomba Serikali izingatie sana katika kuweka mipango thabiti kwa ajili ya SME kwa maana ya wafanyabiashara wadogo na wa kati na hasa ukizingatia nchi yetu watu wengi wamejiajiri kwenye kilimo na kilimo ndiyo kinatoa ajira nyingi kwa maana ya kilimo na wafanyabiashara wa kilimo na watu wa namna hiyo. Kuna mambo mengine ambayo yako kisheria kwa mfano mfumo stakabadhi ghalani upo kisheria lakini ni mfumo ambao unawatoa SME na wafanyabiashara wadogo kushiriki katika biashara ya mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali itafute namna yoyote inavyowezekana ku-accommodate kundi hili kubwa la SMEs jinsi ya kushiriki katika mfumo huo ili kuweza kukabiliana na tatizo kubwa la ajira na ukizingatia Serikalini ajira hamna hata huko sekta binafsi siyo nyingi kiasi hicho kama tunavyofikiria, nyingi tunategemea watu wajishughulishe katika ujasiriamali, mambo ya biashara na mambo mengine. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu utaona hata kule anasema changamoto mojawapo ni urejeshaji wa mikopo kwa sababu vijana wanakwenda kujiajiri lakini wanakosa hizo fursa za kujiajiri kwa sababu fursa zimekuwa chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwatengenezea vizuri namna ya kuwasaidia kwa ajili ya kushiriki katika ujasiriamali hata urejeshaji wa mikopo tutakuwa tumetatua tatizo hilo. Hata hizi fedha ambazo Serikali kwa nia nzuri inataka kuzi-allocate kwa ajili ya kukopeshana kwenye kila kijiji shilingi milioni 50, lakini lazima tuwatafutie kazi za kufanya la sivyo utawapa shilingi milioni 50 kama kazi hakuna watu watakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuishauri Serikali kwenye suala la maji hasa kwenye Bwawa la Kidunda. Bwawa la Kidunda nimeanza kulisikia hata shule sijaanza lakini mchakato wake umekuwa mrefu ukihusisha mambo ya mazingira na kadhalika. Tangu miaka 80 wazee wengine wananiambia tangu miaka ya 70 Kidunda inazungumziwa lakini sasa hivi Serikali imefika mahali pazuri naomba utekelezaji wake uende haraka sana. Kwa kumaliza utekelezaji wa mradi huu Jiji la Dar es Saalam ambalo linategemewa kiuchumi na Tanzania zaidi ya asilimia 70 utaweza kupata maji ya uhakika na viwanda vitaweza kwenda, lakini na sisi huku Morogoro tutaweza kuneemeka na fursa zinazokuja na Bwawa la Kidunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuishauri Serikali kuhusiana na migororo ya ardhi. Serikali imekuja na mpango mzuri wa majaribio katika Wilaya za Mvomero, Ulanga na Kilombero, naipongeza sana. Naomba katika mpango huu kwa sababu sasa hivi Morogoro ndiyo tunaongoza kwa migogoro ya ardhi na sababu kubwa ni kwamba ndiyo ardhi ambayo ina rutuba lakini kuna mashamba pori mengi na pia tuko karibu na soko kubwa la nyama kwa maana ya Dar es Salaam na kwenda nje, lazima mtu apitie Morogoro kwenda ku-export.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nia nzuri ile ya majaribio kwa Wilaya tatu tu ningeomba ingefanyika kwa Mkoa mzima wa Morogoro ili kuondoa hili tatizo, ukiwabana huku wanahamia upande wa pili. Mtamaliza huku watatoka upande wa pili wataenda kule kwa sababu ilishatokea katika ile Operesheni Tokomeza walianza Kilombero wote wakaja kwetu Morogoro Vijijini, operesheni ilivyokwisha wakarudi upande ule ule. Ni vizuri jambo hili lingefanyika kwa mkoa mzima ili kuwadhibiti vizuri hasa wale wavamizi waliokuja bila utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kushauri katika suala la afya. Wilaya ya Morogoro ni kongwe lakini mpaka leo haina Hospitali ya Wilaya. Wilaya hii ina Halmashauri mbili, Manispaa na Morogoro Vijijini lakini mpaka leo hii hatuna Hospitali ya Wilaya. Naomba katika mpango huu ingeingizwa pia na Hospitali ya Wilaya ili tuondoe adha ya watu wa Halmashauri hasa wa Morogoro Vijijini ambao wanatembea zaidi ya umbali wa kilometa 180 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nataka niishauri Serikali katika suala la uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji. Wote tunakubaliana miongoni mwa vyanzo vya maji katika nchi yetu vipo katika milima ya Uluguru kwa maana ya kule Kinole na Tegetero mpaka Mgeta, lakini utunzaji wa vyanzo hivyo inaachiwa Halmashauri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nachukua fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa hotuba yao nzuri na mikakati waliyoiweka katika mipango yao ya kilimo. Kwanza, nachukua fursa hii kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini nina ushauri kidogo wa kuongezea nyama katika mipango ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba ukitaka mali utaipata shambani na anasema vijana wengi tuelekee huko ndiko tutakapoipata mali. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, mali hiyo huko inapatikana ukiwa na ardhi tu na miongoni mwa matatizo makubwa yaliyopo sasa hivi nchini kwetu ni migogoro ya ardhi hasa kwa wakulima na wafugaji, kama alivyoielezea vizuri katika kitabu chake, lakini kwa bahati mbaya, na ninaisema kwa bahati mbaya kwa sababu naujua umahiri wa Mheshimiwa Waziri, lakini hakuiwekea mikakati wala mipango kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii mizuri yote ambayo mmeiweka bila kutatua tatizo la wakulima na wafugaji, yote ni sifuri kwa sababu tuna tatizo kubwa sana huko vijijini na waliosabisha tatizo hili la wakulima na wafugaji ni Wizara ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine. Wanatoa hatimiliki, wanauza mashamba bila kuzingatia hali halisi ya field ikoje. Unakuta wananchi kwenye sehemu husika wameishi miaka 12, 15, zaidi ya 20 lakini anakuja mtu anapewa hatimiliki, ndiye mmiliki halali. Mifano iko mingi, hasa nichukulie Jimbo langu, labda ndipo unaweza kunielewa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shamba la Kidago ambalo zamani lilikuwa la Uluguru Tailors. Ni shamba ambalo wakulima pale wamekaa zaidi ya miaka 40. Leo hii kapewa mwekezaji na kesi iko mahakamani. Sitaki kulizungumza sana kwa sababu lipo, lakini nakuomba Mheshimiwa Waziri uje ili uone hali halisi ilivyo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, kuna shamba la Pangawe, ambapo pale kuna mradi wa mfano, walikuwa wa KOICA (Corea) ndiyo wamewekeza. Leo hii tuna tatizo kubwa sana na mwekezaji. Nakuomba Mheshimiwa Waziri uje katika jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki ili tuweze kukaa na mwekezaji huyu tuone ni namna gani tunaweza kumaliza tatizo hili; kwa sababu nia nzuri mliyokuwanayo, bila kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji tatizo hili litakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine uko kule mpaka Kata za Maturi, Kidugaro, kwenye vijiji vya Ng‟ese huko matatizo ni hayo hayo. Kwa hiyo, ndiyo maana dhamira yako kuu ya kusema vijana twende huko, tunakwenda huko lakini ardhi hakuna. Nina ushahidi ndiyo maana unaona kuna migogoro ya ardhi kila siku nchini kote. Kwanza uje na mkakati, nafikiri baada ya kuja kutoa majumuisho yako, uje utuambie, Serikali na Wizara yako imejipanga vipi katika kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ili tuwe salama tuweze kuongeza uzalishaji katika nchi hii? Leo hii wakulima wa nchi hii hususan wa Morogoro Kusini Mashariki, zamani tulikuwa tunalinda nguruwe na kima, sasa hivi tunalinda ng‟ombe ili wasile mavuno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Sisi Morogoro Vijijini ni wakulima wazuri wa matunda, lakini sijaona katika kitabu chako mpango mkakati kwa ajili ya viwanda vya kusindika matunda, kwa ajili ya kutengeneza soko la uhakika kwa matunda yanayooza katika sehemu kubwa ya nchi yetu hususan Morogoro Vijijini. Sisi ni wakulima wazuri wa ndizi, machungwa, machenza na maembe katika vijiji vya Tegetero, Kinole, Kiloka na sehemu nyingine zote, lakini leo hii matunda yanaoza mtini wakati mwingine kwa kukosa soko la uhakika, hasa viwanda vya kusindika mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, niende kwenye Jimbo langu tena kuhusu Shamba la LMU lililoko Ngerengere. Lile shamba ni la kuzalisha mifugo ya kisasa. Shamba lile lina ukubwa zaidi ya heka 11,000 lakini utaishangaa Serikali kuna ng‟ombe 900 tu, mbuzi 200, nguruwe 50 na eneo lote limebaki ni pori. Hapa ninashauri mambo mawili, kwanza, naiomba Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika uendelezaji wa shamba hili ili lengo lililokusudiwa litimie liweze kutufaidisha watu wa Morogoro Kusini Mashariki hususan Tarafa ya Ngerengere.
La pili, ushauri wangu na ombi kwa Serikali, Ngerengere sasa hivi imekuwa Mji Mdogo, imekua na bahati mbaya hatuna eneo lolote la upanuzi kwa sababu tumezungukwa na vikosi vinne vya Jeshi. Tunamba ombi maalum Serikalini, angalau tupatiwe heka 1,500 katika shamba hili ili tuweze kuliendeleza na shamba hili pia vigawiwe vitalu kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kuendeleza maendeleo ya watu wa Morogoro Kusini Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie katika Bodi ya Korosho na bodi nyingine za mazao nchini. Miongoni mwa majipu yaliyopo katika nchi hii, hizo bodi za mazao ndiyo matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mmoja tu katika Bodi ya Korosho, hapa wadau wa korosho wamezungumza mengi kuhusu makato yanayotokea huko. Miongoni mwa kazi nyingi za Bodi ya Korosho ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji, lakini pia usindikaji (processing), lakini pia kutafuta masoko. Haya yote matatu Bodi ya Korosho inakwenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, mwaka 1973 uzalishaji wa Korosho tulifikia tani 145,000 wakati wa Mwalimu Nyerere, leo hii baada ya miaka zaidi ya 30 tunazungumza uzalishaji tani 154,000. Kwa ushahidi hata nchi zilizokuja kuomba mbegu hapa, kama Vietnam leo zimeshatupita, lakini bodi hii kila mwaka wanakupa projection, wanakwambia tunazalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu kodi nyingi zilizokuwepo kwenye Bodi hii ya Korosho. Mkulima analipa zaidi ya shilingi 640 kwakilo moja ya korosho, ambapo tukichukua tu hesabu hii iliyokuwa ni projection ya mwaka wa 2015 ambayo ni tani 154,000, zaidi ya shilingi bilioni 99 wakulima wa korosho wanaiacha. Hiyo fedha bei ya korosho ingeachwa kwa mkulima ingekuwa kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mkulima wa Korosho anakatwa shilingi 207 huko kijijini, kwa maana ya five percent tunazungumza shilingi 60 kwenye ushuru wa Hamashauri, shilingi 50 ni Chama cha Ushirika, shilingi 10 ni kwa ajili ya mtunza ghala, shilingi 20 Cooperative Union, shilingi moja kwa ajili ya kikosi kazi. Makato hayo jumla yake inafika 207. Achana na hayo, anaambiwa kuna export levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kuwa na export levy ni kwa ajili ya ku-encourage investment katika nchi yetu. Kwa miaka yote ambayo tumekuwepo hapa, Bodi ya Korosho inasema inafanya investment ya ubanguaji wa Korosho nchini. Inachukua 15 percent ya FOB price ambapo kwa mwaka wa 2015 kwa sababu FOB price ilikuwa ndogo, wakachukua bei elekezi ya shilingi 2,900 ni sawasawa na kukata shilingi 435 sawasawa na shilingi bilioni 69. Hakuna kiwanda chochote kilichowekezwa, kitu ambacho… (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kufika siku ya leo, kunipa afya na uzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba niwape pole Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla kwa mafuriko makubwa yaliyowakuta ya mvua ambapo mashamba yao yote yameharibika na mvua hiyo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Dkt. Kebwe na Mkuu wa Wilaya kwa hatua yao waliyoichukuwa ya kutusaidia chakula ingawa kidogo lakini siyo haba, kimesaidia sana waathirika hawa! Nachukua fursa hii kuiomba Serikali, tunaomba misaada zaidi ya chakula katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nampongeza sana Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri ambayo inaonyesha dhamana aliyobeba ya kutimiza matakwa na ndoto za Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Kwa sababu Rais wa Awamu ya Tano tangu anaomba kura mpaka sasa anajipambanua kwamba Serikali yake itakuwa ni ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtie moyo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara angalau ameanza kuleta mpango. Pamoja na wengine wanasema kwamba umekuja na mpango lakini fedha ambazo umeziomba ni chache sana, kuna tatizo moja ambalo kama wazungu wanavyosema, ukitaka kumnyima kitu Mwafrika, kiweke kwenye maandishi. Kwa sababu umeongelea vizuri kwenye ukurasa wa 140 kwenye mikakati yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa naomba ninukuu na umesema; “kuhamasisha sekta binafisi, kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi za hapa nchini na kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya vifungishio (packaging) na kadhalika.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni nini maana yake? Maana yake ni kwamba siyo Serikali ndiyo itajenga viwanda, bali ni sekta binafisi ndiyo itajenga viwanda. Kazi ya Serikali itakuwa ni kuweka mazingira mazuri ya kuivutia sekta binafisi kuja kuwekeza katika viwanda na hatimaye kutoa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu wanaosema kwamba bajeti ni ndogo, nafikiri kwamba hiki kitabu kama ulivyosema au tulivyokiona ni kikubwa sana, watu wanaona uvivu kukisoma chote. (Makofi)
La pili, Mheshimiwa Waziri unalaumiwa na unaambiwa kwamba mpaka leo miezi sita haujaanzisha kiwanda chochote. Hawa wenzetu ndiyo maana tunasema wenzetu vigeugeu! Juzi tu hapa wamekuja walikuwa wanailaumu Serikali hii kuhusu kuhamisha fedha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kuwahudumia Watanzania. Leo hii ndani ya miezi sita, hili ndilo Bunge la Bajeti ya kwanza la Serikali ya Awamu ya Tano; kwa fedha gani ungeweza kuitumia kujenga viwanda hivyo ndani ya miezi sita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ndiyo maana ameleta hapa sasa tumpe ili mwakani akija ndiyo tumkabe koo. Kwa hiyo, niwaombe tu ndugu zangu kwamba pamoja na kwamba tunatamani sana hivyo viwanda vijengwe, lakini haviwezi kujengwa bila kupitisha bajeti na mipango aliyoileta katika Bunge hili na hiyo ndiyo kazi yetu sisi Wabunge, tumpitishie halafu tuje tumhukumu mwakani akija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba nichangie katika mpango wenyewe aliouleta. Mheshimiwa Waziri kama ulivyosema, miongoni mwa changamoto zinazowakabili wawekezaji wengi ni malighafi isiyokuwa ya uhakika, maana yake nazungumzia viwanda ambavyo vipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangaze interest, maana unaweza kusema mimi nazungumzia korosho. Mimi niliwahi kufanya kazi katika kampuni inayohusika na mazao ya biashara miaka 19 kwa ajili ya exportation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoongelea nina uzoefu kidogo wa kujua ni changamoto gani ambazo wanakumbana nazo hususan kwenye korosho, pamba, kahawa, mbaazi, dengu, choroko, mpunga na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie changamoto zinazowakabili wawekezaji wa viwanda vya korosho, kwa sababu viwanda hivi vinabeba uchumi mkubwa sana hasa kwa wakulima wa Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na sehemu ndogo ya Mkoa wa Morogoro katika upande wa Mkulazi kule tulikopakana na Kisarawe. Ndiyo maana nafarijika na hili kulizungumzia mara nyingi kwenye upande wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi kama nilivyowahi kusema mwanzoni, sababu mojawapo ambayo wawekezaji wengi wamefunga viwanda vya kubangua korosho, miongoni mwa sababu mojawapo ni mfumo wa stakabadhi ghalani ambao hauwapi fursa wawekezaji wa ndani kupata raw materials.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mfumo unaoenda kuwashindanisha wawekezaji wa ndani wenye viwanda pamoja na wabanguaji wa India kwenye uwanja mmoja. Haiwezekani hata siku moja mwenye kiwanda cha ndani atafute raw materials mpeleke kwenye mnada akashindane na wabanguaji wa India, hawezi kupata raw material. Ndiyo maana uliona sababu, kulianzishwa viwanda zaidi ya 10, tulishafikia kubangua zaidi ya tani 50,000, nchini leo vyote vimefungwa vimebaki viwili tena vinasuasua!
