Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi (10 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali la nyongeza au ni ushauri kwa Wizara husika. Mafuriko mengi yanayotokea sasa hivi ni kwamba miundombinu au zile njia za maji zimejaa michanga, pamoja na mabwawa yale ambayo ni reserves za mafuriko nazo zimeharibika. Sasa naishauri Serikali, Wizara husika hiyo ya mazingira, pamoja na Wizara ya Maji wawe na mkakati maalum wa kudhibiti zile njia za maji wachimbe zile drainage pattern za mito au/na mabwawa ili ku-conserve au ku-protect mafuriko yasitokee. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea ushauri wake mzuri na ambao tunaendelea kuufanyia kazi siku hadi siku, lakini nitoe wito kwa Wabunge wote, kushiriki siku ya usafi. Inapofika tarehe ya usafi, Waheshimiwa Wabunge wote na viongozi wote lazima tuwe kielelezo kwa wananchi kushiriki usafi huu. Tutashiriki kuzibua hiyo mitaro, kufagia na tutashiriki kuhakikisha kwamba kila eneo linakuwa safi na salama.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, kuna uhusiano chanya kati ya elimu na maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi; je, ni lini Serikali au Wizara itaona umuhimu wa ku-link elimu na maendeleo ya Taifa letu au katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuwa, tayari Serikali imeshachelewa kutathmini; je, tuna upungufu wa aina gani au tunahitaji watu wenye elimu ya aina gani ili kuleta maendeleo katika sekta fulani? Wameji-commit kwamba mpaka mwisho wa mwaka huu wa fedha watakuwa tayari wamekamilisha huo mkakati.
Je, huu mkakati watau-link vipi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi Serikali inatambua mahusiano kati ya elimu inayotolewa na ustawi wa jamii au katika kuleta maendeleo. Ndiyo maana msisitizo uliopo sasa hivi ni kuhakikisha kuwa, course zote zinazoanzishwa hasa katika vyuo vyetu, ni zile zinazojitahidi kujibu changamoto zilizopo katika jamii zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo basi, baada ya kukamilisha mpango huu ambao umeandaliwa, unaoangalia kwa kina sasa kwa jinsi ambavyo Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano lakini pia Dira yetu ya Taifa ya mwaka 2020 - 2025, kwamba tunataka kwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Katika uchumi wa viwanda tutahitaji wataalam mbalimbali watakaoendesha viwanda vyetu, vilevile katika hao watakaoendesha viwanda tunategemea humo kutakuwa na mambo ya aina mbalimbali. Kwa mfano, afya zetu ili hao watumishi waweze kufanya kazi zao vizuri. Pia tunategemea kupunguza madhara kwa akinamama waweze kujifungua salama. Kwa hiyo, kutokana na matatizo kama hayo, ndiyo maana hata sisi sasa mitaala yetu lazima ijibu changamoto ambazo zipo katika jamii.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kuna tatizo pia la mipaka kati ya TFS na vijiji Wilayani Kondoa; vijiji vya Mnenia, Masanga, Itolowe na Kasese ambapo beacon za TFS zimeingilia katika mashamba ya wanavijiji hawa. Sasa ningependa kujua Serikali ina mkakati gani au ni lini itarekebisha tatizo hili ambalo linawaacha wanavijiji hawa njia panda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia akisema kwamba katika vijiji alivyovitaja beacons za TFS kwa kauli yake zimeingia katika mashamba ya wananchi kwenye vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kwamba hii
ndio sababu tumeunda kamati maalum kwa sababu kusema tu moja kwa moja kwamba beacons zimeingia kwenye maeneo ya mashamba ya watu bila kuangalia kwamba upo
uwezekano mashamba ya watu yameingia ndani ya maeneo ya hifadhi haitakuwa sahihi katika hatua hii. Kwa hiyo, tuipe nafasi Serikali iweze kuendelea kufanya kazi ya kwenda kufanya utafiti wa kwenye site wa kuangalia uhalisia ulivyo tukipima kwamba ni kipi kimeingia upande upi lakini wakati huo huo tukiangalia zaidi maslahi ya hifadhi ambayo ndio priority kwa Taifa.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, japo nia ya Serikali ni njema kurasimisha ardhi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa,
lakini kuna concern kwamba tunakuwa tunaendeleza squatters, maeneo ya wazi ambapo miundombinu inakuja
