Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. William Mganga Ngeleja (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwanza na mimi naungana na wenzangu kukupongeza sana kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba yao nzuri. Katika kuwapongeza pia nitawakumbusha baadhi ya mambo yanayohusu Jimbo langu la Sengerema lakini pia nitaomba maombi katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nina ombi langu la muda mrefu, naikumbusha Wizara, naamini watendaji wa Wizara pia wako hapa wanasikiliza. Wilaya ya Sengerema tuna Hospitali Teule ambayo kimsingi inamilikiwa na watu binafisi, ni Shirika la Kidini la Roman Catholic lakini ndiyo hiyo hiyo hospitali ambayo imekuwa ikisaidia wananchi wa Sengerema na maeneo mengine yanayozunguka eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nimekuwa nikikumbusha na leo nakumbusha tena kwa mara nyingine na naamini nitapata majibu sahihi leo kwamba formula inayotumika pale kutoa ruzuku ya Serikali ambao ni utataribu wa kawaida ina-base kwenye vitanda 150 lakini leo hii hospitali ile ina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa vitanda zaidi ya 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu liko Wizarani, naamini Katibu Mkuu yupo anaelewa, ambacho namuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati wanatoa majumuisho ya ufafanuzi wa hoja zao kesho basi hoja hiyo ya ombi letu la Sengerema ambalo ni ombi la muda mrefu walitolee majibu. Hospitali ya Sengerema kwa kweli inasaidia Wilaya nyingi zilizoko upande wa Magharibi mwa Mkoa wa Mwanza, kwa hiyo, naomba nipate ufafanuzi kuhusu ongezeko la ruzuku kwenye Hospitali Teule ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walioshauri kwamba Bohari ya Dawa ifungue maduka yake katika kila Hospitali za Wilaya. Tunafahamu juhudi zinazofanywa katika Hospitali za Rufaa pamoja na Mikoa, lakini haitoshi. Inawezekana kabisa kwamba changamoto yake ni kwenye bajeti lakini kama nilivyoshauri wakati nachangia Ofisi ya Rais na kama Wabunge wengine walivyoshauri, mafungu haya bado hatujaridhia, eneo hili la huduma ya afya ni muhimu sana, usambazaji wa dawa ni mojawapo ya jambo muhimu sana katika uendelezaji wa Taifa letu. Tungependa kuona huduma hii inawasogelea zaidi wananchi hasa katika hospitali za Wilaya. Tuangalie namna ambavyo tunaweza kurekebisha bajeti zetu tukawezesha hii Bohari ya Dawa kupitia Wizara ya Afya tuwasogezee wananchi huduma katika kufungua maduka ya dawa katika hospitali zetu za Wilaya. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa nasoma hotuba ya Wizara, uko ukurasa umeelezea Hospitali za Kikanda hasa za rufaa, nadhani ukurasa wa 52, wameelezea mambo mengi. Nina ombi hapa, Taifa kwa muda wote limekuwa linajitahidi sana kujenga hospitali za rufaa kikanda kurahisisha huduma kwa kusaidiana na sekta binafisi na hasa masharika ya dini. Nafahamu zipo hospitali kubwa ambazo zina hadhi ya rufaa ambazo zinamilikiwa na makampuni ama mashirika binafisi. Hata hivyo, bado Serikali pia haijawahi kusimamia juhudi zake za kufungua hospitali kubwa za rufaa zinazomilikiwa na Serikali. Ombi langu kwa Wizara ya Afya izingatie na itafakari upya mwelekeo wa ufunguaji wa hospitali za rufaa. Ombi langu naloliweka mbele ya Bunge lako Tukufu ni ujenzi wa hospitali inayomilikiwa na Serikali yenye hadhi ya rufaa katika Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 52 hapa utaona zipo kanda ambazo zimeainishwa zingine zina mikoa miwili, sitaki kusema hizi zenye mikoa miwili zidharauliwe, hapana! Ninachotaka kusisitiza pamoja na kwamba Kanda ya Ziwa tuna hospitali inayoitwa Hospitali ya Bugando kwa kweli imezidiwa. Sisi tunaotoka kule tunafahamu huduma zilizoko pale sasa hivi, sitaki kuwabeza juhudi wanazozifanya wauguzi na madaktari waliopo pale, lakini kimsingi wamezidiwa. Hii ndiyo Kanda ambayo ina mikoa mingi zaidi lakini ina hospitali moja tu ya rufaa ambayo kwa kweli kwa mazingira tuliyo nayo sasa hivi haimudu na haikidhi! Huko nyuma tulishatoa ombi hili na tukaahidiwa kwamba Serikali ilikuwa inatafakari kujenga Hospitali ya Rufaa katika Kanda ya Ziwa. Tunaomba sana Serikali kupitia Wizara hii itafakari na baadaye mtupe maelekeo na matumaini tunakoelekea ni wapi. Uwezekano wa kujenga Hospitali ya Rufaa kwa Kanda ya Ziwa upo au haupo? Hilo ni jambo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kushauri na kwa kweli ni kwa kuzingatia hali halisi tu ilivyo ni kuhusu hizi huduma za wazee. Tunaona juhudi za Serikali zinafanyika, madawati ya wazee yamefunguliwa kwa kila Hospitali ya Wilaya lakini jambo hili linahitaji ufuatiliaji wa makini. Nashukuru mmesema sasa hivi kutakuwa na madawati ya kutoa taarifa lakini sisi tulioko site tunafahamu, kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby na Waheshimiwa wengine, kwa kweli madawati yale yamekuwa kama vile ya kutoa huduma za vipimo na kuandikiwa tu ambacho wewe kinakusibu maana wazee wakifika pale mara nyingi hawapati dawa. Naomba jambo hili tuliangalie kwa umakini na kwa macho mawili ili kuimarisha huduma za afya kwa wazee. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri sisi wote tuliopo hapa hata kama siyo wazee ni wazee watarajiwa tu, ndiyo nature ilivyo tutafika hatua hiyo, kwa hiyo, naomba sana wazee wetu tuwazingatie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, naishukuru sana Wizara, Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ummy ameniahidi kwamba baada ya bajeti hii atafika Wilaya ya Sengerema, tunamkaribisha sana. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, miezi miwili iliyopita alikuwa Sengerema tunamshukuru sana kwa juhudi zake alizofanya. Tunaomba tena msichoke kuwazungukia wananchi kwa sababu kadri mnavyofika ndivyo mnavyoimarisha utoaji wa huduma zinazotakiwa katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaalia yaliyotokea mwaka 2015 na hatimaye kupitia wananchi wa Jimbo la Sengerema wakaendelea kuniamini na sasa naungana na timu ya kikosi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea maeneo matatu; la kwanza, nina masuala yangu ya Jimbo ambayo naamini Serikali kupitia Mawaziri husika wanaendela kuyafanyia kazi. Pia nitatoa ushauri kidogo na mwisho nitauzungumzia utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa kuunga mkono hotuba na mapendekezo ya bajeti yaliyoletwa hapa mbele yetu kupitia Mawaziri wawili hapa Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki na wasaidizi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hizi za Waheshimiwa Mawaziri hawa zimebeba mambo mengi sana; na kwa kadiri michango inavyoendelea inaonekana tu wazi ni dhahiri kwamba mambo mengi yamefanyika na kwenye mipango kuna mambo mengi yamepangwa kufanyika.
Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki, nafahamu ninyi mnawakilisha, lakini kuna mambo mnayoyasimamia ninyi yanaingiliana, ni maeneo mtambuka na maeneo mengine na sekta nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo nataka niikumbushe Serikali, pale Sengerema nina ombi langu la muda mrefu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Hospitali yetu teule iliyoko pale imezidiwa. Ruzuku inayotolewa pale haitoshi. Nimekuwa nikiomba na leo nakumbusha tena, ni mwaka wa tatu nakumbusha. Ile ruzuku ambayo iliyotumika kipindi kile wakati hospitali ilikuwa na vitanda 150, sasa ina zaidi ya vitanda 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ombi hili liendelee kufanyiwa kazi na ninaamini, nimeshazungumza na Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, naamini wako hapa wanaendelea kulifanyia kazi, lakini nasisitiza kwamba wananchi wa Sengerema wanahitaji kuona matokeo ya ombi letu yakifanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nikumbushe, tuna ombi letu pale Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini sasa limerudi kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu viongozi hawa wako mbele yetu, Mawaziri hawa walioko katika Ofisi ya Rais, naamini kwamba, wanalifahamu. Tuna ombi la kupandisha hadhi Mji wa Sengerema kutoka Mamlaka ya Mji hadi Halmashauri ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza ni kwamba ombi lile pia limebaki kuwa la muda mrefu. Limechukua miaka kadhaa lakini ahadi za Serikali zimekuwa zinafanyiwa kazi. Naomba nisisitize kwa mara nyingine kwamba wananchi wa Wilaya ya Sengerema wana hamu kubwa kuona Mji wa Sengerema unapandishwa hadhi kutoka Mamlaka ya Mji kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia hizi bajeti lakini tukitambua katikati yake zipo Halmashauri ambazo hivi karibuni zimegawanywa, kumezalishwa Halmashauri nyingine ndani ya iliyokuwa Halmashauri moja. Ombi langu la ujumla, siyo kwa Wilaya ya Sengerema tu ambapo tumepata pia Halmashauri ya Buchosa, naomba Serikali itafakari, ione namna ya kuziongezea bajeti, kwa sababu bajeti tuliyopitisha mwishoni, Halmashauri zote ambazo ndani yake kumetokea Halmashauri nyingine ikiwemo Halmashauri ya Sengerema na Halmashauri ya Buchosa, nimesikia pia Halmashauri ya Chalinze na nyingine. Hili ni ombi la ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu suala la madawati. Kwa hali ilivyo na kwa mahitaji ya madawati yanayohitajika katika nchi yetu ya Tanzania, Halmashauri zote kwa vigezo vya mapato vilivyopo sasa, siyo rahisi sana kuliweza hilo jambo. Tunaomba Serikali izidi kutafakari kwa siku zilizobaki hizi mpaka mwezi wa sita. Kama katika bajeti hii tunapokwenda kupitisha tunaweza kufanya adjustment katika baadhi ya maeneo, tuziwezeshe Halmashauri zetu kupata fedha za kutengeneza madawati ili tuongeze kasi ya kutengeneza madawati kwa kuhudumia wanafunzi ambao sisi tunawalea kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa Jimbo la Sengerema. Jimbo la Sengerema tunahitaji madawati 23,000 leo. Maana yake unazungumzia zaidi ya shilingi bilioni moja; kwa hakika hatuwezi kuzipata kwa miezi michache iliyobaki pamoja na juhudi ambazo zinaendelea. Sisemi kwamba wananchi wakae au Halmashauri na viongozi wa Mkoa wakae tu, lakini ninachosisitiza ni kuona ni namna gani ambapo sisi kama Bunge tunaweza kushirikiana kurekebisha bajeti iliyoko hapa ili tuokoe pia tatizo ambalo ni la Taifa na siyo tatizo la eneo moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nashauri kwamba tunapokwenda kuhitimisha mgawanyo wa mafungu huko mbele ya safari, tutafakari suala la kuwezesha upatikanaji wa madawati kwa kurekebisha bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi niko kwenye Kamati ya Sheria Ndogo. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ameliarifu Taifa habari njema sana, kwamba sasa wameongeza threshold ya Mamlaka ya Halmashauri kupitia vitengo vyao vya sheria kwa maana ya ile mikataba kwamba sasa Halmashauri zote zishughulikie mikataba yote isipokuwa inayozidi kuanzia shilingi bilioni moja na kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo hili tulipe uzito, tukiwezeshe kitengo cha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na hasa Wanasheria walioko katika Halmashauri zetu. Tunaofanya nao kazi, tunaona udhaifu ulioko pale, lakini wakati mwingine ni kwa sababu ya matatizo ya kibajeti. Kwa hiyo, ninachoshauri hapa ni kwamba bajeti yao tuiongeze kwa Kitengo cha Sheria kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili wanasheria walio kule kwenye Halmashauri zetu waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi. Siyo zaidi ya hapo tu, pia kuongeza ikama ya Watumishi katika Halmashauri zetu. Tukifanya hivyo tutafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa sana kuhusu utawala bora, lakini naungana na Watanzania walio wengi kuunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na Mheshimiwa Magufuli kwa sasa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliweka sawa Taifa letu. Historia inaonyesha, nchi zote duniani ambazo zimefanikiwa kupata maendeleo ya kasi, zimepitia vipindi vigumu lakini pia baadhi ya hatua zilizochukuliwa na viongozi wao wa kitaifa ni pamoja na hizi ambazo amechukua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nitatolea mfano wa nchi ya Singapore. Wote tunafahamu wanaofuatilia historia. Yule Waziri Mkuu wao wa kwanza aliyeiongoza ile nchi kwa miaka 31, yule Lee Kuan Yew aliongoza toka mwaka 1959 mpaka mwaka 1990. Mojawapo ya changamoto alizokutana nazo kipindi kile ni wakati ambapo walivunja muungano wao na nchi ya Malaysia wa mwaka 1965, ni muungano uliodumu kwa miaka miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuvunjika, Waziri Mkuu Yew alipata shida sana kutafakari nini kitafuatia, kwa sababu ni nchi ndogo ambayo ukubwa wake ni sawa sawa na nusu tu ya Jiji la London. Alijiuliza kwa sababu walikuwa hawajajiandaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazochukuliwa leo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa hili. Nazungumza haya bila kubeza na kwa namna yoyote ile bila kudharau kazi iliyofanywa na watangulizi wake.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba ni kengele ya kwanza hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya bila kubeza kazi iliyofanywa na watangulizi wa Mheshimiwa Rais wa Awamu Tano, lakini kwa hakika Taifa tulipokuwa tumefikia na sisi wote ni mashuhuda, Taifa hili linahitaji kuumbwa upya. Tunalifinyanga upya ili tusonge mbele kwa pamoja. Kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Singapore, Taifa hili linahitaji juhudi hizo. Waziri Mkuu wa Singapore yule baada ya ule muungano wa Malaysia kuvunjika, alijifungia wiki sita, akaenda Kisiwani kule akakata simu hakuwa na mawasiliano na Baraza lake la Mawaziri, hakuwa na mawasiliano na Wabunge wenzake, akasema yeye anajifungia kutafakari mustakabali wa Taifa lile.
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuapishwa, aliendesha hii nchi pamoja na Waziri Mkuu kama jeshi la mtu mmoja, akitafakari mustakabali wa Taifa hili. Hatua zinazochukuliwa leo zisitufanye sisi kama Taifa kutoka njia kuu. Tunafahamu hapa wapo watu wanalalamika kwamba hatua anazozichukua zinazidi kiwango, lakini fikiria yanayotokea! Soma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, yanayosemwa haya, ni nini kifanyike kudhibiti? Kwahiyo, naungana na wenzangu na ninawashawishi wenzangu kwamba tuungane pamoja kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia habari za wenzetu kusema Ibara ya 18 ya Katiba imevunjwa. Tuache kuwapotosha wananchi. Kinachosemwa kwenye Ibara ya 18 hapa, ni wananchi kupata kuwa na haki ya kupata taarifa, utaratibu umeandaliwa na Bunge hili. Kilichobadilika ni ratiba tu. Kwa nini tunang’ang’nia live? Kuna haki gani inayosemwa “live” katika Katiba yetu? Hakuna haki live inayooneshwa katika Katiba yetu. Kwa nini hawa wenzetu wanapiga kelele? Mambo mengine yanakatisha tamaa sana. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma ukurasa wa 17 wa taarifa ya wenzetu, wanasema Serikali isafishe mtandao wa ufisadi uliojengwa na Wakurugenzi wa Halmashauri na wahasibu wao wa kutoa tender kwa upendeleo. Unalikuta jambo hili limeandikwa katika taarifa ambayo inawasilishwa hapa na inajenga historia ya maamuzi na mapendekezo yanayotolewa na Kambi ya Upinzani. Ni jambo la aibu! Kwa sababu jambo hili la tender kutolewa, sisi Waheshimiwa Wabunge hapa ni sehemu ya Madiwani kule, ni jambo la kusimamia sisi; siyo jambo la kuja kulalamika hapa. Unamlalamikia nani? Kama ni udhaifu wa Halmashauri yenu, ni wa kwenu. Miongozo na taratibu zipo wazi hapa! (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema tu kwamba tusiwapotoshe Watanzania kwa sababu ya hasira tulizonazo. Wote tunafahamu tulivyokumbushwa, huu mchezo hauhitaji hasira, ni lazima uwe tayari. Ukiwa na hasira utapata taabu kidogo, kwa sababu ya mambo yanavyokwenda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na watumishi wote wa Bunge, kama mtakavyokumbuka kwa mujibu wa Katiba ya Bunge Sports Club ambapo wamiliki wake na wanachama ni Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watumishi wote, tarehe 1 Juni, 2016 kwa pamoja mlinichagua kuwa Mwenyekiti wa Bunge Sports Club. Natumia fursa hii kuwashukuru sana. Ahsanteni sana. Ninaahidi kutowaangusha katika masuala ya burudani na michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara ya Fedha na Mipango kwa hotuba yao nzuri, imetupa mwelekeo, lakini shukrani za pekee ni kwa Mheshimiwa Rais, amekuja na bajeti ambayo 40% inakwenda kwenye maendeleo ya Taifa. Tunashukuru sana kwa sababu, ni kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida, kwa taratibu za kawaida za mijadala kama hii, ukiona watu hawaliongelei jambo, maana yake wanakubaliana nalo. Kwa hiyo, hata mimi mwenyewe sitatumia muda mwingi sana kwa mambo ambayo hayana mjadala mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee mambo machache. Ukurasa wa saba wa Kitabu cha Hotuba cha Mheshimiwa Waziri anatukumbusha malengo makuu ya hotuba hii ya bajeti kwamba, la kwanza ni kutatua kero za wananchi, lakini la pili ni kujenga uchumi wa kipato cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini na utulivu kuhusu uchumi wetu huu uliopo sasa. Kwa kweli uchumi wetu uko vizuri. Pamoja na kwamba ni nchi maskini, lakini wote tunakumbuka kwamba kwa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka jana, 2015 mwanzoni Tanzania sasa siyo miongoni mwa nchi masikini sana duniani, tumeshajinasua kutoka kwenye lile kundi. Kwa hiyo, kwa namna yake kwa aina fulani tuna utulivu wa kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja niliyokuwa naisema, yale mambo ambayo hayazungumzwi sana, hayana utata hapa, tunakubaliana nayo; lakini yako mambo yanahitaji Serikali na Wabunge tuyatafakari kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nihoji kuhusu hili lengo la pili la kuusimamia utulivu wa uchumi wetu kwa umakini na kwa ubora ili kuongeza tija na hasa katika suala la ajira. La kwanza, hivi tunapokuwa tunaanzisha kodi ya VAT kwenye huduma za utalii wakati tunafahamu kabisa majirani zetu, washindani wetu wameshaondoa hiyo kodi, huu ni usimamizi makini wa uchumi ambao tunakusudia kuufikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kama alivyosikia Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlivyosikia, Waheshimiwa Wabunge tukiwa wawakilishi wa wananchi, kuna hajo na kuna jambo la kutafakari hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anafanya rejea kwenye hotuba yake wakati anawasilisha, alisema baadhi ya nchi ambazo zimekuwa na utaratibu huo ni pamoja na Kenya, lakini kesho yake kuna gazeti moja liliandika Mheshimiwa Waziri wa Fedha apigwa chenga. Kwa sababu nchi ile siku hiyo hiyo, bajeti zetu kwa kuwa zilisomwa pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati tuna-introduce hiyo kodi, wenzetu wanaiondoa na ni jambo la kusikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri asikate tamaa, hatujachelewa, tuko pamoja hapa tunajadili. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla, wasikilize mawazo na ushauri wa Wabunge kwa sababu ni wawakilishi wa wananchi na ni kwa nia njema, hatushindani, hakuna nani zaidi hapa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hili tulitafakari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, natafakari tu. Ukisoma ukurasa wa 64 tunaongeza ada za usajili wa pikipiki kutoka shilingi 45,000 ilivyo sasa mpaka shilingi 95,000. Nataka niikumbushe Serikali na inafahamu zaidi kuliko sisi. Taarifa iliyotolewa mwezi wa tano mwaka huu na Benki ya Dunia inasema; na mtu mwingine anaweza kusema tusitegemee sana taarifa za Benki ya Dunia, lakini hawa ni washirika wetu, kila siku tunawasifu hapa. Wamesema zaidi ya 50% ya Watanzania ni maskini na katika hao miongoni mwao milioni 12 ni maskini zaidi. Chini ya mstari wa umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia waendesha bodaboda na wamiliki badoboda, pikipiki hizi, ndio kundi la milioni 12. Leo tunapandisha ada ya kusajili vyombo hivi kutoka shilingi 45,000 mpaka shilingi 95,000, tutafakari tu kwa pamoja. Hii kweli tunajenga! Tunasimamia uchumi wetu kwa utulivu na kwa umakini ambao tunauzungumza hapa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tutembee kwenye maneno yetu. We must walk the talk, kwamba hivi ni kweli, hawa ni wapiga kura wetu. Nataka niseme la ziada katika hilo. Ukiongeza hii ada ya kutoka shilingi 45,000 kwenda shilingi 95,000 wanaoathirika miongoni mwetu ni sisi Wabunge hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yaliyopo kwa Waheshimiwa Wabunge kuwasaidia na ujue kwamba fedha hizi ni za mfukoni, kwa sababu Mfuko wa Jimbo hauruhusu mambo haya. Kwa hiyo, nasema Serikali tushiriki kwa pamoja, tusaidiane, tulitafakari tu. Huu ndiyo umakini na utulivu tunaozungumzia? Nadhani hapana. Hata hivyo, halijaharibika jambo, ndiyo maana tunajadili wiki nzima kuhusu jambo hili. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali itafakari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina tafakari nyingine tena ukurasa huo wa 64, kuhusu ada ya usajili kwa namba za magari binafsi. Kwa waliokuwa wanapenda kuandika majina yao kama mtani wangu Mheshimiwa Profesa Maji Marefu, imepandishwa kutoka shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 10 kwa kila baada ya miaka mitatu; natafakari tu. Inavyoonekana ni kama Serikali haitaki kuwaona hawa. Nadhani inasema hawa watu ni kama wanajidai. Ni kama wanaleta mbwembwe, ni kama wanaleta “ubishoo.” Kwa sababu hii kodi ni ya hiyari tu, kwa sababu halazimiki mtu kusajili kwa jina lake. Anaweza kusajili kwa namba za kawaida, lakini kwenye eneo hili pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Waziri anakusudia kupata shilingi bilioni 26. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, kama tuna umakini na utulivu kuimarisha uchumi wetu tulivu kama ulivyo, inakuwaje tunawaongezea hawa? Kwa sababu hawa wanasajili kwa hiyari yao tu. Anyway, kwa nini tunawaongezea sasa? Ni kwa sababu hatutatki tuone watu wamesajili kwa kutumia majina yao? Hii haiwezi kuwa sawa. Tunaishauri Serikali itafakari, tuone kama kuongeza huku tunaweza kufikia lengo tulilokusudia la kuongeza mapato, kwa sababu wataona kama unawapiga penalty na matokeo yake hawataendelea kusajili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nalitafakari, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukurasa wa 44 ukaoanisha na Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anawasilisha ukurasa wa 35, katika mambo ambayo tunakusudia tuimarishe kiuchumi ni sekta ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuuliza, natafakari tu, naiomba Serikali itupe ufafanuzi, kwa nini hatuzungumzii uwekezaji mkubwa wa madini? Kwa sababu hotuba hii ya fedha inazungumzia uchimbaji mdogo. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inazungumzia uchimbaji mdogo, kwa nini hatuzungumzii wachimbaji wakubwa na hapa sizungumzii wachimbaji kutoka nje, tunaweza kuzungumzia wachimbaji wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo madini yetu tuliyoyachimba hapa hayajafikia 20% kwa hiyo, tuna rasilimali ya madini zaidi ya 80%. Kwa nini hatuweki mkakati wa kuendeleza sekta hii itusaidie katika uchumi wetu? Kwa hiyo, natafakari tu, naomba Serikali itusaidie. Kwa nini hatutaki kuzungumzia uchimbaji mkubwa? Au sasa ndiyo mwisho? Naamini kwamba sio mwisho, lakini tunashauriana na ninaamini kwamba tutafika tunakokusidia.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ya kwanza hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia yanayozungumzwa sana. Kodi kwenye gratuity, kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hilo eneo linasema, Mheshimiwa Waziri anasema, kodi hii imeanzishwa kwa sababu ya kuweka usawa katika walengwa, walipa kodi. Fine, jambo zuri, tunakubaliana, hatubishani nalo. Nasi hatuhitaji special treatment, lakini kwa sababu msingi ni huo huo kwamba tusibaguane, kwa nini imeletwa kwa Wabunge tu wakati sisi ni kada ya watu wengi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaishauri Serikali itafakari, watufafanulie tu, kwa nini wasilete watu wote wenye hadhi ya kisiasa hawa; wapo wengi wametajwa; Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa kisiasa. Kwa sababu msingi wa kuweka hii kodi ni kutokuwa na ubaguzi katika wanaolipa kodi. Sasa kwa sababu tumelengwa sisi na msingi wa utungaji sheria, tunakumbushwa waliosoma sheria, mojawapo ya misingi mikubwa inayozingatiwa ni kutokuwa na kodi baguzi. Sasa tunapolengwa sisi Wabunge tu na wengine wakaachwa; hii ndio inayotuchonganisha na wananchi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali itafakari. Kwa sababu mwishoni tutakuwa na muswada, turekebishe tu kwamba kama ni makundi yote yanayopata hadhi hii yote yawekwe hapa, itakuwa fine; lakini isiwe ni Waheshimiwa Wabunge peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine bajeti hii si tunakwenda kukusanya na kutumia? Sasa nilikuwa naangalia, hili suala la gratuity yetu limejitokeza kwenye fungu gani hapa kwenye hiki kitabu? Kwamba leo tunaweka hapa; au ni maandalizi ya kisaikolojia ili tusonge mbele? Natafakari tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma pale, kuna eneo limesema ukusanyaji wa kodi za majengo. Hapa naiunga mkono Serikali, nina sababu zangu. Hapa naomba niiunge mkono Serikali kwa sababu pamoja na wenzangu ambao wamezungumza kwa maoni tofauti, baadhi yao na tumegawanyika hapa, lakini msingi wa Serikali iliokuja nao hapa inasema inakwenda kuimarisha ukusanyaji. Naamini Serikali inasikia kwamba yako maeneo TRA hawajajiandaa vizuri, mojawapo ni Wilaya ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mwezi wa tatu, TRA ni pamoja na Halmashauri, zilikaa pamoja; uwezo wao kwa kweli wa kuyafikia maeneo yote kuhusu eneo hili ni mdogo, lakini kwa sababu Serikali kuna eneo inasema imedhamiria kwenda kuimarisha uwezo wa TRA na kwa sababu lengo ni ukusanyaji, lakini mapato yatazirudia Halmashauri, Majiji na Manispaa kama ambavyo imekusudiwa, tuwape Serikali muda kama alivyosema Mheshimiwa Zungu na Waheshimiwa wengine walivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuipe muda Serikali ikashughulikie hili jambo, lakini kilicholengwa kwenda kwenye Halmashauri kisiende kinyume na hapo. Tuipe nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nasema katika kufanya mambo makubwa ya msingi lazima kuna kuthubutu. Na mimi nina ushuhuda kwa sababu, wakati mwingine nimeshakuwa muhanga nikiwa Waziri wa Nishati na Madini. Wakati nimekwenda China mwaka 2009 nikiongoza msafara wa Serikali kuzungumzia bomba la gesi la kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam wako watu walitubeza sana wakasema Tanzania haiwezi kujenga bomba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati niliitwa kwenye nchi moja kubwa sana duniani, nikaambiwa kwa nini mnafanya hivyo badala ya kuiachia sekta binafsi? Kwa nini msije tukawapa fedha sisi hapa? Tuliwaambia kuna nchi hapa ziliathiriwa na msukosuko wa uchumi wa dunia zilikwenda kukopa fedha kwenye nchi ya China, na sisi tuna historia ya nchi ya China ya urafiki wa miaka mingi, ndiyo maana tumekatiza kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hili nilikuwa naomba tukubali tuipe Serikali muda, kazi yake…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru sana. Na mimi naungana na wenzangu kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana, yeye pamoja na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumzia mambo manne ambayo nimepanga kuyazungumzia, nina salamu za pongezi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tunaipongeza Serikali, lakini kwa hapa tunazungumza mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tufikie salamu kwa viongozi wote wakuu wa nchi yetu pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo mnaratibu shughuli za maendeleo ya Taifa letu. Tunazungumza kama Wabunge tukiwa tumejumuika kutoka katika maeneo mbalimbali. Yapo maeneo ambayo sisi wenyewe kutoka kwenye maeneo tunayofanyia kazi ni mashahidi kwa namna ambavyo shughuli za maendeleo zinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa namna ambavyo imeshughulikia jambo moja kubwa ambalo lilishakuwa kidonda ndugu kwa Taifa letu nalo ni nidhamu ya kazi. Taifa lilikuwa limefikia mahali pabaya. Sisi wote ni mashahidi, tumekuwa tukifika kwenye taasisi za umma na kuona namna ambavyo huduma zimekuwa zikitolewa miaka iliyopita, lakini tuseme kweli kabisa, katika hii Awamu ya Tano, tumeshuhudia mageuzi makubwa ya uwajibikaji kwa
Watendaji wetu. Kwa hilo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini kiranja mkuu katika usimamizi wa Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa namna ambavyo unalifuatilia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Sengerema tuna mambo makubwa yamefanyika, moja, namshukuru sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Jimbo la Sengerema. TAMISEMI pale, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Waziri Simbachawene, kile Kituo cha Afya cha Ngoma A ambacho mmekitengea fedha, wananchi wa Sengerema wamenituma nifikishe salamu zenu kwa shukrani kwa namna ambavyo mnatufanyia kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Engineer Lwenge na msaidizi wako Naibu Waziri, ule mradi mkubwa kabisa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ngazi ya Halmashauri na Wilaya unaofanyika Sengerema, sasa uko katika hatua za mwisho kabisa. Shukrani kwenu pamoja na Serikali nzima kwa namna ambavyo mmesimamia mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene tuna kiporo. Tumezungumza miezi michache iliyopita. Kwenye hesabu za Mfuko wa Jimbo zilizofanywa hivi karibuni, yapo baadhi ya Majimbo ambayo tulipunjwa. Halmashauri ya Sengerema ni mojawapo hali iliyotokana na makosa ya kimahesabu. Mmetuahidi kwamba kufikia mwisho wa mwezi huu fedha zile zitakuwa zimeshafika, lile salio. Naomba Mheshimiwa Simbachawene na Serikali kwa ujmla, jambo la mapunjo ya Mfuko wa Jimbo mlifanyie kazi, fedha zifike mahali pake, zifanye kazi kwa ajili ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizamie kwenye mchango, la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaanzia kwenye ukurasa wa 43. Umeanzishwa mfumo wa wazi wa kielektroniki kufuatilia uwajibikaji na utendaji wa Serikali, jambo hili ni kubwa sana. Ni muhimu tuipongeze Serikali.
Wamesema, kwa kupitia utaratibu huu, wata-track utekelezaji wa ahadi ambazo zimefanywa na Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, matamko, ahadi za viongozi wakuu wa Serikali akiwepo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali katika hili ni kwamba kwa sababu hatuna mashaka yoyote kuhusu umakini na Serikali yetu, lakini pia kwa kutambua kwamba sisi Wabunge ndio daraja la wananchi na Serikali, nilikuwa naomba uandaliwe utaratibu ambao Serikali kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, watakuwa wanatushirikisha Wabunge, tujiridhishe kujua yale ambayo tunaya-track katika maeneo yetu ya kazi ni yapi? Miradi gani ambayo inaonekana katika ule mfumo? Mahali ambapo pamesahaulika, sisi tuwakumbushe kwa kusema hili nalo ni sehemu ya yale mambo yaliyokusudiwa, yafanyiwe kazi kupitia huu mfumo wa kielektroniki ambao utawasaidia Watanzania kufahamu shughuli ambazo zinafanywa na Serikali. Kwa hiyo, naomba na nilikuwa naamini kwamba atakapokuwa anafanya majumuisho Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake, atatusaidia kuona umuhimu
wa kutushirikisha sisi Wabunge tujue miradi ambayo ukigoogle ama ukibonyeza ule mfumo unakuletea miradi iliyotekelezwa katika maeneo yetu. Tusipofanya hivyo, narudia tena kusema kwamba, sina mashaka na utendaji wa Watumishi wa Serikali, lakini binadamu ni binadamu. Sisi ni jicho la pili kusaidia kufikia yale yaliyokusudiwa katika kuyasimamia yaliyotekelezwa kwa namna ambayo tunakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia jambo moja la kufanya maendeleo katika maeneo yetu ya kazi. Tunapanga bajeti, kila mwaka tunaipitisha hapa. Tumekuwa na changamoto ambayo sijapata jibu lake, tutasaidiana kadri ambavyo siku zinaendelea. Suala la disbursement,
kufikisha pesa ambazo tunazipitisha hapa kwenye bajeti kwenda kwenye maeneo yetu. Ninazungumzia kutotimiza jukumu hili ama wajibu huu ambao sisi tunaufanya Kikatiba, tumekuwa tukipitisha bajeti kila mwaka. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hapa
Sengerema kwenye OC ambazo ndizo fedha ambazo zimeidhinishwa kufutilia miradi mbalimbali ambayo tunazungumzia hapa tuna asilimia 20 tu, lakini shughuli za maendeleo tuna asilimia 30. Nafahamu Waheshimiwa Wabunge wengi wanalalamika. Hilo siyo la kumnyooshea
mkono mtu yeyote, lakini ushauri wangu kwa Serikali, tusaidiane kupitia chombo hiki cha uwakilishi wa wananchi tuone namna bora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza na mwaka 2016 tumeshauriana hapa, yapo mambo tulikubaliana kwamba yako mambo hayakunyooka sana, lakini tutumie nafasi hii katika Bunge hili tuelewane vizuri kwa mfumo huu wa bajeti tulionao, tuone namna ambavyo tunaweza kutekeleza bajeti ambazo tunazipeleka kule. Haina maana yoyote kupitisha mafungu hapa kwa kiwango fulani halafu utekelezaji wake unakuwa chini ya asilimia 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza, hili ni letu sote, halina itikadi ya vyama kwa sababu tunazungumzia utekelezaji wa mambo ambayo kwa pamoja tumekubaliana kuyatekeleza. Kwa hiyo, nashauri sana Kamati ya Bajeti pamoja na Serikali kwa ujumla, tushauriane namna bora ya kuhakikisha kwamba mafungu tunayoyapitisha, fedha zilizokusudiwa zinafika mahali pake palipokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, ukisoma Mkataba wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo sasa ziko sita, ukisoma Ibara ya 49 inayozungumzia namna ambavyo tunaweza kuimarisha mtengamano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Inazungumzia habari ya Bunge Sports Club ikiwa ni chombo mahsusi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika michezo hiyo ambayo inafahamika kutokana na Mkataba wa Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia jambo hili kwa sababu ninaona kuna masuala yanaingiliana na hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa lile Fungu la Mfuko wa Bunge. Bajeti ya Bunge Sports Club inatokana na huo mfuko. Naomba Bunge pamoja na Serikali kwa ujumla tuone kwamba ushiriki wa Bunge Sports Club katika michezo siyo jambo la anasa ama la kwenda kutumia pesa hovyo, bali ni nyenzo ya utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Watendaji wote wa Serikali na Bunge kwa namna ambavyo mliwezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 tulikwenda kwenye mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mombasa; tuliondoka katika mazingira magumu kidogo, lakini ninavyozungumza sasa hivi mambo yote yako level seat. Shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Spika na Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo mliwezesha jambo hilo. Tunasema ahsanteni sana. na imeandikwa katika maandiko matakatifu, asiyeshukuru kwa
kidogo hatashukuru kwa kikubwa. Sisi tumepata kikubwa, kwa nini tusishukuru? Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo inayoongozwa na Mheshimiwa Mtemi Chenge. Unapozungumzia fedha nyingi ambazo tunazipitisha hapa, utekelezaji wake unakwenda kutekelezwa kutokana na miongozo na sheria zilizotungwa katika Halmashauri, Taasisi zetu mbalimbali zikiwemo Wizara za Serikali. Ninachotaka kuzungumza hapa ni kwamba tunapozungumzia Sheria zinazotungwa na Halmashauri zetu, ndiyo mpango wa fedha wenyewe. Tumeshuhudia wote kama Taifa, wakati mwingine viongozi wakuu wa Serikali wamekuwa wakitamka matamko ambayo wakati mwingine katikati ya safari wanaamua kuondoa tozo ambazo zimeshakubalika kwa utaratibu wa kisheria kwa namna ambavyo tumekasimu madaraka kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, silaumu katika hilo kwa sababu kama kuna kero ni lazima ishughulikiwe hapo hapo, lakini ninachosema, tuboreshe utaratibu wa namna ambavyo tunaweza kukatiza katikati ya safari, kwa sababu hizi Sheria Ndogo ndiyo zinaongoza mafungu ya kule Halmashauri na hasa mafao yale ambayo yanakwenda kuwawezesha hata Madiwani wetu ambao sisi tulioko hapa tunawategemea na ni Madiwani wenzetu kutekeleza miradi
mbalimbali ambako fedha nyingi zinakwenda. Tusiwakatishe katikati ya safari. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya bajeti hizi, kuwe na utaratibu mzuri wa kukaa pamoja tuelewane kwamba mwaka huu tutaondoa tozo hizi na hizi ili wasizifuate kwenye bajeti zao wanazoziweka. Tukikatisha katikati tutakuja kuwalaumu hawa wawakilishi wa wananchi wenzetu kwamba hawatimizi wajibu wao, lakini kwa kweli mazingira ambayo yamesababisha kumbe nasi tumeyachangia. (Maiofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hili narudia kusema, simlaumu mtu yeyote lakini naomba tulifanyie kazi kwa uzuri kwa namna ambavyo tutaweza kuwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji). MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. WILLIAM M. NGELEJA – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kama ambavyo umeridhia nifanye kazi hii kwa niaba ya Kamati yako unayoiongoza ya Sheria Ndogo naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia mahali hapa tulipofikia na hasa katika uhai wa Kamati yetu chini yako wewe.

