Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba (22 total)

MHE. SALUM MWINYI REHANI (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Hapo kwanza Maafisa Uhamiaji wetu walikuwa wakipelekwa kwenye Balozi zetu kufanya kazi ya kutoa viza kwa wageni wanaotaka kuja Tanzania lakini hivi sasa Maafisa hao hawafanyi tena kazi hiyo na badala yake kazi hizo zinafanywa na Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na hutoa viza hata kwa waombaji wasiotakiwa kupewa:-
(a) Je, kwa nini Maafisa hao wa Uhamiaji waliondolewa kwenye Balozi hizo?
(b) Je, ni sahihi kwa Maafisa wa Mambo ya Nje kufanya kazi za kutoa viza kwa wageni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, lenye sehemu mbili kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Balozi zake mbalimbali nje ya nchi na Ofisi za Wawakilishi wa Heshima (Honorary Consuls) imeendelea kutoa huduma ya viza kwa wageni mbalimbali wanaokusudia kusafiri kuja nchini Tanzania kwa madhumuni mbalimbali. Kazi ya kutoa viza hufanywa na Maafisa wa Serikali ambao wapo Ubalozini kwa nchi zenye Uwakilishi wa Kibalozi na Wawakilishi wa Heshima (Honorary Consuls) kwa maeneo ambayo Tanzania haina uwakilishi wa Kibalozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi za Balozi za Tanzania nje ya nchi huwa na Maafisa wa aina mbalimbali wakiwemo Maafisa Mambo ya Nje, Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji, Waambata Jeshi pamoja na Maafisa kutoka Idara mbalimbali za Serikali kwa kadri ya mahitaji ya Ubalozi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sehemu kubwa ya Maafisa katika Ofisi za Ubalozi huwa ni Maafisa wa Mambo ya Nje. Kutokana na Idara ya Uhamiaji kutokuwa na Maafisa Uhamiaji katika baadhi ya Balozi zake, kazi ya utoaji viza katika baadhi ya Balozi zisizo na Maafisa wa Uhamiaji hufanywa na Maafisa wa Mambo ya Nje. Kazi hiyo huongozwa na taratibu na misingi maalum ya kisheria kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Maafisa Uhamiaji katika Balozi hizi ni kama ifuatavyo:-
(i) Utoaji wa viza kwa wageni wanaotaka kutembelea Tanzania;
(ii) Kushughulikia pasi za kusafiri za Watanzania wanaoishi katika nchi za uwakilishi;
(iii) Kutoa hati za kusafiria za dharura kwa Watanzania walipoteza pasi zao za kusafiria au ambao wameingia nchi za uwakilishi bila pasi za kusafiria;
(iv) Kutembelea magereza zenye wafungwa ambao ni raia wa Tanzania; na
(v) Kuthibitisha uraia wa wageni ambao hufika Ubalozini na kujitambulisha kuwa ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upangaji wa Maafisa Uhamiaji katika Balozi zetu hufanywa na Idara ya Uhamiaji. Maafisa hao hupangwa katika Balozi zetu kulingana na mahitaji ya Idara hiyo. Mathalani Idara ya Uhamiaji iliwarudisha Bwana Sylvester Ambokile aliyekuwa Afisa Uhamiaji London na kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Makao Makuu na Bwana Johari Sururu ambaye alikuwa Afisa Uhamiaji Abu Dhabi na kuteuliwa kuwa Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar. Hivyo, jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni kuwezesha maafisa hawa kutekeleza majukumu yao pindi wanapokuwa vituoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kama ilivyokwishaelezwa si Balozi zote za Tanzania nje ya nchi zina Maafisa Uhamiaji. Hivyo, uwepo wa Maafisa Mambo ya Nje au Maafisa wengine wa Serikali katika Balozi hizo wanaotoa viza kwa wageni mbalimbali wanaokusudia kuja Tanzania hauna madhara yoyote kwa kuwa shughuli hiyo hufanywa kwa kuongozwa na utaratibu na misingi maalum ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haina taarifa inayoonyesha kuwa kuna Maafisa Mambo ya Nje ambao wamekuwa wakitoa viza kwa waombaji wasiostahili katika Balozi zetu zilizo nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Hivi karibuni Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wetu nchini Israel, ambapo Tanzania ilikataa uhusiano hapo nyuma.
(a) Je, ni sababu gani zilizosababisha kubadilika kwa mtazamo wa nchi na kurudisha uhusiano wa Kibalozi?
(b) Ni upi msimamo wa Tanzania katika suala la uhuru wa Palestina ambayo ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya kukataa uhusiano na Israel hapo nyuma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka kuwa Tanzania na Israel zilikuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru, ambapo Israel ilikuwa na Ubalozi wenye Makazi yake Dar es Salaam na Tanzania ikiwakilishwa na Ubalozi wake wenye Makazi Cairo, nchini Misri. Hata hivyo, mahusiano haya yaliingia dosari kuanzia mwaka 1973 hadi 1995 kufuatiwa na maamuzi ya Umoja wa Afrika kuitenga Israel kwa sababu ya sera zake juu ya watu wa Palestina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka huo wa 1973 hadi leo mabadiliko makubwa yametokea katika medani ya Kimataifa ukijumuisha kumalizika kwa vita baridi, kusambaratika kwa Muungano wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Kisoviet, kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kuungana kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi. Pia katika suala la mgongano kati ya Israel na Palestina kumekuwa na hatua kadhaa zinazochukuliwa kulekea kumaliza mgogoro huo pamoja na kutiwa saini kwa Mkataba wa kwanza wa Oslo wa mwaka 1995 na ule wa pili wa mwaka 1993 na 1995 na uwepo wa Mpango wa Amani wa Palestina.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1995 Tanzania ilichukua hatua ya kwenda na mabadiliko ya dunia na kuamua kuhuisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel, ambapo kukawa na ubalozi wa Israel Tanzania mwenye makazi yake Nairobi, Kenya na Tanzania ikiwa na Balozi wa Tanzania Israel mwenye makazi yake Cairo, Misri. Aidha, mahusiano yameendelea kukua hususan baada ya Tanzania kuwa na Sera Mpya ya Mambo ya Nje ile ya mwaka 2001 inayosisitiza diplomasia ya uchumi. Kwa kutambua hatua kubwa iliyopigwa na Israel katika nyanja za kilimo, sayansi na teknolojia Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhuisha mahusiano baina yetu ikiwa ni pamoja na kufungua Ubalozi Nchini Israel.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kufungua Ubalozi wa Tanzania Israel, msimamo wa Tanzania katika kutetea haki za wanyonge Duniani, wakiwemo watu wa Palestina, bado uko pale pale kama tulivyoachiwa na muasisi wetu wa Taifa hili. Hivyo basi, msimamo wa Tanzania katika suala la Israel na Palestina ni kumaliza mzozo huu kwa amani, kwa kuwa na nchi mbili yaani Israel na Palestina huru. Kwa muktadha huo Tanzania itaimarisha mahusiano na Israel, hususan katika mambo ya kiuchumi pamoja na kuendelea kutetea haki ya Taifa la Wapalestina kuwa huru.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango mkakati gani kupitia diplomasia ya uchumi na nchi ya China kuunganisha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa ili kuingia ubia wa kuimarisha viwanda vidogo na vya kati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi nne Barani Afrika ambazo Serikali ya China imezichagua kuwekeza viwanda vyake katika miaka mitatu ijayo (2016 mpaka 2018). Kufuatia uamuzi huo Majimbo mawili ya China ya Jiangsu na Zhejiang yamekwishaelekezwa kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya China imeanzisha Mfuko Maalum wa Fedha kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Afrika kupata mitaji maalum. Mfuko huo umewekwa katika Benki ya Maendeleo ya China na tayari umetengewa dola za Kimarekani bilioni tano. Serikali imekwishaanza mazungumzo na benki hiyo kwa ajili ya kuwezesha mabenki nchini yaweze kukopa fedha hizo ili hatimaye yaweze kuwakopesha wajasiriamali wetu wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wenzao wa China.
Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Agosti, 2016 Wizara yangu iliitisha kikao cha pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya China na mabenki ya Tanzania ili kupewa utaratibu wa namna ya kupata fedha za mfuko huo. Matarajio yetu ni kwamba, mabenki hayo yatakidhi vigezo vya kuchukua fedha kutoka katika Mfuko huo wa China, ili Watanzania waanze kupata mitaji mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, ubalozi wetu nchini China mara kwa mara umekuwa ukiwashawishi wafanyabiashara wa China waje kuwekeza nchini na mara kadhaa umeandaa ziara za makampuni mbalimbali ya China kuja nchini kuonana na Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC).
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo TIC wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa ambao makampuni mbalimbali ya China yameingia ubia na Watanzania kuanzisha viwanda nchini. Mfano mzuri ni ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha nondo na bidhaa za chuma kinachojengwa Kibaha, Mkoani Pwani kwa ubia kati ya Watanzania na Wachina. Kiwanda hicho kitakapokamilika kitazalisha ajira nyingi kwa ajili ya vijana wa Kitanzania.
MHE. SALUM MWINYI REHANI (K.n.y. MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Serikali yetu kwa muda imekuwa na uhusiano wa karibu na watu wa China, Serikali ya Watu wa China ina Ubalozi Dar es salaam na Ubalozi Mdogo huko Zanzibar:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa sasa umefika wakati wa kufungua Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika Mji wa Guangzhou ili kutoa huduma nzuri kwa Watanzania wengi katika mji huo?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika katika kuwapatia visa Watanzania ambao wameamua kuishi China zaidi ya mwaka mmoja.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mpango wa kufungua Ubalozi Mdogo katika Mji wa Guangzhou uliopo katika Jimbo la Guangdong, China. Hatua hii imefikiwa baada ya Serikali ya China kuchagua majimbo matatu yatakayokuwa na uhusiano maalum na nchi tatu za Afrika ikiwemo Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Majimbo haya ni pamoja na Jiangsu, Zhejiang na Guangdong ambayo yamepewa maelekezo mahususi na Serikali ya China kuhamasisha makampuni kutoka kwenye Majimbo yao kuhamisha viwanda vyao katika nchi hizo na kupeleka katika nchi za Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo. Tunaamini kwa kuanzia katika mji huo, si tu tutakuwa na fursa ya kuyashawishi makampuni ya mji huo kuja kuwekeza nchini, bali tutaweza kutoa huduma mbalimbali kwa Watanzania wanaofanya biashara katika Mji wa Guangzhou.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo unawataka Watanzania na wageni kutoka Mataifa mengine walioamua kuishi nchini China zaidi ya mwaka mmoja kuwa na kibali cha kuishi. Kibali hiki kinapatikana kwa kuwasilisha maombi kwenye Wizara inayoshughulikia na masuala ya mambo ya ndani ya China na iwapo watakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za China watapatiwa kibali cha namna hiyo.
MHE. HAWA M. CHAKOMA (K.n.y. MHE. MARIA N. KANGOYE) aliuliza:-
Viongozi wa Dini wanaheshimika sana, wanahimiza utulivu na amani na kuliombea Taifa letu. Hata wakati wa kumwapisha Rais, Viongozi hawa hupewa nafasi ya kumwombea Rais na kuiombea nchi:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa umuhimu kwa Viongozi Wakuu wa kidini kupewa hadhi ya kupitia sehemu ya Viongozi wenye heshima (VIPs) katika viwanja vya ndege na sehemu ambazo kuna huduma kama hizo?
(b) Je, ni vigezo gani au utaratibu gani unaotumika kuwapa Hati za Kidiplomasia watu mbalimbali, lakini viongozi wetu wa kidini hawana hadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya Kumbi za Watu Mashuhuri, (VIPs Lounge) hasa katika viwanja vya ndege nchini, huratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Utaratibu ni kuwa, Kiongozi wa Dini au mtu yeyote anayestahili kutumia sehemu hizo, hujaza fomu za kuomba kutumia na Wizara yangu imekuwa ikitoa vibali vya matumizi ya sehemu hizo pindi itokeapo maombi hayo ikiwa ni pamoja na Viongozi Wakuu wa Dini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa hati na nyaraka za kusafiria za aina zote hufanywa kwa kufuata Sheria Na. 20 ya mwaka 2002 ya Hati na Nyaraka za Kusafiria ijulikayo kama Passports and Travel Documents Act, No. 20 of 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (1) cha Sheria hiyo, Mkurugenzi wa Uhamiaji ndio mwenye mamlaka ya kutoa hati zote za kusafiria. Hata hivyo, Kifungu cha 5 (2) (a) kinamruhusu Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji kumpa uwezo, yaani ana- delegate kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuelekeza utoaji wa pass za kusafiria za kidiplomasia, (power to authorize grant of diplomatic passport).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 10(3) cha Sheria tajwa kinaelekeza kuwa, wanaostahili kupewa Hati za Kidiplomasi wanapatikana katika jedwali Na. 3 katika Kifungu cha “ddd”, ambapo Mkurugenzi wa Uhamiaji amepewa mamlaka ya kutoa Pass ya Kidiplomasia kwa Viongozi Wakuu wa Taasisi za Kidini hapa nchini kwa kadri anavyoona inafaa. Hivyo, viongozi Wakuu wa Dini wamekuwa wakipewa Pass za kusafiria za Kidiplomasia kulingana na kipengele hicho hapo juu na kwa namna ambavyo mamlaka inayosimamia inavyoelekeza katika sheria husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Pass ya Kidiplomasia ni nyaraka maalum inayomwezesha mhusika kufanya kazi zake hasa za kidipolmasia.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine husika zinapitia upya Sheria hii ya Pass na Nyaraka za Kusafiria kwa lengo la kuifanyia marekebisho kwa kuangalia pia uzoefu wa nchi nyingine juu ya nyaraka hii muhimu. Pindi zoezi hili litakapokamilika, mapendekezo ya marekebisho hayo yatawasilishwa katika Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuridhiwa.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Tulipoanza kutekeleza Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, kuna bidhaa kutoka Kenya ziliwekwa kwenye kundi „B‟ ambazo zilikuwa zinatozwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi ilifikia kiwango cha asilimia sifuri mwaka 2010.