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo jepesi, mtu kawekeza mtaji wake, ka-run kiwanda zaidi ya miaka mitano, leo anafunga na Serikali tumekaa kimya, wanahamishia nchi za wenzetu za jirani, kuna tatizo! Naomba kushauri katika hili, kama kweli tunataka kuwavutia wawekezaji wengi waje kwenye kuwekeza Tanzania husasan katika viwanda vinavyotumia malighafi za Tanzania, kwa mfano kama korosho, ni lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ya kuhakikisha wanapata malighafi hiyo, la sivyo itakuwa ni ndoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano tu, kwa mfano, huwezi kushindana na India kwa sababu India wenyewe ukizungumza korosho, unazungumza siasa za India. Wale wana uwezo wa kubangua tani 1,600,000, lakini uzalishaji wao ni tani 600,000 tu. Kwa hiyo, ni lazima wanahitaji tani milioni moja kutoka nchi mbalimbali. Ndiyo maana wanawapa mpaka incentive ya 2% kwa ajili ya mtu ku-export korosho iliyobaguliwa kutoka India, Tanzania kwetu hakuna! Pia mtu akibangua kule, by product kwa maana ya vipande vya korosho, kwa maana ya maganda ya korosho, yote ni biashara lakini Tanzania hakuna. Kwa hiyo, kuna incentive kubwa zaidi India kuliko Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili, tuweke kabisa Sera ambayo inatambulika na itawavutia wawekezaji kwamba mtu yoyote anayewekeza kwenye Korosho hapa Tanzania, tutahakikisha anapata raw material kwanza kwa ajili ya kutosheleza kiwanda chake kwa mwaka mzima, ndiyo turuhusu mnada mwingine kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo watakuja, kwa sababu hata sera yetu nchini hairuhusu ku-import raw material kutoka nje, wakati nchi nyingine kama Vietnam na India wanaruhusu ku-import raw material kutoka nchi nyingine. Sababu ni nini? Kumpunguzia gharama za uzalishaji huyu mwekezaji. Kwa sababu usipomruhusu a-import raw material kutoka nchi nyingine, ukizingatia korosho ni biashara ya msimu ya miezi mitatu, maana yake unamlazimisha mwekezaji wa Tanzania, kama ana kiwanda cha kubangua tani 50,000 anunue hiyo raw material ya 50,000 kwa miezi mitatu na ai-store.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana nyingine gharama itakuwa kubwa kwenye storage, kwenye mtaji, kwenye weight loss, kwenye running na kwenye mishahara kwa ajili ya walinzi na wafanyakazi wengine kulinda hiyo, kitu ambacho kwingine hamna. Wanaruhusu ndani ya miezi mitatu kwa sababu biashara ya korosho ni rotation business in the world.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii biashara, watu wanazunguka, wanunuzi ni hao hao. Miezi mitatu wako Tanzania, baada ya Machi wanakwenda India mpaka Juni; baada ya Juni wanakwenda Afrika Magharibi kwa maana ya Nigeria, Guinea Bissau na Ivory Coast. Kwa hiyo, mtu ana fursa, atakuja kununua hiyo mwezi Oktoba kwa ajili tu ya kutumia hiyo miezi mitatu, baada ya hapo anakwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki sana, nitakuona Mheshimiwa Waziri nikupe mchango zaidi katika hili ili ukusaidie katika kuwekeza katika kilimo hususan mazao ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nisije kusahau nyumbani, sisi ni wakulima wa matunda na ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mwijage kwa juhudi zako kubwa unazozifanya kwa ajili ya kutukumbuka watu wa Morogoro hususan kwenye kilimo cha ndizi na kututafutia wawekezaji kwa ajili ya kiwanda cha ndizi ili tuweze kupata soko la uhakika kwa ajili ya matunda yetu, mananasi, ndizi na menginyo yanayopatikana ndani ya Morogoro Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nitoe ushauri mwingine. Kwa sababu hii korosho tukibangua hapa tutapata ile korosho iliyobanguliwa ambayo kitalaam inaitwa kernel, lakini baada ya kernel kuna vile vipande vipande. Hivi vipande vipande, soko hakuna kwingine zaidi ya India. Ila kudhibiti kutaka watu wakabangue kule, India wameweka import duty kubwa.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri uende kwenye Ubalozi wa India ukawaombe angalau ili kuvutia wawekezaji waje wawekeze hapa, waondoe ushuru huu wa vipande ili tupate soko la hao wanaobangua hapa, vile vipande tukauze India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nakuomba kwa sababu wewe ndio Waziri wa Uwekezaji na Biashara, katika suala la mchakato wa kupata leseni za biashara, ni vizuri ukafungua dawati moja ambalo litarahisisha hao wawekezaji kwa maana ya sehemu zote kupatikana katika…
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Elimu.
Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa nafasi hiyo aliyokuwa nayo. Kama ni mchezaji huyu ni wa kulipwa. Kwa sababu wachezaji local tulikuwepo Wabunge wa CCM wengi lakini kwa mamlaka yake Mheshimiwa Rais alisajili wachezaji wa kulipwa, wewe ni mmojawapo na alikupeleka katika Wizara hii si kwa bahati mbaya. Mimi nasema kama ni upele umepata mwenye kucha, hongera sana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye mchango wangu ingawa wenzangu wengi wamesema lakini na mimi nirudie tu, hasa kwenye ubora wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, ukiangalia na records za nyuma bajeti ya elimu inaongezeka mwaka hadi mwaka, miundombinu inajengwa tukiwashirikisha wazazi, wananchi kwa mfumo uliopo sasa hivi wa D by D, walimu wanaongezeka, Serikali inajitahidi kuajiri walimu wengi na wanafunzi pia wameongezeka, kwa maana hata mwaka huu baada ya elimu bure tumeona wameongezeka wengi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa, output ya elimu na kiwango cha elimu kila siku kinashuka! Sasa ni suala la kujiuliza, kama vitu vyote hivi vinaongezeka, pesa zinaongezeka, madarasa yanaongezeka, vitabu vinaongezeka, lakini elimu inarudi nyuma; tatizo tumejikwaa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni shahidi; yeye mwenyewe amesema kwamba, yeye ni zao la shule za Serikali, Tabora Girls na ametokea huko. Jambo moja tu, hata yeye mwenyewe akienda Tabora Girls leo, ile aliyosoma yeye. Ndiyo leo inafanana na Tabora Girls? Elimu aliyopata pale Tabora Girls, ndiyo ile inayotolewa pale leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mwanzo nimesema, upele umempata mwenye kucha kwa sababu umepata elimu bora na kupitia Serikali hiyo hiyo, sasa umepewa jukumu la kusimamia Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa kabisa ambalo naliona kwa upeo wangu; moja ni kukosa uzalendo na kuzipenda shule hizi hasa kwa sisi viongozi. Nasema hili kwa sababu tulikuwa na Serikali yetu ya CCM ya Awamu ya Kwanza, tulikuwa na Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu. Wengine sisi tulianza Awamu ya Pili mpaka ya Tatu, tulikuwa tunasoma huko na watoto wa viongozi. Wote! Yaani mtu akichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Serikali ni sherehe kijijini au kwenye familia. Leo hii mtu akichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Serikali, ni kilio! Anaambiwa mwanangu nitakutafutia Private uende. Tena mbaya zaidi, hata viongozi wenyewe waliokuwa hata Serikalini, watoto wao wanaosomesha kwenye Shule za Serikali wanahesabika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea nini kama wewe mwenye jukumu la kusimamia na kuboresha hiyo elimu, watoto wako wote hawasomi pale? Wanasoma Ulaya na shule zile ambazo ni za private, zinatoa elimu bora. Kwa hiyo, wewe mwenyewe kiongozi unakubali kwamba zile shule zetu za Serikali hazitoi elimu bora. Sasa nawaomba, ili tuweze kuziboresha kwa ukweli hizi shule, kwanza sisi viongozi turudishe watoto huko; kwa sababu tunajifahamu, hata kule vijijini kwetu, ukisikia kesho mwenge unakuja, ndiyo barabara inachongwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kurudisha watoto wetu waende huko, hata Walimu, kwa sababu utakuwa unapata mrejesho kama kiongozi au Waziri, kila mtoto anapokuja kama anapata elimu bora au sivyo. Hata wale Walimu wa kule lazima wataboresha mazingira ya elimu kwa sababu wanajua mkubwa atafahamu. Kwa hiyo, ukosefu wa ubora wa elimu, output tunapata ndogo ni kutokana na sisi wenyewe dhambi hii tumeibeba. Kama ile ile ya kutokuthamini vyetu, tunathamini vya wageni, sasa tunathamini hata shule nyingine za private na nyingine, tunaacha za kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika suala la ada elekezi, nawezekana nikatofautiana kidogo na wengine. Wengi hapa walikuwa wanazungumza; walikuwa wanasema kwamba, Serikali haina haki ya kuweka ada elekezi katika suala la elimu. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hili suala la ada elekezi ni mjadala mpana.
