Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga (2 total)

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati unahitaji fedha za kutosha na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa muda mrefu kina madai halali sana kutoka Serikalini ambapo chuo kinaidai Serikali kama vile fedha za ada kutoka Bodi ya Mikopo. Fedha hizi zingeletwa mapema zingeweza kusaidia kufanya ukarabati. Je, ni lini sasa Serikali itaweza kulipa madeni haya ili Chuo Kikuu cha Mzumbe kiweze kufanya marekebisho haya madogo madogo na kukifanya chuo hiki kiweze kuwa na muonekano mzuri kuliko ilivyo sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge Dkt. Jasmine ni kweli kuna umuhimu mkubwa sana wa kufanya marekebisho katika chuo hiki, lakini pia katika suala la ada kuna wakati tulikuwa tumeagiza vyuo vyote kufanya uhakiki hasa kwa wale wanafunzi ambao walikuwa hawastahili kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, alishatoa maagizo kwamba Bodi ya Mikopo ipeleke fedha hizo wakati uhakiki ukiwa unaendelea ili wasikwamishe shughuli zinazoendelea. Kwa hiyo, naamini muda wowote ule hizo fedha watakuwa wamezipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imedhamiria kuona kwamba vyuo vyote vikuu vinaongezewa fedha ili kuongeza udahili unaostahili kwa wanafunzi ili kwenda kusoma kwenye chuo binafsi iwe ni hiyari zaidi ya mwanafunzi kuliko kuwa ni sababu ya kukosa nafasi katika vyuo vyetu vya Serikali. Kwa hiyo, naamini mpango huu ukikamilika hali itazidi kuwa nzuri zaidi kwa vyuo vyote ikiwepo Mzumbe.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu haya, maana kwa siku nyingi sana tulikuwa tumeahidiwa na majibu yalikuwa hivi hivi, lakini haya mpaka tumepewa date kwamba Juni tutapata hiyo x-ray digital tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kuuliza maswali ya nyongeza kwamba; kwa kweli pamoja na kupata hiyo digital x-ray lakini bado kuna huduma nyingine ya mashine za kisasa ambazo zitasaidia hawa majeruhi kuweza kuchunguzwa zaidi. Kwa mfano tumeshuhudia hivi majuzi Waheshimiwa wenzetu Wabunge walivyopata ajali ilibidi wakimbizwe haraka sana kwenda Muhimbili kule kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini kama tungekuwa na mashine hizi tungesaidia hata wagonjwa kuokoa usumbufu na maisha yao na gharama; mashine hizo ni MRI na CT-Scan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba kuuliza, je, Wizara ni lini sasa mtatuletea pia katika Hospitali hii ya Mkoa wa Morogoro mashine za MRI na CT-SCAN ili kupunguza hata rufaa kule Muhimbili na kupunguza msongamano lakini pia kuokoa maisha ya wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pale Morogoro kama tunavyoona ile hospitali inapokea wagonjwa wengi sana wa ndani ya mkoa lakini pia na mikoa mingine. Sasa bado kuna huu usumbufu ambao unapata wagonjwa kwamba operating theatre ya mifupa haipo wanatumia theatre moja, je, ni lini sasa pia Serikali itatenga fedha za kujenga theatre hii ili kuokoa maisha ya wagonjwa na kuondoa usumbufu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tisekwa ambaye leo anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa, nimpongeze kwa hilo, lakini nimpongeze vilevile kwa maswali yake mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunaendelea kujipanga; tunatambua kwamba Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salam ziko katika highway na kumekuwa na ajali nyingi ikiwa ni pamoja na ambayo imetokea kwa Waheshimiwa Wabunge wiki iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tuna mradi ambao tunashirikiana na wenzetu wa Benki ya Dunia kuweka huduma za dharura na ajali na tumejaribu sana kulenga katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambapo huduma mbalimbali za dharura zitawekwa ikiwa ni pamoja na ambulance na kuangalia sasa uwezekano wa kuweka hizo huduma za CT-Scan na MRI katika hospitali hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo Serikali imetukabidhi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hospitali zote za rufaa za mikoa. Tumezifanyia tathmini za kina na katika bajeti ya 2018/2019 katika moja ya maeneo ambayo tutaenda kuboresha ni pamoja na kuongeza vyumba vya upasuaji. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono bajeti yetu ya Wizara ya Afya itakapofika.