(a) Je, bidhaa hizo ziliongezeka kwa kiasi gani kuingia Tanzania kuanzia mwaka 2005 – 2015?
(b) Je, viwanda vya Tanzania vinavyozalisha bidhaa za kundi „B‟ vilikabiliwa na changamoto zipi kutokana na kuondolewa kwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi kufikia asilimia sifuri mwaka 2010?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye vipengele (a) na (b), naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Umoja wa Forodha ni kukuza biashara ya bidhaa baina ya nchi wanachama na kuongeza uwekezaji na uzalishaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha, nchi wanachama zilikubaliana kuwa na kipindi cha mpito cha miaka mitano kuanzia Januari, 2005 hadi Disemba, 2009 ambapo baadhi ya bidhaa kutoka Kenya kuingia nchi za Uganda na Tanzania ziliendelea kutozwa Ushuru wa Forodha uliokuwa unapungua taratibu na kufikia kiwango cha sifuri Disemba 2009. Bidhaa za Kenya ambazo hazikuondolewa ushuru moja kwa moja wakati wa kuanza kutekeleza Umoja wa Forodha ziliwekwa katika kundi „B‟ ambazo ni zile zilizosindikwa kwa kiwango cha kati (semi finished goods) na zile zilizokamilika (finished goods).
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye vipengele (a) na (b).
(a) Mheshimiwa Spika, thamani ya bidhaa zilizonunuliwa kutoka Kenya mwaka 2005 ilikuwa ni shilingi bilioni 64.837 ikilinganishwa na hela za Kitanzania shilingi bilioni 174.396 mwaka 2010. Aidha, mwaka 2015, thamani ya bidhaa hizo ilifikia hela za Kitanzania shilingi bilioni 267.881 ambapo manunuzi yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 14.9 katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015. Bidhaa ambazo Tanzania imekuwa ikinunua kwa wingi kutoka Kenya ni pamoja na dawa baridi, mafuta ya kula, saruji, sabuni, vipuli vya kuendeshea mitambo, dawa za mifugo, madaftari, bidhaa za plastiki na vifungashio vya bidhaa ambavyo vingi vinatumiwa na wajasiriamali wadogo wadogo na viwanda vidogo vidogo.
(b) Mheshimiwa Spika, viwanda vya Tanzania vilikabiliwa na changamoto ya ongezeko la bidhaa za kundi „B‟ kutoka Kenya hali ambayo iliongeza ushindani ukizingatia sekta ya viwanda nchini Kenya ni shindani, kuongezeka kwa vikwazo visivyo vya kiforodha kwa bidhaa kundi tajwa zinapoingia nchini Kenya kama vile vinywaji vikali vinavyozalishwa na viwanda vya Tanzania na utamaduni wa Watanzania kupenda bidhaa za kutoka nje zaidi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya kudhibiti na kusimamia uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha, kuboresha mazingira ya uendeshaji wa biashara kwa kuwa na miundombinu iliyo mizuri kama ya barabara, bandari, viwanja vya ndege pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika na bei rahisi na kuhamasisha wafanyabiashara kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya Kimataifa ili kuleta ushindani katika Soko la Afrika Mashariki.
MHE. ALLY SALEH ALLY (k.n.y. MHE. HAJI KHATIB KAI) aliuliza:- Arusha International Conference Center ni miongoni mwa taasisi ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya hiyo mwaka 1977, hivyo hii inaonyesha kwamba taasisi hiyo ina sura ya Muungano. Je, ni kwa nini taasisi hii haionyeshi ushiriki wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), kilianza shughuli zake rasmi tarehe 1 Julai, 1978 kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Kituo hicho kilianzishwa kwa kuzingatia Sheria mama ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969 kwa kupitia establishment order iliyotolewa kupitia notice ya Serikali Na. 115 ya tarehe 25 Agosti, 1978. Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hicho pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere vimemilikishwa kupitia Notisi ya Serikali Na. 84 ya tarehe 4 Aprili, 2014, ambapo vituo vyote vipo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kituo kilianza shughuli zake kikiwa na madhumuni makubwa mawili ambayo ni kuendesha biashara ya mikutano na upangishaji wa nyumba na ofisi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kimuundo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Wajumbe wa Bodi huteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa Zanzibar katika uendeshaji wa kituo kama taasisi ya Muungano, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huwa wakati wote anamteua Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Zanzibar ili kuhakikisha ushiriki wao katika kituo hicho. Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kinafanya kazi chini ya Bodi ya Wakurugenzi na shughuli za uendeshaji za kila siku zinasimamiwa na Mkurugenzi Mwendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale inapotokea fursa ya ajira katika nafasi za utendaji, nafasi hutolewa kwa ushindani na hutangazwa kupitia magazetini ambapo pande zote mbili za muungano huchangamkia nafasi hizo na washindi hupatikana kulingana na uwezo wao katika nafasi walizoomba.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA Aliuliza:-
Jumuiya ya Ulaya inatekeleza Mkakati wa Ajenda ya Mabadiliko.
Je, Tanzania imejipangaje kukubaliana na changamoto zinazotokana na Ajenda hiyo ya Mabadiliko ya Jumuiya ya Ulaya?
NAIBU WAZIRI, MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
AFRIKA MASHARIKI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya ilipitishwa mwaka 2011 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa Sera ya Maendeleo ya Umoja huo. Mabadiliko haya yanahusisha kanuni mbalimbali za kutoa misaada ya maendeleo. Kanuni hizo ni pamoja na utofautishaji wa kiwango cha maendeleo kilichofikiwa na kila nchi inayotarajiwa kupatiwa msaada.
Katika kutekeleza hili, Umoja wa Ulaya unalenga kutoa misaada kwa nchi zenye uhitaji zaidi na mkazo ukiwa katika kusaidia kupunguza umaskini katika nchi hizo. Kanuni nyingine ni kuelekeza misaada yake katika sera za kipaumbele ambazo zimebainishwa katika Mkakati wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu wa 2030. Mkakati wa Ajenda ya Mabadiliko umeainisha maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wake ikiwemo masuala ya haki za binadamu na utawala bora, usawa wa jinsia, vyama vya kiraia na Serikali za Mitaa, rushwa, sera, usimamizi wa kodi na usimamizi wa sekta ya umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo hayo, napenda kuliarifu na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imechukua hatua mahsusi zifuatazo katika kukubaliana na changamoto zitokanazo na Agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya:-
(i) Serikali imeimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha tunapunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;
(ii) Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia Sera ya Ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi ya mwaka 2009 na Sheria ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2010. Mkakati huu unasaidia kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kwa wahisani;
(iii) Serikali inaendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza zaidi hapa nchini. Jitihada hizi zinaenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara nchini na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza hapa nchini; na
(iv) Wizara yangu imeanzisha idara maalum ya kuratibu masuala ya diaspora kwa lengo la kuratibu uhamasishaji wa Watanzania waishio ughaibuni kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja kuwekeza hapa nyumbani.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA Aliuliza:-
Ofisi za Balozi za Tanzania hazipo katika hali nzuri na hii inatokana na ukosefu wa upatikanaji wa fedha ambazo zingewezesha kuimarisha Balozi hizi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuendana na maendeleo ya dunia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFIKA MASHARIKI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raisa Abdallah Mussa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendelea kukarabati na kujenga majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini na imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa kwa kila kipindi cha mwaka wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa Wizara wa miaka kumi na tano wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi wa ubalozini ulioanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Balozi zetu kama vile kufanikisha ujenzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania - New Delhi (India); ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi Tanzania - Washington D.C (Marekani); ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania - New York (Marekani); ununuzi wa jengo la Ofisi na makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania - Paris (Ufaransa); ukarabati wa makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania - Nairobi (Kenya) na ukarabati wa makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania - Tokyo (Japan).
Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara itakamilisha ukarabati wa jengo la ghorofa tisa la ofisi na makazi lililopo Ubalozi wa Tanzania Maputo (Msumbiji); ukarabati wa makazi ya Balozi na nyumba za watumishi zilizopo Ubalozi wa Tanzania Stockholm (Sweden); na ukarabati wa jengo la Ofisi na makazi ya Ubalozi yaliyopo Khartoum (Sudan).
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara inaandaa mpango mwingine wa miaka kumi na tano wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Ubalozini utakaoanza kutekelezwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi kwenye Balozi za Tanzania Harare (Zimbabwe); Kampala (Uganda); Beijing (China); Pretoria (Afrika Kusini); na Cairo (Misri); ukarabati wa nyumba za Ubalozi zilizopo kwenye Ubalozi wa Tanzania Lilongwe (Malawi); Kinshasa (DRC); ukarabati wa jengo la zamani la Ofisi ya Ubalozi lililopo Washington DC; ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini na ujenzi wa Ubalozi wa Tanzania - Addis Ababa (Ethiopia) na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania - Muscat (Oman).
Mheshimiwa Spika, mikakati ya kutekeleza mpango huu ni kuendelea kutumia bajeti ya maendeleo ya Serikali, kuishirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu na kwa kutumia utaratibu wa karadha katika kutoa mikopo ya kutekeleza miradi ya maendeleo Ubalozini kwenye nchi za uwakilishi ambapo utaratibu huo unatumika.
MHE. AHMED JUMA NGWALI aliuliza:-
Tanzania ilibadilisha Sera yake ya Kibalozi ili kuendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi duniani kwa maana ya kujiwekeza katika Diplomasia ya Uchumi (Economic Diplomacy).
(a) Je, ni lini Tanzania ilibadili Sera yake ya Mambo ya Nje ya awali na kujielekeza katika Sera ya Diplomasia ya Uchumi?
(b) Je, mwenendo ukoje kati ya sera hii na ile iliyokuwepo awali?
(c) Je, ni vigezo au vipimo gani vinavyotumika kupima Balozi zetu katika utekelezaji wa sera hii ya Diplomasia ya Uchumi.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, Mbunge wa Wawi, lenye vipengele (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mara baada ya Tanzania kupata uhuru mwaka 1961 na hata baada ya Muungano mwaka 1964, Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliweka msisitizo zaidi kwenye masuala ya kisiasa hususan kupigania uhuru wa nchi za Afrika zilizokuwa zinatawaliwa na wakoloni, kupanga ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo.
Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Tanzania kwenye masuala ya uhusiano wa Kimataifa kabla ya mwaka 2001 uliongozwa na matamko mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa nchi na nyaraka kama vile Waraka wa Rais Namba 2 wa mwaka 1964. Tanzania ilifanikisha jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujijengea heshima mbele ya jamii ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha jukumu la kuzikomboa nchi za Afrika kutoka katika makucha ya ukoloni na vilevile kutokana na mabadiliko yaliyotokea duniani katika medani za kisiasa na uchumi ikiwemo kwisha kwa vita baridi, kuibuka kwa utandawazi, dhana ya demokrasia na uchumi wa soko, Tanzania ililazimika kubadili mwelekeo wa sera yake ya mambo ya nje.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, mwaka 2001 Serikali ilitunga sera mpya ya mambo ya nje ambayo imeweka msisitizo kwenye diplomasia ya uchumi. Sera hiyo ndiyo inayoendelea kutekelezwa hadi hivi sasa.
(b) Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu kwenye kipengele (a), sera ya awali ya mambo ya nje ilijikita zaidi katika masuala ya kisiasa ambapo Tanzania ilishiriki kikamilifu kutafuta ukombozi wa nchi nyingi za Bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sera ya Mwaka 2001 ya Mambo ya Nje ambayo utekelezaji wake umelenga zaidi kupata manufaa ya kiuchumi kutokana na mahusiano yake na nchi nyingine duniani, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la watalii waliotembelea nchi yetu; ongezeko kwenye biashara ya nje na uwekezaji, pamoja na kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na misaada ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa sera ya sasa imejikita katika masuala ya kiuchumi, bado Tanzania inashirikiana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa katika kulinda amani na usalama katika nchi mbalimbali duniani.
(c) Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa Balozi zetu ni pamoja na namna Balozi anavyotimiza majukumu yake kama yanavyoainishwa katika OPRAS na Mpango Kazi wake wa mwaka pamoja na kutekeleza kwa weledi majukumu yake kama kuvutia wawekezaji kutoka nje, kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kuvutia watalii, kutafuta teknolojia sahihi na rahisi, kutafuta misaada ya maendeleo na mikopo ya masharti nafuu na kuendelea kujenga sifa nzuri ya nchi yetu na mambo hayo yamewekwa katika kitabu chao cha Ambassador’s Handbook.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, Serikali inatumiaje fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi (Adaptation Fund) zinazotolewa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia nchi (Adaptation Fund AF) chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi zilizotolewa mwaka 2013 zinatumika kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya Jiji la Dar-es-Salaam. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni tano na zinatekeleza kama ifuatavyo:-
(i) Kujenga ukuta wa bahari katika maeneo ya Barabara ya Obama (zamani Ocean Road wenye urefu wa mita 820) na Kigamboni (Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wenye urefu wa mita 380)
(ii) Kujenga miundombinu ya mitaro ya maji ya mvua katika Mtaa wa Bungoni, Kata ya Buguruni, wenye urefu wa mita 1,003 na Mtaa wa Miburani, Kata ya Mtoni wenye urefu wa mita 800.
(iii) Kurudisha matumbawe katika ukanda wa Bahari ya Hindi, eneo la Sinda, Dar-es-Salaam lenye ukubwa wa mita za mraba 2000.
(iv) Kuendesha mafunzo kuhusu matumizi endelevu ya nishati na kusambaza majiko banifu kwa familia 3000 za Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.
(v) Kupanda mikoko katika eneo la takribani hekari 40 katika maeneo ya fukwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) hutolewa kupitia njia mbili, yaani Mawakala wa Kimataifa (Multination Implementing Entities – MIEs) na Taasisi za Kitaifa (National Entities – NIEs) ambazo zimesajiliwa (accredited) na mfuko huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaotekelezwa katika Mkoa wa Dar-es-Salaam fedha zake zote zimetolewa kupitia katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Hifadhi ya Mazingira (UNEP) ambaye ni Wakala wa Kimataifa. Ili kuweza kupata fedha nyingine Serikali inakamilisha sasa mchakato ambapo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inatarajia kusajiliwa (accredited) baada ya kukamilisha masharti yanayohitajika kuwa Taasisi ya Kitaifa ya kuratibu fedha zinazotolewa na Mfuko huu.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye soko la watu milioni 200 na rasilimali lukuki katika mtawanyika wa nchi 15 wanachama, zikiwemo fursa kubwa za madini, petroli, gesi, ufundi, elimu na utalii.