Pili naendelea kuwapongeza na kuwashukuru sana viongozi wetu wa Bunge tukiongozwa na Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti kama kawaida. Tunaendelea kuwashukuru sana Wabunge wenzetu kwa ushirikiano ambao wametupa na hadi kufikia mahali hapa, taarifa yetu imechangiwa na baadhi ya Wajumbe kwa kadri ambavyo muda umeruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu tu nitambue kwamba waliopata nafasi ya kuchangia kwa kuzungumza ni Mheshimiwa Daniel Mtuka, Mheshimiwa Ester Mmasi, na kwa upande wa Serikali Mheshimiwa Mwenyekiti umemsikia Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mawaziri kwa ujumla waliozungumza kwa kuchangia katika taarifa hizi tatu ambazo zimewasilishwa.

Ninatambua mchango wa Mheshimiwa Ikupa, Mheshimiwa Kakunda hao ni Naibu Mawaziri lakini Mheshimiwa Waziri Jafo, Mheshimiwa Mkuchika wote hawa hakuna hata mmoja ambaye amepinga taarifa ya Kamati hizi na sisi kwa sababu ni sehemu ya Kamati hizi tatu tunatambua mchango wao tunasema ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya majumuisho pia tunakuwa tunajielekeza kwenye kile ambacho Serikali imezungumza. Kwa sababu pamoja na kwamba sisi tunafanya majumuisho ya taarifa hizi, lakini kwa kweli hoja nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge na sisi sehemu ya Kamati tulizozizungumza ufafanuzi wake umetolewa kupitia Waheshimiwa Mawaziri wakati wanachangia, na ndio utaratibu. Kwa hiyo, tunawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kurahisisha kazi hii, na mimi naamini kazi hii haitafika dakika 15 kama ambavyo Mheshimiwa Mwenyekiti umesema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sisitize tu kwamba alichomalizia kukisema Mheshimiwa Jenista, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ni kweli kabisa Kamati yetu imekuwa ikifanya kazi ya uchambuzi, na asubuhi tulizungumza kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja tumefanya uchambuzi wa sheria ndogo 404. Katika sheria hizo 404 sheria 180 zilionekana kuwa na dosari ambazo zilihitaji marekebisho. Sasa ukipiga mahesabu ya haraka hizo sheria 180 maana yake unazungumzia asilimia 44 point kadhaa kuelekea kwenye asilimia 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini, kwa huu mfumo ambao tunao wa utungaji wa sheria ndogo kwa sababu hizi zinatungwa na mamlaka mbalimbali za Serikali, maana yake ni kwamba hizi ni dosari ambazo tumezibaini wakati zimeshaanza kufanyiwa kazi. Ukitaka kwenda zaidi unasema mpaka wakati ambapo tumependekeza marekebisho na Serikali ikafanya marekebisho yaliyofanywa baada ya Kamati kubaini na Waheshimiwa Wabunge kuridhia maana yake ni kwamba madhara hayo yameshawaumiza wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe ndiyo maana tunasisitiza kwamba Serikali iendelee kuimarisha vitengo vya sheria katika mamlaka mbalimbali na umakini wa utungwaji wa hizi sheria ndogo ili tupunguze hiyo fursa ya kuwa na dosari katika sheria zetu ndogo na hivyo kupunguza kabisa ikiwezekana kumaliza kabisa kuwaumiza wananchi kabla ya hizo sheria ndogo hazijafika Bungeni kwa utaratibu na mfumo tulionao sisi wa utungaji wa sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaishukuru sana Serikali kwa kukubali, lakini kwa dhati kabisa kwa niaba yako Mheshimiwa Mwenyekiti naendelea kuwapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu kwa muda waliojitolea. Kwa sababu kama wasingekuwa makini tusingeweza kubaini hii asilimia 45 ya dosari zilizomo katika Sheria Ndogo 180 kati ya sheria 404 tulizozifanyia kazi katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nataja waliochangia kwa kuzungumza pia natambua mchango wa maandishi wa baadhi ya Wabunge wenzetu waliopata fursa hiyo; wa kwanza ni Mheshimiwa Rhoda Kunchela ambaye amechangia kwa maandishi na amezungumzia kasoro zinazopatikana katika baadhi ya Sheria ndogo, lakini pia Mheshimiwa Mary Deo Muro tunakushukuru kwa mchango wako wa maandishi, pia Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, hawa ni wale ambao walichangia kwa kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu Serikali imekubali kwamba inaridhia maoni na ushauri wa Kamati; na kwa sababu maoni na ushauri huu tumezungumza kupitia taarifa yetu na hatimaye tumependekeza Azimio la Bunge kwenye maeneo ambayo tunapendekeza yakafanyiwe marekebisho naendelea kusisitiza kwamba Serikali ifanye hivyo kama tulivyoshauri kwamba kabla ya Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania tutakapokutana hapa hasa kwenye kamati, Serikali iwe imefanya jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tena kusisistiza kwa Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba Sheria ndogo hizi zina umuhimu wake. Mheshimiwa Profesa Kabudi Waziri wa Katiba na Sheria amesema, wakati anaunga mkono hoja na mchango wa Mheshimiwa Daniel Mtuka kwamba hizi sheria ndogo ama kanuni zinapochelewa kutungwa zina athiri na wakati mwingine zinakwaza utekelezaji wa sheria mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumeona Sheria ya Madini kwa namna ambavyo ilikuwa imesimama utekelezwaji wake kwa sababu ya kanuni hazijatungwa kwa sababu ya sheria ndogo hazijatungwa, kwa hivyo ni muhimu sana sana kwamba kanuni ndogo zitungwe ama sheria ndogo zitungwe mapema kadri inavyowezekana na ziwashirishwe Bungeni ili tupunguze ile fursa ile ya kurekebisha dosari ambazo zinaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo sisi kama Kamati kwa niaba yako tunapokea pongezi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri kwa Kamati yako na Kamati zingine, lakini pia na sisi tunasisitiza nje ya taarifa hii nje ya yale ambayo tumeyaazimia kama sehemu ya maazimio na ambao tunaomba Bunge liliridhie Mheshimiwa Jenista Mhagama kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye eneo la ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali tunashukrani na pongezi zetu za dhati kwa kazi kubwa mliyoifanya. (Makofi)

