Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joram Ismael Hongoli (18 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kupewa nafasi hii nami kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 20 Novemba, 2015. Nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa yote aliyonijalia mpaka leo hii nikaweza kuwepo mahali hapa. Lakini pili, niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe kwa imani kubwa waliyoiweka juu yangu mimi wakanichagua na kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ni nzuri sana na kwa kupitia hotuba hii wananchi wa Jimbo langu la Lupembe na wananchi wote wa Tanzania wameifurahia sana, kwani inaonyesha mwelekeo mzuri na matumaini mazuri ya kimaendeleo hasa kiuchumi lakini pia maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ya tarehe 20 Novemba alieleza sana juu ya viwanda hasa viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaajiri watu wengi sana. Viwanda hivi vimekuwa vikiajiri watu wengi na hivi viwanda ni vile viwanda vinavyohusika sana na usindikaji wa mazao mbalimbali kwa ajili ya kuongeza thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Lupembe tuna kiwanda cha muda mrefu sana, Kiwanda cha Chai Igombola ambacho hivi sasa ninavyoongea kwa takribani miaka zaidi ya nane kiwanda hiki kimefungwa, kilifungwa tarehe moja mwezi wa nane mwaka 2008, kutokana na mgogoro uliokuwepo kati ya Wakulima na Mwekezaji. Naomba Serikali ijitahidi au ifanye jitihada za kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinafunguliwa ili wananchi wale wa Lupembe waweze kuuza mazao yao ya chai, lakini pia tuweze kuimarisha uchumi na hatimaye Serikali ikaweza kukusanya kodi kutokana na mishahara ambayo itatokana na wafanyakazi watakaokuwa wameajiriwa pale, lakini pia iweze kupata tozo kwa maana ya kodi kwenye kiwanda kile na hatimaye kuweza kuinua uchumi wa wananchi wa Lupembe ambao umezorota sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kuelezea kidogo juu ya zao letu la chai. Zao hili limekuwa likilimwa maeneo yangu na ndiyo zao kuu tunalolitegemea sana sisi wana Lupembe. Lupembe ipo Halmshauri ya Wilaya ya Njombe, mnafahamu wote ni Halmashauri ya zamani sana hii, na Lupembe ilikuwa ni miongoni mwa maeneo hapa nchini yanayoongoza kwa ulimaji wa chai. Lakini zao hili la chai limekuwa likiuzwa kwa bei ndogo sana ukilinganisha na bei za uzalishaji wa zao hili. Sasa hivi linauzwa kwa shilingi mia mbili hamsini lakini bei ya uzalishaji, gharama za uzalishaji, ukijumlisha zote za kuuzia, gharama za uzalishaji wa kilo moja ya chai ni shilingi 450/=. Kwa hiyo wakulima hawa wanafanya hiki kilimo kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweze kuziangalia kodi mbalimbali ambazo zimeingizwa kwenye zao hili ili ziweze kupungua na hatimaye wakulima wa Lupembe waweze kupata faida kutokana na zao hili la chai.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niweze kuongelea kidogo juu ya elimu, tumesema kwamba Serikali hii sasa kwanza wananchi wangu wamefurahi baada ya Mheshimia Rais kutangaza kwamba sasa elimu ni bure. Kwa hiyo, wananchi wengi waliokuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule sasa wataweza na wameshaanza kupeleka kwa wingi sana. Lakini kupeleka wanafunzi wengi haisaidii kama hatujatengeneza mazingira mazuri kwenye shule hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu moja wapo niiongelee kidogo ni kuhusu walimu hususani madaraja ya walimu, upangaji wa madaraja ya walimu ya mishahara, kumekuwa na tatizo kubwa sana, walimu wamekuwa wakilalamika. Utakuta kwa mfano, mwalimu amefanya kazi miaka saba, nane akiwa na level ya diploma anaenda kusoma degree, anaporudi anapewa daraja lile la “D” halafu anapewa daraja bila kupewa mshahara. Tunaita anapata dry promotion, sasa dry promotion zimekuwa zikikatisha sana tamaa kwa walimu kufanyakazi. Kwa hiyo, tusipoboresha kwenye upande wa walimu hasa madaraja wanapopata promotion ni vizuri yaendane na malipo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa hivi utakuta kwamba mwalimu anaporudi kutoka chuoni kwenda kufundisha wakati alikuwa amefanya kazi muda mrefu anaenda kuanza ngazi ya mshahara sawasawa na yule kijana au mwanachuo anayeanza kazi. Sasa hii inawakatisha tamaa walimu wengi sana na ndiyo maana utakuta tunasomesha walimu wengi lakini mwisho wa siku walimu wanaamua kuhama kada wanahamia kada nyingine, kwa kuwa wanaona kada hizi za walimu kidogo zinausumbufu na maslahi yake yapo duni. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kurekebisha utaratibu huo, mimi naamini kwamba ingekuwa ni vizuri kama mwalimu amefanya kazi ameenda kusoma anaporudi basi angalau aongezee ngazi ya mshahara nzuri zaidi kuliko wale wenzake waliobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hivi utakuta kwamba wenzake waliobaki ambao hawajaenda kusoma wanakuwa na mshahara mkubwa zaidi, wanapewa daraja zuri zaidi kuliko yule aliyeenda kusoma. Kwa hiyo, kwa kada ya walimu kusoma sasa imekuwa kama ni adhabu. Tunaomba Serikali iweze kurekebisha jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kidogo juu ya huduma ya afya. Jimbo langu la Lupembe ambayo ndiyo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mpaka leo hii haina hata hospitali moja na mpaka leo hii ina kituo cha afya kimoja, Halmashauri nzima, Jimbo zima na zahanati ndogo ndogo na vituo vya afya vingine viwili ambavyo bado vipo kwenye ujenzi. Wananchi wale wanapata shida sana ili waweze kujifungua hasa kwa operation kuna baadhi ya wananchi wanatembea kilometa mia moja arobaini na saba kwenda kutafuta Hospitali ya Kibena ili waweze kupata operation za uzazi. Naomba Serikali ijaribu kuliona hili jambo la muhimu sana tunaomba tupewe hospitali ya Wilaya lakini pia vituo vyetu hivi vitatu viweze kuboreshwa viwe na huduma ya operation kwa maana ya theatre ili akina mama wasiteseke kutembea umbali mrefu na wengine kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo juu ya wastaafu. Wastaafu waliostaafu kuanzia mwezi wa sita mpaka mwezi Disemba hawajalipwa mafao yao wanataabika huko, wanalalamika na wanailaumu Serikali. Kwa hiyo tunaomba Waziri mwenye dhamana aweze kuchukua jitihada ya kuhakikisha kwamba hawa wastaafu wetu waliofanya kazi muda mrefu, waliojenga Taifa hili wanapata mafao yao haraka ili waendelee kuishi vizuri na kufurahia kustaafu kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo juu ya jambo moja kuhusu umeme, Jimbo langu Halmashauri ya Wilaya ya Njombe sehemu kubwa halina umeme. Tuna vijiji 49 lakini vijiji tisa tu ndivyo vyenye umeme. Namuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na sisi pia atufikirie kule kijijini tuweze kupata huduma ya umeme ili tujisikie na sisi ni miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongee jambo kidogo kuhusu maji. Katika Jimbo langu la Lupembe na ndiyo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe vijiji vingi havina maji, mpaka sasa hivi ni vijiji nane tu ndivyo vyenye maji. Sasa kwa hali hii ndugu zangu au Serikali tunaomba mtuangalie na sisi tupate maji kama alivyosema Rais hii Serikali ni Serikali ya kuwatua kina mama ndoo ya maji, basi mtutue na sisi kule Wanalupembe na sisi tujisikie kwamba wake zetu, mama zetu, wanafurahia maisha kwa kutuliwa ndoo za maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisema kidogo juu ya Halmashauri yetu ya Wilaya ya Njombe ipo kwenye Halmashauri nyingine, ipo kwenye Halmashauri ya Mji wa Njombe. Sasa Watendaji wengi na wananchi wengi wanapata shida sana kupata huduma na ile ni Halmashauri Mama ni Halmashauri ya zamani sana. Sasa hivi ukienda hakuna hata gari moja……
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hongoli muda wako umekwisha.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kupewa nafasi hii, lakini pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwasilisha Mpango mzuri ambao unaonesha mwanga wa maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba, ili tuweze kuendelea na kufikia uchumi wa kati, tunahitaji mipango mizuri kama ilivyooneshwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/2017 na 2016 - 2020. Katika Mpango huu kuna sehemu moja ambayo nitaiongelea sana hasa miundombinu ya barabara. Ili tuweze kuendelea kama nilivyosema, ni lazima tuwe na barabara nzuri ambazo wakulima wengi wanazitegemea, lakini pia hata viwanda vinategemea barabara au miundombinu. Barabara nyingi zinazokwenda vijijini ambako ndiko tunakoweza kupata malighafi za kuendeshea viwanda vyetu ambavyo tunasema kwamba tunataka tuingie kwenye uchumi wa viwanda, ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na barabara nzuri, tunapokuwa na barabara za lami inakuwa rahisi kwa wakulima hawa kuweza kusafirisha mazao yao ambayo ndiyo malighafi za viwanda na hatimaye wakaweza kuuza mazao yao kwa haraka zaidi na yakapata bei nzuri zaidi; lakini siyo bei tu, hata ubora wa mazao yao na ubora wa bidhaa ambazo zitatokana na haya mazao zitakuwa bora zaidi na hatimaye kuweza kupata faida kubwa au kupata products ambazo zinaweza kuuzwa hata nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, products zetu nyingi zinakataliwa, haziwezi kupata soko la nje kwa sababu tu hazina ubora na inaonekana kwamba ubora huu unakosekana kwa maana ya kwamba bidhaa nyingi zinafika kiwandani zikiwa zimechelewa au zimeharibika. Kwa mfano, kama bidhaa za matunda, zinafika kiwandani zikiwa zimeharibika. Kwa hiyo, hata zao lake au lile zao linalokuja kutoka kiwandani linakuwa halina ubora na hatimaye zinakataliwa kwenye masoko mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia Mpango uweze kuboresha miundombinu ya barabara. Kwa mfano, katika maeneo ya uzalishaji, mimi natoka Jimbo la Lupembe ambapo sehemu kubwa tunazalisha chai, lakini tunazalisha matunda, mananasi, tunazalisha matunda mengine kama parachichi na mengineyo. Barabara za kule hazipitiki kwa hiyo, wakulima wanashindwa kuuza mazao yao.
Mheshimiwa Waziri hasa Waziri wa Ujenzi, ukienda kuangalia jinsi gani wananchi wanavyomwaga haya mazao, jinsi gani chai inavyomwagwa kila siku, utawaonea huruma na utatamani kulia. Kwa hiyo, tuombe miundombinu hasa ya maeneo haya ambayo yana uzalishaji mkubwa, barabara zitengenezwe vizuri ili hatimaye wananchi waweze kuuza mazao yao na hatimaye kupata faida na kama Taifa kuweza kuongeza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu kwa mfano nikisema hii ya Lupembe, ilishaingia kwenye ilani ya mwaka 2010 kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami na mara moja kwenye Bunge la Bajeti fedha zilishakadiriwa kwamba tutapewa, lakini fedha hazikutoka. Nashangaa mwaka huu pia sijaiona kwenye Mpango kama itaaanza kutekelezwa hasa huu Mpango wa mwaka 2016/2017 wakati tayari ilishaahidiwa kwamba hii barabara itatengenezwa kwa kiwango cha lami.
Kwa hiyo, nakuomba Waziri wa Ujenzi nafikiri unanisikia vizuri sana na ni msikivu, hebu tujaribu kuingiza au tuingize kwenye Mpango ili sasa mazao haya ya chai na chai ya Lupembe mnaifahamu ni chai bora na ilikuwa ni moja ya chai bora duniani, ilikuwa na soko kubwa sana na zuri sana. Waliokuwa wanafuatilia mambo ya soko la chai wanajua jinsi gani ile chai ilivyokuwa na soko zuri duniani, lakini leo imepotea kwa sababu pengine ya ubovu wa njia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika Mpango wetu naomba tuangalie sana maeneo yale ambayo wakulima wanazalisha mazao mbalimbali hasa mazao ambayo yanaweza kuuzwa nchi za nje na yakatuingizia fedha za kigeni. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, tutawawezesha wananchi hawa kwanza kuuza mazao yao, lakini pia hata bidhaa zetu ziwe na ubora na kwa kupitia hivyo tutaweza kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara zinapokuwa nzuri, tunawavutia wawekezaji. Tunasema tunaenda kwenye uchumi wa viwanda, wawekezaji hawawezi kwenda kuwekeza kwenye maeneo kama ya Lupembe ambapo barabara haipitiki wakati wa kifuku; maana yake ni kwamba, watapoteza kwa maana ya kwamba watazalisha lakini hizo bidhaa zao au mazao yao ambayo wamezalisha, hawataweza kuyauza yakiwa na ubora wake kwa sababu ya ubovu wa barabara. Kwa hiyo, maeneo haya ya uwekezaji ni lazima tuhakikishe kwamba barabara zinapitika muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, viwanda tunavyovifikiria, ni lazima viwekezwe au twende tukaviwekeze kwenye maeneo ambayo yana uzalishaji. Inakuwa haipendezi wala haina tija kwa mkulima kama kiwanda kinakuwa mbali na maeneo ambayo hawa wakulima wanazalisha. Inapokuwa hivyo ni kwamba, wananchi, wale wakulima wanakosa bei nzuri ya mazao kwa sababu hapo katikati wanacheza wale middlemen, wananunua bidhaa kwa wakulima kwa bei ya chini na wanawauzia wamiliki wa viwanda kwa bei ya juu. Kwa hiyo, tayari wakulima wetu wanapoteza soko la bidhaa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kuwahamasisha wakulima, lakini pia wakulima wetu waweze kupata tija ya mazao wanayozalisha, ni lazima tuwavutie hawa wawekezaji wa viwanda mbalimbali kwenye maeneo ambako hawa wakulima wanazalisha, ndipo hapo utaweza kuwasaidia wakulima wakapata tija kwa kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda peke yake na barabara peke yake haitoshi. Ni lazima huduma za msingi hasa huduma za afya kwa maana ya Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya vijengwe kwenye maeneo haya ambayo kuna uzalishaji mkubwa, lakini pia kuna viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Njombe haina hospitali hata moja. Sasa hutegemei maeneo kama hayo wawekezaji watakuja kuwekeza kwa kuwa huduma ya afya haipo. Ni lazima tuangalie upande mwingine. Tunapotaka kuwekeza tuangalie na factors nyingine ambazo zinaweza zikasababisha wawekezaji waweze kuwekeza au inaweza ikasababisha viwanda vyetu viweze kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi ukiangalia hata kwenye Mpango, viwanda vingi vimeelekezwa mijini. Sasa vinavyoelekezwa mjini tunawanyima asilimia zaidi ya 80 ya wakulima wanaoishi vijijini au watu wa vijijini. Kwa hiyo, tukitaka kufungua fursa za ajira, ni lazima tufikirie sasa kuanza kuwekeza kwenye maeneo ambako wakulima wapo na vijana wengi wanaishi ili tufungue ajira huko vijijini, watu wabaki vijijini kuliko sasa hivi wote wanavyokimbilia mjini. Sasa kama watakimbilia mjini, nani atakayezalisha huko vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba tunafungua viwanda kule Ludewa, sasa bidhaa nyingine ambazo zinategemea hivi viwanda, watapata wapi kama hatutaweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana wetu waweze kubaki vijijini? Kwa hiyo, tunaomba kwenye Mpango pia tuweke vizuri ili hatimaye tuweze kuhakikisha kwamba tunaweza kufanikiwa hasa kuingia kwenye uchumi huu wa kati ambao ni uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishati, nalo ni suala ambalo linaendana pamoja. Tukitaka tuvutie wawekezaji wa viwanda hivi vya kati na vikubwa, ni lazima tuhakikishe kwamba maeneo yetu mengi yanakuwa na nishati ya kutosha; yanakuwa na umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, kwa mfano, eneo langu ni la uwekezaji; kuna mazao mengi ambayo yana tija ambayo watu wengi wanaweza wakapata faida, lakini wawekezaji wanashidwa kuwekeza kwa sababu umeme siyo wa uhakika. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Nishati pia katika Mpango huu tujaribu kulifikiria kuhakikisha kwamba tunasambaza umeme katika maeneo ya uzalishaji hasa maeneo ya Lupembe ambako kuna wawekezaji wengi wazuri, wanakuja lakini hawawezi kuwekeza kwa sababu hakuna nishati ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nijaribu kulisema kidogo juu ya Mpango huu, tujaribu kujadili juu ya kuhakikisha kwamba hawa vijana au wananchi ambao tumesema tutawezesha kwa kuwapa Shilingi milioni 50 kila Kijiji, ni lazima tutengeneze mpango mzuri hasa kwanza, kutoa elimu ya ujasiriamali; elimu ya matumizi ya hii mikopo ambayo tunaipanga iende kwa wananchi kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi walioko vijijini hawana elimu ya kutosha ya ujasiriamali, hawana uelewa wa kutosha wa ku-generate mkopo na mwisho wa siku wapate faida. Ni lazima tuweke mpango ni jinsi gani tutatoa elimu kwa wananchi wa vijijini ili mkopo huo wakiupata waweze kuutumia vizuri na mwisho wa siku waweze kupata faida na ile faida iweze kurudishwa na hatimaye tuweze kuongeza uchumi wa kila mmoja na hatimaye uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tujipange kuhakikisha ni jinsi gani tutatoa elimu na siyo kutoa elimu tu; jinsi gani tutawasaidia katika kuwatafutia masoko ya bidhaa ambazo pengine watakuwa wanazalisha ili ule mkopo uweze kuleta tija? Tukiwaacha tu hivi hivi tukapeleka tu zile fedha, itakuwa kama ilivyokuwa yale mamilioni ya Kikwete. Zitaenda fedha nyingi na mwisho wa siku kitakachorudi, hakuna. Kwa hiyo, tutakuwa tumepoteza mamilioni mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nafikiri inatosha. Nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa hotuba nzuri aliyoitoa leo tarehe 3 Mei, 2016. Pia, nampongeza kwa kujituma, kuwajibika vizuri katika kusimamia Wizara yake. Hii inaonesha kuwa Mheshimiwa Rais hakukosea kumteua katika Wizara hiyo. Ni matumaini yangu kuwa kupitia Waziri huyu, nchi yetu itapata mapinduzi makubwa ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa ushauri mdogo kwenye upande wa kilimo, hususan pembejeo. Serikali yetu ya Awamu ya Nne iliweka utaratibu wa kuwasaidia wakulima wetu kwa kuwapatia pembejeo za ruzuku.
