Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Richard Mganga Ndassa (4 total)

MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya Magu - Bukwimba - Ngudu - Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kuchukua nafasi hii kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011 na 2011/2012, Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilitenga jumla ya shilingi milioni 1200 ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Magu - Ngudu - Jojiro sehemu ya Ngudu Mjini yenye urefu wa kilometa 1.9
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za mradi huo kujulikana, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na ya Pili inaendelea vizuri.
Je, ni lini miradi ambayo haijakamilika itakamilika hasa ikizingatiwa kuwa Serikali iliahidi kukamilika kwa miradi hiyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2015?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilifadhili utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini, Awamu ya Kwanza na ya Pili kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini (REA). Miradi ya awamu ya kwanza imeshakamilika kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha iliyotengwa kutekeleza miradi ya REA Awamu ya Pili ni shilingi bilioni 877.3 na hadi sasa Serikali imeishalipa asilimia 75 na inaendelea kutoa fedha ili miradi ikamilike kabla ya mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Awamu ya Pili, katika Mkoa wa Mwanza ikiwemo Jimbo la Sumve Wilaya ya Kwimba unatekelezwa na Mkandarasi Chico-CCC (BV) JV. Wigo wa kazi wa Mkoa wote kwa Mwanza ni ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 wenye urefu wa kilomita 463. Kadhalika ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 365 na kuunganisha umeme wateja wa awali wapatao 8,990. Utekelezaji wa kazi wa Mkoa wa Mwanza umefikia asilimia 78. Gharama ya Mradi wote wa REA Phase II ni shilingi bilioni 25.36. Mradi unatalajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa ujenzi wa bomba la maji ya Ziwa Victoria kutoka Magu - Sumve - Malya utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inatekeleza miradi ya maji safi na maji taka kwa Jiji la Mwanza pamoja miradi ya maji safi katika miji mitatu ya Magu, Misungwi na Lamadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mji wa Magu mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha Euro milioni 5.3 na Mkandarasi anatarajiwa kuanza ujenzi wa mradi ifikapo mwezi Julai, 2016. Idadi ya wananchi watakaonufaika na mradi huu inakadiriwa kuwa wananchi 73,363 ifikapo mwaka 2040.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miji ya Sumve na Malya, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini gharama za eneo la kupitisha mradi. Kazi ya upimaji pamoja na usanifu itakamalika mwezi Aprili, 2016 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-

Usanifu wa kina wa barabara ya Isandula (Magu) – Bukwimba Station – Ngudu hadi Hungumalwa ambayo ni kilometa 74 umeshakamilika:-

Je, ni lini barabara hiyo itaingizwa kwenye bajeti ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Isandula hadi Hungumalwa yenye urefu wa kilometa 71 ni Barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS). Barabara hii inapita katika Mji wa Bukwimba, Nyambiti na Ngudu na ni barabara muhimu katika kukuza uchumi wa Wilaya za Magu, Sumve na Ngudu. Barabara hii pia ni kiungo kati ya barabara kuu ya Mwanza – Sirari na Mwanza – Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Wizara yangu inaifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami. Kazi ya usanifu wa kina inatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2019. Baada ya usanifu huo kukamilika na gharama kujulikana, barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi huo wa kiwango cha lami ukisubiriwa, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo kuhakikisha kuwa inapitika majira yote.