(a) Je, Tanzania imefaidikaje na soko hili kwa kipindi cha miaka ya uanachama wake?
(b) Je, ni maeneo gani ya ushirikiano yameonekana zaidi kuwa na maslahi na Tanzania?
(c) Tanzania inapakana na majirani ikiwemo Zambia, Msumbiji, Congo DRC na Malawi. Je, tuna miradi au ushirikiano wa kiuchumi na nchi hizo kupitia SADC?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inajivunia kuwa moja ya nchi waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo pamoja na mambo mengine imekuwa ikifaidika sana na fursa za masoko zinazotolewa na nchi 15 wanachama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka 10, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenye nchi za SADC yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 301 mwaka 2007 hadi Dola za Kimarekani bilioni 1,017 mwaka 2016. Bidhaa ambazo Tanzania imekuwa ikiuza kwa wingi katika Soko la SADC zinajumuisha madini mbalimbali yakiwemo Tanzanite na dhahabu, bidhaa za kilimo kama chai, pamba, kahawa, bidhaa za viwandani kama vile vifaa vya plastic, sigara, neti za mbu, vipuri vya magari na simenti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo Tanzania ina maslahi nayo ni pamoja na maendeleo ya viwanda kwa lengo la uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo na madini, afya, usafirishaji, nishati, pamoja na ajira katika sekta mbalimbali. Maeneo haya yatachangia katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa kanda kutoka wastani wa 4% kwa sasa hadi 7%. Utaongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uongezaji wa thamani ya Pato la Taifa kufikia 30% ifikapo mwaka 2030. Utaongeza uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na teknolojia ya kati na ya juu kutoka kiwango cha sasa ambacho ni chini ya 15% hadi kufikia 30% inapofika mwaka 2030 na kuongeza mchango wa mauzo nje ya bidhaa za viwandani hadi kufikia 50% kutoka wastani wa 20% hivi sasa ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inanufaika pia na miradi ya ushirikiano inayoendelezwa katika nchi za SADC hususan miradi inayounganisha nchi jirani, kama vile mpango kabambe wa maendeleo ya miundombinu ya Kanda ya SADC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni pamoja na miradi ya maendeleo ya nishati ya umeme kama vile Mradi wa Zambia – Tanzania – Kenya wenye kilovoti 400 ambayo ni (400Kv Transmission Line) unaounganisha kutoka Tunduma, Makambako, Iringa, Singida – Arusha – Namanga, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan; mradi wa vituo vya pamoja vya mipakani kati ya Tanzania na Zambia, Tunduma, Nakonde, mradi wa maendeleo ya maji na uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe; mradi wa kuendelea Kanda ya Mtwara ambao unahusisha nchi za Tanzania, Msumbiji, Malawi na Zambia, ujenzi wa Daraja la Umoja kati ya Tanzania na Msumbiji, ujenzi wa reli na bandari, ujenzi wa vituo vya forodha kati ya Tanzania na Msumbiji, Zambia na Malawi na mradi wa maendeleo ya skimu ya umwagiliaji kwenye Bonde la Mto Ruhuhu, Bwawa la Kikonge.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiwataka Watanzania waliopo nje ya nchi kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini ili kusaidia kukuza uchumi wetu na hatimaye kuongeza ajira kwa Watanzania.
Je, kwa nini Serikali inashindwa kuweka Sheria ya Uraia wa Nchi Mbili ili iwe rahisi kwa Watanzania hao kuitikia wito huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Diaspora na Balozi zetu nje ya nchi zina utaratibu wa kuwatambua na kuwahamasisha diaspora wenye ujuzi wa taaluma mbalimbali kuja kuwekeza kwa wingi nchini kupitia sekta ya kiuchumi, kuleta ujuzi, elimu na utaalamu wanaoupata huko ughaibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya uraia wa Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 ambayo imebainisha kuwa uraia wa Tanzania upo katika makundi matatu, uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajinisi. Aidha, sheria hii kupitia kifungu cha 7(4)(a)(b) kimeeleza bayana kuwa raia wa Tanzania anaacha kuwa raia kwa kigezo cha kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hivyo basi, kutokana na sheria hii na sera ya Tanzania kuhusu uraia ambayo hairuhusu wala kutambua uraia wa nchi mbili, Serikali haiwezi kuweka sheria ya uraia pacha kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili lilijadiliwa pia wakati wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, Bunge Maalum la Katiba ambalo lilijadili pendekezo hili liliona Tanzania bado haipo tayari kwa sasa na Bunge hilo Maalum likatoa pendekezo kwamba; “Mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano atakuwa na hadhi maalum kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nukuu hii imebainishwa katika Sura ya 6, Ibara ya 72 ya Katiba Inayopendekezwa ya Oktoba, 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya bado haujakamilika, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge avute subira ili mchakato huo uishe.
MHE. SAADA MKUYA SALUM (K.n.y MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri kiuchumi, kiafya na kisiasa na Jamhuriya Muungano wa Watu wa Cuba, lakini Tanzania haina Ubalozi katika nchi hiyo:-
(a) Je, ni lini Tanzania itafungua ubalozi wake nchini Cuba hasa ikizingatiwa kuwa Cuba tayari wana Ubalozi nchini muda mrefu?
(b) Je, Serikali inajua kwamba kutokana na Tanzania kutofunga Ubalozi nchini Cuba, imesababisha sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyeree kutowekwa katika uwanja wa Viongozi muhimu wa Afrika katika Jiji la Havana?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Tanzania na Cuba imekuwa na mahusiano mazuri ya Kidiplomasia, Kisiasa, Kiuchumi, Kielimu, Kiafya na Kiutamaduni kwa muda mrefu yalioanzishwa na waasisi wa Mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Fidel Alejandro Castro Ruz wa Cuba. Kwa ujumla mahusiano haya mazuri yamedumu kwa miaka mingi kutokana na kuwa na maslahi mapana na nchi yanayozingatia usawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ina mpango wa kufungua ubalozi katika Mji wa Havana Cuba. Hivi sasa taratibu za kufungua Balozi hizi zinaendelea, mara zitakapokuwa zimekamilika ubalozi huo utafunguliwa kama ulivyopangwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa katika vita vya ukombozi wa bara la Afrika iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu kuenzi juhudi na harakati hizo pamoja uzalendo wa viongozi hao akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba Tanzania kutokufungua Ubalozi nchini Cuba kumesababisha sanamu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokuwekwa katika Uwanja wa Viongozi Muhimu Afrika katika Jiji la Havana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sanamu hiyo haikuwekwa katika uwanja huo kutokana na muonekano wake kutokuwa na uhalisia wa sura ya Hayati Baba wa Taifa, hivyo utengenezaji wake kuanza upya. Matengenezo ya sanamu hiyo yanaendelea na Serikali inafanya juhudi ili sanamu hiyo ikamilike na kuwekwa sehemu iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa mahusiano ya Tanzania na Cuba yataendelea kuwa mazuri katika nyanja mbalimbali hapa nchini kama vile diplomasia, afya, elimu, michezo, utalii na biashara.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA (K.n.y. MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Ibara ya 89 hadi 101 ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu (exchange of information on technological development and research findings).
