Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba (38 total)

MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa jawabu zake. Kabla sijauliza masuala mawili muhimu ya nyongeza naomba ninukuu kidogo katika majibu yake pale aliposema kwamba; “madhumuni yetu ni kuwatambua kama Watanzania wenzetu, kuwapa huduma wanazo stahiki.”
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania hivi sasa kupitia Wizara hii ya Mambo ya Nchi za Nje, kuna deni ambalo linadaiwa na Hospitali ya London Bridge ambayo ni pounds za Kiingereza 79,567 ambazo zimetokana na Ubalozi wa Uingereza kwa Tanzania kuchukua dhamana ya matibabu ya mmoja kati ya Watanzania anayeitwa Nassoro Moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ndugu Nassoro Moyo aliondoka Zanzibar kama Mtanzania wa kawaida, alipofika London…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hafidh, naomba ufupishe kidogo swali lako tafadhali.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, nafupisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, alipofika pale, Ubalozi ukachukua dhamana ya kumpatia matibabu na bahati mbaya akafa. Hospitali inadai kiwango hicho cha pesa nilichokitaja, lakini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapeleka barua Zanzibar kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kulilipa deni hili kwa barua ya tarehe 17/08/2007 na barua nyingine ni ile ya tarehe 21 Januari, 2016.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Swali. Hivi SMZ kama hawakulipa kiwango hicho cha pesa kama walivyotakiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje watachukua hatua gani? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo inatambulikana nje ya Tanzania, je, Mheshimiwa Waziri ataondoa vipi aibu hii ya pesa ambazo zinadaiwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mtanzania aliyechukuliwa dhamana na Jamhuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, nia ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kutumia Balozi zetu zote zilizoko nje ni kuhakikisha usalama, haki za wananchi wetu walioko nje ya nchi zinalindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamana ambayo Ubalozi wa Uingereza uliochukua ni kuhakikisha tu kwamba mwananchi yule wa Tanzania ambaye yeye mwenyewe amekiri kwamba alikuwa ni Mtanzania, ni kuhakikisha kwanza usalama wake na analindwa kwa kipindi kile. Kwa vile tu Mtanzania huyu alifariki, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikuombea hayo ila ilikuwa inajitahidi kulinda haki za Mtanzania yule.
Kuhusu suala la kwamba deni lile limeletwa kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikikataa kulipa deni lile Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itafanya nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua uwepo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inafanya kazi kwa karibu, inaheshimu taratibu na sheria. Jambo hili litaisha kwa usalama kabisa, nahikikisha hilo.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanavyokwenda katika nchi ya Zambia hasa katika Jimbo la Copperbelt wamekuwa wanakamatwa wakiwa stand na wanapelekwa gerezani bila kupelekwa Mahakamani. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hili kwa sababu kuna vijana wengi sana ambao wako magereza na hawajapelekwa Mahakamani mpaka sasa hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nalipokea na Wizara yangu pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani tutalifanyia kazi, ahsante.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Pamoja na hawa professional staff kutofanya kazi zinazopaswa katika Balozi zetu, mimi nilitaka kujua tu effectiveness ya commercial attaché wetu katika balozi hizo kwa sababu wako dormant. Kiujumla nataka kujua suala zima la utalii pamoja na uwekezaji katika kuongeza pato la Taifa na vilevile kuitangaza nchi linashughulikiwa vipi na Balozi zetu? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza za Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, amelisema kwa ujumla kwamba kama kuna watu wanapelekwa ambao siyo taaluma yao wanafanya hawafanyi kazi vizuri lakini vilevile amesema kwamba baadhi ya Maafisa huwa hawatekelezi kazi zao vizuri. Kama anavyojua hii ni Wizara mpya, sasa hivi kuna mpango wa kuwaangalia hawa Maafisa wote na kupima utendaji kazi wao na wale ambao wataonekana hawatekelezi kazi zao vizuri tutawarudisha na kuwapeleka wale ambao wanastahiki.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
La kwanza, kabla ya kuvunjika kwa uhusiano wetu na nchi ya Israel kulikuwa na miradi mingi ya kimaendeleo inatekelezwa, mfano Hospitali ya Bugando, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Soko la Kariakoo na miradi mingine mingi. Je, baada ya sasa kuwa tumerudisha uhusiano hali ya ushirikiano wa miaradi ya maendeleo ikoje?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kufungua Ubalozi kwenye nchi fulani inahitajika fedha nyingi sana kuendesha. Na ndiyo hali hiyo husababisha nchi kuwa na Balozi chache au nyingi. Sasa kwa sababu, sasa hivi tuna mwendaokasi wa kufungua Balozi mpya, Israel, Kuwait, Qatar na kadhalika. Je, uwezo wetu kama nchi kwa sasa unakidhi kufungua Balozi mpya kwenye nchi nyingi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza, kwamba kabla ya mahusiano yetu kuvunjika na watu wa Israel tulikuwa na miradi mingi sana ya kimaendeleo na akihusisha mradi wa Bugando na anasema sasa baada ya kufungua hali itakuwa vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana nimesisitiza nimesema kutokana na kwamba sasa hivi Sera za Kimataifa zimebadilika na Tanzania imeamua kubadilika. Na kwa sababu tunasisitiza Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi miradi hiyo ambayo ilikuwa imesimama wakati ule, ndiyo maana tunataka tuanzishe mahusiano haya kwa karibu ili kuweza kuendeleza miradi iliyokuwepo, lakini vilevile kufungua fursa mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika suala la pili ambalo Mheshimiwa Mbunge ana wasiwasi kwamba sasahivi kumekuwa na mazoea au mpango mkakati wa kufungua Balozi nyingi zaidi na ufunguzi wa Balozi unahitaji pesa nyingi. Na mimi nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyokuwa ninajibu wakati wa Bajeti kwamba Balozi hizi zitafunguliwa kutokana na uwepo wa pesa itakaokuwanao Serikali ya Tanzania. Sisi tunaelewa kwamba, ufunguzi wa Balozi ni gharama, lakini pia, gharama hiyo ya kufungua Balozi moja baada ya nyingine itategemea kwamba tutafaidika vipi katika ufunguzi wa Balozi hizo. Hatutafungua tu Balozi kwa sababu tunataka kufungua, lakini tutaangalia pia kwamba, tuna uwezo kiasi gani, kwa sababu pia ufunguzi wa Balozi unailetea faida Tanzania. Ahsante.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa spirit hiyo hiyo ambayo Serikali imeiona ya kuweka mahusiano na Israel kwenye masuala ya kiuchumi, Morocco nayo vilevile iko tayari kutaka kuisaidia Tanzania kwenye masuala ya diplomasia ya uchumi. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kushirikiana na Serikali ya Morocco; najua Ubalozi upo, lakini bado Ubalozi huu haujakomaa vizuri wakati wenzetu pale Morocco wako tayari kuisaidia nchi yetu kwenye masuala ya kiuchumi wakiwa na uwezo mkubwa sana kwenye masuala ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe kwamba Ubalozi wa Morocco upo na sijaelewa jinsi alivyoliweka kwamba haufanyi kazi vizuri, lakini labda pengine angetoa ufafanuzi zaidi. Lakini kwa vile nipo nitaonana nae anieleze kwamba, alikuwa na maana gani. Lakini kama kuna tatizo, sisi kama Wizara, tutalishughulikia na sisi tunajua kabisa kwamba tunafanya kazi vizuri na Morocco na kazi inasonga mbele.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema ni gharama kubwa na ni kweli ni gharama kubwa kufungua Ubalozi kamili. Na kwa kuwa, katika mahusiano ya kimataifa kuna kitu kinaitwa Honorary Consul, ambayo haina gharama zozote za kiuendeshaji. Je, sasa Serikali iko tayari kufungua Honorary Consul au Ofisi ya Uwakilishi wa Heshima huko Lubumbashi ili kusudi Tanzania iendelee kulinda maslahi yake ya kibiashara? Kwa kuwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo population kubwa inaishi Eastern Congo na ndio ambayo tunafanya nayo biashara katika Miji ya Lubumbashi, Kalemie, Likasi, Kolwezi, Kisangani mpaka maeneo ya Mbujimai.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kutoka Lubumbashi mpaka kufika Kinshasha kupata huduma ni umbali wa kilometa zinazidi 2,300; yaani mtu akitoka Dar-es-Salaam atafika Lubumbashi na aliyetoka Lubumbashi hajafika Kinshasa. Kwa hiyo, hili strategically ni eneo zuri kibiashara.
