Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Gimbi Dotto Masaba (11 total)

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa mpango au ahadi ya kuwapatia maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria wananchi wa Mkoa wa Simiyu uliahidiwa tangu mwaka 2005 katika Kampeni za Uchaguzi wa Rais wa Awamu ya Nne. Swali, je, ni lini Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaacha kuwachukulia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kana kwamba hawana kumbukumbu na ahadi zinazotolewa na Serikali yako?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali yako itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Habia lililoko Wilayani Itilima, Mkoani Simiyu uliosimama kwa muda mrefu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa inatekeleza ahadi zake kama tunavyoainisha kwenye utekelezaji. Anachokiongea ndugu yangu kwanza akubaliane na mimi kwamba tumeeleza kwenye jibu la msingi kwamba katika Mkoa wa Simiyu, tumekuwa na miradi kadhaa kila Wilaya katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya programu ya maji. Sasa huwezi kusema kwamba hakuna kilichofanyika, kuna kilichofanyika ila hitaji la maji ni kubwa zaidi na ndiyo maana Serikali sasa inakuja na mpango mkubwa wa kutoa maji kutoka kwa Ziwa Victoria ili wananchi wote wa Mkoa wa Simiyu wapate maji, hiyo ndiyo kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi unaenda kwa hatua hapa tumesema hatua ya kwanza lazima tufanye usanifu…
Ili tuweze kujua hitaji la kila mwananchi wa Simiyu ni kiasi gani kwa sababu maji ya kutoka Ziwa Victoria kwanza...
Kwa hiyo, lazima niwaahidi wananchi wa Simiyu kwamba Serikali itatekeleza ahadi yake ndani ya miaka mitano mradi huu utakuwa umekamilika. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa vile nchi yetu ina uhaba wa majengo ya shule, zahanati na vituo vya afya, je, Serikali iko tayari kumuagiza mkandarasi ambaye sasa hivi yuko site kujenga majengo ya kudumu ili baada ya mradi kukamilika majengo hayo yaweze kutumika kwa ajili ya matumizi ya shule, zahanati na vituo vya afya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara za Mkoa wa Simiyu zinaunganishwa na barabara za vumbi na kwa sasa hazipitiki kutokana na mvua zinazoendelea.
Je, Serikali iko tayari kutenga fedha kutoka kwenye Mfuko wa Barabara ili kuweza kutengeneza barabara hizo na ziweze kupitika kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mkandarasi aliyeko site mkataba wake ulishasainiwa. Hata hivyo, nawaagiza TANROADS Mkoa wa Simiyu waangalie uwezekano katika mkataba huo kama inaweza ikafanyika variation au kama kifungu hicho kipo wahakikishe majengo yanayojengwa na mkandarasi huyo yaweze kuangalia matumizi ya baadaye ambayo Mheshimiwa Mbunge ameomba. Kama itashindikana, Serikali itatafuta njia nyingine kupitia Wizara husika ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mfuko huo anaoungelea ndiyo tunaoutumia kujenga na kukarabati barabara zote nchi nzima. Naomba akubali mfumo tulio nao ndiyo huo, hatuna mfuko maalum kwa ajili ya barabara hii peke yake.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Pamoja na majibu ya Waziri katika majibu yake ya msingi amekiri kwamba Serikali inachukua hatua kuhakikisha kwamba wanatatua migogoro inayohusiana na wafugaji na hifadhi.
Sasa swali, Waziri utakuwa tayari kuongozana na mimi kuelekea Mkoani Simiyu kwenda kutatua migogoro inayoendelea katika vijiji vya Nyantugutu, Lumi na Longalombogo kwenda kutatua migogoro hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili wananchi wa Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Maswa wengi wao hawana maeneo ya kuchungia mifugo yao. Je, Serikali itakuwa tayari kurudisha Pori la Akiba la Maswa ili wananchi hawa waweze kutumia kama malisho, kwa sababu pori hilo limekosa sifa ya kuwa Hifadhi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu kama nitakuwa tayari kuandamana na yeye ndani ya Bunge hili kwenda kutatua migogoro, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba labda baada ya kikao cha leo tukutane nimshauri zaidi namna ya kutatua hili kwa sababu itabidi aongee na watu wa maliasili kwa sababu Wizara yetu hasa haihusiki na migogoro kati ya hifadhi na wananchi lakini nitamshauri namna ya kufanya hivyo na nitamshauri vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Pori la Akiba la Maswa kutolewa kwa ajili ya wafugaji nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi ni jirani yake, mimi natoka Ngorongoro nafahamu changamoto iliyopo kati ya wafugaji na pori la Maswa.
