Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ester Alexander Mahawe (19 total)

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa, fedha za own source hazitoshi wakati mwingine kulipa hata posho za Madiwani, ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Dongobesh ili kuondoa msururu mkubwa katika Hospitali ya Haydom kwa ajili ya wananchi wa Mbulu Mjini na Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupandisha Kituo cha Afya cha Dongobesh sisi hatuna matatizo, provided kwamba vigezo vimefikiwa. Ule mchakato Mheshimiwa Ester ninakuamini kwa sababu umenisaidia sana, hata Mzee pale alinisaidia sana, miongoni mwa watu walioshiriki nilivyokwenda katika Shule ya Kisimani pale katika Jiji la Arusha. Kwa hiyo najua ni mpiganaji na unapambana katika mambo mbalimbali. Na mchakato huu mkimaliza mchakato katika vikao vyenu, katika ule utaratibu wa kawaida, maana kuna hilo, lakini ukienda kwa Mheshimiwa Jitu Soni pale, kituo cha Afya cha Magugu na wao wanaomba ipandishwe ifike katika hadhi inayokusudiwa.
Naomba maombi haya sasa yaende pamoja Wizara ya Afya, yakifika Wizara ya Afya naamini Dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa sababu anajali sana haki na matatizo ya akina mama na watoto jambo hili ataliangalia kwa jicho la karibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya, vituo vya afya vinavyotaka vipandishwe viwe katika hadhi inayokusudiwa au katika zahanati kupandishwa kuwa vituo vya afya, provided kwamba vigezo zimefikiwa Serikali haitoshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, naomba niwasisitize kwamba vile vikao vya awali vikishakaa lazima mchakato uende kama unavyokusudiwa katika Wizara ya Afya na mwisho wa siku Serikali itafanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wananchi wake.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa eneo hili la Simanjiro na hasa eneo la Orkesumet ambako ametoa majibu Mheshimiwa Waziri kuhusiana na suala la maji katika eneo la Orkesumet limekuwa likiimbwa kuanzia mwaka 2005. Orkesumet ni eneo dogo tu tofauti na maeneo mengine ambayo yana shida kubwa ya maji. Lile ni eneo la wafugaji ambako akina mama wanatoka kwa saa zisizopungua nane kwenda kutafuta maji. Naomba kauli ya Serikali ni lini haidhuru wananchi wa Simanjiro katika Kata za Narakauo, Kimotorko, Emishie, Naberera, Kitwai, Lobosoiret watapata maji? Pia ni lini hasa mradi huo utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari awamu ya kwanza ya kusaini mkataba mazungumzo yamekamilika. Kwa hiyo, wakati wowote ule pengine kwenye mwezi wa saba, tutakuwa tumesaini mkataba wa awamu ya kwanza na kuanza hiyo kazi. Pia vijiji alivyovitaja, vyote vitapewa maji ikiwa ni pamoja na maji ya mifugo.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza linasema kwamba kuna uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya afya, hasa katika Mkoa wa Manyara kwenye zahanati na vituo vya afya. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha hilo nalo linatatuliwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili tuna upungufu wa dawa hususan Mkoa wa Manyara kwenye hospitali zake zote Je, Serikali ina mpango gani na hili maana afya za wananchi ziko hatiani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika suala zima la watumishi kama tunavyojua ni kwamba maeneo mbalimbali yanakabiliwa na uhaba wa watumishi, hii tumesema ni commitment ya Serikali. Kama nilivyosema katika jibu wakati namjibu Mbunge wa Handeni kwamba Serikali sasa hivi mchakato wa vibali ukikamilika vizuri katika Ofisi ya Utumishi, basi nadhani tutapeleka watumishi kwa kadri maeneo yote yanayowezekana, especially katika Mkoa wako wa Manyara Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, suala zima la upungufu wa dawa ni kweli na naomba kila Mbunge hapa a-pay attention ya kutosha. Nimepita katika Halmashauri mbalimbali Serikali tumeamua kutoa fedha za basket fund awamu mbili zimekamilika, hivi sasa tumeshapeleka fedha za basket fund katika awamu ya tatu, lakini kwa bahati mbaya sana miaka yote uki-track record fedha za basket fund ambayo inakuonesha one third lazima itumike katika kununua madawa na vifaa tiba katika Halmashauri zetu fedha hizo hazitumiki sawasawa.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengine utakuta fedha tumezipeleka lakini wakati natembelea juzi, fedha za awamu ya kwanza na fedha za awamu ya pili utafika katika Halmashauri bado fedha za basket fund kwa ajili ya ununuzi wa madawa na vifaa tiba hazijanunuliwa. Ndiyo maana tumetoa maelekezo kwa DMO wote wahakikishe kwamba fedha zilizopelekwa katika maeneo yao zinaenda kutatua matatizo ya wananchi kama tulivyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, hili nimhakikishie Mheshimiwa Ester, juzi nilikuwa naongea na Mkurugenzi wako kule wa eneo lile na kumwelekeza kwamba zile fedha aweze kununua na ameniambia ameshanunua dawa nyingine, lakini kuna dawa zingine bado anaziomba kutoka MSD, kuna dawa zingine ameambiwa hazipatikani na nimewaelekeza kwamba, wafanye utaratibu kuzipata dawa hizo lengo kubwa ni wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma. Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali na tunajitahidi kufanya kila liwezekanalo ili kuondoa hili tatizo la dawa nchini kote.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa muda mrefu sasa Halmashauri nyingi nchini zimekuwa zikipoteza mapato ambayo yamepotea kupitia kampuni mbalimbali za simu kwa kutokulipa hizo service levy katika maeneo mengi nchini.