kuwa challenge. Sasa badaye mnapotaka ku-implement mambo ya mipango miji au ramani zetu tulizonazo kutakuwa kuna gharama tena husika za kubomolea watu. Je, Serikali nimezingatia hili? Asante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachozungumza nadhani kama nimejibu vizuri, ulinisikiliza wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Allan, si nia ya Serikali kuona kwamba miji inaendelea kuharibika kwa kuendeleza squatter na ndiyo maana nimewaomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote ni Wajumbe wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri zetu, pale ambapo Serikali imeanza kufanya zoezi la urasimishaji katika maeneo ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha kwamba wanasimamia maeneo yao ili kusiwe na muendelezo wa ujenzi holela. Kwa sababu zoezi hili linapaswa kusimamiwa na Halmashauri zenyewe husika, Wizara sio rahisi kushuka kila maeneo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli zoezi tunalifanya na inaonekana ni zuri, lakini tusingependa kuona ujenzi holela
unaendelezwa. Sasa ujenzi huu utasimama pale ambapo kila halmashauri itawajibika katika eneo lake kuhakikisha inakuwa na michoro ya mipango miji kwenye maeneo yao na kusimamia zoezi la ujenzi holela lisiendelee katika maeneo yao. Tukifanya hivyo, miji yetu itakuwa salama na itakuwa inapendeza.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nilitegemea Wizara itaonesha angalau trend ya mapato kutoka kwenye shughuli za uvuvi angalau miaka mitano au kumi tuone kwamba inaendaje, ila wametoa tu mfano kwa mwaka wa 2015/2016. Ukiangalia mapato kutoka uvuvi 2016/2017 huu mwaka uliokwisha, walikuwa na pungufu almost shilingi bilioni tisa kwa sababu walipata tu shilingi bilioni 10. Sasa Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuamka na kuweka vipaumbele katika Sekta hii ya Uvuvi ili kujiongezea mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mfano tu, bajeti ya maendeleo inayotengwa katika Sekta ya Uvuvi, mwaka 2016 na mwaka huu 2017 ni sifuri. Kwa hiyo, ina maana shughuli za doria, mikakati ya kujenga Bandari ya Uvuvi au kuboresha Bandari ya Uvuvi haipo, kujikita zaidi katika kuongeza mapato katika deep sea fisheries, haipo; hii mikakati yote haipo; zaidi kuna project moja tu ya SWIOFish ndiyo ambayo imesimama ambapo fedha zake kutoka World Bank ni za mikopo. Sasa Serikali haioni kwamba hawako fair kwa wavuvi, shughuli za uvuvi na yenyewe pia inajinyima mapato ambayo yangetuletea maendeleo katika nchi yetu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ASDP II na katika Programu hii, yote anayoyazungumzia Mheshimiwa Mbunge, yamo. Ni programu itakayoanza mwaka huu wa fedha mpaka mwaka 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba haoni mikakati yoyote ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi; mkakati lazima utengenezewe mazingira ili uweze kutekelezwa. Kwa hiyo, tusingeweza kupanga mambo ya uvuvi wa bahari kuu bila kuwa na legal framework ambayo inatuwezesha kutekeleza yale tunayotaka kufanya. Kwa hiyo, tulichoanza nacho ni kubadilisha kanuni za uvuvi wa bahari kuu ili sasa yale tutakayopanga kuyafanya, yaweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kusisitiza hapa kwamba akisoma kanuni na natumaini ameshazisoma; ataona wazi kwa vipi sasa hivi tutabadilisha sana sura ya Sekta ya Uvuvi wa bahari kuu hapa nchini na manufaa yataanza kuonekana. Sasa hivi tunapozungumza, wavuvi wa bahari kuu ambao wameomba kukata leseni kwa masharti mapya wapo wengi, wamekwishafika 30 na kadhaa hivi. Kwa hiyo, tuanze tu kutegemea kwamba manufaa makubwa ya uvuvi yataonekana hapa nchini na hicho kinachoitwa blue economy utakishuhudia kinatokea hivi karibuni.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kilometa 180 tu kutoka hapa kuelekea Kondoa – Irangi kuna malikale nzuri, kuna michoro ya mapangoni na miundombinu ya barabara imeimarika. Sasa nataka kujua Wizara hii husika itatengeneza vipi yale mazingira ya kule ili kuimarisha utalii pamoja na mafunzo katika mapango ya michoro ya kale Kondoa – Irangi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vivutio vyote vya utalii ambavyo vinaangukia kwenye eneo la heritage tourism vyote tumefanya utaratibu wa kuviorodhesha halafu baadaye tunavisajili. Kuvisajili maana yake ni pamoja na kuangalia viwango vyake vya ubora na kuona kama kweli vinakidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa tumepokea taarifa hizo kutoka kwenye Wilaya mbalimbali, baadaye hatua inayofuata ni kuvitembelea na kuvihakiki.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kuna changamoto lukuki katika Sekta ya Uvuvi na kwa kuwa wavuvi hao wameongezeka mara dufu zaidi ya asilimia 90 kwa miaka 10 iliyopita pamoja na vyombo wanavyotumia, lakini haviendi sambamba na nini wanachokipata.