Mheshimiwa Spika, kuna mkakati ambao unaendelea sasa Serikalini kama ulivyosikia wiki iliyopita Waziri Mkuu alivyozungumza wa kuangalia namna ya kuondoa migogoro hii, vilevile kuangalia namna ya kutafuta ardhi kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kutafuta uwezekano wa baadhi ya maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya kihifadhi ili wafugaji waweze kugaiwa.
Mheshimwia Spika, hili linaendelea siwezi kusema moja kwa moja sasa kwamba, Pori la Maswa ni moja kati ya haya maeneo lakini kuna mipango ya kujadili suala kama hilo. Nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na migogoro hii kuongezeka lakini bado kama Taifa tuna jukumu la kuhifadhi wanyama, tunafahamu kwamba ni rasilimali muhimu, tusipohifadhi baada ya muda inawezekana tusiwe na wanyama pori ambao wanaendelea kuletea nchi yetu fedha za kigeni lakini vilevile sifa. Nashukuru sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mawazo kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama mtakuwa mmeangalia takwimu za sensa ya mwaka 2012 mtaona kabisa katika ile Sensa ya Watu na Makazi kwamba eneo la asilimia 10 la surface area ya Tanzania Bara limetengwa kwa ajili ya mifugo, eneo hilo bado halitumiki ipasavyo. Niseme tu kwa sababu muda mwenyewe ni mfupi kwamba Serikali haina mpango wa kuhuisha maeneo ya hifadhi kuwa maeneo ya kuchunga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka pia niseme kwamba wote kabla hatujawa Wabunge hapa baada ya kushinda uchaguzi tuliapa kiapo cha uaminifu cha kuilinda, kuihifadhi na kuitunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sehemu ya 27 ya Katiba hiyo inasema; kila mtu anao wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya Tarime Mjini yanafanana kabisa na Gereza la Bariadi Mjini, msongamano wa wafungwa. Naomba niulize kuwa Mheshimiwa Waziri alifika katika Gereza la Bariadi Mjini, hali halisi aliiona jinsi ambavyo wamesongamana hawa watu na Gereza hili linatumika kwa Wilaya zote tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga Gereza ambalo lina hadhi ya Kimkoa? Kwa sababu kesi nyingine zinasababishwa na Jeshi la Polisi kuwabambikizia watu kesi, wakiwemo Madiwani wa Wilaya ya Itilima, Wenyeviti wa Vijiji, Kiongozi Naibu Katibu Mkuu CHADEMA ambaye alishikiliwa takriban siku 12 bila sababu za msingi akiwa na vijana…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pendekezo ama ombi la Serikali kuangalia upya mazingira ya Gereza la Bariadi, nami nilifika, kuna mambo ya kufanyia kazi pale na sisi kama Wizara tume-earmark kwamba kuna jambo la kufanyika ukianzia na nafasi yenyewe ya Gereza, lakini pia na ngome/kuta kwa ajili ya Gereza. Kwa hiyo, hilo tumelipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, sisi ni viongozi. Mimi nimetembelea Magereza, nimeongea na wafungwa na mahabusu. Wale watu ukifika katika mikoa yote nilikotembelea ni mmoja tu ambaye nilipomwuliza kama umefanya kosa ama hukufanya akasema nimefanya. Wengine wote ukiwasikiliza, kama una fursa ya kuwatoa, unaweza ukawatoa dakika hiyo hiyo, wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimekuja kupeleleza baada ya hapo, napeleleza mmoja mmoja; ukipeleleza mmoja mmoja utakuta makosa aliyofanya ni ya kupindukia. Kwa maana hiyo, tunapokuwa tunasemea kwa ujumla wake kwamba Polisi wanabambika kesi, nadhani tuwaamini kwamba wale ni Watanzania ambao wanafanya kazi kwa kiapo. Kama kuna jambo la mtu mmoja mmoja, hayo ndiyo kama viongozi tuyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kule Magerezani, chukueni muda Waheshimiwa Wabunge; ninyi ni viongozi, nendeni mkawasikilize. Ukiwasikiliza wote unaweza ukadhania Gereza hilo limeshika malaika, lakini ukifuatilia undani wake utaona mambo mabaya waliyoyafanya katika familia nyingine ambayo wanastahili kwa kweli kuwa katika maeneo hayo.