Je, Serikali iko tayari kufungua Honorary Consul?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama alivyosema kwamba, je, Serikali ya Tanzania iko tayari? Anajua kwamba, kuna gharama kubwa ya kufungua Ubalozi na anashauri kwamba kwa nini tusifungue Honorary Consul.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimhakikishie tu Mheshimiwa Cosato Chumi, wakati kipindi hiki cha session za Bunge zimeanza wakati huu wa bajeti Wizara yangu pamoja Wizara kama nne hivi tumekaa tukijadili suala la mahusiano yetu kati ya sisi na Congo na Kamati zinaendelea kukaa na hili ni moja ya ufunguzi ambao tumeliwekea mkakati. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, tunajua kwamba Lubumbashi pamoja na Kinshasa ni sehemu mbali tofauti kabisa, lakini tuna wafanyabiashara wengi sana ambao wanakwenda Congo na wanafanya biashara vizuri, ila wanapata tatizo la coordination. Hilo tumeliona na kazi inaendelea kufanyika.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa suala hili linahusu masuala ya Balozi; na kwa kuwa katika nchi yetu tuna Mabalozi wa CCM ambao wanafanya kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo, na pia kusuluhisha migogoro ambayo inajitokeza maeneo ya vijijini; je, Serikali iko tayari kuwasaidia Mabalozi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu nitoe maelezo ya kushauri tu kwamba Mabalozi ninaowazungumzia mimi ni Mabalozi wa Mambo ya Nje. Lakini labda Mheshimiwa Kangi Lugola amewahusianisha hawa Mabalozi wa Mambo ya Nje kwa sababu ya mchanganyiko uliotolewa na Kambi ya Upinzani, kuwafananisha Mabalozi wa Mambo ya Nje na Mabalozi wa Nyumba Kumi Kumi. Lakini nimhakikishie tu kwamba sisi tunazungumzia Mabalozi wa Tanzania wanaotuwakilisha nje ya nchi na wanafanya kazi yao vizuri. Lakini vilevile najua kabisa kwamba, Mabalozi wa Nyumba Kumi Kumi walioko ndani ya Tanzania wanafanya kazi yao vizuri kuhakikisha kwamba masuala yanakaa salama.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pia, niipongeze Serikali kwa kuonesha baadhi ya mikakati yao inayoendelea nayo na ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali kupitia diplomasia yake ya kiuchumi nchini ina mkakati gani wa kuwashawishi wakulima wakubwa wa tumbaku nchini China waje kuingia ubia na wakulima wadogo wa tumbaku Mkoani Tabora, ili wakulima wa tumbaku Mkoani Tabora waweze kupata faida kubwa na yenye tija na kuona kilimo cha tumbaku sasa kinawasaidia, tofauti na hali ilivyo sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi nchini wamejiajiri kwenye biashara ya bodaboda, hususan Mkoa wangu wa Tabora ambao vijana wengi wanaoendesha bodaboda hizo zisizo zao, je, Serikali kupitia diplomasia yake ya uchumi nchini inaweza leo kunihakikishia hapa kwamba, itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha Mkoa wa Tabora unapata kiwanda cha pikipiki kutoka kwenye viwanda vikubwa kama SanLG, labda Boxer na viwanda vingine vyovyote vilivyopo China, ili kuweza kuwapatia vijana hawa pikipiki kwa bei nzuri, ili na sisi watu wa Mikoa ya Tabora, Katavi, Sumbawanga, Kanda ya Ziwa, tuweze kujikomboa kiuchumi kwa kupitia diplomasia hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Munde kwa kufanya kazi kubwa ya kuwatetea wananchi wa Tabora. Naomba niende kujibu maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo linahusu jinsi Wizara yangu inaweza kufanya mkakati gani wa kuweza kuwezesha wakulima wakubwa wa China kujakuwekeza na kufanya kazi pamoja na wakulima wadogo wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba Wizara yangu ilifanya mkakati huo, sisi kama Wizara ni Wizara kiunganishi, tumefanya mkakati na mkakati huo ni kuwahakikishia kwamba watu wa China wanaweza wakawekeza katika zao la tumbaku na nimwambie tu kwa hali sasahivi ilivyo ni kwamba Balozi wa China nchini Tanzania pamoja na Wizara ya Kilimo wako katika mkakati wa majadiliano wa kuweza kufikia makubaliano ya kujua zao la tumbaku na bei ya tumbaku itakuwaje na sisi tumeaachia wao kama Wizara kwasababu sisi kazi yetu ni kuhakikisha kujenga mahusiano mazuri. Tukishawaleta, wakifika nchini tunawapeleka katika Wizara husika. Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nikuhakikishie kwamba wakulima wa Tabora pamoja na wale wakulima wa China watafanya biashara hiyo ya tumbaku lakini baada ya mazungumzo na majadiliano yatakapokwisha kati ya Wizara ya Kilimo na Balozi wa China nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili la kuhusu bodaboda na kuhusu vijana wa bodaboda waliopo Tabora na Kanda ya Ziwa, nikuhakikishie si tu Tabora na Kanda ya Ziwa lakini kwa Tanzania. Nafikiri umeshawahi kusikia ndani ya Bunge hili Waziri wa Viwanda na Biashara amezungumzia kuhusu suala la watu wa china kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza bodaboda hapa Tanzania.
Kwa hiyo, biashara hiyo itakuwepo na watawezeshwa katika namna hiyo na kufundishwa pia jinsi ya kuendesha biashara ndogo ndogo kama ujasiriamali ili kusudi wasiwe tegemezi na waweze kutoka katika utegemezi na kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Munde kwamba sisi kama Wizara kwa kutumia diplomasia ya kiuchumi tutaendelea kupambania Tanzania iende katika kuhakikisha kwamba inatimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Tanzania inatoka katika hali ya kawaida na inakwenda katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, tutatumia diplomasia hiyo kwa kutumia Mabalozi wetu wote waliopo nje na wale waliopo Tanzania na kutumia vijana wetu na watumishi wetu wenye ujuzi na weledi uliostahiki katika kuhakikisha kwamba miradi hii na projects zote ambazo tunazikuta katika mikutano na sehemu mbalimbali zinaletwa Tanzania na kuwafaidisha na kunufaisha Watanzania kwa ujumla wake, ahsante. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru; Mheshimiwa Waziri dhana nzima ya diplomasia ya kiuchumi ni pana sana na hivi karibuni tumeona Tanzania inasita kusaini Mkataba wa EPA pamoja na Jumuiya ya Ulaya. Ni sababu zipi za kimsingi ambazo zinasabisha Tanzania iwe inasuasua, na muda mrefu Wabunge tumekuwa tukiuliza Serikali kwamba haijiandai ku-capitalize kwa fursa zinazotokea? Sasa Mheshimiwa Waziri unasema Serikali imejipanga, ni kwa nini hasa Serikali imekuwa ikisuasua pamoja na kwamba inaweza ikawa na sababu nzuri kusaini huu mkataba pamoja na Jumuiya za Ulaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu kwamba kama tunavyosema kwamba chochote sisi tunachokipigania kama Wizara na kama Serikali ni kwa manufaa ya nchi hii, ni kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, tumesema kwamba hatusaini kwa sababu mkataba ule kwa namna fulani jinsi ulivyokaa uta-affect maslahi ya Tanzania na hasa katika suala zima la kuhakikisha kwamba viwanda vinaweza kuendelea na wewe unajua kuhusu hilo. Kwa hiyo, hatusaini kwa sababu hizo. (Makofi)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini tulikuwa tunataka kujua mkakati gani Wizara inayo wa kuwafanya Wachina hawa kuhamisha teknolojia na viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali kutoka kwao kule kuanzishwa katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo katika Wizara yetu na nchi ya China ni kufanya makubaliano na kusaini makubaliano hayo ya kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi Tanzania na China.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ya msingi amezungumzia juu ya kuleta sheria hii kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia uzoefu wa nchini nyingine juu ya nyara hii muhimu. Swali langu ni kwamba, je, ni lini sheria hii italetwa hapa Bungeni ili iweze kufanyiwa marekebisho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwanyang’anya Diplomatic Passport watu ambao hawana tena sifa ya kuwa nazo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwamba ni lini sheria hii muhimu italetwa hapa Bungeni? Ni pale ambapo Taasisi husika zitakapomaliza kuirekebisha na kupitia process zote. Kwa sababu kurekebisha inahitaji wadau wazungumze, wajadili na ipitie katika Wizara mbili husika na kuwatumia wadau ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika moja kwa moja. Kwa hiyo, itakapokuwa tayari, italetwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili, kwamba tunachukua hatua gani kuwanyang’anya passport wale ambao hawastahili; pale ambapo wanapokuja kubadilisha zile passport, hawarudishiwi tena, wanapewa passport ambazo ni za kawaida kutokana na sheria. Huo ndiyo utaratibu ambao unafanyika.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu lakini ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kipindi cha mpito kilimalizika mwaka 2010 na kwa kuwa tathmini ya uhakika ilitakiwa ifanyike ili kuweza kujua changamoto zilizotokana na kutekeleza utaratibu wa kodi kupungua taratibu, je, ni lini Tanzania ilifanya tathmini ya uhakika kujua changamoto hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanda ya Ziwa, Mwanza, Tanga na Arusha kuna viwanda vingi ambavyo vimelazimika kufungwa kwa sababu ya ushindani wa bidhaa kutoka Kenya; viwanda kama vya mafuta ya kula, maziwa, sabuni na vinginevyo, siwezi kutaja vyote. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inasaidia viwanda hivyo kufufuliwa kwa sababu kufa kwake kumetokana na utekelezaji wa sera ambazo hazikufanyiwa tathmini na kuzirekebisha ili viwanda vyetu visiweze kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo anataka kujua kwamba ni lini tathmini hiyo ilifanywa baada ya kipindi kile cha mpito cha kuanzia 2005 mpaka 2009, niseme tu maelezo niliyotoa yanatokana na tathmini ambayo ilitolewa katika tathmini ya mwaka 2015. Ndiyo maana unakuta katika maelezo yangu nimesema mbinu mbalimbali zimefanyika ili kuweza kuboresha viwanda vyetu na kuhamasisha wafanyabiashara wafanye kazi yao vizuri, kwa hiyo tathmini ilifanyika.
