Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suleiman Ahmed Saddiq (18 total)

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, barabara ya Sumbawanga, Mpanda inafanana na barabara ya Magole, Mvomero - Turiani ambayo nayo ipo katika mapango wa Serikali wa kuweka lami na kwa kuwa kilomita nane za mwanzo zilishawekwa lami baada ya kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa Mbunge nimefuatilia na nimeambiwa fedha za kumalizia mradi huo zinatafutwa na kwa kuwa kipindi hiki mvua kubwa zimenyesha barabara hiyo imeharibika.


Je, Serikali ipo tayari kufanya kazi ya dharura, huku tukisubiri fedha za lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara nyingi hapa nchini sasa zimeharibika kutokana na hali ya mvua inayoendelea kunyesha. Lakini TANROADS imetenga pesa maalum kwa ajili ya kufanya ukarabati kwenye barabara zote ambazo zimeharibika ili tuhakikishe wananchi wanaweza kupata mawasiliano kama kawaida.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Wilaya ya Mvomero ipo miradi ya maji iliyo chini ya Wizara katika maeneo ya Tarafa za Mgeta, Mlali, Turiani na Mvomero na kwa kuwa miradi hiyo imeanza, lakini bado haijakamilika na kwa kuwa Serikali imeshatumia mamilioni ya fedha. Je, Serikali sasa iko tayari kuleta fedha zilizobaki ili miradi ikamilike katika maeneo hayo na wananchi wapate maji safi na salama Wilayani Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, jana kwenye jibu la msingi la matatizo ya maji nilieleza katika awamu ya kwanza ya programu ya maji iliyoanza mwaka 2007 na imeishia mwaka 2012 tulikuwa na miradi 1,855.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi iliyokamilika ni miradi 1,143 na miradi inayoendelea ni miradi 454 ambapo katika hii miradi inayoendelea ipo miradi katika Jimbo la Mheshimiwa Saddiq, sasa hivi mwezi Januari tunaanza progamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kwa hiyo, katika mpango huu nimhakikishie Mheshimiwa Saddiq kwamba fedha itatolewa kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; kwa kuwa tatizo la Kahama la mawasiliano ya simu linafanana na tatizo la Mvomero na kwa kuwa tumepeleka maombi kwa kampuni mbalimbali za simu, na kampuni hizo zimeahidi kujenga minara katika Kata ya Luale, Kikeo, Kinda, Pemba na Kibati. Kwa kuwa minara hiyo hadi leo bado haijajengwa, je, Serikali iko tayari kupeleka ruzuku ya Mfuko wa Mawasiliano katika Kata hizo ili wananchi wa Mvomero sasa wapate mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari kupeleka ruzuku lakini tatizo kubwa sio ruzuku, tatizo kubwa tunatoa ruzuku, lakini makampuni yenyewe hayako tayari. Kwa mtazamo huo, kama nilivyosema kwamba Serikali iliingia na mkataba na kampuni ya Halotel au Viettel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwenye maeneo hayo. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, eneo lake litakuwepo kwenye mpango wa kupelekwa mawasiliano mwaka huu.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa katika Halmashauri zetu, hususani Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kumekuwepo na tatizo kubwa sana la ushuru huu na unaleta matatizo makubwa na kwa kuwa kuna ahadi ya Rais kwamba hizi shughuli ndogondogo zitaangaliwa upya, je, Serikali sasa iko tayari kuziagiaza Halmashauri zote ziangalie upya maeneo ambayo kuna usumbufu mkubwa na ushuru huu, ili marekebisho yafanywe haraka na wananchi wasipate bugudha ikiwemo Wilaya ya Mvomore?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake ya ufasaha, na mimpongeze Mheshimiwa Murad kwa ufuatiliaji wake kwa masuala yanayohusu Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kama ambavyo nilisema wakati nachangia, tunakaa na wenzetu wa TAMISEMI pamoja na Wizara zingine ambazo zinahusiana na sekta ambazo zinahusu mambo ya makato makato na tulishasema tunayafanyia kazi mambo ya makato yote ambayo yanamgusa Mkulima na wafanyabiashara wadogowadogo. Lakini kwa leo nitamke tu kwamba kwa yale makato ambayo hayako kisheria, kwa makato ambayo yanawagusa wakulima ambayo hayako kisheria kuanzia leo hii wale wanaohusika waondoke na tamko hili kwamba wayaache, yale ambayo yako kisheria