Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joyce Bitta Sokombi (8 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utahudu viwanda na biashara na mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda; Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao ulikuwa na Viwanda vikubwa, lakini sasa hivi vimekufa na viwanda hivyo ni MUTEX. Hiki Kiwanda cha MUTEX kimepoteza ajira nyingi sana za wananchi hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili. Ni vizuri Serikali ikajipanga tena upya kufufua kiwanda hiki. Vile vile ningependa kuishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa kufungua mnada wa Tarime mpakani, hii itasaidia kutoa ajira kwa vijana na kuepukana na vitendo viovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mazingira; kutokana na tabianchi hii inayotokana na Mkoa wa Mara kuwa na wafugaji na upatikanaji wa chakula na maji ya mifugo hiyo na kuhamahama kwa mifugo (wanyama) na wingi wa mifugo hiyo wanakandamiza sana ardhi na kusababisha maji kutokupenya ardhini na kusababisha mafuriko na kutuama kwa maji ambayo yanapelekea mazalia ya mbu na kuleta kipindupindu na madhara mengine kwa binadamu na hata kwa mifugo yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu, hii ni sekta ambayo Serikali izingatie na kuipa kipaumbele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu; pili, naishukuru familia yangu na tatu, namshukuru Kiongozi wangu wa Kambi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye upande wa uvuvi. Tanzania imekuwa ikiongoza Afrika Mashariki katika uvuvi wa ndani ya nchi na uvuvi wa maji baridi ambao ni kama mito pamoja na maziwa. Pia katika Maziwa Makuu, imekuwa ikiongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uvunaji mkubwa wa samaki hali ambayo inahatarisha uvunaji endelevu wa samaki. Kwa mfano, sasa hivi samaki kama sato, sangara, wamekuwa ni adimu sana katika Ziwa Victoria na bei yake pia imekuwa iko juu. Kwa mfano, ukichukulia kuanzia miaka mitatu iliyopita, samaki aina ya sangara ulikuwa ukimnunua sh. 5,000/= samaki wa kilo tano au kilo saba, lakini sasa hivi samaki huyo hakamatiki kutokana na uvuvi holela. Je, ni mkakati gani ambao Serikali imeuandaa kwa mwaka wa fedha ili kukabiliana na changamoto hii? Kuchoma nyavu kumekuwa na ugumu mkubwa wa kupata fursa za mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kilimo. Tanzania tumebarikiwa sana kuwa na ardhi ya kutosha na yenye rutuba. Mimi ninatokea Mkoa wa Mara; Mkoa wa Mara tulikuwa tunalima sana zao la pamba na pia tulikuwa na Kiwanda cha Mutex ambacho kilikuwa kinafanya kazi kubwa sana, kilikuwa kinasaidia sana vijana pamoja na wanawake kupata ajira. Pia kiwanda hicho kimekuwa kikiinua sana pato la Taifa. Leo hii kutokana na kutokuwepo na ulimaji wa pamba, imekuwa ni shida kubwa sana na kiwanda hicho kimefungwa na kimekuwa kikisuasua. Je, Serikali iko tayari kuinua zao la pamba ili kiwanda hicho kifunguliwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, nitaongelea hapo hapo kwenye suala la kilimo. Mkoa wa Mara umepakana na nchi ya Kenya. Nchi ya Kenya imejikita sana kwenye zao la maua. Je, kwa nini Serikali yetu pia isijikite kwenye zao la Maua? Ukiangalia kwa mfano, Mkoa wa Mara umepakana sana na Wilaya ya Tarime ambapo iko karibu sana na nchi ya Kenya na hali ya hewa inafanana na nchi ya Kenya; kwa nini na sisi Tanzania tusijikite kwenye kilimo cha maua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa mifugo. Mkoa wa Mara tuna ng‟ombe wengi wa kutosha, lakini wafugaji hawa wanatumia miundombinu ambayo si endelevu. Lazima Serikali ianze kuandaa mpango wa muda mrefu kwa ufugaji wa kisasa kwa sababu tutakapofuga kisasa itatusaidia sana. Pia Serikali iandae majosho na machinjio yawe ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mwenzangu wa Mkoa wa Mwanza, amesema kwamba wao Wasukuma ni wanywaji wa maziwa na sisi wananchi wa Mkoa wa Mara ni wanywaji wakubwa sana wa maziwa na pia walaji wazuri sana wa nyama ya ng‟ombe. Kwa nini Serikali isiweke kipaumbele kuhakikisha kwamba hawa ngombe wanakuwa kwenye malisho mazuri kwa sababu maeneo mengi ya malisho hayapo. Maana mtu ukiwa na ng‟ombe zaidi ya 100 ni shida, utaenda kuwalishia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali iweke kipaumbele kwenye suala la mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite sana upande wa mawasiliano. Mkoa wa Mara mawasiliano ni shida hasa tukienda kwenye kata za Bunda upande wa Neruma, Nachonchwe, Vigicha, Ving‟wani na upande wa Tarime kuna Muriba na Yanungu. Hii ni asilimia kubwa sana ya watu ambao hawana mawasiliano na total yake inakuja ni 15,894 watu hawana mawasiliano. Mtu ukitaka kufanya mawasiliano inabidi uende kwenye mti yaani tunarudi kule kule enzi zile za Mwalimu Nyerere. Kwa kweli upande wa mawasiliano kwa Mkoa wa Mara inatia aibu. Naiomba Serikali ielekeze nguvu zake huko na kuhakikisha wale watu wanajione wako kwenye nchi yao na kwamba wanapata mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye upande wa uwanja wa ndege. Mkoa wa Mara tuna uwanja wa ndege mmoja tu na Mkoa wa Mara una historia kubwa sana ambayo haitafutika. Ni Mkoa ambao ametoka Baba wa Taifa, lakini uwanja wake wa ndege unatia aibu na unasikitisha sana. Tulitegemea uwanja wa ndege Musoma ndiyo uwe uwanja ambao ni wa mfano katika nchi yetu ya Tanzania. Hata kama tuna local airport basi iwe ni local airport yenye kiwango lakini uwanja wa Mara jamani unatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali ielekeze nguvu zote kwenye uwanja wa Musoma. Imefikia hatua tunasema sasa wana Mara na sisi tumechoka ina maana kwamba tunapohitaji kupanda ndege kwenye uwanja mzuri ni mpaka uende Mwanza au Dar es Salaam ina maana watu wa Mara hatufai kupanda ndege kwenye viwanja vizuri kwa hapa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nakuja upande wa barabara. Nitazungumzia barabara itokayo Manyamanyama kuelekea Musoma Vijijini. Barabara hiyo inapita katika vijiji vya Kangetutya, Kabulabula, Bugoji mpaka kufika Musoma Vijijini, kwa kweli hairidhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea katika bajeti hii barabara hii angalau ingekuwa ya kiwango cha lami lakini gharama zake zimewekwa kwenye kiwango cha changarawe. Zile changarawe zinazowekwa ni za kiwango cha chini sana mvua inaponyesha barabara zile zinakatika. Kwa hiyo, hakuna mawasiliano ya barabara kutoka kule Musoma Vijijini kuja Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama mkulima anataka kuuza mazao yake ni lazima mtu atoke kule Musoma Vijijini aje Bunda, usafiri inakuwa ni shida sana kwa sababu watu wengi wenye magari wanaogopa kuweka magari yao yafanye biashara kwenye hizo barabara kwa sababu mtu anaona gari yake inaharibika.
Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba barabara hii inayotoka Manyamanyama kwenda Musoma Vijijini kwa kipindi kijacho inajengwa kwa lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa Kabulabula akitaka kuiona lami ni mpaka aje Bunda au mpaka aende Musoma Mjini, kwa kweli tunaomba na tunasema kwamba wananchi wa kule wamechoka na wanasikitika sana. Mkoa wa Mara mzima barabara ya lami ni ile inayotoka Mwanza - Tarime - Kenya, zile barabara zingine zote hazina lami na nilitegemea kwenye bajeti yetu hii angalau ningeona vipande vya lami lakini sivyo. Lami tumewekewa kilometa mbili tu, ni ndogo sana na ni shilingi bilioni mbili.