Mheshimiwa Spika, vilevile amezungumzia suala la kuhusu viwanda ambavyo baada ya kuruhusu Ushuru wa Forodha kufutwa katika bidhaa hizo zilizokuwa katika kundi „B‟, biashara nyingi au viwanda vingi vya Mikoa kama ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Tanga, Mwanza, Rukwa na hata Arusha viliathirika na najua kabisa na yeye pia anajua kwa sababu katika thesis yake aliyoiandikia Ph.D ilikuwa juu ya hiyo.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kufanya mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya ufanyaji wa kazi katika viwanda na kuwajengea capacity. Kuna mikutano, semina na hata kuangalia vigezo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinafufuka.
Mheshimiwa Spika, mara zote hapa Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa akitoa mikakati mbalimbali ambayo Wizara yake inafanya ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wenye viwanda waweze kufufua viwanda vyao. Moja ya mikakati ni kuweza kutambua viwanda gani ambavyo vimekufa na nani anavyo au kuna viwanda gani ambavyo vimeathirika na tatizo hilo la mambo ya ushuru ili viweze kuwezeshwa na kuanza kufunguliwa upya.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba katika kipindi hicho cha 2009 mpaka 2010, viwanda vinavyozalisha bidhaa kama za saruji vilikuwa vimekufa, lakini kwa sasa hivi tunaona kwamba sehemu kubwa ya viwanda vinavyofanya vizuri ni pamoja viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za saruji pamoja na mafuta ya kupikia. Ahsante.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hiki ni kituo cha pamoja au cha ubia kama ambavyo ingepaswa kuonekana wazi wazi katika taasisi mbalimbali za Muungano. Swali langu linakuja, je, Naibu Waziri anaweza kutuambia pamoja na kueleza kwamba nafasi za ushindani kuna Wazanzibari wangapi walioajiriwa katika taasisi hiyo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba vituo hivi ni pamoja na kufanya biashara na biashara huwa na faida na hasara. Je, Zanzibar imewahi kupata mgao wake wa faida japo nyama ya sungura ya 4.5%?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba kuna Wazanzibari wangapi wameajiriwa katika kituo hicho nimekwisha sema kwamba kwa uelewa wangu mpaka sasa hivi sijaona kama kuna Mzanzibari ambaye ameajiriwa maana yake nimesema kwamba ajira zinatolewa na watu wanatakiwa kuchangamkia fursa hizo na kama wana uwezo na capacity na wanaofanyiwa interview wakishinda basi wataajiriwa. Lakini pia tunawahamasisha zinapotokea fursa na nafasi zinapotangazwa basi watu kutoka Zanzibar waombe nafasi hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala la pili ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliuliza kwamba kituo kinafanya biashara, je, Zanzibar imepata gawio kiasi gani katika miaka yote hiyo. Kama anavyofahamu kwamba kama hii ni taasisi ya Muungano tunajua kwamba gawio huwa linakwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa hiyo, kutokana na huo Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ujumla wake wanapata lile gawio kutokana na Sheria inavyotutaka. Ahsante.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, naomba kuongezea na hasa kile kipengele cha pili kuhusu gawio. AICC haijawahi kupata gawio na hivi sasa Joint Finance Commission na Ofisi ya Msajili wa Hazina wameunda kikosi kazi ambacho kitachambua na kukisaidia kile kituo ili kiweze kupata faida na kuleta gawio Serikalini kuanzia mwaka ujao wa fedha.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa majengo haya ya Arusha International Conference Center (AICC) yalikuwa yakitumiwa na Mahakama ya Kimataifa (ICTR) na kwa hivi sasa Mahakama hii ina majengo yake na imehama katika majengo haya ya AICC. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba heshima iliyokuwepo kwa majengo haya inaendelea kuwepo kwasababu hivi sasa wapangaji wakubwa hao wamekwishahama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwa swali lake la nyongeza kwamba Serikali tutahakikisha majengo haya yanasimamiwa vizuri na kuhakikisha hayaharibiki. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama jana Mheshimiwa Amina Mollel ulisikiliza vizuri kwenye taarifa ya Kamati ya Uwekezaji ya Mashirika ya Umma jana kituo kinafanya kila inachoweza kuhakikisha kinapata watu ambao wanaweza kuja kupanga katika ofisi zile na sisi kama Wizara tutahakikisha tunafuatilia hilo ili kuhakikisha majengo hayaharibiki na yanabaki katika kiwango kinachotakiwa.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: MheshimiwaNaibu Spika, ahsante sana. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa Jumuiya ya Ulaya katika mpango wake wa miaka mitano au kwa lugha nyepesi Multiannual Financial Framework waliahidi kuisaidia Tanzania Euro milioni 629, kwa kuwa hii inaendana na mpango wa Agenda For Change ina dalili ya kupungua misaada hiyo.
Je, kwa Tanzania misaada hiyo itatoka kama walivyoahidi au inapungua kwa kuzingatia sera yao ya ajenda ya mabadiliko?
Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa tunaandaa GSP,
Tanzania tumefanya uamuzi katika Bunge hili kwamba sasa EPA basi ikiwezekana, lakini sasa kwa uamuzi huo maana yake sasa tutafanya biashara ya kupitia GSP au DSP Plus.
Je, kulingana na hii ajenda ya mabadiliko tunajiandaaje sasa kuingia katika mlolongo huu?
NAIBU WAZIRI, MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuthibitisha au kusema kwamba ahadi ambayo ilifanywa na Jumuiya ya Ulaya ya kuahidi kuisaidia Tanzania Euro milioni 628 kwamba itabaki pale pale au itapungua au kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika vigezo ambavyo wao wameviweka kama framework ya kuweza kutoa misaada hiyo ni kuhakikisha kwamba nchi inaweza kuhakikisha inasimamia vizuri suala la la haki za binadamu na utawala bora, usawa wa jinsia, kuhakikisha kwamba vyama vya kiraia vinafanya kazi zake vizuri, kusimamia shughuli zinazofanywa na Serikali za Mitaa, kusimamia vizuri na kuhakikisha kwamba tunapambana na rushwa, kuhakikisha kwamba tunasimamia sera za usimamizi wa kodi na usimamizi wa sekta ya umma. Hivi vyote vinafanyika ndiyo maana unakuta kwamba mpaka sasa hivi hata World Bank wanaendelea kutupa misaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotakiwa kufanya
kama Watanzania ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuishi na kusimamia utawala bora na sekta ya umma inasimamiwa vizuri. Hilo ndiyo jibu langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba katika
Bunge hili liliamua kwamba suala la kusaini mkataba wa EPA sasa basi, kwa hiyo, sasa Tanzania inafanyaje. Tanzania imejipanga vizuri kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi kuhakikisha kwamba inahamasisha sekta binafsi ifanye kazi pamoja na Serikali. Vilevile inahamasisha mashirika ya nje na nchi nyingine za nje kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Wizara yangu imefanya kazi hiyo vizuri na mifano mmeiona. Vilevile kama nilivyosema kwamba diaspora tunaendelea kuwasimamia na kuwahamasisha katika Balozi zetu, Mabalozi wanafanya mikutano na hawa diaspora ili kuhakikisha kwamba wao pia wanatumia fursa ya kuwekeza katika nchi yetu. Katika mwelekeo huo tutakuwa tunalinda maslahi ya nchi yetu na siyo kuyapoteza.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na mlolongo mrefu ambao majibu yake yamepatikana, Watanzania tunaona aibu majengo yetu yaliyopo nje pindi tukitembelea Ofisi za Mabalozi. Kwa muonekano wa wazi kabisa ni kwamba bajeti hasa inayopangwa ambayo ameisema Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ni kwamba haikidhi haja na kutotolewa kwa wakati ile bajeti yenyewe iliyopangwa. Swali la kwanza, je, Wizara haioni umuhimu ya kuachia mapato ya viza au vyanzo vingine vya mapato vinavyopatikana katika Balozi zetu wakaachiwa wenyewe kule Ubalozini ili wakashughulikia suala la kuziimarisha Balozi zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la uchakavu wa ofisi na majengo ni la muda mrefu. Mimi siyo Mbunge wa kwanza na wala hili si Bunge la kwanza kuulizwa masuala haya kuhusu Balozi zetu, lakini inaoneka kama tunababaishwa sasa hatupewi uhalisia ni upi.