Kama sisi humu humu Wabunge tulikuwa tunaisema Serikali hii hii, nitoe mfano mmoja hasa wa sukari; tumesema bei elekezi ya sukari ni shilingi 1,800/=. Kwanini Serikali hamsimamii bei iuzwe 1,800/=? Leo mazao ya wakulima iwe pamba, iwe korosho, iwe tumbaku yanawekewa bei elekezi; mafuta yanawekewa bei elekezi, umeme una bei elekezi, kwanini shule zisiwe na bei elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali wateja wake ni wananchi masikini wa Taifa hili, zaidi ya asilimia 70 wanaishi vijijini, kama tukiacha tu tuseme, watu hawa hizi shule ni za kwao, wamekopa, ndiyo ile kwamba tumegeuza elimu ni biashara badala ya huduma. Kwa hiyo, ni vizuri, kwa sababu hata kwenye mazao, pande mbili za wadau wanakaa; wanunuzi, wazalishaji, wakulima na wadau wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, wakae na wadau wa wamiliki wa shule na wazazi na Serikali yenyewe wapange bei elekezi kutoka na ubora wa shule, wazi-categorize katika qualities zake. Kwa sababu tunakubali kweli kuna shule nyingine zina hali ya juu zaidi, nyingine ni za kati, nyingine ni za chini, lakini zote bei haziwezi kufanana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hapa, kuna hoja ambayo ilikuja upande wa pili kule na ilitolewa mfano wa Shule ya Sekondari ya Almuntazir wanazungumza kwamba imepandishwa bei imekuwa kubwa kutoka shilingi1,600, 000/= mpaka shilingi milioni 1,900,000/=. Mimi nikajiuliza, yaani labda ni factor gani imetumika kuichagua shule hii moja badala kutolea shule nyingi? Kwa sababu kuna shule nyingine nyingi zina ada kubwa zaidi kuliko hii ya Almuntazir. Kuna shule zina ada mpaka shilingi milioni 70, nyingine shilingi milioni 35, nyingine shilingi milioni 20, nyingine shilingi milioni tano, nyingine shilingi milioni tatu; lakini amekuja kuichagua Almuntazir yenye shilingi 1,900,000/=. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tutende haki, tunapotoa maoni yetu, tuweke maoni ya jumla, tusionekane kama tunabagua jamii fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niongelee kuhusu Jimbo langu. Sisi ni Halmashauri ya Morogoro na jukumu moja la Wizara hii, linasema kwamba, ni kusimamia elimu ya ufundi. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, ukija hapa uniambie umejipanga vipi katika kutuunga mkono katika Chuo cha VETA katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini? Kwa sababu eneo tunalo, wananchi wameshajitolea, lakini tatizo tu hatujapata kushikwa mkono na Serikali kwa miaka mingi na Chuo hicho hatuna. Hii inasababisha wanafunzi wengi wanaoishia Kidato cha Nne na cha Sita kukosa nafasi ya kuendelea na elimu ya ufundi baada kukosa nafasi ya Chuo Kikuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kufika siku ya leo tuko ndani ya jengo hili tukiwa na afya njema na uhai.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri ambayo ina mipango inayoonesha dhamira ya dhati. Kuna Mbunge alizungumza jana akasema kwamba zaidi ya asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo kwenye bajeti kuu inakwenda katika Wizara hii ya Ujenzi. Baada ya kupitia kitabu nimeona pesa nyingi imekwenda huku kuna sababu maalum ya kulipia madeni ya wakandarasi. Dawa ya deni ni kulipa na inaonesha ni jinsi gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri kuwalipa wakandarasi hawa ili waendelee kujenga zaidi barabara zetu na kufungua milango ya uchumi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge mmoja jana ametoa takwimu nyingi sana kuilaumu Serikali kwa kusema kwamba pale bandarini mizigo imepungua, mizigo inayoenda Malawi, Zambia, Congo lakini amesahau kusema jambo moja tu kwamba pamoja na kupungua huko lakini mapato yameongezeka. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali pamoja na kwamba mizigo inapungua lakini mapato yameongezeka. Hii maana yake ni kwamba imedhibiti uvujaji wa mapato na hapa tunajali ubora na sio uwingi, bora kiingie kichache lakini tunakusanya zaidi. Hii inatuhakikishia kwamba sasa barabara zetu ambazo tulikuwa tunaomba na zinapitishwa na Bunge lakini pesa hazipelekwi sasa zitapelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo kwa Serikali nitoe angalizo tu, wenzangu wamezungumza lakini na mimi nisisitize kwamba Bunge hili kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Tunapitisha hizi bajeti, lakini tunategemea hizi bajeti zitakwenda kwa wakati ili bajeti hii itekelezwe ili tuendelee kuaminiwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mmoja tu katika Jimbo langu, bajeti zilizopitishwa mwaka jana kwa ajili ya matengenezo ya kawaida tu barabara ya Bigwa - Kisaki, Madamu - Kinole mpaka leo pesa hizo hazijafika na barabara hazijaanza kutengenezwa. Hiyo ni bajeti ya mwaka jana na tumebakiza mwezi mmoja na nusu kumaliza muda wa bajeti ya mwaka wa fedha.
Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ni vizuri mipango ambayo mmeileta hapa na tunaipitisha kuhakikisha kwamba inatekelezwa ili tuendelee kujenga uhalali wa kuongoza nchi hii miaka mingi ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu msongamano wa Dar es Salaam, Mbunge mwenzangu kutoka Morogoro kaka yangu Mheshimiwa Saddiq alivyozungumza lakini amesema mkoa wowote lakini mikoa ambayo ina nafasi kubwa ya kuwa na bandari kavu kama alivyosema ni Pwani au Morogoro, lakini Morogoro una nafasi kubwa zaidi ya kuwa bandari kavu kwa sababu zifuatazo:-
Kwanza, kijiografia inaunganishwa na kanda zote, Kanda ya Kati, Kusini na Kaskazini. Kwa hiyo, tukiweka bandari kavu pale itatuondoshea msongamano kule Dar e Salaam na kufanya shughuli kutekelezeka kirahisi. Pia tutafungua milango ya kiuchumi kwa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine ya jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika Jimbo langu katika Wilaya yangu ya Morogoro Vijijini. Wilaya ya Morogoro Vijijini hususani Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, siasa kubwa katika jimbo lile sasa hivi imekuwa ni barabara hususani barabara ya Bigwa - Kisaki. Ni barabara ya muda mrefu, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi 2005 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami akiwepo Waziri wa Ujenzi ambaye sasa hivi ndiye Rais aliyeko madarakani. Mwaka 2010 tena Rais, Dkt. Jakaya Kikwete akatoa ahadi ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Pia mwaka 2014 alipokuja kutuaga watu wa Morogoro Vijijini akiambatana na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Rais aliyeko madarakani, Dkt. John Pombe Magufuli akaahidi tena kwamba hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii sijaiona katika kitabu hiki, namwomba sana Mheshimiwa Waziri akija katika majumuisho yake atupe matumaini ahadi hii ya Rais itatekelezwa lini kujengwa kwa kiwango cha lami barabara?
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwani inaunganisha mkoa wa Morogoro pale Kisaki na mkoa wa Pwani kupitia Wilaya ya Rufiji. Pia inakwenda katika mbuga ya Selous, lakini ndiyo barabara pekee katika Mkoa wa Morogoro ilikidhi vigezo vya MCC. Hii ndiyo barabara iliingia katika mradi wa MCC. Kama Wamarekani waliona barabara hii ni muhimu naamini kabisa Serikali yetu ya Awamu ya Tano itaona ni muhimu zaidi na itaitekeleza haraka sana kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji mradi huu ulikuwa chini ya MCC. Namwomba Waziri akija atupe matumaini baada ya hao MCC kuleta madoido na kuweka pembeni Serikali ina mpango gani kuchukua jukumu hilo na kuimalizia kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la kupandisha hadhi barabara ya kutoka Ngerengere - Mvuha kuwa ya mkoa.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kupata nguvu ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu ya Nishati na Madini. Pia, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli, kwa hekima kubwa ya kumteua Profesa Muhongo katika nafasi ya Uwaziri wa Wizara hii. Ni kweli ametundendea haki Watanzania kwa maana upele umempata mwenye kucha katika Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo, Naibu wake, Katibu Mkuu wa Wizara na Timu nzima ya Wataalam Wizarani kwa mipango yao na mwanzo mzuri wa utendaji katika Wizara hasa kuleta umeme wa uhakika kwa sisi wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali kuhusu leseni kwa makampuni ya uchimbaji wa madini; wakati wa kuitoa kwa wawekezaji hao (leseni) ni vizuri kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kupitia viongozi wao, kwa maana ya wawakilishi katika vijiji, kata, jimbo na wilaya, ili kuondoa migogoro ya wananchi na wawekezaji katika meneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni vema ifahamike faida na manufaa ya uchimbaji huo kwa jamii na Taifa kwa ujumla, badala ya hali ya sasa mwekezaji anapata leseni Dar-es-Salaam na akifika maeneo husika halipi fidia wala service levies katika Halmashauri husika kwa kisingizio cha madini sio mali ya mtu na wao wameshalipia Serikalini kwa wamiliki wa madini hayo. Nashauri, kabla ya kutoa leseni, Wizara ni vizuri kufanya utafiti katika maeneo husika, ili kufahamu hali halisi ya eneo hilo la uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, machimbo ya marble katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, katika Halmashauri ya Morogoro, katika Vijiji vya Kivuma, Kata ya Kibuko, Tarafa ya Mkuyuni na Kijiji cha Masiyu, Kata ya Gwata. Wawekezaji hawajalipa fidia kwa wananchi na pia, kutolipia ushuru wa huduma katika halmashauri kwa miaka zaidi ya ya sita tangu waanze uchimbaji, Kampuni ya Zhong Fa!
Mheshimiwa Naibu Spika,Sababu hii imekosesha mapato stahiki kwa Serikali, kwa sababu mrabaha wanalipa katika mkoa uliosajili TIN zao, ambao uko mbali na machimbo husika, ambao hawajui kiasi halisi kinachopatikana. Nashauri katika suala la mrabaha washirikishwe TRA Wilaya na Mkoa husika wenye machimbo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba kupatiwa umeme katika Kata ya Mkulazi vijiji vinne, Kata ya Mafuli vijiji vinne, Kata ya Kidugalo vijiji saba, Kata ya Ngerengere vijiji viwili, Kata ya Kiloka kijiji kimoja, Kata ya Gwata vijiji viwili, Kata ya Mkambarani vijiji viwili, Kata ya Mkuyuni vijiji viwili, Kata ya Kinole vijiji vinne, Kata ya Tegetero vijiji vinne na Kata ya Kibuko vijiji vyote vinne.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya vijiji 64 ni vijiji 16 tu ndivyo vyenye umeme, naomba katika REA III tupatiwe umeme katika vijiji hivi na kata hizi kwa ujumla, kwani hata huko tunakotaka kwenda katika uchumi wa viwanda, hasa Kata ya Mkulazi kwenye mradi mkubwa flagship wa Mkulazi Village afya na Bwawa la Kidunda ambalo vijiji vyake vina umbali zaidi ya kilometa 50 toka kijiji kimoja kwenda kingine; mfano Usungwa, Mkulazi, Usangara mpaka Kidunda. Naomba tupatiwe umeme ili katika REA nasi tufanane na Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Ardhi. Kwa sababu kama alivyosema Mwalimu Nyerere, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne na ardhi ikiwa ni mojawapo. Siasa safi tunayo ya ujamaa na kujitegemea, watu tunao, uongozi bora tunao unaotokana na Chama cha Mapinduzi na sera zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni mchakato, hayawezi kuja siku moja kama wenzetu wanavyotaka. Hatukuwepo mwaka 1961 wakati tunapata uhuru, lakini Tanzania ya mwaka 1961 siyo Tanzania ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenzetu wanaosema kwamba hakuna dira; dira ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tena katika utangulizi tu, imezungumza Wazi kabisa nataka pale kunukuu aya ya 6(b) inasema: “kuongeza kasi ya kupima ardhi yao na kuwapatia hatimiliki za kimila ambazo watazitumia kama dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo na kuendeleza shughuli zao za kilimo, uvuvi na ufugaji.