Pembejeo hizi zimekuwa hazimsaidii mkulima hasa wakulima wadogo. Wafanyabiashara na makampuni yamekuwa yakiingia mikataba na Serikali ili kuwasambazia wakulima pembejeo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makampuni yamekuwa yakiwapatia pembejeo hizo kupitia mawakala kwa mtindo wa vocha. Mawakala hawa wamekuwa wakijinufaisha kwa kuwalaghai baadhi ya wakulima kwa kuwaomba wasaini vocha hizo bila kuchukua mbolea au pembejeo hizo kwa kuwalipa fedha kati ya sh. 5,000/= mpaka sh. 10,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbolea hizi zimekuwa zikipelekwa kwa wakulima kiasi kidogo au kwa kuchelewa ili ziwakute wakulima wakiwa wamepanda na kuwashawishi wasaini vocha hizo. Kupitia tabia hizi za mawakala wasio waaminifu, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwasaidia wakulima kwa kulipia baadhi ya gharama za kilimo na pembejeo, lakini zimekuwa hazizai matunda. Naishauri Serikali ione au iweke utaratibu mwingine wa kuwasaidia wakulima kwa kulipia baadhi ya gharama za mbolea au pembejeo ili wakulima wawe huru kwenda kujinunulia mbolea hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niliwahi kushuhudia wakala mmoja akielezea jinsi gani alivyonufaika na usambazaji wa mbolea hizo. Ni vizuri Serikali ifanye utafiti wa kutosha juu ya matumizi ya mbolea za chumvi chumvi kwa baadhi ya maeneo. Mbolea nyingi zinazoenda Mkoa wa Morogoro zimekuwa zikipelekwa Mkoa wa Njombe. Wakulima wengi wa Morogoro wamekuwa wakipelekewa mbolea hizo na kutochukua kwa kupewa fedha kidogo na badala yake mbolea hizi zimekuwa zikipelekwa Mkoa wa Njombe ambako mahitaji ni makubwa. Wafanyabiashara wamekuwa wakiuza mbolea hizo kwenye maduka ya kawaida na kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiajiri vijana wengi wenye taaluma ya kilimo ili kuendelea kutoa mafunzo ya kilimo kwa wakulima wetu; Mafunzo ya matumizi mazuri ya mbolea, uchaguzi wa mbegu bora na mengineyo. Lengo ni kuongeza ujuzi wa kilimo bora kwa wakulima na kuongeza kiwango na ubora katika uzalishaji. Vijana hawa wamekuwa wakikaa tu maofisini bila kufanya kazi zao kama Maafisa wa Kilimo. Ni muhimu kwa Serikali kuweka utaratibu wa kuwafanya Maafisa hawa kuwajibika ipasavyo kwa maendeleo ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Kilimo ni lazima pale wanapofanyia kazi wahakikishe kwamba, wanakuwa na kajishamba darasa (demonstration farms). Ili kuhakikisha kwamba kumekuwa na uwajibikaji wa Maafisa Kilimo, ni lazima kuwe na utaratibu wa kuweka malengo mahususi ya uzalishaji katika eneo husika na Maafisa hawa wapimwe kwa ufanisi wa malengo hayo. Kwa kuweka malengo hayo, Maafisa Kilimo wataweka utaratibu wa kushinda shambani na wakulima ili kuhakikisha kwamba malengo ya wakulima yanafikiwa na malengo yake Afisa yanafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, natoa shukrani zangu za dhati kwa kupata fursa hii ya kuchangia. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, John Pombe Magufuli kwa kuanza kutekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2014, hasa kwa kuondoa au kwa kufanya elimu ya msingi na sekondari iwe elimu bure. Hii imewasaidia Watanzania wengi ambao walikuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule za msingi na sekondari kuweza kupata elimu. Kwa hiyo, imeongeza access to primary and secondary school education. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto ambazo Wabunge wameendelea kuzisema, lakini kwanza tumefungua access, tumewawezesha Watanzania wote waweze kupata fursa ya kupata elimu ya shule ya msingi na sekondari. Hizi changamoto nyingine tutaendelea kuzitatua kadri muda utakavyokuwa unaendelea. Kwa hiyo, lazima uanze kwanza kuweka fursa, lakini baadaye katika fursa unakuwa na changamoto nyingine nyingi ambazo tumesema kuna changamoto za miundombinu, changamoto za resources mbalimbali ambazo tutaendelea kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Elimu kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hii, namwamini, yupo makini na atatufikisha pale ambapo tunatakiwa tufike, lakini pia nimpongeze Naibu wake wa Elimu, Mheshimiwa Stella Manyanya na nimpe pole kwa msiba aliopata wa mama yake. Mungu aendelee kumrehemu na aendelee kumpa nguvu katika kipindi hiki ili arudi kutekeleza majukumu muhimu sana ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika nianze kusema jambo moja linalowakera sana Walimu hasa madai ya Walimu. Pamoja na mambo mengine yote jambo la madai ya Walimu, ndiyo pengine yanachangia kuathiri kiasi kikubwa kufisha elimu au inachangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa elimu. Walimu wanapokuwa wanadai nyongeza ya mishahara, wanapodai kupandishwa madaraja, hii inawakatisha tamaa. Kwa hiyo, muda mwingi wanakuwa wanawaza kuongezewa mishahara, muda mwingi wanawaza madai yao mbalimbali na changamoto mbalimbali, kwa hiyo, wanaenda kazini wakiwa wamevunjika moyo wa kufanya kazi, hivyo hawafanyi kazi vizuri. Pamoja na kwamba tumeajiri Walimu wengi lakini ukifika kwenye mashule tuna Walimu wengi sana, lakini wanaoingia darasani ni wachache, lakini katika wachache wanaofundisha ni wachache sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wengi wanaingia wakiwa wamekata tamaa, wanaingia wakiwa wanawaza maisha, wanawaza mishahara yao, anawaza atarudije nyumbani, anawaza ataishi namna gani kule nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Wizara zinazohusika hasa, Wizara ya TAMISEMI, ihakikishe kwamba madaraja ya Walimu yanapanda kwa wakati na zile stahiki zao kwa maana ya madai yao ya likizo, madai yao ya mishahara mbalimbali na madai mengine yanatekelezwa kwa wakati ili Walimu wawe na moyo wa kufundusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua huwezi kuwa unafanya kazi vizuri zaidi, kama unakuwa na madai mbalimbali, kama unakuwa unalaumu vitu mbalimbali ambavyo hujatekelezewa. Kwa hiyo, niombe Wizara ya TAMISEMI wakishirikiana na Elimu pia, tuweze kuhakikisha kwamba, madai ya Walimu yanalipwa kwa wakati na pia madaraja ya Walimu yanapandishwa kwa wakati. Kuna huu upandishwaji wa madaraja baada ya miaka kadhaa, Walimu wengi wanaokwenda kusoma mara nyingi wamekuwa wakicheleweshewa sana kupanda madaraja yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wamekuwa wakirudi nyuma, akiondoka kwenda kusoma, akirudi anakuta Mwalimu aliyemwacha ambaye ana elimu ndogo kuliko yeye amepandishwa daraja na yeye anabakia nyuma. Kwa hiyo, hili nalo linakatisha sana tamaa Walimu. Kwa hiyo, niombe madaraja ya Walimu yaende sambamba na muda aliyofanya kazi lakini sambamba pia na elimu yake aliyoipata ili angalau tuweze kuwamotisha hao Walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme jambo moja lingine ambalo wamesema Waheshimiwa Wabunge wengi sana juu ya mikopo ya elimu ya juu. Hili nalo limekuwa ni tatizo kubwa wale walengwa ambao wanatakiwa kupewa mikopo wamekuwa hawapati, hasa watoto wa maskini wanaoishi huko Vijijini, wanapewa wakati mwingine asilimia ndogo, asilimia 40 au wakati mwingine asilimia 30 na mwisho wa siku wanashindwa kulipa ada wanabaki wakihangaika tu na wengine imefika mpaka wakati mabinti zetu wanaanza kutafuta njia nyingine za kuweza kupata fedha za kujikimu wanapokuwa chuoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuombe uwekwe utaratibu mzuri kama tulivyosema kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wanafunzi wote watakaokuwa wamedahiliwa kwenda chuo kikuu kwa kuwa wana sifa ya kusoma chuo kikuu wapewe mikopo asilimia 100 na kwa sababu ni mkopo wapewe wote kuliko kuweka haya madaraja kwa maana wengine wanapewa asilimia 80, wengine 70, wengine 60 na 40; hiyo inaleta matatizo na inaleta migomo na maandamano yasiyo na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Elimu alisimamie hili, wanafunzi wote wanaokuwa wamedahiliwa kwenda chuo kikuu, basi wapewe mikopo asilimia 100 ili tupunguze baadhi ya matatizo ambayo wamekuwa wakipata hawa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema na Wabunge wengi wamesema juu ya changamoto za Walimu wa sayansi kwamba Walimu wa sayansi hawapo au wapo wachache, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, tuna upungufu wa Walimu wa sayansi 93 na wakati huo huo tuna upungufu wa Walimu 158 wa shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunasema kwamba, tunataka twende kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda, hatuwezi kwenda kwenye uchumi huo kama hatutakuwa na Walimu wa sayansi wa kutosha. Kwa hiyo, naomba kwanza kabisa tuanze kuwahamasisha wanafunzi wetu toka shule za misingi waweze kupenda masomo ya sayansi. Walimu wa shule ya msingi wawa-encourage watoto waweze kupenda hisabati, waweze kupenda masomo ya sayansi na hatimaye wakifika sekondari waanze kupenda kusoma masomo ya sayansi, ni uamuzi tu, tuwaweze hawa Walimu wanaofundisha, tuwawezeshe Wakuu wa Shule pia ili waweze kusimamia vizuri kuhakikisha kwamba katika shule zao wanafunzi wanafaulu masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest nami ni Mwalimu, nimekuwa Mkuu wa Shule, shuleni kwangu wanafunzi hakuna option, wanasoma masomo yote yale ya msingi, yote yale tisa na wanafaulu zaidi sayansi hata kuliko art. Kwa hiyo, tukiamua tukaweka miundombinu vizuri, tukaweka mazingira mazuri, wanafunzi wanaweza wakafaulu vizuri masomo ya sayansi na hatimaye tukapata wanafunzi wanaokwenda vyuo vikuu kusomea masomo ya sayansi, kwa hiyo, tutaweza kutokomeza jambo hilo, tutaweza kusaidia kupunguza uhaba wa Walimu wa kuanzisha utaratibu wa kuweza kuwahamasisha watoto wa shule za sekondari waweze kupenda masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja kama nilivyosema, la nyumba za Walimu, katika shule zetu nyingi hasa za Kata tuna uhaba mkubwa sana wa nyumba za Walimu, hata katika Jimbo langu tuna uhaba mkubwa sana wa nyumba za Walimu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI watakavyopanga katika ujenzi wa zile nyumba zile 30 ambazo zinachukua Walimu wengi na mimi wanifikirie kule kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule mbili hazina hata nyumba za Walimu kabisa, shule ya Ndinga na shule ya Mrunga kule, kwa hiyo, mnisaidie ili niweze kupata hizi nyumba angalau na Walimu wangu waweze kukaa katika maeneo ya shule na hivyo kufundisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo linguine, wamesema la Mdhibiti wa Ubora, zamani tulikuwa tunaita Kitengo cha Ukaguzi, lakini niseme kwamba Mkaguzi wa kwanza ni mkuu wa shule, tumwezeshe mkuu wa shule aweze kusimamia shule yake vizuri na hatimaye tuwezeshe Kitengo cha Udhibiti Ubora cha Halmashauri au cha Wilaya ili waweze kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao vizuri na Wakaguzi wa Kanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakaguzi hawana fedha kabisa, hawana fedha za mafuta, wanashindwa kwenda kwenye mashule kwenda kukagua. Sasa huwezi kuamini kwamba kama Mkaguzi hawezi kufika kwenye shule kwenda kufannya ukaguzi, je, huko shuleni kutakuwa na kitu gani? Atajuaje ubora kama upo kwenye shule hizo husika. Kwa hiyo, tuombe Wizara husika nazo ziwawezeshe hawa Wadhibiti Ubora kwa maana ya Wakaguzi wetu wa Halmashauri, Wakaguzi wetu wa Knda, lakini pia tumwezeshe Mkuu wa Shule aweze kusimamia vizuri taaluma kwenye shule yake kwa kuwa yeye ni mkaguzi wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iliwekwa ile pesa ya majukumu, sh. 200,000/= kwa Walimu wakuu; Sh. 250,000/= kwa Wakuu wa Shule na sh. 300, 000 kwa Wakuu wa Vyuo. Tukiwapa hizi fedha wataweza kusimamia taaluma vizuri, wataweza kukagua vizuri na kuhakikisha kwamba Walimu wao wanafundisha vizuri. Ilivyo sasa hivi unaweza ukafika Mkaguzi wa Halmashauri au wa Kanda akafikiri Mwalimu anafundisha vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanachofanya darasani kule wanatoa notes, wanatoa kazi, wanasahihishana mle darasani, halafu mwisho wa siku akija Mkaguzi, anaangalia madaftari anakuta kuna mazoezi ya kutosha, anaangalia lesson plan na schemes of work zimekaa vizuri, lakini kumbe kinachoendelea darasani sicho hicho kilichopo kwenye hivi vitabu mbalimbali. Kwa hiyo, tuwawezeshe kwanza Wakuu wa Shule ambao wako jirani na baadaye Idara nzima ya Ukaguzi ili tuweze kuboresha elimu.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza Baraza zima la Mawaziri na Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa ni Tanzania ya Viwanda. Nawapongeza sana! Kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kuhakikisha kwamba tunafikia azma ya kuwa na viwanda au kufikia uchumi wa viwanda katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba hatuwezi kufikia huo uchumi wa viwanda bila kufikiria Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo ndiyo sekta mama ambayo itatuwezesha sisi Watanzania kuingia kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua sote kwamba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, sasa huwezi kuiacha sekta hiyo ya kilimo ukaingia kuwekeza viwanda vya aina nyingine na ukataka kufika kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, ni lazima tuitazame Sekta ya Kilimo, tufikirie kuwekeza kwenye viwanda vya kilimo. Historia inatuambia kabisa kwamba hata nchi zilizoendelea, tunafahamu wote nchi za Uingereza, Ujerumani na Marekani walianza kwanza na viwanda vya Sekta ya Kilimo; Agro Processing Industries ambavyo vilikuwa vinaongeza value ya mazao au thamani ya mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasi Watanzania tukitaka twende huko kwenye uchumi wa viwanda ni lazima tuangalie wakulima wetu waweze kuwa na viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishakamilisha kuwa na viwanda vya uongezaji wa thamani ndipo hapo sasa hawa wakulima watahitaji zana mbalimbali, watahitaji magari ya kusafirishia, basi itafanya sasa kuwe na demand ya vitu vingine ambavyo hivyo sasa vitahitaji viwanda vya mechanical industries na baadaye tutaingia pengine kwenye Chemical Industries.