Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Adamson Sigalla Norman (9 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE
YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kipekee kabisa kwanza
kupongeza wachangiaji wote 15 ambao wamechangia kwa maandishi na 22 wamechangia
hapa Bungeni. Mambo machache tu niangalize.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema shukrani hizo, Waheshimiwa Wabunge
nichukue nafasi hii kipekee kabisa kumpongeza Waziri mwenye dhamana na wasaidizi wake
wote kwa sababu kwa muda wote ambao Kamati imekuwa ikifanya kazi zake wamekuwa
wakitupa ushirikiano mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo machache ambayo mmesisitiza ni pamoja na ujenzi
wa reli ya kati, barabara mbalimbali, bandari zote kwa maana ya Dar es Salaam ,Mtwara,
Tanga na Bagamoyo; lakini pia mmesisitiza upande wa ATCL. Pia Waheshimiwa Wabunge
wamesisitiza sana juu ya ajira pale bandarini na kwamba wako watu walioajiriwa ambao
wamefukuzwa kama hivi; sisi kama Kamati tumepokea taarifa hiyo na Wizara imesikia na sisi
wajibu wetu tutafuatilia kuona kwamba Serikali inafanya inavyopasa kama lililofanyika
halikupaswa kufanyika hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge nitumie nafasi hii kusema mambo
machache tu, na hasa juu ya mradi huu wa reli ya kati. Ninaipongeza sana Serikali kwa sababu
dhamira yake na haya maneno niliyasema Dar es Salaam wakati wa kusaini mkataba juzi wa kutoka Dar es Salam kwenda Morogoro. Nikasema kwa sababu mipango yetu ya kwanza ya reli
yetu haikuwa kilometa 160 kwa saa, kuchelewa huku ndiko kumetupelekea kwenye kilometa
160 kwa saa. Nikasema kama kuchelewa ni huku basi ni kuchelewa kuzuri, maana sasa
tumeenda kwenye spidi kubwa zaidi yenye manufaa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini muhimu kabisa ambalo Wizara ni vizuri ifahamu ni
kwamba kukamilika kwa reli ya kati ni jambo moja, muda wa kukamilika reli ya kati ndio muhimu
zaidi. Kwa sababu zilezile kwamba mzigo tunaotegemea ili uweze kurudisha mkopo wao wote
wa reli ya kati ni ule ule ambao Kenya, Uganda, Rwanda, DRC na Zambia wanautegemea.
Ndio maana nasisitiza tena na Kamati inasisitiza tena kwamba vyovyote itakavyokuwa tumieni
mkandarasi yoyote mnayemjua kwa vipimo mnavyovijua, muhimu reli hii ikamilike haraka kabla
wenzetu hawajakamilisha, hilo ni muhimu kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nisisitize tu kusema pia kwamba naunga mkono vizuri sana,
Mheshimiwa Waziri amesema amegawa vipande vingi vingi kwa maana ya ujenzi wa reli ya kati
na sisi Kamati hatuna tatizo na hilo lakini bado tunasisitiza kwamba standard ya reli na
upatikanaji wa funding ndio unaotengeneza hot cake ya project yoyote. Narudia, project
yoyote haiwi viable kama funding haipo; kwa hiyo ni funding inapokuwa available ndio
inafanya mradi kila mkandarasi aone ni hot cake. Unayejua umuhimu wa kuchukua mizigo
Kigoma au kuchukua Kalemi kule Mpanda ama Mwanza ni wewe Mtanzania; mjenzi
anachoangalia ni funding. Ndiyo maana Serikali mjipange ili kufasili kwa usahihi kwamba
funding iko vipi na kwahiyo tunaelekea wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nichukue nafasi hii tena kuomba sasa
kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lilidhie taarifa ya Kamati ya Miundombinu iwe maelekezo
rasmi kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia, naomba nichukue nafasi hii kipekee kabisa kumshukuru Mungu kwa sababu ya kutuwezesha sisi sote kushinda uchaguzi mwaka jana na kuingia kwenye Bunge hili. Kipekee kabisa nipongeze Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Vyombo vyao kwa kusimamia uchaguzi huo vizuri. Kwa kufanya hivyo, wameniwezesha mimi na mdogo wangu Mchungaji Msigwa, kuingia kwenye Bunge hili. Ahsante sana Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo katika Mpango uliowasilishwa. Kwanza, natambua kabisa kwamba yako maeneo mengi ambayo Mpango umejielekeza na hasa upande wa barabara na reli. Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, naomba nisisitize tu kwamba sisi Watanzania tunaamini kwamba uboreshaji wa Reli ya Kati ile tunayoijua yaani ya kwenda Kigoma – Mwanza baada ya pacha ya Tabora ndiyo tunayoisema na matawi yake ya kwenda Mpanda. Mikoa kumi na tano itanufaika na suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze kwa ufupi, Tanzania ilivyo na hasa Wilaya ya Makete na Mkoa wa Njombe, ni Mkoa ambao ni tegemeo kubwa sana kwa sababu ya uchumi wa Tanzania na hasa uzalishaji wa mazao ya chakula. Naomba sana barabara inayotoka Njombe - Mbeya kupitia Makete ipewe kipaumbele kwa sababu hata Ilani ya CCM imeiweka barabara hii ni barabara ya kwanza. Umuhimu wa barabara hii si tu kwa sababu Norman Sigalla King anatoka Makete ni barabara muhimu kwa maana ya uchumi wa Tanzania kwa sababu Hifadhi ya Kitulo ndiyo hifadhi pekee ya maua Afrika. Hifadhi hii ili iboreshwe ni lazima miundombinu ya barabara za lami iwe bayana na hii itasaidia kukuza utalii ndani ya hifadhi hii na si tu kukuza utalii lakini pia kuboresha uchumi wa Wilaya ya Makete. Kwa sababu Wilaya ya Makete pamoja na uchumi wa mazao ya chakula pia ndiyo Wilaya ambayo inaongoza baada ya Mafinga kwa mazao ya mbao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni jambo la muhimu sana, niishukuru Serikali ya CCM kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuboresha elimu. Wilaya ya Makete pale tuna