Je, ni lini sasa Serikali itazibana kampuni hizo ili ziweze kulipa hiyo service levy?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na Halmashauri nyingi nchini kuwa na vyanzo vichache vya mapato. Je, ni lini Serikali itaweza kufanya mpango wa kuziongezea Capital Development Grants Halmashauri hizo nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MIKOA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ester kwa sababu najua kwamba anaguswa na Halmashauri zake zote ambazo anazisimamia katika mkoa wake. Naomba niwahakikishie kwamba ndiyo maana tumeandaa sheria hii ya fedha, mabadiliko ya Sura Namba 290 kwa lengo la kufanya utaratibu mzuri wa kukusanya hizi kodi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ester amezungumzia suala zima la minara ambalo lilikuwa linaleta mkanganyiko mkubwa sana. Katika jambo ambalo litashughulikiwa kwa undani zaidi ni suala zima la ushuru wa minara ambalo tunaliwekea utaratibu kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, nina imani ikifika hapa Bungeni, tutajadili tuone ni utaratibu gani tutafanya. Ninaamini na sheria itakuja siyo muda mrefu, tutaweka utaratibu mzuri ili tuweze kuwabana vizuri hawa wenye makampuni mbalimbali hasa ya simu, waweze kulipa kodi vizuri. Lengo kubwa ni kuziwezesha Halmashauri zetu ziweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika mchakato huu wote wa sheria hizi, lengo kubwa la Serikali ni kuziongezea Halmashauri zetu uwezo wa kupata mapato ya kutosha kwa ajili ya kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika suala zima la kujiendesha, kuongeza ile Capital Development Grand ni jukumu la Serikali. Ndiyo maana hata ukiachia hilo, ukiangalia ile Local Government Development Grants hata mwaka huu tumeongeza zaidi ya shilingi bilioni 251 kwa lengo tu la ku- facilitate Halmashauri ziweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, eneo hilo tutaangalia nini tufanye Halmashauri zetu ziweze kufanya vizuri tukijua kwamba Halmashauri zikifanya vizuri ndiyo nchi itaenda vizuri katika suala zima la maendeleo.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri baada ya kero hiyo kurekebishwa lakini bado driver guides wanapofika pale getini wanatakiwa kuandikisha majina ya wageni ambao wanawapeleka Ngorongoro ama Serengeti. Kwa hiyo, hilo nalo bado linaleta usumbufu mkubwa kwa sababu counter inayotumika katika uandikishwaji pamoja na ku-submit zile risiti ni moja. Je, Mamlaka haioni kwamba kuna ulazima sasa na umuhimu wa kuongeza madawati yale ya kutolea huduma hiyo ili kuokoa muda wa wageni unaopotea pale getini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa biashara yoyote inahitaji huduma bora kwa wateja yaani customer care na hili limeonekana likikosekana maeneo ya geti la Lodware na Naabi Hill. Je, Mamlaka haioni kwamba wafanyakazi wale wanahitaji kupatiwa indoor training ya mara kwa mara ili kuweza kufanya utalii wa ushindani na nchi jirani ambako customer care iko juu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa maswali mazuri ambayo Mheshimiwa Mahawe ameyauliza. Maswali haya ni relevance kabisa kwa kazi ambayo tunaifanya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la kuongeza madawati tumeliona na pale kwenye lango kuu kutoka Karatu unavyoingia Ngorongoro tumeongeza watendaji kazi kwa ajili ya kuwatambua watu ambao wanataka kuingia ndani ya hifadhi. Shughuli hii ni muhimu kwa sababu za usalama, lakini pia kwa sababu ya kuweza kukagua mapato tuliyokusanya na watu ambao wameingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda nimueleze Mheshimiwa Mahawe kwenye swali lake la pili kwamba ni kweli wafanyakazi wanahitaji kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ubora wao katika customer care, lakini pia katika kushirikisha na kutoa maelekezo kwa wageni. Kwa hiyo, shughuli hii tutaendelea kuifanya kila siku na tunategemea kwamba itaongeza ufanisi wa eneo hili.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika maeneo ya Mkoa wa Manyara hasa Wilaya ya Kiteto na Simanjiro katika Kata za Makame, Ndedo, Lolera kwa upande wa Kiteto na Kitwai, Naberera na vijiji vya Namalulu hali ni mbaya, ule ukanda ni wa wafugaji.