Kwa hiyo basi, naomba na naendelea kuishauri Serikali, kwa hizi kilometa mbili zilizowekwa kwa upande wa Mkoa wa Mara kusema ukweli haziridhishi, hazitoshi ziongezwe. Mkoa wa Mara una population kubwa sana kwa nini Serikali isihakikishe inaweka lami katika baadhi ya barabara za Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na kuishauri sana Serikali iwe makini inapokuwa inakaa kujadili na kupanga bajeti zake. Kwa sababu unapokaa na kupanga ili mradi tu umepitisha bajeti, kaa uangalie ni watu wangapi unaowaumiza. Ina maana wale watu wa vijijini hawatakuwa na maendeleo mpaka lini? Hiyo pia inazidisha kudidimia kwa uchumi wa mahali husika kwa sababu watu wameshazoea ile hali ya kila siku kwamba mimi ni mtu wa kijijini, barabara ni ya vumbi, hakuna lami, hizo lami tutaziona mjini mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajikite sana katika Mkoa wetu wa Mara, tunaomba lami hasa kutoka Bunda kwenda Wilaya ya Musoma Vijijini na pia barabara ya Nata kwa Serengeti, kwa kweli tunaomba mtusaidie barabara za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa upande wa Serengeti ni Wilaya ambayo ina uchumi mkubwa kwanza tuna mbuga ya wanyama na pia watu wengi wanatoka Arusha kuja Serengeti, lakini barabara zile hazipitiki. Hamuoni kwamba tunapoteza asilimia kubwa sana ya uchumi wa Tanzania kwa kupoteza watalii kuja Tanzania kutembelea mbuga ya Serengeti?
Kwa hiyo basi, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Nitajikita sana upande wa Nyamongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Nyamongo ulianzishwa na wananchi wenyewe pale Nyamongo na Serikali ikaleta wawekezaji kwa makubaliano kwamba watawajengea wananchi wa eneo husika watawawekea hospitali, watawawekea maji, watawajengea barabara yenye lami na pia watawajengea kituo cha afya. Matokeo yake hayo makubaliano mpaka leo hayajafanyika, watu wa eneo lile kwa kweli wanatia huruma na inatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haioneshi kwamba wale wananchi wako kwenye nchi yao, ukikaa ukiangalia eneo kwamba linachimbwa madini na kwamba yale makubaliano ya mwaka 2011 walivyoenda Mawaziri yakawa kwamba wao wanachimba ule udongo ili wale wachimbaji wadogo wadogo wawe wanaenda kuchambua ule udongo, matokeo yake wakienda kuuchambua wanapigwa risasi. Je, ni halali kwa mwekezaji kuja kumpiga raia wa Tanzania?
Mheshimiwa Waziri ninakuomba na nina kusihi, hakikisha unaweka mipango ambayo ni mizuri kuhakikisha wale wananchi wa Nyamongo hawapati shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia mkataba wa wale wawekezaji pale Nyamongo uwekwe wazi na mnatakiwa pia muwaulize kama mkataba ulikuwa ni kwamba kuwajengea wananchi kuwawekea lami katika barabara na kuwawekea vituo vya afya, kwa nini hayo makubaliano hayakufanyika?(Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, nitajikita pia upande wa Dangote, nimeenda Mtwara. Dangote amekuja kuwekeza hapa nchini eneo la Mtwara kwa lengo la kutumia gesi yetu ya Mtwara. Lakini matokeo yake Dangote hatumii gesi yetu ya Mtwara anatumia mafuta. Je, yale mafuta wanayoyaagiza, yanalipiwa kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia kuhusu REA. REA ni nzuri na imekuja kwa ajili ya kumkomboa mwananchi ambaye yuko kijijini, lakini mmewasahau wale wananchi ambao wako pembezoni kwenye vile vijiji. REA imepita mjini tu, wale wananchi walioko pembeni ni ile wanakaa tu wanaangalia umeme ule. Jamani tunaomba kama Serikali imeamua kumkwamua mwananchi aliyeko kijijini, tuhakikishe kwamba REA inaenda kwenye kila kijiji na vitongoji vyake kwenye kila eneo, siyo REA ipite upande wengine wapate umeme, wengine wasipate umeme. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini, kwenye hili suala la REA aliwekee mkazo, kwa kweli inatia aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa mfano kule Kangetutya, Kabulabula umeme umepita tu, wale walioko ndani ndani hawana umeme, watafikiwa na umeme lini? Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, jikite sana katika maeneo ya ndani msipitishe tu umeme eneo la barabarani, wale walioko vijijini kwa ndani nao wanahitaji umeme. Mwananchi amezaliwa miaka nenda rudi anatumia kibatari, basi angalau hata miaka hiyo iliyobaki jamani angalau na inabidi aende mjini, yeye awashe umeme ajue umeme huu unawakaje na una starehe gani. Siyo hata ku-charge simu inabidi aende mjini kwenye center zinaitwa, watafanya namna hiyo mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena Mgodi wa Nyamongo. Ninakusihi sana Mheshimiwa Waziri, ninakusihi mno, wale wananchi wa pale kwa kweli wanateseka, watateseka mpaka lini? Wewe ukiwa Waziri tena mwenyeji wa Mkoa wa Mara nina hakika kwamba utaenda kulifanyia kazi kuhakikisha Mkoa wetu wa Mara unainuka, wale wananchi wa eneo la Nyamongo hawatapata shida tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri ukiangalia hata kama wakichimba visima eneo hilo yale maji siyo salama kutokana na ile sumu inayomwagwa kwenye Mto Tigiti, maji inabidi wayafuate mbali sana. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini atusaidie kwa hilo tujikwamue maana hayo mauaji yanayotokea Nyamongo kwa kweli ni aibu kwa Taifa letu. Wawekezaji wanakuja nchini wanakuwa wao ni bora kuliko Watanzania wenyewe tuliozaliwa katika nchi yetu. Tutaendelea kudharauliwa namna hii mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu fidia ndogo kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali kushindwa kuwadhibiti tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyama akimuua mtu au binadamu fidia yake ni ndogo sana. Familia inalipwa shilingi 100,000 au wasipate kabisa kutokana na figisufigisu za viongozi wa eneo husika; lakini endapo mtu akikutwa kaua wanyama, fidia anayotozwa ni kubwa sana na ni kuanzia shilingi milioni sita na zaidi. Swali la kujiuliza je, kipi kina thamani kati ya binadamu na mnyama? Maana hii inaonyesha moja kwa moja kuwa Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, iangalie sheria hii kwa umakini, kwani haiwezekani hata siku moja mnyama akawa na thamani kuliko mtu au binadamu. Ni vizuri wananchi wa eneo husika wapewe elimu ya kutosha juu ya fidia wanazostahili kulipwa maana kila mwananchi akijua juu ya umuhimu wa malipo wanayostahili kulipwa, naamini hakutakuwa na kelele kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya mbuga au hifadhi wananyanyasika sana utafikiri watu hawaishi katika nchi yao (wakimbizi). Wananyanyaswa, wanafukuzwa kwenye maeneo yao wakati Serikali haijawaandalia maeneo ya kwenda kuweka makazi hayo. Ina maana wakati wananchi hao wanajenga, Serikali ilikuwa wapi? Ina maana ilikuwa inawaangalia tu wanapomaliza ndiyo iwaambie wananchi kuwa wamevamia hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana na inasikitisha pia. Inabidi Serikali iwaangalie kwa upya wananchi hawa kwani wanaishi kwa hofu kubwa na maeneo hayo ni Maliwanda, Mihale, Mcharo, Serengeti, Hunyali, Kunzugu na Balili, hivyo vyote ni vijiji vya Wilaya ya Bunda. Kwa upande wa Serengeti ni Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri, Bonchungu na Robanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kuwadhibiti wanyama (tembo) wanaoharibu mazao ya wananchi bila kujali hasara wanayoipata wananchi hao. Kwanza kabisa bila kuwadhibiti tembo hao umaskini hautaisha, kila siku wananchi hawa wataendelea kuwa ombaomba kutokana na umaskini unaotawala kutokana na mazao yao kuliwa na tembo au kuharibiwa na tembo ama wanyama wengine waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikajipanga upya juu ya jambo hili la kuwadhibiti tembo