Chuo cha VETA, bahati mbaya sana yako madarasa lakini hakuna mabweni. Wilaya ya Makete kwa jiografia yake haiwezekani wanafunzi wa kutoka Tarafa za Matamba, Ikuo, Lupalilo, Ukwama, Bulongwa kwenda kusoma kwenye chuo kilichoko Iwawa-Makete. Ni muhimu sana Serikali ijenge mabweni ili kunufaisha wananchi wa Tarafa zote ikiwemo Taarifa ya Magoma. Hili nimeliwasilisha kwa Waziri mhusika, naomba sana kwenye Mpango wetu wa Maendeleo tufasili kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu pia naomba nisisitize jambo moja. Mtihani tulionao sasa ukisikiliza hotuba ni kana kwamba muhimu kwa Watanzania ni kupata shahada ya kwanza, ya pili ama ya tatu. Mtihani tulionao sasa ni aina ya elimu tunayowapa watoto na watu wetu. Sote tunajua nguvu ya uchumi wa Tanzania ni kilimo, asilimia 77 ya watu wetu wanategemea kilimo. Hata hivyo elimu yetu kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu hakuna mahali ambapo mwanafunzi anakutana na kilimo. Ni hatari sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wamarekani na nchi zilizoendelea nguvu yao ni kwenye teknolojia ndiyo maana mtoto wa Kimarekani wa miaka nane au kumi anacheza na komputa, ana-feed data na analipwa. Kwao Wazungu wanasema hiyo siyo child labour lakini Mwafrika, Mtanzania akibeba jembe akiwa na miaka kumi na mbili, kumi na tatu tunamfundisha kilimo ambacho ndiyo nguvu yetu tunasema child labour. Tunaingia kwenye ugonjwa huu, matokeo yake tutakuwa na wanafunzi wanao-graduate kwenye level ya digrii ya kwanza, ya pili na ya tatu lakini hawana mahali pa kutumia elimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, baada miaka ile mitatu ya kujua kusoma na kuandika kwa watoto wetu ni muhimu sana watoto hawa wajifundishe ABC ya kilimo, siongelei kilimo nadharia, kilimo vitendo. Mtu anatoka Kanda ya Ziwa basi ajue akifika darasa la saba ni jinsi gani ya kutumia mbolea kulima pamba, kama anatoka Nyanda za Juu Kusini kwa mfano ajue kwa nini tunatumia DAP na kwa nini tunatumia urea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dozi hiyo ya course inaongezewa uzito anapomaliza kidato cha Nne ili tuwe na Watanzania ambao wakihitimu kidato cha nne hawana haja ya kutafuta shahada maana elimu waliyonayo inatosha kujitegemea. Nafikiri hili Wizara ya Elimu iliangalie kwa namna ya kipekee sana maana vinginevyo tutajuta kwa sababu tutakuwa na watu wengi walio-graduate, lakini hawana mahali pa kutumia elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusisitiza umuhimu wa Bwawa la Lumakali. Kaka yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo yuko hapa. Mto wa Lumakali ambao uko Bulongwa, Wilaya ya Makete, ni kati ya mito michache katika Tanzania ambayo haipungui maji kwa miaka 40 sasa ya utafiti. Document ambayo ni official ya TANESCO inaonyesha kwamba umeme unaotakiwa kuzalishwa kwa kutumia mto ule ni megawatts 640 hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali itekeleze mradi wa Lumakali kwa sababu utasaidia sana kutoa ajira kwa wananchi wa Makete, Mbeya na Njombe kwa sababu ni bwawa kubwa lakini pili utasaidia sana kuongeza umeme wetu. Mheshimiwa kaka yangu Profesa Muhongo chondechonde, naomba sana Mto Lumakali upewe nafasi yake ya kipekee kabisa ili Wilaya ya Makete ipate kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe hotuba yangu kwa kuongelea umuhimu wa kuunganisha barabara ya kutoka Ludewa - Mlangali. Niipongeze Serikali kwa sababu ya kufungua barabara hiyo lakini ni vizuri ifunguliwe kwa kiwango cha lami kutoka Mlangali - Lupila kutokea Ikonda - Makete, kutoka Chimala - Matamba - Kitulo - Mbeya, kutoka Mbeya - Ishonje - Makete - Njombe na kutoka Makete – Bulongwa – Iniho - Ipelele - Isonje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mungu akubariki na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukue nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kunipa heshima ya kuchangia nafasi hii muda huu. Jambo la pili, kama wenzangu walivyosema, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kufanya kwa ajili ya Taifa letu hili. (Makofi)
Tatu, namshukuru Waziri mwenye dhamana hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, rafiki na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufanya na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kwa masikitiko makubwa sana, pamoja na kazi kubwa anayoifanya Waziri wetu, niliposikiliza pamoja na kusoma kitabu cha hotuba yake hii sijaona akisema chochote kuhusu Shamba la Mifugo la Kitulo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere pamoja na Mzee wetu Karume, mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kazi kubwa waliyoifanya ni kuhakikisha uchumi wa Tanzania wanaugawanya kufuata mahitaji. Moja ya walichokiamua ni kuanzisha shamba maalum la mifugo Kitulo, Wilaya ya Makete ili kusaidia wakulima wetu kuachana na kuchunga ng‟ombe, waanze kufuga, wameamua hilo mwaka 1965.