Je, ni lini Serikali itaacha ubabaifu wa majukumu yake ya majengo haya ambayo sasa inaonesha uchakavu ni endelevu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kuhusu Serikali kuachia ukusanyaji wa maduhuli kwa maana ya pesa zinazotokana na visa zitumike kule Ubalozini ili kufanya ukarabati katika Balozi zile zenye uchakavu wa majengo na kadhalika, nafikiri Mheshimiwa Mbunge pia ana uzoefu na Bunge hili linajua kwamba siku za nyuma maduhuli hayo yalikuwa yanaruhusiwa kutumika katika Balozi zetu. Hata hivyo, ilionekana kwamba zinapobakishwa pale baadhi ya Balozi zetu zilikuwa hazitumii vizuri maduhuli yale na utaratibu ule ukabadilishwa wakashauri urudishwe Serikalini.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi hatuwezi tukasema tunaweza tukaachia tu hivi hivi, suala hili sisi tulilipeleka tukalijadili na tumeona kwamba baadhi ya Balozi bado hazijawa na nidhamu ya matumizi mazuri ya maduhuli wanayokusanya katika Balozi husika. Lakini pale tutakapokuwa tumeona kwamba maduhuli au pesa wanazopelekewa wanatumia kwa utaratibu uliowekwa, basi sisi hatutasita kwa sababu tunachotaka ni kuhakikisha kwamba Balozi zetu zinakuwa katika hali nzuri na zinajenga taswira nzuri ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba Serikali iache ubabaishaji, nafikiri Serikali haifanyi ubabaishaji. Ndiyo maana tumesema pamoja na kwamba tunaweka bajeti ya maendeleo ili iweze kutatua tatizo na changamoto ya ukarabati wa majengo yetu ambayo ni machakavu lakini tumesema pia kwamba kuna mpango kazi ambao tumeweka kwa utaratibu kwamba majengo tuliyonayo mangapi na yapi yamechakaa zaidi na yapi yaanze kutengenezwa. Serikali hata siku moja haitakuwa inatumia ubabaishaji katika kutekeleza kazi zake. Hilo tunamhakikishia Mheshimiwa kwamba tutalitekeleza ipasavyo.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naibu Waziri ametaja miradi mingi veryambitious lakini ukweli ni kwamba kwenye Balozi zetu kuna ukata sana kiasi kwamba kuna Balozi zinawakilisha nchi kadhaa, mfano Balozi wa Malaysia anawakilisha mpaka Singapore na Brunei, wa Msumbiji nadhani mpaka Swaziland lakini wanashindwa kutembelea nchi wanazoziwakilisha kwa sababu ya ukata kiasi kwamba hata Ubalozi umekuwa sio deal tena.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amezungumzia tu infrastructure lakini hawajazungumzia hali za Mabalozi wenyewe na staff. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wanaboresha masuala ya kibajeti na kifedha kwenye Balozi zile ambazo zinawakilisha nchi kadhaa ili kutokuathiri mahusiano yetu ya kibalozi na zile nchi ambazo wanatakiwa hawa watu wakatuwakilishe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba mtu anapoteuliwa kwenye utumishi wa umma sio deal ni wajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kusema kwamba tutakarabati sehemu mbalimbali na tumeweka miradi mingi lakini inaonekana baadhi ya Balozi zinasimamia nchi nyingi sana na kwamba kuna ukata. Sisi kama Serikali mipango yetu inatokana na ukusanyaji wa mapato ya kodi zilizoko ndani ya nchi husika. Kama Wizara, bajeti yetu inapangwa kutokana na ukomo wa bajeti tunaopewa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tutakuwa tunahakikisha kwamba pesa tunazopewa na hata tunavyozigawa, hatugawi kwa aina moja kwa maana ya hela zinazofanana, inategemea Balozi anasimamia nchi ngapi na gharama za uendeshaji wa maisha katika nchi husika yakoje. Ndiyo maana unakuta katika mwaka huu wa fedha tumeanzisha Balozi nyingine sita ili kuhakikisha kwamba tunapunguza mzigo wa usimamizi wa Balozi kwa nchi husika.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumetoka katika siasa ya uchumi na tumeingia katika sera mpya ya demokrasia ya uchumi, naomba niuize kwamba Serikali imejipanga vipi katika kuandaa wataalam katika kuhakikisha hiyo dhana halisi ya kufikia hiyo demokrasia ya uchumi inafikiwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nauliza kutokana na hali mbaya za Balozi zetu ambazo kila mmoja anaelewa nadhani kwamba Balozi zetu hazipo katika hali nzuri, Serikali imejipanga vipi kupeleka bajeti na kuhakikisha kwamba bajeti hiyo inatosha kwa ajili kuhudumia Balozi ili waweze hasa hiyo mikakati kwa ajili ya kutekeleza hiyo diplomasia ya uchumi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu Wizara imejipangaje katika kuandaa wataalam ambao wataweza kutekeleza diplomasia ya uchumi; kama tulivyokuwa tumeeleza katika hotuba yetu ya bajeti, katika mpango wetu wa bajeti, katika kila Kitengo cha Wizara tumeweka sehemu ambayo inaangalia mafunzo ya watumishi wetu na katika kila kitengo inaangalia kwamba ina idadi ya watumishi wangapi na wangapi watatakiwa kwenda kwenye training na training hizo zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, mafunzo haya yanafanywa nje na ndani ya nchi. Kuna semina mbalimbali, wanahusishwa katika ushiriki wa Mikutano yetu ya Kimataifa, lakini vilevile wanapelekwa katika training ni za muda mrefu na zile za muda mfupi.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema katika utekelezaji wa diplomasia ya kiuchumi, haihusishi tu Wizara ya Mambo ya Nje, hili ni suala mtambuka, linagusa Wizara nyingine za kisekta na hata tunapojadili miradi ambayo imetafutwa kwa fursa kwa kupitia Wizara yetu, tunahusisha pia Wizara za kisekta na katika Wizara za kisekta tunatumia pia wataalam katika Wizara husika pamoja na Wizara yetu. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika suala la pili ambalo linahusu mkakati wa kusimamia na kuhakikisha kwamba bajeti iliyopangwa inakwenda; sisi kama Wizara tunajua kwamba tunawajibika, tunajua kuna watu ambao wanafanya kazi kwa ajili ya Serikali hii na kazi yetu kubwa kama Wizara ni kuhakikisha kwamba bajeti ambayo tumeiomba na imepitishwa katika Bunge hili inakwenda kwa wakati na tutakuwa tunaendelea kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, pia katika siku zijazo tutaendelea pia kuliomba Bunge hili kuhakikisha kwamba wanapitisha bajeti ambayo tunaiomba ili kuhakikisha kwamba tunatekeleza hii diplomasia ya uchumi kwa ukamilifu zaidi.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, anaweza kutueleza hapa kwamba kuna chuo chochote kile ambacho kinaendesha kozi ya ubobezi ya diplomasia ya kiuchumi hivi sasa? Kama hakipo, je, Serikali ipo tayari kutumia nafasi yake kushawishi specifically kuendesha kozi hizo bobezi katika kiwango cha Masters na Ph.D ili tupate hao watalaam wanaotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, vyuo vya ubobezi wa diplomasia viko vingi, lakini kama nilivyosema kwenye majibu ambayo niliongezea katika maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Ngwali, nimesema kwamba katika bajeti ya Wizara, katika vitengo vyetu tumepanga bajeti ya kuhakikisha kwamba hao watumishi wanapata mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu na mafunzo haya wanayapata kutoka kwenye Chuo cha Diplomasia, vilevile wanapata nje ya nchi ambako kuna mafunzo ambayo ni ya ubobezi pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Ally Saleh kwamba jambo hili Wizara inalitambua.