Sisi tunaofanyia kazi eneo hilo tumeona mapungufu yaliyokuwepo kwenye miaka ya nyuma, lakini baada ya kufanya mabadiliko hasa kwenye Mtendaji Mkuu na timu na kuipanga timu upya katika hicho kitengo ama hiyo Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali tumeona mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakwenda mbele kidogo, kama Wajumbe wa Kamati kwamba kwa sababu aliyepo sasa anakaimu; na kwa sababu anafanya kazi kubwa sisi kazi yetu ni kutoa maoni na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitajali sana basi iongeze kasi ya mchakato ama kumthibitisha ama kumteua CEO ambaye ataisimamia hiyo idara ili maamuzi yote yafanyike. Kwa sababu tunafahamu kwamba kuna tofauti kubwa ya kuwa kaimu na kuwa mwenye mamlaka kamili. Kwa hivi sisi tunatoa mapendekezo yetu na ushauri wetu kwenu kwamba mlifanyie jambo hilo maamuzi ili kazi iendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wajumbe kwa ujumla, ukifuatailia taarifa zetu utakuta kwamba mambo tunayoyasisitiza yenye kasoro kubwa moja ni yale ambayo yanakiuka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kasoro ambazo zinahusu ukiukwaji wa sheria mama, sheria ndogo ambazo zinatungwa na sheria nyingine za nchi, lakini pia yapo masuala ya kiuhariri na kiuandishi, pia ukiukwaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema haya yote yanatokana tu na umakini, kukiwepo na umakini yote haya yatabainika. Ndiyo maana nasisitiza tena kwa mara nyingine kwamba sisi kama Kamati tuliipenda sana Kamati hii na tukafikia hatua ya kuomba kwa sababu tumefurahishwa na jinsi ambavyo changamoto zinazokuja mbele yetu na tunavyozifanyia kazi inaonekana ni jambo la heri sisi tuendelee kuwepo pale. Mheshimiwa Mtemi utakapokuwa una toa mwongozao wako wa mwisho pamoja na kwamba wewe ndiyo Presiding Officer leo, lakini kwa nafasi yako unayo nafasi pia ya kufikisha ujumbe na kuthibitisha haya ninayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa mara nyingine tena yale ambayo yamejitokeza kwenye taarifa ya Kamati zetu na baadhi ya wachangiaji waliochangia hasa wa maandishi yanayohusu Kamati ya Katiba na Sheria nitayafikisha mahali pake. Yako mapendekezo ya kwenye marekebisho ya Sheria Ardhi na Sheria ya Ndoa; lakini kwa mazingira tuliyonayo naamini kwamba hayo ni masuala ambayo yanahitaji muda zaidi na kufuata utaratibu unao kubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naliomba tena kwa mara nyingine Bunge lako Tukufu liliridhie yale tuliopendekeza, tulioyatolea maoni na kutoa ushauri na hatimaye tukapendekeza kwamba Bunge liazime kama ambavyo taarifa yetu rasmi tulivyoiwasilisha inavyosomeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa hatua hii naomba kutoa hoja kwa mara nyingine, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. WILIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimshukuru sana na jirani yangu Mheshimiwa Kiswaga kwa ukarimu wake kwa kunipa dakika tano hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake Dkt. Kalemani kwa kazi kubwa wanayoifanya. Lakini nianze kwa kupeleka salamu maalum za shukrani kuungana na watanzania wengine kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna alivyosimamia uamuzi wa kushirikiana na Uganda kujenga lile bomba la mafuta kutoka Uganda kuja kupitia Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba ujenzi wa bomba lile ulikuwa na ushindani mkubwa, ni hitajio la kila nchi inayopatikana ndani ya mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wae ule, pia umebadilisha siasa za nchi za Afrika Mashariki, kwa hivi tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo tunakupongeza sana kwa namna ambavyo ulisimamia utekelezaji ule ukiongoza kikosi cha wataalam hongera sana pamoja na timu nzima ya Serikali. Dkt. Kalemani miezi miwili iliiyopita ulikuwa Sengerema, tunakupongeza sana kwa ziara iliyoifanya, mafanikio yake tumeshayaona, lakini kuna moja nilitaka nikukumbushe Mheshimiwa Kalemani, tulivyokuwa pale katika ule Mgodi wa Nyanzaga ulisema uliwapa siku 14 wale wachimbaji wenye leseni ile ambayo wamepewa ambayo ni ya Acacia, ulisema utawaandikia barua uwape notice ya siku 14, waeleze kama wana nia ya kuendeleza ule mgodi ama laa, na kama hawatakuwa na nia Serikali ichukue uamuzi mwingine kwa kutoa leseni ile kwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatarajia kwamba Mheshimiwa Waziri, utakapokuwa unafanya hitimisho/majumuisho yako ya jioni ya leo basi utatoa hatima na mwelekeo wa Mgodi wa Nyanzaga ambao unapatikana katika Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 30 wa hotuba ya Mheshimiwa Profesa Muhongo ambayo kwa kweli imebeba mambo mazito na mazuri, mojawapo ya mambo yanayozungumziwa pale ni kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, hayafikiwi na umeme wa Gridi ya Taifa. Na mazingira ya maeneo hayo yanayozungumziwa ni pamoja na visiwa, Jimbo la Sengerema ambavyo msemaji ndio anaiwakilisha ina maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, nina visiwa kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyokuwa anachangia jana Mheshimiwa Dkt. Tizeba alisema hapa, lakini mimi nataka niungane naye kwamba katika yale aliyozungumza ni pamoja na visiwa vya Juma Kisiwani, Chitandele, tuna kisiwa cha Chikomelo kule pamoja na Lyakanyasi. Nilikuwa naomba mtakapokuwa mnatafakari kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi msije mkasahau visiwa vinavyopatikana katika Jimbo la Sengerema na Wilaya ya Sengerema kwa ujumla ikiwemo Jimbo la Buchosa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba na maeneo mengine ambayo tunakumbwa na hilo jambo ambalo tuko katika maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri inatukumbusha kwamba malengo ya Serikali kufikia mwaka 2020 katika eneo la uzalishaji umeme tunakusudia tuwe tumefikia uzalishaji wa umeme kiasi cha megawati 4,915 kutoka kwenye 1,500 tulipo sasa. Nilichotaka kusema nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kufafanua, kuna miradi mingi imetajwa hapa, lakini kwa mahitaji haya na mkakati wa Serikali sasa hivi wa nchi ya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, tunaamini demand itaongezeka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka atusaidie katika mipango tuliyonayo, je,ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya Hydro, inayotokana na nguvu ya maji ama vinginevyo kwa sababu tuna potentials kama Stiegler’s Gorge lakini tuna Mpanga, Ruhuji, Mnyera, Rukose, tuna kule Kilombero, tuna maeneo mengi ambayo yanaweza kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji. Tunataka kujua tu kama katika mpango wetu wa kulitoa Taifa hili, kufika hapo mblele tunakususia kujumlisha hii miradi mikubwa ambayo inaweza kuzalisha umeme kutokana na nguvu ya maji/
Mheshimiwa Mwenyekiti,la mwisho, kwa sababu ni dakika tano tu, tarehe 21 Aprili, Shirikisho la Wachimbaji na Watafutaji wa Madini walitoa taarifa wakifafanua ushiriki na uwezesho na namna ambavyo wao wamechangia katika uendelezaji wa uchumi wa Tanzania. Katika baadhi ya mambo waliyoyazungumzia walitoa hisia zao na taarifa zilitoka kwenye vyombo vya habari vingi tu kwamba mpaka sasa hivi wameshachangia kiasi kikubwa. Lakini hoja ninayoizungumzia hapa ni kwamba tunaiomba Serikali itoe ufafanuzi itakapokuwa inafanya majumuisho, kwa sababu mchango wa kwenye Pato la Taifa wa sekta ya madini sasa hivi ni asilimia tatu pointi kadhaa. Lakini sisi tuna dira ya Taifa hapa inasema katika sekta ya madini tunakusudia mchangowa Taifa uwe umeshafikia asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema kwa sababu maandalizi ni sasa, miaka tisa, kumi iliyobaki sio mingi sana, pengine katika hatua hii Mheshimiwa Waziri, pamoja na Serikali nzima inaweza kukusaidia kutoa mwelekeo kwamba mikakati iliyopo kutoka kwenye asilimia tatu na ukizingatia changamoto zinazopatikana katika sekta ya madini duniani sasa hivi, ni mikakati ipi tuliyonayo ya kutoka hapa kusogea mbele kufikia hiyo asilimia 10 ifikapo mwaka 2025?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa tunayoifanya katika kuendeleza sekta. Lakini pia nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, wameanza vizuri sana wamefanya kazi kubwa sana, tunakushukuru sana na tunawatakia kila la heri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa fursa hii. Naanza kwa kuwashukuru sana viongozi wa Wizara yetu hapa, Mheshimiwa Dkt. Mpango kama Waziri, Naibu Waziri wake Dkt. Kijaji, Katibu Mkuu pia Doto James, Naibu Katibu Mkuu, Wataalam wote wanaoongoza Tume ya Mipango na Watendaji wote katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili bajeti hii sisi ni wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali. Mojawapo ya mambo yanayotuongoza kutafakari na hatimaye ama kuikubali ama kutoikubali bajeti hii ni pamoja na kuona mambo ambayo yamezingatiwa katika maeneo yetu ya kazi tunakotoka pamoja na mambo ya Kitaifa. Naanza kwa kusema naungana na wale wote ambao wanaiunga mkono bajeti hii asilimia mia moja kwa sababu, kule Jimbo la Sengerema ambako mimi nawakilisha, yako mambo ambayo yamejitokeza moja kwa moja kwenye bajeti hii na nitasema kwa ufupi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwa nini naiunga mkono bajeti kwa sababu, naona sekta ya maji. Nampongeza sana Mheshimiwa Injinia Lwenge na Msaidizi wake kule Sengerema ule mradi mkubwa kabisa ambao unaongoza kwa ngazi ya Halmashauri na Wilaya Tanzania umeshakamilika sasa uko hatua za mwisho mno. Baada ya hapa nina hakika kwamba Viongozi Wakuu wa Serikali watakwenda kuuzindua na mimi nawakaribisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule sasa unapokamilika tunaanza kuufungua kuwafikishia maji wananchi wanaozunguka Mji wa Sengerema na maeneo mengine. Sio hivyo tu, kuna miradi kadhaa imebuniwa inayotokana na chanzo cha Ziwa Victoria. Kwa hiyo, hivi tunavyozungumza bajeti hii naiona Sengerema imezingatiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kufika Sengerema unapotokea Mwanza lazima uvuke Ziwa. Tuna barabara ya Lami ya Kamanga – Sengerema pale, nimezungumza na TANROADS wametuahidi kwamba, mwaka huu wa bajeti unaokuja, mwaka mpya wa fedha, wataanza kushughulikia ujenzi wa lami. Pia, tuna vivuko, kutoka Mwanza kwenda Sengerema unavuka kwa kutumia njia mbili, kuna Kamanga pale kwenda Sengerema, lakini pia kuna njia ya Busisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale Busisi kuna mambo mawili yanafanyika kuanzia Kigongo, Jimbo la Misungwi; kwanza kuna ununuzi wa kivuko kipya, naipongeza sana Serikali, lakini pia kuna ferry tatu zinafanya kazi pale, zinafanyiwa matengenezo na bajeti imeonesha hivyo. Ndio maana nasema katika mazingira hayo hakuna namna nyingine, isipokuwa kuiunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maandalizi ya ujenzi wa daraja kubwa, kilometa 3.5 unafanyika pale kwenye kivuko kati ya Kigongo kwenda Busisi ambako ni Jimbo la Sengerema. Yote haya ni maandalizi yanayofanywa kupitia bajeti hii ya fedha. Kwa nini wananchi wa Sengerema tusiunge mkono? Tuiunge mkono kwa sababu tunaona tunafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ina mambo mengi, lakini lingine mojawapo ambalo ni baadhi ya mambo machache ambayo yamenifurahisha na mimi naungana na wenzangu ni kuwatambua rasmi wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama Machinga, lakini wanaofanya kazi za kujiendeleza wenyewe na kuchangia uchumi wa Taifa. Ni jambo muhimu na lazima tuliheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imepunguza ushuru wa mazao, kwa sisi tulioko kule vijijini tunafahamu. Inawezekana tukaongea katika lugha tofauti kwa sababu tunatoka maeneo tofauti, watu wa mjini watatuuliza mambo ya mjini, lakini sisi tunaotoka Majimbo ya vijijini tunafahamu kero ambazo zimekuwa zikiwagusa wananchi eneo hili. Kushusha ushuru wa mazao mpaka mzigo uzidi tani moja ni jambo kubwa sana. Tunasema mazao ya biashara ni asilimia tatu na mazao ya chakula asilimia mbili, hili ni jambo kubwa tunaishukuru sana Serikali kwa kuja na mapendekezo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Sh.40/= pale, tumesema kwenye utaratibu wa Road License sasa ziende kwenye maji. Nasema tufanye uamuzi mgumu, lakini kwa sababu naiona neema inakuja labda tusifike huko, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa Shabiby juzi aliongea vizuri sana hapa, kwamba zile Sh.40/= tunazoziongeza zilikuwa kwenye utaratibu wa kawaida, lakini tumekuwa na kilio cha kuongeza Sh.50/= kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Maji kule. Sasa kwa sababu naiona neema inakuja saa nyingine tusifike huko, lakini ukiniuliza mimi ningesema ushauri wangu ni kwamba, hata ile Sh.50/= ambayo tulikuwa tumeikusudia, tuliyoichangia sana kabla ya bajeti hii tuiongeze kule ziende zote kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia na dunia nzima inafahamu, Bunge jana tumetoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kudhibiti na kuisimamia vilivyo bora zaidi sekta ya madini. Naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita nilichangia hapa nikasema kwa hali tuliyofikia sasa hivi tunahitaji tu maamuzi ya usimamizi wa sheria na sera tulizonazo. Moja ya jambo nililozungumza kupitia kile Kifungu cha 11 cha Sheria ya Madini kinaruhusu kabisa kuipitia mikataba hii, lakini nikasema hata ushiriki wa Serikali kuwa na hisa katika makampuni haya kupitia Kifungu cha 10 tunaweza kabisa kuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo haya na nazungumza mimi nikiwa na Kiapo cha Bunge, lakini pia niko chini ya Kiapo cha Serikali, nilishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini kwa miaka mitano na nusu. Nazungumza nikifahamu michakato, tungefuata utaratibu wa kawaida wa kuanza mchakato wa kuwaalika wawekezaji tushauriane namna ya kuboresha mikataba hii, ingetuchukua miaka. Mheshimiwa Rais ameturahisishia, jana tumesikia wote na dunia imeelewa kwamba, ndani ya wiki mbili hizi mazungumzo yataanza na upo uelekeo wa kuelewana katika hali ya kuwa na win-win situation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tumepitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Rais JPM, lakini ilikuwa ni kabla ya Taarifa ya Mheshimiwa Rais. Kuna utamaduni umezoeleka duniani kwamba mambo makubwa yakifanywa na Viongozi Wakuu wa nchi kwa pamoja, kuna utaratibu na hasa kama hili Bunge, tunaweza sisi, sisi ndio wawakilishi wa wananchi Tanzania nzima. Wapo Wabunge hapa wana simu za kumpigia Mheshimiwa Rais moja kwa moja kumpa pongezi kwa kazi anayofanya, lakini wengine hata namba yake hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaowakilisha wawakilishi wa Watanzania, nilikuwa naliomba Bunge lako dakika moja, tumpe standing ovation Mheshimiwa Rais kwa wale tunaoguswa kuonesha sisi kuguswa kwetu kwa namna ambavyo tumeunga mkono na tumhakikishie kwamba, tuko pamoja. Tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya, tumuunge mkono kwa niaba ya Watanzania wote tunaoguswa na jambo hili, tumhakikishie kwamba vita hii sio ya kwake peke yake ni ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hilo. Kwa kufanya hivyo, hatufanyi kwa sababu ya favour, lakini kwa sababu ya kutambua kazi kubwa anayoifanya. Kupambana katika sekta hii na mmeona katika mitandao inasemekana zipo familia mbili ambazo zimeamua kudhibiti madini yote duniani, lakini Mheshimiwa Rais anaungana na kundi la viongozi duniani ambao wana uthubutu na wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si jambo la kwanza, tunafahamu historia ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere alivyopigana katika mawimbi mazito sana akaifikisha nchi hii hapa, lakini ukienda Marekani kuna Rais yule mnafahamu, Rais Franklin Roosevelt aliikamata ile nchi akaongoza hata zaidi ya kile kipindi ambacho yeye kwa taratibu za Kimarekani kilikuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Franklin aliichukua nchi ikiwa katika hali ngumu sana na akaanzia pale ambapo Marais waliokuwa wamemtangulia, akaivusha Marekani mpaka kifo kilipomkumba. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amejitoa muhanga kwa niaba yetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda China, Mao Tse Tung kuanzia mwaka 1949 walivyofanya mapinduzi China aliongoza lile Taifa mpaka mwaka 1978 akaja kiongozi, Mwanamapinduzi, akaanzia pale alipokuwa ameishia Mao Tse Tung akaichukua ile nchi, anaitwa Deng Xiao Ping, aliichukua ile nchi ni miaka ishirini na kitu tu, China ikabadilika sana kuanzia mwaka 1978 mpaka 1989 alipokuwa anaachia

nafasi. Kwa hivyo, duniani kunawezekana. Nenda Singapore kuna yule Li Kuyan Yew ameichukua ile nchi akaibeba kutoka ilipokuwa ikafika hapa ilipokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, mambo haya yanawezekana. Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwa hii, hatua tulipofikia hapa ni nzuri sana. Pamoja na kwamba, hatujajua tutapata kiasi gani, lakini tunakoelekea ni kuzuri na Mheshimiwa Rais amethubutu na sote tunaungana kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye bajeti. Tunapozungumzia Tanzania ya Viwanda tunazungumzia yako mambo ambayo lazima yafanyike. Huwezi kuzungumzia nchi ya viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. Nataka niseme ninachokifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu sasa linakwenda kufumuka kwa maendeleo. Unasikia sasa hivi Mheshimiwa Rais jana ametuambia akiwa na Mwekezaji ambaye ni Rais na Mwenyekiti wa Barrick amesema kwamba, pamoja na mambo mengine ambayo tutayajadili ni pamoja na ujenzi wa smelter, kunahitajika umeme mkubwa sana, lakini nimesikia reli itakayojengwa itatumia treni inayoendeshwa kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Rais wa Rwanda kule amesema wanaisubiri reli hii inakwenda, unahitajika umeme mwingi sana. Unapozungumzia viwanda unazungumzia umeme mwingi, ushauri wangu kwa Serikali, lazima sasa kama ambavyo tumeji-commit kwenye bajeti hii, tuishirikishe sekta binafsi tusaidiane na Serikali kuwekeza katika vyanzo vya kuzalisha umeme, kwa sababu vinginevyo hatutaweza kuhimili hiyo kasi inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, hapa sasa hivi kuna miradi inatekelezwa pale Kinyerezi One mpaka Kinyerezi Six. Naomba, kama inawezekana kwa sababu, wapo Wakandarasi kwa mfano wanaomalizia ile Kinyerezi One, Serikali imeingia nao utaratibu wanajenga, naishauri Serikali wakati tunaishirikisha sekta binafsi pia, inaweza kuwa-engage hawa Wakandarasi kwa utaratibu kwa sababu, ndani ya miaka mitatu tunaweza kufanikiwa kumaliza mradi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bomba la gesi ambalo limejengwa miaka michache iliyopita na mimi ambaye nilisimamia katika eneo hilo nafahamu, sasa hivi wamesema limetumika asilimia sita tu asilimia 90 haijatumika, inahitaji vyanzo vingi vya kuzalisha huo umeme ili uwafikie wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hii tuna vyanzo vingi vya nishati, tusitegemee gesi peke yake kwa sababu, kwanza gesi ina bei juu kidogo kuliko vyanzo vya maji. Leo hapa tuna Bonde la Rufiji inafahamika, kuna mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge. Nakumbuka mpaka mwaka 2012 tulikuwa tumeshaanzisha mazungumzo na Wabrazil walikuwa tayari kuja kuungana na sisi, una uwezo wa kuzalisha megawatt 2,100. Nchi hii kwa potential tuliyonayo kwenye sekta ya umeme unaoweza kuzalishwa kutokana na maporomoko ya maji ni zaidi ya megawatt 4,600. Naomba Serikali ifunguke kote kule twende tukatumie vyanzo vyote kuhakikisha kwamba, nchi hii inafikia lengo lililokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudie tena kusema umuhimu wa sekta binafsi ulivyojionesha, Mheshimiwa Waziri ameonesha utayari huo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante. Mheshimiwa Mbene, ajiandae Mheshimiwa Musukuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, na mimi ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla kukukaribisha hapa Bungeni kwa mara nyingine. Ni faraja kukuona unaongoza tena jahazi lako hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuipongeza Serikali kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa nafasi hii tunawapongeza sana wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Tunafahamu kabisa kwamba mjadala huu unajenga mustakabali wa Taifa kwahivyo kwa yale mazuri yanayofanywa ni vema kuyasemea.

Moja, nikukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa unayoifanya wewe kama msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali. Umefanya ziara nyingi sana mikoani na maelekezo yako yamesaidia sana kuongeza kasi ya utekelezaji na kurekebisha kasoro ambazo zilikuwepo za kiutendaji. Sengerema tutakukumbuka sana kwa ziara uliyofanya ndani ya mwezi mmoja na nusu uliopita.

Mheshimiwa Spika, ushahidi wa kwamba Serikali inawasikiliza Wabunge na jamii kwa ujumla ni taarifa iliyotolewa sasa hivi na Mheshimiwa Mkuchika, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais. Hongereni sana Serikali kwa kusikiliza mawazo ya wawakilishi wa wananchi, wafanyakazi,
watumishi wetu wa darasa la saba wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hivi ndivyo ambavyo inatakiwa Taifa tuendelee kulijenga kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimia Spika, heshima ya Serikali ni pamoja na namna ambavyo inatayarisha nyaraka zake na kuzitunza. Hapa nazungumzia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Mimi nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge lako Tukufu mara kadhaa tumetembelea Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na kwa miaka mingi amekuwa na changamoto nyingi sana, lakini niseme kuanzia mwaka jana Serikali imechukua hatua kubwa na kwa hili kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tunampongeza sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kama Waziri mhusika kwa hatua za kurekebisha management pale.

Mheshimiwa Spika, ninachokiomba kwa Serikali ni kukamilisha management pale. Mkurugenzi Mtendaji au CEO wa pale sasa hivi anakaimu, lakini amefanya kazi kubwa sana kwa kipindi ambacho amekuwa akikaimu. Naomba Serikali ikamilishe uteuzi, mpate Mtendaji Mkuu ili shughuli ziendelee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumzia pia kwa wale ambao tumeguswa na hii programu ya MIVARF. MIVARF ni programu ambayo inaratibiwa na Serikali kuhusu miundombinu ya masoko lakini uongezaji thamani wa mazao na huduma za kifedha vijijini. Kwa wale tunaoguswa ni programu maalum sana na nzuri sana. Tunashukuru sana kwa wale ambao wamekuwa wakiunga mkono na kujua kwamba kuna taasisi mbalimbali za kimataifa, hii kwa kweli ime-compliment juhudi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Sengerema tuna mradi mkubwa wa umwagiliaji wa maji, uliibuliwa miaka mitano iliyopita, gharama yake ni bilioni 2.5, Serikali ilishaleta milioni 700 lakini
1.8 billions hatujapata. Tumeanza kuzungumza na wafadhili wa MIVARF wako tayari kutusaidia na ndiyo maana tunasema hii awamu ya pili ambayo Serikali inaendelea na mazungumzo tunaiomba sana ikamilishwe haraka kwa sababu inakuja kuisaidia Serikali mahali ambapo ina upungufu wa fedha programu hii itasaidia kukamilisha miradi iliyokwama ikiwemo mradi wa Sengerema wa Katunguru Irrigation Scheme.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ukurasa wa 45 kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inazungumzia habari ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA). Tumeanzisha Wakala na tumeukabidhi majukumu ya kufanyia matengenezo barabara za mtandao wa vijijini, madaraja yake na makalvati mbalimbali. Kuna barabara tumeipa Wakala huu jukumu la kutengeneza kilometa 108,946.2

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa taarifa iliyotolewa na Mheshimwa Waziri Mkuu ya utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha ni kilometa 4,183 tu ndizo ambazo zimetengenezwa ni kwa sababu ndicho kiwango cha fedha tulichokitenga.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba kulishauri Bunge lako tukufu ni kwamba kwa hatua tuliyonayo hii, tukienda kwa speed hiyo kwa huo mtandao wa kilometa zaidi ya 100,000 itatuchukua miaka 26 kuweza kurekebisha barabara zetu za vijijini, leo tunafahamu kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania na hasa uchumi wao unategemea vijijini. Ushauri kwa Bunge lako tukufu na kwa Serikali ni kwamba, ule mgawanyo wa fedha za Serikali kutoka kwenye Mfuko wa Barabara ambao sasa hivi unasimamia kwa asilimia 70 barabara kuu na za mikoa na asilimia 30 kwa barabara za vijijini, tuurekebishe ili tuuwezeshe Wakala huu ufanyekazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba twende 50 kwa 50 na ninasema hilo nikitambua kwamba tuna umuhimu wa kutengeneza barabara za vijijini na mijini, lakini ukilinganisha uwiano wa uwezekano wa kupata mikopo na Serikali imethibitisha hivi karibuni kwamba tunakopesheka. Kwa wale wanaoweza kutukopesha kwa masharti nafuu wataweza kutukopesha kirahisi kwa barabara za mijini ama zinazounganisha mikoa ama barabara kuu, lakini siyo rahisi sana kupata mkopo kwa barabara za vijijini. Tufanye kama tulivyofanya kwenye Umeme Vijijini (REA) tumetumia fedha ya ndani na leo tunajisifu kwa sababu ya hatua tuliyofikia ya kutenga bajeti mahsusi kutoka kwenye vyanzo vyetu. Ninaomba tuurekebishe mgawanyo uwe fifty/fifty vinginevyo uwe 45 kwa 55 ili tupate fedha nyingi za kurekebisha barabara zetu za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine sambamba na hilo ambalo wenzangu wamelizungumza, Wakala huu bado unaeleaelea uwajibike sasa, taratibu na kanuni zirekebishwe, uwajibike kwenye Halmashauri husika na hasa za kule kwenye Wilaya zetu kwa sababu hao ndiyo watakaoshirikiana nao kubaini barabara zipi mbovu na hata mipango wanayoipanga ya kwenda kutekeleza hizo barabara, tukifanya hivyo tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 56 unazungumzia afya, nizungumzie eneo moja tu la huduma za tiba za kibingwa. Taarifa za Serikali kama kumbukumbu yangu iko sahihi na Waheshimiwa Wabunge wengine ni kwamba ugonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road tumekuwa tukitaarifiwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaofikishwa pale kwa matibabu wanatoka Kanda ya Ziwa. Ombi langu ni moja tu, Kanda ya Ziwa tuna Hospitali ya Rufaa Bugando tunaomba ipewe kipaumbele, washirikiane na Bugando Hospital.

Mheshimiwa Spika, najua Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu yupo hapa wamekuwa wakishirikiana vizuri sana, tunaomba waongeze kuna kifaa ambacho kinahitajika ili watekeleze vizuri utaratibu wa kuwasaidia Watanzania wenye magonjwa ya saratani na kwa sababu ni eneo ambalo linahusu wagonjwa wengi, nadhani mkiwasaidia tutafika mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Nape amezungumzia uwekezaji katika sekta ya gesi, nalizungumza suala hili ikiwa ni eneo ambalo ninalifahamu kidogo. Nimekuwa nikiskia Serikali inasema mkakati uliopo ni kwamba inapofika mwaka 2020 tuwe tumeshafikisha megawati 5000 na mwaka 2025 tufikishe megawati 10,000. Kiufupi tu ni kwamba kwa vyanzo vilivyopo ikiwemo cha maji cha Stieglers Gorge havizidi megawati 5000 sasa nataka kujiuliza tunatokaje kuanzia hapo mwaka 2021 kwenda kwenye mwaka 2025 kama hatufanyi mipango ya kuendeleza gesi sasa hivi ikiwemo na huu mradi mkubwa wa kuchakata gesi wa LNG ambao amezungumza Mheshimiwa Nape. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania kama walivyo binadamu wengine wanahitaji kuishi kwa matumaini kwa kupewa mipango ya Serikali. Tunapowataarifu Watanzania kwamba mipango imefikia lengo fulani, tunawajenga kisaikolojia lakini tunawandaa pia kupokea fursa zinazokuja na uwekezaji wa namna hiyo. Kwa hivyo, ninachosisitiza ni kwamba, kwa sababu bomba la gesi tulilo nalo sasa hivi linatumika kwa asilimia sita tu kwa taarifa ambazo zimekuwa zikisikika, asilimia 94 haijatumika, tuendeleze miradi hii, tuhakikishe kwamba gesi pia tusiiache pembeni, kwa sababu mipango yake ya uwekezaji katika gesi inachukua muda mrefu sana siyo suala la miaka miwili/mitatu; kwa hiyo, tusipoanza mapema maana yake ni kwamba tunajiweka katika mazingira magumu mno kufikia lengo ambalo tumelikusudia megawatts 10,000 za umeme mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali izingatie suala hili, tulifanyie kazi, wafunguke pia kwenye upande wa sekta ya gesi. Lakini tunafikaje huko?

Mheshimiwa Spika, sisi wenyewe hatuwezi kuifadhili miradi hii, njia pekee iliyopo na juzi Mheshimiwa Rais amefungua ukurasa mpya wa mahusiano na sekta binafsi, tuipe kipaumbele sekta binafsi itusaidie, isaidiane na Serikali katika kuendeleza miradi hii, vinginevyo kama tulivyo kwa fedha zetu, tunajenga SGR, tunanunua ndege zetu wenyewe, tunajenga Stieglers Gorge kwa fedha zetu, hatujakamilisha miundombinu ya elimu, bado tuna changamoto katika afya, tunataka fedha nyingi kwa ajili ya TARURA, tunahitaji kuboresha huduma za maji, sisi wenyewe kama tulivyo, kama Serikali hatuwezi kufanya hivi na ni nchi chache sana duniani zilizofanikiwa kwa kutegemea vyanzo vyake vyenyewe bila kuishirikisha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba tuipe sekta binafsi kadri itakavyowezekana ushirikiano mkubwa ili waweze kutusaidia kutufikisha kwenye malengo ambayo tunakusudia.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kwenye maji. Mwaka jana tuliongeza shilingi 50 kutoka kwenye lita ya mafuta, naomba tena mwaka huu tuongeze shilingi 50 nyingine ili tuongeze kasi ya kufikisha huduma za maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na fursa hii, nawatakia kila la kheri. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nami naungana na wachangiaji wengine kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wa Wizara hii. Wizara hii ina bajeti ndogo sana lakini tunaona kazi kubwa wanayoifanya kwa manufaa ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni sehemu ya utangulizi wa mchango wangu, niungane na Watanzania walio wengi sana katika nchi yetu kuitakia kheri na kuipongeza timu ya Simba Sports Club ambayo sasa iko kwenye maandalizi ya kukabidhiwa ubingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ambavyo tunafahamu ukilinganisha, kwa sababu soka ni shughuli ya sayansi na inaweza kulinganishwa kwa kupimwa, kulinganishwa na ligi zinazochezwa duniani kote….

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya kweli ambayo ninaizungumza kwamba hapa duniani kwenye ligi ngumu ni timu mbili tu ambazo zimebaki hazijafungwa, iko Barcelona kwenye ligi ya LaLiga na iko Simba sports Club Tanzania. Kwa hivyo mambo yanaenda vizuri na Wanasimba tuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma dira kwenye ukurasa wa nne wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo kimsingi naiunga mkono, dira ya Wizara hii inasema ni kuwa na Taifa linalohabarishwa vizuri, lilishamirika kiutamaduni na lenye kazi bora za sanaa na lenye umahiri mkubwa katika michezo ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 49 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri na hasa kile kipengele kinachozungumzia sekta ya maendeleo ya michezo, kinaelezea, pamoja na mambo mengine kwamba kinaizungumzia Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995 ambayo sasa hivi nafahamu Serikali inaipitia, pale yameelezwa malengo makuu ya sekta ya maendeleo ya michezo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya lengo ambalo limeelezwa katika kipengele hicho kuhusu sera ya michezo ni kuhamasisha umma wa Watanzania kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo, kuwezesha upatikanaji wa viwanja na zana bora kuhusu michezo lakini pia kuandaa na kutayarisha wataalam wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kuchangia kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili. Nianze kwa kulipongeza sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Job Ndugai, kwa sababu sisi kama watunga sheria na wasimamizi kimsingi wa utekelezaji wa sera za nchi yetu tumeshiriki kwa vitendo.