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali zilizofuata ni masikitiko makubwa, hazijapeleka mkazo kwenye shamba hili. Kumbe waasisi wa Taifa hili waliona kwamba ni vigumu sana kutenga eneo la wachungaji, wakasema ili tubadilike ni lazima tuanzishe kituo cha kujifunza kufuga na shamba hili liko Kitulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shamba hili lingepewa haki, kwa maana ya kupelekewa fedha kwa ajili ya kuendeleza, ni wazi kabisa kwamba uchumi wa Watanzania kama walivyo wote maana Mikoa inayochunga ng‟ombe, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini wangeenda kujifunza Makete jinsi ya kufuga. Ng‟ombe mmoja wa maziwa, ni wazi fedha anazozalisha ni zaidi ya mara 20 ya ng‟ombe wa nyama kama ukithaminisha gharama za kuchunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji na Waheshimiwa Wabunge wengine wako hapa wanajua, ng‟ombe mmoja kwa kawaida ili avunwe anachukua kati ya miaka mitatu mpaka saba. Ukichukua wastani wa miaka mitano ili umuuze, ambapo ng‟ombe wengi wanauzwa kati ya shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukua bei ya wastani wa shilingi 500,000, kama ukimuuza baada ya miaka mitano, ni kwamba huyo mchungaji alikuwa analipwa shilingi 8,333 kwa mwezi, kwa miaka mitano yote aliyokuwa anachunga ng‟ombe huyo. Amemuuza ng‟ombe baada ya miaka mitano, lakini akimuuza kwa shilingi 500,000 maana yake kila mwezi alikuwa anapewa ujira wa shilingi 8,333. Ikitokea msimu ng‟ombe amedhoofu kidogo ukamuuza kwa shilingi 400,000 maana yake alikuwa anapewa mshahara wa shilingi 6,666.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi na ni lazima tufike mahali kama Serikali tuamue kwamba majibu ya kujenga uwezo wa wachungaji wa mifugo ni Shamba la Kitulo lililopo Makete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nyie mnafahamu, hata kama ukisema kwamba mchungaji huyu yeye kipato chake ni dola moja, yaani shilingi 2,200 basi kwa miaka hiyo mitano atatumia shilingi 5,600,000 lakini atakuwa amepata fedha ambayo ni shilingi 400,000 mpaka shilingi 500,000 kwa huyo ng‟ombe mmoja. Huyo ng‟ombe amekula shilingi 5,600,000 au shilingi 3,600,000 lakini amepata kati ya shilingi 400,000 na shilingi 500,000 kwa miaka mitano kwa ng‟ombe mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekula shilingi 5,600,000 au shilingi 3,600,000 lakini amepata kati ya shilingi 400,000 na shilingi 500,000 kwa miaka mitano kwa ng‟ombe mmoja. Ombi langu kwa Serikali, ifike wakati sasa ione umuhimu wa kuendeleza shamba la Kitulo, sambamba na kujenga miundombinu inayofanya shamba la Kitulo liweze kufanya kazi. Namsifu rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu, tulipomwomba aje kwenye shamba hili la Kitulo alishangaa sana, maana ni shamba ambalo lina ekari 12,000, ng‟ombe waliopo ni 750, shamba lina uwezo wa kuwa na ng‟ombe 4,500 na kama hii ikifanikiwa ni kila nyumba ya Nyanda za Juu Kusini itakuwa ina uwezo wa kuzalisha maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde naiomba sana Serikali, lazima tuone umuhimu wa kuenzi waasisi wa Taifa hili kwenye vitu ambavyo vinaleta uchumi chanya kwa wananchi wetu, badala ya kuenzi wakubwa hawa kwa vitu ambavyo kimsingi you can not quantify in terms of economic benefits. Ni muhimu sana! Mojawapo ni shamba la Kitulo la Makete, ardhi ipo ni mali ya Serikali, tatizo ni nini? Wanahitaji shilingi bilioni 7.7 ili shamba hili lirudi asilimia 100 kwa full fledged ni shilingi bilioni 7.7
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kuchangia upande wa mbolea. Moja ya mkakati ambao hatujautekeleza vizuri, kama Serikali ya Chama Tawala ni upande wa mbolea ya ruzuku. Naomba sana badala ya kuendelea na mpango huu, ni vizuri Serikali yetu iamue kujenga Kiwanda cha Mbolea, mifuko iandikwe kabisa Not For Export, iuzwe locally kwa bei ya shilingi 10,000, kila mtu mwenye uwezo wa kulima anunue, bila kubagua nani apewe na nani asipewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu binafsi anajenga Kiwanda cha Minjingu pale Manyara, kwa nini Serikali isifanye hivyo? Tunajenga kiwanda kama Serikali, lakini mifuko inaandikwa Not For Export.
Kwa hiyo, kila mkulima mwenye uwezo, anakuwa na uwezo wa kununua. Utaratibu uliopo sasa unamfanya mwenye uwezo wa kulima sana asipewe. Maana Kanuni inasema, anayetakiwa kupewa ni mwenye ekari moja au mbili; ninalima ekari 500 then sistahili kusaidiwa. Sasa swali ni hili, nani ananufaisha uchumi wa Taifa hili? Bila shaka ni yule mwenye ekari nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, naomba niseme kidogo upande wa watendeji wetu yaani Maafisa Ugani. Vijiji vyetu vina Maafisa Kilimo, utaratibu uliopo sasa haufanyi maafisa hawa wawajibike kwa wakulima wetu.
Ombi langu kwa Serikali, Afisa Ugani wajibu wake mmojawapo uwe kuwatembelea wakulima na kujua kwamba ametembelea wakulima wangapi, atoe hesabu hiyo ngazi ya Kata mpaka Wilaya ili tuwe na hakika wakulima wangapi wamefikiwa na wataalamu wetu. Vinginevyo mtu anaweza akaajiriwa leo na asitoe ushauri kwa mkulima yeyote, bado akapata mshahara wake. Ni lazima aseme amemshauri nani? Ametembelea wakulima wangapi? Tukifanya hivyo, nchi yetu itabadilika na itafanikiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sana, ukitaka kufanikisha kilimo, ukitaka kufanikisha ufugaji, jibu ni shamba la Kitulo lililoko Makete. Liwe Shamba Darasa la Tanzania nzima. Mungu awabariki sana, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Waziri Mheshimiwa Mbarawa na msaidizi wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini na mtihani mkubwa walionao wa kuhakikisha kwamba nchi hii inabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie maeneo machache kwa haraka haraka. Umuhimu wa Kuunganisha RAHCO na TRL. Wabunge wengi wamechangia, lakini nimepitia sheria ya uanzishwaji wa TRL pamoja na RAHCO, ambacho nimebaini majukumu ya RAHCO bado ni majukumu ya msingi sana.