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu akisema kwamba hatuna vision, achukue Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hii hapa, kila kitu kimo humu ndani. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu sasa katika Wizara hii ya Ardhi. Ardhi kama tulivyosema, ndiyo rasilimali muhimu sana kwa Taifa lolote lile ikiwemo Tanzania; ardhi na vitu vyake vinavyopatikana katika ardhi. Inawezekana tumepotoka. Kwa mfano tu, inapogundulika mafuta au madini sehemu yoyote ya ardhi, fidia pale kwa Mtanzania ambaye anaimiliki au kijiji atapewa tu labda kama ana migomba, minazi au nyumba yake, lakini mali ile yote ya pale iliyogundulika chini ya ardhi tunaimilikisha kwa wageni. Mtanzania yule anabaki maskini kwa kisingizio cha uwekezaji au tunasema tutapata mrabaha ambao ni mdogo mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri katika hili ili kuendeleza kuwaneemesha Watanzania na kutengeneza matajiri wazawa wa Kitanzania ama kwa kumiliki Serikali au kijiji au yule mwenye ardhi pale, popote pale inapogundulika rasilimali hiyo, basi tutengeneze sheria ije kwamba yule ambaye yupo pale apate hata asilimia fulani katika umiliki ule ili utajiri ule uendelee kubaki kwa Watanzania badala ya sasa kubaki na mashimo na michanga isiyokuwa na faida na mrabaha mdogo ambao tunapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu migogoro ya ardhi. Tena Mheshimiwa Waziri nafikiri labda amepitiwa katika hili. Katika kitabu chake sijaona migogoro yoyote ya ardhi katika Wilaya yangu ya Morogoro katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini na ukizingatia ndiyo tunaongoza kwa mashamba pori yanayomilikiwa na watu wanaojiita wawekezaji, wamekopea tu mapesa, lakini hawayaendelezi. Naomba kama nitaileta tena ile list aingize hiyo migogoro ili tuweze kupatiwa majibu na kuweza kurudishwa kwa wakulima waweze kuyaendeleza baada ya hawa wawekezaji kushindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la migogoro ya ardhi kama Mheshimiwa Waziri alipotuambia pale nyuma kwamba wameshaanza kuitatua, kwa mfano, wameanza kule Kilombero na Ifakara, basi kasi hii naomba iongezwe ili tatizo hili liweze kutatuliwa haraka. La sivyo, katika hatari ninayoiona ambayo inakuja mbele yetu, inayohatarisha umoja wetu, mshikamano na amani nchini, basi ni hii migogoro ya ardhi. Wote ni mashahidi, tumeona watu wenyewe, Watanzania sasa hivi wanavyopigana, wanavyouana, kwa hiyo, naomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itolee kauli hili suala la upimaji wa ardhi na kuwamilikisha ardhi watu wake ili tuweze kuiendeleza tuondoe hili tatizo la migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kutoa ushauri katika hili, migogoro mingi hii inasababishwa na viongozi waliopewa mamlaka kubwa lakini ufahamu mdogo wa kisheria, hasa viongozi wa vijiji na Mabaraza ya Ardhi, kwa sababu huko ndiko kuna migogoro mkubwa. Pia linachangiwa na kupewa dhamana kubwa wakati hawana posho wala mshahara, matokeo yake wanajikita kwenye vitendo vya rushwa kwa mtu ambaye anataka ardhi kwa sababu anajua hawa Wenyeviti wa Vijiji au Viongozi wa Vijiji ndio wenye mamlaka, anakwenda kuwanunua wanapata ardhi kiujanja ujanja, baadaye inatuletea matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda huko vijijini utakuta mwekezaji au mtu yeyote kapata ardhi bila kuwashirikisha wananchi, lakini unakuwa muhtasari upo na sahihi zipo za initial na hati imetolewa mpaka Wizarani kwenye hiyo ardhi. Matokeo yake, hata tukienda Mahakamani, haki hiyo inakuwa hatuipati mpaka labda tumtegemee Rais atengue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba Wizara ya Ardhi, niliwahi kusema hapa kwamba pale Ngerengere sasa hivi ni Mamlaka ya Mji Mdogo; na sera za ardhi zinasema mjini popote hapahitajiki kuwa na shamba, lakini pale tuna shamba la Serikali ya LMU (Livestock Management Unity). Naomba shamba hili tuwape ardhi mahali pengine nje ya mji, ili shamba hili tuweze kulitumia kwa matumizi ya makazi na huduma za kijamii, lakini pia tuweze kuliendeleza kama ukanda wa viwanda vidogo vidogo ndani ya Halmashauri yetu kwa sababu ndiyo sehemu ambayo ina miundombinu mizuri lakini pia lipo karibu na Dar es Salaam, itakuwa ni rahisi sana kupata wawekezaji kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenda uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kujielekeza kwenye National Housing Corporation -NHC. Sasa hivi NHC wamejikita sana kwenye miji mikubwa na matokeo yake kutokana na ushindani uliopo, hata nyumba nyingine zinaanza kukosa wapangaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna Wilaya mpya, Halmashauri mpya na Mikoa mipya na tuna matatizo makubwa ya miundombinu ya majengo na wateja ni Serikali, wapo wa uhakika! Basi tunaomba kama wangeweza kuja kujielekeza huko kuanza kujenga nyumba kwenye mikoa mipya, Halmashauri mpya na Wilaya mpya ili tuweze kwenda kwa kasi na sisi tuwe na majengo na kuwa na ofisi na tutawalipa pango lao kwa kupitia Halmashauri zetu na Serikali Kuu kwa sababu jukumu hilo linatakiwa ni Serikali kujenga miundombinu. Nina uhakika wateja wa uhakika pale wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kujielekeza kwa Mheshimiwa Waziri kumwomba tena kwa mara nyingine aje katika Halmashauri yangu ya Morogoro ili kutatua mgogoro mkubwa wa Mkoa wa Pwani na Morogoro katika Kata ya Magindu Pwani na Kata ya Seregete „B‟ kuhusu mpaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo ni la muda mrefu ambapo wenzetu wa Magindu wanaleta mifugo katika Halmashauri yetu na wanawauzia wawekezaji bila kufuata taratibu, matokeo yake inaleta migogoro mikubwa sana na uhasama kati ya watu ambao ni ndugu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje katika Kata ile ya Kidugaro katika Kijiji cha Seregete hapo Magindu atusuluhishe kwa sababu tumeshakaa muda mrefu wenyewe hatujapata muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mada yetu hii iliyokuwa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukuke fursa hii kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na wataalam wao kwa kuleta bajeti nzuri kwa sababu ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano. Bajeti hii ndiyo inatoa mwelekeo wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na imeonesha anapita kutokana na maneno yake aliyokuwa anaahidi wakati wa kampeni. Aliahidi viwanda na kweli bajeti inatafsiri hivyo, inaanza kujiandaa kwa ajili ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme hii bajeti kubwa imejielekeza hasa kwenye miundombinu na elimu, miundombinu ni asilimia 25 na elimu asilimia 22, jumla 47. Hivi ni vitu muhimu sana katika maendeleo ya viwanda kwa sababu vikwazo vikubwa kwa wawekezaji wengi ilikuwa ni miundombinu sasa bajeti inaenda kutibu hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba kwanza nipate…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nichukue fursa hii nipate tu ufafanuzi kutoka kwa Waziri wakati akija kuleta majumuisho yake hasa kutokana na hotuba yake kwenye ukurasa wa 57 hasa kwenye ushuru wa mafuta ya kulainisha mitambo kutoka Sh. 665 hadi Sh. 699 kwa lita. Kwa sababu kwa ufahamu wangu ushuru wa sasa hivi ni senti 50 kwa lita na kama ushuru ndiyo huu ulioandikwa hapa Sh. 665, ni ushuru mkubwa sana. Kwa hiyo, namwomba tu alete ufafanuzi wakati anakuja kufanya majumuisho yake ipi ni sahihi, hii iliyoandikwa kwenye kitabu au ni hii inayotumika sasa hivi huko field 0.5 cent kwa lita moja ya mafuta ya kulainishia mitambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, naomba ufafanuzi pia kwenye takwimu, nimesoma kwenye kitabu hiki cha Hali ya Uchumi cha mwaka jana hasa kwenye ukurasa wa 149, uzalishaji wa mazao ya mafuta. Nimeona kwenye ufuta, alizeti, kwa mfano alizeti Tanzania tunazalisha tani milioni 2,878,500, karanga tani 1,835,933, ufuta tani 1,174,589. Nichukulie kwenye ufuta tu, hata nchi zinazoongoza ulimwenguni kama ni Myanmar kule na China hawajafikia kiasi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yake wakae vizuri waangalie hasa hii Idara ya Takwimu au hizi mlikozipata kwa sababu hizi data ziko kwenye mitandao na zinaenda, zinaweza zikapotosha wawekezaji wakaja hapa halafu malighafi hakuna au tunaweza kupanga mipango yetu kwa kuamini kwamba malighafi ipo kumbe hamna. Tunazo data za kutoka Custom kwenye Ofisi yake, mwaka jana usafirishaji wa ufuta kwenda nje ya nchi ni tani 133,000 kutoka mwezi Juni mpaka mwezi Desemba. Naomba tu wazipitie vizuri wakalete data halisi ambazo zinaweza zikawa kichocheo kwenye uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda ufafanuzi wa mwisho, kama nilivyosema mwanzoni hii bajeti ni ya miundombinu. Kwa bahati mbaya sana sijaona kwenye bajeti hii miundombinu ya kwetu kule, barabara hasa ile ya Bigwa - Kisaki kwa kiwango cha lami. Mradi ule ulikuwa ugharamiwe na MCC na hao MCC sasa hivi wamejiweka pembeni. Kwa ajili ya mradi ule na miradi mingine Tanzania iliyokuwa inagharamiwa na MCC sijui sasa Serikali imejipangaje kwa ajili ya kutekeleza pengo hili lililoachwa na hawa jamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kwa sasa nijielekeze kwenye mchango wangu. La kwanza ni kuhusu Mfuko wa Maji. Wabunge wengi wamezungumzia suala hili kwa sababu maji ni uhai. Nami lazima nijikite hapa kwa sababu tuna tatizo kubwa sana la maji katika Jimbo langu la Morogoro Kusini hasa katika vijiji kama vya Mkuyuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa maji uko miaka 15 haujawahi kufanyiwa ukarabati na vijiji vile ambavyo vilikuwa vitongoji sasa hivi vimekuwa vijiji kama vijiji vya Kivuma, Kibuka na Mwalazi wanategemea maji ya mradi huo huo ambao uliwekwa tanki la 10,000. Tukiomba tunaambiwa kwamba vijiji vingine havijapata maji wakisema ni lazima wamalize vijiji vingine ndiyo waje kwenye ukarabati wakati sasa vile vitongoji vimeshakuwa kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kibuka kilikuwa Kitongoji cha Mkuyuni sasa hivi ni kata inategemea mradi wa kijiji hicho hicho. Kwa hiyo, nimwombe Waziri akubaliane na mawazo mengi ya Wabunge kuongeza hii Sh. 50 katika lita ya petrol na diesel ili twende kutatua tatizo la maji vijijini. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, Wabunge wote wana kilio cha maji na Sh. 50 kuongezwa. Wabunge kazi yetu ni kuishauri Serikali namwomba Waziri apokee ushauri huu ili tukatatue tatizo la maji na vituo vya afya na zahanati kwa sababu mzigo huu wananchi walishabeba muda mrefu sana kwa kuchangia zahanati na vituo vya afya huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuchangia ni kupunguza tatizo la msongamano Dar es Salaam ili kufungua fursa za uchumi na kuharakisha maendeleo ya uchumi. Tatizo la msongamano Dar es Salaam linaathiri sana uchumi wa Taifa letu kwa sababu watu wanatumia muda mrefu kufika kazini na wanatumia muda mchache kufanya kazi. Tatizo hili nilishawahi kusema siku moja, ni lazima tufungue vituo vikubwa vya kibiashara na bandari kavu nje ya Dar es Salaam na ukisema nje ya Dar es Salaam basi Morogoro ina sifa mojawapo ambayo baadhi ya mikoa mingine haina.