ili wananchi wanapolima mazao yao wavune na kupata chakula na wananchi wengine wanahamia ili wapate kuvuna mazao yao na kuyauza kwa ajili ya kusomesha watoto wao, lakini tembo wanamaliza mazao ya wananchi kabla hawajavuna na kuendelea kuwadidimiza wananchi hawa kuwa maskini. Ninaamini Mheshimiwa Waziri atalishughulikia suala hili kwa ukaribu ili kuwasaidia wananchi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu fidia ndogo kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali kushindwa kuwadhibiti tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyama akimuua mtu au binadamu fidia yake ni ndogo sana. Familia inalipwa shilingi 100,000 au wasipate kabisa kutokana na figisufigisu za viongozi wa eneo husika; lakini endapo mtu akikutwa kaua wanyama, fidia anayotozwa ni kubwa sana na ni kuanzia shilingi milioni sita na zaidi. Swali la kujiuliza je, kipi kina thamani kati ya binadamu na mnyama? Maana hii inaonyesha moja kwa moja kuwa Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, iangalie sheria hii kwa umakini, kwani haiwezekani hata siku moja mnyama akawa na thamani kuliko mtu au binadamu. Ni vizuri wananchi wa eneo husika wapewe elimu ya kutosha juu ya fidia wanazostahili kulipwa maana kila mwananchi akijua juu ya umuhimu wa malipo wanayostahili kulipwa, naamini hakutakuwa na kelele kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya mbuga au hifadhi wananyanyasika sana utafikiri watu hawaishi katika nchi yao (wakimbizi). Wananyanyaswa, wanafukuzwa kwenye maeneo yao wakati Serikali haijawaandalia maeneo ya kwenda kuweka makazi hayo. Ina maana wakati wananchi hao wanajenga, Serikali ilikuwa wapi? Ina maana ilikuwa inawaangalia tu wanapomaliza ndiyo iwaambie wananchi kuwa wamevamia hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana na inasikitisha pia. Inabidi Serikali iwaangalie kwa upya wananchi hawa kwani wanaishi kwa hofu kubwa na maeneo hayo ni Maliwanda, Mihale, Mcharo, Serengeti, Hunyali, Kunzugu na Balili, hivyo vyote ni vijiji vya Wilaya ya Bunda. Kwa upande wa Serengeti ni Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri, Bonchungu na Robanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kuwadhibiti wanyama (tembo) wanaoharibu mazao ya wananchi bila kujali hasara wanayoipata wananchi hao. Kwanza kabisa bila kuwadhibiti tembo hao umaskini hautaisha, kila siku wananchi hawa wataendelea kuwa ombaomba kutokana na umaskini unaotawala kutokana na mazao yao kuliwa na tembo au kuharibiwa na tembo ama wanyama wengine waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikajipanga upya juu ya jambo hili la kuwadhibiti tembo ili wananchi wanapolima mazao yao wavune na kupata chakula na wananchi wengine wanahamia ili wapate kuvuna mazao yao na kuyauza kwa ajili ya kusomesha watoto wao, lakini tembo wanamaliza mazao ya wananchi kabla hawajavuna na kuendelea kuwadidimiza wananchi hawa kuwa maskini. Ninaamini Mheshimiwa Waziri atalishughulikia suala hili kwa ukaribu ili kuwasaidia wananchi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchukua nafasi hii kuunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa ushauri wangu kuhusu mabaki ya mjusi wetu yaliyoko Humberg. Ni aibu kwa Serikali yetu na nchi yetu ya Tanzania kushindwa kuyarudisha mabaki ya mjusi wetu. Hayo mabaki tunaendelea kuwanufaisha Wajerumani na sio Watanzania. Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuyarudisha mabaki hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishauri Serikali ifanye jitihada na kila iwezalo kuweza kurudisha mabaki hayo ili yanufaishe Watanzania kwani Watalii watakuwa wanakuja kuangalia mabaki hayo kwa tozo ya kiingilio. Ili Serikali iweze kurudisha heshima yake kwa wananchi wake wa Tanzania ilete mabaki ya mjusi wetu yaweze kunufaisha Watanzania wenyewe na si vinginevyo, ni aibu kwa Serikali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi za Balozi zetu zipo hoi, yaani zina hali mbaya sana. Nilitegemea safari hii Serikali ingeona umuhimu mkubwa sana na kuweza kutenga fedha za kutosha ili kukarabati hizo ofisi ili ziwe kwenye hali nzuri. Ni aibu unapokwenda nchi za nje, ukienda ofisi za Ubalozi wa Tanzania ni aibu kubwa, pia inatia uchungu kwa nchi yetu. Balozi zetu kuwa mfano wa ofisi mbaya kuliko kawaida, yaani kuliko nchi yoyote hapa duniani halafu Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anasema, watafungua Balozi zingine. Je, ni kwa gharama zipi? Kwa nini Serikali isione umuhimu wa kukarabati kwanza Balozi zilizopo halafu ndiyo ione umuhimu wa kufungua hizo ofisi za Balozi zingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishauri Serikali ifanye jitihada ya kuwa na Ubalozi wa Uingereza hapa nchini kwetu. Kwani mtu ukitaka kuomba viza ya kwenda Uingereza ilikuwa lazima uende Nairobi, Kenya. Sasa hivi ukitaka viza ya Uingereza sio tena Kenya bali inabidi uende South Africa. Kwa nini Serikali isione umuhimu juu ya jambo hili kwani inaleta usumbufu mkubwa sana na kero kwa Watanzania. Natumaini Mheshimiwa Waziri, kati ya majukumu yake yote, aweke kipaumbele kwa Ubalozi wa Uingereza uwepo hapa Tanzania.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, utangulizi; awali ya yote napenda kunukuu katika kitabu Kitakatifu cha Biblia, Mithali, Sura ya 11, mstari wa 14; mstari huo unasema: “Pasipo mashauri Taifa hupotea, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya nchini; ni dhahiri hali ya uchumi wa nchi unayumba. Kuyumba huku kwa uchumi ni hatari sana katika sekta nzima ya afya. Kumekuwepo na malalamiko makubwa katika sekta ya afya kwa muda mrefu sasa na hayajatatuliwa. Takwimu zinaonesha huduma za afya na ustawi wa jamii zilikua kwa asilimia 8.1 mwaka 2014, lakini kwa mwaka 2015 ni asilimia 4.7 pekee. Hii ina maana kwamba, utoaji huduma za afya na ustawi wa jamii umepungua kwa asilimia 3.4. Hivi karibuni nilifanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Musoma, Mara ni kilio kwa kweli! Vitanda havitoshi, madawa hakuna, kiasi kwamba wanaokwenda hospitali wakiwa wanaugua malaria wanatoka na typhoid au kifua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kauli tata sana na za aibu kwenye sekta hii ya afya. Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa ukosefu wa dawa nchini, ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake wanasema kuna dawa za kutosha katika Bohari ya Dawa Nchini (MSD). Wananchi nao wanalalamika kwa kukosa dawa mahospitalini. Huduma za tiba zinadorora kwa kuwa hakuna vifaatiba katika mahospitali mengi. Pamba na gloves zimeadimika, wagonjwa wanalazimika kwenda na pamba na gloves; akinamama na watoto wamekuwa wahanga wakubwa katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka kuna siku hapa Mheshimiwa Mbunge mmoja aliuliza swali kuhusu Mpango wa Serikali kupambana na ugonjwa wa fibroid kwa wanawake. Ni ajabu sana Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwa kubeza kuwa, fibroid siyo ugonjwa tishio kwa kiasi hicho. Lakini sisi akinamama tunajua ni kwa namna gani akinamama wenzetu wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Fibroid kwa akinamama ni tishio na ni tishio kubwa sana maana sasa linawakumba mpaka mabinti wadogo. Hili suala siyo la kuchukulia kimzaha tu! Tunapoteza nguvukazi ya Taifa ha hatuoni mpango madhubuti wa Serikali katika kukabiliana na tatizo hili kama walivyofanya kwa ugonjwa wa malaria kwa akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu kuona Serikali ikinunua ndege ambazo zinawanufaisha tabaka la watu wachache