tunaenda kufuata utaratibu na kuangalia kama yote yabaki ama yabaki kiasi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunawapa unafuu wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini yale hayako kisheria na yale ambayo hayahusiani moja kwa moja na uendelezaji wa zao husika hayo yakome moja kwa moja kufuatana na kwamba yamekuwa yakiwapa mzigo wakulima bila kuleta tija katika kuongeza uzalishaji wa zao husika. Na tutachambua moja baada ya lingine na yale ambayo yanaafikiwa kwa kupitia makubaliano ya wadau wahusika, wasikubaliane wao na kuanza kuyatumia mpaka wapate ridhaa ya Wizara kwamba kuna mambo haya wamekubaliana na sisi tuweze kupima umuhimu wa kuwepo makato hayo katika uendelezaji wa zao husika. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Ni kweli kuna juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika Wilaya ya Mvomero kuondoa tatizo la wakulima na wafugaji, na kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa kupitia Waziri Lukuvi, Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, tunawashukuru Mawaziri hawa, wamefanya ziara mbalimbali. (Makofi)
Swali la kwanza, kwa kuwa juhudi ambazo tunaendelea kuzifanya kama Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero zinahitaji bajeti, na kwa kuwa tayari Mawaziri hawa tumeshawapa bajeti zetu ili tuondoe mgogoro huu na wakulima na wafugaji wawe na maeneo yao. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ambazo tuliziomba na fedha zile ziko kwenye bajeti?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna mashamba sita yamerudishwa, na mashamba mengine zaidi ya 29 bado hayajarudishwa.
Je, lini Waziri mhusika pamoja na Mheshimiwa Rais, watayafuta yale mashamba yaliyobaki ili tuwagawie wananchi maeneo ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la bajeti, Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenye bajeti yake imetenga fedha pamoja na mambo mengine kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, vilevile kwa ajili ya kuweka miundombinu ya huduma za mifugo, kwa ajili ya Wilaya ya Mvomero.
Kuhusu swali la pili, tayari mashamba mengine yameshapelekwa Wizara ya Ardhi ili yaweze kufutiwa hati. Wilayani Kilosa mashamba 73 yenye ukubwa wa ekari 429,625.3 tayari yameshabainishwa na kupelekwa ili yaweze kufutwa. Vilevile Wilayani Mvomero mashamba 84 yenye ukubwa wa ekari 119,382.6 nayo yameshapelekwa Wizara ya Ardhi ili kufanyiwa kazi. Lengo ni kwamba haya mashamba yote yakiweza kufutiwa hati baada ya hapo utaratibu utakaofuata ni kuwagawia Wafugaji na Wakulima ili kuweza kuondoa tatizo kubwa lililopo la ardhi na hatimaye kupunguza migogoro hiyo ya ardhi.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa maeneo ya Ludewa yanafanana sana na maeneo ya Mvomero katika kilimo na kwa kuwa tuna miradi mingi ya umwagiliaji katika maeneo ya Kata za Kanga, Mkindo, Sungaji, Lukenge, Dakawa na Mlali; na baadhi ya miundombinu ilishajengwa, lakini Serikali haijatoa fedha za kumalizia miradi hiyo: Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kufuatana nami mara baada ya Bunge hili, uende ukaone fedha ambazo zimetumika na nyingine zinazohitajika ili miradi ile ikamilike na ilete tija kwa wananchi wa Mvomero na Taifa kwa ujumla?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema kama tuko tayari kwenda kuangalia maeneo ambayo yanafaa kwa umwagiliaji. Hiyo tuko tayari. Nataka niongezee, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema ni lini Serikali itaacha kutegemea wafadhili? Katika bajeti ya mwaka huu ambayo Waheshimiwa Wabunge mmepitisha kwenye Sekta ya Maji, asilimia 75 ni fedha ya kwetu wenyewe. Kwa hiyo, huo ndiyo mwelekeo, kwamba wafadhili wameshaanza kupunguza misaada katika miradi yetu ya maendeleo. Kwa hiyo, tunakwenda huko. Tutafika mahali tutafanya miradi yetu kwa asilimia 100.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji wa Nyamugali unafanana na Mradi wa Maji wa Mvomero hususani katika eneo la Dihinda, Kanga, Mzia na Lubungo; na kwa kuwa katika maeneo hayo kuna visima virefu vilichimbwa na Wizara mwaka jana. Visima vile vimeachwa kama maandaki na Serikali imetumia mamilioni ya fedha.