Mheshimiwa Naibu Spika, Morogoro ni mkoa ambao umepitiwa na reli zote mbili, reli ya kati na reli ya TAZARA. Tunaweza kutumia reli hizi ili kuingiza na kutoa mizigo bandarini kwa kutumia treni badala ya magari yote kutoka mikoani na nchi zingine zikapakia mizigo pale Morogoro. Pamoja na juhudi kubwa za Serikali kutatua changamoto ya foleni Dar es Salaam lakini kwa kuanzisha bandari kavu Morogoro tutakuwa tumepata suluhu ya kudumu kumaliza changamoto hii lakini pia tumeinua hali za uchumi wa sehemu hizo zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kuchangia katika sekta hii ni suala la kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na wengi wamechangia umuhimu wa kilimo, unaajiri asilimia 70 ya watu wetu, pato la Taifa asilimia 25, hela za kigeni zaidi ya asilimia 30 inatoka kwenye kilimo, chakula asilimia 100, malighafi asilimia 65 lakini bajeti hii imejikita zaidi kwenye miundombinu badala ya kutatua uchumi wa watu wengi walikojiajiri kwenye kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba niliona kwenye Mpango kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo katika suala la Mkulazi, lakini sikuona kwenye Mpango wa 2016/2017, nilijua sasa kilimo ndiyo kitapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri katika hili…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu ambayo ni ya Mipango na Fedha. Nichukue fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kufika siku ya leo. Pia nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sijampongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango na timu yake kwa hotuba nzuri na mipango ambayo tunaiona Tanzania mpya iko mbioni kuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nichukue fursa hii kukupongeza wewe binafsi. Nakupongeza kwa umahiri wako mkubwa, kwa weledi mkubwa na unavyoendesha Bunge hili la Kumi la Moja. Usitishike na hivi vitisho kutoka upande wa pili, simamia hapo kwa sababu ya kutenda haki. Walizoea kupindisha sheria, sasa wamekutana na nguli wa sheria ambaye ni wewe ndio maana wanagonga ukuta. Usivunjike moyo, sisi tuko nyuma yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nijielekeze katika kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii hasa kwenye Benki ya Kilimo kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili. Serikali kwa kuliona hilo walianzisha Benki mahsusi ya Kilimo na Bunge hili la Kumi ambalo sisi hatukuwepo lakini tulikuwa tunasoma kwenye magazeti na taarifa mbalimbali lilipitisha sheria ya Serikali kuweka mtaji wa kutosha katika benki ile ili kutatua changamoto za wakulima wa nchi hii. Kwa sababu tatizo kubwa la nchi hii, sekta kubwa inayoajiri watu wengi ambayo ni kilimo imekuwa haikopesheki na niipongeze Serikali kwa kuliona hilo kwa kuanzisha benki hii. Walitenga zaidi ya shilingi bilioni 300 iwe kwenye Benki ya Kilimo, lakini mpaka sasa nasikitika Serikali wamepeleka shilingi bilioni 60 tu. Hizi shilingi bilioni 60 hazitoshi kutimiza malengo na mipango ya Serikali iliyopanga kwa ajili ya kukwamua Watanzania walio wengi waliojiajiri katika sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili limekuwa ni kubwa sasa matokeo yake benki hii badala ya kujielekeza katika lengo kuu la kuendeleza sekta ya kilimo hasa zile skimu za umwagiliaji na kuwakopesha wakulima, wanafanya kazi kama za benki za biashara, kutoa mikopo ya muda mfupi kwa sababu wanaogopa kupata risk kubwa. Wanaweza kutoa mikopo ya muda mrefu na pesa ikazama na wakakinzana na masharti ya Benki Kuu ya mtaji unaohitajika. Kwa dhamira hiyohiyo ambayo Serikali mliiona mwanzoni na mipango mizuri iliyokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii benki iongezewe fedha ili iweze kujitanua na kuwawezesha wakulima wengi kufaidika wakiwepo na sisi huku wa mikoani katika Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki na Tanzania kwa ujumla, hii benki ndio mkombozi wa mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ikiiwezesha benki hii inaweza kufungua matawi yake na kuongeza rasilimali watu. Kwa sasa hivi ule mtaji waliopewa hawawezi kujitanua zaidi ya kuwa Dar es Salaam ambapo ndiyo makao makuu, lakini kama mnavyojua Dar es Salaam siyo wadau wakubwa sana wa kilimo, kilimo kiko mikoani, Morogoro na sehemu nyingine. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu iongeze mtaji katika benki hii ili lengo na kusudio lililokusudiwa liweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili nijielekeze katika Tanzania Commodity Exchange. Ni wazo zuri kwa sababu utakuwa ndiyo muarobaini wa soko la uhakika la bidhaa zetu za kilimo hususan kwa wakulima wa Tanzania. Kwa sababu ni soko ambalo litatoa haki kwa wadau wote wa soko hili kuanzia mkulima, madalali, wafanyabiashara, mawakala lakini hata na wanunuzi wenyewe. Pia kutakuwa na uhakika wa ubora ambao unajulikana kwa sababu mambo yataenda kisheria na kimtandao, hawezi mtu yeyote kudanganywa, bei itakuwa wazi lakini hata na ubora utajulikana, ule udanganyifu mdogomdogo utaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu tu katika hili na niiombe Serikali kwa sababu katika utaratibu wa soko hili miongoni mwa wadau wakubwa watakuwa wale madalali wa hilo soko, madalali wa wanunuzi na wa wauzaji. Katika kitabu cha hotuba nimesoma anasema mpaka sasa hivi kuna makampuni matano ambayo yameshajiorodhesha katika soko hili. Kwa hiyo, niombe wakati anakuja kujumuisha angetutajia angalau makampuni haya ni yapi ili tuwe na uelewa mpana zaidi na tuone ni makampuni yale yale ya kiujanja ujanja yameshakamata fursa au sasa ni makampuni ya ukweli yako kwa ajili ya kumkomboa mkulima halisi wa Tanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ni pana sana na imeajiri watu wengi kwa maana ya wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wa kati, mawakala, madalali, ajira zao kubwa ziko hapa. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali pamoja na kwamba tunaenda kwenye utaratibu huu wa soko ambao ni mzuri sasa makundi haya ni vizuri tukayatambua katika ushirika wao mbalimbali. Kwa mfano pale Dar es Salaam kuna Chama cha Madalali cha Mazao ya Mahindi na Ufuta lakini Morogoro pia viko vyama vya madalali na mikoa mingi vipo. Kwa sababu mitaji yao ni midogo ni vizuri tukawatambua kisheria kwenye umoja wao huo tukaweka utaratibu wakaingia kwenye soko hili nao wakatumika kama ndio madalali wa wakulima au wa wazalishaji. Badala ya kuwaacha nje tukaachia makampuni makubwa ndiyo yashike kazi hiyo basi tujue tutakuwa na kundi kubwa la vijana wa Kitanzania watakosa ajira jambo ambalo ni hatari. Sisi lengo letu kubwa ni kutengeneza ajira kwa ajili ya kuongeza vipato kwa wananchi wetu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu katika taratibu huu, Wizara hii ivitambue vikundi vyote au umoja wowote wa madalali Tanzania nzima. Kwa sababu kwanza itasaidia sana wakitambuliwa kisheria na kupewa leseni inaweza kuwa tax base nyingine kwa sababu nafahamu wanapata mapato makubwa hawa madalali wa mikoa mbalimbali. Suala la udalali mtu akienda kununua atatumia dalali na akiuza atatumia dalali. Wakitambuliwa kisheria na mapato yao yakijulikana watasaidia kuchangia katika pato la Taifa kwa maana ya kulipa kodi na kila kitu. Pia kama Serikali mkawatengenezea fursa ya kushiriki katika huu utaratibu mpya unaokuja ili tusiliache kundi kubwa nyuma baadaye tukaenda wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo siyo kwa sababu ya umuhimu, hii Wizara ndiyo Wizara nyeti inayogawa mafungu ya fedha. Sisi kama Bunge hapa tunapitisha bajeti lakini kuna changamoto kubwa pesa haziendi kama tulivyopitisha na pia hazifiki kwa wakati. Nimuombe Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango, ni mpya kwenye Wizara hii na ndiyo maana sasa hivi hatuwezi kuchangia sana tunampa nafasi, changamoto zilizotokea huko nyuma tunaomba uzirekebishe ili pesa hizi tunazopitisha zifike kwa wakati na zifike kama tulivyopitisha ili zile shughuli za maendeleo tulizopanga katika Majimbo yetu na Wilayani kwetu ziende kama zilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja tu, suala la MKUKUTA katika Halmashauri yangu ya Morogoro Vijijini mwaka wa tatu huu haijafika hata senti tano. Hata ile miradi ambayo ilianzishwa imeishia palepale badala yake tumeelekeza nguvu kwamba wananchi wajichangie, wameshajichangisha tumeshamaliza vyumba vya madarasa zaidi ya miaka mitatu lakini mafungu hayapo. Kwa hiyo, nimuombe kwa niaba ya Serikali hiyo basi walete haya mafungu ili tuweze kumalizia miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja kwa 100% na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango uliopo mbele yetu. Kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kutendo cha kudhibiti matumizi hasa kwenye taasisi zake na mashirika ya umma. Kubwa kuliko lote hasa kitendo cha kuhamisha akaunti zote za taasisi hizi kuwa BOT, ni kitendo ambacho ni cha kizalendo sana na hili nalisema kwa kinaga ubaga na mifano ipo hai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna baadhi ya wenzetu wanasema kwamba hali halisi ya maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya kitendo hiki, siyo kweli. Siyo kweli kwa sababu hizi benki zilianzishwa, kazi yake ni kuhudumia wateja, kutoa mikopo kwa wafanyabiashara. Lakini hujuma zilizokuwa zinafanyika nitoe mfano mmoja tu wa taasisi moja kama ya bandari, yenyewe iliweka bilioni 440, kwenye fixed account kwenye mabenki mbali mbali kwa rate ya 3.5%, bilioni 440. Halafu yenyewe tena ikaenda kukopa kwenye benki hizo hizo bilioni 100 kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu hapa, baada ya Serikali kuona hujuma hizo, kupeleka hizo akaunti BOT anasema Serikali imenyonga wafanyabiashara, siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taasisi nyingine hizo hizo, hii mifuko yetu ya kijamii, inakusanya shilingi bilioni 38 kwa mwaka, shilingi bilioni 27 matumizi kwa sababu fedha zipo tu za kutumia, inachangia kwenye mfuko shilingi bilioni mbili tu kwa mwaka mzima, leo Serikali imeona hujuma hizo imepeleka hizi fedha zote zikapate udhibiti BOT mtu anasema wafanyabiashara wamenyongwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kitendo hiki cha kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na ovyo ambacho sasa tuiombe tu Serikali ifanye mfumo mzuri ambao kama hizi benki zipo ziende sasa zikakope kule BOT kwa rate inayokubalika ya sokoni siyo ile ya kiwizi wizi ya 3.5 halafu fedha nyingine zinaenda kwa wajanja wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa sababu huu unasema ni wizi alafu hizo hizo benki zilikuwa zinaikopesha Serikali kwenye treasure bill, Serikali ikiwa na tatizo inakwenda kukopa kwenye benki zile zile kwa rate kubwa zaidi ya asilimia 15, 20. Kwa hiyo, niwaombe Serikali hapo msilegeze, msimamo ni huo huo ili kwamba tuwe na nidhamu katika matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili kuhusu makusanyo hasa kwenye TRA, nilikuwa naomba Waziri Mpango katika mapendekezo ya kuongeza tax base, kweli tumepata muhamasisho wa Rais na watu mbalimbali kwamba watu wajitolee kwenda kulipa kodi kwa hiyari, lakini kitendo cha Mtanzania, wengi wanahofia ukisema leo nataka kuanza kulipa kodi, TRA sasa hawaanzi pale, watakupa hizo kodi miaka kumi ijayo hata kulipika hazilipiki. Ni sawa sawa sasa wanakwenda kufilisi, matokeo yake watu wanaogopa na watu walipakodi wanaendelea kubaki walewale, ni kitu ambacho hakitaisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu, kama kuna uwezekano toweni muda maalum kwamba watu wajitokeze kulipa kodi ili muongeze wigo wa tax base, lakini mkasamehe hayo makando kando ya nyuma ili watu waanze kulipa kuanzia hapo kwenda mbele. Tutaongeza wigo mpana wa kulipa kodi kuliko kung’ang’ania kusema mpitie makando kando hayo watu hawana risiti, hawana uthibitisho zaidi ya kuwafilisi, matokeo yao watafilisika, hamtakusanya tena hizo kodi uko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine sasa hivi kwenye makusanyo hayo ya kodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyokuwa mbele yetu. La kwanza nijielekeze kwenye ukurasa wa 76 wa kitabu cha PAC. Kwanza nitangaze interest kuwa mimi ni Mjumbe wa PAC hasa kuhusu suala la muamala uliokwama wa shilingi bilioni 100 TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili kwa sababu ni suala mtambuka, TAMISEMI kama tunavyofahamu ni Wizara mama na inayobeba Halmashauri zetu. Tumewasikiliza Wajumbe waliotangulia wengi tulikuwa tunalalamika pesa haziji kwenye Halmashauri yetu kwa wakati, na tulikuwa tunatafuta mchawi ni nani? Katika hili ni vizuri Serikali ikachukua hatua stahiki kujua liko nini hapo Hazina, kwamba imetoa exchequer ya shilingi milioni 287 kwenda TAMISEMI, halafu wanarudisha nyuma shilingi bilioni 100 bila taarifa ya TAMISEMI wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI wanaandika cheque kuwalipa wateja wao wanakwenda benki wanakuta hewa, na hili sio jambo dogo. Katika Bajeti ile ambayo ilikuwa ya shilingi milioni 287 ambayo pesa zilizoletwa hizi ni sawasawa na asilimia 47, maana yake nini? Kama asilimia 47 pesa hazikuja TAMISEMI ukizingatia hata bajeti yetu mpya ya maendeleo ni asilimia 40 hii mpya, hiyo ya zamani ilikuwa chini ya hapo. Ndiyo maana kumbe tunalalamika kwenye Halmashauri zetu pesa haziji tatizo liko huku huku kwa watoa fedha wenyewe. (Makofi)
Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano, tuko pamoja kama alivyosema Mheshimiwa Rais alipokuja hapa Bunge tumsaidie na sisi Wabunge tuko tayari kumsaidia katika vita vyake vya kifisadi ili kuangalia hizi shilingi bilioni 100 ziko wapi. Kwa sababu bila kuchukua hatua stahiki mchezo huu utaendelea na hali itakuwa kama hivi, kila siku tutagombana, miradi haiendi, pesa haziji baadaye tunaweza kuweka rehani utekelezaji wetu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kuhusu NFRA kupata hasara ya shilingi bilioni 6.7. Hasara hii ni kubwa sana. Nakubaliana na sababu zilizotolewa na Kamati lakini kubwa ni kuchanganya biashara na siasa. Kuna watu wamesimamishwa, lakini binafsi nasema wamesimamishwa kiuonevu kwa sababu sio makosa yao. Ilipitishwa hapa kwamba uwezo wa NFRA kuhifadhi ni tani 140,000 kwa ma-godown yao yote, lakini baada ya NFRA kununua mahindi haya viongozi hawa hawa wa juu na sisi viongozi wa kisiasa kila mtu anataka mahindi yake yanunuliwe katika eneo lake na kutoa maagizo kwa viongozi wa NFRA wanunue bila kuzingatia uwezo wa kuhifadhi waliokuwa nao.
