Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Azza Hilal Hamad (15 total)

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu wa kisima kirefu cha maji Mji Mdogo wa Tinde gharama yake halisi iliyotolewa na SHIWASA ilikuwa ni milioni 400 na mpaka sasa hivi Serikali imeshatoa milioni 300 kwa awamu.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kutoa milioni 100 ili kukamilisha mradi huo?

Swali la pili, mradi huu wa maji, unategemewa kuhudumia zaidi ya watu 10,000 katika Mji mdogo wa Tinde. Vituo vilivyowekwa vya kuchotea maji havitoshelezi kabisa ukilinganisha na idadi iliyopo.

Je, Serikali haioni kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza vituo vya kuchotea maji ili wananchi waweze kuchota maji hayo bila bugudha?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikiri kwamba katika Bunge lililopita hapa la Bajeti, kwa kumbukumbu zangu Mheshimiwa Azza alishika mshahara wa Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya tatizo la maji. Kwa hiyo, hapa ninakiri kwamba Mheshimiwa Azza amekuwa akipigania jambo hili kwa muda mrefu sana, hilo suala la kwanza.

Mheshimiwa Spika, suala zima la mradi huu bajeti yake ni shilingi milioni 400, lakini mpaka sasa tumepeleka milioni 300. Nadhani hata Mbunge atakiri hapa wazi kwamba upelekaji wa milioni 100 za awamu ya kwanza, upelekaji wa milioni 200 ambao umefanyika mwezi Novemba, bado milioni 100. Suala hili nadhani kila Mbunge hapa atasimama na kusema mradi wake hapa haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ni kwamba upelekaji wa fedha hivi sasa Serikali imejipanga, na ninyi wote ni mashahidi kwamba katika kipindi hiki mchakato wa kukusanya mapato ya Serikali umekuwa mkubwa sana lengo lake ni kwamba kuhakikisha viporo vya miradi vyote inatekelezeka ndani ya muda.

Mheshimiwa Spika, naomba nikuambie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imejipanga lengo kubwa ni kwamba commitment ya Serikali na Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwa Tanzania kumwondoa ndoo kichwani mwanamama, hii ni ajenda kubwa tutaendelea kuifanya. Naomba uiamini Serikali yako itaenda kufanya mchakato mpana ili mradi huu ukamilike na wananchi wapate huduma.

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili, ni jinsi gani mradi ulikuwa na vituo vinne lakini population ni kubwa, naomba niseme kwamba Mamlaka ya Maji sasa iangalie ni jinsi gani ya kutatua kwa sababu population imeongezeka. Hali kadhalika, watu wa Tinde, hata huyu Mheshimiwa Mbunge alikuwa ana changamoto kubwa sana wakati wa kampeni, hali ilikuwa ni tete pale Tinde. Lakini ukija kuangalia sasa hata huo mradi ukikamilika ukiweka vituo vinne bado changamoto ya maji katika Mji wa Tinde kwa sababu ya population itakuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ajenda kubwa hapa ni kama nilivyosema ni lazima kama Wabunge tushikamane tukusanye mapato ya Serikali ili mapato yale yasaidie hata ule mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka katika Mji wa Kahama pale, yanakuja Tinde yanaenda Nzega, yanaenda Igunga mpaka Tabora. Ni mkakati mpana kusaidia ukanda ule wote uondokane na tatizo la maji. Kwa hiyo, tumesikia hiki kilio Serikali itaifanyia kazi. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo ya Busokelo yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, na kwa kuwa, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini tumeanzisha kwa nguvu zetu wenyewe ujenzi wa Hospitali ya Wilaya toka mwaka 2007, na mapato ya Halmashauri ni kidogo, Halmashauri imekuwa ikijenga kidogo kidogo kwa kushirikiana na wananchi wake, lakini ukamilishaji wa hospitali hii umekuwa ni mgumu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuipa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ombi maalum la fedha ilizoomba kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Azza nakumbuka mwaka 2015 alitaka kushika shilingi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhusiana na suala zima la mambo ya maendeleo katika Mkoa wa Shinyanga. Na nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba mwaka huu ulikuwa na kilio kikubwa sana cha suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba, Serikali imesikia kilio hiki, tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo. Lengo kubwa ni kwamba, juhudi unazozifanya kwa wana-Shinyanga, kama Mbunge wao wa Viti Maalum, naomba niseme tutakuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninakumbuka kuna lile ombi maalum Serikali imesikia hili. Jambo kubwa ni kwamba, tushikamane kwa pamoja tukusanye mapato, Serikali iwe na nguvu, miradi tuliyoipanga na maombi tuliyoyapeleka yote yaweze kufanikiwa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Azza ondoa hofu, Serikali yako, na mimi mweyewe niseme na Waziri wangu mwenye dhamana, tuko tayari kuhakikisha kwamba Wanashinyanga wanapata huduma bora ya afya katika eneo lao.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake lakini nitumie fursa hii kumpa pole kwa ajali aliyoipata jana, hakika Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya gharama zake ni kubwa sana na kwa kutegemea bajeti ya Halmashauri inaonesha wazi Hospitali hii haitakamilika kwa wakati. Toka ujenzi huu umeanza ni takribani miaka saba leo na Hospitali haijaanza kufanya kazi. Je, ni lini Serikali itaipa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ombi la fedha maalum kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hii?