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami nasema kwamba, ni muhimu Waziri wetu wa Viwanda aanze sasa kuangalia maeneo hasa ya uzalishaji ili kuwavutia Wawekezaji ili waweze kuwekeza viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuongeza thamani ya mazao, kwanza kabisa itatusaidia kutoa ajira kwa vijana wetu. Tunatambua vijana wengi wako huko vijijini na sasa hivi wanakimbilia mijini wakifikiria kutafuta kazi kwenye Maofisi au kwenye viwanda mbalimbali na wakifika huko wanakosa hizo ajira. Sasa tuanze kufikiria kuanzisha viwanda hivi vijijini ili vijana wetu wengi waweze kuajiriwa kwenye viwanda hivyo, wabaki kule na kufanya kazi ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapata changamoto moja kubwa; mimi natokea Jimbo la Lupembe ambapo tunazalisha chai, kahawa, tunazalisha mazao ya matunda, kama mananasi, ndizi, machungwa na matunda mengine mengi tu, lakini kule Lupembe mpaka sasa hivi wale wananchi hawawezi kuuza mazao yao vizuri kwa sababu ya tatizo moja na hata Wawekezaji hawapendi kuwekeza maeneo yale kwa sababu ya tatizo la miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa hiyo, lazima tunapofikiria uchumi wa kati, tunapofikiria uanzishwaji wa viwanda kama nilivyosema lazima tuhakikishe kwamba kwenye maeneo ya uzalishaji ambapo huko ndiko tunategemea kuanzisha viwanda, ni lazima miundombinu ya barabara, tuhakikishe kwamba tunakuwa na barabara nzuri ambazo zinapitika muda wote ili watakaowekeza waweze kusafirisha hizo bidhaa kirahisi zaidi na hatimaye kufikia soko au kufikia maeneo ambayo wanaweza wakaongeza thamani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lazima tufikirie kuwekeza kwenye umeme. Kwa hiyo, unaona hapo Wizara nyingi sana zinahusika. Ni lazima tuwe na umeme wa kutosha kwenye maeneo haya ili tuweze kuwavutia wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo haya ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni lazima tuwe na maji. Tukiwa na maji ya kutosha automatically tutavutia wawekezaji, kwa sababu naamini kwamba, siyo Serikali itakayokwenda kujenga viwanda, wanaojenga viwanda ni wawekezaji wa ndani na nje. Sasa hawa lazima kuwe kuna huduma hizi muhimu. Huduma za maji, umeme, lakini pia huduma za afya ni lazima ziwe za kutosha ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa kwenye maeneo mengi ya uzalishaji, watu hawapendi kwenda kuwekeza kwa sababu hizi huduma muhimu hazipo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, tunapotaka kuwekeza, ni lazima tufikirie mambo hayo muhimu na hasa tufikirie kuwekeza kwenye kilimo ambacho kwanza viwanda vyenyewe ni vya bei ndogo, ni rahisi kuwekeza, lakini pia vinaweza vikaajiri Watanzania wengi na katika sera yetu tumesema kwamba lazima tuanzishe viwanda, tuanzishe shughuli ambazo zitawaajiri vijana wengi kwenye sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ili tuweze kupata uwekezaji mzuri na hatimaye uwekezaji ukawa na tija, ni lazima tufikirie maeneo ya kuwekeza, hasa maeneo yale ambayo kuna uzalishaji, maana tunaweza tukawekeza kama ilivyokuwa kwenye viwanda vile vya tumbaku, badala ya kuwekeza Songea na Tabora ambako tumbaku inazalishwa, vikawekezwa Morogoro. Hatimaye utakuta wakulima wanakata tamaa kwa sababu hawawezi kusafirisha mazao yao kuyaleta Morogoro. Kumbe viwanda hivi vingekuwa vimewekezwa sehemu zile ambazo wanazalisha, basi wakulima wangeweza kupata faida kubwa na wangehamasika kuzalisha hilo zao na hatimaye nchi kupata faida kubwa au uchumi wetu kuweza kukua kwa kuwa viwanda vimewekwa kwenye maeneo ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunapoweka viwanda kwenye maeneo ya uzalishaji tunawasaidia wakulima wetu kuweza kupata faida katika kilimo. Ilivyo sasa hivi wanaofaidika sio wakulima, wanaofaidika ni wale middlemen, wale watu wanaonunua mazao toka kwa wakulima na kwenda kuwauzia watu watu wenye viwanda.
Kwa hiyo, haiwasaidii wakulima kama tutawekeza viwanda vyetu mbali na kule wanakozalisha. Kwa hiyo, tuweke jirani na eneo la uzalishaji ili wakulima wetu waweze kuuza mazao yao na kupata faida na hatimaye Taifa lipate faida kupitia viwanda na ajira hizi ambazo tumewekeza kupitia viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijaribu kuongelea suala la kodi. Mara nyingi kumekuwa na kodi nyingi sana kwenye mazao, hasa mazao ya biashara. Kwenye zao la chai, kahawa, tumbaku na pamba, kuna kodi nyingi au kuna utitiri wa kodi. Utakuta kodi za mazao haya hufika mpaka 20 nyingine mpaka 25 au 27. Sasa mwisho wa siku anayekuja kulipa hizi kodi zote ni mkulima. Kwa hiyo, utakuta kupitia hizi kodi, tunamnyonya huyu mkulima ambaye kwanza anapata shida sana kuzalisha hili zao na soko lake halina uhakika; sehemu ya kuuzia kwenye kiwanda, hakina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku anauza zao lake; anauza chai yake, kahawa, pamba au tumbaku yake kwa bei ya chini kwa sababu ya kuwa na kodi nyingi. Kwa hiyo, tunapofikiria viwanda au uzalishaji ni lazima tufikirie pia na hizi kodi, tujaribu kuzipunguza ili angalau mkulima aweze kupata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu wawekezaji wazawa. Mara nyingi tumekuwa tukiwavutia wawekezaji wa nje tunawasahau wazawa. Tunasahau kuwahamasisha wananchi wale wanaotaka kujiunga kwenye vikundi vidogo vidogo na kuanzisha viwanda au kuna maeneo mengine tayari kuna wakulima ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo na kwenye viwanda, ni vizuri Serikali tuwe na utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawawezesha kwa kuwapa mikopo au kwa kuwasaidia kuweza kupata mikopo rahisi na kuweza kuwekeza kwenye viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu kuna mkulima mmoja anataka kuwekeza kwenye kiwanda cha chai, kwenye processing industries, lakini anashindwa kupata utaratibu gani mzuri ili aweze kupata mkopo na hatimaye aweze kufungua kiwanda cha chai. Kwa hiyo, naomba tunapofikiria uwekezaji, tuwafikirie sana Watanzania wenzetu ambao wanataka kuwekeza kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wangu wa viwanda ajaribu kuhamasisha au kututafutia wawekezaji wengi kwenye mazao ya chai. Kule Lupembe tuna viwanda viwili tu na vile viwanda haviwezi kutosha, havikidhi mahitaji ya chai ya Lupembe. Lupembe tunazalisha chai nyingi na vile viwanda viwili haviwezi ku-process ile chai yote, matokeo yake chai nyingi zinamwagwa na wananchi wanapata hasara kubwa sana. Kwa hiyo, naomba, kama kutakuwa na mwekezaji wa kiwanda cha chai, tunaomba aje awekeze Lupembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye matunda, nanasi na…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mawaziri; nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayofanya, anavyojituma kufanya kazi kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata hii huduma ya afya vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Naibu Waziri wake, naye ni jembe, anafanya kazi vizuri sana, tunaomba mwendelee hivyo hivyo, katika kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma ya afya hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia yangu machache niseme kidogo juu ya huduma ya afya hasa kwenye maeneo ya vijijini. Nafikiri wote tunatambua kwamba Watanzania wengi wanaishi vijijini na ndiko huko Watanzania hawa wanapata matatizo makubwa sana ya huduma za afya. Kwa hiyo, tunapotaka kuboresha ni lazima tuwafikie hasa Watanzania walio wengi wanaoishi maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera yetu imekaa vizuri kwamba kila kwenye kijiji tuwe na Zzhanati na kila kwenye Kkta lazima pawe na kituo cha afya na angalau kwenye Halmashauri kuwe na huduma ya hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niende kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 45, lakini zaidi ya asilimia 70 kuna zahanati. Tukija kwenye vituo vya afya, tuna viwili tu. Kimoja kipo Lupembe, kilometa takriban 80 kutoka Njombe Mjini au toka kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo ipo Halmashauri ya Mji na kingine kipo maeneo ya Kichiwa karibu kilometa 50 toka mjini. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi gani wananchi wa maeneo haya wanavyopata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa kwangu kule, kuna baadhi ya watu wanatembea zaidi ya kilomita 47 ili kupata huduma ya zahanati. Mgonjwa anatembea kilomita saba ili aweze kupata angalau huduma ya zahanati. Akikosa hapo anatembea umbali mwingine zaidi ya kilomita 25; angalau kukutana na kituo cha afya, halafu akitoka hapo akishindwa kupata huduma, anatakiwa kutembea takriban umbali wa kilomita 80 kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba kwenye Jimbo langu hakuna Hospitali ya Wilaya wala ya Serikali hata tu zile za binafsi, hazipo. Kwa hiyo, tuombe Wizara katika mipango yenu ya uboreshaji, angalau muwafikirie wananchi hao walio wengi wanaoishi vijijini. Hasa sehemu kubwa wanaoathirika hapa ni akinamama na akinamama wajawazito. Kule kwangu kwa sababu ya ubovu wa njia, hospitali kuwa mbali na vituo vya afya kuwa mbali, wengi wao wamekuwa wakijifungulia njiani, wakipoteza maisha wakiwa njiani kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupata huduma ya upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika mipango ya Wizara pia kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI angalau tuhakikishe kwamba vituo vya afya vilivyoko vijijini, viwe na huduma ya upasuaji ili tuweze kuokoa maisha ya akinamama wengi wa Tanzania wanaopoteza maisha yao wakati wanapotimiza haki yao ya msingi ya kuongeza watu hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama walivyosema wenzangu juu ya huduma ya CHF (Community Health Fund), inawasaidia wananchi wengi hasa wa vijijini na wengi wao wanaifurahia huduma hii. Lipo tatizo moja, kwamba wakishakatiwa hii CHF, haitumiki kwenye kata nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ziweze kuunganishwa na Hospitali za Wilaya. Wakishakatiwa hii CHF basi waweze kuitumia hata kwenye Hospitali ya Wilaya au kwenye hospitali iliyo katika kata nyingine, ili kama anakosa matibabu, huduma au dawa hazipo kwenye hospitali ya Serikali au kwenye Kituo cha Afya cha Serikali, basi aweze angalau kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya na akapata matibabu; kuliko ilivyo sasa hivi, wagonjwa hawa au wananchi wetu wakikosa kwenye kituo cha afya pale hawezi kwenda sehemu nyingine akatumia CHF. Kwa kuwa tumesema kwamba sasa matibabu yatakuwa yanatumika pia na TEHAMA, kwa kuwa jina litakuwa lipo kwenye database basi aweze kutibiwa sehemu nyingine kwa kutumia hii huduma ya CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo juu ya matibabu kwa wazee kama walivyoongelea wenzangu. Wazee wetu wanapata shida na tumesema kwenye ilani kwamba sasa tutaboresha huduma hasa kuhakikisha kwamba wazee wetu walio na umri unaozidi miaka 60 waweze kutibiwa bure. Bado kuna changamoto kubwa, kwa kuwa hospitali nyingi au zahanati na vituo vya afya vingi havina dawa za kutosha, hawa wazee wetu wamekuwa wakikosa matibabu. Tukumbuke kwamba wazee wetu hawa hawana uwezo wa kuzalisha, kwa hiyo, hawana uchumi mzuri, hawana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba ni vizuri sasa badala ya kuwapa CHF, wapewe Bima ya Afya. Kwa kuwa ni wachache, basi Serikali ione umuhimu ya kuwapangia bajeti maalum wazee wote waliofikisha miaka 60 na wakapewa Bima ya Afya ili waweze kwenda kutibiwa kwenye hospitali zozote zilizoko hapa nchini kama ilivyo kwa wanufaika wengine wa Bima za Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine juu ya miundombinu. Hospitali zetu na vituo vya afya vingi miundombinu yake bado siyo mizuri kwa maana ya huduma kama vile za umeme na maji. Utakwenda hospitali nyingi, utakuta zimejengwa vizuri, au kituo kimejengwa vizuri lakini hakuna maji. Naomba katika sera, katika mpango kwamba kila panapojengwa kituo cha afya au hospitali na maji pia yaweze kupelekwa katika maeneo hayo ili kuwepo na huduma bora. Wagonjwa wanaokwenda kwenye vituo hivi vya afya au hospitali basi wapate na huduma ya maji safi, kuliko ilivyo hivi sasa ambapo utakuta kuna hospitali nzuri, lakini inapofika kwenye huduma ya maji, haipo. Kwa hiyo, wanachota sehemu nyingine mtoni. Sasa hii ni hatari kwa mgonjwa kama kutakuwa na hospitali ambayo haina maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni umeme. Tumeona kwenye hospitali nyingi sana hasa zilizoko vijijini, hazina hata umeme! Tupeleke umeme! Kama siyo kupeleka umeme ule wa REA basi tuwe na mipango ya kupeleka umeme wa solar, unaweza ukasaidia. Kwa hiyo, kila tunapojenga hospitali au tunapopeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ni lazima tufikirie pia na umeme, tuanze kufikiria na power itakayotumika kwenye kijiji, kituo cha afya au hospitali, ili wananchi waweze kupata umeme kwenye hizi hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho niseme kama walivyosema wenzangu juu ya unyanyasaji wa kijinsia. Tunaomba tuweke mipango rasmi kabisa ya kuhakikisha kwamba unyanyasaji wa kijinsia nchini kwetu unatokomezwa. Mpaka sasa hivi kuna maeneo mengine, akinamama ambao wamefiwa na waume zao, wanalazimishwa kwenda kuolewa na wadogo wa wenzi wao waliofariki. Bado kuna maeneo mengine wanalazimishwa kugawanya mali. Maana ndugu wanachukua mali za huyu marehemu aliyefariki, eti kwa sababu ya kulelea familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tujaribu kujitahidi kuhakikisha kwamba akinamama wanaopoteza wenzi wao wajane hawa, wanatetewa na mali zao zinabaki kwa ajili ya kuendelea kuhudumia familia zao kuliko ilivyo sasa hivi kwa baadhi ya maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumbua wote wabadhirifu na mabaradhuli wote wanaoharibu uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya pekee niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa wanazofanya hasa za kuhakikisha kwamba uchumi wan chi hii unakua. Lakini nimpongeze pia Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo na Naibu wake Waziri kwa kazi kubwa wanayofanya kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na hatimaye tuweze kuwa na viwanda vya kutosha na shughuli nyingine za uchumi ziweze kuboreshwa kupitia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nimpongeze tena Mheshimiwa Waziri, nirudie, kwa kuhakikisha kwamba Jimbo langu la Lupembe pia linapata umeme. Nashukuru katika wiki hii vijiji viwili vimeweza navyo kupata mwanga wa umeme kwa mara ya kwanza kati ya vijiji 45; kwa hiyo, bado vijiji 33 havina umeme kati ya vijiji 45. Niombe Mheshimiwa Waziri na vile vijiji 33 vilivyobakia tuendelee kuvipigania ili viwe na umeme nao wajisikie wapo nchini Tanzania kama Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba maendeleo ni umeme. Uwepo wa umeme kwa maana ya nishati ya kutosha ya umeme na nishati yenye uhakika, lakini pia yenye bei nafuu ndipo tutaweza kuwa na maendeleo, lakini kama nishati itakuwa bado bei yake ipo juu wananchi wengi hawawezi ku-afford kuipata bado hatutaweza kuhakikisha kwamba tunaenda kwenye uchumi ambao tunauhitaji.