Leo mahindi yameharibika, tunawatoa kama mbuzi wa kafara wakati kimsingi siyo waliosababisha tatizo hili. Kwa sababu wasingetekeleza maagizo ya wakubwa wao waliyokuwa wanaambiwa kwamba lazima mahindi ya wakulima yanunuliwe bado wangetambuliwa tatizo lingekuwa liko pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hili naomba Serikali ifanye uchunguzi hasa na kila mtu apate haki yake stahiki kwa sababu uwezo wa kuhifadhi ni tani 140,000 unamuambia mtu anunue tani zaidi ya 200,000, ataziweka wapi? Lazima aziweke nje na akiziweka nje mvua zikija lazima yaharibike. Sasa yakiharibika unakuja kumuadhibu wakati wewe ndiyo uliyemuelekeza kwamba anunue na hela umempelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nataka tu nilizungumze vizuri sana, Serikali siyo mnunuzi wa mahindi. Tunapowazuia wakulima wasiuze mahindi yao nje wakati tunajua uwezo wa kuzalisha mahindi Tanzania ni zaidi ya tani milioni tatu na uwezo wa Serikali kununua ni mdogo, kwenye bajeti mwaka huu tumetenga kununua tani 100,000, wewe utajihesabu ni mnunuzi? Matokeo yake wakulima wanaacha kuuza mahindi yao sehemu zenye wateja baadaye yanakosa soko, kipato cha wakulima kinaenda chini na kudhoofisha uchumi wa wakulima wetu. Kwa hiyo, naomba sana hata mwaka huu mnapokuja tena kununua hifadhi ya chakula tusije kuwazuia wakulima kuuza mahindi yao kwa wateja wengine kwa kusema Serikali itakuja wakati tunajua uwezo huo wa kununua mahindi yote ya wakulima wetu hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, niungane na maoni ya Kamati yangu hasa kuhusu suala la NSSF kwa sababu huu ni mfuko muhimu sana, ni mfuko wa wapigakura wetu, wastaafu wako huko, ni vizuri Bunge hili likaridhia Kamati hiyo ikaenda kujiridhisha na hali halisi iliyokuwepo huko NSSF. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwa hatua stahiki ilizochukua kukabiliana na matatizo na changamoto zilizokuwepo ndani ya NSSF.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe angalizo sana hasa kwenye ule Mradi wa Dege kwa sababu ile ardhi mpaka leo bado ni ya Azimio kwa mujibu wa title, lakini pia kuna mkataba ambao NSSF umeingia na mbia wake. Kwa hiyo, suala hili siyo la kukurupuka, ni vizuri kujipa muda wa kutosha kuangalia kwa kina na kujiridhisha mikataba inasemaje ili siku za usoni tusije kuingia kwenye matatizo makubwa zaidi ikiwa tutakurupuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wote wanaotuhumiwa bado ni watuhumiwa tu, tusije kuwahukumu kama wakosaji wakati chombo cha kuhukumu ni mahakama. Wote tujipe subira kama Kamati yangu ilivyosema, twende huko tujiridhishe, iletwe taarifa ambayo imekamilika. Kwa sababu jambo hili bado liko kwenye uchunguzi tuviachie vyombo vingine vya uchunguzi viendeee kufanya kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nataka kusema kwamba tumefanya kazi yetu katika mazingira ya kutegemea paper work na maelezo tu kutoka kwa management na Bodi tulizokutana nazo, lakini kiuhalisia PAC tumeshindwa kwenda kutembelea mradi wowote. Kama unavyofahamu siku hizi kuna watumishi hewa, wanafunzi hewa, tunaamini pia kuna miradi hewa. Kwa hiyo, ombi langu kwako kwa sababu tunakwenda kwenye mchakato wa bajeti ni vizuri bajeti ya Bunge ikaongezwa ili na bajeti ya PAC na LAAC zikaongezwa kuziwezesha kutembelea hii miradi tusije kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa sababu tunaweza kusema mradi fulani upo kumbe haupo. Ni vizuri tukatembelea miradi na mashirika hayo kwenda kujiridhisha zaidi. Pia tupate nafasi ya kutembelea hata makampuni au mashirika mengine ya umma yanayofanana na mifuko hii kwenda kujiridhisha kwa sababu mashirika mengi yanafanya mambo kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho niombe Serikali ifuatilie hii mifuko. Kwa mfano, NSSF wenyewe kama tunavyofahamu wana majengo mengi lakini cha ajabu majengo yao hawakai, wenyewe wanapanga, ni kitu cha ajabu kabisa. Wana majengo mazuri kwa nini wasikae kwenye majengo yao kuokoa fedha? Kwa hiyo, niishauri Serikali iwape mwongozo kwa sababu hivi vyombo vinasimamiwa na Benki Kuu na Mdhibiti wa Mifuko wawashauri NSSF na mifuko mingine yote warudi kwenye nyumba zao walizojenga wakae huko kuliko tafsiri ya sasa hivi inavyoonekana kwamba wanalazimika kwenda kupanga kwa sababu labda ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye miradi ya uwekezaji, mifuko mingi kwa ujumla inawekeza….
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango huu katika mada iliyopo mbele yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye asilimia kumi ya vijana na akinamama. Niungane na wajumbe wenzangu waliotangulia, wengi wameshachangia mada hii hasa kutilia msisitizo kwenye hii asilimia tano ya vijana na asilimia tano kwa akinamama. Pamoja na kuchelewa kwa fedha za OC kwenda Halmashauri kwa sababu jambo hili ni la kisheria na jambo hili ambalo kwa sisi ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tuliahidi kwa wananchi.
Naishauri Serikali ni vizuri ikafunguliwa akaunti maalum katika Halmashauri zetu kutenga fedha ili kila mwezi kwenye mapato bila kujali OC imekuja au haikuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kwenye bajeti zetu kule kwenye Halmashauri kama tulivyoona asilimia kumi inakwenda kwa vijana na akina mama, asilimia hamsini kwenye miradi ya maendeleo na asilimia arobaini kwenye matumizi ya ndani. Sasa mara nyingi wakati mwingine bajeti zinawekwa kubwa kwa ajili ya kupata hiyo asilimia 40 ya OC na matokeo yake kila hela inayokusanywa kwa kisingizio kwamba OC haijaja hela yote inatumika katika matumizi ya kawaida na matokeo yake hakuna mradi wowote wa maendeleo unakuwa umetekelezwa kwa kutumia fedha za ndani wala kwenda kwenye hii asilimia kumi kwa vijana na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri kwamba kila mwezi kila fungu ambalo tulilolipangia kwenye mipango yetu katika Halmashauri likawekwa kwenye akaunti yake ili kama OC haijaja basi athari iwe kwenye OC, katika ile miradi ya maendeleo iendelee ili tukifika mwisho tunajua OC tumekwama wapi ili wajibane wapi na ile miradi yetu ya maendeleo asilimia ile hamsini iliyotengwa hata kama tusipoimaliza yote lakini angalau kwamba kwingine tutakuwa tunaipunguza, la sivyo itakuwa kila kitu inaishia kwenye OC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye suala la semina kwa viongozi. Ndugu zangu kama tulivyoona asilimia arobaini ya bajeti ya Serikali inakwenda kwenye miradi ya maendeleo. Hiyo miradi ya maendeleo inakwenda kule chini na watekelezaji na wasimamizi wakubwa ni Madiwani, lakini mpaka tunavyosema hivi hao wasimamizi wa miradi mikubwa na kutazama value of money kule chini hawana semina yoyote. Maana yake ni nini? Hawajui wanachoweza kukisimamia, kipi ni kipi. Ni vizuri pamoja na kujibana tukawapa mafunzo hawa Madiwani ili wawe na uelewa mpana wa kusimamia kile wanachopaswa kusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; pia hata wale Viongozi wetu kule wa Serikali za Vijiji, kwa sababu kule hela zote hizi zinakwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji na Afisa Mtendaji. Afisa Mtendaji ni mwajiriwa wa Serikali ana mshahara, lakini huyu signatory ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji hana posho wala mshahara na ukizingatia ile asilimia ishirini haiendi huko. Kwa hiyo, anasimamia kitu ambacho yeye hafaidiki na chochote, sasa matokeo yake hata kudanganywa na Watendaji ili miradi hii isitekelezwe kwa kiwango kilichokubaliwa inakuwa ni rahisi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yangu tukaangalia ni namna gani tunaweza kuwalipa chochote hawa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa au posho ili waweze kusimamia miradi yetu kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye utawala bora; suala hili la utawala bora hasa katika ngazi za Mikoa na Wilaya. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uteuzi mzuri alioufanya kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini pamoja na uteuzi huo bado hawa watu wanahitaji semina elekezi. Nasema hivyo kwa sababu kuna mambo mengi yanatokea hasa kwenye mgongano wa kimadaraka kule katika Halmashauri zetu.
Nitoe mfano tu kwenye Halmashauri yetu, unakuta Baraza la Madiwani wakati mwingine limeamua kwa mujibu wa kanuni na sheria lakini anaweza kuja Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa akasitisha yale maamuzi ya Baraza la Madiwani yasifanyike na matokeo yake Mkurugenzi anakuwa katika wakati mgumu amsikilize nani, alisikilize Baraza la Madiwani au amsilikize Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tuna ushahidi dhahiri upo umetokea kwenye Halmashauri zangu na matokeo yake Mkurugenzi huko analaumiwa na huku analaumiwa. Wakati mwingine tunawalaumu Wakurugenzi siyo maamuzi yao lakini kwenye kutumikia mabwana wawili na wakati mwingine majukumu yao hawayajui na mipaka ya kazi zao hawaijui, wanakuwa wanayumba yumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja tu ambao ulifanyika ndani ya Baraza la Madiwani; tumefanya maamuzi sahihi ya kuhamisha Halmashauri yetu kutoka Morogoro Mjini kwenye vijijini kwamba kikwazo kilikuwa pesa, tumepata pesa baada ya kushauriana na Wizara ya TAMISEMI yenyewe kwa msaada mkubwa ambao ametupa Mheshimiwa Waziri Simbachawene na timu yake, yule mdaiwa sugu matokeo yake akatulipa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, jali muda wangu maana muda wenyewe mchache, siku yenyewe moja tunaijadili hii.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa hiyo, kwanza nampongeza Mheshimiwa Simbachawene kwa ushirikiano mkubwa sana alioipa Halmashauri ya Morogoro mpaka huyu mdaiwa sugu akatulipa hela zetu, tukapanga muda ndani ya mwezi mmoja tuhamie Makao Makuu kwenda Mvuha, kutoka Mjini kwenda Vijijini, lakini kabla ya maamuzi yale hayajafanyika, anajiandaa Mkurugenzi na timu yake anakuja Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa kupitia RAS anawabeba Wakuu wa Idara kawapeleka Mvuha kawabwaga pale anasema anayetaka kazi ndiyo hapa nimemfikisha, asiyetaka hamna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile halina choo, halina ofisi wala kitu chochote, lakini kwa kukubali kwamba ni mkubwa amesema hawa watu wakakaa kule, matokeo yake nini? Huo ni mfano mmoja mdogo sana. Sasa ni vizuri hawa watu wakapewa semina elekezi ili kila mmoja ajue madaraka yake na kila mtu ajue mipaka yake. Kwa sababu hawa wananchi Baraza la Madiwani ndiyo tunatakiwa tutetee maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu watumishi kutokujiamini katika kutoa maamuzi, huu ni mfano hai upo ndani ya Halmashauri ya Morogoro, tuna tatizo kubwa sana kule la wakulima na wafugaji, lakini ni kosa kwa kiongozi wa kuchaguliwa, uwe Mbunge au Diwani kusema kuna tatizo la wakulima na wafugaji. Umetokea mfano Diwani mmoja wa Kolelo amewekwa ndani mara mbili na vyombo vyenye mamlaka kwa kusema kwenye Kata yake kuna tatizo la wakulima na wafugaji, anaonekana ni mchochezi, sisi Wabunge ndiyo tulienda kumtoa zaidi ya mara mbili. Tunasema haya ni nini? Lakini Mungu siyo Athuman baadae yakaja kutokea mapigano makubwa sehemu ile ile viongozi waliyokuwa wanakataa kwamba hakuna mapigano ya wakulima na wafugaji; hakuna tatizo la wafugaji kuvamia kwenye mashamba ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi ni kwa nini? Kwa sababu hawa viongozi wetu walishapewa miongozo kwamba sehemu yoyote kwenye tatizo la wakulima na wafugaji likitokea basi Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa hana kazi. Sasa wakati mwingine wanatumia kuficha maovu kwa kuogopa wao kuja kuchukuliwa hatua. Niombe sana tuwape moyo hawa viongozi, ni bora waseme ukweli ili tutatue tatizo kuliko kuficha baadaye mambo yanakuja kuharibika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TASAF; kwanza niipongeze sana Serikali kwa mradi huu wa TASAF umesaidia sana kaya maskini, lakini naomba sana elimu iongezwe hasa kule vijijini hakuna elimu, wananchi hawajapata elimu sawasawa, kwa sababu wanaamini hasa wazee kwamba huu ni mradi wa kusaidia wazee, hawajui kwamba ni mradi wa kusaidia kaya maskini. Sasa ni lazima iongezwe ijulikane kuna tofauti ya kusaidia wazee na kusaidia kaya maskini. Mara nyingine unaona kuna mgogoro wanakwambia kijana ana nguvu zake lakini yupo kwenye mradi wa TASAF, kumbe ni kijana lakini hana uwezo kiuchumi. Kwa hiyo, ni vizuri elimu ikaongezeka kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niongelee sasa kwenye Kamati ya Katiba na Sheria kuhusu suala la NSSF. Niungane na maoni ya Kamati kwa sababu ya