MHE.GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Serikali ipo tayari kufanya utafiti ili kubaini faidi na vitu muhimu vinavyohitajiaka katika suala zima la pombe hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa vile Tanzania inahitaji uchumi wa viwanda Serikali ipo tayari kuwapeleka wajasiriamali hawa China, Japan na Afrika Kusini ili kujifunza zaidi na waweze kutengeneza kitaalam zaidi kama ilivyo pombe ya konyagi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, faida za kinywaji hiki gongo zinafahamika. Wataalam wangu wana uwezo na faida za kinywaji hiki, tatizo letu ni usalama. Kwa hiyo, mimi nitawaelekeza wataalam wangu waje kwenye jimbo lako Mheshimiwa Mbunge kusudi wahakikishe kwamba kile kinywaji kama kinatengenezwa kitengenezwe salama.
Lakini kwenye jibu langu nilikuambia watu wengi wanaokunywa gongo hawapendi gongo wanapenda ile ladha yake. Sasa tutatafuta ladha tuwatengenezee kinywaji salama chenye radha ya gongo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwapeleka Watanzania kwenda China, nikimjibu Mheshimiwa Dotto napenda nitoe taarifa kwa Bunge lako Tukufu tarehe 7 mpaka 11 Disemba, 2016 nimewaalika watengeneza viwanda wote na wenye viwanda kwenye uwanja wa Sabasaba kusudi wawaoneshe Watanzania mitambo mbalimbali ambayo ni viwanda na namna ya kuitumia.
Kwa hiyo, badala ya kuwapeleka China, na Watanzania ni milioni 53 sina nauli ya kuwapeleka, njooni Sabasaba kila mtu uangalie kiwanda anachopenda, korosho, kahawa na kila kitu kitakuwa pale.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, wakati Serikali inahamasisha wadau na jamii kujenga viwanda hivi, je, Serikali inatoa kauli gani kwa viwanda ambavyo ilivianzisha na imevitekeleza, kama vile kiwanda cha Nasal Ginnery, Ngasamwa Ginnery, Rugulu Ginnery, Malampaka Ginnery na Solwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kukosekana kwa bei nzuri ya ng’ombe na wananchi wa Mkoa wa Simiyu kulazimika kusafirisha ng’ombe wao kupeleka Jiji la Dar es Salaam, je, Serikali inatoa kauli gani na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba wanajenga viwanda vya nyama kama alivyojibu kwenye swali lake la msingi, kwamba watajenga Bariadi na Itilima. Ni lini mkakati wa makusudi wa kuharakisha kujenga viwanda hivyo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la pili, sehemu ya Mkoa wa Simiyu ni maarufu kwa ufugaji wa ng’ombe na zao la pamba. Juzi Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Anthony Mtaka alikutana na wataalam wangu wa uwekezaji katika jitihada za kusaidiana kutafuta wawekezaji. Wawekezaji wanatafutwa, kwa hiyo, tunachofanya ni sekta binafsi itakayowekezwa kwa hiyo tunatafuta wawekezaji waje wawekeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali langu la pili nilikuomba Mheshimiwa Mbunge na wewe uingie kwenye boti hiyo hiyo ya kuwatafuta wawekezaji. Tunatafuta wawekezaji ili wawekeze, ndiyo namna ya kupata wawekezaji. Nitumie fursa hii, kuwashukuru Wabunge ambao mmekwenda maili moja zaidi na kuwatafuta wawekezaji, ambapo mimi kazi yangu ni kuwaondolea vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza, kwamba vipo viwanda ambavyo vilibinafsishwa, vipo viwanda ambavyo vimekwama, kauli ya Serikali ni kwamba wale waliokuwa na viwanda vile, walio vinunua au vya kwao wavirudishe katika shughuli vifanye kazi. Tunachofanya sasa chini ya Treasure Registrar Wizara yangu na Wizara za kisekta zinazohusika tunawafuata wale kuwashawishi kutumia nguvu zote ili warudi katika shughuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu viwanda vya pamba naomba niwatoe hofu watu wanaolima pamba, chini ya mkakati wa pamba mpaka mavazi tuna imani kwamba uzalishaji wa pamba kwa tija utalazimisha viwanda vile vifufuke kwa sababu the supply itakuwa nyingi na viwanda vitafanya kazi, tuwe na subira.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Waziri alivyosema kwamba usanifu wa majengo utakamilika mwezi Novemba 2017, swali langu linauliza, ni maeneo gani yaliyobainishwa kujengwa chuo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu, Serikali ina mpango gani kuwasaidia vijana wanaomaliza kidato cha nne wanaokosa sifa ya kuendelea na kidato cha tano? (Makof)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Mkoa cha Simiyu kinategemewa kujengwa eneo ambalo lipo umbali wa takribani kilometa tisa mpaka kumi ambapo kilikuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC), eneo linalojulikana kama Kinamhala, nashindwa kidogo kutamka jina hilo, lakini ni eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika swali lake la pili juu ya Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na hawajafanikiwa kidato cha tano. Kwanza ni kwamba tunavyo vyuo mbalimbali vinavyoweza kuchukua wanafunzi wa aina hiyo lakini vilevile Serikali kupitia mpango mpya wa ESPJ, mpango ambao unajipanga katika kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wetu wale waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na ngazi nyingine zote ili waweze kupata ujuzi kamili wa kuweza kujiajiri. Kwa hiyo, kuna fedha tumeshapata nyingi kabisa, niwafahamishe tu Waheshimiwa Wabunge, Waziri wangu ameshatoa maelekezo kuwa kutakuwa na semina kwenu ya kuwapitisha juu ya mpango huo ambao utakuwa na manufaa makubwa sana katika nchi yetu.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Watanzania zaidi ya asilimia 65 wanategemea kilimo cha mikono; na kwa kuwa kilimo kimechangia asilimia 29.1 sawa na dola za Kimarekani bilioni 13.74 kwenye pato la Taifa yaani GDP ya mwaka 2016/2017...
e, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa wa kuondoa kodi na tozo zote kwa zana za kilimo hasa matrekta pasipo kuwepo na ukomo kama ilivyo kwa sasa? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wengi Tanzania wana matamanio ya kupata matrekta kwa wingi, je, Serikali haioni kwamba inatakiwa ihamasishe kupata viwanda vya kuunganisha matrekta ili wananchi walio wengi waweze kuyanunua kwa wingi ili kuweza kuboresha kilimo cha kisasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu ni shahidi, katika kipindi cha mwaka huu wa 2017/2018 Serikali kwa kutambua umuhimu wa wakulima na mchango wao mkubwa kwenye pato la Taifa, iliondoa kodi na tozo mbalimbali ambazo zilikuwa zinamsumbua mkulima na hii ni dhamira njema ya Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa kodi hizi ni mchakato wa kisheria na Serikali ya Awamu ya Tano tumekuwa tukimsikia Mheshimiwa Rais wetu akisema, yuko tayari kabisa yeye na Serikali yake kuhakikisha kodi zote zile ambazo ni sumbufu kwa wakulima zinaondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza 2017/2018 kuondoa zaidi ya kodi 15 kwa wakulima wetu na tunaendelea na mchakato sasa wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018/2019. Dhamira ya Serikali ni njema tu tutaendelea kutekeleza hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kutoka kwenye ukomo huo, Serikali inatambua. Tuliweka ili kuangalia mazingira ya ufanyaji kazi, tunaendelea kulishughulikia na litakaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kuhusiana na viwanda vya kuunganisha matrekta, naamini Mheshimiwa Waziri wa Viwanda yuko hapa na amekuwa akisema vizuri. Tayari tuna kiwanda pale Kibaha cha kuunganisha matreta, tumeanza kutekeleza dhamira ya Serikali ili kuhakikisha kilimo chetu kinaongeza uchangiaji wake katika pato letu la Taifa na kuwawezesha Watanzania walio wengi katika shughuli hii muhimu kwa Taifa letu. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nami nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Kigoma Kaskazini linafanana kabisa na tatizo la wananchi wa Mkoa wa Simiyu kwa wakulima wa pamba. Katika Mkoa wa Simiyu kumezuka wadudu waharibifu wanaoharibu zao la pamba na mahindi na hitaji la dawa za wakulima hawa ni sawa na chupa milioni moja na laki nne, lakini mpaka sasa wakulima hawa wamepatiwa chupa 350 tu ni sawa na asilimia 25. (Makofi)
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwasaidia wakulima hawa ili kuhakikisha kwamba mazao hayo hayaharibiki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Gimbi Masaba kwa swali lake la kuhusu pamba pamoja na wakulima wa zao la pamba na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanatoka katika Mikoa inayolima pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa habari njema naomba niseme tu kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba zao la pamba ambalo mdudu wa kweleakwelea pamba mbegu zake zinaharibika. Serikali imeshatoa shilingi bilioni tatu tayari kuhakikisha kwamba mpango huu wa dharura na tatizo hili la dharura linafanyiwa kazi na vilevile shirika la FAO limeshatupatia US dollar milioni 250 kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niwahakikishie kabisa wakulima wa pamba kwamba tatizo hili litatatuliwa hivi karibuni. Ahsante. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi naomba niulize swali la nyongeza.