Naomba tu kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini sasa watu hawa wataweza kupata huduma hii ya mabwawa kwa ajili yao wenyewe pamoja na wanyama?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba tuelewane, suala la vijiji anavyovisema na hayo mabwawa anayoyasema tumetoa mwongozo. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge tushiriki katika kuweka vipaumbele katika wilaya zetu kulingana na bajeti ambazo tunaziweka kwamba mwaka huu tunapeleka maji katika vijiji kadhaa na mwaka unaofuata vijiji kadhaa. Pia tumesema kwamba kila Halmashauri iweke katika mapato ya ndani mipango ya kujenga mabwawa.
Kwa hiyo, mambo yote haya yanaibuliwa kwenye Wilaya na Halmashauri husika, ukiniuliza swali la nyongeza hapa nitakujibu kiujumla. Kwa hiyo, mimi nilifikiri ni vizuri sana tukashiriki kuibua miradi kwenye Wilaya ili hivyo vijiji anavyovisema viweze kuwekwa kwenye mipango.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu lilikuwa kuhusu ukosefu wa nyumba za polisi katika Mkoa wa Manyara ikiwemo Ofisi ya RPC. Ni lini sasa Serikali itaona kwamba kuna umuhimu wa Jeshi la Polisi kupatiwa nyumba ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba tunayo changamoto kubwa sana ya ukosefu wa nyumba za askari wetu, lakini katika mipango ya Wizara tumejiwekea utaratibu kwamba pindi pale bajeti itakaporuhusu tutahakikisha kwamba tunaifikia Mikoa yote ili kuwaondolea adha ya ukosefu wa nyumba watumishi wa Serikali hasa wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondolee hofu Mheshimiwa Mbunge bajeti ikikaa vizuri basi tutafikia katika maeneo yote katika kuondoa hadha hii.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba uniruhusu nimshukuru sana na kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kujenga ukuta katika eneo lote ambalo Tanzanite inachimbwa katika Mkoa wa Manyara hususan eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Job Ndugai ambaye alimua kwa dhati kabisa kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuchunguza upotevu wa fedha kupitia madini hayo ya Tanzanite yanayopatikana peke yake duniani eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonesha kumekuwa na upotevu wa pesa kwa sababu wageni wanaotoka nje wanaokuja kununua Tanzanite hawalipi VAT, lakini wazawa waliopo pale eneo la Simanjiro, ama Arusha na Manyara wao ndio wanaolipa VAT. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro unaohusiana na mitobozano hususan kwa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo la Mererani, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuzuia migogoro hiyo isiyo ya lazima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linalohusiana na VAT, kwa kawaida VAT huwa hatozwi mtu mgeni. Vilevile ni kweli kabisa kwamba katika mnada huu, wageni walikuwa wanunua Tanzanite kwenye mnada bila kutozwa VAT, lakini kwa wale wenyeji walikuwa wanatozwa VAT. Mfano ukienda sehemu nyingine ni kwamba VAT unatozwa kule unakonunua bidhaa, kisha unaenda kurudishiwa kwenye kituo cha ndege (airport).