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuangalia mpango wa kitaifa ambao ulikuwa umeweka vipaumbele 13 ambao ni National Adaptation Program of Action kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi Serikali iliweka vipaumbele 13 ambavyo vya kwanza vilihusu masuala ya maji pamoja na kilimo, lakini katika utekelezaji Serikali hela iliyopata imeweka katika ujengaji wa ukuta katika barabara ya Ocean Road na miundombinu mingine katika maeneo ya Dar-es-Salaam. Sasa Serikali haioni kwamba, inaruka vipaumbele vyake ambavyo iliviweka mwanzo na inakwamisha sasa kuhakikisha kwamba, nchi inakuwa na uwezo wa kuwa na uhakika wa suala zima la usalama wa chakula katika kuangalia hilo suala la vipaumbele?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni katika suala zima la NEMC ambalo lilichaguliwa na Makamu wa Rais, ili kuweza kupata hii ithibati. Imechukua sasa miaka mitano kupata hii accreditation na NEMC hawajaweza kupata. Tunavyopata pesa kupitia Multinational Implementation Entities Serikali inakatwa asilimia 10 na hizo taasisi kwa hiyo, NEMC ilivyopata hizo hela tulikatwa asilimia 10 kwa hiyo, inapunguza hela ambazo zingesaidia katika utekelezaji wa miradi ya kuweza kupunguza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali ina mkakati gani na lini hasa kwa sababu, NEMC imeshachukua miaka mitano, Serikali sasa ni lini itakamilisha mchakato mzima na kukamilisha vigezo vyote, ili hatimaye Serikali iweze kuwa inapata hela zake moja kwa moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, linahusu Serikali ilikuwa imeweka vipaumbele 13, lakini Serikali ikaamua kuchukua mradi ule wa Dar-es-Salaam kuhakikisha kwamba, wanaokoa fukwe zetu na kutekeleza shughuli zile ambazo zinahusu kutengeneza mifereji ya maji ya mvua na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, vipaumbele vyote ni muhimu, lakini pia tunaangalia katika vipaumbele vile, ukiacha pembeni kipaumbele ambacho tumeshaanza kukifanyia kazi, huwezi ukasema kwamba, hakina umuhimu kuliko hiyo ya kilimo. Hata hivyo, niseme tu kwamba, kama anavyojua katika ombi mradi huu una sehemu ya pili ambayo sasa hivi Serikali inaifanyia kazi. Suala la kusema kwamba labda NEMC imechukua muda mrefu, sasa miaka mitano kufanya process ya kupata usajili, ili iweze yenyewe moja kwa moja kuomba sehemu ya pili ya fedha hizi, kwa sababu najua kwamba ilikuwa inatakiwa iwe milioni kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Peneza kwamba tayari NEMC imeshapita vile vigezo vyote ambavyo vilikuwa vimewekwa na hivi karibuni itaanza sasa yenyewe. Itapata usajili na kuanza kuomba ile sehemu ya pili ya fedha ambazo zinatakiwa kuokoa mazingira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimwambie tu kwamba, NEMC baada ya kupata huu usajili itaanza sasa kuangalia hivi vipaumbele ambavyo yeye amevizungumzia; kuhusu mambo ya kilimo. Vile vile labda nimwambie kwamba licha ya Serikali kutumia Mfuko huu wa Adaptation Fund tuna Mifuko mingine ambayo pia inaangalia masuala ya kilimo na umwagiliaji. Kwa hiyo, labda nimhakikishie tu kwamba, baada ya NEMC kupewa usajili ambao tayari imeshapita katika vigezo vile, sasa hivi tunasubiri wapewe hiyo barua ya accreditation ili waweze kuianza hii process ya kuchukua hizi hela milioni tano.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bunge hili limenipa heshima ya kuwa mwakilishi katika Bunge hili la SADC, lakini mpaka hivi sasa sifikiri kama SADC inaeleweka sana kwenye umma wa Watanzania. Ili kuongeza uhalali wake.
Je, Waziri haoni sasa kuna haja ya kuijulisha SADC kwa umma zaidi kuliko ilivyo hivi sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine ni kwamba kwa kuwa fursa zilizopo ni nyingi mno na jana tulijadili sana suala la economic diplomacy ambayo siku zote ni two way na inataka uwe very aggressive katika kuikabili; fursa zilizopo ni nyingi sana.
Je, Serikali haioni kwamba sasa wakati umefika mkakati wa Watanzania kunasa fursa zilizoko SADC uwe wazi ili Watanzania wengi waweze kuzinasa fursa hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Ally Saleh kwamba wakati umefika wa kunadi fursa zilizoko katika Jumuiya hii ya SADC. Na sisi kama Wizara, kama mnavyojua kwamba tumeweka mkakati wa kutangaza na kutoa vipindi tofauti tofauti katika redio, tv, brochures, lakini pia tutaweka mkakati wa makusudi kwenda sehemu mbali zaidi kwa kuwaita wafanyabiashara na watu wa kawaida ili waweze kujua fursa zilizoko katika SADC.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Fursa ambazo Tanzania imezipata kupitia SADC ni sawa na ambavyo tunapata fursa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sambamba na mikoa mingine ambayo inazunguka nchi za Afrika Mashariki, Mkoa wa Kigoma na hususan Wilaya ya Kakonko, hatuna fursa ambazo tunazipata kwa kupakana na Burundi, matokeo yake Warundi wanateswa na kusumbuliwa katika Wilaya ya Kakonko na mwambao wote unaoambaa Wilaya zote za Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kupata maelezo ya Serikali, Burundi siyo sehemu ya Afrika Mashariki? Kama ni hivyo, kwa nini waendelee kuteswa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho, wiki iliyopita pia alisema kwamba kuna raia wa Burundi kama 300 wamepigwa sana, lakini mimi nimefuatilia suala hilo sijaliona. Kama kuna sababu zozote zinazoonesha kwamba labda Burundi wanawafanyia ndivyo sivyo Watanzania, ningepata tu ushahidi na tutafuatilia, kwa sababu, katika vikao vyetu vya Mabaraza ya Mawaziri yanapotokea mambo ambayo hayaendani na utaratibu wa kisheria, huwa tunakaa na kuyatatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mbunge aniletee taarifa hiyo, ili sisi kama Wizara tufuatilie. (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda sasa nchi za SADC ili kukuza fursa za uwekezaji na soko la pamoja zimeendesha mradi wa ku-harmonise au kuwianisha sera na sheria za nchi hizi ili kuweza kuvuna rasilimali hizi, lakini pia soko liwe la pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ya Tanzania imeshirikije kwenye mradi huu mpaka sasa? Tumefikia wapi? Maana bila ku-harmonise sheria zetu, soko hili haliwezi kuwa la pamoja na wala hatuwezi kuvuna rasilimali hizi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Nje, huwa tuna-co-ordinate na kuhamasisha Wizara za Kisekta ili zihakikishe kwamba sera au sheria ambazo zinatofautiana na sheria au sera zilizowekwa na jumuiya, ziwe zimekuwa harmonized na zoezi hili ni endelevu kwa sababu inategemea na matukio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa data zilizokamilika nitampa Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuelewa tulipofikia.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwanza Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba mchakato wa Katiba Mpya haujakamilika anakwenda kinyume na dhana ya Mheshimwa Rais ambapo amesema Katiba Mpya siyo kipaumbele chake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali sasa. Swali la kwanza, kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa na tumeona nchi nyingi zimefaidika kwa kuwatumia raia wake walioko nje kwa kuwapatia hadhi ya kuwa na uraia wa nchi mbili.
Je, Serikali haioni kwamba tunapoteza fursa muhimu ambazo tunazipigania kwa raia wetu walioko nje ya nchi kuwa na uraia wa nchi yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amenijibu akisema kwamba Watanzania wenye nasaba watapewa hadhi maalum itakayowatambua lakini hivi karibuni zimetolewa kauli tata na Serikali za kuwavunja moyo na kuwatisha Watanzania walioko nje ya nchi kuhusu umiliki wa mali katika nchi yao ya Tanzania ikiwemo tishio la kuwanyang’anya ardhi na nyumba zao.