Serikali haioni sasa ijikite kwenye ku-promote acquaculture na mariculture kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Sware ametabahari sana katika masuala ya uvuvi, kwa hiyo, anafahamu fika kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili, moja kati ya masuala ambayo yametiliwa mkazo sana ni namna gani ya kujenga uwezo wa wavuvi na Watanzania wengi kushiriki katika ufugaji wa viumbe kwenye maji katika maana ya acquaculture.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba acquaculture ndiyo hasa tunakoelekea tunavyozungumzia kuhusu blue economy. Kwa hiyo, ni kweli kama alivyosema, lakini ni kweli kwamba tumewekea mkakati. Tunataka ikiwezekana kila Halmashauri iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba wananchi wanafuga samaki, badala ya kuendelea kutumia rasilimali tulizonazo za uvuvi ambazo kwa kiasi kikubwa zimepatwa na changamoto kutokana uvuvi usio endelevu.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ahsante kwa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, napenda kujua Serikali imefikia hatua gani kwenye kulipa fidia au kuboresha mazingira ya wanakijiji wa Uvinje vis-a-vis TANAPA?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kwa vijiji vile vinavyozunguka au vilivyo ndani ya Saadani kuona vinashirikishwaje katika shughuli za kitalii ili kudumisha au kuboresha uchumi wao? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu fidia kwenye vijiji alivyovitaja. Kwa kuwa hadi nasimama hapa bado nilikuwa sijapata taarifa zilizokamilika kuhusiana na madai hayo, nimuahidi nikitoka hapa anipe kwa ufafanuzi vijiji hivyo ni vipi na kwa nini vinastahili fidia ili niweze kuangalia tumefikia katika hatua gani pale Wizarani kuweza kukamilisha utaratibu huo wa kuwalipa fidia ikiwa watakuwa wanastahili kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la namna gani Wizara au Serikali inashirikisha vijiji vinavyozunguka maeneo ya Hifadhi ya Saadani katika masuala ya kuendeleza vivutio, utaratibu wetu kwa kawaida ni kwamba kila wakati tunapofikiria kuanzisha mradi, wadau wa kwanza kabisa na hii nimeisema hata katika swali la msingi, kwamba uendelezaji wa vivutio katika hifadhi zote unashirikisha jamii zinazozunguka katika maeneo ya hifadhi na Serikali pamoja na mashirika binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa upande wa vijiji alivyovitaja katika Hifadhi hii ya Saadani tumeweza kuwashirikisha kwa mujibu wa taratibu tulizonazo lakini kama ana mawazo ya kuweza kuipatia Serikali ili tuweze kuboresha zaidi namna ya kuweza kushirikisha wananchi hawa au wadau hawa wanaoishi kwenye maeneo ambayo ni jirani na hifadhi basi tupo tayari kupokea ushauri huo tuweze kuboresha zaidi taratibu zinazotumika katika kuboresha vivutio kwenye maeneo ya hifadhi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: MheshimiwaMwenyekiti, nashukuru. Nimepata masikitiko makubwa sana kutika kwenye Wizara husika ambayo inasimamia shughuli za mazingira nchini. Kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia au inaongoza Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2014; na kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo inasimamia Mfuko wa Mazingira Nchini; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo ina fedha kutoka mashirika mbalimbali nchini na duniani kote inayosimamia shughuli zote za mazingira nchini, inanijibu kwamba haitoi, haihangaiki, haina chochote, hamna jibu linalohusu shughuli za kusimamia fedha za ku- address issues za climate change nchini na tunaona dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yameleta madhara makubwa, majira ya mvua hayajulikani, kuna ukame, na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kujua, hii Wizara ipo au haipo? Na kama ipo, mbona imenyamazia kimya issue ya mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninamheshimu sana Dkt. Sware ambaye Ph.D yake ameisoma kule Stockholm, Sweden, Masters yake ameichukulia Norway, namheshimu sana, lakini kwa sababu anashindwa kutofautisha kati ya maneno mawili ambayo ni rahisi sana, yeye ameuliza swali la ruzuku na ruzuku kwa kiingereza kwa faida yako Dokta tunaita subsidies, lakini kuna kitu kingine tunaita misaada, misaada ni grants.