Je, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia visima vile na kutoa kauli ni lini miradi ile itapata fedha ili ikamilike na wananchi wapate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeshachimba visima, kilichobaki sasa hivi ni kuweka mtandao wa mabomba ili maji sasa yaweze kuchukuliwa kutoka kwenye visima kuwafikia wananchi. Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi kwamba mwaka huu tayari tumeweka fedha kwenye Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba sasa fedha hizo zitumike kuweka mtandao huo wa maji ili wananchi waweze kupata maji kwa sababu uwekezaji wa visima tayari umeshafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufuatana naye, tusubiiri tumalize Bunge, Mheshimiwa Mbunge hiyo ni kazi yetu tutapita kila eneo ili kwenda kuangalia matatizo yaliyopo na kushauriana jinsi ya kuyatekeleza.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanawake wa Simiyu wamehamasika vizuri sana na wanafanana kabisa na wanawake wa Mvomero na wanawake wa Sumve.
Je, Waziri atatueleza ni lini sasa katika suala zima la maendeleo zile shilingi milioni 50 zitakwenda Sumve na Mvomero kwa sababu wanawake wale wameshajiunga kwenye vikundi na vikundi vile vimeshasajiliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie wanawake wa Mvomero na wale Wasukuma wa kule hawawezi kufanana, hilo ni jambo la kwanza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba nimtoe shaka, najua Mheshimiwa Murad ni mpiganaji mkubwa sana, Serikali itahakikisha watu wa Mvomero, Bariadi, Sikonge na wa maeneo yote fedha zile zinapatikana na zinawafikia wananchi ili mradi wahakikishe wanajihusisha katika shughuli za ujasiriamali. Suala hili Serikali imelisikia ndiyo maana imeweka katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Wilaya ya Mvomero kuna migogoro mikubwa sana ya wakulima na wafugaji zaidi ya Wilaya ya Kilosa na kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imefanya mikakati mbalimbali kupunguza migogoro hii na zipo juhudi kubwa sana zilifanyika na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alifika mara mbili na aliahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga majosho na malambo; fedha ambazo hadi leo hazijapatikana. Majosho na malambo yale yatasaidia ng’ombe wale kwenda kupata maji katika maeneo ambayo yapo nje ya mashamba ya watu.