Pendekezo langu ni muhimu sana RAHCO aondolewe kwenye kusimamia reli ya kati, kwa sababu aliikuta, irudi TRL lakini majukumu ya RAHCO yaendelee kwenye reli mpya zote ambazo hatujajenga ikiwemo reli ya Mtwara Corridor. Miundombinu ya reli zote mpya ambazo hazijajengwa zibaki kwa RAHCO lakini aondolewe kwenye kusimamia reli ya kati, Reli ya kati ibaki TRL. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo naomba nisisitize umuhimu wa ujenzi wa reli ya kati kama wenzangu walivyosema kwa kutoa dimension tofauti kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa sasa duniani kote concession agreement ndio utaratibu wa uchumi wa dunia hii, uchumi wa tender ni wa kizamani kidogo nachelea kusema. Watu wanaotafuta biashara duniani anakushawishi, niko tayari kufanya a, b, c, kwa faida hii na mimi nitakupa hivi. Hivi ndivyo walivyofanya Kenya, Rwanda, Uganda, Djibouti na Ethiopia kujenga reli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa utaratibu wa concession agreement nchi haingii kwenye hasara ya kulipia kwa sababu deni linalipwa na uendeshaji wa mradi husika, ndiyo maana ni muhimu sana viongozi wetu wanaoisimamia Wizara hii walione hili kwa namna ya kipekee sana ili kuharakisha ujenzi wa reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niweke mfano mwepesi ili twende pamoja na wenzangu. TRL yenyewe kabla ya uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa sasa ilikuwa inaenda hovyo. Baada ya kuteuliwa CEO wa sasa ndugu Masanja TRL Inafanya vizuri, hii inakupa picha kwamba si wakati wote tatizo ni mfumo, kuna wakati mwingi na sehemu kubwa ya Waafrika tatizo letu ni watu wanao-execute nafasi hizo. Ukichagua CEO mbaya shirika linaweza likafa siyo kwa sababu ya mfumo, ndio maana TRL leo inafanya vizuri hakuna kilichobadilika. Sheria ni zile zile lakini baada ya kubadilisha CEO tu TRL inaenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashawishika kusema ni wajibu wa Serikali kuangalia kwamba competency based on recruitment, promotion and appointement become the key in terms of allowing other people to execute these positions. Lazima tuteue, tuajiri na tuwapandishe vyeo watu wetu kwa kufuata weledi usiotia mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo habari TRA na TPA na hasa utaratibu wa kutoza kodi mbili (storage charge na wherehouse charge). Ni vizuri sana Wizara iharakishe kuondoa kabisa TRA asitoze tozo la kutunza mizigo libaki TPA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni vizuri sana niongeze kusema habari ya simu fake.
T A A R I F A...
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo kuhusu simu fake. Watu wengi fasili ya simu fake wanadhani kwamba ni simu za shilingi 30,000; shilingi 25,000 ndizo simu fake. Ukweli ni kwamba simu nyingi za bei ndogo ni simu genuine. Mpaka sasa hivi, baada ya TCRA kuanzisha utaratibu huu ni asilimia 14 tu ya simu ambazo hazijahakikiwa. Wengi wanasema kwa nini waagizaji hawakufanya hivi kabla ya hapo?
Naomba niseme kwamba hili limetokana na kwamba TCRA haikuwa na mitambo ya kutambua simu fake na simu original. Baada ya kupata mitambo ni lazima tuingie sasa kwenye utaratibu wa kuhakiki simu hizo. Wengi mnajua simu fake madhara yake ni nini. Ninaweza kukupigia simu wewe nikakugombanisha, nikakufanyia madhara na mfumo wa utambuzi ukashindwa kutambua, ndiyo maana ni lazima tuwe na simu halisia ili kulinda afya na ulinzi wa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kidogo kuhusu barabara. Niipongeze Serikali kwa kutenga fedha kwenye barabara, lakini naomba nisisitize barabara zinazounganisha mikoa kwa mikoa chonde chonde, ni Katavi kwenda Tabora, Kigoma kwenda Tabora barabara ya Njombe kwenda Makete kwenda Mbeya, barabara ya kutoka Chimala - Matamba kwenda Hifadhi ya Kitulo ni muhimu sana zikapewa kipaumbele kwa sababu ya uchumi wetu na kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niombe sana Wizara ikamilishe viwanja vya ndege hasa vile ambavyo kwa sura ya kijiografia vinaunganisha na nchi jirani. Viwanja vya Songwe - Mbeya, Mwanza, Kigoma, Mtwara na viwanja kama hivyo. Baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii.
Kwanza kabisa napende kumpongeza Mheshimiwa Sospeter Muhongo na msaidizi wake na timu yake nzima kwa kazi kubwa ambayo wanalifanyia Taifa hili kuhakikisha kwamba nishati ya umeme inapatikana. Sambamba na hilo, napongeza kwa sababu ni ukweli ulio bayana kwamba kwa sasa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri zaidi Afrika, kwa maana ya coverage, yaani kwenda kwa kasi katika kusambaza umeme. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua uwezo wako na weledi wako, lakini nimesikitika sana ulipokuwa unawasilisha bajeti yako, hasa baada ya kuona Mto Lumakali ambao uko Makete ambao study yake ya kwanza imekamilika mwaka 1998 ikionesha kwamba tuna uwezo wa kuzalisha umeme megawatts 222; ikarudiwa tena mwaka 2002, ikaonesha kwamba tuna uwezo wa kuzalisha megawatts 340.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mto pekee ambao study kwa miaka 60 inaonesha kwamba maji yake hayapungui. Ninatambua changamoto tuliyonayo kwenye mito mingi iliyoko Tanzania, ni kupungua kwa maji. Ndiyo maana wakati nachangia Mpango wa Serikali nilisema Mheshimiwa Sospeter Muhongo anaonekana ana ugonjwa wa gesi; bila shaka nilimtania, lakini najaribu kusema kwamba upo umuhimu mkubwa wa kupeleka nguvu kubwa kwenye mradi wa maji wa Mto Lumakali unaopatikana Makete, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unajumuisha kuweka kingo za bwawa. TANESCO wameshafika mara nyingi kule, makampuni ya Afrika Kusini, China yamefika kule, yameshawaweka tumbo joto wananchi wangu wa Makete kwamba mpaka hapa tutakuwa na bwawa. Wameendelea kusubiri toka mwaka 1998 bwawa hilo halitokei.