Je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kuwatoa hofu na wasiwasi huu uliotokana na kauli iliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba hatuzioni faida zinazoletwa na Diaspora wetu kama tutabadilisha na kuwapa uraia wa nchi mbili, sisi tunasema kwamba hawa watu kwanza hawapotezi haki yoyote. Kama tu watu ambao siyo raia wa Tanzania wanaruhusiwa kuwekeza Tanzania na kwa vile pia kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi sheria hairuhusu lakini bado watu hawa wanawekeza na ndiyo maana sisi kama Wizara tunawahamasisha na tutaendelea kuwahamasisha na kuwajulisha fursa mbalimbali tulizonazo katika nchi hii ili watumie fursa hizo kwa faida yao na familia zao hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba hivi karibuni Serikali au Tanzania imewavunja moyo wale Diaspora walioko nje kwa kuwanyang’anya ardhi, nafikiri nimeshasema na sheria zinasema wazi mwenye kuweza kumiliki ardhi Tanzania ni Mtanzania, ni raia wa Tanzania kwa sheria zilizoko hapa nchini lakini hawanyang’anywi ardhi kama wao ni raia wa Tanzania. Wako raia wa Tanzania ambao wanaishi nje ya nchi hii wanamiliki ardhi na wanaruhusiwa kuwekeza kama raia wengine wowote.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mipango inaendelea kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kufungua Ubalozi. Hata hivyo, tunaomba tu awaambie Watanzania hii mipango imefikia hatua gani ili na wao wapate confidence kwamba Ubalozi huu utafunguliwa karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa upande wa mashirikiano, Zanzibar inashirikiana kwa karibu sana na Cuba hasa katika nyanja ya afya na imekuwa ikipeleka wanafunzi mbalimbali kwa ajili ya masomo ya muda mfupi na mrefu. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuchelewa kufungua Balozi hii katika Mji wa Havana kunawapa maisha magumu wanafunzi wale kwa maana wanakuwa hawajui wanapopata matatizo wakimbilie wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Saada Mkuya akitaka kujua hatua iliyofikiwa kwa sasa hivi. Naweza kumwambia tu utaratibu wa mwanzo huwa tunafanya kutafiti kutengeneza gharama za kuanzisha Balozi, uanzishwe wapi, watu wangapi wapelekwe, lakini mwisho kabisa ni lazima tuwe tumejiandaa kwamba tuna pesa ya kutosha na imewekwa kwenye bajeti ndipo hapo Ubalozi unaweza ukafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa pia anajua kwamba tuna Balozi nyingine sita ambazo zimefunguliwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambazo bado tunataka tuhakikishe kwamba tumekamilisha mambo yote yanayohusiana na staffing, gharama za nyumba na uendeshaji. Hatuwezi tu tukafungua kwa sababu tumesema, tukishakuwa tumejiandaa tutaweza kusema ni lini. Hata hivyo, utaratibu wa kuangalia aina ya watu watakaopelekwa na gharama za uendeshaji zimekwishakamilika, tunasubiria kwanza zile ambazo zimepangwa zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili tunatambua kwamba mahusiano baina ya Tanzania na Cuba ni mazuri na Zanzibar kama yeye anavyojua kwamba ni sehemu pia ya Tanzania. Nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wanasoma kule Cuba kwa kozi za muda mrefu na mfupi watakuwa wanaendelea kusimamiwa na Balozi yetu ya Canada maana ndiyo wanaosimamia wanafunzi au wafanyakazi wote wa Tanzania walioko Cuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimwambie mahusiano hayo hayako mazuri tu kwa upande wa Zanzibar ni mazuri kwa Tanzania nzima. Kwa kumpa tu taarifa mwaka jana Manesi 16 pamoja na Madaktari kwa mkataba wa miaka miwili wa kutoka Cuba watakuwa wanafanya kazi katika Hospitali yetu ya Muhimbili na Waziri wa Afya yuko hapa anaweza kukiri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mahusiano mazuri kwenye suala la elimu, kuna Madaktari na Wataalam wa afya ambao wanatoa mihadhara katika vyuo vyetu vikuu. Kwa hiyo, nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wamepelekwa kutoka Zanzibar wataendelea kuhudumiwa na Balozi yetu ya Canada.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki katika kushirikiana katika masuala ya chakula na mifugo, waliipitisha mpango kazi wa usalama wa chakula, je, utekelezaji wa mpango huo umefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wakuu wa nchi pia katika kikao chao walitoa mapendekezo ya kuanzisha ufugaji wa kisasa katika nchi za Afrika Mashariki, je, utekelezaji wake umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango kazi wa chakula na utekelezaji wa usalama wa chakula katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulijadiliwa na wakuu wa nchi, kwa sasa hivi ni kwamba kwa utaratibu wa sheria na kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi husika zinachukua uzoefu na makubaliano waliokuwa wamefikia wakuu wa nchi ili kutekeleza lile waliokubaliana nalo. Nafikiri katika suala hili Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo Wizara ya kisekta inaweza kuwa na jibu sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ufugaji wa kisasa zimechukuliwa jitihada za makusudi za kuhamasisha wakulima na wafugaji hasa wa kuku ili kuweza kujifunza kutoka kwenye nchi hizi za Jumuiya kuweza kupata uzoefu wenzao wanafanyaje ili kuweza kuendeleza area hii ya ufugaji wa kisasa. Wafugaji hawa ni wafanyabiashara wanaweza kuwa wakubwa na wadogo na wameweza kuwa wamejifunza katika mikutano ile ya wafanyabiashara ambayo huwa inaitwa katika East African Council katika jumuiya ili kuweza kupeana uzoefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na mikutano hii wanaweza kujadili jinsi wenzao kwenye nchi zinazotoka kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyofanya basi na wao wanaweza kujifunza. Ninachoweza kusema kwamba Tanzania kama Tanzania wanafanya vizuri katika area hii ya ufugaji wa kisasa na hasa kuku.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninayo maswali mawili tu ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, na Serikali ina nia nzuri tu ya kuwasaidia vijana na kuwapatia ajira, lakini kuna baadhi ya waajiri bado wanateswa wafanyakazi hao na wananyang’anywa simu wanapofika, passport, wanafungiwa ndani, hawajui waende wapi. Je, Serikali, ina mkakati gani wa kuifuatilia na kulikomesha tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali inatuambia nini? Ni ubalozi upi ambao umefanikiwa kupambana na matatizo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema kuna baadhi ya waajiriwa huwa wakifika wananyang’anywa simu, passport, na kadhalika na kwamba Serikali ina mkakati gani juu ya kushughulikia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Balozi inapokuwa inapata taarifa za namna hiyo inachukua hatua na ninachokiomba tu kwa waajiriwa wote walioko katika nchi hizi za kiarabu, linapotokea tatizo kama hilo wataarifu Balozi, ndio maana tunasema wanapewa mikataba na mikataba ile inalinda haki zao, lakini pia inalinda wajibu wa mwajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kuhusu Ubalozi upi umefanikiwa kufanya hayo, balozi zote zinafanya kazi hizo. Cha muhimu ni kujua tu kama kuna changamoto au kuna kadhia yoyote wale waajiriwa wanatakiwa kutoa taarifa kwa Balozi husika. Wao wanafanya kazi na sisi tunaendelea kufuatilia kwamba, wanatekeleza kzi yao ipasavyo.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, tuhuma hizi zimekuwa zikijirudia mwaka hadi mwaka na kwa muda mrefu. Nchi nyingi duniani huwatumia watu wake kwenda kufanya kazi nje ya nchi ili kuingiza remitance, fedha za kigeni. Mfano India ni nchi ambayo inaongoza dunia kwa remitance, inaingiza dola za Kimarekani bilioni 69. Je, ni kwa nini sasa Serikali yangu isione umuhimu wa kuingia makubaliano na nchi hizi zinazohitaji wafanyakazi, ili kukuza sekta hii, kuwalinda na kuiboresha zaidi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba nchi nyingi zimeingia mikataba na nchi ambazo zinaajri watu ambao wanatoka nje ya nchi nyingine na kwamba, wanapata remitance. Kama nilivyowaambia kwamba, sisi tumeweka makubaliano, yani kuna mikataba kati ya sisi pamoja na nchi hizi za kiarabu kwa hiyo, mikataba ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu tuweke utaratibu wa kuzihusisha nchi nyingine, nadhani zaidi ya hizi nchi za kiarabu, tutafanya hivyo na tunaupokea ushauri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Ninaomba nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa kipindi kirefu tumekuwa sasa tukipokea hayo malalamiko ya namna Watanzania na baadhi ya wafanyakazi kutoka nchi nyingine za Afrika wanavyopata shida kule wanakokwenda kufanya kazi nje ya nchi zao. Huduma hii ya kuwaunganisha Watanzania na watafuta wafanyakazi nje ya nchi ya Tanzania inasimamiwa na Sheria ya Wakala wa Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa katikati, mwaka huu mwezi wa pili kwenda wa tatu, nilisimamisha huduma hizo kwa nchi nzima ya Tanzania ili kufanya ukaguzi wa kutosha wa kujiridhisha kama wakala hawa wanafanya kazi zao kwa kufuata sheria. Wanafahamu Watanzania wanaoenda kufanya kazi huko nje wanaishije, wana matatizo gani na nini kifanyike ili kuwaokoa kwenye kadhia wanayoipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliunda timu imefanya utafiti na matokeo hayo wameshaniletea. Tumegundua kwamba ziko fursa nyingi za ajira kule nje ya nchi yetu ya Tanzania kama vile Saudi Arabia, Qatar na nchi nyingine. Lakini aina ya ujuzi unaotakiwa kule nje kama tutajipanga vizuri ndani ya Serikali na ninalihakikishia Bunge lako tutaanza kufanya hivyo, tuna uwezo wa kuwapeleka Watanzania wengi kwa mikataba rasmi na wakarudisha mapato ya kutosha kwenye nchi yetu na wakapata ajira nje ya nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu; kule Saudi Arabia wanahitaji wafanyakazi takribani 2,000 wa ujuzi wa kati na ujuzi wa juu kwenye fani kama za marubani, madaktari, walimu, madereva na za kazi za namna hizo ambazo zina ujuzi.