Je, Serikali ipo tayari kutimiza ahadi hiyo ya Waziri ili tuweze kupata fedha za kujenga malambo na majosho Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alitoa ahadi kuhusu miundombinu hiyo ya malambo na majosho. Nipende tu kusema kwamba alifanya hivyo kama Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na hakufaya kama binafsi. Kwa hiyo, ahadi aliyoitoa bado ipo kwenye Wizara yangu hajahama nayo. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu itaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Mvomero ili kuhakikisha kwamba ahadi yetu hiyo ya Wizara inatekelezwa. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza kuhusu Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kwa kuwa Serikali inaongeza wanafunzi kila mwaka; na kwa kuwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Mzumbe kwamba Serikali itatoa fedha kwa ajili ya Ofisi za Walimu na nyumba za wafanyakazi; na kwa kuwa ahadi hiyo hadi leo haijatekelezwa.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne pamoja na kuongeza nyumba za watumishi pale main campus Mzumbe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ilielezwa hapo awali, niseme tu kwamba katika Vyuo Vikuu ambavyo vina kipaumbele katika uongezaji wa miundombinu kwa mwaka huu unaokuja wa fedha 2017/2018 ni pamoja na Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kwa hiyo, naomba ajue hilo.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la Wilaya ya Mlele linafanana kabisa na suala la Wilaya ya Mvomero na kwa kuwa Wilaya ya Mvomero tayari tumeshajenga Hospitali ya Wilaya ambayo imekamilika kwa asilimia 80 na kwa kuwa kuna fedha ambazo
tunazisubiri kutoka Serikalini ili tukamilishe na wananchi waanze kupata huduma; je, Serikali iko tayari kukamilisha ahadi yake ya kuleta zile fedha na hospitali ile iweze kufunguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naam, Serikali iko tayari na ndiyo maana katika kipindi cha sasa katika sekta
ya afya tumekuwa tukipelekeza pesa nyingi sana katika eneo hilo, na ndiyo maana naomba nikuhakikishie sio suala zima la miundombinu hata katika suala zima la madawa tumefanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Murad naomba tukitoka hapa tuwasiliane tuangalie jinsi gani katika bajeti yenu ya mwaka huu kipi kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo
kuweza kumalizia, lakini jinsi gani tufanye tuweze kusukuma kwamba katika bajeti ya mwaka huu ambayo imetengwa tusukume ilimradi fedha zipatikane suala la ujenzi likamilike ilimradi wananchi wa Mvomero waweze kupata huduma ya afya kama inavyotarajiwa.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mkoa wa Kilimanjaro matatizo yake yanafanana kabisa na Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Morogoro unakua
sana na viwanda vipo vingi na vingine vinaendelea kujengwa, lakini Kikosi cha Zimamoto katika Manispaa ya
Morogoro kinafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, kutokana na uchakavu wa magari katika Manispaa ya Morogoro, je,
Serikali iko tayari kushirikiana na Manispaa ya Morogoro kupata magari mapya katika Manispaa ya Morogoro?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alichosema Mheshimiwa Murald na
nimpongeze sana kwamba maeneo ambayo yana viwanda gharama za bima huwa zinakuwa juu sana kama magari ya zimamoto ama huduma za zimamoto zisipokuwa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nature ya Mkoa wa Morogoro Serikali iko tayari kushirikiana na Mkoa na Mji wa
Morogoro kuweza kupata magari mapya. Kwenye taratibu hizi tunazoendelea nazo za upatikanaji wa magari mapya,
tutazingatia maombi na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona, lakini vilevile niipongeze sana
Wizara hii.
