Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga (2 total)

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Chuo Kikuu cha Mzumbe ni chuo kikongwe chenye historia tangu mwaka 1953 kipindi cha ukoloni na mwaka 1972 kupandishwa hadhi kuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo (IDM) kikiwa na miundombinu ya kukidhi wanafunzi wasiozidi 1,000. Kwa sasa chuo hiki kina jumla ya wanafunzi 11,282 ambapo idadi hii ni sawa na ongezeko la 874.3% wakati hali ya majengo na miundombinu kwa kiasi kikubwa bado ni ile ile ya mwaka 1972:-
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga miundombinu mipya ikiwemo madarasa, mabweni, ofisi za Wahadhiri, jengo la utawala na kadhalika ili kukidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wanafunzi na Wahadhiri waliopo na watakaokuja na kukifanya chuo hiki chenye historia kubwa kiwe na taswira ya chuo cha kisasa na hadhi ya kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaanza kujenga miundombinu mipya kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kudahili na kuleta tija kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kati ya mwaka 2010/2011 hadi 2015/2016, Serikali ilitenga na kutoa jumla ya Sh. 8,075,490,199 fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati na kujenga majengo na miundombinu mipya katika Kampasi za Mzumbe, Mbeya na Dar-es-Salaam. Aidha, kwa mwaka 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na majengo katika Kampasi Kuu ya Mzumbe na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya katika Kampasi ya Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilidhamini chuo kujenga jengo jipya la ghorofa tano lenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kumbi za mihadhara, maktaba, ukumbi wa mikutano na ofisi katika Kampasi ya Dar-es-Salaam ambalo limekamilika na linatumika. Katika Kampasi ya Mbeya jengo jipya la ghorofa mbili la maktaba lenye vyumba vya maabara ya computer na ofisi limekamilika na limeanza kutumika mwaka 2015/2016. Vilevile ujenzi wa jengo la taaluma na utawala lenye ghorofa mbili unaendelea na unafadhiliwa na Serikali pamoja na mkopo kutoka kwa Mamlaka ya Elimu (TEA) kwa thamani ya shilingi bilioni 2.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi hizi za ukarabati, ujenzi na mipango inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuinua hadhi ya chuo hiki na hivyo kuweka mazingira stahiki ya kufundishia na kujifunzia.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na changamoto zinazoikabili za kuwa na wagonjwa wengi, kukosekana kwa Hospitali za Wilaya, kupokea majeruhi wa ajali mbalimbali lakini hadi sasa hospitali hiyo inatumia X-ray za zamani ambazo ni chakavu hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray ya kisasa (Digital X- ray) ili kuondokana na adha kubwa wanayopata wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali namba 13 lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua umuhimu wa huduma ya uchunguzi kwa kutumia mionzi ya rediolojia. Aidha, Wizara inatambua changamoto ya uchakavu wa mitambo ya radiolojia na gharama kubwa za matengenezo inayoathiri upatikanaji wa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kuleta mashine mpya 34 za kisasa za digital ambazo zinatengenezwa na Kampuni ya Philips, na hii inatokana na mkataba wa matengenezo wa mwaka 2012 na 2016 ambao mbali ya matengenezo waliyotakiwa kufanya walitakiwa vilevile kubadilisha mashine chakavu na kuweka mashine mpya. Mashine hizi zitafungwa katika hospitali za rufaa zote za mikoa Tanzania Bara ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Awamu ya kwanza ya kuletwa mashine hizi inatarajiwa kuwa ni Juni, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na gharama kubwa ya kununua na kufanya matengenezo ya vifaa vya uchunguzi Wizara imeanza kufanya uchambuzi ikiwa ni pamoja na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine ambazo zilishaanza kuweka utaratibu wa kukodisha vifaa na kulipia huduma. Wizara inatarajia kutumia uzoefu huo kuandaa miongozo itakayowezesha kutekelezwa kwa utaratibu huo kwa ufanisi.