Ninalihakikishia Bunge lako baada ya ripoti hii sasa tutajipanga sawasawa na Watanzania watapata ajira zenye staha nje ya nchi na watarudisha mapato ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni miaka 20 sasa toka pale ambapo Zanzibar ilitakiwa ijiondoe kwenye Jumuiya hii ya OIC. Zanzibar ilijiunga na Jumuiya ya OIC kwa maslahi ya kiuchumi na si siasa wala siyo dini kama vile wengine walitafsiri katika kipindi hicho. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, sasa kwa sababu Tanzania kwa miaka 20 imeshindwa kujiunga kama ilivyoahidi ipo tayari kutoa ruhusa kwamba Zanzibar ina haki ya kujiunga na taasisi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri ametaja miradi mingi na ameenda mbali lakini nataka kuona tu kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, anionyeshe kwa Ibara kwamba Zanzibar ina nafasi hii ndani ya Jumuiya za Kimataifa lakini yeye kazungumza masuala mengine ambapo na mimi nitaelekeza nguvu zangu huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kataja miradi hapa, miradi hii kwa bahati mbaya au nzuri yote imetekelezwa upande mmoja wa Kisiwa cha Unguja, si vibaya yote ni Zanzibar, lakini katika ahadi ambayo imekuwa ikiwekwa kila bajeti ni upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na bandari ya Mkoani Pemba. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze ni lini sasa bandari hii na huu uwanja wa ndege kupitia Jumuiya hizi za Kimataifa utakelezwa na itapanuliwa kama walivyoahidi? Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, anasema kwamba kwa miaka 20 Zanzibar imejiondoa katika kujiunga na ile Jumuiya ya Kiislam na kwamba sisi kama Tanzania iko tayari kuiruhusu Zanzibara kujiunga na taasisi hiyo? Jibu langu nasema bado liko vilevile kama lilivyojadiliwa katika Bunge hili katika siku za nyuma na maamuzi yaliyofanyika siku za nyuma kwamba kama ni faida bado Tanzania ikiwemo Zanzibar inaweza ikafaidika tu kwa mahusiano yaliko baina yetu na nchi ambazo ni wanachama katika Jumuiya hiyo hiyo ya Kiislam.
Mheshimiwa Spika, kama anavyojua kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala la dini tumesema kwamba si suala ambalo tunataka tulijadili au kujihusisha na kuweza kuweka utenganishi kati ya sehemu ya nchi na nchi nyingine. Kwa hiyo, bado msimamo uko pale pale kwamba sisi kama Tanzania hatujakubaliana kwamba Zanzibar ijiunge na taasisi hiyo. Hata hivyo, faida za taasisi hiyo bado tunaweza kufaidika nazo kwa kufanya mikataba baina sisi kama Tanzania au upande wa Zanzibar kushirikiana na nchi hiyo kwa kufanya bilaterals. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niulize swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri kumekuwa na malalamiko nafasi nyingi za Balozi Wazanzibari wengi wanapelekwa nchi za Kiarabu. Je, kama malalamiko haya ni kweli hamuoni kama sasa kuna umuhimu wa kufanya uwiano sawa ili Wazanzibari wengi wasipelekwe nchi za Kiarabu nao wapelekwe nchi hizi nyingine kama Marekani, Ulaya na kwingineko?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, anasema kwa siku nyingi sana wamekuwa wakilalamika kwamba Watanzania ambao wanatoka Zanzibar wanapoteuliwa kuwa Mabalozi wanapelekwa kwenye nchi za Kiarabu zaidi. Naomba niweke taarifa hii sawa kwamba tunapowateua Mabalozi tunawateua kwa kigezo cha weledi, ufahamu wao na uwezo wao wa kushika nafasi hiyo ya kiubalozi. Tunapowateua kuwapeleka mahali popote iwe ni kwenye nchi za Kiarabu, Afrika, Ulaya au Latin America wako sawa kabisa kwa status.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu siyo tu kwamba katika hizi nchi za Kiarabu wako Watanzania ambao wanatoka Zanzibar yaani Mabolozi ambao wanatoka Zanzibar tu wapo pia wameteuliwa na wamekwenda huko wanatoka pia Tanzania Bara. Naomba hisia hizo za kusema kwamba tunawapeleka Mabalozi kwenye nchi za Kiarabu wale tu ambao wanaotoka Zanzibar zitolewe.
Mheshimiwa Spika, vilevile niseme tu kwamba sisi tunapowapeleka Mabalozi mahali popote iwe nchi za Kiarabu, tunaangalia pia additional value ambayo anaweza akaifanya. Sisi tunapowapima wale ambao pengine wanatoka Zanzibar au Bara tunajua kabisa kwamba kwa kufanya kazi kule watasimamia maslahi ya Taifa na maslahi wa nchi hii kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, wako Watanzania Mabalozi ambao wanatoka Tanzania Bara wameteuliwa hivi karibuni na wamekwenda kule. Nafasi hiyo itaendelea kufanywa hivyo na wale wanaotoka Zanzibar na wao ikifika wakati tunaweza tukawachukua tukawapeleka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hakuna upendeleo wala dharau kwamba wanapopelekwa kwenye nchi za Kiarabu maana yake kwamba tumewaonea na wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kuniona. Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu swali la msingi hapa alitaja Balozi, sasa nataka kujua Balozi zote za Tanzania duniani ziko ngapi na Zanzibar wamegaiwa ngapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, Balozi za Tanzania ziko 40 na Mabalozi wanaotoka Zanzibar wako tisa na hiyo ni asilimia 22.5 ya Mabalozi wote waliopo. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza majengo ambayo yatajengwa katika nchi mbalimbali na ukarabati ambao utafanyika katika nchi mbalimbali katika Balozi hizo. Hata hivyo, Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka kwamba katika jambo kubwa ambalo linatupa aibu nje ya nchi ni viwanja ambavyo tumepewa na wenzetu walioko nje na hasa nchini Uingereza ambapo imetishia usalama wetu na inaonekana kwamba sisi kama Watanzania hatukuwa na fadhila nzuri ya kupewa vile viwanja na tunatishiwa hata kupelekwa Mahakamani au kunyang’anywa viwanja vile ambavyo viko Uingereza na Sweden.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini Watanzania kuepukana na aibu hii ya viwanja tulivyopewa kule Uingereza ambavyo vimekuwa ni pori/kichaka na tunatishiwa kunyang’anywa sambambana majengo ya kule Sweden ambayo hayaendelezwi? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa suala zima la mikakati ya kibiashara, lakini moja ya mkakati mkubwa katika suala zima la biashara ni diplomasia ya kiuchumi (economic diplomacy). Hata hivyo, inaonekana Serikali haina mkakati na dhamira iliyo nzuri kuelekea kwenye economic diplomacy. Nini mkakati husika wa nchi ambazo amezitaja wa kuelekea kwenye diplomasia ya kiuchumi ili nchi yetu ipate manufaa zaidi? Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanja vyetu 11 vilivyoko nje ya nchi nimesema kwamba tumeweka mkakati na mkakati huu Mheshimiwa Masoud kama Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama anaufahamu. Mkakati huu ulianza mwaka 2002/2003 na ukaisha 2017. Katika jibu langu la msingi nimesema kwamba katika mkakati huo tumeainisha viwanja vyetu vyote na kuvitengenezea utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunavijenga ili kuweza kuweka vitega uchumi. Hilo ndiyo jibu langu kwa swali lako la kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili kwamba Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza diplomasia ya uchumi, nataka tu nimweleze kwamba moja ya majukumu makuu ya Mabalozi wetu tunapowateua kwenda nje ya nchi pamoja na watumishi ambao tunawapeleka katika Balozi zetu ni kuhakikisha kwamba wanatekeleza diplomasia ya uchumi kwa kuhakikisha kwanza wanajenga mahusiano mazuri baina yetu na nchi hizo zilizoko nje ya nchini lakini pili waweze kutangaza na kutafuta fursa mbalimbali za kijamii, kiuchumi na za uwekezaji na wanapimwa kwa mambo hayo ili kuhakikisha kwamba sisi tunafaidika na uwepo wao nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Abuja kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba iko katika mpango na tayari mazungumzo yanaendelea na Mheshimiwa Masoud anajua.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni hatua gani kali na za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wanaosafirisha vijana wa Kitanzania hususan vijana wa kike kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kufanya biashara isiyo rasmi ikiwemo kuuza miili yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni ipi sasa kauli ya Serikali dhidi ya madai ya kusikitisha sana kuwa baadhi ya Watanzania wanasafirishwa kwenda nje ya nchi kuuzwa figo zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Hawa Mchafu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hatua gani kali za kisheria zimechukuliwa kwa wafanyabiashara ambao wamewapeleka wasichana nje na kwenda kufanya biashara ya kuuza miili yao, kwa kweli niseme tu kwamba kama taarifa hiyo ikijulikana hatua za kisheria za nchi yetu zitachukuliwa. So far mimi sina data za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Watanzania ambao wamepelekwa nje na kwamba figo zinachukuliwa pia hiyo tutaifuatilia ili kama kuna ukweli, basi hatua kali zitachukuliwa kwenye nchi husika.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika maelezo yake amekiri kwamba tatizo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara; na kwa kuwa katika maelezo yake amejiridhisha kwamba wavuvi kutoka Pemba wamekuwa wakivua katika mwambao wa Bahari ya Hindi upande wa Kenya kutoka mwaka 1960; na vilevile katika maelezo yake amejiridhisha kwamba mwaka 1976 Serikali ya Kenya na Tanzania ilifanya makubaliano juu ya wavuvi wa nchi hizi mbili:-
Je, ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi kukaa na Serikali ya Kenya kupitia mkataba ambao niliuwasilisha hapa Bungeni ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wavuvi hawa kabla hawajaenda kuvua katika bahari ya Kenya wamekuwa wakienda kukutana na Maofisa Uhamiaji, Fisheries pamoja na BMUs za sehemu ambazo wamekuwawakienda kuvua.