Katika Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi iliweka ahadi kwamba
itaweka lami barabara ya kutoka Korogwe - Kwa Shemshi - Dindila - Bumbuli hadi Soni, lakini mpaka leo hii hakuna ufafanuzi wowote wa kujengwa kwa lami. Nataka Serikali iwahakikishie wananchi kule kwamba barabara ile ni lini sasa itajengwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, hii barabara anayoizungumzia ya kuanzia Korogwe kuelekea Bumbuli – Dindila mpaka kule mwisho ni barabara ambayo amekuwa akiiongelea mara nyingi kuanzia kipindi cha bajeti ya mwaka jana. Nimhakikishie tu yale ambayo tulimueleza, kwamba barabara hii kwanza itaanza kujengwa kutokea Korogwe, kama ambavyo usanifu ulionesha.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, nimhakikishie kwamba haya anayoyasikia kuhusu hii barabara sio kweli. Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi yake ya kuijenga hii barabara kwa lami. Kama nilivyomueleza mara nyingi tu ofisini na maeneo mengine na hata alipomuona Waziri wangu, nikupongeze sana kwa namna unavyofuatilia kwamba barabara hii tutaijenga baada ya kukamilisha hizi barabara ambazo sasa hivi zinatuletea madeni mengi, tunataka tuziondoe kwanza hizo ili tuzianze hizi nyingine, lakini kimsingi katika miaka hii mitano ahadi hiyo tutaitekeleza.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, naomba nami niulize swali moja dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Waziri umetembelea Wilaya ya Mvomero na umejionea mwenyewe hali halisi ya Wilaya; leo gari la afya ambalo linatumika kwa ajili ya chanjo ndilo linatumika kwa ajili ya kukusanya mapato, lakini Idara ya Ujenzi haina gari, magari yote ni chakavu.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutusaidia sisi watu wa Mvomero ili tuweze kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, anachosema ni kweli. Siku ya Alhamisi tulikuwa Jimboni kwake pale na tulitembelea mpaka Hospitali ya Wilaya na kubaini changamoto na jiografia ya eneo lile kuanzia Turiani na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, eneo lile ni kweli, hata nilipokutana
na wataalam pale, kuna changamoto ya magari. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema pale awali ni kwamba mchakato wa ununuzi wa magari mara nyingi sana unaanza na kipaumbele cha Halmashauri yenyewe, lakini kwa sababu tuko pamoja hapa na Mbunge siku ile tulikubaliana mambo mengine ya msingi. Tutaendelea kushirikiana vya kutosha kuona ni jinsi gani tutaiwezesha Halmashauri ya Mvomero iweze kufanya vizuri. Ndiyo maana Serikali hata katika suala zima la miundombinu, wewe unafahamu jinsi tunavyowekeza pale hata katika ujenzi wa lami. Lengo kubwa ni kwamba wananchi wa Mvomero wapate matunda mazuri ya Mbunge wao.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itashirikiana naye, pale kwenye mahitaji ya haraka tutafanya kwa ajili ya wananchi wake na watendaji waweze kufanya kazi vizuri katika Jimbo la Mvomero.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kutumia Bunge hili kupiga marufuku magari ya chanjo kutumika kwa shughuli tofauti na chanjo. Kuanzia sasa hivi magari ya chanjo tutayandika herufi kubwa neno “CHANJO” na lisitumike kwa matumizi mengine yoyote. Kwa sababu chanjo ni muhimu kuliko masuala mengine katika Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, niliona nitumie Bunge lako kutoa ufafanuzi. Kwa hiyo, ni marufuku Halmashauri ya Mvomero kutumia gari la chanjo kwa ajili ya kukusanyia mapato. Ahsante.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Mikumi National Park imepakana na Wilaya ya Mvomero na kata za Doma, Msongozi, Melela, Malaka pamoja na Mangaye; kwa kuwa wanyama waharibifu wanaingia sana katika mashamba ya wakulima na wanaharibu sana mazao ya mahindi, mpunga, nyanya na kadhalika na kwa kuwa tembo wengi sana wameshafanya uharibifu mkubwa, je, Serikali sasa iko tayari kuongeza Askari wa Wanyamapori katika maeneo hayo angalau kila kata kuwe na askari mmoja ili kuondoa tatizo ambalo wananchi wanakabiliana nalo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Mvomero ina upungufu mkubwa wa vitendea kazi, je, Serikali iko tayari sasa kuisaidia Wilaya ya Mvomero vitendea kazi pamoja na masuala mengine ya usafiri ili tuweze kukabiliana na hali hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wanyama wakali