Bunge Sports Club inawakilisha, kwamba tumekuwa tukishiriki katika masuala ya michezo na hasa kufanya mazoezi viwanjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho nawaalika Wabunge wote tushiriki kuanzia saa 12 asubuhi kwenye lango kuu kama tulivyotangaziwa asubuhi, Wadhamini wetu NMB watashirikiana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye matembezi ya mwendo wa pole, kwenye shughuli ya kukimbia kwa mwendo wa taratibu lakini pia na matembezi kuanzia hapa mpaka uwanja wa Jamhuri. Hii ni mojawapo ya utekelezaji wa sera ya michezo Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa letu iko michezo mingi kwa sababu hatuwezi kuzungumzia yote kwa pamoja kwa mtu mmoja kwa dakika kumi, nataka nijielekeze kwenye mchezo unaopendwa sana duniani. Siyo kwamba najielekeza huko kwa sababu michezo mingine haipendwi, hapana! Nazungumzia soka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa. Nimesoma dira ya Serikali inasema kufikia mwaka 2025 tuwe Taifa ambalo limeshapiga hatua kubwa sana kimichezo, lakini leo ukiwauliza Watanzania toka miaka ya 1980 ambapo timu yetu ya Taifa ilifanikiwa kushiriki kwenye mashindano ya kombe la Afrika kwa kipindi chote hiki tumekuwa tukiugua maumivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itufungulie na ijifunue wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya winding up atusaidie kuelezea mikakati ya Serikali ya kututoa hapa tulipo kwenda kulifikisha Taifa lilipokuwa miaka ya 1980, miaka ya 1970 na hata mwanzoni mwa miaka ya 1990. Tuna uwezo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona maelezo ya ujumla ya kisera na kisheria lakini kwakweli ukiangalia soka letu ilipo hapa sasa hivi tuko mahututi. Sasa hivi kwenye ranking za FIFA tuko 130 na kitu. Ni jambo ambalo linatia aibu lakini naamini kabisa juhudi anazozifanya Mheshimiwa Waziri zinaweza kututoa hapa na kutusogeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona changamoto kwenye Baraza la Michezo ni tatizo, hapa nataka niseme ambacho nimekiona kwa sababu mwaka kesho tumepewa heshima ya kuandaa, tutakuwa wenyeji wa mashindano ya vijana walio chini ya miaka 17 kwenye mpira wa soka, mashindano yanafanyika hapa Tanzania, lakini kuna Kamati ya Maandalizi ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja katika ukurasa wa 49 na 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona hapa tunafanya yale yale kwa miaka yote. Nataka nishauri, hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema imezingatia maelekezo na maudhui ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyotoa hapa wiki mbili au tatu zilizopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Kamati ilivyoundwa hapa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisisitiza kwamba katika kufanya mambo yetu Kitaifa lazima tuishirikishe Sekta Binafsi. Sasa ukiangalia hapa kilichopo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona hata kipengele kimoja ambacho kinaelezea kwa dhamira ya dhati kabisa kuishirikisha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi sana tukafanikiwa bila kuishirikisha sekta binafsi, kwa sababu ukurasa wa 71 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anaizungumzia sekta binafsi ishiriki katika kuendeleza habari ya shughuli zetu za maendeleo na michezo ni mojawapo. Kwa hivyo, ushauri wangu ni kwamba tushirikishe sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumzia habari ya maendeleo ya michezo na sanaa kwa ujumla, yako maeneo ambayo lazima tuyape kipaumbele, ‘Bongo Fleva’ sasa hivi imetutoa. Tunamzungumzia Msanii kama Diamond, tunaungana na Watanzania wote kumpongeza kwa hatua aliyofikia kutambuliwa kwamba awe mojawapo ya watu wanaotunga wimbo maalum kwa ajili ya Kombe la Dunia mwaka huu, hii ni heshima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikusudii kusema kwamba hatuthamini sanaa zingine, lakini muziki wa Bongo Fleva, nafahamu akiwemo ‘Profesa Jay’ ambao wameshiriki sana kuufikisha muziki hapo ulipo, Diamond, Ali Kiba na wengine wote lazima tuwape kipaumbele katika shughuli hii ya kuendeleza sanaa hii kwa sababu ni heshima kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini na naishauri Serikali kwamba huko tunakoelekea sasa hivi ambapo Diamond atakwenda kutuwakilisha, Wizara ya Maliasili na Utalii itam- package kwenda kuitangaza nchi yetu, Diamond kwa sababu yeye ni nembo ya Taifa. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwapa ushirikiano watu kama hawa kwa sababu kuna faida kubwa kuwa nao katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera inazungumzia kujenga viwanja na kuimarisha miundombinu ya michezo. Tumezungumzia Chuo cha Malya hapa. Kwa bajeti ya Serikali kama ilivyo hatuwezi kufanikiwa lakini tutakuwaje na Wataalam waliobobea kama hatuna vyuo ambavyo vinaendeleza na kutengeneza weledi maalum kuendeleza michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tena kwa mara nyingine, kama tulivyozungumza kwenye Kamati kwamba Mheshimiwa Waziri aendelee kushirikisha sekta binafsi aone, wapo watu wanapenda tu. JK Youth Park pale Dar es Salaam Kidongo Chekundu umejengwa uwanja mzuri kwa ufadhili na udhamini wa kampuni binafsi. Tuendelee kushirikiana tuone namna gani sekta binafsi inaweza kutusaidia katika kuboresha viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kwamba kwenye ile ruzuku ambayo tunaipata kila mwaka kutoka FIFA pengine tuitumie pia kujenga, kuimarisha viwanja huko Wilayani kwa sababu nafahamu kwa ngazi ya mkoa angalau

tuna viwanja, lakini wachezaji wengi siyo lazima watoke Makao Makuu ya Mikoa tu. Ombi langu ni kwamba hili fungu ambalo tunapata kutoka FIFA kila mwaka tulitumie pia kuendeleza viwanja vya vijijini na Wilayani ambako tunaamini kwamba pia kuna uwezekano wa kuwapata wachezaji wengi wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtemi Chenge, ahsante sana kwa fursa hii. Nimesimama hapa nikiungana na Waheshimiwa Wabunge walio wengi kuipongeza sana Serikali. Kwa kuanza kabisa, naunga mkono hoja ya Serikali iliyoko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utangulizi wetu kwenye hotuba hii ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi inasema namna ambavyo hotuba hii imeandaliwa, lakini moja ya mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hapa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, nikiwawakilisha pia Watanzania kwa ujumla wake kwamba, hivi karibuni tumesikia taarifa zilizoenea kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, kwamba ule utengenezaji wa kivuko cha pale Kigongo Busisi, eneo ambalo linaunganisha Wilaya ya Misungwi kwa Mheshimiwa Charles Kitwanga pamoja na Busisi upande wa Sengerema sasa uko hatua za mwisho kabisa na kile kivuko kimeshaanza majaribio kwa sababu, kimeshashushwa ziwani tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2020. Kwa hiyo, kwa dhati kabisa naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, natumia fursa hii kuishukuru sana Serikali na nitataja baadhi ya Mawaziri kwa mambo ambayo wameiwezesha hivi karibuni kwa taarifa nilizonazo. Kwanza ni Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo. Wanakatunguru pale Jimboni Sengerema kwenye Kituo chetu cha Afya, mjiandae tumepata fedha za maboresho shilingi milioni 400 zinakuja. Sengerema Sekondari tumepata zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia utekelezaji wa miradi ya maji Sengerema na Taifa kwa ujumla, nasi hujatusahau, maelekezo yake yanaendelea kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri, Mheshimiwa Kakunda ufuatiliaji wa malipo ya fedha zile, ziara yake imezaa matunda, tumeshapata fedha kwa ajili ya Mkandarasi wa mradi wa maji Buyagu, Kangalala, Bichocho na utaratibu wa ukamilishaji unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy kwa msaada wake ambao ametupa. Nataja hawa wachache kwa niaba ya Serikali nzima kwa sababu muda hauruhusu kutaja wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizamia kwenye hotuba yetu iliyoko mbele yetu na hasa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Taarifa za Kiserikali pamoja na Kamati; naipongeza sana Serikali, lakini pia Kamati ya Bunge ya Bajeti pamoja na Kamati ya Uongozi kwa ujumla wake kwa maelekezo ya Mheshimiwa Spika, kwa namna ambavyo walizitumia zile siku sita kushauriana. Wameshauriana mambo mengi. Yale mazuri tumeshayasema sana na yapo wazi, lakini katika Taarifa ya Kamati ya Bajeti, pia zipo changamoto ambazo ziliainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie changamoto inayohusu sera za matumizi, kama ambavyo imeainishwa katika Taarifa ya Kamati ya Bajeti na hasa katika ukurasa wa 32, wakati nafanya mapitio na kupitia taarifa hiyo kuhusu Mpango wa Fedha na Matumizi kwa mwaka huu wa fedha mpya unaokuja mwaka 2018/2019. Moja ya jambo kubwa lililojitokeza ni kwamba kwa miaka kadhaa sasa kama nchi tumekuwa na changamoto ya kutokidhi matarajio ama maoteo ya bajeti tunazozipanga hapa, aidha kwa kutotimiza malengo kutokana na vyanzo vya ndani, lakini pia kwa kutopata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshauri hapa kwamba, kwa mujibu wa kanuni na ni jukumu la kikanuni, lakini pia inatokana na Katiba, kama Bunge tuna wajibu wa kuishauri Serikali; wameshauri kwamba suluhu ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo Serikali inafanya sasa hivi, natambua ujenzi wa reli ya kisasa, Stiegler’s Gorge, lakini ununuzi wa ndege na miradi mikubwa kwa mfano kule Mkulazi pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iridhie ushauri wa Bunge lako kupitia Kamati ya Bajeti na michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sasa kwa mazingira tuliyonayo na uwezekano wa kukusanya vyanzo vya mapato ambavyo tumeviainisha kwenye bajeti kwa asilimia 100 ni mdogo, tunaiomba Serikali na naamini kwamba Mheshimiwa Rais anafuatilia mjadala huu, tukakope kwa masharti nafuu. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametuthibitishia kwanza kukopa siyo dhambi, lakini sisi kama Taifa kwa mahesabu yetu bado tunakopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali itafakari jambo hili. Najua kuna kipindi fulani ilionekana kwamba pengine kukopa kungetuongezea madeni (liability), Deni la Taifa, lakini kwa nchi kama yetu, kama nchi tajiri zinakopa kwa nini sisi tujivunge kukopa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali ikakope kwa mikopo yenye masharti nafuu ya muda mrefu, tujipe muda kwa vyanzo vyetu vya mapato vilivyopo ndani, tupumue, lakini tuweze kutekeleza miradi inayogusa wananchi moja kwa moja, miradi inayohusu Sekta za Kilimo, ambacho ndiyo kipaumbele, kinabeba wananchi zaidi ya asilimia 66, lakini mchango wake tunaona kwenye pato la Taifa ni 4% tu. Hili ni jambo ambalo tunahitaji kuliongezea muda wa kulifanyia kazi vizuri. Kwa hiyo, tukakope, lakini tuishirikishe sekta binafsi na pia tufanye miradi kupitia utaratibu wa ubia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalizo lake, nchi zote duniani zinapoelekea kwenye chaguzi na hasa miaka ya uchaguzi, bajeti zake huwa zinaathiriwa kwa sababu ya suala la uchaguzi. Sisi Tanzania mwaka kesho tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2020 tuna Uchaguzi Mkuu; vyovyote itakavyokuwa hatuwezi kukwepa kwamba kuna rasilimali fedha nyingi na hasa ya ndani itakwenda kwenye uchaguzi. Kwa sababu hiyo ndiyo msingi katika mustakabali wa Taifa letu. Tutafanyaje kama hatutakuwa na mikopo yenye masharti nafuu ya kutusaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaomba sana Serikali izingatie ushauri huu, tufungue milango, tukakope kwa masharti nafuu, tuendeleze nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchambuzi, lipo jambo nimeliona nikasema niliseme tu niishauri Serikali. Kwa namna ambavyo lipo kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti ni kama linaashiria hivi, kuna taratibu ambazo tumeziweka kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu ni kama kuna viashiria hivi tunaelekea kuvikiuka. Hatujafikia hatua hiyo, kwa sababu Hotuba ya Bajeti na Mheshimiwa Spika, alielezea vizuri sana siku ile wakati Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alivyowasilisha kwamba haya mapendekezo tunayoyajadili sasa hivi, sisi ndio tunatengeneza bajeti ya nchi. Nashauri kwa yale maeneo ambayo Kamati yenu mliyabaini Serikali isikilize ushauri, kwa sababu viashiria vyake sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza inaonekana kuna viashiria vya kukiuka sheria kuhusu matumizi ya fedha ambazo zimetengwa kwa maeneo maalum na hasa Mifuko mbalimbali ambayo imeanzishwa kisheria. Halijafikia pabaya kwa sababu, sisi ndiyo tunaamua, hebu tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine inaonekana Kamati imebaini kwamba Wizara ya Fedha na Mipango inaanzisha utaratibu wa kubadili matumizi ya fedha zilizotengwa kisheria kwa ajili ya matumizi maalum. Sasa hili siyo jambo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili la kupendekeza kuanzisha Akaunti Maalum ama Akaunti Jumuifu ya Hazina. Sasa ukisoma ukurasa wa 40 mpaka wa 41 tumeelezwa kwamba hii imetokana na makubaliano ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; lakini Kamati ya Bajeti ilipozamia kule imebaini kwamba kumbe sisi kama nchi tuna fursa ya kuliangalia jambo hili kwa namna yake; na madhara yake ni kwamba kama itaanzishwa hii single account maana yake ni kwamba hata ile Mifuko ambayo tumeanzisha kisheria tukatenga fedha, kama suala la umeme, masuala ya barabara, reli na masuala ya korosho na mengine, miradi ya maji, nazo zitahitajika kwenda kwanza Mfuko Mkuu wa Hazina halafu ndio zije. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa ushauri wangu ni kwamba jambo hili linahitaji mjadala mpana zaidi, ni zaidi ya kupitia kwenye bajeti hii, kwa sababu, tulianzisha sheria maalum na mpaka sasa ukiangalia ni kama hatujaathirika, matokeo yake naona mifuko ile imekuwa ikitekelezwa kwa utaratibu ambapo matokeo yake ukiyapima ni chanya zaidi kuliko hasi. Sasa labda tujipe muda zaidi tuangalie, tuendelee na utaratibu, twendenao kwa sasa, lakini kama kuna haja ya kufanya hivi, basi tufanye mjadala mpana zaidi kuliko ilivyo sasa kupitia utaratibu wa bajeti kwa sababu, tukifanya vile tunaweza kuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti tumeyabaini kwa mfano, makusanyo ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania, ziko fedha zaidi ya 1.5 trillion. Sizungumzii lile suala la CAG, zimesemwa hapa kutokana na masuala ya kodi kulikuwa na mabishano na makampuni fulani, hazijakusanywa kwa sababu ambazo hazijaeleweka. Sasa kama Serikali yenyewe kuna mambo haijayaweka sawa, tunashauri kwamba tusiongeze tena mzigo wa fedha zote kwenda kule. Tujipe muda kidogo, nadhani tunaweza kufanikiwa, lakini wazo inawezekana limekuja kwa nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naona kama kiashiria chake siyo kizuri, tunasema tukisoma Katiba yetu ya nchi, Ibara ya 145 na Ibara ya 146, zimeanzisha utaratibu wa Serikali za Mitaa maalum kabisa na zikatambuliwa. Hili jambo nilivyokuwa nalisoma kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti, ni kama vile Kamati inasema: “Kwa namna ambavyo baadhi ya hatua zinazochukuliwa za Serikali Kuu ni kama vile zinakwenda kuathiri uhalali na umuhimu wa kuwepo kwa hizi Mamlaka za Serikali za Mitaa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siyo jambo zuri sana, kwa sababu, ile Decentralization By Devolution tuliyoanzisha miaka ile kwa mujibu wa Katiba, lakini pia mwaka 1998 kulikuwa kuna Tamko la Kisera na tunafahamu manufaa ambayo tumeyapata; na kwa sababu, kuanzisha utaratibu ule ilitokana na uzoefu ambao tuliona kwamba kuendesha nchi kwa msingi wa kutoka Serikali Kuu peke yake ni mgumu sana duniani na utaratibu huo umekwaza baadhi ya nchi nyingi tu duniani na ndiyo maana sisi tuka-opt kwenda kwenye hiyo route ya kusema tuwe na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za Mitaa ni Serikali kamili kabisa. Kwa hiyo, nashauri kwamba tupunguze uwezekano wa kiashiria hiki kushamiri kwa sababu bado tuna muda na jambo halijaharibika na Waheshimiwa Wabunge tulitazame Kitaifa zaidi, tusiangalie kwamba kwa kufanya hivi tutakuwa tunakwaza kitu gani, hapana. Ni kwa faida yetu, nami naamini kwamba utaratibu ule haujatuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunafahamu kwenye ngazi ya Halmashauri, wapo Madiwani, zipo Halmashauri zimeshindwa kufanya vikao vyake kabisa na hawajalipwa stahiki zao kwa sababu hakuna fedha. Ni kwa sababu tunazi- cripple. Nashauri kwamba, hili jambo tuliangalie tena na naamini kwamba bado tuna fursa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Deni la Taifa, napendekeza solution tu. Mengi yamesemwa, lakini nataka nirejee miaka ya 1990 ilivyokuwa. Serikali ilikuwa na utaratibu wa kununua dhahabu, baadaye baadhi ya Watendaji hawakufanya vizuri sana, hatukufanikiwa, tukajiondoa, lakini wakati tunajiondoa wakati ule bei ya dhahabu kwa mfano kwa kigezo cha ounce… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya dhahabu haikuzidi dola 270, leo ni zaidi ya dola 1,400. Kilichotokea ni nini? Shilingi toka miaka ya 1990 Serikali tulivyojitoa kwenye kununua dhahabu, shilingi yetu imeporomoka kwa kiwango cha 80% na wataalam wa uchumi wako hapa wanaweza kurekebisha, lakini dhahabu imepanda ka zaidi ya 700%. Tungekuwa na dhahabu zetu ambacho tungekuwa tunafanya katika wakati wa mshtuko, unatoa dhahabu yako kutoka kwenye ghala lako, unaingiza sokoni unauza, unapunguza Deni la Taifa. Nikadhani kwamba Serikali itafasiri hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa gesi. Miaka ya 1992 tulipigwa na ukame ndiyo maana yakaja masuala ya IPTL ambayo yamekuja kuliyumbusha Taifa, ilitokana na ukame. Kutegemea chanzo kimoja kuna risk kubwa.

Ninashauri kwenye eneo ambalo nalifahamu kidogo. Suala la gesi tuliyonayo, leo tunajivunia trilioni 57 cubic feet za gesi ambazo tunasema ni probable, lakini ukizileta sasa kwenye uzalishaji normaly unazalisha 30% ya hiyo gesi uliyonayo. Asilimia hiyo 57 tunayoizungumzia, unaongelea trilioni 10 ziko nchi kavu, trilioni kama 40 na kitu ziko baharini kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ianze kuwekeza kwenye hii gesi iliyoko nchi kavu, kwa sababu, tusitegemee chanzo kimoja tu cha miradi ya maji, ni hatari kubwa kwa Serikali ya viwanda ambayo tunaitarajia kama tutakuwa na chanzo kimoja. Miaka ya 1990 tulikwama na ndiyo maana tukaenda kwenye mipango ya dharura, matokeo yake tukaja kuyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda huu tunaouzungumzia, hauwezi kuhimiliwa na Megawati 2,100 tu za Stiegler’s Gorge ama za viwango vingine vilivyoko hapa, ni pamoja na miradi ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana. Serikali itafakari, twende kwa pamoja, uwekezaji wa Stiegler’s Gorge ni mzuri, lakini tusipuuze pia suala la uwekezaji katika sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nami naanza kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla kwa hotuba yao nzuri, lakini pia na mipango ambayo wameonesha katika hotuba yao.

Mheshimiwa Spika, katika maisha ya mwanadamu hakuna jambo lisilokuwa na changamoto, lakini kiukweli kabisa ukifuatilia utendaji kazi wa Wizara kwa sasa pamoja na wasaidizi wao, unaungana tu na wanaosema usipokuwa muungwana hutakubali hata kidogo unachokipata, lakini ukiwa muungwana utasema ahsante. Tunazungumza hapa lakini kila mmoja anazungumzia eneo lake na ndilo lenye uzoefu kuonesha namna ambavyo mipango ya Serikali kupitia Wizara hii ilivyosimama vizuri ama kama ina kasoro zinazohitaji kufanyiwa maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Katibu Mkuu Injinia Kalobelo, nikitambua staff nzima ya Wizara ya Maji nimtaje Mkurugenzi wa Maji Vijijini, kaa sijakosea Engineer Mafuru. Kwa wale ambao tumepata nafasi ya kufanya nao kazi utakubali kwamba wanajitahidi kwa kadri inavyowezekana kuisukuma sekta hii kuisogeza mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu mimi ni miongoni mwa watu wanaotoa ushahidi wa kuona kwa sababu nimekaa nao na nimeona reflection ya yale ambayo tumeyazungumza wakati tunafuatilia miradi kwenye hotuba hii. Hapa nazungumzia kuona utekelezaji wa visima vya Vijiji vya Nyamililo, Mlaga, Imalamawazo, Nyamatongo, Kinyenye, Ishishang’olo, kule Sengerema sasa, maana yake hapo nazungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Hivi ni visima ambavyo nimeahidiwa baada ya kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naona kuna miradi ambayo inatekelezwa kutokana na chanzo cha Ziwa Victoria. Hapa nauona Mradi wa Buyagu, Kalangalala hadi Bitoto nakotoka mimi.

Pia naona Mradi wa Chamabanda kwenda Nyandakubwa, ni mambo ambayo tumezungumza nao yameingizwa kwenye mpango na hatimaye tunaiona taswira ya hotuba ikiwa imezingatia haya ambayo tumezungumza nao. Ndiyo maana nasema wanachokistahili tuwape, lakini kwenye changamoto tuwasaidie kuboresha mazingira ya kazi yalivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Sengerema pia tumepata bahati, Sengerema tuna hadhi ya Mamlaka ya Mji na tuna mradi mkubwa wa maji ambao Mheshimiwa Rais mwaka jana aliuzindua tarehe 4 Julai. Ni mkubwa kiasi kwamba wana mitambo ambayo mpaka sasa hivi hatujaweza kuitumia kwa ukamilifu. Kwa kuzingatia hilo, tumekuwa na mipango ya kupanua miundombinu iwafikie wananchi wengi zaidi katika vijiji vingi zaidi. Hapa nauona mradi huo ukiwa umetengewa fedha kwa ajili ya kuuboresha kuwafikishia wananchi maji katika vijiji ambavyo mitambo ama miundombinu ya mradi huo inapita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri nasema imeandaliwa kutokana na mambo mengi, moja ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mpango wa Maendeleo Awamu ya Pili, pia umezingatia ahadi na maelekezo ya viongozi wetu wakuu na hapa nazungumzia kuanzia Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Sengerema lilivyo tuna bahati ya aina yake, Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, anapokwenda Chato kama anatokea Mwanza lazima atapita Jimbo la Sengerema. Kwa sababu ni Mheshimiwa Rais aliyechaguliwa kutokana na kura za wananchi ni utaratibu wa kawaida kila anapopita anazungumza na Wanasengerema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Sengerema tumebahatika kupata ugeni wa Mheshimiwa Rais mara mbili toka achaguliwe na amezungumza na wananchi pamoja na mambo mengine amezungumzia habari za maji, ameahidi kufikisha maji katika baadhi ya maeneo. Nawashukuru wataalam na Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanyia kazi ahadi ambazo Mheshimiwa Rais ametoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumzia mpango wa kufikisha maji kwenye Kijiji cha Nyampande ambacho Mheshimiwa Rais aliahidi, lakini pia naona mipango ya kufikisha maji kwenye Vijiji vya Sima, Tunyenye, Nyamililo pamoja na Nyamahona ambako ndiyo chanzo cha maji kinaanzia. Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara hii kwa namna ambavyo imezingatia ahadi ya Mheshimiwa Rais na inaonekana katika hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukipitia majedwali ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, katika ukurasa wa 124 unaelezea fedha ambazo zimegawiwa katika halmashauri mbalimbali kusaidia miradi ya maji vijijini. Naishukuru Serikali kwa sababu Sengerema tumepagiwa shilingi 1,700,000,000. Ahsanteni sana kwa kutusikiliza na kuzingatia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ambayo yanakwenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa Watanzania. Kwa sababu miradi hii itakapokamilika kwa hakika kwa vyovyote vile tutakuwa tumefaidika.