(a) Je, ni taarifa zipi kiutafiti ambazo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeshirikiana?
(b) Je, ni taarifa zipi za sekta ya kilimo na mifugo ambazo nchi zimeshirikiana?
(c) Je, ni watumishi wangapi waandamizi kutoka Tanzania ambao wamepata ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzungwanko, Mbunge wa Kasulu, lenye vipengele (a), (b) na (c), naomba kutoa maelezo mafupi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 89 hadi ya 101 ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika uendelezaji wa sekta ya uchukuzi kwa maana ya barabara, reli, bandari, usafiri wa anga na majini, taratibu za usafirishaji wa shehena, huduma za posta na simu, mawasiliano, hali ya hewa na nishati. Aidha, Ibara ya 103 ya Mkataba huo imeweka misingi ya ushirikiano kwenye sayansi na teknolojia ikiwemo kubadilishana taarifa za utafiti wa kisayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kujibu swali sasa la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsazungwanko, Mbunge wa Kasulu, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinashirikiana katika kuandaa taarifa za kitafiti hususani katika hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya kikanda inayotekelezwa kwa pamoja miongoni mwao kama vile Mpango wa Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara na Reli wa Afrika Mashariki.
Aidha, nchi wanachama zinashirikiana kwenye tafiti za kuandaa sera, mikakati, sheria za Jumuiya ili kupata matokeo tarajiwa. Vilevile nchi wanachama zimeanzisha Kamisheni ya Pamoja ijulikanayo kama Kamisheni ya Afrika Mashariki ya Sayansi na Teknolojia ambapo makao yake makuu yapo Jijini Kigali, Rwanda. Uwepo wa Kamisheni hii utaiwezesha nchi wanachama kufanya utafiti kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na hata kunufaika pamoja kutokana na matokeo ya tafiti hizo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 105 ya Mkataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana katika sekta ya kilimo na mifugo. Katika eneo hili nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kushirikiana katika masuala yanayohusu mbegu, madawa ya mimea na mifugo, usalama wa chakula na udhibiti wa magonjwa ya wanyama na mimea.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na muundo wa utumishi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ina nafasi tano za Maafisa Waandamizi Wateule ambapo Tanzania inashikilia nafasi mbili ambazo ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Mipango na Miundombinu na Mwakilishi wa Majeshi. Kwa upande wa nafasi zinazojazwa kupitia ushindani ambazo ni Wakuu wa Taasisi za Jumuiya katika nafasi saba Tanzania ina nafasi mbili ambazo ni Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Utafiti wa Afya na Naibu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi wa Ziwa Victoria. Kwa upande wa nafasi za Wakurugenzi, kati ya nafasi 12 katika Jumuiya Tanzania ina nafasi nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo tuna jumla ya Watanzania nane wanaoshikilia nafasi ya watumishi waandamizi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zake.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Tanzania ni moja kati ya nchi wanachama wa Nchi za Kiafrika wa Kujitathmini Wenyewe kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM).
Je, Serikali imejitathmini kwa kiasi gani katika dhana nzima ya demokrasia na utawala bora, utawala wa kisiasa, usimamizi wa uchumi na maendeleo ya kijamii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) ulibuniwa na Wakuu wa Nchi za Kiafrika kwa lengo la kuimarisha utawala bora katika nchi zao. Nchi hujitathmini yenyewe kwanza na kutoa ripoti na mpango kazi na kisha nchi nyingine zilizojiunga katika mchakato huu huja kuitathmini nchi hiyo na kutoa ripoti ya nchi ya utawala bora. Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 35 zinazoshiriki katika mchakato huu ambapo ilijiunga mwaka 2004 na Bunge la Tanzania liliridhia makubaliano hayo mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kujitathmini, Watanzania wa kada mbalimbali walieleza mambo bora yaliyofanywa na nchi yetu na kuonesha changamoto zilizopo. Tathmini hizi ziliangazia maeneo makuu manne ambayo ni utawala bora katika siasa na demokrasia, usimamizi wa uchumi, utendaji wa mashirika ya kibiashara na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika tathmini iliyofanyika na ripoti yake kutolewa mwaka 2012, baadhi ya maeneo ambayo Tanzania ilibainika kufanya vizuri ni pamoja na kuingia kwa amani katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, kurithishana madaraka ya Urais kwa mujibu wa Katiba, matumizi ya lugha kuu ya Kiswahili, kuimarika kwa jitihada za kupambana na rushwa, kuboresha usawa wa jinsia, usuluhishi wa migogoro, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwekwa wazi na mafanikio katika kupanuka kwa utoaji huduma za jamii na nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya changamoto za utawala bora zilizobainishwa ni pamoja na changamoto kama Tume ya Uchaguzi; ukuaji wa uchumi usiowiana na kupungua kwa umaskini; tatizo la fedha haramu na dawa za kulevya; changamoto katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na elimu iliyo bora na uhaba wa vifaa katika huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kutekeleza hatua zenye lengo la kutatua changamoto za utawala bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya APRM. Inatarajiwa mwaka huu 2017, Serikali ya Tanzania itawasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa APRM kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki mchakato wa mpango huu.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Imekuwa ni mazoea sasa vijana wetu wengi, hasa wa kike wanapokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za Uarabuni kama vile Oman, Dubai na Saudi Arabia, kunyanyaswa na kuteswa na hata wakati mwingine wanauawa.