Niseme kwanza nipongeze kwa kupunguza bei, na umeme toka 1.5% mpaka 2.4%, lakini pia nipongeze kwa kutoa tozo la maombi ya uunganishaji wa umeme ambayo ni application fee shilingi 5,000; lakini pia nipongeze kwa kutoa service charge, hii ilikuwa inawakwaza wananchi wengi sana. Na nipongeze kwa niaba ya wananchi wangu wa Lupembe kwa kupunguza hii kodi maana wananchi kipato cha chini, wataweza kuingiza umeme kwa kutumia tu angalau shilingi 5,000 wanaweza wakapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia kuhusu mradi wa REA. Katika eneo langu na katika Jimbo langu mradi wa REA Phase I hatukupata, lakini tukapata mradi wa REA Phase II, lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kupata umeme hata kijiji kimoja katika REA II. Basi tunaomba vijiji vyote hivi viingizwe kwenye REA III kwa maana ya vijiji vyote 33, tunaomba mtusaidie kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kuna Shirika ambalo linafanya kazi kule kwa ushirikiano wa Serikali, Shirika la CEFA ambalo limeingiza vijiji viwili, sasa tatizo bado ni kadri ya mkataba ile asilimia ambayo Serikali ilitakiwa ichangie naomba tujitahidi tuweze kuwapatia lile Shirika ili liweze kuendelea na kuhakikisha kwamba linasambaza umeme kwenye vijiji vingine ambavyo tayari nguzo zimechomekwa lakini bado nyaya hazijafungwa na hawajazambaza umeme, kwa hiyo niombe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niombe kupitia ile mradi ambao wa kwanza ulikuwa TANESCO, ile Gridi ya Taifa iliyowenda mpaka vijiji vile vya Lupembe na Igombora, basi kuna baadhi ya vijiji vilirukwa haukushushwa umeme, umeme umekatiza tu umepita katikati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mara nyingi wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba umeme umepita kwenye vijiji vyao, lakini vijiji hivyo havina umeme au vitongoji mbalimbali ambavyo umeme umepita juu haujashushwa. Tuombe tunapopeleka umeme kwenye maeneo hayo au kwenye maeneo mengine tuhakikishe kwamba yale maeneo ambako umeme unapita basi wananufaika na nishati ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia bei ya umeme ilivyo sasa hivi pamoja na kwamba tumepunguza kutoka kwenye asilimia 1.5 mpaka 2.4 bado bei hizi ziko juu. Kuna baadhi ya wananchi wengi wanashindwa kulipia gharama hizi, tuangalie uwezekano wa kupunguza gharama za umeme angalau zishuke kabisa kutoka kwenye ile asilimia ziende chini kidogo ili wananchi wengi wa kipato cha chini waweze kununua na kutumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, tunasema mazingira yanaharibika kwa kutafuta mkaa, wananchi wanatumia mkaa walio wengi lakini pia wanatumia kuni katika kupata nishati. Tukishusha bei ya umeme ukawa wa gharama ndogo au ukawa gharama ambayo wananchi wa kipato cha chini wanaweza wakaununua basi yale madhara ya misitu kwa maana ya kutafuta nishati ya mkaa na kupata kuni yatapungua. Wengi wao watahamia kwenye umeme kwa kuwa umeme utakuwa una bei ndogo, utakuwa wa bei rahisi na wataweza kununua umeme na kwa upande mwingine tutakauwa tunapunguza madhara ya kupotea kwa misitu, tutakuwa tunapunguza uharibifu wa mazingira kupitia kutumia hizi nishati za mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tujitahidi tuweze kuhakikisha kwamba umeme unapungua uwe na bei ndogo ili tuweze kuokoa mazingira yetu na misitu yetu ambayo kila siku tani za miti zinakatwa kwa ajili ya kupata nishati hii ya kupikia kwa maana ya mkaa na kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba huduma ya umeme hii lazima tufikirie kuisambaza hasa kwenye maeneo yenye taasisi kama vile shule, maeneo ya Hospitali,na maeneo ya huduma muhimu za binadamu. Kwa hiyo lazima tufikire hilo pia tunasema kwamba tunataka shule zetu ziwe na E-schools, tuwe na E-learning ni lazima tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na umeme ili mipango ya kuwa na E-learning, E-schools kwenye shule zetu uweze kukamilika. Kwa hiyo, tunaomba tupeleke pia kwenye huduma hizi za kielimu na huduma nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naona kuna Waheshimiwa Wabunge wengi wamelalamika sana juu ya kuweka vinasaba kwenye nishati ya mafuta. Kwanza lazima tujiulize sababu zipi zilizosababisha Serikali iweze kuhakikisha kwamba inaweka vinasaba. Ni kutokana na kwamba kulikuwa na uchakachuaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa, magari yamekuwa yakiharibika, pampu za magari zikiharibika mara kwa mara na baada ya sisi wananchi kulalamika na Wabunge tukaja tukaa na tukajadili, tukaamua kwamba tupitishe sheria ya vinasaba. Kwa hiyo, vinasaba hivi ni muhimu, naomba Waziri na Baraza zima la Mawaziri viendelee, kama kuna matatizo madogo madogo basi yafanyiwe uchunguzi tuweze kuyatatua lakini sio kusimamisha hili suala la vinasaba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeona faida zake, udhibiti wa uchakachuzi wa mafuta umepungua lakini pia Serikali imekuwa inapoteza mapato mengi sana hasa kwenye mafuta yale yaliyopo on transit kama walivyosema wenzangu. Kwa hiyo, kwa kuweka vinasaba tunaweza tukabaini kwamba haya mafuta yamepitiwa na vinasaba, watu wanaokagua vinasaba na haya mafuta hayajapitiwa. Kwa hiyo, kwa kwa kufanya hivyo tutadhibiti upotevu wa kipato cha Serikali na hivyo Serikali itaweza kupata pato lake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hasara kubwa kama nilivyosema ya haya mafuta kulikuwa na wizi mkubwa sana wa mafuta ambayo yanakuwa kwenye on transit, kulikuwa na wizi mkubwa sana wa mafuta yaliyopo kwenye migodi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo maana yake tutapunguza madhara ya wizi wa mafuta ambao ulikuwa unapelekea hasara kubwa hasa wenye migodi wenyewe, lakini kwa upande mwingine ulikuwa unapelekea hasara Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana kwa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi na Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika kutatua migogoro. Ni kweli migogoro imepungua sana ukilinganisha na siku za nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze na jambo moja hasa kuhusu property tax (kodi za majengo). Kodi hizi ni kubwa mno ukilinganisha na kipato cha wananchi hasa wastaafu na wale wenye kipato cha chini, inakuwa vigumu sana kwao kuilipa. Kwa mfano, mfanyakazi ambaye amestaafu alikuwa anapata kima cha chini amejenga nyumba yake yenye thamani ya shilingi milioni 40, anatakiwa kulipia kodi Sh. 46,000 kwa mwaka na ukigawa kwa mwezi ni kama Sh. 3,840 hivi, kodi hii ni kubwa. Kwa hiyo, tuombe Serikali ijaribu kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hizi za majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Sheria ile ya Ardhi hasa inayosema juu ya vyanzo vya maji kwamba mwananchi haruhusiwi kujenga mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji au kwenye kingo za mto. Hii sheria kwenye maeneo mengine hasa ya nyanda za juu (highlands) haitusaidii sana au inawaathiri sana wananchi. Kwa mfano, utakuta kuna milima midogo na kutoka mlima mmoja mpaka mwingine au kutoka bonde mpaka bonde, ukipima kutoka kwenye kingo za maji mpaka unapoishia mlima utakuta unafika kwenye mlima pale katikati kwenye kigongo cha mlima. Kwa hiyo, maana yake hilo eneo utakuta milima miwili au mitatu hawaruhusiwi wananchi kujenga maeneo hayo kwa sababu ya sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Sheria hii ya Ardhi iwe applicable kwenye baadhi ya maeneo lakini kwenye maeneo ya milimani angalau waweze kupunguziwa zile mita 60 ziende kwenye mita 30 au 20 hivi ili wananchi nao waweze kujenga kwenye maeneo hayo vizuri zaidi kama ilivyo katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia jambo lingine ni migogoro hii ya mipaka. Kwangu kule kuna migogoro hasa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Halmashauri ya Jimbo la Mlimba. Naomba ule mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa maana ya Jimbo la Lupembe na Jimbo la Mlimba uweze kutatuliwa haraka ili tuendelee kufanya shughuli za kimaendeleo. Kwa sababu ukiwauliza watu wa Njombe wanasema mpaka wao unaenda mpaka kwenye mto, lakini watu wa Mlimba nao wanasema hapana siyo mto ni ndani zaidi ya Njombe. Kwa hiyo, bado ule mgogoro unatuathiri sana katika maendeleo kwa hiyo tunaomba muutatue ili tuweze kujua mpaka halisi upo sehemu gani maana umedumu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hizi nyumba za National Housing, bei yake ni kubwa mno. Lengo la nyumba za National Housing tukimrejea Mwalimu Nyerere alikuwa na lengo la kuwasaidia watu maskini na wafanyakazi na watu wenye kipato cha chini. Sasa hivi zile nyumba mwananchi wa kawaida au mfanyakazi wa kima cha chini hawezi kununua, nyumba ya vyumba viwili kwa shilingi milioni 70, kwa kweli hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe wajaribu kurekebisha baadhi ya taratibu, inawezekana pengine ni Sheria ya Manunuzi ndiyo inayopandisha bei, basi tuirekebishe ili wananchi hata wale wa kipato kidogo waweze kunufaika. Ilivyo sasa hivi hizi nyumba za National Housing na hata zile zinazojengwa na NSSF sehemu kubwa wanaoweza kununua ni watu wenye kipato kikubwa, ni matajiri na wafanyakazi wenye kipato kikubwa ndiyo wanaoweza kumudu kununua nyumba hizi tofauti na lile lengo hasa la msingi la kujenga hizi nyumba kwa ajili ya watu wa kipato cha chini. Otherwise hawa watu wenye kipato cha chini wataendelea kuwa wapangaji na hawataweza kumiliki nyumba zao kwa sababu bei ya nyumba hizi ipo juu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Idara ya Ardhi kwenye Jimbo langu la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, hatuna Afisa Ardhi Mteule. Kwa hiyo, kunapotokea migogoro ya ardhi tunashindwa kuitatua wakati mwingine inabidi twende kwa wenzetu wa Halmashauri ya Mji waweze kutusaidia kwenye baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, tuombe Halmashauri zote ambazo hazina Maafisa Ardhi Wateule basi waajiriwe ili tuweze kutatua migogoro ya ardhi na mipaka ambayo inajitokeza huko kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme jambo moja juu ya ucheleweshwaji wa hati miliki, inachukua muda mrefu sana kupata hati miliki ya ardhi au ya viwanja. Tunaomba basi kwa kuwa sasa hivi ni ulimwengu au ni wakati wa sayansi na teknolojia, basi ziwe printed haraka ili zisiwe zinachukua muda mrefu sana ili wananchi waweze kunufanika na hili suala la kupata hati miliki kwa maana ya mashamba madogo na makubwa na viwanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu wananchi walishapimiwa ardhi ili kupata hati miliki za mashamba ya chai, lakini imechukua muda mrefu sana na ukiuliza sababu wanasema hatuna Afisa Ardhi Mteule ambaye anaweza akasaini hati hizo. Sasa hivi baada ya kumwona Afisa Ardhi wa Mji ndiye anatusaidia angalau ku-process zile hati miliki ili kuwawezesha wananchi wangu wa Lupembe kupata hati zao kwa ajili ya mashamba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa nafasi hii, naunga tena mkono kwa mara ya pili kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo kwenye hii bajeti ya mapato na matumizi. Nianze kuanza kwa kukushukuru wewe binafsi na kukupongeza kwa kuendelea kukalia hicho Kiti, usiwe na wasiwasi wewe tulia kama jina lako linavyosema, sisi tuko pamoja na wewe kuhakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Bajeti yao iliyoletwa inaonyesha weledi na umahiri mkubwa wa kazi ambayo wamepewa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, inaonyesha kazi hii wanaweza wakaimudu vizuri na watatusaidia kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kidogo kwenye upande wa huduma ya maji. Tumesikia Wabunge wengi wamesema sana hapa kuhusu suala la maji na wametoa mapendekezo mengi sana, tunaomba jambo hili tulitilie mkazo sana na tulifanyie kazi. Wabunge wapendekeza kwamba tuwe na tozo ya Sh.50 ili kwenye shilingi bilioni 125 basi ziongezeke zifikie shilingi bilioni 250 ili wananchi wetu wengi ambao wanaishi huko vijijini waweze kupata maji, tatizo liko wapi? Kama sisi ndiyo tunaopanga na tunawashauri kwa nini tusiongeze hizi Sh.50 kwa lita ya mafuta ili wananchi wengi wanaoishi vijijini waweze kupata maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijijini kule sasa hivi tunawahamasisha wajenge vyoo vya kisasa lakini vijiji vingi havina maji. Hata ukiangalia kwenye bajeti ya maji, miradi mingi ya maji mikubwa mikubwa imeelekezwa mijini na hata fedha iliyotengwa kwa maana ya maji vijijini bado zinaelekezwa mijini. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majumuisho tunataka kujua ni nini amefanya hasa kuhakikisha tozo ya Sh.50 kwa kila lita moja ya mafuta inaongezeka na kuwa Sh.100 na hatimaye tuweze kuongeza usambazaji wa maji vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo kwenye kilimo, niipongeze Serikali kwa kuondoa kodi hasa kwenye mazao ya matunda na mboga mboga kwa maana ya mazao yale ambayo hayajafanyiwa processing, niwapongeze sana. Pia niipongeze Serikali kwa kupunguza kodi kwa baadhi ya mazao ya biashara kama vile chai, kahawa, korosho na mazao mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba pamoja na kupunguza kodi kidogo bado tusipokuwa makini tutafanya Watanzania wabaki kwa kutokuwa na uwezo wa kulima kwa kiasi kikubwa na kuweza kuzalisha kiasi ambacho kitatutosha kulisha hivi viwanda vyetu ambavyo tunaanza. Ni lazima tuhakikishe kwamba hawa wananchi wanawezeshwa ili kuzalisha kwa kiasi cha kutosha, kingi zaidi na kuzalisha matunda ambayo yanakuwa ni bora ili yaweze kupata soko, waweze kupata kuuza kwenye hivi viwanda ambavyo tunatarajia vitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutawezaje kufanya hivyo? Ni lazima tuwawezeshe kwa kuwapelekea Maafisa Ugani. Vijiji vingi sasa hivi havina Maafisa Ugani, wananchi wanalima kilimo kile kile cha utamaduni bila kuzingatia kanuni bora za kilimo. Kwa hiyo, tuombe Wizara husika kwa pamoja tupeleke Maafisa Ugani wa kutosha ili waboreshe kilimo vijijini na hatimaye waweze kupata faida kwenye mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nijaribu kuchangia kwenye upande wa elimu. Ni kweli Serikali imepeleka fedha nyingi, tumeona ina mpango wa kupeleka trilioni 4.77 ambayo ni sawasawa na asilimia 22.1. Fedha hizi ili ziweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa. Ni muhimu sana hizi fedha zipelekwe kwenye maeneo haya ya shule kwa wakati. La sivyo fedha hizi hazitafanya yale malengo ambayo yamekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejifunza miaka ya nyuma, fedha zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya kuendeshea mashule, lakini zinakwenda kwa kuchelewa, zinaenda miezi ya Tano na Sita; na inapofika tarehe 30 wale Wakurugenzi na Wakuu wa Shule wanatakiwa kurejesha hizi fedha tena Hazina, zinarudi tena bila kufanya kazi. Kwa hiyo, niombe mamlaka husika zipeleke hizi fedha kwa wakati ili zifanye kazi ambazo zimekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo pia kwenye suala la afya. Ni kweli, nitoe pongezi kwa Serikali, tumetenga trilioni 1.99 ambayo ni sawasawa na asilimia 9.2 ya bajeti nzima na hizo fedha tumesema zinaenda kwa ajili ya vifaa tiba, vitendanishi (reagents) na miundombinu, kwa hiyo, tuombe hizi fedha ziende kwenye vituo vya afya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi wanategemea sana hivi vituo vya afya, kwa hiyo ni muhimu sana kuviboresha ili kuhakikisha kwamba angalau vituo vyote vya afya vinatoa huduma ya upasuaji pamoja na huduma kwa akinamama. Tunasema wanawake na watoto wengi wanafariki, ni kwa sababu huduma za afya hasa vijijini hazijaboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia statistics wanaokufa wengi ni wale watu wa vijijini, ni kwa sababu wanakwenda hospitalini kwanza kwa kuchelewa kutokana na kutembea umbali mrefu, wakifika hakuna huduma nzuri, wanatakiwa wasafiri au wasafirishwe kwenda kwenye Hospitali za Wilaya ambazo zipo mbali. Wanafika huko wakiwa wamechelewa, hatimaye watoto wao wanafariki au wanapata operation na mwisho wa siku wanapata matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisemee kidogo kuhusu hii sheria ya magari, kwa maana ya kodi ya usafiri na uhamisho wa umiliki, ambayo ipo Sura namba 124, hasa kwenye upande wa pikipiki. Katika Ilani yetu tulisema tunataka hawa bodaboda sasa kwa hizi kazi wanazozifanya za kusafirisha, ziwe ni kazi rasmi. Nilitegemea kwamba leo hii tungekuwa tunaongelea kupunguza kodi za pikipiki, kwa kuwa hizi pikipiki nyingi wanazozitumia ni zile ambazo wamekodishwa na matajiri. Sasa tunataka hawa waendesha bodaboda waendelee kubaki maskini? Waendelee kuwasaidia watu wengine wenye fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba hili ongezeko la kodi kutoka sh. 45/= mpaka 95/= liondolewe ibaki ile ile na ikiwezekana ipunguzwe zaidi ili vijana wetu ambao huko nyuma walikuwa wanafanya kazi za wizi, utapeli na kupiga watu nondo wajiajiri kwenye uendeshaji wa boda boda. Kwa kuwa boda boda zimesaidia kutafuta ajira kwa hawa vijana wetu, basi tupunguze kodi za pikipiki ili nao waweze kununua pikipiki na hatimaye wakapata fedha kwa ajili ya kuendeshea familia zao na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamesema pia juu ya kodi ya mitumba. Hakuna mtu ambaye hatambui, wote hapa ni Watanzania na wengi wetu tunatoka vijijini, wananchi wengi wanaoishi vijijini ndizo nguo wanazozitegemea. Mwananchi wa kijijini hutegemei akaenda kununua nguo dukani, anategemea mwisho wa mwezi aende kwenye mitumba apate nguo za kuweza kujisitiri, sasa sisi tunaongeza kodi. Ni vizuri tufanye kwanza utafiti, au wakati huu ambao tunataka kupeleka viwanda vya uzalishaji wa nguo basi kodi ziwe za chini, ili wananchi wengi waishio vijijini waweze kumudu kununua nguo. La sivyo wananchi wetu vijijini watashindwa kununua hata nguo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa uamuzi wa kutoa elimu bure toka shule ya msingi mpaka kidato cha nne. Hii imesaidia kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Ufaulu wa watahiniwa wa darasa la saba na wale wa kidato cha sita unaendelea kupanda wakati ngazi ya chini, yaani sekondari, umeshuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hapa ni Walimu. Walimu wa masomo ya sayansi ni wachache sana. Kuna baadhi ya shule hazina kabisa Walimu wa masomo ya Hisabati, Fizikia, Biolojia na Kemia. Shule ambazo hazina Walimu wa masomo haya bado ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne ni mbaya sana. Hivyo, ni muhimu katika mipango ya Serikali tuwekeze vya kutosha katika kuzalisha Walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nyumba za Walimu katika shule nyingi zimekuwa chache sana. Walimu wengi bado wanakaa mbali na shule, kuna baadhi wanatembea umbali wa kilometa tano mpaka saba kwenda shuleni, hasa maeneo ya vijijini; hivyo, hufika shuleni wakiwa wamechoka na wakati mwingine kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwasaidia wanafunzi. Serikali iweke utaratibu madhubuti wa kujenga nyumba za Walimu, hasa kwa shule zilizopo vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa hatua inayochukua ya kuanzisha Vyuo vya Ufundi (VETA) kwenye baadhi ya maeneo. Kwa kuwa, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, hasa viwanda vya kati, tuhitaji zaidi mafundi mchundo ambao ndio watafanya kwenye viwanda hivi. Hivyo ni muhimu kuweka utaratibu wa kujenga vyuo hivi kwa kila Wilaya. Kuendelea kuongeza Vyuo Vikuu haitusaidii sana kutatua tatizo la ajira na nguvukazi, kwani wahitimu wa Vyuo Vikuu ni Maafisa ambao wanatarajiwa kwenda kusimamia kazi katika sekta mbalimbali. Je, ni nani atafanya kazi katika viwanda hivi kama hatuna watu hawa wenye elimu ya kati?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali katika kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, bado vijana wengi wamekuwa wakikosa mikopo hiyo. Vijana wengi, hususan watoto wa maskini wanaotokea vijijini ndio ambao wamekuwa wakikosa mikopo. Serikali ipitie upya vigezo vinavyotumika katika utoaji wa mikopo. Vigezo hivyo viwe wazi na ikiwezekana Wakuu wa Shule za Sekondari wapewe hayo maelekezo ya jinsi Bodi ya Mikopo inavyotoa tathmini ya kukopesha wanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwe na utaratibu wa kufanya projection/forecast mapema ili kujipanga na kujua mahitaji ya kiasi cha fedha kitakachohitajika kwa mwaka husika ili tuingize kwenye bajeti ya Serikali. Hii inaweza kufanyika kwa kujua ni vijana wangapi watahitimu kidato cha sita kwa mwaka huo wa fedha? Tunatarajia watafaulu wangapi? Hii itatusaidia kupunguza baadhi usumbufu na matatizo yanayowapata kwa kukosa mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naipongeza Serikali kwa kuweka mpango wa kuendeleza utafiti katika kilimo kwa mazao mbalimbali. Serikali sasa ijikite kwenye utafiti wa masoko ya mazao haya. Wakulima wetu, hususan vijijini, wamekuwa wakijituma katika kuzalisha mazao mbalimbali. Tatizo kubwa limekuwa ni kupata soko la mazao hayo. Kuna baadhi ya maeneo, mfano, Lupembe; mazao ya matunda kama vile nanasi, maembe, parachichi, yamekuwa yakiozea shambani kwa kukosa soko la uhakika. Pia, barabara mbovu au zisizopitika wakati wa kifuku zimekuwa zikiathiri soko la mazao haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali ikaweka utaratibu wa kutengeneza barabara zinazoenda kwenye maeneo ya uzalishaji ili kuokoa mamilioni ya fedha yanayopotea au hasara wanayopata wakulima kutokana na ubovu wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nampongeza Waziri wa Fedha na Watendaji waliopo chini ya Wizara hii kwa kuunda mpango huu. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa maana ya Rais mwenyewe, Baraza la Mawaziri na watendaji wote wa Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuiweka nchi yetu vizuri ili watu wakae sawa na mwisho wa siku wananchi wapate usawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wenzangu, nianze kuipongeza Kamati yangu kwani nami nipo kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, kwa kazi kubwa ambazo tumezifanya kwa ushirikiano wa pamoja. Pamoja na pongezi hizo, kama walivyosema wenzangu, changamoto za Kamati zipo na zimetusababishia pengine tusiweze kutekeleza majukumu yetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa ambayo tumekumbana nayo ni Kamati kutokuwa na fedha za kutosha hasa fedha kwa ajili ya ziara. Kama walivyosema wenzangu, kiasi kilichotengwa ni kidogo mno hivyo kimetusababishia kukwamishwa katika kutekeleza majukumu yetu. Kamati inapopewa fedha ya ziara inaiwezesha kwenda kujifunza juu ya majukumu yake. Kwa hiyo, Kamati inapokuwa haipati fedha za kutosha inashindwa kutekeleza majukumu yake vizuri ya kuisaidia na kuisimamia Serikali.
Mheshimwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika bajeti zinazokuja tuombe Serikali iweze kutoa fedha za kutosha tukizingatia kwamba Kamati ya Katiba na Sheria ni Kamati ambayo inasaidia wananchi wake kupata haki. Kwa hiyo, tusipojifunza kwa nchi nyingine au kwa wengine wanafanyaje shughuli zao inakuwa ni vigumu kutunga sheria ambayo itakuwa inatenda haki. Kwa hiyo, tuombe awamu inayokuja angalau Kamati zipate fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake hasa ya kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ziara zinatuwezesha sisi Wabunge kuweza kujua fedha zilizopelekwa kwenye taasisi mbalimbali kama zimefanya kazi ile ambayo imekusudiwa. Kwa hiyo, inatusaidia kujua value for money. Sasa Kamati inaposhindwa kwenda kwenye eneo husika kwa maana ya site na inapewa taarifa kwenye makaratasi tu lakini haiwezi kuona kitu kilichotendeka kwa uhalisia basi ile value for money hatuwezi kuiona vizuri. Kwa hiyo, niiombe Serikali yetu katika bajeti inayokuja ijitahidi kuhakikisha kwamba inatoa fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya ziara ili Wabunge waweze kwenda ziara na kukagua miradi mbalimbali ambayo tumeitengea fedha ili kuona ilivyotekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linahusu OC kwenye Halmashauri zetu. Halmashauri zimekuwa hazipelekewi fedha za kutosha kwa maana ya OC na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake. Kwa mfano, Kitengo cha Ukaguzi, siku hizi tunasema Udhibiti Ubora wa Elimu. Kitengo hiki kimeshindwa kufanya kazi yake kabisa, shule nyingi zimeshindwa kufikiwa na wameshindwa kwenda kukagua kutokana na kukosa fedha hasa kwa ajili ya mafuta ya kuendea kwenye maeneo hayo. Hii ni hatari kama tunakuwa na shule ambazo hazikaguliwi. Kuna shule nyingine utakuta miaka mitatu au mitano imepita hazijakaguliwa. Labda ukaguzi unaofanyika ni ukaguzi ule wa muda mfupi wa kuangalia mambo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji shule zetu ziweze kukaguliwa, Walimu waweze kupitiwa ili wakaguzi waweze kuwashauri juu ya mbinu za kujifunzia na kufundishia. Tusipofanya hivyo, itakuwa ni vigumu kuwaweka Walimu katika wakati wa kisasa na kuweza kuenenda kadri inavyopaswa kufundisha kulingana na syllabus na mambo ya taaluma yanavyobadilika. Kwa hiyo, ni muhimu hizi Halmashauri zipewe OC za kutosha ili taasisi zote zinazosimamiwa na Halmashauri kwa maana ya Ukaguzi na sekta nyingine ziweze kutekeleza majukumu yake vizuri na hatimaye tutaweza kupata elimu bora na tutaweza kuwa na watendaji wazuri kwa kuwa wana OC ambazo zitawawezesha kwenda kutekeleza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nipongeze (kama walivyopongeza wenzangu) juu ya Mfuko wa TASAF, TASAF amekuwa mkombozi wa wanyonge. Huko vijijini sisi Wabunge tunaopita huko tumeona jinsi maisha ya watu yanavyobadilika na kuna maeneo mengine tumeshahamasisha hao wananchi ambao walikuwa wana kipato cha chini waweze kuanzisha miradi midogo midogo ili waweze kujikimu katika maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali pindi itakapopata hela za kutosha iendelee kuongeza fedha za TASAF ili wananchi wengi maskini waweze kunufaika na fedha hizi kwa ajili ya kujikwamua katika maisha yao na hatimaye kuendelea kuanzisha miradi midogo midogo ambayo hiyo itawaondoa kutoka kwenye umaskini na hatimaye kuwa na hali nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye TASAF pia kuna tatizo limejitokeza kama wenzangu walivyosema, kuna baadhi ya wananchi walifanyiwa tathmini na wakaonekana kwamba wao ni kaya zile za hohe hahe (kaya maskini) na wakaingizwa kwenye mpango wa kupewa fedha lakini baadaye maafisa