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yeye ameuliza ruzuku, ndio nimemjibu sisi hatuna ruzuku. Lakini haya aliyoyasema leo kama angejiongeza akauliza hayo, kwa faida ya Watanzania, kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na nchi yetu mpaka leo kuanzia tarehe 6 mpaka 17 wako Bonn, Ujerumani wanashiriki mkutano mkubwa wa kimataifa kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Na sisi Tanzania ni nchi wanachama ambao tulisaini Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kule Mjini Paris na tunayo mifuko ifuatayo ambayo sisi tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa kwanza unaitwa Adaptation Fund, yani kwa maana kwamba ni mfuko wa kuhimuli mabadiliko ya tabianchi. Mfuko wa pili, unaitwa ni Least Developed Countries Fund, yaani kwa maana Mfuko wa Nchi Maskini Duniani. Na mfuko mwingine ni GEFT ambao ni Global Environmental Facility. Mfuko mwingine ni Mfuko wa Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumepata grants hizi ambazo sasa tunapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi maeneo mbalimbali hapa nchini. Tuna mradi mkubwa sana ambao Ocean Road pale kwa sababu kina cha bahari kimeongezeka tunajenga ukuta mkubwa wa kilometa moja, ili kingo za bahari zisije zikasombwa na kuharibu makazi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni tunajenga ukuta mkubwa ili kudhibiti kingo zisiendelee kubomoka. Vilevile kupitia grants hizo kule Rufiji tunarudishia mikoko ambayo ilikuwa imekatwa na mradi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Zanzibar Kisiwapanza, kule Zanzibar Kisakasaka pamoja na Kilimani mifuko hiyo inaendelea. Kule Pangani tunajenga ukuta pamoja na kurudishia mikoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bagamoyo tunajenga visiwa 28 kwa wananchi wa Bagamoyo, zikiwepo na sekondari mbili mojawapo inaitwa Kinganya ambayo ni ya Mheshimiwa Dkt. Kawambwa. Mifuko hiyo, tunaitumia kwa ajili ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa wananchi wengi wanahamasika na ufugaji wa samaki na kwa kuwa kuna uchache wa mbegu bora ya samaki na kusababisha samaki kutoka nje kuagizwa hasa mbegu za sato na hii inaweza kuwa hatarishi kwa samaki wetu asilia nchini. Napenda kujua Serikali inajipanga vipi kuboresha na kuwekeza katika tafiti mahsusi za uzalishaji wa mbegu bora za vifaranga wa samaki na pia kuboresha maeneo mahsusi, hizi hatcheries za uzalishaji wa vifaranga vya samaki nchini. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inahamasisha katika ufugaji wa samaki na tunazo taasisi zetu za utafiti mathalani TAFIRI na vituo vyetu vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki kama kile kituo chetu kilichoko pale Morogoro Kingolwira. Vituo hivi vimejipanga vyema, vina vifaranga wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wafugaji wote wa samaki wawe tayari sasa kuweza kwenda katika vituo vyetu vilivyopo katika zones mbalimbali, kimojawapo hiki cha zone ya Mashariki hapa Morogoro kwenda kuchukua vifaranga bora kabisa na wataweza kufanya ufugaji huu wa samaki na kujipatia kipato na lishe wao wenyewe bila wasiwasi wowote.