Wilaya ya Itilima iliyoko Mkoani Simiyu ni miongoni mwa Wilaya zilizoanzishwa mwaka wa fedha 2012/2013, lakini ninavyozungumza hivi Wilaya hiyo haina Kituo cha Polisi. Ni lini mkakati wa Serikali kuhakikisha Wilaya hiyo mpya inapata Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Wilaya ya Itilima ina changamoto hiyo, lakini kama ambavyo tunatambua maeneo mengine vilevile na tuna mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo, kama nilivyozungumza katika majibu yangu ya msingi na hili nalo tunalichukua, tunalijua na tutalifanyia kazi. Pale ambapo hali itakaporuhusu kituo kitajengwa katika Wilaya hiyo.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amekiri wazi kwamba Serikali ina mpango wa kuanzisha shule ya kidato cha tano na cha sita katika maeneo ya Mkula tofauti na maeneo yanayotumika kwenye majengo yaliyoachwa na Kampuni ya Group Sogesca.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; itambulike kuwa shule hii ambayo ameizungumzia kwamba ni ya kutwa iko kwenye mgogoro baina ya wananchi pamoja na Kampuni ya SK iliyoko mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu Mheshimiwa Waziri Mkuu anaujua. Alipokuja kwenye ziara tarehe 2 mwezi wa tatu mwaka wa jana aliukuta mgogoro huu wa wananchi, kwamba shule hii iko kwenye majengo ambayo yana mgogoro. Nataka kusikia kauli ya Serikali, Waziri Mkuu aliagiza kuwa majengo yale yarudi kwenye mikono ya wananchi ili shule ile iweze kuendelea vizuri. Sasa nataka kuuliza, nini kauli ya Serikali kuhusu shuke iliyoko kwenye majengo yenye mgogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kipaumbele cha Serikali ni masomo ya sanyansi. Mkoa wa Simiyu walimu wa masomo ya sayansi ni changamoto kubwa sana hususan shule iliyoko Wilayani Itirima, shule ya Mwarushu ina mwalimu mmoja tu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusikia sauti ya Serikali ni nini mkakati wa Serikali kupeleka walimu wa sayansi katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Dada yangu Gimbi Dotto, kumbe alikuwa anataka aniingize katika choo kisichokuwa na jinsia maalum, kwamba shule kumbe ina mgogoro halafu tuanzishe kidato cha tano na cha sita. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mgogoro lakini nadhani Naibu Waziri wa Ardhi atazungumzia hasa katika suala hili la mgogoro jinsi gani Serikali imejipanga mara baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoa maagizo; Serikali inayafanyia kazi hayo yote kwa pamoja na nikuhakikishie Mheshimiwa Gimbi kwa sababu najua wewe ni mpiganaji mpaka umeniletea walimu ambao walikuwa na matatizo katika eneo lako kule. Siku zote unaniletea taarifa ofisini kwangu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba tutashughulikia matatizo katika Mkoa huu wa Simiyu kwa kadri iwezekanavyo ili mambo ya elimu yaende vizuri. Kuhusu shule ambayo haina walimu wa sayansi, naomba tuseme kwamba katikati tulipeleka walimu wa sayansi lakini si kwamba tumeziba gap zote za walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunaendelea kupeleka walimu wa sayansi. Tutaichukulia hii shule ambayo unaisemea kuwa ni kipaumbele, tutafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kwamba tunapeleka walimu wa sayansi wa kutosha. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu vizuri. Kwa hiyo naomba uendelee na hizo juhudi zako nzuri za kuwawakilisha vizuri wananchi wako wa kule.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali dogo la nyongeza ambalo limeulizwa. Ninamshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye amejibu swali lake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimfahamishe Mbunge pengine wakati mwingine ni muhimu pale ambapo Serikali inachukua hatua tuwe tunaweza kuweka kumbukumbu zetu vizuri. Mgogoro huu anaouzungumzia tayari Serikali ilishaumaliza, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Lukuvi alishakwenda kule na yule Bwana alinyang’anywa title yake na Mheshimiwa Rais alishaifuta, kwa hiyo hakuna mgogoro pale na SK Investment si mmiliki tena wa eneo lile kwa sababu Serikali imeshafuta umiliki wake na ilitangazwa kwenye vyombo vya habari, naomba tuwe tunafuatilia vizuri ili tusiwe tunachanganya haya mambo. (Makofi)