tu huku hakuna uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya ambayo inamgusa kila mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema, pasipo mashauri, Tanzania itapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la utawala bora; hakuna maendeleo kama hakuna utawala bora. Ndani ya Serikali hii, washauri mbalimbali na watalaam wamekuwa wazito katika kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Tatizo kubwa linaloitafuna Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kutokuzingatia misingi ya utawala bora, kufuata sheria, Kanuni pamoja na kuruhusu mawazo huru kwa kila Mtanzania. Utawala bora ni pamoja na kukaribisha mawazo kutoka katika maeneo mbalimbali bila kujali itikadi za vyama. Ni pamoja na kuwa na kifua cha kupokea changamoto ikiwa ni pamoja na kukosoa na kukosolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu pale ninapoona Vyama vya Upinzani ambavyo ni jicho la pili la Serikali, ni jicho linaloweza kuona pale Serikali isipoweza kuona, ni mdomo wa kuwasemea wadau mbalimbali ikiwemo ninyi Wabunge wa Chama Tawala na Mawaziri pale ambapo mna mambo ambayo hamuwezi kuyasema waziwazi kwa Serikali kwa sababu ya hofu za nafasi au maslahi binafsi. Upinzani ni msaada kwa kuwa, ndiyo Serikali mbadala (Alternative Government). Tunapoona Mawaziri au Wabunge wakichukia Upinzani au kuwa na mawazo potofu kuwa, upinzani ni kupinga inashangaza sana!
Ni vema Waheshimiwa Wabunge wakapewa elimu ili kujua upinzani ni kitu gani ili linapokuja suala la kujadili mambo ya msingi ya kimaendeleo kwa faida ya nchi yetu waweze kuwa-change kwa kupokea, kuyachambua yale yanayofaa hasa katika kujadili Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maendeleo inakwama kutokana na sanaa katika mambo ya msingi. Mfano, Mkurugenzi anatumbuliwa tena kwa barua kutoka Ikulu halafu anapelekwa nje ya nchi kuwa Balozi; tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi imekuwa na msururu wa kodi kwa wafanyabiashara wazawa tena wale wenye mitaji midogo. Maliasili kuna kilio kikubwa cha kodi hizo mfano, kodi ya kulipia magari, leseni, mageti na kadhalika. Hii ikiwa ni jumla ya kodi 32 katika biashara ya sekta ya utalii. Yaani inaweza kuchukuwa takribani miezi miwili mpaka mitatu katika kulipia kodi. Hii ni aibu kubwa kwa Serikali, ambayo inashindwa kuleta tija katika kuwasaidia watu wake ambao tayari wengi wao wanapambana na ukuta mkubwa wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, kuna baadhi ya viongozi wanabeza na kusema, eti Watanzania ni wavivu! Kwa wingi huu wa kodi ambao unawafanya wafanyabiashara kushindwa kuendelea kumudu biashara zao, Serikali haioni kuwa tunazalisha wimbi la majambazi na vibaka tena kwa bidii?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kuwa, Serikali iangalie upya namna ya kukusanya kodi. Iangalie ni aina gani za biashara za kukusanya kodi na kwa kiasi gani ili kupunguza mzigo mkubwa uliowaelemea wafanyabiashara wadogo au wachuuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Watendaji wa Serikali na wanasiasa wakaheshimu kazi kubwa inayofanywa na upinzani. Mheshimiwa Rais aheshimu Sheria na Katiba ya nchi ambayo kimsingi inawaruhusu wanasiasa kufanya mikutano yao kwa uhuru na amani. Rais awe ni mfano wa kusimamia Sheria na Katiba ya nchi. Kila Kiongozi ataweza kutekeleza shughuli za maendeleo na kuleta tija katika Taifa endapo kuna uhuru na haki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho; niombe Waziri wa Fedha aweze kupitia tena vipaumbele hivi vya mpango na kuangalia ni namna gani sekta ya utalii inaweza kuchangia zaidi. Kwa kuwa, awali sekta hii ndiyo ilikuwa inachangia pato kubwa la Taifa takirbani asilimia 27.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.