Naomba sana Waziri mhusika aone umuhimu wa kipekee sana kupeleka bwawa hili. Bwawa hili pamoja na uzalishaji wa umeme litakuwa muhimu kwa uchumi wa Nyanda za Juu Kusini na Tanzania kwa ujumla. Utakuwa umepanda zao jipya la samaki kuvunwa katika bwawa hili la Lumakali pamoja na Mto wenyewe wa Lumakali. Kwa hiyo, ni muhimu sana jambo hili likatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena Wizara ione umuhimu wa kupeleka maeneo yaliyosalia umeme wa REA na hasa Kata za Lupila, Mbalache, Ukwama, Mang‟oto, Kipagalo, baadhi sehemu za vijiji vya Tarafa ya Magoma, Tarafa ya Ikuo, Tarafa ya Matamba na Tarafa ya Lupalilo. Ni jambo la msingi sana ili wananchi wa Makete wapate kuleta maendeleo kwenye nchi yetu. Kwa bahati nzuri unatambua, wananchi wa Makete kwa asili ni wachapakazi, kwa hiyo, nishati ya umeme kwao ni nguzo pekee ya muhimu itakayowezesha tukimbizane na maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kidogo eneo la madini. Sheria ya Madini ni muhimu sana ikafanyiwa marekebisho. Utaratibu uliopo sasa wa kupata leseni Makao Makuu na kupewa eneo Makao Makuu bila ushiriki wa Halmashauri husika, hautendi haki. Ni muhimu sana tutengeneze mahusiano kati ya Mamlaka ya kutoa leseni na Halmashauri mama yenye kumiliki ardhi ambayo inaangukia kwenye eneo hilo ili kuondoa migongano isiyo na sababu lakini pia ili kuwapa faida wananchi ambao maeneo haya kimsingi ni ya kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie EWURA. Wenzangu wallyotangulia walikuwa wanasema kwamba wana interest na maeneo hayo; nami kwenye madini pamoja na mafuta nina-declare interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Makete pale mjini ina vituo vinne vya mafuta. Wamekwenda Maafisa wetu wa EWURA kufunga vituo vyote. Makete hakuna transit, kwa maana ya malori yanayobeba mafuta kupita Makete. Mafuta haya yanatwaliwa Dar es Salaam kwenye depot. Ni muhimu sana Maafisa wetu wa EWURA wajikite kwenye ku-control quality Dar es Salaam yanakotoka mafuta. Wajikite kwenye kufanya mahusiano stahiki na mamlaka nyingine zinazohakikisha kwamba mafuta yanayokwenda nchi jirani yanakuwa monitored ili kwamba mafuta hayo yasipelekwe mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo sahihi hata kidogo, inaonekana kama ni uonevu hivi kidogo, pale ambapo mafuta yanatoka Dar es Salaam, muuzaji wa mafuta yuko Makete, kilometa 900 kutoka Dar es Salaam, hakuna barabara inayopita kule kwenda nchi jirani, barabara yenyewe ni mbovu, halafu wafanyabiashara hawa wanafungiwa vituo vyao kwa sababu tu ya maafisa wetu wa EWURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa labda nimwombe Mheshimiwa Waziri, ninaamini sana katika competence based recruitment, ninaamini Sheria ya EWURA ni nzuri, kwenye hili, tatizo ni la watu. Tusioneane haya kwenye hili. Tatizo ni la maafisa wetu. Ni muhimu sana, maafisa wetu, sheria hata ingekuwa nzuri, kama an official ni corrupt ata-jeopardize the entire system.
Kwa hiyo, ni muhimu sana maafisa wetu hawa waangaliwe ili wanapofanya maamuzi, basi waone madhara ya uchumi pia. Tukisema hivi, hatumaanishi kwamba sasa watu waendelee kuvunja sheria, hapana. Tunachojaribu kusema ni kwamba mafuta yanakotoka yanajulikana, ni Bandari ya Dar es Salaam pekee inayoingiza mafuta Tanzania. Kwa hiyo, eneo la ku-control linajulikana. Inaumiza sana kuona watu wa Makete nao wanafungiwa vituo vyao kwa sababu tu ya maafisa hawa wanaoshindwa kuzingatia umuhimu wa kuzingatia mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize kusema kwamba Tanzania kwa sasa ninafahamu, tunakoelekea ni kuzuri, tena kuzuri sana na kazi hii kwa vyovyote vile nitakuwa nimekosa nidhamu kutokumsifia Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi yake ya kuongeza bajeti ya jumla ya maendeleo kufikia asilimia 40. Leo Waziri mwenye dhamana anatuambia, asilimia 94 ya bajeti yake inakwenda kwenye maendeleo. Mungu aibariki sana Tanzania na Mungu aibariki sana Serikali ya CCM kwa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, Mungu awabariki sana. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Lukuvi na Naibu Waziri Angeline Mabula pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri, Hifadhi ya Kitulo imechukua hata eneo ambalo kimsingi halitumiki kwa utalii wa maua. Kwa hiyo hifadhi imepora eneo ambalo ndilo tegemeo kwa kilimo cha wananchi wa Tarafa za Matamba, Ikuwo, Lupalilo na Magoma, hasa kata zifuatazo Mfumati, Itumbu, Kigala, Ipelele, Mlomwe na Kitulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri ashirikiane na Waziri mwenye dhamana ya Utalii kurekebisha mipaka ya Hifadhi ya Kitulo ili kuondoa malalamiko ya wananchi na kuwasaidia kuendeleza mashamba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ifahamike kuwa ulinzi wa Hifadhi ya Kitulo unategemea wananchi hawa. Ni muhimu wailinde huku wakiwa na eneo lao kwa ajili ya kulima. Mheshimiwa Waziri alishughulikie jambo hilo hasa miezi ya kuanzia Juni mpaka Septemba wakati wa kiangazi. Nawasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mungu kwa kutupa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano na mikakati yake ya kuiendeleza Tanzania. Kwa vyovyote vile ametumia weledi stahiki wa Marais waliomtangulia ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa nchi ya neema.