na waharibifu wameongezeka katika maeneo mbalimbali hapa nchi na katika eneo la Wilaya ya Mvomero wanyama hawa wameongezeka sana katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saddiq Murad Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya tumetembelea hayo maeneo ambayo yamezidiwa sana na uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu. Wizara itaongeza askari kusaidiana na wale walioko katika Wilaya ya Mvomero ili kupambana na kadhia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wizara itashirikiana na Halmashauri ya Mvomero kwa kuipa vitendea kazi zaidi pamoja na kuwasaidia katika usafiri ili waweze kukabiliana na tatizo hili ambalo limeongezeka sana katika Wilaya hiyo. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nasafi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri na pamoja na bajeti ambayo wameipanga, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ambalo limeulizwa la polisi Mazizini linafafana kabisa na suala la Mvomero katika Kituo cha Polisi Turiani. Kituo cha Polisi Turiani kipo katika jengo la mabati na jengo lile lilijengwa tokea enzi ya mkoloni na hadi leo kituo kinatumika. Hata hivyo, wananchi na wadau mbalimbali tumeamua kujenga kituo cha polisi na sasa hivi kimefikia hatua ya lenter na ujenzi huo umefanyika zaidi ya miaka kumi iliyopita. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea Turiani na kuonesha nia yake kuweza kumalizia kituo cha polisi Turiani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Turiani ni sehemu ya Wilaya ya Mvomero migogoro ya wakulima na wafugaji ni mingi na jitihada kubwa zimefanyika. Je, yuko tayari kutusaidia gari kwa ajili ya Kituo cha Polisi Turiani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Murad kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa karibu sana masuala ya wananchi wake wa Jimbo la Mvomero. Natambua Jimbo la Mvomero jiografia yake ni ya tofauti sana kwa sababu kuna baadhi ya tarafa ziko ukanda mwingine huku kama unaelekea barabara hii ya kwenda Mikumi na upande mwingine ndiko huko Turiani anakokusemea. Kwa hiyo nianze tu kwa kusema kwamba niko tayari na si mbali kutembea kituo hicho anachokisemea ili kuweza kujionea kazi nzuri ambayo wananchi wameshafanya kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tutaweka kipaumbele kwenye upande wa kuipatia wilaya yake vitendea kazi ikiwemo gari kwa kuzingatia hali halisi ya migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza katika Wilaya ya Mvomero pamoja na Kilosa ambayo inahitaji sana vitendea kazi kama hivyo. Kwa hiyo tunazingatia punde tutakapokuwa tumepata magari kwa ajili ya kusaidia vituo vya polisi. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo lililopo Maswa Magharibi linafanana na la Mvomero, na kwa kuwa Mvomero kuna maji mengi, kuna mabonde mazuri sana na kwa kuwa wananchi wa Mvomero wamejipanga katika kilimo cha umwagiliaji, na kwa kuwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Maji injinia Isack kwa kusaidia mabonde mawili, Bonde la Kigugu na Bonde la Mbogo, je, ni lini fedha zile zitatoka ili kuleta tija kwa wananchi wa Mvomero na Taifa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa miradi ya Kigugu na usanifu umekamilika, wakati wowote Mheshimiwa Murad nikuhakikishie hatutaingia kwenye kutangaza tender kuhakikisha kwamba hiyo miradi imetekelezwa.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi hii. Naomba niungane na Mheshimiwa Azza, naomba niulize swali moja dogo la nyongeza. Wilaya ya Mvomero imejaaliwa baraka kubwa na Mwenyezi Mungu, maji ni mengi, mabonde ni mengi, Waziri alituahidi miradi miwili ya umwagiliaji. Mradi wa Mbogo na mradi wa Kigugu yenye thamani ya shilingi bilioni tatu toka mwaka jana. Je, ni lini sasa fedha hizo zitatolewa ili wananchi wale waweze kujiendeleza katika miradi hii ya umwagiliaji. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli aliahidiwa na Mheshimiwa Waziri wangu kupewa miradi miwili ya umwagiliaji na kwa kuwa ahadi ni deni, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sasa hivi tunapitia mapitio ya mpango kabambe wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili tuweze kujiridhisha. Nataka nimhakikishie ahadi ile tutaitekeleza katika kuhakikisha wananchi wake wa Mvomero wanapata miradi hiyo yote miwili ya umwagiliaji.