utawala bora na kwa sababu tuna mihimili mitatu, Bunge, Mahakama na Serikali na Serikali imeshaanza kuchukua hatua katika wale watuhumiwa ipo kwenye vyombo vya uchunguzi, ni vizuri sana tukaipa nafasi Serikali ikamaliza uchunguzi wake, lakini naomba kuishauri baada ya uchunguzi huo walete taarifa hapa Bungeni ili ukweli ubainike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ya Kamati ya Bajeti. Kwanza niunge mkono hoja ya Kamati ya Bajeti kwa sababu mambo mengi, changamoto ambazo zinaikabili nchi yetu kama Taifa, mengi Kamati imezingatia, kwa hiyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa makusanyo makubwa ya mapato na kubana matumizi kulingana na mapato hayo halisi bila kutegemea misaada mingine. Baada ya pongezi hizo niwe na ushauri mdogo, kwa sababu tumeona pamoja na makusanyo makubwa ya mapato hayo item mbili ndio zinakula; mishahara pamoja na madeni. Kwa bahati mbaya sana madeni mengi ambayo yanalipwa kwenye kandarasi kubwakubwa na nyingi hizi zinatoka nje, maana yake ni nini? Serikali inatumia hizo bilioni zaidi ya 900 kwa mwezi lakini hela zile baadaye zinahama kutoka nchini zinakwenda nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba ushauri katika hili, Serikali sasa ni vizuri ili kusisimua uchumi ndani ya nchi nao kuwalipa wawekezaji wa ndani ili kwanza waweze kusisimua uchumi, wakiendelea kufanya biashara wataendelea kutoa ajira kwa wananchi wetu lakini pia mzunguko wa pesa utakuwepo ndani ya nchi lakini kuendelea kuwalipa na yale madeni ya nje tu maana yake zile hela zinakwenda kuimarisha mzunguko kwenye nchi za wenzetu. Tunajua dawa ya deni ni kulipa lakini tuwe na balance ya sehemu zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunasema tuna uchumi wa viwanda, ni kweli kabisa tuna uchumi wa viwanda lakini pamoja na uchumi huu wa viwanda Serikali peke yake lazima inaitegemea sana sekta binafsi. Sekta binafsi hizi zingine ziko ndani ya nchi, kwa hiyo tunapowalipa wadeni wa ndani tutakuwa tunawarahisishia kushiriki kwenye uwekezaji wa ndani ya nchi kwenye uchumi wa viwanda. Kwa mfano tu, Serikali leo ikiweza kulipa mifuko ya jamii ambayo wanaidai Serikali mifuko hii itakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda na sekta nyingine hapa nchini na kutoa ajira na kuimarisha uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye suala la kilimo; kama ukurasa wa 42 unavyosema kilimo ndio uti wa mgongo, kinaajiri zaidi ya asilimia 70, lakini kwa bahati mbaya sana kilimo hicho hicho ukuaji wake kila mwaka unakwenda chini, sasa hivi tunaambiwa ni asilimia tatu ambayo hata yale makubaliano tu ya Maputo kule tunatakiwa angalau tuchangie asilimia 10, lakini kwa mwendo huu inaonekana bado tuna safari ndefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye hili, kwa sababu huwezi kutatua matatizo ya kilimo au kilimo kipande bila kutatua matatizo yanayokabili Sekta yenyewe ya Kilimo, wenzangu wamezungumza mengi lakini lazima Serikali ije na mkakati mzito kwenye kutatua hili tatizo la mipango bora ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa kama zamani wakati wa Mwalimu Julius, ilikuwa inajulikana kabisa mikoa gani ya wafugaji na mikoa gani ya kilimo, kwa sababu hata tunapozungumza matumizi bora ya ardhi maana yake ni kwamba tukatenge ardhi zetu wapi panafaa kwa kilimo, wafugaji wakae wapi, makazi yake wapi. Sasa mpango huohuo uanzie ngazi ya Kitaifa kwanza kwa sababu haiwezekani ukawaweka pamoja wafugaji na wakulima, haiwezekani kukaa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tujue kabisa mikoa gani itatupa tija kwa ajili ya mifugo na mikoa gani itatupa tija kwa ajili ya kilimo. Nitoe mfano, Mkoa wangu wa Morogoro, tumeambiwa Ghala la Taifa, Ghala la Taifa maana yake ninyi mko zaidi kwenye mambo ya kilimo lakini hali inayoendelea kule kama hii mipango bora hatutaizingatia kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya itakuwa ni hadithi. Kwa hiyo, niombe tu hii mipango bora ya ardhi ianze kuanzia ngazi ya Taifa, itangaze kabisa mikoa gani mahsusi kwa ajili ya kilimo na mikoa gani mahsusi kwa ajili ya mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo katika kilimo, leo kilimo hakivutii wakulima wapya, hakivutii mtu kwenda kuwekeza kwenye kilimo sababu kilimo chetu bado kinategemea mvua, huna uhakika wa kuvuna. Ndiyo maana leo bajeti ya kilimo kwenye mbolea kila mwaka inaongezeka lakini tija inapungua. Kwa nini? Mtu anaweza akapata mbolea, anaweza kupata trekta anaweza kupata mtaji lakini kama hana maji hayo yote ni bure, kama tunavyoona mwaka huu mvua haijanyesha, watu wamewekeza lakini watapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mfano mzuri ndiyo maana unaona hata Benki ya Kilimo yenyewe ina hela zaidi ya bilioni 59 lakini imekopesha bilioni tatu tu kwa sababu anaona kwamba hata akikopesha uhakika wa kulipa hamna. Ushauri wangu katika hili ni vizuri sasa Serikali tujielekeze zaidi katika mipango yetu kuwekeza kwenye maji, hasa kwenye mabwawa. Kwa hiyo, naungana na maoni ya Kamati kuongeza ile shilingi 50 kila lita ili iwe 100 ili Wizara hii iwe na Mfuko wa kutosha wa maji twende kutatua changamoto za maji na kukabiliana na hali halisi inayolikabili Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi tuna ukame, mara nyingi tunakuja na mipango ya kukabiliana na matokeo hatukabiliani na chanzo kilichosababisha ni nini. Sasa hivi tuna tatizo hili la ukame sasa tukawekeze kwenye masuala ya mabwawa ya umwagiliaji ili kilimo chetu kiwe cha uhakika, mtu yeyote akienda kuwekeza kwenye kilimo awe na uhakika wa kuvuna kwa sababu maji ya kumwagilia yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi hata hizi benki za biashara tutakuwa tumetatua suala la mitaji kwa wakulima kwa sababu watawakopesha kwa sababu wanawafahamu kwamba wana uhakika wa kulipa kwa sababu wana uhakika wa kuvuna katika uwekezaji huo wa kilimo. Hata tukiongeza mbolea, hata tukiongeza madawa kama uhakika wa maji hamna, kama kilimo cha umwagiliaji hamna, hamna benki yoyote – iwe ya kilimo au iwe ya kibiashara ambayo inaweza kuwekeza kwenye suala la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuhusu kukopa zaidi ndani, ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi, kuna mmoja alikuwa anazungumza anasema kwa nini sasa hivi hatukopesheki huko nje, kuna sababu gani. Sababu ziko wazi tu, sababu ni kwamba sasa hivi demand imekuwa kubwa kuliko supply, hata hao wakopaji uwezo wao sasa hivi nao ni mdogo. Mfano mdogo tu tunauona sasa hivi hata Marekani wenyewe huyu Rais mpya aliyeingia anasisitiza viwanda vyao wawekezaji warudi kuwekeza ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limeishtua kidogo hata China. China wanasema sasa wanataka kubadilisha badala ya kwenda kuwekeza zaidi nje ya nchi wanaona ni bora kufanya innovation kwenye teknolojia yao ili kupunguza gharama za uzalishaji ili waendelee kuzalisha ndani ya nchi zao, maana yake wa-reduce production cost ili waendelee kulinda ajira yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni signal sio nzuri kwetu tunaposema kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda maana yake support kutoka kwa Mataifa makubwa itakuwa ni ndogo kwa sababu haya sasa na wao sasa hivi wataangalia zaidi Mataifa yao kuliko kuja kuwekeza kwetu kwa sababu wanaona kwamba kuja kuwekeza huku kama wanahamisha ajira za watu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii kama Serikali tuichukue na twende kwa tahadhari. Ni vizuri katika hili tukajielekeza zaidi katika yale mambo ambayo tuna uwezo nayo na tuko wazuri katika uzalishaji zaidi kuliko haya ya kutegemea wawekezaji kutoka nje. Hawatapenda kwamba tuendelee kama wao halafu tuje tuendelee kugombania soko lilelile, wao wanapenda waendelee kututumia sisi kama soko badala ya kuwa partner wazalishaji wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, katika suala la hizi milioni 50, ni vizuri kwamba Serikali ikaleta haraka sana, ndani ya bajeti hii kabla haijaisha ni vizuri hizi hela zikafika huko vijijini ili ziweze kwenda kusisimua hali ya uchumi na kuongeza mzunguko wa uchumi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni vizuri Serikali tukawa na vipaumbele vichache ambavyo vinalingana na uwezo wetu badala ya kuwa na vipaumbele vingi ambavyo tunaviandika tu, wakati mwingine utekelezaji wake unakuwa hafifu. Ni vizuri tukavichagua vichache tukavitekeleza na kutokana na hali hali sasa hivi – kama alivyosema mwenyewe Waziri wa Fedha – upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu nje imekuwa ni michache sana, mikopo inayopatikana sasa hivi ni ya kibiashara. Kama mikopo inapatikana nje ya kibiashara maana yake itakuwa na masharti magumu na matokeo yake hata tukikopa zaidi itakuwa na riba kubwa na itakuwa ni mzigo mkubwa sana kwa Taifa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kamati, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa dakika tano na mimi nichangie hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye ukurasa wa 24 wa kitabu cha Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji hasa kwenye miradi mikubwa ya mabwawa nchini ambayo haijatekelezwa kwa muda mrefu. Kama kuna mradi ambao haujatekelezwa muda mrefu kuliko yote hapa nchini basi ni mradi wa Bwawa la Kidunda. Huu mradi wa Bwawa la Kidunda kabla ya uhuru mwaka 1955 ndiyo wazo hili lilianza na andiko lake la kwanza usanifu ulifanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uhuru chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1962 akaubeba mradi huu akasema huu ndio ukombozi wa uchumi imara kwa sababu nchi yetu inategemea uchumi wake kwa kiasi kikubwa kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua Bwawa hili la Kidunda lilikuwa ndio liwe mkombozi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji lakini kwa ajili ya maji ya uhakika kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, ujazo wa wakati ule ulikuwa ukubwa wake zaidi ya cubic meter milioni 450, Serikali zote zilizokuja ziliendelea kuubeba mradi huu lakini haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu kuanzia mwaka 1994 pamoja na mahitaji ya maji kuendelea kuongezeka mradi huu ulibadilishwa matumizi kutoka katika multiple use maana ya kwamba mahitaji ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji yakawekwa tu kwa ajili ya single use yaani matumizi ya binadamu na kupunguza ukubwa wa bwawa kutoka cubic meter milioni 450 mpaka 190, kwa kusikiliza tu wadau wa maendeleo wasiotutakia mema kwa ajili ya maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua wakati mwingine wadau wa maendeleo wakitaka kukuzuia wanaweza kukusingizia tu wakakwambia bwana hapo Selous hapo kuna nyoka hayupo ulimwengu mzima yupo hapo tu, mkilijenga hilo bwawa huyo nyoka atakuwa amepotea, na sisi tumekubali hiyo akili tukapunguza bwawa kutoka cubic meter milioni 450 mpaka 190. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nchi ulimwenguni sasa hivi inatanguliza maslahi ya wananchi wake zaidi kuliko ya mtu yeyote. Wamarekani wanasema Marekani kwanza, Waingereza wanasema Uingereza kwanza na Wachina wanasema China kwanza ni lazima tufanye maamuzi magumu katika hili ili tukubaliane na changamoto zinazotukabili nchini kwetu hasa ya ukame. Lazima turudi kwenye usanifu wa awali wa ule ujazo wa 450 milioni badala ya huu wa 190 tu kwa ajili ya matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tuende na andiko lile la asili ambalo liliandikwa tangu mwaka 1955 wakati ule hata mahitaji ya maji yalikuwa machache sana kuliko sasa hivi mahitaji ya maji ni makubwa zaidi, hata Mto Ruvu unaanza kupungua maji hususan wakati wa kiangazi. Kwa hiyo, hili Bwawa la Kidunda utekelezaji wake ndiyo utakuwa ni uokozi kwa ajili ya uchumi wetu kama tunavyojua Dar es Salaam tunaitegemea zaidi ya asilimia 75 kwa uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili kwa Serikali ni kwa sababu miaka yote 62 mradi huu haujatekelezwa shida kubwa ni fedha. Leo hii kule Mkulazi ndiyo kinajengwa kiwanda kikubwa kuliko chote cha sukari kupitia kampuni ya Mkulazi Holding, lakini kwa tatizo la maji huu mradi hautatekelezeka. Bwawa hili ni lazima lijengwe ndiyo huu mradi wa Mkulazi nao u-take-off.