Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi (5 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
(a) Je, Serikali inasafirisha nje ya nchi mbao na magogo kiasi gani kwa mwaka?
(b) Je, ni nchi gani inaongoza kwa kununua mbao na magogo kutoka Tanzania?
(c) Je, ni fedha za kigeni kiasi gani zimepatikana kutokana na mauzo ya magogo na mbao nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2015?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 50 ya Kanuni za Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, inakataza usafirishaji wa magogo kwenda nje ya nchi. Aidha, Kanuni hiyo hairuhusu uuzaji nchi za nje wa mbao zenye unene unaozidi inchi sita. Kanuni hii na sheria vinaweka zuio ili kutoa fursa ya kukuza viwanda vya ndani ya nchi na ajira kwa Watanzania katika kupasua mbao na utengenezaji wa samani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya mita za ujazo 333,404.91 za mbao chini ya inchi sita ziliuzwa na kusafirishwa kwenda nchi za nje.
Aidha, kwa mujibu wa takwimu nchi ya India inaongoza kwa kununua mbao kutoka Tanzania ambapo katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya meta za ujazo 210,968.07 zilisafirishwa kwenda India, ikifuatiwa na nchi ya China ambayo ilinunua mita za ujazo 68,337.04.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya fedha zilizopatikana ni shilingi 269,985,300,000 kutokana na mauzo ya mbao nchi za nje. Aidha, hakuna kiasi cha fedha kilichopatikana kutokana na mauzo ya magogo kwa kuwa biashara ya magogo kwa mujibu wa sheria haikufanyika.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI) aliuliza:-
Sekta ya maliasili na utalii ni rasilimali inayobeba uchumi wa Tanzania, ikitumika vizuri kwa uendelevu, italeta maendeleo katika jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kuipa kipaumbele sekta ya utalii?
(b) Je, ni lini Serikali itaboresha mazingira ya kazi ya askari wanyamapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sekta ya maliasili na utalii inatoa mchango mkubwa na kubeba uchumi wa Tanzania. Kwa mfano, sekta hii imechangia takribani asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo yaani 2012/2013 – 2014/2015 na hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii imechangia pia katika ajira nchini ambapo takribani ajira 500,000 za moja kwa moja ambayo ni takribani asilimia 11 ya ajira zote na ajira takribani 1,000,000 zisizo za moja kwa moja zimetolewa. Aidha, sekta hii imeendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, elimu, mawasiliano, burudani usafirishaji na uzalishaji wa huduma mbalimbali kwa watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mipango ya uendelezaji wa sekta ya utalii kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 na mipango ya kila mwaka wa fedha. Kwa ujumla mipango ya uendelezaji wa sekta inajumuisha utunzaji na uboreshaji wa vivutio vya utalii vilivyopo, uainishaji na uboreshaji wa vituo vipya vya utalii, uboreshaji wa miundombinu ya utalii, uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa watalii na kwa umuhimu wa pekee kuongeza mbinu na jitihada za kutangaza utalii wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande mwingine Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya utalii. Kwa mfano, kwa kipindi cha mwaka 2017 – 2022, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itatekeleza mradi wa kuboresha utalii Ukanda wa Kusini mwa Tanzania kwa gharama ya takribani Dola za Kimarekani zisizopungua milioni mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa na ngumu inayofanywa na Askari Wanyamapori wanapotekeleza majukumu yao ya kutoa ulinzi na kusimamia uhifadhi kwa ujumla wa wanyamapori hususani kupambana na ujangili. Aidha, kuanzia mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kazi ya Askari Wanyamapori sambamba na watumishi wengine ambapo kwa upande wa Askari Wanyamapori, upatikanaji wa vitendea kazi, uboreshaji wa stahili zao na usimamizi bora zaidi wa utendaji kazi ni miongoni mwa malengo ya Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). Mamlaka hii imeanzishwa tarehe 16 Oktoba, 2015 ili ifanye kazi sambamba na Mamlaka ya Ngorongoro na TANAPA katika kutekeleza lengo kuu la udhibiti wa ujangili nchini.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
(a) Je, ni wanafunzi wangapi walifuzu kwa kiwango cha Diploma na Digrii katika Sekta za Sanaa na Ubunifu, Habari, Teknolojia na Sayansi, Elimu ya Afya kwa Mwaka 2010-2015?