Mheshimiwa Spika, lakini nauona Mradi wa Nyasigu, Lubungo, Ngoma A ambao sasa hivi mchakato wake unaendelea, Serikali mlishatupa kibali, tenda ilishatangazwa, tunakamilisha taratibu za kupata mkandarasi. Nauona Mradi wa Chamabanda/Kasomeko; nauona Mradi wa Kamanga/ Chinfunfu na hapa ndipo napompongeza sana Mkurugenzi wa Maji Vijijini, Engineer Mafuru, ametusikiliza, ametuma wataalam wamekuja kufanya upembuzi wa awali na hatimaye wameonesha kwenye mipango yao ya utekelezaji. Kwa hiyo, sisi Sengerema tunasema ahsante sana, kwa hapa mtakuwa mmetusaidia kupunguza adha ya Watanzania kwenye kiwango cha maji wanachokipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali, ukisoma ukurasa wa 189 utakuta Miji ya Sengerema, Nansio na Geita tumetengewa shilingi bilioni 4.7 na huu ni mwendelezo wa miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa katika miji ambayo inazunguka Ziwa Victoria. Ninachokiuliza na naomba Serikali mfafanue mtakapokuwa mnafanya majumuisho, katika utatu wetu huu, huu mgawanyo wa shilingi bilioni 4.7 umesimamaje, Sengerema sisi chetu ni kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kitabu hapa kinavyoonesha mmetufunga wote watatu, mnasema ni shilingi bilioni 4.7. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi ukurasa wa 189; Nansio wanapata kiasi gani huko Ukerewe, Geita wanapata kiasi gani na sisi Sengerema tunapata kiasi gani ili iwe rahisi kufuatilia kujua Wanasengerema wanastahili kiasi gani na tunachokistahili kuwafikishia wananchi kwa sababu hizi fedha zinakuja kuendelea kuboresha hudumaya maji katika Mji wa Sengerema na vijiji vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezungumza kwa mtazamo tofauti hapa Bungeni. Tupo tunaoamini kwamba changamoto kubwa iliyopo katika Wizara hii siyo fedha isipokuwa ni utekelezaji na tupo tunaoamini kwamba fedha ni tatizo. Mimi naamini kwamba pamoja na yote yanayofanyika lakini bado kuna ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, tuna taarifa hapa ya Kamati inaonyesha kiwango cha fedha ambacho kimeshatoka kwenye miradi ya maendeleo kinatofautiana na ambacho kimesemwa na Mheshimiwa, tunaamini Mheshimiwa Waziri atakuja nalo. Taarifa hizi zinavyosema ni mpaka tarehe 31 Machi, lakini leo ni tarehe 8 Mei, inawezekana Serikali labda ina taarifa za hivi karibuni hatujui lakini watasema wao.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kusema kwa vyovyote vile fedha hizi hazitoshi kutufika kwenye lengo letu la kufikisha maji mijini asilimia 95 na vijijini asilimia 85 mwaka 2020. Kwa hiyo, lazima tufanye yale ambayo tunaona yanaweza kutufikisha mbali.

Moja ni hilo ambalo tumekuwa tukisema, naungana na taarifa ya Kamati kwamba tuongeze shilingi 50 kwa mara nyingine kwenye mafuta ya dizeli na petroli. Tulifanya mwaka jana zimepatikana fedha kiasi fulani na zimetufikisha pazuri na sasa naomba tena tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisema hapa, tulivyoanzisha Wakala wa Umeme Vijijini tulifanikiwa sana na hivi karibuni kwenye barabara tumetengeneza TARURA na hapa tulisema tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini, tunaomba hili jambo likamilike. Najua Serikali inasema kwamba mchakato wa kuanda wakala huo unaendelea, tunaomba basi ifanyike haraka ili tuone manufaa tuliyoyakusudia kwa sababu tunaamini tukiwa na wakala unaosimamia maji vijijini tutafika mbali zaidi kwa kasi kubwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu skimu za umwagiliaji, narudia hoja yangu ya kila mwaka, ukisoma hata Hansard utaona, nadhani Wizara ya Maji mnanisikia vizuri, tumeongea na watendaji, sina hakika kama mnayo inventory ya miradi ambayo Serikali ilishaianzisha lakini ikakwama na haiendelei. Kwangu wamesema kuna huo Mradi wa Katunguru, kwa nini fedha mlizoziweka pale shilingi milioni 700 hamuongezi tuukamilishe kwa sababu ulikuwa unahitaji shilingi bilioni 2.5.

Mheshimiwa Spika, nimepata maelezo kwamba wanafanya uchambuzi kwanza waone hatua za kuchukua, nasema kwa niaba ya wananchi wa Sengerema tukamilishe uchambuzi huu haraka halafu mradi uendelee kwa sababu shilingi milioni 700 zilizowekwa pale ni kama zimetupwa na sisi hatuamini kama Serikali ilikuwa nia ya kutupa fedha hizo. Kwa hiyo, naomba sana huu Mradi wa Katunguru tuukamilishe.

Mheshimiwa Spika, mawili ya mwisho, moja, taarifa katika ukurasa wa 97 Serikali imetukumbusha Waheshimiwa Wabunge hapa madeni ambayo taasisi zake zinadaiwa na hasa hizi Mamlaka za Maji kwenye maeneo mbalimbali imewasilisha madeni hayo Wizara ya Fedha ili yalipwe juu kwa juu. Nazungumza hili nikikumbushia kilichotokea mwishoni mwa mwaka jana na mwazoni mwaka huu, Halmashauri nyingi ziliathirika ikiwemo Sengerema, wananchi waliadhibiwa na kama tunavyofamu hakuna fidia, wananchi wameumia kwa makosa ambayo hayakuwa ya kwao. Kwa yale madeni ya Serikali tunaomba jambo lile lisijirudie na niipongeze Serikali kwa kuonesha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa siyo kwa umuhimu, miradi mingi hapa tunalalamika Waheshimiwa Wabunge siyo kwa sababu haina wakandarasi mingi ina wakandarasi lakini certificate walizonazo ambazo wamekuwa wakizileta kwa utaratibu wa kawaida wapate huduma waendeleze kazi zile hazijalipwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, naomba certificates ambazo zimeshaletwa Wizara zilipwe ili miradi iendelee.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa yale aliyotujalia.
Pili, nikupongeze wewe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nakuomba unifikishie salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Spika pamoja na Wenyeviti ambao tumewachagua hivi karibuni kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutuongoza. Naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ambayo kwa kweli, mimi nailinganisha na tangazo la vita, kwa namna ambavyo ilipangiliwa, lakini kwa namna ambavyo imetoa taswira ya kero za Watanzania na mikakati iliyopo ya namna ya kuzitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wenzangu wamesema mengi, lakini kama ninavyosema hili ni tangazo la vita kuhusu maadui zetu wale ambao walianza kutajwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ujinga, umasikini, maradhi, lakini sasa yakaongezeka pia ufisadi, rushwa, uzembe na mambo ambayo yanakwaza maendeleo yetu, sina budi na mimi kupita katika baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya kurasa 36 aliyoyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana kwa dhamira yake aliyoionesha na tayari ameshaanza kutenda kwa matendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili ni tangazo la vita kwa sababu Mheshimiwa Rais baada ya hotuba yake na hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri na kwa nafasi hii pia nawapongeza sana wateule Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wengine ambao wameteuliwa kumsaidia Mheshimiwa Rais; tayari Mheshimiwa Rais aliingia vitani, alishaanza kufanya kazi na akaanza kutumbua majipu kwa lugha ambayo imezoeleka sasa kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana, lakini kubwa tunazungumzia uwezeshaji wa huduma kwa Watanzania ambao sisi ni mojawapo ya wadau wakubwa sana katika kuwezesha hilo. Lakini tunapozungumzia kuimarisha huduma za Watanzania tunazungumzia uwezo wa makusanyo ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha inayopatikana kutoka kwenye makusanyo yanayofanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya na sisi Watanzania wote, tukiwemo sisi Wabunge, ni dhahiri na jambo la msingi kumuunga mkono na kumpongeza ni hili la kuongeza mapato. Kwa muda mfupi tu ambao amekuwepo Ikulu, kama Kiongozi wetu Mkuu wa Taifa, Mheshimiwa Rais amefanikisha kuongeza mapato ya Serikali yanayokusanywa kwa mwezi kwa kiwango ambacho kimetangaziwa Watanzania, kwa mwezi uliopita tuliambiwa makusanyo yalikuwa shilingi trilioni 1.4! Si jambo dogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba kwa mwendo huu dira ambayo inaonekana sasa, tunajenga uwezo wenyewe wa Taifa kwenda kusimamia kwa kiwango kikubwa sana kuwezesha utekelezaji wa huduma mbalimbali na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine, ametuambia na Watanzania tunakiri kwa matendo anayoyafanya kwamba, anataka kuiona Tanzania ya Viwanda katika kipindi chake cha utumishi wa takribani miaka 10 ijayo, tunaamini itakuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda tunazungumzia mambo mengi, lakini mimi hapa ni mwakilishi wa Jimbo la Sengerema ambako ninawashukuru sana wananchi hawa walionituma, nikiunganisha nguvu na wawakilishi wa Majimbo mengine kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, tunapozungumzia viwanda kwa vyovyote vile tutashuka chini kuzungumzia viwanda vinavyotuhusu katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuungana na wenzangu ambao wamekuwa wakizungumzia umuhimu wa kuwa na viwanda katika Taifa letu na kwa Kanda ya Ziwa na hasa Mkoani Mwanza, Jimbo la Sengerema, viwanda ambavyo navizungumzia hapa ni vile ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza sana, viwanda vya pamba. Nazungumza hapa nikiwa namuona Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini nawaona pia, baadhi ya Mawaziri ambao wanahusika na mambo ambayo yanabeba uchumi wa Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nijielekeze zaidi kwenye maeneo haya, zao la pamba. Ninafahamu, Mheshimiwa Rais kwenye kampeni zake amelisisitiza sana, kufufua viwanda vya kuchambua pamba, lakini na viwanda vingine ambavyo vinategemea mazao ambayo tunayalima katika Kanda ile. Sisisitizi hili katika mtazamo wa Kikanda, nazungumzia yale ambayo wananchi wa Jimbo la Sengerema na Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanatarajia kuyaona yaki-reflect ile dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika eneo la viwanda, si pamba tu! La pili, ni hasa mazao ambayo yanatokana na samaki, mazao yanayotokana na mifugo na mazao yanayotokana na kilimo kwa ujumla. Katika hili, naungana na Mheshimiwa Rais, juzi alipokuwa Arusha alisema na mimi nawaomba Waheshimiwa Wabunge eneo hili tumsaidie sana Mheshimiwa Rais pengine kwa kutolea maelekezo au kupitia Azimio kwa kadri itakavyokuwa ama kupitia taratibu za Kamati zetu mbalimbali za Bunge, hili la kulishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kuendesha na kusimamia baadhi ya viwanda ambavyo tunaviona vinaweza kutumia rasilimali ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo la kuachia lipite hivi hivi, kwa sababu tunaliweza, tunaweza kulifanya, malighafi iliyopo hapa hapa nchini, nikadhani kwamba ni jambo la msingi Bunge lako Tukufu tujipange tuone namna ambavyo tunaweza kum-support Mheshimiwa Rais kutekeleza hiyo azma ya kuweza kuwa na viwanda ambavyo Wanajeshi kwa ujumla wao wanashiriki katika kusukuma hili eneo la viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuzungumzia linahusu sekta ya afya. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, pale Sengerema tuna hospitali ya mission ambayo imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya, na kwa utaratibu wa sera ya afya hiyo hospitali ina hadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Kimkoa. Hospitali ile tumekuwa na matatizo ya muda mrefu, nimeyazungumzia sana, lakini kikubwa ambacho ninakizungumzia sasa hivi ni kwamba, ruzuku inayopatikana kwenye hospitali ile haitoshelezi na miaka kadhaa tumekuwa tukiomba na hatujafanikiwa sana katika ombi letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahesabu ya ruzuku yanatokana na vitanda 150 vilivyokuwa vinatajwa kipindi kile wakati Mkataba wa Serikali na wa-missionary wenye hospitali hii ulivyofungwa, leo hii ina vitanda zaidi ya 300. Ninachoomba Mheshimiwa Waziri wa Afya, ombi letu liko Wizarani pale, ninakuomba sana ombi letu ulizingatie la kuongezewa ruzuku kutokana na vitanda ambavyo viko pale vinavyohudumia wananchi wa Jimbo na Kanda ile ya Sengerema.
Mheshimiwa Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais inayoshughulika na masuala ya TAMISEMI, Mji wa Sengerema mnaufahamu Jimbo la Sengerema, Wilaya ya Sengerema mnaifahamu, Mji wa Sengerema una hadhi ya Mji Mdogo, lakini kwa miaka minne iliyopita tulileta ombi letu na tulikidhi vigezo wa kuubadili ule mji ufikie Halmashauri ya Mji. Nafahamu Serikali imekuwa ikishughulikia jambo hili, nina wajibu wa kukumbushia hili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, kwamba tunamba ombi letu la kufanya Mamlaka Mji Mdogo wa Sengerema ifikie hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Simbachawene kuna lingine tuliongea na wewe la madawati, ombi langu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, sisi tulikuwa na Kikao cha RCC kule Mkoani, tumezungumza tukasema Wakuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa malengo na Serikali ya kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi na sekondari, inakuwa na madawati ya kutosha. Sasa sisi Wilaya ya Sengerema tumebahatika kuwa na msitu wa Serikali shamba la miti linafahamika liko Jimbo la Buchosa na kwa sababu Wakuu wa Wilaya na Mkoa wamepewa mamlaka ya kuomba ridhaa ama kupata vibali kutoka Mkoani, nilikuwa naomba sana tusaidiane pamoja na Mheshimiwa Profesa Maghembe tupate hivyo vibali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aelezwe na Wakuu wa Wilaya ili sisi tutengeneze madawati kwa ajili ya kusaidia vijana wetu wanaosoma katika shule za sekondari na sule za msingi kwa Wilaya na Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Bunge hili linahitaji kutengeza action plan, namna ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kuitekeleza hotuba hii ina mambo mengi. Sisemi hili kwa maana ya kwamba hatuiamini Serikali yetu, lakini sisi kama wadau muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo, na naamini unalifahamu na mkakati naamini wa Kamati ya Uongozi upo, sisi ni muhimu sana tutengeneze action plan kwa masuala yanayozungumziwa hapa tuone ni namna gani tunajipanga kumsaidia Mheshimiwa Rais na moja ni hili ambalo tumeshalifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamati ya Sheria Ndogo imeundwa ni Kamati mpya, mimi ni mmojawapo ya Wajumbe katika Kamati hiyo, ninaamini kwamba tutakuwa na jukumu la kupitia sheria zote ambazo ni kero kwa wananchi na hasa zinawezesha kutoa ushuru ambao ni kero kwa wananchi katika Halmashauri zote za nchi yetu. Lakini tukishakuwa na action plan katika Bunge hili tutaisaidia sana Serikali kuikumbusha kutekeleza yale ambayo yamesemwa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana, nakupongeza sana, naungana na wenzangu kwa mara nyingine tena kuunga mkono hoja, kuunga hotuba hii nzuri ambayo ni tangazo la vita kwa ajili ya kuondoa na kupunguza umasikini wa Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa hiyo fursa uliyonipatia ya dakika tano, nashukuru sana. Nimesimama hapa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wanzangu kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo inatuunganisha Watanzania endapo mambo haya yatatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea kuchangia, wiki moja iliyopita Taifa zima lilipata habari ya mauaji yaliyotokea Jimboni Sengerema. Nasimama hapa kwa niaba ya Wanasengera na Watanzania wengine kuwaombea marehemu wetu waliouwawa kikatili sana, Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia navishukuru sana vyombo vya habari kwa jinsi ambavyo vimezungumzia jambo hili na kupeleka ujumbe mahsusi kwa jamii. Kwa fursa hii navishukuru na kuvipongeza sana vyombo vya dola kwa namna ambavyo vimefanya kazi kubwa na kwa kweli sasa hivi watuhumiwa wameshatiwa mbaroni na naamini kwamba haki itatendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa sababu ya matumaini kwamba yakitekelezeka yaliyomo humu ndani Taifa litakuwa linasonga mbele kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ninalotaka kuzungumzia ni masuala ya jimboni kwangu. Nimeona pale kuna masuala ya ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi, zimetengwa shilingi milioni 600, naipongeza sana Serikali kwa ajili ya kupata Mhandisi Mshauri ili afanye usanifu, mambo ya design na mambo mengine ili hatimaye ujenzi wa daraja uanze, naishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwaka jana tulipitisha bajeti ya ununuzi wa kivuko kingine hapo hapo Busisi Kigongo na hapa tumeelezwa kwamba taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu, taratibu za kufanya upembuzi yakinifu ulishakamilika na sasa taratibu za manunuzi ya hicho kivuko yanaendelea vizuri. Nashukuru sana na naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku nne zilizopita tulikuwa na sakasaka na hekaheka kule Sengerema kwenye kivuko cha Kamanga. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana pamoja Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wako kwa kutatua hilo tatizo na sasa vivuko vyote vinafanya kazi, kwa hiyo nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu nimetengewa fedha za matengenezo ya barabara lakini nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri nafahamu kwamba hii ni bajeti ya kwanza kama walivyozungumza Wabunge wengine, siyo rahisi sana mambo yote yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hata kwenye mipango yetu yakawa reflected kwenye bajeti hii. Nonachoomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho asisahau kuzungumzia barabara ya Kangama - Sengerema kilometa 35 ambapo ukisoma Ilani ya Uchaguzi, ukurasa wa 60 utaona imehaidiwa kujengwa kwa lami. Pia kuna barabara nyingine ya Sengerema – Nyehunge, Jimbo la Buchosa kwa Mheshimiwa Dkt. Tizeba, kilometa 68 iko kwenye ahadi. Tuna barabara nyingine ya kutoka Busisi, Jimbo la Sengerema kwenda Jimbo la Nyang‟hwale na kuelekea Msalala hadi Kahama kwenye Jimbo la Mheshimiwa Maige. Hii ni barabara ambayo imeahidiwa na Mheshimiwa Rais kujengwa kwa lami. Ni barabara inayounganisha mikoa mitatu, mkoa wa Mwanza, Geita pamoja na Shinyanga. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho azungumzie hilo pia kutupa matumaini kwamba mipango ya utekelezaji itafanyika lini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la reli limezungumzwa sana na hasa nazungumzia reli ya kati. Kitu ambacho nataka niseme, hizi hotuba zinavyokuja hapa zina miongozo yake, hotuba tunazozijadili hapa zinaletwa kwa miongozo. Mojawapo ya mazingatio ambayo hotuba hizi zinatakiwa kuyazingatia ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa sababau ndiyo Serikali iliyoko madarakani lakini pia na ahadi na maagizo au maelekezo ya wakuu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia ujenzi wa reli ya kati, jambo hili siyo jipya wala siyo geni, tumelizungumza kwenye Mpango wa Maendeleo, tumelizungumza katika mazungumzo yetu ya kawaida na pia tumekuwa tukizungumza katika bajeti zilizopita. Kwenye Ilani yetu unafahamu, ukisoma ukurasa wa 66, ahadi ya 69 utaona tumesema upembuzi yakinifu ulishakamilika, kwa hiyo ilikuwa ni kwenda sasa kufanya upembuzi wa kina zaidi ili hatimaye ujenzi uanze na kikwazo kikubwa ilikuwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa uchungu kwa sababu inavyokuja ni kama vile ujenzi wa reli ya kati haujawekwa wazi hapa. Ukisoma ukurasa wa tano na wa sita wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema, hotuba hii imetayarishwa kwa kuzingatia Ilani ya uchaguzi, mambo mengine pamoja na maagizo ya Serikali. Tarehe 25 Aprili, Serikali kupitia Msemaji wa Ikulu, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano…
NAIBU SPIKA: Kengele ni moja Mheshimiwa Ngeleja, dakika tano zimekwisha.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimesimama hapa kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama ambavyo imewasilishwa kwa uzuri. Pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, pia natumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote katika Wizara Kuu inayosimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natumia fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati, Taarifa zilizowasilishwa hapa, zimefanya uchambuzi mzuri unaoturahisishia sisi kuchangia katika hotuba hii. Ni jambo la msingi na kimsingi tumeelezwa hapo kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, utekelezaji ama taarifa yake hii aliyoitoa hapa akiomba fedha za utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika bajeti ijayo itakayoanza mwezi Julai mwaka huu umeongozwa na mambo matatu; moja ni ule Mpango Mkuu wa Miaka Mitano, lakini pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ujumla wetu hapa ni pamoja na kutoa ushuhuda wa namna ambavyo Serikali imekuwa ikitekeleza yale ambayo tumeyaahidi. Nasimama kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema kuwathibitishia Watanzania wenzangu kwamba, Serikali inatenda inayoahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza hapa, lakini moja kubwa ambalo nataka niwakumbushe Watanzania ambalo linaendelea sasa hivi katika Jimbo la Sengerema na Jimbo la Misungwi ni ule mpango wa ujenzi wa daraja kuu litakalounganisha Wilaya ya Misungwi na Wilaya ya Sengerema na hasa Jimbo la Sengerema. Tenda ilishatangazwa na imeshafunguliwa tayari na sasa wanaendelea na tathmini kumpata mkandarasi atakayefanya ujenzi. Hili ni jambo kubwa sana, linaunganisha sio Tanzania tu wala sio mikoa ya Tanzania, lakini ni pamoja na nchi za jirani zinazotoka upande wa Mashariki Kenya, lakini pia upande wa Magharibi DRC, Burundi, Rwanda na hata majirani zetu wa Uganda. Kwa hivi, jambo hili litaongeza, litasisimua uchumi, lakini pia, litapunguza bughudha na usumbufu ambao tumekuwa tukiupata abiria ama wasafiri tunaounganisha maeneo hayo ya kanda ya ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumesikia ujenzi wa meli katika Ziwa Viktoria, lakini Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Mambo haya ni makubwa ambayo yanakuja kuleta impact kubwa katika uchumi wa Taifa. Katika kutekeleza haya na kuhakikisha kwamba, Serikali inatekeleza na kutenda iliyoyaahidi ufuatiliaji wake pia, unafanywa na Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu hata Naibu Makatibu Wakuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa nikitoa shukrani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema kwa ugeni ambao tumeupata hivi karibuni, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mheshimiwa Kandege pamoja na Mheshimiwa Engineer Nditiye kutoka Wizara ya Ujenzi walifika Sengerema kujionea utekelezaji wa haya ambayo tunayazungumza. Katibu Mkuu Wizara ya Maji pia, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na wengine wametutembelea hivi karibuni, yote haya ni kutaka kuonesha kweli Serikali inachokizungumza ndio kile ambacho kinawafikia na wananchi kutendwa kwa ajili ya maslahi na manufaa yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi haya ni mambo makubwa ambayo tusipoyazungumza, kama ambavyo wenzangu wamekuwa wakiyasema, pengine mawe yatakuja yazungumze siku moja, lakini Serikali inafanya kazi kubwa na chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu kama mtendaji mkuu tukiongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kazi inafanyika. Hii kazi inayofanyika wala haihitaji hata majadiliano kwa sababu ni mambo ya kuyaona moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaitafuta kuifikia nchi ya viwanda Tanzania tunafahamu kwamba, tuna mzigo mkubwa wa miradi viporo. Nimesikia akitajwa hapa Mheshimiwa Chumi hapa na Mheshimiwa Chumi ni mwanzilishi wa hoja ya miradi viporo hapa kwa kadiri ambavyo tumeizungumza miaka miwili iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kutoa chagizo kwa Serikali. Najua sasa hivi fedha za miradi hasa ya sekondari zimeshaanza kutoka, lakini tuna miradi mingi inayohusu elimu ya msingi, miundombinu, nyumba za Walimu wa shule za msingi, lakini sekta ya afya kwa mfano, zahanati na baadhi hata ya maeneo ya vituo vya afya na ujenzi wa nyumba za Serikali za Vijiji pamoja na baadhi ya majengo katika ngazi ya kata. Naiomba Serikali kwa kadiri ambavyo iliahidi na hasa mwaka jana, tuliahidiwa hapa na Serikali kwamba, ilikuwa inakwenda kutimiza ahadi yake ya kupeleka fedha katika miradi yote ambayo imeanzishwa miaka iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii miradi viporo natoa msisitizo tena kuiomba Serikali, speed iliyoanzanayo sasa iendelee ili tuikamilishe hii miradi ili wananchi wetu waone thamani ya nguvu ambavyo tayari wameshakwisha kuitumia kwa sababu, tunafahamu mpango wetu wananchi wanajenga maboma Serikali inakuja kumalizia. Sasa kadiri tunavyochelewa tunawavunja nguvu wananchi, lakini pia tunaanza tena moja kwa majengo ambayo yatapata kuharibika hasa wakati huu wa mvua. Kwa hivi naiomba sana Serikali iikamilishe ahadi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanasengerema tuna jambo la kuishukuru Serikali, tumepata fedha za kuanza ujenzi wa hospitali itakamilikiwa na Serikali kwa ngazi ya wilaya. Tunasema ahsante sana Wizara ya Afya, ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kulisimamia hili. Tunafahamu sasa hivi kwamba, kuna programu ya ujenzi wa hospitali 67, lakini Sengerema pia, tumepewa taarifa kwamba, milioni 500 zimetengwa na zitafika Sengerema hivi karibuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya wilaya. Sisi tunasema ahsante sana kwa sababu, hatuwezi kuifikia nchi ya viwanda kama tuna wananchi dhaifu na ambao hawapati huduma nzuri za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaunganika pia na huduma za afya zinavyoimarishwa ngazi ya Kitaifa. Ni jambo jema, sasa hivi tumeona fedha ambazo zinaokolewa badala ya kwenda kutibiwa watu nje kwa maana kwamba, fursa ya kwenda kutibiwa ipo, lakini kwa sasa kwa kweli, kwa sababu, na kutibiwa nje kwa mara nyingi pia zimekuwa ni bajeti za watu binafsi, tunaona kabisa kwamba, ujenzi na uimarishaji wa sekta hizi unatupa afueni sana kama Taifa kuhusu uimarishaji wa huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linanipa msisimko na kuiunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni hili suala la kusisitiza sekta binafsi, limejitokeza sana na wazungumzaji waliozungumza kabla yangu wamelizunguza kwa kina kwamba, tunahitaji kuipa sekta binafsi nguvu na heshima inayostahili. Tunajua tumekuwa katika kipindi cha mpito na ndio maana ukiangalia kwa mfano katika aya ya 143, Ukurasa wa 67 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukiangalia takwimu za ajira kwa hotuba hii tunavyozungumza, kiasi kikubwa kimetoka kwenye sekta ya umma aslimia 66 na asilimia 34 inatoka kwenye sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu inatokana na miradi mikubwa inayofanyika sasa hivi ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, lakini sasa tunakwenda pia kwenye Stiegler’s Gorge, lakini pia, tuna miradi mingi mikubwa inayofanywa na Serikali. Hili ni jambo jema sana, lakini kwa asili tunafahamu kwamba, miradi ya umma mara nyingi ina vipindi vyake, itakapokwisha sekta ambayo itakwenda kututoa na kusisimua ajira kwa Watanzania walio wengi ni sekta binafsi. Ndio maana naungana na wenzangu wote na msisitizo aliotoa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, Serikali inajielekeza sasa kwenda kusisimua ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa Taifa letu. Ni jambo la heri, ni jambo jema, ni muhimu sana kuiunga mkono Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tunaweza kuyafanya, lakini tumejiwekea utaratibu kuendesha nchi yetu kwa misingi ya kisheria, nazungumzia utungwaji bora wa sheria. Kama unavyofahamu wewe ni Mwenyekiti wetu kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, tumekuwa tukitunga sheria bora, sheria mama, lakini sote tunafahamu miongozo inayoongoza utekelezwaji wa sheria nyingi nchini ni sheria ndogo. Nataka kuelezea msingi na umuhimu wa kuimarisha utungwaji wa sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfumo tulionao sisi kama Taifa, sheria ndogo hizi zinatungwa kwanza na Serikali, halafu ndio zinakuja katika Bunge kuzifanyia kazi kupitia Kamati ya Sheria Ndogo, lakini tuna ushahidi na ilifikia wakati fulani hali ilikuwa mbaya sana tulivyoanza Bunge hili. Hata hivyo, kwa kadri ambavyo taarifa zilikuwa zinaletwa kwenye Kamati yetu ilifikia mpaka asilimia 75 ya sheria ndogo zilizokuwa zinaletwa kwenye kamati yetu zina hitilafu, zina kasoro ambazo bila jicho la Bunge hili Tukufu kupitia Kamati yake ya Sheria Ndogo unayoiongoza wewe Mheshimiwa Mtemi Chenge wananchi wengi wangeumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa rai kwa Serikali kuendelea kuboresha utungwaji wa sheria ndogo. Ndio maana na ushahidi upo, juzi tulikuwa na mshikemshike wa suala la kanuni za kikokotoo, wote tunafahamu, Taifa lilisimama… ambazo hazikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa…