wetu wamepita na kusema kwamba hizo kaya hazina sifa za kuendelea kunufaika na mfuko wa TASAF. Baadhi ya kaya zilizo nyingi, kuna hizo kaya za wazee ambao hawana uwezo na kuna kaya nyingine wameondolewa kwenye mpango, uwezo wao ni mdogo, wanashindwa kusomesha watoto wao shule na hatimaye kuleta usumbufu na matatizo makubwa. Wengine wametoroka nyumba zao wakihofia kwamba watakamatwa na Serikali kwa kuwa maafisa waliokuwa wanaenda huko wanawatishia kwamba wasiporudisha hizo fedha basi watafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Watanzania wanaogopa kufungwa, kwa hiyo wamekuwa wakiacha nyumba wakikimbia kuogopa kushikwa na mkono wa sheria kwa maana ya kurudisha fedha hizi. Tuombe basi Serikali ijaribu kuliangalia jambo hili, kama kweli ni kaya maskini, naomba tujaribu kuwaachia waendelee kunufaika na fedha hizi ili hatimaye waweze kusaidia familia zao kuweza kupata mahitaji muhimu hasa mahitaji ya kujikimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya uhamisho wa watumishi wa Serikali. Tulikuwa na zoezi la uhakiki, natumaini kwamba Serikali sasa imeshahakiki watumishi, imeshajua nani ni mtumishi hewa, nani ni mtumishi ambaye hana sifa za kuendelea kufanya kazi katika Serikali. Sasa kwa kuwa uhakiki umekwisha basi turuhusu hao watumishi wetu waweze kupata uhamisho. Sasa hivi kuna Walimu wengi wanaomba uhamisho wanakataliwa, kuna watumishi wa sekta ya afya wanakataliwa uhamisho kwa kisingizio kwamba bado tunafanya uhakiki wa watumishi hewa. Tuombe Serikali iweze kufungua milango hasa ya uhamisho ili watumishi wetu waweze kuhama. Kwa sababu ilivyo sasa hivi tukiwaacha hawa watumishi waendelee kuishi huko walipopangiwa kazi wasipate uhamisho ni hatari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wameoa, kuna mabinti wameolewa wanataka kwenda kwa wenzao, lakini wanazuiwa kwa sababu ya kisingizio cha uhakiki wa watumishi. Kwa hiyo, tuombe kwa kuwa Serikali yetu ina mpango na inadhibiti maambukizi ya UKIMWI, tukiwaacha hawa vijana huko ambao wameoa na kuolewa baadaye tutakuta tumewapoteza kwa kujiingiza kwenye vitendo ambavyo vitawapelekea kupata UKIMWI kwa sababu ya kukaa na wenza wao mbali. Kwa hiyo, niombe Serikali yangu iweze kufungua milango ya uhamisho ili vijana wetu waweze kuhama na waweze kwenda waliko wenzi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie na wenzangu wamelizungumzia ni juu ya semina za viongozi. Semina hizi ni muhimu hasa kwa hawa wanaoteuliwa, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Kwa hiyo, tuombe wapewe semina za kutosha ili waweze kuongoza vizuri. Naamini kwamba wametoka kwenye kazi mbalimbali na kama walivyosema wenzangu kuna wengine hawaifahamu vizuri kazi ya Ukuu wa Wilaya na wengine Wakuu wa Idara, tuwape mafunzo ili waweze kusimamia vizuri majukumu yao na wasiwabughudhi watu. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna baadhi ya maeneo wamekuwa wakiwatishia wananchi na watumishi…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa namna ya pekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi anazofanya hasa za kuiongoza nchi yetu Tanzania. Niwashukuru Mawaziri wote kwa namna ya pekee nimshukuru Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya na Mheshimiwa Jenister Mhagama na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa wanazofanya usiku na mchana kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa walioifanya kwa kuimarisha viashiria vya kukua kwa uchumi, hasa kwenye upande wa ujenzi wa barabara. Lengo la Serikali ilikuwa ni kujenga na kukarabati barabara kilomita 692, lakini tumefanikiwa kukarabati na kujenga barabara kilomita 430 ambayo ni sawa na asilimia 62. Naipongeza sana Serikali yangu inayosimamiwa na John Pombe Magufuli na inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo kidogo juu ya barabara yetu, hasa barabara yetu ya Lupembe. Barabara ya Kibena, Lupembe, Madeke ni miongoni mwa barabara zilizopangwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami, mwaka jana kwenye Bunge la Bajeti tulipitisha shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, mpaka sasa bado tenda ya ujenzi wa barabara hii haijatangazwa, nimwombe Waziri mwenye dhamana na Waziri Mkuu mwenyewe aliona ile barabara jinsi ilivyo angalau tuweze kutangaza tender na ianze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, ile barabara ya Lupembe kwanza inatuunganisha watu wa Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Jimbo la Mlimba. Barabara hii imekuwa ni barabara muhimu ambayo wananchi wetu wa Lupembe wanasafirisha mazao yao. Lupembe tunalima chai, Lupembe tunazalisha mbao, tunazalisha nguzo za umeme, tunazalisha maharage, mahindi, viazi na kila aina ya matunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea barabara ile kutokana na mvua zinazoendelea sasa hivi haipitiki tena, imekuwa-blocked, kuna eneo kubwa gari zimekuwa zikikwama na hivyo wananchi kupoteza uchumi mkubwa sana kwa mazao yao kuozea barabarani kwa kutoweza kusafirisha au kupitisha kupitia ile njia, kwa mtindo huo maana yake tunakwamisha uchumi wa wananchi wa Lupembe. Naiomba Serikali yangu sikivu itenge hizi fedha ili tuweze kupata uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Mkoa wetu wa Njombe ni moja ya mikoa ambayo tunaitegemea sana katika uzalishaji wa mazao ya chakula, pia nguzo kama nilivyosema na zao hili la chai. Sasa kama tutakuwa bado hatuna barabara nzuri, itakuwa ni vigumu wananchi
wanazalisha kwa wingi, lakini hawatoweza kuuza au mazao haya hayataweza kufikia soko kwa sababu barabara yetu siyo nzuri na haipitiki wakati wa kifuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba atakavyokuja kusimama baadaye niweze kujua ni lini sasa Serikali itatangaza tender ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kadri ilivyokuwa tumekubaliana katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi pia katika bajeti ya mwaka jana, kwa hizo fedha tulizotenga bilioni nane.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa kilimo, Mkoa wetu wa Njombe ni moja ya mikoa ambayo inategemewa sana katika uzalishaji. Mikoa mingine inapopata njaa sisi ndiyo watu tunaohusika katika kutoa chakula au wananchi wa Njombe ndiyo wanaosambaza chakula katika mikoa mingine tukishirikiana na Mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Mikoa hii pia iweze kupewa consideration maalum katika kuhakikisha kwamba tunaipatia kipaumbele hasa kwenye upande wa pembejeo. Mara nyingi pembejeo zimekuwa zikija kwa kuchelewa, zinafika wakati tumepanda, sasa bei yenyewe iko juu, wananchi wetu hawawezi kununua kwa bei hiyo kwa sababu kipato chao ni kidogo, tunaomba bei ya mbolea ipungue, pia iwahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe huwa tunalima mara mbili, tunalima mwezi wa Sita kwenye bustani baadaye mwezi wa Kumi tunalima sehemu za milimani ambako kunazalisha magunia ya kutosha au mazao ya kutosha. Kwa hiyo, tuombe mbolea zije mapema na
ikiwezekana zianze kuja mapema mwezi wa Sita ili wananchi wetu waweze kutumia mbolea vizuri na hatimaye waweze kupata mazao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee zao moja la chai ambalo tunalima hasa maeneo ya Lupembe na maeneo ya Luponde. Zao hili limekuwa likiuzwa kwa bei ndogo sana ukilinganisha na gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukipiga hesabu ya mbolea inayotumika shambani, kuhudumia ule mmea mpaka unapofikia kuanza kutoa chai, kilo moja ya chai inagharimu takribani shilingi 450 na zaidi, lakini bado tunauza kwa shilingi 250, sielewi ni kwa nini zao hili limekuwa likiachwa tofauti na mazao mengine kwa hiyo tuombe wananchi wetu ili wasiendelee kuzalisha kwa hasara, angalau tupunguze baadhi ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali mmeshapunguza tozo la moto na uokoaji, nipongeze sana Serikali kwa jitihada hizo lakini bado bei ya kuuzia wananchi haijapanda, pamoja na kwamba baadhi ya kodi imepungua, bado bei imebaki palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kuna kodi nyingine ambazo zinafanya hili zao liuzwe kwa bei ndogo basi nazo tuziondoe ili waweze kunufaika na kilimo cha chai. Wote tunajua chai tunaitegemea sana hakuna mtu ambaye hatumii chai hapa ndani na ni zao ambalo kila mmoja
linamgusa hasa kwenye matumizi ya majani ya chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwenye upande wa elimu, kwa kutoa elimu bure hasa kupeleka fedha kwenye shule zetu za sekondari na msingi kwa ajili ya kugharamia elimu bure. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutoa fedha hizi idadi ya wanafunzi wanaoingia
darasa la kwanza imeongezeka, hata watoto wa sekondari wanaoacha yaani drop out zimepungua baada ya kuanza kupeleka hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi walikuwa wanashindwa kulipa hizi ada na hatimaye kuwaondoa watoto shuleni na kuwarudisha
nyumbani, hasa watoto wa sekondari na shule za msingi, baada ya hii elimu bure tumeona shule nyingi zinakuwa na watoto wengi pia shule za msingi wanaoingia darasa la kwanza wameongezeka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo lipo kwenye walimu wa sayansi, pamoja na kwamba tumeajiri walimu elfu mbili na kitu, tuombe basi hao walimu wasambazwe kwenye hizi shule za sekondari ili tuwe na mkakati na ni lazima tuwe na mkakati wa kudumu wa kuhakikisha kwamba
tunawapata walimu wa sayansi wa kutosha, mkakati huu lazima tuanze mapema, tuwe na mkakati wa muda mrefu na wa muda mfupi. Tulichofanya sasa hivi ni kama muda mfupi, ni lazima tuanze kuandaa watu wetu hasa kuanzia shule za msingi kupenda masomo ya sayansi na wakienda sekondari wachukue masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawezaje kufanya hivi, ni lazima sasa kule sekondari tusiweke option, tunapowaambia watoto wachague kuchukua combination za sayansi au kutosoma hasa chemistry na physics, tunafanya hawa watoto sasa waanze kukata tamaa mapema. Hivi sasa ukienda kwenye shule hizi za msingi, ukiuliza mtoto wa darasa la tano, utapenda kusoma masomo gani sekondari, atakwambia mimi nitasoma art. Nataka kuwa Mwanasiasa nataka kuwa Mwanasheria, ni lazima tutengeneze mazingira, tuwamotivate kwa kuhakikisha kwamba watoto wote wanapokwenda kidato cha kwanza… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kupata fursa ya kuweza kuchangi kwenye Wizara hii ya Miundombinu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kununua ndege sita. Ni jambo lisilo la kawaida kwa nchi kama ya kwetu ambayo tumekuwa hatuna ndege na akaamua kununua ndege sita, kwa hiyo na mpongeza sana kwa uamuzi wake huo, ambo ni mzuri sana ambao utatusababishia Watanzania tuweze kuwa na ndege za kutosha na hatimaye kuweza kuboresha uchumi wetu wa Tanzania kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hotoba yake nzuri ambayo inaleta matumaini katika kuboresha miundombinu. Nimpongezi Naibu wake Waziri, niwapongeze pia watendaji wa Wizara hii ya Miundombinu kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa kuhakikisha kwamba miundombinu kwa maana ya barabara, reli na bandari na pia mawasiliano yana boreshwa kwa ajili ya kuimarisha na kuchochea uchumi wetu wa Tanzania; niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwa pongeze wajumbe wa kamati ya miundombinu kwa kutuletea taarifa nzuri na kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kushirikiana na Wizara katika kuandaa mipango na kuishauri vizuri Wizara ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii, niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa sababu katika taarifa yao wameeleza vizuri sana kwamba kuna baadhi ya mikoa ambayo bado haijaunganishwa na mikoa ile ya Njombe na Morogoro, mikoa ya Mbeya na Njombe, mikoa ya Katavi na Kigoma, mikoa ya Kigoma na Kagera, lindi na Ruvuma na mikoa mingine. Ukiangalia hii mikoa ambayo wameitaja ambayo haijaunganishwa ni mikoa ya uzalishaji. Ni mikoa ambayo tunaitegemea sana hasa katika kuzalisha mazao ya chakula lakini pia kuzalisha mazao ya biashara. Pia ni mikoa ambayo ina mvua nyingi sana, maana kwa kuwa ni mikoa yenye mvua nyingi lakini pia ndiyo mikoa inayozalisha chakula kwa hiyo barabara zake sio nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe katika mipango na nimeona mmeeleza na mmeiandaa vizuri sana; katika mikoa hii mmeanza kutekeleza kuhakisha kwamba inapata barabara nzuri, moja wapo ikiwa ni barabara ile ya Lupembe, barabara ambayo inasaidia sana katika kuhakikisha kwamba mazao ya biashara na mazao ya chakula kama nilivyosema yanasafirishwa. Kwa hiyo, niwashukuru kwa hilo, kwa kuhakikisha kuwa barabara yetu pia ya Lupembe inaendelea kuwekwa katika Bajeti na kuongezewa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mwaka wa jana tuliingiza kwenye bajeti tulitengea fedha na mwaka huu pia imetengewa fedha. Sasa naomba kujua, pengine Mheshimiwa Waziri utakaposimama utatueleza vizuri, je, zile fedha ambazo zilitengwa kwenye Bunge la Bajeti mwaka jana ambapo unaishia mwaka huu, na hizi fedha ambazo zimetengwa mwaka huu je, zitajumlishwa pamoja au zile za mwaka huu ambao unaisha zimeshapitwa na wakati au hazitatumika au hazitajumuishwa na tutegemee kupata tu fedha hizi za mwaka huu?