Je, inapotokea kadhia hiyo, kwa nini Balozi wetu anaewakilisha nchi yetu hatoi taarifa mapema na inachukua muda mrefu kujulikana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za kiarabu zimekuwa zinatoa fursa nyingi za ajira katika kada mbalimbali kwa Watanzania na Serikali inapata faraja kuona vijana wake wanapata kazi hizo zinazowawezesha kuendesha maisha yao na familia zao. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika baadhi ya maeneo wanayofanyia kazi na haya yameonekana zaidi upande wa akina dada wanaokwenda kufanya kazi za ndani nchi za kiarabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia ripoti mbalimbali kuhusu kadhia wanazopata Watanzania walioajiriwa katika nchi za kiarabu, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira, ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), kwa kushirikiana na Wizara zinazoshughulikia masuala ya kazi na ajira na balozi zetu zilizopo nchi mbalimbali huko Mashariki ya Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia matakwa ya mikataba inayosainiwa na waajiriwa hao pamoja na waajiri wao na kushuhudiwa na Balozi zetu, haki za Watanzania zinalindwa ipasavyo na hutakiwa kuripoti Ubalozini pale ambapo waajiri wao wanakiuka mikataba hiyo, ikiwemo kunyanyaswa au kuteswa. Mara baada ya kupokea taarifa hizo Serikali kupitia Balozi zetu zilizopo maeneo hayo huchukua hatua za mapema kuwasiliana na muajiri pamoja na mamlaka husika katika nchi hizo katika kusimamia na kutetea maslahi ya Watanzania. Hivyo, ni muhimu Watanzania wote wakaelewa kwamba mikataba hii ina dhamira ya kuwalinda dhidi ya madhara yanayoweza kuwatokea, kama ajali na majanga mengineyo. Serikali itaendelea kudhibiti mawakala kwa lengo la kulinda maslahi ya Watanzania wanaochangamkia fursa za ajira katika nchi mbalimbali na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kukuhakikishia kuwa, balozi zetu hufanya juhudi na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia masuala ya vifo yanapotokea na kujulikana na kutoa taarifa mapema kadiri zinapopatikana. Inawezekana kuna nyakati baadhi ya taarifa hizi, hasa za kiuchunguzi zinachelewa kupatikana kulingana na matukio au mazingira na utaratibu wa utendaji wa nchi husika. Na endapo hilo linajitokeza, Serikali hulazimika kusubiri, lakini wakati hilo linafanyika ndugu pamoja na vyombo vinavyohusika wanapewa taarifa kuhusu kinachoendelea.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Je, Zanzibar ina nafasi gani katika Jumuiya za Kimataifa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake, masuala ya Mambo ya Nje yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikihakikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashiriki kikamilifu kwenye masuala yote ya kimataifa. Masuala hayo ni pamoja na ziara za viongozi na mashirika mbalimbali ya kimataifa zinazofanyika nchini, ziara zinazofanywa na viongozi wa Kitaifa kwenye nchi mbalimbali, mikutano ya mashirika na Taasisi za Kimataifa na Kikanda na mikutano ya pande mbili (bilateral) na Zanzibar kuwa mwenyeji wa mikutano na makongamano ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, aidha, viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa wakiongoza ujumbe wa nchi kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa. Kwa mfano kwa mwaka 2017/2018, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshiriki katika mikutano ipatayo 11 ya mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa; imeshiriki katika ziara nne za viongozi mbalimbali wa mashirika na taasisi waliofanya ziara hapa nchini; imekuwa mwenyeji wa mikutano na warsha zilizosimamiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na kunufaika na miradi ya miundombinu, afya, kilimo na maji safi inayofadhiliwa na mashirika ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, miradi hiyo ni kama vile ujenzi wa barabara mbalimbali zikiwemo barabara za Mahonda – Mkokotoni Kilomita 31, Fuoni-Kimbeni kilomita 8.6, Pale – Kiongole kilomita 4.6 na Matemwe - Muyuni kilomita 7.6 inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kadhalika, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula na Kilimo (FAO), linatekeleza miradi mbalimbali ya kilimo na lishe Zanzibar, ukiwemo mradi wa aquaculture.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Tanzania inaonekana kupanua uwanda wake wa kidiplomasia kwa kuanzisha Balozi mpya maeneo kadhaa, lakini pia kumekuwa na malalamiko ya makazi ya Wanabalozi wa nchi hii huko ughaibuni.
• Je, Serikali haioni haja ya kuwekeza katika eneo hili kwa kujenga ofisi ambazo pia zinaweza kuwa kibiashara?
• Kama hilo linafanyika, je, limefanyika wapi na wapi hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Wziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Tanzania imeendelea kufungua Balozi zake mpya katika nchi mbalimbli duniani ili kuimarisha mahusiano na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika nchi hizo. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya Balozi mpya sita zimefunguliwa katika nchi za Sudan, Algeria, Israel, Korea Kusini, Qatar na Uturuki.
Mheshimiwa Spika, halikadhalika Serikali inatambua umuhimu wa kuendelea kujenga majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini na imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa kwa kila kipindi cha mwaka wa fedha. Hadi hivi sasa Serikali inamiki jumla ya majengo 106 yalipo katika nchi mbalimbali ambayo yanatumika kama makazi ya watumishi na ofisi za Balozi zetu.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inatambua kuwa na majengo ya vitega uchumi katika Balozi zetu ni muhimu ili kuwezesha kupatikana kwa fedha zitakazokuwa zikitumika kuziendesha Balozi hizo na hatimaye kuipunguzia mzigo Serikali. Kwa mfano, Serikali inamiliki majengo ya Ofisi ambayo pia yanatumika kama kitega uchumi katika Balozi zetu za Tanzania Maputo, Msumbiji; New York, Marekani na Paris, Ufaransa. Aidha, Serikali imeanza kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za fedha zilizopo nchini kwa ajili kujenga majengo ya vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo Abuja, Nigeria na Lusaka, Zambia.
Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa Wizara ya miaka 15 wa ujenzi, ununuzi, ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini ulioanza kutekelezwa mnamo mwaka wa fedha 2002/2003, Wizara imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Balozi zetu kama vile kufanikisha ujenzi wa jengo la ofisi ya Ubalozi New Delhi, India; ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi Washington D.C, Marekani; ununuzi wa jengo la ofisi ya Ubalozi New York, Marekani; ununuzi wa jengo la ofisi ya makazi ya Balozi Paris, Ufaransa; ukarabati wa jengo la makazi ya Balozi Nairobi, Kenya; ukarabati wa makazi ya ya Balozi wa Tanzania Tokyo, Japan; na ukarabati wa jengo la ghorofa tisa la ofisi na makazi lililopo Ubalozi wa Tanzania Maputo, Msumbiji ambalo litatumika kama ofisi ya Ubalozi na kitega uchumi cha Serikali nchini humo.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara imeandaa mpango mwingine wa miaka 15 wa ujenzi, ununuzi, ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini ulioanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2017/2018. Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi kwenye Balozi za Tanzania Harare, Zimbabwe; Kampala, Uganda; Beijing, China; Pretoria, Afrika Kusini; Cairo, Misri; ukarabati wa nyumba za Ubalozi wa Tanzania Lilongwe, Malawi; Kinshasa, DRC; ukarabati wa jengo la zamani la ofisi ya Ubalozi lilipo Washington DC; ujenzi wa makazi ya Balozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia na ujenzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Muscat, Oman.