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na kwa hatua hii naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, nasimama hapa kuiunga mkono Serikali, kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote walioko katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yako mengi na muda ni mchache katika hotuba hii. Mimi nitajielekeza katika sekta ya michezo lakini pia sanaa. Mwaka huu umekuwa ni wa Taifa la Tanzania kwa mafanikio katika sekta ya michezo na hasa soka pamoja na tasnia ya sanaa. Wote tumeshuhudia tokea mwaka jana wakati ambapo Bunge lako Tukufu lilivyokwenda kushiriki Mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kule Bujumbura, Burundi, wachezaji wako wa timu ya Bunge Sports Club wakijumuisha michezo mbalimbali walishiriki kwa ufanisi mkubwa sana. Tumepata medali nyingi za kumwaga za Dhahabu, Fedha na nyingine ambazo zilikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kusema tu ni kwamba yote hii imetokana na maandalizi mazuri. Kwa nafasi ya Bunge Sports Club tunampongeza sana Mheshimiwa Naibu Spika, wewe Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati na Wabunge wote kwa ujumla kwa namna ambavyo mmekuwa mkiunga mkono sekta hii na sisi ndiyo wasimamizi wa sheria zinazohusisha mambo ya michezo, sanaa na mambo mengine. Kwa hivi tumetembea katika maneno yetu na tumeonyesha kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na tunampongeza sana Mheshimiwa Spika. Ndiyo maana hata leo asubuhi wakati anasimamia session ya maswali na majibu ametoa taarifa kwa Watanzania kupitia Bunge hili Tukufu kwamba tarehe 26 Aprili, tutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya Bunge Sports Club kwa football na netball pamoja na Baraza la Wawakilishi, ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ushiriki wetu si wa kupoteza muda kwa sababu tunatumia fedha za Serikali lakini pia zinatupa fursa sisi kama Taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujua na kufanya itifaki ama kufanya utafiti kwa yale ambayo yanatuhusu kwa manufaa ya Taifa letu. Kupitia hili dirisha la ushiriki wetu naamini kwamba Serikali kimkakati inaweza kujua kinachotokea kwenye nyumba za jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitazungumza kwa maneno mengi lakini nayafahamu Watanzania na hasa wanaoshiriki katika mambo yao kusimamia maeneo haya wanajua namaanisha nini. Ukijua kwa jirani kunatokea nini ni rahisi sana kujipanga na kujua kesho kutakuwaje kwa manufaa ya Taifa letu, kwa hivi tuendelee kuuunga mkono ushiriki wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili naipongeza sana Timu ya Taifa, mmefanya kazi kubwa Mheshimiwa Waziri Mwakyembe, Daktari na Mwalimu wetu pamoja na wenzako mmefanya jambo kubwa. Ni miaka 39 imepita tangu tushiriki Mashindano ya Fainali za AFCON mwaka huu tunakwenda kushiriki. Ni jambo jema sana, hatujafikia hapa kwa bahati mbaya ni kwa sababu ya maandalizi. Tumeona ushiriki wa Serikali na hata Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa hamasa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake, wananchi kwa ujumla na sisi kama Bunge tukiwa sehemu ya wahamasishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda fainali lakini fainali hizi zimechagizwa sana na ushindi wa Simba uliopatikana katika ushiriki wa Klabu Bingwa ya Afrika. Wote tunafahamu kwamba Simba imefikia kuingia hatua ya robo fainali, kuanzia ushiriki wa Mashindano haya Klabu Bingwa Afrika kwa ligi ya mwaka 2021 Tanzania kwa hatua iliyofikiwa na Simba Sports Club tunakwenda kuingiza timu nne; Kombe la Shirikisho zitakwenda timu mbili na Kombe la Klabu Bingwa zitakwenda timu mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Ushabiki pembeni ukweli ni kwamba kama Taifa tunatembea vizuri. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe na safu yako. Kwa ushiriki wa Simba tumepata pointi 15 kujumlisha na tatu ambazo Yanga aliziweka katika ushiriki wake wa miaka mitano, tumepata kile kigezo ambacho kinatuwezesha kuingia kwenye timu 12 na sasa tunapata ruksa ya kushirikisha timu nne katika mashindano haya makubwa, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kupata fursa hiyo tunakwenda kutangaza Taifa letu. Wachezaji wetu wanajitangaza, Mbwana Samata Samata alikuwa mchezaji wa Timu ya Taifa kabla hajakwenda TP Mazembe pale na sasa hivi anacheza katika ligi ya nchi ambayo kwa vigezo vya ubora wa soka duniani, Ubelgiji ndiyo timu ya kwanza kwa ubora wa viwango vya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna mchezaji anatoka Tanzania Mbwana Samata aliyewahi kukipiga katika Soka la Simba Sport Club na baadaye akaenda kule TP Mazembe, huyu ni mchezaji anayecheza ligi katika nchi ambayo kwa viwango ni FIFA namba moja duniani. Si jambo dogo na ni mfungaji bora anaongoza ana magoli 21 kwenye ligi, wapo akina Msuva na wapo wengi wanakuja. Kwa hiyo, ushiriki wa timu zetu nne utakwenda kuleta faida kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nataka kusema tunakwenda kwa sababu Serikali, wadau na sekta binafsi zinashiriki. Jambo langu ambalo nataka kulipendekeza kwa Serikali na hasa kupitia kwa Waziri mhusika hapa ni kwamba tuimarishe sana Sports Academy. Watu wote hatuwezi kuwa Wabunge, ma-engineer, walimu au kusoma mpaka vyuo vikuu, hizi ni fursa kwa manufaa ya Watanzania. Tujenge Sports Academy nyingi na ikiwezekana tujenge Sports Academy Kikanda na pale Sengerema tuna uwanja mkubwa sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu nilishamuomba na nishaiomba Serikali, tutakapofikia hatua hiyo kama Serikali itaridhia utaratibu huo, niiombe sana Serikali ije pale Sengerema ijenge Sports Academy kwa maana ya Kanda ya Ziwa, tutapeleka zingine Kanda mbalimbali lengo lake ni kujenga fursa kwa ajili ya kuendeleza michezo na ni jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naishauri Serikali, sasa tunahitaji kufungamanisha sekta ya michezo na hamasa tunayoiona pamoja na uchumi wake. Dunia nzima imeshuhudia na sisi wote ni mashahidi kwamba mataifa makubwa kiuchumi duniani yanawekeza pia katika michezo. Miaka 30 iliyopita Marekani ambalo ni taifa kubwa kiuchumi duniani lilikuwa halijajielekeza sana katika michezo lakini kuanzia mwaka 1994 waliibuka sasa na kuanza kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia hasa soka na hata michezo mingine. Nachotaka kusema sisi tufungamanishe uchumi wetu, kama tunasema uchumi wetu sasa unakua kwa kasi na tuko katika miongoni mwa nchi tano Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ni lazima i-reflect katika kuendeleza sekta za michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uchumi mkubwa hapa Afrika, South Africa, Nigeria, Egypt, wote wanafanya vizuri katika michezo. Kwa hiyo, tusibaki nyuma katika hilo na sisi ni ma-giant watarajiwa katika uchumi wa Afrika, tutumie nafsi hii ku-link uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watu wengi maarufu (celebrities), leo ukingia madukani pale New York City, utakuta majina ya Watanzania wamejifungamanisha kupitia shughuli za kibiashara na makampuni makubwa ya design. Wapo akina Flaviana Matata, Happiness Magesa (MiIlen), wapo Watanzania wengi. Leo tunao akina Diamond, Rayvan, Ally Kiba, hawa tunahitaji kuwafungamanisha wakashirikiana na sekta ya utalii naamini kwamba tunaweza kuendeleza vizuri sana sekta ya utalii na kufungua fursa kwa Watanzania wengi na hatimaye tukafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye mafanikio hapakosi challenges na nafahamu katika hili yako mambo ambayo tunaweza kufanya vizuri kwa sababu ya hamasa tu. Nataka nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mhamasishaji na Msemaji Mkuu wa Simba Sports Club, mtani wetu, Ndugu Haji Sunday Manara, amekuwa ni kigezo ni kielelezo mpaka FIFA wamemtambua. Juzi nimeona hata Instagram amefikisha followers zaidi ya milioni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Simba Sports kwa miaka imekuwa ndiyo timu pekee ambayo inaujaza Uwanja wa Taifa kwa kuingiza zaidi ya watu 60,000 kwa kiingilio. Maana yake ni nini? Tunahitaji kuhamasishana kama Taifa tusimame pamoja. Nafahamu wako wasemaji wa vilabu vikubwa hapa Tanzania, wao wanacheza kwenye Blog tu, lakini huwezi kuwasikia lakini michezo hii inahitaji kusema na kusikika. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Msemaji wa Bunge Sports. (Kicheko)

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachoomba Watanzania tusimame kwa ujumla wetu, tuhamasishe michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mahali fulani kwamba baadhi ya mambo yaliyosababisha makusanyo yakawa machache katika Wizara hii ni pamoja na kuonyeshwa michezo hii live kwenye television na kwenye App. Nasema kama Simba waliweza kuujaza uwanja na hii michezo inaonyeshwa kwenye television kwa nini tusihamasishane kama Taifa, tutumie hiyo fursa watu kuonyeshwa hii michezo live isiwe kigezo cha kupunguza mapato yetu kwa sababu tunao sisi kama Taifa kupitia Simba Sports Club. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Watanzania tutumie huu uzoefu ambao tumeupata kutoka kwa Msemaji wa Simba Sports Club, Ndugu Haji Sunday Manara tuupeleke sasa katika level ya kitaifa zaidi. Naamini kwa kufanya vile Taifa litaendelea kunufaika na fursa zinazojitokeza katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimalizie jambo moja, tuna Television ya Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kushiriki kwenye mjadala huu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia zote. Mchango wangu utakuwa na sehemu mbili, kwanza ni shukrani na pongezi kwa yale ambayo yamefanyika Jimboni Sengerema, lakini la pili nitakuwa na ushauri kwa yale mambo ambayo naona ni kazi zinazoendelea kwa sababu hazijakamilika.

Mheshimiwa Spika, katika pongezi, naomba niungane na wenzangu kusema kwamba Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa pamoja na wenzake Mheshimiwa Naibu Waziri Jumaa Aweso, Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu, Eng. Kalobelo pamoja na Wakurugenzi na wataalamu wenginge wanaopambana kadri inavyowezekana, wanajitahidi sana.Tumeona na inawezekana kukawa na udhaifu katika baadhi ya maeneo lakini dhamira yao naiona kabisa.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mmoja wa mashahidi kwa namna ambavyo wanajitahidi kutatua kero katika nchi yetu. Mheshimiwa Waziri ameshafika Jimboni Sengerema, Mheshimiwa Naibu Waziri anaendelea kutembelea maeneo mbalimbali nchini, pia Katibu Mkuu mwenyewe alishafika Sengerema, Naibu Katibu Mkuu ameshafika na Wakurugenzi wanaendelea kufanya ziara mbalimbali kutatua kero za maji. Kwa hiyo nachosema ni kwamba wanapambana na sisi Mkoa wa Mwanza Mamlaka ya Maji MWAUWASA inaendelea kufanya kazi nzuri, ingawaje ziko changamoto.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Sengerema wamenituma niipongeze Serikali kwa haya yafuatayo. Tumekuwa na kilio cha muda mrefu cha upatikanaji fedha lakini hivi karibuni Sengerema tumepata shilingi milioni 502 kwenye mradi wa maji unaohusu Kijiji cha Buyagu, Kalangalala hadi Bitoto. Pia tumepata shilingi milioni 58 kuhusu uchimbaji wa visima katika Vijiji vya Ilekanilo, Kasomeko na Igulumuki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma ukurasa wa 121 kwenye kitabu cha hotuba cha Mheshimiwa Waziri, unaona katika mgao wa fedha za miradi ya maji vijijini. Sisi Halmashauri ya Sengerema tumetengewa shilingi milioni 886, asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru hata kwa kikubwa. Tunasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa 63, ambao unahusu miradi ya maji katika vijiji vilivyomo pembezoni mwa Maziwa Makuu, ukisogea kidogo chini ukurasa wa 64(iii), kuna mradi mkubwa umebuniwa na Serikali, unahusu kutoa maji Ziwa Victoria na kuwafikia walengwa katika Vijiji 301. Hapa nazungumzia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Mara pamoja na Mkoa wa Simiyu. Sisi kwenye Halmashauri ya Sengerema tuna zaidi ya vijiji 26, tunasema ahsanteni sana kwa kuiweka Sengerema katika ramani ya huo mradi mkubwa na tunaamini fedha zikipatikana za kutosha mradi huu utatekelezwa. Serikali imetoa commitment hapa, kwamba baada tu ya kukamilisha zoezi ambalo linaendelea sasa hivi la usanifu, ujenzi wa mradi huo, utaanza, ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo kuna kazi zinazoendelea, naikumbusha Serikali, nimekuwa na mawasiliano mazuri, nashukuru tumepata hizi fedha ambazo nimesema zaidi ya shilingi milioni 500 lakini kuna fedha zingine tunazisubiria kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi ya kufikisha maji kwenye kijiji cha Ibondo kwa Mwarabu, Mwabalugi kule na hasa eneo la Zanzibar, kule Sengerema pia kuna Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia tuna miradi ambayo tunasubiri fedha kama mradi unaohusu Vijiji vya Mwaliga, Kang’washi na Sima, pale kuna ujenzi wa kisima pamoja na kisima cha Kijiji cha Nyamahona. Haya ni maeneo ambayo tunasubiri tu fedha, Serikali ilitoa fedha hivi karibuni round ya kwanza, lakini itatoa tena fedha nadhani labda kufikia mwishoni mwa mwezi huu ili tukaikalimishe miradi hii. Tunasema ahsanteni sana Serikali kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna kazi zinazoendelea na hapa naikumbusha Serikali kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Nyasigru, Bungo na Ngoma. Mradi huu unahusu kutoa maji Ziwa Victoria umebuniwa zaidi ya miaka miwili iliyopita na utaratibu wa kumpata mkandarasi, atakayeshughulikia mradi huu ulikamilika Mei, 2018, leo ni mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, naelewa sana baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaposema ziko changamoto katika Wizara hii. Imagine tumempata mkandarasi kwa utaratibu wa kawaida wa Serikali Mei, 2018 na hapa katikati mimi sijalala, nimekuwa nina mawasiliano na Serikali mazuri tu lakini mpaka leo mkandarasi hajaingia site. Bado kuna reservation, technically wanasema kuna hili na lile lakini kwa nini ichukue mwaka mzima? Haya ndiyo mambo ambayo tunasema yanahitaji kuongezewa kasi ya utatuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nikumbushe MWAUWASA wako hapa wanasikiliza, pale kwenye mradi mkubwa Mjini Sengerema pale na vijiji vingine ambavyo vinapitiwa na mradi ule kuna eneo la Kizugwangoma, Misheni pamoja na Bujora kuna ahadi ya kujenga booster ili kufikisha maji maeneo hayo. MWAUWASA waliahidi kwamba ujenzi ungekuwa umeshaanza toka Aprili, 2019, mpaka ninavyozungumza bado na mimi nafuatilia kila siku. Kwa hivyo, unaweza kuona hizi changamoto zilizopo, tunaamini kwamba fedha zipo lakini katika kasi ya utekelezaji kuna mahali hatuendi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, tuna Mradi wa Nyampanda ambao tayari taratibu zote za kumpata mkandarasi zimeshakamilika, tarehe 25 Aprili, ilikuwa tushuhudie kusainiwa kwa mkataba kwa mkandarasi aliyepatikana. Hivi karibuni Serikali iliahirisha tusisaini tarehe 25 Aprili hadi tarehe nyingine itakapopangwa.

Mheshimiwa Spika, najua nina wito wa kukutana na Watendaji wa Wizara hii baada ya hapa tukayajadili haya tupeane update lakini nawaomba wajiandae kunipa majibu kwamba ni nini mkandarasi wa Nyasigru, Bungo, Ngoma yeye hajapatikana? Ujenzi wa hii booster niliyosema ili kuyafikisha maji kwenye maeneo ya Misheni, Kizugwangoma, Bujora lakini lini mtasaini mkataba wa kuyafikisha maji katika Kijiji cha Nyampande? Pia tuna Kijiji cha Sima ambako kinaingia kwenye programu ya kuanzia mwezi Julai lakini kuyafikisha maji katika Kijiji cha Tunyeng’e.

Mheshimiwa Spika, kwenye sehemu ya ushauri nina jambo la kusema ukisoma ukurasa wa kumi wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu alivyokuwa anaelezea hali halisi ya upatikanji wa maji katika nchi yetu na nijielekeze hata katika maeneo ya vijijini. Kwenye ukurasa huu wa kumi wa hotuba hii anasema kufikia mwezi wa nne mwaka huu upatikanaji wa maji katika vijiji ulikuwa ni asilimia 64.8 lakini lengo ni kufikia asilimia 85 ili tufikie lengo lile kuu la kuhakikisha kwamba wannachi hasa vijijini wanapata maji ndani ya mita 400.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo ukisoma ukurasa wa 106 hadi 108 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri anakubali kwamba kinachotukwamisha kufikia malengo yetu ni changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati na fedha za kutosha. Pia hotuba ya kamati inayoshughulikia wizara hii Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ukurasa wa tano wamezungumzia changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, katika hili nimeshindwa kuelewa sitaki kuwa vuguvugu ama baridi ninashindwa kuelewa tunakwama wapi kwa sababu hapa tumezungumza na katika hili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema ninasimama na wote wale wanaounga mkono tuongeze shilingi 50 katika ule mfuko ili tuongeze kasi ya kuwafikishia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninafahamu wasiwasi uliopo lakini nataka ni-share uzoevu kidogo nilionao. Baada ya mdororo wa uchumi kuikumba dunia mwaka 2007 hadi mwaka 2009 mwaka mmoja au miwili baadaye sisi kama Taifa tulikumbwa na tatizo kubwa sana la uchakachuaji katika mafuta hasa bidhaa ya petrol kwa maana ya diesel na petroli. Na tatizo lililokuwa limesababisha kutufikisha hapo ni kwa sababu katika bidhaa zile tatu, mafuta ya taa, diesel na petrol kwenye ushuru sisi tulikuwa tumetoa exemption kwenye mafuta ya taa, kwa hivyo uchakachuaji ukawa ni mkubwa sanan zaidi ya asilimia 87. Lakini tukajadiliana sana na jambo likawa gumu