Kwa hiyo, nitaomba utakapo kuja kufanya majumuisho basi nipewe ufafanuzi wa juu ya zile fedha ambazo tulikuwa tumetenga mwaka jana na hizi fedha shilingi bilioni mbili ambazo zimetengwa mwaka huu kama zitakuwa zitajumuishwa kwa pamoja na barabara ile ianze kufanyiwa utengenezaji au ujenzi wa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza, kama tulivyosema nimeangalia kwenye taarifa pia mmeweza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara nyingine, ile barabara ya kutoka Ilunda mpaka kuelekea Igongolo, ni barabara ambayo ni ya muhimu sana katika uzalishaji wa mazao, kwa maana ya uzalishaji wa wananchi wa maeneo yale. Kwa hiyo nipongeze sana kwa fedha zile ambazo zimetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe badala ya kuendelea kutenga fedha kwa kiwango cha kokoto ni vizuri tuanze kujielekeza kutenga fedha kidogo kidogo kuanza kutengeneza kidogo kidogo lami na hatimaye barabara nzima zitakuwa zimekamilika au tuanze kutengeneza zile sehemu ambazo tunafikiri kwamba ni korofi, sehemu ambazo wakati wa kifuku wananchi/wakulima wetu wadogo wadogo hawawezi kupitisha mazao yao yakafikia kwenye masoko basi angalau zianze kujengwa maeneo hayo kwa kiwango cha lami na hatimaye tutaweza kumaliza barabara nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisubiri tu fedha itakuwa ni ngumu lakini tukianza na hizo fedha ndogo ambazo tunatengenezea vifusi vya kokoto, tukaanza kutengeneza kiwango cha lami kwenye maeneo yale ambayo ni korofi na hatimaye barabara zote zitatengenezwa kirahisi zaidi na zitaweza kupitika wakati wote hata wakati ule wa mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kwenye upande wa mawasiliano. Imeelezwa hapa kwamba maeneo mengi ya vijijini bado mawasiliano ni shida, bado hayafikiki mawasiliano na maeneo haya ya vijijini ndiyo maeneo ambayo tunayategemea, kama tulivyosema, kwenye uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula; kwa kuwa maeneo haya hayana mitandao ya simu au hayajajengwa minara ya simu. Kwa mfano katika Jimbo langu la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, kuna kata tano hazina mawasiliano. Kuna kata za Ikondo, Ninga, Mfiliga, Idamba na Ukalawa hazina mawasiliano, kwa hiyo vijiji vyote vya maeneo hayo simu hazipatikani kwa urahisi zaidi. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri maeneo hayo tuweze kujengewa minara ili wananchi wale waweze kupata mawasiliano kirahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nichangie juu ya suala mtambuka. Niwapongeze Wizara kwa uamuzi wa kuanzisha mafunzo maalum kwa wakandarasi wa kike, mafunzo hasa yanayohusika na ukarabati na matengenezo
ya barabara na uandaaji wa zabuni. Hii itasaidia akina Mama wengi kujiunga na ukandarasi au kusoma masomo ya ukandarasi, masomo ya sayansi, lakini pia itawasaidia wanafunzi wetu wa shule za sekondari kuanza kupenda masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hivi wanafikiri kwamba ukandarasi au uhandisi au u-engineer ni kwa ajili ya wanaume tu. Kwa hiyo tukiwawesha hawa na wanapoenda huko kwenye maeneo haya ya ujenzi wa barabara wakiwaona basi watahamasika kusoma masomo ya sayansi na kuhakikisha kwamba wanafaulu vizuri, na tutakuwa na wanawake wengi ambao wanakuwa ni Ma- engineer na hatimaye kuwa na ma-engineer wa kutosha kuliko ilivyo sasa hivi, ma-engineer wengi ni wa kiume kuliko ma-engineer wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nichangie juu ya ajira hasa ajira za vibarua, wale ambao they are not trained kwenye maeneo huko ambako shughuli za ujenzi wa barabara zinaendelea. Niombe tuweke utaratibu wa kuwaangalia wale watu wanaowekwa kwenye maeneo ambako miradi hii inatengenezwa. Tukifanya hivi itasaidia kuwapa ajira vijana wa maeneo husika ambako barabara zinajengwa, lakini pia itawafanya hawa vijana wasiharibu miundombinu ya barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine vijana au watu wa maeneo yale wanaharibu kwa sababu wanaona kama ile barabara kwao hawajanufaika, wanapoona wajenzi wa barabara au wanaoshiriki kutoa labour force ya zile ambazo hazihitaji wasomi wanatumika watu wa kutoka maeneo ya mbali. Na kuna maeneo mengine wamekuwa wakiiba vifaa vya ujenzi au waki- vandalize vifaa vya ujenzi kwa sababu tu wao hawajashirikishwa katika ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukiwatumia vijana wa maeneo husika, maeneo ambako mradi unafanyika itawasaidia vijana wenyewe kuanza kupenda shughuli zile na kuhakikisha kwamba wanakuwa walinzi wa vifaa na mali zilizoko katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa na Serikali. Nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa utumishi uliotukuka katika kuwasaidia Watanzania, katika kuwa na afya na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii zilizopo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya wagonjwa (ambulance); magari haya ni muhimu sana kama ilivyo muhimu kuwa na dawa za kutosha, vifaa tiba vya kutosha. Pia ni muhimu kila hospitali na baadhi ya vituo vya afya vilivyopo maeneo ya vijijini ndiyo vinavyohudumia watu wengi sana ambao wanategemea kupata matibabu katika vituo hivi pekee tofauti na maeneo ya mjini ambako kuna hospitali na vituo vya afya visivyo vya Serikali. Mfano, katika Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe eneo hili lina takribani watu zaidi ya 100,000 lakini ina vituo vitatu tu vya afya na hakuna hospitali yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wagonjwa wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata matibabu kwenye kituo cha afya kilichopo Lupembe umbali wa kilometa 75 toka Hospitali ya Kibena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kituo kipya cha Kichiwa kipo umbali wa kilometa 50 toka Hospitali ya Kibena na kituo cha Sovi ambacho kipo umbali wa kilometa 45 toka Hospitali ya Kibena. Katika Halmashauri yetu tumekuwa tukipoteza akina mama wengi kwa kucheleweshwa kupata upasuaji kutokana na kutokupata msaada wa usafiri kwa ajili ya kupelekwa Hospitali ya Kibena kwa ajili ya upasuaji. Hivyo tunaomba tupewe gari angalau moja kwenye vituo hivi vitatu kwa ajili ya kuwasaidia usafiri akina mama wajawazito na wagonjwa mahtuti ili kuwahi matibabu au huduma kwenye Hospitali ya Kibena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Wilaya, Jimbo letu na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe haina hospitali. Tumeanza jitihada za kujenga hospitali ya Wilaya. Wananchi kwa kutambua umuhimu wa kuwa na hospitali ya Wilaya, wamejitolea eneo lao lenye ukubwa wa ekari 52 ili eneo hili litumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali. Tunaomba Serikali itusaidie kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazee ambao ni wazazi wetu ambao sisi watoto wao tuna wajibu wa kuwasaidia kwa malazi, mavazi, chakula na kuwahudumia pale wanapokuwa na matatizo ya kiafya. Wazee wengi wanafariki kabla ya muda wao kutokana na ugumu wa maisha na msongamano wa mawazo unaotokana na watoto wengi hawatunzi wazazi wao, hata kama watakuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea wazee wanatunzwa vizuri na Serikali kwa kushirikiana na watoto wao. Hii inawafanya waishi miaka mingi tofauti na Tanzania na nchi nyigine za Afrika. Hivyo basi, napendekeza Serikali ije na sheria itakayotutaka Watanzania kuhakikisha kwamba wanawatunza wazazi wao hasa wanapokuwa wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mara nyingi watoto wakipata kipato huwa wanawasahau wazazi waliowalea, wazazi wanataabika vijijini bila chakula na makazi duni wakati wao wakiwa na maisha mazuri. Hivyo sheria ikitungwa itawabana watoto wao kuwa na wajibu wa kuwalea wazazi wao, angalau kwa kuwapa huduma za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa maeneo ya vijijini.Mara nyingi watumishi wa afya wakianzia kazi mjini huwa hawapo tayari kuhamia vijijini pale wanapopata uhamisho wa kwenda vijijini. Hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuwafanya watumishi wawe flexible kwenda popote atakapopangiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ipeleke watumishi wa afya katika maeneo ya vijijini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Pia pale penye upungufu wa watumishi au watumishi kutakiwa kufanyakazi masaa ya ziada tunaomba Halmashauri na Wizara kuwalipa malipo yao ya kazi za ziada au on call allowances wapewe na ikiwezekana Serikali iwaongezee, shilingi 25,000 ni ndogo sana. Serikali ione uwezekano wa kuongeza kiwango hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba za utotoni na ukatili wa watoto; pamoja na tatizo hili kuchangiwa na mila na desturi pamoja na imani za kishirikina, pia wazazi kutotimiza wajibu wao wa malezi inachangia watoto wengi kupata mimba wakiwa na umri mdogo. Kila mzazi anatakiwa na ana wajibu wa kumlea mtoto wake katika maadili mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi wanaacha watoto wao walelewe na house girls na television, vitu hivi ndivyo vinavyochangia watoto wengi kukosa malezi bora. House girls na television ndio wamekuwa walimu wa watoto hususani kwenye upande wa ngono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalosababisha mimba za utotoni na ukatili kwa watoto ni umbali wanaotembea watoto wetu kwenda shuleni. Mtoto anayetembea zaidi ya kilometa tano kwenda shule ya msingi au sekondari, ana hatari kubwa ya kukumbana na vishawishi vya ngono kuliko mtoto anayetembea chini ya kilometa tano. Shule nyingi zilizopo maeneo ya vijijini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wapo hatarini kujiingiza kwenye vitendo hivyo na hatimaye kupatikana na ukatili wa kijinsia au mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kutatua matatizo ya mimba za utotoni ambazo kwa sasa zinasababishwa na vijana wanaotoa msaada wa usafiri (lift) bodaboda na magari na kuwafanyia ukatili watoto wetu, ni vizuri Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI, tuje na mpango wa kujenga hostels kwenye shule zetu za msingi na sekondari ili kuwaepusha watoto wetu kuingia kwenye vishawishi vitakavyopelekea kwenye matatizo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za damu salama, bado kuna changamoto ya watu kujitolea kuchangia damu na maeneo mengine hasa vijijini wananchi wengi hawapo tayari kuchangia damu mpaka walipwe. Hivyo Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi waishio vijijini juu ya umuhimu wa kuchangia damu. Hii itaongeza mwamko wa wananchi waishio vijijini kuchangia damu bila malipo pale wanapoombwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Elimu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake mzuri kabisa wa kuamua kujenga mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mabweni haya yamejengwa kwa shilingi bilioni 10 na yataweza kutosha kuwa-accommodate wanafunzi 3,840. Nimpongeze sana kwa jitihada hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, nimpongeze Waziri wa Elimu na Naibu wake na pia Katibu wa Wizara na watendaji wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu na kupitia elimu hiyo tuweze kupata maendeleo katika nchi yetu maana bila elimu hakuna maendeleo. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu kama walivyosema wenzangu ni msingi wa kila kitu. Elimu ndiyo msingi wa maisha, bila elimu hakuna maisha. Kwa hiyo, ili tuweze kupata elimu nzuri ni lazima kuwepo na mwalimu, miundombinu mizuri lakini pia ni lazima tuwe na vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Mimi nizungumzie juu ya walimu, walimu tunao japo tuna upungufu lakini kuna changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo na ndiyo maana unakuta sasa inapofika katika kupata ile outcome tunakuwa na matatizo kwa sababu hatujawaweka vizuri walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa juu ya madeni ya walimu. Haya madeni ndiyo kikwazo katika utoaji wa elimu bora. Kwa wale waliowahi kuwa darasani (walimu) wanajua, mwalimu ili aweze kufundisha vizuri ni lazima awe vizuri psychologically. Huwezi kutegemea mwalimu akafundisha vizuri na akawawezesha watoto kupata elimu nzuri kama psychologically yupo disturbed. Mwalimu anapokuwa na madeni, mwalimu anapokuwa na kero mbalimbali za kwake binafsi ni vigumu kufundisha vizuri. Anaweza akaingia darasani akajipanga kutaka kufundisha vizuri wanafunzi lakini akikumbuka tu deni wakati anaendelea na jukumu la kufundisha, tayari huyu mwalimu hataweza kufundisha vizuri wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuipongeze Serikali mmeanza kulipa lakini bado speed ya ulipaji wa haya madeni sio nzuri sana. Tumeambiwa hapa na Kamati imetoa taarifa kwamba madeni ya walimu ambayo wanaidai Serikali mpaka sasa ni shilingi trilioni 1.6 na madeni yaliyolipwa ni shilingi bilioni 33.1 ambayo ni sawa tu na 32%, speed hii bado ni ndogo. Tuiombe Serikali iweze kulipa madeni haya. Tunajua madeni yanazidi kuongezeka kwa sababu wanapopandishwa madaraja madeni yanaongezeka na kwa kuwa yanaongezeka ni vizuri yalipwe mapema haya mengine ambayo yapo ili kupunguza sasa walimu wengi ambao wanakuwa frustrated. (Makofi)

Mheshimia Mwenyekiti, hali iliyopo sasa hivi na ukizingatia kuna mambo haya ya vyeti fake na ukaguzi na walimu wengine wameambiwa kuna baadhi ya vyeti havipo halali na hawajajua hatma yao. Kwa hiyo, hali iliyopo sasa hivi kwenye mashule walimu wengi hawafundishi bali wanahudhuria madarasani wanaofundisha ni wachache. Wengi wao wamekuwa disturbed na haya madeni na vyeti fake. Kwa hiyo, naomba Serikali yangu Tukufu tujaribu kujipanga kulipa madeni haraka lakini pia na hili zoezi la vyeti fake hili liweze kukamilishwa haraka ili walimu waingie darasani wafundishe wasiingie darasani kuhudhuria tu vipindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali na Waziri nafikiri anaelewa vizuri naposema mambo haya. Nafikiri atayashughulikia vizuri ili walimu wetu waweze kuendelea kufundisha na hatimaye tuje kuweza kutoa elimu bora. Tusipofanya hivyo, tutaendelea kuwaweka wanafunzi shuleni wanashinda wanacheza, wanakula chakula, wazazi wanafikiri watoto wanasoma kumbe hawasomi. Hata walimu wakuu wanafikiri walimu wanaingia darasani kumbe humo darasani hawafundishwi, mwisho wa siku matokeo yake yatakuwa ni mabaya. Kwa hiyo, niombe tukamilishe hili zoezi la vyeti fake lakini pia tukamilishe kulipa madai ya walimu ili walimu wetu hawa waweze kufundisha vizuri darasani na watoto wetu waweze kupata elimu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine upande wa walimu pia, kuna upungufu mkubwa sana wa walimu katika shule zetu za msingi ukilinganisha na sekondari. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha, vivyohivyo na hii inaathiri matokeo, inaathiri mwisho wa elimu kwa ujumla. Kwa hiyo, tuombe mamlaka zinazohusika ziajiri walimu. Tumeshaona kwenye hili zoezi la vyeti fake nalo limeondoa walimu wengi sana hasa wa shule za msingi. Ukiangalia idadi kubwa ya walimu wenye matatizo ya vyeti fake ni wale walimu wanaofundisha shule za msingi, kwa maana hiyo tufanye replacement haraka ili ku-rescue situation inayoendelea kwenye hizo shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa elimu maalum kwenye shule zetu hasa shule zetu za msingi. Kwa mfano, kwenye Halmashauri yangu mimi tuna shule moja pale ya Matembwe ambayo yenyewe ni shule jumuishi, inachukua wanafunzi ambao wana ulemavu tofauti tofauti, lakini tuna mwalimu mmoja tu anayefundisha kwenye ile shule. Kwa hiyo, tuombe tupeleke walimu wa kutosha na pia vifaa vya kutosha kwenye elimu hii jumuishi ili watoto hawa ambao wana ulemavu tofauti tofauti waweze kupata haki yao ya msingi, haki yao ya kupata elimu kama watoto wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema juu ya drop outs hasa hizi kesi za mimba kwenye shule zetu. Ukiangalia shule nyingi ambazo watoto wanapata mimba ni zile shule za kutwa, shule hizi za kata. Kwa nini wanapata mimba? Ni kwa sababu ya ukosefu wa mabweni. Watoto wengi wa kike wanatembea umbali mrefu sana na tunajua watoto wetu wa siku hizi hawawezi kutembea kama tulivyokuwa tunatembea sisi zamani. Kwa hiyo, kinachotokea ni kwamba wanatumia usafiri wa bodaboda maeneo mengine wanatumia taxi. Hawa wanaowapeleka shuleni ili waweze kuwahi vipindi ndio hao wakati mwingine wanawageuka kuwashawishi watoto kuingia kwenye hivyo vitendo vya ngono na mwisho wa siku wanapata mimba na wengine wanapata maambukizi ya UKIMWI na wengine wanaamua kuacha shule kwa sababu tayari wameshapata wapenzi na wanaenda kuolewa. Tunaipongeza Serikali kwa mpango huu wa kujenga mabweni.

Naomba pia katika Jimbo langu na katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Njombe na shule za kata za kutwa ambazo watoto wengi wanatembea umbali mrefu, katika ule mpango wa ujenzi wa mabweni basi na mimi nipate mabweni ili tuwaokoe watoto hawa ambao wanatembea umbali mrefu tuwakinge na mimba ambazo wanaweza wakazipata kutokana na vishawishi wanavyovipata njiani wanapoenda kwenye shule hizi za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia umbali unachangia wanafunzi wetu kufeli. Wanatumia muda mwingi kutembea kwenda shuleni, anapomaliza kipindi anafikiria kuanza kutembea kwenda nyumbani na akifika nyumbani anakutana na shughuli za nyumbani kwa sababu ni watoto wa kike wanapewa shughuli za pale nyumbani za kupika, kutafuta maji, za kutafuta kuni lakini mwisho wa siku utakuta huyu mtoto anapoteza muda mwingi wa kusoma. Kumbe akibaki bwenini anapata muda mwingi wa kusoma na kufanya discussion na wenzake jioni mwisho wa siku atakuja kufaulu vizuri. Kwa hiyo, nashauri tujenge mabweni kwenye shule zote hizi za sekondari ili watoto wetu waweze kusoma vizuri na hatimaye waweze kupata elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana kwenye suala la vitabu. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuamua kutoa kitabu kimoja nchi nzima cha kufundishia (text book). Nipongeze kwa jitihada mlizochukua, lakini nisikitike kwa kutoa vitabu ambavyo vina makosa, ni aibu kubwa sana wakati tuna wataalam wameajiriwa, wanafanya editing ya hivi vitabu, inakuwaje vitabu vingi namna hii vinakuwa na makosa mengi ya spelling, ya kisarufi na makosa mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe ndugu yangu, dada yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, tukae na watu wa editing ili tujue nini kimetoea? Maana tumetumia fedha nyingi na itatakiwa tubadilishe tutatumia gharama kubwa, watuambie ni kwa nini wamekubali kutoa vitabu hivi ambavyo vina makosa? Haijawahi kutokea katika miaka yangu yote ya kusoma kwangu na katika maisha yangu yote kupata mwaka ambao vitabu vimetoka na makosa mengi namna hii, zaidi ya vitabu vya masomo karibia matano, sita, vina makosa!