Swali la pili, kwa kuwa Naibu Waziri amefika Shinyanga na akajionea hal halisi ya matatizo ya huduma ya afya na katika Mkoa mzima wa Shinyanga ni Wilaya moja tu ambayo inatoa huduma za Hospitali ya Wilaya, je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba inausaidia Mkoa wa Shinyanga na kuhakikisha Hospital ya Wilaya ya Shinyanga na Hospitali ya Wilaya ya Kishapu zinapewa kipaumbele kwa kuanza kutoa huduma kwa majengo yaliyokamilika na kuwapa watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli tarehe 11 mwezi Agosti nilikuwa pale Shinyanga na miongoni mwa ajenda, miradi tuliyotembelea ilikuwa ni miradi ya afya, hospitali yetu ya Mkoa na Hospitali yetu ya Rufaa inaendelea kujengwa.
Mheshimiwa Spika, suala zima la ombi maalum ni kweli, mwaka huu walileta ombi maalum la shilingi bilioni tatu lakini katika mchakato wa bajeti ombi lile maana yake halikupewa kipaumbele, lakini ni imani yangu kwamba kwasababu lengo kubwa la Serikali hii ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya afya na nilieleza katika vikao vilivyopita kwamba lengo letu ni kwamba kila Halmashauri ipate Hospitali ya Wilaya na kwa sababu Serikali imejielekeza katika ukusanyaji wa mapato; mimi imani yangu ni kwamba wananchi wa Shinyanga itapewa kipaumbele katika mwaka wa fedha ili mradi hospitali hiyo iweze kufanya kazi iweze kukamilika wananchi wa Shinyanga wapate huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili lililkuwa ni suala zima la Hospitali ya Shinyanga na Hospitali ya Kishapu ni kama nilivyosema awali, lengo kubwa ni kuboresha huduma ya afya na mimi nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tulifika pale na tulitembelea maeneo yote mpaka ile Hospitali ya Mkoa ambayo ya Rufaa mmefanya kazi kubwa sana, mmetumia pesa ni chache, lakini miundombinu iliyojengwa pale ni miundombinu nimetembelea ni hali ya juu sana. Mimi naamini Serikali yetu iko mbioni katik ahilo na mimi nalichukua hili kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI lakini Serikali ikijua kwamba jinsi gani tutafanya kuhusu kero za wananchi hasa katika sekta ya afya. Ahsante.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Tatizo la Benki ya Wanawake limekuwa ni kubwa katika mikoa yote, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni kwanini Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto isikae na kukubaliana na benki ambazo zinapatikana kwa kila mkoa kama NMB, CRDB na NBC ili waweze kuweka angalau dirisha moja kwa kila mkoa kuweza kutoa huduma hizi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kweli kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Lengo la benki lilikuwa ni kufikisha huduma za mikopo yenye riba nafuu kwa wanawake hasa walio vijijini. Katika jitihada ambazo zimefanyika hatukuweza kwa kweli kufikia lengo hilo ni lazima nikiri hilo. Nimshukuru sana Mheshimiwa Azza kwa wazo zuri tunalipokea na tayari nimeshapata baadhi ya benki ambazo ziko tayari kushirikiana na Benki ya Wanawake ili sasa tuweze kufungua dirisha la Benki ya Wanawake katika benki ambazo ziko katika mikoa na wilaya mbalimbali. Kwa hiyo, kwa kweli naamini ndani ya miezi mitatu tutaweza kuja na suluhisho maalum la kuhakikisha huduma za Benki ya Wanawake zinafika hasa kwa wanawake walio vijijini.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na
majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji nina maswali
mawili ya nyongeza. Naibu Waziri amekiri miradi hii imechukua muda mrefu
kutoka 2012 mpaka leo hii haijakamilika; Je, Wizara haioni sasa ni muda muafaka
