Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joyce John Mukya (2 total)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya michezo vimegeuzwa kuwa viwanja vya usheherekeaji wa sherehe mbalimbali na badala ya kuviendeleza kama viwanja vya michezo ambavyo vingeweza kuwasaidia vijana, wanawake na watoto katika kujenga, kufurahia kuimarisha afya zetu na kuchangamsha miili yetu na hata kutupa afya njema kila siku. Hatimaye viwanja hivyo vimegeuzwa kuwa sehemu ya kufanyia sherehe za Kitaifa na sherehe za Chama cha Mapinduzi (CCM). Mbaya zaidi viwanja hivi vimegeuzwa viwanja vya CCM, kwa sababu vyama vya upinzani hawaruhusiwi kufanya shughuli zao katika viwanja hivi isipokuwa Chama cha Mapinduzi tu. Nina ushahidi na hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie viwanja hivi vitumike kwa shughuli za michezo na kama ni shughuli nyingine basi kuwe na usawa na haki kwa sababu vyama au itikadi ni mapenzi ya mtu binafsi tu, lakini mwisho wa siku Utanzania wetu unabaki pale pale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama nilivyoainisha hapo juu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea tatizo la wafanyakazi kutopata ajira za kudumu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nilishafanya kazi na Jumuiya kabla sijawa Mbunge kuanzia mwaka 2006 mpaka 2009 kama IT Assistant. Wakati najiunga pale nilikuta wafanyakazi wa temporary ambao wanafanya kazi kama vibarua, naweza kusema hadi leo hii ni muda wa miaka 10 na zaidi sasa, baadhi yao hawajaajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua toka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini ajira za hawa wafanyakazi zitatangazwa ili waweze kuajiriwa? Kwa sababu wangekuwa hawatakiwi, wasingekuwepo kazini hadi leo hii. Naweza kukupa majina yao kama utahitaji pia na wengi ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, ni Serikali yetu kutopeleka fedha za kuendesha Jumuiya kwa wakati. Mfano, tokea makubaliano ya bajeti iliyopita kati ya Partner States hadi leo hii nchi yetu ya Tanzania haijapeleka au kukamilisha mchango wake wa kuendesha Jumuiya hiyo. Hii ni aibu sana kwa nchi yetu na ukizingatia Jumuiya hii Makao Makuu yake yapo Tanzania. Ilitakiwa tuoneshe mfano kwa nchi wanachama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni wafanyakazi wa ngazi ya profession kutokupatiwa Diplomatic Passports. Kama yalivyokuwa makubaliano ya nchi wanachama, yaani Headquarters Agreement, wafanyakazi wa level hii wanaotoka nchi nyingine wana diplomatic passports isipokuwa nchi yetu. Hili nilishalisemea tena Bungeni mara mbili na Mheshimiwa Waziri akaahidi watapewa kwani ni haki yao, lakini hadi leo imekuwa ni hadithi tu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kujua ni lini watapewa haki yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wa Jumuiya wamekuwa na shida ya kupata Work Permit. Ni aibu kubwa sana kwa hili jambo. Mtumishi ana mkataba wa miaka mitano, lakini bado Serikali haimpi Work Permit ya miaka mitano na kusababisha kero kubwa kwa nchi wanachama wanaokuja kufanya kazi nchini ambako ndiyo sehemu Headquarter ilipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba Mheshimiwa Waziri anijibu maswali yafuatayo:-
(1) Ni lini Wizara hii itaanza kukaa na Wabunge wa EAC ili kujadili mambo mbalimbali, kama mtakavyojipangia ratiba, kama Wizara ya EAC ya Awamu ya Nne ilivyokuwa inafanya?
(2) Ni lini mtawapatia ofisi Wabunge wa Tanzania ambao wanaunda Bunge la Afrika Mashariki na waache kufanyia kazi hotelini au nyumbani mwao?
(3) Ni lini Serikali ya Tanzania itaanza kuwapa mikopo ya magari Wabunge wa EAC kama zinavyofanya nchi wanachama, mfano Kenya na Uganda, ili waache kutumia mishahara yao na posho kununua magari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.