Kwa hiyo, hebu tukae tujue kuna nini kimetokea? Inawezekana hao watu wanaohusika na editing walitaka kuhujumu tu Serikali ili kuonesha kwamba Serikali yetu haifanyi kazi vizuri. Nakuamini dada yangu, naomba kakae na hii Kamati au Kitengo kinachohusika na mambo ya editing ya vitabu ili tujue ni kwa nini wametoa vitabu vyenye makosa namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Maji na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai; bila maji hakuna maisha ya binadamu wala viumbe hai vingine. Tatizo la uhaba wa maji nchini na duniani linazidi kuongezeka. Hii kama wataalam wanavyosema, inaashiria, vita kubwa duniani itakayotokea itakuwa ni vita ya kuvigombea (scramble for) maji. Hivyo ni muhimu kwa nchi yetu, Serikali yetu kupanga vizuri juu ya mipango mizuri ya usambazaji maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe bado tuna vijiji vingi havina maji safi na salama. Mfano vijiji vya Matiganyora, Nyombo, Lole, Igongolo, Tage, Mende, Kichiwi, Ilengititu, Ibiki, Kidegembye, Havanga, Iyembele, Isoliwaya, Kanikelele, Iwafi, Lima, Welele, Ikang’asi na Igombola havina maji. Tunaomba vijiji hivi navyo viwekwe kwenye mpango wa kupewa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji imekuwa ikitekelezwa kwa kuchelewa sana na wakati mwingine imekuwa haikamiliki vizuri. Hii ni kutokana na kucheleweshwa na taratibu za manunuzi na zabuni. Mara nyingi wanaochelewesha zabuni hizi na taratibu za manunuzi ni watendaji wetu waliopo kwenye Halmashauri zetu. Hivyo nadhani umefika wakati Serikali iwapime Watendaji wetu waliopo kwenye Halmashauri kwa idadi ya miradi ya maji iliyokamilika ndani ya muda ndani ya Halmashauri zao. Mfano, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri atabaki kwenye nafasi yake kwa kupimwa kwa speed yake ya kusimamia miradi ya maji, ubora wa kazi ilivyofanyika, utoaji wa elimu bora kwa watumiaji wa maji kupitia Kamati za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado fedha inayotengwa kwenye Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Maji haitoshelezi mahitaji ya maji safi na salama nchini. Hivyo, nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba iongezwe sh.50/= kutoka kwenye kila lita ya mafuta. Tatizo la maji mijini na vijijini linawaingizia gharama kubwa wananchi, kutokana na gharama ya kununua maji kwa wale wanaouza maji; gharama ya muda ambao akinamama wanatumia kwenda kutafuta maji; gharama kubwa wananchi wanazotumia kutibu magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maji nchini ni muhimu tuongeze sh.50/= kwenye bei ya mafuta ili fedha hizi ziende kwenye mfuko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu tumejaliwa kuwa na vipindi vya mvua ya kutosha kila mwaka. Maji yanayotokana na mvua hayatumiki vizuri, yamekuwa yakipotea tu. Ni muhimu Serikali ipitishe sheria ndogo ya uvunaji wa maji toka kwenye majengo yetu, pia maeneo ambayo yana mvua nyingi. Ni vizuri tukaanzisha utaratibu wa kujenga mabwawa ya maji ili yatumike wakati wa kiangazi kwa shughuli mbalimbali, pia uvunaji wa maji maeneo ya mvua nyingi itasaidia kupunguza mafuriko maeneo ambayo maji haya huelekea, yaani maeneo ya uwanda wa chini (low land).

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kidogo juu ya Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa wa mwaka 2016 (The Access to Information Act, 2016).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria na Serikali kwa ujumla kwa kuuleta huu Muswada wakati huu. Muswada huu umekuja kwa wakati muafaka kabisa ambapo Watanzania wengi wanahitaji kupata taarifa. Pia Muswada huu unaendana kabisa na kauli mbiu ya Serikali ya „Hapa Kazi Tu‟ kwa maana ya dhana ya uwajibikaji na uwazi. Kwa hiyo, kwa kuwa na Muswada huu kutasaidia kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwazi kwenye Serikali zetu hasa kwenye Halmashauri zetu ambako huko ndiko kuna matatizo mengi hasa ya utoaji wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba inasaidia Viongozi wetu kwa maana ya Watendaji wetu wa Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali kuweza kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu mikakati ya maendeleo, mapato na matumizi, mipango yao na miradi yao ya kimaendeleo katika maeneo yao. Hizi ni taarifa muhimu sana kwa wananchi kuzipata ili waweze kujua nini Serikali imepanga na Halmashauri zao zimejipanga namna gani kwa ajili ya maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kupata taarifa hizi zinawasaidia wananchi au Serikali kuhakikisha kwamba kero mbalimbali za wananchi zinapunguzwa. Hivyo sasa hivi ukipita katka maeneo mengi hasa vijijini, utakuta wananchi wanalalamika hawapewi taarifa ya miradi, hawapewi taarifa za mapato na matumizi kwenye vijiji vyao. Kwa hiyo kwa kuweka sheria hii kwa kupitia Muswada huu utawawezesha hawa viongozi wetu walioko huko chini waweze kutoa taarifa mapema na hivyo wananchi kuwa na uelewa wa mambo ambayo yanaendelea kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwamba ni muhimu sasa Serikali itengeneze utaratibu mzuri kuwe na client service charter kwa kila taasisi ili kupitia hizo wananchi au watafuta taarifa au walaji wa taarifa wajue watazipataje hizo taarifa na hizo taarifa zinapatikana kwa muda gani. Kama tulivyoona wengi huwa wanalalamika kwamba taarifa zinachelewa, mtu anakwenda ofisini anaambiwa uje kesho, uje keshokutwa au uje mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukiwa kuna clients service charter hii na wananchi wakijua, kwa sababu ile inaonesha ni taarifa ipi itapatikana kwa muda gani. Kuna taarifa nyingine za saa moja au siku moja, kuna nyingine za wiki moja, wiki mbili na nyingine za wiki tatu, wakishajua utaratibu huu ukiwepo kwenye Taasisi zote za Serikali inakuwa rahisi kujua yule mtu anayetafuta taarifa kujua hii taarifa nitaipata kwa muda gani, kuliko ilivyo sasa hivi. Kwa hiyo, niombe Serikali iweke utaratibu kuhakikisha kwamba kila Ofisi ya Serikali, kila ofisi zinazohusika na Sheria hii au na Muswada ambapo itakuwa Sheria basi iwe na clients service charter kwa ajili ya kuwawezesha watu kujua ni lini watapata taarifa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja juu ya utunzaji wa taarifa. Imetajwa kwamba angalau taarifa zikae kwa muda wa miaka 30. Kwangu naona ni muhimu kwamba tuwe na utunzaji wa taarifa kwa kuwa taarifa zikitunzwa vizuri zinatusaidia baadaye. Watu wengine wanatumia hizi taarifa, ripoti mbalimbali na taarifa mbalimbali kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali, pia taarifa hizi zinatumika pengine kwa ajili ya kupata historia ya jambo fulani lililotokea mwaka fulani au maamuzi yaliyowahi kufanyika muda fulani na watu fulani au taasisi fulani au Serikali. Hivyo, ni muhimu kuwa na utunzaji wa taarifa wa muda mrefu ili zitumike kwenye mambo ya historia, lakini pia ziweze kutumika kwa ajili ya tafiti mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilisemee kidogo ni juu ya hizi taarifa. Tumesema kwamba zitatumika kwa Serikali au kwa Taasisi za Serikali zinazonufaika na Serikali au zilizo chini ya Serikali, haijasema kwamba je, taasisi nyingine ambazo siyo za Serikali ambazo ni taasisi za binafsi au tunaita taasisi zisizo za Serikali kama vile makampuni mbalimbali. Kuna makampuni mengi hapa nchini ya uwekezaji kwa aina mbalimbali, Muswada hauelezi vizuri jinsi gani hawa walaji wa taarifa wataweza kupata taarifa kwenye Taasisi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiiacha ikaelea elea hivi itakuwa shida sana kupata taarifa kwenye makampuni kwa sababu wanasema hii sio taasisi inayosimamiwa na Serikali, ni taasisi binafsi, ambayo inajitegemea. Kwa hiyo ni muhimu hii Sheria ifafanue vizuri. Tutamwomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho basi afafanue vizuri ni sehemu gani zina-cut across hii Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni muhimu sana kwenye taasisi hizi zisizo za Serikali nazo pia ziweze kutoa taarifa, kwa sababu wananchi wanahitaji kujua haya mashirika pengine yasiyo ya Kiserikali yanafanya nini na baadhi ya taarifa ni muhimu sana kwao. Kwa hiyo, ni muhimu kukawa na utaratibu au Sheria ikawagusa ili nao waweze kutoa taarifa na wananchi waweze kunufaika na hizi taarifa ambazo watakuwa wanazitafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo la adhabu, imeelezwa hapa kwamba adhabu kwa atakayekuwa ametoa taarifa zile zinazohusu mambo ya usalama, basi kifungo itakuwa ni miaka 15 na isiyozidi miaka 20. Naunga mkono hiyo, pia kwa wale ambao watakuwa wametoa taarifa nyingine kwa mfano wamepotosha taarifa na tunajua sasa hivi ilivyo, magazeti mengi yanapotosha taarifa, vyombo vya habari vingi vinapotosha taarifa, ni muhimu kumbe wawe na hii adhabu kwamba angalau basi anayekuwa amepotosha taarifa ataenda kifungo cha miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano. Kwa hiyo, naomba hii pia tuiwekee utaratibu mzuri na makosa yaainishwe vizuri ili mtu anapohukumiwa asilalamike kwamba adhabu pengine imezidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muswada ni mzuri na umekuja kwa muda muafaka na unaofaa sasa hivi kwa jinsi hali ilivyo na mahitaji ya jamii yetu yalivyo. Kwa hiyo, naunga mkono hoja, naunga mkono Muswada huu uweze kupitishwa vizuri na uanze kufanya kazi haraka sana. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2017
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Muswada huu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kuleta Muswada huu sasa baada ya kuona kama alivyosema msemaji wetu wa kwanza, Mheshimiwa Mhagama, baada ya kufanya tathmini kuona kwamba practically utaratibu wa zamani hauleti tija, basi ameamua kuja na marekebisho haya ili tuweze kuisaidia Serikali na Wizara iweze kuwa na tija katika kutoa taarifa zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashangae baadhi ya Wajumbe wa Kamati hasa upande ule wanaolalamika juu ya Muswada huu. Tumefanya kazi wote na Waziri amekuja na maelezo mazuri na Mwanasheria Mkuu ametoa ufafanuzi mzuri, Kamati tukaelewa, tukaona umuhimu wa kukubaliana na marekebisho au kukubaliana na haya maombi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshangaa dada yetu pale, mama yetu Riziki. Ndiyo matatizo ya kuwa mtoro kwenye Kamati, ungekuwepo jana ungepata taarifa vizuri. Kwa hiyo, nikubaliane na Muswada huu, ni utaratibu wa kawaida popote pale kwa Serikali zote duniani, marekebisho ya baadhi ya Sheria kama tunavyosema kwamba ni progressive process kwa hiyo kilichofanyika…

T A A R I F A...

taarifa kwa sababu kikao cha jana kilikuwa ni muhimu sana kwetu Wanakamati na ndiyo maana tumekuja na msimamo huu kama Kamati kwa sababu yale yaliyoletwa jana na Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo iliyotujengea tuweze kuamini kwamba huu Muswada ni wa muhimu kuupitisha, kwa hiyo ndugu yangu hukuwepo basi ndiyo maana mambo yamekupita. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaona hata kwenye halmashauri zetu taarifa zetu, kama huwa mnahudhuria vikao
Waheshimiwa Wabunge mnaweza mkajifunza tu kwenye halmashauri, kwenye halmashauri Kamati za Fedha na Mipango zinakaa kila baada ya miezi mitatu mitatu, unaweza ukajifunza jinsi gani taarifa zile zilivyo, unakuta zina matatizo mengi. Sasa je, katika National Level kwa maana ya Wizara na Wizara hizi zinategemea kupata taarifa hizi kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, mojawapo ikiwa ni halmashauri, kunakuwa na matatizo makubwa. Kwa hiyo, ni kweli kabisa Serikali isingeweza kufanya majukumu yake vizuri na wasingeweza kuja kuwa na taarifa nzuri kama sehemu ambazo wanategemea kupata taarifa hizi kama taarifa za mapato na matumizi, zinakuwa siyo realistic.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipongeze Wizara kwa kuja na utaratibu huu wa miezi sita, kuna uhakika kwamba Serikali itakuwa na muda wa kutosha wa kufanya kazi. Itafanya kazi angalau miezi mitano na ule mwezi mmoja wata-complied taarifa na sisi Wabunge tutapata taarifa ambazo zimekuwa realistic, taarifa ambazo ni za uhalisia. Kwa hiyo, hiyo ni moja ya faida ambayo tutaipata kupitia Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni utaratibu wa makampuni mengi makubwa, makampuni ya kimataifa, lakini ni utaratibu hata wa nchi nyingine, Wabunge wengi mmezunguka nchi mbalimbali, kama mmewahi kukutana na Mawaziri au kujifunza taratibu za uwasilishaji wa bajeti, utakuta mara nyingi wanawasilisha mara mbili kwa mwaka. Kwa hiyo na sisi tunajifunza which are the best practices toka kwenye nchi nyingine. Kwa hiyo hii itasaidia pia kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaweza ikatoa taarifa vizuri, taarifa ambazo hazina walakini, taarifa ambazo hazina upungufu, kwa hiyo nami pia naunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni gharama, Waziri amekuwa akichapisha vitabu hapa vinajaa pale kwenye Pigeonholes zetu, hatusomi wakati mwingine, lakini tukiwa na taarifa mbili, vitabu viwili tunakuwa na muda wa kusoma vizuri. Vile vile tunapunguza gharama kwa Serikali ya kuchapicha vitabu. Pia tutapunguza gharama ya muda ambao watumishi wetu wa Serikali wanakaa kwa ajili ya kuandaa taarifa, kila baada ya miezi mitatu wanaandaa taarifa. Ni gharama ya muda, lakini pia financial cost, kuna financial cost implication pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwamba naunga mkono hoja kwa utaratibu huu ili tuweze ku-save gharama ya muda lakini pia tuweze ku-save gharama za kuchapisha vitabu. Vilevile niunge pia mkono kwa hii sheria kutaja ni nini kitafanyika kwa afisa yeyote ambaye hatatekeleza majukumu yake vizuri maana yake hapa ungeweza kutokea uzembe. Kwa hiyo, niunge mkono kwamba Sheria imesema vizuri kwamba huyu Afisa atakatwa mshahara wake wa miezi sita, lakini pia na taratibu nyingine za kijinai zitachukuliwa. Hii itawafanya pia watumishi wetu ambao wana jukumu la kuandaa taarifa waweze kuwa makini katika uandaaji wa taarifa na wahakikishe kwamba wana-meet deadline iliyotolewa na Wizara kuwasilisha taarifa hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naomba Sheria iweze kupitishwa vizuri ili ianze kufanya kazi.