wanapokuwa wamepelekewa certificate waweze kulipa malipo haya kwa
muda muafaka kwa sababu wanawachelewesha wakandarasi. (Makofi)
Swali la pili; miradi hii imechukua muda mrefu sana mpaka muda huu
imefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Mheshimiwa Naibu Waziri haoni ni muda
muafaka sasa wa kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali
la kwanza amesema Serikali ione haja ya kulipa haraka certificate, tunafanya
hivyo Mheshimiwa Mbunge kwamba certificate ikishawasilishwa kwenye Wizara
yetu na Halmashauri yoyote, kitu cha kwanza lazima tuihakiki, hatuwezi kulipa
moja kwa moja bila kuhakiki kwa sababu imetokea huko nyuma tulipotoka, mtu
analeta certificate unatoa hela, halafu hela inakwenda kukaa kwenye
Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine ucheleweshaji wa
kulipwa unatokana na ule uhakiki ili kujiridhisha kwamba kweli kazi imefanyika na
kwamba hela ile ikifika ni moja kwa moja inakwenda kwa mkandarasi mhusika ili
kazi iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwamba Serikali sasa haioni kwamba
ni wakati muafaka wa kutafuta fedha. Kwa bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge
katika bajeti iliyopita ambayo sasa hivi tunaitekeleza mlipitisha ninyi wenyewe
fedha za Mfuko wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katika Bunge hili amesema
mpaka sasa tayari tumeshapokea zaidi ya bilioni 71 ambazo zimetokana na
Mfuko wa Maji na fedha hizi mpaka hapa ninapoongea Waheshimiwa Wabunge
kwamba tayari tuna fedha kwenye Wizara, kwa hiyo, wakati wowote certificate
ikifika tunailipa. Kwa hiyo, Serikali tayari inakusanya fedha kuhakikisha kwamba
miradi mingi ambayo ilikuwa imekwama inaendelea na utekelezaji wake ili iweze
kukamilika.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kijiji cha Ishololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kilitengewa fedha kwa ajili ya Mradi wa Umwagiliaji, zaidi ya shilingi bilioni moja. Mradi huu haujaweza kukamilika na Mkandarasi kuweza kuondolewa na Serikali kwa sababu, mradi huu haukuisha kwa wakati. Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari sasa kuja katika Kijiji cha Ishololo na kuona mashimo tuliyoachiwa na mkandarasi yule na mradi huu kuwa hauna tija kwa wananchi wetu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niko tayari kutembelea miradi yote ya kilimo cha umwagiliaji. Labda niseme tu, hii miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika sehemu kubwa, mingi ina matatizo. Kwa sababu ya matatizo, kweli tumekwenda tumekuta miradi mingi haifanyi kazi jinsi inavyotegemewa.
Mheshimiwa Spika, ili tuweze kurekebisha hivi, ndiyo maana Serikali tulianzisha Tume ya Umwagiliaji. Kazi yake ya kwanza ilikuwa kurekebisha miradi yote iliyokuwa imeanzishwa kwa ufadhili mbalimbali huko nyuma ikiwa chini ya Wizara ya Kilimo, tuweze kurekebisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwahidi Mheshimiwa Azza, fedha hata zikipatikana katika bajeti ya mwaka huu, tutaweza kuona nini tufanye katika kurekebisha mradi huu ambao Mheshimiwa Mbunge anauelezea.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Awali ya yote nianze kuishukuru sana Serikali kwa sababu, swali hili leo ni mara ya nne naliuliza ndani ya Bunge lako.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaendelea katika Kituo cha Wazee cha Kolandoto. Natumia fursa hii kuishukuru sana na kuipongeza Serikali kwa kazi ambayo wanaifanya, wamesikia kilio cha wananchi na wazee wa Kolandoto.