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme mambo machache. Mimi ni mmoja wa waumini wa kodi, nashukuru wenzangu waliotangulia wamesema pia kuhusu kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kodi za kawaida za VAT kwenye maduka yetu na huduma zingine za mahoteli, mpaka sasa nchi yetu, kwa maana ya TRA hawajaitendea haki Tanzania kwa maana ya ukusanyaji wa kodi kwa wanaotakiwa kulipa kodi. Ingia maduka ya jumla yaliyoko Dodoma, ingia maduka ya jumla yaliyoko Dar es Salaam, migahawa mikubwa iliyoko Dodoma na of course Tanzania ona ni wapi ambapo wanalipa kodi? Hawatoi risiti, TRA wapo;na kwa sababu kutokulipa kodi ni criminal offence, naomba niishauri Serikali kwenye hili hakuna awareness creation. Huwezi ukahamasisha watu kulipa kodi, ni lazima ufanye coercion, ni lazima utumie nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, badala ya Jeshi letu la Polisi kukaa barabarani na kusimamisha magari yanayokwenda kasi, waingie mtaani kukamata watu wasiolipa kodi na hasa kwenye maduka. Ni lazima wote tukubaliane kwamba tutengeneze nchi ambayo inaabudu kulipa kodi na kwa kuanza hiari haipo, haiwezekani. Huwezi ukasema unatoa tangazo redioni ili mtu alipe kodi, haipo, ni lazima uende kwa shuruti, mtu aone adhabu ya mtu anayopata baada ya kukwepa kodi ndipo wengine wanaanza kulipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai pale. Wachaga wakawa wananiambia kitu gani kiliwafanya wao walime kahawa. Wakasema haiwezekani ukahamasisha watu walime zao ambalo wao hawalijui. Wakasema wakoloni walichofanya ni kushurutisha watu ili walime kahawa, lakini baada ya kukomaa ile kahawa wameuza, wale Wazungu wakawaambia sasa haya mapato ni ya kwenu ndiyo waka-induce spirit ya kupenda kulima kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema ni kwamba, kwenye kodi hakuna lelemama, ni lazima kama nchi tukubaliane, kwamba Jeshi letu la polisi tunalo, tunajua maduka hata hapa Dodoma hawalipi kodi, Dar es Salaam tunajua miji yote hawalipi kodi lazima tulipe kodi. Kodi ndiyo itakayoifanya nchi yetu isonge mbele. Kwa hili TRA lazima waongoze, lakini Police Force nayo ifundishwe jinsi ya kufuatilia kodi zetu badala ya kwenda kwenye vitu ambavyo kimsingi havizalishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Bajeti ya Waziri wa Fedha, ameonesha kuanzisha kodi kwenye transfer of shares, yaani unapouza hisa zako, basi wewe utozwe kodi. Nasikitika Mheshimiwa Philip Mpango rafiki yangu na Waziri wetu its unacceptable from all economic point of view; haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukatoza kodi kwenye transfer ya hisa; NMB kwa mfano ilipouza hisa mara ya kwanza iliuza kwa sh. 150, zikapanda mpaka 5000, zimeshuka mpaka 1,500 uliyemtoza capital gain kwenye transfer ya hisa ilipofika 5000; anapo encounter capital loss Serikali itamfidia? Anataka kuuza hisa zake alizonunua kwa 4,000 na bei ya soko ni shilingi 1,000 utafidia hiyo difference ya 3,000? Huwezi kufanya hivyo. Kwa hiyo, siyo ya kiuchumi wala siyo ya kinadharia wala siyo ya kivitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya, Rwanda, South Africa hawafanyi, kwa maana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hakuna anayeifanya hiyo ninyi mnaitoa wapi? Kenya waliiweka kwenye sheria wakaiondoa hata kabla hawajaitekeleza na tukumbuke ni vizuri Waziri afahamu, moja ya sababu ya kuanzisha Soko la Dar es Salaam ni kuhamasisha uwekezaji. Unaposema mtu akiuza unamtoza kodi unafukuza wawekezaji kwenye nchi yetu, chonde chonde naishauri Serikali iachane kabisa na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya miamala ya simu. Kaka yangu Mheshimiwa Zungu ameliongelea sana, naomba nisisitize. Bahati nzuri mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; chonde chonde Watanzania kodi hii ni lazima itozwe. Ni kweli miamala hii ni kati ya trilioni 40 mpaka 50 kwa mwaka, Serikali inakosa fedha nyingi kwenye hili. Naomba sana katika hili tuiunge mkono Serikali iendelee kutoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono haraka haraka Kamati ya Bajeti ya kupendekeza ongezeko la Sh. 50 kwenye mafuta ili tuwe na maji. Hivi ni nani ambaye atakataa kwenye hili? Ndiyo maana sioni kigugumizi cha Serikali kinatoka wapi; Wabunge tunapoongea, tunaongea kwa niaba ya wananchi wa Tanzania; this is the feeling of Tanzanians, tunajua kabisa ukiongeza sh.50, kama ukituma salamu kwamba ni kwa ajili ya maji hakuna atakayekataa kigugumizi kinatoka wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisemee kidogo milioni 50 kwa dhima ya Rais wetu. Marais wote duniani wana-dictate vision, lakini kufasili vision ni wajibu wa watendaji kama Waziri na sisi Wabunge kwa nafasi zetu. Rais, Magufuli alichosema kila kijiji atatoa milioni 50, mwenye kufasili utekelezaji huo sio Rais wetu, siyo kazi yake, ni Mawaziri, ni sisi Wabunge. Hakuna uchumi duniani wa kugawa hela.