MHE. HAWA M. CHAKOMA (K.n.y. MARIA N. KANGOYE) aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya matukio ya kikatili dhidi ya Watanzania wanaosafirishwa nje ya nchi na kufanyishwa kazi zisizo rasmi:- Je, Serikali imechukua hatua gani kudhibiti changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wanaopata fursa za kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania wanafanya kazi katika mazingira mazuri na yanayolinda staha na utu wao. Hata hivyo, katika baadhi ya nyakati zimekuwepo taasisi ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikitumia njia zisizo halali na kuwarubuni Watanzania kutofuata taratibu zilizopo za kupata ajira nje ya nchi. Kundi hili la wafanyakazi ndilo linalokumbana na kadhia ya kufanya kazi kwenye mazingira yasiyokuwa mazuri na hata matukio ya kikatili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambayo Serikali imechukua ni kuweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu na Kamisheni ya Kazi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Balozi zetu zilizopo nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo unaelekeza kila mfanyakazi kuwa na Wakala rasmi na kupata mkataba kutoka Ubalozini. Kwa utaratibu huo, Ubalozi unakuwa na taarifa katika kila hatua ambayo Watanzania wanapitia wakati wa maandalizi ya kwenda kufanya kazi, hivyo kusaidia kulinda maslahi yao. Aidha, mwajiri anayetaka kuajiri mfanyakazi kutoka Tanzania, atatakiwa kusoma na kuelewa mwongozo na baada ya kukubaliana nao, anatakiwa kujaza fomu ya kuomba kumwajiri Mtanzania na kuwasilisha Ubalozini kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Maombi hayo yatafuatiwa na mkataba wa kazi ambao umetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na Kiarabu kwa nchi za kiarabu ili kurahisisha mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Watanzania ambao tayari walikuwa nje ya nchi bila kuwa na mikataba wala mawakala, Balozi zetu zimeanzisha utaratibu wa mikataba na alama za utambuzi ambazo zitatumika kwa ajili ya wafanyakazi ambao walikuwa nje ya nchi kabla ya kupata mikataba rasmi. Vilevile, katika kuhakikisha Watanzania waliopo nje wanakuwa salama katika maeneo wanayoishi, Wizara imeelekeza Balozi zetu zote kukusanya taarifa muhimu za Watanzania wanaoishi katika maeneo yao ya uwakilishi na kuwahamasisha kuwa na utaratibu wa kujiandikisha katika Ofisi za Ubalozi pamoja na Jumuiya mbalimbali za Watanzania walioanzisha katika nchi wanazoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa rai kwa Watanzania wenye nia ya kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka husika kwa kuwa pamoja na mambo mengine inawapa kinga na kuepuka mazingira mabaya ya kazi yasiyotarajiwa na pia kurahisisha kupata msaada pale wanapohitajika.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojiunga na Mpango wa Kujitathmini Wenyewe (African Peer Review Mechanism) kisiasa, kiuchumi na kadhalika.
Je, Serikali imejitathmini kwa kiasi gani hali ya uchumi wa Tanzania unaokwenda sanjari na kupungua kwa umaskini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tanzania ilifanya tathmini ya APRM na kutoa ripoti yake ambayo iliwasilishwa kwenye Kikao cha Wakuu wa Nchi mwaka 2013. Tathmini hiyo ilifanyika katika maeneo makuu manne, usimamizi wa uchumi, utendaji wa mashirika ya biashara, siasa na demokrasia na maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la usimamizi wa uchumi, tathmini hiyo ilibainisha masuala mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika kuboresha hali ya kiuchumi ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika kuibua miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao; kuimarisha mfumo wa kifedha ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu; ongezeko la taasisi za kifedha, hivyo kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wananchi; na kuimarisha ushiriki wa nchi kwenye taasisi za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mheshimiwa Spika, pamoja na tathmini hiyo kubainisha masuala mazuri yaliyofanywa na Serikali, imebainisha pia changamoto mbalimbali za usimamizi wa uchumi. Baadhi ya changamoto zilizobainishwa na Watanzania ni ukuaji wa uchumi usio sanjari na kupungua kwa umaskini na kukosekana kwa mfumo maridhawa wa uwiano wa mapato yanayotokana na mikataba ya kiuchumi ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, tangu ripoti ya APRM Tanzania itolewe na kujadiliwa na Wakuu wa Nchi mwaka 2013, hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi kwa lengo la kupunguza umaskini wa wananchi. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kujenga uchumi wa viwanda ambao unaendelea kutengeneza ajira na kupunguza umaskini; kuimarisha ukusanyaji, usimamizi na matumizi sahihi ya mapato ya Serikali; kudhibiti ukwepaji kodi; kusambaza umeme vijijini ili kuchochea shughuli za kiuchumi hususan viwanda vidogo vidogo; ujenzi na uboreshaji wa miundombinu; uwekezaji katika kutoa elimu bure na kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi; na kupitia upya sera na sheria mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kuleta uwiano wa mapato yanayoendana na mikataba ya kiuchumi ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba inafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa juhudi hizi za Serikali, ni dhahiri kuwa umaskini utaendelea kupungua hatua kwa hatua ambapo hadi kufikia mwaka 2017 kiwango cha umaskini kimepungua na kufikia asilimia 26.3.
MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejenga tabia ya kufuatilia matatizo wanayopata Watanzania wakiwa nje ya nchi hasa wavuvi ambao wanakwenda kuvua Pwani ya Kenya.
i. Je, Serikali inatatua matatizo haya baada ya ufuatiliaji?
ii. Je, ni kwa nini Serikali isishirikiane na Balozi zetu zilizopo Nairobi, Kenya ili kujua changamoto zinazowakabili wavuvi hasa Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni, lenye kipengele (a) na (b), napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la matatizo yanayowakabili wavuvi wanaokwenda kuvua Pwani ya Kenya limekuwa likijirudia mara kwa mara. Hii inatokana na mwingiliano mkubwa wa wavuvi uliopo kutoka Tanzania na Kenya wanaouvua samaki kwenye Bahari ya Hindi. Wavuvi kutoka Pemba wamekuwa wakienda kuvua katika mwambao wa Bahari ya Hindi upande wa Kenya tangu mwaka 1960.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1976 yalifikiwa makubaliano kati ya Tanzania na Kenya ya kuruhusu wavuvi hao wanaokwenda kuvua nchi ya Kenya kwenda kuvua bila matatizo. Hata hivyo, kutokana na kujitokeza kwa changamoto za kiusalama na vitendo vya kigaidi, mamlaka za Kenya zimekuwa zikichukua hatua za kuwakamata mara kwa mara wavuvi siyo tu kutoka Tanzania, bali hata wale wanaotoka nchi za jirani. Ingawa wavuvi wa Tanzania wamekuwa wakikamatwa, huachiwa pindi mamlaka za Kenya zinapojiridhisha kwamba siyo tishio kwa usalama na kwa wavuvi hao na kama hao wavuvi wamefuata sheria na kanuni za nchi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni muhimu kwa wavuvi wa Tanzania wanaovua katika mwambao wa Bahari ya Hindi kuzingatia sheria zilizopo katika shughuli zao za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, napenda sasa kujibu maswali ya Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni lenye kipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Balozi zake ikiwemo ya Nairobi, Kenya, imekuwa na utamadumi wa kufuatilia matatizo wanayoyapata Watanzania wakiwa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na wavuvi wanaokwenda kuvua Pwani ya Kenya.
Aidha, Wizara inaendelea kufanya mawasiliano na wadau wote ikiwemo Serikali ya Kenya, Ubalozi, Wizara za Kisekta husika ili kufikia makubaliano ya kudumu katika eneo hili. Wakati suala hili likiwa linatafutiwa ufumbuzi, napenda kutoa wito kwa wavuvi wetu kufuata sheria na taratibu za nchi husika ili wasiweze kupatwa na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inafanya kazi kwa karibu sana Ubalozi wetu Nairobi kwa sababu ndiyo inayowakilisha Tanzania nchini Kenya. Kwa kupitia wawakilishi hawa, Serikali inahakikisha changamoto wanazopata wavuvi hao zinashughulikiwa ipasavyo. (Makofi)