Mheshimiwa Spika, naomba nimwulize Naibu Waziri swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, jengo hili linaonekana litapendeza sana baada ya kukamilika. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanawapelekea wazee hawa vitanda na magodoro ili waweze kuishi kwa raha mustarehe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Naona dada yangu Mheshimiwa Azza Hillal Hamad amefurahishwa sana na kazi inayoendelea pale Kolandoto mpaka amekosa swali la nyongeza la kuuliza.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kujenga jengo jipya kubwa na la kisasa ambalo lina miundombinu yote kuanzia miundombinu ya malazi, kila mzee atakuwa na chumba chake, lakini pia kuna ukumbi wa television, kuna ukumbi wa burudani mbalimbali, wazee watakuwa wanapumzika pale, kuna majiko ya kisasa ya gesi, tumewanunulia Bajaj wazee wa Kolandoto na vituo vingine takribani 17 nchi nzima, ili waweze kupelekwa hospitali na kupewa huduma mbalimbali za kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Nadhani ndiyo maana Mheshimiwa Azza amekosa swali la kuuliza kwa sababu hatuwezi kushindwa kununua magodoro kama tumeweza kujenga na kuweka vifaa vyote hivyo. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikuliza swali hili toka nilivyoingia ndani ya ukumbi huu mwaka 2010. Ujenzi wa hospitali hii umeanza toka mwaka 2007 mpaka hivi tunavyoongea fedha inayoonekana hapo ndiyo ambayo imeshafika katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, lakini wakati nauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nipongeze Serikali kwa hatua kubwa ambayo wameamua kuchukua katika uboreshaji wa vituo vya afya kikiwemo Kituo cha Afya cha Tinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuhusu ukamilishwaji wa ujenzi huu kwa kuwa umekuwa ni wa muda mrefu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali imeweka mpango gani madhubuti ili kuhakikisha kwamba pindi ujenzi huu wa vituo vya afya unapokuwa umekamilika unaweza kupata wataalam wa kutosha katika majengo yetu ya upasuaji na huduma zingine zinazostahili? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika na mimi tangu nimemfahamu Mheshimiwa Azza amekuwa akipigania ujenzi wa hospitali, lakini kama hiyo haitoshi ni pamoja na kupigania Vituo vya Afya na Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Naomba kwa pekee nimpongeze kwa jitihada zake hizo na ndizo ambazo zimezaa upatikanaji wa vituo vya afya viwili, kwa maana ya Kituo cha Afya Tinde na Kituo cha Afya Samuye ambacho kimoja ni shilingi milioni 400 na kingine milioni 500.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija upande wa maswali yake, anataka ahadi ya ukamilishaji wa hospitali hizo. Kama ambavyo nimekuwa nikijibu hapa, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa hospitali 64 katika Wilaya ambazo hazina Hospitali za Wilaya na hasa kwa wananchi wa wilaya yake ambao wameshaonesha moyo kwanza kwa kutenga eneo lakini pia ujenzi umeshaanza na ndio maana OPD imeweza kukamilika. Kwa kadri bajeti itakavyoruhusu hakika naomba nimuhakikishie tutatupia jicho letu kuhakikisha kwamba hospitali hiyo inakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ametaka kujua juu ya suala zima la hospitali inapokamilika na wataalam wawepo. Naomba nimuhakikishie, ni azma ya Serikali, si suala la kujenga majengo tu, tunataka tujenge majengo ambayo yatumike. Kwa hiyo, pale ambapo ujenzi unakamilika na wataalam watakuwa wamepatikana ili waweze kutoa huduma kwa wananchi waliokusudiwa. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amejibu lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kituo hiki cha Buhangija kimekuwa na msongamano kutokana na wimbi kubwa la mauaji ya Albino na kukifanya kituo hiki kuwa na watoto wengi zaidi na hatimaye watoto wale kuweza kuishi pale shuleni. Je, ni lini Serikali itakiangalia kituo hiki na kukipelekea fedha ya kutosha ili kiondokane na tatizo kubwa la chakula linalokuwa linakikumba kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha kwa ajili ya watoto wasioona, wasiosikia na wasiosema? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Azza kwa kazi nzuri anayoifanya na tumekuwa tukishirikiana sana katika kuhudumia watoto katika kituo hicho. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Azza na nadhani wananchi wa Shinyanga wanasikia pongezi hizi za Serikali kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maswali yaliyoulizwa na Mheshimiwa Azza Hilal ni maswali ya msingi na swali la kwanza angependa kujua ni kwa namna gani sasa Serikali itaendelea kuhudumia vizuri kituo hicho na hasa kuhakikisha wale watoto wanapata chakula kinachotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, tulipata shida kubwa sana wakati ule ambapo mauaji ya wenzetu wenye ualbino yalipokuwa yamekithiri katika nchi yetu ya Tanzania, wengi wenye ualbino waliona pale ni mahali pekee na salama kwao, kwa hiyo wengi walikimbilia hapo haikuwa shule tena, ilikuwa ni kituo cha kuwahifadhi wenye ualbino watu wazima, vijana pamoja na hao watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baada ya Serikali kufanya kazi nzuri ya kudhibiti mauaji hayo, tumeshafanya utaratibu na tumeweza kuwaondoa wale watu wazima na vijana ambao siyo wanafunzi kutoka hiyo idadi ya 407 mpaka idadi hiyo ya 228 na sasa basi huduma hizo nyingine zinapatikana vizuri na sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia chakula na mahitaji mengine yapatikane sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba kituo hicho kinapatiwa fedha za kutosha, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Azza Hillal tumeshaanza mkakati wa kuhakikisha pale panakuwa mahali salama na mahali panapostahili. Kwa kuanzia tumeshapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho na tutaendelea kupeleka mahitaji mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi mmeona Mheshimiwa Waziri Mkuu amepokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya wenye ulamavu kwenye taasisi zetu, kwa hiyo na kituo hicho tutazingatia kukipa huduma zote zinazostahili kwa mujibu wa taratibu za Serikali.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mradi huu wa maji ni ahadi ya toka mwaka 2006 ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu hivyo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Wizara ya Maji ipo tayari sasa kuondoa vikwazo vyote vilivyopo Wizara ya Maji na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha mradi huu unaanza mara moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na hofu kubwa kwa wananchi wangu wa Mji Mdogo wa Tinde kutokana na kwamba mradi wa maji wa Ziwa Victoria bomba kubwa linapita mbali sana na Mji Mdogo wa Tinde, hivyo kuwa na hofu kubwa kwamba mradi huu hautawezekana kufika kwa wananchi wa Tinde. Je, Wizara ya Maji imefikia wapi kuwaondoa hofu wananchi wa Tinde kuhakikisha kwamba wanapata maji safi na salama katika mradi huu wa mkubwa wa maji ya Ziwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Azza kwa jinsi ambavyo anawapenda wananchi wa Shinyanga na jinsi anavyowatetea katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa kwamba miradi hii ilianza bajeti ya mwaka 2006/2007 na Mheshimiwa Mbunge naomba tu akumbuke ndipo tulioanza ile program ya maendeleo ya sekta ya maji, tukaweka kwamba tutajenga miradi 1,810. Tumeshakamilisha miradi 1,468, bado miradi 366 na mradi wake ukiwa ni mmojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, umechelewa kwa sababu usanifu ulichelewa, lakini kwa sasa tunamhakikishia kwamba hakuna vikwazo vya aina yoyote, tunatekeleza kwa mujibu wa sheria. Mradi wowote baada ya usanifu, baada ya manunuzi ili kuepuka upotevu wa fedha lazima tuupeleke kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaufanyie vetting, tusaini, ndiyo tuanze utekelezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba mradi utatekelezwa bila ya wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli bomba la KASHIWASA limepita mbali kidogo mbali na ule Mji wa Tinde, nimemwagiza Mhandisi Mshauri anayesimamia huu mradi wa Tabora na tayari ameshabaini vijiji vitakavyopelekewa maji ukiwemo Mji wote Tinde na vitongoji vyake na amekamilisha utaratibu wa awali sasa hivi tunaingia kwenye usanifu wa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunaendelea na utekelezaji wa mradi wa Tabora basi wakati unakamilika na Tinde yote itakuwa imeshapata maji. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga hawana mradi hata mmoja wa umwagiliaji na hivyo kuwepo kwa mradi huu tulitegemea kuleta tija kwa wakulima wetu, hasa wakulima wa mbogamboga na vitunguu.