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Serikali tunaangalia namna mpya ya kuhakikisha kwamba katika mnada ule, watu wote wanaonunua Tanzanite, sasa hivi tutaanza kuwatoza kodi ya VAT halafu mgeni aende akarudishiwe kule airport. Huo ndiyo msimamo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la pili, kuhusu mitobozano. Ni kwamba mitobozano ni mgogoro wa muda mrefu pale Mererani na kuna kamati nyingi zimeundwa kuhakikisha kwamba wanakwenda wanatatua tatizo la mitobozano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba sasa hivi Umoja wa Wachimbaji wa Tanzanite pale pale Mererani wameweka mkakati wa namna wa kutatua mgogoro wa mitobozano. Kuna mkakati wameutengeneza na wamekubaliana kwa pamoja. Kwa hiyo, mkakati huo, ambao tuna hakika kwamba tukiufuata na utataribu ambao wameuweka mgogoro wa mitobozano utakwisha. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Waziri amekiri kwamba kwa sasa Mfuko wa Barabara unatoa asilimia chache sana ambazo ni asilimia 30 kwa barabara za vijijini ambazo ni nyingi kuliko barabara zinazohudumiwa na TANROADS na TANROADS zinapata asilimia 70. Je, ni lini Waziri sasa ataleta mabadiliko ya sheria hii katika Bunge hili ili tuweze kunusuru barabara ambazo zinatumiwa na wananchi wengi ambao ni maskini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Waziri ameona suluhisho la kudumu ni kuanzisha Wakala wa Barabara zinazohudumiwa na Serikali za Mitaa kama ilivyo kwa TANROADS. Je, ni lini hasa Wakala huu utaanzishwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba ni kweli kwa mujibu wa sheria yetu ni kwamba asilimia 30 inaenda Halmashauri Serikali za Mitaa na asilimia 70 inaenda TANROADS, hili nadhani ni takwa la kisheria na siwezi kutoa commitment hapa leo kwamba ni lini sheria italetwa, kwa sababu jambo hili ni mpango mpana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Miundombinu ambayo ndiye mmiliki mkubwa wa sheria hii, tutaangalia jinsi gani tutafanya. Kama Watanzania tunajua jinsi gani tuna changamoto na ukifanya rejea katika mijadala mingi sana ya Wabunge jambo hili wamelijadili kwa kina. Kwa hiyo, Serikali tulichukue halafu tuone ni jinsi gani tutafanya, lengo kubwa ni wananchi wetu wapate huduma.
Mheshimwa Naibu Spika, Serikali za Mitaa zinafanya mikakati mingine mbadala ya kuhakikisha tunapata fedha nyingi sana. Ndiyo maana hata juzi nilikuwa nikipita katika mikoa mbalimbali kuangalia zile barabara ambazo TAMISEMI tunazihudumia kupitia fedha kutoka World Bank, ndiyo maana Miji yetu mikubwa yote ukianzia Arusha, Mbeya, Dodoma, Iringa na maeneo mengine tunajenga hizi barabara za Serikali za Mitaa kwa kutumia njia zingine mbadala, tuna source fund ili maeneo yetu yaweze kupitika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuanzisha Mfuko wa Barabara katika Serikali za Mitaa hili nimesema, mchakato sasa unaendelea katika ofisi yetu. Naamini wataalam wetu wa sheria watakamilisha zoezi hili na siyo muda mrefu inawezekana tuka-table kwa mara ya kwanza. Lengo kubwa ni kwamba, Wabunge tujadili kwa pamoja kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mlima Kilimanjaro ni kivutio kikubwa na kinachoingiza pesa za kigeni kwa kiwango kikubwa kama kilivyotajwa. Je, ni lini sasa Serikali itaboresha miundombinu ya upandwaji wa milima huo kama inavyofanyika katika nchi zingine za Brazil, kule Rio De Janeiro na Cape Town, South Africa kwa kutumia cable ili kuongeza mapato zaidi kupitia mlima huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Mahawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini tutaboresha miundombinu, tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu katika hifadhi zetu. Hili alilolipendekeza kuangalia uwezekano wa kuweka labda vitu kama cable car na vitu vinginevyo basi tutaliangalia kwa kadri bajeti itakavyoruhusu pale ambapo tunaweza kutekeleza ili liweze kuwavutia watalii wengi zaisi na kuweza kufanikisha hili jambo.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa ruzuku hii iliyotajwa hapa kila Halmashauri imejipangia namna gani itatumia hizo ruzuku na hakuna uniformity katika matumizi hayo, na kama ambavyo tulimaliza suala la upungufu wa madawati na maabara nchini, je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kutoa maagizo makali kidogo ili kumaliza suala hili la upungufu wa vyoo mashuleni?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wanaoteseka sana katika suala zima la upungufu wa vyoo nchini ni hasa mabinti walioko kwenye shule za sekondari. Kila mtu anafahamu wanapokuwa kwenye mzunguko ule kidogo wanapata taabu kulingana na ukosefu wa vyoo tena vyenye maji safi.
Je, ni lini sasa hususani katika Mkoa wetu wa Manyara Serikali itachukua hatua ya kumaliza tatizo hili hasa katika shule ya Komoto na Bagara Sekondari pale Babati Mjini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Ester Mahawe kwa swali la msingi pamoja na maswali yake ya nyongeza. Ni changamoto kubwa sana ambayo tunakabiliana nayo na yeye mwenyewe ni shahidi manake ni mdau katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyozungumza tumekuwa na mikakati mbalimbali kuhusu miundombinu mbalimbali hususani maabara na madarasa. Lakini kwa wakati huu ambao bado tunahangaika kumalizia ujenzi wa maabara hususani kumalizia maboma ya maabara na kuzipatia vifaa, na bado wananchi wanaendelea kuchangia; mimi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Mahawe aungane na sisi kwamba tutoe kwanza kipaumbele kwenye hizi fedha ambazo zimetengwa ili kusudi tuone zitafikia hatua gani wakati huo huo tunamalizia suala la maabara ili baadaye tuweze kuchukua hatua zaidi kama anavyopendekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu miundombinu ya maji katika shule zetu. Tumeshatoa maelekezo kwamba kila shule inapopanga ujenzi wa madarasa ni muhimu sana wakazingatia kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Hiyo ni miundombinu ambayo ni ya gharama nafuu badala ya kuwa na miradi ya maji ya kutumia vyanzo vingine ambavyo vinatumia fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hilo ni agizo lilishatolewa na maelekezo yalishatolewa. Inatakiwa sasa Wakurugenzi wa halmashauri zote pale ambapo shule inajengwa lazima kuwe na miundombinu ya maji ya mvua, ikiwa ni pamoja na shule ambazo amezitaja, baada tu ya kikao cha leo nitafuatilia kule Halmashauri ya Babati ili kusudi tuweze kujua hizo shule Mkurugenzi ana mpango gani kuzipatia huduma za maji. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wahenga wanasema samaki mkunje angali mbichi. Nakumbuka zamani tulikuwa tunajifunza masomo ya kilimo katika shule za msingi na sekondari nchini, lakini kwa bahati mbaya sana masomo hayo yakafutwa. Sasa labda tupate Kauli ya Wizara ya Elimu ni kwa nini masomo haya yalifutwa na tunategemea vijana baada ya kumaliza vyuo vikuu ndio wanaoweza kupata sasa ajira kupitia kilimo na ufugaji wakati hawakuandaliwa tangu mwanzo?
Swali la pili ambalo linasema ni maeneo gani hasa yaliyoandaliwa na yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo kwa ajili ya vijana hawa wanapohitimu masomo yao ya Vyuo Vikuu na kukosa ajira katika maeneo mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajibu swali la pili, la kwanza atajibu Mheshimiwa Waziri wa Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kama kuna maeneo ambayo yamekwishakutengwa kwa ajili ya shughuli hizi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 Novemba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya kikao na Wakuu wa Mikoa wote wa nchi nzima hapa Dodoma. Katika kikao hicho iliamuliwa kwamba kila Mkoa uende kutenga maeneo maalum ambayo tutayaita Youth Special Economic Zones, ni Ukanda Maalum wa Uchumi kwa ajili ya Vijana, lengo lake ni kuwafanya vijana hawa wahitimu na vijana wengine wote wa Kitanzania ambao wangependa kufanya shughuli ya ujasiriamali, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maeneo ili kupitia utaratibu huu waweze kupatiwa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa tayari Mikoa mingi imekwishatenga maeneo haya na zimekwishatengwa tayari ekari 85,000 nchi nzima kwa ajili ya shughuli za vijana.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Ester Mahawe, kuhusiana na Serikali kufuta masomo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali haijafuta masomo ya kilimo, masomo ya kilimo bado yanafundishwa shuleni na hata katika matokeo ya wanafunzi wanaoenda Kidato cha Tano ambayo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameyatangaza juzi wapo wanafunzi waliochaguliwwa kwenda kusoma combination zenye kilimo. Vilevile Serikali na Chuo Kikuu Maalum cha Kilimo cha Sokoine na Serikali ina mpango wa kuendelea kuimarisha masomo ya kilimo katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili katika vyuo vikuu kwa sababu tunatambua kwamba, kilimo ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)
MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu inapopangwa inahusisha wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza elimu yao ya msingi na sekondari na kwa kuwa wazazi wa hawa wanafunzi wanakuwa tayari wamechangia bajeti kuu ili kuweza kusomesha wanafunzi hawa kwa kupitia elimu bure. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuendelea kuondoa kodi na tozo ambazo sio lazima kwa wazazi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa moja ya malengo ya fedha za mitihani ni pamoja na kutafsiri mitihani kazi ambayo kimsingi ni jukumu la Baraza la Mitihani na siyo kwamba wazazi hawa wanaosomesha watoto katika shule ambazo sio za Serikali ni matajiri. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuondoa tozo hizo watapata nafasi ya wanafunzi wengine wengi kusajiliwa katika shule hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Mahawe, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuboresha mazingira ya wao kuwekeza katika elimu. Tutaendelea kuboresha mazingira yaliyopo ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niseme kwamba sekta binafasi wamekuwa walipaji wazuri wa kodi na wanatambua umuhimu wa kodi katika maendeleo ya Taifa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tupo tayari kujadiliana nao kuhusiana na namna ya kuweza kupunguza hizo kodi lakini bado tutaendelea kusisitiza kwamba ni vizuri wote tukashirikiana ili kuhakikisha kwamba baadhi ya gharama ambazo ni muhimu ziweze kulipwa na wale ambao wanaweza kuchangia. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Manyara ni mkoa mkubwa tu na una wilaya tano na majimbo saba na haiwezekani kuwapeleka wazee wote katika kituo kimoja tu kinachopatikana Magugu. Je, ni nini juhudi za Serikali katika kuhakikisha Wilaya ya Hanang’, Simanjiro, Kiteto na Mbulu tunapata kituo kingine cha wazee? Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ester Mahawe kwa kufuatilia maendeleo ya Manyara na Babati Mjini. Kwanza kwa mujibu wa Sera ya Wazee tunahamasisha wazee walelewe katika familia. Kwa hiyo Serikali haina mpango wa kujenga makazi ya wazee zaidi ya makao ya wazee 17 ambayo tunayo.
Mheshimiwa Spika, tunakusudia kutunga Sheria ya Wazee ambayo itatoa wajibu kwa watoto kutoa matunzo kwa wazee wao. Kwa sababu katika yale makambi kuna wazee wana watoto wao, wametelekezwa na familia zao. Kwa hiyo nitoe wito, niwausie Watanzania wazee hawa, wazazi wetu, wametulea, wamepigania nchi na sisi ni wajibu wetu kuwalea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na niwaambie hata Wabunge tukichukua mzee mmoja au wawili tukakaa nao kwenye familia zetu ni baraka kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Asilimia 90 ya wanariadha wanatokea Mkoa wa Manyara, lakini pia wapo wengi na taarifa iliyosomwa hapo na Naibu Waziri ni kuanzia miaka ya tisini kurudi nyuma, wapo wengi, akina John Yuda Msuri, Fabian Joseph, Andrew Sambu Sipe; wote hawa rekodi zao hazijavunjwa mpaka sasa kwa kuwa walikuwa wameshiriki mbio mbalimbali za kimataifa. Swali langu la msingi lilisema; ni lini utaratibu wa kuwaenzi wanariadha hawa utafanyiwa kazi sasa? Muda mfupi uliopita tulizungumza habari hapa na Waziri wa TAMISEMI alijibu suala la Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaofanya vizuri kuwa recognized na kupewa vyeti, habari gani kwa ajili ya wanariadha hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, amejibu hapa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba picha zao zitawekwa kwenye jumba la makumbusho, je, hiyo inatosha? Wapo wanariadha wengi ambao hali zao za kimaisha ni duni, naomba kujua wanafanyiwa lini mchakato wa kutambuliwa juhudi zao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya michezo. Nikianza na swali lake la kwanza, ni kweli kwamba sisi kama Wizara tunatambua kwamba wapo wanariadha wengi sana ambao wanatoka kwenye Mkoa wa Manyara kama ambavyo yeye mwenyewe amewataja, lakini sisi kama Serikali hatuwezi kuangalia tu mkoa mmoja, ni wanariadha wengi ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba sisi kama Serikali tunao mpango wa kuanzisha makumbusho rasmi kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua sasa hivi sisi kama Wizara tunayo ile kampeni yetu ya uzalendo ambayo kila mwaka tumekuwa tukiifanya na kitu ambacho tunafanya ni kuweza kuwaenzi watu mbalimbali ambao wameliletea heshima kubwa Taifa hili. Mwaka jana nakumbuka tulianza kwa wanamuziki lakini mwaka huu tutajipanga kuangalia namna gani ambavyo tunaweza tukawaenzi wanariadha wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pia niipongeze Serikali kwa kutuletea fedha hizo shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya unaoendelea hivi sasa, lakini pamoja na majibu haya mazuri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwanza kabisa kuna msongamano mkubwa bado katika Kituo hiki cha Afya cha Dongobesh kwa sababu ya huduma ambayo si nzuri sana kwenye zahanati zetu. Je, ni nini kauli ya Serikali wakati tukisubiri kukamilika kwa ujenzi ambao ndio kwanza umeanza wa Hospitali ya Wilaya ambao utapunguza msongamano kwenye kituo hicho cha afya kupeleka huduma ya vifaa tiba pamoja na watumishi kwenye zahanati zinazozunguka Kituo hiki cha Afya cha Dongobesh?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Tarafa ya Yaeda Chini haina kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itapeleka Kituo cha Afya katika tarafa ya Yaeda Chini ambayo mioundombinu yake migumu na huko ndiko wanakoishi wenzetu Wahadzabe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Mahawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tupokee pongezi za kutoka kwa Mheshimiwa Esther. Nilipata fursa ya kwenda Kituo cha Afya Dongobesh na pia nikapata fursa ya kushiriki kuzindua ujenzi wa Hospitali ya Dongobesh kwa maana ya Hospitali ya Wilaya. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mahawe pamoja na Mheshimiwa Flatey Massay kwa ushirikiano mkubwa pamoja na wananchi wao katika kuhakikisha kwamba, huduma za afya zinaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake anaongelea juu ya suala zima la kupeleka watumishi katika zahanati ili kusiwe na msongamano. Wewe ni shuhuda. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumepeleka maombi ya ajira elfu 15 kwa ajili ya watumishi wa Kada ya Afya kwa kadri kibali kitakavyopatikana, naomba nimhakikishie Mbunge na huko nako hatutawaacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anaongelea juu ya suala zima la kujenga Kituo cha Afya katika Tarafa ya jirani ambako wanaishi jamii ya Wahadzabe ambao wanauhitaji mkubwa. Naomba aendelee kuiamini Serikali tumeahidi tunatekeleza na naamini na yeye anaridhika na mwendo ambao tunaufanya katika kujenga vituo vya afya.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na jitihada za Serikali, bado maeneo mengi ya Mkoa wa Manyara yana tatizo kubwa la mtandao. Ukiacha upatikanaji wa sauti, lakini bado kuna shida kubwa katika upatikanaji wa internet, kwa hiyo shughuli nyingi za Serikali zikiwemo hospitali, shule na ofisi mbalimbali zinashindwa kufanyika ipasavyo kutokana na ukosefu huo wa mtandao. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha data zinaweza kupatikana katika Mkoa wa Manyara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni stendi ya Mji wa Babati ilihamia nje kidogo ya mji na tuna tatizo kubwa sana la mtandao katika stendi hiyo. Ni mtandao wa tigo peke yake ndiyo unaopatikana na kama tunavyofahamu shughuli zilizoko stendi ni nyingi na abiria ni wengi wanaotumia mitandao mbalimbali.

Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba mtandao unapatikana katika stendi ya Mji wa Babati na ni lini labda pia Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuona tatizo hili kubwa katika Mkoa mzima wa Manyara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ester Mahawe kwa jinsi anavyofuatilia Mkoa wake mzima suala la upatikanaji wa mawasiliano. Ni kweli kwamba maeneo mengi ambayo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulikuwa unatoa pesa kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano, walikuwa wanapeleka minara ambayo ina- supply 2G ambayo inahudumia voice na data kwa maana ya text peke yake lakini internet hakuna. Kuanzia tenda iliyotangazwa na kusainiwa Desemba, 2018, tulizielekeza kampuni zote kwamba sasa hivi kuanzia 2019 minara yote itakayojengwa iwe na access ya 3G ili wananchi wa maeneo hayo waweze kutumia data na mpaka sasa hivi minara inayoendelea kujengwa ambayo tunategemea itakamilika Juni, 2020, mingi sana itakuwa na huduma ya data kwa maana ya 3G, 4G na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili ni kweli kwamba stendi ya Babati ina mawasilino ya tigo peke yake. Niyashauri makampuni mbalimbali yanayotoa huduma za mawasiliano nchini yachukue nafasi hii kuona fursa ya kuweka minara hiyo katika maeneo ya stendi ya mabati kwa sababu kuna mkusanyiko mkubwa wa watu, kuna uchumi mwingi, kwa hiyo wakiweka mawasiliano pale itasaidia sana kuhakikisha kwamba wananchi wa Babati kwenye stendi pale wanaweza kupata huduma ya mawasiliano kutoka kwenye makampuni mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa mimi niko tayari kuongozana na tutatembea na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Manyara na Mheshimiwa Ester Mahawe kwa ruhusa yako. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake lakini nimfahamishe tu kwamba miaka mitatu iliyopita wananchi wa maeneo ya Mruki, Hangoni, Sinai pamoja na Kwere walizuiwa na Halmashauri kuendelea kuendeleza maeneo yao yaliyohisiwa kwamba ndiko barabara itakapopita wakiwa wamefanyiwa tathimini nakuhadiwa fidia. Je, kwa kauli ya Serikali sasa wananchi hawa wanaruhusiwa kuendelea na majukumu yao ya kuendeleza maeneo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa majibu ya Serikali pia hayajatoa time frame yaaani lini sasa upembuzi huo wa kina utakamilika. Je, Serikali iko tayari kusema ni lini upembuzi utaanza na kukamilika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge Mahawe kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo ya Babati na Manyara kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Halmashauri kuwazuia wananchi au kuwaelekeza wananchi kwa vyovyote vile haikuwa sahihi sana kwa sababu ilitakiwa Mamlaka inayohusika na ujenzi wa barabara ifanye hivyo. Kwa hiyo, niwaombe mahali popote kutakapokuwa na miradi ya barabara tusubiri kupata kauli ya Mamlaka halisi ili tusiweze kuwachanganya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya usanifu inaendelea sasa hivi kuanzia tarehe 01 Julai, 2019 kazi hiyo imeanza na wakati wowote tutapata inspection report, kwa maana ya report ya awali itakapokuwa imepatikana tutaweza kufanya sasa maamuzi, kwa sababu tutakuja na altenative kama tatu, halafu Serikali iamue tuende hatua ya mwisho sasa ya kukamilisha michoro pamoja na kuona kwamba tunapata gharama halisi za kuwafidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uvute subira kazi inaendelea na ninalishukuru sana Bunge lako limetupitishia fedha kwa ajili ya kazi hii ya usanifu wa hii barabara na kwamba kazi itaisha haraka sana, katika mwaka huu wa fedha kwa sababu fedha tunazo na kazi inaendelea itakamilika, gharama zitajulikana na wananchi tutawajulisha wale watakaopitiwa na mradi na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tuko pamoja hapa taarifa hizi za kuhusu wananchi ni wepi watapitiwa na mradi ili tuweze kuwalipa fidia tutaweza kuwasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Tarafa ya Bashnet iliyopo Babati Vijijini haina kituo cha afya hata kimoja na kilichopo kinatoa huduma sawasawa na zahanati. Je, ni lini Serikali itakumbuka Tarafa ya Bashnet? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto ya Mkoa wa Manyara kwa ujumla wake na ndiyo maana Serikali tulitoa 3.9 billion kwa ajili ya vituo vya afya vile vyote na tumetoa takribani shilingi bilioni 3 kwa ajili ya hospitali za wilaya. Lakini hata hivyo, nafahamu Babati Vijijini ina changamoto kubwa ndiyo maana tulianza na Kituo cha Afya cha pale Magugu na kituo cha afya kingine, lakini mwaka huu tumewapatia ujenzi wa hospitali ya wilaya katika bajeti ya mwaka huu ambayo nimeisoma si muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo hilo Mheshimiwa Mahawe alilolizungumza tutalichukua kulifanyia kazi, nini kifanyike kwa haraka kwa mpango wa Serikali kuwahudumia wananchi wa Babati Vijijini, tunafahamu wengine wanatoka mbali na huduma hizi ni huduma za msingi kuokoa maisha ya akina mama wajawazito. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mahawe naomba ondoa hofu, kama upiganaji wako ulivyo wa kawaida kwa Mkoa mzima wa Manyara, kilio chako kimesikika tutakifanyia kazi.