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu, kwa mfano, Wilaya ya Makete ina vijiji 103, ukikipa kila kijiji milioni 50 maana yake ni Sh. 5,150,000,000/=; Bilioni tano zinatosha kuanzisha Community Development Bank ya Makete na kwenye Tarafa zake sita ukaweka ofisi kwa sababu mtaji wa Community Development Bank ni bilioni tatu. Kwa hiyo, bilioni tano zangu Wilaya ya Makete, ukiwapelekea wakope kwa riba nafuu, hao wote mnaotaka vijiji vikope sasa zitakwenda kwenye Community Development Bank, mtaji ni wa Serikali, wa bilioni tano na Community Development Bank bilioni tano, kwa hiyo Wilaya nzima itanufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama si hivyo, ukiwauliza Wabunge wanajua, kwangu mimi ukipeleka bilioni tano ambazo zinatakiwa kwa milioni 50 kila kijiji, umemaliza kabisa tatizo la maji Makete. Badala ya kugawa milioni 50 waulize wananchi wa Makete watakwambia tunataka lami, tunataka maji. Bilioni tano zinatosha kufuta tatizo la maji, kutengeneza benki Wilayani Makete na Wilaya nyingine za Tanzania ili tuweze kupata maendeleo. Sina hakika kama ni kengele ya kwanza ama ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme naunga mkono hoja na Mungu ambariki Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wake ili twende kwenye haya tuliyopendekeza. Amina.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzangu walivyochangia, nimpongeze Profesa Maghembe na wenzake kwa kazi nzito waliyonayo. Mmoja alisema mzigo mzito mpe Mnyamwezi nadhani kwa mzigo huu hata Mnyamwezi anaweza akashindwa kuubeba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimemsikiliza sana Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Maghembe nikafikiri sikumsikia vizuri. Nikaisoma hotuba yake nikaridhika kwamba nilichosikia jana ndicho kilichoandikwa. Nimesikitika sana kuona katika kitabu chake chote ameacha hifadhi pekee ya maua kwenye Bara letu la Afrika lakini ukisoma kitabu chake, utalii Tanzania unapungua. Yeye hasemi chochote kabisa kuhusu habari ya kuendeleza Hifadhi ya Kitulo iliyoko Makete, hasemi chochote kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Makete wa Kata za Mfumbi, Mlondwe, Matamba, Kinyika, Ikuwo, Kigala, Ipelele pamoja na Kitulo yenyewe, wamehamishwa ili kupisha hifadhi hii muhimu. Sasa miaka inakwenda Wizara haifanyi chochote na bahati mbaya sana kwenye hotuba ya Waziri hasemi chochote kabisa juu ya mkakati wake wa kuendeleza Hifadhi ya Kitulo. Nimesikitika sana na nasikitika sana, kwa vyovyote vile sitaunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi utalii katika nchi yetu unachangia kiasi kikubwa sana cha Pato la Taifa lakini mkakati wa Wizara ni nini kuongeza watalii? Hasemi chochote juu ya kuboresha Hifadhi ya Kitulo, hasemi chochote juu ya kuboresha miundombinu ili angalau sasa watalii waone Makete kwenye Hifadhi ya Kitulo ni sehemu ya kukimbilia. Sikutaka kushawishika kwamba Mheshimiwa Profesa Maghembe yeye anaziona hifadhi zilizoko Kaskazini tu, sikutaka kufika huko, lakini naanza kushawishika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, ni lazima Waziri aje na majibu ni jinsi gani anafanya kwenye bajeti hii kuwafanya wananchi wa Makete ambao wanaitunza hifadhi hii, wamehama kuacha maeneo yao wasilime ili kuheshimu Pato la Taifa, basi wagawane Watanzania wote, maana wangelima wao mapato yale ni ya kwao. Wamepisha ili sasa hifadhi hii iwe mali ya Watanzania wote. Waziri atoe majibu hapa anaifanyia nini hifadhi hii ili kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Ngorongoro na Serengeti zimetajwa lakini Waziri anafahamu moja ya sifa zilizopelekea Hifadhi zetu za Ngorongoro, Serengeti na Manyara kuongeza watalii ni baada ya kuboresha miundombinu hasa barabara ya kutoka Arusha kuelekea Manyara na Monduli pia kuelekea kwenye lango la Ngorongoro, Kitulo mnafanyaje? Ni wazi ni lazima barabara ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo - Makete ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuimarisha utalii kwenye hifadhi hii, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufikiri heuristically kwa sababu ni kweli utalii ni leisure, utalii ni burudani, siyo mateso. Hakuna mtalii atakayekwenda Kitulo kama miundombinu mingine haionyeshi kuwasaidia wao. Sambamba na hilo, ndiyo maana nilimfuata Mheshimiwa Profesa Maghembe nikasisitiza umuhimu wa TANAPA kuweka hoteli au kutengeneza mazingira ya kuweka hoteli za kitalii eneo la Matamba ili kuboresha au kuongeza Pato la Taifa, kwenye hotuba yake, kimya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo kuhusu mwingiliano wa mipaka kati ya mifugo pamoja na hifadhi zetu. Kwa suala hili ni lazima Serikali ijipange, bahati nzuri mimi natoka wilaya ambayo ina wachungaji wa ng‟ombe, ina wafugaji wa ng‟ombe, ina wakulima na pia ina hifadhi. Narudia, ina wachungaji, ina wafugaji na ina wakulima lakini hifadhi pia inayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani dhana hapa, pia weledi kidogo unatofautiana kwenye kufasili kwa usahihi juu ya wachungaji wa ng‟ombe. Duniani kote inajulikana, ukisema unafanya kuchunga, wachungaji wote wanafuata malisho, nchi