Mheshimiwa Spika, mradi huu umetumia fedha nyingi sana na umeachwa na mashimo mengi ambayo hayana maana yoyote kwa wakulima wetu. Swali la kwanza, je, Serikali ipo tayari sasa kutoa kipaumbele katika mradi huu ili uweze kuleta tija kwa wananchi kama ambavyo Serikali ilikuwa imekusudia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari sasa kwenda katika Kijiji cha Ishololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga akajionee mwenyewe hali halisi ambayo iliachwa na Mkandarasi pamoja na fedha nyingi kutumika katika mradi ule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ni Mbunge mfuatiliaji, ni mpambanaji wa matatizo ya wananchi wake wa Shinyanga, lakini kubwa la msingi kwa kuzingatia umuhimu wa umwagiliaji, Serikali itatoa kipaumbele katika suala zima umwagiliaji katika Kijiji cha Ishololo katika kuhakikisha wananchi wa Shinyanga wanawekeza katika umwagiliaji ili tupate bidhaa au fursa ambayo itaweza kuwekeza katika suala zima la viwanda.
Mheshimiwa Spika, la msingi lingine ambalo ameniomba nifike katika eneo la Ishololo, niko tayari, mimi ama Waziri wangu tumejipanga katika kuhakikisha Bunge litakapokuwa limekwisha, kutembelea maeneo yote ambayo tuliahidi Waheshimiwa Wabunge kufika ili kujionea changamoto na maeneo yote ambayo tutakuta yana changamoto tutachukua hatua.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini niseme tu suala la tathmini linachukua muda mrefu na tathmini hii haijulikani itakwisha lini. Narudi palepale kuuliza swali langu la nyongeza, ni lini Serikali italeta Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo la upungufu wa watumishi katika sekta ya afya limekuwa ni tatizo kubwa hata katika vituo vyetu vya afya na zahanati. Je, Serikali inajipanga vipi kuhakikisha upungufu tulionao katika vituo vya afya na zahanati unakwenda kumalizika kabisa ama kupungua kwa kiasi kikubwa? Nakushuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi katika sekta ya afya, watumishi tuliokuwa nao ni takribani asilimia 52 tu ya idadi ya watumishi ambao hatunao. Katika mkakati wetu wa kwanza ameuliza ni lini tutapeleka Madaktari Bingwa, Serikali inaendelea kufanya jitihada kama nilivyosema tumeshakamilisha zoezi la tathmini tunajaribu sasa kuhakikisha kwamba wale wachache tuliokuwa nao baada ya kupata taratibu za kiutumishi tutawahamisha, lakini sambamba na hilo tunatarajia kupata kibali kipya cha ajira ambao wale watumishi watasambazwa katika maeneo mbalimbali ya kwenye uhitaji ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Hospitali za Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati kulingana na mahitaji. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini sasa naomba nimuulize Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ipo tayari sasa kuipa kipaumbele Skimu ya Umwagiliaji ya Ishololo ili iweze kuleta tija kwa wakulima wetu mara itakapokuwa imepata fedha?

Mhesimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itachimba bwawa katika Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida ambayo imekuwa ikitegemea maji ya mto ambao ni wa muda?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Azza Hillal kwa kuonesha uongozi kwa mfano. Tunamfahamu ni mdau wetu mzuri katika sekta ya kilimo, ni mkulima mkubwa wa mpunga, anawaongoza watu wake wa Shinyanga yeye mwenyewe kwa kuwa mbele na wale wanaoongozwa kuwa nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kujibu swali lake la nyongeza la kwanza, nimhakikishie kwamba Serikali ipo tayari kuipa kipaumbele hii Skimu ya Ishololo pale ambapo tutaanza kupata pesa. Kama nilivyosema kwenye majibu yetu ya awali, tumeshaanza mazungumzo na wadau wetu mbalimbali ikiwemo Serikali bya Japan kupitia Shirika lake la JICA.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kuhusu suala la ujenzi wa bwawa katika hii Skimu ya Nyida, nimhakikishie Mheshimiwa Azza Hillal Serikali inafahamu na ipo katika mipango mikakati yetu kwa miradi yote ile inayotumia maji katika mito ambayo ni ya msimu kuijengea mabwawa ukiwemo huu wa Nyida ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta kilimo chenye tija, chenye manufaa kwa wakulima wetu.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya serikali. Sasa naomba niulize maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya miradi ya umwagiliaji imekuwa haina tija kwa wakulima wetu, na hii ni kutokana na kwamba inategemea maji ya mvua za msimu.

(i) Je, serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuanza kujenga mabwawa badala ya kuanza kujenga mitaro ili tuweze kuvuna kwanza maji na baadaye kuweza kuyasambaza katika mashamba yetu?