Mheshimiwa Spika, wakati huo nikiwa Waziri wa Nishati na Madini na-share huu uzoevu tulinganishe hofu iliyokuwepo. Tulikwenda mara ya kwanza tukapa ushauri na Mheshimiwa Shabiby sijui yuko wapi alikuwa hapa alishauri kwamba ondoeni tufanye harmonization ya ushuru katika bidhaa zote hizi petrol, diesel na mafuta ya taa. Tulivyorekebisha tulivyounganisha ule ushuru hapakuwepo na uchakachuaji na tukasonga mbele na hofu kubwa ilikuwa kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watanzania kwa maana ya Nishati ya Mwanga wanatumia mafuta ya taa lakini…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ngeleja.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, hapakuwa na shida hiyo ndio maana nasema, nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja lakini Serikali tu itafakari tu ushauri wa Wabunge naamini kwamba tutaelewana tutafika mahali pazuri na sio lazima tuongeze mafuta tunaweza kuongeza kwenye maeneo mengine pia kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge, asante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote kabisa naungana na wenzangu kuiunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri, Engineer Kamwelwe. Pamoja na hayo, nitumie nafasi hii kumpongeza yeye, kuwapongeza Waheshimiwa Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Engineer Kwandikwa na Mheshimiwa Engineer Nditiye, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote katika taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo imejitokeza hapa na mjadala unavyoonyesha, ni kwamba Wizara hii imepata fedha nyingi na imekuwa ikiendelea kupata fedha nyingi kwa sababu ni mhimili wa uchumi wetu kwa kadri ambavyo tunaelekea kuifikia nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajadili hoja iliyoko mbele yetu tukiwa tuko katikati kama Taifa kwenye majonzi ya msiba wa Marehemu Mzee Mengi na tunafahamu kwamba jana amelazwa katika makazi ya milele, nasi ndio tunasubiri ratiba yetu kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujalia. Kwa hiyo, natumia nafasi kuungana na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa familia ya Mzee Mengi, ndugu na jamaa, lakini kuungana na Watanzania kumwombea Mzee Mengi aendelee kulazwa mahali pema Peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kuhusu Jimbo la Sengerema. Kitabu hiki ambacho kwa ujumla wake kinaomba karibu shilingi trilioni tano, Sengerema ni mojawapo ya wanufaika katika miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa na ile ambayo iko katika hatua za mwisho kabisa kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaarifu wananchi wa Jimbo la Sengerema kwamba ile barabara yetu ya kutoka Sima kwenda Ikoni inayosimamiwa na TANROADS Mwanza, Barabara yetu ya kutoka Sengerema kwenda Ngoma A zinaendelea vizuri. Pia ile ya Sima – Ikoni, Mkandarasi wetu KASCO anamalizia kipande cha kutoka Sengerema kwenda Nyamazugo. Atakapokimaliza kile, anahamia Sima kwenda Ikoni kuunganisha na Jimbo la Geita Vijijini. Kwa hiyo, ni kazi inayoendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiingia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali imetukumbusha kupitia hotuba hii kwamba maandalizi ya bajeti hii yamezingatia pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, maelekezo ya Viongozi Wakuu pamoja na Mpango wetu wa Miaka MItano. Sasa kwenye ukurasa wa 60 pale wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kuna barabara inayotajwa pale ya Kamanga – Sengerema kilometa 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwani hatua za awali zilishafanyika; upembuzi na usanifu wa kina tayari na sasa nawaarifu Wana-Sengerema kwamba wajiandae kwa sababu mipango yote sasa imeshahamia Serikalini na hasa kwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Engineer Mfugale. Nimekuwa na mawasiliano naye, iko kwenye mpango, tunasubiri muda muafaka utakapofika, itatangazwa tenda kwa ajili ya kupata mkandarasi kuanza ujenzi wa lami kwa barabara ya Kamanga – Sengerema na ule mchepuko wake wa Katunguru kwenda Nyamazugo, kilometa 21. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu pia kwamba upembuzi yakinifu unaendelea na usanifu wa kina kwenye barabara ya Nyehunge kuja Sengerema ama Sengerema – Nyehunge, kilometa 78. Napo tunaishukuru Serikali kwa sababu ni kazi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimsikia Mheshimiwa Maige asubuhi na Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumzia barabara inayotuunganisha mikoa mitatu. Nazungumzia barabara ya Busisi kwenda Buyagu – Ngoma A mpaka Nyang’hwale ambalo ni Jimbo lililopo ndani ya Mkoa wa Geita na kuelekea Jimbo la Msalala ambako ni Mkoa wa Shinyanga. Hii ni barabara muhimu na tunaomba Serikali iendelee kujipanga vizuri na sisi tunaikumbusha ili kwamba tunapofika mwaka kesho, basi ama maandalizi yake yawe yameshamilika ama ujenzi uwe umeanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Engineer Nditiye, kwa kazi nzuri aliyofanya alivyotembelea Jimbo la Sengerema kuhusu mawasiliano, ambako bado kuna upungufu, nafahamu kwamba Mheshimiwa Kwandikwa amefika na Mheshimiwa Eng. Kamwelwe kama Waziri amekuwa akipita maeneo mbalimbali pamoja na wasaidizi wake. Pia kwa hili natambua kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Engineer Nditiye alifanya alipofika Jimbo la Sengerema kuhusu maeneo ambayo yana upungufu wa mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Daraja la Kigongo – Busisi, daraja kubwa miongoni mwa madaraja makubwa kabisa katika Bara la Afrika linajengwa pale. Sasa hivi mkandarasi wachambuzi wanaendelea na tathmini ya kumpata kwa sababu tenda imeshafunguliwa. Tunaipongeza Serikali tunasema ahsanteni sana kwa kazi kubwa inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine ambayo nilitaka niyakumbushe, wenzangu wamezungumza. Ukiangalia jiografia ya nchi hii, naomba ATC na ninaamini kwamba wanasikiliza hapa, ile mipango yenu ya kuanzisha route nyingine kutokea hapa Dodoma kwenda Mbeya na kuanzia hapa Dodoma kwenda Mwanza kwa maana ya kuhudumia Mikoa ya Kanda ya Ziwa ifanyike haraka, kwa sababu tunaamini kwamba itarahisisha sana kuokoa rasilimali fedha nyingi inayotumiwa na watumishi wanaokuja hapa kama Makao Makuu ya nchi kwa ajili ya kufanya shughuli za kikazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kuna ujenzi wa meli unaendelea, Ziwa Victoria na maziwa mengine, lakini viwanja vya ndege ikiwemo Kiwanja cha Mwanza, tunasema ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja nataka nizungumze. Tuna miradi mikubwa na ukisoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 67 tulipokuwa tunajadili, katika ajira ambazo zimezalishwa mpaka mwezi wa pili mwaka huu tumeambiwa kwamba asilimia 66 imetokana na ajira zilizotokana na uwekezaji wa Serikali kwenye miradi mikubwa, hasa ujenzi wa miundombinu na asilimia 34 imetokea Private Sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niiombe Serikali katika hili, wanaofuatilia mitandaoni, mwezi wa Pili mwishoni pale kulitokea taarifa iliandikwa na mwandishi mmoja akisema asichokijua Mheshimiwa Rais kuhusu ujenzi wa SGR. Alichokuwa anasema ni unyanyaswaji wa Watanzania wanaopata kazi kumsaidia mjenzi mkuu wa miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze hili kwa kina kwamba katika fedha ambazo tunaziingiza katika miradi mikubwa hii, lazima tuwe na utaratibu wa kuwasaidia Wakandarasi wetu wadogo ambao ni subcontractors katika main contractors hawa. Yule mwandishi aliandika akasambaza mitandaoni akataja na jina lake na namba yake ya simu. Mtu mwingine anaweza kusema tusifuate mambo ya mitandao, lakini mtu anapokuwa ameandika na akataja kinachowakera Watanzania, kinachowasibu katika maeneo hayo akaweka na jina lake, ule utayari wake lazima utushtue sisi na liwe ni fundisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Eng. Nditiye, namtaja kama Naibu Waziri kwa sababu nilisikia alifuatilia kwa kile ambacho wananyanyaswa wale subcontractors kwenye ujenzi wa miradi yetu na hasa mradi wa SGR. Wanaingia katika kazi hizo, wanapewa kazi malipo hawalipwi ndani ya muda, matokeo yake wanafilisika kwa sababu wameingia katika ujenzi na wengine wanategemea mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yule bwana mpaka alitaja baadhi ya makampuni. Sasa sitaki kuwa specific nitaje baadhi ya makampuni kwa sababu sina interest yoyote. Ninachotaka niseme, kama Taifa, kwa fedha ambazo tunaziwekeza kwa sababu ni za walipa kodi, lazima tuziandalie utaratibu mzuri wa kuwasaidia Watanzania wenzetu ambao wameingia kule kusaidia. Kwa kadri wanavyonufaika hawa, ndivyo Taifa litakavyokuwa linanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chagizo langu ni kuiomba Serikali tuandae utaratibu mzuri wa kusimamia na hasa kuratibu wale subcontractors kwa maana ya local content, wale Watanzania wenyewe hasa ili manufaa haya ya miradi mikubwa tuyaone kwa uhakika na yawe na madhara chanya katika uhai wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Niabu Spika, yapo mambo mengi yamekuwa yakizungumzwa hapa. Limezungumzwa deni kuhusu TRC na Serikali kwa ujumla wake na baadhi ya wachangiaji. Mimi sitaki kujibu, lakini ninachotaka kusema, tuwe makini sana. Unapozungumzia deni linaloihusu TRC inawezekana kukawa na deni ambalo linahusu Serikali kwa ujumla kutokana na mkopo ambao tulikopeshwa na Serikali ya Uchina kwa maana ya ujenzi wa Reli ya TAZARA, lakini siyo malimbikizo kwa ujumla wake kwa fedha ambazo zimetajwa hapa kama vile ndiyo zinazostahili kwenda kwa wastaafu au wafanyakazi. Kwa hiyo, naomba nitahadharishe, tuyachambue kwa kina haya tusije tukapeleka taarifa potovu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja na Wanasengerema wajiandae kunufaika na mipango mizuri ya Serikali ambayo imeoneshwa hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii na naungana na wenzangu kumuunga mkono mtoa hoja Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Hotuba hii ni elekezi kwa maana ya utendaji Serikalini lakini pia mengi yaliyozungumzwa sisi ni mashahidi yanavyoendelea katika maeneo yetu tunakotoka. Ni ukweli ambao haufichiki kwa kweli, nikisema almost kila Jimbo limeguswa labda nitakuwa nazungumza kwa niaba ya wenzangu ambao mahali pengine sina taarifa sahihi, lakini ukweli ni kwamba, mambo makubwa sana ndani ya miaka mitano hii yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano tu, sisi huko Sengerema kwa mfano kwenye bajeti hii ambayo tunaihitimisha tarehe 30 mwezi Juni, tumetengewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya jambo jema kabisa kama ambavyo zimo halmashauri nyingine 26 ukijumlisha na kwetu tunakuwa na 27. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaonesha kwamba kwenye bajeti hii ambayo 2018/2019 kulikuwa na hospitali za halmashauri 69 zimejengwa, kwa hivi ni jambo kubwa ambalo hatukuwahi kulifanya miaka mingi toka nchi yetu ipate uhuru.

Mheshimiwa Spika, pia huko Sengerema wamenituma niipongeze Serikali kwa kutenga fedha shilingi milioni 750 kwenye bajeti ambayo itaanza tarehe 01Julai, mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, jengo la Mkurugenzi pamoja na ofisi nyingine. Sisi tunasema ahsanteni sana Serikali kwa kutujali, kwa kutukumbuka, kama ambao mnawakumbuka maeneo mengine, hatuwezi kuyazungumza yote kwa sababu mijadala ya kisekta inakuja.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu waliochangia kukupongeza wewe kama Kiongozi wetu Mkuu wa Mhimili huu, wewe pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge hili Tukufu wakisaidiwa na Watendaji wakiongozwa na Katibu wa Bunge, Ndugu Kagaigai mmefanya kazi kubwa sana. Ni vyema tuweke kumbukumbu sahihi, pamoja na kwamba Bunge hili majukumu yake ya msingi ni ya kutunga sheria na kuisimamia Serikali, lakini yako mambo ya msingi wewe uliyoyafanya ni vyema taifa likaendelea kuyakumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, umelifanya Bunge hili litoke kwenye utengaji kazi wa analogy tukahamia kwenye digital, tunafanya kazi kwa kutumia mitandao, umelifanya Bunge liwe e-parliament ni jambo la msingi sana tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 18 aya 32 utaona pale Serikali inakiri yenyewe kwamba michango ya Bunge lako Tukufu imesaidia sana kuanzisha Mfuko wa Maji, lakini pia tukatengeneza utaratibu wa kuanzisha chombo maalum kwa ajili ya maji vijijini (RUWASA) jambo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa tunakupongeza wewe na wasaidizi wako kwa namna ambayo ulisaidia kusimamia hii hoja hatimaye Serikali kwa kushirikiana na wewe, kwa kushirikiana na Bunge Tukufu hili tukafanikiwa kuanzisha hiki chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo tunakukumbuka wewe, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wetu ni kwa kuanzisha na mimi nazungumza hapa nikiwa na interest, kuianzisha ile Kamati ya Sheria Ndogo, naomba Waheshimiwa Wabunge wanisikilize vizuri hapa, simaanishi kwamba Kamati ya Sheria Ndogo ni ya muhimu sana, lakini wenye historia ya Bunge hili wanafahamu hii ni kamati ambayo imekuwa ikiingia na kutoka. Tunafahamu ilishaingia huko nyuma ikatoka, ikarudi ikatoka na sasa imeingia tena.

Mheshimiwa Spika, umefanya jambo kubwa sana tunakupongeza kwa sababu yale ambayo tunayafanya sisi chini ya uongozi wetu wa Mheshimiwa Chenge kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kama kusingekuwa na kamati mahsusi maalum kuzungumzia mambo haya na hii ni Kamati inayoshughulika na Sheria Ndogo. Masuala ambayo kila siku ndiyo yanasimamia uendeshaji wa maisha ya Watanzania, ina maana kwamba wananchi kwa kiwango kikubwa wangekuwa wanaumia kwa yale ambayo Serikali ilipitiwa ama kwa kutoyaona au kwa kutoyapa tu nafasi yake na sisi tunakuja kuyabaini na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo tunakupongeza sana, lakini tujipongeze wote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne ambalo napenda kuliweka kwenye kumbukumbu zaidi ni kwa namna ambavyo una-support suala la michezo. Suala la michezo si la mchezo, suala la mchezo ni fursa lakini suala la mchezo ni afya na suala la mchezo ni kiwanda kinachotembea. Tukizungumza kwa muktadha wa hapa Bungeni mimi ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, nakupongeza na kukushukuru sana kwa namna ambavyo umetupa support kwa miaka mitano yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze jambo moja ambalo nimelibaini kwenye hotuba hii. Ukisoma mafungu haya na hasa uchambuzi wa Kamati ya Bajeti. Wanasema kwenye bajeti makadirio ya fedha iliyotengwa mwaka mpya wa fedha unaokuja hatujatenga fedha kwa ajili ya ushiriki wa michezo kwa Bunge hili, kwenye mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki. Nina ushauri, ni jambo la kawaida kwamba na tunafahamu wenye historia nzuri katika mashindano haya kwamba kwa kila nchi ambayo inakuwa ndani ya mwaka huu wa mashindano ina Uchaguzi Mkuu taratibu zinaruhusu nchi hiyo isishiriki.

Mheshimiwa Spika, nataka nitofautishe ushiriki na mashindano haya yanakofanyikia mwaka huu, mwenyeji wa mashindano haya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka huu ambayo yatafanyika mwezi wa 12 yanafanyikia Jijini Arusha na wenyeji wa mashindano haya ni Bunge la Afrika Mashariki. Kiutaratibu wenyeji ni EALA, lakini kiuhalisia yanafanyikia Tanzania. Naomba Bunge lako Tukufu litafakari vizuri na hasa Kamati ya Bajeti, ile nadharia ya kwamba nchi ambayo ina Uchaguzi Mkuu isishiriki mazingira ya mwaka huu ni tofauti. Jambo la pili juu ya hilo ni kwamba gharama zake kwa mwaka huu kwa sababu mashindano yanafanyika ndani ya nchi ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, nafanya hesabu tu rough hapa, sisi kwa mahesabu tuliyofanya kwa ushiriki wa mwaka huu tukichukulia wachezaji 100 ambao wanaweza kwenda kushiriki pale Arusha gharama yake haifikii hata silimia 50 kama mashindano yangefanyika nje ya nchi. Kwa hivyo, najaribu kuzungumzia hili jambo tulitafakari vizuri wakati tunaendela kufanya majadiliano kadri ambavyo majadiliano yanaendelea, kwa sababu kadri tunavyozungumza kwa mfumo tulionao wa bajeti, ndipo pia tunaweza kupata fursa nyingine za kurekebisha mahali hapa ama kule. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba sana turuhusiwe.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni lile ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelizungumzia kuhusu mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara Tanzania. Ni kweli takwimu zinaonesha kwamba tumesogea kidogo kutoka namba ya 144 tukasogea nafasi ya 141, lakini hii inaonesha mazingira yetu ya ufanyaji biashara na uwekezaji bado tuna changamoto kubwa. Ile blueprint ambayo imetayarishwa na wataalam wetu nashauri kwamba ifanyiwe kazi, tuitekeleze rasmi kwa sababu inafungua fursa lakini pia inarekebisha kasoro nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kasoro moja, mimi ni mpenzi wa kuwa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na umma kikanda. Tunafahamu Dodoma kuna Chuo Kikuu cha Serikali, Dar es Salaam vipo, Nyanda za Juu Kusini Mbeya kipo, Arusha kipo, lakini mikoa saba ile ya Kanda ya Ziwa hatuna. Pale Sengerema Sekondari Mheshimiwa Profesa Ndalichako Waziri wa Elimu yuko hapa ni shahidi, kwa maboresho yaliyofanyika kwenye shule kongwe Tanzania na Sengerema Sekondari ni eneo lisilopungua ekari 143, linafaa kabisa kama Serikali itaamua kutafakari vizuri. Tuigeuze ile Shule ya Sekondari kuwa Chuo Kikuu, lakini hilo naiachia Serikali itaendelea kutafakari.

Mheshimiwa Spika, la mwisho Corona; naomba uniongezee dakika moja katika hili, nataka nizungumze kama mwananchi wa kawaida ambaye sina taaluma yoyote katika masuala ya afya, lakini nataka nizungumzie jambo moja la kimapokeo. Tumekuwa tukielezwa kwamba iko tiba ya mafua ambayo ni ya kienyeji ile ya kujifukizia, sijaelewa ni kitu gani ambacho kimetukumba kama Taifa, sina taarifa sahihi lakini mimi nafahamu pale Muhimbili hasa MUHAS pale kuna Kitengo cha Tiba Mbadala. Yaliyotokea China leo wamedhibiti ugonjwa wa corona huu hatufahamu siri zake kwa sababu siri zote hazijitokezi. Ninachotoka kusisitiza na kuliomba Bunge lako Tukufu, wewe unaweza kutumia Kanuni ya 5 kutoa mwongozo kwa Serikali ama Serikali itafakari. Kwa nini hii tiba mbadala ya kimapokeo ambayo wengi tumetibiwa na tukapona kwa miaka mingi hatuipi nafasi katika vita hii.

Mheshimiwa Spika, tuna corona hapa ambayo ni janga la kidunia.

SPIKA: Mheshimiwa Ngeleja, malizia.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, hili janga naomba kila nchi ipambane na hali yake kwa mazingira iliyonayo. Kama tulivyosema China hatujajua kitu gani kimewafanya wakadhibiti, lakini kama hili jambo halina madhara kuli-promote kwa maana ya Serikali kulizungumza Watanzania wakafanya.

Mheshimiwa Spika, chukulia mfano kila mtu ajifukizie asubuhi yeye na familia yake, kuna hasara gani kama tumejifukizia na tukapata nafuu lakini itatokea nini kama inawezekana kujifukizia kunatibu halafu sisi hatuipi nafasi hii fursa, maana yake ni nini.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, narudia tena kuunga mkono hoja, lakini naomba jambo hili mlitafakari vizuri. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naungana na wenzangu kukupongeza sana wewe kwa namna ambavyo umesimamia zoezi la maandalizi ya Sheria hii ambayo tuna marekebisho ya Sheria tunayokwenda kuyafanya. Kwa mwongozo wako ndiyo kilichowezesha Kamati ikafanikisha kuzihusisha Taasisi kwa maana ya wadau 21, lakini watu binafsi zaidi ya 400 na kwa usahihi kabisa 410. Pia wewe umeturuhusu kwa utaratibu wa kikanuni za Bunge sisi Wabunge wengine kushiriki kwenye Kamati ya Katiba na Sheria kwenye maandalizi ya marekebisho haya ya Sheria hii ya Vyama vya Siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze Serikali kwa kuandaa marekebisho haya. lakini pia kwa namna ambavyo walikubali kushirikiana na Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na wadau wengine walioshiriki katika maboresho ya Sheria hii. Pongezi maalum kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa kwa kufanya kazi kubwa na Wajumbe, lakini pia niwapongeze sana wadau wote nje ya Bunge hili, waliotenga muda wao kuja kutoa ushauri katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatunga Sheria na kama ambavyo wenzangu wamesema sheria huwa hazitungwi tu lazima kuwe na jambo ambalo linatakiwa kurekebishwa. Haya yamesema sana na wenzangu na mimi sitapenda kurudia, lakini ukweli kabisa ambao nataka kuusisitiza ni kwamba baada ya mashauriano makubwa yaliyofanyika kuanzia kwa wadau hadi kwenye Kamati na hapa tulipo sasa, sina wasiwasi wala sina mashaka kusema kwamba marekebisho haya tuliyonayo sasa ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo tulivyoanza kupokea Muswada wa marekebisho haya. Ndiyo maana tunafanya rejea ya vifungu vichache tu ili kukubaliana na marekebisho yaliyofanywa ili hatimaye marekebisho haya yawe Sheria na yakatekelezwe.

Mheshimiwa Spika, tumesikia na tumeshauriana lakini wapo watu wana mashaka na kifungu cha 3(5)(c) kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama kufuatilia chaguzi za ndani. Wapo wanaotia mashaka kwamba kwa nini Msajili huyu apewe mamlaka ya kwenda kuingilia mambo ya ndani, lakini Mheshimiwa Sixtus Mapunda asubuhi na wengine wametukumbusha sisi sote tuko katika Taifa hili, tunafahamu kinachoendelea hatuko tofauti na yanayofanyika katika uendeshaji wa vyama vyetu, si jambo la siri, ni jambo la wazi, migogoro imekuwepo katika chaguzi za ndani na mara kadhaa watu wameshapelekana Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunajenga platform na fursa ya kulishughulikia jambo hilo kabla halijafikia huko Mahakamani, kwa sababu huko tunakokwenda pia kunatumika rasilimali za Taifa na ndiyo msingi tunaoutaka kuufanya hapa kuimarisha hili eneo ili kupunguza ule uwezekano wa kuwa na migogoro katika chaguzi za ndani.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 3(5)(g) elimu ya uraia kimelalamikiwa sana, lakini kimsingi Serikali imefafanua na Kamati imesema. Ukisoma maelezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu lengo la kwa nini Msajili amepewa mamlaka haya ya kuratibu hiyo elimu ya uraia ambayo inaweza kutolewa na Taasisi za ndani na nje ya nchi tunaona kabisa kwamba nia ni njema na hatuhitaji kuwa na mashaka.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, wamesema lengo lake moja ni kudumisha Umoja wa Kitaifa. Tunataka kuona kabisa kwamba hii elimu inayokwenda kutolewa haiendi kuparaganyisha Taifa. Pia wamesema kukuza uzalendo wa nchi yetu; kuzuia elimu inayolenga kupandikiza chuki miongoni mwa jamii na mifarakano kati ya vyama vya siasa vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Ni jambo la kawaida, hivi ni kweli dhamira ambayo inaelezwa hapa mtu mwenye akili timamu kama sehemu ya Mtanzania mzalendo anaweza kupinga jambo hili? Hiyo ni fursa yetu kushauriana lakini kwa hakika jambo hili halijakaa vibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kinanipelekea nifuatilie kwa karibu alichokuwa anasema rafiki yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe hapa. Ametukumbusha na akafanya rejea ya mtu aliyeangamiza maisha ya wanadamu duniani, Hitler. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alichokuwa anakizungumza Mheshimiwa Zitto na nafahamu mazingira aliyokuwa nayo, samahani sana. Najua Mheshimiwa Zitto ameongea lakini alikuwa hajasoma marekebisho ya Serikali yaliyoletwa hapa. Ukisoma ukurasa wa tano ile ‘R’ ndiyo iliyorekebisha kifungu ambacho ulikuwa unakizungumzia Mheshimiwa Zitto, hupata nafasi ya kufuatilia lakini yalizingatiwa na tukasema mwongozo wa Katiba ndiyo utuongoze katika kufikia maamuzi yanayoweza kufanywa na Msajili na hata maamuzi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka niwakumbushe Watanzania wanaofuatilia, nafahamu Bunge haliko live lakini teknolojia inaturuhusu, watu wataingia Youtube, watafuatilia mijadala hii. Wananchi wafuatilie sana, tusiendeshwe na intensity ya sauti inayopazwa hapa isipokuwa tuzingatie maudhui, ukweli na uhalisia wa michango inayotolewa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dada yangu Mheshimiwa Esther Bulaya ulisema lakini nataka nikurejeshe kwenye ukurasa wa 6 wa taarifa jambo ambalo ulikuwa unalilalamikia sana kwamba kwa nini Msajili anapewa mamlaka haya. Mheshimiwa Esther katika paragraph ya pili, ulichokuwa unakilalamikia kimetolewa ufafanuzi pale. Wewe unapinga jambo hilo lakini unasema kama mamlaka haya ingepewa Tume ya Uchaguzi sisi tungeunga mkono. Sasa inawezekana jambo hapa ni tofauti na mitazamo kuhusu Msajili wa Vyama vya Siasa lakini siyo mantiki na umuhimu wa kifungu ambacho tunakizungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5A kuhusu taarifa ya siku 30 kabla ya zoezi la elimu ya uraia kutolewa, ni jambo la msingi tu na zuri. Pia limelalamikiwa kwamba endapo Msajili atakataa kutoa hicho kibali yeye atatoa sababu au anafanyaje lakini jambo hili kwenye Muswada limesemwa. Ukienda kwenye Muswada wetu, ukurasa wa 5, kipo kifungu cha 5A(2) kinasema Msajili lazima atoe sababu kwa nini anapinga kutoa kibali hicho, sasa kwa nini tuendelee kubishana katika hili? Maana yake ni nini? kama Msajili wa Vyama anapewa masharti ya kutoa sababu maana yake ni kwamba yeyote atakayeathirika na kifungu hicho anaweza kwenda Mahakamani kupinga sababu ambazo zimetolewa na Msajili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 6A(5), umuhimu wa Mwenge na Mapinduzi ya Zanzibar, hili limezungumzwa lakini mimi nataka ninukuu maneno yaliyosemwa mwaka 1961 na ambayo yamekuwa yakisemwa kila wakati ambapo Mwenge wa Uhuru unapandishwa kwenye Mlima Kilimanjaro, Mwalimu Nyerere pamoja na Waasisi wengine wamekuwa wakisema na yamekuwa yakirudiwa wanasema: “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike nje ya mipaka yetu ili pale palipo na mashaka ulete matumaini, pale palipo na dharau ulete heshima na pale palipo na uonevu ulete haki”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini sisi wote ni waumini hapa ama Mkristo ama Muislam inawezekana ukawa huna imani. Kule kwenye Quran na Biblia maandiko ni yale yale lakini ni kanuni ya maisha kwamba mambo mema tunakumbushana kila siku. Wanaoshauri kwamba jambo hili lingebaki kwenye maabara ama likabaki kwenye makumbusho hawaelewi kwamba changamoto za wananchi walizonazo hazijengi mazingira ya wao kujikumbusha na kuona kilichofanyika miaka ya 1940, 1960, 1970 iliyopita na ndiyo maana tunasema mwenge uzidi kuwakumbusha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya yote, nini sasa langu, Serikali hii ni sikivu sana na imethibitisha usikivu wake katika Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria kwa sababu ulivyokuja na ulivyo sasa ni tofauti kabisa. Wako watu wanaotumia maneno magumu sana kwamba Muswada huu una uharamu lakini wengine pia wanasema una ujinai. Nataka niseme shughuli ya kisiasa siyo eneo ama siyo shughuli ambayo inajenga uficho wa watu kufanya mambo maovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mwanasheria mmoja hapa anahoji, kwa nini tumeweka vifungu vingi vya kuwachukulia hatua wale ambao watakiuka sheria hii. Kwa msingi wa kawaida wa utungaji wa sheria mnafahamu, makatazo yanapowekwa lazima kuwe na hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa kama kuna mtu atakiuka. Hili jambo hata huyu ambaye tunamwona kama ndiyo central focus katika mjadala huu, Msajili wa Vyama, akikiuka kifungu chochote na yeye inakula kwake. Hizi adhabu ambazo tumezitaja hapa hazijamuacha mtu yeyote salama kama atakiuka kifungu chochote katika sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nikasema Taifa hili tunalijenga kwa pamoja lakini tusijifanye tunapokuwa hapa hatuyaoni mazuri yanayofanyika ndiyo maana nasema mimi na wenzangu naunga mkono kabisa mapendekezo yaliyoletwa na naamini kwa pamoja tutaendelea kujenga nchi yetu vizuri. Naipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Muswada huu ulioko mbele yetu. La kwanza ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ametuongoza kufikia siku ya leo, lakini zaidi ya hapo nitumie nafasi hii kusema kabisa kwamba naungana na taarifa ya Kamati yetu kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu Mtemi Chenge na tunaiunga mkono hoja ya Serikali pamoja na Marekebisho ambayo yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Llakini jambo la pili, likiwa ni sehemu ya utangulizi kwa niaba ya Kamati yetu naongezea maneno ya kukushukuru sana wewe Mheshimiwa Spika, Kamati yetu ya Kudumu ya Sheria Ndogo ni mara ya kwanza inapewa heshima ya kuchambua Muswada kwa asili ya Kamati yetu tumekuwa tukichambua Sheria zingine ambazo zimeshapitishwa na Bunge ama Sheria Ndogo ambazo zinaletwa kwa ajili ya uchambuzi. Lakini tunakushukuru sana kwa heshima uliyotupa na kimsingi Kamati yako iko tayari kuendelea kufanya uchambuzi wa Miswada mbalimbali kwa kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atakujalia kuipa majukumu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekutana na Serikali na mimi naungana na Mheshimiwa Mwenyekiti wangu kuipongeza sana Serikali ikiongozwa na Mheshimiwa Jenista Mhahama pamoja na Profesa Kilangi kwa namna ambavyo wametushirikisha kufafanua maeneo ambayo tulikuwa na wasiwasi na matokeo yake ndiyo haya ambapo tunaona kuna jedwali la marekebisho mengi ambayo kimsingi ni maridhiano kati ya Serikali na Kamati yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, kabla sijahamia kwenye uchambuzi wa vifungu vya Sheria, ni dakika chache zimepita toka ulipozungumza kati ya maneno makubwa uliyozungumza leo ikiwa ni taarifa ya Mheshimiwa Spika, umetumia fursa ya jukwaa leo kunipongeza mie lakini pia na wenzangu kwa hatua tuliyoichukua ya kumuomba radhi Mheshimiwa Rais kwa yaliyotokea bila kufungua mjadala nataka niseme na ni kwa sababu wanajua kibinadamu, wote tunajua msamaha siku zote unaleta faraja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii, mimi mwenyewe, lakini pia kwa niaba ya Wapiga kura wa Jimbo la Sengerema kuelezea faraja niliyo nayo ya kupata huo msamaha lakini pia kukushukuru sana kwa namna ambavyo umeliweka, ahsante sana na ninaamini kwamba Mwenyezi Mungu atazidi kumjalia Mheshimiwa Rais, kukujalia wewe, Watendaji Wakuu, Viongozi Wakuu wa Serikali, Makamu Rais pamoja na Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla na sisi kwa nafasi kama Taasisi kuendelea kutimiza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Muswada uliowasilishwa kwetu kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti ulikuwa unapendekeza marekebisho katika Sheria Tisa, mimi nitapita katika baadhi ya maeneo nikijenga msingi wa kuwashawishi baadhi ya watakaopata nafasi kwa niaba ya Bunge lako kuiunga mkono Serikali kwa sababu maeneo haya mengi yaliyoletwa mbele yetu yamefanyiwa uchambuzi wa kina na tumeelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kwanza, naanza kuchangia ni sehemu ya Sheria ya Mamalaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji, jambo kubwa lililojitokeza hapa ilikuwa ni kuingiza dhana ya ushirikishwaji wa watendaji ambao wako chini ya hii Mamlaka ya Udhibiti EWURA zikiwemo Wizara zingine nje ya Wizara ambako Mamlaka inaripoti.