zetu hizi ni za ki-tropic, kwa hiyo mvua ina kiangazi na masika. Wakati wa kiangazi lazima mchungaji, siyo mfugaji, mchungaji atahama na mifugo yake kufuata malisho, lazima ugomvi na wakulima utakuwepo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naunga mkono hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mbinga Mjini, Mheshimiwa Sixtus kwamba Wizara lazima wakae, and on this you must be strict. Hamuweze ku-compromise na Wabunge kwa sababu its impossible, kama anatoka eneo ambalo watu wanachunga nitatetea wananchi wangu na ndiyo sifa kwangu. Ninyi lazima mje na ukweli kwamba pamoja na kwamba unatetea wachungaji wako lakini dunia ya sasa ni ya kufuga siyo ya kuchunga, lazima tuelewane hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara husika ishirikiane na Wizara nyingine kutengeneza mkakati ambao ni endelevu. Ni lazima tutafika mahali tutachagua, tunataka hifadhi au tunataka ng‟ombe wa kuchungwa. Kama tunataka wa kufuga, yes you can set aside a piece of land kwa ajili ya kuchunga lakini huwezi kutengeneza eneo kwa ajili ya kuswaga ng‟ombe, haiwezekani, kiangazi kitaingia lazima watatafuta malisho. Sisi ambao tumetumika sehemu mbalimbali kwenye eneo ambalo ni la wafugaji zikiwemo Wilaya za Hai, Siha, Mbeya, Songea na Makete kwenyewe tunajua, uko mtihani mkubwa wa ku-harness kati ya ufahamu wa kuchunga na kufuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize hoja yangu kwa kusema, ndiyo maana nilisema Mwalimu Nyerere na Mzee Karume wamezikwa kaburini lakini wana hekima kuliko sisi, wao waliweka shamba la mifugo Kitulo ili wachungaji wakajifunze kufuga Kitulo. Bahati mbaya Serikali haisemi chochote kuhusu hili. Ni muhimu sana shamba lile lifufuliwe ili wachungaji, waswagaji wa ng‟ombe wajue kwamba zama za sasa ni kufuga siyo kuchunga siyo kuswaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ifufue shamba la mifugo la Kitulo lililopo Makete pamoja na hifadhi ile ili liwe shamba darasa kwa mikoa yote Tanzania. Tutapona na tutaondoa migongano kati ya wafugaji na wakulima, vinginevyo haiwezekani, narudia, vinginevyo haiwezekani. Ukitaka kutibu hili ni lazima ukumbuke shamba darasa ni shamba la mifugo kule Makete, lakini Hifadhi ya Kitulo ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize, nakusudia kushika shilingi kama Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe hatakuja na majibu ya kwa nini katika mpango wake Hifadhi ya Kitulo ameiacha kirahisirahisi tu, ameiacha tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Profesa Maghembe (Waziri) pamoja na wasaidizi wake wote. Masikitiko yangu makubwa ni juu ya mambo mawili:-
(i) Kutoweka mikakati ya kuendeleza Hifadhi ya Maua ya Kitulo. Hifadhi ya Maua Kitulo ni muhimu sana, lazima uboreshaji wa miundombinu ya utalii ikiwa ni pamoja na barabara za lami kutoka Chimala – Matamba – Kitulo; Mbeya – Kitulo – Makete; Njombe – Makete – Kitulo. Pia kuweka hoteli ya kitalii Matamba na Makete ili kuongeza utalii.
(ii) Ugomvi wa wachunga ng‟ombe na Hifadhi ya Taifa. Ni muhimu sana kutambua kuwa haiwezekani ukatenga eneo la kuchunga ng‟ombe, unaweza kutenga eneo la kufuga tu. Watu wetu sisi ni wachungaji ambao tabia yao kuu ni kufuata malisho. Nchi yetu ni ya kitropiki ina misimu ya hali ya hewa mikuu miwili yaani masika na kiangazi. Wakati wa masika migogoro ni michache kwa kuwa malisho ni mengi, wakati wa kiangazi migogoro ni mingi kwa kuwa wachungaji wataswaga ng‟ombe kufuata malisho. Muhimu ni Wizara kuamua kisayansi, haiwezekani kutenga eneo la kuchunga ng‟ombe, ni lazima wachungaji wafundishwe kufuga na hili ni muhimu kufanyika kupitia kufufua shamba la mifugo Kitulo.
(iii) Shamba la mifugo Kitulo. Shamba hili likifufuliwa litatumika kama eneo la kutoa mafunzo kwa vitendo juu ya ufugaji wa ng‟ombe wa maziwa na nyama. Shamba hili lilianzishwa mwaka 1965 na Mwalimu Nyerere pamoja na Mzee Karume, walijua huwezi kutenga eneo la kuchungia ng‟ombe, lazima twende kwenye uchumi wa kufuga ng‟ombe wa maziwa na nyama. Ng‟ombe wa maziwa wana faida kubwa kwa binadamu kiuchumi na kiafya.
(iv) Sheria ziwekwe na zisimamiwe kwa ukali. Waheshimiwa Wabunge bila shaka baadhi wana ng‟ombe wanaoswaga, hivyo hawawezi kuunga mkono hoja hii lakini sheria zisimamiwe kwa ukali. Mfano huruhusiwi kuswaga ng‟ombe kutoka Wilaya moja kwenda nyingine bila kibali, sheria hizi zizingatiwe.
(v) Trespass kwenye hifadhi. Ni vizuri Wizara ifahamu kuwa watu wanaochunga ng‟ombe kwenye buffer zone, baadhi yao ndiyo hubadilika na kuvuna pembe za ndovu. Kwenye hili, Wizara lazima isimamie hifadhi hizi kwa ukali. Nchi jirani ya Kenya, ukipeleka mfugo au binadamu kwenye hifadhi unapigwa risasi na wamefanya hivi kwa sababu ni vigumu kutofautisha jangili na mchunga ng‟ombe kwenye hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ni muhimu sana kwa Taifa letu, si tu uchumi wa Taifa bali kiikolojia. Hifadhi ni msaada mkubwa wa kuhifadhi ikolojia ya mvua. Kama tukiruhusu uvamizi wa hifadhi, nchi yetu itakuwa jangwa. Serikali isimamie sheria kwa ukali, no compromise.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.