Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Suleiman Ahmed Saddiq (1 total)

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakushukuru sana kwa majibu hayo. Kwa kuwa viwanda vya ndani vimejipanga, na kiwanda cha sukari Mtibwa ambacho kiko katika Jimbo la Mvomero na Wilaya ya Mvomero kimejipanga vizuri sana. Je, Serikali iko tayari kuvisaidia sasa viwanda hivi vya ndani ili viweze kukamilisha lengo la Taifa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saddiq kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, wakati wote tumekuwa tukiendesha mazungumzo kati ya viwanda vyote vya ndani ikiwemo vya sukari, namna bora ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa zao na bidhaa zenye ubora kwa namna ambayo Serikali inaweza na utayari wake iliyonao, kuvisaidia viwanda hivi kuweza kuzalisha zaidi. Kama ambavyo nimesema kwenye jibu la msingi, Serikali imekaa mara nyingi na wazalishaji wa sukari, kuona mwenendo wa uendeshaji wa viwanda vyao na uzalishaji wake, kupata changamoto zinazowakabili kwenye uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imedhamiria kulinda viwanda vya ndani na kusaidia uzalishaji mpana, tunao mpango na tumeandaa pia njia nzuri ya viwanda hivi kupata msaada wa kuendelea kuzalisha ikiwemo kupata mitaji, kupitia mabenki tuliyonayo na pia kuhamasisha wakulima wanaolima jirani ili waweze kuzalisha mazao yanayofanana na yale ili kuongeza uzalishaji. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuwa pamoja na wazalishaji ili kuweza kuzalisha zaidi zao la sukari.