(ii) Je, serikali imechukua hatua gani kwa miradi ya umwagiliaji ambayo imejengwa chini ya kiwango na imekuwa haina tija kwa wakulima wetu ukiwepo Mradi wa Masengwa na Mradi wa Ichololo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilaly Hamad kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua je hatuoni umuhimu wa kuanza kabla ya miundo mbinu ya umwagiliaji. Nitake kwanza kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Azza Hilaly kwa uongozi wake kwa mfano, kwa sababu anatuunga mkono kwenye kilimo na amejenga bwawa la umwagiliaji eneo lake kwa kilimo cha mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama nilivyojibu swali la msingi, kwamba Serikali tupo tayari na tulishaanza kupitia Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Mwaka 2012 tangu mwaka 2018. Kwa ajili sasa kwenda kuanza ujenzi wa miundo mbinu ya bwawa kabla ya hii miundo mbinu ya uwagiliaji kwa sababu tumeeona kwamba maji mengi wakati wa mvua yanakwenda baharini na kwenye mito na baadaye tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji.

Kwa hiyo serikali tumeshaaza mpango huo na huo mpango umeshakamilikia ambao tumeugawa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza miaka mitano kuanzia mwaka huu mpaka mwaka 2025 na awamu ya pili itakuwa kuanzia mwaka 2025 mpaka mwaka 2035.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; kwamba je, Serikali tumechukua hatua gani kwa miradi iliyojengwa chini ya kiwango. Kwanza, hatua tuliyoichukua kama Serikali ni kuhamisha Tume yenyewe ya Umwagiliaji kutoka kwenye Wizara ya Maji kuja Wizara ya Kilimo ili kukiweka pamoja kilimo pamoja na umwagiliaji. Pili ni kuimarisha Muundo wa Tume ya Umwagiliaji; kwamba badala ya kuwa na watalamu kwa ngazi ya kanda tu sasa tuna wataalamu kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na kanda ili kuwe na usimaizi wa karibu sana katika miradi hii ya umwagiliaji siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tuko kwenye hatua za kufanya tathmini ya kina ili kujua mapungufu ya msingi yaliyosambisha miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango na baada ya hapo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote ambao walitufikisha hapa ili tupate majibu sahihi ya nini cha kufanya kuendeleza miradi hiyo.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali ya nyongeza. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaifanya katika kuhakikisha inaboresha miundombinu katika shule zetu. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha inajenga mabweni katika shule zetu zilizoanzishwa kimkakati zaidi katika shule ya sekondari Samuye, Kizumbi, Isagenhe na Ukenyenge zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga kwa sababu Wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali mrefu na hivyo kukumbana na vishawishi vingi barabarani na kupelekea kupanga mitaani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Je, Serikali hamuoni sasa ni wakati muafaka wa kuweza kufikiria kutokuwapangia shule zilizoko mbali wanafunzi hawa kwa kuwa kila Kata sasa hivi ina shule?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikiri, Mheshimiwa Azza takribani wiki mbili au tatu zilizopita alikuwa akinijulisha suala zima la changamoto ya miundombinu ya elimu katika Mkoa ule wa Shinyanga na nilimuhakikishia kwamba Serikali tutafanya kila liwezekanalo, lile linalowezekana tutaenda kulifanyia kazi alichanganye pamoja na ajenda hiyo ya elimu pamoja na ajenda ya afya.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo naomba niseme kwamba Serikali tutaangalia kila kinachowezekana katika maeneo uliyoyaainisha lile litakalowezekana kwa sasa tutaweza kulifanya. Lakini ni azma ya Serikali kuhakikisha tunapambana miundombinu inaimarika kama tulivyofanya pale sekondari ya Tinde ambapo Mbunge tumeenda wote pamoja pale kwa ajili ya kuona eneo gani lazima tufanye hilo.

Mheshimiwa Spika, suala la kutowapangia mbali kwa vile kila Kata sasa ina shule, jambo hili ndiyo kielelezo chetu ni kwamba kama katika Kata hasa zile zetu ambapo kama kuna vijana wamefaulu katika eneo lile ni vyema sasa watoto wakapangiwa kwa karibu zaidi kuepusha usumbufu huo mabao Mheshimiwa Mbunge ulizungumza. Kwa hiyo, tumelichukua Serikali na tutalitolea maelekezo katika maeneo mbalimbali.