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata fursa ya kuchangia Kamati hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uzima hata tumekutana jioni hii ya leo. Lakini pili, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa sera yake ya viwanda na kwa kuanza kwa vitendo, natoa mfano kwenye jimbo langu. Mwaka wa jana wakati nakuja hapa watu wengi majirani zangu hapa walikuwa wananiambia kwamba Mgumba Mkulazi, lakini kilio kile kimemfikia Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka mazingira mazuri na tumepata mwekezaji, Mkulazi Holding Company Limited, kampuni tanzu ya Mifuko ya Jamii ya NSSF na PPF inawekeza kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa sukari katika Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki, chenye uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka na kuondoa adha ya sukari hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kwenda kwa vitendo utekelezaji wa sera ya viwanda. Haya sio maneno, kama mtu anabisha aje kule Mkulazi anaona ujenzi unavyoanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo sasa niende moja kwa moja kwenye ushauri. La kwanza, naomba kuishauri Serikali hasa kwenye suala hili la TFA (Shirika la Mbolea) na kama walivyosema Kamati, suala kubwa hili shirika ni muhimu sana hasa kwenye sekta ya kilimo. Hili shirika ndio tunalitegemea kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwenye zana za kilimo, lakini kama Serikali haiwezi kulilea vizuri lazima madeni haya yataendelea kuongezeka na shirika hili litakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Serikali, leo hii kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati, shirika hili lilianza na mtaji wa shilingi bilioni 17.9 leo wana mtaji wa negative billion 12.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini na sababu ni nini? Ni kwa sababu, mara nyingi Serikali, hasa kwenye taasisi zake hasa inapopata huduma kwenye ulipaji au fidia ya ile ruzuku ambayo inaagiza taasisi zake itumie inachelewa kwa muda mrefu sana, athari yake inakuwa kubwa na matokeo yake haya mashirika yanapoteza uaminifu kwa wadau na taasisi nyingine za fedha, hata kwa wasambazaji wengine wa mbolea kule wanakochukulia mbolea hizi na matokeo yake wanashindwa kukopesheka, athari kubwa inaenda kwa wakulima wetu kutokupata mbolea kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali inapohitaji huduma kwenye shirika lake, kwa mfano kama hapa, shirika hili linaweza kwenda kununua mfuko labda wa mbolea shilingi 50,000 lakini Serikali kwa ajili ya kurahisisha ipatikane kwa bei nafuu, ikaiambia TFC uzeni shilingi 30,000 nyingine ni ruzuku. Sasa ile ruzuku ambayo Serikali ina top up ni vizuri ikaipeleka kwa wakati ili kufidia shirika liweze kujiendesha kibiashara na ziweze kulipa madeni yake kule ambako inakopa. Badala ya kutoa miongozo kwamba toeni ruzuku, shirika linatoa ruzuku, lakini hela haziendi kwa wakati, ndio matatizo haya ya negative ya mtaji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili niishauri Serikali kuhusu kwenye Bodi za Mazao. Bodi za Mazao zimekuwa nyingi na mara nyingi tunavyoziona nyingine hazipo kwa ajili ya manufaa ya kilimo chetu wala kwa wakulima wa Tanzania. Sasa ushauri wangu kwa Serikali, ni vizuri tukaunda bodi mbili tu, moja ikawa kwa ajili ya mazao ya biashara ambayo itasimamia mazao yote ya biashara yale makubwa yaliyokuwa na bodi kwa sasa; kwa mfano labda ile Bodi ya Korosho, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pareto, Bodi ya Pamba, zote zikaunganishwa zikawa bodi moja na bodi ya pili ikawa Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Hizi zikiwa mbili itakuwa ni rahisi, moja inashughulikia mazao mchanganyiko nyingine mazao ya biashara, kwa kufanya hivyo hata menejimenti yake inakuwa ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu Mifuko ya Jamii. Katika hili nakubaliana na mapendekezo ya Kamati, wanapozungumza kwamba Msajili wa Hazina (TR) anatakiwa atambulike kisheria kwenye mifuko hii. Nilikuwa naomba tu Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuja kufunga hoja yake; bado mimi sijaelewa vizuri. Kwa uelewa wangu mdogo najua hii Mifuko ya Jamii ni mali ya wanachama. Sasa kama mali ni ya wanachama Serikali ipo kama mdhamini lakini si moja kwa moja kama ilivyo kwenye yale mashirika ya Serikali kwa mfano kama TTCL na mashirika kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia mali ya wanachama labda TR aingie moja kwa moja kule kama msimamizi mali ya Serikali wakati ile si mali ya Serikali moja kwa moja ni mali ya wanachama, naomba ufafanuzi katika hili ili tuweze kupata uelewa wa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa katika kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha na uwekezeji, lakini pamoja na nia nzuri ya kupunguza matumizi, bado utaalam na ubora unatakiwa uzingatiwe, sasa kumezuka tabia moja hasa kwenye mashirika haya ya Serikali, iwe NHC au TBA utakuta mwenyewe ndiye mkandarasi, wakati huo huo ni mshauri mwelekezi wa mradi na pia ndiye msimamizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali hii haipo kisheria, kwasababu pamoja na yote kuna mambo ya Kisheria. Lazima iwe kwamba engineer awe mwingine, msimamizi awe mwingine, ili kuonesha kama kazi inayotekelezwa inakidhi ubora unaotakiwa. Tukiachia hali hii iendelee, pamoja na nia nzuri ya kupunguza matumizi, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuja kupata miradi ambayo inakuwa chini ya kiwango, baadaye hata tija au value for money ikakosa kuonekena huko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. OMARY T. MGUMBA: Nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika hoja iliyo mbele yetu.
La kwanza niipongeze Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuleta sheria hii katika Bunge lako, ili tuweze kuifanyia mabadiliko. Sheria hii ni muhimu sana tena imechelewa sana kuleta, kwa sababu ni sheria kandamizi ambayo ilikuwa inasababisha mzigo mkubwa kwa wananchi, Serikali kutumia fedha nyingi kuliko gharama halisi ya bidhaa ambazo zilikuwa zinatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Sheria hii ilikuwa inachelewesha maendeleo, hasa Serikali kuwahudumia wananchi wake kutokana na mchakato mrefu ambao ulikuwa unafanyika kupitia sheria hii; ambao zaidi siku 90 kwa maana ya zaidi ya miezi mitatu, kitu ambacho kilikuwa kina sababisha kuchelewa kupata huduma kwa wananchi wetu.
Baada ya utangulizi huo naomba kushauri vitu vichache kama ulivyosema nitumie muda vizuri kwa sababu muda siyo rafiki; nitaenda kwa haraka haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza kama sheria yenyewe inavyotaka lengo kubwa ni kwenda hasa kuzingatia value of money, ni kwa sababu ya kupata thamani halisi ya pesa ambazo zitatumika. Kwamba kama tukanunue bidhaa kutokana na bei ya soko ni kweli kabisa, lakini ni jambo zuri, ningeishauri Serikali sasa ijipange kuwa na fedha taslimu katika akaunti zake ili mtoa huduma huyu anapotoa huduma apate malipo yake kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hutoweza kupata bei ya soko kama mtu utamlipa ndani ya miezi mitatu, miezi sita au mwaka mmoja wakati mwingine mpaka miaka miwili inachukua mtu hajalipwa, halafu unategemea upate huduma ya soko, matokeo yake tutaweka sheria lakini sheria ambayo itakuwa haitekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ninao mfano hai kabisa ambao umetokea kwenye Mawakala wa Mbolea kwa mfano, Mawakala wa Mbolea wametoa huduma kwenye Serikali lakini leo wengine wana zaidi ya mwaka hawajalipwa na hivi vimesababisha matatizo makubwa sana kwa ucheleweshaji wa pembejeo kwa wakulima wetu. Kwa sababu hawa mawakala wamekosa sifa za kukopesheka katika mabenki, lakini pia wamekosa sifa za kukopesheka kwa wasambazaji wakubwa kupewa zile mbolea kuzipeleka kuzisambaza kwa wakulima wadogo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali kwa jambo hili limekuja zuri na tumaimani kabisa litapunguza gharama za bidhaa na litaleta unafuu mkubwa kwa wananchi wetu, lakini sasa kwa imani tuliyokuwa nayo ya Serikali ya Awamu ya Tano ukusanyaji huu wa mapato nayo ijipange hivyo hivyo kurahisisha ulipaji wa fedha kwa watoa huduma ili waweze kutoa huduma kwa wakati na haya malalamiko kwa wananchi na sisi wenyewe yaweze kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ambalo ushauri mwingine katika hili suala la mchakato wenyewe wazabuni ni hapa, kwa sababu ndio miongoni mwa matatizo makubwa kuna rushwa kubwa sana inafanyika katika mchakato huu wa manunuzi. Kwa sababu mchakato mrefu unahusisha watu wengi na lazima wale wanaosimama kwenye kutoa haki wanataka cha juu sasa watoa huduma wengi wanapigia hizo gharama zote kwenye bei ya bidhaa na bei hizi zote zinakuja kumlalia mlaji kule mwisho.
Kwa hiyo, ninaomba Serikali katika suala hili tuongeze uwazi ili bei ijulikane gharama halisi za bidhaa husika na ijulikane ni kipindi gani muhudumu akitoa huduma atalipwa na Serikali ili ikitokea serikali iki-default kumlipa yule basi kiwepo kipengele kabisa Serikali ibebe riba ya kulipa kwa kipindi chote ambacho itakaa na hizo hela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pamoja na kulipa hiyo riba ilipe fidia kwa mfanyabiashara yule ambaye katoa huduma na Serikali imechelewesha malipo, kwa sababu kwa kukaa na pesa ya mtoa huduma kwa kipindi kirefu unamsababishia yeye a-block yaani hafanyi biashara yoyote, hafanyi shughuli nyingine yoyote ya kiuchumi kwa ajili ya kujiongezea kipato, pesa zake unazo wewe kwa maana nyingine umesimamisha kila kitu yeye kwenda mbele kwaajili ya maendeleo. (Makofi)
Sasa sio kulipa riba tu lakini ni kumfidia ni faida gani angeipata kwa pesa ile kwa wewe kuwa nayo kwa kipindi kile lazima katika hili tuwe msumeno tusiwe visu tukate huku na huku. Kwa sababu mara nyingi watoa huduma waki-default kutoa huduma tuna-cancel mikataba yao na tunawafutia, lakini Serikali inapochelewesha kumlipa hata miaka mitatu anakuja kulipwa kiasi kile kile ambacho amechukua miaka mitatu iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunazungumza value of money tuzungumze value of money pande zote mbili hata kwa kuchelewesha pesa ile kwa muda mrefu Serikali inapaswa ibebe majukumu hayo ya kumlipa riba zake na pia faida aliyotaka kutarajia kuitengeneza ndani ya kipindi chote ambacho Serikali imeshikilia hela hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache nashukuru sana niwaachie wengine nao watoe mchango wao, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye muswada uliokuwa mbele yetu.
Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai na uzima wa siku ya leo. Pia na mimi naungana na Wajumbe wenzangu wengi ambao michango mizuri iliyotolewa, kwanza nianze kwa kuunga mkono hii hoja kwa asilimia mia moja kwa sababu ni muswada ambao ni mzuri na umekuja wakati muafaka ambao utatua changamoto kubwa zilizokuwepo kwa Wathamini ambao walikuwa baadhi yao wengine ni wadanganyifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nasema ni muswada mzuri kwa sababu mpaka taasisi kwa mfano kama za kifedha zilikuwa zinakosa hata uaminifu kwa baadhi ya wathamini wengine na ndiyo maana walikuwa wanachagua hata Wathamini maalum wa kufanya kazi zao. Sasa hii ilikuwa inakosesha fursa kubwa sana kwa wananchi wetu kupata kile walichokuwa wanatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, wenzangu wameshachangia mengi lakini naomba tu kwenye kile kifungu cha 52(2) na tumeona hapa kwenye amendment ametuletea Mheshimiwa Waziri leo; kama tunavyojua tarehe ya uthamini ni siku ile ya uthamini na ardhi mara nyingi huwa inapanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu valuer, ule muda ambao valuation inakua kwa miaka miwili tunakubaliana ni sawa, lakini sasa inaanza kutumika mpaka pale valuer anapotia saini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba katika kipengele hiki tu hata huyu Valuer Mkuu baada ya kuthibitishwa ile, uwekwe muda maalum kuliko kuacha hivi hivi tu. Ni vizuri kupendekeza iwekwe kama miezi sita hivi, kwa sababu tukiacha hivi hivi kuna athari, wakati mwingine valuation inaweza ikafanyikakwa nia njema kabisa ikafika kwake na wakati huo labda hana uwezo au hana fedha ya kulipa akauchelewesha kwa makusudi hata miaka mitatu, minne, mitano, matokeo yake itamwathiri yule mwananchi au yule ambaye ni mnufaika wa valuation ile, kwa sababu anakuja kulipwa wakati ile value ya land au the property imeshapita muda wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri hata huyu valuer akawekewa muda maalum aseme kwamba, yaani ikifika mezani kwake ile document basi izungumze kabisa ndani ya miezi sita anatakiwa asaini, ili tusije kuondoa maana nzima ya ile evaluation report ambayo ilikuwepo mbele yetu. Nisema tu, ilikuwa mchango wangu leo ni huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi.