Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Charles Muhangwa Kitwanga (2 total)

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza.
Natambua kwamba chanzo cha maji Ihelele ndicho kinachopeleka maji katika Mji wa Shinyanga na Kahama; lakini tangu tumepewa ahadi ya kuwekewa maji katika vijiji hivyo mwaka 2008 maji hayatoki mpaka leo. Sasa Serikali ina mpango gani, maana wananchi wanasema kama hakuna mpango mkakati, tutaungana na mimi nitaungana nao kwenda kuzima mtambo wa maji wa kwenda Shinyanga. Nitawasindikiza wananchi kwenda kuzima.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais mwaka 2008 alitoa ahadi ambayo itahakikisha eneo lote la Ihelele linapata maji ya kutoka KASHWASA. Baada ya ahadi hiyo; na kwa kwa mujibu wa taratibu za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, tulianza kufanya utafiti na utafiti huo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba umekamilika. Ili kuweza kusambaza maji katika eneo lako la Ihelele tunahitaji shilingi bilioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika hii bajeti sasa ambayo tunaiandaa sasa hivi ya mwaka 2017/2018, basi tutaanza kutenga fedha ili kutekeleza sasa mradi wa kuwapatia wananchi maji Ihelele kutoka kwenye huo mradi wa KASHWASA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwa ahadi hii yeye na wananchi wake hamna haja ya kufunga yale maji kwa sababu tunawaletea maji.
MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna mradi mwingine ambao umekuwepo kwa muda mrefu sana; mradi wa kutoa maji katika Ziwa Victoria sehemu ya Butimba kupeleka Wilaya ya Ilemela, vilevile kuleta Usagara Wilaya ya Misungwi pamoja na Kisesa Wilaya ya Magu. Kumekuwa na muda mrefu sana tunaambiwa watasaini mkataba. Naomba basi nifahamu leo hii ni lini mkataba utasainiwa na mradi huo uanze haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli Mheshimiwa Kitwanga ni miongoni mwa Wabunge ambao ni wafuatiliaji ususani mambo yanayohusu wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Mheshimiwa Kitwanga sio mara moja analizunguzia hili jambo, nataka nimhakikishie serikali ya awamu ya tano ni serikali ya matokeo sio serikali ya mchakato. Na kwa kuwa sisi tupo karibu sana na Wizara Fedha nikuombe Mheshimiwa Mbunge nikuombe hebu tukutane leo ili tukae na wenzetu wa Wizara ya Fedha hili jambo tuweze kukalisha na wananchi wako waweze kupata huduma hii muhimu sana safi na salama.