(b) Je, Serikali imefanya tathmini katika maeneo ya utumishi yenye uhaba wa taaluma tajwa hapo juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha stashahada kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2015 katika sekta za Sanaa na Ubunifu (Fine and Perfoming Arts) ni 254, Habari yaani waandishi ni 1,565, Teknolojia ya Sayansi ni 12,538 na Elimu ya Afya ni 14,177, jumla walikuwa 28,534. Aidha, kwa upande wa wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha shahada kwa kipindi tajwa, takwimu zinaonesha kuwa katika sekta za Sanaa na Ubunifu ni 136, Habari 2020, Teknolojia na Sayansi ni 11,953 na Elimu ya Afya ni 5,043 ambapo jumla yao walikuwa ni 17,334
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba inaeleweka kuna upungufu wa wataalam katika baadhi ya fani, kama vile Uandishi wa Habari, Afya, Ualimu wa masomo ya Sayansi, Uandishi wa Teknolojia na Gesi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tayari imeandaa Andiko(Concept Note) kwa lengo la kufanya tathmini ya kina katika sekta mbalimbali, zikiwemo zilizotajwa kwenye kipengele (a) cha swali la msingi ili kuainisha mahitaji na upungufu wa Rasilimali watu, kiidadi na kiujuzi katika Utumishi wa Umma na hatimaye kuweza kuandaa mkakati wa namna ya kushughulikia upungufu utakaoonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati utakaoandaliwa ambao unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2016/2017 utaiwezesha Serikali kuwa na matumizi mazuri ya Rasilimali iliyopo ili kufikia Malengo na Mipango ya Taifa ya Maendeleo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi ni muhimu kwa uchumi wa nchi, sekta hii ikiwezeshwa ina uwezo angalau kufikisha shilingi bilioni 12 kama kipato kwa mwaka:-
Je, ni lini na kwa vipi Serikali itaipa kipaumbele Sekta ya Uvuvi nchini ili kuboresha utendaji na kuongezea nchi kipato?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya Uvuvi ili iweze kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa kupitia mikakati na mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji. Aidha, kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha miundombinu ya uvuvi, ikiwemo bandari ya uvuvi na kuimarisha ubora na usalama wa samaki na mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2015/ 2016, Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ilikusanya maduhuli kiasi cha shilingi bilioni 19 ambayo ni zaidi ya asilimia 100 ya lengo la bilioni 18 ilizokuwa imepangiwa kukusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeandaa kanuni za kusimamia uvuvi katika Bahari Kuu ya Tanzania ambapo zimetoa fursa kwa meli kubwa za uvuvi zinazovua bahari kuu kushusha samaki katika Bandari ya Dar es Salaam (Gati Na. 6) na Zanzibar (Gati Na. 3). Aidha, samaki wanaovuliwa bila kukusudiwa (by-catch) watashushwa katika bandari hizo ambapo itatochea uzalishaji wa samaki nchini, ukusanyaji wa maduhuli, upatikanaji wa ajira na kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeanza mapitio ya Mpango Kabambe wa Uvuvi (Fisheries Master Plan) wa mwaka 2015 kwa lengo la kutoa mwongozo wa utekelezaji wa mpango ili kuchangia katika kuongeza usalama wa chakula, lishe, ajira, kuchangia uchumi wa nchi pamoja na kuongeza pato la Taifa. Aidha, Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo awamu ya pili (ASDP II) ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka 2017/2018 hadi 2022/2023.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI Aliuliza:-
Suala la mabadiliko ya tabianchi ni mtambuka na linagusa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Je, ni mashirika ya umma mangapi yamepokea ruzuku kutoka Wizara/Idara au kwa wafadhili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita? Je, nini madhumuni ya ruzuku hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mashirika ya umma yanayopata ruzuku kutoka kwenye Wizara, Idara au wafadhili.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye kipengele (a), haiwezekani kuelezea madhumuni ya ruzuku ambayo haitolewi.