Mheshimiwa Spika, kwa mfumo tuliokuwa nao kwa sasa, tulio nao sasa hivi EWURA wanaripoti kiutaratibu kwenye Wizara ya Maji, lakini kuna Wizara zingine ambazo majukumu yake pia yanadhibitiwa na EWURA ikiwemo Wizara ya Nishati. Sasa hapa wanaleta dhana ya kuwashirikisha katika baadhi ya mambo, Katibu Mkuu ama Makatibu Wakuu katika Wizara ambazo siyo Wizara ya Mama ambako Mamlaka inaripoti ikiwemo Wizara ya Nishati lakini pia Mawaziri husika katika maeneo haya. Ni wazo zuri, na sidhani kama linahitaji mvutano katika hili kwa ajili ya kuelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye sehemu ya nne ya Muswada ambao inahusu Marekebisho ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha yako mambo mengi yamezungumzwa. Lakini moja ni kuweka bayana sasa kwamba Kifungu cha 9A kinazungumzia kuwapa fursa Watuhumiwa watakaobainika katika haya makosa ya kufifilisha compounding offence ya kujitetea.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo jema, kwa sababu mkishakubaliana kwenda nje ya utaratibu wa kimahakama, ni vyema huyu mtu ambaye unakubali sasa kwamba anaweza kutimiza majukumu yake nje ya mfumo wa kimahakama basi mpe nafasi ya kujitetea na kujieleza. Kwa hili ni jambo jema na kwa kweli tumelizungumzia, tumeelewana na Serikali na imeridhia ushauri ambao Kamati yako imeutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine katika eneo hili, eneo hili la mchezo wa kubahatisha lina sura mbili. Upande mmoja ni chanzo cha mapato binafsi kwa wanaocheza lakini biashara kwa wanaochezesha na kwa upande mwingine lina ukakasi wa kiimani, yote yamezingatiwa. Ndiyo maana tunasema, kwa namna ambavyo limeletwa na Serikali na tafakari tuliyoifanya kwa pamoja, hapo tulipofikia ni pazuri na nawashawishi wenzangu tuiunge mkono Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tano ya Sheria kuna suala la tafsiri ya sharia. Moja katika vifungu ambavyo vinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ni cha 54. Nimesikia mjadala utaendelea, nadhani tutaendelea kushauriana vizuri, lakini Serikali imekuja kutufafanulia vizuri kwamba Serikali inaleta mabadiliko kwamba kwa kipindi ambacho kitakuwa cha mpito Bodi haijateuliwa basi Makatibu Wakuu wapate nafasi ya kutimiza majukumu ambayo kimsingi yanatekelezwa na Bodi katika taasisi ambazo zinalengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa ni jambo la hekima na busara lakini pia na uhalisia, Serikali ina mambo mengi, tunajua Bodi zina muda wake na nyingi zina muda wa miaka mitatu, lakini hizi sheria wakati mwingine zina contemplate, zinatungwa zikijaribu kubashiri hali ambayo inaweza kujitokeza, sasa kama hamjaweka utaratibu mzuri wa ku-address changamoto hizo ambazo zinaweza kujitokeza bila kutarajiwa inakuwa shida kidogo katika maamuzi na wakati mwingine maamuzi makubwa yanafanywa. Kwa hiyo, tunaamini kwamba Serikali imekuja na marekebisho haya kwa nia njema, naamini kwamba jambo hili litakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Saba inahusu marekebisho katika makosa mbalimbali ambayo yameingizwa lakini kikubwa ambacho tunaipongeza Serikali ni kuridhia ushauri wa Kamati kwamba yako baadhi ya mambo, matukio ya picha ambazo zinazungumzwa hapa, kwa mfano masuala ya misiba, labda unasafiri ukakuta ajali imetokea, unapiga picha lakini lengo lako unataka kutuma taarifa sasa kwenye mamlaka husika, labda kwa RPC au Mkuu wa Trafiki ama Mheshimiwa Waziri mhusika, jambo hilo lisiwe kama ni kosa kwa sababu wewe utakuwa unafikisha taarifa kwenye mamlaka husika. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kheri na tunaiomba Serikali ilikubali. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge tukubaliane katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nane inahusu Sheria ya Utumishi wa Umma na kubwa katika hili Katibu Mkuu Kiongozi anafanywa kuwa ndiyo mkubwa, ndiyo mamlaka ya mwisho kabisa katika masuala ya uhamisho pamoja na masuala mengine lakini hili jambo ni kama lilikuwa ni formality. Tunafahamu Katibu Mkuu Kiongozi au Chief Secretary ndiye mkuu wa nidhamu katika utumishi wa umma, sasa masuala ya uhamisho ni sehemu ya utumishi wa umma. Kwa kweli hili jambo na la lenyewe, nadhani haliwezi kuleta mvutano mkubwa, lilikuwa ni jambo la busara na hekima kukubali kwamba liingizwe katika utaratibu unaopendekezwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tumeliona ni katika maeneo ya sheria inayohusu Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii na hii ni Sura ya 135. Tunaishukuru Serikali, imetafakari, sheria hii kwa kweli inaondoa sasa uwepo wa muundo wa kitaasisi au mamlaka ambayo ilikuwa inaanzishwa katika ile Sheria ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii lakini majukumu yake yanahamia katika Wizara husika.

Mheshimiwa Spika, kubwa katika hili ambalo napenda kulizungumzia ni kwamba mojawapo ya mambo makubwa ambayo yamezungumziwa ni kuhakikisha kwamba fursa ya mlalamikaji yeyote kwa ajili ya fao lolote linalomhusu, halijawekewa ukomo, ukomo umeondolewa, kiasi kwamba sasa kama mtu anaweza kuwa amejisahau, baadaye akabaini kwamba kuna fao lake halijatendewa haki, hana ukomo wa kuendelea kufuatilia ama kuwasilisha malalamiko yake. Sisi tukaona kwamba ni jambo kubwa kwa sababu lina manufaa kwa wananchi wetu ambao wananufaika na mifuko hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ni hili la kurekebisha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, ni jambo zito, tumelizungumza sana. Ipo miradi mingi ambayo tunaifadhili wenyewe kwa fedha yetu ya ndani lakini iko miradi mikubwa inafadhiliwa kutokana na fedha za mikopo ya kibiashara, ama mikopo yenye masharti nafuu lakini kwa msimamo wa sheria zetu imekuwa ni kikwazo na kwa sababu Kodi ya Ongezeko la Thamani kimsingi imekuwa ikiongeza gharama za utekelezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Spika, Sasa kwa utaratibu ambao tumeshauriana na Serikali na Serikali tunajua kwamba itakuja itoe ufafanuzi wa ziada namna ambavyo tutaikwamua miradi ambayo sasa imeshaanza kutekelezwa, naamini kwamba tutakwenda vizuri na tutapunguza gharama na tutarahisisha utekelezaji wa miradi hiyo na ni kwa manufaa ya Watanzania wote, hili halilengi mradi wowote kwa manufaa ya mtu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, naunga mkono ya Serikali, naendelea kuwashawishi wenzangu tuiunge mkono Serikali tukatimize majukumu kwa mafufaa ya Watanzania wote. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. WILLIAM M. NGELEJA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa niaba ya Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Sheria Ndogo Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge ninaomba kuhitimisha hoja yetu iliyowasilishwa asubuhi ya leo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kukushukuru wewe kutuongoza vizuri siku ya leo kama ilivyosiku zote, lakini pili kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliochangia hizi taarifa tatu ambazo zimewasilishwa leo kwa upekee nawashukuru sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri pamoja na Waziri kwa ujumla wake. Kwa kufafanua hoja ambalimbali ambazo ziliibuliwa na Waheshimiwa wachangiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kamati ya Sheria Ndogo tunaendelea kupokea salamu hizi za upendo salamu za pongezi kwa kadri ambazo ambazo zimejitokeza kwenye mjadala huu na tunalihakikishia Bunge lako tukufu kwamba Kamati yetu ya Sheria Ndogo iko tayari itaendelea kuyatenda yaliyomema kwa maslahi ya Taifa letu na tunaendelea kumshukuru sana rafiki yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa coordination nzuri unayoifanya tupo tayari tulishawahi kujadili huko nyuma kwamba kwa kadri ambavyo Serikali na viongozi wetu wa Bunge mtakavyoona inafaa kwa sababu sheria ndogo zimekuwa nyingi leo umesikia habari ya sheria ya mia nane tisini na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposikia kwamba kati ya sheria 897 zilizowasilishwa lakini zinaonekana zinadosari labda ni sheria ya 73 haimaanishi kwamba sheria zingine zote hazikuchambuliwa maana yake kwamba sheria zote kamati imezipitia kwa hiyo, inatumia muda mwingi. Kwa hiyo, tulishawahi kuweka wazo na tunaendelea kushauri kwamba kwa sababu kwamba kwa sababu katika mfumo wetu wa uendeshwaji Bunge kuna baadhi ya Kamati ambazo kwenye mikutano yetu ya kawaida huwa zinatangulia angala wiki moja kabla ili tuondoe tupunguze stress ya muda tunaotumia kuzichambua hizi Sheria Ndogo utawala, mtaangalia kama hilo linawezekana ili Kamati ya Sheria Ndogo pia ipate hiyo fursa hili tufanye kazi kwa utulivu zaidi kuliko tunavyofanya sasa pamoja na kwamba haijaathiri ubora wa kazi tunazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea kuhitimisha hoja yetu kuna mambo matatu tunataka tukumbushe na ninaikumbusha Serikali kwa sababu wenyewe wamekuwa wakiwasilisha hizi Sheria Ndogo kwetu. La kwanza ni jambo la ujumla kwamba tunauzoefu wa kuona kwamba kwenye taasisi nyingi za Serikali wanasheria hasa wenye taaluma ya ususi wa uandishi wa hizi sheria kimsingi kuna uhaba wake na tunahitaji kuongeza ajira katika eneo hili na kuboresha ama kuboresha mafunzo kwa waliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunaomba Wizara ya Sheria kwa ujumla wake na hasa kitengo hiki cha Uwandishi wa Sheria legislative draft file tunaomba sana kipewe nafasi tupate kuongeza nguvu kazi pale kwa ajili ya kuboresha shughuli za uandishi wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ambalo tunakumbusha Serikali ni kwamba tumeshuhudia sisi kwenye Kamati zetu katika utendajiwetu wa kazi wa kila siku ziko baadhi ya Sheria Ndogo zinazokuja kwa namna ambavyo zimetungwa ni kama zinapoka mamlaka ya na madaraka ya Sheria ambazo zimeziazisha hizi Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni changamoto inawezekana si rahisi sana kuielewa tulivyozungumza lakini kwenye Kamati tunaweza kuelewa, tuna utungaji wa Sheria Ndogo na misingi yake sasa inapotokea kwamba Sheria Ndogo zile ambazo kimsingi zinatungwa kutokana na Sheria mama zenyewe tena zinakuwa na mamlaka na masharti ya kupoka sheria ya mama ambazo ndiyo kwanzo ndiyo zimetungwa kutokana na hizo Sheria mama tunakuwa na tabu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunaiomba sana Serikali pamoja na vyombo vingine vinavyoshiriki katika utungaji wa sheria ndogo ili kupunguza muda wa kuzipitia hizi Sheria Ndogo lakini pia usumbufu wa kila wakati kukumbushana ili jambo pia lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho lakini siyo la umuhimu, tunaikumbusha Serikali kwamba katika utungaji wa hizi Sheria Ndogo na hasa tunapoanza kutunga Sheria mama, Sheria yake inamchakato wake kuna Muswada unajadiliwa sasa katika masharti ambayo yamekuwa nyakati nyingine inatokea masharti inayopendekezwa katika Muswada wa Sheria unaokuja kuzaa Sheria ambayo baadaye zinatungwa Sheria Ndogo. Wakati mwingine kunakuwa na baadhi ya masharti ama vifungu vya Sheria hizo mama yanakataliwa kwenye mjadala kama hapa bungeni ama hata upande wa Serikali kutokana na mashauriano ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo masharti hasi ambayo yanakataliwa mara nyingi huwa tunaona yanaibukia tena kwenye Sheria Ndogo sasa hili ni jambo ambalo limekuwa likitukwanza kidogo kama kamati lakini yote kwa yote ndiyo umuhimu wa kuwepo Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge lako Tukufu ndiyo ni sehemu yetu ya kazi yetu tunaamini kabisa kama haya yote yasingekuwepo bali isingekuwa na uhalali wa kuwepo. Lakini jambo jema kukumbusha kwamba kwa yale masharti ambayo yamekuwa yakikataliwa kwenye utungaji wa sheria mama yasije tena kupitia mlango wa nyuma yakaibukia huku kwa sababu huku milango imefungwa, ni jambo la kukumbusha ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa mara nyingine niwashukuru sana Wabunge wenzangu ahsanteni sana tupo tayari kushirikiana na ninyi na kwahauta hii sasa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo naomba kutoa hoja kwa mara nyingine tena ahsante sana. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilishaunga mkono hoja dakika chache zilizopita wakati nawasilisha kwa niaba ya Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie jambo moja la uelewa lakini pia na ushauri kwa Serikali. Ukiondoa kasoro ambazo tumekuwa tukiziona katika hizi sheria ndogo za kiuandishi wakati mwingine mambo madogomadogo yale ya kawaida, jambo kubwa ambalo nataka kulizungumza kwa niaba ya Kamati yetu lakini lenye manufaa kwa nchi kupitia Bunge lako Tukufu, na ni jambo la kukumbushana, ni kutambua kwamba mfumo tulionao wa utungaji wa sheria ndogo hizi za aina yoyote ile kimsingi hautoi fursa ya kuzifanyia marekebisho zile kasoro ambazo zimebainika katika sheria hizo ndogo kabla hazijaanza kutumika. Na hiyo ndiyo changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo la kufumua huo mfumo ni jambo kubwa sana, hatuwezi kuzungumza katika muktadha huu. Ushauri wangu kwa Serikali na kwa kupitia Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawaziri waliopo; inaweza kutumika hekima na busara tu administrative ya kiuongozi kwamba pengine hizi sheria ndogo zinapokuwa zimemaliza kutungwa, na kutokana na uzoefu tuliouona kwa sababu zipo kasoro zingine ni za msingi ambazo tunazibaini ambazo kimsingi kwa sababu ya ule uasili wake kwamba sheria ndogo au kanuni zikitungwa na Serikali zinaanza kutumika kabla hazijafika Bungeni, wananchi wengi wanaweza kuumia wakaathirika na hizo sheria zenye kasoro kubwa za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali na hasa kwa Ofisi ya Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali; waone kama unaweza kufanyika utaratibu wa kiutawala tu hekima ikatuma na busara kwamba hizi kanuni na sheria ndogo zote ambazo zinatungwa kabla hazijatumika zile ambazo zinakidhi vigezo vya kuletwa Bungeni, zisianze kwanza kutumika, zije Bungeni zipitiwe na Bunge halafu ndiyo zikafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu utaratibu umeaza lakini huu umeanza kwa hekima na busara za Mawaziri katika baadhi ya maeneo. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe tunaye hapa, tunampongeza sana, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mpina, na Waheshimiwa Mawaziri wengine wamekuwa wakinisimamisha, nakumbuka Ofisi ya Nishati na Madini pia tulishawashari mara kadhaa. Sasa tunashauri huu utaratibu na hekima hizi zirasimishwe kiutawala kwa sababu kufumua ule utaratibu, narudia tena, inahitaji mjadala mpana wa kisera na mfumo mzima wa sheria, huko ni mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili nikirejea ambacho kilishawahi kufanywa na Bunge hili Tukufu pamoja na Serikali yetu. Mwaka 2007 wakati nchi iko kwenye kiwango cha juu kabisa cha perception au niseme mgogoro uliokuwa unajitokeza ama tafsiri na dhana na namna ambavyo sisi tunanufaika na rasilimali za madini na hasa katika kuiona na ule usiri ya mikataba, Bunge lako Tukufu lilikaa na Serikali wakakubaliana. Kwa wale wanaohitaji kuiona ile mikataba ya madini ambayo kwa utaratibu wa kisheria wakati huo ilikuwa siyo rahisi mwananchi yeyote kuiona, hata sisi Wabunge, ulianzishwa utaratibu hapa Bungeni kama mtu anahitaji mikataba kupitia Ofisi ya Bunge mikataba ilianza kutolewa hapa kupitia Ofisi ya Bunge. Aifikie mtu asome ayaseme anayotaka kuyaona halafu aishauri Serikali ama Bunge namna bora ya kuboresha maeneo hayo, kabla hatujarekebisha zile sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hata hili kwa sasa Serikali inaweza kutafakari vizuri, narudia tena, administratively tu wakaona kwamba pengine sasa kweli kama ambavyo Bunge limekuwa likipewa-concerned wakae pamoja, kanuni yoyote inapoingizwa hapo Mezani isitumike kwanza kule mpaka sisi tutakapoipitia Kamati ya Sheria Ndogo. Na sisi Kamati ya Sheria Ndogo tuko tayari sana, sana kuliko ilivyokuwa jana, kuliko ilivyokuwa juzi, kuzipitia kanuni zote ambazo Serikali inatutumia hata kwa uharaka wanaokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika. Nimesimama kuchangia Muswada huu ulioko mbele yetu lakini la kwanza kabisa ninaunga mkono hoja hii iliyoko mbele yetu. Pamoja na yale tunayoyapendekeza kupitia marekebisho ya Muswada huu yaliyowasilishwa na Serikali lakini pia na ushauri wa Kamati kama ambavyo Taarifa yetu ya Kamati ilivyowasilishwa na Mheshimiwa mtemi Andrew Chenge, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongea jambo kubwa sana katika maslahi ya Taifa letu na jambo jema siku zote linabaki kuwa jema lakini sote tunafahamu katika historia ya maendeleo ya mwanadamu kwamba yako mambo ambayo huwezi kuyakwepa. Moja, ni mabadiliko. Kama wanadamu, kama jamii hatuwezi kukwepa mabadiliko. Ni mabadiliko peke yake ndiyo yanayobaki kuwa permanent katika uhai wake lakini mambo mengine yote tutabadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema huu utangulizi nikijenga hoja yangu kwangu mabadiliko yaliyowasilishwa na Serikali katika huu muktadha wa kutunga sheria mpya ya usuluhishi Tanzania yameletwa katika wakati muafaka na yanastahili tuiunge mkono Serikali yetu lakini pia tunatambua kwamba Serikali yenyewe itakuwa sikivu kwa yale ambayo tunashauri yakiwa na maslahi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria iliyokuwepo ni ya mwaka 1931, leo ni sheria yenye miaka almost 89. Katika hali ya kawaida kabisa, ya tafsiri ya kawaida na tathmini unaona kabisa kwamba sheria iliyokuwepo imeshapitwa na wakati na hii ndiyo sababu yangu ya kwanza kabisa kuiunga mkono Serikali katika Muswada huu kwamba ni wakati muafaka sasa kuwasilisha sheria nyingine, kutunga sheria nyingine ya usuluhishi inayoweza kutusogeza mbele zaidi ya tulivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunajadili uwasilishwaji wa Muswada huu na vifungu vyake ni muhimu sana kutambua usikivu na kuipongeza Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Dkt. Mahiga. Amefanya kazi kubwa sana akishirikiana na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu pamoja na Katibu Mkuu akiwa mwandishi mkuu wa sheria, tumeshirikiana kwa uzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unavyoona hii schedule of amendment imetokana na ushauri tunaoshauriana na tukakubaliana kimsingi kwamba badala ya sisi Kamati kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Muswada utakaokwenda kuwa sheria, Serikali yenyewe iyachukue, iya-absorb iyalete mbele yetu. Ni jambo kubwa linalo-reflect maridhiano tuliyokuwa nayo katika kuelewa muktadha na maslahi ya Taifa hili. Kwa hivyo hili si jambo la kusema kwanini Serikali imeleta sasa. Ni kwa sababu in azingatia maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sheria inayopendekezwa kutungwa mojawapo ya tofauti yake na sheria iliyokuwepo ni kwamba hii inapanua wimbo wa scope/concept nzima ya usuluhishi. Sheria tuliyokuwa nayo imejielekeza katika baadhi ya mambo tu lakini hii wanatanua dhana nzima ya kwenda kusuluhisha migogoro inayotokana katika level mbalimbali;

(i) Ni kwamba kwa sasa hivi utaangalia hata kama unazungumzia ukifanya tathmini ya Muswada huu kwa namna ambavyo intervention zinafanyika za usuluhishi ama hata za Kimahakama, zinaanzia Mahakama za Wilaya. Unaweza kuona jinsi ambavyo ilivyo sasa. Imetanuliwa sana ili wananchi wengi wafaidike na hii maana yake, lengo ni kupunguza gharama ambazo zinawakabili wananchi inapojitokeza migogoro kama hii;

(ii) Kuongeza kasi ya usuluhishi wa migogoro kama hii. Kwa hivyo hili ni jambo la msingi nan i mojawapo ya sababu za msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu nimesema kama nilivyosema unafungua wigo. Lakini una maeneo yake mahsusi, moja unajielekeza kutatua usuluhishi wa migogoro ya ndani pia una muktadha mwingine wa usuluhishi wa migogoro ambayo inahusu muktadha wa Kimataifa imeelezwa vizuri kuliko ilivyokuwa awali. Sasa katika mazingira hayo, kuna sababu gani ya kutoiunga mkono Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jingine la muhimu Muswada huu unapendekeza kuanzisha kituo cha usuluhishi Tanzania. Mheshimiwa Salome Makamba nimekusikia, unazungumzia kituo cha usuluhishi kilichoko pale Arusha, ni moja. Lakini hili leo tunasikia kuna vituo vya usuluhishi wa migogoro London, unakwenda Paris, unakwenda Singapore, mazingira ambayo Serikali imekuja nayo katika kupendekeza Muswada huo inalenga huko ambako tunatazamia wote kufika kwamba hata sisi Tanzania baada ya miakadhaa tutakuwa na kituyo chetu cha usuluhishi wa migogoro am bao hata Mataifa mengi yatakuja hapa. Jambo jema kama hili kuna sababu gani ya kuipinga Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasema kwenye Kifungu cha 77 pale ambacho kinapendekezwa kinaelezea umuhimu wa kuanzishwa hicho kituo na namna gani hiki kituo kitashirikiana na Taasisi zingine za Kimataifa tunazozitambua kupitia conventions mbalimbali ambazo Serikali kwa niaba ya Taifa letu tumeridhia kuwa sehemu ya hiyo mikataba au maridhiano ya Kimataifa. Kwa hiyo, tunakwenda vizuri na ndiyo maana nasema ni muhimu sana kuiunga mkono Serikali katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu cha 99 na 100 kwenye lile suala la maliasilia. Naomba nimalizie kwa dakika moja…

NAIBU SPIKA: Malizia sentensi Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: … kwamba Serikali imelifafanua vizuri sana katika hatua tuliyokuwa nayo usimamizi wa migogoro yote inayohusu rasilimali zetu, madini, gesi, mafuta n.k itaendelea kutekelezwa kusimamiwa kwa sheria zetu za Tanzania lakini tukitambua pia mikataba mingine tuliyoridhia, convention zile za Kimataifa ambazo tumeziridhia na mratibu wake mkuu atakuwa ni hiki kituo chetu ambacho tunakwenda kukianzisha cha Tanzania Arbitration Centre.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)