Je, ni kwa nini Serikali hii au ni kwa nini Serikali hii au Mheshimiwa Waziri asiwaambie wavuvi hawa leo ili wawe na matumaini kwamba tatizo hili litakuwa halijirudii tena mara kwa mara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema na kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, nimesema kwamba Serikali sasa imechukua hatua ya kuwasiliana na sekta husika ikiwemo Wizara za kisekta kwa maana ya upande wa Tanzania na upande wa Kenya na Balozi ikihusishwa ili kuweza kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto hiyo, siyo tu tunakaa, lakini pia katika kujadiliana ni pamoja na kupitia mkataba ule. Mkataba huu tunajua kwamba ulifanyika mwaka 1976 kabla ya kuvunjika kwa Umoja Jumuiya ya Afrika, kabla ya wa sasa hivi kuundwa upya. Ulikuwa ni wa zamani sana. Kwa hiyo, tumeona hii changamoto na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tumesema tumeanza mazungumzo baina ya wadau wote wanaohusika ikiwemo Serikali ya Kenya, Tanzania kwa maana ya Wizara za Kisekta pamoja na Ubalozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba wavuvi hawa kabla hawajaenda kuvua katika upande ule wa Kenya huwa wanakutana na Maofisa Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wamekwenda kuwaona Maofisa Uhamiaji, nimesema kwenye jibu langu la msingi kwamba sisi kama Wizara na tukiwakilishwa na Ubalozi wetu, tunapokuta hawa wametendewa ndivyo sivyo, tunashughulikia jambo hilo. Ila tunawaasa wale ambao wanakwenda kule bila kutumia uratatibu wa kisheria; na ndiyo hao ambao kwa sehemu kubwa wanapata matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nawaasa kwamba sheria na kanuni zifuatwe kwa sababu suala la kushughulikia uvuvi, kwa maana ya uvunaji wa mazao ya uvuvi hasa samaki, ni masuala ambayo ni makubaliano kati ya nchi husika yaani nchi mbili Tanzania na Kenya. Na sisi tutaendelea kusimamia kuona haki inatendeka kama wavuvi wetu wamefuata utaratibu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wavuvi kupata matatizo katika nchi za nje, inaendana na tatizo hili ambalo liko ndani ya Jimbo langu la Mtambile katika Kijiji cha Likoni na Chole upande wa Shehia ya Mwambe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda wa miezi saba sasa wavuvi hao wako uko Pemba wamewekwa Gerezani, walifuata sheria na taratibu zote, lakini hadi leo wale ambao wanashughulikia wenzao ambao wako Gerezani wamefanya bidii kubwa ya kwenda katika Ubalozi wetu huko Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema nini na ina mkakati gani wa ziada kuhahakisha kwamba wale wavuvi wa Chole pamoja na Likoni wanaotendewa ndivyo sivyo wanapatiwa taratibu zilizo sahihi? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimniwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumetoka hapa, tukutane ili niweze kushughulikia hilo kwa karibu zaidi.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya wavuvi wa Pemba yanafanana na matatizo ya wavuvi wa maeneo mengine ya kKusini mwa Tanzania vikiwemo Visiwa vya Mafia na Mtwara. Matatizo ya wavuvi pia yanafanana na matatizo ya wafanyabiashara wa Tanzania hasa wa malori ambao wanakamatwa katika nchi ya Congo.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kulinda raia wake waliopo nje wanaopata matatizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama tulivyosema katika nchi ya DRC Congo tuna Ubalozi wetu na Mabalozi wetu kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba haki kwa ajili ya wananchi wa Tanzania walioko nje ya nchi inatekelezwa. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba watafanya kazi hiyo na huo ndiyo wajibu wao wa msingi, hatutawaacha na tumefanya hivyo siku zote.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu swali lake, alisema mazungumzo yamefanyika na Serikali ya Kenya. Namwomba tu Mheshimiwa Naibu Waziri, mazungumzo hayo yamefanyika Tanzania au Kenya? Yamefanyika lini na yatamalizika lini ili wananchi wetu wapate nusura ya kutokuhenyeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mazungumzo tunafanyia wapi, siwezi kueleza hapa kwamba tunafanyia wapi kwa sababu inategemea na sisi wenyewe tutakavyokuwa tumeamua. Nimesema mazungumzo yanaendelea kati ya Serikali hizi zote pamoja na Ubalozi baada ya kujua kwamba hili tatizo linafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu ni kuhakikisha kwamba changamoto hii inatatuliwa. Mimi kama Serikali nataka kumhakikishia kwamba mazungumzo yameshaanza, sisi kama Wizara tayari tumeshawaandikia Wizara ya kisekta ambayo inahusika na uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tayari tumeshakubaliana kwamba sisi kwa upande wetu pamoja na Ubalozi wetu na Ubalozi wa Kenya tutashughulikia hilo jambo. Sasa tunafanya wapi? Hayo ni maamuzi ya Serikali.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa swali la msingi linahusu matatizo yanayowapata Watanzania wakiwa nchi za nje; na ni kweli kwamba kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa, Watanzania wanakufa nje ya nchi, lakini unakuta wanaleta picha kwa mfano kutoka Marekani, watu wamekufa, watafutwe ndugu zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua Serikali ina kanzidata (database) ya Watanzania wanaoishi nje ili angalau pale wanapopata matatizo iwe rahisi kufuatilia? Vilevile hii itasaidia pia remittance ya kujua ni watu wangapi wanaishi nchi za nje?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Susan kwamba sisi katika Balozi zetu zote na sasa hivi zinafikia 40 kwa zile 35 za mwanzo, tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba kila Balozi anahamasisha wale diaspora wanaoishi katika nchi husika kuanzisha jumuiya ambazo zinatupa record za Watanzania wangapi wako huko na wanafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia hiyo diaspora tunaweza kujua kwamba huyu mtu yuko wapi na ni nani? Pale ambapo labda pengine Mtanzania ambaye yuko huku hajaweza kutoa taarifa zake kwenye Ubalozi ndipo tunapopata tatizo. Kule ambako tumeanzisha jumuiya na Watanzania ambao wamekwenda kutoa taarifa kwenye Ubalozi, tunakuwa tuna data zao.