Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joyce John Mukya (2 total)

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shida kubwa ya maji katika Mkoa wa Arusha especially Jiji la Arusha inatokana na tatizo la mgao wa umeme tatizo ambalo katika nchi yetu tunaona kabisa haliishi leo wala kesho. Kwa mfano, Arusha Mjini tulikuwa tunapata maji lita laki moja kwa siku lakini mwaka 2013 tunapata maji lita 45,000 na katika Kata ya Mushono ni magaloni matano kwa siku hadi kufikia sasa kwa wiki mbili unapata maji mara mbili. Tatizo hili limekuwa kubwa sana na hatuoni kama kuna mkakati madhubuti wa Serikali kusaidia tatizo hili kwa sababu shida kubwa ni ya umeme na umeme wa nchi hii hata siku moja haujawaka frequently. Ni nini mkakati wa Serikali kuhusu kusaidia kutatua changamoto hii kwa sababu umeme katika nchi hii bado ni wa mgao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mradi huu ni wa muda mrefu, lakini shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni shida ya kudumu na ya muda mrefu sana kama ulivyosema katika jibu lako …
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi huu ni wa muda mrefu na shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni ya muda mrefu, nini mkakati wa Serikali kutatua kwa haraka tatizo hili ili wananchi wa Arusha wapate maji kwa haraka?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimfahamishe Mbunge vitu asivyovifahamu. Kwanza pale KIA tumeweka sub-station kwa ajili ya umeme wa KIA na maeneo ya pale tu. Ukienda Mererani, katika wachimbaji 10 wa Tanzanite wachimbaji tisa wanatumia umeme bila kulipa, wanaiba umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba ukitaka umeme wa uhakika shughulika na wezi wa umeme wa Arusha, ahsante.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu sehemu ya pili ya swali lake kwamba mradi huu ni wa muda mrefu, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ili tuweze kufanya kazi nzuri lazima kwanza tufanye usanifu ili tuwe na uhakika kabisa kwamba maji yatakuwepo ya kutosha maeneo yote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avumilie na mpango unaoletwa na Serikali ni wa uhakika kwamba tupate maji ya kutosha mpaka mwaka 2025.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kumekuwa na tabia mbaya na chafu ya udhalilishaji wa hawa waajiri wa madini ya kuwapekua wafanyakazi sehemu za siri. Hii imefanyika katika Kampuni ya Tanzanite one kule wanapovuna madini ya Tanzanite, wanawapekua sehemu za siri hasa sehemu za kujisaidia haja kubwa. Je, hakuna njia mbadala ya kufanya zoezi hilo zaidi ya kuwadhalilisha hawa wafanyakazi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI,VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge, mimi mwenyewe nilikwenda pale Tanzanite one katika mgodi huo, nilikutana na changamoto hiyo kubwa ambayo wafanyakazi waliieleza mbele yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ziara ile nilitoa maelekezo na taratibu zote za namna ya ukaguzi unavyopaswa kufanyika ili usidhalilishe utu wa wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika migodi hiyo. Maelekezo yalitolewa ya kwamba zipo taratibu za kufuata katika ukaguzi lakini siyo za kumdhalilisha mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maelekezo tayari yapo, kama vitendo hivi vinaendelea basi niwaombe wafanyakazi wale waripoti tuchukue hatua stahiki zaidi.